Simulizi : Nyayo Za Damu
Sehemu Ya Pili (2)
Wakati huo daladala iliyokuwa na watu wachache ilisimama kituoni, yule mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Nasra alikimbilia ndani ya gari na kuwahi siti mbili moja yake na nyingine ya mke wa Sule. Lakini mke wa Sule miguu ilikuwa mizito kuingia kwenye gari lile.
Yule mwanamke aliyewahi kwenye gari alimwita ili akae kwenye siti iliyomshikia.
“Shoga mbona umeganda kama sanamu, njoo nimekushikia siti.”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tangulia
shoga kuna mtu namsubiri.”
Daladala ile iliondoka na kumuacha mke wa
Sule kituoni, baada ya kuondoka alijikuta akijawa na mawazo juu ya yule mwanamke
ambaye amekuwa akigeuka kila dakika mara Nargis mara mwanamke mwingine mara jina
la Nargis mara Nasra.
Japo magari yaliongezeka wazo la kwenda tena
Bagamoyo alilifuta kwa siku ile, aliamua kurudi nyumbani kufanya shughuli
zingine. Alirudi nyumbani taratibu hadi karibia na kwao, alipofika alishangaa
kuwaona Thabit na Nargis wakitoka kuoga.
Kwa vile aliwaona yeye kabla
hawajamuona, aligeuza kwa kuamini yule mwanamke hakuwa Nargis bali wasi wasi
wake. Lakini hakufanya kosa kwa vile asingeweza kuongozana naye Lugaro hospital
sehemu ambayo haikuwa kusudio lake.
Kwa haraka aligeuka na kurudi
kituoni ili awahi safari yake ya Bagamoyo kwa mganga Kigobile. Alipofika kituoni
kwa haraka alipanda daladala lililokuwa limejaa na kusimama hadi Mwenge.
Alipofika Mwenge aliingia kwenye daladala ya kuelekea
Bagamoyo.
Alitulia kitini kwa vile siti zilikuwa zimebakia chache gari
haikuchelewa, baada ya kuenea abiria kwenye siti iliondoka kituo cha Mwenge na
kuelekea Bagamoyo. Moyoni mke wa Sule alimuomba Mungu amfikishe salama na mganga
amkute.
Safari iliendelea huku akiwa amejituliza kwenye siti yake,
gari lilivuka Tegeta huku likishusha abiria wa safari fupi na kupandisha
waliokuwa wakienda Bagamoyo. Gari lilipofika Bunju mke wa Sule alishtuka kumuona
mtu kama Nargis akitelemka katika gari alilokuwa amepanda na kushangaa mbona
hakumuona muda wote mpaka wakati wa kushuka.
Bado aliamini ni moyo wa
wasi wasi wa kumuhofia Nargis, gari nalo liliendelea na safari yake kwa kushusha
na kupandisha watu njiani. Alishangaa wote walitozwa nauri lakini yeye
hakuguswa. Alijiuliza ina maana konda amemsahau au vipi.
Gari
lilisimama kituoni Bagamoyo, watu walitelemka, kwa vile alikuwa amekaa nyuma
alikuwa wa mwisho kutelemka. Hakutaka kuondoka bila kulipa alifungua pochi yake
alipe nauli.
“Umeisha lipiwa dada yangu,” konda alimweleza mke wa
Sule.
“Na nani?”
“Na dada mmoja mrembo mwenye asili ya
Kisomali.”
“Mmh, dada mmoja alinijuaje?”
“Mimi nitajuaje
aliniambia na dada huyo hapo nyuma alikuonesha wewe.”
“Mungu wangu,
dada huyo alipandia wapi?”
“Mlikuwa ameongozana kwa wewe kuwahi
kuingia na kukaa siti ya nyuma na yeye alikaa ya mbele nyuma ya
dereva.”
“Mmh, alitelemkia wapi?”
“Kwani vipi nakuona umejaa
wasiwasi.”
“Kaka yangu huu si muda wa maswali zaidi ya kusubiri
jibu.”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Dada
yule aliteremkia Bunju”
“Mungu wangu nimekwisha,” mke wa Sule alisema
huku akishika kichwa.
“Kwani vipi, mbona
sikuelewi.”
“Kaka yangu weee tuyaache.”
“Kwani kuna ubaya
dada yule alipokulipia?”
“Hakuna tatizo, alitaja jina
lake?”
“Sikumuuliza jina lake kwa vile alikuwa na shida naye, ila
alikuwa na mkufu mmoja wa Dhahabu wenye kidani kilichoandikwa jina la
Nargis.”
“Eti nani?” Mke wa Sule alishtuka kusikia jina
lile.
“Nargis”
“Mungu wangu nimekwisha
amenifuata mpaka huku.”
“Kwani yule dada ana ubaya gani mbona
anaonekana mstaarabu kama angekuwa adui yako asingekulipia.”
“Mmh,
makubwa.”
“Kwani vipi dada?”Konda wa daladala alizidi
kumshangaa.
Mke wa Sule aliona anapoteza muda kwani hata kama
angemueleza yule konda asinge msaidia
chochote.
“Hayana muhimu sana
kuyajua,”
alisema huku akiondoka kuelekea maeneo ya mganga ambayo
yalikuwa nyuma ya uwanja mkongwe wa mpira pale Bagamoyo wa Mwana Kalenge.
Alitembea mwendo mdogo mdogo kuelekea kwa mganga huku moyo wake ukiwa mzito kwa
kuamini huenda kila kona aliyopita lazima Nargis atakuwa yupo pembeni
yake.
Baada ya mwendo mfupi mke wa Sule alisimama ili aamue moja
kurudi au aendelee na safari yake. Wazo moja lilikuwa arudi Dar japo ameisha
fika Bagamoyo, lakini moyo mwingine ulimueleza aende kwa mganga huenda maeneo
yale akaogopa kujitokeza.
Aliamua bora aende kwa
mganga kwani aliamini Nargis alikuwa akimhofia na ndiyo maana alikuta akimtolea
vitisho.
Alikwenda hadi kwa mganga bila kizuizi chochote na kuingia
ndani ya uzio wa nyumba ya mganga, kulikuwa na watu wachache kama kumi. Naye
alijisogeza kwenye foleni ya watu baada ya kusalimilia alikaa pembeni na
kusubiri zamu yake.
Ajabu ilipita zaidi ya saa nzima bila mtu
aliyeingia ndani kutoka, ilibidi watu waanze kuzungumza juu ya mgonjwa huyo
kuchelewa kutoka kwani alichukua muda mrefu. Baada ya muda pazia ilifunguliwa na
mgonjwa aliyeingia kuonana na mganga alitoka.
Mke
wa Sule hakuamini alichokiona mbele yake, mgonjwa aliyetoka ndani kwa mganga
alikuwa Nargis, hakukubaliana na macho yake aliyapikicha ili kuondoa wazo la
kufikirika. Kabla hajapata ufahamu wa kitu alichokiona Nargis
alimsamilia.
“Ha! Mpenzi na wewe huku unafika?”
Mke wa Sule
mdomo ulikuwa mzito kwa kuamini bado kile alichokiona ni kiini
macho.
“Basi mimi natangulia tutakutana
nyumbani.”
Baada ya kusema vile bila kusubiri majibu ya mke wa Sule,
Nargis aliondoka.
Wakati huo wagonjwa wengine waliendelea kuingia.
Japo alikuwa akisogea aliamini siri yake yote ipo nje hata akienda kwa mganga
huenda alichokidhamiria kisitimia.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lakini alipiga moyo
konde na kujisemea: “Liwalo na liwe.”
Ilipofika zamu yake aliingia kwa
mganga huku akiwa na mawazo lukuki kichwani juu ya kumueleza mganga
kilichompeleka, akikiri adanganye na kuacha kukisema kilichompeleka huko
Bagamoyo.
Aliingia ndani kwa mganga na kukaribishwa kwenye
mkeka.
“Karibu mama yangu,” mzee Kigobile
alimkaribisha.
“Asante babu.”
“Karibu uketi mjukuu
wangu.”
Mke wa Sule aliketi kwenye mkeka na
kutulia kumsikiliza mzee Kigobile aliyekuwa akiweka vizuri dawa zake zilizokuwa
zimedondoka chini kwenye kapu dogo lililokuwa pembeni yake.
“MH!
Mjukuu wangu una shida gani?” alimuuliza bila kumtazama.
“Babu mimi
naitwa Mariamu Musa natokea Dar maeneo ya Buguruni...,” alitulia kidogo na
kuendelea kusema.
“Babu nina tatizo moja
linanisumbua.”
“Tatizo gani hilo?”
“Mh!” Alijikuta
akishindwa aanzie wapi hasa baada ya kumuona Nargis akitoka ndani, alishindwa
kuelewa kule kwa mganga alifuata nini.
“Vipi mama
mbona upo mbali una tatizo gani?” Mzee Kigobile alimshtua katikati ya dimbwi la
mawazo.
“Eti mzee yule mwanamke alikuja kufanya
nini?”
“Mwanamke gani? Sina tabia ya kutoa siri za wateja wangu kwa
vile kila mtu anayekuja hapa ana matatizo yake ambayo ni siri
yake.”
“Mh! Basi wacha tu nirudi nina imani huwezi
kunisaidia.”
“Mbona sikuelewi, huyo mwanamke unayemsema anahusiana
vipi na matatizo yako?”
“Ndiye aliyenifanya
nifunge safari kuja huku.”
“Mh! Una matatizo naye?”
“Tena
makubwa.”
“Mwanamke gani huyo?”
“Kuna mwanamke mrembo shombe
wa Kiarabu.”
“Shombe wa Kiarabu?” Mganga alionesha
kushtuka.
“Ndiyo tena alichelewa sana
kutoka.”
“Si kweli leo sijahudumia mteja kama
huyo.”
“Babu una siri gani na huyo mwanamke au babu siku hizi huwezi
kutusaidia sisi wateja tusio na uwezo?”
”Binti mbona sikuelewi, akili
yako ipo sawa?” Kauli ile ilimshtua mke wa Sule na kuamini huenda
alichokizungumza sicho. Alikumbuka hata Msamvu Morogoro alipofika kwa miguu watu
walimuuliza swali hilo hilo.
Alituliza akili yake
akiamini huenda hofu ndiyo iliyomtawala kufikia hatua ya kuchanganyikiwa na
kufikia hatua ambapo kila apitaye mbele yake alimfananisha na
Nargis.
Baada ya kutulia kwa muda aliamini kabisa yote yanayomtokea ni
viinimacho, lakini alikumbuka Morogoro alipotokea na haikuwa kiini macho bali wa
ukweli.
Hapo alizidi kuwa njiapanda, lakini
aliamini akifika kwa mganga ambaye anafahamika kuwa kiboko ya majini basi
atakuwa salama zaidi.
Alijikuta akiamua kusema ukweli huku akirudia
kauli yake ya awali ya liwalo na liwe. Alijitengeneza vizuri na kuanza kumweleza
kilichompeleka pale.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Babu,” alianza kwa
sauti ya chini kumwita mganga.
“Rabeka.”
“Nina
tatizo.”
“Tatizo gani?”
“Kuna kitu kinanisumbua na kutishia
uhai wangu.”
“Kitu gani hicho mama?”
“Kuna jini
linanisumbua.”
“Jini?”
“Ee..ee.ee..ha.ha.a.pana,”
mke wa Sule alipatwa na kigugumizi cha ghafla baada ya kumuona aliyekuwa
akizungumza naye si mzee Kigobile bali jini Nargis.
“Eeh, unasema
nani anakusumbua?”
Mke wa Sule alituliza macho yake kuhakikisha kama
alichokuwa anakiona mbele yake kilikuwa au kilikuwa
kiinimacho.
Aliyekuwa mbele yake hakuwa mganga Kigobile bali Nargis
aliyekuwa amevaa kama mganga na kujifunga rubega na kiremba chekundu. Mwili wake
alionekana wazi uliokuwa mweupe usio na doa.
Mke
wa Sule alifikicha macho tena asiamini aliyekuwa mbele yake ni Nargis kweli au
amechanganyikiwa. Aliamini kama kweli ni Nargis basi adhabu yake ni kubwa ambazo
alishindwa kuifananisha na kitu chochote.
“Vipi mbona umepigwa na
mshangao wa ghafla?” Sauti ya mganga Kigobile ilimshtua mke wa Sule ambaye
alikuwa kama mtu aliyerukwa na
ufahamu.
Alipoangalia vizuri bado alibakia njia
panda asipate jibu la kile alichokiona mbele yake, kilikuwa kweli au ni mauzauza
ya dunia. Aliyekuwa mbele yake alikuwa mganga Kigobile na si
Nargis.
“Binti mbona sikuelewi tulikuwa
tunzazungumza vizuri mbona umebadirika ghafla?”
“Aaa..aa..babu,” mke
wa sule alipatwa na kigagaziko.
“Una tatizo
gani?”
Kabla ya kujibu alijiangalia kwa kujikagua
kama ni yeye au mwingine, alipepesa macho kukiangalia chumba cha mganga ambacho
hakikubadilika chochote na aliyekuwa mbele yake ni mzee Kigobile. Alivuta pumzi
ndefu na kuzishusha alijipa moyo na kujisema kwa sauti ya ndani kuwa liwalo na
liwe hata mbele ya sura yake asimame nani atasema shida yake.
“Mmhu,
binti mbona unaonekana haupo sawa?”
“Ni kweli babu
kuna mwanaharamu mmoja anataka kunichezea akili yangu, nahitaji msaada
wako.”
“Msaada upi maana nilipokuuliza ulichokisema ulishtuka na
kukuona ukinishangaa kama nimegeuka simba.”
“Ni hivi babu nyumba
ninayo ishi kuna mpangaji mwenzangu tuna wasiwasi mpenzi aliyenae ni
Jini.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
”Toka
ameanza mahusiano kumekuwa na mambo ya miujiza ambayo si ya kibinadamu,” mke wa
Sule alielezea yote aliyokutananayo toka alipoanza kumfuatilia Nargis na onyo
alilopewa.”
Mzee Kigobile baada ya maelezo yale
alitoa simbi kwenye kikopo na kuzitazama kisha alizitupa juu ya msala wake.
Aliziangalia kwa kuma huku akisoma moja baada ya nyingine kisha alinyanyua uso
wake na kusema.
“Binti.”
“Abee
babu.”
“Ni kweli kabisa huyo mwanamke ni Jini,
tena jini hilo lipo chini ya miamba bahari, lakini jini huyu ni mwenye huruma
sana tofauti na majini mengine ni jini asiyependa kuua. Jini huyu anaitwa Nargis
ambaye ana dada yake aitwae Hailati.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jini huyu alitokea
kumpenda Thabit na kumlinda na kifo siku ambayo Thabit aliona miujiza pale kituo
cha basi cha Mwenge. Aliweza kumshawishi Thabit na kukubali kwenda chini ya
bahati kulala bila kujijua. Hata Thabit alikuwa na wasiwasi na mpenzi wake
ambaye aliogopa kujitambulisha kwa kuhofia familia yake kumuua
Thabit.
Jini Nargis alijikuta anaingia katika kazi ya kuua si kwa
hiyari yake bali kwa shinikizo la dada yake. Kutokana na matatizo yaliyompata
kutokana kutendwa na wanadamu basi wamekuwa maadui zao
wakubwa.
Nargis amekuwa akikutisha ili uache
kumfuatilia lakini umekuwa mbishi,
tena kichwa
ngumu.”
“Sasa mganga maelezo hayo hayanisaidii utanisaidia
vipi?”
“Nitakupa dawa za kufukiza na kuoga ili
kumfanya asikufuate.”
“Lakini shida yangu kubwa ni kummaliza
kabisa.”
“Kwa nini ummalize wakati yeye hakutaka
kukumaliza.”
“Siwezi kuishi kwa raha kama
ataendelea kuwepo.”
“Mmh, sawa nitakupa dawa hiyo ambayo inatakiwa
ujasiri kaichimbie kwenye mlango wa Thabit akiiruka na mchezo unaishia
palepale.”
“Ndiyo ninayoitaka.”
Mzee
Kigobile alimpa mke wa Sule dawa ambayo alielezwa aifanye pindi afikapo nyumbani
kwa kuanza kuichoma na kufukuza vitu vibaya majini na
wachawi.
Baada ya kulipa pesa aliaga na kuondoka,
akiwa na furaha moyoni kwani aliamini amepata dawa ya kumkomesha adui yake.
Alipofika kituoni alipanda daladala ambayo ilikuwa imebakiza siti chache,
alibahatika kupata siti ya mbele alikaa kwenye siti yake kusubiri gari liondoke
kituoni.
Baada ya daladala kujaa safari ya kurudi
Dar iliwadia, alitulia kitini huku akiomba Mungu gari lifike salama ili
akamuonesha Nargis kuwa yeye ni nani kama alimtembeza kwa miguu kwa siku tatu
basi yeye atampoteza katika ramani ya dunia .
Gari
lilikwenda huku dereva akitembeza gari kwa kasi kutokana na barabara kuruhusu,
mke wa Sule naye alikuwa akiimba taratibu nyimbo ya taarabu iliyokuwa ikiimbwa
kwenye gari ile kwa kuifuatiliza.
Gari liliondoka
Bagamoyo na kuanza kuitafuta Bunju, dereva nae alizidi kukanyaga mafuta, gari
lilopokuwa linateremsha mtelemko uliokuwa karibu ya daraja wote waliokuwa mbele
walishangaa kuona mti mkubwa uliokuwa katikati ya barabara ambao ilikuwa vigumu
kuukwepa na kasi ile.
Dereva alijitahidi kwa uwezo
wake wote kuukwepa ule mti mkubwa ulikuwa katikati ya barabara na gari kuhama
njia na kuangukia chini ya
daraja.
Abiria wote walipiga
kelele za kuhofia maisha yao
Gari liliangukia bondeni na kufanya watu
wote wapate majeraha hata hivyo hakuna abiria aliyekufa, wasamaria wema
walijitokeza kuwasaidia majeruhi hao. Mke wa Sule aliyekuwa amebanwa sehemu za
kifua alibebwa na mtu mmoja aliyemuweka mbali na gari lililokuwa
limepinduka.
Dereva naye hakuamini baada ya gari kupinduka mti mkubwa
aliouona awali hakuuona tena barabarani. Alipomuangalia mtu aliyekuwa akimsaidia
mke wa Sule kwa kumnyoosha viungo vilivyokuwa vikimuuma, ghafla alihisi mapigo
ya moyo nayanaenda kasi na kupata mshtuko uliosababisha apoteze
fahamu.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kupata
ufahamu alijikuta kwenye miamba ambayo hakujua kule ni wapi pia kulikuwa na
harufu kali, alisikia kama mawimbi yakipiga kwa nje kuonesha ni karibu na bahari
akiwa peke yake amelala juu ya mwamba wenye baridi. Alisimama na kujiuliza yupo
maeneo gani na alifikaje huko, kwani alikumbuka kwa mara ya mwisho alikuwa
katika majeruhi waliopata ajali ya gari baada ya dereva kuukwepa mti hewa na
kulifanya gari kupinduka.
Kilichomshtua ni harufu ya mafuta ambayo
hupendwa kutumiwa na adui yake Nargis.
“Mariamu
mwanamke katili,” sauti aliyoizoea iliisikia.
Hakujibu bali mapigo ya
moyo yalimwenda mbio na kujua siku zake za kuishi duniani zilikuwa zimefika
kikomo.
Alipogeuka alikutana uso kwa uso na Nargis akiwa katika uso
wa tabasamu tofauti na siku zote anapokasirika uso wake hugeuka kama wa mzee.
Alihisi tumbo la kuhara likimshika kwa hofu, lakini Nargis aliendelea kutabasamu
huku akipiga hatua taratibu kumsogelea.
“Mariamu,” alisema huku
akipiga makofi ya dharau, mke wa Sule alibakia kimya.
“Mariamu nakuita
sitaki kiburi, nimekusamehe sana huu ni wakati wa mimi kukuonesha ni nani, nina
uwezo gani na nilichokuahidi nitakitimiza.”
“Sa...sa...mahani Nargis,”
mke wa Sule alipiga magoti mbele ya Nargis.
“Niite
Jini si Nargis.”
“Ha...ha...pana wewe si Jini.”
“Mariamu
nimefanya kila hila uachane na nyendo zangu imeshindikana, kwa mdomo wako
umedhamiria kuniangamiza. Mariamu nimekufanyia nini kibaya ambacho kimekufanya
uwe adui yangu?
Nimejitokeza kwa kila aina ili ujue kila ukifanyacho
mimi nipo jirani yako, lakini inaonesha jinsi gani ulivyo na roho ngumu, Mariamu
una masikio ya kenge husikii mpaka utoke damu na sasa muda wako
umefika.
Sina nia ya kukuua bali kukutesa japo
wewe ulidhamiria kuniua, nimeipindua gari makusudi ili niweze kukupata baada ya
kuipata dawa ambayo kweli ingeniangamiza. Baada ya kupinduka gari dawa zile
zimepotea na kunipa nguvu za kukupata.
Ni kweli wewe ni mwanamke
jasiri ambaye hakika ulikuwa umefanikiwa kuniangamiza kwani baada ya kufika
nyumbani nisingekuweza tena. Na kwa vile dawa ya mlangoni nisingeiona basi
nilikuwa naangamia bila kujua.
Mariamu hebu leo nielezee
nilichokukosea mpaka kufikia hatua ya wewe kunitafuta usiku na mchana ili
uniangamize?” Swali lile hakujibu alibakia kama bubu.
“Mariamu
usiniudhi nitakufanya kitu kibaya ambacho hujafanyiwa toka uzaliwe.” Uso wa
Nargis ulibadilika na kuweka makunjanzi.
“Kabla sijakujibu nieleze
huku wapi na nimefikaje?” Mke wa Sule aliuliza kwa ujasiri huku moyoni
akijisemea liwalo na liwe.
“Huku ni chini ya mwamba bahari ambako
huwafunga majini na wanadamu wenye kiburi, juu yetu kuna bahari kama unavyosikia
mawimbi yake.”
“Haya nieleze shida yako nini
kwangu?”
“Sina shida na wewe ila nataka nitimize ahadi niliyokuahidi,
nitakugeuza nguruwe na kwenda kukutia kwenye banda la nguruwe la jirani yenu na
mwisho wa wiki utakuwa mmoja wa nguruwe watakaochinjwa.”
“Eti?” Mke wa
sule alishtuka.
“Eeh, nilitaka kukutesa kama nilivyokuahidi lakini
kila nitakapo kuona moyo wangu utakosa amani, lakini nawe ukipotea katika sura
ya dunia itamaliza malumbano yasiyo ya msingi.”
“Usinitishe fanya
lolote huna uwezo wa kuniua ila Mungu pekee.”
“Napenda viumbe wenye
kiburi kama wewe.”
Baada ya kusema vile Nargis alimnyooshea kidole
mke wa Sule na kumuamuru ageuke nguruwe.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuanzia sasa
maisha yako yatakuwa katika umbile la nguruwe.”
Baada ya kusema vile
pale pale mke wa Sule aligeuka nguruwe, lakini mke wa Sule kwake hakuona
mabadiliko yoyote zaidi ya kujiona yupo kawaida.
“Mbona sijabadilika?”
Aliuliza kwa kiburi.
“Mh! Sogea pale kwenye jiwe linalong’aa kama kioo
ujione.”
Mke wa Sule aliona utani kwa kuamini Nargis alikuwa
akimuogopa na kuamua kumtisha kila kukicha. Aliposogea kwenye jile lile
lililokuwa kama kioo alishangaa kuona mbele ya jiwe lile kuna
nguruwe.
Hakuamini alijaribu kuchezesha mikono
nguruwe aliyembele yake alifanya vile, aliinamisha kichwa vile vile nguruwe yule
alifanya vile. Kila alichokifanya nguruwe yule alifanya na kumfanya aamini
kabisa yule nguruwe ni yeye.
Lakini bado hakuamini alijua ni kiini
macho tu Nargis cha kuendelea kumtisha ili aachane naye.
Akiwa bado
anajiangalia asijimalize kama kweli yeye ndiye anayeonekana katika umbile la
nguruwe Nargis alisogea karibu yake na kumsemesha.
“Najua bado huamini
ila mwisho wa wiki utaamini ukiwa mmoja wa nguruwe watakao
chinjwa.”
“Nargis usinitishe hiki ni kiini macho tu huwezi kunigeuza
nguruwe wewe si Mungu,” Licha ya vituko vya Nargis, mke wa Sule
hakutetereka.
“Nitakuacha huku na usiku
nitakufuata na kukupeleka kwenye banda la nguruwe wenzako.”
Baada ya
kusema vile Nargis aliondoka na kumuacha mke wa Sule chini ya miamba bahari.
Hakumfunga kamba alimuacha huru na kumfanya mke wa Sule azunguke kila kona ya
miamba ile bila mafanikio.
Majira ya usiku Nargis alimchukua mke wa
Sule aliyekuwa katika umbile la nguruwe na kwenda kumuweka katika banda la
nguruwe kisha aliondoka na kumuacha mule. Kwa mara ya kwanza toka atoke tumboni
kwa mama yake mke wa Sule alikumbana na adhabu
kali.
Ndani ya jumba lile kulikuwa na uchafu na
harufu kali ambayo haivumiliki kwa mtu kukaa mule kwa muda mrefu, mwanzo alikuwa
akijitahidi kuwakimbia wale nguruwe wasimsogelee kwani alijiamini kabisa yeye ni
mwanadamu na wale ni nguruwe.
Kwa kuwa alikuwa na muonekano wa nguruwe
jike, nguruwe dume walimsumbua sana kumtaka kimapenzi kitu kilichomfanya akimbie
bandani lakini hakuweza kutoka nje. Harufu kali ya nguruwe waliokuwa
wakimsogelea kwa kuamini ni nguruwe mwenzao ilimkera sana.
Siku hiyo
alilala na njaa baada kushindwa kula uchafu waliokuwa wakila nguruwe, alitamani
kufa kuliko mateso yale na kama Nargis angetokea mbele yake, angempigia magoti
na kumuomba amuue au amsamehe.
Njaa na kiu ilikuwa
kali hakukuwa na maji zaidi ya maji ya tope ambayo nguruwe halisi waliokuwemo
bandani walikuwa wakiogelea na kunywa. Alisogea pembeni ya banda na kuanza kulia
kilio kilichokuwa kikitoa mlio wa nguruwe.
Muda
ulivyozidi kwenda ndivyo kiu na njaa kali vilivyokuwa vikimshika, alihisi
kizunguzungu huku nguruwe watoto wakimsogelea kutafuta kunyonya. Aliwasukuma kwa
miguu na kuwapiga vikumbo vilivyowafanya waanguke chini na kumuacha. Mke wa Sule
alimuomba Mungu amuue kuliko adha ile ya kuteseka kukaa na viumbe ambavyo ni
haramu na najisi hasa yeye akiwa muislamu.
Kiu
kilipokuwa kikali alijaribu kunywa maji yenye mchanganyiko na matope lakini
alipofikisha pua yake maji yalimshinda kutokana na harufu kali yaliyokuwa
yakinuka. Alijuta kumfuatilia Nargis kiumbe ambaye hakuwa na ubaya na yeye zaidi
ya kumuonya asimfuatilie nyendo zake.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alijilaumu kwa
kushindwa kuwa msikivu na matokeo yake kuishi kama nguruwe tena kwenye banda
chafu lisilostahili mwanadamu kuishi. Alijiuliza ataishi vile mpaka lini na
kukumbuka kauli ya Nargis ya yeye kuchinjwa mwishoni mwa wiki akichanganywa na
nguruwe wengine.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment