Search This Blog

TANZIA - 3

 





    Simulizi : Tanzia

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Mama Kaguba alilia kwa uchungu, japo haikufaa kitu. Wakarejea kwenye teksi yao na kusubiri kadari ya Mungu tu iwakute maana hawakuwa na namna nyingine.

    Walikaa pale bila ya kupata msaada mpaka jioni ikawakuta wakiwa palepale huku hofu, mchoko na njaa vikizidi kuwashambulia. Ndipo ghafla wakatokea vijana wawili waliovaa nguo chafu na chakavu wakiwa wanakusanya kuni.

    “Habari zenu jamani?” Kungurume aliwasalimu vijana wale baada ya kuteremka kwenye gari na kuwasogelea. Akiwa na dada yake kwa pembeni.

    “Nzuri tu…” walijibu vijana wale.

    “Jamani samahani tunahitaji msaada wenu…sisi tumeharibikiwa na gari na tupo na mgonjwa aliye mahututi sasa tunaomba tafadhali mtudaidie jamani?”

    “Mnakwenda wapi na huyo mgonjwa wenu?”

    “Tunampeleka kwa mganga mmoja hivi anaitwa Babu Gao.” Jibu hilo la Kungurume likawafanya vijana wale waangaliane kwa udadisi.

    “Dereva wenu yuko wapi?” Aliuliza mmoja kati ya vijana wale wawili.

    “Dereva aliteremka ili kuangalia hiyo hitilafu iliyotokea, cha ajabu hatukumuona tena akawa ametoweka.” Jibu hili alilitoa mama Kaguba, japo inaonekana alimkera kaka yake kwa kusema jambo hilo ambalo lingeweza kuwatisha na kuwaacha na maswali mengi zaidi badala ya kuwapatia msaada.

    “Mnh!” aliguna kijana mmoja.

    “Nd’o yuleee?” kijana mwingine akamsaili mwenziye ambaye alitikisa kichwa kuashiria kukubali alichoulizwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Iko hivi jamani…” Alianza kuongea kijana aliyekuwa na upanga mkononi mwake. “…Sisi ni vijana wa huyo Babu Gao mnayemfuata, huku tulikuja kusanya kuni na kuwinda kitoweo lakini muda mfupi tu uliopita tumekutana na kijana mmoja amevaa kofia nyekundu akatuambia kuwa amepotezana na wenziye na kwamba yeye ni dereva teksi…itakuwa nd’o huyo eeh?” Safari hii sasa ikawa zamu ya Kungurume na Mama Kaguba kutazamana kwa mshangao.

    Hii ndiyo faida ya kuwa mkweli maana kama Mama Kaguba angedaganya basi pengine vijana wale wasingejua kisanga hicho kuwa kinahusiana na huyo kijana waliyemuona.

    “Nd’o huyohuyo alikuwa amevaa kapelo nyekundu.” Jibu la hilo kutoka kwa Mama Kaguba likamfanya kijana mmoja atoke mbio akielekea porini kujaribu kumtafuta huyo dereva waliyekutana naye.

    “Huyu mgonjwa wenu atakuwa amerogwa vibaya sana…” Alianza kuongea kijana aliyebaki na akina Mama Kaguba wakati mwenziye amekimbia mle porini. “…maana si ninyi tu, bali wengi wakiwa wanakuja kwa Babu hupotea ghafla au kuharibikiwa safari mpaka wanaamua kurejea huko mjini. Ila ondoeni shaka hata kama gari itaharibika basi tutambeba mgonjwa wenu kwenye miti mpaka tutamfikisha kwa Babu, na hata hapa tulipo bila shaka Babu atakuwa amekwisha tuona kupitia ‘Tivii’ yake ya asili.”

    “Yaani hata hatuamini kama tumepona aisee, ahsanteni sana. Kwahiyo ninyi ni wajukuu kabisa wa Babu Gao?”

    “Naam, mi’ ni mjukuu wake kabisa, mtoto wa wa mwanaye. Ila huyo aliyekimbilia huko porini ye’ ni Kanumba(msaidizi’ mganga) wake.

    Wakiwa wanaendelea kupashana habari, ndipo yule aliyekimbilia porini akarejea akiwa na yule dereva teksi. Maongezi yakafa kwanza! Hapakuwa na haja ya kupiga soga tena, wakaingia kwenye teksi kisha yule Kanumba akatoa dawa fulani na kuimwagia teksi…na kumuamuru dereva awashe gari.

    Kama mchezo wa kuigiza vile, gari ikakubali na safari ikaanza. Ndani ya teksi walibanana wote. Akina Kungurume na mgonjwa wao, pamoja na wale vijana wa Babu Gao.

    Kumbe wala hawakuwa mbali sana na nyumbani kwa Babu Gao kwani muda mfupi wa safari waliwasili na kumkuta Babu gao akiwa amejipinda na shughuli ya kutengeneza mipini ya majembe.

    Wakateremka kutoka garini na kumsogelea Babu Gao, cha ajabu Babu aliendelea na shughuli zake kama hajawaona wageni licha ya muungurumo wa gari yao kuvuma tangu wanaingia eneo lile, hali hiyo iliwashangaza si tu akina mama Kaguba, bali hata wale vijana wake walihisi kitu.

    “Babu shikamoo!” Mama Kaguba na Kungurume walimsalimu Babu Gao.

    “Marahaba,” aliitikia salaam ile Babu Gao huku akishindwa hata kukitaabisha kichwa chake japo tu kuwatazama.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Habari za hapa?” Mama Kaguba alisaili kwa fadhaa.

    “Nzuri.” Babu aliendelea kujibu ki-mkato.

    “Babu tumekuja na mgonjwa yumo ndani ya gari…ni mjomba Mtandi amepoteza fahamu kabisa.”

    “Sasa?”

    “Tumekuja kwako Babu tunaomba msaada wako!”

    “Amepotezea wapi fahamu?” alisaili Babu Gao.

    “Tangu nyumbani…ilikuwa hivi alikuwa akitu…” Kabla mama Kaguba hajamalizia kauli yake akakatizwa na Babu Gao.

    “Sasa fahamu amezipotezea huko kwenu halafu mnakuja kuzitafutia kwangu! Mi’ siwezi kuzipata naomba muondoke haraka tafadhali nina kazi nyingi za kufanya.”

    Heeh…!

    “Babu siye ni wajukuu zako, au umetusahau?”

    “Sina wajukuu kama ninyi…na kama ni wateja wangu ni kwamba sihitaji kufanya kazi nanyi kabisa jamani mwende au mpaka niwafanyie kitu kibaya?”

    Laiti kama mzee Mtandi angekuwa na fahamu angetambua ukweli wa kile alichokisikia kwa binti Sambayu akimueleza Kaguba kuwa wamemtisha na hata kutaka kumuhonga Babu Gao ili aache kufuatilia kesi hiyo hivyo yawezekana mganga huyu amesalimu amri.

    Babu Gao alikuwa amebadilika kabisa na kuwa kama hajui lolote kuhusu wageni wale. Kama haitoshi Babu akanyua uso wake ili awakaripie vijana wake tabia za kuokota watu huko na kuwaleta pale kwake. Alipoinua sura yake tu kabla hajawakaripia vijana wake akakutanisha macho yake na nyuso zilichoka na kukata tamaa kabisa kutoka kwa Kungurume na Mama Kaguba.

    Waswahili wanasema wao kuwa Ukitaka kumuua Nyani, usimwangalie usoni…utamuonea huruma. Hivyo ndivyo ilivyokua kwa Babu Gao alijikuta akishusha pumzi za huruma. Badala ya kukaripia kama alivyokusudia, badala yake akawaambia vijana wake waondoke ili abakai na wageni wake. Vijana wakaondoka!

    “Sikilizeni jamani…jambo lenu ni kubwa sana na limenielemea kiasi cha kutishia maisha yangu…” Alianza kuongea Babu Gao baada ya kuweka pembeni zile zana zake alizokuwa akizitengeneza. Akawaelezea kwa kirefu ugumu wa suala lao lile, akawapasha habari jinsi alivyofuatwa na kutishiwa maisha yake na wafuasi wa Kaguba na mambo mengine mengi tu.

    Mjadala ulikuwa mpana sana. Akina mama Kaguba walimlilia babu na kusaga meno ili awasaidie mpaka hatimaye Babu Gao akalegea. Akawaambia wamteremshe mgonjwa kutoka ndani ya gari kisha wamuingize ndani. Vijana wakaitwa kusaidia zoezi lile.

    Baada ya kukamilisha zoezi hilo, Kungurume akamlipa dereva teksi na kumwacha aende zake kwani kwa mujibu wa mganga, wao walipaswa kulala palepale. Kuwafahamisha nyumbani kwao haikuwa tabu kwani tangu walipofika kwa Babu hapo mtandao ulikuwa ukifanya kazi.



    ******CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Babu Gao akarejea katika ule ukarimu wake wa kawaida na wa kila siku. Akawakirimu chakula wageni wake, akawapa maji ya kuoga huku yeye akazianza sarakasi zake za kumtibu mzee Mtandi aliyekuwa hajarejewa na fahamu muda wote ule. Tiba ilikuwa kubwa na ngumu sana, ilichukuwa muda mrefu mpaka giza la usiku likaingia, na hapo Babu Gao akawaandalia wageni wake sehemu ya kulala. Walipolala, yeye akaendelea na patashika yake.

    ***

    “Jamani kazi ni ngumu sana kama nilivyokuambieni tangu jana…” Babu Gao aliwaambia akina mama Kaguba baada ya kumka asubuhi. “…Huyu bwana kuna siri kubwa sana aliigundua kuhusiana na hao wachawi wenu, bahati mbaya alipokuwa akiwaelezeni ninyi hakujua kuwa nyumba ile si salama kujadili vitu hatari kama vile…mle ndani kuna wachawi kila kona…”

    “Lakini Babu wakati mjomba anatuhadithia habari hiyo mpaka ikamkuta hali hii, tulikuwa tumewatoa nje watu wote wasiohusika.” Mama Kaguba alidakia.

    “Una uhakika gani kuwa kati yenu mliokuwa pale sebuleni hakuna mchawi? Kwani ninyi mlitegemea kuwa yule mtoto mdogo Kaguba angeweza kuwa mchawi?” alisaili kwa umakini Babu Gao.

    “Mnh! Kwahiyo kuna mtu kati yetu kule nyumbani ni mchawi?” Alihoji kungurume.

    “Sina maana hiyo, nilitaka tu kukuonesheni kuwa hamko makini na jambo hili kwakuwa hamuujui uchawi ninyi…iko hivi sasa, siku ile mlipokuwa mnaongea mambo haya mle ndani palikuwa na Paka amejilaza kwenye kiti, basi yule hakua Paka asilani!”

    “Ama!” Alimaka Kungurume huku akivuta kumbukumbu ya siku ile.

    “Alikuwa ni mwanaadamu yule aliyejibadili na kuwa kama Paka japo miaka yote mmekuwa mkiamini kuwa ni Paka wa kufugwa ila hayati Masonganya alikuwa akimtamua kama mtumishi wake, na muda mrefu huwa anawafatilia mambo yenu. Sasa aliposikia habari ile mbaya akatoka nje na kwenda kumpa taarifa Kaguba aliyekuwa akicheza nje na wenziwe’ Kaguba naye haraka akawasilisha taarifa ile kwa Binti Sambayu kwa njia wazijuazo wenyewe ndipo likatumwa pigo lile lilomfanya mjomba wenu awe hivi…ila tutajitahidi sana kuhakikisha anapona.”

    “Tutashukuru sana Babu.”

    “Vizuri!”

    “Unajua nini Babu…” Kungurume alianza kuongea huku akitembeza macho yake katika chumba kile cha uganga. “…sisi hata hatukujua ni kipi hicho ambacho mjomba alikigundua toka kwa hao wachawi kwani alipofikia tu kwenye pointi hiyo nd’o akaanguka, sasa we’ unaweza kututajia hicho alichokigundua?” Swali hilo likamfanya Babu Gao apikiche viganja vya mikono yake na kisha kuifumbata mikono yake kifuani.

    Kimya kikatawala.

    “Siwezi kusema uongo kabisa katika hili, ni kwamba sijabahatika kukijua hicho kitu. Hata haya machache niliyowahabarisha nimeyapata kwa ufundi wangu wa hali ya juu, niliingia kichwani mwa mjomba wenu na kuanza kuzisoma fikra zake lakini habari niliyoipata ni ile kama mliyokuwa nayo ninyi, yaani niliishia palepale alipoanguka tu. Nadhani leo atazinduka na tutakwenda kufanya kafara kubwa makaburini ambapo tukimaliza atatuhabarisha yeye mwenyewe.

    ***CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Asubuhi yote, na mchana kutwa Babu Gao alikuwa akishughulika na jambo lile zito mpaka kwenye saa kumi alasiri ndipo mzee Mtandi akarejewa na fahamu. Ilikuwa ni kazi nzito, kazi ya kutibu huku akipambana na nguvu za wachawi zilizokuwa zikimshambulia mara kwa mara kiasi cha kumvurugia kabisa kazi yake. Baada ya Mzee Mtandi kuzinduka akaachwa apumzike, kisha baadaye akapewa chakula na kupelekwa kuoga akiwa amebebwa. Afya yake haikuwa mbaya sana japo tatizo kubwa alilokuwa nalo ni kutoweza kutembea mwenyewe pamoja na kupoteza kumbukumbu…hakuwa na kumbukumbu zozote za kulichotokea. Hilo Babu Gayo alilitarajia.

    Saa moja magharib msafara wa kwenda makaburini ukaanza. Kungurume, Mama Kaguba, Babu Gao na Kanumba wake wakiwa wamembeba mzee Mtandi wakaongozana kuelekea makaburini ambapo zindiko kubwa liliratibiwa kufanyika.

    “Tukifika makaburini hatutoruhusiwa kuongea chochote labda kama nitawaelekeza kufanya hivyo,. Sawa?” Aliunguruma Babu Gao.

    “Ndiyo!” “…Tawire.” Walijibu.

    “Kuna kazi ndogo tu kama ya dakika kumi hivi tutaifanyia juu ya kaburi. Tukifika we’ bwana Mtandi tutakuwekea kigoda juu ya Kaburi kisha utaketi, tutakupa kinu kitakachokuwa na dawa ndani yake, utakishikilia kwa mikono yako miwili halafu mimi nitatwanga dawa itakayokuwa humo kwenye kinu…” Walikuwa wakimsikiliza kwa kina Babu Gao akitoa maelekezo maana walijua wakifika huko makaburini hawatopata nafasi ya kuongea kama walivyopewa hadhari mapema.

    “…Nikishamaliza kutwanga tu dawa utainuka na kutoka hapo kaburini kisha dawa hiyo tutaichanganya kwenye kinu na sote tutaioga na kuinywa. Hapo tutakuwa tumemaliza kazi yetu.” Alihitimisha Babu Gao na kuruhusu maswali kwa ambaye hajaelewa, hapakuwa na swali. Wakatembea mpaka wakawasili katika viwanja vya makaburi. Japo alikuwa amebebwa, mzee Mtandi alisikia na kuelewa maelekezo yote yaliyotolewa na Babu Gao.

    Viwanja vya makaburi vilikuwa kimya kabisa, upepo ukiiyumbisha miti kadhaa iliyopandwa kwa kulizunguka eneo hilo kiasi cha kuyaangusha majani dhaifu yaliyolegea. Wakati huo giza lilikwishaanza kutanda na kufanya eneo hili la makaburini kutisha haswa!

    Wakaingia na kwenda mpaka katikati ya makaburi, Babu Gao akachagua kaburi moja lilionesha kuwa si la muda mrefu sana tangu lihifadhi mtu ndani yake. Haraka Kanumba wa Babu akaweka kigoda juu ya Kaburi hilo sambamba na Kinu chenye dawa kisha akarudi hatua moja nyuma. Babu Gao akasaidiana na Kungurume kumnyanyua mzee Mtandi na kumkalisha juu ya kigoda kile juu ya kaburi. Baada ya kuketi, mzee Mtandi akakishika kinu kwa mikono yake miwili na hapohapo Babu Gao akiwa amesimama kwa karibu japo yeye hakupanda juu ya kaburi, akainua juu mchi wake wa kutwangia na kuanza kuongea maneno yake ya kiganga. Wakati huo Mama Kaguba, Kungurume, na yule Kanumba walikuwa wamesimama kwa kulizunguka kaburi.

    Baada ya Babu kumaliza kuongea tu maneno yake, akaanza kutwanga dawa iliyomo ndani ya kinu kilichoshikiliwa na mzee Mtandi huku akiimba nyimbo kwa lugha ya kiha.

    Ghafla wakati Babu Gao akitwanga dawa ile kikaibuka kizaazaa kilichowafanya wote wataharuki mpaka Babu Gao mwenyewe.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Ilikuwa ni wakati Babu Gao akitwanga ile dawa, ndipo Kaburi lililokaliwa na mzee Mtandi lilipoachama kama mamba, na wote wakashuhudia Mzee Mtandi aliyekuwa ameketi kwenye Kigoda akizama na kupotelea ndani ya kaburi pamoja na kinu chake kisha kaburi likajifunga.

    Mama Kaguba alijikuta amemshikila shati kwa nguvu kaka yake hofu kuu ikimkumba, wakati huo Kanumba naye alikuwa amehamanika na kumuangalia Babu Gao aliyebaki na mchi wake mkononi asijue cha kufanya.

    Ghafla!

    Wakaanza kusikia kukurukakara na vurugu vikitokea ndani ya kaburi aliliozama mzee Mtandi. Ilikuwa ni kama vile uchukue dumu kubwa halafu uliwekee mawe madogo na kuanza kulitikisa kwa nguvu ndivyo zile vurugu mle kaburini zilivyozizima.

    “YALAAAH…UWIIIII NAKUFAAA JAMANI!” Sauti ya mzee Mtandi ilisikika ikitokea mle kaburini licha ya kuwa kaburi lilikuwa limejifunga. Babu Gao uzalendo ukamshinda, akautupa mwichi wake na kutaka kukimbia ndipo haraka Kungurume akamrukia na kumkwida.

    “Unataka kukimbia wapi?” Kungurume alibwata.

    “Tuondokeni jamani hii si hali ya kawaida,” alijibu Babu Gao. Kabla Kungurume hajajibu lolote ndipo tena mkanda ukaendelea. Kaburi likajapasua katikati halafu katikahali isiyokuwa ya kawaida, mzee Mtandi akarushwa kwa nguvu kutokea mle kaburini na kwenda angani, yeye kule, kigoda na kinu huko. Kisha akatua chini kama kifurushi. Kitokeo cha hapo mzee Mtandi akainuka na kuanza kutimua mbio kali, kufikia hapo sasa akina Kungurume pamoja na mganga wao nao wakatimka.

    Mgonjwa aliyekuja amebebwa, mara ghafla ameondoka akikimbia kama amefungwa mota miguuni. Chezea kifo wewe!!!

    Walitimka kwa kasi ya ajabu mpaka nje ya viwanja vile vya makaburi ambapo hawakumuona kabisa mzee Mtandi, hawakujua amepitia njia gani. Kutokana na hali ile ya kuogofya hawakuendelea kupoteza muda, wakaendelea kukimbia na kuelekea nyumbani kwa Babu Gao.



    “Poleni jamani, nini hasa kilichotokea maana nimeshangaa kuona mgonjwa amerudi mbio na kupitiliza mpaka chumbani.” Mke wa Babu Gao aliwapokea akina Babu Gao pamoja na Kungurume ambao nao waliingia hapo nyumbani kwa kasi ya ajabu. Hakuna aliyemjibu mama yule zaidi ya kuendelea kutweta kwa mchoko na kihoro, japo hawakupumzika baada ya kusikia kuwa mgonjwa yuko ndani. Wote wakafuatana na kuingia chumbani kwa mgonjwa.



    Wakamkuta mzee Mtandi akiwa amelala kitandani hoi bin taabani…hana hali, hana kauli. Yaani mgonjwa aliyekuja nyumbani huku akikimbia ghafla amekuwa hoi asiyeweza hata kuinua mkono acha kusimama!



    Kungurume kila alipokumbuka jinsi Babu Gao alivyotaka kuwakimbia alitamani hata amnase kelbu lakini akahofia kuvuruga mambo. Wakaanza kumhudumia mzee Mtandi. Mpaka kwenye saa nne usiku hali haikuwa imetengemaa ikawabidi waingie tu kulala. Hakuna aliyelala zaidi ya kuhesabu paa tu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakiwa bado wamejilaza vitandani mwao ghafla wakamsikia mtu akipita nje ya nyumba huko ambapo baada ya kusikia akipiga ngoma kisha akinena kwa sauti kubwa. “TANZIA…TANZIA…TANZIA Familia ya bwana GAO aliye mganga kiboko inasikitika kuwatangazia kifo cha mteja wake bwana mtandi Bin Kalukalange kilichotokea usiku wa kuamkia leo, maziko yatafanyikia Kibondo mjini.”



    Tangazo hilo liliwafikia kila mmoja mahala alipolala…hofu mpya ikaibuka hasa kwa akina Kungurume ambao kioja cha namna hiyo kilishapata kuwakumba kwa ndugu yao Bi Nyanzala. Wote wakainuka baada ya tangazo hilo kuisha na kuingia chumbani kwa mzee Mtandi.



    Loohsalale!



    Mzee Mtandi alikuwa amefariki. Kilio kikaibuka hapohapo. Babu Gao akajitahidi kuwatuliza ili ajaribu kuangalia kwenye ‘bainokyula’ yake…na hata alipopiga ramli zake zilimthibitishia kuwa mzee Mtandi amekwishaaga dunia. Simu zikapigwa mjini kwa ndugu ambao nao baada ya kuangua vilio vikubwa vilivyokusanya majirani, walijipanga wakakodi gari na kuufuata mwili wa marehemu pamoja na akina mama Kaguba.



    ********



    “…hii siyo bure, kuna jambo zito humu ndani. Na wasipokuwa makini watatikitia kama utitiri…” aliongea Bi mkubwa mmoja aliyehudhuria msibani hapo kwa hayati Masonganya.



    “Haswa! Maana ndani ya muda mfupi tu wamekufa watu watu. Alianza Bi Masonganya, akafuatia Nyanzala, na sasa mjomba wao bwana Mtandi…haiwezekani.” Waliungana mikono akina mama hao.



    “Aaah kwa Mungu madogo hayo, si ajabu kufa watu watatu kutoka katika familia moja…Mungu hata akitaka kuwamaliza nchi nzima kwa sekunde hashindwi kamwe!” alijibu dada mwingine huku ‘akiwabyeda’ wenziye.



    “We’ mtoto mdogo huna ujuacho kaa kimya!”



    Wakati mjadala mzima ukuiendelea huko uani kwa akina mama, upande wa mbele wa nyumba wanaume nao walikuwa wakizungumzia jambo hilohilo mpaka walipokatizwa na gari iliyokwenda kufuata maiti. Ilikuwa ikirejea huku imewasha taa ikiwa ni ishara kuwa wamebeba maiti. Wanaume wakasimama mpaka Gari ilipoegeshwa, wakaisogelea na kusaidiana kuupokea mwili wa hayati Mtandi.



    Muda wa mazishi ulipangwa kuwa ni saa kumi alasiri ya siku itakayofuata ili kuwasubirisha watoto wawili wa marehemu waishio Kigoma mjini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ebyomunyumba tebi totolwa,” Alisema Kungurume kuwaambia dada zake kwa kutumia lugha ileile ya marehemu mjomba wao. Naye akiwa na maana ileile kuwa wasiyaweke hadharani mambo yao.



    ***



    Siku iliyofuata majira ya saa tano asubuhi waliwasili watoto wawili wa marehemu ambao ni Lubambi na Ilumbi…pamoja nao waliandamana na Nyembo. Wafiwa walitoka kuwapokea ndugu zao hao huku wakilia lakini baada ya akina Ilumbi kuingia ndani tu sura za akina mama Kaguba pale nyumbani zikawabadilika kutoka kwenye huzuni na simanzi ya kufiwa na kuwa hasira ya Nongwa, hapakuwa na mazungumzo yoyote zaidi ya kupotezeana tu. Tatizo kubwa likiwa ni Nyembo.



    Nyembo pia ni mtoto wa hayati Bi Masonganya hivyo ni ndugu yao na akina mama Kaguba japo tofauti yao ni moja tu, wakati wao wanamwita Bi Masonganya mama, huyu Nyembo yeye anamuita Baba. Naama Bi Masonganya ni baba yake kabisa na Nyembo, na hivyo ni miongoni mwa vimbwanga vya hayati Bi Masonganya.



    Watoto wote wa Bi Masonganya walimchukulia Nyembo kama ni kielelezo cha uchawi uliokubuhu wa mama yao kiasi cha kuwafanya waoneshewe vidole kila wakatizapo wakiwa na Nyembo. Wakamchukia sana kijana yule kiasi cha kumuanzishia mizozo na ghasia za kila aina mpaka hayati bwana Mtandi alipoamua kumchukuwa na kwenda kuishi naye Kigoma mjini baada ya kuombwa kufanya hivyo na dada yake. Hiyo ikawa ni neema kubwa kwa Nyembo kwani alinusurika kulelewa kichawi na pia akiwa huko alibahatika kusomeshwa mpaka kidato cha sita na mzee Mtandi, tofauti na nduguze walioishia darasa la nne na wengine la saba tu.



    ***



    Kwa kawaida ya genge la wachawi wa pale Kibondo ni kwamba ni lazima kwa kiongozi wao mkuu kuwa na mke, hivyo ilipolazimu kumsimika ukuu huo hayati Bi Masonganya, ililazimu pia apewe mke japo naye ni mwanamke. Mke huyu alipaswa kumfanyia Bi Masonganya kila ambalo mke humfanyia mumewe japo tendo kuu bila shaka lisingewezekana kwakuwa wote ni jinsia moja. Haikuwa taabu kumpata mke kwani mmoja wa wachawi aitwaye bwana Kalombola alimtoa binti yake pekee kwa heshma kubwa ili aoelewe na mkuu wake huyo mpya. Binti huyo aliitwa Masunga.



    Maisha yakaendelea huku bi Masonganya akiwa ni mume wa Bi Masunga, na wakati huohuo akiwa ni mke wa bwana Muhonge ambaye ndiye baba yao na akina Kungurume. Ilimlazimu Bi Masonganya kumchukua huyo mkewe na kuishi naye nyumbani kwake kitu ambacho kilipekea usiri ulioligubika jambo hilo kuvuja, ming’ono ikashamiri kwa majirani na hatimaye wilaya nzima na baadaye habari zikamfikia bwana Muhonge kuwa mkewe naye ni mume wa mtu. Ikawa ni balaa kubwa, mzozo na magomvi yaliibuka kwa kasi na hicho nd’o kilichopelekea kifo cha kutatanisha kwa bwana Muhonge. Hapo ndipo Bi Masonganya alipojinafasi na kujitandaza na mkewe huyo bila kificho…kila mtu akaamini sasa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miezi sita ya ndoa hiyo ya ajabu, hatimaye Bi Masunga akapata ujauzito, haikueleweka kirahisi nini ambacho Bi Masonganya alichomtenda Bi Masunga mpaka kushika ujauzito ule. Kama aliyeitegemea hali ile, Bi Masonganya kila siku akawa anamuosha na kumfukiza madawa ya kila aina Masunga mpaka zilipotimu siku zake za kujifungua. Na alipojifungua, Laahaullah mtoto alitoka kafanana kila kitu na Bi Masonganya(Baba yake), yaani mpaka kucha. Tukio hilo la ajabu lilizagaa karibu kila kona ya Kibondo kiasi cha kumfanya mtoto aliyezaliwa(Nyembo) kuwa mfano wa kivutio cha watalii wa ndani(wambea). Nyembo alikuwa vizuri tu huku akipata malezi kama wapatayo nduguze wengine aliowakuta japo kwake yeye Bi Masonganya alikuwa ni Baba.



    Hicho ndicho kilichowafanya watoto wa Bi Masonganya kumchukia Nyembo na kugombana naye mara nyingi mpaka mama Nyembo akawa anaingilia na hatimaye kusababisha ugomvi ule kuwa mkubwa zaidi. Bi Masunga alifariki Nyembo alipokuwa na umri wa miaka mitano na hapo ndipo ilipomlazimu Bi Masonganya amuombe kaka yake, mzee Mtandi amchukue ili kunusuru vurugu zilizokuwa zikiendelea kuota makucha. Nyembo akahamishiwa Kigoma, huko aliishi na mzee Mtandi mwenyewe pamoja na watoto wake kwa raha mustarehe hata akasahau habari za Kibondo. Ilipomlazimu mara mojamoja kwenda kumsalimu Bi Masonganya alikwenda japo hakukaa muda mrefu, na siku zote alizokaa huko muda mwingi aliutumia akiwa ndani tu na mama yake, kitu kilichowazidishia hofu nduguze kuwa atakuwa anarithishwa uchawi tu…na hicho ndicho kilichozidi kupalilia uadui wao.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog