Search This Blog

MALAIKA? AU SHETANI? - 5

 





    Simulizi : Malaika? Au Shetani?

    Sehemu Ya Tano (5)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno hayo yakazalisha simanzi zaidi moyoni kuliko faraja, ukawatembezea macho yako wote mle chumbani, kisha nawe ukauliza. “Kwahiyo baada ya kupasua hiyo nazi huko njiapanda, itatubidi kukaa maeneo hayohayo kabla hatujarejea tena huku kwako mpaka atakapopatikana mtu wa kuiokota na kuila?”



    “Swali zuri, huku kwangu hamtakiwi kurudi tena. Ikitokea mmefanikiwa, mumshukuru Mungu na muelekee kwenu, sitahitaji malipo ya kazi hii kwa sababu nimeifanya kwa ajili ya shoga yangu. Na, ikitokea hamkufanikiwa, mkatafute mganga mwingine,” Nyahinga alifafanua, “pia suala la kumsubiri mtu atakayeokota nazi hiyo, ni la lazima ili muondoke mkijua kama kafara imekubalika, au sivyo. Juu ya hayo, hampaswi kumzuia wala kumwelekeza mtu yeyote kwenda kuokota nazi.”



    Siku ya Alkhamisi mkaimaliza nyumbani kwa Nyahinga, halikadhalika na Ijumaa. Hatimaye siku ya Jumamosi ikatimu, maandalizi yakafanyika. Mkanunua kondoo kama mlivyoagizwa, mkawa tayari kusubiri giza liingie mwende makaburini.



    “Tutakwenda watu watatu tu: Muga, mimi na msaidizi wangu,” Nyahinga alisema.

    Muda ulipotimu mkaondoka nyumbani, na kuelekea makaburini.



    __________



    KAMA kawaida, mazingira ya makaburini hasa katika nyakati za usiku, hutisha na kuogofya mno. Mliingia katika viwanja vya makaburi mkiwa watatu kama mlivyoondoka nyumbani. Nyote mlijifunga vipande vyeusi vya kaniki katika mtindo wa lubega.



    Baada ya nyimbo za kiganga kumalizika, Nyahinga na msaidizi wake wakamshika Kondoo, ukaamriwa umchinje kwa kukilengesha kichwa chake kwenye chungu cheusi kilichokuwa na dawa yake ili damu ichuruzikie humo. Ukafanya hivyo, na zoezi likakamiliza.



    “Haya, kunywa!” Nyahinga alikuamuru unywe ile damu ya kondoo iliyochanganyika na dawa kwenye chungu. Ukatii.

    Damu iliyobakia ilitumika kuchorea maandishi kwenye nazi utakayokwenda kuipasua njia panda kama ulivyoelekezwa awali.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hali ambayo haukuitegemea, mlikuta kaburi likiwa tayari limekwishachimbwa bila ya kumtambua mchimbaji; ukatakiwa umzike kondoo yule, ukafanya hivyo bila kusaidiwa na mtu yeyote.



    “Weka hicho chungu juu ya kaburi,” Nyahinga alikuelekeza.

    Ulipomaliza kukiweka, akasema: “Omba msamaha kwa ulichomtendea yule Ombaomba, kisha Muombe Mungu akunasue kwenye mkosi huu!”



    Wakati ukimalizia kufanya kama ulivyoelekezwa, ukashuhudia kile chungu kikizama chenyewe kaburini taratibu na kupotelea humo.



    “Dalili njema; tuondokeni, mwiko kugeuka nyuma!” Nyahinga alihitimisha, na papo hapo mkaanza kutoka nje ya uga wa makaburi. Ngwe ya kwanza ikakamilika bila ya rabsha zozote.



    Mama na nduguzo wakafurahi kukuona umerejea salama salmini. Mkaendelea kuwapo nyumbani kwa Nyahinga mpaka ilipotimu siku ya Jumatatu.



    “Kusanyeni noti mojamoja: ya shili miatano, ya elfu moja, ya elfu mbili, ya elfu tano na ya elfu kumi, kisha, endapo kama hiyo nazi itavunjika bila tabu hapo utakapokwenda kuipasua, ndipo na hizi pesa mtazitupa papo,” Nyahinga akakuelekezeni huku akikupeni nazi moja iliyochorwa maandishi kwa damu ya kondoo. “Kazi hii, mkaifanye saa kumi na moja jioni. Isiwe kabla wala baada ya hapo. Nakutakieni kila la kheri!”



    Baada ya kutoa shukrani na kuagana kwa kutakiana kila la kheri, mkafungasha kila kilicho chenu, mkaondoka na kurejea nyumbani kwako. Mkiwa huko, kichwani mwako ulijawa na mawazo lukuki, nduguzo walijaribu kukufariji, bi Mwanakatwe naye alijikita kwenye maombi kila mara.



    “Kwa sababu zoezi lililobakia ni dogo, hakuna tena sababu ya kuandamana pamoja kwenda kutafuta njia panda,” ulisema wakati mkijiandaa. “Mama na Shella ninyi mtatusubiri tu, nitakwenda na Kamugisha.” Ulihitimisha kwa sauti ya ushawishi na upole.



    Haikuwa rahisi kumshawishi bi Mwanakatwe akubali kukuacha uende peke yako, huku akiamini huenda hali yako ikabadilika ghafla ukiwa huko, na kuzuwa dhahma mbele ya kadamnasi. Ila kwa kushirikiana na na nduguzo, hatimaye akaafiki.

    Muda ulipoanza kujongea, mkatoka wewe na Kamugisha na kuingia kwenye gari yenu ndogo tayari kuianza safari … safari ya matumaini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maeneo hayo unayoishi wewe, ziko njia panda nyingi mno, lakini haukutaka kuzitumia hizo kwa kuogopa vijicho vya walimwengu wanaokufahamu. Mkaenda hadi mitaa ya Tabata ambako mlikutana na njia panda nyingi pia ambazo ungeweza kukidhi haja yako. Huko nako tatizo kubwa likawa ni wingi wa watu hasa kwa muda ule wa saa kumi na moja ambapo baadhi wanatoka makazini huku wengine wakiendelea kujitafutia riziki.



    Wakati mkiendelea kukimbizana na muda, kwa mbali ukaanza kuhisi maumivu mkononi, hofu ikakita moyoni mwako, mashaka ya zoezi yakaanza kukuandama.

    ***

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog