Search This Blog

MIRATHI YA HAYAWANI - 4

 





    Simulizi : Mirathi Ya Hayawani

    Sehemu Ya Nne (4)



    Mkuu wa Kituo, bwana Jeff English, alimkaribisha Imam Chaullah. Na mara baada ya Imam kuketi alimwambia, “Bwana Chaullah, wafuatiliaji wako wamekamatwa,”

    “Oops, niliomba wafuatiliwe tu, si kuwakamata kabla ya kujua dhamira yao na aliyewatuma,” Imam Chaullah alijibu.

    Majibu ya Imam Chaullah yalimfanya bwana Jeff atikise kichwa. Aliaanza kumsimulia tukio zima lilivyokuwa hadi wale vijana walipomteka yule mzungu na kwenda kumuua baada ya mapambano yaliyoibuka baina yao. “…mbaya kuliko zote, huyo aliyeuawa, ni mtoto wa kigogo mkubwa hapa jijini, hivyo, msako mkali dhidi wahusika wakuu, utaleta maana endapo hadi wewe tutakutia nguvuni.”

    Kusikia kutiwa nguvuni ili kusaidia upelelezi, macho yalimtoka pima Imam Chaullah.

    “Wafuatiliaji wako wameanza kuutapika ukweli baada ya kukaribishwa vyema hapa kituoni. Ni kwamba, waliagizwa kfuatilia nyendo zako na bosi wao, ambaye naye alipewa kazi hiyo na mtu kutoka Tanzania, anaitwa Makame.”

    “Makame ninamjua, ndiye mtoto wa marehemu mzee Tafawa, Mtanzania niliyekufahamisha kuwa alizikwa nchini mwenu baada ya kufa kwa kifo tatanishi.”

    “Hilo halituhusu sisi,” bwana Jeff alijibu kwa mkato, “ilikuwa nikuweke ndani muda huu, lakini kwa sababu ya kazi yako ya upelelezi, na hadhi yako katika jamii, nakuruhusu uondoke na urejee hapa kesho asubuhi, au muda wowote utakaohitajika. Hakikisha simu yako inakuwa hewani na inapokelewa.”

    “Sawa, ahsante!” Imam Chaullah alijibu huku akiinuka kwa ajili ya kuondoka.

    “Kuanzia sasa, nakuasa kutoendelea na upelelezi wako ili kutoharibu uchunguzi wetu wa awali–ukikiuka usijekunilaumu.” Bwana Jeff alihitimisha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Imam Chaullah alirejea Grand Plaza akiwa hoi bin taaban. Ingawaje alitamani kupumzika, walakini, muda haukumpa nafasi hiyo. Aliitisha kikao cha dharura na akina mzee Jumbe. Aliwapasha baadhi ya habari zilizobeba matukio tatanishi kufuatia kifo cha mzee Tafawa. Alihisi kwamba isingelikuwa busara kuwaficha kila kitu wazee wale, kama ambavyo haingelikuwa hekima kuwaeleza kila kitu.

    Kwa usalama wao, pamoja na Imam mwenyewe, na kwa kuhofia usumbufu wa Polisi ambao ungechelewesha mambo yao, kwa kauli moja waliafikia kuondoka London siku inayofuata ili kurejea Tanzania. Haraka waliwafuata akina Hashim (vijana wa mzee Tafawa) kwa ajili ya kuwapa mpango wa safari. Tofauti na matarajio yao, hawakuwapata hadi walipoingia kulala usiku.

    Kutokana na kuwakosa akina Hashim na Makame, walishindwa kuipanga safari kwa wakati, hivyo, waliongeza tena siku moja mbele, ambapo waliifanikisha mipango safari yao, na kurejea jijini Dar es Salaam.

    __________

    WALIPOWASILI uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, majira ya saa kumi na mbili magharibi, walijongea kila mmoja na kijibegi chake kidogo mkononi, hadi nje ya lango kuu kwa ajili ya kuchukua usafiri wa teksi. Nje ya uwanja walikutana na vijana wakizinadi teksi zao kwa wageni.

    “Sheikh Chaullah, Assalamu aleykum,” Kijana mmoja, alimsalimu Imam kwa bashasha.

    “Waalyekum Salaam,” Imam alijibu huku akimtaza. Sura ilimjia japokuwa pamoja na jitihada za ubongo wake kuvuta kumbukumbu, hakufanikiwa.

    “Ulikuwa safari?” Kijana aliuliza, hali sura yake ikiwa na dalili ya furaha ya kujipatia riziki.

    “Swadakta, nd’o nimewasili bwana.”

    Kijana aliwageukia akina mzee Jumbe, akawatolea salaam pia. Muda huo Imam Chaullah aliendelea kupigana na taswira ya kijana huyo iliyoendelea kutalii kichwani mwake bila ya kumpa uhakika wa mahala alipomwona kwa mara ya kwanza.

    “Vyema, nina teksi hapo nje, kama mnahitaji usafiri binafsi,” Kijana alisema huku akipokea begi la Imam Chaullah.

    Imam alimwachia begi, wakafuatana hadi mbele kidogo ambako kulikuwa na teksi kadhaa. Kijana aliisogelea teksi yake, akafungua milango ya teksi; mzee Jumbe aliingia na kuketi mbele, Imam Chaullah na mzee Nzila wakaketi siti za nyuma. Baada ya kuifunga milango kijana alizunguka nyuma ya teksi, akatokezea upande wa malngo wake, akaingia na kuianza safari.

    Bila ya akina Imam Chaullah kugundua, kijana aliitoa simu yake ya mkononi akaandika ujumbe mfupi wa maandishi uliosomeka; ‘Tayari nimekwishawapokea, tukutane kwenye mataa ya tazara’ kisha akautuma kwa wenziye. Safari ilianza mara baada ya kijana kuingia ndani ya gari, na kuukamata usukani.

    Walipokwisha karibia kuyafikia mataa ya Tazara, yaliyopo njiapanda ya barabara ya Nyerere na Mandela, ndipo kumbukumbu za Imam Chaullah kwa kijana yule, ziliposalimu amri. Alimkumbuka na kuikumbuka siku aliyomwona kwa mara ya kwanza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa siku ile Makame alipomzulu Imam Chaullah ofisini mwake kuulizia masuala ya Mirathi, akifuatana na yule binti aliyejitambulisha kwa jina la Johari, ndipo kijana huyo alipoingia ghafula ofisini akiwa amejibandika plasta usoni, akimletea simu Makame. Safari hii hakuwa na ile plasta usoni wala dalili ya kovu.

    Kengere ya hadhari iligonga kichwani mwa Imam Chaullah, hakutaka kuipumbaza akili yake kwamba kijana yule ni dereva teksi wa kawaida, na kwamba labda ilitokea kama sadfa tu kukutana naye hapo uwanjani. Aliiona ishara ya uratibu wa mpango ule toka kwa Makame, akaamua kufanya jambo ili kuyahami maisha yao.

    Tayari muda huo walikwishayafikia mataa ya tazara. Kwa ghafula, dereva alitanua upande wa kushoto wa barabara ili magari yakiruhusiwa, aweze kukatisha na kuambaa na barabara ya Mandela inayopita buguruni. Wakiwa wanasubiri ruhusa ya taa za kijani kuendelea na safari, mara alitokea askari wa usalama barabara (Trafiki), akawasogelea. Dereva alishusha kioo na kumsalimu kwa taadhima.

    “Kwanini unatanua barabara?” Trafiki aliuliza.

    “Oh, samahani mkuu, nilikuwa najaribu kutafuta nafasi ili tukiruhusiwa hapa niingie barabara ya Mandela?”

    “Ndivyo ulivyofundishwa hivyo?”

    Kabla dereva hajajibu, taa ziliruhusu magari yaondoke.

    “Weka gari pembeni.” Trafiki aliamuru, na dereva akatii.

    Walipoegesha pembeni, Trafiki aliwasogelea tena na kusema, “Naomba leseni yako.”

    Kijana akaanza kuhamanika akiitafuta leseni huku na kule; alifungua droo kadhaa za humo garini bila mafanikio, alijipekua mifukoni bila mafanikio.

    “Hata leseni huna, kwanza mmetokea wapi?” Trafiki alisema kwa mshangao.

    “Ah, nafikiri nitakuwa nimeisahau kwenye suruali niliyoivaa jana – tumetoka Airport.”

    “Isijekuwa mmebeba magendo humu–lazima mkakaguliwe,” Trafiki alibwata.

    “Hawa ni viongozi wa dini kaka, hawana tatizo,” dereva alisema.

    “Viongozi wa dini ndo wanaongoza kwa kupitisha dawa za kulevya Airport–hebu shukeni na mabegi yenu,” Trafiki aliwaamuru huku akigeuka nyuma na kumwita mwenziye.

    Waliposhuka; waliulizwa vitu walivyobeba kwenye mabegi, wakajibu; mahala watokeako, wakajibu pia. Kwa niaba ya wenziye, Imam Chaullah alijitahidi kuwatoa hofu wale trafiki kwa ushawishi wa kiungwana. Pamoja na hayo, trafiki waligoma kuelewa, waliwaamuru waingie ndani ya gari kwa ajili ya kwenda kituoni kukaguliwa.

    Imam Chaullah pamoja na trafiki wawili, waliingia kwenye teksi waliyotoka nayo Airport; mzee Nzila na mzee Jumbe wao waliambiwa waingie kwenye gari waliyoikuta pale ikiwa na trafiki mmoja tu. Safari mpya ikaanza.

    __________

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    KATIKA Jengo alilohifadhiwa Sauda, walikutana kwa kikao cha dharura; mama Makame, kamanda Tibaijuka, na Makame mwenyewe, aliyeingia jijini Dar es Salaam, siku moja nyuma, akitokea London, alipokimbia kufuatia tukio la kukamatwa kwa vijana waliomuua mzungu.

    Makame aliwaelezea kila kilichotokea. Wote waliafikiana kwamba sasa Imam Chaullah, mzee Jumbe, mzee Nzila, na Sauda, hawana budi kuuawa ili kufuta kabisa ushahidi unaoweza kuwagharimu huko mbeleni.

    “Vijana wangu walioko Tazara, wameniandikia ujumbe,” kamanda Tibaijuka alisema huku akimtazama mama Makame, “wamefanikiwa kuwadhibiti hao akina Chaullah, na sasa wako njiani wanakuja nao huku.”

    “Good,” Makame alisema, “wakifika tu, tusiwacheleweshe.”

    “No, hatwendi hivyo. Lazima tuwahoji kwanza, hata ikibidi kwa kutumia nguvu ili watupe kila kitu kabla ya kuwazima. Kumbukeni kwamba huyo anayeitwa Kondella hatujampata bado.”

    __________

    HATUA chache baada ya safari kuanza, ndipo Imam Chaullah alipotambua dhamira halisi za trafiki wale. Ilikuwa ni baada ya trafiki mmoja kutoa bastola na kumwelekezea huku akimuasa, “Utulie vivyo hivyo, na ufuate maelekezo yangu pasi na usumbufu wowote endapo unayapenda maisha yako.”

    Imam Chaullah alitulia tuli huku akijutia uzembe alioufanya wa kuwachelesha hadi wamemdhibiti. Milango ya gari ilifungwa vilivyo huku umakini wa trafiki wale ukiwa ni wa kiwango cha hali ya juu. Uvamizi huo dhidi ya Imam Chaullah, pia uliwakumba akina mzee Jumbe, kule kwenye gari waliyopandishwa.

    Imam Chaullah aliendelea kuomba Mungu, ili maharamia hao wafanye kosa japo dogo tu litakalowagharimu maisha yao. Aliendelea kuwategea kwa umakini huku akijiweka tayari bila mafanikio hadi walipowasili porini kabisa, lilipo Jumba lile la kutisha.

    Mapokezi waliyokutana nayo kuanzia nje, hadi ndani ya jumba hilo, ni tofauti kabisa na yale waliyopatiwa na Trafiki kwenye mataa ya Tazara. Huko porini walishushwa garini hangehange, kama haitoshi walisukwasukwa makofi, ngumi, ngwara, na kila aina ya adha, huku wakiporomoshewa matusi na manyang’au waliowakuta pale.

    Kama ambavyo Imam alitarajia, yule dereva wao, wala hukuguswa na mtu, zaidi ya kupongezwa kwa umahiri wa kazi aliyoifanya. Baada ya hapo, Imam Chaullah, mzee Nzila, na mzee Jumbe walijumuishwa kwenye kile chumba alichohifadhiwa Sauda, nao wakafungwa kamba kwenye viti maalum kwa ajili ya kusubiri hatua zaidi.

    Sauda alikuwa amechakazwa kwa mateso, hasa ya mijeredi aliyocharazwa kama Punda, ngozi yake ilisawajika vilivyo. Usoni alibakiwa na mabaka ya michirizi ya damu, jasho, na machozi.

    Wakiwa katika chumba hicho cha mateso, ndipo waliwashudia Makame na mama yake wakiingia kwa tambo na dharau. Kilichomwacha mdomo wazi Imam Chaullah, ni pale alipomwona na kamanda Tibaijuka akiingia pamoja nao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Chaullah, nakujua vyema, na naifahamu kazi yako. Najua wewe ni mzoefu wa mambo haya. Jambo likishafikia hatua hii, huna budi kutoa ushirikiano, vinginevyo utarejea kwa Mola wako ukiwa na viungo nusu,” mzee Tibaijuka alimuasa Imam Chaullah baada ya kumsogelea.

    “Najua mlisainiana mkataba, wa usimamizi wa mali na hayati mzee Tafawa; nahitaji kujua kati yako wewe na Kondella ni nani hakuchukua nakala yake, na kwanini? Pia nahitaji kujua matokeo ya mazungumzo baina yako na Kondella, ikiwa pamoja na thamani ya mali husika mliyokabidhiwa, na mahala ilikohifadhiwa.”

    Kimya!

    “JIBU!” Makame alimkaripia baada ya kuona anachelewa.

    Imam Chaullah alijibu, “Kondella ndiye hakuchukua nakala yake kwakuwa alikuwa mbali. Lakini mpaka sasa ametugeuka, amegoma kunitajia thamani ya mali wala mahala iliko, amenitaka kufunga kinywa changu, na akaniahidi kuwa kama nitatii ataangalia kiasi cha kunipoza.”

    Mzee Tibaijuka alimgeukia mama Makame, alimtazama kwa muda, kisha alihamishia macho yake kwa Makame aliyeonyesha kuyastaajabia majibu hayo yaliyotaka kumwingia kichwani.

    “Muongo, tutakushughulikia hadi utakapoamua kusema ukweli,” mzee Tibaijuka alijibu huku akirudi kinyumenyume hadi usawa wa mlango walioingilia, akaugonga kidogo tu, halafu akatembea tena kwa kusogea mbele.

    Mlango ulifunguliwa, taratibu akaingia mwanaume mmoja mrefu. Usoni akiwa amebandika miwani. Haikumchukua muda mrefu Imam Chaullah kumtambua mbabe yule, aliyepata kumtembelea nyumbani kwake alipojitambulisha kama Malakul Mauti. Kovu kubwa jichoni mwake, lilifichwa vyema na miwani aliyoitinga.

    ‘Kumekucha’ Imam Chaullah alijisemea.

    ______

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA
    Pseudepigraphas

0 comments:

Post a Comment

Blog