IMEANDIKWA NA : HASHIM AZIZ
*********************************************************************************
Simulizi : Nilibadilika Na Kuwa Jini Bila Kujijua
Sehemu Ya Kwanza (1)
Kijana Gamutu Mwakatika ni mtoto wa kipekee kutoka kwenye ukoo wa kichifu wa Mzee Kapalala Mwakatika. Maisha yake yote amekulia Sumbawanga kwa bibi zake wa ukoo wa baba yake mzazi kabla ya kuhamia Bagamoyo, iliko asili ya mama yake.
Gamutu alilazimika kulelewa na bibi na babu yake baada ya kutokea matatizo ya kimila yaliyosababisha vifo vya kutatanisha vya wazazi wake vilivyohusisha imani kali za kishirikina akiwa bado mdogo.
Historia ya maisha yake inasisimua sana kwani anaelezea jinsi alivyowahi kubadilika kutoka kwenye ubinadamu wa kawaida na kuwa jini bila mwenyewe kujijua mpaka alipoanza kuambiwa na watu wake wa karibu kuhusu hali yake, kabla ya kukombolewa na ndugu wa ukoo wa mama yake walioamua kuuza mali zao zote na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji huko Bagamoyo, mkoani Pwani.
Licha ya umri wake mdogo wa miaka 17 tu, Gamutu amepitia mambo mengi ya kishirikina, mauzauza na uchawi wa kiwango cha juu, ambao hata akiusimulia ulimwengu ni wachache watakaoamini.
Kwa sasa anaishi maisha ya kawaida baada ya kukombolewa na mganga maarufu wa kienyeji huko Bagamoyo, ingawa bado analalamika kuwa kuna wakati huwa anatamani kurudi kwenye hali yake ya zamani ya kuwa jini.
Katika mfululizo huu, anaeleza kwa maneno yake mwenyewe namna alivyobadilika na kuwa jini, kisha alivyokombolewa na kuwa binadamu wa kawaida baada ya nguvu kubwa kutumika. Ungana na mwandishi wako Hashim Aziz aliyezungumza na kijana Gamutu Mwakatika wakati anasimulia historia ya maisha yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni Jumatatu ya kwanza ya mwezi Januari, miaka kadhaa iliyopita nilipoanza kutokewa na hali ambayo mwanzoni sikuielewa, lakini baadaye nikaja kuambiwa maana yake na babu mzaa baba.
Sitaisahau siku hii kwa sababu iliyafanya maisha yangu yabadilike kabisa. Nianze kwa kueleza kuwa kipindi hicho nilikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, katika shule ya msingi Tindiga, iliyopo Sumbawanga vijijini nilikokulia.
Kutokana na hali ngumu ya maisha ya kijijini, mimi pamoja na watoto wengine wa kijijini kwetu tulikuwa tukitembea umbali mrefu kuelekea shuleni, miguuni tukiwa pekupeku huku miili yetu ikiwa imesitiriwa na nguo chakavu.
Siku hiyo asubuhi, nikiwa nimeongozana na watoto wenzangu tukielekea shuleni, niligongwa mguuni na kitu ambacho sikufanikiwa kukiona kwa macho zaidi ya kuhisi maumivu makali sehemu kitu hicho kiliponigonga.
Sikuwaambia wenzangu tunaosoma nao kwani kwa mazingira ya kijijini, kuumia ni jambo la kawaida. Nilijikaza bila kuonesha dalili yoyote mbaya, na safari ikaendelea mpaka shuleni. Tulipofika shuleni, tuliingia darasani kwa kuibia maana tulikuwa tumechelewa sana.
Baada ya mimi kukaa darasani, nilianza kusikia sauti kama za watu wakiniongelesha masikioni, lakini kila nilipogeuka sikumuona mtu zaidi ya wanafunzi wenzangu ambao tulikuwa wote darasani.
Mwalimu alipoingia darasani na kuanza kufundisha, zile kelele nilizokuwa nazisikia zilizidi kuongezeka mara dufu, mpaka kichwa kikawa kinaniuma. Nikawa nashtuka mara kwa mara, hali iliyofanya hadi baadhi ya wenzangu niliokaa nao jirani kuanza kunitazama mara mbilimbili.
Sikuwa na ujanja zaidi ya kuomba ruhusa kwa mwalimu nikidanganya kuwa naumwa tumbo. Nilitoka na kuzunguka nje ya darasa, nikaenda kukaa chini ya mti wa mparachichi uliokuwa nyuma ya madarasa yetu.
Nilipokaa nilihisi kama hali yangu ndiyo inazidi kuwa mbaya kwani zile kelele zilikuwa zikizidi kuongezeka. Niliamua kujikaza na kuinuka, nikaanza kuhesabu hatua kuelekea nyumbani kwetu. Nifafanue kuwa kwa kipindi hicho nilikuwa bado naishi na bibi yangu mzaa baba, Bi Lubunga ambaye alikuwa akinipenda na kunijali sana.
Wakati nikiondoka kuelekea nyumbani, nikiwa nimefika umbali wa kama mita mia moja kutoka eneo la shule, wingu zito lilianza kutanda angani na kusababisha hali ya kigiza japokuwa ilikuwa ni mchana. Bibi Lubunga alishawahi kuniambia kuwa nionapo hali kama hiyo, nijue kuwa kuna mvua kubwa yenye madhara inakuja, hivyo niharakishe kurudi nyumbani.
Nilipoona hali hiyo niliongeza kasi, nikawa natembea kwa kujivuta kwani pale nilipogongwa na kitu nisichokijua mguuni mwangu, palianza kunisababishia maumivu makali kupita kiasi. Nilianza kuhisi mguu wote unavuta kutokana na maumivu, lakini sikujali! Nikawa nazidi kuongeza mwendo. Wingu lilikuwa likizidi kutanda kuashiria mvua kubwa.
Nikiwa nimefika mbali kabisa na shule, nikiwa nakatisha vichakani kufuata njia ndogo ya miguu iliyokuwa inaelekea nyumbani kwa bibi, nilishangaa kuanza kusikia upya sauti kama zile nilizokuwa nazisikia darasani baada ya kugongwa na kitu mguuni. Safari hii sauti hizi nilizisikia karibu kabisa na masikio yangu, zilikuwa kali kiasi cha kunifanya nizibe masikio kwa kutumia mikono yangu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipotazama angani, niliona wingu jeusi likizidi kujikusanya usawa wa pale nilipokuwepo. Nilikuwa bado sijafika nyumbani, lakini pia nilikuwa nimeshafika mbali na shuleni. Mbele kulikuwa mbali na nyuma kulikuwa mbali. Mara manyunyu yakaanza kudondoka na kunilowanisha mwili mzima. Sikuwa na ujanja zaidi ya kutafuta mahali pa kujisitiri.
Wakati manyunyu yakizidi kudondoka, nilihisi mguu ukizidi kuniuma, ikabidi niutazame vizuri kwani sijui kwa nini tangu niumie asubuhi, sikujiangalia vizuri sehemu niliyogongwa.
Sijui ni kwa sababu nimezoea kuumia mara kwa mara au usugu wa ngozi yangu, lakini sikujishughulisha kabisa kujitazama vizuri. Nikaona niutumie vizuri muda huo kujiangalia. Nilikaa chini ya mti mkubwa wenye matawi mapana yaliyokuwa yanazuia manyunyu ya mvua kuniloanisha.
Nilipokaa, niliuinua mguu wangu na kuusogeza karibu na macho yangu, nikaanza kujitazama kwa umakini. Japokuwa wingu zito la mvua lilisababisha kigiza, niliweza kujiona vizuri na kwa hakika sikuamini kile nilichokiona. Kumbe maumivu yote na taabu niliyokuwa napata, ilikuwa ni kwa sababu ya kugongwa na nyoka! Hakika sikuamini.
Meno mawili yalikuwa yamejikita kisawasawa kwenye ngozi ya mguu wangu, na damu nyeusi ilikuwa ikitiririka huku ikisafishwa na manyunyu ya mvua.
“Mungu wangu! Kumbe nimeng’atwa na nyoka, nimekwisha!” Nilijisemea pale chini ya mti nilipokuwa nimekaa huku mwili wote ukianza kunitetemeka.
Niweke wazi kuwa kule Sumbawanga kulikuwa na mauzauza mengi sana ya binadamu kuwatumia wanyama kama simba, chui, fisi, nyoka wenye sumu na hata wakati mwingine mvua yenye radi kali kwa ajili ya kuwadhuru wabaya wao.
Ilikuwa ni nadra sana kukutana na mnyama aliyetumwa, akakuuma au kukudhuru kwa namna yoyote halafu ukasalimika na kuendelea kuishi. Wote waliowahi kukutana na matukio kama hayo, walikufa siku chache baadae. Nilianza kusali kimoyomoyo ili yule nyoka aliyenigonga asiwe ni wa kutumwa, kibaya zaidi ni kwamba sikufanikiwa hata kumuona.
Manyunyu yalizidi kuongezeka na sasa mvua ikawa imekolea. Nilizidi kujificha pale chini ya mti. Mara radi kali zilizoambatana na ngurumo za kutisha zikaanza kupiga mfululizo. Bibi Lubunga alishawahi kuniambia kuwa nikiona kuna mvua ya radi, nisikae chini ya miti mikubwa kwani huwa kiunzi kizuri cha kupitisha radi kutoka angani hadi ardhini.
Mambo mawili yakawa yananielemea kwa wakati mmoja, kuwahi kujifunga kamba mguuni ili sumu ya nyoka aliyening’ata isizidi kusambaa mwilini japokuwa nilishachelewa sana, na pili kuondoka chini ya mti ule kukwepa radi.
Nikiwa bado nahangaika, nilisikia sauti ya mtu kutoka kwenye ule mti ikiniita kwa kutaja jina langu. Wakati nataka kugeuka ili nitazame sauti ile ilikotokea, nilishangaa nikimulikwa na mwanga mkali wa radi, nikashuhudia ule mti ukichanwachanwa vipande… japokuwa ulikuwa mkubwa sana, niliuona ukipasukasuka na kuwa kama kuni.
Kufumba na kufumbua mwanga mwingine, mkali kuliko ule wa kwanza ulimulika tena…nikatambua kuwa radi ile ilikuwa imenipata kisawasawa. Nikajikuta mwili na roho vikianza kutengana. Nikadondoka chini na kupoteza fahamu. Sikujua kilichoendelea.
Baada ya radi kali kupiga pale chini ya mti alipokuwa amejisitiri mvua, Gamutu alipoteza fahamu. Hakuelewa chochote kilichoendelea mpaka alipokuja kushtuka na kujikuta akiwa ndani ya pango linalofanana na nyumba.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pembeni yake kulikuwa na wanawake wawili ambao kiumri walionekana kuwa wazee sana. Alipotazama vizuri alimuona bibi yake akiwa ameambatana na wale wanawake wawili, wakawa watatu.
Gamutu alibaki kushangaa amefikaje mahali pale, na nini kilichoendelea baada ya mwanga mkali wa radi kummulika.
Niliwatazama vizuri wale waliokuwa wamenizunguka, nilimtambua bibi Lubunga akiwa na wanawake wenzake wawili, ambao kiumri walikuwa wanakaribiana. Japokuwa kulikuwa na mwanga hafifu wa kibatari, niliweza kuona kila kilichokuwa kinaendelea mle ndani.
“Bibi hapa ni wapi?” Nilimuuliza bibi yangu huku nikikitazama vizuri kitanda cha ngozi na kamba nilichokuwa nimelazwa juu yake.
Badala ya kunijibu, bibi alinisogelea na kunigusa kichwani, kisha akawa anatikisa kichwa chake kwa masikito makubwa.
“Pole mjukuu wangu Gamutu,” aliongea bibi kwa Kiswahili kibovu. Niweke wazi kuwa lugha ya mawasiliano tuliyokuwa tunaitumia kule kijijini kwetu ilikuwa ni Kifipa. Watu karibu wote walizungumza Kifipa na hata tukiwa shuleni tulikuwa tukiwasiliana kwa lugha hiyo isipokuwa mwalimu anapokuwepo tulilazimishwa kuongea Kiswahili.
Alinieleza kuwa nilikuwa kwenye vita kali, na akanipongeza kuwa kama isingekuwa uanaume wangu, basi siku ile ndiyo ingekuwa ya mwisho mimi kuishi hapa duniani. Sikuelewa maana ya kauli ile. Akazidi kunifafanulia kuwa nilizaliwa nikiwa na nguvu za kipekee ambazo ndizo zilizoniwezesha kusalimika siku ile. Bado sikumuelewa.
Nilipozidi kutazama huku na kule ndani ya pango lile tulimokuwemo, nilibaini kwamba kumbe nilikuwa nyumbani kwa waganga wa kienyeji. Hiyo ilitokana na mafuvu mengi ya wanyama, ngozi zao pamoja na tunguri zilizokuwa zimetundikwa karibu kila kona ya pango lile ambalo hata nikisema ni nyumba nitakuwa sikosei.
Nilipogeuka upande wa pili kwa taabu, niliwaona wale wanawake wawili wakiandaa dawa kwa kuisaga kwenye mawe makubwa yaliyokuwa kwenye kona moja ya ile nyumba. Mwingine akawa anatingisha kibuyu kikubwa ambacho sikujua ndani yake kulikuwa na nini.
Walipomaliza, walianza kuninyunyizia dawa mwili mzima huku wakitamka maneno ambayo sikuyaelewa. Kwa taabu niliinua mguu wangu ambao niling’atwa na nyoka wakati naenda shuleni, nikaona nimefungwa kitambaa cheusi kilichochanganywa na dawa.
Wakati wale wengine wakiendelea kunifanyia dawa, bibi alikuwa ameketi pembeni yangu akinikanda kichwani na maji ya uvuguvugu.
“Bibi niling’atwa na nyoka asubuhi,” nilianza kumueleza bibi kwa sauti iliyokosa matumaini.
“Hakuwa nyoka, ulikuwa ni uchawi uliotegwa barabarani ili kukudhuru.
“Lakini pia nilipigwa na radi wakati narudi shuleni,” nilizidi kumhoji bibi.
“Haikuwa radi halisi, kuna maadui zangu wengi wanaonitafuta, lakini baada ya kunishindwa ndiyo wameamua kujaribu kukuua wewe mjukuu wangu kwa kuwa wametambua kuwa wewe ndiye kipenzi changu.”
“Kwani kulitokea nini? Mbona sikumbuki kitu?”
“Pale wakati umekaa chini ya mti ulipokuwa unarudi kutoka shuleni, ulikuwa umejiingiza kwenye mtego hatari. Mimi nilikuwa shambani kuangalia mbaazi zangu, ghafla machale yakanicheza kuhusu usalama wako, nilipoamua kukutafuta kwa njia ninayoijua nilikuona ukiwa umekaa kwenye mtego bila mwenyewe kujijua.
“Muda huohuo radi ilikuwa imetegwa kichwani kwako tayari kukumaliza. Nilipokuita kwa sauti kubwa uligeuka na kuangalia juu ya mti sauti yangu ilikokuwa inatokea, kwa kufanya hivyo ukawa umeikwepa radi bila mwenyewe kujijua, bila hivyo tayari ungekuwa maiti saa hizi.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Habari ile aliyonieleza bibi ilinishtua na kunisisimua sana. Japokuwa nilikuwa na maumivu makali mwili mzima, nilijikuta nikisisimka sana.
Nilizidi kumhoji bibi huku wale wanawake wengine wakizidi kunifanyia dawa mwili mzima. Mmoja kati yao ambaye ndiye aliyeonekana kuwa mkubwa, alimkataza bibi kuendelea kuniongelesha kwa madai kuwa nilikuwa namaliza nguvu ya dawa.
Ikabidi ninyamaze. Baada ya kumaliza kunifanyia mambo yao ambayo sikuyaelewa yanaamnisha nini, walitoka nje na kuniacha na bibi Lubunga.
“Bibi niambie ukweli, hivi mtu akipigwa na radi anapona kweli? Mbona mimi sijafa?”
“Wewe ulitaka ufe? Hukupigwa na radi Gamutu, bali mti uliokuwa umekaa chini yako ndiyo uliopigwa, wewe ulizimia kwa sababu ya hofu, lakini uko salama kwa sababu nilikuwepo eneo lile kukulinda.”
“Sasa hapa tuko wapi na tunafanya nini?”
“Yule nyoka aliyekung’ata alikuwa na sumu kali ya kichawi ambayo kama tusingewahi kukuleta hapa, ungekufa na kugeuzwa msukule.”
Bibi alinielekeza kuwa baada ya kupatwa na masaibu yale, alifika kwa haraka na kunitoa eneo la tukio ndipo aliponileta nyumbani kwa yule bibi mganga ili anitibu. Kila alichokuwa ananieleza bibi kilikuwa kama mauzauza kwangu. Nilikuwa sielewe aliwezaje kufanya yote yale bila ya mimi kutambua uwepo wake.
Niweke wazi kwamba pale kijijini kwetu kulikuwa na wazee wengi ambao nilikuwa nikisikia watu wakisema kuwa ni wachawi sana, na hutafuta sababu ya kumroga yeyote wanayemtamani, hata bila hatia.
Niliwasikia pia wakisema kuwa bibi yangu ndiyo kiboko yao. Sikupata nafasi ya kuelewa kauli ile ilikuwa na maana gani. Mara kwa mara nilikuwa nikishuhudia watu wanaokumbwa na matukio ya kutisha ya uchawi, huku wengi wao wakiishia kufa.
“Kutokana na yaliyokusibu, mganga amesema ni bora akufanyie zindiko la maisha,” aliniambia bibi Lubunga huku akiwa ameniinamia pale nilipokuwa nimelazwa.
Usiku ule ulikuwa mrefu sana kwangu. Kila kiungo cha mwili wangu kilikuwa kikiniuma. Kumbukumbu za matukio ya kutisha ya kung’atwa na nyoka bila mwenyewe kujijua na mwisho kunusurika kuuawa kwa kupigwa na radi, yalikuwa yakijirudia kichwani mwangu kama mkanda wa kutisha wa filamu za kichawi. Sikupata hata tone la usingizi.
***
Baadaye wale wanawake wawili walirudi, wakaongea mambo fulani na bibi ambayo mimi sikuyaelewa. Ilikuwa tayari usiku wa manane. Bibi Lubunga aliniamsha kutoka pale kwenye kitanda kile cha ngozi na kamba za miti, akanishika mkono na kunitoa nje. Bado sikuwa na nguvu za kuweza kutembea mwenyewe, bibi akawa msaada wangu.
Tulipotoka nje ya lile pango, wale wanawake wawili walitangulia mbele na tukaanza kuwafuata nyuma. Yule wa mbele alikuwa amebeba chungu kinachowaka moto ambacho kilitumika kama mwanga wa kutumulikia taa.
Baada ya kutembea kwa kitambo kirefu huku tukiloanishwa na umande mwingi uliokuwa umetanda kwenye njia tulizokuwa tunapita, tulitokezea makaburini.
Nilijikuta moyo ukinilipuka paah! Sikuwahi kufika makaburini nyakati za usiku wa manane kama ule, na yule bibi aliyekuwa mbele alituongoza mpaka kwenye kaburi moja lililokuwa wazi. Tukalizunguka mara saba huku wakiimba nyimbo ambazo sikuzielewa, kisha mmoja wao akatoa amri.
“Ingia ndani ya hili kaburi!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kufanya nini?” Nilihoji kwa wasiwasi mkubwa huku nikitetemeka. Bibi aliniambia kuwa nisibishane na mganga kwani tutaua nguvu ya dawa, ikabidi nitii wito. Nilipoingia tu, nikasikia kitu kama tetemeko kubwa likitokea, kuta za lile kaburi zikaanza kumomonyoka na kunifuka, hali iliyonifanya nipige yowe kuu lakuomba msaada. Nilishangaa kuona sauti haitoki.
Nilipokuja kushtuka, nilijikuta nikiwa bado kulekule makaburini, ila nilikuwa nimelala juu ya kaburi lingine, tofauti na lile nililokuwa nimefukiwa usiku huo.
Nilijaribu kukumbuka hali ilivyokuwa, kumbukumbu zangu zikawa zinaishia mahali ambapo upepo mkubwa ulikuwa ukifukua kaburi nililokuwa nimefukiwa ndani yake.
Nilimkumbuka yule fisi wa ajabu aliyekuja na kimbunga pale kaburini na yote aliyoyafanya.
Sikuelewa maana ya yale yote yaliyotokea, nikajiapiza kuwa nikiondoka salama eneo lile, nitamkazania bibi anieleze maana ya kila kitu kilichonitokea.
Nikiwa bado nimelala pale juu ya kaburi, nilisikia maumivu makali ya kichwa, nikapeleka mikono kichwani na kujishika. Nilijikuta nikipigwa na butwaa baada ya kugundua kuwa nywele zangu zote
zilikuwa zimenyolewa. Sikukumbuka nani kaninyoa na kwa muda gani… nikahisi labda kitendo hicho kilifanyika wakati nikiwa nimepoteza fahamu. Lakini ni nani aliyefanya kitendo kile wakati niliachwa peke yangu kule makaburini? Sikuwa na jibu la haraka. Huo ukawa ni muujiza mwingine kwangu.
Nikiwa bado nimelala palepale chini, niliwaona bibi Lubunga na wale waganga wawili wakija, huku wakiwa wamejitwisha kitu ambacho nilikitambua kuwa ni jeneza jeusi, mikononi mwao kila mmoja alikuwa ameshika mshumaa…wakawa wanakuja huku vichwa vyao wakiwa wameviinamisha na kujitanda mashuka meusi kama watu walioko msibani.
Walikuwa wakija kwa hatua za taratibu huku wakiimba wimbo kama wa maombolezo. Nikakaa mkao wa kutaka kuona kitakachotokea.
Niliwaona wakija moja kwa moja mpaka juu ya kaburi lile nililokuwa nimelala juu yake, wakanizunguka mara tatu huku wakiendelea kuimba, kisha bibi mganga mmoja akapiga magoti upande wa kichwa changu, akanishika kwa mikono miwili na kunipapasa.
Wakati anafanya hivyo aliwageukia Bibi Lubunga na yule mganga mwingine, akawaambia jambo kwa ishara, kisha nikashangaa wakibadilisha wimbo waliokuwa wanauimba na kuanza kupiga vigelegele.
Niweke wazi kuwa kwa muda wote huo, sikuwa na uwezo wa kunyanyuka kutoka pale nilipokuwa nimelala kwani mwili haukuwa na nguvu hata kidogo.
Kitu pekee nilichoweza kukifanya ilikuwa ni kugeuza shingo na kuangalia huku na kule.
Sauti bado ilikuwa haitoki kama ilivyokuwa tangu awali, nikawa mtazamaji tu.
Wakati wakiendelea kupiga vigelegele, waliliweka lile jeneza pembeni, wakaniinua na kuniingiza ndani yake, kisha wakalifunika. Kwa kuwa halikuwa na tundu hata moja,
nilijikuta nikishindwa kupumua vizuri, nikawa natamani niwaambie lakini sauti haikutoka. Nikawa nagongagonga mbao za jeneza lile kwa ndani.
Walipoona nasumbua, yule bibi mganga alitoa kichupa kidogo chenye dawa nyeusi, akamimina kidogo kiganjani na kunipulizia usoni, nikajikuta nikilegea na fahamu zikawa kama zinanitoka ingawa bado niliweza kusikia, kuona na kutambua baadhi ya vitu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walinifunika na kitambaa cheupe ambacho nahisi ilikuwa ni sanda. Wakanibeba kwenye jeneza lile na safari ya kurudi kule kwa waganga ikaanza.
Sikuwa naelewa chochote kwa kuwa nilikuwa nimefunikwa kabisa na jeneza, kitu pekee nilichoweza kukisikia ni sauti za bibi Lubunga na wenzake ambao walikuwa wakiendelea kuimba huku wakipokezana kubeba jeneza nililokuwa ndani yake.
Tulipofika, walinitoa ndani ya jeneza na kunivua sanda, kisha wakanikalisha kwenye kiti cha miguu mitatu na kuanza kuniogesha na maji yaliyokuwa yananukia.
Walipomaliza walinifunga shuka jeusi, bibi Lubunga akanishika mkono na kunirudisha kule ndani ambako awali nilikuwa nimelazwa.
Safari hii sikulala tena, nikakaa kwenye kile kitanda cha kamba, wakaanza kunichanja chale ndogondogo sehemu mbalimbali za mwili wangu na kunipaka dawa iliyokuwa inauma sana.
Walipomaliza, nilishangaa kuona sauti yangu ikitoka kama kawaida.
Nikaita…Bibi! Bibi!...wote watatu walishangilia kwa sauti ya juu huku wakipiga vigelegele, wakaniambia kuwa huo ndiyo mwisho wa tambiko lile la maisha.
Ilikuwa ni tayari alfajiri japokuwa bado kulikuwa na giza, wakawa wananipongeza huku wakiniambia kuwa japokuwa umri wangu bado ni mdogo, mimi ni mwanaume wa shoka. Bado nilikuwa na maswali mengi kichwani ambayo sikupata majibu.
Baada ya kumaliza shughuli ile nzito, bibi aliniambia kuwa tunatakiwa kuanza safari ya kurudi nyumbani alfajiri ile ile. Tukawaaga wale waganga huku wakiniambia kuwa masharti yote ya zindiko lile walishamwambia bibi, hivyo tukifika nyumbani atanielekeza.
Mimi sikuona sababu ya kuwashukuru kwa sababu bado akili yangu ilikuwa haielewi kitu kutokana na mambo mengi na ya kutisha niliyokumbana nayo ndani ya muda mfupi sana.
Walinifungashia dawa nyingi ambazo walimpa bibi anibebee na wakampa maelekezo yote muhimu.
Tulipomaliza kila kitu, walituzungusha nyuma ya lile pango walilokuwa wanaishi, tukasimama juu ya kitu kama ungo mdogo, bibi akawa amebeba dawa alizopewa kwa ajili yangu huku akiwa amenishika mikono yote miwili.
“Fumba macho!” bibi aliniambia. Sikuwa mbishi. Lakini kabla sijafumba macho, niliwaona wale waganga wakitupungia mikono kwa ishara ya kwa heri. Nikaangalia huku na kule lakini hakukuwa na njia ya kuondokea mahali pale tulipokuwepo.
Sikutaka kuhoji wala kuleta ubishi, nikafumba macho. Bibi akazungumza maneno fulani kwa lugha ambayo sikuielewa, kisha akanielekeza kuwa nisifumbue macho mpaka atakaponiambia. Nilifuata maelezo yale.
Aliponiambia nifumbue macho, nilishangaa kupita kiasi baada ya kujiona tayari tumefika nyumbani.
Nilishtukia tukiwa pembeni ya nyumba ya bibi, nikawa najihisi kama niko ndotoni. Lile giza la alfajiri lilianza kupungua na sasa nuru ikaanza kulipendezesha anga.
“Hongera!” Bibi aliniambia huku akinipa mkono wa pongezi. Nikamhoji sababu ya kunipa pongezi, akaniambia kuwa nimeonesha uwezo mkubwa sana wakati nafanyiwa tambiko hadi wale waganga wamenivulia kofia.
“Wameniambia kuwa tangu waanze kazi, hawajawahi kukutana na mtu mwenye karama ya kipekee kama wewe.
Wameniambia kuwa kama utapenda kwenda kujifunza uganga kwao milango iko wazi.”
Bibi aliniambia huku akiwa na furaha kubwa moyoni mwake.
Aliniambia kuwa kuanzia muda huo, nitakuwa na uwezo wa kutambua mazingira ya hatari zozote zitakazokuwa zinanikabili kwa kutumia nguvu za machale.
Akanieleza kuwa kila jambo baya litakapokuwa linanikaribia, nitakuwa nasikia sauti kutoka ndani ya nafsi yangu itakayokuwa inanielekeza nini cha kufanya.
Akanitahadharisha kuwa sitakiwi kupuuza chochote nitakachokisikia kutoka ndani ya nafsi, hata kama ni kibaya.
Baada ya kijana Gamutu kufanyiwa tambiko la maisha lililojaa matukio ya kutisha yanayohusisha imani kali za kishirikina, hatimaye anaruhusiwa kurudi nyumbani huku akielekezwa kuwa endapo atahitaji kuendelea kujifunza mambo ya uganga, milango iko wazi kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wanapofika nyumbani kwa bibi yake, anakuwa ni kama aliyezaliwa upya. Anaanza kwa kumhoji maswali mengi bibi yake akitaka ufafanuzi juu ya kile alichokuwa anafanyiwa. Bibi Lubunga anamueleza kama alivyoelezwa na wale waganga, kwamba atakuwa na uwezo mkubwa wa kujikinga dhidi ya hatari zote za maisha.
“Bibi nataka kujua ukweli juu ya jambo moja ambalo linanitatiza sana.”
“Jambo gani mjukuu wangu?”
“Wakati niko kule makaburini mlikokuwa mneniacha, nani alikuja kuninyoa nywele zangu? Na kwanini alininyoa?”
Badala ya kujibu swali nililomuuliza, alianza kunipa maelekezo marefu juu ya namna nywele zinavyoweza kutumika kwenye shughuli za uganga.
Alinieleza kuwa hata wanasayansi huwa wanatumia nywele kupima mabaki ya mwili uliookotwa ili kubaini alikuwa ni mtu wa aina gani.
“Nywele, kucha na mifupa ndiyo utambulisho wako wa mwisho hata mwili huu unaouona utakapopotea.”
“Lakini hujanijibu swali langu bibi.”
“Ulinyolewa na mkuu wa matambiko na lengo lilikuwa ni kuweka kumbukumbu zako katika himaya ya nguvu za giza. Vinasaba vyako vimehifadhiwa na sasa una uwezo wa kutumia nguvu ulizojaaliwa kwa manufaa yako mwenyewe.”
“Kwa hiyo nywele zangu zimepelekwa kwa wachawi?”
“Siyo wachawi mjukuu wangu, lazima ujue kutofautisha wachawi na waganga.”
“Kwani tofauti ni nini?”
“Waganga wanatibu, kukinga na kuponya watu, wachawi wanadhuru, kuonea na kuua watu psipo hatia.”
Alizidi kunieleza kuwa kuna waganga ambao huzaliwa wakiwa na karama ya uganga bila kujifunza mahali popote na kuna wale wanaorithishwa mikoba ya uganga au wanaofundishwa kwenye madarasa maalum.
“Wale waganga wameniambia kuwa wamegundua kuwa wewe ni miongoni mwa watu wachache hapa duniani waliozaliwa wakiwa na karama ya uganga.”
“Mimi sitaki kuwa mganga, nataka kusoma mpaka chuo kikuu ili nije kuwa mwanasheria.”
“Yote yanawezekana, ila hiyo karama ya uganga lazima uitumie vinginevyo itakutesa sana maishani.
“Ukiongezeka umri kidogo nitakusimamia kuhakikisha unaitumia karama yako vizuri ili isikusababishie madhara.”
***
Saa moja asubuhi, Gamutu alikuwa ameongozana na wenzake kuelekea shuleni. Kama kawaida yao, walikuwa wakitembea pekupeku wakikatiza vichaka na mapori mpaka walipofika shuleni.
Tangu wakiwa njiani, wanafunzi wenzake walikuwa wakimtania Gamutu kwa jinsi alivyonyolewa nywele kichwani, huku sura yake ikibadilika na kuwa nyeusi sana.”
“Cheki Gamutu walivyompunyua nywele kichwani, yaani amekuwa mbaya! Mtazame…”
“Wamemnyolea kipande cha chupa au wembe butu, ndiyo maana hakuja shuleni.”
“Halafu mbona amekuwa mweusi sana usoni na mwilini, yaani kabadilika sana aisee,” wanafunzi wenzake walikuwa wakimsema Gamutu huku wengine wakimdhihaki na kumtusi. Hakujibu kitu bali alinyamaza kimya, akawa anawaza yake. Waliendelea kumsumbua kwa muda mrefu, lakini bado hakuwajibu kitu.
“Mi sitaki utani na mtu, mbona mimi huwa siwatanii?” alijitetea Gamutu lakini hakuna aliyemjali, wakaendelea kumchezea.
Walipoendelea kumtania sana, Gamutu alikasirika na kwenda kuwasemea kwa mwalimu wao wa darasa. Alipoingia kwenye ofisi ya walimu, kila mmoja alibaki kumshangaa.
“Mbona umebadilika namna hiyo wewe Gamutu, umepatwa na nini?”
Baada ya kusikia hata walimu wake wakimshangaa jinsi alivyokuwa, Gamutu alianza kuamini kuwa ni kweli amebadilika ghafla.
Akadanganya kuwa alikuwa anaumwa sana. Mwalimu wake alimpa msaada wa kuongozana naye hadi darasani ambapo aliwaadhibu wanafunzi waliokuwa wanamchezea na kutoa onyo kuwa wasijaribu tena kumchezea kwani mwenzao alikuwa mgonjwa.
Muda mfupi baada ya mwalimu kuondoka, wanafunzi waliendelea kumchezea Gamutu. Akapandwa na hasira na kuamua kulipiza kisasi.
Alimvamia yule mwanafunzi aliyekuwa anawaongoza wenzake kumtania na kumuangusha chini, akamng’ata shingoni na kuzamisha meno yake makali hadi ndani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kelele alizopiga mwanafunzi yule kutokana na maumivu, ziliwafanya wengine waanze kukimbilia nje ya darasa.Baadaye mwalimu wao alikuja tena na kuwatuliza, lakini yule mmoja akashindwa kuendelea kukaa darasani kwani pale alipong’atwa na Gamutu palikuwa pakivuja damu nyingi.
“Nilishawakataza msimchezee mwenzenu, ona sasa yaliyokupata,” aliongea mwalimu wao huku akihangaika kumpa huduma ya kwanza.
Baada ya kumtoa nje, wanafunzi wengine waliingia darasani na utulivu ukarudi kama awali. Hakuna aliyemtania tena Gamutu. Yule mwanafunzi akarudishwa nyumbani kwao.
Masomo yaliendelea mpaka majira ya mchana ambapo kengere ya dharula iligongwa na wanafunzi wote kwenda mstarini kusikiliza walichoitiwa. Mwalimu wao aliwapa taarifa kuwa wametembelewa na wageni kutoka shirika la msalaba mwekundu ambao walikuja kwa lengo la kuwaomba wanafunzi kuchangia damu.
“Tone moja la damu linaweza kuokoa uhai wa mtu, jitoleeni damu ndugu wanafunzi ili muokoe maisha ya wenzenu walioalazwa mahospitalini,” Mkuu wa msafara ule wa msalaba mwekundu alikuwa akiwahimiza wanafunzi kuchangia damu kwa hiyari. Aliwapa maelekezo kuwa wanaoruhusiwa kuchangia damu ni wale wenye umri wa miaka 18 na kuendelea tu.
Wanafunzi wengi walijitokeza kuchangia damu hasa ukizingatia kuwa wengi walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 18. Gamutu naye alijitokeza kutaka kuchangia damu lakini mwalimu wake akamzuia.
“Gamutu wewe si jana tu umesema ulikuwa unaumwa, halafu umri wako bado haujafikia miaka 18, huwezi kuchangia damu, wapishe wenzako.”
Kauli ile haikumfurahisha Gamutu, akaondoka na kwenda kukaa peke yake nyuma ya darasa. Wale wanafunzi wengine wakaingizwa kwenye chumba maalum na zoezi la kuwatoa damu likaanza.
Akiwa nyuma ya darasa, Gamutu alisikia harufu ambayo ilimfanya ainuke kutoka pale alipokuwa amekaa na kuanza kuifuata harufu ile. Hakujua ni harufu ya nini lakini alijikuta akiipenda, akataka kujua inatokea wapi.
Baada ya kufuatilia, aligundua kuwa inatoka ndani ya chumba ambacho waliingia wale wanafunzi waliokubali kujitolea damu kwa hiyari.
Aliifananisha na harufu ya maji aliyoogeshwa kule kwa waganga wa kienyeji alikopelekwa na bibi yake. Akasogea mpaka dirishani na kuanza kuchungulia ndani.
Alishangaa kuona wanafunzi wenzake wakiwa wamelazwa kwenye vitanda maalum huku mirija ya rangi nyekundu ikiwa imeunganishwa kwenye miili yao na chupa maalum.
Alipotazama vizuri, aligundua kuwa kumbe walikuwa wakitolewa damu ambayo ilikuwa inakusanywa na kuwekwa kwenye chupa kubwa zilizokuwa mle ndani. Alitazama huku na kule bila ya mtu yeyote kumshtukia lakini hakuona kitu kingine zaidi ya vile, akabaki kujiuliza ile harufu inatokea wapi bila kupata majibu.
Alichohisi ilikuwa huenda ile ni harufu ya damu ingawa hakuwa na uhakika. Alijishangaa kwa nini avutiwe na harufu ya damu badala ya harufu nzuri kama za maua au manukato.
Alichohisi ilikuwa huenda ile ni harufu ya damu ingawa hakuwa na uhakika. Alijishangaa kwa nini avutiwe na harufu ya damu badala ya harufu nzuri kama za maua au manukato. Alipojaribu kukumbuka zaidi, aligundua kuwa harufu ile ilikuwa sawa kabisa na harufu ya maji aliyoogeshwa na waganga wakati akifanyiwa tambiko.
“Ina maana waliniogeshea damu ya binadamu?” alijiuliza huku akiacha mdomo wazi. Alishtuka kupita kawaida. Licha ya kushtuka, alishangaa kuona bado anavutiwa na ile harufu, na sasa akawa anatamani asogee jirani kabisa ili ainuse vizuri.
Akiwa bado anashangaa, wazo jingine lilimjia akilini mwake. Alitaka kuiba moja kati ya chupa za damu na kutoroka nayo. Alitazama huku na kule, hakuna aliyekuwa anamuangalia. Akaingia kwa kunyata, akachukua chupa yenye ujazo wa lita moja, akaificha ndani ya shati lake la shule na kuondoka haraka eneo lile bila kushtukiwa na mtu yeyote.
Hakukumbuka hata kuchukua madaftari yake, akazamia kwenye vichaka vilivyokuwa nyuma ya shule na kutokomea kuelekea kusikojulikana.
Alipofika mbali na shule, alitafuta mahali penye kivuli na kukaa chini. Aliifungua ile chupa na kunusa ndani. Alichokuwa akikihisi kilikuwa sawa. Ni harufu ile ndiyo iliyomvutia, akasogeza pua karibu na mdomo wa chupa, akawa anavuta kwa nguvu huku akijisikia hali ambayo hakuwahi kuihisi awali.
Baada ya kunogewa na harufu ile, alitaka kuonja mdomoni ladha yake ilivyo.
“Usijaribu kunywa! Ni hatari…” alisikia sauti masikioni mwake ambayo hakuelewa imetokea wapi. Aligeuka huku na kule lakini hakumuona mtu yeyote.
Alijaribu tena kuinywa, lakini akasikia sauti kama ile ya mwanzo ikimkataza, safari hii kwa sauti kubwa zaidi. Alipogeuka huku na kule hakuona mtu yeyote. Cha ajabu ni kwamba aliitambua sauti ile kuwa inafanana kwa kiasi kikubwa na sauti yake mwenyewe.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akakumbuka kauli ya bibi yake aliyomwambia kuwa akisikia sauti inamkataza au inamuamrisha kufanya jambo fulani basi atekeleze bila kusita. Akiwa bado anajiuliza cha kufanya, wazo lilimjia kuwa aichukue chupa ile iliyokuwa imejaa damu hadi kwa bibi yake. Alilitekeleza hilo na muda mfupi baadaye akaanza kuchanja mbuga kuelekea nyumbani kwa bibi yake.
***
“Jamani mbona chupa moja haionekani?”
“Chupa gani?”
“Ya lita moja, zilikuwa nne, sasa moja haionekani.”
“Ilikuwa ina kitu ndani?”
“Ilijaa damu mpaka juu.”
“Angalieni vizuri, hakuna aliyeingia humu zaidi ya hao wanaoendelea kutolewa damu,” wafanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu walikuwa wakiulizana mahali iliko chupa moja baada kutoiona mahali ilipokuwa imewekwa. Juhudi za kuitafuta zilifanywa lakini hakukuwa na mafanikio yoyote. Hakuna aliyekuwa na jibu la haraka la nani aliyeichukua chupa ile na kwa kazi gani.
“Tangu nianze kazi ya kuhamasisha watu kuchangia damu kwa hiyari haijawahi kutokea kama ilivyotokea leo. Hii ni mara yangu ya kwanza kushuhudia.”
“Acha imani potofu, inawezekana ulikosea mwenyewe kuhesabu, nani aibe damu? Halafu huku kijijini hawajui hata inavyotumika.”
“Niliwahi kusikia kuwa huku kuna imani kali za kishirikina…”
“Ilikuwa zamani bwana, hakuna sehemu iliyotulia siku hizi kama huku. Wachawi wote walishakufa, wamebaki walokole watupu.”
Hata baada ya kupekua chumba kizima, wale wafanyakazi wa msalaba mwekundu hawakuipata chupa ile, ikabidi watoe taarifa kwa mwalimu mkuu wa shule ile.
Baada ya kupokea taarifa, mwalimu mkuu aliwakusanya wanafunzi na kuanza kuwahoji.
“Mwalimu mi nilimuona Gamutu amekaa kule nyuma ya darasa, lazima atakuwa amemuona aliyefanya kitendo hiki.”
Mwalimu mkuu aliagizwa Gamutu atafutwe haraka ili atoe maelezo kama amemuona aliyeichukua chupa ile. Alitafutwa maeneo yote ya shule lakini hakuonekana.
“Kwani ameenda wapi?”
“Atakuwa ametoroka, leo tangu asubuhi hayuko sawa,” alijibu mwalimu wake wa darasa. Mwalimu mkuu aliwatuma wanafunzi wakubwa wawili kumfuata nyumbani kwao. Wakaondoka kwa kasi na kuanza kukimbia kukatisha vichaka na mapori kuelekea nyumbani kwao.
***
“Hee! Mwenzetu hiyo chupa umeipata wapi? Halafu hicho kilichomo ndani ni nini?” Bibi Lubunga alimpokea mjukuu wake kwa maswali mfululizo.
Gamutu hakujibu kitu, akapitiliza hadi ndani ambako aliificha chupa ile nyuma ya chungu cha maji, akatoka nje na kuanza kuongea na bibi yake. Alimueleza kila kitu kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Kwa hiyo unataka kuifanyia nini?”
“Nataka niendelee kunusa harufu yake.”
“Ili iweje?”
“Basi tu, najisikia vizuri kunusa harufu ya damu, halafu nilikuwa nataka nionje ladha yake.”
“Hapana Gamutu! Bado hujafikia hatua ya kufanya hayo, usikimbilie mambo makubwa,” alisema bibi yake huku akiingia ndani kule Gamutu alikoificha chupa ile.
“Ni mapema mno wewe kuanza kuyafanya haya, mpaka utakapokomaa ndiyo utaruhusiwa,” alisema bibi Lubunga huku akitafuta mahali chupa ile ilikofichwa.
“Umeweka wapi?”
“Nyuma ya chungu cha maji ya kunywa.”
Muda mfupi baadaye, wanafunzi waliotumwa kutoka shuleni kwa kina Gamutu walikuwa wamewasili.
“Shikamoo bibi?” Waliamkia kwa pamoja.
“Tumetumwa kuja kumchukua Gamutu, Mwalimu Mkuu ametutuma.”
“Kwani kuna nini? Mbona alikuwa huko huko na saizi ndiyo anaingia?” Aliuliza Bi Lubunga huku akilini akiwa tayari na majibu ya alichokifanya mjukuu wake.
Aliingia ndani na kumkuta Gamutu akiwa amejificha nyuma ya mlango, akamshawishi na kumueleza kuwa ni bora arudi shuleni ili wakayamalize na mwalimu wake.
“Mimi nitakuwepo kukulinda, wala usiwe na wasiwasi.”
“Kwa hiyo nirudi na hii chupa?”
“Hapana, we nenda ila wakikuuliza kama umeichukua, kataa. Hata wakikuchapa fimbo, usikubali hata kidogo.”
Gamutu alikubali kurudi shuleni huku akimsisitiza bibi yake kuwa ni lazima awepo kumlinda. Aliongozana na wale wanafunzi waliotumwa na wakawa wanakatisha vichaka na mapori kuelekea shuleni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walipoondoka, Biu Lubunga aliichukua ile chupa yenye damu na kuanza kuitazama vizuri. Japokuwa alikuwa akijua mabadiliko ambayo Gamutu angekuwa nayo baada ya kufanyiwa tambiko lile, alishangaa kuona akibadilika kwa haraka mno.
“Yaani hata wiki moja haijaisha tayari kesi zimeanza, huyu Gamutu atanisumbua sana, lazima niwe naye makini sana,” alijisemea Bi Lubunga huku akitafuta mahali pa kuificha chupa ile.
Baada ya kuificha, aliingia chumbani kwake na kutulia, akavuta uzingativu na kuanza kujiona kama na yeye tayari ameshawasili shuleni kwa kina Gamutu, akataka kujua kitakachoendelea kwa mjukuu wake
Gamutu anafanya tukio linalovuta hisia za wengi. Baada ya kukataliwa kuchangia damu kama wenzake kutokana na umri wake kuwa mdogo na hali yake ya afya kutoimarika, anaamua kuiba chupa ya damu na kutoroka nayo. Yeye mwenyewe haelewi kwa nini anavutiwa na harufu ya damu. Bibi yake anamsaidia kumaliza kesi shuleni kiulaini kwa kutumia nguvu za kishirikina.
Siku inayofuata, wanafunzi wote wanamtenga Gamutu darasani hali inayomfanya ajisikie vibaya sana. Wakati hayo yakiendelea, jambo lingine linatokea. Msichana aliyevunja ungo darasani anamfanya Gamutu aanze upya kupata hisia za kutamani damu.
Anajifanya kumuonea huruma na kuahidi kumsaidia kumbe nyuma ya pazia ana lake jambo. Je, atafanya nini? Endelea...
“Nani kachukua chupa yenye damu mle ndani?”
“Sijui!”
“Kwa nini hujui wakati wenzako walikuona wewe ukiwa kule nyuma ya darasa?”
“Mwalimu mi sijui, kwanza nilitaka kujitolea damu mwalimu akanikataza na ndiyo maana nikakaa kule nyuma kwa hasira.”
“Kama hukuichukua wewe lazima unamfahamu aliyeichukua.”
“Hapana mwalimu, sijachukua wala simjui aliyeichukua.”
“Utasema ukweli tu, hebu kakateni fimbo, atasema tu,” aliongea mwalimu mkuu na wanafunzi wawili wakatoka kwenda kukata fimbo.”
“Piga magoti hapo, kwa usalama wako ni bora useme ukweli.”
Licha ya kutishiwa sana, Gamutu alikataa katakata kuhusika na upotevu wa chupa ile. Alijiapiza kuwa hata wamfanye nini kamwe hatasema ukweli.
Bibi Lubunga tayari alishawasili shuleni pale kimazingara. Alikuwa akishuhudia kila kilichokuwa kikiendelea na akafahamu fika kuwa asipofanya jambo kumsaidia mjukuu wake lazima atawajibishwa ipasavyo kwa kitendo kile.
Wale wanafunzi waliotumwa kutafuta fimbo walipoondoka, Bi Lubunga aliwafuata kimazingara. Lengo lake lilikuwa ni kuwapumbaza na kuwafanya wasahau walichotumwa.
Alifanikiwa lengo lake kwani walipofika porini, walisahau kama wametumwa na badala yake wakaanza kucheza juu ya miti.
Mwalimu mkuu na wenzake waliendelea kusubiri fimbo bila ya mafanikio, walipoona wanazidi kuchelewa, waliwatuma wanafunzi wengine wawili.
Kama ilivyokuwa kwa wenzao waliotangulia, Bi Lubunga aliwachezea akili nao wakaanza kucheza badala ya kufanya kazi waliyotumwa.
Baada ya kusubiri sana, Mwalimu mkuu na wenzake walijikuta wakiahirisha kesi ya Gamutu, wakamruhusu arudi kwao ila asubuhi afike pale shuleni akiwa na mzazi au mlezi wake.
“Mi naishi na bibi yangu, sina wazazi.”
“Uje na huyohuyo bibi yako. Usipokuja naye na wewe usije.”
Gamutu aliporuhusiwa kurudi nyumbani, wale wanafunzi waliotumwa kukata fimbo walirudiwa na akili zao na kuanza kujishangaa walichokifanya.
Kwa haraka walikata fimbo na kuzipeleka shuleni lakini kinyume chake fimbo zile zilitumika kuwaadhibu wao wenyewe kwa kuchelewa sana kurudi.
“Una bahati sana, nisingekuwepo pale leo ungekiona cha mtema kuni.”
“Asante bibi, ndiyo maana niling’ang’ania uwepo. Mwalimu alikuwa amekasirika ile mbaya, angeniua leo.”
“Sasa usirudie tena kufanya ujinga wako, ukirudia tena watakufukuza shule.”
“Sitarudia bibi, lakini kwa nini nafurahishwa na harufu ya damu? Halafu mbona harufu hii inafanana na harufu ya yale maji niliyoogeshwa siku ile kule kwa waganga?”
“Hapana Gamutu, yale ni maji yaliyochemshwa na aina fulani ya mimea inayotoa maji mekundu kama damu. Mimea hii inaitwa ‘nyahungo’ na hutumiwa sana kuongeza kiwango cha damu kwa wagonjwa. Harufu na mwonekano wake ni kama damu.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Habari ile ilimfurahisha Gamutu, akamuomba bibi yake akamuoneshe hiyo mimea ili badala ya kunusa na kutamani kunywa damu ya watu aitumie mimea hiyo kukata kiu yake.
“Haipatikani kirahisi, subiri siku utakayokuwa huendi shule nitakupeleka milimani inakoota mimea hiyo,” walikubaliana na kila mmoja akaendelea na shughuli zake.
“Sasa ile damu ya kwenye chupa utaifanyia nini?”
“Nitaihifadhi ninavyojua mwenyewe.”
“Haitaharibika?”
“Nimeichanganya na dawa ya kuzuia kuganda.”
***
Alfajiri na mapema, Gamutu alimuamsha bibi yake na kumueleza kuwa wanatakiwa waongozane pamoja mpaka shuleni ili kumalizia kesi ya jana yake.
“Tangulia mimi nakuja sasa hivi.”
“Wakiniuliza je?”
“Hakuna atakayekuuliza, yale mambo yalishaisha jana ile ile, kama huamini mwenyewe utaona.”
Gamutu alimuitikia bibi yake na kuanza safari ya kuelekea shuleni. Tofauti na siku zote, alishangaa kuona marafiki zake wakikataa kuongozana naye kwenda shuleni. Kila alipowakaribia wenzake walikuwa wakimkimbia, jambo lililomshangaza sana.
Alipofika shuleni, mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa ni mwalimu mkuu wao ambaye alimwambia kuwa yale mambo ya jana yameisha kwani wamegundua kuwa yeye (Gamutu) hakuhusika na upotevu wa chupa ile ya damu.
Alichoambiwa kilikuwa sawa na kile alichoambiwa na bibi yake asubuhi hiyo. Akaitikia kwa nidhamu kisha akaelekea darasani kufanya usafi.
Akilini mwake alikuwa akijiuliza namna kesi ile kubwa ilivyomalizwa kirahisi namna ile. Aliyakumbuka maneno ya bibi yake na kujikuta akitabasamu peke yake.
Walipoingia darasani, wanafunzi wote walikuwa wakiogopa kukaa naye dawati moja. Kila alipohamia kukaa dawati lingine, wanafunzi wote walikuwa wakihama na kumuacha peke yake. Hali hiyo ilimfanya ajisikie vibaya sana. Kwa kuwa shule yao ilikuwa na walimu wachache, siku hiyo hakuna mwalimu hata mmoja aliyeingia darasani. Akaendelea kunyanyapaliwa na wenzake kutwa nzima.
Kengele ya mapumziko ilipogongwa, wanafunzi wote walitoka nje na kumuacha Gamutu peke yake darasani. Dakika chache baadaye, mwanafunzi mwingine wa kike alirudi darasani huku akiwa amejishika tumbo. Alionekana wazi kuwa alikuwa akisumbuliwa na maumivu makali ya tumbo. Alienda kukaa kwenye kona peke yake, akainamia chini huku akigugumia kwa maumivu.
Gamutu aliinuka kutoka pale alipokuwa amekaa na kumsogelea. Alishangaa kuona michirizi ya damu ikielekea kule alikokaa msichana yule. Hali ile ilimshtua Gamutu na mapigo yake ya moyo yakaanza kumuenda mbio. Alipomsogelea, alizidi kushangaa kuona sketi ya msichana yule ikiwa imeloana kwa damu.
“Umeumia na nini?” Yule msichana alishtuka kusikia mtu anamsemesha, alipoinuka alikutana na uso wa Gamutu uliokuwa na mshangao mkubwa.
“Sijaumia Gamutu, ondoka niache peke yangu, mi nakuogopa.”
“Lakini ukiniambia naweza nikakusaidia.”
“Huwezi Gamutu, haya ni mambo ya wanawake. Yamenikuta ghafla na sijui nitaondokaje mimi, wenzangu wakiniona watanicheka sana.”
“Mbona sikuelewi?”
“Nimevunja ungo,” alijibu yule msichana lakini bado Gamutu hakuelewa chochote. Moyoni mwake alianza kuvutiwa na harufu aliyokuwa anaitoa msichana yule. Ilikuwa ni harufu kama ile aliyovutiwa nayo jana yake, harufu ya damu.
YULE msichana alimuomba Gamutu amsaidie kufuta michirizi ile ya damu ardhini ili wenzake wasije wakamgundua. Kwa haraka Gamutu alitekeleza alichoambiwa na alipomaliza alienda kukaa dawati moja na yule msichana.
“Najua wanafunzi wote wanaogopa kukaa dawati moja na mimi, kama unataka wasikugundue kubali tukae wote. Hakuna atakayesogea hapa mpaka muda wa kurudi nyumbani ukifika.”
Yule msichana aliitikia kwa kichwa kutokana na kuzidiwa na maumivu ya tumbo, wakakaa pamoja. Hakuelewa kuwa ile ilikuwa ni janja ya Gamutu ili aendelee kufaidi harufu ya damu.
Wanafunzi wengine waliporejea darasani hawakugundua kinachoendelea ingawa kila mmoja alishangaa iweje yule msichana asimuogope Gamutu na kukaa naye dawati moja.
Muda wa kurudi nyumbani ulipofika, Gamutu na yule msichana walibaki darasani mpaka wengine wote walipotoka. Baada ya hapo Gamutu akamsaidia kusimama, wakaanza kuondoka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Utaweza kutembea mwenyewe?”
“Hapana, nisindikize.”
Kwa Gamutu, ile ilikuwa ni nafasi ya kipekee ambayo alijiapiza kuwa ni lazima aitumie ipasavyo. Alimshika mkono, wakatoka darasani na kuanza kutembea taratibu kuelekea kwao. Walikuwa wameshikana mikono kama watu walioko kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu.
“Gamutu hapa mwalimu akituona hawezi kujua kwamba unanisaidia, atahisi mambo tofauti.”
“Kwa hiyo tufanyeje?”
“Ngoja mi’ nitangulie halafu wewe uwe unafuata nyuma taratibu, tukifika kule ndiyo tuongozane.”
“Sawa, hakuna tatizo,” alijibu Gamutu na kumuacha yule msichana atangulie.
Baada ya dakika chache, Gamutu alimfuata na kumkuta amekaa chini ya mti akimsubiri, wakaendelea kusindikizana.
“Gamutu wewe una huruma sana, yaani wenzangu wote hakuna aliyenijali hata mmoja ila wewe umeamua kunisindikiza mpaka nyumbani, nimefurahi sana.”
“Usijali Sabina, twende nikufikishe mpaka kwenu.”
Wakati wakizidi kutembea pamoja, Gamutu alianza kuhisi hali isiyo ya kawaida. Kwa kipindi chote walichokuwa wameongozana, Gamutu alikuwa akifurahia harufu ya damu kutoka kwa yule msichana, akawa anataka kufanya jambo lakini nafsi yake inasita.
Akasikia sauti ikimuamuru akilini mwake kuomba kufanya mapenzi na yule msichana. Hakuwahi hata mara moja kukutana kimwili na mwanamke, hakujua tendo lenyewe likoje wala wakati gani ni muafaka wa kulifanya.
Alitaka kupingana na sauti ile lakini alipokumbuka maneno ya bibi yake, akajikuta akibaki njia panda. Alimtazama usoni kwa muda, kisha akajikuta akipata ujasiri wa kumweleza kilichokuwa akilini mwake.
“Mwenzio naumwa Gamutu, siwezi halafu mi sijawahi.”
“Mi mwenyewe sijawahi na kuhusu kuumwa usijali, tukimaliza nitakupa dawa ambayo bibi alinifundisha kuwa inatibu matatizo ya wanawake.”
“Hapana Gamutu, kama ndiyo lengo lako basi bora urudi nitafika mwenyewe nyumbani.”
“Basi nisamehe Sabina, ni shetani tu amenipitia,” alijibu Gamutu kwa shingo upande huku akiona aibu.
Waliendelea kutembea kila mmoja akiwa kimya, sauti ile ikasikika tena kichwani mwa Gamutu ikimuelekeza kuwa ni lazima akutane kimwili na yule msichana ili kukamilisha dawa ya zindiko la mapenzi.
Aligeuka kumwangalia Sabina usoni, hakusema neno, akayapeleka macho yake haraka chini, akawa anaendelea kusikiliza malekezo anayopewa bila Sabina kuelewa kilichokuwa kinaendelea.
“Naomba nisubiri kidogo dada Sabina.”
“Unaenda wapi?”
“Nimebanwa na haja ndogo, nakuja sasa hivi,” alisema Gamutu huku akichepuka na kuingia kichakani.
Alikuwa ameelekezwa aina ya mzizi ambao alitakiwa kuuchimba haraka na kuutafuna kisha ndipo amuombe upya Sabina kukutana naye kimwili.
Alipozama kichakani, alitafuta mmea ambao bibi yake alimfundisha kuwa unaitwa mtangetange wenye mizizi yenye rangi mbili, nyekundu na nyeupe. Alifukua kwenye shina na kukata mizizi iliyokuwa na rangi nyekundu pekee kama alivyokuwa ameelekezwa, akaitafuna na kwa haraka akarejea.
“Vipi nimechelewa?”
“Wala hujachelewa, hivi ulikuwa unasema unataka tufanye nini?”
“Naomba nifanye mapenzi na wewe.”
“Mi naogopa, nikipata ujauzito utanioa?”
“Huwezi kupata ujauzito, halafu sisi bado ni wadogo kuoana. Naomba kidogo tu!”
Katika hali ambayo hata Gamutu mwenyewe aliishangaa, Sabina aliingia kiurahisi sana kwenye mtego. Licha ya kuwa alikuwa na maumivu makali baada ya kuvunja ungo akiwa shuleni, alikubali kukutana kimwili na Gamutu. Wakazama kichakani, sehemu ambayo haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kuwaona. Kazi ikaanza.
***
Miongoni mwa masharti ambayo Bi Lubunga, Bibi yake Gamutu alipewa walipoenda kwa waganga kwa ajili ya kumfanyia tambiko la maisha mjukuu wake, ilikuwa ni kwamba haruhusiwa kukutana na mwanamke wa aina yoyote mpaka atakaporudishwa tena kwa waganga kwa mara ya pili ili kukamilisha taratibu ya kuhitimisha zindiko lile, miezi mitatu baadaye.
Kwa kuwa Bi Lubunga alikuwa akiamini kuwa Gamutu bado ni mdogo na hajaanza kuwa na hisia za kimapenzi, hakuona umuhimu wa kumueleza, akawa anaamini kuwa miezi mitatu itaisha bila ya kumtamani wala kukutana na mwanamke wa aina yoyote. Hakujua kuwa kumbe tayari Gamutu alishabalehe na alianza kuwa na hisia za kimapenzi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitendo cha yeye kukutana na mwanamke kabla ya miezi mitatu haijaisha, tena akiwa na damu ya hedhi ilikuwa ni kosa kubwa ambalo madhara yake yangekuwa makubwa. Bi Lubunga aliamini kuwa kwa sababu Gamutu tayari alikuwa amefanyiwa tambiko, isingekuwa rahisi kwake kufanya jambo la hatari bila kusikia sauti kutoka ndani yake ikimkataza.
Alisahau kwamba tambiko la maisha halifanani na tambiko la mapenzi. Kwa kuwa alishafanyiwa tambiko la maisha, hatari zote za maisha angeweza kuziona na kuzisikia, lakini upande wa mapenzi alikuwa kama kipofu kwani alikuwa bado hajakamilishiwa zindiko la pili la mapenzi.
Kutokana na hali hiyo, hakuwa na uwezo wa kuona hatari yoyote inayomkaribia kimapenzi, akajikuta akikiuka miiko na masharti aliyopewa.
Wakati Bi Lubunga akitwanga mahindi kwenye kinu kikubwa nje ya nyumba yake, machale yalimcheza kwamba mjukuu wake huko aliko hayuko salama.
Alikimbia hadi ndani na kufanya mambo yake ya kishirikina, dakika chache baadaye akawa anavuta uzingativu mkubwa huku akifanya tahajudi za kichawi.
Muda mfupi baadaye akawa anashuhudia mjukuu wake alichokuwa anakifanya kichakani.
“Uuuwi! We Gamutu!” Bi Lubunga alijikuta akipiga kelele baada ya kushuhudia alichokuwa anakifanya Gamutu.
Alikuwa akivunja amri ya sita na yule msichana aliyeonekana kuwa amepoteza fahamu. Pembeni kulikuwa na kikopo kidogo kilichoonekana kuwa na damu ndani yake.
Kelele zile kutoka kwa bibi yake zilimfanya Gamutu ashtuke na kuacha kile alichokuwa anakifanya, akainuka haraka haraka na kuvaa nguo zake, akachukua kile kikopo kilichokuwa na damu na kuanza kutimua mbio akiwa haelewi anapoelekea.
Simama, Gamutu simama ni mimi bibi yako,” aliita kwa sauti Bi Lubunga lakini Gamutu alizidi kutimua mbio kuzamia vichakani. Alitimua mbio kuliko kawaida, hakutegemea kama bibi yake anaweza kutokea mazingira kama yale na kumshuhudia aliyoyafanya. Kwake ilikuwa ni zaidi ya aibu kuonwa na bibi yake. Alijikuta akijilaumu kwa uzembe alioufanya.
Baada ya kuhakikisha amefika mbali, alikaa chini ya mti huku akihema kwa nguvu. Kichupa cha damu kilikuwa pembeni yake, akawa anaitazama kama anayetamani kuinywa. Akiwa bado amekaa palepale chini, bibi yake alifika kimiujiza na kumtokea ghaflambele zake.
“Umefanya nini sasa Gamutu!”
Hakuwa na jibu zaidi ya kujiinamia huku akikificha kile kikchupa kilichokuwa na damu mgongoni.
“Umevunja masharti makubwa sana, ni lazima nifanye jambo kukuokoa, vinginevyo kila kitu chako kitaharibika na utaishia kuwa jini,” aliongea Bi Lubunga kwa sauti ya masikitiko.
Alimweleza kuwa wale waganga walikuwa wamempa masharti ya kutokutana na mwanamke mpaka atakaporudishwa tena kwa mara ya pili kufanyiwa tambiko la mapenzi.
“Nisamehe bibi, nilipitiwa tu.”
“Kama kweli ulipitiwa na unakiri kosa, lete hiyo chupa ya damu.”
Aliongea Bi Lubunga kwa sauti kavu, Gamutu akawa anasita huku akizidi kuificha ile damu mgongoni.
“Lakini bibi, ile chupa ya kwanza niliyotoka nayo shuleni uliichukua na hukunirudishia mpaka leo, saizi unataka na hii nayo uichukue.”
“Acha ujinga Gamutu, mi nafanya yote haya kukuokoa wewe halafu unajifanya kuhoji. Nitaacha kukusaidia mimi halafu tuone mwisho wake, unajifanya umeshakuwa mkubwa?”
Gamutu alinyamaza kimya baada ya kuona bibi yake amecharuka.
“Sasa inuka hapo chini sasa hivi, twende ukamsaidia mtoto wa watu kumrudisha kwao, bila hivyo utafukuzwa shule kama atawaambia walimu ulichomfanya.”
Baada ya kusikia hivyo, Gamutu ilibidi awe mpole na kumpa bibni yake ile chupa yenye damu. Alikubali kuongozana na bibi yake mpaka pale alipomwacha yule msichana (Sabina) akiwa amepoteza fahamu. Walipofika eneo la tukio, Bi Lubunga alimuelekeza dawa ya kumpa, akamchimbia mizizi ya mtangetange, akaisaga kwenye jiwe kubwa lililokuwa jirani na kumkamulia maji yake mdomoni.
Alipomnaliza kumywesha dawa ile, Bi Lubunga alimwachia malekezo Gamutu kuwa ahakikishe anamfikisha nyumbani kwao yule msichana atakapozinduka. Akapotea na kumuacha Gamutu akiwa haelewi cha kufanya. Muda mfupi baada ya kuondoka, Sabina alizinduka kutoka kwenye usingizi wa kifo na kujikuta yuko porini na Gamutu.
“Hapa ni wapi?”
“Nilikuwa nakusindikiza nyumbani kwenu, ghafla ukapoteza fahamu njiani. Hivi ndiyo unazinduka sasa hivi.”
“Mungu wangu, nisaidie kufika nyumbani tafadhali.”
“Usihofu, simama twende,” Gamutu alimshika mkono na kutaka kumsaidia kusimama.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Uuh! Naumia… niacheee!” Alisema Sabina huku akijinasua kutoka mikononi mwa Gamutu. Alihisi maumivu makali sana katikati ya miguu yake kiasi cha kushindwa kusimama. Alishangaa iweje maumivu yahame kwani awali kabla ya kupoteza fahamu alikuwa akiumwa na tumbo lakini sasa yalikuwa yameongezeka mara dufu.
Hakugundua kwa haraka nini kilichotokea mpaka akapoteza fahamu kutokana na kupumbazwa na dawa za kienyeji alizopewa na Gamutu na bibi yake. Aliendelea kukaa pale chini huku akiugulia maumivu makali. Baada ya zile dawa kuanza kufanya kazi, maumivu yalianza kupotea na akajikuta anaweza kusimama.
“Saizi angalau naweza hata kupiga hatua, twende unisindikize basi,” aliongea Sabina huku akimpa ishara Gamutu. Wakawa wanatembea kukatiza vichaka kuelekea nyumbani kwa kina Sabina. Muda ulikuwa umeyoyoma na Sabina hakujua ataeleza nini nyumbani kwao kutokana na jinsi alivyochelewa. Alipomfikisha karibu na kwao, Gamutu aliaga na kuondoka zake wakiahidiana kukutana kesho yake shuleni.
***
Umefanya makosa sana Gamutu, ni lazima le oleo nikurudishe kule kwa waganga, vinginevyo maisha yako yapo hatarini.”
“Kivipi bibi?”
“Kwani hujui ulichokifanya?”
“Lakini si uliniambia nikishazindikwa hakuna kitakachonidhuru?”
“Hapana, sikukwambia uanze kushirikiana na wanawake, lile lilikuwa ni zindiko la maisha lakini hukufanyiwa zindiko la mapenzi wewe. Lazima tufanye jambo la haraka.”
Aah! Mi siendi tena kwa wale waganga. Masharti yao ni magumu na kuna mambo ya kutisha sana. Halafu siku ile wanafunzi wenzangu walinicheka nilivyorudi, mi siendi tena.”
“Wewe! Mbona unafanya masihara kwenye mambo ya hatari kama haya?”
“Mi nimeshasema siendi tena kwa wale waganga, kwanza walisema wanataka nirudi wakanifundishe uchawi.”
“Lakini Gamutu kiburi cha kubishana na mimi umekipata wapi? Au kwa sababu umeanza kuwajua wanawake.”
Bi Lubunga alikuja juu: “Kwa taarifa yako lazima nikupeleke tena, siwezi kukubali kuona unapotea wakati uwezo wa kukuokoa ninao.”
Gamutu alipoona bibi yake anazidi kumwandama, aliamua kuondoka nyumbani kwao kuepusha makuu. Alichokuwa anakisema kilikuwa kinatoka moyoni mwake. Kwa mambo aliyoyashuhudia siku ile alipoenda kufanyiwa tambiko la maisha, yalimfanya akatae kabisa kurudi kwa wale waganga. Alijiapiza kuwa hata bibi yake afanye nini, kwamwe hatarejea kwa sababu kwanza alihisi unaandaliwa mpango wa siri wa yeye kurithishwa mikoba ya uchawi.
Akiwa amejiinamia peke yake kichakani, mita kadhaa kutoka nyumbani kwao, Gamutu alikumbuka kuhusu chupa yake yenye damu aliyomtoa kimazingara msichana Sabina. Akainuka haraka na kurudi ndani bila ya bibi yake kumuona. Alipitiliza mpaka pale alipomuona bibi yake akiihifadhi ile chupa. Cha ajabu hakuikuta mahali pake.
Akaanza kutafuta kona zote za nyumba bila mafanikio. Wakati akipekua huku na kule, bibi yake aliingia na kumkuta akiwa kwenye harakati.
“Unatafuta nini?”
Gamutu hakuwa na jibu zaidi ya kujiinamia chini. Bibi yake alimuuliza tena alichokuwa akikitafuta lakini bado hakuwa na jibu. Akatambua moja kwa moja kuwa hamu ya kunywa damu ndiyo iliyokuwa inamtesa.
***
MIAKA 17 ILIYOPITA
“Jikaze mwanangu, huwa inatokea ujauzito unapitiliza mpaka miezi kumi na mbili. Huyu mtoto utakayejifungua atakuwa na karama za kipekee, wala usichoke. Jikaze mwanangu.”
“Hapana mama, kwa nini wenzangu wote wajifungue bila matatizo? Ujauzito wenyewe wa kwanza, bado nikee nao miezi kumi na mbili!”
“Jikaze mwanangu, tusubiri kama yule mkunga alivyotuambia. Hali ikibadilika tutamuita kuja kukusaidia kujifungua hapahapa nyumbani.”
Licha ya Bi. Lubunga kujitahidi kwa kadri ya uwezo wake wote kumtuliza mkwewe, mke wa mwanaye wa kwanza, bado aliendelea kulia kwa uchungu baada ya ujauzito wake kupitiliza muda wa kawaida wa kujifungua hadi miezi kumi na mbili. Haikuwa kawaida kwa mjamzito kufikisha mpaka miezi kumi na mbili bila kujifungua.
Kwa mujibu wa mila za kwao, mtoto anayezaliwa akiwa na umri wa miezi kumi na mbili ni lazima awe mganga wa kienyeji au mtabiri kwa sababu huhesabiwa kuwa amezaliwa akiwa na karama ya kipekee. Hatimaye siku ya kujifungua iliwadia, mkunga akaenda kutafutwa kwa ajili ya kumsaidia mjamzito kujifungua salama.
Hatimaye mkwe wa Bi Lubunga alipata uchungu baada ya kusota na ujauzito kwa miezi 12. Uchungu wake ulikuwa wa kimiujiza kwani ulitawaliwa na mambo mengi yasiyo ya kawaida. Baada ya kubanwa sana, Bi Lubunga alitoka mpaka kwa mkunga kumpa taarifa kuwa tayari mambo yameiva lakini kwa bahati mbaya hakumkuta, hali iliyomchanganya na kubakia ameishiwa nguvu asijue cha kufanya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wazo pekee lililomjia akilini mwake ilikuwa ni kumsafirisha mjamzito mpaka kijiji cha pili ambako kulikuwa na mkunga mwingine wa jadi. Ilio kufika kijiji cha pili, ilikuwa ni lazima uvuke mapori makubwa nay a kutisha kisha uvuke mto mkubwa.
Bi Lubunga alirudi nyumbani haraka na kuwapa taarifa waliokuwepo kuwa mkunga hayupo na inabidi wambebe mjamzito mpaka kijiji cha pili. Huo ulikuwa ni mtihani mwingine kwani hakukuwa na magari wala njia nzuri ya kupita kuelekea kijiji cha pili. Usafiri pekee uliooonekana kufaa kwa wakati ule ilikuwa ni baiskeli ya jirani mmoja wa Bi Lubunga.
Mipango ya kuazima baisklei ilifanywa haraka haraka, muda mfupi baadaye ikapatikana. Tatizo lingine ikawa ni nani atayeiendesha baiskeli hiyo hadi kijiji cha pili kwa mkunga? Mwanaume aliyekuwa anahusika na ujauzito ule alikuwa yu mgonjwa taabani na alipelekwa vijiji vya mbali kwa waganga wa kienyeji kuaguliwa na kutibiwa.
Aliondoka na kumwacha mkewe akiwa na ujauzito wa miezi saba.
Mtu pekee wa kutoa msaada akawa ni Bi Lubunga na majirani zake wawili wanawanke ambao kiumri walikuwa wanakaribia kulingana. Mama mjamzito akapakizwa juu ya baiskeli huku akiugulia maumivu makali ya uchungu.
Msafara wa wanawake watatu wa makamo ukaanza kuikokota baiskeli kuelekea kijiji cha pili.
“Jikaze mwanangu, karibia tunafika,” alisikika Bi Lubunga akimfariji mjamzito aliyekuwa akilia kwa maumivu makali yaliyosababishwa na uchungu wa kujifungua.
Safari ilikuwa ngumu kwani wanawake wale kuna kipindi walikuwa wanachoka na kushindwa kuendelea na safari kutokana na kuzidiwa na uzito wa mjamzito na uzoefu mdogo wa kukokota baiskeli.
Walipofika katikati ya pori kubwa ambalo wenyeji wa eneo lile walikuwa wakiliita ‘Takhirijo Ghamuthu’ likiwa na maana ya msitu wa miujiza, uchungu ulimzidia mjamzito, akashindwa kuendelea kukaa juu ya baiskeli.
Bi Lubunga na wenzake walichanganyikiwa kwani walikuwa ndiyo kwanza wako katikati ya safari ya kuelekea kwa mkunga.
Katika hali ambayo hawakuitegemea, wingu zito lilitanda angani na kusababisha hali ya kigiza cha kutisha. Mgurumo za hapa na pale zilianza kusikika na muda mfupi baadaye manyunyu ya mvua yakaanza kudondoka. Bi Lubunga akavua vitenge vyake na kumfunika mjamzito aliyekuwa hajitambui kutokana na mumivu aliyokuwa anayapata.
Hapakuwa na sehemu yoyote ya kujisitiri na mvua ile, wale wanawake wengine walishauri kuwa wakakae chini ya mti mkubwa kupisha mvua imalizike lakini Bi Lubunga akakataa katakata kwani kwa mila za kwao, lilikuwa ni kosa kubwa kukaa chini ya mti wakati mvua inanyesha kutokana na matukio mengi ya watu kupigwa na radi za kimazingara. Hakutaka hilo litokee.
Mvua ikawa inazidi kunyesha. Wakati hayo yakiendelea, mtoto tayari alikuwa akijongea kwenye mlango wa kutokea. Cha ajabu ni kwamba alityanguliza miguu kabla ya kichwa.
Wale wanawake wakiongozwa na Bi Lubunga wakaanza kumsaidia mjamzito kumsukuma mtoto bila kujali mvua kubwa iliyokuwa inaendelea, huku wakiwa na matumaini kidogo ya kumaliza zoezi lile salama kwani kwa kawaida mtoto akitanguliza miguu husababisha matatizo makubwa na huweza hata kufariki au kusababisah kifo cha mzazi.
Mjamzito alivuja damu nyingi sana ambayo ilikuwa ikiyeyushwa na maji ya mvua na kusombwa kuelekea bondeni. Baada ya vuta nikuvute iliyodumu kwa muda mrefu, hatimaye alijifungua mtoto wa kiume.
Katika hali ambayo haikutarajiwa kabisa, mtoto alipoanza kulia kwa mara ya kwanza na kufumbua mdomo, alionekana kuwa tayari na meno mawili ya juu.
“Uuuwi! Mkosi gani tena huu jamani?” Aliongea kwa sauti ya juu Bi Lubunga.
“Kwani vipi?”
“Hebu angalieni, mtoto kazaliwa na meno.”
“Hebu tuone?”
“Heee! Kweli jamani… maajabu gani haya, mi nilikuwa nasimuliwa tu, leo nimejionea mwenyewe.”
Hakuna aliyeamini kilichotokea. Tatizo la kwanza lilikuwa ni mtoto kutanguliza miguu lakini kama hiyo haitoshi, alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya juu, jambo ambalo ungeweza kuliita ni maajabu ya karne.
Kwa mujibu wa mila za kina Bi Lubunga, mtoto akizaliwa huku akiwa ametanguliza miguu, ilikuwa ni lazima auawe muda huohuo kwa kupigwa na kitu kizito kichwani hadi afe kwani iliashiria balaa na mkosi mkubwa kwa familia yake na jamii kwa ujumla. Kama hiyo haitoshi, mtoto kuzaliwa akiwa tayari na meno ilichukuliwa kama ni laana kali kwa ukoo mzima na ilikuwa ni lazima mtoto wa namna hiyo akatwe kichwa na kwenda kutolewa kafara kabla hajatimiza umri wa siku tatu.
Ni kweli mila za kwao zilikuwa zikisema hivyo lakini Bi Lubunga hakuwa tayari kuona mjukuu wake aliyemtesa mwanae kwa muda wa miezi kumi na mbili tumboni akiuawa kikatili eti kwa sababu ametanguliza miguu na kuzaliwa akiwa na meno.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sasa tufanyeje jamani,” alihoji mwanamke mmoja huku mvua ikizidi kumwagika kwa hasira.
“Tumsitiri mtoto na tuangalie namna ya kumuokoa mama yake maana amepoteza damu na nguvu nyingi.
“Tumsitiri wa nini wakati tunajua atakufa tu, kashinjeghe (jina lililotumika kwa watoto wa namna ile) ni wa kufa tu, tuangalia namna ya kumuokoa mama yake.
Hawakujua kuwa wakati wakizungumza hayo, mama yake alikuwa kwenye hatua za mwisho za uhai wake. Baridi kali iliyosababishwa na mvua iliingia kwenye tumbo la uzazi na kumfanya mama yule abanwe na kifua kikali.
Ukichanga tayari alikuwa amepoteza damu nyingi na nguvu, kifo kilikuwa karibu yake. Akapiga yowe kuu kisha akatulia kwenye maji ya mvua huku damu nyingi ikizidi kumwagika. Alikufa kifo cha uchungu na maumivu makali.
Vilio vilianza kusikika eneo la tukio. Bi Lubunga akawa analia kwa uchungu wa kuondokewa na mwanae aliyemuachia mjukuu mwenyematatizo na anayetakiwa kuuawa mara moja. Wenzake walimtuliza kwa muda, akatulia na kuanza kuulizana mwenzake nini cha kufanya.
Tubebe maiti ya mama, huyu mtoto tumuache hukuhuku porini. Ni bora tukadanganye kijijini kuwa mtoto kafia tumboni kuliko kusema kazaliwa na meno huku akiwa ametanguliza miguu. Ukoo wetu utatengwa na huenda tukapata matatizo makubwa.
“Hapana, nyie ondokeni kurudi kijijini, mi niacheni na mwanangu na mjukuu wangu. Siwezi kukubali afe, ataziba pengo la mama yake.
“Lubunga umechanganyikiwa nini? Atazibaje pengo wakati huyu ni kufa? Tangu lini Kashinjeghe akaishi?”
“Najua nitakachokifanya, nyie niachieni kila kitu mimi, naomba tu mnitunzie siri.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment