Simulizi Fupi : Dracula
Sehemu Ya Pili (2)
Ilipoishia jana..
Bw. Kiseto alibaki amekaa pale hajielewi macho yake hayakuweza kufumba yalibaki pima, mboni zake hazikuwa zikicheza aliganda tu kama kinyago cha mpapule, mfumo wa taka mwili ulishindwa kufanya kazi yake vyote viliishia hapo na yeye mwenyewe alibaki katika hali hiyo hiyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Songa nayo sasa…
Polisi wa doria walifika nyumbani kwa Bw. Kiseto usiku ule maana baada ya kutaka kumsimamisha wakashangaa yeye anatimua mbio hivyo wakaanza kumfuatilia na mwisho walifika katika nyumba hiyo, nyumba iliyojitenga peke yake, njyumba kubwa sana hata kimo chake kwenda juu kisingemfanya aliye ndani kulalamikia joto, nje ya nyumba hiyo kulikuwa na miti mirefu na mingi iliyofanya kivuli safi wakati wa jua, nyasi za wastani na maua ya kuvutia. Usiku ule jumba lile liling’azwa na mataa mzauri ya nje na kumfanya aingiaye kuona hata pini iliyoanguka hapo. Polisi wale wakashuka katika gari yao wakiwa na bunduki zao walipokaribia mlango wa jumba hilo taa za nje zikazimika zote, wote wakshofu na kurudi nyuma
“Oya, analeta janja ya nyani tu, songa mbele tutoke naye” mkuu wa doria hiyo alitoa amri kwa vijana wake wakakamavu. Wakiwa bado wamesimama mbele ya ule mlango, mmoja wao alisogea kuugonga mara kaupepo kakali kakapita kati yao kana kwamba kuna kitu kimepita kwa kasi kuelekea upande wa pili, miili yao ikasisimka na nywele kuwasimama
“Washikaji hapa sio penyewe” yule aliyekuwa mlangoni alishuka ngazi na kuwaeleza wenzake.
“Mnakuwa kama wanawake bwana” kiongozi wa doria aliwasema wenzake na akashuka kwenye gari kuiendea nyumba hiyo, kabla hajafika waliona kiumbe kile mbele yao meno yake mekundu marefu kikimsogelea yule kiongozi wa doria, kikamkamata kwa mkono wake mmoja na kumng’ata shingoni kwa meno yake makali kilitulia pale kwa muda kisha kikamtupa chini yule polisi akiwa mfu, na kutoweka kama kilivyokuja.
“Dracula!” mmoja wa wale polisi alijikuta akitamka na papo hapo alipoteza fahamu.
???
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hospitali ya mkoa wa Kahama ilifurika watu, wengi wao wakija kumuona Bw. Kiseto baada yakusikia mkasa uliyomkuta, kila aliyeingia hakutaka kuingia tena.
Bw Kiseto alikuwa amekaa kitandani kajikunyata kama mtu anayesikia baridi kali sana macho yake yalikuwa yamekodoa bila kufunga alikuwa hawezi hata kuongea mara kwa mara alikuwa akiweweseka tu na kulia machozi hakuna alichosema zaidi. Ilikuwa kazi ngumu sana kwa madaktari bingwa kuweza kupata kujua ni nini kimemtokea.
Bw. Kiseto aliona kiumbe cha ajabu ambacho hajawahi kukutana nacho maishani, lakini pia hakujua ni vipi kimemfuata yeye tangu kule barabarani usiku ule.
Polisi hawakuwa na la kufanya baada ya mmoja wao kufa kifo kilekile, na yule aliyeshuhudia tukio hilo alianguka akapoteza fahamu na mpaka sasa unaposoma simulizi hii hajaamka. Mkuu wa Polisi OCD Magari alibaki kuzungukazunguka tu mle ndani ya ofisi yake hakujua afanye nini, moyo wake ulishikwa na jinamizi la hasira angetamani aonane na huyo kiumbe mnyonya damu, lakini angemfanya nini. Aligundua kuwa sasa wanapambana na ulimwengu wa giza. Kichwani uamuzi wa kuwakusanya waganga wa jadi ulimjia lakini akaona si busara kwani wao bado hawajashindwa kazi, mara alijiuliza kama risasi zao na mabomu vinaweza kumteketeza kiumbe huyu lakini alijiona yeye ni mpumbavu kwa wazo hilo kwani kiumbe mwenyewe haonekani ovyo, kazi kwelikweli!
???
Mzee Shukuru Masoso, askari mstahafu alikuwa shambani asubuhi hiyo akipalilia mahindi yake, alifurahi sana kwa kuwa shamba lake hilo lilimpa mazao sana, ardhi ilikuwa na rutuba ya kutosha, akiwa na kofia lake kubwa la kukinga jua aliendelea kupiga mruzi huku akifanya palizi katika mahindi yake bila wasiwasi wowote. Katika kichaka kilicho mbele yake alisiki kitu kama mlio wa panya aliyebanwa na mtego, akpuuzia na kuendelea na kilimo chake, mlio ule uliongezeka na kuyasumbua masikio yake akaokota jiwe na kurushia katika kichaka hicho na kubaki akiangalia, sekunde kama tano jiwe lile lilirushwa kutoka ndani ya kichaka kile na kumpiga kichwani, Mzee Shukuru alitoa yowe la uchungu na kupepesuka damu ikimtoka katika paji la uso, alihisi kama kitu kikimtambaa mguuni aliinama kuangalia hakuamini macho yake, mguu wake ulikuwa unavimba na kutoa majimaji meupe mazipo kwenye ncha za kucha zake, alijikuta hawezi kuunyanyua mguu kana kwamba umeota mizizi eneo lile, alipiga kelele za msaada ma ra wanakijiji walifika kumsaidia, waliliona jembe lake lakini mwenyewe hawakumuona, walisimama mbali wakasikia sauti yake kule walikotoka, walipoona mambo magumu wakatimua mbio mpaka ofisi ya kijiji kutoa taarifa kisha kuripoti polisi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Polisi waliingia ndani ya shmba lile wakiwa na mbwa waliokuwa wakipiga kelele na kuongoza njia kuingia mpaka shambani, walifika eneo la tukio lakini hawakuona mtu wala kitu isipokuwa jemba lilikuwa liko palepale hakuna aliyeliondoa. Wakijaribu kutafuta huku na kule wakisaidiwa na mbwa wale wenye mafunzo maalimu lakini haikusaidia kitu, mzee Shukuru Masoso alikuwa ametoweka.
Baada ya zoezi lile lililochukua takribani nusu saa na halikuzaa matunda polisi wale waliondoka kurudi kituoni.
???
Nyumba ya marehemu mzee Bushir Sultan, ilikuwa imejengwa ndani ya msitu kidogo sehemu yenye utulivu sana ikizungukwa na miti na maua ya kila aina, ilivutia kwa kila aliyepita mbele yake. Nyumba hii hata tangu alipoishi mwenyewe Bushir ilikuwa ni nyumba iliyo kimya sana hakuna mtu aliyekuwa na mazoea na nyumba hii hata kidogo, si mchana si usiku ukimya uliotawala hapo kila mtu aliutilia shaka, wengine walisema Bushiri ni mnyonya damu, wengine waliamini kuwa si binadamu wa kawaida ili mradi kila mtu alitafsiri ukimya huo kadiri ya fikra zake.
Wengi waliuliza kama Bushiri alikuwa na mke lakini hawakupata jibu katika hilo, miaka ilienda na siku zikapita, mzee huyu tajiri aliyekuwa na maduka mengi katika miji tofauti alikuwa maarufu na wengi walimwita ‘mzee wa manyoka’, wapo baadhi yao waliodiriki kusema kuwa mzee huyu alikuwa akifuga majini, kila mtu aliamini maneno haya.
Hata siku alipokufa mzee huyu watu waliogopa kwenda msibani kwa kuwa wote waliokuja walikuwa wamevaa manguo meusi yaliyowafunika mwili mzima, hakuna aina yoyote uombolezaji ulioonekana hapo zaidi ya harufu za udi na ubani ambazo zilitapakaa eneo lote. Baada ya msiba ule kuisha nyumba ile ilikuwa ikikaa peke yake hakuna mtu aliyeishi ndani yeke. Wazungu waliokuja katika kuchimba madini wa kampuni ya Mkurabita Goldmines waliikodi nyumba hii na kuifanya ya kampuni, kila aliyeishi humo hakuchukua muda mrefu akahama akilalamika ndani humo hamkaliki kutokana mambo ya ajabu yanayoonekana usiku au hata mchana, wengi walilalamika kuwa wakiamka asubuhi hujikuta chini ya vitanda lakin hawajui ni nani aliyewahamisha na kuwaweka chini humo. Familia kama sita zilipita katika nyumba hiyo mpaka sasa Bw Kiseto alipewa nyumba hiyo, wengi walimwambia juu ya nyumba hiyo lakini Kiseto aliona kuwa wanambania labda wana wivu kwa kuwa yeye kapewa nyumba kubwa. Alihamia na kuanza kuishi ndani ya jumba hilo tulivu. Bw Kiseto alikuwa haamini kabisa juu ya yasemwayo kuhusu hilo ndipo siku moja alipojikuta.
*********************************
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
???
“Ile nyumba, mwenyewe Bushiri aliambiwa pale asinunue kiwanja kwa sababu palikuwa n makaburi ya kale” sauti ya kizee ya kitetemeshi iliingia masikioni mwa Amata, babu huyu aliyekula chumvi nyingi wengi waliamini kuwa ni mchawi, siku hii alikutana uso kwa uso na kijana huyu machachari aliyekuja kijijini hapo kuchunguza vifo hivi vya ajabu chanzo ni nini.
“kutokana na mihela aliyokuwa nayo akanunua lile eneo, si unajua jeuri ya pesa mjukuu wangu, akabomoa yale makaburi na kujenga ile nyumba.”Amata alikuwa akisikiliza kwa makini bila kuuliza swali.
“Yeye akahamia na mkewe akafuata baadaye, walikaa pale kama miaka miwili, hatukuwa tunamuelewa yule bwana, mara utsikia harufu ya ubani mara udi. Siku moja jioni tuliona watu wengi wamevaa nguo nyeupe wako pale, tukashangaa sana watu wale wametoka wapi, muda kidogo tu hatukuwaona tena” Mzee yule akakohoa kidogo na kujiweka sawa katika kijikiti kile alichokalia
“Unasikia mjukuu, yule Bushiri hakuwa mtu wa kawaida hata kidogo, alikuwa anafuga madudu mle, akikaa na wafanyakazi wandani utaona tu hawaonekani tena, kumbe yale madudu yake huwa yanataka damu, na wafanyakazi wake wote walikuwa hawatoki kijijini hapa, unasikia?” Amata akatikisa kichwa kuashiria kuwa anasikia na kuelewa vyema, mpaka hapo hakuwa ameuliza hata swali, alikuwa tu anafuatilia simulizi ile ya kusisimua, babu akaendelea,
“Sasa yale madudu yake yakawa mengi yamemzidi uwezo, hayatoshelezwi na damu, yakaanza kuua watoto wake mwenyewe” Amata akajikohoza kidogo na kumkatisha babu
“Sasa babu, kwa nini Bushiri alikuwa anafuga hayo madudu, sijui manini hayo!?” Amata aliuliza
“Yule bwana alikuwa na biashara ya madini, hivi hilo shimo hapo yeye ndiyo muanzilishi hawa wajeremani wamekuja siku hizi tu, sasa yale ndiyo yalikuwa yanamfanyia kazi na vibarua wengi wamekufa mle, wote hao kafara” Babu alijibu swali la Amata, na kuendelea kuhabarisha
“Wakati mke wake yupo walikuwa na msichana wa kazi mdogomdogo tu, siku moja yule msichana alikuja hapa kwangu kwa kukimbia kufika tu hapa akazirai, baada ya kuamka akanisimulia yaliyomkuta. Amekaa sana kwangu hapa nikamfanyiafanyia dawa hapa ili yasimrudie hayi madudu” akatulia kidogo na kuendelea
“Hali ni mbaya pale, baada ya kufa mwenyewe Bushiri ile nyumba ilibaki hauna mtu lakini usiku utaona taa zinawaka, nani kawasha humjui. Kuna familia ikaamia asubuhi wanaamka wanakuta sebule yote imajaa damu, wakifungu mabomba yanatoa damu, ndoo za maji zina damu, wakashindwa wakahama. Na wengine hivo hivo, ile siyo nyumba mjukuu kuna mdudu mle. Sasa we kijana wangu una dawa gani maana yale sio watu” babu ailimuuliza Amata
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Aa Babu, mimi sina dawa yoyote, nimekuja kufanya uchunguzi wa nini tatizo na tutamaliza vipi” Amata alimjibu yule babu kizee
“Aaaa acha kabisa huo mchezo mjukuu, utapoteza maisha. Sasa hivi yale madudu yametoka nje ndiyo maana unaona vifo hivi, yenyewe yanataka damu tu na si kingine, ynakunyinya damu yoooote yanakuacha hapo. We usijiingize hapo hata kama ni kazi angalia na kazi za kufanya, waulise wenzako hao wamekiona cha mtema kuni wiki jana hapo” babu alimaliza simulizi yake na kuchukua ugolo wake tayari kwa kuvuta. Kaupepo kwa ghafla kakapita katikati yao na kutikisa mimea midogomidogo iliyopo hapo jirani, Amata na afande aliyekuwa nae hapo wakashtushwa kidogo na hali hiyo.
“Msiogope, wamepita tayari” Babu alimwambia Amata na mwenziye. Amata hakuelewa maana ya maneno hayo.
“Sasa babu kwa nini ninyi msiyadhibiti madudu hayo?” Amata alimchokoza kwa swali
“Mjukuu, si kitu kidogo unachokisema, kumbuka hayo madudu hayatumii nguvu za kawaida. Yameanza kutoka nje siku hizi baada yakukosa chakula chao. Una haki kuuliza hilo swali mjukuu, hata sisi tunajaribu lakini ni vigumu sana, ni vigumu sana kwa kweli” babu alimjibu Amata
“Sawa, babu mimi nimekuja kuhakikisha hali hii haitokei tena” Amata alimwambia yule babu.
“Kijana, una nia njema sana lakini huwezi kupambana nayo hivi hivi lazima uwe na kinga” babu alimueleza Amata
“Sawa, nipe hiyo kinga sasa ili nianze kazi mata moja” Amata alitoa ombi kwa babu huyo
“Uje kesho saa sita mchana jua likiwa la utosi. Uje na nyoya jeupe la kuku, sawa?”
“Sawa babu!” Amata alijibu na kunyanyuka, wakapeana mikono na yule babu kisa wakaondoka zao.
Amata akiwa chumbani kwake katika nyumba ya wageni aliyofikia, alishtuka usiku wa manane, kijasho chembaba kikimtiririka na kamasi jepesi, hewa iliyochanganyika na pilipili ilikuwa ikipita karibu na pua zake, alivuta kamasi kurudisha zilikotoka lakini haikusaidia, ziliendelea kutoka. Mezani aliona kitabu alichokuwa akisoma muda si mrefu kikijifunua chenyewe kurasa moja baada ya nyingine, macho yalimtoka pima, hakuelewa ni nini kinachoendelea. Kitabu kile kiliendelea kujifunua kurasa zake sasa kikiongeza kasi kidogo, kadiri kurasa zile lilivyojifunua ndivyo upepo nao aulitengenezwa na funusho hilo. Sasa kurasa zile zilikuwa zikifunuka kwa kasi na hazikutulia na upepo nao ulizidi kuvuma chumbani mle, ndani ya upepo ule alianza kusikia sauti ya mtu akiongea ‘Amata ga Imba, damu, damu, damu, mauti, mauti, mauti’ sauti ile ilizidi kuwa kuongezeka ikichanganyika na mwangwi wa sauti za ajabu na za kutisha. Amata alifuta kamasi lililokuwa likitiririka puani lakini aligundua si kamasi tena bali damu nzito ilikuwa ikitoka puani mwake.
“Aaaaaaaahhhh!!!!” Amata alipiga kite cha ukulele, mara ghafla upepo ulikatika na kitabu kile kiliacha kujifunua na hali ikawa shwari ghafla. Amata alikurupuka kitandani akihema, du! Ndoto zingine bwana… hivi we ushawahi kuota ndoto kama hizi?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
???
“Konstebo Magreth, utafanya kazi sambamba na Kamanda Amata katika mchakato huu. Wengine mtakuwa tayari katika hali ya hatari muda wowote mtaitwa kutoa msaada. Patrol lazima ziendelee usiku wa leo kama jana” OCD Magari aliongea kwenye kikao cha dharula, alichoitisha ofisini mwake ili kupanga kazi katika kupambana na adui asiyejulikana.
“Ha! Mimi mkuu, ntaweza kweli?” Konstebo Magreth aliuliza huku akitetemeka
“Ndiyo, wewe. Katika wote hawa nimeona wewe ndiyo unaweza kuingia katika pambano hili” OCD Magari alikazia uamuzi wake. Kila aliyekuwa kwenye kikao hicho alimtumbulia macho OCD, hakuna aliyemuelewa anachokizungumza. Askari wote walikuwa na woga hasa kwa tukio la jana usiku la mwenzao aliyekumbana na Dracula wakati wakitaka kumkamata Bwana Kiseto, na mwenzao aliyezimia mpaka sasa unavyosoma bado hajaamka na hatuna mategemeo labda tumpeleke India.
“Afande!” Koplo Sijali alisimama kwa ukakamavu kabisa “adui tunaepambana nae katuzidi uwezo kwa kila hali, kwanza haonekani. Hivi afande itakuwaje maana tunaweza kwisha sote na yeye akabaki anavinjari”.
“Kiapo ulichoapa pale CCP kilikuwa ni kulinda raia na mali zao, sivyo afande?” OCD aliuliza, na wote wakaitikia “Ndivyo”, kisha akaendelea “ni jukumu letu kupambana na adui awaye yote, awe Pepo au mzimu, na lazima ushindi huwe kwetu” alipotoa kauli hiyo minong’ono iliijaza ofisi ile. OCD akagonga fimbo yake mezani kuomba ukimya kisha akaongea kwa sauti ya chini;
“Hivi Kamanda Amata ni binadamu au siyo binadamu?” aliuliza huku akiwakazia macho kisha akaendelea “Mbona amekubali jukumu alilopewa na ofisi? Kwa nini sisi tuogope?” sasa aliongea kwa ukali kidogo.
“Twende tukamsake, awe Kinyamkera au yoyote” alimaliza na kufunga kikao kile cha dharula.
*********************************
::: Je Nini kitaendelea katika simulizi hii matata na ya kusisimua?? LIKE na COMMENT bila kusahau SHARE ni muhimu katika ukurasa huu wa simulizi ili Simulizi iweze kuwafikia wengi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment