Search This Blog

MALAIKA? AU SHETANI? - 4

 





    Simulizi : Malaika? Au Shetani?

    Sehemu Ya Nne (4)



    “Uuh!” bi Mwanakatwe, aliyejifunga kipande cha kanga kiunoni, akatweta. Pembezoni mwako, Shella akajifuta jasho. Nyumba nzima ilikuwa kimya.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimemwona,” Nyahinga alisema.

    Nyote mkamgeukia.



    “Bora umemwona mwenyewe–hiyo ndiyo hali halisi ya mwanao,” bi Mwanakatwe akamjibu.



    “Sina maana hiyo,” Nyahinga akakazia. “Nimemwona huyo kiumbe anayemsumbua!”

    Nyote mkamakinika na taarifa hiyo.



    “Ulimfanya nini huyo kiumbe?” Nyahinga akakuhoji.

    “Sina kumbukumbu ya kumfanyia ubaya wowote mtu yeyote!” ukajibu.



    “Ndiye huyu mwenye nywele chafu na meno mabovu?” Nyahinga akakuuliza huku akiangalia kwenye kioo chake.

    Ili kutafuta ithibati ya mambo, Nyahinga akakusogelea na kukuonyesha mtu aonekanaye kwenye kioo.



    “MAMAAA!” Ukajikuta ukipiga kelele za uoga, baada ya kuiona sura ya yule Ombaomba kwenye kioo. “Ndiye huyo!”

    Akakirejesha kioo chake juu ya ungo, kkabaki mkitazamana.



    “Twende huku!” Nyahinga akasema huku akikushika mkono na kukuinua.



    Akakuingiza kwenye chumba kingine. Ni chumba chenye mwanga hafifu; michoro ya majiniwatu na viumbe wa ajabuajabu, mafuvu ya watu na wanyama, nk. Katikati ya chumba hicho kuna kitanda cha kamba; vile vitumikavyo kuoshea maiti.



    “Panda hapo kitandani!” Nyahinga akakuamuru.

    Nitapandaje ilhali miye si maiti? Ukajiuliza.



    Baada ya kijitafakari, ukaafiki kishingo upande. Ile kupanda tu na kujilaza kitandani hapo, Nyahinga akaanza kupiga ngoma zilizokuwamo humo chumbani, kwa nguvu huku akiimba. Mara ukaanza kuhisi kizunguzungu, mara macho mazito kuona, kisha kitu kama usingizi kikayazidia nguvu macho yako. Na hapo ikaanza kama ndoto kichwani…

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    __________



    MKIWA maeneo ya Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaa, wewe na sahibu yako, mlikutana na bwana mmoja, dhalili wa hali na dhaifu wa afya, akakusogeleeni kwa haraka na kukutakeni pesa. Taashira ya ufukara ilijishajihisha maungoni na mavazini mwake.



    Pengine kutokana na kuchoshwa na wimbi la Ombaomba maeneo yako ya kazi, ukampuuza fakiri yule. Walakini, bila kutegemea, rafiki yako akatoa noti ya shilingi elfu kumi, na kumpa.



    “Wewe, pesa yote hiyo unampa ya nini?” ukamzuia rafiki yako.



    “Ah, mwache tu. Inaonekana ana hali ngumu sana!”



    “Utaweza kusaidia Ombaomba wa mji wote?” ukahoji, “Kungejua mpaka kufika jioni huwa wamekusanya pesa nyingi mno hawa, kuliko hata wewe mfanyabiashara, wala usingetaabika nao.”



    Ukiwa umemzuia rafiki yako, ukatoa sarafu ya shilingi mia mbili na kumpa huyo Ombaomba badala ya ile elfu kumi.

    Kwa ghadhabu na uchungu, Ombaomba akatoa msonyo mrefu, huku akikukata jicho la hamaki.



    Hukujali. Zaidi, ukamkaripia, “Unachagua pesa? Katafute za kwako!” ukamgeukia rafiki yako na kumwambia, “Tuondoke zetu!”



    Mkaondoka na kumwacha Ombaomba akiendelea kukutazama kwa chuki na hasira. Kila ulipogeuka nyuma, ulimwona Ombaomba akiwa vilevile, amesimama palepale, bila kutikisika –akikutazameni. Hakuondoka pale, hadi mlipofika mbali zaidi ya upeo wa macho yenu kumwona.



    Hukuwa na na mashaka wala tafakuri juu yake, kwa kutambua Ombaomba kama yule hano lo lote la kukufanya.



    Siku nyingine, ikiwa imekatika miezi kadhaa tangu ulipomtindikia riziki yule Ombaomba, ukiwa unatokea kazini kwako majira ya saa kumi na mbili jioni kwa miguu, ndipo ukakutana tena na Ombaomba yuleyule, akiwa amesimama maeneo ya ilala…! Kumbukumbu ziligoma kurejesha mkanda wa tukio la awali lililokukutanisha naye kwa mara ya kwanza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    __________



    GHAFLA, ukashituka usingini, ukatoka kitandani huku ukitweta na kutaka kukimbia. Kumbukumbu ya mkasa wa namna ulivyokutana na yule Ombaomba vilijidhihirisha ndotoni, ukiwa kitandani kwa mganga.



    Nyahinga akakushika mkono, kisha mkatoka nje na kujumuika na ahli yako, wamejiinamia. Baada ya kuketi, Nyahinga alisema, “Haya, tayari Muga amekwisha kumkumbuka mtu wake.”



    Wote wakakutazama kwa mshangao. Nyahinga akamalizia, “Sasa, tueleze hatua kwa hatua, namna ulivyokutana na mtu yule.”



    Bado ulikuwa ukistaajabia ufundi wa Nyahinga kuweza kukurejesha kumbukumbu za matukio yaliyopita, kwa kukulaza juu ya kitanda cha kuoshea maiti, na kukupigia ngoma za kiganga. Bila kufanya ajizi wala zohali, taratibu ukaanza kusimulia kuanzia 'alif mpaka yee'.



    Pamoja na kujaribu kuonesha namna ambavyo hukudhamiria uadui na Ombaomba yule, lakini kwa simulizi ile, ulistahiki kulaumiwa kwa kitendo cha dharau, choyo na jeuri uliyomwoneshea, tena kwa pesa isiyo ya kwako.



    Baada ya ukimya kutuama kufuatia kuhitimika kwa simulizi ya mkasa wako, Nyahinga akaendelea, “Tuna kibarua kigumu cha kumtambua kiumbe huyo–maana bila ya kutambua tunapambana na nani, itakuwa kazi ya bure bileshi. Kiumbe hicho, kilichojivika umbile la kibinaadamu, hakioneshi asili yake; si mtu, si jinni, si mzimu.”



    “Sasa, kama kiumbe hicho si katika jamii ya wanaadamu, majini wala mizimu–kumbe ni nini hasa?” Kamugisha akahoji.



    “Ndiyo nikasema, hilo liko nje ya uwezo wetu; yawezekana ni Shetani au hata Malaika, maana hao ndiyo viumbe wasiokamatwa na ramli za kiganga wala kichawi. Kama ni shetani, basi tutapambana yae kwa msaada wa Mungu; na endapo kama ni Malaika, hilo tutamwachia Mungu mwenyewe kwani ndiye huwatuma Malaika wake kwa lile alitakalo yeye!” Nyahinga akajibu kwa unyonge na kukata tamaa.



    Baada ya mjadala, tiba zikaendelea kwa wastani, hadi ulipotimu muda wa chakula cha mchana. Mkajumuika kupata chakula, na baada ya chakula tu, Nyahinga akakuelezeni, “Hapa, inatakiwa tutoe kafara.”



    “Kafara ya nini?” bi Mwanakatwe akahoji.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwanza, tutaandaa sadaka ya chakula kwa watoto na wasiojiweza. Kisha, tutatupa sadaka ya pesa kwa watoto pekee. Watoto ni wasafi tamthili ya Malaika, kwa hivyo, kwa kuwatumia wao kama ngao yetu ya kuombea msamaha, asaa tukasamehewa. Na ikawa mwisho wa dhila hii kwa Muga.”



    “Tawire,” bi Mwanakatwe alijibu.



    “Jumamosi ndiyo siku nzuri kufanya kafara hilo. Tutahitaji kumwaga damu ya mnyama, na mnyama mwenyewe ni vyema akawa Kondoo kwa sababu ya upole na ukimya wake, huenda ikawa sababu ya kulituliza baa hili. Kimsingi, hatuna uwezo wala sababu ya kupambana na kiumbe hicho cha ajabu, tutapaswa tu kukiomba msamaha. Tutakwenda makaburini usiku, bila kujali kama hali ya Muga itakuwa imebadilika na kuwa mbaya au laa, huko makaburi, tutamchinja kondoo huyo na kisha tutamzika kwenye kaburi.”



    “Baada ya kafara hiyo ya makaburini, siku ya Jumatatu ndipo tutakapotoa sadaka ya chakula, kisha mtakwenda njia panda, kupasua nazi na kutupa sadaka ya pesa!”



    “Bora salama tu fundi,” bi Mwanakatwe alisema.



    “Nasikitika kukuambieni jambo moja,” Nyahinga akaanza tena. “Maelekezo niliyopewa na mizimu ni kwamba, kwanza ni lazima nazi hiyo ipasuke kwa pigo moja tu, hakuna kurudiarudia, hivyo, mpasuaji ambaye ni Muga mwenyewe, atapaswa kutumia nguvu kwa kuielekeza nazi kwenye kitu kigumu kama vile jiwe. Nazi ikishapasuka, ni lazima mtu aiokote na kuila–na mwokotaji wa kwanza, atatakiwa awe ni wa jinsi ya kiume.”



    “Mnh, nani huyo atakayeokota nazi na kuila?” Shella aliuliza.



    “Mbona wako wengi tu; kuna watoto wasiojua lolote, kuna wehu wasio na akili timamu, na wako hata walimwengu wenye dhiki kali. Hayo yakifanyika kikamilifu, maana yake kafara itakuwa imekubalika na kuanzia hapo, Muga atakuwa amepona. Lakini, endapo kama nazi haitovunjika, au ikavunjika halafu mtu wa kwanza kuiokota akawa ni wa jinsi ya kike, basi mjue kafara imeshindikana, na mzimu wangu hautokuwa na uwezo tena wa kupambana!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog