Search This Blog

MIRATHI YA HAYAWANI - 5

 





    Simulizi : Mirathi Ya Hayawani

    Sehemu Ya Tano (5)



    Mlango ulifunguliwa, taratibu akaingia mwanaume mmoja mrefu. Usoni akiwa amebandika miwani. Haikumchukua muda mrefu Imam Chaullah kumtambua mbabe yule, aliyepata kumtembelea nyumbani kwake alipojitambulisha kama Malakul Mauti. Kovu kubwa jichoni mwake, lilifichwa vyema na miwani aliyoitinga.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    ‘Kumekucha’ Imam Chaullah alijisemea.
    Baada ya muda, aliingia yule kijana aliyewabeba kwenye teksi akijifanya ni dereva. Na punde aliiingia Hashim, kijana mtiifu wa marehemu mzee Tafawa. Kitendo cha kumwona Hashim kilimfanya mzee Jumbe ashindwe kujizuia, akaropoka, “HASHIM, HATA WEWE?”
    Makame alimsogelea mzee Jumbe, akamzaba kelbu la uso huku akimkaripia, “Umeruhusiwa na nani kuzungumza?”
    “Makame mwanangu, unaniadhibu mimi?” mzee Jumbe alijibu huku akitema mate yaliyochanganyika na damu.
    “Mwanao ni huyo Sauda, siyo mimi. Au unajifanya hauji kama mimi ni mtoto wa mwanajeshi?” Makame alijibu kwa kibri huku akirejea usawa ule aliokuwa amesimama.
    Mzee Nzila aliyamaliza majina yote ya Mungu akimtaka msaada, alipoona harufu ya wokovu I mbali nao, alianza kulia kama mtoto.
    “Anzeni na huyu hapo hadi atakapokuwa tayari kusema ukweli wote ndiyo mtatuita, tunakwenda kwenye mazungumzo kidogo,” kamanda Tibaijuka alitoa amri kwa vijana wa kazi.
    “Okay, ngoja niongeze vitendea kazi,” Hashim alijibu huku akiuendea mlango na kutoka nje ya chumba hicho.
    “Narudia tena, ukweli pekee ndiyo utakaowakomboa,” mama Makame alisema wakati wakimsubiri Hashim arudi.

    Hakuna aliyemjibu.
    Haikuchukua muda mrefu mlango ulifunguliwa, na Hashim aliingia na kiti kikubwa mkononi, akakisukumia pembeni, kisha akasema, “Ifuatayo sasa ni surprise!”
    Wote walijikuta wakimtazama anataka kufanya jambo gani. Aliurudia mlango na kuufungua, kisha hapo aliingia mtu aliyefanya chumba kizima kizizime kwa taharuki. Mtu huyo aliandamana na vijana takribani saba, wote wakiwa na bunduki mikononi mwao, tena zikiwa zimewaelekea akina kamanda Tibaijuka.
    “TOBAAA!” mzee Jumbe alimaka.
    “MAMAA YANGU NIMEKWISHA!” mama Makame alipiga kelele huku akitaka kukimbia.
    Hakuna aliyeweza kuhimili kilichotokea mbele yao. Kumwona mtu aliyefariki na ikathibitika kuwa alizikwa, halikuwa jambo rahisi katika milki ya mwanaadamu. Aliyeingia alikuwa mzee Tafawa bin Haidari.
    Mmoja kati ya vijana waliofuatana na mzee Tafawa, alimrukia na kumuwahi kamanda Tibaijuka, akamtia ngwara, alipokwenda chini akamshika mikono na kumfunga pingu. Alipokwisha, akahamia kwa Makame aliyekuwa amepagawa asijue cha kufanya. Naye akadhibitiwa na kumfungwa vilevile.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    “Wafungue hao,” mzee Tafawa alimwamuru mmoja kati ya askari alioingia nao, awafungue kamba akina Imam Chaullah. Kisha akaenda kwenye kile kiti kilicholetwa na Hashim, akaketi.
    Wakati akina mzee Nzila wakifunguliwa kamba, mzee Tafawa alimwelekea mama Makame na kumwambia, “Hivi kweli ulitegemea, Hashim anisaliti mimi? Ulifanya kosa kubwa sana kujipumbaza vile. Sijapata kuona mwanamke safihi kama wewe, wema wote niliokutendea kwa miaka yote tangu kipindi kile ulipotelekezwa na yule mwanajeshi wako, nikakuoa bila kujali ulikuwa mjamzito, nikakulea wewe na ujauzito wako hadi ulipomzaa Makame, naye nikajihini kumridhisha kwa kila hali, lakini malipo yake ndo haya uliyodhamiria dhidi yangu?”
    Chumba kizima kilimezwa na utulivu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    “Kwa taarifa yenu, mimi ni mzima, bukheri wa afya. Wala sikufa kama mlivyoitengeneza ile ajali,” mzee Tafawa alibainisha. “Mpango wenu wa mauaji nilidokezwa mapema siku ya tukio, hivyo, sikuingia garini, nilibaki ndani nikikufuatilieni. Mlipoteza tu muda kuligonga gari langu na kurusha risasi mkidhani nilikuwamo garini. Na, hata dereva wangu naye hamkufanikiwa kumdhuru, kwani alijiandaa vyema. Mlipokaribia tu kuligonga gari, kwakuwa alikwishajua kifuatacho, alifungua mlango na kuruka kabla hamjamgonga.”
    Makame alilia kama mwanamke aliyefiwa na mume. Mzee Jumbe alimsogelea na kumtandika makofi ya haja, “Tuondolee kelele.”
    “Ba’mkubwa nisamehe!” Makame alilia kwa kuomboleza.
    “Nani baba yako? Mi sina udugu mwanajeshi aliyemuasi mama yako.”
    Mzee Tafawa, akaendelea, “Baada ya ajali, kwa kushirikiana na akina Hashim, nilitoweka na kukuhadaeni kwamba niliwahishwa nje ya Nchi kwa matibabu. Ni mimi niliyeusuka mpango wa kukulaghaini kuwa nimekufa ili mpate kudhihiisha dhima yenu.”
    “Alhamdulillah,” Imam Chaullah alijikuta akisema huku akijifuta uso wake kama ishara ya kumtukuza Mungu.
    Mzee Tafawa alimgeukia Imam na kumwambia, “Kila ulichokifanya ili kuhakikisha unatetea maslahi ya mtu ambaye ulijua amekwishafariki ninakifahamu, kwani nilikifuatilia kwa karibu. Mbali ya malipo yako yanayokusubiri kwa Mungu, kuna mengine nitakupa mwenyewe kama shukrani, najua utayafurahia.”
    “TAFAWA,” Mzee Almasi aliyekuwa bado hajaamini kila kinachoendelea, alijikuta akiropoka.
    “Ndiyo mimi swahiba, nimeuona urafiki wako kwangu,” mzee Tafawa alijibu na kuendelea, “fauka ya hayo, kila kilichofanyika humu chumbani, kilirekodiwa kupitia kamera za siri, hivyo, hapana shaka yoyote, ushahidi umekamilika mbele ya vyombo vya dola. Bahati mbaya ni kwamba, Makame una kesi nyingine inakusubiri London, kwa kuwatumia wahalifu waliomuua mtoto wa mfanyabiashara wa mafuta. Ulitaka kujichotea Mirathi isiyo stahiki yako, matokeo yake Mirathi umeikosa, na utakwenda kuozea jela.”
    “Alhamdulillah, siamini macho yangu,” mzee Jumbe alishukuru, “nlikwambia Imam Chaullah, mali ya ndugu yamgu haiwezi kurithiwa na huyu hayawani.” Alimalizia huku akimsonta Makame.
    “Na lau angelifanikiwa, hakika ingelikuwa Mirathi ya hayawani!” alijibu mzee Tafawa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    Baada ya maelezo hayo, mzee Tafawa aliwaamuru wale askari alioingia nao, wawachukua watuhumiwa na kuwafisha mbele ya sheria. Wakiwa wanachukuliwa, mzee Tafawa alimwambia kamanda Tibaijuka, “Kamanda mzima, uliyeaminiwa, ukapewa dhamana kuu ya usalama wa raia na mali zake, kumbe unashiriki matendo machafu namna hii? Tayari taarifa zako ziko mpaka Ikulu, hutachomoka wewe wala hao askari wako wanatii amri zako za kihalifu.”
    TAMATI

0 comments:

Post a Comment

Blog