Search This Blog

MIRATHI YA HAYAWANI - 3

 





    Simulizi : Mirathi Ya Hayawani

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Kupitia lango kuu la kuingilia Backingham Gates lililokuwa wazi, vijana wawili walifanikiwa kumwona Imam Chaullah akiteta jambo na yule mzungu huku wakielekezana. Kwa bahati kabla hawajafanya lolote, walimwona mzungu akitoka na kwenda usawa waliokuwapo wao.



    Kijana mmoja kati ya hao wawili alifungua mlango wa teksi yao, akateremka, na kujifanya kunadi usafiri wao, ilhali yule mwenziye akijifanya ndiye dereva. Aliwahi kumchangamkia yule mzungu, “Twende bosi.”



    Mzungu aliifikia teksi yao, ambayo tayari mlango wa mbele tayari ulikuwa wazi, akaingia na kusema, “Nipeleke Pharell Café.”



    Bila kufanya zohali, kijana aliyejifanya tingo, alimsaidia mteja wao kuufunga mlango wa mbele, kisha yeye akaufungua wa nyuma, akaingia na kuketi. Walipokwishafunga milango, dereva aliwasha gari na kuanza kuondoka eneo lile taratibu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hawakufika mbali, dereva akapata upenyo, akalitoa gari barabarani na kulisogeza pembeni katika eneo ambalo halikuwa na wingi wa watu wala magari. Hali ile ikamtisha yule mzungu, na kabla hajauliza sababu za dereva kulihamisha gari barabarani, tayari aliimaizi ishara toka kwa dereva kwenda kwa konda wake aliyeketi nyuma.

    __________



    GHOROFA ya nne ilisheheni ofisi na maduka ya bidhaa anuai. Na kama alivyosema yule mzungu mbaguzi, sehemu hiyo ilikuwa ina watu weusi wengi, kwa maana ya machotara, ingawaje yeye aliwatusi kwa kuwafananisha na Nguruwe.

    “Karibu,” kijana mmoja alimlaki Imam Chaullah.



    Unadhifu wa mavazi pamoja na mwili, vilimfanya kijana huyo avutie kumtazama; ni mrefu wa kimo, mng’avu wa rangi. Meno yake meupe yalionekana mara zote alipokuwa akiongea kwa kutabasamu. Alistahiki hasa kuwekwa pale ofisini kama mkaribisha wageni.



    “Ahsante, unaweza kunisaidia mahala iliko ofisi ya maalim Kondella?”



    Kijana alipiga kimya kidogo, kisha alisema, “Una shida naye binafsi au kiofisi?”



    “Vyotevyote,” Imam alisema. Hakutaka kuonyesha kumhitaji kibinafsi pekee, wala kikazi zaidi.



    “Haya, twende huku.” Kijana alijibu huku akianza kutembea. Wakafuatana; Kijana mbele, Imam Chaullah nyuma.

    Walishuka ghorofani na kuelekea kulekule chini alikotokea Imam Chaullah na kujibiwa vibaya na yule mbaguzi.



    Walipofika chini, waliiendea moja kati ya ofisi kadhaa zilizopanga. Kijana alimtaka Imam Chaullah asubiri kidogo kisha yeye akaingia mle ofisini. Baada ya dakika kama mbili, kijana alitoka na kumwambia aingie. Huku akimtazama usoni kwa udadisi, Imam Chaullah aliufungua mlango wa ofisi na kuingia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndani ya ofisi, Imam Chaullah aliketi kwenye kiti cha sofa alichoelekezwa mara baada kukaribishwa. Nyuma ya meza kubwa ya duara, aliketi bwana mmoja chotara mwenye asili ya kiaraibu, kichwani alivalia kofia pana tamhtili ya wachunga farasi (pama).



    Sehemu kubwa ya ofisi hiyo ilizungukwa na makabati yenye makablasha mbalimbali, huku picha kadhaa zikiwemo za viongozi wa nchi, zikipamba kuta.



    Baada ya kusabahiana, kwa lugha ya Kingereza, “Nina shida na maalim kondela.”



    Chotara aliinua uso wake kumtazama Imam Chaullah kwa sekunde chache bila kumjibu, kisha akarudi kuiinamia meza yake na kuendelea kupanga makaratasi yaliyozagaa mezani.

    Baada ya kukusanya makaratasi yake vizuri, aliinua tena uso na kusema, “Ukimwona utamjua?”



    “Kwanini nishindwe?” Imam alijibu kwa mtindo wa swali. Chotara alitabasamu.



    “Sasa mbona unayemuuliza, ndiye unayesema unamfahamu?” kabla Imam Chaullah hajajibu, bwana yule aliongezea, “kumekuwapo malalamiko mengi toka kwa baadhi ya wateja, wakidai kukumbana na mikono ya madalali na matapeli wajitambulishao kwa jina langu. Hivyo, sishangai kuona nawe ukijaribu kuhakikisha usahihi wa unayeongea naye.”



    “Vyema, nafurahi kukufahamu.” Imam Chaullah alisema huku akitabasamu, “naitwa Imam Chaullah, toka Dar es Salaam.”

    Aliamini bila shaka yoyote, mzee Tafawa alikwishamweleza maalim Kondella kuhusu yeye, hivyo, kujitaja jina moja kwa moja alidhamiria kurahisisha mjadala, walakini, tofauti na matarajio yake, Chotara aliyejitambulisha kama maalim Kondella hakuonyesha chembe ya mshituko.



    “Ndiyo bwana–karibu,” maalim Kondella alisema, huku akimtulizanishia macho yake Imam Chaullah.



    Jibu hilo la baridi lilimfikirisha zaidi Imam Chaullah. Alichoanza kukihisi kwa haraka ni kwamba, huenda maalim Kondella tayari alikwishazipata taarifa za kifo cha mzee Tafawa, lakini ameamua kudhulumu mali aliyokabidhiwa, ambayo kimsingi ni yeye pekee ajuaye mahali iliko, pamoja na thamani husika, nd’o maana anajifanya kutomtambua licha ya kujitambulisha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimekuja kufuatia kifo cha mzee Tafawa, mimi ndiye niliyesaini sehemu ya ule mkataba wa usimamizi wa mali zake.” Imam Chaullah aliongezea.



    Pamoja na maelezo hayo, bado maalim Kondella, alionekana kutoshituka, zaidi ya kupoa tu kama maji ya mtungi. Baada ya Imam Chaullah kutulia, ndipo alijibu. “Naomba huo mkataba wako niuone.”



    Kutokuwa na nakala ya mkataba wake, ilikuwa ni kikwazo kikubwa sana kwake katika kutimiza jukumu hilo. Ingawaje hata angekuwa nao, yamkini asingeutoa haraka namna ile.

    Kwa mujibu wa maelezo ya mzee Tafawa, ni kwamba maalim Kondella ni mtanzania pia. Hivyo, Imam Chaullah aliona iko haja ya kujadiliana kwa lugha ya Kiswahili ili kuipata ithibati mtu huyo. Haraka Imam alimtupia swali kwa lugha ya Kiswahili, “Je, wewe ulikwisharejeshewa mkataba wako na marehemu?”

    __________



    WAKATI hayo yakiendelea mjini London, huko Dar es Salaam nako mipango iliyoratibiwa na mama Makame iliendelea kutekelezwa. Sauda alitekwa, na kupelekwa nje kabisa ya mji. Kilometa kadhaa kama unaelekea wilayani Bagamoyo.



    Uliandaliwa mchezo mdogo tu, Sauda alichukuliwa na dereva teksi aliyesema ameagizwa na mama Makame ammpeleke kule hospitali alikolazwa. Sauda alikubali na kuondoka na dereva yule ambaye kwa kushirikiana na mwenziye walimgeuka, wakampiga na kitu kizito kichwani. Alipoteza fahamu, walimchukua na kumfikisha hadi kwenye jumba moja kubwa lililoko nje ya mji. Kimsingi, jumba hilo ni mali ya mzee Tafawa, alilokuwa akilitumia kuhifadhia nafaka.



    Mama Makame alifanikiwa kumshawishi na kumlaghai Hashim, kijana mtiifu kwa mzee Tafawa, aliyekabidhiwa usimamizi wa jumba hilo na vilivyomo, amsabilie matumizi ya jumba hilo kwa mambo yake ya faragha.



    Fahamu zilimrudia Sauda mara baada ya kumwagiwa maji ndoo nzima, ikiwa ni dakika thelathini tangu alipofikishwa katika jumba hilo. Alijikuta akiwa amening’inizwa kwa kufungwa kamba mikono yake yote miwili, huku mwilini akibakizwa nguo za ndani tu.



    “Naona umeamka mtoto mzuri,” Mtu aliyevalia bukta ya jinsi alisema huku akimwangalia Sauda, kisha akaenda mbele kidogo ya chumba hicho kilichosheheni zana madhubuti kwa uteseaji, alivuta kiti cha chuma akaketi na kusema, “Utaning’inia hapo hadi utakapokuwa tayari kunijibu maswali yangu.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwanzo alihisi kama yu ndotoni, lakini punde aliamini kuwa yuko katika tukio halisi. Pamoja na hayo, bado aliendelea kustaajabia kila kilichopita mbele ya upeo wa macho yake. Hakutambua mahala alipo wala sababu za kuwapo hapo, wala hakumtambua mtu huyo aliyempa maelekezo ya kumtaka ajibu maswali yake.



    Maumivu yaliyoichakaza mikono yake, ndiyo yaliyomfanya aanze kulia, akiomba msaada toka kwa jamaa yule ambaye muda huo alikuwa ameshikilia kipande cha gazeti akisoma. Sauti yake haikuweza kutoka kwa sababu ya mdomo wake kufumbwa kwa karatasi yenye gundi maalumu.



    Pamoja na kilio cha uchungu toka kwa Sauda, jamaa hakujitaabisha kumtazama, aliendelea kusoma gazeti kama vile hakumsikia vile. Baada ya dakika mbili, ndipo jamaa alinyanyuka na kumsogelea. “Haya, utajibu maswali yangu?”



    Sauda aliishia kutikisa kichwa kama ishara ya kuafiki. Jamaa alimsogelea na kumtolea ile karatasi–papo hapo Sauda alianza kukohoa kwa nguvu huku udenda ukimtoa mdomoni.



    “Nataka uniambie ni mali kiasi gani ulizoachiwa na marehemu mzee Tafawa, na ziko mahala gani?”



    Swali hilo ndilo lililomzindua kwamba yuko pale kufuatia utekwaji nyara aliofanyiwa kwa sababu za mali ya baba yake, lakini hakujua chochote kuhusu hayo anayoulizwa. Aliuliza, “Mali gani?”



    Kuuliza hivyo tu, jamaa aliachia msonyo mrefu, akaenda mbele kidogo, akachukua mijeredi na kurejea nayo pale aliponing’inizwa. Kazi ikaanza.

    __________



    KABLA mzungu hajajibiwa chochote na dereva, ghafula alisikia akipigwa kabali na kijana aliyeketi siti ya nyuma yake, kisha akawekewa bastola kisogoni.



    “Kama ni pesa chukueni zote jamani, ila msinue tafadhali,” Mzungu alisema huku macho yakiwa yamemtoka.

    Kikapita kimya wakati dereva akiangalia nje kama kuna ye yote aliyehisi cho chote, alipojiridhisha na hali, alimgeukia mzungu aliyekuwa katikati ya kabala na kumhoji, “Ulikuwa ukiongea nini na Imam Chaullah?”



    “Imam Chaullah?” Mzungu aliuliza kwa taabu na mshangao.



    “Usiniulize tena maswali, jibu ulichoulizwa!” Dereva alifoka.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana, simjui mtu huyo.”



    “Yule kijana uliyekuwa ukiongea naye wakati unatoka mle Bickingham Gates ni nani?”



    Mzungu alivuta kumbukumbu wakati alipotoka mle jengoni, akamkumbuka mtu aliyezungumza naye, akajibu, “Nimekumbuka … nimekumbuka!”



    “Haya sema taratibu.”



    “Yule kijana alikuwa akimuulizia Kondella!” Mzungu alijibu huku akizungusha macho yake kuungalia mtutu uliokuwa jirani kabisa na kichwa chake.



    Dereva alirudia tena kuangaza nje, alipojiridhisha na hali ya usalama, alimgeukia tena na kumuuliza, “Ofisi hiyo iko ghorofa ya ngapi?”



    “Haimo mle jengoni–ofisi ya Kondella ni AL-FIRASHI, ile iliyopo katika jengo linalotazamana na hapo Bickingham Gates!”



    Jamaa walitazamana–haikuwaingia akilini. Dereva alimuuliza kwa hasira. “Unaleta mchezo, enh?”



    Kabla hajajibu, akaulizwa na yule aliyemshikia bastola kwa nyuma, “Kama hiyo ofisi aliyoiulizia iko nje, ikawaje basi ukawa unamwelekeza kule ndani kabisa?”



    Swali hilo lilimfanya mzungu ashindwe kulijibu, kiasi cha kufanya aonekane muongo, ingawaje alichokisema ni ukweli mtupu. Ofisi ya maalim Kondella iitwayo Al-Firash Law and Shariah Center, iko katika jengo hilo linalotazamana na Bickingham. Alichokifanya pale awali kumwelekeza Imam Chaullah kule ndani zaidi, ni khiyana tu katika mwendelezo wa dharau na ubaguzi wake, akidhamiria kumpoteza. Sasa khiyana yake inageuka nakama kwake.



    Kuchelewa kwake kujibu, kulimfanya dereva amtandike ngumi ambayo ilimfanya mzungu ayumbe pembeni. Pamoja na maumivu makali yaliyosababishwa na ngumi hiyo, mzungu alipata upenyo wa kugeuka kwa kasi ya ajabu na kumpiga yule kijana aliyekuwa kule nyuma, kwa kiwiko cha mkono wake hadi bastola ikamponyoka. Vita ikajinadi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “TULIAA!” Dereva alipaza sauti huku akijaribu kumrukia Mzungu. Lakini hakufanikiwa, mzungu alimwahi na kumpiga kichwa usoni, na dereva alihisi rangi ya kijivu ikiyafunika macho yake.



    Wakati mzungu akishughulika na dereva, yule aliyekuwa nyuma, aliwahi kuiokota bastola yake, na papohapo alifyatua risasi zilizopenya shingoni mwa mzungu kiasi cha kumrusha hadi kwenye kioo cha mbele cha gari.



    “ARRGHHH…” Sauti ya mzungu ilifuatana na damu iliyotapakaa kuanzia shingoni na kuchuruzikia kifuani. Haraka kijana aliteremka ili afungue mlango wa mbele aweze kumtoa na kumtelekeza palepale, ili watoweke.



    Akiwa amekwisha kuufungua mlango wa mbele, mara ilitokea gari moja iliyoingia eneo lile kwa kasi, na iliposimama tu milango ikafunguliwa. Waliteremka askari watatu wakiwa na bunduki. Kuona hali hiyo, kijana alitaka kukimbilia ndani ya teksi achukue bastola yake aliyoiacha juu ya kiti, lakini hakufika hata mlangoni akawa amepigwa risasi ya mguu iliyomtupa chini. Askari hawakuishia hapo, waliyafyatulia risasi matairi yote ya gari hilo kabla ya kulisogelea na kumkamata yule dereva aliyekuwa akiugulia maumivu ya kichapo cha mzungu.



    Askari hawakufika pale kwa bahati mbaya, walianza kulifuatilia gari la vijana wale tangu kule kituo cha polisi ambamo Imam Chaullah aliingia kuripoti. Ni baada ya Imam Chaullah kumaliza mambo yaliyompeleka mle, ndipo aliwatonya maaskari kwamba kuna gari ameigundua kuwa inamfuatilia tangu atokako, na kuwaomba askari nao waifuatilie kwa nyuma wakati yeye akitoka. Na ndivyo ilivyokuwa, baada ya kuwaelekeza gari husika, askari walianza kuwafuatilia vijana hao, ambao nao walikuwa wakimfuatilia Imam Chaullah. Baada ya vijana kumchukua mzungu na kuondoka naye, iliwachukua muda askari wakijadili endapo wabaki wakihakikisha usalama wa Imam Chaullah aliyeingia jengoni, au wawafuatile hao vijana. Kuchelewa kwao kufanya maamuzi ndiko kulikowapa fursa maharamia hao kumdhuru na hatimaye kumuua mzungu.

    __________



    BAADA ya Chotara kuzubaa kufuatia swali la Imam Chaullah kwa lugha ya Kiswahili, alijibu kwa Kingereza, “Mazingira haya si rafiki kutumia lugha hiyo, tuendelee na kingereza!”



    ‘Kwa vipi mazingira yasiwe rafiki kutumia lugha ya Kiswahili?’ Imam Chaullah alijiuliza. Tayari alikwishatilia shaka mtu azungumzaye naye kuwa si Maalim Kondela amtakaye.

    Kabla hajatupa swali lingine, mara simu yake ya mkononi iliita, akaitoa na kupokea, “Hallow!”



    “Imam Chaullah?” Sauti toka upande wa pili wa simu ilimsaili. Pumzi nzito toka kwa mpigaji wa simu hiyo zilisikika zikipanda na kushuka baada ya kuuliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Uko sahihi,” Imam Chaullah alijibu.



    “Uko matatizoni, ondoka haraka eneo hilo. Ufike hapa kituoni haraka.” Simu ikakatwa.



    “Samahani, nina dharura, nitarejea nikipata wasaa,” Imam alisema, huku akisimama na kuanza kutembea kuelekea mlangoni.



    Alipofika nje, hakupoteza muda, alichukua teksi na kumwelekeza dereva ampeleke kituo cha Polisi cha West End.



    Alipowasili kituoni, alilipa gharama za usafiri wake, kisha akaingia ndani na jitambulisha mapokezi, ambapo alichukuliwa na kupelekwa hadi kwa mkuu wa kituo.



    Mkuu wa Kituo, bwana Jeff English, alimkaribisha Imam Chaullah. Na mara baada ya Imam kuketi alimwambia, “Bwana Chaullah, wafuatiliaji wako wamekamatwa,”



    “Oops, niliomba wafuatiliwe tu, si kuwakamata kabla ya kujua dhamira yao na aliyewatuma,” Imam Chaullah alijibu.



    Majibu ya Imam Chaullah yalimfanya bwana Jeff atikise kichwa. Aliaanza kumsimulia tukio zima lilivyokuwa hadi wale vijana walipomteka yule mzungu na kwenda kumuua baada ya mapambano yaliyoibuka baina yao. “…mbaya kuliko zote, huyo aliyeuawa, ni mtoto wa kigogo mkubwa hapa jijini, hivyo, msako mkali dhidi wahusika wakuu, utaleta maana endapo hadi wewe tutakutia nguvuni.”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog