Search This Blog

MIRATHI YA HAYAWANI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : MAUNDU MWINGIZI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mirathi Ya Hayawani

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Simu ya mezani iliita kipindi Imam Chaullah akijiandaa kutoka ofisini mwake, kwa ajili ya kuwahi ibada ya sala msikitini. Muda ulikwisha kutimu sita na nusu adhuhuri. Jina lake kamili ni Hussein Chaullah; Imam ni wadhifa wake kama kiongozi mkuu wa masuala ya kiibada na kiuongozi kwa ujumla msikitini.



    Simu iliendelea kuita hali imami akimalizia kuhifadhi nyaraka kadhaa mahala pake, kisha alijongea mezani na kuutwaa mkonga wa simu, “Labbaika.”



    “Imam, kuna mgeni anahitaji kukuona!” Sango, katibu muhtasi wa Imam Chaullah, alijibu simuni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mbali ya kuwa Imam, Imam Chaullah pia ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Maarifa Consultations Centre, ambayo pamoja na shughuli nyingine za siri, hujishughulisha na ushauri wa kitaalamu wa masuala ya shariah za dini; Talaka, Mirathi, Ndoa, Eda, Zaka, Hijjah, nk.



    “Umeangalia muda kwenye saa yako?” Imam Chaullah alimsaili Sango.



    Kwa kawaida na taraibu za ofisi ile, ukishawadia muda wa ibada, haparuhusiwi kufanya kazi hadi baada ya kumaliza ibada, hivyo, kitendo cha Sango kuomba kumuingiza mgeni ofisini kwa muda ule, ilikuwa ni kinyume na utaratubu wao.



    Sango alipiga kimya cha muda, akitafakari cha kujibu, kisha kwa utulivu alisema, “Ni mtoto wa mzee Tafawa.”

    Baada ya jibu hilo, ikawa zamu ya Imam Chaullah kupiga kimya akitafakari. Mtoto wa mzee Tafawa ni nani mbele ya Ibada?



    Huku akitambua udhaifu wa atendalo, Imam Chaullah, alitoa idhini, “Ah, haya mruhusu aingie.”



    Kumi bora ya watu wenye ukwasi mkubwa jijini Dar es Salaam, isingeliweza kutimu pasi na kulitaja jina la mzee Tafawa bin Haidari; ambaye tofauti na matajiri wengine wengi, mzee huyu alikuwa mkarimu, mpole, mchamungu, mwenye kusaidia watu.



    “Assalamu aleykum,” Makame, mtoto wa kiume wa mzee Tafawa, alitoa salamu mara baada ya kufungua mlango na kuingilia ofisini.



    Pamoja naye, aliandamana na binti; mrefu na mwembamba, rangi yake maji ya kunde, hijabu la rangi nyeusi lilimkaa vyema maungoni huku ushungi ukimpendezesha wajihi wake.

    “Waaleykum salaam warahmatullahi wabarakatuh,” Imam Chaullah alijibu huku akisimama kuwalaki wageni wake. “Haya, karibuni waungwana.”



    Mara ya mwisho Imam Chaullah kumwona Makame, ilitokezea kwenye moja kati ya vipindi vya runinga, alipokuwa akilinadi shindano la kumsaka mrembo wa wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.



    Imam Chaullah, aliyekuwa amevalia kanzu ya rangi ya dongo, huku kichwani akibandika baraghashia yenye mshabaha na rangi ya kanzu, aliketi kwenye kiti chake kipana kilichopachikwa vizuri nyuma ya meza ya mpingo. Akina Makame waliketi kwenye viti vya wageni vilivyopangwa kwa kutazamana mbele ya meza hiyo.



    Juma moja limepita kabla ya ujio huo wa Makame, mzee Tafawa naye alimzuru Imam Chaullah, kwa mazungumzo nyeti na ya faragha. Hii ilikuwa ni moja kati ya sababu zilizomfanya Imam Chaullah amruhusu Makame kuingia ofisini, akiamini kwamba huenda aliagizwa jambo muhimu na baba yake.



    “Haya, karibuni!” Imam aliwakaribisha kwa mara nyingine huku akiwatembezea macho yake kwa awamu.

    “Ahsante Imam,” Makame alijibu kwa sauti kavu iliyoathiriwa na pombe kali.



    Baada ya kujibu, huku akijikuna sharafa zilizosambaa mashavuni mwake, Makame alimgeukia binti aliyeambatana naye. Na, kama aliyemdokeza jambo, papo hapo binti alianza kfungua ukurasa, “Aam – mi’ naitwa Johari, kilichon–ileta ni shida, au tuseme ni ushauri kuhusiana na mambo ya mirathi.”

    Kwa haraka, Imam Chaullah aling’amua kitu toka kwenye kitetemeshi cha sauti, pale alipotamka neno ‘kilichonileta’, ni kama aliyetaka kutamka ‘kilichotuleta’.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana taabu, mirathi ni somo pana, liwezalo kuchukua zaidi ya mwaka kulihitimu. Kwa hivi, itakuwa aula endapo utapambanua hitaji lako; unahitaji kushauriwa nini hasa?”

    Johari, kama alivyojitambulisha, alimtupia jicho Makame kama dalili ya kutahayari, kisha kwa wepesi alimgeukia Imam na kusema, “Ninachohitaji ni kujua namna mgawanyo wa mirathi uwavyo, endapo nitaamua kuacha wosia kwa ahli yangu, kabla sijafariki.”



    Shahada yake ya kwanza katika Law and Shariah, Imam Chaullah aliipata katika chuo kikuu cha Al-azhar, Misri, kabla ya kuendelea na hatua nyingine za kimasomo nchini Uingereza.



    “Kwa mujibu wa dini, mirathi hugawanywa na Mungu mwenyewe, ambaye kimsingi ndiye mwenye kujua siri ya lini utafariki, utaacha mali kiasi gani, nani kati ya warithi wako atakayekuwa hai wakati wewe unafariki, nk. Hivyo, mara baada ya mja kutokwa roho, mali yake hujigawa yenyewe kwa kadiri ya warithi waliopo,” aliweka kituo kidogo kuyapatia fursa maneno yake kupenya kichwani mwa muulizaji. “Haupaswi kuandika mirathi, juu ya nani atachukua nini endapo ukifariki, ilhali hakuna ajuaye ni nani atatangulia mbele ya haki.”



    Kimya kilichopita baada ya Imam kutoa majibu, kilimdhihirishia kwamba kipo kitu kingine nyuma ya ujio huo, kwa namna wanavyotaabika kujenga maswali.



    “Okay, tuchukulie amefariki mwanamume; akaacha baba, mama, watoto watatu na mke … mgawanyo utakuwaje?” Johari alisema.



    Imama aling’amua kitu kingine tena, Johari aliyekuwa anataka kujua mgawanyo wa mirathi, kwa ajili ya wanaye na nduguze, sasa amebadilika na kutaka kujua kuhusu mwanamume aliyefariki na kuacha mali pamoja na familia. Badala ya kujibu swali, Imam alimtazama usoni Johari kwa sekunde kadhaa, kisha aliinuka kitini angali ametabasamu, na kuliendea jokofu kubwa lililokuwa upenuni mwa kabati lake la vitabu.



    Alipolifungua, aliwageukia wageni wake, “Mnakunywa vinywaji gani waja wa Mola?”



    “Oh, usijali sheikh, sisi hatuli wala hatunywi,” Makame alijibu huku Johari akimuunga mkono kwa kutikisa kichwa.



    “Laa hasha, msijivike sifa ya malaika; wao ndiyo hawali wala hawanywi,” Imam alijibu na kuongezea, “kunyweni hata maji basi, ili tu mniachie baraka zenu!”



    Imam aliendelea kusubiri jibu ilhali mlango wa jokofu u–wazi, naye akiwa amesimama angali amewageukia wao.

    “Duh – haya sheikh,” Makame alikubali kishingo upande, alionekana mwenye haraka na mshawasha.



    “Mashaallah – tumeelekezwa kuwakirimu wageni,” Imam alisema huku akichukua chupa mbili za maji, kisha alilifunga jokofu.



    Alipokwisha, akanyoosha mkono hadi juu ya jokofu hilo, alichukua bilauri mbili na kurejea nazo mezani, ambapo aliwawekea kila mmoja chupa moja ya maji na bilauri yake, kisha alizunguka nyuma ya meza yake na kuketi.



    Imam Chaullah alianza kujibu swali aliloulizwa hapo awali, “Inanipa taabu kutafuta namna sahihi ya kukujibu, kutokana na aina yako ya uulizaji. Kwa kawaida, wateja wangu hupaswa kujipambanua kunako hitaji husika. Mathalani, unaweza kuniambia hivi, ‘Imam, nimefiwa na mume, ameacha watoto watatu: mmoja alimzaa kwa mke mwingine, na wawili nimewazaa mimi. Ameacha baba na mama, na ameacha mali zenye thamani kadhaa. Hapo, inakuwa rahisi kwangu kukokotoa na kukupa mwongozo wa mgawanyo wa mirathi, kwa mujibu wa kitabu na Sunnah – walakini, kwa mtindo wa uulizaji wako, unazalisha tena maswali badala ya majibu.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Makame alikuna kichwa, Johari akashusha pumzi nzito huku akiupachika mguu wake wa kulia juu ya ule wa kushoto. Bado majibu ya Imam Chaullah hayakukidhi matlaba zao.

    _________



    NJE ya nyumba ya mzee Tafawa, maeneo ya Msasani, jijini Dar es Salaam–upande wa pili wa barabara, iliegeshwa gari aina ya Prado. Ndani ya Prado, waliketi wanamume wawili: aliyeketi nyuma ya usukani, alivalia miwani myeusi ya jua huku hereni ya dhahabu ikionekana kwa tabu, kutokana na sehemu kubwa ya kichwa chake, hadi usawa wa masikioni, ukifunikwa na kofia pana aina ya mzula. Aliyeketi siti ya nyuma, alivalia fulana mchinjo ya rangi ya manjano, huku sehemu kubwa ya uso wake ikizungukwa na ndevu.



    Wakiwa wametulizana kimya ndani ya Prado, mara walishuhudia geti la nyumba ya mzee Tafawa likifunguliwa taratibu, kulipisha gari la kifahari, aina ya V8, limbebalo mzee Tafawa. Haraka jamaa mwenye miwani aliliwasha gari na kulielekeza usawa ule litokeapo gari la mzee Tafawa.



    Kijana alieketi siti ya nyuma, katika Prado, alitoa simu yake na kupiga mahala, ili kutoa taarifa ya zoezi lililokuwa likielekea ukingoni, walakini, simu yake iliita bila kupokelewa. Baada ya kupiga zaidi ya mara moja hali majibu yakiwa ni yaleyale, hatimaye alimwamuru kutekeleza wajibu wake.



    Ilipokuwa gari ya mzee Tafawa tayari imekwishapanda mwinuko utokeao usawa wa nyumba yake, na kuifikia barabara, ndipo Pajero ilipongeza mwendo kwa kasi, kulielekea gari la mzee Tafawa. Kama ambavyo mpango ulivyokuwa umesukwa, Pajero lilifanikiwa kulipamia gari la mzee Tafawa, kwa kuulenga upande wa kushoto wa dereva, akaapo mzee Tafawa.



    Kishindo kikubwa kilisikika, kufuatia ajali hiyo, huku gari ya mzee Tafawa iliyokuwa imekaa tenge kutokana na mwinuko iliyokuwa ikiupanda, ilibamizwa na kushindwa kuhimili; iliporomoka kwa kasi tokea kule juu ya mwinuko hadi chini kabisa usawa wa nyumba yake ikiwa imeharibika vilivyo.



    Pajero iliyosababisha ajali, ilibaki juu barabarani. Japo dereva wake alijitahidi kuidhibiti isipinduke, walakini, nayo iliharibika sana upande wa mbele, licha ya kuwa na ngao madhubuti.

    _________



    “KIMSINGI, yako mafungu ya migawanyo ya Mirathi kwa kila mrithi halali. Mathalani; Mke hurithi thumni (moja ya nane) ya mali yote, endapo mumewe ameacha mtoto au watoto. Na, ikitokea mume hakujaaliwa kupata mtoto, basi mke hurithi robo (moja ya nne) ya mali ya mumewe,” Imam Chaullah alianza kuichambua mirathi.



    Imam Chaullah aliangalia saa yake ya mkononi na kutanabahi kwamba muda wa sala ulikwishampita. Aliganda kidogo, kutafakari kipi cha kufanya, punde alipitisha uamuzi kwamba angelisali baada ya mazungumzo na wageni wake. Maelezo marefu ya Imam Chaullah, hayakuwapamba vichwani akina Makame, wala hayakuonesha dalili ya kukidhi haja zao.



    Si shida ya Makame kujua mke hupata nini, kipo ambacho alikikusudia, lakini Imam Chaullah, kwa makusudi hakukigusia, aliendelea na maelezo yasiyo na tija kwa wageni wake, “Cha kuzingatia, mgawanyo wa Mirathi, kwa mujibu wa dini, utatekelezwa baada ya kuhakikisha kwanza, yamelipwa madeni yote ya marehemu endapo alikuwa akidaiwa. Waama, gharama zote za mazishi, zitatolewa kwenye mali yake marehemu kabla ya kugawa Mirathi. Na, pia –”



    Kabla Imam Chaullah hajamalizia maneno yake, Johari alimkatisha, “Hebu Imam ngoja kwanza – mafungu ya watoto yakoje, endapo marehemu ameacha watoto wawili; wakike na wakiume?”



    Wanataka kujua, vipi urithi utagawanywa, endapo marehemu ameacha mwana na binti; hiyo ndiyo ilikuwa shida yao haswa. Na, Imam Chaullah alianza kuwajibu angali ametabasamu, “Hapo kuna maelezo kidogo tu, ni kwamba–”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kabla Imam Chaullah hajaifikisha mwisho kauli yake, mlango wa ofisini uligongwa kwa nguvu, na kabla hajatanabahi, aliingia kijana; mwembamba, mweusi, mrefu wa wastani, chini ya ukingo wa jicho lake la kushoto alibandika plasta. Alisema, “Aisee, samahani –”



    “Vipi tena?” Makame alimsaili.



    Majibizano yao, ndiyo yaliyomfanya Imam Chaullah atulize nafsi, baada ya kujiridhisha kwamba kijana yule yuko pamoja na akina Makame.



    “Max anapiga simu muda mrefu, nafikiri kuna jambo,” Kijana alijibu huku akiikabidhi simu husika kwa Makame.

    Makame aliitwaa simu, na kusema, “Tusubiri nje.”



    Baada ya kijana kutoka, Johari alimgeukia Imam Chaullah na kusema, “Tuendelee Imam!”



    Simu iliyoletwa na kijana, ilianza tena kuita wakati Imam Chaullah akijiandaa kuendelea na maelezo yake. Ilimbudi apige kimya huku akimtazama Makame, ambaye aliduwaa kwa sekunde kadhaa kabla hajaipokea simu, “Hallow!”



    Ukimya ulitanda ofisini, wakati Makame akisikiliza sauti ya mtu aliyempigia. Ghafula, macho yalimbadilika, kasikika akibwata, “Whaat! lakini – hatukukubaliana leo – kwanini mmeam-”



    Makame alihamanishwa na taarifa alizopokea simuni, macho yake makubwa yazidi kutandazika kiasi cha kuudhihirisha wajihi wake wa kikatili. Imam Chaullah na Johari walibaki wakitazamana bila kumaizi kinachoendelea. Mara, Makame alikata simu na kumwambia Johari, “Tuondoke!”



    Bila kuhoji zaidi, Johari alisimama, akafungua pochi yake na kutoa noti mbili za dola miamoja. Alimkabidhi Imam Chaullah na kumuaga, “Ahsante kwa darasa zuri, tutarejea kumalizia somo.”



    “InshaAllah – karibuni siku nyingine.” Imam alisimama wakati wakiagana.



    Johari aliungana na Makame, aliyekuwa tayari amekwishautwaa mlango, wote kwa pamoja walitoka nje – wakatoweka.



    Imam alijibwaga kitini, viwiko vya mikono yake akivitenga juu ya meza huku vikishirikiana na viganja, kukipakata kichwa chake.



    Akiwa anakiandaa kichwa chake kuyatafakari naa kuyachambua mazungumzo yake, dhidi ya wageni waliondoka muda mfupi uliopita, mlango wa ofisini mwake uligongwa, Imam Chaullah alipoinua macho yake kutazama mlangoni, papo mtu aliingia.



    Baada ya kumwona aliyeingia, alirudisha macho yake mezani, kisha alipikicha viganja vya mikono na kuufuta uso wake kabla hajasema, “Oh, Mzaramo–karibu akhui.”



    Mzaramo ni lakabu aliyobandikwa, kwa sababu ya kuongea sana, walakini, jina lake halisi ni Kibwana Mnubi. Ofisi ya mzaramo, pamoja na ya Imam Chaullah, zinapatikana katika jengo hilo la NSSF lililopo Kariakoo, ambapo shughuli zifanywazo na ofisi ya Mzaramo ni huduma za bima.



    “Unazo khabari?” Mzaramo alihoji angali amesimama.

    “Hata salamu sheikh? Hebu keti kwanza yakhe,” Imam alijibu, huku akiustaajabia ujio wa Mzaramo.



    Bila ya kusalimu, Mzaramo alifunguka, “mzee Tafawa amepata ajali mbaya ya gari – hana kauli!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mzaramo aliketi hali Imam Chaullah akisisima huku mikono yake akiwa amejitwisha kichwani.



    “Laahaullah…” Imam Chaullah aliiacha kauli yake hiyo ikielea angani.



    “Walaa kuwwata!” Mzaramo alimalizia kauli.



    Imam aliporudi tu kuketi, mzaramo akasimama na kuaga, “Haya Imam, nilikuja kukupasha khabari hizo tu.”



    “Hebu keti kwanza mzaramo!” alipoketi, Imam akaendelea, “enhe, saa ngapi na wapi? Na, chanzo cha khabari hizi ni kipi?”



    Mzaramo alitandaza miguu yake, kisha akauegesha mgongo wake sehemu ya nyuma ya kiti alichokalia huku uso wake ukiangalia juu ya dari kwa sekunde kadhaa. “Nimemwona Makame akitokea ofisini mwako, nikadhani amekuja kukujuza taarifa hizi – kumbe alifuata nini?”



    “Tuachane na hayo ya Makame, hayana faida kwa sasa, nijibu kuhusu ajali!”



    “Nimepigiwa simu hivi punde, kwamba mzee Tafawa, amepata ajali ya gari, mbele kidogo tu ya nyumba yake, gari yake hasa ule upande aliokuwa amekaa yeye, ndiyo umeharibika nyang’anyang’a,” alitongoa kwa uto, “Majirani wanadai, kishindo hicho cha ajali kilifuatiwa na mlio wa bunduki.”



    “Wewe–usiniambie?”



    “Nd’o nimeshakwambia sasa–nd’o maana nilitaka kujua kuhusu ujio wa Makame hapa kwako kwa maana–” aliiacha kauli yake ikielea.



    Ujio wa Makame pale ofisini kwa wakati ule, ulianza kumtengenezea maswali mapya kichwani Imam Chaullah. Na, alipoyakumbuka mazungumzo ya Makame, pale aliposema, ‘Hatukukubaliana leo–kwanini mme–’ na ‘Tuondoke–’, vilimpa majibu lukuki.



    “Takribani siku nne zilizopita, mzee Jumbe alikuja Dar akitokea kwao Tanga kufuatia wito aliopewa na mdogo’ake, mzee Tafawa, kuhusu mambo nyeti yahusianayo na mali zake–bila shaka harufu ya hatari alikwishaanza kuinusa. Hivi majuzi, alinitembelea nyumbani kwangu tukateta, na hivi jana tu, aliondoka akirejea Tanga.”



    Pamoja na Imam Chaullah kufahamu kwamba, mzee Jumbe Haidari na mzee Tafawa Haidari, ni ndugu; mtu na kaka yake, kwa baba na mama, na kwamba mzee Jumbe ni mkubwa kwa miaka mitatu mbele ya mzee Tafawa, pia aliufahamu usuhuba uliopo baina ya Mzaramo na mzee Jumbe, kwa hivyo, hakuyapuuza maneno toka kinywani mwa Mzaramo.



    Juma moja iliyopita, mzee Tafawa alimfikia Imam Chaullah ofisini kwake, na kuzungumza naye mambo mazito kuhusiana na mali zake. Na, kwa mujibu wa mzaramo, mzee Jumbe naye aliwasili jijini Dar es Salaam, kwa mazungumzo ya mali. Kengere ya hadhari iligonga kichwani mwa Imam Chaullah.



    “Inawezekana kuna wanaotaka kumfanyia mchezo mchafu nini?” Imam Chaullah alimsaili Mzaramo.



    Huku akiyakodoa macho yake, Mzaramo alisema, “Unauliza tongotongo machoni?”



    “Mnh–yaani familia yake mwenyewe ndo imuhujumu?”



    “Kikulacho kinguoni mwako sheikh!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mazungumzo yao yalihitimishwa na maafikiana kwamba, wajiandae ifikapo saa kumi alasiri, wafike nyumbani kwa mzee Tafawa wakampe pole na kumjulia hali.



    “Nimempigia simu mzee Jumbe, amesema yuko njiani anakuja Dar!” Mzaramo alimalizia kauli wakati akitoka ofisini, na kuurejesha mlango.



    Fikara na mawazo ya Imam Chaullah, vilimrejesha muda wa juma moja nyuma, pale mzee Tafawa alipomtembelea ofisini mwake, na baada ya masikitiko na hofu ya mambo yanayomuwinda, alihitimisha kwa hivi, “…hii ndiyo hatari inayoniwinda kwa sasa, na kwa sababu hiyo, ndipo nilianza kupunguza miradi yangu, pamoja na pesa taslimu, na kuvihamishia ughaibuni.”



    “Huko ughaibuni, mali zako ziko kwa jina lako?” Imam Chaullah alimsaili mzee Atrashi.



    Mzee Tafawa alifungua mkoba wake na kutoa bahasha ya kaki, ndanimwe mlikuwa na karatasi tatu; alizitoa na kuzibwaga mezani huku akimtupia macho Imam Chaullah. “Situmii jina langu; nimemwandikisha binti yangu, Sauda, ingawaje hata yeye hajajua chochote. Tujuao khabari hizi ni watu watatu tu: Mimi, wewe na maalim Kondella ambaye ndiye niliyemkabidhi kusimamia mali hizi.”



    “Makubaliano yako hivi,” alianza kudhihirisha dhamira yake, “malengo yangu ni kumkabidhi rasmi Sauda, mali zangu mara baada ya kuhitimu masomo yake, walakini, endapo ikitokea kabla sijatekeleza hayo, mauti yakanifika, nataka ninyi mumkabidhi binti yangu, Sauda, mali yote. Kisha, mali hii iliyobaki Tanzania, muigawanye mirathi kidini. Warithi wangu ni bi Zainab, mke wangu; bwana Jumbe, kaka yangu; na bi Msimbe binti Haidari, dada yangu.”



    “Je, itakuwaje endapo kama ulivyokwisha kusema, ukatangulia mbele ya haki, halafu huyo maalim Kondella akaingiwa na sheytwani, akadhulumu mali ambayo kimsingi ni yeye ndiye anayeifahamu na kuisimamia?”



    Badala ya kuonesha makini yake, mzee Tafawa alitabasamu na kusema, “Nimemchagua maalim Kondella kwa sababu ni mtu adili kama ulivyo wewe, ni mchamungu tamthili yako, na hana makuu. Pia, sijampa jukumu hilo peke yake, bali nimekuchagua nawe, ili uwe sehemu ya mkataba huu wa siri. Sasa, kama maalim Kondella atataka kuniangusha, itambidi kwanza afanikiwe kukushawishi na wewe uwe upande wako–itakuwa ngumu mno kwa wasomi wawili. Lakini pia, Kondella naye ni mbobezi wa shughuli kama hizi ufanyazo!”



    “Shughuli zipi–hizi za usheikh; ushauri wa shariah za dini?” Imam Chaullah alitatarisha maneno.



    “Shughuli zako zote; za siri na dhahiri!” mzee Tafawa alitabasamu, “nakujua vyema Sheikh Chaullah!”



    Midomo ilimshuka Imam Chaullah; alitamani kucheka na kununa kwa wakati mmoja, hakuweza, badala yake alitengeneza sura ya mfadhaiko.



    “Na, tayari maalim Kondella amekwishatia sahihi yake kwenye mkataba huu akiwa kama msimamizi wakwanza, nawe nakuomba utie sahihi yako kama msimamizi wa pili, kisha nami nitakwenda kutia sahihi yangu, halafu kila mmoja wenu nitamrejeshea nakala yake. Katika kipindi chote ambacho tutakuwa pamoja, nitakuwa nikikulipeni kila mwezi kwa kuwa wasimamizi na waangalizi wa mali hiyo.”



    Maongezi yaliendelea, mzee Tafawa alimweleza Imam Chaullah kwamba, maalim Kondella ni mtanzania aishiye London, katika jimbo la Hergh, ambapo ndipo zilipo shughuli zake. Baada ya majadiliano hayo, hatimaye waliafikiana, Imam Chaullah alitia sahihi katika nakala zote tatu ambazo mzee Tafawa aliondoka nazo kwa miadi ya kurejesha nakala moja wiki moja baadaye–ndiyo hakurudi tena mpaka ajali ilipomfika.

    _________

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    KUTOKEA Kariakoo, zilipo ofisi za akina Imam Chaulla, hadi nyumbani kwa mzee Tafawa, Msasani, si mbali sana. Bali, mshonano wa magari katika foleni ndiyo uliowafanya Imam Chaullah na Kibwana Mnubi, almaarufu Mzaramu, wawasili Msasani majira ya saa moja magharibi, tangu saa kumi na moja jioni walipoondoka kariakoo.



    Macho ya Imam Chaullah, aliyekuwa akitafuta mahala pa kuegesha gari yake, yalilakiwa na umati mkubwa watu waliojumuika nje ya nyumba ya mzee Tafawa. Baada ya kuliegesha gari, wakwanza kuteremka alikuwa Mzaramo, akifuatiwa na Imam Chaullah aliyekuwa akitumia leso nyeupe kujifutia jasho. Si kwamba garini hamkuwa na kiyoyozi, La hasha; kilikuwemo, bali hakikuwa na ubavu wa kudhibiti joto la mji huo.



    Magari yaliyopata ajali, yalikwishaondolewa eneo la tukio. Taathira pekee iliyoonekana ni damu kiasi, na viapande vya vioo vilivyovunjika wakati wa ajali.



    “Aisee ilikuwa ajali mbaya sana eenh,” Mzaramo alisema baada ya kusalimiana na wenyeji.



    “Hakuna ajali nzuri!” Mzee mmoja alimjibu.

    Huko ndani zilihanikiza sauti za wanawake wakilia kwa maombolezo. Sauti zao ziliwafikia akina Imam Chaullah kwa taabu.



    “Kwahiyo, mzee Tafawa mwenyewe yuko wapi? Tunahitaji kwenda kumwona,” Imam Chaullah alimsaili mzee huyo aliyeonekana mwenyeji, kwa kuwakaribisha na kuwapa muhtasari wageni.



    Badala ya kutoa majibu, mzee yule alimgeukia Imam na kumtupia jicho la mshangao, kisha alisema, “Hutoweza kumwona yeye, ila mwili wake tu muda ukifika.”



    Macho yalimtoka pima Imam Chaullah, aliielewa hekima ya maneno yale. Alijikuta akisema, “Innalillahi wainna…”

    Kama kawaida yake, Mzaramo akaimalizia kauli ya Imam Chaullah, “Wainna ilayhi raajiun!”



    “Pamesemwa kwamba, kufuatia ajali, bwana Tafawa aliumia sana, hivyo, ukafanywa mpango wa ndege ya dharura, kuwahi matibabu ya uhakika nje ya nchi, walakini, ambacho hawakukijua ni kwamba, bwana Tafawa tayari alikuwa katika ‘sakaratil mauti’. Mpaka ndege inashusha matairi yake uwanja wa ndege wa London, tayari bwana Tafawa alikwishatokwa roho, kwa hivyo, safari ya hospitali ikahamia mochwari.”



    “Sub-hanllah!” Imam Chaullah alitahayari.



    “Lo–Mungu mkali mno!” Mzaramo aliongezea.



    “Tunamsubiria bwana Jumbe, kaka wa marehemu, ili tusikie msimamo wake kuhusu mazishi, ijapokuwa ziko fununu kwamba, marehemu, katika nyakati za uhai wake aliusia kwamba, atakapofariki, azikwe kwa mujibu wa dini yake ya kiislamu; mojawapo ni kuzikwa mahala afiapo, na sasa amefia London.”



    Imam Chaullah na Mzaramo walilowa jasho la simanzi chapa. Kwa yakini, mzee Tafawa alikuwa ni moja kati ya nguzo za jamii ya waungwana.



    “Tunaweza kuingia kumwona bi mkubwa?” Imam Chaullah aliomba kuingiandani kumwona mjane, mama Makame.



    “Alipatwa na shtighali baada ya kupokea taarifa za kifo, na sasa amekimbizwa hospitali–Aghakan,” mzee alijibu, na kuongeze, “labda yule Sauda, binti wa marehemu, nd’o yuko ndani, ingawaje naye kila saa anapoteza fahamu!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kama mama Mkame amekimbizwa hospitalini, kutokana na hali yake kuwa mbaya kufuatia mshituko wa kifo cha mumewe, viweje basi anatajwa kuzimia kila mara akaachwa tu? Swali hilo, lilikosa majibu kichwani mwa Imam Chaullah.



    Usiku, wa Siku hiyohiyo, majira ya saa mbili, kikao cha kifamilia, kilichojumuisha ndugu na jamaa wa karibu, kiliongozwa na mzee Jumbe Haidari, aliyewasili jijini Dar, usiku wa kuamkia siku hiyo, kiliheshimu wosia wa marehemu, ambao kimsingi ni maamrishoo ya dini yake, kwamba azikiwe kwa mafundisho ya dini, ikiwa ni pamoja na kuzikiwa mahala atakapofia, hivyo, waliteuliwa watu wachache kwenda kushiriki mazishi mjini London, Uingereza.



    Kutoka na umbali, pamoja na uhaba wa fedha, waliopendekezwa na familia kwenda kudiriki mazishi hayo ni; Makame Tafawa, mtoto wa marehemu; mzee Jumbe Haidari, kaka wa marehemu; mzee Almasi Nzila, rafiki wa marehemu; na Imam Chaullah, kiongozi wa dini na sahibu yake marehemu. Walakini, milango i–wazi kwa yeyote atakayehitaji kuungana na msafara huu kwa gharama zake binafsi–atoke wapi?



    Uteuzi huo ulimpendeza Imam Chaullah, ilikuwa ni fursa adhimu kwake, ambayo ingemkutanisha na maalim Kondella huko London ili kujadiliana naye kuhusu mkataba wao na marehemu. Fauka ya hayo, maombi yake yalibakii kwenye jambo moja tu, walau maalim Kondellah awe na nakala yake ya mkataba, kwakuwa yeye hakurejeshewa.

    _________



    IMAM Chaullah aliwasili nyumbani kwake majira ya saa nne usiku akitokea kikaoni, nyumbani kwa mzee Tafawa. Tofauti na siku nyingine, siku hiyo nyumba ya Imam Chaullah, maeneo ya Sinza kwa Remmy, ilikuwa kimya huku giza likizizima; giza na ukimya ambao hata yeye, vilimshangaza.

    Alipokwisha kuufikia mlango, alitoa funguo za mlango, akazipachika kitasani, kisha taratibu aliufungua na kuingia ndani. Kutokana na giza, aliurudisha tu mlango bila kuufunga hadi mwisho, ili kwa kutumia nuru hafifu ya mwanga itokeayo nje, aweze kuona na kujongea hadi ilipo swichi ya kuwashia taa sebuleni.



    Alipoikaribia swichi, ghafula kwa nyuma yake, alisikia mchakacho wa nyayo za miguu ya mtu, kisha alisikia kitasa cha mlango kikishikwa taratibu. Aligeuka haraka kuuelekea mlango aliouacha wazi, lakini kabla hajatanabahi, aliushuhudia ukifungwa. Na, pao hapo ile nuru hafifu iliyokuwa ikiingia ndni ilitoweka.



    Badala ya kwenda kuwasha taa kwenye swichi kama alivyoazimu, alirudi kwa kasi hadi mlangoni. Akiwa amekwishaufikia mlango, kabla hajaugusa, mara taa ziliwashwa, na mwanga mkali ulihanikiza sebuleni nzima. Mwanzo alitaka kujilaghai kwamba huenda umeme ulikuwa umekatika, na kwamba ndiyo umerudi, lakini alikumbuka kuona taa za majirani zikiwa zimewaka kwa umeme huko nje, hivyo haukukatika. Aligeukia usawa ilipo swichi ya taa za sebuleni, sasa swichi zilikuwa zimewashwa lakini muwashaji asionekane.



    Kwa haraka na umakini, aliikunja kanzu yake kiunoni, kiasi cha kuifanya kaptula yake kuonekana, yu–tayari kwa mchezo wowote utakaotokea. Sebule kubwa ilikuwa kimya huku kukiwa hakuna dalili ya mtu yoyote. Hilo halikumpumbaza hata kidogo.



    Macho yake yalianza kuitalii sebule kwa udadisi na hadhari ya hali ya juu. Alianza na mashariki mwa sebule ambapo kabati kubwa la vyombo lilikuwa baina ya meza ya chakula na kiti cha sofa. Aliyahamisha macho yake hadi kushotoni mwake, ilipo korido ielekeayo msalani–hakuna mtu. Alihisi nywele zikimsisimka kichwani huku vinyweleo vikimtutumka kwenye ngozi, haraka aliinua shingo na kutupa macho darini, aliishia tu kujiridhisha na usalama kufuatia unadhifu wa jipsam zilizotumika kuipamba dari.



    Alipoyahamishia macho yake magharibi mwa sebule, ndipo alipigwa na mshituko pamoja na butwaa baada ya macho yake kupiga moja kwa moja jirani na jokofu kubwa. Alimwona mkewe akiwa amefungwa kamba mikononi na miguuni ilhali mdomoni akiwa amewekwa dubwasha linalomzuia kutoa sauti.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Allaahu Akbar,” Imam Chaullah alisema kwa sauti huku akisogea kule alikoketishwa mkewe.



    “Unatoa adhana, au?” Sauti nzito na kavu ilimdhihaki Imam Chaullah.



    Ingawaje Imam Chaullah hakumwona huyo kidume aliyemdhihaki, lakini aliisikia sauti ilikotokea; mbele kidogo, upande wa kulia, inakoanzia korido nyembamba inayoelekea chumbani mwake.



    Pumzi alizozishusha Imam, Ngiri haoni ndani. Kwa hadhari, alijongea taratibu hadi alipoifikia korido. Naam, aliwajihiana na jitu jeusi lenye miraba minne, likiwa limekunja nne juu ya kiti lilichoketi, huku sehemu kubwa ya kichwa chake ikimemezwa na kofia pana, na macho yake yakifunikwa na miwani myeusi.



    “We ni nani?” Imam Chaullah alisema kwa ukali, “na umefuata nini humu?”



    Zaidi ya kuendelea kuvuta sigara yake kwa dharau, jitu lile halikujisumbua hata kidogo kujibu. Baada ya kuona hajibiwi, Imam alijiweka tenge, ili aweze kuwaona wote wawili: mkewe, aliyekuwa kushotoni mwake, na wakati huohuo mvamizi wake, aliyekuwa akiendelea kuiteketeza sigara mdomoni mwake.



    Alipoashiria kutaka kumsogelea mkewe, sauti kavu ya lile jitu ilivuma, “Mara kadhaa nilizobahatika kuhudhuria mahubiri yako msikitini, nilipata kukusikia ukimwelezea Malakul mauti, waumini wengi wakusikilizao huonekana kumwogopa sana kiumbe huyo, kwa bahati mbaya, leo nawe umetembelewa na kiumbe huyo.”



    Imam Chaullah aliporejesha macho yake kwa jitu lile, tayari alilikuta likiwa limekwishainyanyua bastola yake na kumwelekezea yeye.



    Malakul Mauti, au kwa lugha ya Kiswahili Malaika wa kifo, si jina geni masikioni wala kinywani mwa Imam Chaullah. Hivyo, hata sababu za jitu lile kujinasibisha na Malaika huyo mwenye kutisha kwa dhamana aliyokabidhiwa na Mungu ya kuchomoa roho za viumbe wote haikuwa mbali ya upeo wake.



    Wakati Imam Chaullah akiendelea kuilazimisha akili yake kufanya kazi kwa kasi, jitu lile lilimtupia jicho mara moja tu kisha likamwashiria kumwita kwa kidole chake cha kati. Kwa sekunde kadhaa Imam alibaki wima, akilitazama jitu lile kwa ghadhabu, kisha aliafiki kwa kusogea hatua kadhaa karibu yake.



    “Simama vivyo hivyo, na usithubutu kujifanya huujui uwezo wa ajabu alio nao Malakul Mauti,” Jitu lilisema, lilipuliza angani moshi wa sigara, kisha likaendelea, “la kwanza, nahitaji kuondoka na nakala ya mkataba uliyobaki nayo baada ya kusainiana na mzee Tafawa; la pili, nahitaji kufahamu mahala alipo mtu aitwaye Kondella; la tatu, nahitaji maelezo ya kina kutoka kwako juu ya kiasi gani cha mali ya mzee Tafawa na mahala mlikokihifadhi kwa ajili ya kumkabidhi Sauda.”



    Kufikia hapo, Malakul Mauti, kama alivyojitambulisha, kwa kasi ya umeme, alibadili uelekeo wa bastola yake toka kwa Imam Chaullah aliyekuwa amemwelekezea, na kulilenga pipa la plastiki lililokuwa limeegeshwa kwenye pembe ya korido ile, kisha alilifyatulia risasi mbili mfululizo. Na, papo hapo aliurejesha mdomo wa bastola yake, aliyoifunga kiwambo cha kuzuia sauti, kwa Imam Chaullah.



    Macho ya Imam Chaullah yalishuhudia maji yaliyokuwa ndani ya pipa, yakivuja kwa kasi kupitia tundu lililoachwa baada ya risasi kupenya.



    “Hivyo ndivyo mwili wa mkeo utakavyovujisha damu punde tu endapo utachelewa kujibu au kubabaisha majibu,” Malakul mauti alionya.



    Imam alijikuta akimeza funda la mate kwa hofu, kisha alisema, “InshaAllah nitakujibu, lakini sifikiri kama ni hikma kujadiliana katika hali hi–vyema ukaweka silaha pembeni, nikupe kila utakacho kwa amani. Pia, si vibaya kama utaniambia ni nani aliyekuagiza vitu hivyo, ili nijue nimemkabidhi nani?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nilipowasili, nilichungulia vyumbani, nikawaona wanao wamelala. Ninakuahidi, endapo utanijibu vizuri maswali yangu, nitakuchomoa roho taratibu bila kuwabughudhi wanao, ila ukikaidi nitawaamsha waje washuhudie ninavyoing’oa roho ya mama na baba yao kifedhuli mno, kitu ambacho kitawaathiri mno kisaikolojia kipindi chote cha uyatima wao.”



    Kwamba hata kama atatoa ushirikiano, suala la kuchomolewa roho litabaki palepale, kazi kwake; kutii ili auawe kistaarabu, au kukasiri ili auawe kinyama.



    _________



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog