Search This Blog

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU - 1

 





    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Safari Yangu Ya Kwanza Kuzimu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Nilisimama juu ya mlima mmoja mkubwa, mawingu yalikuwa yametanda angani huku radi zikianza kupiga mfululizo hali iliyoonyesha kwamba muda wowote ule mvua kubwa ingenyesha.

    Nilikuwa nikiogopa sana, pembeni ya mlima ule mkubwa ambao sikujua nilifikaje, kulikuwa na miti mingi iliyosababisha giza kuwa kubwa kitu kilichoniongezea hofu kubwa moyoni mwangu.

    Sikuwa na msaada wowote mahali hapo, nilijaribu kuangalia huku na kule nikiamini kwamba ningeweza kupata msaada lakini hakukuwa na mtu yeyote. Wakati nikijiuliza nilifikaje mahali pale, ghafla nikaanza kusikia vishindo vikubwa vikija kule nilipokuwa. Sikujua vilikuwa vishindo vya nani, nikabaki nikitetemeka kwani nilijua kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha yangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwili wangu ulikuwa ukitetemeka sana, nilitamani kukimbia kutoka mlimani hapo, kitu cha ajabu, sikuweza kukimbia, miguu ilikuwa mizito kuinuka, hivyo nikabaki nikiwa nimesimama tu.

    Ghafla, nikawaona watu zaidi ya ishirini wakija mbele yangu, walikuwa ni binadamu wa kawaida ila walikuwa na muonekano wenye kutisha sana. Walikuwa watupu, viunoni walivaa vitu kama ukili, nyuso zao hazikuwa zikionekana vizuri.

    Walikuwa wakinisogelea huku wakicheza wimbo ambao sikujua ulitoka wapi. Walikuwa wakiniangalia huku wakichekacheka kama watu wasiokuwa na akili fulani. Walitisha, nilitamani kuyafumba macho ili nisiweze kuwatazama lakini nilipotaka kufanya hivyo, nilishindwa pia.

    Nikabaki nikiwa nimesimama, dakika ziliendelea kwenda mbele, cha ajabu, idadi hiyo ya watu haikuishia ishirini tu bali iliendelea kuongezeka mpaka wakafika watu zaidi ya sitini.

    Baada ya dakika kama thelathini hivi, nikawaona watu kadhaa wakija pale niliposimama huku wakiwa wameshika beseni kubwa, nilipochungulia ndani, niliona damu nzito za watu, zilikuwa mbichi kabisa na kila aliyekuwa akizingalia, alionekana kuzitamani.

    “Umeshawahi kunywa damu wewe?” aliniuliza mwanamke mmoja, alikuwa na umri usiopungua miaka sabini, alikuwa hajiwezi lakini ndiye aliyeonekana kucheza kwa nguvu mahali hapo.

    “Sijawahi kunywa damu, na siwezi kunywa,” nilisema kwa sauti tena kwa kujiamini sana.

    “Hahaha....hahaha...hahaha...” niliwasikia watu wale wakicheka tena kwa nguvu kiasi kwamba nikahisi kwamba ngoma za masikio yangu zilitaka kupasuka.

    “Utakunywa tu, tena hadi nyama utakula,” alisema mwanamke yule na hapohapo kuanza kuwaita watu wengine ambao walikuwa na sinia kubwa, lilikuwa limejaza nyama za watu na pia walikuwa na jagi kubwa, hilo lilikuwa na damu nyingi.

    “Mlisheni naye ashibe, anaonekana ana njaa kali,” alisema mwanamke yule, hapohapo watu watatu wakanishika na kuanza kunilisha nyama zile na damu ile kinguvu.

    *****

    Nilishtuka kutoka usingizini, jasho lilinitiririka mno, mapigo ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida huku mwili wangu ukisisimka sana. Niliangalia saa yangu ya ukutani, ilionyesha tayari ilikuwa saa tisa usiku, nilipochungulia nje, giza totoro lilikuwa limetawala.

    Nikakaa kitandani, picha kamili ya ndoto ile ikaanza kunijia kichwani mwangu, nilikumbuka kila kitu kilichokuwa kikinitokea kuanzia wale watu walivyonifuata na kuanza kunilisha nyama zile.

    Huku nikiwa sifahamu kilichokuwa kimetokea, mara macho yangu yakaanza kuwa mazito, sikufahamu nini kilitokea, lakini ghafla nikajikuta nikiwa pembeni ya bahari moja kubwa, sijui kama ilikuwa ni Hindi, Pasifiki au bahari gani.

    Huku nikiwa ninajiuliza maswali hayo yote, kwa mbele nikamuona mwanamke mmoja aliyesimama juu ya maji, alivalia gauni kubwa jeupe, alikuwa na nywele ndefu mpaka mgongoni, miguu yake haikuwa kama yetu, ilikuwa ni kwato za ng’ombe, alininyooshea kidole na kuanza kuniita.

    Kiukweli niliogopa, sikutaka kumfuata lakini ghafla nikajikuta nikianza kupiga hatua kumfuata huku nikiwa na hofu kubwa moyoni. Sikuzama kwenye maji yale, na mimi nilikuwa natembea juujuu mpaka nilipomfikia.

    Alikuwa msichana mrembo mno, kwa kumwangalia harakaharaka ungeweza kusema kwamba alistahili kuwa mrembo wa dunia, alikuwa akitabasamu tu.

    “Hujambo Michael,” alinisalimia.

    “Sijambo, wewe nani?” nilimuuliza huku nikitetemeka, sikutaka hata aniguse.

    “Ninatwa Yusnath.”

    “Ndiye nani?”

    “Mimi ni msichana mrembo kuliko wote duniani na kuzimu, nimekuleta kwa ajili ya kukuonyesha mambo fulani hivi,” aliniambia huku tukiwa tumesimama juu ya bahari.

    “Mambo gani?” niliuliza kwa kuhamaki.

    “Mambo yanayofanywa na watu kisiri. Upo tayari tuondoke?”

    “Hapana, unataka twende wapi?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Kuzimu.”

    “Kuna nini?”

    “Kuna siri kubwa sana zimejificha, nataka nikuonyeshee watu wanaofanya mambo mabaya huku nyie mkiwaamini. Upo tayari?” aliniuliza.

    Sikuwa tayari lakini kilichonishangaza, eti nikakubaliana naye bila tatizo lolote. Mara ghafla, kwa mbali likaanza kuja wimbi moja kubwa likija kule tulipokuwa, naweza kusema kwamba ukubwa wake ulikuwa ni sawa na jengo lililokuwa na ghorofa sita, niliogopa sana, nikataka kukimbia kuelekea ufukweni, mwanamke yule akanidaka mkono, akaning’ang’ania nisimkimbie, nikaanza kupiga kelele huku wimbi lile likiendelea kutufuata pale tulipokuwa.

    Wala hazikuchukua dakika nyingi, wimbi lile likatupiga, tukaanza kuzama, nikaanza kupiga kelele za kuomba msaada mahali pale, ghafla nikajikuta nimetokea sehemu nyingine kabisa, ulikuwa mji mwingine ambao kwa kuuangalia harakaharaka, ulikuwa na majengo mengi yaliyonifanya kujiuliza, ilikuwaje kuhusu ile bahari? Mbona hatukuwa baharini tena?

    “Karibu kuzimu tuanze kazi,” aliniambia mwanamke yule, nikapigwa na butwaa baada ya kusikia kwamba pale nilipokuwa palikuwa ni kuzimu.

    *****

    Nilipigwa na mshangao mkubwa, sikuamini kama pale nilipokuwa kulikuwa kuzimu. Hakukuwa na watu, eneo zima lilikuwa kimya kabisa hali iliyonifanya kuogopa sana. Mwanamke yule Yusnath akaniambia nimfuate, nikafanye hivyo.

    Ardhi yao haikuwa kama hii yetu kwamba kuna mchanga, yao ilikuwa ni kama changarawe kwamba kama ukitembea pekupeku ni lazima uumie nyayo zako. Tulitembea huku nikiangalia huku na kule kana kwamba nilikuwa nikimtafuta mtu fulani.

    Hakukuwa na mazingira mazuri hata kidogo na kila hatua niliyokuwa nikipiga, nilitamani kurudi duniani, yaani kwa jinsi mazingira ya kule yalivyokuwa, sikuwa na hamu ya kuendelea kukaa.

    Tulitembea kwa mwendo wa taratibu na kuingia sehemu moja hivi. Ilikuwa ni sehemu yenye viumbe vingi mno. Kwa mbali walionekana kuwa kama binadamu lakini ukweli ni kwamba hawakuwa binadamu.

    Maumbo yao yalitisha mno, hawakuwa na vichwa kama hivi vyetu, vichwa vyao vilikuwa ni vya wanyama.

    Kuna wengine walikuwa na vichwa vya paka, macho makubwa mithiri ya machungwa, vichwani walikuwa na mapembe lakini cha kushangaza, miguu yao ilikuwa kwato za ng’ombe.

    Ukiachana na hao, kulikuwa na viumbe vingine vilivyokuwa na vichwa vya ng’ombe, walitembea huku miguu yao ikiwa mikubwa mno na mgongoni walikuwa na mabawa yaliyoonekana kuchoka.

    Kila nilipokuwa nikiwaangalia, waliniogopesha mpaka kipindi kingine kuyapeleka macho yangu pembeni kabisa. Kila tulipokuwa tunapita, kulikuwa na majagi makubwa yaliyokuwa na damu ndani yake.

    Duniani watu waliendelea kufa kwa ajali na kule kuzimu damu ziliendelea kukusanywa kama kawaida. Tulitembea mpaka kwenye jumba moja kubwa, lilionekana kuwa zuri lakini kwa nje kulisimikwa mafuvu ya watu na sehemu nyingine kuwa na miguu ya binadamu.

    “Unaiona hii?” aliniuliza huku akiiangalia ile miguu ya watu.

    “Naiona.”

    “Hii ilikuwa miguu ya maiti, ngoja nikuonyeshee kitu,” aliniambia na kisha ghafla kukatokea kitu kama televisheni na kuanza kutazama kile alichotaka nikitazame.

    Nililiona kundi kubwa la watu, ilikuwa ni usiku sana, walisimama sehemu moja ambayo kwa haraka sana niligundua kwamba ni makaburini. Kulikuwa na makaburi ya kila aina, sehemu nyingine majeneza yalikuwa nje huku sanda zikitundikwa juu ya makaburi, tena sanda nyingine zikiwa na damu mbichi kabisa.

    Niligundua kwamba kulikuwa na maiti ambazo zilichukuliwa pindi tu zilipozikwa na ndiyo maana damu zile mbichi ziliendelea kuwepo. Hapo, katikati ya watu kulikuwa na mtoto mmoja, alionekana kuwa na sura ya kipole lakini Yusnath akaniambia kwamba huyo ndiye alikuwa malkia huko duniani, yaani wachawi wote wa Tanzania walikuwa wakimuabudu yeye.

    Kazi kubwa iliyokuwa ikifanyika mahali hapo ni kufukua makaburi tu. Maiti zilikuwa zikihitajika kwa nguvu zote kwa ajili ya nyama ambayo huliwa kila inapofika siku ya alhamisi ambayo kwao kule kuzimu huwa ni siku ya sherehe.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ufukuaji wa makaburi yale haukuwa wa kawaida, yaani kulikuwa na mwanamke anasimama juu ya kaburi huku akiwa mtupu, anacheza kwa kukatika viuno huku wakati mwingine akikaa juu ya kaburi na kuanza kuyasugua makalio yake hapo kaburini na ghafla kaburi linaanza kujifukua lenyewe.

    Kuna maiti nyingine zilikuwa zikija juu huku zikiwa na sanda tu na nyingine zikiwa na suti. Zilikuwa maiti hizihizi ambazo zilikuwa zikizikwa hivi karibuni au kama hakukuwa na maiti mbichi, zoezi la kwenda mochwari huanza mara moja.

    Zile maiti zinapotolewa na kuonekana zimeanza kukauka, zoezi la kwenda mochwari huanza mara moja. Siku hiyo, hakukuwa na maiti iliyokauka, nyingi zilionekana mbichi kabisa na hivyo kuzichukua na kuziweka juu ya kaburi.

    Mambo yote yaliyokuwa yakitokea nilikuwa nayaangalia kwa macho yangu. Nilikuwa nikiogopa na kusisimka mwili lakini sikuwa na jinsi, kwa wakati huo nilitakiwa kuangalia kila kitu kilichokuwa kikitokea usiku huo.

    “Unamuona yule mtoto?”

    “Ndiyo! Amefanya nini?”

    “Yule ndiye kiongozi wenu duniani, yeye ndiye anayepanga ratiba ya kuyashughulikia makanisa na misikiti, yeye ndiye mpangaji wa kila kitu,” aliniambia Yusnath.

    “Anaishi wapi?”

    “Duniani.”

    “Sehemu gani?”

    “Hahaha! Hahaha! Hahaha!” alicheka Yusnath, ghafla, na mimi nikajikuta nikiwa nimesimama katikati ya makaburi, nilikuwa nimezungukwa na watu wengi waliokuwa watupu kabisa, sijui kama waliniona au la, lakini niliwasikia wakianza kucheka kwa pamoja. Nilipogeuka na kuangalia pembeni yangu, kulikuwa na maiti moja ya mwanamke mjauzito, ghafla, ikafumbua macho na kuanza kuniangalia.

    “Nisaidieeee....nisaidieeee....” ilisema maiti ya mwanamke yule, nilitamani kuzimia.

    Nilibaki nikitetemeka tu, sikuamini kile nilichokuwa nikikiona, maiti kuongea, tena ikiniomba msaada makaburini, hakika niliogopa mno.

    Maiti ile haikunyamaza, bado iliendelea kuniomba msaada mahali pale huku wachawi wengine wakibaki wakicheka tu. Sikujua ni msaada wa aina gani aliokuwa akiuomba kwani mimi nilikuwa mgeni mahali pale, hivyo sikujua ni kwa namna gani ningeweza kumsaidia.

    Wala hazikupita sekunde nyingi, nikaanza kujisikia kuwa kwenye hali ya tofauti kabisa, baridi kali likaanza kunipiga makaburini pale. Sikuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwani hakukuwa na siku ambayo nilihisi baridi kali kama siku hiyo usiku.

    Nilikwishawahi kukaa Mbeya, Iringa na hata Arusha lakini sikuwahi kusikia baridi kama nililokuwa nikilisikia Makaburini hapo kulijaa mauzauza mengi yaliyonifanya niogope mno na kujiona kama nilikuwa sehemu moja iliyonifanya nihisi kwamba muda wowote ule kuanzia sasa ningekufa.

    Huku nikihisi baridi kali kiasi cha kujishika vilivyo kwa staili ya kuipitisha mikono kifuani mwangu, ghafla nikaanza kusikia sauti za watoto wakilia kwa sauti za juu kabisa. Sikujua watoto hao walikuwa wapi zaidi ya kusikia sauti hizo pale kaburini.

    Nilianza kuangalia huku na kule ili kuona ni wapi watoto hao walipokuwa, baada ya sekunde kama ishirini nikawaona wanawake kama kumi wakisogea pale kaburini huku wakiwa wamewabeba watoto waliokuwa kwenye sanda, wanawake hao walikuwa kama walivyozaliwa.

    “Hao ni watoto kutoka mahospitalini, wazazi wao waliwazaa lakini wameonekana kwamba wamekufa. Kiukweli, hawajafa bali tunawachukua hasa tunapokuwa na uhitaji wa kula nyama,” aliniambia mwanamke yule kwa sauti ya juu.

    Hapa nikagundua kitu kwamba kwa kipindi chote nilichokuwa hapo makaburini, hakukuwa na mtu aliyekuwa akiniona zaidi ya ile maiti tu na ndiyo maana alipokuwa akisema kwamba anahitaji msaada, wale wachawi wengine walikuwa wakicheka tu kwa kuona kama alikuwa akiongea peke yake.

    Niliwaonea huruma watoto wale waliokuwa wakilia tu, mbali na hao, nikawaonea huruma wanawake waliokuwa wakiwazaa watoto hao na kuona kwamba wamekufa na wakati ukweli wa mambo ni kwamba hawakufa zaidi ya kuchukuliwa na kupelekwa kwa ajili ya kuliwa nyama tu.

    “Lete sinia,” alisema mwanamke mmoja, alionekana kuwa kiongozi chini ya yule mtoto mdogo. Sinia likaletwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndani ya sinia lile kulikuwa na kisu kikali kilichokuwa kimefungwa kitambaa chekundu. Hakikuwa kisafi, japokuwa ilikuwa ni usiku na mahali pale kulikuwa na giza lakini niliona damu zilizoganda zikiwa katika kisu kile hali iliyoonyesha kwamba kilitumika sana katika kukata nyama za watoto makaburini hapo.

    Kwa macho yangu nikashuhudia watoto wale wakianza kuchinjwa na mwanamke yule. Hakuonekana kuwa na huruma hata mara moja, alianza kumchinja mtoto wa kwanza huku kila damu ilipokuwa ikitoka, alikinga mdomo wake na kuanza kunywa.

    Niliumia zaidi, kitendo kilichokuwa kikiendelea makaburini hapo kilinitisha zaidi kiasi kwamba kuna kipindi sikutaka kabisa kuangalia zaidi ya kutaka kuyafumba macho yangu. Nilipojaribu kufanya hivyo, sikuweza, macho yangu yaliendelea kuangalia kile kilichokuwa kikiendelea.

    “Imetosha, naomba unitoe hapa,” nilimwambia Yusnath.

    “Bado, kuna mengi ningependa uyafahamu hapa makaburini na kuzimu, kuwa mvumilivu,” alisema mwanamke yule.

    Ndugu yangu, makaburini kunatisha, usione kwamba unapita nyakati za mchana basi ukajua kwamba hata usiku huwa hivyohivyo tu. Huwa ninawashangaa hata wezi wanaokwenda makaburini nyakati za usiku na kufukua makaburi kwa ajili ya kuchukua vitu alivyozikwa navyo maiti.

    Kwa kile nilichokuwa nikikiona usiku ule, kilikuwa ni cha kutisha mno. Baada ya kuhakikisha kwamba watoto wpote wamechinjwa, mwanamke yule akaanza kuwakatakata vipande.

    Wachawi wengine wakaanza kuzigombania nyama zile kama tunavyogombania vitu fulani kwenye minada hasa masokoni. Kila aliyefanikiwa kuzipata nyama zile, alizitafuna harakaharaka kama mtu aliyeambiwa kwamba asiungefanya hivyo basi angepokonywa.

    Ilikuwa kama sherehe kwao, wakaanza kuzila zile nyama huku wengine wakijilamba kuonyesha kwamba zilikuwa tamu mno. Niliendelea kusimama mahali pale mpaka walipomaliza na ndipo mwanamke yule aliyekuwa akicheza kama alivyozaliwa akalifuata kaburi moja na kuanza kucheza huku akiyasugua makalio yake katika kaburi lile.

    Kama lilivyokuwa kaburi la kwanza, na lile likaanza kujifukua na baada ya dakika kadhaa, moshi mzito ukaanza kufuka na maiti moja kutoka huku ikiwa na sanda. Alipoifunua, ilikuwa maita ya mwanaume mmoja, alionekana kuwa mzee kama wa miaka sitini.

    Wachawi wale wakaanza kucheka sana, walicheka huku vicheko vyao vikiwa kero masikioni mwangu kwani sikufurahia kabisa kile walichokuwa wakikifanya makaburini pale.

    Walipoona kwamba maiti imetoka ndani ya lile kaburi, walichokifanya ni kuiweka pembeni na kisha mwanamke yule aliyekuwa na kisu kusogea na kuanza kumkata tumbo mpaka alipohakikisha utumbo unatoka, akauchukua na kuanza kuutafuna huku wenzake wakimwangalia kwa matamanio makubwa.

    Katika hili ngoja nikwambie kitu kimoja jinsi ukweli wa mambo ulivyop. Si maiti zote zinazozikwa huwa na viungo vilivyokamilika, kwa mfano maiti hii ya huyu mzee, haikuwa na sehemu za siri, nahisi zilikuwa zimekatwa tangu ilipokuwa mochwari ambapo biashara ya viungo vya maiti hufanyika mara kwa mara.

    Nilijiuliza kama wachawi wale walikuwa wakihitaji kuitafuna maiti yote au la kwani hawakuonekana kutosheka, yule mwanamke mchovumchovu alipokuwa akikata kipande na kula, kilichofuata alikikata na kuwapa wenzake ambao walivipokea kwa shangwe na kuanza kula.

    “Nataka niondoke,” nilisema huku nikiwa sitaki kuendelea kuwa mahali hapo.

    “Subiri kwanza,” aliniambiaYusnath.

    “Nisubiri nini sasa? Sitaki kuangalia zaidi,” nilimwambia huku nikionekana kukasirika.

    “Hutaki kumuona mkuu wa makaburini?”

    “Mkuu wa makaburini?”

    “Ndiyo! Kila sehemu huwa kuna mkuu wake, subiri, muda si mrefu atafika mahali hapa, usiogope,” aliniambia Yusnath.

    Nikaanza kusubiria, nikashangaa nikiingiwa na hamu ya kumuona huyo mkuu wa makaburini.



    Huu ni mwanzo wa hadithi yetu hii ya kutisha na kusismua. Muendelezo wake utakuja siku ya Jumatatu, kuna mengi yanaendelea kwa wachungaji na mashehe lakini huyajui, kupitia simulizi hii utakwenda kufahamu mengi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-

    Nilikuwa nikijifikiria kuhusu huyo mkuu wa makaburuni aliyetarajiwa kufika mahali hapo, sikujua alikuwa vipi na alifanana vipi. Wachawi wale waliokuwa makaburini pale waliendelea kula nyama za watu.

    Zilipita kama dakika mbili hivi, ghafla wachawi wale waliokuwa wakizungumza yao huku wakisherehekea kwa kula nyama zile nikawaona wakikaa kimya na kiviinamisha vichwa vyao chini kama ishara ya kutoa heshima fulani.

    Hapohapo nikaanza kusikia tena baridi kama nililolisikia kipindi cha nyuma. Kwa wakati huu, baridi lile liliambatana na upepo mkali huku nikisikia majani ya miti yakilia vuuu vuuu muda wote.

    Mara nikaanza kusikia milio mikubwa kama ngurumo za radi makaburini pale huku kwa mbali kukiwa kama na tetemeko la ardhi. Kiukweli niliogopa lakini nikajua ndiyo kwanza yule mkuu wa makaburini alikuwa akifika mahali hapo, nilichokifanya ni kusubiri ili na mimi nimuone.

    Kwa mbali nikaanza kumuona mtu mkubwa sana akija, alionekana kuwa na mwili mkubwa kama walivyo wacheza mpira wa kikapu wa Marekani. Alikuwa amejazajaza. Alipokuwa kwa mbali nilimuona kuwa binadamu wa kawaida kwa sababu ya giza lakini mara aliposogea kule walipokuwa wale wachawi ndipo nikagundua kwamba hakuwa binadamu wa kawaida.

    Mwili wake ulikuwa na manyoya mengi kama simba, miguu ilifanana na miguu ya sokwe, hakuwa na uso wa binadamu, alikuwa na uso wa mbweha huku kichwani akiwa na mapembe makubwa mithiri ya urefu wa chupa ya soda na masikio makubwa mithiri ya sahani ya chakula.

    Jitu lile la ajabu lilipokuwa likitembea, bado wachawi walikuwa wameviinamisha vichwa vyao chini kama kumpa heshima yake, lilitembea mpaka mbele kabisa, juu ya kaburi moja ambalo kwa juu kulikuwa na sinia jingine lililokuwa na nyama na jagi lenye damu za watu kisha kuanza kula.

    Hakuwa akitafuna kama binadamu wa kawaida wanapotafuta vitu bali alikuwa akitafuna kana kwamba alitafuta kitu kigumu tena alichotakiwa kukimaliza kwa haraka sana.

    Nilishindwa kuvumilia kubaki mahali hapo kwani kila nilipokuwa nikiliangalia lile jitu la kutisha, mwili wangu ulikuwa ukisisimka tu, nilichokifanya ni kumwambia Yusnath kwamba ninataka kuondoka.

    “Umeridhika?” aliniuliza.

    “Ndiyo! Naomba tuondoke,” nilimwambia.

    Akaunyoosha mkono wake, ghafla pale nilipokuwa nikaanza kuvutwa lakini sikukiona kile kilichokuwa kikinivuta. Nilipelekwa mpaka kule alipokuwa Yusnath na aliponishika mkono tu, tukapotea na kuibukia kule mlimani.

    Pale mlimani hatukukaa sana, akaniambia niyafumbe macho yangu kwani sehemu tuliyokuwa tukienda ilikuwa na watu wengi lakini hiyo njia ambayo tulitakiwa kuipita ilikuwa na mauzauza mengi ambayo hakutaka niyaone. Hilo halikuwa tatizo, nikayafumba macho yangu.

    Ghafla tukaibukia sehemu ambayo ilikuwa na watu wengi mbele yetu, watu wale walikuwa wameviinamisha vichwa vyao, walikuwa wengi zaidi ya watu elfu moja. Nikaanza kujiuliza watu wale walikuwa mahali pale wanafanya nini.

    “Hawa ni wenzako kutoka duniani ambao wamefika hapa kwa ajili ya kumuabudu mkuu wetu,” alinijibu Yusnath japokuwa swali lile nilijiuliza moyoni mwangu na sikujua alijuaje kama nilijiuliza vile.

    “Kuna ninaowafahamu?”

    “Wapo wengi tu, unataka kuwaona?”

    “Ndiyo!”

    “Basi subiri!”

    Niliendelea kusubiri, nikawa na kiu kubwa ya kutaka kuwaona hao watu waliokuwa mahali hapo ambapo Yusnath aliniambia kwamba kulikuwa na wengine niliokuwa nikiwafahamu kabisa.

    Nilisubiri mpaka baada ya dakika kadhaa, nikasikia muungurumo mkubwa mithiri ya simba, Yusnath akaniambia nifumbe macho kwani yule aliyekuwa akija ndiye alikuwa kiongozi wao, yaani shetani mkuu.

    Kwanza nikajifanya kupinga kimoyomoyo kwani nilihisi kutokana na mahali hapo kuwa usiku basi Yusnath asingeweza kuona kama macho yangu hayakufumbwa bali nilikuwa naangalia kisirisiri tu.

    Muungurumo ule uliendelea kusikika na mara kule ambapo Yusnath aliponaimbia kwamba ndiyo ingekuwa njia ya shetani kufika mahali hapo kukaanza kufuka moshi mkubwa na mzito, tena ulikuwa ukifuka kwa kasi kubwa.

    Nilibaki nikiangalia tu, ghafla nikaanza kuyaona macho yangu yakiwa mazito. Nilijitahidi sana kuyaacha wazi lakini ikashindikana, nikashtukia yakiwa yamefumba kabisa kitu kilichonifanya nikubaliane nacho.

    Nikasikia kishindo kikubwa cha mtu aliyekuwa akitembea, kishindo kile hakikuwa cha kawaida hata kidogo na alikuwa akitembea kuelekea kule kulipokuwa na watu wengi waliokuwa wameinamisha vichwa kama ishara ya kumuabudu.

    Sikujua alikuwa akifanya nini, ila baada ya dakika kama kumi, nikaambiwa niyafumbue macho yangu, nikafanya hivyo. Yule shetani hakuwepo tena, alikuwa amekwishaondoka na nilipowaangalia wale watu ambao waliyainua macho yao, sikuamini kabisa kama watu kama hao ningeweza kuwakuta mahali hapo.

    Mtu wa kwanza kabisa kumuona, aliitwa Fabian Joseph. Huyu alikuwa mchungaji wa kanisa fulani hivi lililokuwa maarufu sana huku duniani nchini Tanzania. Waumini wengi walikwenda kwake kuabudu, aliponya wagonjwa kwa kuwapaka mafuta ambayo kwake alisema kwamba aliyatoa Israel.

    Viwete walitembea, hakufanya hivyo tu bali kulikuwa na miujiza mingi aliyokuwa akitokea kanisani kwake. Leo hii, mchungaji huyo ambaye alijiita mtume, naye alikuwepo huko kuzimu akipewa nguvu.

    Hebu ngoja nikwambie vizuri kuhusu huyu mchungaji.

    *****

    Kanisa lilianza kama utani, nakumbuka kipindi kile kulikuwa na washirika kama wanne, watu wengi waliokuwa wakipita karibu na kanisa lile, walikuwa wakishangaa ilikuwaje mchungaji awe na nguvu ya kutoa huduma na wakati watu walikuwa wachache sana.

    Watu tulipuuzia, mchungaji yule ambaye alipenda sana kujiita mtume akaanza kuchapisha matangazo na kuyabandika mitaani kwamba alikuwa akiponya magonjwa mbalimbali, wanawake waliokuwa tasa waliitwa pia kwa ajili ya kuwekewa mikono na kupokea uponyaji.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hilo halikuwafanya watu kulisogelea kanisa lile kwani kitu walichokuwa wakikihitaji ni kuona miujiza ili waamini. Baada ya mwezi mmoja, watu walewale wanne waliokuwa ndani ya kanisa lile wakaanza kuwaambia watu wengine kwamba kulikuwa na miujiza ilikuwa ikitendeka hivyo watu wawapeleke wagonjwa kwa mtume yule.

    Kama unavyojua binadamu kuna kitu kujaribu. Kuna mwanamke aliyekuwa akiishi karibu na mtaa uliokuwa na kanisa lile, miaka nenda rudi alikuwa na kibiongo. Watu walimuonea huruma sana lakini baada ya kusikia kile kilichozungumziwa kuhusu mtume na miujiza aliyotarajiwa kuitoa, mwanamke yule akaingia.

    Sijui nini kilitokea kanisani lakini siku moja baadae nilipomuona mwanamke yule, hakuwa na kibiongo. Hapo ndipo watu walipoanza kuamini kwamba ile miujiza iliyokuwa ikitangazwa kweli ilikuwa ikifanyika, kanisa likaanza kujaza watu.

    “Nilifahamu hilo tu, hebu niambie kingine nisichokijua,” nilimwambia Yusnath.

    “Subiri,” aliniambia na kunipeleka sehemu iliyokuwa na kitu kikubwa kama televisheni na kuanza kunionyeshea maisha halisi ya mchungaji yule.

    Lile kanisa halikuwa kanisa kama tulivyokuwa tukiliona, lilikuwa pango kubwa ambalo lilikuwa na muonekanao wa kichwa cha paka, mlangoni kulikuwa na miti mikubwa iliyokuwa imesimikwa huku juu yake kukiwa na mafuvu mawili ya binadamu na mafuvu mengine ya mnyama nisiyemfahamu.

    Mlangoni hapo kulikuwa na mtungi mkubwa wa damu, kila mshirika aliyekuwa akiingia kanisa, ilikuwa ni lazima kuinama mlangoni kisha kuingia. Unapoinama pale mlangoni, unauinamia ule mtungi bila kujua na katika hali ambayo sikuifahamu, kuna kiasi kidogo cha damu unachangia katika mtungi ule.

    Unajiona kwamba umevaa nguo lakini unapouvuka mlango wa kuingia kanisani, nguo zako zinaachwa mlangoni na wewe kuingia mtupu.

    Kanisani mule hakukuwa na washirika tu bali kulikuwa na viumbe vingine vya ajabu ambavyo kazi zao zilikuwa zilezile za kuwavuta watu. Viumbe hivyo vya ajabu havikuwa ndani ya kanisa tu bali vilikuwepo mpaka pale nje.

    Ushawahi kupita nje ya kanisa fulani, unasikia kuwa na hamu ya ghafla kuingia kanisani humo kwa ajili ya kuabudu? Yaani moyo wako unakusisimka na kutamani zaidi uingie. Ndugu yangu, hiyo inakuwa ni kazi ya hivyo viumbe vya ajabu ambavyo husimama nje na kukuvuta wewe.

    Nilimuona mchungaji yule akiwaombea watu, mkononi alikuwa na kitambaa cheupe, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwapiga watu na kile kitambaa ambacho Yusnath aliniambia kwamba kilikuwa chao na walimpa kwa ajili ya kufanyia kazi hiyo.

    Mtu anapopigwa na kitambaa kile, kwanza akili yake inachanganyikiwa, hakuna kitu kingine anachokipenda zaidi ya kuingia kanisani humo na huwa mtumwa wa moja kwa moja.

    Mambo niliyokuwa nikiyaona ndani ya kanisa lile yalinishtua sana. Pembeni ya kiti cha mchungaji kulikuwa na joka kubwa, kazi yake ilikuwa ni kukaa hapohapo huku akiwaangalia washirika.

    Ukiachana na joka lile, kulikuwa na joka jingine ambalo lilikuwa likitembea huku na kule, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwatemea watu mate ambayo Yusnath aliniambia kwamba mara unapotemewa mate yale, hata kama kuna mtu atakuja na kukwambia yule mchungaji ni mchawi, mzinzi, huwezi kuamini na unaweza kugombana na mtoa taarifa.

    “Kumbeeee....” nilisema.

    “Kumbe nini?”

    “Nilipokuwa nikipita nje ya kanisa lake nilitamani kuingia,” nilimwambia.

    “Hiyo ndiyo kazi ya vile viumbe, kuwavuta nyie tu.”

    “Sawa. Kuna kingine?”

    Hakutaka kuniambia hivihivi tu, alitaka kunionyeshea kila kitu kupitia televisheni ile. Nilimuona mchungaji akichukua mafuta fulani hivi, alijipaka mikononi, alipokuwa akimuona mshirika mwanamke mzuri, alikuwa akimfuata na kumpaka mafuta yale na kumwambia kwamba yalitoka kwa Mungu kumbe hakuna lolote lile.

    Baada ya kupakwa mafuta yale, akili ya msichana huyo inachanganyikiwa, muda mwingi anamuwaza mchungaji na mwisho wa siku kulala naye kitanda kimoja.

    Kila nilichokuwa nikikiangalia, kilinifanya nichukie, nilikuwa mkristo, lakini sikuwa mtu wa kwenda kanisani lakini yale yaliyokuwa yakifanywa kwa baadhi ya makanisa likiwepo lile la mchungaji huyu, lilinisikitisha sana.

    “Unajua watu wanaponywa vipi magonjwa yao?” aliniuliza Yusnath.

    “Hapana! Inakuwaje?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Njoo huku,” aliniambia, akanishika mkono na kuanza kuelekea katika chumba kimoja.

    Kilikuwa kikitisha sana, kulikuwa na maiti nyingi zilizokuwa zimetobolewatobolewa, sikujua na nini lakini nyingine zilivarishwa sanda nyeupe kabisa zisizokuwa na doa hata kidogo.

    Chumbani mule kulikuwa na milio ya ajabu, wakati mwingine ilisikika milio ya paka lakini wakati mwingine ya bundi, kila nilipoisikia, niliogopa sana. Yusnath hakutaka kujali, aliendelea kunishika mkono na kuelekea mbele zaidi huku sakafuni kukiwa na damu nyingi zilizokuwa zikinuka mno.

    Tukafika sehemu moja iliyokuwa na uwanja mkubwa, sikujua kama ilikuwa makaburini au la, alichoniambia ni kwamba nisimame imara, nikatii, akaniambia kwamba kuna mambo mengine ya mtume huyo nitayaona, nikamwambia hakuna tatizo, hivyo nikaanza kusubiri huku mwili ukinisisimka mno kwani sehemu ile ilitisha sana.





    Nilianza kuyaona mambo kama mtu anavyoona maono au kuota ndoto fulani hivi. Nilimuona mchungaji yule akiwa amevalia vazi la ajabu sana, lilionekana kuwa kama kaniki fulani nyeusi tii, uso wake ulikuwa tofauti kabisa kwani ulipakwa na vitu ambavyo vilioonekana kama masizi.

    Alikuwa akitisha sana, nilimkazia macho kumwangalia kwa umakini kile alichokuwa akikifanya. Alikuwa amesimama katika uwanja wa makaburi, alisimama katikati ya makaburi mawili, moja lilikuwa la mtoto mdogo na moja likiwa na mtu aliyekuwa na ulemavu wa ngozi (albino).

    Mchungaji yule alikuwa akizungumza maneno nisiyokuwa nikiyaelewa huku akichezacheza wimbo ambao sikuwa nikiusikia. Kuna kitu fulani kikaibuka ghafla juu ya kaburi lile la mtoto aliyekuwa na miaka minne kabla ya kufariki.

    Nilikitolea macho kile kitu, sikuweza kukifahamu lakini alipokichukua na kukifunga mkononi mwake, nikagundua kwamba ilikuwa ni hirizi iliyofungwa kwa kitambaa chekundu.

    Mchungaji yule aliendelea kukaa pale makaburini huku akizungukazunguka huku na kule, ghafla, likaja kundi la wachawi wengi, walikuwa na muonekano kama aliokuwa nao yeye, walimfuata na kuanza kuzungumza naye maneno mengi ambayo sikuweza kuyasikia.

    Miongoni mwa watu wale waliokuwa wamemfuata, alikuwepo mtu ambaye nilimfahamu sana kwa sura, hakuwa mgeni kabisa machoni mwangu, alikuwa mchungaji mwingine ambaye naye nitakupa stori yake hapo baadae nikimalizana na hawa watu niliowaona kule kuzimu.

    “Ninataka kuwa na washirika wengi zaidi,” nilimsikia mtume yule akisema kwa sauti ya juu huku wengine wakimsikiliza.

    “Kingine?” aliuliza mchungaji yule.

    “Ninataka niwe na mvuto mkubwa,” alisema mtume.

    “Hakuna tatizo, subiri.”

    Aliposema hivyo, watu wote wakainamisha vichwa vyao chini akiwemo huyo mtume mwenyewe. Ghafla nikaanza kuona moshi mkubwa ukianza kufuka kutoka katika sehemu iliyokuwa na giza totoro, nilibaki nikiangalia na sikutaka kuyaamisha macho yangu.

    Mara akatokea mzee fulani, alionekana kuwa dhaifu na mwendo wake ulionyesha kwamba alikuwa ameumia mguu. Kwa kumwangalia tu, isingekupa wakati mgumu kugundua kwamba mzee yule alikuwa mchawi mkubwa sana.

    Alimsogelea mtume yule huku akiwa ameshika tunguli moja kubwa ambayo kwa juu aliifunga kwa kitambaa cheusi. Alipomfikia, akamwambia apige magoti, mtume yule akafanya hivyo na kisha kumuwekea tunguli ile kichwani mwake.

    Alizungumza maneno ambayo nayo sikuyaelewa na mwisho wa siku kumgawia kisu mtume yule na kumwambia akichomeke kaburini, katika lile kaburi la mtoto mdogo, akafanya hivyo.

    “Ninataka utoe kafara,” alisema mzee yule.

    “Hakuna tatizo, nipo tayari bwana wangu,” alisema mtume yule.

    “Chukua hii tunguli, kuna damu ndani yake, nyunyizia katika kaburi hilo.”

    Sauti ya mzee yule haikuwa ya kawaida, alikuwa akizungumza huku ikisikika kuwa na utetemeshi mkubwa, mtume yule akachukua tunguli ile na kufanya kama alivyoagizwa. Sikuwa nimejua kabla kama ndani yake kulikuwa na damu, akaanza kunyunyizia katika kisu kile kilichochomekwa kaburini, nikaanza kusikia sauti kutoka ndani ya kaburi lile.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unatoa kafaraaaaaaaaaaaaa....” niliisikia sauti hiyo vilivyo kabisa.

    “Ndiyo bwana wangu.”

    “Tunahitaji damu kutoka kanisani kwako.”

    “Nipo tayari kutoa.”

    “Chukua hicho kisu, ujikate na damu unyunyizie kaburini,” ilisikika sauti kutoka ndani ya kaburi lile.

    Alichokifanya mtume yule ni kuchukua kisu kile na kufanya kama alivyotakiwa kufanya. Damu yake ilipoangukia juu ya kaburi lile, wachawi wengine waliokuwa kaburini pale wakaanza kucheka kwa furaha kwani waliamini kwamba kila kitu kilikuwa kikifanyika.

    ****

    Baada ya tukio hilo la ajabu, nikaanza kuyaona maono mengine, nikatolewa kaburini na kuonyeshwa nikiwa ndani ya kanisa. Taarifa zikaanza kuzagaa kwamba kulikuwa na msiba uliokuwa umetokea usiku uliopita, mshirika mmoja wa kanisa hilo alikuwa amefariki dunia katika kifo cha kutatanisha sana akiwa anachota maji usiku uliopita.

    Kwanza nikashangaa, sikujua chanzo cha kifo cha huyo mtu ila Yusnath alinikumbusha kwamba ile kafara iliyokuwa imetolewa kule makaburini, ilikuwa ni ya huyo mtu aliyekuwa amefariki dunia.

    “Unasemaje?”

    “Hiyo ndiyo kafara yenyewe. Kanisa hili limesimama kwa ajili ya makafara yanayotolewa kila leo,” alisema Yusnath huku akinitaka niendelee kuangalia kile kitakachoendelea kutokea kanisani.

    Ndugu zangu! Kanisa linapokuwa halina nguvu za Mungu watu wengi wanaingia, tena wale wenye nguvu za aina tofautitofauti. Kanisa lile halikuwa na washirika wa kawaida tu, bali washirika wengine waliingia wakiwa watupu kabisa tena wengine wakiwa na hirizi mikononi mwao.

    Wachawi kwa kawaida huwanga usiku lakini ndani ya lile kanisa, mpaka mchana wakawa wanawanga. Mtume huyo alipokuwa akisimama na kuhubiri, watu wengine walikuwa wakipigwa na pepo la uchovu na kujikuta wakianza kusinzia.

    Hilo ndilo pepo kubwa lililowekwa kanisani, pepo la usingizi lilishika kasi zaidi kiasi kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyeelewa.

    “Unamuona mtume alivyo?” aliniuliza Yusnath, nikayahamishia macho yangu kwa mtume.

    “Mmmh!”

    “Unaona nini?”

    “Naona joka likihubiri...mhh! Mtume yupo wapi?” niliuliza huku nikiwa nimestaajabu sana.

    “Hiki ndicho kinachotokea, si kila siku anahubiri mtume, wakati mwingine mtu anayehubiri huwa ni jini kutoka kuzimu, ila huwezi kujua hilo kama wewe si mmoja wetu,” alisema Yusnath.

    “Ni kwa makanisa yote?”

    “Hapana. Makanisa mengine yana Mungu wa kweli, hata kuyasogelea tunaogopa kwa kuwa tunaungua sana kila tunaposogea, ila haya yenye wafuasi wetu, ni rahisi kuingia kwa kuwa ni watu wetu. Na ndiyo makanisa yenye watu wengi zaidi kwani kazi yetu kubwa ni kuwavutia kanisani,” alisema Yusnath.

    “Sasa mchungaji yupo wapi?”

    “Swali zuri sana, ngoja nikuonyeshee,” alisema Yusnath.

    *****

    Mara baada ya kuliona joka lile likiendelea kuhubiri kanisani pale, Yusnath akaamua kunichukua na kunipeleka sehemu ambayo sikujua ni wapi, sehemu ambayo nilijua kwamba ndipo kulipokuwa na yule mtume.

    Safari hiyo wala haikuchukua muda mrefu, tulifika sehemu moja, ilikuwa porini sana, ilikuwa chini ya mti mmoja mkubwa wa mbuyu, chini ya ule mti kulikuwa na kitambaa kikubwa chekundu kilikuwa kimefungwa huku kukiwa na tunguli nyingi.

    Ukiachana na hivyo, kulikuwa na michirizi mingi ya damu ambayo yote hiyo ilinifanya kuona kwamba sehemu ile haikuwa ya kawaida hata kidogo. Hakukuwa na mtu yeyote yule, sehemu ilikuwa kimya na ni upepo tu ndiyo uliokuwa ukisikika mahali hapo.

    “Mchungaji yupo wapi?” nilimuuliza Yusnath.

    “Subiri! Utamuona tu,” aliniambia.

    Wala hazikupita sekunde nyingi, ghafla nikamuona paka mmoja mkubwa akija pale mbuyuni. Paka huyu hakuwa wa kawaida kabisa, alikuwa na umbo la paka lakini uso wake ulikuwa ni uso wa binadamu.

    Najua unaweza kushtuka kwamba ilikuwaje lakini hivyo ndivyo nilivyokuwa nikimuona. Mkononi mwake alikuwa amevaa hirizi moja kubwa iliyokuwa na pembe nne ambayo ilikuwa nyeusi tii na kiunoni mwake alivaa ushanga mkubwa ambapo kil alipokuwa akitembea, ushanga ule ulikuwa ukiburuzika chini.

    “Huyu ni nani?” niliuliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hata kabla sijajibiwa swali langu, ghafla paka yule akaanza kuwa mkubwa, nilishtuka sana na ilikuwa kidogo tu nikimbie. Kadiri alivyokuwa akikua na ndivyo alivyokuwa akibadilika na mwisho wa siku kuwa binadamu kamili.

    Kila kitu kilichokuwa kikiendelea nilihisi kama naangalia filamu moja ya Kinaigeria, sikuwahi kuyaona mambo hayo kwa macho yangu mawili. Alipokuwa mtu kamili, nikapigwa na bumbuwazi baada ya kugundua kwamba paka yule alikuwa ndiye yule mtume wa kule kanisani.

    “Mungu wangu!” nilisema kwa mshtuko huku nikishika mdomo wangu.

    “Usishangae.”

    “Lazima nishangae, sikuwa nikitarajia kuona hili.”

    “Huyu ndiye mtume, wakati joka likiendelea kuhubiri kanisani, yeye yupo huku,” aliniambia Yusnath huku akiniangalia usoni, tena kwa kunikazia macho.

    “Huku anafanya nini?”

    “Amekuja kuomba nguvu za kuliendesha kanisa. Ngoja nikwambie kitu kimoja,” aliniambia.

    “Kitu gani?”

    “Makanisa mengi yanayofunguliwa huwa na nguvu kutoka huku, wachungaji wapo kifedha zaidi na si kama zamani na ndiyo maana tunapata nguvu ya kufanya mambo yetu tupendavyo,” aliniambia, nikajifikiria, nikagundua kwamba lile alilokuwa akilizungumza, lilikuwa kweli kabisa.

    “Kwa hiyo naye huyu ni mchawi?”

    “Ndiyo! Ila mtu akipata nguvu zaidi, wakati mwingine anakuwa na uwezo wa kugeuka jini,” aliniambia, nikashtuka.

    “Unasemaje?”

    “Ndiyo hivyo! Huyu mchungaji ni mchawi wa kawaida sana, ila anasomea masomo maalumu, akimaliza, atakuwa na uamuzi wa kuchukua nguvu za kijini pia,” aliniambia, niliendelea kushangaa.

    Wakati akiendelea kuniambia mambo mengi, nikashtukia kuona paka wengine wakija mahali pale, walikuwa wa rangi tofautitofauti, walikuwa wekundu, weupe na weusi na muonekano wao ulikuwa uleule.

    Waliposogea mahali pale karibu na mtume yule, akawapulizia unga fulani na hapohapo paka wale wakaanza kubadilika maumbo yao na kuwa binadamu. Niliwafahamu vilivyo, mmoja alikuwa mke wa mtume, mwingine alikuwa mchungaji msaidizi na mwingine alikuwa mwalimu wa kwaya.

    “Mmmh!”

    “Usishangae, hivi ndivyo tunavyofanya kazi yetu.”

    “Naomba niulize swali.”

    “Endelea.”

    “Kama hawa wamekuja huku, kule kanisani wamebaki wakina nani?” niliuliza huku nikiwa na hamu ya kutaka kujua.

    “Twende ukaone,” aliniambia na kisha kuyafumba macho yangu, nilipoyafumbua tu, tulikuwa kanisani.

    Watu walikuwa bize na ibada, wakati joka lile lililokuwa na muonekano wa mtume likiendelea kuhubiri, watu wengi kanisani pale walikuwa wamesinzia kwani ile ilikuwa moja ya kazi ya kule kuzimu.

    Sikutaka kujali sana, nilichokifanya ni kuyapeleka macho yangu na kuangalia kule ambapo mke wa mtu alipokuwa akikaa, sikuona mtu zaidi ya paka mkubwa mithiri ya binadamu alikuwa amekaa huku lile joka likiendelea kuhubiri kama kawaida.

    Nilishtuka, hakukuwa na mtu yeyote kanisani aliyekuwa akiliona hilo, nikayapeleka macho yangu hata kwa watu wengine wale waliokwenda chini ya ule mbuyu kule porini, nao walikuwa na muonekano uleule, walikuwa paka wenye maumbo makubwa mno. Nilibaki na mshangao uliojawa na hofu kubwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog