Search This Blog

MIRATHI YA HAYAWANI - 2

 





    Simulizi : Mirathi Ya Hayawani

    Sehemu Ya Pili (2)



    Kwamba hata kama atatoa ushirikiano, suala la kuchomolewa roho litabaki palepale, kazi kwake; kutii ili auawe kistaarabu, au kukasiri ili auawe kinyama.

    _________



    WAKATI maji yakielekea kuzidi unga nyumbani kwa Imam Chaullah, upande mwingine wa jiji, wodi maalumu (VIP) aliyopumzishwa mama Makame, katika hospitali ya Aghakhan, ilipata ugeni muhimu. Haikuwa katika taratibu za hospitali hiyo ya kifahari, kuruhusu wageni muda ule wa usiku, lakini aina ya wageni ndiyo iliyomfanya mganga wa kuruhusu waingie.

    Mama Makame aliketi kitandani, huku sehemu kubwa ya mwili wake akiwa ameifufutika ndani ya shuka za hospitalini. Makame aliketi kuliani mwa mama yake, bahasha ya kaki ikiwa mikononi mwake. Mbele ya kitanda, palikuwa na kiti kidogo kilichokaliwa na mkuu wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, kamanda Tibaijuka.



    “Makosa mliyoyafanya ni makubwa mno,” kamanda Tibaijuka alisema huku macho yake yakiwazungukia Makame na mamaye. “hamkupaswa kumuua yule mzee hadi kwanza mhakikishe mmekwisha kupata uhakika wa mahala zilipo hizo nakala nyingine za mkataba wake.”



    Kitu pekee kinachoweza kuutambulisha umri mkubwa wa kamanda Tibaijuka, ni maneno yake ya hekima na busara, na ugeni wa mvi uliaonza kupiga hodi kichwani mwake. Vinginevyo, mazoezi na chakula bora, viliufukuzia mbali uzee kiasi cha kumfanya aonekane kijana .



    “Kiukweli, hatukudhamiria kulifanya hilo mapema, lakini–”



    “Lakini nini? Yaani vijana wamekwenda na gari hadi kwake, wamemsubiri atoke, wamemgonga, wakarsha na risasi, halafu useme hamkudhamiria?” kamanda Tibaijuka alifoka.

    Makame alinywea kama puto lililochomwa na mwiba.



    “Jamani hakuna haja ya kulumbana tena, kama ni makosa yamekwisha kufanyika, cha msingi, tutazame namna ya kuyamaliza!” mama Makame aliingilia kati huku akimtazama kamanda Tibaijuka.



    “Nafikiri mzee Tibaijuka hukuielewa maana yangu, niliposema hatukudhamiria,” Makame alijibu. “Ni kwamba, kweli huu mpango tayari tulikwishausuka mapema, na tuliafikiana na wale vijana wa kazi, lakini tulichanganyana kwenye tarehe ya kufanya hivyo, niliwaambia kwamba zoezi lifanyike tarehe kumi na saba ya mwezi ujao, wao wakafikiri ni tarehe kumi na saba ya mwezi huu … nisingeweza kuwaruhusu kumaliza zoezi lile bila kukuarifu mzee.”



    Kamanda Tibaijuka alitikisa kichwa na kusema, “Makame, kila uchao nimekuwa nikikukingia kifua kwa majanga yasababishwayo na maamuzi yako ya kukurupuka, sasa unaelekea kunichosha–” kamanda Tibaijuka alibwata.



    “Jamani tuyaache hayo, mzee Tibaijuka, tusifikie huko nakuomba, hebu tujadili kwanza tunalifanyaje hili!” mama Makame alirai.



    Macho ya kamanda Tibaijuka yaliyohama kwa Makame, yalirudi kwa mama Makame, kisha alisema, “Mlizobahatisha kuzikamata, ni nakala mbili tu za huo mkataba, lakini kwenye kila mkataba kuna sahihi za watu watatu; Kondella, Chaullah, na mzee Makame mwenyewe. Sasa bila shaka kati ya Chaullah na Kondella, mmoja alikwisharejeshewa mkataba wake baada ya kusainiwa na pande zote. Je, ni nani huyo, na tutamjuaje? Ilipaswa mzee awe hai ili tuchunguze nyendo zake tuweze kulibaini hilo–sasa amekufa na siri yake kifuani!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwakuwa maelezo yaliyomo kwenye mkataba yanaonyesha kwamba, mali iko London, na anayeishi huko ni huyo Kondella, bila shaka ndiye ambaye alikuwa hajakabidhiwa mkataba wake, kutokana na umbali. Nafikiri Imam Chaullah atakuwa ndiye aliyerejeshewa nakala yake, hivyo, kuna vijana wangu wa kazi wamekwenda kumtembelea muda huu, bila shaka watahakikisha anautapika ukweli wote kabla hawajauchukua huo mkataba aliona kabla ya kumuua.”



    “Makame unafanya nini?” kamanda Tibaijuka alifoka, “usikurupuke kufanya mamuzi kwa hisia. Je, kama huyo kondella amekuja nchini, na alianza yeye kupewa huo mkataba halafu mkamuua Chaullah ambaye hana madhara, mkamwacha mwenye madhara?”



    Maelezo ya mzee Tibaijuka yalimchoma mama Makame, akatikisa kichwa kuafiki.

    Baada ya ukimya mfupi, mzee Tibaijuka akaendelea, “Pia hakuna yeyote kati yetu amjuaye japo kwa sura tu huyo Kondella, wala mahala ambako hizo mali zilihifadhiwa. Sasa kwanini usingetuliza munkari, mkaenda kwanza huko mazikoni, London, kisha ukahakikisha mkiwa huko, unamfuatilia kwa umakini huyo Chaullah, ambaye bila shaka atakwenda tu kumtembelea shadi mwenziye Kondella kwa minajili ya kujadili kuhusu jukumu waliloingia mkataba na marehemu? Na, endapo ukifanikiwa kumjua Kondella, na mahala anapofanyia shughuli zake, bila shaka utafanikiwa kujua mahala zilipo hizo mali zenyewe.”



    Mama na mwana walitazamana, kisha wakajikuta wakishusha pumzi kwa pamoja. Mama Mkame alisema, “Nimekupata. Kwa hivi, kipi kianze?”



    “Kwanza, Makame waarifu haraka hao watu wako wa kazi wasimdhuru wala wasimbughudhi Chaullah ili wasije wakamgutua; Pili, haraka kesho au keshokutwa inabidi yule binti aliyeandikishwa mali, Sauda, atekwe nyara, akafichwe mbali, naye ateswe kidogo ili kama kuna chochote alichodokezwa na marehemu aweze kusema. Ila tu asijue kwamba yeyote kati yenu amehusika kumteka. Baada ya hapo, ndipo tutaamua afuatie nani kati ya Chaullah na Kondella, itategemea na matokeo ya uchunguzi wako huko London, juu nani aliyerejeshewa nakala ya mkataba wake.” kamanda Tibaijuka alielekeza.



    “Naunga mkono hoja.” mama Makame alisema.

    “Uko sahihi, mzee,” Makame aliongezea.

    “Nafikiri mnaiona kazi hii namna ilivyo ngumu, hivyo itabidi muongeze kiwango cha mgao, maana itanibidi niwashirikishe na baadhi ya vijana wangu wengine.”



    “Nafikiri unanielewa kamanda–hilo halina shaka kabisa,” mama Makame alimhakikishia.

    Baada ya kuhakikishiana usalama na malipo, yalifuatia maongezi ya mwisho katika kujazia nyama tu, walipokwisha, waliagana baada ya Makame kumkabidhi mzee Tibaijuka ile bahasha ya kaki, aliyomwekea nakala moja ya mkataba baina ya marehemu mzee Tafawa, Imam Chaullah, na maalim Kondella.

    __________



    KIKAO kikiwa kinaendelea huko wodini, harufu ya kifo iliendelea kuhanikiza nyumba ya Imam Chaullah. Baada ya mkwara mzito, Malakul mauti alimpandishia nyusi Imam Chaullah ikiwa ni ishara ya kumtaka aanze kutoa majibu ya maswali yake. Lilipoona Imam Chaullah angali ameduwaa, kwa kasi kama ile ya awali, liliigeuza bastola yake na kuilengesha kwenye kitasa cha mlango wa chumba cha watoto ili likisambaratishe kwa mkwara. Hilo likawa kosa lake la kwanza.



    Kwakuwa tangu awali alikuwa ameikunja vyema kanzu yake, Imam Chaullah hakufanya ajizi, aliruka kwa hatua mbili mbele akamfikia mgeni wake na kuupiga teke kali mkono uliokuwa umeshikilia bastola.



    “SHHIIT,” Jitu lilibwata.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Bastola pamoja na miwani, viliruka hewani na kusambaratikia sakafuni. Kwa wepesi wa hali ya juu, jitu liliruka na kurudi nyuma.



    Alichokiona Imam Chaullah kufuatia miwani kumvuka mvamizi wake, kilimhadharisha juu ya mtu anayepambana naye. Sehemu iliyostahiki kuwepo jicho la kushoto usoni mwa mtoto huyo wa ibilisi, palizibwa na kovu kubwa lenye kuogofya, lililoanzia chini kidogo ya nyusi na kutandazika hadi mwishoni kabisa mwa ilipostahiki kuishia jicho husika.



    Kama kovu tu linatisha namna ile, sijui kipindi lilipokuwa kidonda hali ilikuwaje! Na, haifahamiki huo upanga uliosababisha kidonda hicho, ulikuwa wa namna gani. Kovu kubwa namna ile, ni udhihirisho wa uzoefu mkubwa wa mapambano lilionalo jitu lile.



    Bila kulaza damu, Imam Chaullah aliruka tena juu, mguu wa kulia ukatua juu ya ukuta wa kulia mwa korido, kisha bila ya kutua chini akarukia ukuta wa upande wa kushoto kwa mguu wake wa kulia, akarejea hivyo tena kwenye ukuta wa kulia. Aliendelea kuruka kwa mtindo huo wa aina yake huku akimsogelea yule mvamizi wake, ambaye muda huo alikuwa mwisho kabisa mwa korido ile.



    Jicho lilimtoka mvamizi. Pengine awali hakuambiwa anakwenda kukabiliana na Imam mwenye taaluma nyingine za ziada. Sasa, baada ya kuona kasi ya Imam inazidi kumkurubia, alijirusha mzimamzima, akaupamia mlango wa chumbani kwa watoto na kujitoma nao ndani.



    “MAMAA!” Sauti ya mtoto mdogo wa Imam Chaullah ilisikika tokea mle chumbani.

    Imam aljizungusha kama jongoo, na kujitoma chumbani kwa mtindo wa kubiringita kama tairi la gari. Baada ya kuingia chumbani, lile jitu lilirukia juu ya kitanda cha watoto, na kujirusha kwenye dirisha la vioo lilisombaratika kiasi cha kumtoa nje kabisa ya chumba kile.



    Malaika mtoa roho amekimbia kutolewa roho!

    Imam hakutaka kujiathiri na mabaki ya vioo vilivyovunjika dirishani, kwa kutokea dirishani, badala yake aligeuza na kutoka humo kwa kasi humo chumbani, ambako watoto walioamshwa na vishindo waliendelea kulia kwa kupiga mayowe. Alipoufikia mlango wa sebuleni na kuufungua, haukufunguka–ulifungwa kwa nje. Hakutaka kurefusha muda, aliukita na kuuvunja kwa mapigo kama matatu tu ya mguu na kutoka nao nje.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitarudi siku nyingine, Imam.” Sauti ya yule mvamizi, iliyotokea ndani ya gari, iliyokuwa ikitoweka eneo lile, ilimfikia Imam Chaullah aliyekuwa amesimama akitweta nje ya mlango wake.



    Jamaa walikuwa wawili; mmoja ndiye yule aliyemalizia kuufunga mlango kwa nje wakati ule Imam alipoingia alipowasili; na wa pili ndiye huyo anayejiita malaika mtoa roho.



    Imam aliachia tabasamu la ghadhabu huku akiingalia gari ile isiyokuwa na namba za usaji ikitoweka. Alirejea ndani na kumsogelea mkewe aliyekuwa akilia na kujitahidi kupiga kelele bila mafanikio, akamfungua kamba pamoja na kumtolea lile dubwasha alilowekewa mdomoni, kisha aliinuka na kuwafuata wanaye chumbani mwao, akarejea nao sebuleni.



    Ilimwia ugumu mno kuwabembeleza watoto pamoja na mama yao waliokuwa wakishindana kulia. Wakati huo alijitahidi kuutafakari ugeni ule wa malakul mauti uliomfikia na kutoweka kiaina.



    Baada ya takribani robo saa ya kubembelezana, walitulia. Na, ndipo mke alipoanza kusimulia tangu alipoupokea ugeni ule uliojitambulisha kuwa umetokea Zanzibar kwa ajili ya masuala ya kidini, lakini ghafla ukambadilikia na kumfunga kama ambavyo alivyomkuta. Hawakumtendea ubaya mwingine wo wote.

    Ili kutoiathiri safari yake, ambayo kwa namna yoyote alipaswa kuidiriki siku iliyokuwa inafuata, Imam Chaullah hakutaka kumsimulia mkewe mkasa wa kifo cha mzee Tafawa, ambao kimsingi, ndiyo sababu ya mapokezi ya ugeni ule uliomjia kwa namna ya kipekee. Pamoja na hayo, usiku huohuo, aliichukua familia nzima, na kuwapeleka Ilala, kwa dada yake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakutaka kuwapa faida askari, kwa kuwaarifu juu ya tukio hilo, kwa hivyo, kitokea cha nyumbani kwa dada yake, alirejea moja kwa moja nyumbani kwake, ambako alijikita kuirekebisha nyumba sehemu zote zilizoathirika. Alipohakikisha kila kona iko salama, akaifunga na kwenda kulala hotelini kwa ajili ya kuisubiri safari siku iliyofuata.

    __________



    SIKU iliyofuata, majira ya saa tano asubuhi, msafara teule toka jijini Dar es Salaam uliwasili uwanja wa ndege wa London Airport, uliopo barabara ya HartMan, mjini London, na kupokewa na Hashim, mmoja kati ya vijana watiifu wa marehemu mzee Tafawa, waliotangulia London na mgonjwa.



    Tangu mwanzo wa safari kule jijini Dar es Salaam hadi walipowasili London, Makame na Imam Chaullah hawakuzungumzishana chochote zaidi ya kutupiana macho ya udadisi kila mmoja akiwa na lake moyoni. Kupitia kwa vijana aliowatuma, Makame alikwishapata mkasa mzima uliojiri usiku wa kuamkia siku hiyo, hivyo, alianza kumakinika na kiongozi huyo wa kiimani kwa mtazamo mpya kabisa.

    Kwa upande wa Imam Chaullah, naye ilikwishamdhihirikia pasi na shaka yo yote kwamba, mratibu wa uvamizi nyumbani kwake alikuwa ni Makame.



    Walipowasili uwanja wa ndege, jijini London, walilakiwa na vijana wa mzee Tafawa waliokuwa wakiwasubiri.



    Hashim aliwatolea salamu baada ya kuwafikia, “Assalamu aleykum,”



    “Waaleykum Salaam!” Waliitika huku wakipeana mikono.



    “Poleni kwa hekaheka,” mzee Jumbe, aliyekuwa amevalia kanzu ya rangi ya dongo huku kichwani akijitanda kilemba chekundu, alisema.

    Baada ya salaam na pole, Hashim aliwachukua wageni na kutoka nao nje ya uwanja wa ndege, ambapo walikwenda hadi katika kituo cha treni. Kwa hapo London, usafiri wa umma wenye uhakika, usalama, usio na foleni, wala gharama za juu, ni treni.



    Kwa sababu ya kupata viti vilivyo mbalimbali, hawakuketi pamoja, hivyo, kutokuwa na fursa ya kuzungumza chochote zaidi ya kutulia kwenye viti vyao wakati treni ikishika kasi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hapakuwa na treni ya kuunganisha moja kwa moja, hivyo iliwalazimu kubadili treni katika vituo kadhaa, ikiwemo Canning town ambapo wapanda treni ya kuelekea Jubilee, iliyokwenda kuwashusha tena kituo cha Green park, ambapo walipanda nyingine ya kuelekea Piccadilly. Safari iliendelea hadi walipofika kituo cha Earl’s Court, hapo walibadili tena na kupanda inayoelekea District. Mwisho wa safari ulikuwa katika kituo kikubwa cha West Brompton. Ilikuwa ni safari iliyogharimu takribani saa nzima.



    “Poleni kwa usumbufu, tumeshafika,” Hashim alisema, wakati walipokuwa wakitembea kwa miguu, wageni wakiwa nyuma yake.



    Mshituko wa kwanza ulimkumba Imam Chaullah baada ya macho yake kupiga juu ya geti kubwa la kuingilia sehemu hiyo ambayo Hashim alikuwa akiwapeleka. Haraka alimgeukia mzee Jumbe ambaye naye alistaajabishwa na maandishi yale. Palisomeka, ‘WEST BROMPTON CEMETERY’



    Nje ya uzio mkubwa wa West Brompton Cemetery, msafara ulilakiwa na vijana wengine wawili, wafanyakazi wa marehemu mzee Tafawa, ambao walikuja London pamoja na Hashim. Baada ya kujuliana hali, kwa pamoja walianza kulielekea lango kuu.



    West Brompton Cemetery, kama ambavyo jina linavyojieleza, ni eneo maalum lililotengwa hapo magharibi mwa mji wa Brompton kwa ajili ya kuzikia. Ni eneo kubwa mno, lenye ulinzi mkali, lililozungushiwa uzio maalumu. Ili kuingia katika eneo hilo, iwe kwa ajili ya maziko au ziara tu ya makaburini, ni lazima kulipia ndipo uingie baada ya mahojiano.



    Hashim alionekana kulielewa vyema eneo lile na masharti yake, kwani alizipitia njia zote hadi kulifikia lango kuu, ambapo alilipa gharama za kuingia kwa kadiri ya idadi ya watu alioambatana nao.



    Baada ya maswali mengi ya kiusalama, hatimaye walinzi waliwaruhusu kuingia. Vazi la kanzu lilioutawala msafara ule liliwashitua walinzi wale wa kizungu. Pengine hawakuzoea kupata wafiwa wenye mionekano ya namna ile, au pengine ni imani potofu tu dhidi ya kila avaaye kanzu hasa katika nchi hiyo.



    “Hashim, mbona kama sielewielewi?” mzee Jumbe aliuliza baada ya kuingia ndani kabisa ya uwanja huo uliosheni makuburi.



    “Kivipi mzee?” Hashim aliuliza. Waliendelea kujongea mbele taratibu.



    “Hapa ni wapi?”



    Hashim alimgeukia mzee Jumbe kwa mshangao, na kusema, “Ah, mzee Jumbe si unaona tuko makaburini halafu unauliza? Au hamkutaka kuanzia huku?”



    Kabla hajauliza kitu kingine, wakawa wamelifikia kaburi moja lililojengewa kwa sehemu ya mbele tu. Macho ya kila aliyekuwa kwenye msafara ule, yalishuhudia maandishi yaliyoandikwa mbele ya kipaa cha zege cha kaburi hilo;



    JINA: Tafawa Bin Haidari

    KUZALIWA: May, 1952

    KUFA NA KUZIKWA: December, 2014



    Wageni wote walionekana kupigwa na mshangao. Wakalizunguka kaburi. Na kwa wahka, mzee Almas Nzila alisaili, “Ina maana mmekwisha kuzika?”



    “Kwani hamkuwa na taarifa?” Hashim alistaajabu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kama tungekuwa na taarifa, tungekuja haraka namna hii kuwahi nini?” Imam Chaullah aliuliza.

    Kabla Imam hajajibiwa, mzee Jumbe aliuliza tena, “Nani aliyekupeni rukhsa ya kufanya hivi?”

    Hashim alimtupia jicho Makame aliyekuwa amenyamaza muda wote toka uwanja wa ndege, kisha alijibu. “Tuliwasiliana nanyi kwamba, wosia wa marehemi unaelekeza azikwe kwa kuzingatia taratibu zote za dini, ikiwemo kuzikiwa mahala atakapofia na kuzikwa kwa wakati; aliyekufa asubuhi, mchana usimkute; aliyekufa mchana, usiku usimkute; aliyekufa usiku, asubuhi isimkute. Au, kuna maelekezo mengine ya dini jamani?”



    Imam Chaullah aliyekuwa akimtazama Hashim kwa ghadhabu, aliyahamishia macho yake kwa Makame, kisha akashusha pumzi nzito. Hakuwa na hoja pingamizi mbele ya maamrisho ya dini ambaye yeye ni kiongozi.



    “Mmefanza makosa makubwa mno,” mzee Jumbe alisema huku akitikisa kichwa chake kwa masikitiko, “gari ya marehemu imekutwa na matundu mawili ya risasi, kuna uwezekano alipigwa risasi wakati wa ajali, hivyo, ilipaswa mwili ufanyiwe uchunguzi kabla haujazikwa.”



    Kimya kikatanda, hakuna aliyeongeza neno, hadi Makame alipouvunja ukimya, “Basi sasa, nd’o tumekwishachelewa.”



    “Tutaufukua mwili kwa kibali maalumu.” Mzee Jumbe alijibu.



    “Mnh, itawezekanaje?” kama aliyepagawa, Makame alidadisi.



    Mzee Jumbe alimkata jicho Makame, kisha akamwambia, “Utaona itakavyowezekana.”

    “Tuondokeni hapa.” Mzee Almasi alirai.



    “Hatumfanyii dua hata kidogo?” Hashim aliuliza.



    Mzee Jumbe alimgeukia na kumkata jicho kali–likawa jibu tosha. Waliondoka makaburini hadi kwenye lango kuu.



    Walipofika langoni, mzee Jumbe alimuuliza mlinzi, kwa lugha ya kingereza, “Hapa jirani kuna msikiti?”

    Muda wa sala ulianza kukaribia.



    “Ninyi ni waislamu?” mlinzi aliuliza.



    “Jibu swali.” Imam Chaullah alikazia kwa lugha hiyo ya kingereza huku macho yake makali yakimwangalia mlinzi huyo.



    “Oh, nendeni hapo Goodge street Mosque!” mlinzi alijibu. Aliwaelekeza eneo husika, walipoelewa wakaondoka.



    Baada ya sala, walirejea katikati ya jiji (city center), ambako walikodi vyumba vya kulala wageni katika jengo maarufu la Grand Plaza Service Apartments.



    Mzee Jumbe, Imam Chaullah, na mzee Nzila walichukua ghorofa (Apartment) ya kujitegemea; waliosalia, wakiongozwa na Makame, nao walichukua ghorofa (apartment) yao chini ya ile ya akina mzee Jumbe.

    __________



    KATI ya wote waliojumuika katika msafara huo, ni wawili tu walio na uenyeji katika mji huo wa ugenini: Makame na Imam Chaullah.

    Makame alianza kuzuru mji huo wa London, tangu alipoanza kujishughulisha na biashara za dawa za kulevya na uandazi wa matamasha ya ulimbwende, hivyo, kufanya umaarufu wake katika mji huo kuwa wa kiwango cha kuridhisha kiasi cha kuweza kufanya baadhi ya mambo ajisikiayo.



    Imam Chaullah aliingia katika mji huo kwa mara ya kwanza, akitokea masomoni, nchini Soud Arabia, ambako alihitimu shahada ya kwanza katika sheria za dini na zile za kidunia (Law and Shariah). Akiwa hapo London, alihitimu mafunzo ya upelezi na kuwa mpelelezi wa kujitegemea (Private Investigator), katika chuo mahususi cha mafunzo hayo, na kutunukiwa cheti maalumu kinachomruhusu kufanya kazi za kipelelezi duniani kote, ambako nchi husika zinaruhusu upelelezi wa kujitegemea na zina mafungamano na makubaliano ya kikazi toka nchi ambayo afisa husika alihitimu.



    Ili kutuzwa cheti cha upelelezi wa kujitegemea, ilimbidi kwanza asome na kuhitimu shahada ya kwanza ya Criminal Justice kwenye moja kati ya vyuo elekezi, ikifuatiwa na mafunzo (training) ya vitendo katika matumizi ya akili na mwili (eneo ambalo alilifaulu vizuri, kama ilivyomdhihirikia mgeni ajiitaye Malakul Mauti), kisha alilazimika kuajiriwa kwa muda wa miaka mitatu katika chuo alichohitimu ili kumuongezea uzoefu.



    Ili kufanya kazi za kipelelezi, humbidi mpelelezi husika kuwa na cheti halali. Mpelelezi anaruhusiwa kutembea na vitendea kazi vyake, ikiwemo bastola, pingu, nk, na kuvitumia kwa kuzingatia sheria, kwa ajili ya tahadhari au ufanisi wa kazi yake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kutokana na sheria za nchini Tanzania, kutoruhusu shughuli za upelelezi wa kujitegemea, ilimwia ugumu Imam Chaullah kujikita katika shughuli hizo kama afanyavyo katika masuala yake ya kidini, ingawaje mara chache alifanya kazi hizo kwa uficho na usiri mkubwa pale ilipomlazimu. Kwakuwa ameingia katika nchini ambayo si tu kwamba inaruhusu upelelezi wa kujitegemea, bali pia ndiko alikohitimu na kutunikiwa cheti chake cha kufanya kazi hizo, alikuwa tayari kuifanya kazi yake.

    __________



    ASUBUHI ya siku iliyofuata, akina mzee Jumbe walijidamka kwa ajili ya kuidiriki sala ya Alfajiri. Baada ya sala, waliendelea na visomo vya Kurani kama sehemu ya maombi kwa marehemu mzee Tafawa. Kulipopambazuka, walikwenda kustaftahi.



    Wakiwa mezani, mzee Jumbe alifungua mjadala, “Waungwana kama tulivyogusia jambo hili jana, ninafikiria kufuatilia kibali cha kuufukua mwili, kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi. Ninawatilia mashaka mno hawa vijana. Kwanini azikwe kwa haraka namna ile ilhali tulikwishawaarifu kuwa tu njiani twaja? Yamkini walihofia kuwa lau wasingaliuzika mwili, tungalizigundua athari za risasi walizomfyatulia. Kwa ajili ya tamaa ya mali, Makame amevijua utu na kujivika uhayawani, sitakubali Mirathi ya ndugu yangu iende kwa hayawani huyu!”



    Imam Chaullah alikuwa kimya akiendelea kuhangaika na kikombe chake cha sturungi mkononi.



    “Binafis nakuunga mkono, walakini, ninakunasihi kunako subra kabla ya kufikia khitma ya maamuzi yako–ni vyema ukawasiliana na familia kabla ua kutenda.”



    “Juu ya hayo, hilo halitofanyika kienyeji, itahitajika nyaraka zenye vielelezo toka kwa jeshi la polisi la nyumbani, Tanzania, kuhusu utata wa kifo husika, na sababu mahsusi za kuufukua mwili. Mbaya zaidi, Polisi kwa urasimu wao watahitaji kuonana na mwakilishi wa familia kabla ya kutoa taarifa za kiuchunguzi kwa mtu au chombo chochote, na wasimamizi wote mko huku,” Imam Chaullah alisema.



    Mjadala uliendelea huku staftahi ikimalizika, na hatimaye waliafikiana kuwasiliana na familia iliyoko Tanzania, kwa ajili ya ufuatiliaji. Baada ya hapo, kila mmoja aliingia chumbani mwake kujipumzisha, Imam Chaullah aliwaaga kwamba atakwenda mahala mara moja na angerejea kiasi cha takribani saa mbili mbele.



    Kabla hajatoka, alitumia takribani dakika thelathini kuuchangamsha mwili kwa mazoezi. Baada ya kwisha kumaliza, aliingia bafuni kuutaka radhi mwili.



    Ili kuendana na mazingira ya jijini la London, Imam Chaullah hakuiona haja ya kuendelea kuvaa kanzu, badala yake alivalia shati la mikono mirefu la rangi ya samawati; alilolichomekea kinadhifu katika suruali yake ya kadeti ya rangi ya ugoro. Miguu aliitumbukiza kwenye viatu vya rangi hudhurungi. Uhaba wa ndevu katika wajihi wake, ulimfanya aonekane angali kijana mdogo mno.



    Alishuka ghorofani huku mkononi akiwa na kijibegi cha wastani alichohifadhia baadhi ya nyaraka zake muhimu, aliziendea teksi zilizoeegeshwa jirani ya barabara kwa ajili ya kusubiria abiria. Akaichagua moja na kujitoma ndani.



    “Assalamu aleykum warahmatullah wabarakatuh,” dereva teksi alianza kumsabahi Imam Chaullah.



    “Waaleykum Salaam habiby!”



    “Keyfal umur?” dereva teksi alisema kwa kiarabu, akimaanisha ‘vipi mambo?’



    “Al-umur jayyid,” Imam alijibu, akimaanisha ‘mambo poa’

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Katika nchi kama Uingereza, ni aghalabu kumsikia mtu akikusabahi, achilia mbali kukusaili, kwa lugha ya kiarabu. Hilo lilimtaabisha kichwa Imam Chaullah, lakini hakupaparika kuliulizia.



    Imam Chaullah alimwelekeza dereva teksi, ampeleke kituo cha polisi cha West End. Dereva aliwasha gari, na safari ikaanza, huku Imam Chaullah akiongeza umakini kwa dereva huyu.

    Lengo la Imam Chaullah kwenda kituo cha Polisi; kwanza, ni pamoja na kwenda kujitambulisha kama mpelelezi wa kujitegemea, kama ambavyo sheria inaelekeza; pili, kuelezea dhamira yake ya kuchunguza kifo cha Mtanzania aliyezikwa nchini humo; tatu, kujaza na kulipia fomu kwa ajili ya kuhuisha (ku-renew) kibali chake cha upelelezi kilichokuwa kimebakiza mwezi mmoja tu kuisha muda wake (expire).

    __________



    TANGU Imam Chaullah aliposhuka toka ghorofani, na kuifikia ile teksi, palikuwa na vijana wawili pembezoni mwa jengo alimolala usiku wa kuamkia siku hiyo: mmoja mwenye mwonekano wa kijerumani, na mwingine mzungu halisi, walitulia ndani ya teksi yao wakimfuatilia nyendo zake kwa umakini.

    Baada ya teksi aliyopanda Imam kuanza safari, haraka yule mjerumani, akatoa simu yake ya mkononi, akabofya namba, na kuiweka sikioni ili kutoa taarifa kwa aliyemkabidhi jukumu hilo. Baada ya kujibiwa, aliondoa teksi yao na kuifuatilia teksi aliyoingia Imam Chaullah.



    Ndani ya teksi, Imam Chaullah aliendelea kuangaza huku na kule, akiyakumbukia baadhi ya maeneo aliyokuwa akiyazuru kipindi akiishi hapo London, hakuwa na haja ya kusemezana chochote na dereva wake. Mara kadhaa aliangaza huku na kule na kutabasamishwa na kila kilichosawirishwa na macho yake.



    Dakika takribani arobaini na tano za mwendokasi, zilitosha kabisa kumfikisha Imam Chaullah kituo cha Polisi cha West End kama alivyokusudia. Pilika za watu waingiao na kutoka kituoni hapo, zilikuwa kubwa mno. Pamoja na dereva kuzima gari baada ya kuegesha hapo kituoni, Imam Chaullah aliendelea kutulia kuketi kimya kama anayetafakari jambo. Aliangaza huku na kule kama aliyemfananisha mtu.



    “Okay, may I ask you something please?” Imam alimsaili dereva wake kwa lugha ya kingereza, akiwa na maana ya kuomba ridhaa ya kumuuliza jambo.



    Dereva alijibu kwa lugha hiyohiyo ya kimombo huku akimgeukia Imam Chaullah, na kuchanulisha tabasamu usoni mwake. Maongezi yakaendelea kwa lugha hiyo ya kingereza.



    “Kwanini ulianza ulinizungumzisha kwa lugha ya kiarabu?” Imam Chaullah alisaili. Dereva alicheka huku akijifuta uso kwa viganja vya mikono yake.



    “Nilikuoneni jana mlipowasili pale Grand Plaza mkiwa mmevalia kanzu na kofia, na vilemba, nikajua tu huwenda mkawa ni waislamu.”



    “Kwahiyo kila Muislamu anajua kiarabu, siyo?” Imam Chaullah aliuliza.



    “Kwakuwa hiyo ndiyo lugha waitumiayo katika ibada zao, nafikiri inafaa wakiimudu vyema.”

    Baada ya jibu la dereva teksi, Imam Chaullah aliondosha hofu na kufungua mlango, kisha akamshika dereva wake begani na kumwambia. “Nisubiri, narejea punde.”



    Aliteremka, na kuanza kutembea akielekea ndani ya kituo. Ile teksi iliyowabeba wale vijana wawili, nayo iliwasili hapo kituoni, na kuegeshwa pembezoni mwa barabara. Vijana waliendelea kufuatilia nyendo za Imam Chaullah, na kutoa taarifa mahala panapo husika.



    Ndani ya ofisi ya kituo cha polisi, Imam Chaullah alipokelewa vizuri, na kuhudumiwa kwa wakati. Takribani dakika thelathini na tano, akawa tayari amemaliza, na kutoka. Aliingia ndani ya teksi na kumwelekeza dereva wake, “Sasa, nipeleke Backingham gates.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Bila shaka. Umbali gani tokea hapo Backingham gates?”



    “Ni kwenye jengo hilohilo la Backingham gates.”



    Mzee Tafawa, alipata kumwambia Imam Chaullah kwamba maalim Kondella, anamiliki ofisi yake katika jengo la kibiashara la Backingham gates, inayojihusisha na shughuli kama hizo afanyazo yeye pale AL-AMIN CONSULTATION. Ingawaje yeye, Imam Chaullah, ana kazi zaidi ya moja, ikiwemo upelezi, ushauri wa masuala ya kidini, uongozaji ibada msikitini, nk. Kwa hivi, hakuitambua hasa kazi ya maalim Kondella ni ipi.



    Backingham Gates, ni moja kati ya majengo makubwa ya kibiashara jijini London. Jengo hilo lilisheheni ofisi na maduka mbalimbali yaliyopangishwa kwa makampuni na watu binafsi walioweza kumudu gharama.



    Teksi iliyombeba Imam Chaullah iliegesha kwenye maegesho ya magari ya wageni. Kabla ya kuteremka, Imam Chaullah alifanya kama alivyofanya kule kituo cha polisi; aliketi kwa muda, kisha kwa umakini aliangaza kulia na kushoto. Safari hii swali lake kwa dereva liliashiria mwisho wa msafara wao: “Bei gani wanidai?”



    Dereva alipotaja bei, Imam Chaullah aliingiza mkono mfukoni, akatoa pochi yake iliyosheni dola na paundi, akahesabu na kumlipa dereva wake kabla hajateremka.



    Wakati Imam akishuka kwenye teksi, wale vijana waliokuwa wakimfuatilia, nao waliwasili na kuegesha teksi yao upande wa pili wa jengo hilo, na kuendelea kufuatilia kila hatua.



    Imam alitembea hadi kwenye mlango mkuu wa Backingham, alimsogelea bwana mmoja mzungu aliyeonekana mwenyeji wa jengo hilo na kumsabahi, “Habari.”



    “Nzuri.” Mzungu alijibu hali akiendelea kutembea kwa kuelekea nje.



    “Samahani, naomba msaada kidogo,” Imam alisema, na mzungu akasimama huku akimgeukia.



    “Unaweza kumfahamu maalim Kondella?”

    Sura ya mzungu ilibadilika na kuwa mfano wa mtu aliyeona kinyesi. Alimtazama Imam Chaullah kwa sekunde kadhaa, kisha alisema, “Hivi ninyi watu weusi huwa mna weusi hadi kwenye ubongo? Yaani, niache kazi zangu nikae nakariri majina ya watu?”



    Mzungu hakuona tusi zuri wala adhabu kali zaidi ya ubaguzi wa rangi. Hilo halikumshitua sana Imam Chaullah kwani katika kipindi akiishi hapo London, aliyazoea hayo ya kubaguliwa kwa sababu ya rangi. “Oh, niwie radhi bwana, huyo ninayemuuliza anahusika na masuala ya Di–”



    Kabla hajamalizia kauli yake, mzungu alimkatisha, “Sikiliza mtu mweusi–nenda ghorofa ya kwanza ndiko wamepanga nguruwe weusi wengi, wanaweza kukusaidia.”



    Ghadhabu ilianza kumcheka Imam Chaullah, lakini alijizuia. Aligeuka nyuma, akaondoka na kuelekea huko alikoelekezwa. Wakati Imam akiiendea lifti ili impeleke juu, yule mzungu mbaguzi alitoka nje ya jengo, alivuka hadi upande wa pili wa barabara ambako kuna teksi nyingi zilizoegeshwa zikiwasubiri wateja.



    Kupitia lango kuu la kuingilia Backingham Gates lililokuwa wazi, vijana wawili walifanikiwa kumwona Imam Chaullah akiteta jambo na yule mzungu huku wakielekezana. Kwa bahati kabla hawajafanya lolote, walimwona mzungu akitoka na kwenda usawa waliokuwapo wao.



    Kijana mmoja kati ya hao wawili alifungua mlango wa teksi yao, akateremka, na kujifanya kunadi usafiri wao, ilhali yule mwenziye akijifanya ndiye dereva. Aliwahi kumchangamkia yule mzungu, “Twende bosi.”

    Mzungu aliifikia teksi yao, ambayo tayari mlango wa mbele tayari ulikuwa wazi, akaingia na kusema, “Nipeleke Pharell Café.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Bila kufanya zohali, kijana aliyejifanya tingo, alimsaidia mteja wao kuufunga mlango wa mbele, kisha yeye akaufungua wa nyuma, akaingia na kuketi. Walipokwishafunga milango, dereva aliwasha gari na kuanza kuondoka eneo lile taratibu.



    Hawakufika mbali, dereva akapata upenyo, akalitoa gari barabarani na kulisogeza pembeni katika eneo ambalo halikuwa na wingi wa watu wala magari. Hali ile ikamtisha yule mzungu, na kabla hajauliza sababu za dereva kulihamisha gari barabarani, tayari aliimaizi ishara toka kwa dereva kwenda kwa konda wake aliyeketi nyuma.

    __________



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog