Simulizi : Padri Mla Nyama Za Watu
Sehemu Ya Pili (2)
“Sawa.”
Pale pale alitembea kuelekea nilikokuwa mimi, akaniwekea mkono kichwani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
Wiki moja ilikatika toka hayo yatokee, lakini hakukuwa na jipya jingine, sikuwahi kumwona mtu mwingine akinijia nyumbani wala kanisani ninapokuwa nafanya kazi za Mungu.
Lakini siku hiyo, nikiwa nimelala majira ya saa saba usiku, nilishtuka ghafla. Nikatupa macho mlangoni. Kwa sababu ya giza sikuona vizuri, ila dalili ya kama kitasa cha mlango kikifunguliwa.
Nilinyoosha mkono hadi kwenye taa ya kitandani (bed switch) nikawasha kwa umakini sana ili mlio wa swichi usisikike.
Kitasa kikawa kinakaribia chini, lakini kikanata kwa muda. Nadhaani ni baada ya mimi kuwasha taa.
Hali hiyo ilinifanya nitoke kitandani na kusimama katikati ya chumba huku macho yote yakiwa kwenye kile kitasa mlangoni.
Huku taa ikiwa bado inawaka, kitasa kiliendelea kwenda chini, yaani kufunguka, lakini ilionekana aliyekuwa anakifungua yupo makini sana kwani kwa kukitazama haraka tu ilikuwa vigumu kujua kitasa kinafunguka kwa kwenda chini.
Mara mlango ukaanza kusukumwa polepole na mimi nilisimama nikaza macho kujua nani aliyekuwa akifanya kazi ile. Wazo kwamba ni mwizi sikuwa nalo kwani nawajua wezi, wao ni papara au kushtukiza.
Mlango uliendelea kusukumwa mpaka ukawa wazi wote, yaani kama kuna mtu alisimama kwenye korido angeona chumbani, lakini cha kushangaza hakukuwa na binadamu wala kiumbe chochote nyuma ya mlango.
Nilipotaka kuuliza nani mwenzangu, nikasikia sauti ya mtu kukohoa kwa kujibana. Halafu nikasikia mlio wa viatu, ko! Ko! Ko! Ko! Ukisikika kuingia ndani ya chumba, nikarukia kusimama pembeni kwani niliamini aliyekuwa akiingia angeweza kunikumba.
Mlio wa viatu kutembea uliposimama ukafuata mlio wa kufunguliwa kwa dirisha la chumba, na kweli likawa linafunguka hadi mwisho, halafu pazia ikawa inakunjwa na kufungwa katikati kama vile mkunjaji alitaka upepo uingie kwa vizuri.
Baada ya hapo, nikiwa nimesimama pembeni, mlio wa viatu ukatembea kwa mwendo ule ule wa ko! Ko! Ko hadi ukutani kwenye swichi, ghafla nikasikia tap na giza likatanda. Ina maana huyo mtu alizima taa.
Halafu mlio wa viatu ukaendelea tena hadi usawa wa kitanda, ukakwamba pale. Giza likiwa limetanda, nikasikia hali ya mtu anayepanda kitandani kwani kitanda kilitoa mlio Fulani na baadaye, kama baada ya dakika moja ikasikika sauti ya mtu kukoroma.
“Khooooo! Khoooo!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliamini ni uonevu usiokuwa na maana kwangu kwani sikuwa na kosa la kunifanya nishindwe kulala na kulala mtu mwingine, nilikasirika sana . Nikatembea kijeuri hadi ukutani na kuwasha taa.
Ile inawaka tu, ile swichi ya kitandani ikasikika ikizimika, tap! Kukawa giza tena.
Niliifuata kwa fujo ile swichi ya kitandani, nikaiwasha na macho yangu yakakimbilia moja kwa moja kitandani. Mtu mnene, mrefu alikuwa amejifunika shuka huku akiwa amenyoosha miguu na anaangalia juu, yaani amelala chali.
“Wewe ni nani?” Nilimuuliza bila woga.
“Msafiri,” sauti nzito ilijibu kwa mkato.
“Ndiyo jina lako au msafiri unakwenda mahali?”
“Siendi popote.”
“Khaa! Sasa hapa kwako?”
“Hapana.”
“Sasa kwanini umefungua mlango bila hodi na umepanda kitandani kulala bila ridhaa yangu?”
“Nisamehe sana .”
“Basi ondoka.”
Kauli yangu hiyo haikupata jibu zaidi ya mlio wa kukoroma kusikika kama mwanzo.
Nilimsogelea yule mtu pale kitandani kwa lengo la kumfunua shuka na kumwona vizuri. Niliishika shuka kwenye ncha moja, nikaifunua kwa nguvu…
“Ha ha ha ha ha ha!” Alicheka sana yule mtu huku akitoka kitandani na kuficha uso kwa mkono mmoja.
Nilijitahidi sana kuhakikisha namwona uso yule mtu, lakini na yeye alikuwa akawa anaangalia ukutani huku akiendeelea na kicheko chake.
“Wewe ni nani?” Nilimuuliza kwa ukali kidogo.
“Ha ha ha ha! Msafiri bwana, si nilikwambia!”
“Umetumwa?”
“Hapana.”
“Umekuja tu mwenyewe?”
“Ha ha ha ha! Eee!”
Kusema ule ukweli nilichanganyikiwa, kwani sasa nikawa sijui ukweli upo wapi, kila ninachomuuliza ananijibu kinyume na matarajio yangu.
“Basi mimi naomba uondoke humu chumbani kwangu,” nilimwamuru.
“Ha ha ha ha ha! Sawa,” alisema akielekea mlangoni na kutoka kweli lakini nikiwa sijafanikiwa kuona sura.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa hiyo mpaka hapo nikawa sijui ni nani yule.
Alipovuka tu ukuta wa chumba changu, nikajikuta napata wasiwasi na woga tofauti na mwanzo alipoingia.
Nilifunga mlango ili nipande kitandani kulala, lakini kabla sijapanda, nikasikia vishindo ti ti titi! Watu kama sita walisimama katikati ya chumba changu.
“Mtumishi wa Mungu vipi? Habari za kulala?”
“Salama.”
“Aaa, tumetumwa kwako.”
“Na nani?”
“Aaa, vaa miwani yako kwanza kisha utuangalie vizuri.”
Nilipeleka mkono kwenye stuli ndogo iliyokuwa pembeni ya kitanda na kuchukua miwani, nikaivaa na kuwaangalia.
Walikuwa tofauti na nilivyowaona wakati wanatua. Walikuwa wamevaa viguo vyeusi (kaniki) kukatisha kiunoni kwenda chini ya mapaja, kila mmoja alionekana amekasirika na hana utani na usoni walipaka vitu vyeupe, kama si unga, basi chokaa.
“Unatuona vizuri sasa?”
“Ndiyo.”
“Basi ndivyo tulivyo, toa miwani.”
Nilipotoa tu, walirejea na kuwa kama walivyotua, wamevaa kawaida.
“Unatakiwa kuhudhuria mateso ya waumini wako usiku wa sasa,” mmoja wao aliniambia, wengine wakatingisha vichwa kama ishara ya kukubaliana na maneno ya mwenzao.
“Wapi?”
“Katika kila nyumba yenye muumini au waumini wako.”
“Ni mateso ya aina gani?”
“Utajua huko huko na huna hiyari katika hili, kwani ulishapata baraka zote za uchawi.”
Nilijikuta nasimama, naanza kutembea kuwafuata kutoka nje mpaka uwanjani mbele ya nyumba, wakaanza kutengeneza duara na mimi nikawa mmoja wa wanaduara.
Mmoja akapeleka mikono na kuwashika wa kulia na kushoto kwake, wengine wakafanya hivyo mpaka mimi. Tukawa tumekamatana mikono. Yule aliyeanza kushika, akainama kama dalili ya kusujudia, wengine wakafuatia na mimi pia, kufumba na kufumbua, tukajikuta tukipaa juu na kutua chini ya mti mkubwa wa Mvule. Sikumbuki tulitumia dakika ngapi kuwa angani na kushuka.
Milio ya ngoma iliyotawala pale ilinifanya niamini kuwa, kweli nilikuwa katikati ya maskani ya kichawi.
“Bila kupoteza muda sasa tunaingia mitaani, hasa kwenye nyumba za waumini wa kanisa ambalo padri wao tunaye kwenye kundi letu na kufanya kazi ya kuwatesa, sawa?” Sauti nzito, iliyokuwa ikisikika na kitetemeshi ilisema.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipomwangalia msemaji huyo, ni mzee mmoja aliyekuwa amevaa kanzu ndefu nyeusi, juu, yaani kichwani alivaa pembe za mnyama, mkononi alishika mkia, pia wa mnyama.
“Sawa,” wenzangu waliitikia kwa sauti ya juu.
Kifupi mimi nilikuwa sijui kitu chochote. Nilikuwa sijui watafanyaje huko kwenye kutesa watu, sijui nani atakayeteswa, kama ni waumini wote pia sikujua. Ila, mzee mmoja alinifuata na kuniambia:
“Tuondoke mimi na wewe.”
Nikawa namfuata hadi kando kando ya ule mti mkubwa, akasimama ghafla hadi nikamkumba.
Kufumba na kufumbua, tulitua nje ya nyumba ya muumini wangu mmoja ambaye anamiliki mashine ya kusaga na trekta moja.
“Haa! Hapa si kwa..?”
Kabla sijamaliza kusema, yule mzee akaniambia kwa kunikatisha:
“Ulisikia tulivyoambiwa kule?”
“Kwamba?”
“Tunawatesa akina nani?”
“Waumini wangu.”
“Sasa unauliza nini?” Alinijibu huku akitembea kwa kurukaruka kwa mguu mmoja.
Alipoona mimi nimezubaa akanifuata:
“Jipige kifuani kwa mkono.”
Nikafanye hivyo.
“Hapo sawa sasa, nifuate mimi kwa kila hatua mpaka ndani na kuanza kazi, sawa?” Aliniuliza.
Tulikwenda hadi kwenye mlango mkubwa, nikadhani atagonga ili tufunguliwe, kumbe sivyo bwana.
“Kila ninachofanya mimi na wewe unaniiga, sawa?” Aliniambia akinigeukia, kwani nilikuwa nimesimama nyuma yake.
“Sawa.”
“Haya tunaanza sasa.”
Alijipiga tena kifua na mimi nikajipiga. Kufumba na kufumbua tukawa ndani, sebuleni.
“Sasa niigize kwa kila kitu.”
“Sawa,” nilimjibu kwa sauti ya chini kama ile aliyoitumia yeye kuniambia.
Alitembea kwa kurukaruka kwa mguu mmoja, huku mguu wa pili ukiwa unaning’inia tu. Kwa mimi nilivyoona, hakukuwa na sababu yoyote ya kutembea vile, ila kwa kichawi nadhani ni sawa na ni kawaida kwao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Na mimi niliruka ruka kwa mguu mmoja huku mwingine ukining’inia hadi kwenye mlango wa kuingia kwenye vyumba, yule mzee akasimama, lakini kwa mguu mmoja.
Tulisimama vile mpaka mimi nikabadili msimamo, nikatumia mguu mwingine maana nilichoka sana .
Ghafla akaweka mguu mwingine chini huku akigeukageuka kuniangalia.
“Sasa tunaingia chumbani kwa baba mwenye nyumba, sawa?”
“Sawa.”
“Una swali lolote kabla hatujaingia?” Aliniuliza.
“Ndiyo.”
“Enhe, lipi hilo ?”
“Haaa…”
“Uliza haraka.”
“Sawa, hatutaonekana?”
“Wapi?”
“Tunakokwenda.”
“Kwani si nimekwambia kila kitu unaigiza kwangu?”
“Kabla sijaigiza je?”
“Hatutaonekana.”
“Basi, swali langu ni hilo tu.”
“Kwa hiyo huna swali jingine?”
“Sina na wala sitakuwa nalo.”
“Oke nifuate.”
“Niko nyuma yako.”
Aliinua mikono juu, akapiga makofi na mimi nikafanya hivyo hivyo. Kufumba na kufumbua tukawa tumesimama katikati ya chumba.
Yule mzee akanigeukia, akaniangalia lakini hakusema kitu. Mdomo akauangalizia juu na kufanya tendo kama anapuliza moto, na mimi nikafanya hivyo hivyo. Akamsogelea mzee mwenye nyumba aliyekuwa amelala usingizi mzito wa chali, akamkalia tumboni huku akijisotesha kuanzia kiunoni kwenda kifuani na kurudi.
Mimi nikawa mtazamaji tu, lakini yule mzee akaniangalia na kunipa ishara kwamba na mimi nimpandie mke wa yule mwenye nyumba ambaye alikuwa amelala kitanda kingine na mtoto mdogo kama wa mwaka mmoja.
Nilipanda bila kujiuliza maswali kwanini napanda, nikajisotesha kama alivyokuwa akifanya yule mzee, lakini nilipotua macho usoni kwa yule mama ambaye naye alilala chali, nikamjua kuwa ni muumini wangu mzuri pale kanisani.
Kusema ule ukweli niliumia sana moyoni, nikajihisi ni mtenda dhambi nisiyestahili msamaha wa aina yoyote ile.
Lakini ilinibidi niendelee tu na kazi niliyokuwa naifanya kwani ni jukumu ambalo nilishalivalia njuga sikuwa na budi kulimaliza sawasawa na safari yetu ya kuingia ndani ya nyumba ile.
Mara yule mzee alishuka kutoka kwenye tumbo la yule mzee mwenye nyumba huku akinifanyia ishara ya mimi pia kushuka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulishuka wote, tukasimama tukiangaliana. Mara mwenzangu akaufuata ukuta sehemu ya kichwani ya yule mzee, akasimama na kumwinamia kisha akapeleka mkono hadi jirani na shingo yake na kuukunja kama vile ameshika shingo na kumkaba.
Yule mwenye nyumba akawa anarusharusha miguu kama anayeitafuta pumzi baada ya kuziba kwa pua na kinywa, huku akisema maneno yasiyojulikana:
“Mmmh! Mmmmmm! Mmm!”
Alivyokuwa akiendelea kubana mkono ndivyo na yule mtu alivyokuwa akizidi kulalamika, sasa akapeleka mikono kwenye koo lake na kujishika huku akizidi kulalamika.
Alichofanya yule mchawi, akawa anambana huku mkono mmoja anafanya kama anamtisha kwa ngumi ya uso yule mzee. Alipokuja kumwachia, akasimama pembeni yake kisha yule mtu mwenye nyumba akashituka kutoka usingizini na kukaa huku akikohoa sana.
“Mungu wangu, Mungu weee! Ooo! Mama,” alisema akiendelea kushika koo lake.
Akamwita mkewe kwa sauti ya juu, naye akashituka na kumuuliza kulikoni:
“Kuna nini mume wangu?”
“Nimekabwa vibaya sana .”
“Na nani?”
“Najua ni wachawi tu hao.”
“Umejuaje?”
“Wamenishika koo kwa kunikaba kisha wakanipiga ngumi za uso. Kwani huoni kama umevimba?”
“Nini?”
“Uso wangu?”
“Hata, ila macho kama mekundu.”
“Ni hao hao lakini mmoja kama nimemwona.”
“Unamjua?”
“ Kama namjua.”
“Ni nani?”
“ Kama ..!”
“Vipi tena mume wangu?”
“Tumbo nalo kama limejaa, ooo linauma sasa, wachawi hao mke wangu.”
Mara mkewe naye akaanza kulia huku akishika tumbo lake na kulalamikia.
************************************************************************
Nilijifanya kushtuka na kwamba siyajui hayo huku ukweli ni kwamba, kila kitu alichokiaongea mimi ndiye nilikuwa kinara ingawa si kweli kwamba tuliwalimisha.
“Sasa waliwatambua?”
“Hapana, mchawi unaweza kumtambua?”
“Kweli huwezi.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Eee, mchawi hata akiwa baba yako au mama yako, anaweza kukuingilia na usimjue, labda kama una malaika wakali,” alisema.
Tuliagana, akaendelea na safari yake na mimi na safari yangu. Mbele nikasimamishwa na mzee mmoja, huyu mzee tunaelewana sana kupita wote wanaoabudu katika kanisa lile. ENDELEA…
“Bwana nilikuwa nataka kuja kwako,” alisema.
“Sasa?”
“Sasa basi, labda niongee hapa hapa.”
“Ongea mzee wangu.”
Alianza kwa kuniambia kuwa, kuna watu wanajiandaa kwenda kwa Askofu kutoa malalamiko kuhusu siku ambayo mimi nilipanda madhabahuni na pajama badala ya mavazi ya kitumishi.
Nilishtuka sana kusikia hivyo, nikamuuliza majina ya hao wazee, miongoni mwao ni wale wote waliosimama siku hiyo na kujifanya wanajua zaidi, akiwemo yule tuliyemcheza mpira yeye na mkewe usiku.
“Aaa, sasa kwani kuvaa pajama jamani si bahati mbaya tu, wao walichukuliaje?”
“Wao walichukulia ulikuwa unatuwangia. Na hivi sasa kanisa limegawanyika, wengine wanasema wewe ni mwanga, wengine wanakataa, Padri hawezi kuwa mwanga.”
“Wewe unanichukulia mimi ni nani?” Nilimuuliza yule mzee.
“Ni mtumishi wa Mungu aliye hai.”
“Sawa, usimwambie mtu maneno hayo, waache wafikirie hivyo hivyo.”
Tuliagana, akaondoka zake lakini mbele kidogo, nikasimamishwa na mwanamke mmoja, mzee sana, yaani bibi kizee, sijawahi kumwona hata siku moja. Lakini kwa rika langu angeweza kuwa mama yangu mzazi.
“Shikamoo mama.”
“Marhaba, hujambo mwanangu?”
“Sijambo mama, haya unasemaje?”
“Ah! Nina usemi basi, njaa tu.”
“Hujala mama?”
“Nimekula, tena nimeshiba sana,” alinijibu.
“Sasa njaa ya nini?”
“Nyama.”
“Nyama! Nyama gani mama, ya ng’ombe?”
Badala ya kunijibu, alinisogelea hadi mlangoni kabisa kwenye gari, akanyoosha shingo ili kunifikia sikioni.
“Nyama nzito.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mh! Mama, mbona sijakuelewa, nyama nzito ni ipi?”
“Ile yenye minofu minene.”
“Mbona siijui, ya nguruwe?”
“Hapana, ya mtu! Najua unaweza kufanya nikapata.”
Damu zilinisisimka mwili mzima, nikahisi kupoteza fahamu huku nikiwa nawaza yule mama alinifikiriaje au alisikia nini kuhusu mimi mpaka kusema maneno yale.
“Sasa mama, mimi nyama ya mtu nitaipata wapi?”
“Popote pale.”
“Kama wapi?” Nilimuuliza.
“Utanipa hunipi?” Aliuliza kwa sauti ya juu sasa.
Nilitaka kufunga kioo cha gari niondoke, lakini kwa vile sikuwa nimemjua kiundani sana, niliamua kuacha.
“Nataka uniletee nyumbani kwangu usiku wa leo.”
“Wapi?”
“N’takuonesha,” alisema huku akianza kutembea kwenda upande mwingine.
-
Sikujua atanionesha kwa mimi kumnyima nyama ya mtu au wapi atapatikana ili nimpe hiyo nyama. Niliamua kumpuuza na kuendelea na safari yangu.
Nilifika njia panda moja ambapo nilitakiwa kwenda kulia, lakini nikaona kuna mlima upande huo ambapo kawaida huwa hakuna mlima kama nilivyoona pale.
Nilisimama kwa muda wa kama nusu dakika nikiuangalia ule mlima. Ulianza kurefuka, ukaendelea kidogo kidogo huku ukiota majani ya kijani pembeni. Urefu wake ulizidi hata mlima Kilimanjaro, lakini kufumba na kufumbua ukafutika na kusindikizwa na sauti nzito.
“Huo urefu wa mlima ndiyo utakuwa wako katika ulimwengu wa kichawi.”
Ile sauti ikakata, barabara ikaonekana kama kawaida, nikaelekea upande huo.
***
Usiku wa siku hiyo, nikiwa nyumbani, nilianza kumfikiria yule mama aliyesema anataka nyama ya mtu na alivyoondoka. Pia nilifikiria ni kwanini baada ya kuondoka tu, mbele ya safari yangu ndiyo mlima mkubwa ukachipuka kimaajabu?
Nikiwa bado nawaza, nikachukuliwa na usingizi mzito sana, kuja kushtuka nikasikia filimbi ya kuitwa kwenye makutano yetu wachawi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilisimama, nikageuka kuangalia kitandani, nikanyoosha mkono pembeni na kuchukua shuka jeupe, nikalivaa kama taulo, kufumba na kufumbua nilikuwa kwenye makutano yetu. Waliokwishafika walikuwa wakipiga ngoma na kucheza huku wote waliokuwa wakicheza wakitumia mguu mmoja kutembelea eneo lile lote.
Baada ya wachawi wengi kufika, nilisimama katikati yao na kunyoosha mikono yangu juu, wakatulia, nikapiga makofi, wote wakaunga kwa makofi.
“Pa pa pa pa pa!”
Kabla sijasema, mwanamke mmoja wa kanisani ambaye pia ni mchawi alipita mbele akasimama jirani yangu, huku akiinamisha kichwa akasema:
“Unanikumbuka mkuu?”
Nilimwangalia kwa umakini sana, nikawaza kwanini anasema vile wakati wachawi wote wa kanisani tunajuana na ni siri yetu.
“Nakufahamu vizuri sana,” nilimjibu nikimkazia macho.
“Uliniona wapi?”
“Khaa! Wewe si tuko pamoja hapa na pia kule kanisani?” Nilimhoji.
“Ndiyo najua, lakini je, hukumbuki leo tumeonana mahali?”
“Sikumbuki, labda unikumbushe wewe.”
Alinikazia macho huku taratibu akianza kuzeeka na nguo alizovaa zikianza kubadilika. Ilifika mahali akawa ni yule bibi kizee aliyeniomba nimpatie nyama ya mtu na kusema atanionesha.
“Ha!” Mimi nilishtuka kumwona akiwa vile.
“Ee,” alisema.
“Si umenikumbuka sasa?”
“Ndiyo mama.”
“Haya endelea,” alisema akarudia katika hali yake ya kawaida.
Kifupi sikuwa nimejua maana ya tukio lile. Lakini pia sikutaka kuhoji wala kuuliza kwa mchawi mwingine.
Mimi niliendelea kuongea maneno ambayo hadi leo huwa najiuliza yalitoka wapi!
“Leo ni siku ya kupanga mikakati mikubwamikubwa ya kuangamiza watu, hasa wale wanaojifanya wanakwenda sawa sawa, sawa?”
“Sawa,” walinijibu.
Niliwaambia nimetumwa kutoka kwa kiongozi mkuu wa wachawi duniani kote akisema kuwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanawake wanaozaa salama.
“Si kweli jamani?”
“Kweli.”
Nikawaambia miongoni mwa mikakati inayotakiwa kufanywa ni pamoja na huo, kuhakikisha wanawake kuzaa salama kunapungua na ikiwezekana kufa kabisa, kivipi?
“Tunatakiwa kuhakikisha tunawashughulikia wajawazito wote ili wanapokwenda kujifungua wapasuliwe, sawa?”
“Sawa.”
“Kingine! Kingine, ni kuchukua damu za watoto wachanga waliopo matumboni.”
Watu walipiga makofi sana, ikafika mahali wakawa wanachezacheza.
“Sasa kwa kuanza kazi hii, usiku huu huu tunaanza kuingia mitaani mpaka asubuhi. Halafu tutarudi majumbani kupumzika kama saa moja tu, kisha tutatoka tena na kurudi mitaani kushughulikia wanawake wanaokwenda kliniki asubuhi, sawa?”
Walisema sawa huku wakitawanyika katika vikunndi vidogovidogo vyenye wachawi watano watano.
Wachawi siku zote wanapenda sana hilo, miongoni mwa masharti yao ni kutumia namba zisizogawanyika kwa mbili katika kila walifanyalo, mfano, kutembea katika makundi ya watu watatu, watano, saba, tisa, kumi na moja.
Au hata wanapotaka kutengeneza kitu kwa siku, hupenda kutumia namba hizo hizo, siku tatu, tano, saba, tisa nakadhalika. Hizi namba hupendwa hata na waganga wa kienyeji, mara nyingi akikupa dawa au masharti fulani atakwambia utafanya hivi kwa siku tatu, tano, saba, tisa na kuendelea.
Ndivyo walivyoondoka wachawi wenzangu, na mimi nikaongozana na wengine wawili, jumla tukawa watatu.
Kila safari ilikuwa na kinara wake, kwenye kundi langu mimi niliendelea kuwa kinara katika safari hiyo.
Mimi na wale wenzangu tulikwenda kuingia kwenye nyumba moja ambayo tulikuwa tukiamini kuwa, kuna mwanamke ambaye ni mjamzito.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni ajabu, kwani kwa muda huo tulimkuta yeye na mumewe wamekaa sebuleni wanaongea, mtoto wao mmoja alikuwa amelala kwenye kochi kubwa hapo hapo sebuleni.
Niliwasimamisha wenzangu ambao walikuwa nyuma yangu, wakasimama huku wakipeleka vichawa pembeni kuona mbele. Nilisimama na kuwageukia wote nikalaza kidole changu kwa kuwawekea alama mdomoni kama ishara ya kusema shiiii.
Nilipomaliza kufanya kwa ishara hiyo, niliwageukia wale watu, nilimsogelea yule mwanamke maana lengo sasa lilikuwa ni kuhakikisha namtoa mtoto ndani ya tumbo.
Nilipomfikia na kuwa naye sambamba, nilinyoosha mkono na kulishika tumbo bila mwenyewe kufahamu kama anashikwa tumboni.
Nililiminyaminya lile tumbo, nikautembeza mkono kila kona huku naendelea kuliminya, ghafla alishtuka na kulishika tumbo lake kwa maumivu ya kushtukiza.
“Nini tena?” Mumewe alimuuliza na yeye akionekana ameshtuka sana.
“Tumbo mume wangu, tumbo,” alianza kulia.
“Linafanyaje?”
“Linakata sana mume wangu.”
Mumewe alisimama, wakati huo huo mimi nilirudi nyuma na kusimama na wenzangu mstari mmoja. Tukawa tunaita kwa mikono, ghafla kitoto kichanga kikiwa hewani kilielea kuja kwetu tukiwa tumekinga mikono ili kukipokea kisigonge ukuta. Lakini wakati wote huo, yule mwanamke alionekana bado ni mjamzito kama awali huku akiendelea kulalamikia maumivu ya tumbo lake. Nilikibeba kitoto kile na kukielekezea juu kisha nikamkabidhi mchawi mwingine aliyekuwa kushoto kwangu. “Twende hospitali basi,” alisema mume, lakini mke hakujibu kwani alikuwa tayari kwa lolote lile ambalo lingetokea. Na sisi tulikubaliana kwenda mpaka huko hospitali kuangalia kitakachotokea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment