Search This Blog

TANZIA - 2

 





    Simulizi : Tanzia

    Sehemu Ya Pili (2)



    Yaani wamemsikia hivihivi ndugu yao waliokwishamzika, akilia kwa uchungu huku akiteswa sana, hakika siku iliwaharibikia. Kilio kikaanza upya, hata wanaume walishindwa kujizuia nao wakawa wanalia. Inaonekana hao wanaomtesa Nyanzala waliamua kwa makusudi kabisa kuja kumtesa mbele yao wakiwaoneshea umwamba wao. Hawakua na la kufanya, wakanyamazishana na kwenda kulala! Vitanda vilikuwa vichungu.



    ***



    “Heeh! NYA-NZALA?” Mama Kaguba aliyekuwa akipika uani alihamaki baada ya kumuona Nyazala akiingia mle uani akiwa mchovu, mchafu, hoi bin ta’aaban.



    “Abee dada.”



    “Ni wewe kweli?”



    “Ni mimi dada yangu, nimepigwa sana, hapa sina hali.”



    “Enhee Ulikuwa wapi kwanza? Na ninani huyo aliykupiga hivi? Mbona umeumia hivi jamani mdogo wangu?” Maswali mfululizo yalimtoka mama Kaguba.



    “Nilichukuliwa kwa Binti Sambayu nd’o nimewekwa huko, napigwa sana na kupewa kila aina ya mateso!”



    “Heeh! Binti Sambayu?” Mama Kaguba alishangaa kusikia kumbe siku zote zile Nyanzala alikuwa kwa Binti Sambayu japo hakuelewa kuwa kwanini Bi mkubwa yule amchukue ndugu yao na kumtesa vile. Binti Sambayu ni mdogo’ake na hayati Bi Kibena, yule mchawi aliyeshindwa kumtapisha mpigi hayati Bi Masonganya mpaka naye kifo cha kidhalili kikamkumba.



    “Sasa kwanini anakutesa kiasi hiki?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Anasema kuwa mi’ nisingeshiriki kumuua Bi Masonganya nisingesababisha ndugu yake akafa kifo cha fadhaa namna ile hivyo anamalizia hasira zake kwangu…sasa leo kuna kazi alinipa ya kufyeka ile michongoma inayozunguka nyumba yake, nilipofika karibu na kule chooni kwake nikaangusha upanga niliokuwa nikiutumia kufyekea majani, nilipouangalia chini sikuuona kabisa ndipo akaja yeye mwenyewe na kuanza kunipiga sana na kunichoma na vijinga vya moto…akaniambia niondoke haraka nije kuwaambieni kuwa anataka upanga wake hivyo ninyi mumlipe Laa sivyo atanitesa sana na hata ikibidi kumuua mtu mwingine humu ndani.” Nyanzala alikuwa akiongea huku akilia kiasi cha kumfanya mama Kaguba naye alie sana kwa uchungu wa mdogo’ake.



    “Sasa mbona umevaa ndala mguu mmoja?” Mama Kaguba alimsaili mdogo wake baada ya kumtupia jicho mguuni.



    “Wakati nakimbia kipigo cha Binti Sambayu nd’o nikaangusha ndala moja kulekule nyumbani kwake, nyuma ya choo nilipokuwa nikifyeka michongoma yake…Dada acha mimi niondoke nisije kufuatwa tena huku ikawa balaa jingine.”



    “HA-PA-NA Nyanzala, usiondoke tafadhali,watakuua huko mdogo’angu..” Kabla mama Kaguba hajamilizia sentensi yake, tayari Nyanzala alikwishatoweka mbele ya upeo wa macho yake.



    “NOOO, NYANZALAAAAAA, USIENDE HUKOOOO.”



    Sauti kali aliyoitoa mama Kaguma nd’o ikamtoa usingizini, na kujikuta akiwa kitanda amelala. Kumbe ilikuwa ni ndoto tu.



    Sauti yake hiyo iliwafanya karibu nyumba nzima washituke, wote wakihamaki kumsikia ndugu yao akiweweseka kwa kumtaja marehemu. Wakamkimbilia chumbani mwake ambapo walimkuta ameketi juu ya kitanda, akihema kwa kasi sana kama aliyekimbizwa.



    “Nini tena mama Kaguba?” alisaili dada yake na mama Kaguba.



    “Nimeota Ndoto…mbaya sana!”



    “Ndoto gani hiyo?” Kabla mama Kaguba hajaanza kusimulia ndoto yenyewe. Ndipo Kaguba aliyekuwa ameshaamka akaingilia kati kama kawaida yake.



    “Halafu huyu ma’mdogo Nyanzala tatizo lake ni kiburi sana, shauri yake watamuua bure…ye’ ameambiwa awaambie tu mumlipie upanga wa watu alioupoteza halafu ye’ anakuja kusema mpaka hayo mambo mengine ya kuteswa na Bi Kibena. Wakimsikia shauri yake tuu.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Laah!



    Damu zikawasisimka wote mle chumbani, hakuna aliyeamini kusikia tena maneno ya mtoto Kaguba. Ikabidi wamgeukie mama Kaguba aliyepigwa na Butwaa kuona mwanaye anasimulia kitu ambacho amekiota yeye. Hapo ndipo akajua kuwa ile haikuwa ndoto ya kawaida na pia sasa ikazidi kuwadhihirikia kuwa Kaguba si mtu kawaida. Kwa hofu na kihoro cha hali ya juuakaanza kuwasimulia ndoto aliyoota, kila moja alihisi mwili ukimfa ganzi kwa woga.



    Hapakulalika tena mapa kulipopambazuka.



    Walijaribu kumbana sana Kaguba bila mafanikio. Walipoona jitihada zao zimeshindikana ndipo wakakubaliana watafute mganga awasaidie.



    “Jamani pamoja na kuwa mmependekeza kuwa twende kwa waganga ila mi’nina rai moja…” alinena Mzee Mtandi. “…Tusilikalie kimya jambo hili la kuteswakwa ndugu yenu…”



    “Mjomba, si nd’o tunataka kumleta mganga kwakuwa hatujakubali kulikalia kimya hili!” alijibu kwa haraka bwana Kungurume, mtoto wa kiume wa hayati Bi Masonganya.



    “Sina maana hiyo…” wote wakamgeukia mjomba wao ili wajue ni nini azma yake hasa. “…nashauri asubuhi hii tukanunue upanga mpya kisha tumfuate bila uoga huyo binti Sambayu tukamkabidhi ili aache kumtesa mtoto wetu.”



    “Aah mjomba hiyo haiwezakani kabisa, hivi hata huyo bibi si atatushangaa kuyabeba mambo ya kwenye ndoto halafu tukampelekee yeye!” Alipinga Kungurume.



    “Na tutanzia wapi sasa kufanya hivyo jamani? Tutaonekana vituko..” Aliongezea Kabinga, mjukuu wa hayati Masonganya.



    “Mnaona haiwezekani eeh? Lakini nachowaambieni mimi ni kwamba hii siyo ndoto ya kawaida bali ni ujumbe maalumu tuliotumiwa na kama mko radhi kuona ndugu yenu anaadhirika kila siku haya shauri yenu…mi’ mwenzenu nimekuwa zamani nimeona mambo mengi sana. Waswahili wanasema Awashwaye, ndiye ajikunaye…ni lazima tujikune wenyewe!” Rai hiyo ilikuwa ngumu sana ila baada ya majadiliano ya kina, na kutokana na heshma na imani waliyonayo wanafamilia kwa mjomba na babu yao mzee Mtandi, waliafikiana.



    ***

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nje ya nyumba ya Binti Sambayu walisimama watu watatu; Mama Kaguba, Mzee Saadallah, na Kungurume wakiwa na upanga wao mkononi. Ila kabla hawajaingia wakawa wanastaajabu kuona ni kweli michongoma ilikuwa inaonekana kufyekwa siku si nyingi,bila shaka nd’o kazi aliyokuwa akiifanya Nyanzala.



    Roho ziliwachinyota sanakwa uchungu.



    Wakapatwa na wazo jipya, kabla ya kuingia ndani wakazunguka nyuma ya choo walipotajiwa na Nyanza kupitia ndoto ya mama Kaguba.



    Hamaad!



    Wakaikuta ile ndala moja ya mguu wa kushoto ambayo ya kulia yake ilikuwa imevaliwa na Nyanzala kule ndotoni. Kufikia hapo sasa hawakuwa na pingamizi kuwa Nyanzala hakufa kamwe, na kwamba anateswa na Bi mkubwa yule.



    Wakabisha hodibaada ya kuutwaa mlangowa kuingilia ndani kwa Binti Sambayu, wakakaribishwa na kuingia ndani. Wakamkuta Bi mkubwa yule mweusi kama pampu mpya akiwa ametuna juu ya kiti cha uvivu akiwa ameliatamia jiko lake la mkaa akiota moto licha ya joto kali lililotamalaki karibu Kibodo nzima.Kwa jinsi alivyousokota uso wake kwa ghadhabu na ule mdomo alivyouvuta kama Ndomolomo hakika kama ungepata nafasi ya kumtupia jicho mara moja, usingekuwa na hamu ya kumtazama kwa mara ya pili.



    Wakamsalimu na kuketi.



    “Mama siye tumekuja tunaomba utupokee, na tunaomba utuwie radhi kwa hili kama tutakosea. Tumepoea salamu zako kutoka kwa Nyanzala kuwa kuna upanga wako aliupoteza hivyo unamuadhibu sana…tumeleta upanga mpya, tunaomba sana mama yetu uupokee na umpe ahueni binti huyo ili apumzike japo kidogo.” Mzee Mtandi aliongea kwa niaba ya wenziye.



    Kikapita kimya cha kama dakika moja hivi! Mzee Mtandi akainuka na kumkabidhi Binti Sambayu upanga ule mpya.



    Bila aibu wa soni, Binti Sambayu akaupokea upanga ule kisha akainuka na kuelekea naousawa wa chumba chake ambacho kimefunikwa gunia zito kama nd’o pazia. Akapotelea humo.



    “NIMEWAELEWA, MNAWEZA KWENDA.” Sauti kali ya binti Sambayu ikitokea kule chumbani iliwaijia mpaka pale sebuleni walipoketi. Wakatazamana kisha Mzee Mtandi akajibu kwa nidhamu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ahsante bi mkubwa, tunakwenda.” Hawakujibiwa.



    Wakasimama na kuondoka kimyakimya mpaka nyumbani kwao ambako walizua kilio kipya,hakika ilikuwa ni simanzi kubwa kwao.



    SEHEMU YA TATU



    Baada ya siku kadhaa kupita bila mauzauza yoyote kuwakuta ndipo wakaketi kikao tena ambapoKwa kauli moja wakaafikiana kuwa wamuendee Babu Gao, yule mganga bingwa aliyemtapisha ‘mpigi’ hayati Bi Masonganya. Wakajiteua baadhi na kumfuata Babu Gao ambaye aliwakubalia ombi lao la kwenda huko kwao. akawaahidi kuwa angekwenda kesho yake hivyo wao warejee tu Kibondo mjini.



    Ndugu waliokuwa wakiishi mbali na Kibondo walishindwa hata kuondoka tena kutokana na si tu vimbwanga vya mtoto wao, Kaguba bali msiba mpya wa ndugu yao Bi Nyanzala. Japo watoto wa mzee Mtandi waishio Kigoma, wao iliwabidi kuondoka kutokana na majukumu ya ajira zao. Wafiwa waliobaki wkiwa hapo nyumbani ndipo bingwa akawasili, Babu Gao akiwa na kilekile kikapu chake japo safari hii aliingilia mlangoni tofauti na awali.



    “Karibu sana bwana mkubwa!” Mzee Mtandi kama kiongozi wa familia alimkaribisha Babu Gao, wakati huo wanafamilia wote wakiwa wamejumuika pamoja hapo sebuleni.



    “Karibu…ahsante, karibu…ahsante,” alijibu Babu Gao kwa mkwara na mbwebwe za kiganga huku akitoa dawa zake na kuanza kumwaga huku na kule ikiwa kama ni kinga yake na familia yote katika muda atakaokuwa hapo.



    Baada ya utulivu, mzee Mtandi alitaka kutoa muhtasari wa kilichojiri hapo nyumbani lakini Babu Gao akamzuia na kuanza kuongea.



    “Kwanza poleni sana kwa msiba mpya na kila lililotokea…jana usiku sikulala kabisa ilinibidi kwanza niyaangalie haya mambo yenu kwa jicho la mwewe ili kabla ya kuja huku niwe ninajua cha kuwaelezeni…” alianza kutiririka Babu Gao. “…najua nyote mlifurahia kuwa Bi Masonganya amekufa akiwa hajamrithisha yeyote uchawi wake, hapo ndipo mlipokosea…alikwishamrithisha mtu siku nyingi, na mtu mwenyewe mwenyewe mnaye humuhumu ndani...” Wakatazamana wanafamilia kwa macho ya mashaka huku kila mmojaakimhisi mwenziye. Babu Gao akaendelea tena kufunguka. “Aliyerithishwa uchawi ni huyo mtoto wenu Kaguba!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Loohsalalee!



    “KA-GU-BA?...haiwezekani! amewezaje kumrithisha mtoto mdogo kama huyu?” alijibu kwa wahka na kihoro mama Kaguba.



    Ukumbi mzima ukatulia na kumtupia macho Babu Gao ili kumsikia akijibu swali pingamizi kutoka kwa mama Kaguba.



    “Hilo ni jambo la kawaida sana kwa wachawi wengi tu duniani kuwarithisha vitunga vyao watoto wadogo kutokana na ukubwa wa uchawi wenyewe…kama uchawi ni mzito sana hulazimika kumkabidhi mtoto mdogo kwakuwa hatoukataa, tofauti na mtu mzima ambaye anaweza kuogopa masharti yaliyomo ndani ya vitunga hivyo vizito vya uchawi…” Aliongea kwa utulivu mkubwa Babu Gao kisha akatulia ili maneno yake yakite katika vichwa ya wateja wake, halafu akaendelea tena “…Iko hivi kama kuna mchawi mkubwa katika ukoo na anataka kuurithisha kwa mtoto mdogo basi hufanya hivi…kila anapozaliwa mtoto ndani ya ukoo yeye hufika mapema akiwa na dawa fulani ya uchawi aliyoifunga kwenye pindo la kanga yake, kisha anapopata nafasi ya kukibeba kichanga hicho kuna jambo hufanyika hapo kisirisiri ila ya kuonekana na mtu…si mnajua mtoto akiwa mchanga, muda wote hukunja viganja vyake vya mikono kama aliyekunja ngumi eenh?” alisaili Babu Gao na kuitikiwa kwa vichwa tu wanafamilia waliokuwa wameingiwa na hofu, kisha akaendelea.“…Vizuri, sasa huyo mchawi humkunjua vidole mtoto huyo na kumwekea dawa hiyo na hapo ndipo miujiza hutokea…mtoto huyo yeye mwenyewe huukubali uchawi huo ama kuukataa!”



    “Kivipi mtoto mchanga asiyejua lolote akubali ama kukataa huo uchawi ambao kwanza hata haujui?” aliuliza Mzee Mtandi.



    “Swali zuri, sasa iko hivi endapo mtoto huyo ataukataa uchawi huo basi hutokea tu hatokifunga kiganja chake cha mkono baada ya kuwekea dawa na huyo mchawi…na hapo utamuona huyo mchawi akiwa amekasirika kabisa na huenda hata akaondoka na kumwacha mtoto akiumwa ovyo tu. Na endapo mtoto huyo ataukubali uchawi huo, basi atakapoachiwa tu mkono wake baada ya kukunjuliwa kiganja chake na kuwekewa ile dawa ya kichawi, hapohapo huukunja mkono wake na kuifumbata vizuri dawa ile ambayo hupotelea katikati ya kiganja chake…hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Kaguba alipozaliwa, baada ya kuupokea uchawi ule akawa ni miongoni mwao hivyo haikuwa taabu kwake kujifunza vitu vya jamii yake hiyo ya kichawi maana wahenga walinena;Kifaranga hakifunzwi kuchakura,” Alinena kwa utuo Babu Gao.



    Wanafamilia wakaanagaliana, hakuna aliyekuwa na cha kubisha maana ni kweli marehemu Bi Masonganya alikuwa akipenda sana kumtembelea mtoto wake yeyote punde tu mara baada ya kujifungua, na hata yeye mama Kaguba aishiye wilayani Kasulu alipojifungua huyo Kaguba wake, Bi Masonganya aliwasili huko na haraka aliwahi kumbeba mtoto yule kama ilivyo ada, hakuna aliyemzuia wala kumshitukia. Bila shaka hapo ndipo alipopata fursa ya kutenda huo ufedhuli wake!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Uchawi aliokabidhiwa huyu mtoto wenu ni mkubwa sana, hivi sasa yeye ndiye kiongozi mkuu wa wachawi wote wa ukanda huu wa magharibi licha ya umri wake huo mdogo…na ameshauwa watu wengi sana ambao hata mkitajiwa hamtoamini,na hata huyu aliyefariki juzi naye amemalizwa na mtoto wenu huyo kwa maelekezo au tuseme maombi aliypewa na mmoja kati ya watendaji wake wakubwa wa kichawi. Ila angalizo tu kwenu ni kwamba mtoto huyo bado ni mdogo sana asiyetambua lolote na anayeongozwa na kiini tu cha uchawi kilichomo ndani yake sasa mkimwendea vibaya kwanza hatowajibu lolote kwani kuna muda anakuwa na akili za kitoto kama walivyo watoto wengine na pia zitakapomjia akili zake za kichawi anaweza hata kuwateketeza nyumba nzima…” Babu Gao akiwa anaendelea kuongea, uzalendo ukamshinda mama Kaguba na kuanza kulia kwa uchungu na fadhaa! Ikaanzaa sasa kazi mpya ya kumbembeleza.



    “Hebu mleteni hapa huyo mtoto,” aliagiza Babu Gao, na hapohapo akatoka mtu mmoja mpaka uani walipokuwa wakicheza watoto wengi. Akamchukua Kaguba na kurejea ndani.



    Cha ajabu, Kaguba aliingia huku akirukaruka ki-mchezo kama wafanyavyo watoto, ila alipoingia tu mle sebuleni na kutupa macho yake kwa mganga, hapohapo akaanza kulia kwa hofu huku akitetemeka kwa woga.



    “Unalia nini sasa wewe?” Mzee Mtandi alimhoji Kaguba wakati alipofikishwa pale sebuleni.



    “Namuogopa huyo…naomba mnisamehe msinipige.” Kila mtu alielewa kuwa mtoto Kaguba ni mchawi na nd’o maana ameweza hata kumtambua mganga. Babu Gao hakuongea lolote, akaingiza mkono kwenye kile kikapu chake akatoa kitu kama kibuyu hivi akiwa amekizungushia shanga za rangi za njano, nyekundu na nyeusi…



    “Nami’ ninacho sasa ukileta mchezo nitakuua sasa hivi hapa, haya tueleze ukweli kwanini umemuua ma’mdogo Nyanzala?” Babu Gao alimfokea na kumtisha Kaguba.



    “Nisameheni Babu, mi’ nililazimishwa tu kumuua kwakuwa yeye ndiye aliyemuua Bibi!” Kaguba alijibu huku akilia kwa sauti yenye kitetemeshi cha uoga.



    “Ni kina nani hao walokulazimisha?”



    “Wale wachawi ninao waongozaga usiku nd’o waliniambia ni lazima tulipize kisasi!”



    “Umeshawaua watu wangapi?”



    “awwwh..niii.. ni wengi tu!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wataje haraka.”



    “Dada Shumbana, mjomba Makanya, kaka Ndugai, mjomba Zumbe, ma’mdogo Nyanzala na majirani”



    Balaa!



    Nyanzala, Makanya na Zumbe wote ni watoto wa marehemu Bi Masonganya, na Shumbana pamoja na Ndugai ni wajukuu waliofariki kwa awamu tofautitofauti katika mazingira ya kutatanisha!



    “Kwanini sasa huwa mnauwaua wenzenu hivi?”



    “Siye usiku huwa tunakula nyama za watu, kwahiyo ikifika zamu yetu ya kutoa chakula nd’o mimi na bibi tulikuwa tunamuua mtu mmoja kwa ajili ya kumla usiku, na wengine huwa hatuwaui ila tu tunawachukua kwa ajili ya kutufanyia kazi ngumu za usiku,” Alijibu Kaguba.



    “Tutawapataje hao watu uliowaua?”



    “Mnh…haiwezekani kuwatoa huko labda ma’mdogo Nyanzala tu nd’o bado hajakatwa ulimi, ila naye akikatwa hawezi tena kurudi huku.”



    Kimya kikapita.



    “Haya nenda ukacheze.” Babu Gao alimruhusu Kaguba atoke nje, na alipotoka tu Babu Gao akawageukia wanafamilia na kuwatupia swali.



    “Mmeamini jamani? Mmemsikia mwanenu wenyewe?”



    “Ndiyo Babu.”



    “Basi hiyo nd’o hali halisi…mtoto huyu ni hatari, kila siku usiku kabla hajatoka hutumia muda mwingi yeye na wenziye kuwachezeeni, hakika huwasumbueni sana…” hakuna aliyebishana na Babu maana ni kweli mara nyingi huamka wakiwa hoi kama waliotoka shamba kulima.



    “…Nimemaliza kazi yangu, naomba niondoke!”



    “Tunashukuru sana kwa msaada wako mkubwa uliotupa…” alianza kuongea Mzee Saadallah “…lakini tunakuomba sana utusaidie ili tulimalize tatizo hili kivyovyote maana sasa mbali ya kumpoteza huyu mtoto pia tunaweza hata kuangamizwa na hao wachawi ukoo mzima.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wanyankole wana msemo wao usemao ‘Omusote oguli muntamu’ yaani ‘Nyoka ndani ya mtungi wa Udongo’wakiwa na maana kwamba kumuua unataka lakini hautaki kuharibu mtungi wako wa udongo…mnataka kuutoa uchawi ndani ya nafsi ya Kaguba, lakini hamtaki kumdhuru. Jamani hili jambo siyo dogo kama mnavyodhani, wanaweza kufa wengi hapa kama umakini na hatua za makusudi zisipochukuliwa. Na hata kama tutafanikiwa kuutoa uchawi huo ndani yake bila kumdhuru ila mkumbue wahenga walinena ‘Chombo kilichopikiwa samaki, hakiachi kunuka uvumba’…” Alisema Babu Gao akiwa na maana kwamba hata kama watafanikiwa kuutoa uchawi ule ndani ya Kaguba,yawezekana akabakia nashombo ya uchawi huo. na kumalizia. “…Mimi kwa sasa sina msaada wowote kwenu ila inabidi niende kwanza kwangu nikaongee na mizimu yangu, sasa endapo kama itanipa mbinu ya kupambana na suala hili basi tutawasiliana…kwa leo nitawaachia dawa tu ambazo mtaziweka mlangoni, juu ya bati, na kwenye pembe za nyumba hii ili kumzuia mtoto huyu asitoke usiku kwenda kwa hao wafuasi wake ili asije akawaeleza mipango yetu, sawa?”



    “Sawa babu, tunakusikiliza wewe tu!”



    Babu Gao akafungua tena kikapu chake na kutoa kibuyu kingine na vipande vya magazeti ambavyo alivitumia kufungia dawa fulani nyeusi aliyoitoa ndani ya vibuyu vyake, akawafungia na kuwakabidhi kisha baada ya kuwapa maelekezo akaondoka zake!



    Wakazindika kila kona kama walivyoelekezwa na mganga kisha wakaendelea na mambo mengine kama kawaida.



    ***



    Siku iliyofuata, tofauti na siku zingine wanafamiliawaliamka wakiwa na nguvu na siha njema.bila shaka dawa za Babu Gao zilisaidia na kuwafanya wasichezewe kichawi. Shughuli za kila siku zikaendelea kama kawaida japo kwa simanzi, hofu namashaka.



    Sasa wakati mama Kaguba akifagiafagia huku wenziye wakiendea la mapishi huko jikoni, ndipo kikazuka kioja kingine cha mwaka.



    SEHEMU YA NNE



    “Mama…angalia hapo unapofagia,” Kaguba aliongea kwa kumtahadharisha mama yake. Kutokana na vimbwanga vya mtoto yule, sasa alikuwa si wa kupuuzwa kwa kila anachotaka kukisema.



    “Kuna nini?” Alisaili mama Kaguba huku akitupia macho yake eneo hilo alilokuwa akiliswafi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapo si nd’o mmechimbia ile dawa mliyopewa na yule Babu ili mnizuie nisitoke usiku! Sasa ukifagia vibaya utaifukua buree mwishowe usiku nitatoka tena.”



    Heeh!



    Yaani kumbe Kaguba alikwishajua kuhusu dawa zilizochimbiwa mahala pale kwa siri kubwa? Tena wakati babu Gao anatoa maelekezo ya dawa ile yeye alikuwa nje huko akicheza…hii kali kuliko.



    “We’ mtoto wewe! Nani amekwambia kuwa kuna dawa hapa?” Mama Kaguba alimhoji mwanaye huyo mtata, wakati huo na ndugu kadhaa nao wakisogea kusikiliza habari hiyo mpya ya kuchachafya ubongo.



    “…halafu mama leo nasikia kichwa kinaniuma sana…jana wachawi wote walikuja kunipitia lakini wakashindwa kuingia ndani, na mimi nikashindwa kutoka kutokana na hiyo dawa mliyoweka, sasa wakawa wananiita kwa makelele sana mpaka nikashindwa kulala!” kabla hajajibiwa akaendelea mwenyewe “…unajua mi’ nd’o mkubwa wao tangu mlipomuua bibi maana alishaganikabidhi vitunga vyake vote vya uchawi. Mama mi’ mwenziyo ni bosi we’ nidharau tuu.”



    Majanga!



    Mama Kaguba na nduguze wakaangaliana kwa kihoro. Kama ilivyo kwa mtoto mwingine yeyote, Kaguba alisimama na kutoka zake nje kwenda kucheza na wenzake bila ya kujali athari ya maneno yake aliyoacha ameyabwata mbele ya wazazi wake.



    Hakuna kilichofanywa zaidi ya kuendelea kuishi kwa mashaka huku wakisubiri kama Babu Gao angerejea na mpya gani. Siku kadhaa zikakatika bila ya Babu Gao kurejea, japo bilaya kupatwa na mauzauza mengine yoyote kutoka kwa Kaguba wala kwa hayati Nyanzala.



    ***



    “…mkuu tunaomba japo idhini yako tu ili tumkate kabisa ulimi Nyanzala maana tunaona wazazi wako wanaanza harakati za kwenda kwa waganga, sasa tusije tukamkosa,” Binti Sambayu aliongea kwa kumbembeleza Kaguba, akiwa nje ya nyumba baada ya kushindwa kuingia wala kumtoa Kaguba ndani kutoka na zindiko kali la Babu Gao.



    “Hapana, msimkate kabisa ulimi ma’mdogo wangu mpaka n’takapokuja mwenyewe,” Alijibu Kaguba kwa kutokea ndani. Ilikuwa ni usiku wa manane, Kaguba akiwa dirishani kwa ndani ya chumba huku Binti Sambayu akiwa kwa nje wakijibizanana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Pia tulimfuata usiku wa jana huyo Babu Gao ili tumpe hongo yoyote atupe dawa ya kuziua nguvu zile ndumba alizozindika lakini amekataa katakata.”



    “Achaneni naye…”



    “Sasa hali hii itakuwa mpaka lini mkuu?”



    “Muda si mrefu nitawatoka tu hawa na huyo Babu Gao nitamuua kwa mkono wangu…kuna kibuyu chenye uchawi na dawa zote kali, bibi alikichimbia chini ya kitanda chake, sasa nashindwa kukifukua kwakuwa kuna watu bado wanalala humo chumbani mwake walipopafanya kama ufuo. ila nikikipata tu hakuna atakayethubutu kunisogelea…” Alisema Kaguba.



    “Sasa mkuu, kama hao nduguzo watakigundua hicho kibuyu itakuaje?”



    “Itakuwa hatari sana maana hicho ndicho chenye nguvu zote za uchawi wa bibi…kama watakipata na kukichoma moto au kukidumbukiza chooni basi tutateketea wachawi wote wa kambi yetu ya Kibondo. Ila ondoa shaka hakuna atakayeweza kukisogelea maana mtu wa kawaida akikigusa kwa mkono wake bila ya kukishika kwa majani ya Vibumbasi, atapigwa na kitu mithili ya radi kali na kufa hapohapo.”



    “Sawa mkuu.”



    “Watangazie wachawi wote kuwa jumatano nitatoka na nitakuja kusikiliza shida za kila mtu, nadhani msiba utamilizika siku ya jumanne hivyo mpaka kufikia jumatano nitakuwa nimepata nafasi ya kukichimbua hicho Kibuyu…ila kwa sasa msiruke umbali mrefu, muishie mikoa ya jirani tu…nawatakia uwangaji mwema.” Pamoja na Kaguba kumuaga binti Sambayu ila maswali kadhaa yaliwafanya waendelee na mjadala wao. Waliendelea na majibizano kwa umakini wa hali ya juu kwa kuhofia kusikika na mtu wa kawaida maana kama angetokea mtu akiwa macho angeweza kuwasikia kwa kuwa kwa muda ule iliwabidi wawasiliane kama watu wa kawaida tu kwakuwa haikuwa rahisi kwao kuwasiliana kwa mtindo wao wa kichawi kwani nyumba ile ilikuwa imezindikwa.



    Walipomaliza mazungumzo wakaagana.



    Mtoto Kaguba na Binti Sambayu wakaagana na kuachana wakiwa na matumaini ya kukamilisha mpango wao. Siku hiyo ilikuwa ni Alkhamisi hivyo ingewagharimu siku kama sita ili kukipata kibuyu chao.



    ***

    ***

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kulipopambazuka kila mmoja aliamka na kuanza kutekeleza majukumu ya kila siku, wapo waliokwenda kuchota maji, wapo waliokuwa wakipika huku wengine wakisafisha nyumba na wengine wakiwa wameketi tu sebuleni. Watoto nao, pamoja na Kaguba waliendelea na majukumu yao ya kucheza!



    Mzee Mtandi alikuwa chumbani kwake akiwa amemakinika na kijitabu chake kidogo ambacho hupendelea sana kuandikia kumbukumbu zake za kila siku. Alikuwa akisoma hikina kuandika kile, alimuradi alijishughulisha na alichokijua mwenyewe. Alipoona amemaliza, akakirejesha kitabu chake kwenye mfuko wa begi lake la nguo na kutoka mle chumbani mpaka uani.



    “Jamani mi’ n’natoka kidogo kuna pahala ninakwenda mara moja, nitarejea baadaye!” Mzee Mtandi aliwaaga wapwa zake.



    “Mjomba si’ ungesubiri stiftahi kwanza?” alijibu kwa kusaili Kungurume.



    “Hapana, mtaniachia tu nikirudi nitakula ninashida na bwana mmoja hivi maeneo ya stendi huko.” Baada ya mazungumzo ya hapa na pale Mzee Mtandi akadandia baiskeli yake mkangafu na kuondoka. Hakwenda stendi kama alivyodai, ila kuna sehemu alikuwa ana shida kubwa sana, shida ambayo usiku kucha aliumaliza akiifikiria. Alipotimiza shida yake akapitia kwenye mihangaiko ya hapa na pale kisha akarejea nyumbani ambapo kabla ya kuingiza chochote kinywani akaitisha kikao cha familia nzima nzima.



    Wote wakajumuika sebuleni.



    “Nimekuiteni hapa wanangu, kuna mambo mazito kidogo nataka kukuelezeni…naomba muwe na staha na na utulivu wa hali ya juu…” Alianza kuongea Mzee Mtandi baada ya kufungua na kutuliza baraza. “…Kuna jambo zito nimelivumbua, jambo ambalo kama tutachelewa kufanya ma’arifa basi matokeo ya uvumbuzi wangu wa hatari ni vifo vyetu wenyewe, tutapitiana hapa na kufa kama wagonjwa wa kipindupindu.”



    Kimya kilitanda huku kila mmoja akisikiliza kwa makini, Mzee Mtandi akaendelea.“…Siku zote hizi ninyi mkiwa mmelala, mi’ huwa naamka usiku na kujaribu kuchunguza mwenendo wa mjukuu wangu Kagubamaana kwa sasa hakuna asiyejua u-hatari wake. Yapo mengi huwa nayang’amua ila hili nililoling’amua usiku wa kuamkia leo ni kubwa na la hatari zaidi…ni kweli kama alivyosema mwenyewe kuwa dawa za Babu Gao zinamzuia kukutana na wachawi wenziye, hilo nimeligundua baada ya kumshuhudia kwa jicho langu akiongea na Binti Sambayu kupitia dirishani, na nimegundua hila nzito walizozipanga ili kutuangamiza sisi sote, na hakika tusipokuwa makini tutakufa sote hapa na kwenda kutumikishwa huko kwenye ulimwengu usioonekana kama misukule.” Vinyweleo viliwatutumka kwa hofu wanafamilia wale waliokuwa kama kondoo anayesubiri kuvamiwa na chui akiwa hana msaada.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati wanaongea walihakikisha hakuna mtu mwingine yeyote tofauti na wao tu kama walengwa wakuu, hata watoto wao wadogo wa rika la Kaguba hawakuruhusiwa kuingia ndani. Kama palikuwa na kiumbe chochote kinachoonekana basi labda ni yule paka wao wanayemfuga aliyekuwa amejilalia zake juu ya kochi. Na hata alipoona maongezi yale yakiendelea, Paka alijitokea zake nje.



    “…Bahati nzuri ni kwamba mbali ya mipango yao ya kutudhuru, pia nimepata mbinu kali ya kuwaangamiza wote wanaojihusisha na uchawi kutoka katikamazungumzo yao wenyewe…” Aliendelea kuogea Mzee Mtandi kiasi cha kuzidi kuwamakinisha wanafamilia wote. “…Nilipowaambia nakwenda mara moja stendi, haikuwa hivyo. Nilikwenda kwa Bi mkubwa mmoja hivi kumuulizia juu ya wapi nitapa majani yanayoitwa vibumbasi maana hiyo ni moja ya kinga tutakayoitumia wakati wa kuishika silaha kuu ya maangamizi na kuumaliza huu udhia unaotutesa.”



    Ni kweli mzee Mtandi aliushuhudia mchezo mzima kati ya Kaguba na binti Sambayu. Sasa wakati anaanza kuwapa habari ilivyokuwa wakati wakiwasiliana ndipo kikaibuka kitimtim kipya.



    Walishangaa tu kuona ghafla mzee Mtandi akinyamaza kimya kama aliyezimwa kwa rimoti. Na hapohapo akaonekana kuishiwa nguvu, mara akaanguka chini ‘PAAA’ macho yakamtoka, povu likimfumka mdomoni. Taharuki ikawavaa wanafamilia, ikawa ni mshikemshike mpya.



    Hakuna mtoto mdogo pale mpaka asielewe kilichotokea kuwa ni tukio la kivamizi la kishirikina lililoazimia kumzuia Mzee Mtandi asitoe siri aliyokuwa nayo, na hata ikibidi afe nayo kifuani.



    Watoto hawakukubali kumpoteza mjomba wao pamoja na siri yake kubwa yenye lengo la kuwafaa wote. Haraka teksi ikaendewa na baada ya makubaliano safari ya kuelekea kwa Babu Gao ikaanza. Pamoja na Mzee Mtandi mwenyewe, ndani ya teksi ukitoa dereva aliingia pia Mama Kaguba na Kungurume.



    Wakati wanaondoka, yule paka wao wa kufugwa aliyetoka wakati walipokuwa wakiendelea na mazungumzo yao alirejea na kuketi palepale kwenye kochi.



    ***



    Safari ilikuwa mbaya na ya matumaini tu maana kila baada ya hatua kadhaa gari iliwaharibikia, kila dereva alipojaribu kutengeneza na kuendelea na safari walitembea umbali mfupi tu kabla ya kuharibikiwa tena. Wakati huo hali ya Mzee Mtandi ikizidi kuwa mbaya, hakuwa na fahamu kabisa hivyo alikuwa amebebwa tu kama mzigo.



    Safari iliendelea hivyohivyo kimungumungu tu mpaka walipofika katika moja ya mapori kadhaa ambapo ilikuwa wakilimaliza pori lile tu wangewasili nyumbani kwa Babu Gao, ndipo kilipoibuka Kimbunga kikali kilichoishambulia ile teksi mpaka ikazima.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kimbunga kumalizika na upepo kutulia ndipo dereva akateremka ili kutengeneza gari yake,hilo likawa kosa kubwa!



    SEHEMU YA TANO



    Ilikuwa kama maigizo tu, mbele ya macho ya Kungurume na mama Kaguba pale waliposhuhudia dereva wao akiyeyuka na kupotea punde tu mara baada ya kuteremka garini. Wakahaha na kuanza kupiga makelele ya kutaka msaada lakini hakuna aliyewasikia. Ukimya uliendelea kutuama eneo lile laporini. Walipiga kelele mpaka wenyewe wakatulia, hakuna aliyetokea kuwahami. Labda simu zao zingewasaidia ili wawasiliane na ndugu huko mjini kama kungekuwa na mtandao katika pori lile, haikuwa hivyo!



    Walikaa pale wakiwa ndani ya teksi mbovu huku dereva akiwa ametoweka kimiujiza huku hali ya mjomba wao ikizidi kudorora. Ndipo baada ya muda fulani ikatokea gari aina ya Landrover. Haraka Kungurume akajivisha ujasiri maana yeye nd’o mwanaume aliyebaki, akateremka ndani ya gari na kulipiga mkono gari lile lililokuwa likipita akidhamiria kuomba msaada. Cha ajabu gari ile iliwapita kama nyumba inayoungua moto. Hakujua ni nini hasa kilichopelekea hali ile ya kutelekezwa na gari ile.



    Labda hawakumuona! Labda walimuogopa wakidhani ni mtego wa majambazi, au nd’o hila za akina Kaguba na Binti Sambayu. Hakuna jibu sahihi!Kungurume akabaki amejishika kiunoni kwa mikono yake iliyojazia huku macho yake yakitalii mazingira ya kijani kibichi yaliyotawala pori lile. Akarudi ndani ya gari huku akitweta, akiwa amepoteza kabisa matumaini.



    “Mwenzangu, hali ngumu,” Alisema Kungurume akimwambiadada yake.



    “Kivipi?”



    “Kuna mawili tu yanayoonekana hapa…tutampoteza mjomba hapahapa mikononi mwetu au tutaangamia pamoja naye…”



    “Mbona unanitisha kaka?” Kabla Kungurume hajajibu, ndipo ikaibuka tena gari nyingine aina ya Landcruiser. Haraka Kungurume akateremka ili kujaribu tena bahati. Akapunga mkono wake ikiwa ni ishara ya kuomba msaada. Bahati ikawa yake, gari ile ikasimama.



    “Habari zenu wakuu?” Alisalimu Kungurume.



    “Nzuri, vipi kuna shida gani?” Dereva wa gari ile alijibu akiwa ndani ya gari yake bila hata ya kuteremka.



    “Jamani tumepata matatizo, tuna mgonjwa ndani ya teksi yetu na tumeharibikiwa hapa…hali ya mgonjwa inazidi kuwa mbaya tu tunaomba msaada wenu tafadhali.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Gari imeharibika kitu gani?”



    “Kwakweli hata sijui kilichoharibika.” Jibu hili likamfanya dereva wa ile Landcruiser aangaliane na mtu aliyembeba.



    “Dereva wa teksi hiyo yuko wapi?” Swali hili sasa kutoka kwa mtu aliyebebwa kwenye ile Landcruiser lilimfanya Kungurume ajigonge asijue cha kujibu, maana kama ataeleza ukweli kuwa ametoweka katika mazingira ya kutatanisha, hakika asingepata msaada kwani asingeaminika kabisa na hata kama angeaminika basi angekuwa amekwishawatisha sana watu hao. Baada ya fikra fupi alijibu.



    “Dereva baada ya kujitahidi kutengeneza gari bila mafanikio ndipo akapata lifti ya kwenda mjini kuendea sijui kifaa gani huko…sasa sisi tuna mgonjwa hatuwezi kuendelea kukaa hapa wakati hali ya mgonjwa ni mbaya na amepoteza fahamu.” Alidanganya Kungurume akichelea kupoteza msaada.



    “Sasa huku mnampeleka wapi mgonjwa wenu? Kuna hospitali kweli huku?” alisaili dereva.



    “Huku tunampeleka kwa mganga wa kienyeji.” Jibu hilo pia likawafanya mtu na dereva wake waangaliane na kutikisa vichwa.



    “Yaani kaka mbona unaoekana kama ni msomi hivi halafu unadriki kuamini mambo haya ya kishirikina?” Alihoji dereva.



    “Kaka, Kitanda usichokilalia huwajui Kunguni wake…Laiti mngejua masaibu tunayopitia mpaka tumesalimu amri na kuja huku bila shaka mngetuonea huruma…imebidi tufanye hivi tu.”



    “Okay iko hivi kaka sisi hatuwezi kuwapeleka huko kwa mganga kwakuwa tuna mambo ya muhimu tunawahi mjini…sasa msaada pekee tunaoweza kukupeni ni kuwapakia kwenye gari yetu na kurejea nanyi mjini na tutukwenda kuwaacha hospitalikama hamtojali…Upo hapo?”



    Duuh!



    Haikuwa lengo kabisa, Kungurume akashusha pumzi nzito ya kushindwa kabisa. Akawaomba mabwana wale wamsubiri asogee upande wapili ilipo teksi akaongee nadada yake amweleze kuhusu msada huo wa kurejea mjini. Wakamkubalia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya Kungurume kuifikia teksi yao na kuongea na dada yake, wakashuka ndani ya teksi na kuisogelea ile Landcruiser. Baada ya mama Kaguba kusalimiana na watu wale, alijaribu kuwasihi na kuwabembeleza ili tu wawapeleke huko kwa Babu ambapo hapakuwa mbali kutokeahapo walipo…na ikibidi hata kwa kuwalipa. Mjadala ukaanza upya huku jamaa wakiwa na msimamo wao uleule lakini kama ilivyo falsafa ya hayati Albert Mangwea kwamba ‘Mwanaume kwa mwanamke, ni sawa na mfupa kwa fisi’ Dereva na patna wake wakasalimu amri, wakageuza gari na kuisogeza usawa wa teksi. Wakateremka na kusaidiana kumbeba Mzee Mtandi na kumpakia ndani ya gari yao.



    Wakaingia wote ndani ya gari baada ya kuhakikisha ile teksi wameifunga vizuri. Dereva akalitia moto gari, likawaka. Lakini kila alipoigiza gia ili waondoke gari iligoma kuondoka. Hila za kifundi zilimwisha dereva yule bila ya mafaniko. Gari iligoma kabisa kuondoka na baada ya purukushani ikazima kabisa.



    Balaa!



    Wakashuka wote na dereva akalala chini ya uvunguwagari kuangalia hitilifu, lakini hakuliona tatizo. Akaingia tena ndani ya gari peke yake huku wengine wakimsubiri nje wakati akijaribu kuendesha. Alipojaribu kuliwasha likawaka. Alipoliingizia gia likakubali na kuondoka, wote wakafurahi. Baada ya gari kusimama wakalisogelea na kuingia ndani ya gari kwa ajili ya safari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walipoingia tu, mchezo ukawa uleule gari likatia mgomo tena. Ndipo dereva akageuka mbogo baada ya kugundua kuwa watu hawa hawakuwa wa kawaida. Akawateremsha pamoja na mgonjwa wao licha ya maombi ya huruma kutoka kwao. Alipowateremsha tu gari likakubali tena, akaliwasha na kulitia gia..akawachia vumbi tu. Mama Kaguba alilia kwa uchungu, japo haikufaa kitu. Wakarejea kwenye teksi yao na kusubiri kadari ya Mungu tu iwakute maana hawakuwa na namna nyingine.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog