Search This Blog

NYUMBA YA MISUKULE - 2

 





    Simulizi : Nyumba Ya Misukule

    Sehemu Ya Pili (2)



    Bi.Marium akatoka mbio chumbani kwake hadi kule jikoni kuliposikika kelele,

    BI.MARIUM: (Huku akihemea juu juu), kuna nini, kuna nini hapa?

    MARIANA: Mama hapa kuna maajabu, hebu ona,(huku akionyesha lile sufuria lililokuwa na chakula).

    BI.MARIUM: Nione nini sasa?

    MARIANA: Hakuna kitu mama, chakula chote kimeliwa.

    PENDO: Nani kala sasa?

    MARIANA: Sijui kwakweli.

    PENDO: Mama, mie ndo sielewi kabisa yani!! Labda usikute Mariana anapeleka chakula kwa mabwana zake kweli.

    MARIANA: Jamani hapo mnanisingizia, hata kama ningekuwa na bwana yani ndio nimpelekee chakula chote?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BI.MARIUM: Hapo ndipo huwa mnanishangaza, yani chakula humu humu ndani kiende wapi kama sio kuna mmoja wenu anachukua?

    PENDO: Mama itakuwa ni Mariana tu.

    Kwahiyo Mariana akasingiziwa tena, na kwavile yeye ndio alikuwa mfanyakazi wa mule ndani hata alivyokataa ilionekana ni bure tu.

    Mariana akaenda kwa mama Sarah kupata ushauri.

    MARIANA: Kwakweli nimeshapachoka pale ndani, kila kitu nasingiziwa mie.

    MAMA SARAH: Vumilia tu, yote maisha mdogo wangu.

    MARIANA: Kwakweli nitarudi kwetu tu, maisha haya yamenichosha.

    Jioni yake kama kawaida akapika na kuandaa chakula.

    Wakala wakamaliza, baada ya hapo Pendo akaenda kuoga maana ndio alikuwa wa mwisho kurudi.

    Wakati yupo bafuni anaoga, mara taa ya bafuni ikazimwa, akabaki anashangaa, akaenda akaiwasha, ile anajimwagia maji taa ikazimwa tena. Akajikuta anatoka bafuni mbio hadi sebleni,

    BI.MARIUM: Nini wewe?

    PENDO: Mama hata sijui nani ananizimia taa bafuni.

    BI.MARIUM: Labda taa imeharibika mwanangu.

    PENDO: Naogopa kwenda kuoga mwenyewe, twende ukanisubirie mama.

    Ikabidi, Bi.Marium akamsubiri mwanae hadi amalize kuoga.

    Baada ya hapo wakaingia kulala,

    Pendo akaenda kulala na mama yake, wakiwa chumbani,

    BI.MARIUM: Zima taa ile Pendo tulale.

    PENDO: Hapana mama naogopa.

    BI.MARIUM: Yani wewe mwanangu msomi mzima ila uoga upo mbele kisa taa ya bafuni loh.

    PENDO: Mama mambo mengine hayana cha usomi.

    Wakiwa wanaongea hayo mara taa ya chumbani mwao ikazimwa, hapo ndipo Pendo alizidi kuwa na uoga huku akimkumbatia kwa nguvu mama yake. Mara ikawashwa tena, wote mtoto na mama wakawa wanahema juu juu kama wamekimbizwa.

    Pendo akaamua kukaa na kuiwasha kompyuta yake,

    BI.MARIUM: Heee inamaana leo hulali?

    PENDO: Mama, acha tu nicheze game hapa na kusikiliza miziki, sitaweza kulala kwakweli.

    Kesho yake ikabidi bi.Marium aende kuongea na watu ili wakaifanyie maombi nyumba yake.

    Akafika na watu wawili pale nyumbani kwake, wakaongea mawili matatu ila wale watu wakagoma kuifanyia maombi ile nyumba.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BI.MARIUM: Jamani, kwanini hamtaki kuifanyia maombi nyumba yangu?

    MTU 1: Mama, nyumba yako ni nzito sana. Kwakweli hatutoweza.

    BI.MARIUM: Niambieni kwanini?

    MTU 2: Mama, hatutaki matatizo sisi. Kwakweli nyumba yako ni nzito sana.

    BI.MARIUM: Basi ombeeni hivyo hivyo.

    MTU 2: Mama, hapa hata tukifanya hayo maombi, ni sawa na kupiga kelele basi.

    Wale watu wa maombi wakamuaga na kuondoka.

    Kwakweli bi.Marium akabaki na maswali mengi sana kichwani mwake.

    Siku hiyo asubuhi kama kawaida ya pale kwenye nyumba yao, Amina alianza kulalamika,

    AMINA: Yani hii tabia ya humu ndani siku hizi siipendi kabisa, haya nani kanywa juisi yangu na kuniachia box tupu?

    PENDO: Atakuwa Mariana huyo.

    MARIANA: Jamani, kila kitu humu ndani mnanisingizia mimi, hata sijui kwanini.

    AMINA: Ndio utakuwa wewe Mariana, ila hapo unajifanya kuonyesha hudhuni eti tuseme umesingiziwa loh! Hii tabia ni mbaya, kwakweli siipendi.

    Mchana wa siku hiyo Mariana akaamua kumuaga mama mwenye nyumba kuwa anataka kusafiri kurudi kwao.

    MARIANA: Mama, kesho nataka kwenda nyumbani Iringa nimewakumbuka kweli.

    BI.MARIUM: Mbona gafla hivyo jamani Mariana?-

    MARIANA: mama, sitakaa sana naenda kuwasalimia tu.

    Bi.Marium hakuwa na jinsi zaidi ya kumruhusu aende kwao.

    Kesho yake, Mariana akasafiri kwahiyo pale nyumbani wakabaki watatu, bi.Marium na binti zake wawili.

    Swala la kutokukuta chakula wanachoacha usiku liliendelea na ndipo hapo wakaweka mkakati wa kupika chakula cha kutosha tu ili kisibakie.

    Siku moja Amina akiwa jikoni anapika, mara akamuita gafla mama yake huku akipakimbia kule jikoni,

    BI.MARIUM: Nini wewe?

    AMINA: Mama, nilikuwa napika huko jikoni ila kila nikisogea naona kuna mtu nyuma yangu nae ananisogelea.

    BI.MARIUM: (Huku akimshika Amina mkono), haya hebu nionyeshe ilivyokuwa.

    Amina akaana kumuonyesha jinsi ilivyokuwa,

    BI.MARIUM: (Huku akicheka), kweli wewe bwege, hujui kama unakimbia kivuli chako mwenyewe?

    AMINA: Jamani mama, sio kivuli bhana ni mtu kabisa.

    BI.MARIUM: Haya kama ni mtu, niambie yuko wapi?

    AMINA: Sijui.

    BI.MARIUM: Basi ndio hivyo ulikuwa unakimbia kivuli chako mwenyewe.

    AMINA: Jamani mama!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BI.MARIUM: Unajua mtu unapotawaliwa na uoga basi hata kivuli chako unaweza kuhisi labda mtu anakufatilia ila si kweli, kwahiyo acha uoga mwanangu.

    Basi Amina akamaliza kupika na akaandaa wakala kile chakula.

    Kesho yake usiku, Amina akiwa bafuni anaoga, akahisi kuna mtu anampapasa mgongoni ila kila akigeuka haoni mtu, akawa anajiuliza "inamaana kivuli changu kinauwezo wa kunipapasa hadi mgongoni?"

    Akaendelea kuoga, akahisi tena ameguswa mgongo, uoga ukaanza kumtawala akashindwa kabisa kuendelea kuoga. Akakimbilia chumbani kwake ili alale, ila akaogopa kuzima taa. Wakati anapanda kitandani tu akasikia taa imezimwa yani hapo akashindwa hata kujisogeza kwa uoga kwani alikuwa anatetemeka kupita kiasi, alishindwa kuuliza wala kupiga kelele.

    Wakati anatetemeka vile, mara taa ikawashwa tena, Amina aliogopa hata kuangalia mbele alitamani akimbilie chumbani kwa mama yake wakalale wote.

    Wakati akifikiria hayo taa ikazimwa tena halafu juu ya bati ikawa kama mtu anamwaga mchanga kule juu.



    Amina hakuweza kulala kabisa alijikuta akijiziba sura kwa viganja vyake hadi kunakucha. Na hata hiyo asubuhi alijikuta bado akiogopa kuinuka pale kitandani hadi mama yao alipoingia mule chumbani,

    BI.MARIUM: Wee, Amina vipi kuamka?

    AMINA: (Akashtuka gafla pale alipojiziba sura), abeee mama!

    BI.MARIUM: Vipi wewe?

    AMINA: Mama hapana kabisa, hii nyumba ni yetu lakini kwa matatizo ya jana usiku sitaweza kuvumilia.

    BI.MARIUM: Unamaana gani?

    AMINA: (akainuka pale kitandani), Mama ngoja nikaoge kwanza.

    Amina akaenda kuoga nje, hakutaka kuoga bafuni siku hiyo kabisa. Alipomaliza akaenda kuvaa na kuweka baadhi ya nguo zake kwenye mkoba halafu akamfata mama yake sebleni ili kuongea nae,

    AMINA: Mama kwakweli nimeshapachoka humu ndani.

    BI.MARIUM: Amina mwanangu, mbona unakuwa na akili fupi namna hiyo. Yaani unasema umepachoka kwenu, sasa utaenda wapi?

    AMINA: Mama, mimi naenda kukaa kwa John.

    BI.MARIUM: (Huku akionyesha kuchukizwa), hivi huyo John si tulishakukataza kuwa na mahusiano nae!!

    AMINA: Hata kama, mimi John nampenda na haya maswahibu ya hapa ndani bora nikaishi nae tu.

    BI.MARIUM: Huyo John wako wote hatumtaki humu ndani, hata baba yako alipokuwa hai alikukataza yaani leo hii amekufa unajifanya kujichukulia maamuzi!!

    AMINA: Mama, mtanisamehe tu ila ndio hivyo naenda kwa John.

    BI.MARIUM: Mungu wangu, hapa mtoto sina kwakweli.

    Amina huyo akainuka na kujiondokea.

    Bi.Marium alichukizwa sana na kitendo alichofanya Amina, akadhidi kuelekeza hasira zake za waziwazi kwa kijana John.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kijana huyu alijikuta akikataliwa na hii familia kutokana na ugomvi wao wa kifamilia wa muda mrefu ambapo kwa hapo zamani hawa wazazi wa familia hizi waliwahi kugombana, kitendo cha dharau kilichoonyeshwa na familia ya John kilifanya familia hii kuweka chuki iliyodumu kwa muda mrefu hadi hapo binti yao alipokwenda kumtambulisha John kwao ikawafanya wazazi wakumbuke ya nyuma na kumkataa John bila kujali kwamba aliyetenda mabaya si yeye.

    Bi.Marium akiwa na mawazo ya yale mabaya waliyofanyiwa na wazazi wa John, mwanae Pendo akaenda kumliwaza mama yake.

    PENDO: Mama, mwanao yule ni mpumbavu tu kwahiyo usijari sana, si anajifanya kayapatia mapenzi we mwache tu atajutia mwenyewe.

    BI.MARIUM: Yaani roho inaniuma mwanangu, tatizo mlikuwa wadogo sana ndiomana hamjaelewa walivyotufanyia wale.

    PENDO: Najua jinsi gani umechukizwa mama, ila usiwaze sana.

    BI.MARIUM: Yani jana kajifanya hapa mara sijui mtu ananifata mgongoni wakati napika kumbe anatafuta sababu ya kwenda kwa huyo mpumbavu wake John.

    PENDO: Mama, mi nilijua tu kama alikuwa anatafuta sababu.

    BI.MARIUM: Ndio hivyo mwanangu.

    Wakaamua kuendelea na shughuli zao za kila siku.

    Siku hiyo usiku, bi.Marium akiwa chumbani amelala, Pendo alikaa sebleni akiangalia tamthilia kwenye luninga.

    Katika ile tamthilia kulikuwa na mazishi, mara gafla akaona jeneza limewekwa mezani kwenye sebule yao, Pendo akaanza kupiga kelele na kukimbilia chumbani kwa mama yake, bi.Marium naye akashtuka kutoka usingizini,

    BI.MARIUM: Nini wewe?

    PENDO: Mama naogopa, (huku akimsogelea mama yake na kumkumbatia).

    BI.MARIUM: Unaogopa nini mwanangu?

    PENDO: Mama, sebleni kuna jeneza.

    BI.MARIUM: Wee Pendo, hebu nitolee mauzauza yako. Jeneza sebleni litafute nini?

    PENDO: Mama, kweli nakwambia. Nimeona kwa macho yangu kabisa.

    BI.MARIUM: Kwahiyo hata Tv hujaizima?

    PENDO: Ningeizimaje mama wakati mbele yangu kuna jeneza?

    BI.MARIUM: Yaani wanangu kwa mauzauza hamjambo, haya twende huko sebleni tukaone.

    Pendo na mama yake wakaanza kuelekea sebleni huku Pendo kamshikilia mama yake kwa nyuma.

    Kufika sebleni lile jeneza halikuwepo tena.

    BI.MARIUM: Si unaona, mitamthilia yenu hiyo ya ajabu ajabu ndio inakuletea mauzauza hayo.

    PENDO: Ila mama nimeona kweli.

    BI.MARIUM: Haya kama umeona kweli liko wapi sasa?

    PENDO: sijui kwakweli.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BI.MARIUM: Basi elewa kwamba hayo ni mauzauza yako tu mwanangu.

    PENDO: Sasa mauzauza si ndio hayo mambo ya ajabu mama?

    BI.MARIUM: Yani mawazo mabovu humo kichwani mwako ndio yanasababisha yote hayo.

    Ikabidi waende kulala muda huo.

    Kulipokucha, bi.Marium akapigiwa simu kuwa kuna msiba umetokea huko kijijini kwa mumewe.

    Ikabidi yeye na mwanae wajifungashe na wasafiri hadi huko kijijini sababu aliyekufa alikuwa ni mtu wa karibu.

    Wakiwa pale msibani, mama mkwe akamuita bi.Marium.

    MAMA MKWE: Kwahiyo kuja kwenye misiba huku unaweza ila kuleta misiba ya mwanangu na mjukuu wangu huku ulishindwa?

    BI.MARIUM: Mama sio kwamba nimefanya kinguvu kuzikia kule ila baba alinipa ruhusa hiyo jamani.

    MAMA MKWE: Hata kama, siku zote mama ni mama tu. Je wewe ungefurahi mwanao kuzikwa mbali?

    BI.MARIUM: Nisingefurahi mama ila ingetegemea na mazingira.

    MAMA MKWE: Kwamaana hiyo, mazingira ya huku hayakufaa mwanangu kuzikiwa huku?

    BI.MARIUM: Hapana mama, sina maana hiyo.

    MAMA MKWE: Sijapenda na sitaipenda kamwe tabia kama hii, kwa kifupi umenikera sana Marium.

    BI.MARIUM: Mama nisamehe na yote yaishe.

    MAMA MKWE: Umeshachelewa Marium.

    Halafu akaondoka na kwenda kufanya mambo mengine.

    Bi.Marium akarudi kwa binti yake na wao kuendelea na mambo mengine.

    Wakati wa kuzika ukafika, ila Pendo alionekana kushtushwa na jambo na kumwambia mama yake.

    PENDO: mama, lile jeneza ndio lile lile nililoliona juzi usiku sebleni.

    BI.MARIUM: Wee Pendo, hebu acha mauzauza yako.

    PENDO: Kweli kabisa mama hata sio mauzauza.

    Wakafanya harakati za mazishi wakamaliza.

    Waliporudi pale kwa bibi yao na wakina Pendo, bibi akamuita Pendo na kuongea nae.

    BIBI: Mjukuu wangu, usipende kuropoka ropoka.

    PENDO: Naelewa bibi, hata hivyo mimi sio mropokaji.

    BIBI: Sawa, halafu pia mjukuu wangu wewe ni msomi usipende sana kuamini mambo ya kishirikina.

    PENDO: Yani bibi, mimi ndio huwa sina kabisa imani na mambo ya kishirikina.

    BIBI: Halafu usipende kuwaamini waganga, ni wabaya sana hawakawii kukwambia kuwa hata wewe ni mchawi.

    PENDO: Kweli kabisa bibi, kwanza hatujawahi kwenda kwa waganga kwani naelewa wazi ukiwekea imani uchawi ndio unakutokea. Ila kwa mimi siamini kama kuna uchawi duniani.

    BIBI: Kama huamini mbona nasikia huwa unaogopa ndani?

    PENDO: Bibi, wanadamu tumeumbiwa hofu. Ila siamini uwepo wa uchawi kabisa.

    BIBI: Vizuri mjukuu wangu na hiyo ndio faida ya kuwa msomi.

    Basi Pendo na bibi yake wakakumbatiana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku hiyo ikabidi walale huko na kesho yake wakaianza safari ya kurudi kwao bi.Marium na Pendo.

    Wakiwa njiani, bi.Marium akamuuliza mwanae,

    BI.MARIUM: Ulikuwa unaongea nini na bibi yako?

    PENDO: Mengi tu mama ila kwa kifupi bibi amenipa ujasiri mkubwa sana.

    BI.MARIUM: Ujasiri gani huo?

    PENDO: Ndio kama hivi, sasa nimetambua kuwa lile jeneza nililoona usiku ni maono tu kuwa kuna msiba na ndio hivi umetokea.

    BI.MARIUM: Basi sawa kama bibi yako amekupa ujasiri huo.

    Wakiwa bado wako njiani, gari yao ikatandwa na ukungu kwa mbele na tena ilikuwa gafla kabisa.

    Mara gafla ule ukungu ukapotea, halafu wakaona kitu mbele kilichofanya wao na dereva wao kushtuka sana.



    Wakiwa pale njiani, walishtushwa na kitu walichoona mbele yao.

    Kwani waliona paka mwenye sura ya binadamu kabisa tena sura yake ilikuwa ya yule marehemu waliyotoka kuzika kijijini, kila mtu aliishiwa nguvu isingekuwa ujasiri wa yule dereva wao basi wasingeweza kuvuka eneo lile.

    Yule dereva alitumia ujasiri wa hali ya juu, wakajikuta wapo eneo lingine.

    BI.MARIUM: Mmh ilikuwa hatari pale.

    DEREVA: Mama, mimi nimechanjiwa bhana! Ingekuwa mtu wa kawaida pale lazima tungepata ajari.

    PENDO: Aah!! Acheni imani za kishirikina jamani.

    DEREVA: Inamaana Pendo yule paka hukumuona vizuri?

    PENDO: Yule ni paka tu kama paka wengine.

    BI.MARIUM: Mmh!! Mwanangu, hata mimi hapo imani imenitoka. Maana paka mwenyewe anasura ya binadamu tena sura ya yule marehemu.

    PENDO: Mama, wewe si huwa unasema hayo ni mauzauza? Basi tusiogope tulichoona kwani ni mawazo yetu tu.

    DEREVA: Sikulaumu sana Pendo maana najua wasomi wengi hamuamini kama uchawi upo.

    BI.MARIUM: Hata mimi huwa siamini ila yule paka amenitisha sana, hadi nimetetemeka.

    PENDO: Halafu wewe mama ndio umemwambia bibi kuwa mimi huwa naogopa ndani.

    BI.MARIUM: Hapana sijamwambia kabisa.

    PENDO: Sasa bibi kajuaje?

    BI.MARIUM: Sijui ila itakuwa mauzauza yake tu.

    DEREVA: Ila ninyi nyote nahisi hamuelewi vizuri maana ya mauzauza. Ila sitasema mengi. Siku zote kitu kikikupata ndio utajua kama kipo..

    Safari ikaendelea ya kurudi kwao.

    Huko kwenye nyumba ya bi.Marium, palikuwa na mlinzi pekee aliyeachwa pale ndani.

    Mama Sarah akapita na kumkuta mlinzi amekaa nje tena anasinzia ikabidi amshtue,

    MAMA SARAH: Wewe vipi, mbona upo nje, halafu unasinzia hapo?

    MLINZI: Mama, wee acha tu.

    MAMA SARAH: Kwani vipi?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MLINZI: Hapa nangoja warudi nidai changu nisepe, hii nyumba majanga.

    MAMA SARAH: Kwanini? Hebu nieleweshe.

    MLINZI: Mama, humo ndani hakuna mtu, wote wameenda msibani yaani mama na Pendo, na Amina nae hayupo.

    MAMA SARAH: Sasa kama hawapo tatizo ni nini?

    MLINZI: Hata ungekuwa wewe usingeweza, yaani nyumba haina watu ila utaona mara taa imewashwa mara imezimwa halafu mara nyingine utasikia kama watu wanatembea tembea ndani.

    MAMA SARAH: Mmh! Mbona makubwa hayo! Hivi ni kweli kabisa?

    MLINZI: Ndio ni kweli, na hiyo ndio sababu iliyofanya nikae nje humo ndani ujasiri umenishinda kabisa.

    MAMA SARAH: Mmh!! Haya basi wangoje warudi.

    Bi.Marium na mwanae Pendo wakawa wamewasili kwenye nyumba yao na yule dereva akawaaga na kuondoka.

    Wakiwa getini, wakamshangaa mlinzi wao akiwa pale nje,

    MLINZI: Bora mmerudi, nimewangoja sana hapa.

    BI.MARIUM: Loh hata salamu?

    MLINZI: Samahani mama, shikamoo.

    BI.MARIUM: Marhaba, eeh bora tumerudi nini?

    MLINZI: Nataka kuwaaga mama, nataka kwenda kuangalia familia yangu.

    BI.MARIUM: Ndio hima hima hivyo hata kabla hatujaingia ndani?

    MLINZI: Aaah nimeona nikwambie kabisa mama.

    BI.MARIUM: Basi, ngoja tupumzike halafu tutaongea vizuri.

    MLINZI: Dah mama!!

    BI.MARIUM: Kwani tatizo nini? Utakuja ndani halafu tutaongea vizuri.

    Basi bi.Marium na mwanae Pendo wakaingia ndani, mlinzi akiwa pale nje akawa anawaza mambo mbalimbali, akawa anajiuliza

    "hivi wanawezaje kuishi na mauzauza ndani namna hiyo? Ni watu wa kawaida kweli hawa? Au wenyewe hawayaoni?"

    Ikabidi nae aingie ndani ili akaongee nao na kuwaaga vizuri.

    Pendo ile kufungua mlango wa ndani akabambana na mende wengi wakizunguka huku na kule wengine wakiwa wale mende wa kuruka,

    PENDO: Mama, ona mende walivyo wengi.

    BI.MARIUM: Hata mimi nawashangaa hao mende mwanangu.

    MLINZI: Jamani hao sio mende ila ni watu.

    BI.MARIUM: Na wewe hebu acha huo uchizi wako.

    MLINZI: Hata sio uchizi mama.

    Mara wale mende wakasambaratika na hawakuonekana kwa muda huo.

    Wakiwa pale sebleni wakasikia kama vitu vinakimbizana juu ya dari. Bi.Marium akamgeukia mlinzi wake na kumwambia,.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BI.MARIUM: Tafadhari ukatutafutie dawa ya mende na panya.

    MLINZI: Mama, fungua macho yako. Humu ndani hakuna cha mende wala panya.

    BI.MARIUM: Ila kuna nini?

    MLINZI: Sijui, nimejisemea tu ila mimi nimekuja kuwaaga naondoka kidogo mama ila nitarudi.

    BI.MARIUM: Unajua hata Mariana alisema hivyo hivyo ila hajarudi hadi leo.

    MLINZI: Hapo mama hapanihusu ila tafakari na chukua hatua, haki elimu.

    BI.MARIUM: Yaani wewe kila muda ni mizaha tu.

    MLINZI: Mimi huwa najisemea tu mama.

    BI.MARIUM: Kwahiyo unataka kuondoka lini?

    MLINZI: Leo mama, nataka kuondoka leo.

    BI.MARIUM: Mbona haraka sana?

    MLINZI: Usijari, nitarudi tu.

    Basi, Bi.Marium akaenda kumchukulia pesa zake akamkabidhi na kumuaga,

    BI.MARIUM: Ila urudi kama ulivyoahidi, kumbuka hapa sina mlinzi mwingine.

    MLINZI: Sawa mama ila fanyia kazi maneno niliyokwambia.

    Halafu akaondoka.

    Wakiwa ndani ya nyumba yao Pendo na mama yake,

    PENDO: Kwani mama tulivyoondoka, uliacha unga kilo ngapi?

    BI.MARIUM: Kilo kumi mwanangu.

    PENDO: Mama, basi umeisha hakuna unga wala mchele.

    BI.MARIUM: Acha maneno hayo, yaani unga na mchele vimeisha, kamaliza nani sasa? Au huyu mlinzi alikuwa anatufanyia mchezo kabeba vyakula vyote?

    PENDO: Hata sielewi mama.

    BI.MARIUM: Tutakula nini sasa?

    PENDO: Labda tuagize chips mama maana giza limeanza kuingia.

    Wakaamua kuagiza chips maana Pendo alikuwa na namba ya baadhi ya wapika chips, baada ya muda kidogo wakaletewa.

    Wakiwa wanakula mezani, mara wakasikia kelele za sufuria yaani kama mtu anazigonga, wote wawili wakashtuka na kuanza kuulizana "nini?"

    Wakaamua kwenda jikoni ili kushuhudia ni kitu gani ila hawakuona chochote.

    Kurudi mezani, wakakuta chips zote zimeliwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog