Search This Blog

TANZIA - 1

 





    IMEANDIKWA NA : MAUNDU MWINGIZI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Tanzia

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa ghafla tu, Pepo kali zilipovuma karibu kila kona ya wilaya ya Kibondo, mkoani kigoma. Taratibu mawingu mazito yakalifunika anga kiasi cha kuifanya saa tisa ile ya alasiri ifanane na usiku wa manane, usiku wa kiza, usiku wa hofu. Ingawaje ilikuwa ni msimu wa kiangazi na kwamba ni aghalabu mvua kunyesha, lakini hakuna aliyeipuuza dalili ya mvua ile ambayo ni mawingu.



    Kilichowafanya wakaazi waogope zaidi ni jinsi giza lilivyozidi kuumeza mwanga, maana hata kama nd’o dalili yenyewe ya mvua, hii sasa ilizidi! Baadhi ya wafanyabiashara wakaanza kufunga maduka yao, wanafunzi wakikimbilia makwao, na hata mifugo nayo ikaanza kurejea mabandani ikijua kuwa usiku umewadia. Wale wenzangu na mimi wenye nyumba za udongo zilizosheheni ‘mawakili’ karibu katika kila ukuta walianza ‘kudhikiri’ vyumbani mwao wakimuomba mola awasitiri…maana bila hata ya mvua tu, kila siku ukuta unakuuliza ‘Nikuuwe?’ sasa je ikishuka si kuta zitageuka biskuti?



    Upepo mkali uliendelea kuvuma mithili ya kimbingunga huku baridi kali ikiwa imeshtadi kwelikweli, cha jabu hapakuwa na mingurumo, radi, wala manyunyu…ni upepo, Baridi na giza tu.



    ***



    Wakati hali hiyo ya hewa ikizidi kuchafuka, katika wilaya hiyohiyo ya Kibondo nyumba ya Bi Masonganya binti Kalukalange ilifurika umati mkubwa wa wana-ukoo kutoka sehemu mbalimbali. Watoto, wajukuu, vitukuu na vilembwe wakiwa wamekusanyika kwa kukizunguka kitanda cha chuma alipolala Bi Masonganya.



    Ni wana-ukoo hao pekee ndiyo waliokuwa wakijua siri ya hali ya hewa kubadilika ghafla katika eneo lote la kibondo. Ni kwamba bibi na mama yao kipenzi, Bi Masonganya alikuwa akikaribia kukata roho baada ya kuishi kwa takribani miaka miamoja na sitini! Kwa kawaida kifo huja ghafla tu na hakuna anayeweza kupata taarifa kabla…ila kwa wana-ukoo hawa walikitumainia kifo cha mama na bibi yao yule.



    “Yreeeeeeeew! Watemi woseeee! mizimu yoose! Makulwa na madoto, na makashindyeee! Mumsaidie mtu wenu.” Maneno hayo yalitamkwa kwa sauti kali na babu mmoja aliyekuwa amesimama pamoja na wana-ukoo wale kisha akatoa chafya kwa nguvu na sauti kali sana!



    Nje ya chumba hicho, usawa wa dirisha alikuwa amesimama binti wa mwisho wa Bi Masonganya, akiwa ameshika mwichi mkononi akisubiri ishara aliyoelekezwa ili atekeleze zoezi muhimu…na ishara hiyo ilikuwa ni ile chafya aliyoisikia ikitokea ndani. Kitendo bila kuchelewa akauinua juu ule mwichi aliokuwa ameushikilia, kisha akaukita kwa nguvu chini ya ukuta ambao kwa ndani amelala mama yake akiwa amezungukwa na wana-ukoo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada tu ya kuukita mchi ule chini ya ukuta, kule chumbani wana ukoo wakashuhudia mama yao akihangaika kitandani kwa sekunde kadhaa huku akikakamaa kama askari wa kikoloni akijiandaa kupiga saluti kwa bwana wake, haikuchukua hata dakika mbili, Bi Masonganya akanena kwa sauti kavu ya kukoroma.



    “…Akkh…wana-ngu…mme-niwe-zaa mme-ni-u-waaa!” Hapohapo Bi Masonganya akakata roho.



    Sauti za vigeregere, nderemo na vifijo kutoka kwa wana-ukoo vilizizima chumbani humo, japo havikuwa vigeregere vya furaha bali viashiria vya kukamilika kwa kifo kile kilichowabidi kukilazimisha. Laiti wangejua kilichokua kikiwanyemelea, wala wasingenyanyua vinywa vyao kupiga vigeregere. Lakini nd’o hivyo tena hakuna aijuaye kesho hata mtunzi wa kalenda.



    Baada tu ya Bi Masonganya kukata roho, muda huohuo hali ya hewa ikabidilika tena, mwanga ukarejea na upepo ukatulia kiasi cha kuwastaajabisha wakazi wa Kibondo.



    ***



    Sifa kubwa ya Bi Masonganya ilikuwa ni uchawi. Uchawi uliokubuhu, aliorithishwa na marehemu bibi yake mzaa mama ambaye kwa asili ni mtu kutoka Kongo. Uchawi huo ulimfanya Bi Masonganya aheshimike na kuogopwa karibu na kila mtu. Wapo aliowaangamiza kutokana na uchawi wake, na wapo aliowasaidia, lakini mchawi ni mchawi tu hana muamana asilani.



    Ilikuwa Bi Masonganya akaikwambia kuwa hautoliona jua la jioni basi kimbia haraka ukamtake radhi, vinginevyo utakufa kweli. Na hata uwe na kesi ya namna gani endapo utamfuata kumtaka msaada na akaamua kuivalia njuga basi piga geuza utashinda tu. Mpaka viongozi wakubwa serikalini wanaouhusudu ushirikina huwasili kwa Bi Masonganya kufanyiwa ndumba.



    Kuna madhila yaliwahi kumpata Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili mjukuu wa Bi Masonganya aitwaye Ndoza, hiyo nayo ikawa ni historia ya kushangaza na kusikitisha! Ni kweli Ndoza alibaka haswa tena saa saba mchana watu wakishuhudia dhahiri akimng’ang’ania binti wa watu aliyekuwa akipita na safari zake, akamvutia kwenye pagara lilikouwa jirani na kumfanyia ushenzi. Sasa kesi ilipoonesha dalili zote za kumuelemea Ndoza, ndipo Bi Masonganya akaibuka na kuikingia kifua. Akamfuata jaji, akamkanya kwa maneno makali ya vitisho kuwa endapo ataendelea na mpango wake wa kutaka kumfunga jela mjukuu wake basi atakiona kilichomfanya kuku aanze kuota manyoa mkiani…Jaji akapuuza, pengine kwakuwa naye alikuwa amejiganga.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ya hukumu sasa Jaji akiwa anaingia mahakamani baada ya umati kufurika ndipo ghafla walipoibuka nyuki hata wasijulikane walipotokea, ikawa ni patashika ya nguo kuchanika kila mmoja akitafuta njia yake. Kama Nyuki nao huwa na kichaa, basi hawa nao walihitaji chanjo. Walikua wanauma ovyoovyo, na wakikuuma, hayo maumivu yake ni kama umegongwa na koboko.



    Matokeo ya hila za nyuki wale ni pamoja na mafaili yote yaliyobeba kesi ya Ndoza kupotea japo hilo halikuwa kubwa sana. Lililoshitua zaidi ni kitendo cha wale nyuki kumfakamia Jaji licha ya kelele za kutaka msaada alizokuwa akipiga bila mafanikio mpaka walipomtoa roho.



    Kifo cha Jaji kwa kuumwa na nyuki mahakamani kikazagaa kama moto wa pumba, huku kila mmoja akijifanya ni fanani wa mkasa ule.



    Kesi ya ndoza ikatulia kama maji ya mtungi



    Kama ilivyo kawaida ya mawingu, huwa hayatandi milele…kuna siku husambazwa na kutawanywa kwa upepo! Na hivyo ndivyo habari ile ya kifo cha Jaji ilivyosahaulika na kisha baadaye ikapangwa tena upya tarehe ya kuendelea kwa kesi ya ubakaji inayomkabili Ndoza na kukabidhiwa kwa Jaji mwingine.



    Huyu sasa naona alikuwa mwepesi kama tishu maana kazi ya Bi Masonganya ilikuwa ni kama kupuliza kibatali tu na kukizima kabisa. Ilitokea kama maskhara tu, siku ya hukumu Jaji akiwa anatoka nyumbani kwake, kwa bahati mbaya akajikwaa na kuanguka mpaka chini, hakuinuka akiwa hai bali alinyanyuliwa na kubebwa akiwa maiti!



    Wakati huohuo Jaji anaanguka, binti aliyebakwa na Ndoza naye alijikwaa kama ilivyokuwa kwa Jaji! Na wakati maiti ya Jaji inanyanyulia, na ya binti yule naye ilinyanyuliwa tokea pale alipoangukia. Vifo viwili, vilivyofanana japo vimetokea sehemu tofauti kwa watu wanaohusika na kesi moja vilizua gumzo mjini Kibondo…kesi hata ilkopotelea!



    Unadhani Jaji gani asiyependa kuishi?



    Yapo mengi ya kumhusu Bi Masonganya, hata humohumo kwenye ukoo wake mbali ya kuwasaidia pindi wapatwapo na matatizo, pia ameshawamaliza sana watoto na wajukuu kwa kuwachukua kichawi.



    Mbali ya vimbwanga hivyo vya uchawi, pia inasemekana Bi Masonganya alipata kumeza ‘mpigi’. Mpigi ni dawa ya mtishamba ambayo ukiimeza basi haufi kirahisi mpaka utapishwe kwanza dawa hiyo, vinginevyo utazeeka mpaka ubakie kama mzoga huku ukiwa hai.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sasa tayari Bi Masonganya alikuwa amekwishazeeka kiasi hata cha kushindwa hata kutembea mwenyewe, na kuwafanya wajukuu zake kuwa wanamtoa nje kumuanika mara mojamoja…na siku akitolewa kuanikwa, utafikiri alikuwa akitoa sumu angani maana kama kuna wagonjwa au watoto wadogo maeneo ya jirani, basi siku hiyo watashinda ovyoovyo tu wakiwa ta’abani mpaka Bi Masonganya atakaporejeshwa ndani.



    Hata yeye mwenyewe Bi Masonganya alitamani sana tu kufa sasa ili akapumzike kama kweli atapata nafasi hiyo, lakini inasemekana kabla hajaitapika ile ‘mpigi’ pia kuna fununu kwa nduguze kuwa alitaka kwanza aache amemrithisha mtu mmoja uchawi wake wote kabla hajafa…hilo nd’o lililowagutua wana-ukoo na kuamua kumsaidia kufa mapema kabla hajarithishwa mtu mwingine huo mzigo wa ulozi. Ndipo akaitwa mtaalamu ambaye aliusuka mpango mzima wa kumuondoa duniani bi mkubwa yule. Hivyo ule mwichi uliokitwa chini ya ukuta baada ya maneno yale ya kimila yaliyofuatiwa na chafya ya bila kunusa ugoro ulikuwa nd’o pigo la mwisho la kummaliza, na kweli wakammaliza…sasa kwanini wasipige vigeregere?



    Ambacho hawakukikumbuka ni kimoja tu, kwamba Bi Masonganya amekufa na ‘mpigi’ yake kifuani…hawakuijua hekaheka yake.



    ***



    Baaada ya taarifa kusambaa kila kona kuwa Bi Masonganya amefariki, kila mmoja alifurahi. Ndugu kutoka sehemu mbalimbali wakajumuika kwa ajili ya maziko. Ulikuwa ni msiba wa kimila zaidi, wafiwa wote walipakwa pemba usoni na ilikuwa ni marufuku kwa mfiwa yeyote kulia. Na katika kipindi chote maiti ikiwa ndani, palikuwa na ngoma maalum ikipigwa taratibu bila kuzimwa, endapo mpigaji wa ngoma akichoka basi anampasia aliye jirani yake naye anaendelea kuipiga mpaka atakapochoka na kumpa mwingine aendeleze.



    Siku ya maziko ilipowadia ndipo kikaibuka kizaazaa kipya, ndugu walipoingia chumbani ili kuubeba mwili wa marehemu, wakaikuta maiti ikiwa imefumbua macho!



    TOBAA!



    Ilikuwa ni mpishempishe kila mmoja akigombea mlango wa kutokea…ilikuwa ni hali ya ajabu na kuogofya japo kwa wajuvi wa mambo waliitegemea hali ile.



    “Hebu kaeni chini tusikilizane…” aliongea mzee mmoja aliyetapakaa mvi karibu robo tatu ya kichwa chake. Mzee huyo ni kaka wa Bi Masonganya aitwaye mzee Mtandi bin Kalukalange. Umati ukamsogelea na kumsikiliza, kisha akaendelea “…Iko hivi, haya ni mambo makubwa lakini ni ya kawaida hasa anapokufa kiongozi mkubwa wa kimila kama Bi Masonganya…hivyo kuna mambo yanarekebishwa na wakubwa kisha kila kitu kitatengemaa na sote tutakwenda malaloni kumsitiri bi mkubwa, cha msingi ni utulivu wenu tu.” Akamaliza kuzungumza babu yule.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni mambo gani hayo yanayorekebishwa na wakubwa huko ndani?” Aliuliza mmoja wa majirani waliojumuika msibani pale “…Na ni wakubwa gani hao?” akaongezea huku akimtazama jirani mwenziye.



    “Mtoto yasiyokuhusu waachie baba na…”



    “Na mama..” Wakaachia kicheko cha kimbea kilichokatizwa na majibu ya swali lao kutoka kwa Bi mkubwa mmoja aliyebarizi pembezoni mwa mpera.



    “Kuna kitu alimeza kitambo kirefu sana, hivyo bila ya kutapishwa itakuwa kama mchezo…atafumbua macho kila atakapokaribia kupelekwa kuzikwa, na hao wakubwa waliotajwa ni wachawi magwiji nd’o wanasubiriwa kama wataweza kumtapisha!”



    “Heh…makubwa!”



    “…madogo yana nafuu.”



    “Hivi kuna gwiji wa uchawi kuliko Bi Masonganya?”



    “Avumaye baharini ni Papa, na wengine pia wamo…magwiji wapo japo hawajavuma kama yeye!”



    “Sasa je kama watamzika hivyohivyo akiwa macho itakuwaje?” mpambe mwingine alisaili.



    “unataka wapitiane ukoo mzima kama kuku wenye mdondo? Chezea wachawi wewe!”



    “Na ikitokezea hao magwiji wakashindwa kumtapisha, itakuwaje jamani?”



    “Hapo nd’o watakapocheza naye makida.”



    Saa moja baadaye, aliwasili Bi Kibena akitokea maeneo ya Kakonko. Huyu alitumainiwa kuwa angeweza kumtapisha Bi Masonganya ile ‘mpigi’ aliyomeza ili akazikwe maana Bi Kibena naye ni kiboko kwa uchawi. Baada ya kusalimiana na wafiwa aliingia mpaka chumbani ilipolala maiti na kuwaamuru watu wote watoke nje, walipotoka tu akaanza vimbwanga vyake!



    Laahaullah!



    Kilichomkuta Bi Kibena alikijua yeye na Mungu wake, watu walisikia kukurukakara ya haja ikiendelea mle chumbani mpaka ikabidi wafungue haraka mlango. Ndipo wakamkuta bi kibena akiwa kama mchawi aliyeenda kucheza mahepe kwenye nyumba iliyozindikwa na hatimaye akaya-bhula…haja kubwa na ndogo vilihitimisha kifo cha bi Kibena alipofikishwa nyumbani kwake!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Jamani ndugu wafiwa na majirani, maziko yameakhirishwa mpaka hapo mtakapotangaziwa vinginevyo.” Sauti ya Mzee Mtandi ambaye ndiye msimamizi wa msiba ilihitimisha na watu wote kusambaa.



    Kifo cha Bi Masonganya kilijizolea umaarufu kutoka kila pembe ya mkoa wa Kigoma huku kila mmoja akiwana mshawasha wa kutaka kujua nini hatma yake…ikawa kama mchezo sasa, haipiti japo saa moja bila ya Bi Masonganya kufumbua macho japo vipimo vyote vya waganga na hata madaktari wa kawaida walioshirikishwa vilionesha kuwa amekwishafariki.



    Zikapita takribani siku tatu bila ya mwili wa Bi Masonganya kuzikwa, huku ndugu wakiswampa kila uchao kutafuta waganga wa kulitatua tatizo lililoikumba familia yao, kila mganga aliyefuatwa alipokaribia tu na nyumba ilimo maiti aliishia nje na kuingia mitini! Haikuwa kazi rahisi.



    Siku ya tano, mwili wa marehemu ukiwa umekwishaanza kutahayari ndipo wana-ukoo walipofanikiwa kumpata mganga maeneo ya vijiji vya mbali kidogo tokea Kibondo mjini.



    Ilichukuwa karibu saa saba kutokea huko vijini kwa mwendo wa gari mpaka kufika hapo Kibondo mjini. Wakiwa bado hawajafika nyumbani ulipo msiba ghafla mkwara wa Babu-mganga ukaanza, akapandisha mashetani yake kichwani na kuanza kufanya vurugu kubwa ndani ya gari. Alipotulia akamuamuru dereva asimamishe gari kisha yeye akashuka na kikapu chake kichafu na kilichochakaa kama nguo zake alizozivaa…wafiwa waliomuendea nao wakashuka.



    “Vipi babu?”



    “Mizimu imenikatalia kwenda kwa gari huko nyumbani kwenu…yaonekana huyo aliyekufa hakuwa mtu wa kawaida asilani.” Wafiwa wakaangaliana, kisha mmoja akamsaili tena.



    “Kwahiyo tunafanyaje?”



    “Hakuna cha tunafanyaje hapa…twendeni kwa miguu tu!”



    Haikuwa mbali sana na nyumba, hivyo walitembea kwa karibu nusu saa wakawasili na kupokelewa na ndugu na majirani walioanza kufurika.



    “Jamani mi’ si mkaaji hapa…” alianza kuongea mganga. “…nataka kufanya kazi yangu haraka iwezekanavyo ili niondoke zangu.”



    “Sawa babu karibu ndani,” Alijibu mtoto wa kiume wa marehemu huku akifungua mlango mkubwa wa mbele na kumpisha Babu-mganga aingie ndani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana mi’ sipitii mlangoni, naomba mniruhusu nipande juu ya bati la nyumba yenu kisha nipitie huko kwa juu.”



    Heh!



    “Sasa utapitiaje kwa juu babu?”



    “N’tafumua bati pamoja na singibodi kama iko kisha n’taibukia chumbani kwa mtuhumiwa wenu.”Ilikuwa ni mzaha mwingine msibani hapo, ila kwakuwa walikuwa wanashida wakamkubalia, Babu akapanda juu ya nyumba huku watu wakimshangaa na baadhi ya wafiwa wakitangulia chumba chenye maiti.



    Watu walimshuhudia babu akipanda mpaka juu na kufumua bati kisha akidumbukia kwa ndani kiasi cha kuachia kishindo kizito…nyumba nzima ikatulia, walio nje wakisubiri taarifa ya kitakachojiri huko chumbani.



    Zilipita dakika takribani thelathini nyumba ikiwa kimya kila mmoja akijiandaa kutimua mbio endapo maiti itazua songombingo. Haikuwa hivyo,badala yake zilisikika sauti za vigeregere na shangwe kutokea chumbani, ikiwa ni ishara ya kazi kukamilika. Bi Masonganya alitapishwa mpigi yake.



    Haikuchukuwa muda mrefu Babu akatoka akiwa na kikapu chake mkononi akifuatiwa na wafiwa. Akaaga na kuondoka zake.



    Bi Masonganya akaandaliwa na kwenda kuzikwa kimila, akiwa ameviringishwa ndani ya ngozi ya Ng’ombe mweusi.



    Msiba ukaisha.



    Majirani wakasambaa, na wafiwa wakarejea kwao kumalizia siku tatu zamsiba kabla na wao hawajasambaana!



    ***



    “Mamaa…mamaa.” Kaguba alikuwa akimgasi kwa kumuita mama yake wakati kikao cha kumalizia msiba wa Bi Masonganya kikiendelea. Kaguba ni mjukuu wa marehemu Bi Masonganya, mtoto wa kike wa mwanaye wa pili kutoka mwisho.

    “Mamaaa…mama.” Kaguba aliendelea kumgasi mama yake aliyekuwa amempakata miguuni. Mama Kaguba alimpuuza mwanaye akiamini hana jipya pengine na umri wake kuwa mdogo. Kaguba alikuwa ni mtoto wa miaka takribani minne tu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mama ujue mi’ n’namuonea huruma sana ma’mdogo Nyanzala,” alisema Kaguba na kufanya kikao kipige kimya kidogo huku watu wote wakimuangalia kama kituko vile kwa ile kauli yake aliyoitoa baada ya kuona mama yake hamjibu chochote akiendelea kufuatilia kikao. Wakajikuta wote wamecheka!



    “Unamuonea huruma ya nini mama?” Mama Kaguba alimuuliza kimzaha Kaguba wake huku wengine wakimsikiliza.



    “Hivi kwanini sasa ma’mdogo Nyanzala alikubali kupiga mwichi chini ya ukuta ili amuue bibi?” alisaili mtoto Kaguba na kuwaacha midomo wazi wote mle ndani.



    Haikuwa jambo la kawaida kwa mtoto mdogo wa umri wa Kaguba kutambua jambo lile lililofanyika kisiri. Na hata wakati yote hayo yalipokuwa yakitendeka yeye(Kaguba) alikuwa uani huko akicheza na wenziye, sasa ameyajuaje haya.



    “Shauri yenu, mjue wamekasirika sana huko.” Kaguba aliropoka tena.



    Ama!



    “We’ Kaguba, akina nani hao wamekasirika? amekwambia maneno hayo?” Mzee Mtandi ambaye ni kaka wa marehemu alimsaili mjukuu wake kwa kihoro kikubwa.



    “Eeenh…nyie ngojeni tu! Kesho mtaona tu ma’mdogo Nyanzala naye anakufa!”



    SEHEMU YA PILI



    Ukumbi mzima ulizizima kwa hofu na mashaka. Hali ile haikuwa ya kawaida hata kidogo. Walipojaribu kumdodosa Kaguba wao tena hakuendelea kusema chochote cha maana zaidi ya kubwabwaja maneno yasiyo na maana yoyote, maneno ya kitoto tu!



    Raha ikawaisha, kikao kikafa kimyakimya!



    Nyanzala alichanganyikiwa maradufu, hofu kuu ilimvaa, mishipa ya shingo ikawa inampwita kama moyo wa chura. Kila mara alikuwa akilia tu akihofia kifo alichobashiriwa na mtoto wa dada yake. Ndugu walijaribu kumfariji na kumsihi kuwa yale yalikuwa ni maneno ya mtoto tu ambaye pengine ilitokezea akawasikia wakiongelea juu ya mpango wao huo. Haikumuingia akilini kamwe!



    Siku hiyo walishinda ovyoovyo tu, chakula hakikulika. Hatimaye usiku ukaingia na kuzidisha simanzi kwa wanafamilia. Nyanzala akiogopa kufa, mama Kaguba naye akiogopa hata kulala na mwanaye, huku ndugu wengine wakihofia balaa inayotaka kuukumba ukoo wao. Usingizi ukaota mbawa. Lakini hali hiyo ya mang’amng’am iliduma kwa muda tu. Baadaye usingizi ukawapitia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku hiyo usingizi ulikuwa mzito kwa karibu kila mmoja wa wanafamilia wale, kama ungebahatika kukatiza nje ya nyumba yao kwa usiku ule, ungedhani kuna helkopta zinajiandaa kuruka kwa jinsi walivyokua wakikoroma. Walilala fofofo!



    Kilichowashitua asubuhi na mapema ni TANZIA(Tangazo la kifo) iliyokuwa ikinadiwa kutoka katika spika kubwa za msikitini. Haikuwa jambo la ajabu sana kusikia Tanzia kutoka katika spika za msikitini maana huo ni utaratibu wa kawaida kwa waumini wa dini zote kubwa kupashania habari kupitia spika hizo bila kujali tofauti ya dini zao, ila hii ilikuwa ni taarifa ya kushitua kwao.



    “…ifuatayo ni Tanzia, familia ya hayati Bi Masonganya wa kilogho, Kibondo inasikitika kutangaza kifo cha mtoto wao, Bi Nyazala. Kilichotokea usiku wa kuamkia leo…maziko yatafanyika leo saa kumi Alasiri.” Sehemu ya Tanzia hiyo ilisikika ikinadi.



    Heeh!



    Nyanzala amekufa?



    Familia nzima ilikumbwa na mshituko na woga kutokana na tangazo hilo. ukizingatia kuna hadhari ambayo ilikuwa ni kama Tanzia kabla ya tukio waliyopewa na mtoto Kaguba na sasa kimeibuka kioja kipya kwamba tangazo limenadiwa kuhusu kifo cha Nyanzala bila ya hata wao kama ndugu na wahusikawa karibu kujua lolote!



    “Mama Kaguba…” Aliita Mzee Mtandi kwa sauti ya mashaka na wahka. “…Mama Kagubaaa..” aliita tena Mzee yule kutokea chumbani kwake.



    “Abee Mjomba,” Alijibu Mama Kaguba.



    “Umesikia hilo Tangazo la kifo?”



    “Kumbe nawe’ umelisikia?” Jibu hilo la mama Kaguba liliwafanya familia nzima ishituke, kumbe kila mmoja kutokea chumbani kwake alilisikia vyema Tangazo lile. Wote wakatoka wakiwa bado na mang’amng’am ya usingizi mpaka sebuleni, wakautwaa mlango wa chumba cha Nyanzala na kuugonga zaidi ya mara tatu bila kujibiwa.



    Hofu ikiwazidia!



    Hapakuwa na la ziada, wakauvunja mlango kisha wote wakakivamia kitanda cha Nyanzala na kumkuta akiwa amejilaza kiubavu huku roho ikionesha dalili kuwa iliuacha mwili ule karibu hata saa tano mbele. Alitulia tuli akiwa amepoa kabisa!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Vilio vikalipuka. Ndugu walilia kwa maombolezo na vihoro vya hali ya juu, hakika msiba ule wa maajabu uliwaumiza sana.



    Haya sasa Nyanzala ni kweli amekwishaaga dunia lakini sasa kwanini kifo chake kilibashiriwa na mtoto mdogo Kaguba? Na kwanini Tangazo la kifo(Tanzia) linadiwe huko kwenye vipaza sauti ilhali wao kama wanafamilia waliolala naye nyumba moja wakiwa hawajapata taarifa ya kifo hicho? Maana kwa kawaida wao kama ndugu ndiyo walipaswa kupeleka taarifa za msiba wao msikitini ili watangaziwe watu…hapakuwa na majibu ya kutosha zaidi vilio vikali vilivyogubikwa na hofu na mashaka.



    Majirani kama ilivyo kawaida yao wakajaa tele kama pishi la mchele wakishirikiana bega kwa bega mpaka walipohitimisha safari ya mwisho ya Nyanzala. Familia ilijitahidi kuficha ukweli uliokigubika kifo kile kuwa ulibashiriwa na Kaguba, ila hawakuwa wapuuzi wa kulipuuzia jambo lile zito. Wakaendelea kumuandama kwa maswali Kaguba huku wakimtishia kumchapa viboko lakini walaa hakusema lolote la maana, ni kama hakuwa yeye aliyeropoka maneno mazito juzi yake tu. Na hata walipowakabili viongozi wa msikitini kuhusu ni nani aliyepeleka tangazo lile bila ya wao kuhusika? Majibu yalizidi kutatanisha, hata wao hawakumjua aliyetangaza maana japo walikuwa wameufunga msikiti lakini waliweza kusikia tangazo hilo likitokea katika spika hizo…na kweli sauti ya aliyetangaza haikuwa ile ya siku zote.



    Utata!



    Hatimaye katika hali hiyohiyo ya sintofaamu, Nyanzala akazikwa…na shughuli za msiba zikaendelea kama ilivyo ada.



    “Ebyomunyumba tebi totolwa!” Mzee Mtandi aliwasihi wanawe kwa lugha ya Kinyankole. Wote walimuelewa kwakuwa alipendelea sana kulitumia neno hilo kwenye muktadha wa namna ile. Msemo huo ulimaanisha kwamba ‘Ya vyumbani, hayajadiliwi hadharani.’ Hivyo siri zilizogubika kifo hicho wasiweke hadharani.



    ***



    Siku moja ndugu kadhaa wa familia ya Bi Masonganya wakiwa wameketi nje ya nyumba yao kwa upande wa barabarani huku wengine wakiwa wameketi juu ya viti na wengine juu ya daraja kubwa la maji linalotenganisha nyumba na barabara kubwa, ikiwa ni siku kadhaa tangu wamalize msiba wa ndugu yao kipenzi, ndipo wakasikia sauti iliyowashitua sana…sauti ya mwanamke anayeonekana kuchoka sana.



    “Uuuh…uuh ja-maaa-ni ni-sa-me-he-ni, msi-ni-pi-ge…nipelekeni taratibu.” Ilikuwa ni sauti waliyoifahamu fika, sauti ya ndugu yao kipenzi hayati Nyanzala. Sauti hiyo ya kulalamika kutoka kwa Nyanzala ilitokea usawa wa chini ya lile daraja kubwa walilokuwa wameketi juu yake huku wamening’iniza miguu yao kwa starehe. Wakiwa wameduwaa ndipo tena ikafuatia sauti nyingine wasiyoifahamu ikimkemea Nyanzala kwa ghadhabu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tulia mbwa we’.. tembea haraka…” Sauti hiyo ilifuatiwa na milio ya mijeredi ya nguvu kama kuna ng’ombe au punda anayeadhibiwa.



    “Uwiiii…naku-faa.. jamani mtaniua, nioneeni huruma jamani.” Baada ya hapo familia nzima ilipitiana mieleka, wa huku, kule! Na wakule huko! Wote wakigombea mlango ili waingie ndani. Hakika hofu iliwavaa.



    Yaani wamemsikia hivihivi ndugu yao waliokwishamzika, akilia kwa uchungu huku akiteswa sana, hakika siku iliwaharibikia. Kilio kikaanza upya, hata wanaume walishindwa kujizuia nao wakawa wanalia. Inaonekana hao wanaomtesa Nyanzala waliamua kwa makusudi kabisa kuja kumtesa mbele yao wakiwaoneshea umwamba wao. Hawakua na la kufanya, wakanyamazishana na kwenda kulala! Vitanda vilikuwa vichungu.



    ***



    “Heeh! NYA-NZALA?” Mama Kaguba aliyekuwa akipika uani alihamaki baada ya kumuona Nyazala akiingia mle uani akiwa mchovu, mchafu, hoi bin ta’aaban.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog