Simulizi : Tanzia
Sehemu Ya Tano (5)
Nyanzala naye akajikuta akiwaogopa nduguze waliokuwa wametaharuki kwa kupiga makelele huku wakiparamia meza na viti vilivyokuwapo sebule hapo. Akajikuta akikimbilia chumbani ambako ndiko alikokimbilia mzee Mtandi!
Kelele kali za akina mama Kaguba ziliweza kuvuma sana kutokana na hali ya utulivu wa usiku mnene kama ule kiasi cha kuwaamsha majirani ambao baadhi wenye ujasiri walitoka na kuja kujumuika nao kujua kilichotokea huku wale wenzangu na mimi wakiishia kuchungulia madirishani mwao tu kama njiwa manga. Majirani walizidi kumiminika, na hapo ndipo walipokutana na kioja kile cha mwaka, kwamba watu wawili kutoka katika familia moja waliokufa na kuzikwa kabisa eti leo wamefufuka na kurudi nyumbani, tena kwa kufuatana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni mtafutano.
Wakati hayo yakiendelea, Kaguba alikuwa ametulia kimya, macho yakiwa yamembadilika na kuwa mithili ya Paka. Alikuwa akiona mbali sana, aliwaona wachawi wenzake wakiwa wametaharuki ovyo baada ya kuhangaishwa sana kutokana na mchezo uliokuwa ukifanywa na Nyembo katika kile kibuyu. Sasa walikuwa wamepata ahueni tangu kibuyu kilipoachwa peke yake chooni, wakawa kama mazezeta hivi wasioelewa kilichowakumba, na baada ya Binti Sambayu kupiga ramli yake kupitia kibuyu akagundua yaliyowakuta, akawaamuru wafuasi wake wote watawanyike, wakawa wanatimka mbio kuelekea majumbani huku yeye(Binti Sambayu) akifanza maarifa.
‘Kibuyu kipo chooni, kimbia haraka kakichukue na umuangamize huyo Nyembo haraka, halafu uwapoteze hao akina Nyanzala kabla hawajasema chochote, nasi tuko njiani tunakuja hukohuko vinginevyo tutakufa sote.’ Sauti ya Binti Sambayu aliyekuwa akikimbia ilimjia waziwazi kichwani Kaguba ikimtaka kukiwahi kibuyu kule chooni. Hakuna aliyeisikiasauti ile zaidi ya Kaguba mwenyewe.
‘Sawa’ Kaguba naye alijibu kwa kutuma hisia zake moja kwa moja kwa Binti Sambayu. Kisha Kaguba akakata mawasiliano hayo ya ki-hisia na kuanza kutoka pale alipokuwa ameketi.
Alipofika sebuleni, Kaguba aliwaangalia harakaharaka wazazi wake waliokuwa bado wametaharuki kIsha kwa kasi ya kustaajabisha akaanza kuelekea ulipo mlango wa kutokea nje ili akakiwahi kibuyu chake. Haraka Nyembo akahisi kitu cha hatari, damu ikamsisimka akajikuta akiacha kuzungumza na nduguze, na kumuangilia Kaguba ambaye alikuwa ameshakaribia kutoka nje. Haraka, na kwa kasi ya umeme Kungurume akatoka mbio ili amzuie Kaguba asitoke nje, lakini alikwishamchelewa. Kaguba alikuwa amekwishatoka uani.
******
Japo Kaguba alikwishatoka uani kabla ya kufikiwa na Nyembo, lakini hakupata nafasi ya kuufikia mlango wa chooni, Nyembo akawa ameshamfikia na kumkumba kama mchezo wa mieleka. Kaguba akaanguka chini na kuanza kugaagaa huku akilia kwa sauti kiasi cha kuwapa hofu wakubwa kule ndani ambao wote wakatoka kwa kasi ili wajue Nyembo amemtenda nini. Walipotoka hawakuona kilichotokea, zaidi ya kumwona Kaguba akihangaika pale chini karibu na mlango wa kuingilia chooni. Majirani waliojumuika walizidi kuchanganywa na mchezo ule unaondelea kutukia!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati Nyembo akiwa mle msalani akakiona kile Kibuyu kikiwa palepale kilipoangukia, lakini alisita kukigusa baada ya kukumbuka maelezo aliyoyakuta kwenye kile kitabu kilichoandikwa na mzee Mtandi ambaye sasa haijulikani aitwe hayati, msukule, ama maiti wa zamani! Kilichomsitisha Nyembo ni ni yale majani ya ‘Vibumbasi’…hakuwa nayo maana yalisambaa ovyo wakati wa ile mpishempishe. Kichwa kikamvurugika asijue la kufanye. Kumbukumbu zikamjia kuwa kuna majani kiasi aliyabakiza kwenye begi la mzee Mtandi kule chumbani, lakini sasa angewezaje kutoka mle maliwatoni na kumwacha Kaguba pale mlangoni akiwa peke yake, yaani amwachie fisi bucha? Haiwezekani.
Ambacho Nyembo hakukijua ni kwamba, kadiri anavyopoteza muda kufikiria nini chakufanya ndivyo genge la wachawi lilivyokuwa likizidi kuja kwa kasi katika nyumba ile ili kukiwahi kibuyu chao! Na kweli walibakiza kama mitaa miwili tu kufika hapo.
Baada ya tafakuri ya muda, Nyembo akaamua kutoka mpaka pale uani. Tayari uwanja ulifurika uamati wa watu, majirani na ndugu. Wote wakamlaki kwa macho tofautitofauti, wapo waliomchukulia kama shujaa, na wapo waliohisi labda naye ni mchawi tu. Hakujali!
“Nahitaji haraka majani ya vibumbasi yapo ndani ya Begi la mzee Mtandi!” Maneno ya Nyembo yakawafanya watu watazamane maana majani hayo ni mashuhuri kwa mambo ya kishirikina tu japo akina Kungurume wakakumbuka kauli ya mzee Mtandi muda mfupi kabla hajakumbwa na yale maswaibu, alipata kuwatamkia habari za majani hayo, pia kauli hiyo ilimfanya Kaguba amtazame kwa tahadhari sana Nyembo maana kusikia anahitaji majani yale kukampa jibu kuwa mtu huyo anaelewa hatua kwa hatua za kukitwaa kibuyu na hata kutishia uchawi wao. Lakini angefanyaje sasa? Akaanza kuizungusha akili yake.
“Ilumbi…au Lubambi, hebu nichukulie haraka hayo majani kwenye begi ndani, Laa sivyo sote hapa tutaangamizwa sasa hivi, nataka nikichukuwe Kibuyu ila sasa sipaswi kukigusa bila ya majani hayo,” Alisisitiza Nyembo baada ya kuona kama haeleweki hivi. Lakini bado haikusaidia kitu ilikuwa kazi bure tu, sawa tu na kumpiga konzi kinyago.
Kauli hiyo ya Nyembo ilipenya dirishani, na kuingia mpaka chumbani, chini ya uvungu wa kitanda walipojificha Nyamizi na mjomba wake. Sauti ya Nyembo haikuwa ngeni masikioni mwa mzee Mtandi hivyo Kauli hiyo ikamzindua na kumpa ishara fulani, ishara ya hatari kuwa Kibuyu tayari kipo chini ya himaya ya Nyembo na kwamba anahitaji ‘vibumbasi’ vya kushikia. Kwa jinsi anavyomjua Nyembo kwa utamaduni wake wa kusomasoma hivyo hakupoteza muda kujiuliza kuwa ametoa wapi taarifa za kibuyu kile hatari maana alimtambua fika kuwa atakuwa alisoma tu kumbukumbu alizoacha ameziandika kwenye kile kijitabu chake. Na kwakuwa alitambua utata wa jambo hilo hivyo ilimdhihirikia kuwa ingekuwa ni vigumu kwa wengine kumuelewa. Akachomoka tokea chini ya uvungu kama mshale, haraka akasimama na kuanza kuangaza huku na kule, akaliona begi lake likiwa limewekwa juu ya stuli, akalisogelea na kulifungua.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kulifungua na kupekuwapekuwa akayatambua majani ambayo ni yeye mwenyewe ndiye aliyeyaweka mle, yalibaki kidogo sana kiasi cha kumpa jibu kuwa yalitumika baadhi. Akili ya kibinaadamu ikaanza kumjia, akajuwa tu hata kuponyoka kwao kule makaburini bila shaka kulitokana na jitihada zilizofanywa pale Nyumbani…bila shaka na Nyembo. Akayachukua yale majani na kuanza kutoka nayo nje haraka.
Alipotoa uso wake tu pale uani, Loosalale uwanja wote ulivurugika, kelele za taharuki kutoka kwa majirani zikazizima, kila mmoja akiamini kuwa mzee Mtandi alikwishakufa, vije tena awepo pale. Ndugu nao utadhani nd’o wanamuona mzee wao huyo kwa maraya kwanza, maana nao waliungana na majirani wenzao na kukimbia ovyo. Wote wakaelekea ulipo mlango mkubwa wa kuingilia na kutokea uani ili watawanyike…na walipoukaribia tu mlango, ndipo kilipozuka tena kizaazaa kipya na cha kipekee!
Wakiwa hapo mlnango ndipo wakakutana uso kwa macho na kundi kubwa la watu zaidi ya kumi. Wengine wakiwa watupu kama walivyozaliwa huku wengine wakiwa wamejivisha vibwaya vidogo vilivyositiri sehemu nyeti tu za maungo yao, watu hao wakiwa wamejipaka pemba nyekundu na nyeupe katika miili yao, ukijumlisha na vumbi zilizowatapakaa nd’o kabisa walizidi kutisha. Watu hao ndiyo wale wachawi waliokuwa wakiserebuka kule makaburini kabla mzee Mtandi na Nyanzala kuwaponyoka na kufuatiwa na patashika iliyowavuruga kabisa. Hawakuwa japo na chembe ya aibu, maana akili zao zilikwishavurugika hivyo kwao wao, Kibuyu nd’o kilikuwa cha muhimu kuliko kitu chochote.
Hakuna aliyethubutu kuendelea kutoka nje, wote waliokuwa wakimkimbia mzee Mtandi wakiamini kuwa msukule umewatokea, wakajikuta wakipiga kelele kwa nguvu huku wakirejea tena kulekule walipotokea, ilikuwa ni bora kukumbana na mzee Mtandi kuliko kuvaana na genge hili la wachawi waliopagawa. Cha ajabu mzee waliporejea huku uani hawakumwona tena mzee Mtandi ila walikumbana na kioja kingine kilichowafanya wachanganyikiwe zaidi. Walimshuhudia Nyanzala akiwa anatokea mlemle ndani alikotokea mzee Mtandi, japo yeye(Nyanzala) alionesha hofu na woga wa haliya juu, alikuwa akitetemeka tu na kuhema juujuu.
Taharuki mpya ikaibuka ikiwa ni kukimbia ovyo tu bila muelekeo huku wakipamiana na kwenda mieleka mpaka chini. Nyanzala alipowashuhudia wale wachawi wakiingia kwa tambo mle ndani akakimbia kwa kasi na kurejea kule chumbani ambako alishindwa kubaki peke yake kwa woga uliomvaa baada ya mzee Mtandi kutoka.
Licha ya Pemba na vumbi vilivyowatapakaa wale wachawi, ila wote walitambulika kwa sababu ni wakaazi wa eneo hilo na huwa wanafahamika kwa michezo yao hiyo ya ingawaje hawakuwahi kukamatwa!
Hakuna hata mchawi mmoja aliyekuwa na mpango na Nyanzala, wote walikatiza kona mbele ya banda litumikalo kuanikia dagaa wakielekea sasa kule msalani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kule msalani nako, mambo yalikwishawiva. Mzee Mtandii aliamua kuifanya kazi mwenyewe, aliingia moja kwa moja msalani akifuatiwa na Nyembo, akiwa na ‘vibumbasi’ vyake mkononi, akakitwaa Kibuyu kile na baada ya manuizi tu akaanza kazi ya kukizungusha huku akikipuliza kama firimbi.
Laahaulah!
Hakuna hata mchawi mmoja aliyepiga hata hatua moja tangu kibuyu kilipoanza kuzungushwa. Walipamiana na kutupwa ovyo, wale huku, hawa kule. Vilio vyao vya kichawi vikaunguruma mle auani huku wakitapatapa kutafuta msaada. Iliwachukua muda mrefu wakihangaika hata majirani pamoja na wanafamilia waliokuwa wametawanyika, sasa wakarejea kushuhudia mtanange ule. Walikuwa wakilia kwa uchungu, fedheha, na kukata tamaa huku wakiomboleza kutaka msaada.
Wakati mzee Mtandi akiendelea kucheza na kile Kibuyu, ndipo Nyembo akatoka sasa huko msalani na kuwakuta wachawi wale waliokuwa wamezungukwa na kundi la watu, wakiendelea kutapatapa kama wagonjwa walio taabani bin Sambamaji.
Baada ya dakika kama kumi za kutapatapa pale chini, ghafla wale wachawi wakajihisi ahueni kidogo. Taabu zikawatoka kiasi, wakawa wanatweta tu huku wanaangaliana wenyewe kwa wenyewe. Vurugu na zogo kutoka kwa wakaazi waliozidi kumiminika pale vilitishia usalama wao maana kila mtu alikuwa akisema lake na kupanga hukumu yake dhidi yao.
“KAA CHINI MWANGA MKUBWA WE!” Nyembo alibwata huku akiwa amemtole macho Binti Sambayu aliyekuwa amesimama akitaka kukimbia. Binti sambayu alihisi kurejewa na nguvu hivyo akaamini muda wa kutoweka umewadia. Haikuwa hivyo. Hakujua kuwa ahueni ile imetokana na Nyembo kumwambia mzee Mtandi kuwa aache kidogo kuzungusha kile Kibuyu ili sasa aseme nao, sasa kutokana na ujuaji wa Binti Sambayu ikambidi Nyembo aliyekuwa amewasimamia wale wachawi pale uani ampe ishara nyingine mzee Mtandi akiwa kule msalani ili aendeleze kutoa kiminyo, naye bila ajizi akaianza tena kazi ile iliyozua tabu kwa wachawi wale. Walitaabika vilivyo, inaonekana kiminyo kiliwazidia mpaka baadhi wakaanza kutapika, huku wengine wakitokwa na haja kubwa na ndogo palepale ikiwa ni ishara mbaya kwa mchawi yeyote akikamatwa. Ishara ya kifo!
Kama haitoshi Nyembo akachukua mijedeli na kuwagawia wananchi wenye hasira kali kisha wakaanza kucharaza viboko vya nguvu, Wachawi walihangaika na kulia mpaka wakabaki hoi ndipo Nyembo akamwambia mzee Mtandi aache kidogo kazi yake. Akawasogelea karibu wale wachawi na kuwamwagia maji ya baridi kutoka katika ndoo aliyotoka nayo mle msalani, kisha sasa akaanza kusemanao kwa utulivu na umakini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
”Leo mkifanya mchezo mtakufa hapahapa…cha msingi ili mpate msamaha ni lazima mtueleze kila kitu, kila siri na kila mchezo mliokwishawahi kuufanya hapa wilayani kwetu na kwingineko…Mmenielewa?” Alibweka tena Nyembo. Wakamuitikia kwa vichwa tu huku nyuso zao wakiziinamisha chini kwa fadhaa. “…Kwanza kabisa nataka mtueleze kwanini mliwachukua kichawi akina Nyanzala na mzee Mtandi. Pili mtutajie watu wote mliowahi kuwaua na tatu mtueleze jinsi mlivyokuwa mkifanya kazi zenu za kichawi hatua kwa hatua, Sawa?” Nyembo alitamba. Muda huo akina mama Kaguba. Kungurume, Ilumbi, na wengine walikwishajongea eneo la tukio, wakiwa nyuma ya Nyembo wakimwona kama mkombozi wao licha ya kuwa mwanzo walimbeza na kumdhihaki.
“Simama juu we’ Binti Sambayu utoe maelezo!” Alifoka Nyembo, na hapohapo akasimama Binti Sambayu na kuanza kutoa maelezo huku umati wote ukiwa kimya!
SEHEMU YA KUMI
“Mimi ni kweli mchawi wa siku nyingi ila sikupenda kuwa mchawi jamani, nilirithishwa tu na hayati Bi…”
“NITAKUADHIBU TENA WEWE? SITAKI STORI HAPA, NATAKA UJIBU MASWALI YANGU NILIYOKUULIZA.” Alifoka Nyembo na kumfanya Binti Sambayu aanze kuelezea mambo mazito yawahusuyo wachawi wa hapo Kibondo na sehemu kadhaa wanazohusiana nazo kikazi.
“…Sisi ni wachawi ambao tulirithishwa tu uchawi kutoka kwa wazazi, mababu, na mabibi zetu. Uchawi wetu uko chini ya mzimu mkubwa uitwao GULUGUJA, Tumefunzwa na kukuzwa katika tamaduni za kichawi mpaka tukafuzu. Wengi wetu tuliingizwa humu tungali watoto wadogo japo kuna baadhi walishawishiwa na kuingizwa katika kikundi chetu cha uchawi wakiwa watu wazima…” Umati mkubwa uliofurika uani kwa hayati masonganya uliokuwa kimya ukisikiliza, ulishitushwa na ujio wa ghafla katika usiku ule wa mzee mmoja ambaye baadhi walimtambua na baadhi wakiwa hawajamtambua. Cha ajabu wakati mzee huyo alipoingia tu mle uani, hapohapo binti Sambayu akaanza kulia kwa sauti ya hofu na uchungu na kuwafanya wengi kuogopa.
Mzee yule bila ya kusalimiana na yeyote, akakatiza katikati ya watu, akamsogea binti Sambayu na kumnyang’anya kibuyu kidogo alichokua amekishikilia kisha akaingiza mkono kwenye kikapu chake cha rangi ya kaki kilichoathiriwa na uchafu mpaka kikaonekana ni cheusi, akakiweka kile Kibuyu na kisha akatoa kitu kama mkufu hivi uliosukwa kwa ukindu, akamvisha binti Sambayu shingoni. Baada ya hapo akarejea mpaka alipokuwa amesimama bwana Kungurume na kumpa mkono huku akimsalimu. Alikuwa ni Babu Gao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Msiogope jamani nimemvisha kitu kinachoitwa Mkanyafe yaani mkufu wa kifo, endapo atadiriki kusema uongo basi ataangamia na kufa hapahapa yeye na wafuasi wake wote waliopo hapa na waliopo huko majumbani mwao, kuna mambo mengi na ya ajabu ambayo anapaswa kuyaongea huyu mchawi…mimi nimetembea usiku huu kwa miguu kutokea huko kwangu mbali ili kuja kushiriki katika kuuona mwisho wao hawa watu wabaya.” Babu Gao aliongea kwa sauti yake kavu na ya kukoroma kisha akamuashiria Binti Sambayu aendelee. Naam binti Sambayu akasimulia historia yao ya kuingia kwenye uchawi na namna wanavyoendesha shughuli zao hatua kwa hatua.
“Ndani ya hiki kibuyu kuna nini hasa kinachofanya kiwe na nguvu na uwezo mkubwa kiasi hiki?” Nyembo alimsaili binti Sambayu baada ya kutoa historia yao ambayo haikuwa na umuhimu mkubwa sana.
“Humo kuna dawa za mitishamba tu zilizochanganywa na vitu vingine tofautitaofauti.”
“Ni vitu gani hivyo?”
“Aaa…hu.. ku..na nywele, mkaa na..” Kabla binti Sambayu hajafikisha neno lake mwisho watu walimshangaa akianza kuhangaika na kutapatapa huku mikono yake akiipeleka shingoni kujaribu kuuzuia ule Mkanyafe uliokuwa ukimkaba mpaka akashindwa kuhema na kuanza kukoroma. Alikoroma huku udenda ukimtoka na macho yakimlegea mfano wa mtu anaye karibia kufa.
“We’ si nimekukanya kusema uongo? Sasa unataka kufa si’ ndiyo eeh?” Babu Gao alimfokea binti Sambayu ambaye sasa hakua hata na uwezo wa kujibu zaidi ya kunyanyua mikono yake huku na kule kutaka msaada. Haraka Babu Gao akamsogelea na kufanya cha kufanya mpaka mkufu ule ukalegeza.
“Narudia tena, ukithubutu kusema uongo hapa leo utakufa…eleza ukweli wa kila kitu,” Alibwata Babu Gao. Watu walijikuta wakishangilia kwa tukio lile lililowafanya sasa waamini kuwa Wachawi wampatikana. Kufikia hapo sasa binti Sambayu akaamua kusema kila kitu kuhusiana na uchawi wao akihofia kuuawa na mkufu wa Babu Gao.
“…Naomba msituue jamani, ninaahidi kuwa hatutarudia tena mchzo huu wa uchawi, tumekoma jamani. Nitaelea…nitaeleza kila kitu…” Alilalama binti Sambayu huku akilia na kuendelea. “…ndani ya Kibuyu hicho kuna mchanganyiko wa vitu vingi sana. Kuna mafuta ya watu, ngozi za maalbino, nyongo za koboko na za simba, kitovu cha mtoto mchanga, moyo wa kondoo, utumbo wa mwanamke mjamzito…”
“Vitu vyote hivyo huwa mnavipataje?” alidakia Nyembo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“…Huwa tunwaua kwa hila watu tuwatakao, tukishawaua ndipo usiku huwa tunawachoma na kuwakamua mafuta yao, kama maiti ni ya mjamzito huwa tunampasua tumbo tunamkata utumbo wake, na kama ni ya mtoto huwa tunachukua kitovu chake. Pia huwa tunazifukua maiti za albino na kuchuna ngozi zao, hao Koboko na Simba huwa tunawatega kichawi ambapo tukishawakamata huwa tunachukua vitu kadhaa ndani ya miili yao huku wakiwa hai…”
“Lengo la vitu vyote hivyo ni nini hasa?” Alisaili tena Nyembo akiwa amewasimamia wale wachawi na mijeledi yake.
”…utumbo wa mwanamke mjamzito huwa tunauchanganya na madawa ya kienyeji kisha tunafukia katika njia panda basi hapo kama kuna mjamzito tuliyemkusudia, ataumwa uchungu na kuhangaika bila kuzaa mpaka atafariki. Na hizo nyongo za Koboko na Simba mara nyingi huwa tunazitumia kuwasukumizia hasira watu tuwatakao ambao hushindwa kujizuia na kujikuta wakifanya mambo wasiyoyatarajia kama vile kuwa na nguvu za ajabu na kumpiga mtu mpaka kumuua, au kujinyonga mwenyewe nk. Kitovu cha mtoto mchanga huwa tunakichangaya na majani yatumikayo kupikia mboga ya mlenda kisha tunamnuizia mtu tumtakaye ambapo baada ya kukizika hicho kitovu katika kaburi la mlemavu yeyote aliyepata kufariki, huku kwenu huyo tuliyemfanyia hivyo ataanza kuumwa sana na kukonda mfano wa muathirika wa Ukimwi, na hata mkienda kumpima hospitali huonekana na ugonjwa huo kumbe Laa!”
“Hebu tutajie majina ya watu mliowahi kuwauwa hapa Kibondo, pia ututajie namna ya vifo mlivyowaua…” Babu Gao alichombezaswali hilo akiwa na lengo maalum la kuwafanya wakaazi walichukulie lile tatizo kuwa si tu la akina mama Kaguba, bali ni la kwao wote. Alikuwa na uhakika kuwa wapo watakaouguswa na simulizi chafu za binti Sambayu. Na kweli hapo ndipo kazaazaa kilipoanza maana binti Sambayu alianza kutaja majina ya watu waliokufa zamani na siku za karibuni kwa vifo vya aina kwa aina. Baadhi ya waliotajwa kuuawa kwa ajali barabarani, magonjwa kama Ukimwi, vifo vya uzazi nk ndugu zao walikuwapo hapo eneo la tukio. Wapo waliolia kwa uchungu na wapo walioishia kutetemeka kwa hofu na kwa hasira, ndipo wakajitokeza wananchi wachache wenye ghadhabu na kuanza kuwashambulia kwa mawe na mikoma wachawi wale kiasi cha kuvuruga mjadala ule mtamu.
Wakati kichapo kikiendelea, ghafla wakaingia askari polisi pamoja waliokuwa wamearifiwa juu ya tukio hilo la ajabu. Walipofika tu wakaanza kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiendelea kuwasulubu wale wachawi, kisha baada ya utulivu kurejea, wakabaki na watuhumiwa wa Uchawi pamoja na wahanga wa tukio hilo pamoja na mzee Mtandi aliyetolewa kule chooni alipokuwa amesimama na Kibuyu chake ambapo walifanya nao mahojiano ya awali na kuamua kuwachukua na kwenda nao kituoni kwa ajili ya mahojiano zaidi. Pamoja na Wachawi, ndani ya gari ya Polisi waliingia akina Mzee Mtandi, Nyanzala na Kugurume.
Mara tu baada ya Polisi kuondoka, Babu Gao alikichukua kile kibuyu, akakifanya alivyojua na kukilipua moto. Kilipiga mlipuko mkali kama bomu kabla ya kuanza kuteketea mpaka kikaisha chote.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati Kibuyu kikiteketea, Wachawi wote waliokuwa ndani ya gari ya Polisi waliteketea na kufa wote. Cha ajabu kuna baadhi ya watu waliokuwa majumbani mwao, nao waliteketea kama ilivyokuwa kwa wale wachawi hivyo kudhihiri kuwa nao walikuwa ni wachawi tu japo siku ile hawakutoka kwenda kuwanga.
Huo ukawa mwisho wa Wachawi wote wa wilayani hapo.
Siku mbili baadaye baada ya Polisi kujiridhisha na kilichotokea huku wakiendelea na uchunguzi, waliwachia akina Nyamizi na mzee Mtandi ambao walirejea kwenye jamii yao wakiwa na mengi ya kusimulia familia zao.
TAMATI.
0 comments:
Post a Comment