Search This Blog

TANZIA - 4

 





    Simulizi : Tanzia

    Sehemu Ya Nne (4)



    Ilipomlazimu mara mojamoja kwenda kumsalimu Bi Masonganya alikwenda japo hakukaa muda mrefu, na siku zote alizokaa huko muda mwingi aliutumia akiwa ndani tu na mama yake, kitu kilichowazidishia hofu nduguze kuwa atakuwa anarithishwa uchawi tu…na hicho ndicho kilichozidi kupalilia uadui wao.



    ***CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Sasa leo amekuja tena Kibondo kwakuwa mzee Mtandi amefariki, na makubaliano ni kwamba angezikiwa palepale Kibondo hivyo ni lazima aje amzike baba yake mdogo(mjomba).



    “Ilumbi…” Aliita Bi Chakupewa ambaye ni dada yake na mama Kaguba, kisha akaaendelea kuongea kabla hajaitikiwa. “…Nadhani we’ si’ mgeni wa mambo ya humu ndani, sasa imekuaje tena unatuletea hiki kituko?” Alihitimisha Chakupewa huku akimsonta Nyembo kwa kidole chake. Wanafamilia wote wakajikuta wametazamana.



    “Ulitaka asije kumzika mzazi wake aliyemlea kisa magomvi yenu?” alijibu Ilumbi na kukazia tena “…nachojua mimi, Nyembo ni ndugu yetu fullstop…kama kuna makosa waliwahi kufanya wazazi wake basi sisi hayatuhusu kama yasivyomuhusu yeye.”



    “Nakwambia hivi Ilumbi kama udugu leo utauzika, ila huyu Nyembo humu ndani hakai labda mkamtafutie sehemu nyingine ya kulala. Angalia huko alipoingia tu majirani wakaanza kumzungumza, mnasababisha familia yetu ionekane ya kichawi, hivi tutaishi vipi na jamii yetu jamani? Alibwata mama Kaguba.



    “Sasa unatutishia kuvunja udugu? Aliyekuambia si’ tunashida na udugu nani? Udugu wenyewe huu wa nazi kukutania pakachani, acha upumbavu wako wewe…” Safari hii alibwata Lubambi, mtoto wa kiume marehemu. “…Iko hivi, aliyekufa ni baba yetu sisi japonanyi ni mjomba wenu. Sasa kama hamtaki tushiriki sote pamoja na Nyembo wala tusibabaishane tunaichukua maiti na kwenda kuizikia kwetu, kama ni uwezo nasi’ pia tuko fiti!” Majibu hayo ya Lubambi nd’o kama yalichochea vurugu, ikawa ni majibizano, majigambo na kila aina ya upuuzi mpaka baadaye kabisa walipouingilia ugomvi ule wazee wengine kutoka katika familia hiyo ambapo hekma na busara zao ziliwatuliza ndugu wale na kuwapatanisha. Maneno ya waze yaliwaingia sana akina mama Kaguba hasa pale waliposisitizwa kuwa Nyembo hakuwa mwenye hatia kamwe kwa kosa lililofanywa na wazazi huko nyuma, wakalainika ukizingatia hata ile hofu yao kuwa Nyembo alikuwa akikabidhiwa uchawi na marehemu Masonganya ilikwishapotea baada ya kupata ithibati mpya kuwa kama ni uchawi alikabidhiwa mtoto wao wenyewe, Kaguba. Kufikia hapo kidogo amani ikarejea na shughuli za maziko zikaendelea kupangiliwa.



    Suluhu yao ikawa ni pigo kwa kambi ya akina Kaguba waliokuwa wakiombea mzozo ule uwe mkubwa ili maiti iondolewe mle ndani ili Kaguba apate nafasi ya kuingia kule ufuoni akakichimbue kile kibuyu kinachomzuia kutoka nje ya nyumba kwenda kuwanga.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Saa kumi Alasiri baada ya kufanyika visomo vya dua maalum na sala kwa maiti, hatimaye jeneza la mzee Mtandi likabebwa na wanaume na kuelekea makaburini kuzika. Wanawake walibaki nyumbani wakilisindikiza kwa macho jeneza lile. Hakika kifo kile kiliwachoma na kuwaingia sana.



    Hiyo nd’o ikawa safari ya mwisho ya bwana Mtandi.



    ***



    Saa tisa usiku, kundi kubwa la wachawi likiongozwa na Binti Sambayu lilikusanyika kwa kulizunguka kaburi alilozikwa hayati Mtandi, wakiwa watupu kama walivyozaliwa. Ngoma na nyimbo za kichawi zilirindima kisawasawa, kila mmoja alijiachia atakavyo bila ya kujali ni athari gani atakayoacha kutokana na kubinuka akiwa mtupu mbele ya wenziye ambao wengine ni wa jinsia tofauti na yake. Mbali ya kuserebuka nyimbo hizo pia kulikuwa na vinywaji na vitoweo murua, Damu na nyama za watu, pamoja na pombe kali vilihusika.



    “Jamani mida inayoyoma, sasa tutekeleze kilichotuleta ili tutawanyike…karibu mkuu!” Aliongea Bi mkubwa mmoja ambaye alitapakaa vumbi kali ya makaburini kutokana mtindo wa kugaagaa wakati alipokuwa akiserebuka. Alipomaliza tu kuongea, wachawi wote wakaketi chini na hapo ndipo akasimama Binti Sambayu na kuanza kuongea.



    “Bila kupoteza muda napenda kuwapa salamu kutoka kwa mkuu wetu Kaguba anasema yuko pamoja nasi na kwamba siku si nyingi atajumuika nasi na kutatua matatizo yetu yote…” kufikia hapo vigeregere vikazimama, kisha akaendelea. “…pamoja na hayo ni kwamba tulikuwa tuwe na mazoezi makubwa mawili hapa leo. Moja ni kumkata rasmi ulimi Nyanzala ili aingizwe katika daftari letu la kudumu la misukule, na pili ni kumfukua bwana Mtandi na kumzindika kabla ya siku yake ya kukatwa ulimi. Ila kutokana na maagizo toka kwa mkuu Kaguba ni kwamba hatutomkata ulimi leo Nyanzala mpaka atakapokuja mwenyewe hivyo tutabakiwa na suala hili moja tu la kumfukua huyu bwana mjuaji!” Alipomaliza tu kusema maneno hayo binti Sambayu mara kijana mmoja aliyekuwa amejihifadhi kichawi chini ya miembe akaibukia akiwa amemshika mkono Nyanzala na kumkabidhisha kwa wachawi wale. Nyanzala aliyekuwa amevishwa kijigauni chepesi huku miguuni akiwa peku kama bata, alikuwa akitetemeka kama mtoto mwenye homa.



    Baada ya Nyanzala kuwekwa chini, sasa wakalisogelea Kaburi la hayati bwana Mtandi na kuanza kubinuka tena mahepe yao. Dakika chache tu Binti Sambayu akakipiga kwa nguvu chungu cheusi juu ya kaburi lile na hapohapo kaburi likapasuka na kuachia kijinjia chembamba.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Macho ya Nyanzala aliyekuwa ameketi jirani kabisa, yalishuhudia kupitia katika ufa huo uliopasuka hapo kaburini akichomoza maiti aliyevaa sanda nyeupe. Kutokana na upenyo huo finyu hapo kaburini, maiti ilikuwa ikichomoza kwa tabu sana mpaka takribani dakika tano maiti ikawa juu ya kaburi.



    Muda wote huo wale wachawi walikuwa wakiendelea kuimba kwa shangwe huku wakicheza na kufurahia tukio hilo. Maiti ile haikuwa maiti ki-ukweli maana ilipomwagiwa dawa fulani kutoka katika kibuyu kidogo cha binti Sambayu hapohapo ikainuka. Alikuwa ni Mzee Mtandi.



    Mara macho ya Nyanzala yakakutana na yale ya mjomba’ake mzee Mtandi. japo wote walikuwa kama wapumbavu tu kwa jinsi walivyopumbazwa akili na madawa. Nyanzala akaanza kulia japo bila ya kutoa sauti.



    Wakati mzee Mtandi akiwa amesimama kama mlevi wa dawa za kulevya, akashituliwa kwa kumwagiwa maji ya baridi yakifuatiwa na mijeredi ya nguvu! Akashituka kutokana na maumivu yale, na sasa akili zikawa zimeanza kumreja…hicho nd’o walichokuwa wakikitaka wale Wachawi. Kumzindua!



    Kwa kawaida Wachawi wale wakishamfufua mtu, humfanyia madawa yao pamoja na kumshitua kwa maji ya baridi na mijeredi ili kuiamsha akili yake ambayo ilidorora mchana kutwa tangu afukiwe kaburini na ndugu zake wakiamini amekwishakufa, kisha zoezi linalofuata ni kumfanyisha mazoezi. Huwa wao wanasimama na msukule wao karibu na kaburi alilofukuliwa kisha wanamuamuru akimbie mpaka sehemu waliyoweka alama yao halafu anarejea tena mpaka walipo wao…hufanya hivyo kwa takribani mizunguko mitano kabla hawajamzuia na kuondoka naye mpaka nyumbani atakapofikishiwa kwa shughuli nyinge zaidi. Hivyo na mzee Mtandi naye akaamriwa aanze kukimbia kama ilivyo desturi!



    ***



    Katika usiku huo mkubwa wakati wachawi wakifanya vitu vyao kule makaburini, huku nyumbani nako watu walikuwa wamelala isipokuwa Nyembo pekee aliyekuwa amejiegesha katika godoro lake aliloliweka juu ya turubai kubwa lilitandikwa chumbani humo. Kilichomfanya awe macho mpaka muda ule alikuwa akihangaika kuchimbua pale kilipochimbiwa kile kibuyu cha maangamizi cha hayati Masonganya, kilichomchelewesha na kumkawiza kukifikia ni hofu ya kushitukiwa na nduguze ambao baadhi yao walikuwa wamelala humohumo chumbani. Hakutaka kabisa kuonekana.



    Aliendelea kuchimbua taratibu na kwa umakini wa hali ya juu mpaka alipokifikia kile kibuyu. Alipofikia hapo akaacha kidogo zoezi hilo. Akaingiza mkono katika mfuko wa koti lake akatoa majani ya ‘Vibumbasi’ akayasambaza vizuri mikononi mwake na kisha akaingiza mkono katika kijishimo alichokichimba na kukitoa kile kibuyu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipohitimisha tu zoezi lile, haraka akatoka mle chumbani akiwa na kibuyu chake mkononi, akaelekea na mpaka uani kisha akaingia chooni ambako alianza kufanya kitu kikubwa kuliko umri wake.



    Hatua zote anazozipitia Nyembo, tangu kukifukua kibuyu, na kukibeba tena kwa ustadi wa kujikinga na majani ya vibumbasi na kukimbilia nacho chooni alizipata kupitia maelezo yaliyoandikwa na bwana Mtandi katika kijitabu chake cha kumbukumbu(Diary). Mchana kutwa wakati ndugu wakishughulika na mambo makubwa zaidi kimuonekano hapo msibani, Nyembo alikuwa makini akisoma kitabu hicho cha kumbukumbu ambapo mbali ya mambo mengine ikiwemo madeni, ndipo akakumbana na siri nzito ambayo mzee Mtandi aliisikia kutoka kwa Kaguba na Binti Sambayu na kuiandika humo kabla hajakutwa na ile hali ya sintofahamu wakati akiwasimulia akina Kungurume bahati na majani hayoya vibumbasi aliyakuta humo kwenye begi. Tabia hii ya kujisomeasomea taarifa muhimu, Nyembo alijizoesha kupitia huko shuleni alikokuwa anasoma na pia alijifunza kupitia kwa mzee Mtandi.

    “Akkhhhhh….OHHHHKH KHAAA NAKUFAAAAAAAAA.” Sauti ya Kaguba ilivuma kwa kasi kutokea chumbani alikolala. Ilikuwa ni kama mashetani fulani yaliyompanda kichwani. bila shaka ni kutokana na kitendo kilichofanywa na Nyembo kuingia chooni na kile Kibuyu. Watu wote wakaamka kwa mshituko.

    “HAAGHHAAAAAAA HATARIIIIIIIIII…CHOOOONI. NIFUNGULIENIIII NIKAUUUE.” Kaguba aliendelea kulalama kwa hasira kiasi cha kuwafanya wakubwa wote waingiwe na hofu na kihoro cha kujua nini kipo huko chooni.

    Wote waliamka na kujumuika pamoja isipokuwa Nyembo tu nd’o hakuonekana alikokwenda, hofu mpya ikawakabili.

    ****

    Kule makaburini nako mambo yalikuwa yakiendelea kama yalivyopangwa, tayari mzee Mtandi alikwishaanza kufanyishwa mazoezi na tayari alikuwa amekimbia karibu mzunguko wa pili.

    Wakati mzee Mtandi akikimbia mzunguko wa tatu, wachawi walishangaa ghafla lilipotokea jambo fulani lisilo la kawaida, pale ambapo mzee Mtandi badala aishie kwenye uzio wa makaburi ambako ndiko alipokuwa amewekewa alama ya kuishia katika mizunguko yote anayokimbia, na alifanya hivyo tangu mwanzo, sasa alipitiliza kwa kasi ya ajabu mpaka nje kabisa ya uga wa makaburi ambako kuna barabara inakatiza. Kama haitoshi mzee Mtandi akiwa katika kasi ya ajabu alitokomea gizani kabisa.

    Wachawi wote wakajua kilichotokea kuwa mzee Saadallah amewakimbia, haikuwa kitu cha kawaida kwa msukule wao ambaye wameshammwagia dawa na kumpunguza akili atoweke kwa mtindo ule. Bila shaka kuna nguvu ya ziada imetumika!

    “Haiwezekani…kuna namna hapa. MKIMBIZENIIIII,” Alliongea kwa mshituko na mashaka Binti Sambayu.

    “Mkuu ungemuangilia kwenye kioo chako kwanza maana sisi hatumuoni kwa upeo wetu!” alijibu kijana yule aliyemleta Nyanzala. Wakati mjadala ukiendelea ndipo ghafla tena ilipowadhihirikia hali mbaya zaidi kwao, ilikwa ni kama vile wamewekwa ndani ya boksi halafu mara wabinuliwe juu chini, mara kulia na kushoto. Waliyumbishwa bila kujielewa mpaka wakawa kama walevi au wanaojisikia ‘kizunguzungu’ huku wengine wakicheua nyama na damu za watu walizokula na kunywa. Nyanzala naye kama aliyezinduliwa kutoka usingizi akajikuta akili za kibinaadamu zikimrejea naye akatimua mbio kali kama mjomba wake, hakuna mchawi hata mmoja aliyeweza kumuangalia Nyamizi akitoweka kwa jinsi walivyokuwa wakiona maluweluwe ya kubinuliwa bila kujielewa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ***

    “We’ Kaguba una nini lakini?” Alisaili Bi Chakupewa.

    “Mamaaa na-ku-faa…nasikia kizunguzungu mamaaa!” Sasa Kaguba alianza kuongea, na mara akaanza kutapika. Kutokana na vimbwanga vya mtoto huyu kila mmoja akajua labda pengine alikuwa akijaribu kufanya ‘mchezo’ ndipo akakutana na dawa zilizozindikwa.

    “Ulikuwa unafanya nini lakini we’ mtoto?” Mama Kaguba naye alihoji kwa woga.

    “Mama nakufaaaa aakkkhh…mjomba Nyembo anatuuwa.” Aliendelea kulalama Kaguba.

    Baada ya Kaguba kumtaja Nyembo, ndipo kila mtu akawa kama aliyefungukiwa na kitu kichwani kwani muda wote wa tukio hilo, Nyembo hakuwemo mle ndani.

    “Jamani kwani Nyembo yuko wapi?” Alisaili Ilumbi.

    “Tuwaulizeni ninyi mliyelala naye huko ufuoni!” alijibu Kungurume.

    “YU-KO CHO-O-NI ANATAKA KUNIMALIZAAA AKKHH Uhuaakh!” Kaguba alijibu haraka huku akitoa milio ya ajabu isiyoeleweka kabisa. Haraka wote wakatoka mpaka uani ambako giza nene lililokuwa limetanda. Wakawasha taa na kuelekea mpaka huko chooni.

    Hamad!

    Wakakamkuta Nyembo akiwa amesimama katikati ya choo huku mikono yake miwili ikiwa imeshika kile kibuyu kilichozungushiwa shanga nyingi kwa juu huku kwa ndani kukiwa na vitu vya ajabu na kuogofya!

    “Ilumbi mnaonaa? Mnaonaa? Si’ tuliwaambia sisi kuwa huyu Nyembo si mtu mzuri mkawa mnamtetea!?” Alibwata kwa ghadhabu Mama Kaguba. Akina Ilumbi nao wakajikuta wakiduwaa tu na kumkodolea macho Nyembo ambaye alikuwa akikizungusha kile kibuyu chini juu, juu chini, mara kulia. Mara kushoto. Hakuna aliyeelewa akifanyacho zaidi ya kumuona kuwa ni mchawi tu.

    “Nyembo unafanya nini huku chooni saa hizi na hicho kibuyu?” Lubambi alimsaili Nyembo kwa kihoro na woga.

    “Unamuuliza anafanya nini wakati unamwona anawanga kabisa hapo, au unataka akuambie anasali?” Alidakia Kungurume.

    “Embu tulieni ninyi msiwe kama majuha…ningekuwa nawanga sasa inakuaje huyo mtoto wenu ambaye ndiye mkubwa wa wachawi apige kelele kiasi hicho?” Alijibu kwa kujiamini Nyembo kiasi cha kuwafanya wote mle chooni wazidi kubutwaika. Baada ya hapo Nyembo akaendelea kukizungusha kile Kibuyu chake, na hapohapo wakaanza kumsikia Kaguba akilia kwa sauti huku akiweweseka kama awali. Kufikia hapo sasa mama Kaguba chango la uzazi likamshituka akajikuta uzalendo ukimshinda akamvaa Nyembo ili amnyang’anye hicho kibuyu. Wakaenda mweleka mpaka chini, ikawa ni patashika ya haja!

    Wakati vurugu hiyo ikiendelea mara ghafla kikawakumba kioja kikubwa na cha nguvu kuliko hicho cha kumkuta Nyembo akihangaika na Kibuyu huko chooni. Wakati baadhi wakiwa chooni, kuna wengine walibaki wamesimama uani. Sasa hao nd’o walianzisha vurugu na kelele zilizowatoa wote kule chooni.

    “UWIIIIIII JAMANIII BABU MTANDI HUYOOO,” Alipiga kelele Kilanga, mtoto mdogo wa kike wa Kungurume, waliokuwa uani hapo wote wakamshuhudia mzee Mtandi akiingia ndani kwa kasi. Kusikia kuwa mzee Mtandi akitajwa kuonekana, kikazuka kimuhemuhe cha hali ya juu. Wakasambaana wote na kukimbilia ndani ambako mzee Mtandi naye akaingia. Japo Nyembo alitegemea kutokea kwa jambo zito kutokana na maelezo yaliyoandikwa kitaalamu kwenye kile kitabu cha kumbukumbu lakini naye kihoro kikamkumba, akajikuta akitimka na kuelekea ndani huku kile kibuyu akikiacha kule chooni kilipoanguka tangu alipokumbwa na mama Kaguba kilimponyoka na kuanguka chini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “WEEE LUBAMBI USIINGIE HUKO, MJOMBA ND’O AMEINGIA HUKO!” Chakupewa alimhadhari Lubambi asiingie chumbani ambako mzee Mtandi ameingia. Japo Lubambi alitaka kumuona kama ni kweli baba yake lakini hofu iliyomvaa ilimsukuma na kujikuta akikimbilia kule waliposimama nduguze. Haikuwa jambo jepesi kumwona mzazi wako aliyekufa na ukahakikisha mmemzika halafu ghafla atokee tena. Si rahisi hata kidogo.

    Mara tu baada ya Nyembo naye kuingia ndani, hakutaka kupoteza muda, akawasogelea ndugu zake ambao walijikuta wakipiga kelele za kumuogopa wakimwona tu kama mchawi.

    “Acheni upuuzi ninyi, nilichokuwa nakifanya huko chooni nd’o kimemrejesha mzee Mtandi, sikutaka kuwaambia mapema kwakuwa tungeharibu mpango mzima na yangetokea kama yaliyotokea wakati mzee Mtandi alipokuwa akiwasimulia ninyi alichokigundua…” Aliongea Nyembo kwa kujiamini kama ilivyo kawaida yake japo ndiyo kabisa alizidi kuwachanganya nduguze ambao hawakumwelewa kwanini alijua kuwa mzee Mtandi aliyekufa na kuzikwa kuwa angerejea? Na wapi alikipata kile kibuyu kilichofanya Kaguba awe anapiga kelele. Akaendelea Nyembo. “…haya tujivisheni ujasiri, tuingie chumbani tukajaribu kumtuliza mzee Mtandi ili tuzungumze naye na endap…” Kabla Nyembo hajafikisha neno lake mwisho kikazuka kizazaa kipya na cha kuogofya zaidi.

    Mlango wao wa kutokea uani ulisukumwa kwa nguvu, na hapohapo wote wakamshuhudia msichana akiingia kwa kasi kama anayekimbizwa. Wote kwa pamoja walimshuhudia na kumfahamu, alikuwa ni Nyanzala.

    “UWIIIIIIII JAMANI TUNAKUFAAA..NYANZALAAA!” Alipiga kelele za woga mama Kaguba, huku akisaidiwa na nduguze wengine akiwemo Ilumbi, Chakupewa, na wajukuu. Hakika ilikuwa ni siku ya ajabu sana kwao, hakuna aliyeelewa kama anoyaona kweli matukio yale ya ajabu au anaota. Nyanzala naye akajikuta akiwaogopa nduguze waliokuwa wametaharuki kwa kupiga makelele huku wakiparamia meza na viti vilivyokuwapo sebule hapo. Akajikuta akikimbilia chumbani ambako ndiko alikokimbilia mzee Mtandi!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog