Search This Blog

VITA YA WACHAWI - 5

 





    Simulizi : Vita Ya Wachawi

    Sehemu Ya Tano (5)





    ILIPOISHIA:

    Baada ya kusubiri kwa muda waliona watu wakitoka makaburini, walijawa na hamu ya kutaka kujua nini kimejiri huko.

    Alibahatika kumpata mmoja wa watu waliokuwa wakitoka mazishini kwa kuvizia ili wengine wasijue anamuuliza nini.

    "Vipi unatoka makaburini?"

    "Ndiyo."

    "Vipi za huko?"

    "Mmh! Nzuri kiasi."

    "Kwa nini unasema hivyo?" Andendekisye moyo wake ulianza kufurahi kwa kuamini walichokikusudia kimetimia."

    "Tumezika katika wakati mgumu sana."

    "Hakukuwa na tukio lolote?"

    "Mmh! Mwaka huu mbona kijiji kimefanywa cha majanga ya uchawi."

    SASA ENDELEA...

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Ehe!" Andendekisye alijiandaa kumsikiliza.

    Alielezwa matukio yaliyotokea makaburini tukio la bundi kumfuata mke wa Amangise lakini kabla ya kumfikia mganga alifanya mambo yake na yule bundi kuganda kisha alipasuka vipandevipande kabla hajamfikia mkusudiwa.

    Tukio lingine lilikuwa la nyoka aliyedondokea kaburini akiwa amekufa huku mwili wake wote kutapakaa damu kila kona kama alikuwa akiogelea kwenye dimbwi la damu.

    "Duh!" Andendekisye alishtuka kusikia vile.

    "Yaani kila kukicha kinazaliwa kituko kipya."

    "Kwa hiyo Amangise na mkewe wanaendeleaje?"

    "Kivipi, kwani walikuwa wakiumwa?"

    "Hapana kutokana na tukio lile kipi kimewatokea?"

    "Wapo salama, lakini inasemekana bila mganga basi Amangise na mkewe wangemfuata mtoto wao kuzimu."

    "Umesikia tetesi watu wanasema nani anahusika na matukio yake?" Andendekisye alidodosa.

    "Mmh! Kwa kweli kila mmoja anasema lake japo kuna watu wanakuhusisha wewe kutokana na kauli zako."

    "Mi sihusiki bali siku ile nilisema kwa hasira," Andendekisye alijisafisha.

    "Basi kauli yako imeumba, watu wote wanajua wewe ndiye uliyemuua Ambakisye na kutaka kuwaua Amangise na mkewe."

    "Mbona hawasemi Amangise alivyomuua mwanangu?"

    "Ni vigumu kujua kwa vile wewe ulijitapa mbele ya watu kuwa ulimuua Ambakisye sasa unafyeka ukoo mzima."

    "Hakuna siwezi kufanya hivyo zile zilikuwa hasira."

    "Watu wanasema mara ya kwanza ulipoondoka ghafla kabla ya kumzika mwanao ulienda kumtengeneza Ambakisye."

    "Si kweli."

    "Wewe unasema hivyo, lakini kila mmoja anajua wewe ndiye mhusika mkuu, pia tukio la leo linaambatana na wewe na mkeo kuondoka jana usiku baada ya mazishi ya mwanao. Inasemekana ulienda kuwamaliza Amangise na mkewe lakini mpango wako safari hii umefeli."

    "Watakuwa wamenielewa vibaya, hakuna kitu kama hicho."

    "Basi ndiyo hivyo kauli yako haijaondoka vichwani mwa watu."

    "Kwa hiyo hakuna yeyote aliyeathirika na tukio lile?" Andendekisye alizidi kuchimbua.

    "Wapo wachache waliochubuka wakati wa kumkimbia bundi na mmoja ameumia mkono wakati wa kumkimbia chatu aliyeangukia kaburini."

    "Amangise hakuingia kaburini?"

    "Ndiyo."

    "Kwa nini hakumzika mwanaye si mnaona mnaniita mchawi wakati mchawi mnamuacha."

    "Alikatazwa na mganga alisema akiingia angezikwa na mwanaye."

    "Mmh! Huyu mganga anatoka nchi gani?" Andendekisye aliuliza macho yamemtoka pima.

    "Walaa, wa hapahapa nchini."

    "Haiwezekani lazima Amangise alisafiri mbali."

    "Mbona mganga mwenyewe unamjua wa kijiji cha pili."

    "Nani?"

    "Si yule kijana aliyemrudisha mtoto wa Mwakasege."

    "Yule si mganga alipanga ili kuvutia biashara yake nilichunguza na kuujua ukweli."

    "Basi ndiye aliyefanya kazi ya kuokoa maisha ya Amangise na mkewe."

    "Kama yule hana lolote yule kijana tapeli, mganga awe kijiji cha jirani?" Andendekisye aliendelea kubisha.

    Andendekisye aliupinga uwezo wa mganga kwa yule kutokana na kuamini sana waganga wa kweli wapo Malawi na si Tanzania.

    "Halafu mganga amesema kila mmoja anayejihusisha na ushirikina aache mara moja, wote tumeambiwa tukitoka makaburini tukachome tunguri zetu kama tunazo."

    "Na wasipochoma?"

    "Amesema kiama chao kinakuja cha watu kuumbuka hadharani."

    "Anawatisha tu watu, hana jeuri hiyo."

    "Wewee! Yule kijana anatisha, nina wasiwasi wachawi wa kijijini siku ya kuumbuka inakuja kwa atakayekaidi amri yake."

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Kama kweli basi ataanza kuumbuka Amangise na mkewe, maana wale wanatisha kwa uchawi."

    "Basi wacha niwahi msibani watu wamepita muda."

    "Hakuna tatizo tutaonana baadaye."

    Andendekisye aliagana na mtu aliyempa taarifa ya makaburini na kumfanya kichwa kizidi kuchanganyikiwa alirudi ndani kwa mganga aliyekuwa akisubiri majibu ya kazi yake makaburini. Sura ya Andendekisye ilimshtua mganga na kutaka kujua kulikoni.

    "Vipi?"

    "Mambo mabaya."

    "Mabaya kivipi?"

    "Tumefeli tena."

    "Muongo!"

    "Kweli, hakuna cha bundi wala chatu."

    "Kwani imekuwaje?"

    Andendekisye alimweleza yaliyotokea makaburini ya kupasuka vipandevipande kwa bundi na kuokotwa kwa nyoka kaburini akiwa ametapakaa damu mwili mzima kama alikuwa akiogelea kwenye bahari ya damu.

    "Mmh!" mganga aliguna baada ya kuona ngoma aliyokuwa akicheza si ya kitoto.

    "Sasa tunafanyaje?"

    "Yaani nazidi kukutana na vikwazo, sielewi nimekosea wapi, hebu twende nyuma ya nyumba tukaangalie bomu lingine. Siamini kama mtu ninayepambana naye ana uwezo mkubwa kama huo lazima kuna kitu nimekosea."

    "Nasikia kuna kijana mmoja ndiye aliyezuia zoezi letu bila hivyo kazi ingekwenda vizuri."

    "Hakuna kiumbe kinachoweza kuzuia kazi yangu, hebu tukaangalie ili niangalie nimekosea wapi. Wachawi walioshindikana hupiga saluti mbele yangu itakuwa mganga huyu kwanza anatoka wapi?"

    "Kijiji cha jirani."

    "Hapahapa Tanzania?"

    "Ndiyo."

    "Tanzania hakuna waganga, subiri nikamtie adabu."

    Walizunguka nyuma ya nyumba kuangalia mtego mwingine unaonesha kitu gani.





    Makaburini baada ya mganga kutoa onyo kwa wachawi wote aliondoka na watu walikwenda kuzika na walirudi msibani. Alipofika kwa Amangise aliongeza nguvu kwenye dawa alizoweka kutokana na kuona uzito wa kazi ulivyokuwa na vita iliyokuwa bado inaendelea. Baada ya kumaliza kazi yake alizungumza chemba na Amangise na mkewe.

    "Nina imani kazi imekwisha, ninataka kuwaeleza vita yenu ni kubwa, kama nisingekuwa mjuzi wa mambo haya tulikuwa tunawazika kesho mtu na mkewe. Uchawi uliotumiwa ni mkubwa sana. Nyoka yule alitumwa kuja kukumaliza ukiwa kaburini ungemuona wewe tu baada ya kukuuma angetoweka hakuna mtu mwingine angemuona.

    Kama angekuuma kusingekuwa na dawa ungekauka muda uleule na yule bundi alitumwa kuja kwa mkeo angemgusa tu basi angepata mshtuko ambao ulikuwa ndiyo safari yake, lakini nimewahi. Kuna makombora mawili nimeyazima hukohuko yalipokuwa majibu ya kazi yangu mtayasikia kama si usiku basi kesho.

    "Kuna kitu nataka mkifanye usiku huu, nikitoka hapa tunguri zote mzitoe ndani na kuzitia moto na wala usijihusishe tena na mambo ya kishirikina. Mkimfanyia mtu ubaya wowote ujue unawarudia wenyewe. Wiki ijayo nitakuwa na kazi ya kukomesha uchawi kijiji hiki na ninyi mkiendelea kuuficha uchawi shauri yenu," mganga alitoa onyo.

    "Tumekusikia, tunakuahidi kuachana na kila ovu madhara yake tumeyaona," Amangise alimuahidi mganga."Sasa baba, tutaweza kwenda kanisani kweli?" mke wa Amangise aliuliza.

    "Kanisani mwende kwa vile mtakuwa watu wema ambao mtamuogopa Mungu na si kuingilia kazi ya Mungu kuua na kutesa."

    "Basi tunakuahidi kuwa viumbe wapya."

    "Mimi nimemaliza kama mnanifurahisha ili niondoke kitakachowatokea naomba msinishirikishe."

    "Nakuahidi kusimamia kila kitu kuteketeza kila kitu," mama Ambakisye alimuahidi mganga.

    Baada ya mganga kuyasema yake aliondoka kurudi nyumbani kwake na kuwaacha watu wakiwa msibani huku watu wakiwa makundimakundi kuzungumzia matukio ya wiki ile. Kuna mtu alisema alimuona Andendekisye mchana ule akielekea kwake akiwa na mgeni wa kiume.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wapo waliojiuliza mkewe kamwacha wapi, lakini wapo waliofikiria labda alimpeleka kwao. Wanaomfahamu walipinga kwa kusema mkewe hakuwa na ndugu baada ya kufiwa na wazazi wake pia Andendekisye alikuwa hapatani na ndugu zake hivyo maisha yake yote hakuwahi kumuona akienda kusalimia ndugu zake.

    Wapo walioamini huenda alikwenda kwa mganga kutokana na kauli yake na aliyeongozana naye huenda ndiye mganga lakini ajabu mkewe hakuonekana na kujiuliza mkewe yupo wapi. Kwa vile yalikuwa hayawahusu waligeukia kauli ya mganga kuhusu watu kuteketeza tunguri zao.

    "Unajua yule kijana anatakiwa kudhibitiwa kwa vile anaweza kuwaumbua watu wazima."

    "Atadhibitiwa vipi, lakini si amesema watu waharibu tunguri zao kila aliyekuwa nazo kabla siku ya kuwaumbua watu."

    "Watu wengine familia zetu zinafanya hivyo si mwanzo wa kuumbuka."

    "Hakuna jinsi ni kukubaliana naye bila hivyo aibu inakuja."

    "Anatakiwa kudhibitiwa kabla ya siku hiyo."

    "Mmh! Mnafikiri mtafanyaje?"

    "Tutamfuata na kumuomba asitishe zoezi lake."

    Wazee waliweka mikakati ya kumdhibiti mganga kabla siku ya kuwaumbua watu haijafika. Walipanga kumfuata kwake na kumuomba aachane na zoezi lile ambalo lingeleta picha mbaya kijijini.

    ***

    Andendekisye na mganga wake walizunguka nyuma ya nyumba kuangalia chungu kitupu kilichowekewa kisu kina matokeo gani. Mganga alishangaa kukuta chungu kipo vilevile kama alivyokiacha. Alirudi ndani na kuchukua dawa ya unga na kwenda kuiweka kwenye chungu na damu kidogo ya kuku huku akisema:

    "Hawezi kuzuia nguvu zangu, ngoja nimtie adabu."

    Baada ya kuweka dawa na damu kidogo kwenye chungu alitulia kwa muda hali ilikuwa ileile. Alikitoa kisu kwenye chungu na kusema maneno yake kisha alikichoma kwa nguvu ndani ya chungu na kutulia kwa muda kisha alifumbua macho kuangalia kwenye chungu kumetokea nini.

    Ghafla ndani ya chungu kulitoka damu iliyoruka kama mtu aliyekata kwa ghafla na kumpata usoni ambayo ilimuingia machoni. Aliachia kisu na kujifuta damu iliyomrukia usoni na kuingia machoni ambayo iliwasha kama pilipili. Baada ya kujifuta alifumbua macho lakini hakuweza kuona kitu zaidi ya macho kuendelea kuwasha.

    "Andendekisye sasa ni saa ngapi?"

    "Saa kumi na mbili jioni."

    "Kuna giza?"

    "Hakuna kwani vipi?"

    "Kama mchana mbona sioni?"

    "Labda damu imekuingia machoni jisafishe."

    "Ndiyo tena inaniwasha kama pilipili."

    "Nikuletee maji."

    "Niletee tena fanya haraka macho yanauma kama kuna kaa la moto."

    Andendekisye alikimbilia maji ndani na kumuacha mganga akijilazimisha kuangalia lakini kila alivyofumbua macho yaliongeza kuwasha. Baada ya kuletewa maji aliyaosha macho lakini hakukuwa na mabadiliko zaidi ya kuanza kuvimba mpaka mishipa ya kichwa kusimama.

    "Mungu wangu sijui nini hii mbona naumbuka mtoto wa Msioka."

    "Sasa itakuwaje?" Andendekisye aliuliza huku ameshika kichwa.

    "Hata sijui macho yananiuma kama kidonda nakufa najiona."

    "Sasa umekosea wapi?"

    "Siwezi kujua, bora angeniua kuliko kunitia upofu nitarudije nyumbani nitawezaje kufanya kazi zangu mbona majanga?"







    "Sasa hebu niambie nifanye kitu gani ili nikusaidie?"

    "Mtafute mwanamke anayenyonyesha mtoto aje anikamulie maziwa machoni."

    "Ngoja nijaribu."

    Andendekisye alitoka nyumbani kwake bila kujua atampata wapi mwanamke anayenyonyesha. Alitembea kama mwenda wazimu, hata watu wake wa karibu aliwapita bila kuwasemesha, alionekana mtu aliyepagawa, akizungumza peke yake huku akilitaja jina la Amangise, akijipiga mikono kifuani kwa nguvu akiapa kumtia adabu kwa gharama yoyote.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kutokana na kuchanganyikiwa na tukio lililompata mganga aliyekuwa akimtegemea, alijikuta akifika kijiji cha Mbako bila kujua. Alishtuka baada ya kuulizwa na mtu anakwenda wapi ndipo alipogeuza kurudi kijijini kwake. Wakati huo giza lilikuwa limeingia. Njia nzima alirudi akiwa amepagawa na kujiuliza mganga amefanya nini au na yeye ndiyo yamemkuta kama ya mkewe.

    Katika kumjua mganga hakuwahi kumwona akilia kama mtoto kama siku ile, alijiuliza kama kweli mganga amepofuka atafanya nini na atawezaje kumrudisha kwao.

    Alifika nyumbani kwake saa tatu za usiku na kukuta mganga bado ameshikilia macho huku akilia kwa uchungu.

    Alipowasha taa alishtuka kuona macho ya mganga yakivuja damu, aliamini kwa hali ile alikuwa ameumbuka ataieleza nini jamiii ambayo inaamini kabisa yeye ni mchawi aliyehusika na vifo vya baadhi ya watu pale kijijini kikiwemo cha Ambakisye mtoto wa adui yake.

    "Andendekisye nakufa naomba msaada wako," mganga alilalamika huku akigaragara chini.

    "Nikusaidie nini maana nimechanganyikiwa?" Andendekisye hakujua afanye nini?"

    "Hujapata mwanamke anayenyonyesha?"

    "Yaani hata sijui nitampata wapi?"

    "Huna majirani?"

    "Ninao lakini nawaogopa wataniuliza nina shida gani na maziwa yao wakati sasa hivi kijiji kizima kinajua mimi mchawi."

    "Kwa hiyo upo tayari kuniona nakufa, Andendekisye kumbuka nimetoka mbali kwa ajili yako."

    "Ni kweli lakini sina ujanja."

    "Kwani huyo mganga anakaa wapi?"

    "Kijiji cha jirani."

    "Naomba chondechonde kaniombee msamaha ili niepukane na adha hii, naumia mwenzio macho kama kuna mtu anayakata kwa ndani."

    "Hii ni ajabu, ndiyo maana damu zinatoka kwa wingi."

    "Mungu wangu natoka damu?" mganga alishtuka.

    "Ndiyo."

    "Nakufa mimi mjukuu wa Msioka."

    "Ngoja basi niwahi kwenda kwa mganga sijui kama atakubali."

    "Mbembeleze bila hivyo naamini siwezi kufika asubuhi lazima nitakufa."

    "Sawa."

    Andendekisye alipitia baiskeli na kuwahi kwa mganga ambaye aliamini ndiye aliyefanya mchezo ule. Alipiga pedeli kwa nguvu ili kuwahi, alichukua dakika 17 kufika. Alipofika alimkukuta akiwa amekaa uani kwake akizungumza na wateja wake waliokuwa wakipata tiba.

    Kutokana na kasi aliyoingia nayo, alijikuta akifunga breki ya nguvu na kusababisha kupiga mwereka. Wote walishangaa jinsi alivyoingia na kupiga mwereka. Andendekisye aliponyanyuka hakujali baiskeli alikwenda moja kwa moja mbele ya mganga na kupiga magoti kuomba msaada.

    "Mganga naomba msaada wako hali ni mbaya."

    "Sina msaada, wewe si kiburi kaendelee na bado kiama chako kinakuja."

    "Ha..ha..pana, sina jeuri yoyote kwako."

    "Si umekuja na mganga toka Malawi, sasa kaloge tena baada kumpoteza mkeo sasa ni zamu yako endelea kushindana na wenye nguvu. Umeua wengi lakini nilikaa kimya hata hili bila kufuatwa na jirani yako ningekaa pembeni mmalizane.

    "Nilitoa onyo mapema kuhusu mtu anayetaka kupima maji kwa kidole sasa subiri kiama chenu kinakuja.

    "Na kamwambie mganga wako akijitia kujua utamrudisha maiti, mimi si mchawi bali mganga wa kutibu watu, sasa huyo mchawi mwenzako mwambie akifanya utani atarudishwa kwao maiti."

    "Najua nimefanya makosa mengi kwa ubishi wangu lakini naomba msaada wako."

    "Umekuja kunijaribu?"

    "Ha..ha..pana."

    "Unataka msaada gani wewe mwanga?"

    "Mganga wangu macho yamepofuka."





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    "Si umpeleke hospitali?"

    "Si ungonjwa wa hospitali anateseka macho yanatoka damu."

    "Kwani kafanya nini?"

    "Alikuwa anatengeneza dawa ghafla akasema haoni."

    "Dawa ya nini?"

    "Ilikuwa ya matatizo yangu."

    "Ukisema kweli nitakusaidia kama husemi ukweli naomba uondoke kabla hajakukuta yaliyomkuta mchawi mwenzako."

    "Alikuwa akinitengenezea dawa baada ya matatizo ya nyumbani kwangu."

    "Nani kamuua mkeo?"

    "Si..si..jui."

    "Sikiliza Andendekisye mimi ni mdogo sana kiumri lakini nafahamu mengi ya kidunia kuliko wewe. Sasa kama umekuja kunijaribu naomba uondoke mara moja."

    "Nashindwa kusema kwa vile linanihusu."

    "Basi mimi sina msaada wowote mpeleke Malawi atapona."

    "Naomba unisaidie kijana wangu, nimeishaumbuka, nakuahidi kufanya yote uliyosema makaburini ya kuachana na mambo ya ushirikina."

    "Ukinijibu maswali yangu vizuri nitakusaidia lakini ukinidanganya naomba unanze kuondoka baada ya mwenzio kupofuka macho wewe utapata ukurutu mwili mzima."

    "Nitayajibu."

    "Nani kamuua Ambakisye mtoto wa Andendekisye."

    "Mimi."

    "Kwa nini?"

    "Kwa vile baba yake alimuua mwanangu."

    "Amangise hakumuua mtoto wako bali kajiua mwenyewe."

    "Una maana gani?"

    "Ni kisasi cha aliyemuua ambaye ni mchumba wa Ambakisye akishirikiana na bibi Tumwambilile ndiyo maana vifo vyao vilifanana na vya muda mmoja. Kwa vile huna busara na tamaa ya mchawi wako akamuua asiye na kosa."

    "Nilikuwa sijui."

    "Nani kamuua mkeo?"

    "Mimi."

    "Nani alituma nyoka na bundi makaburini?"

    "Mimi."

    "Kwa sababu gani?"

    "Nilikuwa sijui, nilitaka kulipa kisasi cha kuuliwa mwanangu."

    "Kwa nini mganga amepofuka?"

    "Kuna mtego mwingine baada ya bundi na nyoka kufeli alitengeneza bomu analolitegemea ndilo lililomlipukia."

    "Sasa msaada wangu kuondoa maumivu ya macho lakini macho ndiyo amekuwa kipofu kweli hata pona tena mpaka anakufa."

    "Na..naomba hata hiyo kwani anateseka sana."

    Mganga alikwenda ndani na kumletea dawa ambayo alimweleza akachanganye na maziwa mabichi na kumnawisha uso maumivu yote yataondoka.

    "Nashukuru."

    "Ukifanya ujanja wowote tusilaumiane."

    "Nakuahidi sitafanya chochote kibaya nimegundua makosa yangu."

    "Basi wahi kumpatia tiba mganga wako."

    Andendekisye alipanda baiskeli kuwahi nyumbani kumpatia tiba mganga ambaye alikuwa akilia kama mtoto kutokana na maumivu makali ya macho. Alipofika alikimbilia kwenye zizi na kumkamua ng'ombe mwenye kunyonyesha kisha alichukua maziwa na kuichanganya na dawa na kumnawisha mganga baada ya sekunde chache macho alitulia na kumfanya mganga kupitiwa usingizi mzito baada ya kuteseka kwa muda mrefu kwa maumivu ya macho.

    ***

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ya pili baadhi ya wazee walikwenda kumwona mganga kumweleza wanachotaka akifanye. Baada ya kufika aliwakaribisha kama wazazi wake na kuwasikiliza.

    "Karibuni wazee wangu."

    "Asante za toka jana?"

    "Namshukuru Mungu."

    "Kijana tumekuwa na shida moja ambayo tunataka tuzungumze."

    "Hakuna tatizo, mna shida gani?"

    "Kutokana na kauli uliyotoa jana makaburini kuhusu ushirikina tunaomba zoezi hilo ulisitishe."

    "Mpaka lini?"

    "Siyo mpaka lini bali lisimamame kabisa."

    "Kwa sababu gani?"

    "Unajua kijiji chochote hakikosi mila na destuli hivyo unachotaka kukifanya ni kutaka kukiumbua kijiji."

    "Kwani nani ataumbuka kama huhusiki?"

    "Hata kama tunahusika sisi kama wazee wa kijiji tunaomba uachane na zoezi hilo mara moja."

    "Wazee wangu nimewasikia lakini ninachotaka kukifanya siyo mimi ni vitu vyangu vilivyomo kichwani mwangu ndivyo vimenituma hivyo lazima nitimize nilichoagizwa nikiacha nitaadhibiwa mimi."

    "Kafanyie sehemu nyingine bila hivyo tutakufukuza kijiji hiki."

    "Najua uwezo huo mnao lakini katu sitabadilia ninachotaka kukifanya, najua wote uliokuja mnaishi kwa ushirikina sikutaka kukuumbueni wakati mnaingia. Wewe mzee ndani mwako kuna misukule saba miwili ni watoto wa jirani yako mnayesali naye kanisa moja, uongo?" Mzee aliyeulizwa alibakia kukapua macho.

    "Na wewe mkeo anauza pombe akiwa uchi na upawa anaotumia ni kiganja cha mtu na wewe ili kuongeza wateja, unajua ndiyo maana umekuja kuzima. Na wewe umemuua jirani yako kwa wivu kwa vile analima sana lakini hakuna mtu anayejua. Kwa vile mmekuja wenyewe mkitoka hapa yote niliyowaeleza kwa siri mkayaache mara moja atakayebisha kiama chake kinakuja," mganga alisema kwa kujiamini tofauti na umri na umbile lake dogo.

    "Kijana tunakuapia hutafanikiwa kufanya hivyo kabla ya wiki tutakuwa tumekuhamisha," wazee walimpiga mkwara.

    "Hakuna tatizo lakini mmechelewa lazima mtaumbuka."

    Wazee waliondoka kwa hasira huku wakijipanga kumkwamisha kufanya mkutano wake wa kuwaumbua wachawi.

    Usiku wakati Andendekisye alipokuwa amelala alimuota mkewe akiwa amemshikia kisu akitaka kumuua huku akimwambia na yeye lazima afe kwa vile alimuua bila sababu. Alishtuka usingizini lakini ajabu bado alimuona live mkewe amemshikia kisu, alikurupuka na kutoka nje lakini alimfuata na kuamua kutimua mbio kuokoa maisha yake.







    Alishangaa nje alimkuta Ambakisye mtoto wa jirani yake aliyemuua pia na kijana mmoja aliyekataa kumuoa binti yake na kumuua. Wote walikuwa nje kila mtu kashika silaha yake na kuanza kumfukuza.

    Alikimbia usiku kucha kuokoa maisha yake na kusababisha kujijeruhi kila alipoanguka.

    Asubuhi watu walimuona kama mwenda wazimu kila alipotulia alishtuka na kuanza kutimua mbio huku akisema mke wangu usiniue na alipoanguka chini alipiga magoti kuomba msamaha huku akisema kuwa alimuua mke wake kwa bahati mbaya.

    Kauli ya Andendekisye ilifanya watu wajue kumbe mkewe naye alimuua mwenyewe, kuna kipindi alikimbia mpaka akapoteza uwezo wa kupumua na kupoteza fahamu. Taarifa ile ilimfikia mganga ambaye aliamini kabisa kupitia Andendekisye ndiyo siku ya kuwaumbua wachawi.

    Alibeba zana zake za kazi na kwenda mjini ambako alikuta Andendekisye amezungukwa na watu huku wengine wakitaka apelekwe hospitali lakini wengine walitaka aachwe afie mbali kwa vile alimuua Ambakiksye na mkewe kwa roho mbaya yake.

    Wapo waliotaka kumtia moto lakini wazee wa kijiji waliingilia kati, bahati nzuri mganga alifika eneo la tukio na kuwafanya watu waliomzunguka kumpisha ili afanye mambo yake. Aliwaomba vijana wambebe mpaka uwanja wa mpira, walifanya vile wakati huo watu walikuwa wakikusanyika kujionea mganga anataka kufanya nini.

    Baada ya kumfikisha Andendekisye aliyekuwa hajitambui, watu nao walikusanyika kama waliopigiwa mbiu ya mgambo baada ya kupashana kilichompata jirani yao ambaye alimuona ndiye mchawi wa kijijini. Baada ya vijana kumlaza chini, mganga aliandaa dawa zake kisha alisema kwa sauti ya juu.

    "Jamani vijana wenzangu mnapajua nyumbani kwa Andendekisye?"

    "Ndiyo," walijibu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Naomba mkamlete mtu mmoja mlemavu wa macho hapa."

    Vijana wale walikimbia nyumbani kwa Andendekisye, walipofika walimkuta mtu mmoja amelala nje. Walipofika aliuliza kama Andendekisye amerudi huku akilaumu kuondoka bila kumuaga huku akijua mwenzake haoni na pia hajala tokea jana.

    "Andendekisye kumbuka wewe ndiye umenisababishia balaa hili, bila wewe nisingekuwa hivi. Kibaya umeondoka ukijua kabisa sioni, sijala tokea jana hii ndiyo shukurani yako?" mganga aliuliza akiwa bado amejilaza chini.

    "Mzee sisi tumetumwa na mganga tukupeleke uwanjani."

    "Mganga gani?"

    "Mganga mtoto."

    "Ana shida gani na mimi?"

    "Wewe twende utajua hukohuko."

    "Kwani Andendekisye yupo wapi?"

    "Naye yupo huko."

    "Lakini mimi njaa inaniuma nipeni kwanza chakula."

    "Utakula huko."

    "Jamani mbona siwaelewi kila kitu mnasema huko."

    "Sisi tumetumwa wala si wenyeji wa hapa."

    "Haya twendeni."

    Walimshika mkono na kwenda naye hadi uwanjani ambako kulikuwa kumejaa watu, wakati wote mganga alikuwa akifanya mambo yake bila kumshughulikia Andendekisye aliyekuwa bado amelala kama amekufa.

    Baada ya kufika alisogezwa kwa mganga, vijana wale walimweleza jamaa ana njaa, ilibidi atafutiwe uji na viazi baada ya kushiba alisogezwa mbele ya mganga. Muda wote watu walikuwa kimya kutaka kujua kuna nini wakati huo wazee waliokwenda kwa mganga alishtuka kusikia mganga kajaza watu uwanja wa mpira akiwa na Andendekisye na mganga wake aliyeonekana kapofuka macho.

    Walijifikiria kwenda polisi kuzuia anachotaka kukifanya lakini walijiuliza wataeleza azuiwe kwa sababu gani ikiwa serikali haitambui ushirikina, japo viongozi wake wanategemea nguvu za giza kutawala.

    Baada ya kila kitu kukamilika mganga alimfanyia dawa Andendekisye aliyenyanyuka na kushangaa kuona umati wa watu na kumuuliza mganga.

    "Nimefikaje hapa?"

    "Tulia utajua tu kwa vile mwisho wa ubaya ni aibu."









    Baada ya kuelezwa vile alipewa uji uliochanganywa na dawa na kuelezwa anywe kisha atulie. Mganga aliachana na Andendekisye na kuwageukia watu waliokuwa wamejaa na kusema kwa sauti ya juu yenye kusikika.

    "Jamani nina imani jana makaburini kwa waliokuwepo waliona kila kitu kilichotokea pia katika misiba miwili iliyotangulia. Mnakumbuka nilieleza watu wafanye zoezi la kuharibu tunguri zao. Nina imani wengi hawaamini ila leo nitawaonesha kwa nini nilisema vile.

    "Jana baada ya kueleza watu waachane na ushirikina, wapo wazee wangu ambao nawaheshimu sana walinifuata niache zoezi langu ili hali hii iendelee kijijini kwa watu kufanyishwa kazi kwenye mashamba ya watu. Watu kutupiga magonjwa bila sababu. Watu kulishwa vitu vichafu bila kujua.

    "Vilevile watu kuuana kama mlivyoshuhudia vifo vya vita ya kichawi ya familia mbili. Hii imekuwa tabia ya watu wa maeneo ya karibu na mpakani kwenda Malawi kufuata uchawi ili kuwadhuru wenzao. Hii imekuwa ikiwaumiza watu wasio na uwezo wa kwenda huko kiasi cha kujiona wao ni miungu watu.

    "Najua nitaondoka hapa kijijini lakini kabla sijaondoka nitaacha historia. Jana nilizungumzia wale nyoka na bundi na kuwaeleza usiku mpaka leo majibu yatapatikana na haya ndiyo majibu yake. Mzee wangu baada ya kumuua mtoto wa jirani yake kwa ugomvi wa kijinga aliona raha ya kuendelea kuua akishirikiana na mganga wake ambaye mimi namuona ni mchawi.

    "Walipanga kuiteketeza familia ya Amangise lakini matokeo yake wamemuua mke wa mteja wake. Bado hawakushtuka kwa nini amemuua mkewe wakapanga kuja kutengeneza uchawi wao Tanzania kwa kutufanya waganga wa Tanzania hatujui kitu.

    "Jana wametega bomu likamlipukia mganga. Na mwenzake anateswa na vivuli vya roho za watu alizozitoa bila hatia ambavyo vitaendelea kumtesa na asiposaidiwa ndiyo itakuwa chanzo cha kifo chake.

    "Nilipanga kazi yangu kuifanya mwisho wa wiki lakini kwa dharura hii nimeonelea niifanye leo. Ila sitaifanya kama nilivyopanga, nitaifanya kwa mtindo mwingine kabisa. Kabla ya kuanza zoezi langu nilikuwa nataka nimuulize kaka yangu hapo mganga.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Eti kaka wewe ni mwenyeji wa wapi?"

    "Matipa Malawi."

    "Umekuja hapa kufanya nini?"

    "Kumtibu bwana Andendekisye."

    "Nini kimekupata?"

    "Hata mimi nashangaa kwa vile kimetokea ghafla."

    "Naomba useme ukweli nini kimekuleta Tanzania na sababu ya kupatwa na tatizo la macho bila hivyo hurudi tena Malawi kwa vile muda wako wa kuishi unahesabika."

    "Kwa kweli lazima niseme ukweli."

    Mganga toka Malawi alielezea jinsi alivyofuatwa na Andendekisye na kumweleza kuwa jirani yake amemuua mwanaye hivyo naye aliomba kulipa kisasi, naye alifanya kama mteja wake alivyotaka na alimrudishia majibu. Mara ya pili alirudi tena na kutaka kummaliza jirani yake na mkewe lakini ilikuwa tofauti, uchawi walioufanya ulimrudia mwenyewe kwa kumuua mkewe bila kujua.

    Pia alielezea jinsi alivyokuja Tanzania ili ammalize adui yao, lakini vilevile ilikuwa tofauti baada ya bundi na nyoka kutofanya kazi. Baada ya kushindwa ndipo alipotega mtego mwingine uliosababisha kupofuka macho.

    Baada ya kumaliza maelezo yake yaliyowaacha watu midomo wazi, aliomba msaada wa matibabu ili apone macho.

    "Najua nimefanya makosa, naomba unisaidie basi niweze kuona nirudi kwetu."

    "Dawa niliyompa mwenyeji wako kuondoa maumivu ya macho ulikuwa uwezo wangu wa mwisho lakini kupofuka ni kazi ya Mungu, sina uwezo huo, hakuna wa kuyaponya macho yako."

    "Basi naomba msaada wa kunirudisha nyumbani."

    "Atakurudisha aliyekuleta."

    "Mmh! Sawa."





    "Sasa ndugu nina imani mmesikia jinsi wanadamu tulivyo wabaya, nataka kuwaambia hapa katika kundi la watu kuna wachawi wengi wakubwa na watoto. Hapa kuna dawa nitaweka kwenye maji kila mmoja atakuja kunawa uso mchawi atajulikana."

    Mganga alifanya mambo yake kwa kuweka maji kwenye beseni kisha alisema kuwa kama kuna mtu anayejihusisha na mambo ya kichawi basi atoke mbele na kujipaka maji yale.

    "Jamani nataka watu waje wanawe maji haya."

    Katika umati uliokuwa pale uwanjani, walitoka wachache ambao walifika na kunawa maji, lakini wengi walibakia wamesimama walipokuwa wamesimama na kumfanya mganga aseme kwa sauti:

    "Kwa hiyo hawa ndiyo wasafi na ninyi wote mliobaki ni wachawi?"

    Watu wote walikaa kimya, alimwita mtoto mmoja wa miaka saba aliyekuwa amesimama kifua wazi. Yule mtoto alisogea mbele kwa mganga ambaye alimwambia anawe yale maji lakini alikataa na kufanya watu washangae. Mganga alimuuliza:

    "Kwa nini hutaki kunawa?"

    "Nitaungua."

    "Mbona hakuna moto."

    "Beseni lote linawaka moto na maji nayaona yanachemka nitaungua."

    Aliitwa mtoto mwingine na kuombwa anawe, alinawa bila tatizo lakini alipoambiwa tena yule mtoto aligoma na kusema ataungua. Watu waliokuwa wakiona kama utani, mganga alimwita mzee mmoja ambaye aligoma na kuamua kuondoka.

    "Ndugu zangu nataka niwaambie kitu kimoja kijijini kwetu uchawi umetawala, ni kweli anachosema mtoto kuwa ameona moto kwa vile ni mchawi.

    Huyu mtoto anatumiwa na bibi yake usiku katika kuwanga na ndiye dereva wa ungo. Naweza kumwona mtoto mdogo lakini usiku anafanya kazi kubwa ya kuwabeba magwiji wa kijiji hiki akiwemo bibi yake.

    "Kama mnabisha ngoja nimuulize, eti jana usiku mlikwenda wapi?"

    "Nigeria."

    "Kufanya nini?"

    "Bibi aliniambia kulikuwa na mkutano."

    "Nini kiliwapata?"

    "Tulipofika sehemu wanasema Kameruni, ungo ulianza kuyumba nilijitahidi kuuweka sawa lakini mmoja wetu alianguka."

    "Bibi yako alifanya nini?"

    "Alipata presha."

    "Yupo wapi?"

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Yupo ndani anaumwa."

    "Mmesikia?" Aliwauliza watu waliokuwa wameshika mdomo wasiamini kilichokuwa kikisimuliwa na yule mtoto.

    "Ndiyo," waliitikia wote.

    "Mmeona, sasa hebu jiangalieni wote," aliwaeleza watu waliokuwepo pale.

    Watu wote walitazamana bila kujua mganga alikusudia nini. Baada ya muda aliwauliza.

    "Jamani kuna mtu hakuvaa nguo hapa?"

    "Hapana wote tumevaa," walijibu kwa pamoja.

    "Basi nataka kuwaeleza hapa kuna watu zaidi ya kumi hawana nguo na wamekuja kujaribu ninachokifanya. Nataka kuwaeleza kuwa wanajisumbua zaidi ni kuumbuka, ndugu zangu hakuna faida ya uchawi zaidi ya kuishi maisha magumu huku ukiingilia kazi ya Mungu kuua na kutesa.

    "Watu wamefilisika kutokana na mchezo wa chuma ulete bila kujua wanawafanyia watu kazi. Nina imani baada ya tukio la leo nitahamishwa kijijini kwa vile wenye nguvu wameshasema, lakini nataka kuwaeleza nitakachokifanya leo wachawi wote wataanza upya kutumia nguvu za kichawi kwa vile nitaua nguvu zao zote.

    Kwa muda mfupi kila mtu ataona mabadiliko ya mwili wake kama hutolewa usiku na kugeuzwa farasi wa kubeba wachawi bila kujua. "Wagonjwa wenye maradhi yasiyoonekana yatapata ufumbuzi, wenye uzito kwenye kazi na biashara baada ya zoezi langu watashangaa mabadiliko yatakayotokea.

    "Kila mwenye tatizo la kichawi ataona mabadiliko ila mwenye tatizo la kudra ya Mungu aendelee kumuomba atapona. Nilisema kuna watu wapo uchi hawana nguo inawezekana mnaona natania, kwa hiyo mnataka kumuona?"

    "Ndiyooo!" Waliitikia wote.

    "Sasa nitamtoa mmoja mbele ambaye amekuja kunipima," baada ya kusema vile alitembeza macho kwenye kundi la watu na kusema:

    "Namuomba mwanamke mmoja mwenye kanga ili mtu akiumbuka awahi kumfunika ili kumsitiri."

    Mwanamke mmoja alitoka mbele na kanga mkononi, baada ya kupita alimwita bibi mmoja aliyekuwa amesimama pembeni mkono amekunja ngumi. Lakini yule bibi alikataa, mganga aliwatuma vijana kumleta mbele. Walimbeba juujuu na kumpeleka mbele.

    Baada ya kufikishwa yule bibi aliweka mkono mdomoni kama mwanamwali na kuangalia chini kama mtu mwenye aibu. Baada ya kufikishwa mganga alimuomba mwanamke mwingine afike mbele, alitoka mwanamke mwingine mbele.

    "Sasa ninataka kuwaonesha kitu mnamjua huyu bibi?

    "Hatumjui."

    "Huyu ni mgeni ila ameletwa kwa ajili ya kukabiliana na mimi ndiyo maana nikasema wapo zaidi ya kumi wote mtawajua."

    Baada ya kusema vile aliweka maji mdomoni na kumpulizia mwanamke aliyeitwa mara ya mwisho. Kisha aliwageukia watu na kuwauliza:

    "Mmeona nini?"

    "Hatujaona kitu."

    "Huyu mama amevaa hajavaa?"

    "Amevaa."

    "Mama simama hapo, bibi simama hapa."

    Yule bibi alisimama alipokuwa amesimama mwenzake kisha mganga alijaza maji kinywani na kumpulizia. Ghafla kukawa na sinema ya bure na kuwafanya watu wote wapige kelele baada ya yule bibi kubakia mtupu. Alimuomba mama aliyekuja na nguo amfunge kisha aliwageukia watu na kuwauliza.

    "Mmeona?"

    "Ndiyo."

    "Basi huyu ni mmoja wa wachawi waliopo hapa japokuwa wapo wengine wamevaa, tunakaa nao lakini ni viumbe wabaya ndugu zetu wanapotea kumbe wamegeuzwa misukule. Ndugu zetu wengine wanakufa katika mazingira tata kumbe wazazi wetu wanawatoa sadaka ya nyama kwa vile wanakula nyama za watu. Hii imefanya nyumba nyingi ziwe tupu kwa ajili ya tamaa ya wazazi.





    tupu kwa ajili ya tamaa ya wazazi.

    "Lakini leo nitafanya nilichokitangaza huu ni wakati wa kila mtu kuleta uchawi wake hapa, una hiyari ya kuleta au kutoleta wenye kiburi leo ndiyo siku yao ya kuumbuka hadharani."

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kauli ile iliwafanya watu watazamane kila mmoja akimhofia mwenzake huenda ni mchawi. Upande wa wachawi walikuwa na tumbo moto huku wakiamini wanaumbuka.



    "Leo nitakuwa na kazi moja ya kuua uchawi nyumba zote zenye uchawi pia kuua nguvu za watu wanaowatesa wenzao. Najua siwezi kumaliza ila wengi mtakutana nao wakiwa wamechanganyikiwa baada ya zoezi langu la usiku wa leo.

    "Nina imani kwa zoezi langu watu wengi mtaona mabadiliko makubwa ya miili yenu kwa vile wengi mmekuwa mkitumika katika kuwafanyia kazi watu kama kulima na kubeba mizigo. Miili yenu mmekuwa kama mmebeba vitu vizito bila kujua.

    "Pia sehemu zenu za biashara na kazi kuwa na nuru kutokana na kutiwa giza la kichawi. Nyumba zenu magonjwa hayaishi bila kujua wachawi kuna vitu wamechimbia mbele ya nyumba zenu.



    "Kazi nitakayoifanya itaua kila kitu, narudia kusema kuwa maisha yangu yapo hatarini, ila nasema hawaniwezi zaidi ya kuzidi kuwaumbua. Mpango wao mmoja tu ndiyo unaoweza kufanikiwa wa kunifukuza, naamini nikiondoka mtawajua wabaya wenu ni kina nani."



    "Namalizia kwa kumuomba Amangise na mkewe wapite mbele ili wamalize tofauti zao na jirani yao Andendekisye kwa vile kila mmoja alitumia kiburi cha nazi na matokeo yake mmepata hasara wote."

    Baada ya kusema vile Amangise na mkewe walipita mbele na kusimama, mganga alisema:

    "Mnajua sababu ya kukutana hapa ni kati ya ugomvi wa familia mbili ambazo umesababisha kupoteza watu wanne ambao wamekufa bila sababu kwa ubabe, familia ambazo walikuwa na ufumbuzi mwingine wa kutatua tatizo lao matokeo yao kukimbilia kurogana na kusababisha mauaji ya kutisha.



    "Si hawa wapo watu wengi hapa kijijini ndiyo tabia zao, jambo dogo tu anavuka mpaka kwenda Malawi kuchukua uchawi na kuja kumuumiza mwenzake wakati suluhu si nguvu bali busara. Wengine ukiwaona ni wacha Mungu wazuri kwenye nyumba za ibada, wapo mstari wa mbele lakini wakitoka hapo wanavaa roho zao za kikatili na kuwanga usiku kucha.



    "Kuna mtu simsemi ila kuanzia leo mtashangaa mashamba yake hayataendelea kulimwa kwa vile akiwatumia misukule wataonekana hana nguvu za kuwaficha tena. Na muda si mrefu watu mtawaona ndugu zenu ambao mlijua wamekufa na kuwazika lakini kumbe kilikuwa kiini macho watatoka katika nyumba walizofichwa kwa vile hakuna kizuizi cha kuwazuia tena.



    "Sitamtaja mtu aliyefanya vile kwa sababu nitakuwa nimetengeneza vita lazima ndugu zao, lazima watu watauana na mimi nitakamatwa na jeshi la polisi kwa vile serikali haiamini uchawi japo asilimia kubwa ya viongozi wake wanaongozwa na nguvu za giza.

    "Sasa nia yangu ni kuwaomba kuondoa tofauti zao kwa vile yaliyopita yamepita, Andendekisye kama ulivyoniahidi nataka uyatekeleze ukienda kinyume sitakuwepo. Amangise na mkewe hii ni fursa ya kudhihirisha kuwa mmesafisha mioyo yenu na kumrudia Mungu kwa kumsaheme jirani yenu.



    "Napenda kuwaeleza sisi ni waganga lakini mganga wa kweli ni Mungu. Mkiishi kwa kumtegemea Mungu itawasaidia kuishi kwa furaha. Yapo magonjwa ya kawaida ambayo sisi waganga huyatibu lakini si ya kurogana."

    Baada ya kusema vile Amangise na mkewe walisema wamejifunza kitu katika yaliyotokea na kusema wapo tayari kumsamehe Andendekisye kwa yote yaliyotokea. Naye Andendekisye huku akilia alisema ameona faida ya kumtegemea mwanadamu kuliko Mungu matokeo yake kampoteza mkewe na mwanaye.



    Wote walikubali kusameheana na kufanya watu wote washangilie, baada ya zoezi lile kwisha. Mganga alimgeukia mganga kutoka Malawi na kusema:

    "Ndugu yangu najua fani yetu ni kutibu watu ila umeigeuza na kuwa mchawi wa kuwaua watu na kuwatesa. Hili ulilokutana nalo ni funzo, nilitaka kukuacha uwe kipofu na usingepona sehemu yoyote unayojua kutokana kuwa mchawi na si mganga."

    "Nakuahidi nikiweza kuona sitarudia tena kufanya nilichokifanya," mganga alitoa ahadi nzito.

    "Umeua watu wangapi kwa mtindo huu?"

    "Ni wengi ndugu yangu."

    "Nakusaidia uone ukirudia macho yakifumba hayatafumbuka tena, wewe ni mganga tibu watu na si kuwaroga."

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nitafanya kwa kila utakaloniagiza."



    Mganga aliagiza maziwa mabichi yasiyochanganywa na kitu, aliweka dawa na kumpa mganga toka Malawi anawe. Alinawa na kuwashangaza watu kutoka vitu vyeusi kama udongo. Alipiga kelele za maumivu macho yaliuma zaidi ya mwanzo.

    "Jamani nakufa au ndiyo unanimaliza?"

    "Maumivu hayo ndiyo kupona kwako."



    Aliendelea kunawa mpaka maziwa aliyonawa yakawa yanatoka na rangi yake ileile. Baada ya kumaliza kunawa alipewa maziwa mengine bila dawa ambayo alinawa na kuambiwa afumbue macho.

    "Si..si..amini nimeona...nimeona..asante..asante," mganga toka Malawi alipiga magoti mbele ya mganga mwenzake.

    "Kaka nyanyuka mimi sina hadhi ya kupigiwa magoti bali muumba wako, nataka kukwambia kitu kimoja chagua kitu kimoja uwe mchawi uwaroge watu au uwe mganga uwatibu watu."

    "Nataka kuwa mganga."



    "Basi achana na uchawi, babu yako mzee Msioka alikuwa mganga mkubwa sana, aliwasaidia watu hakuua wala kutesa, mwenye kazi ya kutesa na kuua ni Mungu tu kwa nini uingilie kazi yake?"

    "Najua nimefanya makosa."



    "Sasa wote mtakuja kunywa maji kwenye ndoo hii, atakayefanya uchawi wowote hataomba maji atakufa papohapo au kuwa kichaa kisichopona. Naomba vijana wahakikishe kila mtu anakunywa maji haya."

    Zoezi lilianza kwa watu kunywa maji kidogokidogo, baada ya zoezi lile kwisha, mganga alipita nyumba baada ya nyumba huku akimwaga vitu.



    Baada ya zoezi lile alirudi nyumbani kwake na kuacha gumzo kila kona. Mganga kutoka Malawi aliondoka siku ileile kurudi kwao huku akiamini yeye si mganga bali wapo waganga zaidi yake.

    Hakuamini kijana mdogo kama yule kumuumbua lakini alimshukuru kwa huruma yake. Usiku wa siku ile baadhi ya wazee wenye imani ya kishirikina walioona wameumbuliwa walikodi vijana wa kijiji kile kumhamisha kinguvu yule mganga usiku uleule walihakikisha wanamtoa nje ya mji wa Kyela na kumwambia akirudi wanamuua. Zoezi lile lilifanyika kwa siri hakuna aliyejua huku nyuma nyumba yake ikatiwa moto.





    Andendekisye baada ya kuumbuliwa japokuwa alisamehe, bado aliona sehemu ile si salama tena kwake kwa kuamini kila mmoja atamnyooshea kidole kwa yote yaliyotokea.Aliuza kila kilicho chake na kuhama mji wa Kyela na kuhamia sehemu nyingine ambayo hakutaka mtu yeyote ajue amekwenda wapi. Huo ukawa mwanzo na mwisho wa habari zake.



    Lakini jirani yake Amangise yeye hakwenda popote, alibakia huku akiwa mwana kondoo aliyerudi zizini kwa kuokoka na mkewe. Lakini baada ya miaka miwili Amangise alifariki baada ya kupooza upande mmoja. Baada ya mazishi yaliyosimamiwa na kanisa, mke wa Amangise alichukuliwa na ndugu zake waliokuwa wakiishi sehemu iliyoitwa Ipinda.



    Siku zote katika maisha yake alihubiri watu wamtegemee Mungu na si mwanadamu, pia kutumia busara kwa jambo lolote zito kwa kumtanguliza Mungu mbele. Kutokana na busara zake za kiutu uzima, kila majirani walipogombana alitumiwa kusuluhisha kwa kutumia kisa chake cha kweli mpaka naye mauti yalipomchukua na kuacha ushuhuda huu unaomaliza kuusoma leo.



    Nashukuru wote tuliosafiri pamoja kwenye mkasa huu toka mwanzo mpaka mwisho, nina imani kuna kitu mmejifunza. Hakuna ategemewaye chini ya jua zaidi ya Mungu, hakuna amani kwa ncha ya upanga bali maelewano.



    Dunia nzima watu wengi wamepoteza maisha na wataendelea kupoteza maisha kwa kutumia ubabe kuliko mazungumzo.

    Muombe akupe busara na hekima na kumtanguliza yeye katika kila kitu hakika moyo wako siku zote utakuwa na amani. Siku zote

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    amtegemeaye mwanadamu amelaaniwa. Mganga hutibu anayeteswa na si kuua au kuchukia maendeleo ya mwenzako ni uchawi. Mpende jirani yako kama nafsi yako amani itatawala milele, zingatia na kufanyia kazi, asante. Kwa kuacha shughuli zenu kunifuatilia Hadithi hii ya ajabu.



    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog