IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
*********************************************************************************
Simulizi Fupi : Dracula
Sehemu Ya Kwanza (1)
Nyumba ilikuwa ikitikisika, makabati ya vyombo na vitabu yalikuwa yakianguka huku na kule, hakika hali ilikuwa tete kabisa, hakuna aliyevumilia kila mtu alikimbia na kujificha alikojua yeye, Paulina na Paulino walijibanza chini ya meza kubwa ya chakula na kitambaa cha meza hiyo kiliwafunika wasionekane, mama yao Bi Kiseto alijifutika ndani ya kabati la nguo akijizungushia makoti ya mumewe mzee Kiseto ambaye mpaka wakati huo hakuwa amerudi kazini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Upepo haukuwa wa kawaida taratibu vitu vya mle ndani vilianza kuzunguka mduara vikipiga kelele, watu watatu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo hawakuwa na lakufanya hamna aliyethubutu kutoka mafichoni alipo, madirisha yalifunguka yenyewe na milango kujibamizabamiza ovyo. Mara nyumba ile kubwa ikaanza kutetemeka na kufanya hali ya kuogofya zaidi. Bi Kiseto kule alikokuwa aliwakumbuka watoto wake, moyo ulimuuma sana hakujua afanyeje kila alipotaka kutoka hali ile ilimuogofya lakini afanyeje aliona bora afe lakini awe kafanya lolote kwa watoto wake hao wadogo, alipiga moyo konde na kuamua kusukuma mlango wa kabati lile, alipojaribu kuusukuma akakuta ukibamizwa tena na sasa ukafungwa kwa nje. Bi Kiseto alianza kulia kwa uchungu akiwa hajui sasa afanye nini juu ya watoto wake Paulina na Paulino.
Sauti kama za watu waliokuwa wakiongea kwa kukoroma zilisikika sebuleni, Bi Kiseto alijua sasa watoto wake wanakufa, hakujua ni nani au ni nini kinachotokea huko nje ya kabati.
Paulina na Paulino walitulia palepale wakiwa wanatetemeka kama wagonwa wenye homa kali, walichokuwa wanakiona hapo hakikuwa cha kawaida hata kidogo, mioyo yao midogo ilienda mbio kuliko uwezo wake, bahati nzuri walitulia pale kwa utulivu mkuu, hakuna aliyepiga kelele wala kujitikisa.
Mara mlango ukagongwa na kila kitu kikanyamaza na kurudi katika hali yake ndani ya sekunde mbili tu. Mzee Kiseto alifungua mlango na kuingia ndani, alishangaa hakuna mtu wa kumlaki kama kawaida ya watoto wake wafanyavyo siku zote.
“Paulina!!!” Mzee Kiteto aliita, lakini hakusikia muitiko wowote
“Paulino!!!” Bado hali ikawa ile ile
Akavuta hatua chache kuingia sebuleni, akawasha luninga iliyokuwa hapo akatazama kidogo kasha akaenda chumbani kwake
“Mama P!!!” alimwita mkewe lakini ukimya ulitawala. Akajitupa kitandani na kushusha pumzi ndefu hakujua familia yake imeenda wapi. Mara akasikia kabati likigongwa, Mzee Kiteto alishtuka na kuinuka kutoka pale kitandani na kulielekea kabati lile akafungua kikomeo na kuuvuta mlango, hakuamini alipomuona mkewe akitweta kama mbwa aliyekimbizwa.
“Mi sitaki, sitaki mume wangu hii nyumba tuhame” alimueleza mumewe huku akitoka ndani ya kabati lile akiwa kaloa jasho mwili mzima.
“Paulino na Paulina!” Bi Kiseto aliita huku akielekea sebuleni. Paulino aliposikia sauti ya mama yake akamvuta mkono dada yake, Paulina na kuelekea chumbani kwa wazazi wao, wakiwa wanalia walimkumbatia mama yao, baba yao alibaki akishangaa tu hakuelewa ni nini kinaendelea ndani ya nyumba hiyo.
Mzee Kiseto aliketi kitandani na kujishika tama akitafakari hali ile, haikuwa mara ya kwanza kwa familia yake kumlalamikia juu ya mauzauza wanayoyaona ndani ya nyumba ile, lakini daima alikuwa hakubaliani nao ‘tatizo mnapenda sinema za mazombie ndiyo maana mnaona maluweluwe’ kauli ya mara kwa mara kwa mke na watoto wake, lakini leo yeye mwenyewe alikuta mambo tofauti nyumbani hapo. Alitafakari afanyeje lakini hakupata jibu, aliamua kwenda kuripoti ofisini siku ya pili yake juu ya mambo hayo ambayo yanaitokea familia yake katika nyumba hiyo ambayo ni miezi sita tu tangu kampuni yao impangishie.
Alichukua muda kuwaweka sawa watoto na mama yao na siku hiyo aliamua kuwatoa out ili kuwapa faraja. Japokuwa yeye mwenyewe bado hakuamini hayo wanayosema ila kwa wakati huo kidogo alianza kupata hisia za mauzauza hayo.
???
Polisi wa doria waliokota maiti ambayo shingoni ilikuwa ina jeraha kubwa, jeraha ambalo baada ya kulichunguza waligundua kuwa ni jeraha lililosababishwa na meno makali ya mnyama Fulani.
“Marehemu anaoneka ameshambuliwa na mnyama Fulani kama Simba au Chui, kutokana na vipimo vyetu, lakini tunachoshangaa ni kuwa mwili huu hauna damu kabisa na ninyi kwenye ripoti yenu mmesema hamjakuta damu katika eneo la tukio, hii inashangaza!” Dr Kimbell aliwaeleza maofisa wa polisi waliokuwa hapo.
Maofisa hao wa polisi walishangaa kwa kuwa katika eneo la tukio hapakuwa hata na michirizi au miburuziko kusemakuwa marehemu huyo alietwa hapo kutokea eneo lingine, utata!
“Vijana, inabidi tufanye uchunguzi wa kina katika hili” Sergeat Kibona aliwaeleza vijana wake, kasha wakatoka kurudi kituoni.
Taarifa ya daktari ilifika kwa OCD Magari na kuisoma kwa umakini huku akiirudia rudia japokuwa ilikuwa ikimchanganya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Simu ya kituo cha polisi iliita pale kaunta
“Helo, hapo ni polisi?” sauti ya pili ilisikika wazi kuwa ni mtu anayetweta kwa woga
“Ndiyo hapa ni kituo cha polisi, unaongea na Konstebo Magreth, nikusaidie nini” simu ilijibiwa na Konstebo Magreti aliyekuwa zamu mchana huo
“Kuna mtu amekufa hapa, mtaa wa Mkanyageni karibu na shule ya msingi, tunatoa taarifa” mara simu ile ikakatika.
*********************************
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Konstebo Magreth alitoa taarifa hiyo kwa wengine na mara moja ikaamriwa gari kuelekea eneo la tukio haraka.
Muda mfupi tu defender ya polisi iliwasili eneo hilo na kukuta kundi la watu likiwa likiwa limezunguka eneo hilo, walipiga king’ora kidogo ili watu kupisha.
Maiti ya mwanamke ililala kifudifudi huku shingoni ikiwa na jeraha kubwa sana ambalo lilikata mshipa mkubwa wa damu. Waliipiga picha maiti ile na kuibeba kuipakia kwenye gari baada ya mahojiano machache na walioshuhudia tukio hilo.
Majibu ya uchunguzi wa daktari yalikuwa yaleyale hakuna lililobadilika. Picha ishirini na tano za marehemu wa mtindo huo zilikuwa mezani kwa OCD Magari, yeye na jopo lake walikuwa wakiziangalia na kuchunguza kwa makini pamoja na taarifa zote za kidaktari, haikuwa kazi rahisi kama ambavyo wewe ungefikiri. Mjadala nao ulikuwa mzito sana wengine wakisema ‘itakuwa ni Simba au Chui’ wengine wakisema ‘hapana Simba na Chui wasingeweza kunyonya damu na kuacha nyama’ , basi hakuna jibu la uhakika lililopatikana.
“Tangu nimeanza kazi hii sijawahi kukutana na vitu kama hivi” OCD Magari alitoa lake la moyoni.
“Haya ni mapepo mkuu” Askari mpelelezi alitoa hoja yake
“Yaani we mpelelezi mzima unaamini mapepo!” OCD alifoka.
“Ok sasa leo usiku, tufanye doria kali mitaa yote tuhakikishe tunajua ni nini chanzo cha vifo hivi, halafu polisi wengine wavae kiraia waingie maeneo yote tuliyookota maiti hizi wadodose dodose kama kuna story yoyote juu ya hili.” OCD alimaliza na kikao kikaghairishwa.
???
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Bw Kiseto, sisi tumekupa ile nyumba kwa heshima ya cheo chako kazini, wewe unatuambiaje kuwa eti nyumba ina mauzauza? Mbona sikuelewi?” Mkurugenzi wa Mkurabita Goldmines Bw. Alexander Gosh alimueleza Bw Kiseto kwa upole.
“Familia yangu inateseka, kila siku siamini hilo lakini jana nililoliona nyumbani limenifanya kuchukua hatua hii.” Bw. Kiseto alimueleza mkurugenzi wake.
“Ok nitalifanyia kazi. Promise!” Alexander Ghosh alimaliza kuzungumza na Bw. Kiseto na kuagana.
Siku hiyo haikuwa nzuri kabisa kwa Bw. Kiseto, mchana huo alituma gari la ofisi na kuwachukua watoto wake kuwapeleka mjini kwa dada yake wakakae kwa muda mpaka atakapopata ufumbuzi wa jambo hilo.
Bw Kiseto hakuwa mnywaji wa pombe lakini siku hii alikunywa pombe nyingi sana hata alikuwa akipepesuka njia nzima, mara ajikwae na kuanguka kisha alijicheka mwenyewe na kuongea maneno ya ajabu ajabu
“mke wangu na watoto wanasema eti mauzauza, mauzauza? Ndiyo madudu gani hayo?” aliongea kwa sauti ya kilevi huku akiyumba njia yote na chupa yake ya Safari Lager mkononi, akasimama na kujipigapiga kifuani kuonesha umwamba
“Sikuogopi hata kama wewe Shetani, ulikuwa unamuonea yule mwanamke na watoto njoo kwangu mimi Kiseto wa Kiseto nimezaliwa kule kulikoungua shoka ukabaki mpini, usilete hadithi za Msitu wa Solondo hapa” aliendelea kuongeaonge na njia nzima alikuwa peke yake maana watu wote walikuwa wakiwahi kulala siku hizo kutokana na vifo vya ajabu vilivyowapata wengi.
“We mlevi!” askari wa doria waliita huku wakimfuata Bw. Kiseto
“Mlevi baba ako!” Kiseto aliwajibu wale polisi huku akirudi nyuma mara akajikwaa na kuanguka kwa nyuma, kabla ya yote kwanza alianza kuitafuta pombe yake lakini hakuiona alipogeuka mbele alimuona mtu mwenye tambo kubwa macho yake ni mekundu yaking’aa katika giza, Kiseto alikata network na alipozinduka alinyanyuka haraka na kutimua mbio, alikimbia kwa mbio zake zote japokuwa alikuwa na kitambi lakini siku hiyo alijiona yeye ana uwezo wa kumfunika Hussein Bolt, kila alipogeuka nyuma alimuona mtu yule naye akija kwa kasi kweli kweli, Kiseto alifungua mlango wa nyumbani kwake na kuingia ndani kisha kuufunga na kusogeza kochi kubwa kabisa mlangoni, haikujulikana hata nguvu hizo zote kazitoa wapi, kisha akarudi nyuma na kujibanza ukutani akitetemeka kama mtu mwenye homa kali macho yalimtoka pima na mara alihisi kimininiko chenye joto safi kikishuka katikati ya miguu yake, mojo! Kono lenye kucha kali lilipiga mlango na kuuchana vibaya haikujalisha mlango ule ulikuwa wa mpingo au mninga, kono lile likavutwa nje na kupigwa tena mlango ukafumuka na kuvutwa nje, sauti za ajabu zikaanza kusikika ndani ya nyumba ile zikimuumiza masikio Kiseto, kila alipoita msaada hakuna aliyemsikia, lile jitu la kutisha likamsogelea Bw Kiseto amaye alikuwa amejibanza ukutani na hajui nini cha kufanya katika hilo. Ngurumo kubwa ya radi ilipiga nje na michoro yake kulikata anga zima, lile jitu likatoa mlio mkali sana na kupotea mbele ya macho ya Kiseto. Bw. Kiseto alibaki amekaa pale hajielewi macho yake hayakuweza kufumba yalibaki pima, mboni zake hazikuwa zikicheza aliganda tu kama kinyago cha mpapule, mfumo wa taka mwili ulishindwa kufanya kazi yake vyote viliishia hapo na yeye mwenyewe alibaki katika hali hiyo hiyo.
*********************************
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
::: Je Nini kitaendelea katika simulizi hii matata na ya kusisimua?? LIKE na COMMENT bila kusahau SHARE ni muhimu katika ukurasa huu wa simulizi ili Simulizi iweze kuwafikia wengi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment