Search This Blog

MALAIKA? AU SHETANI? - 2

 





    Simulizi : Malaika? Au Shetani?

    Sehemu Ya Pili (2)



    Cha ajabu, kama aliyekuwa akikusoma mawazo yako, akakushushua huku amekutolea macho, “Siyo kutokutoa msaada. Hivi, wewe una msaada wa kunipa, au mimi ndo wa kukusaidia wewe?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ukiwa unashangaa namna alivyoweza kukisoma kile ulichokiwaza kichwani, akaendelea, “Unakumbuka ulichonitenda? Kiumbe una roho mbaya wewe ya kumnyima nzi kinyesi!”



    Ukazidiwa na mshangao. Kwamba inaonekana uliwahi kukorofishana naye, lakini haukumbuki ni wapi na kwa vipi.

    "Nakuuliza halafu haujibu eenh?"



    Sasa ungemjibu vipi wakati sauti haitoki?

    Papo hapo, akiwa amekudhibiti hata usipate upenyo wa kujikukurua, Ombaomba akakusogezea mdomo wake hadi kwenye kiwiko cha mkono wako, kisha akakubandika jino kama sindano. Toka ndani ya jino hilo ambalo muda huo lilikuwa limechoma sehemu ya mkono wako, akawa anatoa kitu kama funza, kilichokuwa kikikuingia mkononi mwako na kukuachia maumivu makali.



    ‘Arrghhhh!’ kila ulipojaribu kupiga kelele, uliishia kukoroma tu kwa namna alivyokukaba koo. Baada ya kuhakikisha amekwisha kuingizia kijidudu hicho mwilini mwako kupitia mkononi, aliutoa mdomo wake na kukwambia, "Mpaka hapo tutakapokutana tena–usiku mwema."



    Akakuachia na kutoweka. Ukabaki ukikohoa mfululizo hali udenda ukikutoka. Kwa taabu na maumivu, ukajiinua na kuketi kitandani huku mikono yako ingali imeshika sehemu ya shingoni mwako. Ukajipigapiga kichwani ili kuona kama uko ndotoni au La! Ukamaizi kwamba haikuwa ndoto, bali ni kweli yametokea. Maumivu yaliyokuwa yakipungua taratibu mkononi, yakakufanya ujitazame kwa uangalifu mahala ulipoumwa jino.



    Ni bora hata usingejitazama kwa ulichokiona!

    Macho yako yakashuhudia kitu mithili ya funza, kikimalizikia kuingia mkononi mwako kupitia tundu la sehemu ile uliyobandikwa jino. Na, kilipomalizika tu, tundu likajiziba na mwili ukarudia kama mwanzo tu – hakuna tundu–hakuna jeraha.



    Kwa kihoro kikubwa, ukaruka toka kitandani na kusimama, huku ukitamani kuukimbia mkono wako mwenyewe. Nani angetulia tu hali ameona kitu kikimuingia mkononi mwake?

    Mungu wangu – nimemkosea nini yule kiumbe? Ukajaribu kuusugua mkono wako, mahala pale palikoingiwa na mdudu funza; hakuna kilichobadilika. Kwa woga na hamaniko, ukaukimbilia mlango wa chumba chako–ukaufungua na kutoka. Huko nje nako, giza la kutisha likakupokea; mashaka na woga vilivyokutoa nje, vikakurudisha ndani. Ukaendelea kuhatahata na chumba; ndani uchungu, nje ukakasi. Ukiwa umesimama katikati ya chumba, mara ukasikia adhana za alfajiri–kumepambazuka.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mapambazuko hayo ndiyo yakakupa ujasiri wa kutoka tena nje na kuketi kibarazani. Kila ulichowaza na kuwazua, hakikukufikisha katika uteguzi wa kitendawili kilichokufika. Nani utakayemfikia akakuamini? Kama mwanzo tu, ulipowasimulia marafiki zako kuhusu sauti ya ajabu katika simu yako, ulkaonekana kuchanganyikiwa. Je, hili la kutokewa na mtu uliyepata kumwona hapo kabla, akakukaba koo, akakukaripia, na kama haitoshi, akakubandika jino mkononi na kukuingizia kijidudu kilichosambaza maumivu mwili mzima–utaaminika? Kibaya zaidi, kijitundu kilichobaki baada ya kijidudu kukuingia, kimejiziba chenyewe. Yuko atakayemakinika na simulizi yako?



    Baada ya kuzama kwenye tafakuri ya kina, ukakata shauri la kutomwambia mtu yeyote juu ya kilichokutokea, japo moyo uliendelea kukukereketa kuuweka wazi mkasa huo kwa watu. Wapangaji wenziyo na majirani waliamka na kukukuta umebarizi hapo nje ukiwa umebarizi. Kama desturi, mkasabahiana kwa taadhima huku kila mmoja akiendelea na pilika zake asubuhi. Nuru ya jua na pitapita ya watu, vinakufariji na kukupunguzia hofu. Ukarejea ndani, na baada ya kujinadhifu mwili ukatoka kama ada, kwenda kutarazaki.



    Siku hiyo, shughulini ulipwaya; hali ya furaha, amani na kujiamini vikatoweka kabisa kiasi cha kukuondolea ufanisi wako. Pamoja na kujitahidi kuzidhibiti hisia mbaya, lakini kila mara kumbukumbu zilipokurejesha usiku wa siku iliyopita, moyo ulikulipuka na kukufanya usinyae kwa simanzi. Haukuwa mkasa wa kawaida kutokea kwa kijana wa hirimu yako.

    Hali ilikuwa hivyo hadi jioni ikaingia, muda wa kurejea nyumbani kupumzika ukawadia. Kishingo upande, ukafunga biashara na kuanza kuondoka. Njia ya kutoa Kariakoo kwenda Buguruni unakoishi, ni ileile ipatayo Ilala Boma ambapo ulipomwona yule Ombaomba. Pamoja na woga kukuvaa, walakini, haukuwa na namna nyingine ya kufanya, kwa sababu njia nyingine mbali ya hiyo ni ya mzunguko mkubwa mno. Ikakubidi ujikaze kisabuni na kuazimu kupita njia hiyo. Kama kawaida ya foleni ya jiji, kwa nyakati kama hizo za jioni, ikakubidi kama ilivyo kawaida yako, utembee kwa miguu. Ulitembea salama salmini, hadi ulipoanza kuyakaribia maeneo yale uliyomwona yule ombaomba na mara ikakutokea sauti ya ajabu kwenye simu, ndimo damu inakuchemka kwa mashaka, mwili ukakusisimka kwa hofu, nywele za kichwani zikajizoa kwa woga, vinyweleo vinajitutumua juu ya ngozi kwa simanzi.



    Taswira ya Ombaomba akiwa amekukaba koo, huku jasho chafu likimtiririka ikaanza kukuijia. Ukajikuta ukifumba macho kwa mzizimo wa hisia mbaya kichwani. Kitendo cha kufumba kwako macho kwa hisia za hofu huku ukitembea barabarani, almanusura kikusababishie ajali.

    “We bwege acha kulala barabarani!” Dereva bodaboda aliyekosa kukugonga, akakukaripia kwa maneno ya unyambi na ufidhuli.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno ya dereva bodaboda huyo ndiyo yaliyokutanabahisha na kukurejesha katika umakini wa barabarani. Mfadhaiko ukakushambulia baada ya kumaizi kwamba wapiti njia wengi walibaki kukushangaa wewe. Hayo yote yanatokea ikiwa ni kituo kimoja tu kimesalia kufika mahala ulipotokewa na yule Ombaomba siku moja nyuma.

    Kwanini nipate taabu yote hii!. Ukawaza huku ukitafakari hatua ya kuchukua ili kumkwepa Ombaomba.



    Katika kutafuta suluhu ya mambo, ukaamua kupanda gari badala ya kupita kwa miguu eneo lile lililokuachia kumbukumbu mbaya kichwani. Bila ajizi, ukachagua moja kati ya daladala zielekeazo maeneo ya Gongo la mboto, kupitia barabara hiyo ya uhuru, ukapanda. Dalala hiyo nayo inakwenda kwa mwendo wa kinyonga, taratibu mithili ya chatu aliyevimbiwa - foleni imeuma kwelikweli. Kwa mwendo huo, inakuchukuni takribani dakika ishirini na tano, kulifikia eneo lile aliposimama Ombaomba siku iliyopita. Kumfikiria ombaomba kukakufanya uikumbuke tena ile kadhia iliyokutokea usiku; taswira ya kinywa kichafu cha ombaomba akiwa amekukaba kooni inakuijia; ile minyoo inachungulia kupitia ncha za meno yake machafu. Kwa hofu na msisimko ukajikuta ukifumba macho na kuugulia maumivu ya hisia.



    Katika hali hiyo ya hisia. Ukahisi kama Ombaomba amekukamata tena tena na kutaka kukubandika jino. Bila kutaraji wala kutambua ufanyalo, ukajikuta ukipiga mayowe, “ANANIUMAAA!”



    Abiria ndani ya daladala wakataharuki na kuamsha zogo, ndipo kama uliyetoka usingizini, ukazinduka, fadhaa ikakukumba; ukaangaza huku na kule, na kuona kila abiria akikushangaa na kukutazama kwa mtazamo wa wasiwasi. Wapo waliodhani umechanganyikiwa, wengine wakahisi umekumbwa na kitu kibaya. Balaa likabaki kwa abiria walioketi na kusimama karibu yake, wakikuogopa na kutaka kukuepuka, lakini kwa namna abiria walivyojaa na kubanana, hakuna aliyepata nafasi ya kukukimbia. Ili kuepuka wahka na taharuki ya abiria, ukaamua kuomba kushuka, “Konda niache hapo.”



    Ingawaje hapakuwa na kituo cha dalala mahala hapo, lakini Konda aliona vyema kukushusha kama ulivyoomba ili kunusuru mkanyagano wa abiria. Kwa bahati, dalala zilikuwa haziendi kutokana foleni kushtadi barabara, hivyo, Kondakta akakufungulia mlango ili uteremke.



    Ukiwa unaanza kushusha mguu chini kutoka kwenye dalala, ukagundua kwamba kumbe ndo kwanza mlikuwa mfika eneo lilelile ulipomwona yule Ombaomba jana yake, na kutokewa na sauti ya vitisho simuni. Sasa, ukajikuta ukiduaa; kushuka chini hautamani, kurudi ndani ya dalala unagwaya. Ukajikuta ukining’inia mlangoni kama wewe ndiye Kondakta. Hali hiyo, ikazidi kuwafanya abiria pamoja na Konda wazidi kukushangaa na kujitanibu nawe.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Oya, hebu teremka bwana we!” Konda akabwata huku akikusukuma. Ukajikuta ukiteremka kama uliyechanganyikiwa.

    Ukashuka huku ukiyumba kwa kusukumwa, na kubaki ukiduwaa barabarani.



    “Kama hajarogwa kwa wizi wa wake za watu, basi Mbu wamemsababishia maleria,” Abiria mmoja akadhihaki.



    “Mkiambiwa rudisheni vitu mlivyoiba misikitini–hamtaki!” Konda naye akakutupia maneno ya dhihaka.



    “Mngechelewa kumshusha, angeanza kupiga watu humu!” Abiria mwingine akapaza sauti huku akicheka.



    Maneno ya abiria kwenye daladala hayakukutaabisha kichwa. Akili yako ilimakinika na Ombaomba. Pamoja na kuangaza kwa umakini, walakini hukumwona bwana yule aliyekukosesha raha njia nzima. Ukahama upande huo wa barabara, ukaongeza mwendo na kutoweka eneo hilo.



    Baada ya hatua ndefu za mashaka, hatimaye ukafika kwako ukiwa hoi bin taabani. Ukaingia ndani mwako na kujitupa kitandani kwa mchoko na mawazo. Usingizi nao haukukufanyia hiyana, ukakulaki na kukuchukua.



    Kilichokutoa usingizini baada ya saa kadhaa za kulala, ni njaa ya mchana kutwa. Ukashituka na kuangalia muda: Saa nne na robo usiku. Ukasimama na kuvua viatu ulivyokuwa umelala navyo, ukabadili nguo na kutoka kwenda kupata chakula.

    Baada ya chakula, ukarejea ndani ukiwa walau na nguvu mpya, ukalala. Usiku ukapita bila ya bughudha za ombaomba wala rabsha za ndotoni. Siku hiyo, walau uliamka na amani kwamba yale mauzauza yamekwisha, na kwamba unaendelea na maisha yako kama kawaida.



    Mizunguko ya utafuta ilimalizika kama iwavyo siku nyingine, ukarejea nyumbani salama bin salmin. Mchezo ukakaanza baada ya kumaliza kupata chakula na kupanda kitandani kulala. Ndani ya mkono wako wa kushoto, maumivu makali mfano wa sumu ya nyoka yalianza kutambaa kwa kasi. Kitu mfano wa funza kilikuwa kikitembea ndani kwa ndani na kuacha uchungu usiosemekana. Fikara na hisia, vikakurejeshea kumbukumbu ya kile kilichokuingia mkononi kupitia jino la Ombaomba. Kadiri muda ulivyokuwa ukiyoyoma, ndivyo maumivu yalivyozidi kukumaliza. Mdudu aliyekuwa akikutembea mkononi, aliambaa kuanzia chini ya bega mpaka karibu ya kiwiko–. Uzalendo ukakushinda–ukaanza kulia.



    Kwa mchomo wa maumivu, ukatamani kuita watu, walakini hunacho cha kuwaambia. Nani atakuamini? Kukosekana japo ushahidi wa kijitundu kilichopitisha hicho kijidudu kisambazacho sumu mwilini, kingefanya usisikilizwe. Na, suala la kwanini haukuwaeleza watu kama ulivamiwa na jitula ajabu usiku, lingekunyima haki ya kueleweka. Hapo awali, hukutazama mbali, ukaamini hakuna madhara makubwa, hivyo, ukalifuga tatizo moyoni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog