Search This Blog

VITA YA WACHAWI - 4

 





    Simulizi : Vita Ya Wachawi

    Sehemu Ya Nne (4)





    ILIPOISHIA:

    Alirudiwa na fahamu baada ya tukio kutulia, alipoombwa kwenda kwenye kaburi akaangalie kumetokea nini alikataa kwa kuhofia maisha yake. Ilionekana uchawi uliotumika pale ulikuwa mkubwa kuliko uwezo wa nguvu zake za kiganga.

    Mzee Andendekisye na mkewe walipagawa na kumshtumu moja kwa moja kwa sauti kuwa Amangise baba wa Ambakisye ndiye aliyefanya vile na kuapa kula naye sahani moja. Alijikuta akisema kwa sauti na kujisahau yupo mbele za watu.

    “Wewe si umefanya hivi basi moto utakuwakia, nimeanza na mtoto sasa nafagia ukoo mzima.”

    SASA ENDELEA...



    Kauli ile ilifanya watu wote makaburini wagune na kuanza kunong’ona chinichini kuonesha kumbe yeye ndiye muhusika wa kifo cha Ambakisye mpenzi wa mwanaye. Walijiuliza alifanya vile ili iweje na kujiuliza kama aliyefanya yake makaburini ni Amangise amefanya kwa faida gani. Wapo waliojiuliza anajiamini nini kusema hadharani yeye ndiye kamuua Ambakisye.

    Kwa vile ndani ya kaburi hakukuwa na kitu zaidi ya jeneza lililoloa damu walishindwa kuzika. Baadhi ya watu waliamua kutoka makaburini kukiwa na sintofahamu huku mzee Andendekisye na mkewe wakisema hawatoki makaburini mpaka wamuone mtoto wao.

    Wazee wa kijiji ilibidi waitane pembeni ili kutatua tatizo lile, mmoja alitoa wazo wamfuate mtaalamu kijiji cha Mbako kabla giza halijaingia ili wajue hatima ya mwili wa Atuganile ni nini kwani ilikuwa wiki ya miujiza. Walitumwa vijana na baiskeli kwenda kijiji cha Mbako kumfuata mtaalam.

    Kukiwa na sintofahamu baadhi ya watu waliotoka makaburini mtu wa karibu na Amangise walikwenda kumwambia maneno aliyosema Andendekisye makaburini baada ya tukio la kushangaza na kutisha katika kaburi la Atuganile. Baada ya kumsikiliza alisema kwa masikitiko.

    “Hivi mimi nimuue Atuganile ili iweje?”

    “Basi mwenzako anatamba kamuanza mtoto, sasa anahamishia majeshi kwenu na atahakikisha unaufagia ukoo mzima.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unasema watu wote msibani wamesikia?”

    “Ndiyo, yaani namshangaa sana jamaa yule kujisifia kwamba kamuua Ambakisye kwa vile wewe ulimuua mwanaye na pia wewe ndiye uliyetuma mamba kumla mwanaye makaburini.”

    “Kwa kweli Mungu ndiye anayejua kama mimi ndiye niliyetia mkono kumuua Atuganile atanihukumu. Ni kweli mwanangu nilimtafutia mchumba baada ya siku moja kwenda Kilasilo na kumuona mtoto wa Ambokile, Bupe.

    “Kwa kweli binti wa Ambokile alinivutia kwa heshima aliyonionesha na kupenda awe mkwe wangu. Nilizungumza na wazazi wake wakanikubalia na kuanza mipango ya kuoa mara moja. Ni kweli nilikuwa najua mwanangu ana uhusiano na mtoto wa Andendekisye lakini hakuna hata siku moja mwanangu alinieleza kuwa anataka kumuoa.

    “Tumeona watoto wangapi wanaanzisha uhusiano na baadaye kila mtu kufanya mambo yake. Kama mzazi niliamini nilitakiwa kumtafutia mwanangu mke bora hasa kwa historia ya familia yake na yeye mwenyewe. Bupe alikuwa binti ambaye kila mmoja anamsifia kama mzazi unataka nini kama una mtoto wa kiume si kumtafutia amuoe.”

    ‘Ni kweli.”

    “Basi nilianza maandalizi na kupeleka posa kisha nilimbeba mwanangu kwenda Kilasilo kuonana na mchumba wake. Ni kweli mwanangu alishtuka kusikia nimemtafuta mwanamke mwingine wakati ana mpenzi wake. Nilimweleza sikuwa na lawama kwa vile sikuona malengo yao.

    “Kibaya zaidi wakati huo Atuganile alikuwa na ujauzito ambao baadaye kwa bahati mbaya ulitoka. Hapo ndipo wenzetu wakasema tumeutoa na kuanzisha vita ya kishirikina iliyopelekea kumuua mwanangu bila kosa,” mzee Amangise alijitetea kwa uongo wenye ukweli kidogo.

    “Sasa ndugu yangu akumulikae mchana usiku anakuchoma, kama ulikuwa hujui basi kamuanza mwanao sasa mnafuata wenyewe. Kwa hiyo liwahi neno kabla halijadondoka chini.”

    “Itabidi niondoke baada ya mazishi ya mwanangu ili niwawahi kabla hajaniwahi.”

    “Wewe Amangise, uzembe wako ndiyo uliofanya umpoteze mwanao. Mwenzio kajipanga wewe unafanya mchezo. Sasa tegemea kumpoteza mkeo kisha wewe mwenyewe,” Amangise alipewa tahadhari.

    “Sasa nitafanyaje wakati unajua siwezi kutoka kabla ya mazishi ya mwanangu, unafikiri watu si wataamini maneno ya Andendekisye kuwa mimi mwanga na pengine mkewe au yeye afe jamii itanielewa vipi ikiwa tayari kanipaka kinyesi masikioni kwa watu kuwa nimemuua mwanaye.”

    “Kwani unataka kwenda wapi?”

    “Kalonga.”

    “Huko si Malawi?”

    “Ndiyo kuna rafiki yangu mtaalam wa mambo haya.”

    “Unajua ninyi ndiyo mnaofanya kuonekane Tanzania hakuna watu wa kuweza kuwadhibiti watu kama hawa mpaka Malawi, kila mtu utamsikia amevuka mipaka wakati humuhumu ndani kuna watu wakali kuliko hao mnaowafungia safari.”

    “Wengi watu wa hapa wanatibu hawawezi kulipua mabomu.”

    “Kweli umechanganyikiwa, nani alimrudisha mtoto wa Mwakasege.”

    “Ooh! Nilimsahau yule kijana.”

    “Basi yule kijana kazi yake ni kulinda na kutega bomu mtu akitaka kukufanyia kitu kibaya linamlipukia.”

    “Mi sitaki la kujilinda tu bali kulipa kisasi kwa kifo cha mwanangu kwa vile sihusiki chochote kwenye kifo cha mtu.”

    “Hiyo vita lazima akirudisha linakupata, siku zote kilio cha kuonewa husikilizwa kuliko kujilinda mwenyewe.”

    “Jirani moyo haunipi kujikinga tu kwani nitakuwa nimemuogopa wakati kaniulia mwanangu bila kosa.”

    “Nataka kukueleza kitu dawa ya huyo kijana ni zaidi ya kuloga, kwa vile ameahidi kufyeka familia yako. Ukishajizindika akija kukumaliza anajimaliza mwenyewe hata watu wakienda kwa waganga kuangalia atakuwa amejimaliza mwenyewe.”

    “Una uhakika moto utamuwakia?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nina imani jamaa nilivyo mjua lazima usiku wa leo atasafiri kwa vile kabla ya mazishi ya mwanaye alisafiri na inaonekana majibu ni kifo cha mwanao.”

    “Basi nipeleke.”

    “Nitakupeleka, yaani jamaa sijui anajiamini nini kwa kusema kuwa kamuua Ambakisye?” jirani wa Amangise alisema kwa masikitiko.

    “Anajivunia uchawi wake, aliua nguvu za kiume za mwanangu eti kwa vile anataka kuoa mwanamke mwingine tofauti na mwanaye.”

    “Wewee!” jirani alishtuka.

    “Yaani nimemvumilia vya kutosha sasa too much.”

    “Sikiliza jirani usimfanye lolote wewe twende huko jibu utaniambia.”

    “Nitafanya hivyo japo nilitaka tupambane kwa uchawi tuone nani zaidi.”

    Majira ya saa mbili usiku Amangise aliondoka msibani na kuwaacha watu wakiombeleza na kupanda baiskeli kuelekea kijiji cha jirani ambako alikuwepo mganga kijana ambaye hakuwa mwenyeji wa mkoa ule. Walikwenda kwa saa moja mpaka kwenye kijiji hicho.

    Bahati nzuri walikuta mganga amerudi jioni ya siku ile toka Mbeya mjini alipokwenda kufanya kazi zake. Walipofika aliwapokea na kuwasikiliza shida zao. Jirani wa Amangise ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu na kueleza kilichowapeleka pale.Mganga alikuwa kijana mdogo sana, baada ya kuangalia rada zake alitikisa kichwa na kusema:







    "Hii ni vita kubwa tena kubwa sana ambayo msipotumia busara hakuna atakayebaki, uchawi unaotumika ni mkubwa sana bila sababu ya msingi. Vijana wenu mmewaua bila sababu na kama mngewasikiliza, yote haya yasingetokea. Adui yako anaamini wewe ndiye mhusika kwa vile kuna kitu ulimtendea mwanaye kabla. Lakini kifo cha mwanaye mhusika ni mwingine kabisa.

    "Kifo cha mpenzi wa mwanao na yule bibi ni lipizo toka kule ulipotaka kuoa ambao hawakukubali kumpoteza mtoto wao ambaye unajua kifo chake kilivyokuwa, walihangaika na kujua aliyemuua ni nani walipomjua na walirudishia majibu."

    "Unataka kuniambia aliyemuua mchumba wa mwanangu ni bibi Tumwambilile na Atuganile?" Amangise aliuliza kwa mshangao.

    "Ndiyo waliohusika lakini sababu kubwa ni wewe, kwani alifanya vile ili aolewe na mwanao, msaada mkubwa alifanya yule bibi aliyekuwa mzoefu wa kazi ile."

    "Mmh!" Amangise na jirani yake waliguna kusikia taarifa ile.

    "Baada ya kufanikiwa kumuua yule binti, mazingira ya kifo chake yalifanya familia ihangaike na kuvuka mipaka. Baada ya kumjua mbaya wao, nao walirudisha mashambulizi. Kombora lililotumwa liliwafikia wakusudiwa tu, lakini mzazi wa mchumba wako alitumia hasira bila kuchunguza na kumuua mwanao bila kosa lolote. Bado dhamira yake ni mbaya sana kwako kuhakikisha anaifuta familia yako na usiku huu ana safari ya mbali ambayo akirudi anataka akute matanga kama alivyofanya kwa mwanao."

    "Duh!" Amangise na jirani yake walishika midomo.

    "Kuna kitu kimoja kimetokea leo makaburini cha mamba kutokea ndani ya jeneza na jana siafu, maji na nyoka kwenye kaburi la bibi Tumwambilile, vitu vile vinamaanisha nini?" Jirani wa Amangise aliuliza.

    "Ule ni uchawi uliotumika kumuua yule binti aliyetaka kuolewa na mwanao, yale ni majibu ya uchawi wao."

    "Mbona kuna mganga alisema wazike hakuna kitu, wakati mwanzo katika kaburi la kwanza tuliona nyoka, la pili tuliona maji na la tatu siafu?"

    "Alisema tu lakini kwa tabia za yule bibi za kichawi vyote mlivyoviona ndivyo alivyozikwa navyo. Kaburi lake amezikwa na maji, nyoka na siafu si rahisi kwa macho ya kawaida kuona."

    "Mmh!" waliguna tena kwa pamoja.

    "Na tukio la leo la mamba ni kweli mamba alitokea lakini hakumla mtu kama mlivyoona, ila amechukua baadhi ya viungo kama sehemu za siri na ulimi tu."

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mungu wangu!" walisema huku wakishika vichwa.

    "Hilo ndilo kosa alilolifanya mwenzako, baada ya kifo cha mwanaye japo alijua wewe ni adui yake angefanya uchunguzi kabla ya kuchukua uamuzi mzito wa kutoa roho ya mwanao."

    "Sasa mzee wangu tulikuwa tunataka msaada wako," alisema jirani.

    "Msaada gani? Kama vita mi siwezi kwa vile nitachukuliwa muda wa kupigana na watu nisio na ugomvi nao. Siku zote vita ya kisasi haina mshindi, kila atakayepigwa atataka kurudisha."

    "Sasa wewe utatusaidia vipi?"

    "Msaada wangu mkubwa ni kumlinda mzee na mkewe ili baya lolote watakalotupiwa lisiwapate na kila mwenye dhamira mbaya basi imrudie mwenyewe." "Hata huo msaada mkubwa sana kwani jirani yangu amenisihi nisilipe kisasi hata marehemu mwanangu alinieleza kitu hicho kabla ya kufa," alisema Amangise.

    "Ni kweli, kwa vile adui yako anajiamini sana kishirikina, wewe jikinge, majibu utakuja kuniambia."

    "Sawa."

    "Sasa unatakiwa upatiwe kinga na mkeo kwa vile mbaya wenu inaonekana yupo safarini, dhamira yake akirudi asikie matanga kama alivyosikia kwenye msiba wa mwanao."

    "Sasa utatusaidiaje nasi tupo msibani hatuwezi kuondoka wote?" Amangise aliuliza.

    "Hakuna tatizo, nitakwenda kuifanyia kazi yangu hapohapo kwenu."

    "Pia vipi kuhusu mazishi, hakutakuwa na mauzauza kama yaliyotangulia?" jirani wa Amangise aliuliza.

    "Hayawezi kuwepo kwa vile marehemu hakujihusisha na uchawi kama wenzake, atazikwa kawaida tu."

    Walimchukua mganga mpaka Ibungu na kumpeleka msibani kama watu wengine, kwa vile kulikuwa na hali ya sintofahamu ilijitokeza. Mganga aliomba kufanya kazi yake kutokana na mambo yanayotokea pale kijijini ili kuweka mambo sawa. Alipewa nafasi na kufanya mambo yake sehemu yote kisha aliwafanyia zindiko Amangise na mkewe na kuondoka usiku uleule.

    ***

    Upande wa pili, Mganga toka Mbako alifika Ibungu saa moja na nusu usiku na kwenda makaburini huku baadhi ya watu wenye mioyo migumu wakielekea eneo la makaburini. Mganga alipofika eneo la makaburini alifanya dawa zake na kumwagia kaburini huku akizungumza anayoyajua kisha aliuliza.

    "Kuna la ziada?"

    "Shida yetu kujua hali iliyojitokeza kama tulivyokueleza," mzee mmoja alimweleza mganga.

    "Nimemaliza kazi mliyoniletea, vipi mnaweza kuzika usiku huu au kesho?"

    "Kuzika nini?" mzee Andendekisye aliuliza.

    "Mwili wa binti yako umo kwenye jeneza kama kawaida ila hauna baadhi ya viungo."

    "Huo mwili upo wapi?"

    "Ndani ya kaburi, kama kuna watu wenye nguvu waingie ndani kulitoa jeneza nje."

    Vijana walikuwepo pale waliogopa kuingia ndani ya kaburi, lakini mganga alitangulia kuingia ndani ya kaburi. Vijana baada ya kumuona mganga ameingia nao waliingia ndani na kushangaa kukuta jeneza lipo kama lilivyowekwa kaburini halikuwa limepasuka.

    Walilibeba jeneza kulitoa nje, wakati wanalibeba jeneza lilikuwa na uzito wa mtu kuwemo ndani lakini kwa chini kulikuwa na damu iliyokuwa ikidondoka kutoka ndani ya jeneza. Walilitoa nje ya kaburi na kuliweka pembeni na kusubiri kauli ya mganga yaliyekuwa amesimama pembeni na usinga wake.

    Aliomba jeneza lifunguliwe, vijana walilifungua na kuutoa mwili wa Atuganile na kuulaza chini.

    Walielezwa wauchunguze kama kweli ni yeye, walitazama kila kona na kukubali ni wenyewe lakini sehemu za siri na mdomoni kulikuwa na damu. Mganga aliwaeleza mwili wa marehemu umetolewa viongo sehemu za siri na ulimi vilikuwa vimechukuliwa.

    Mzee Andendekisye aliuliza kama vinaweza kupatikana, mganga alimwambia kupatikana vigumu kwa vile vimepelekwa mbali. Pia mwili ule ulitakiwa kuzikwa usiku uleule kwa vile ungelala ungeharibika na kushindwa kuuzika.

    "Kwa hiyo tutafanyaje?"

    "Mzikeni na mazishi yake yasilale."

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/





    IlibidI Atuganile azikwe usiku uleule na watu wachache kwa maelezo ya mganga, baada ya mazishi mzee Andendekisye alipanga usiku uleule asafiri na mkewe kurudi Malawi kwa mganga wake ili akamalizia kazi iliyobakia na kuifyeka familia ya Amangise. Ili kupata nafasi ya kuweza kuondoka usiku ule alitangaza hakuna matanga.

    Watu walitawanyikia msibani na yeye na mkewe na baadhi ya majirani zake walirudi nyumbani. Lakini baada ya kufika nyumbani waliwaeleza majirani kuwa hawatalala pale, kwa vile walikuwa wamejiandaa walipanda baiskeli na kuwaacha majirani wakirudi majumbani kwao wakiwa wamepigwa na mshangao juu ya mambo ya jirani yao.

    Mmoja alisema huenda anakwenda kuyafanya aliyoahidi makaburini kuufuta ukoo wa Amangise. Wapo waliosema kuwa kifo cha Ambakisye kilitokea baada ya kusafiri na kuuacha mwili wa mwanaye ndani na aliporudi majibu yalipatikana kwa kumuangusha kijana mbichi.

    Walijiuliza mwisho wao nini katika vita ile ambayo ilionesha imetawaliwa na uchawi. Wazee wa kijiji walipanga baada ya mazishi ya mtoto wa Amangise waitishe kikao ili kuyaweka mambo yale sawa kwani picha iliyokuwa ikijionesha ilikuwa na mwisho mbaya.

    Walipotoka kwa Andendekisye walikwenda kwenye msiba wa Ambakisye ambako nako walikuta mtaalamu akifanya mambo yake na kuzidi kuamini kijiji kinapokwenda kina hatari ya kuharibu jamii iliyowazunguka hasa kutokana na heshima ya wazee wale kijijini pale.

    Lakini hawakusema kitu waliungana na majirani wengine kwenye msiba.

    Wengi walikuwa na wasiwasi huenda na Amangise naye ataondoka usiku ule, lakini haikuwa hivyo baada ya mtaalamu kufanya mambo yake aliondoka na kuacha watu msibani kama kawaida.

    Kwa vile usiku ule wazee wote walikuwepo msibani pale, Amangise alitumia nafasi ile kuzungumza nao kuhusu kinachoendelea kijijini na kauli za jirani yake juu yake na vitisho alivyovitoa kwa familia yake. Baada ya kuwapatia pombe, alisimama na kuzungumza na kufanya wote waelekeze masikio kwake.

    “Wazee wenzangu na majirani, nina imani kipindi kifupi kumetokea mshtuko kijijini kwetu cha vifo vya watu watatu kwa mpigo, bibi yetu Tumwambilile, mkwe wangu Atuganile na mwanangu Ambakisye. Kwa kweli vifo vyote hivyo vimetingisha Ibungu na vijiji vya jirani kutokana na mazingira yake.

    “Na baada ya vifo hivyo kumetokea vitu vya kushangaza kwenye mazishi ya Atuganile na bibi Tumwambilile. Japo mimi sikuwepo kutokana na msiba wa mwanangu.

    Nimesikia maneno mengi ya mzazi mwenzangu Andendekisye juu ya kifo cha mwanaye kuwa mimi ndiye niliyemuua pia ametoa maneno mazito kuwa ndiye mhusika wa kifo cha mwanangu ikiwa kulipa kisasi na pia atahamia kwetu. Nimefikiria mengi kuhusiana na kauli ya kuniua mimi na mke wangu.

    “Wazee wenzangu naapa tena mbele yenu katika usiku huu kama mimi nilitia mkono kwenye vifo vyote basi Mungu anihukumu nife sasa hivi. Ni kweli tulikuwa na ugomvi wa chinichini kutokana na mimi kumtafutia mke wa kuoa mwanangu wakati tayari walikuwa na uhusiano na mwanaye.

    “Kweli ile ilileta mpasuko mkubwa, nakumbuka majuzi mwanangu alikuja na kunieleza tukae chini kumaliza tofauti zetu na kama nisingemsikiliza angeondoka nyumbani. Japokuwa nilikuwa na hasira kwa kitu alichomfanyia mwanangu za kumuua nguvu za kiume ili asioe.

    “Nilikubali na kuwa tayari kumrudisha mwanangu Ambakisye kwa mpenzi wake Atuganile, nilikubali kukutana na familia ya Andendekisye ili tumalize tofauti zetu ili wanetu waoane.”

    “Samahani mzee mwenzetu, ulisema ulimtafutia mwanao mke Kilasilo, kwa hiyo angeoa wanawake wawili?” mzee mmoja aliuliza baada ya kushindwa kumuelewa.

    “Nilisahau kuwaeleza habari za mchumba wa mwanangu wa Kilasilo, wakati tunajiandaa kupanga tarehe ya harusi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuchukuliwa na mamba wa kimuujiza.

    “Alipatikana baada ya siku mbili akiwa amekufa, hapo niliona ni muda muafaka wa kumsikiliza mwanangu. Lakini upande wa pili bado walikuwa na hasira na sisi. Baada ya kukubaliana na mwanangu tukae chini tumalize tatizo, siwezi kuelezea jinsi nilivyopata mshtuko baada ya kuelezwa kuwa Atuganile amefariki.

    “Lakini niliumizwa nilipoelezewa kuwa mimi ndiye niliyemuua Atuganile pamoja na bibi Tumwambilile. Kwa kweli iliniuma sana hasa kutokana na hatua niliyofikia na mwanangu. Siku iliyofuata kulikuwa na mazishi ya mchumba wa mwanangu Kilasilo ambapo ilitubidi twende tukazike ili tuwahi mazishi ya Atuganile na bibi jioni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Lakini tukiwa njiani mwanangu alianza kulalamika kichwa na kufanya tusimame, baada ya hapo aliendelea kulalamika kichwa huku akikishika na kusema kinataka kupasuka. Ghafla alianguka chini na kuanza kuzungumza kwa shida na kuniambia anakufa.

    “Ila aliniomba kama atakufa basi nisilipe kisasi, nina imani alijua aliyefanya vile ni Andendekisye kwa vile mwanzo alimuua nguvu za kiume. Ghafla sauti ilipotea na kuanza kutokwa damu puani, mdomoni, masikioni, machoni na kufariki mikononi mwangu,” alipofika hapo sauti ilibadilika na kuzungumza kwa huzuni na kufuta machozi ya uchungu na kuondoa kamasi nyembamba.

    “Wazee wenzangu kwa kweli nimeumizwa sana tena sana na kifo cha mwanangu halafu kuna mtu anajisifu ndiye kamuua, kwa kosa gani au uhakika gani kama mimi nimemuua mwanaye. Nami kusema ukweli wa Mungu nilichokipanga kukifanya kwa Andendekisye wala nisingemvukia boda kutafuta wachawi ningekwenda kumchinja kama kuku nyumbani kwake kwa mkono.

    “Lakini niliheshimu usia wa marehemu mwanangu, nimeamua kumuachia Mungu najua majibu yake yatapatikana hapahapa duniani. Najua wapo wengi wana maswali juu ya mtaalamu aliyekuja hapa. Lazima niseme ukweli mwenzangu katangaza vita na tayari kanichukulia jicho langu, lazima na mimi nijihami lakini si kwa kulipa kisasi bali kujikinga na mashambulizi ya adui yangu.”

    “Mi nafikiri suala hili tunatakiwa kulizungumza kwa kuwakutanisha ili tumalize uadui kwa vile hali inayokuja mbele ni mbaya sana,“ alisema mzee John.

    “Ni kweli, suala hili hatutakiwi kulifumbia macho kwa vile wote watu wetu hatuwezi kuona mnaumizana tunawatazama,” mwingine alichangia.

    “Amangise upo tayari kukutana na mwenzako tuyazungumze?”

    “Nipo tayari hata usiku huu ili kesho tukiamka tuanze upya japo kaniulia mwanangu.”

    “Mzee Mwakyoma unaweza kwenda kwa Andendekisye kuzungumza naye ili tulizungumze?”

    “Nipo tayari, lakini baada ya mazishi Andendekisye na mkewe wameondoka nyumbani kwao na hawakutueleza wanakwenda wapi lakini amesema hakuna matanga na kutufanya wote tuliokuwa msibani kuondoka.”







    “Mmh! Sasa atakuwa amekwenda wapi usiku huu baada ya mazishi?”

    “Labda ndiyo amekwenda kuufuta ukoo wangu,” Amangise alisema.

    “Basi tumsubiri arudi tuyazungumze.”

    “Mtazungumza na nani kama amesafiri na akirudi atakuta mimi na mke wangu tumegeuka mizoga.”

    “Kivipi?”

    “Si aliondoka baada ya kifo cha mwanaye na aliporudi kakuta mwanangu kawa mzoga.”

    “Huenda alisema kwa hasira tu, sidhani kama kuondoka kwake kaenda kufanya hivyo.”

    “Mmh! Sawa, kama hakwenda uko atatukuta tutayazungumza nipo tayari hata aletwe mtaalam aseme ukweli wa vifo vyote na kama mimi nahusika nipo tayari kufa. Lakini kama amekwenda na mengine msiache kunizika na mke wangu nina imani tutakufa wote.”

    “Amangise nina imani Mungu atawalinda.”

    “Ndugu zangu kuyasema haya usiku huu nilitaka kuliweka jambo hili wazi mbele yenu hata kama atakuja leo nitalisema haya mbele yake bila kuacha hata moja,” Amangise alisisitiza kauli yake.

    “Tumekusikia mzee mwenzetu, kila kitu tutakifanyia kazi nina imani amani itarudi mioyoni mwenu.”

    “Kwangu nimekubali kumpoteza mwanangu tena kwa uhakika wa mdomo wake, lakini ajue amenionea kifo cha mwanaye sihusiki lolote. “

    “Tumekuelewa.”

    Kwa vile muda ulikuwa umekwenda baada ya chakula cha usiku, walikubaliana kuzike kesho yake saa saba mchana. Wapo waliolala msibani na wengine alirudi majumbani ili kujipanga kwa mazishi ya siku ya pili.

    ***

    Andendekise na mkewe waliondoka usiku ule na kufika mpakani saa tano na nusu za usiku. Kama kawaida aliweka sehemu baikeli yake na kuvuka upande wa pili wa nchi ya Malawi ambako alipanda gari mpaka Matipa kwa mtaalamu wake. Alikuta hajalala kwa vile usiku ule alikuwa na kazi ya mteja mmoja naye kutoka Tanzania.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofika alibidi asubiri mpaka saa kumi za usiku ndipo walipokutana na mganga ambaye kwanza alitaka kupata jibu la kazi aliyoifanya.

    “Vipi za huko?”

    “Mmh! Ni matatizo makubwa.”

    Alimuhadithia kilichotokea makaburini siku ya kumzika mwanaye.

    “Kama ningejua tungeondoka pamoja, hao washenzi ningewafanya kitu kibaya ambacho hakijawahi kuonekana duniani kote. Ila nitawakomesha waliofanya hivyo, nataka kila mtu akuone kama moto, hakuna wa kukusogelea wala kukugusa.”

    “Nitafurahi sana.”

    “Vipi kazi yangu?”

    “Imekwenda kama ulivyosema, mtu kaanguka.”

    “Umeamini mimi si mtu wa maneno bali vitendo?”

    “Nimekuamini unatisha ila utatisha zaidi kama utammaliza na yule jamaa.”

    “Hakuna tatizo kwangu hiyo kazi ndogo sawa na kunusa na kutoa chafya.”

    “Fanya mambo, nataka nikirudi kesho nikute matuta mawili.”

    “Hilo limefanikiwa omba jingine.”

    “Kama vyote ulivyonifanyia nina imani hiki ni muhimu kuliko vyote.”

    “Kipo, nilitee beseni na maji nusu na kisu kikubwa,” mganga alimwita msaidizi wake.

    Baada ya muda Kipo alileta beseni lenye maji nusu na kisu cha kuchinjia mbuzi na kuviweka pembeni ya mganga aliyekuwa akichukua dawa kwenye vikopo huku akisema:

    “Kipo weka hapo nataka kuwaonesha Watanzania kwamba sisi ndiyo wajukuu wa wachawi tuliorithisha sio wao wa kununua.”

    Aliliweka beseni katikati ya Andendekisye na mkewe na kuwauliza:

    “Ndani ya beseni hili mnaona nini?”

    “Hamna kitu,” walijibu pamoja.

    “Mmh! Jamani hata maji hamyaoni?”

    “Maji tumeyaona tulidhania kitu kingine.”

    “Zaidi ya maji kuna nini?”

    “Hakuna kitu.”

    “Angalieni vizuri.”

    “Hakuna kitu.”

    Baada ya kusema vile mganga alichukua kitambaa chekundu na kufunika juu ya beseni kisha alimimina dawa ya maji juu ya kitambaa na kusema maneno ya Kinyasa na kuchukua dawa ya unga na kunyunyiza juu ya kitambaa na kuuliza.

    “Mbaya wako anaitwa nani?”

    “Andendekise.”

    “Na mkewe?”

    “Tuntufye.”

    Baada ya kutajiwa majina yale aliyarudia huku akinyunyiza dawa ya unga juu ya kitambaa. Alichukua kibuyu kidogo na kukizungusha kwenye beseni huku akiendelea kusema maneno yake. Baada ya muda walisikia ndani ya beseni kama kuna vitu vinacheza. Mganga aliacha kuzungusha kibuyu na kusema:

    “Nina imani mambo yamekwenda vizuri mnaweza kufunua.”

    “Afunue nani?” Andendekise aliuliza.

    “Wewe mwanaume ambaye ndiye utakayeifanya kazi hii.”

    Andendekisye alifunua kitambaa na kushtuka baada ya kuona watu wakiwa ndani ya beseni kama sinema.

    “Umeona nini?”

    “Watu wawili.”

    “Unawafahamu?”

    “Ndiyo.”

    “Nani na nani?”

    “Amangise na mkewe.”

    “Ni wenyewe?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo.”

    “Hebu shemeji angalia.”

    Mke wa Andendekiye alichungulia na kusema:

    “Ni wenyewe.”

    “Sasa tunafanya kazi moja.”

    “Ipi?”

    “Iliyowaleta. Hapa ni pigo moja, hakikisha unachoma kwenye moyo.”

    “Sawa.”

    “Uchawi huu haukopeshi, ukichomoa kisu na mtu kule ameondoka.”





    Dah! Hii ni kiboko.”

    “Tena nitakupa dawa hii kila anayekuchezea unaweka maji kwenye beseni na dawa nitakayokupa, lazima kwanza uchinje kuku mwekundu ambaye damu yake utaweka kidogo kwenye maji na kumuona mbaya wako hapo lazima afanye kama hapa haipiti muda utasikia mtu yupo chali.”

    “Mbona mwaka huu nitawafyeka wabaya wangu wote,” Andendekisye alijigamba.

    “Unaanza na nani?” mganga alimuuliza.

    “Na huyu mbaya wangu namba moja,” alimuonesha Andendekisye.

    “Haya chukua dawa hii jipake mkononi .”

    Andendekisye alichukua dawa na kujipaka mikononi kisha akashikishwa kisu na kuambiwa:

    “Nyanyua juu kisha teremsha kwa nguvu choma kwenye moyo kwa mikono miwili.”

    Andendekisye alishika kisu na kukinyanyua juu na kukiteremsha kwa nguvu kwenye maji kuchoma kwenye kifua cha Amangise mpaka maji yakaruka juu.

    Baada ya kuchoma kisu mganga alimsifia.

    “Vizuri kazi ya kwanza umeifanya vizuri.”

    Wakati anachoma ndani ya maji mkewe alishtuka na kupiga kelele huku akijishika kifua. Wakati huo maji ndani ya beseni yaligeuka rangi na kuwa damu tupu yenye kutoa harufu ya damu mbichi.

    “Nini mke wangu?” Andendekisye aliuliza baada ya kumuona mkewe ameshika kifua.

    “Nimesikia kitu kama kisu kikinichoma kwenye moyo wangu.”

    “Eti nini?” mganga alishtuka.

    Ghafla mikono iliyopo kifuani ilianza kutapakaa damu na kufanya mke wa Andendekisye alalamike.

    “Jamani nakufa, nasikia maumivu makali kifuani.”

    “Mungu wangu,” Andendekisye alishtuka kuona mikono ya mkewe imejaa damu.

    “Mganga hii nini?”“Mmh! Hebu subiri,” mganga alisema huku akiangalia kwenye beseni na kushtuka kuona kitu tofauti.

    “Kabla ya kuchoma uliona picha gani?”

    “Ya Amangise na mkewe.”

    “Si kweli hukuangalia vizuri.”

    “Vizuri kivipi hata mke wangu aliona picha hiyo.”

    “Nasema hukuangalia vizuri wakati unachoma ilibadilika na kuwa picha ya mkeo, kumbuka nilikukataza usifumbe macho,” mganga alimlaumu.

    “Mganga unataka kunilaumu bure, nimefuata yote sikufumba macho na niliyemchoma alikuwa Amangise si mke wangu.”“Mbona hapa kuna picha ya mkeo akielea kwenye damu.”

    “Eti nini?”

    “Hapa panaonesha aliyechomwa ni mkeo.”

    “Mungu wangu sasa tutafanya nini?”

    “Nitajitahidi lakini sijui.”

    “Mganga chondechonde okoa maisha ya mke wangu,” Andendekisye alipagawa.

    Wakati huo mkewe alikuwa ameegemea ukutani macho yakiwa yamechoka kama mtu aliyefanya kazi ngumu iliyomchosha.

    “Mmh! Hebu subiri.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mganga alisema huku akitoka nje na kumuacha Amangise na mkewe. Alimsogelea mkewe aliyekuwa akimtazama kwa jicho kama ana usingizi mzito.

    “Mke wangu.”

    “A..aa..bee.”

    “Unajikiaje?”

    “Mmh! Nasikia baridi kali moyoni.”

    “Subiri mganga atakupa dawa.”

    “Siwezi kupona lazima nitakufa inaonesha kabisa mganga hawezi kurudisha alichokitoa.”

    “Una maana gani mke wangu?”

    “Dawa imeshafanya kazi hawezi kuirudisha ni wazi amekata tamaa.”

    “Huwezi kufa, kama ameroga mwenyewe ashindwi kuzuia.”

    ‘Mume wangu baridi linazidi nahisi viungo kufa ganzi, nakufa mume wangu.”

    “Huwezi...huwezi.”

    Andendekisye alishtuka kuona mganga akichelewa kurudi wakati hali ya mkewe ilizidi kuwa mbaya. Alitoka nje kumtafuta mganga alishangaa kumkuta akiwa amekaa na msaidizi wake akivuta tumbaku. Hali ile ilimshangaza sana baada ya kumkuta mganga akipiga stori na msaidizi wake wakati ndani amemuacha mkewe kwenye hali mbaya.

    ” Mkuu vipi?” Andendekisye aliuliza.

    “Bado natafuta njia ya kuyaokoa maisha ya mkeo.”

    “Unatafuta vipi wakati nimekukuta unazungumza na msaidizi wako huku unavuta tumbaku?”

    “Umeshawahi kuniona navuta hata sigara?” mganga alimuuliza Amangise akiwa amemkazia macho.

    “Sijawahi kukuona ndiyo leo.”

    “Basi ukiona hivi ujue akili imegota mwisho kuvuta huku ni kutaka msaada wa mizimu.”

    “Mmh! Mpaka mizimu ikusaidie mke wangu bado atakuwa hai?”

    “Mkeo ana nafasi ya kuishi kwa asilimia moja tu na siwezi kukuahidi kumponya. Dawa ile huwa haina kinga ikimpata mtu.”

    “Sasa ilikuwaje ikampata mke wangu?”

    “Andendekisye niache kwanza nitafute tiba ya mkeo unavyonisemesha unaongeza ukubwa wa tatizo.”

    Ilibidi Andendekisye awe mpole na kusubiri maagizo ya mganga, kuendelea kuwa nje kulimshinda na kumfanya arudi ndani kumtazama mkewe.

    Alipoingia alimkuta mkewe ameegemea kwenye ukuta shingo ikiwa imeanguka. Alimshika na kukuta mwili umepoa. Hakukubali alimtikisa mkewe huku akimwita jina lake.

    “Sara mke wangu mbona hivi?”

    Mkewe hakuwa na jibu kwa vile roho ilikuwa imeachana na mwili, alitoka nje huku akilia mpaka kwa mganga.“Mganga njoo umuone mke wangu.”

    “Hata nikija sitabadili kitu.”

    “Hapana mganga njoo umuone mke wangu.”

    “Najua kilichotokea hata mizimu imeona, asilimia moja haikuwa na nguvu kuzuia kifo cha mkeo.”

    Kusikia vile Andendekisye aliangua kilio kama mtoto mdogo huku akiapa kumfanyia kitu kibaya Amangise. Zoezi la kumteketeza Amangise na mkewe lilisitishwa na kuushughulikia mwili wa mke wa Andendekisye.

    Kwa vile nyumbani Tanzania ilikuwa mbali na safari yake haikufuata taratibu za uhamiaji walikubaliana mwili wa mkewe uzikwe kulekule Matipa nchini Malawi.

    Mganga hakutaka maiti ilale kwani ingemletea picha mbaya kwa wateja wengine, ilibidi kaburi lichimbwe usiku uleule na watu watatu kwa kupokezana Mganga msaidizi wake na Amangise mwenyewe kwa vile wagonjwa waliokuwepo walikuwa wanawake watupu.





    Japokuwa Andendekisye alikuwa na uchungu wa kifo cha mkewe lakini alilazimishwa na mganga kusaidia kazi ya kuchimba kaburi kisha waliuchukua mwili wa mke wa Andendekisye na kwenda kuuzika watu watatu usiku uleule. Baada ya kuzika walirudi nyumbani kwa mganga ambaye kichwa kilimuuma kwa kilichotokea, toka aanze uganga hakuwahi kutokewa na kitu kama kile.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofika kilingeni kwake aliangalia rada zake, ajabu kila alipoangali ilikuja sura yake kuonesha ndiyo iliyofanya vile. Kila njia alitumia ili aone nani aliyefanya vile hakukuwa na jibu lingine zaidi ya kujiona yeye kuwa ndiye mhusika wa kifo cha mke wa Andendekisye.



    Baada ya kuchemka alimwambia Andendekisye:

    “Inaonekana jirani yako makombora ya mbali hayamuwezi nitaondoka na wewe mpaka kwako nikatege bomu langu karibu. Hawezi kunichezea akili sijawahi kuchezewa akili, naapa nikimshindwa naacha uganga.”



    “Yaani siamini kama ukishindwa nitakwenda popote ili nimtie adabu hawezi kunitia hasara mara mbili,” Andendekisye alisema kwa uchungu.

    “Tunaondoka muda huu ili mchana itukute Tanzania natega vyangu baada ya majibu naondoka usiku kurudi kwangu.”



    “Yaani nipo radhi kutumia kiasi chochote cha fedha hata kuuza shamba langu lote ili nimtie adabu.”

    “Wala hutaingia hasara yoyote majibu utayapata leo hii hii kama yeye anajua hivi sisi tunajua vile. Sijawahi kushindwa na kitu chochote, wachawi wote wanajua mimi ni nani. Kama kombora la mbali limemkosa sasa vita naihamishia Tanzania, kitu nitakachomfanya hakitasahaulika katika midomo kijijini Ibungu na vitongoji vyake- na Tanzania nzima.”



    “Nataka pigo limalize mpaka kizazi chake chote hata kama kuna ndugu zake hakikisha unafagia mpaka sisimizi anayemuhusu.”“Hiyo kazi ndogo, hata jengo analoishi litageuka kichunguu, amenichokoza huwa sichezewi, mimi ndiye mchawi niliyeogopwa mpaka na shetani,” mganga alijitapa kwa hasira.



    Baada ya mganga kuchukua makombora ya maangamizi, waliondoka alifajiri ile na kuacha wagonjwa chini ya wasaidizi wao huku akiwaeleza atarudi usiku wa siku ile ili kuendeleza tiba zao na kama kuna mmoja atakuwa bado hajapata nafuu japokuwa aliamini dawa aliyowapa ilikuwa ni nzuri, wamuongezee dozi.



    Walipanda magari mpaka mpakani na kuvuka mpaka hadi Tanzania na kupitia baikeli yake mpaka Ibungu ambako walifika saa saba mchana wakati huo watu walikuwa katika maandalizi ya mazishi ya Ambakisye. Alipofika alikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwake na kuingia ndani.

    “Mkuu taarifa wanazika saa kumi jioni,” Andendekisye alimweleza mganga baada ya kudodosa habari za kijijini.



    “Basi kazi itaishia makaburini wote watarudi na pumzi lakini si Amangise na mkewe, hilo kombora ni moja ya silaha, huzitumia kwa nadra hasa kwa watu wenye kutaka kupimana nguvu na mimi.”

    “Yaani nikisikia wamekufa mbona nitafanya sherehe, nitachinja ng’ombe wawili.”

    “Hiyo kazi ndogo namaliza kazi yangu kachague hao ng’ombe kabisa.”



    “Hilo halina tabu, yaani mpaka sasa nashindwa kulia kwa kifo cha mke wangu kipenzi, naona kama bado nipo ndotoni na asubuhi nikiamka naona kama zamelala pembeni yangu.”

    “Najua, lakini moyo wako wa kuvumilia unanipa nguvu ya kuifanya kazi vizuri.”

    “Nataka kilio changu kigeuke kicheko.”

    “Jioni haipo mbali.”



    “Sasa hivi sitasema kitu nasubiri majibu toka makaburi juu ya vifo cha Amangise na mkewe.”

    “Mmh! Sasa kazi ndiyo inaanza kabla hawajaenda makaburini. Nipatie unga, ungo na chungu.”

    Andendekisye alifanya vile haraka kwa kumletea mganga alivyoomba kisha alikaa pembeni. Mganga alifungua makombora yake na kutoa- dawa aliyochanganya na unga na kipande cha ngozi ya chatu na kufunika kwa ungo.



    Kisha alichukua dawa nyingine na kuchanganya na unga- na kucha ya bundi na kuvifunika na chungu, walitoka nje na kuomba chungu kingine kipya.

    “Nipatie kuku mwekundu.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Andendekisye aliingia bandani na kuchukua jogoo jekundu na kumpa- mganga ambaye alimchukua na kumlisha hirizi ndogo kisha alimzika akiwa hai. Chungu alikichukua na kukiweka nyuma ya nyumba na kuomba kisu.



    “Nichome tena kisu?” Andendekisye alishtuka.

    “Hapana , kazi yote nafanya mimi kama bomu wacha linilipukie.”

    “Mmh! Hapo sawa, maana sasa hivi kisu nakiogopa sidhani kama nitachinja hata kuku katika maisha yangu kwani sasa hivi nikishika kisu nitakuwa kama namuua mke wangu.”



    “Ondoa wasi kazi yote nimeamua kuifanya mwenyewe wewe subiri majibu utajua huwa sibahatishi kwenye kazi yangu.”Baada ya mganga kuchukua kisu na chungu kipya alikiweka nyuma ya nyumba na kukiweka kisu ndani ya chungu bila kitu chochote.



    Kisha walirudi ndani na kumwambia- Andendekisye. “Fungua kwenye chungu,” alimwambia afunue chungu- kilichowekwa dawa na kucha ya bundi.--- -

    Andendekisye alisogea kwenye chungu na kufungua, alishtuka na kusababisha kukidondosha chungu baada ya kumkuta bundi mkubwa ndani yake aliyetengenezwa na dawa alizochanganya mganga ambazo ziligeuka kuwa ndege huyo

    “He!”



    “Unashangaa nini?”

    “Siamini.”

    “Kazi umeanza, hii ndiyo silaha itakayommaliza mke wa adui yako,” mganga alisema huku akimtoa bundi na kumuweka pembeni kisha alimgeukia Andendekisye aliyekuwa bado amepigwa na butwaa baada ya kuona maajabu yale kwa mchanganyo wa dawa kutoa bundi.



    “Hii nitafunua mwenyewe kwa vile unaweza kufa kwa mshtuko, utakachokiona usishtuke ni silaha za maangamizi.”

    “Kwani kuna nini?”

    “Utaona tu.”





    Mganga alisogea kwenye ungo na kufungua, Andendekisye kidogo atimue mbio baada ya kutoka chatu mkubwa.

    "He!" alishtuka."

    "Usishangae kazi ndo' kwanza imeanza, hili kombora litammaliza adui yako akiingia kaburini tu atakutana na hii kitu inamgonga bila watu kujua kisha inapotea."

    "Mmh! Kweli unatisha, na hivi vingine?"

    "Zote ni zana za maangamizi, hii ya kuku kuzikwa nayo itakuwa na kazi hukohuko makaburini kwani, kama la nyoka litashindwa basi hii itafanya azikwe akiwa hai."

    "Azikwe akiwa hai! Kivipi?" Andendekisye alishtuka.

    "Wakati wameinama kuzima kuna dongo litaanguka na kuwafukia wote."

    "Mmh! Na ya chungu?"

    "Ni kama tuliyotumia Matipa sasa hii ni dijitali kila kitu kitajiendesha chenyewe tukikuta damu tujue kazi imekwisha."

    "Mmh! Sawa."

    "Basi ngoja nitege tusubiri majibu."

    "Sawa."

    Mganga aliingia kwenye kazi ya kutega mabomu kwa kuwachukua bundi na chatu ambao aliwaweka sehemu moja na kuwafunika na shuka nyekundu kisha alichukua dawa na kunyunyizia juu huku akisema maneno yake baada ya sekunde chache vitu vile vilitoweka na kumfanya Andendekisye azidi kuchanganyikiwa na mambo ya mganga akiamini kiama cha Amangise kimefika.

    "Vimeenda wapi?" Andendekisye aliuliza macho yamemtoka pima.

    "Vimekwenda kufanya kazi iliyonileta Tanzania huwa sitaki mchezo kwenye kazi zangu, majibu utayapata jioni."Baada ya zoezi lile waliendelea na mambo mengine huku wakisubiri majibu kwenye mazishi ya Ambakisye.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    KIJIJINI IBUNGU

    Kama kawaida wanakijiji walikusanyika katika nyumba ya mzee Amangise kwa ajili ya kumsindikiza kijana wao Ambakisye aliyeondoka bado mbichi. Katika vitu vilivyokuwa tofauti siku ile ni mazishi ya Ambakisye kuzikwa kama muislamu bila sanduku na kaburi lake kuwekewa mwana ndani.

    Pia hata maiti yake haikuvalishwa nguo ya kawaida ilivishwa sanda ya kawaida, yalikuwa maagizo ya mganga ili wachawi wasimle nyama. Baada ya misa ya mazishi kufanyika kisha kumuaga marehemu na kusababisha vilio kwa watu waliomfahamu Ambakisye na tabia yake ya upole kwa kuwajali wakubwa na wadogo.

    Matayarisho yote yalikwenda vizuri muda ulipofika waliubeba mwili na kuupeleka makaburini huku wakina mama wakimsindikiza kwa vilio.





    Mama Ambakisye ilibidi ashikiliwe kutokana na kukosa nguvu na maumivu makali ya moyo kutokana na kumpoteza mwanaye kipenzi. Japokuwa upande mmoja alimlaumu mumewe kwa kiburi chake cha kulazimisha mambo, bado alimuona hata jirani yake naye hakutakiwa kuchukua uamuzi wa hasira kumuua mtoto wake bila sababu, japokuwa hakujua nani aliyemuua Atuganile.

    Watu walimshika hadi makaburini ambako walimuweka chini ya mti na kumpepea baada ya kuonekana akihema kwa shida huku presha ikimpanda kutokana na kulia sana.

    Baada ya jeneza kuwekwa pembeni ya kaburi, padri alisogea kuliombea kaburi na mwili wa marehemu kisha aliomba mwili uingizwe kaburini.

    Ilikuwa tofauti na imani za Kikristo ya kuzikwa kwenye jeneza, mwili wa Ambakisye uliteremshwa kaburini chini kukiwa na watu wanne ili kuupokea.

    Walianza kuingia watu kaburini akiwemo mzee Amangise ambaye aliingia kaburini amzike mwanaye. Mganga aliyekuwa amesimama karibu na kaburi, machale yalicheza na kupiga kelele kumuomba Amangise asiingie kaburini.

    "Itakuwaje nisimzike mwanangu?" Mzee Amangise alimshangaa mganga.

    "Nina maana yangu, acha wazike wengine, utajua baadaye."

    Mzee Amangise alitoka ndani ya kaburi shingo upande na kusimama pembeni. Mganga alisimama na kuwaeleza wazikaji wasizike kwanza, nao walifanya hivyo. Alitoa kitu mfukoni na kukiminya na kuanza kuzungumza kama anakemea pepo kwa muda huku jasho likimtoka.

    Haukupita muda, alitokea bundi na kuelekea alipokuwa amelazwa mke wa Amangise akipepewa, lakini alipokaribia aliganda kama amefungwa kamba, watu wote waliokuwa eneo lile walitimua mbio na kumuacha mke wa Amangise peke yake.

    Mganga alizidi kuzungumza huku akiminya alichokuwa amekishika hadi kikapasuka kama bomu.

    Ajabu baada ya kupasuka bundi aliyekuwa akienda kwa mke wa Amangise naye alipasuka vipandevipande. Watu wote walishtuka na kuzidi kuyaona maajabu kwenye mazishi ya wiki ile.

    "Hivi watu wana faida gani kushiriki uchawi? Nawaambia kila mmoja akitoka hapa akaache uchawi kama si hivyo nitawaumbua. Nawajua wengine tupo hapa mnashangaa lakini ndiyo michezo yenu. Sasa hivi mmewaingiza mpaka watoto wenu kila kona uchawi unanuka.

    "Mji huu si salama tena, narudia, wote wenye mchezo huu mkachome tunguri zenu na kuacha tabia ya kuwatesa watu bila sababu," mganga alisema kama mtu aliyepandisha mashetani.

    Baada ya kusema vile alitulia kwa muda kisha alisema kwa sauti yake ya kawaida:

    "Mnaweza kuzika."

    "Vipi naweza kuingia?" Mzee Amangise aliuliza.

    "Mzee wangu nayapenda maisha yako na mkeo, yule bundi ilikuwa safari ya mkeo angemgusa tu naye tungemzika kesho. Nina sababu ya kukuambia usiingie kama unataka uzikwe na mwanao basi ingia umzike."

    "Mmh! Basi waendelee."

    Wazikaji walipoanza kuzika walishtuka kuona kitu kikianguka ndani ya kaburi, walipoangalia waliona joka kubwa lililokuwa likivuja damu. Walipiga kelele na kutoka nje ya kaburi kwa kujirusha nje. Lakini mganga aliwaeleza wamtoe kwa vile wamemuwahi alikuwa ametumwa kufanya ubaya kama yule bundi.

    "Nyoka aliyetumwa amekufa."

    Baada ya kumtoa nyoka aliyekuwa amekufa ambaye alikuwa ametapakaa damu kama alikuwa wakiogelea kwenye mto wa damu, zoezi la mazishi liliendelea vizuri bila tatizo lolote.

    Baada ya msiba mganga aliomba kuzungumza tena.

    "Wazee wangu, kijijini kwetu kumekuwa na michezo mingi ambayo watu wengi hawaioni kwa macho ya kawaida.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nimekuwa nikiyaona kwa macho lakini nilikaa kimya, wapo niliowafuata kuwaeleza waache mchezo huo na walipokaidi amri yangu wanajua nini niliwafanya.

    "Sasa leo kwa mara ya kwanza nalisema hili kwa sauti kubwa, wote wenye tabia ya kishirikina waachane na tabia hiyo mara moja.

    "Hii inasababisha waganga sasa hivi badala ya kutibu tunaroga kutokana na matatizo ya kijinga tu ambayo ni ya ujirani ya kuzungumza na kuyamaliza.

    "Wengi mmekuwa mkikimbilia Malawi kuwaumiza wenzenu, nasema kuanzia leo uwe mwanzo na mwisho. Narudia kusisitiza najua kuna watu wana masikio ya kenge, hawasikii mpaka watokwe damu masikioni, wachawi wote mnaombwa kuacha mara moja na mkitoka hapa mkatupe tunguri.

    "Najua wapo wanaowanyooshea vidole wenzenu na kuonekana wema hata kwenye nyumba za ibada. Hao ndiyo wanaokaa mbele lakini ni watu wabaya sana, wamewaweka wenzao misukule. Sasa mkitoka hapa mkaiachie misukule la sivyo nitawaumbueni.

    "Kuna mtu kafanya mchezo wake majibu yake yatapatikana kuanzia usiku huu na mwengine kiyama chenu kinakuja.

    "Samahanini kwa usumbufu wa kuwaweka makaburini baada ya kuzika ila anayeona natania, siku hiyo sitataka msamaha wa mtu. Najua wapo wachawi wanaotaka kunijaribu, nawakaribisha ila kila atakayekuja kwangu hatarudi, mtazika wiki nzima na kila nyumba itakuwa na kilio," alisema kwa kujiamini, tofauti na waganga wengi kuwa watu wazima lakini yule alikuwa kijana mdogo wa miaka kumi na saba au kumi na nane ambaye alionekana kujiamini kupita kiasi.

    Wakati huo Andendekisye na mganga wake walikuwa wakisubiri majibu ya kombora walilolituma. Walisubiri majibu kutoka makaburini kwa watu ambao wangerudi na jibu la kilichotokea. Baada ya kusubiri kwa muda waliona watu wakitoka makaburini, walijawa na hamu ya kutaka kujua nini kimejiri huko.

    Alibahatika kumpata mmoja wa watu waliokuwa wakitoka mazishini kwa kuvizia ili watu wengine wasijue anamuuliza nini.

    "Vipi unatoka makaburini?"

    "Ndiyo."

    "Vipi za huko?"

    "Mmh! Nzuri kiasi."

    "Kwa nini unasema hivyo?" Andendekisye moyo wake ulianza kufurahi kwa kuamini walichokikusudia kimetimia."

    "Tumezika katika wakati mgumu sana."

    "Hakukuwa na tukio lolote?"

    "Mmh! Mwaka huu mbona kijiji kimefanywa cha majanga ya uchawi."



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog