Search This Blog

MALAIKA? AU SHETANI? - 1

 





    IMEANDIKWA NA : MAUNDU MWINGIZI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Malaika? Au Shetani?

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kama kawaida, mwanga unapoanza kumezwa na giza la magharibi, shughuli za utafutaji riziki kwa wengi hukoma hadi siku inayofuata. Jioni hiyo, nawe ulifunga biashara yako baada ya kupitia hesabu zako. Taabu na adha za usafiri, zisababishwazo na foleni ndefu, zinakulazimu kutembe kwa miguu badala ya kupanda daladala, pengine sababu nyingine ni ukaribu wa eneo unaloishi kwa kutokea hapo Kariakoo. Unaianza safari; mguu mosi, mguu pili.



    Ukiwa maeneo ya Ilala boma; takribani nusu ya safari yako, ukamwona bwana mmoja amebarizi pembezoni mwa barabara, usawa uliokuwa ukiambaa nao katika njia yako. Watu ni wengi barabarani, kila mmoja na hamsini zake, kwa hivi, hapakauwa na sababu ya msingi ya kukushitua kumwona mtu yule.Kwa jijini Dar es Salaam, viumbe wachafu, waliochakaa na kusawajika miili yao, kutokana na sulba za kimaisha ni wengi mno, kuliko hata huyo bwana uliyemwona. Baada ya kumtazama kwa muda mrefu kadiri ulivyokuwa ukimsogelea, macho yako yakapeleka taarifa haraka kwenye ubongo kwamba mtu yule ulipata kumwona mahala. Wapi? Haukumbuki!



    Ingawa hukumkumbuka, lakini kwa namna sura yake inavyokujia, yamkini ulipata kumwona kabla ya hapo. Na, huenda ulimfahamu–lakini ulimfahamu kivipi? Hilo lilikuwa nje ya milki ya kumbukumbu zako.



    Ulipomkaribia, mwonekano wake ulidhihirisha dhiki na adha za kimaisha alizonazo, hivyo, kutambulika kama Ombaomba wengine warandao huku na kule kuomba pesa. Na, kwa namna ya usimamaji wake barabarani wakati ukimsogelea, ilikufunulia fikara nyingine, kwamba baada ya kukuona ukielekea usawa wake, alikuwa akikusubiri umfikie akuombe pesa.



    Mbali ya kuwa ombaomba, bwana yule alitia shaka kumtazama mara mbili: rundo la nywele chafu lilijisokota kichwani mwake, uchakavu na uchafu wa nguo alizovaa, ulifanana na ngozi yake ya mwili. Mkononi alikuwa ameshika fimbo aliyoifanya kama mhimili wake wa kusimama. Ingawaje tayari magharibi ilikwisha kuingia, na kwamba joto la mchana kutwa lilimezwa na upepo na vivuli, lakini ombaomba huyo alikuwa akitiririkwa jasho jeusi, linalofumkia ukingoni mwa kichwa chake na kutengeneza mifereji myeusi pembezoni mwa mashavu yake. Juu ya hayo, sura aliukunja kiasi cha kutengeneza mfano wa matuta katika paji la uso wake, yawezayo kumhofisha ye yote ambaye angewajihiana naye.



    Kwa mwonekano ule wenye kukirihisha nafsi na kuogopesha macho, ukajionea vema umpishie mbali kwa kuambaa sanjari na lami ya barabarani ili kujitanibu wowote uwezao kusababishwa naye. Wa ima, ulipoona tayari umemfikia, ukajibaraguza kutoa simu, ambayo wala haikuwa ikiita, ukaiweka sikioni kama uliyepigiwa. Yote hiyo ukikwepa asikusemeshe wala kukuomba pesa. Cha ajabu, ombaomba uliyemhofia, hakukusemesha wala kukuomba pesa, zaidi aliendelea tu kukukazia macho hadi ulipompita na kumwacha nyuma.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ili usionekane umeiweka simu sikioni kama toi, ukajifanya kuongea. "Eeh hallow!"



    Bila kutegemea, ukaisikia sauti ikikujibu toka ndani ya simu: "Hallow nini wewe? Acha kuzuga–unahangaika utafikiri umelazimishwa kutoa msaada!"



    Ukapigwa na butwaa huku ubaridi wa hofu ukikutambaa mwili mzima. Kwakuwa ni kitu ambacho hukukitegemea, haraka ukaitoa simu sikioni, ukajaribu kuiangalia endapo kama iko namba iliyojipiga kwa kibahati mbaya ... Hakuna!



    Simu haikupigwa wala kujipiga. Sasa kumbe nini?

    Katika kutafuta ithibati ya kadhia hiyo, ukajikuta umeirejesha sikioni kuona kama ulichokisikia ni sawa au mawenge tu. Kama mchezo wa kuigiza, ile kuiweka tu simu sikioni, sauti ile ikaendelea, "Utagongwa na magari bure kwa upuuzi wako, kutoa ni moyo wala si utajiri, hujaombwa wala hujalazimishwa..."



    Kabla sauti haijaendelea, kwa wahka na taharuki ukaitoa tena simu sikioni. Safari hii badala ya kuiangalia tena kama ulivyofanya awali, ukageuka nyuma kumwangalia yule ombaomba, kwa namna ulivyomtilia mashaka tangu ulipomwona, hisia zako zilikutuma kwamba huenda maajabu yale yanatoka kwake. Katika hali usiyoitegemea–akumwona tena–Alitoweka!



    Ilikuwa ni hatua chache tu ulizopiga baada ya kumpita, sasa kutoweka kwake hata asionekane akitembea, ikawa ni kitendawili kilichokosa mteguaji. Ikawa kama uliye ndotoni, kwa maana yadhihirikayo mbele yako ni muhali kutokea katika uhalisia. Katika kuchanganyikiwa kwako, bila kujitambua ukapelekaa tena simu sikioni ukiwa kama haujaamini. Sauti ileile ilikupokea, "Huna lolote–roho mbaya tu inakusumbua. vijihela vyenyewe vya mbogamboga tu hivyo, sijui ungekuwa na pesa haswa ingekuwaje!"



    Ulitamani kukimbia, miguu haikuwa na nguvu; ukatamani machozi yaakawa mbali na macho; katamani kupiga mayowe, koromea likaigomea sauti kutoka; katamani kuitupa simu, mikono ikagoma kutii maamuzi yako. Hofu ilikuvaa kuanzia kwenye kucha ya kidole cha mguu hadi kwenye unywele wa utosi.



    “Au simu imeingiliwa na kirusi!” ukabaki kujisemea peke yako kama mwendawazimu.



    Kila ujasiri uliotaka kujipatia haukuwa na chembe ya tija. Safari hii ulipotaka tena kuiweka simu sikioni ili umuulize huyo anayeongea ni nani, mikono yako ikaanza kutetemeka, hofu kuu ikiushambulia moyo wako. Baada ya mpambano baina ya dhamira na hisia, ukajikaza na kuipeleka sikioni. Simu ikawa kimya, hapana sauti tena.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kipi kinanitokea?”

    Kwa kukosa majibu ya maswali yako wala ufafanuzi wa hisia zako, kama uliyefungwa mota miguuni, ukajikuta ukiondoka kwa kasi eneo lile huku ukigeuka huku na kule kuona kama yuko anayekufuatilia.



    Baada ya takribani dakika thelathini, hatimaye ukawasili mahala unapoishi, Buguruni Malapa. Kabla hujaingia ndani, ukaona namna pekee ya kutafuta ufumbuzi na tiba ya msongo wa mawazo unaongeza kasi kichwani, ni kutafuta ushauri kwa kuwasimulia sahibu zako. Ukajongea hadi kijiweni kwa vijana wenyeji wa pale.



    Kama kawaida ya vijiwe vya vijana; ulipowasalimu, wapo walioitika kwa shangwe, wapo walioitikia chini ya mwamba wa pua, na wapo ambao hawakuchukua taabu ya kuitikia salamu yako. Baada ya michapo uliyokuta ikizungumzwa hapo kujiweni kuisha, ndipo nawe ukapenyeza mkasa wako. Kufikia tamati ya mkasa wako, yakapatikana makundi mawili; wapo waliocheka, wakakudhihaki na kukupuuza; na wapo waliokuonea huruma wakiamini kwamba Mbu wamekusababishia Malaria kali kukupanda kichwani na kukushauri ufike kituo cha afya.



    Makundi yote mawili, hayakuonesha msaada wala matumaini kwa kadhia yako. Kwa hivyo, ukaondoka kama ulivyofika. Huko nyuma ukaacha gumzo na mjadala. Kukosa kwako msaada japo wa nasaha tu, kukakupelekea kwenda kulala ukiwa umevurugikiwa kichwani.



    Pengine kukosa ndugu jijini Dar es Salaam, ndiko kulikokufanya ukose pa kukimbilia. Lakini jamaa wa nyumbani kwenu, Bukoba, waishio Dar es Salaam ni wengi, na wanao umoja wa kufaana katika shida na raha, walaki siku zote umekuwa ukipuuza kujimuika nao–leo utaanzia wapi kuwafuata? Unapiga moyo konde na kukubali kusubiri kadari ya Mola.



    Usiku huo, haukupata hata lepe la usingizi, usingizi uliparama kwa sababu ya moyo kuvamiwa na hofu. Taswira ya yule ombaomba ilijirudia kichwani mwako na kuitawanya sumu ya hofu kila kona ya mwili wako. Raha ilikutoka. Baada ya kitambo kirefu, hofu iliyokita moyoni muda mrefu na kuanza kuzoeleka, na taratibu ikaanza kuyeyuka kama theluji juani. Kwa hivi, kumbo la usingizi likakumba.

    __________



    ILIANZA kama ndoto. La, si ndoto, ni kama Jinamizi, maana hilo ndilo huwakaba watu usingizini kiasi cha kuwafanya washindwe kupiga kelele wala kupumua vizuri.

    Naam, hivyo ndivyo ilivyokutokea ukiwa usingizini; ulikabwa, ukatapatapa, ukaishiwa pumzi na kuhangaika mno. Tofauti na ilivyo kwa majinamizi ambayo hukaba kwa muda mfupi, na baada ya usingizi kuparama nayo hutokomea, kwako ilizidi kipimo ukahisi kama kwamba roho inakaribia kuuacha mwili.

    Tumezoea kwamba, Jinamizi hukaba usingizini tu, na usingizi ukikutoka, nalo hutoweka. Kama hivyo ndivyo; inakuwaje pale inapotokea Jinamizi likaendelea kukukaba hata baada ya kushituka toka usingizini?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndivyo ilivyokutokea siku hiyo, baada ya kudhibitiwa na Jinamizi kwa muda mrefu, hatimaye usingizi ukakuruka kichwani. Cha ajabu, Jinamizi liliendelea kukukaba kiasi cha kukufanya apaparike kama kuku anayechinjwa.

    ‘Hili sasa siyo jinamizi tena’ uliwaza. Kwa shida na maumivu ukajitahidi kufumbua macho. Kwa ulichokiona, aheri ungeendelea kukabwa kuliko kushuhudia akukabaye.



    Fikra za jinamizi zikayeyuka rasmi kichwani mwako baada ya kukutanisha macho yako na yale yaliyoko kwenye sura mbaya isiyo na mvuto, yenye kutisha isiyo na wema, na yenye ghadhabu zisizo mithilika. Ni sura ya yule Ombaomba uliyekutana naye maeneo ya Ilala boma.



    Ukiwa hujui kipi cha kufanya kati ya kufumba macho, kupiga kelele au kumtoa mikono yake yenye kucha ndefu na chafu shingoni mwako, Ombaomba yule alipofunua kinywa chake na kucheka kwa sauti ya juu. Kinywa kilikuwa kilichohifadhi meno machafu yaliyotengeneza rangi ya manjano na kuachia mapengo kwenye baadhi ya maeneo, kilikuwa kikitoa reha mbaya, mithili ya mzoga uliooza.



    Ukiwa hujui kipi cha kufanya kati ya kufumba macho, kupiga kelele au kumtoa mikono yake yenye kucha ndefu na chafu shingoni mwako, Ombaomba yule alipofunua kinywa chake na kucheka kwa sauti ya juu. Kinywa kilikuwa kilichohifadhi meno machafu yaliyotengeneza rangi ya manjano na kuachia mapengo kwenye baadhi ya maeneo, kilikuwa kikitoa reha mbaya, mithili ya mzoga uliooza.



    Muujiza mkubwa ulikuwa kwenye meno yake ya mbele: yalikuwa kama yametengeneza vijitobo katika ncha zake. Na, kutokea kwenye vijitobo hivyo, vijidudu mfano wa funza vilikuwa vikijitokeza na kurudi ndani kadri alivyokuwa akifunua kinywa chake na kukifumba wakati akicheka. Mtu anawezaje kuishi na funza ndani ya matundu ya meno yake?

    Kuhamanika kwako na staajabia hali hiyo, kukamfanya Ombaomba azidi kukucheka, japo tazamo la mtu yeyote lisingeliafiki kwamba lile kuitwa cheko. Ni cheko gani lifanyalo sura izidi kuwa mbaya namna ile? Hata anayelia huwa hawi hivyo.



    "Si ulijifanya mjanja..?" Ombaomba akadhihaki.

    Kwa namna alivyokukaba kooni, usingeweza kutoa sauti ya kumjibu. Wazo likaishia kupita kichwani mwako, ‘Ujanja gani sasa, Kutotoa msaada wa pesa kwa ombaomba?’

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog