Search This Blog

URITHI WA BABU - 1

 





    IMEANDIKWA NA : FAKI A FAKI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Urithi Wa Babu

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jina langu ni Kassim Fumbwe. Nina umri wa miaka ishirini na minane. Mkazi wa jiji la Dar es Salaam.

    Wazazi wangu walifariki dunia wakati nikiwa mdogo. Nakumbuka tulikuwa tunasafiri kutoka Dodoma kuja Dar, basi tulilokuwamo likagongana na lori uso kwa uso.

    Baba yangu na mama yangu pamoja na abiria wengine kadhaa walifariki hapo hapo. Mimi nikanusurika.

    Nakumbuka nilipata jeraha dogo tu kwenye mkono wangu wa kushoto baada ya kukatwa na vioo vya dirisha vilivyokuwa vimevunjika.

    Babu yangu mzaa baba, Mzee Fumbwe Limbunga alipopata habari ya ajali ile alitoka Dar kwa gari lake akaja Morogoro. Majeruhi wa ajali ile tulikuwa tumelazwa katika hospitali ya Morogoro.

    Mimi sikuwa nimeumia sana lakini kwa vile wazazi wangu walikuwa wamefariki ilibidi nibaki hapo hospitali ili niweze kutambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zangu.

    Babu alipokuja akanichukua. Aliichukua pia miili ya marehemu baba yangu na mama yangu.

    Siku ya pili yake habari za ile ajali zilichapwa kwenye magazeti. Kila gazeti lilikuwa limechapa picha yangu ikielezea jinsi nilivyonusurika kimiujiza.

    Baada ya msiba huo, nikawa ninaishi na babu. Babu yangu alikuwa tajiri lakini alikuwa hana mke. Aliachana na mke wake tangu alipokuwa kijana na hakutaka kuoa tena.

    Kwa hiyo alinitafutia mtumishi wa kunihudumia kwa kila kitu ikiwa ni pamoja na kunipeleka shule. Nilipoanza masomo ya sekondari babu akanihamisha katika nyumba yake nyingine. Zote zilikuwa Tegeta lakini zilikuwa mitaa tofauti.

    Ile nyumba aliyonihamishia upande mmoja ilikuwa na mpangaji, upande mwingine ndio niliokaa mimi.

    Kila jumatatu babu alikuwa akinipa pesa za kutumia kwa wiki nzima. Baadhi ya siku nilikuwa ninapika mwenyewe nyumbani na siku nyingine nilikuwa ninakula kwenye mikahawa..

    Baada ya kumaliza masomo yangu nilipata kazi Morogoro. Lakini babu alinishauri niache kazi nifanye biashara. Aliponipa mtaji nikaacha kazi. Nilifungua maduka matatu ya vifaa vya ujenzi pale Morogoro.

    Yalikuwa maduka makubwa. Niliajiri karibu wafanyakazi kumi na watano. Kila duka lilikuwa na wafanyakazi watano. Biashara ilianza vizuri. Baada ya miezi sita tu nikaja Dar kununua gari la kutembelea.

    Sasa nikawa nafikiria kutafuta mke nioe. Sikumaliza hata mwaka mmoja ile kasi ya biashara ikaanza kupungua. Maduka yangu yaliyokuwa yamejaa vitu yakaanza kuwa matupu. Haukupita muda mrefu nikaanza kupunguza wafanya kazi. Mwisho kila duka likabaki na mfanyakai mmoja.

    Nilifikia mahali nikahisi kuwa pengine sikuwa na nyota ya kujiajiri. Nikajuta kuacha kazi niliyokuwa nayo mwanzo. Ikabidi yale maduka mawili niyafunge nikabaki na duka moja ambalo nililisimamia mwenyewe. Duka hilo nalo likafilisika nikalifunga. Nikawa sina kazi.

    Nilifikiria kwenda kumueleza babu ili anipe mtaji mwingine lakini nilishindwa kwani nilijua asingekubali tena kunipa pesa zake. Nikauza lile gari. Siku ile nauza gari babu akanipigia simu na kunijulisha kuwa alikuwa anaumwa na alikuwa amelazwa katika hospitali ya Aga Khan.

    Nikapanda basi kuja Dar. Nilipofika Dar nilikwenda moja kwa moja katika hospitali katika hospitali ya Aga Khan..

    Vile nafika tu na babu yangu anakata roho. Hata sikuwahi kuzungumza naye lolote.

    Kifo chake babu hakikunishitua sana kwa sababu alikuwa na mali na mimi ndiye ambaye ningemrithi.

    Dereva wake nilimkuta hapo hapo hospitali, alinieleza kuwa Mzee Fumbwe alianza kuumwa siku tatu zilizopita lakini usiku uliopita ndio alizidiwa. Presha ilikuwa juu na sukari ilipanda. Hali ikawa mbaya.

    Kwa kushirikiana na dereva huyo tuliuchukua mwili wa Mzee Fumbwe siku ya pili yake kwa ajili ya maziko. Baada ya maziko nikaanza mchakato wa kukagua mali za marehemu.

    Nilichokuwa nikikifahamu awali ni kuwa babu yangu alikuwa na maduka kadhaa Dar es Salaam. Alikuwa na vituo vitatu vya mafuta na malori sita.

    Pia alikuwa na nyumba alizokuwa amezipangisha ambazo sikujua zilikuwa ngapi.Nilikuwa nikijua nyumba mbili tu, ile aliyokuwa akiishi yeye na ile niliyokuwa nikikaa mimi kabla ya kuhamia Morogoro.

    Mali zake nyingine alikuwa akizijua yeye mwenyewe. Niliingia chumbani mwake nikafungua makabati na kuanza kupekuwa nyaraka zake alizozihifadhi kwa lengo la kutambua mali hizo.

    Jambo ambalo lilinishangaza, nilikuta hati ya nyumba yake aliyokuwa akiishi na hati za gari alilokuwa akilitumia. Sikukuta hati wala nyaraka nyingine zinazohusu mali zake.

    Wakili wake nilikuwa namfahamu. Nikaenda ofisini kwake barabara ya Samora na kumjulisha kuhusu kifo cha mteja wake.

    “Oh mzee amefariki?” akaniuliza kwa mshituko.

    “Amefariki juzi, tumemzika jana”

    “Alikuwa mgonjwa?”

    “Wakati anaumwa mimi nilikuwa Morogoro. Juzi akanipigia simu yeye mwenyewe akaniambia kuwa anaumwa na amelazwa hospitali. Muda ule ule nikapanda gari kuja kumuona. Mpaka nafika Dar nikakuta ameshafariki”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Oh pole sana. Aliwahi kuniambia kuwa mwanawe alifariki dunia”

    “Mwanawe ni baba yangu. Alifariki mimi nikiwa mdogo”

    “Kwa hiyo mrithi wake utakuwa wewe. Kwa maana hakuwahi kuandika wasia wowote ila alinieleza kuwa hakuwa na ndugu wala mtoto mwingine isipokuwa mjukuu”

    Wakili alipoleta suala la urithi akawa amenirahisishia tatizo lililokuwa limenipeleka kwake.

    “Hilo ndilo lililonileta kwako”

    “Umefanya vizuri kuja kunifahamisha. Sasa unatakiwa ufungue mirathi mahakamani ili uweze kumrithi babu yako”

    “Kabla ya kufungua mirathi kuna suala moja ambalo limenishitua sana”

    “Suala gani?”



    “Kuhusu mali za marehemu. Babu yangu alikuwa tajiri lakini katika kumbukumbu zake nimekuta hati ya nyumba moja aliyokuwa anaishi pamoja na hati ya gari alilokuwa akitumia”

    “Sasa kama hakuna hati wala nyaraka zozote utazijuaje mali zake nyingine?”

    “Kwanza hizo nyaraka zitakuwa zimekwenda wapi?”

    “Nenda kapekue vizuri. Inaweekana aliuza baadhi ya mali zake”

    Kutokana na ushirikiano alionipa wakili huyo kutafiti mali alizokuwa akimiliki marehemu babu yangu, tuligundua kuwa mpaka marehemu anafariki duniani hakuwa na mali yoyote aliyoacha zaidi ya nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na gari lake.

    Hata baada ya kufungua mirathi mahakamani na kuthibitishwa kuwa mimi ndiye mrithi wa marehemu, sikukuta pesa ya maana katika akaunti yake ya benki. Akaunti yake ilikuwa na shilingi elfu kumi tu.



    Kwa Kweli mimi na wakili wa marehemu tulishangaa sana. Kila mtu alikuwa akifahamu kuwa Mzee Fumbwe alikuwa ni miongoni mwa matajiri wazawa wa jiji la Dar es Salaam. Jinsi alivyokufa akiwa masikini ni jambo ambalo halikueleweka.

    Katika utafiti nilioufanya baadaye niligundua kuwa Mzee Fumbwe alikuwa ameuza baadhi ya mali zake zikiwemo nyumba na vituo vya mafuta siku chache kabla ya kufariki dunia.

    Lakini uchunguzi wangu ulishindwa kubaini marehemu alipeleka wapi pesa zake kwani benki hakukuwa na kitu.

    Kwa kipindi cha karibu wiki mbili nilikuwa nikiendelea kufanya utafiti kwenye nyaraka za marehemu ili kupata uhakika kwamba kweli babu hakuwa na kitu.

    Nikaja kugundua kitabu cha kumbukumbu cha marehemu ambacho alikuwa akiandika mambo yake. Nilipopekua karasa na kitabu hicho niliona kulikuwa na watu ambao walikuwa wakifanya biashara na babu na kwamba babu alikuwa akiwadai wafanyabiahara hao pesa nyingi.

    Nilikuta majina ya wafanya biashara wanne. Katika watu hao ni mmoja tu aliyekuwa akiishi hapo Dar, wengine walikuwa wakiishi nchi za nje. Mwenyewe aliandika kama ifuatavyo

    Abdul Baraka wa Mbezi Dar es Salaam. Namdai dola milioni moja.

    (Aliandika na namba ya simu yake)

    Isaac Chusama wa Harare Zimbambwe. Namdai dola milioni mbili na laki tano.

    (Aliandika namba ya simu yake na mtaa aliokuwa anaishi)

    Benjamin Muhoza wa Gaborone Botswana. Namdai dola milioni moja na laki tano.

    (Aliandika namba ya simu yake na mtaa aliokuwa akiishi)

    Dumessan Dube wa Cape Town Afrika Kusini. Namdai dola milioni tatu.

    (Aliandika namba ya simu yake na mtaa aliokuwa akiishi)

    Hapo nikajua kuwa marehemu babu alikuwa akidai fedha nyingi kwa watu waliokuwa wakiishi nje ya nchi.

    Kitabu hicho cha kumbukumbu kiliendelea kunjulisha siri ya babu ambayo nilikuwa siifahamu. Babu alikuwa akifanya biashara ya madini. Tena madini ya Tanzanite na kwamba alikuwa akiwauzia wafanya biashara hao.

    Kumbukumbu za nyuma za kitabu hicho zilionesha ameshawahi kuwauzia madini wafanyabiashara hao kwa thamani ya dola ya Kimarekani. Na kwamba alikuwa akilipwa kwa awamu.

    Nikajiuliza babu alikuwa akipata wapi madini mengi kiasi cha kumpatia mamilioni hayo ya dola?

    Swali jingine nililojiuliza ni wapi babu yangu alikokuwa anaficha fedha hizo, isingewezekana afe akiwa hana kitu.

    Niliitafuta paspoti yake na nikaipekua. Nikagundua kuwa mara kwa mara alikuwa akitembelea Zimbabwe, Botwana na Afrika kusini.

    Nilipopekua zaidi kwenye mafaili yake nikaipata mikataba yake na wafanya biashara hao. Alikuwa amelipwa pesa nusu na nusu alikuwa akiwadai. Tarehe ya kuwafuata wafanya biashara hao wammalizie deni lake ilikuwa imeshapita.

    Nikajiambia kama nitafanikiwa kupata fedha hizo nitakuwa tajiri mkubwa hapa Dar kwani kwa pesa za Kitanzania dola hizo zilikuwa ni mabilioni ya shilingi.

    Kwa vile marehemu aliandika namba za simu zao, nikaanza kumpigia Abdul Baraka aliyekuwa hapo Dar. Nilimpigia kwa kutumia laini ya marehemu. Simu yake haikupatikana.

    Nikampigia Isaac Chusama wa Harare. Simu iliita kwa sekunde chache kisha ikapokelewa.

    Nikashangaa kusikia sauti ikinisalimia kwa Kiswahili.

    “Habari yako Bwana Fumbwe?”

    “Nzuri lakini mimi siye Bwana Fumbwe. Bwana Fumbwe amefariki wiki tatu zilizopita, mimi ni mjukuu wake. Naitwa Kassim Fumbwe”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Heh! Mzee Fumbwe amefariki?”

    “Amefariki. Hivi sasa ni wiki tatu zimeshapita”

    “Oh pole sana”

    “Asante. Sasa kumbukubu za babu zinaonesha kwamba alikuwa akikudai dola milioni mbili na laki tano. Na mkataba wa makubaliano yenu ninao hapa”

    “Ndio ni kweli ananidai”

    “Kwa vile tarahe ya kumlipa imeshapita, ninataka nije Harare unipatie hizo fedha. Mimi ndio mrithi wake”

    “Sasa nitakuaminije Bwana Fumbwe?”

    “Nitakuja na hati zote zikiwemo hati za mahakama zinazoonesha kwamba mimi ndiye mrithi wa marehemu, cheti cha kifo chake na mikataba ya makubaliano yenu”

    Pakapita kimya cha sekunde kadhaa kabla ya sauti ya mtu wa upande wa pili kusikika tena.

    “Unatarajia kuja lini?”

    “Baada ya siku mbili tatu. Hivi sasa ninajiandaa kwa safari”

    “Utakapokuja utanijulisha”

    “Sawa”

    Isaac akatangulia kukata simu.

    Hapo hapo nikampigia Benjamin Muhoza. Nilishukuru naye alipopokea simu.



    Alinisalimia kwa Kingreza kwa kutumia jina la marehemu babu yangu. Na yeye nikamjulisha kuwa Mzee Fumbwe alikuwa amefariki dunia na kwamba mimi nilikuwa mjukuu wake.

    “Ulikuwa unataka nini?” akaniuliza.

    “Kumbukumbu za babu zinaonesha kwamba anakudai dola milioni moja na laki tano. Mikataba yenu ninayo hapa. Mimi ndiye mrithi wake”

    Simu ya upande wa pili ikawa kimya. Nilipoona amenyamaza nilimwambia.

    Ninazo hati za mahakama zinazothibitisha kuwa mimi ndiye mrithi wa marehemu. Nina cheti cha kifo chake na nina mkataba wa makubaliano yenu”

    “Utakuja kunionesha?” Benjamin akaniuliza.

    “Nitakuja kukuonesha ili uthibitishe kuwa Mzee Fumbwe amefariki na kwamba mimi ndiye ninayepaswa kulipwa madeni yake”



    “Utakuja lini?”

    “Nitakujulisha siku ambayo nitakuja”

    “Sawa”

    Nikakata simu kisha nikampigia Dumessan Dube wa Afrika Kusini.

    Yeye nilizungumza naye kama nilivyozungumza na wenzake lakini yeye hakushangaa nilipomwambia Mzee Fumbwe amefariki. Aliniambia ameshapata habari.

    “Umepata habari hiyo kutoka wapi?” nikamuuliza.

    “Nimeipata kutoka kwa marafiki mbalimbali ambao anafanya nao biasharara”

    “Ni vyema kama umeshapata habari. Kwa hiyo mimi ndiye mrithi wake. Nimekuta una deni la dola milioni tatu ambazo babu anakudai”

    “Umelikuta wapi deni hilo?”

    “Kwenye kumbukumbu zake na mkataba wenu wa makubaliano pia ninao hapa”

    “Sawa” Dube aliniambia baada ya kimya kifupi kisha akaniuliza.

    “Sasa ulitakaje?”

    “Nimeona tarehe ya malipo ya hizo pesa imeshapita. Nilitaka nije Afrika Kusini unipatie pesa hizo. Nitakuja na hati zote”

    Baada ya kimya kingine kifupi, Dube aliniambia.

    “Sawa. Unatarajia kuja lini?”

    “Nitakujulisha”

    “Sawa”

    Kusema kweli baada ya kuzungumza na wafanyabiashra hao waliokuwa nje ya nchi nilifarijika sana. Yule mfanyabiashara aliyekuwa Dar es Salaa ambaye simu yake ilikuwa haipatikani nilimuacha kiporo.

    Niliona sasa urithi wa babu ulikuwa unakuja mikononi mwangu taratibu. Nikajiambia kama pesa hizo nitazipata zote ningekuwa miongoni mwa matajiri wakubwa katika jiji hili.

    Nilimshangaa marehemu babu yangu kwa kuacha kiasi kikubwa cha pesa nje ya nchi bila kunishirikisha mimi mjukuu wake. Kwa kweli alikuwa msiri sana na pia alikuwa tajiri japokuwa mali alizokuwa akimiliki hapo Dar bado zilikuwa ni kitendawili.

    Sikwenda kumueleza wakili kuhusu madeni hayo. Niliacha yabaki kuwa siri yangu. Sasa nikaanza kujiandaa kwa safari ya nchi hizo tatu huku ndoto za utajiri zikiwa zimetawala akili yangu.

    Baada ya wiki mbili nikawa nimeshapata pesa za kuniwezesha kuzuru katika nchi hizo. Mipango yangu ya safari ilipokamilika nikaanza safari yangu. Kwanza nilipanga kwenda Harare Zimbabwe. Kabla ya kuondoka nilimpigia simu Isaac Chusama kumjulisha kuwa ninakwenda Zimbabwe.

    “Sawa. Ukifika utanipigia simu kunijulisha kuwa umefika” akaniambia.

    “Sawa”

    Nilifika Harare kama saa nane mchana. Nikiwa katika kiwanja cha ndege cha Harare nilimpigia simu Chusama kumjulisha kuwa nilikuwa uwanja wa ndege wa Harare. Nilitumia simu ya malipo iliyokuwa pale kiwanja cha ndege.

    “Kama umeshafika kodi teksi. Mwambie dereva akupeleke Chapachapa Hotel. Nimekukodia chumba namba 35”

    “Natumaini madereva wa teksi watakuwa wanaifahamu ilipo hoteli hiyo”

    “Wanaifahamu. Ni hoteli maarufu”

    “Sawa. Ngoja nikodi teksi”

    Baada ya kumaliza kuzungumza na mwenyeji wangu huyo nilitoka nje ya uwanja wa ndege na kukodi teksi. Sasa nilikuwa natumia kingereza kitupu.

    Nilimwammbia dereva wa teksi anipeleke Chapachapa Hotel. Baada ya mwendo wa saa moja kasorobo akanifikisha katika hoteli hiyo iliyokuwa katikati ya jiji la Harare.

    .

    Baada ya kumlipa dereva pesa aliyotaka niliingia hotelini humo. Unapoingia unakutana na ukumbi mwanana uliokuwa na viti na meza.

    Kwenye meza moja iliyokuwa karibu na mlango aliketi msichana mmoja mrembo aliyekuwa akinywa soda huku akisoma gazeti. Upande wa kushoto wa ukumbi huo ndio palikuwa mapokezi.

    Nikaenda hapo mapokezi na kujitambulisha kuwa nilikuwa mgeni wa Isaac Chusama na kwamba aliniambia kuwa amenikodia chumba namba 35.

    “Oh ndiye wewe! Hebu lete paspoti yako tuione” Mhudumu wa mapokezi ambaye alikuwa msichana akaniambia.

    Nikampa paspoti yangu iliyokuwa mkononi kama kitambulisho changu huku tukizungumza Kiingereza.

    Baada ya kuifungua paspoti yangu na kuiona picha yangu alinirudishia.

    Nikapelekwa chumba namba 35 kilichokuwa ghorofa ya kwanza. Nilikuta kiyoyozi, tv na simu ya mezani iliyowekwa kwenye kimeza kilichokuwa kando ya kitanda. Pia kulikuwa na kochi moja refu na kabati la kuwekea nguo pamoja na meza ya kuvalia iliyokuwa na kioo kikubwa.

    Nilipoona ile simu niliweka begi langu juu ya kochi nikaketi kitandani na kuinua mkono wa simu.

    Simu zilikuwa zinapitia kwa opereta aliyekuwa hapo hoteli ambaye alipopokea simu yangu nilimpa namba ya Isaac Chussama.

    Sekunde chache tu baadaye nikaisikia sauti ya Chusama.

    “Helow!”

    “Mimi ni yule mgeni wako kutoka Tanzania, nimeshafika katika hoteli ya Chapachapa”

    “Umepewa chumba?”



    “Ninaongea na wewe nikiwa chumbani”

    “Sawa. Kama utahitaji chakula au kinywaji chochote agiza tu, nimeweka oda kwa ajili yako”

    “Sawa”

    “Nitakuja kuonana na wewe baada ya dakika chache”

    “Nakusubiri”

    Baada ya hapo kukawa kimya. Nikaurudisha mkono wa simu kisha nikatoka humo chumbani. Nilifunga mlango kwa funguo nikashuka chini.

    Unaposhuka chini unatokea pale mapokezi, nikaenda kukaa kwenye meza moja katika ule ukumbi. Yule msichana niliyemuona ameketi nilipoingia alikuwa bado ameketi akisoma gazeti.

    Nilikuwa nimevutiwa na umbile lake la kupendeza na sura yake jamali.

    Lakini laiti kama ningetambua tukio ambalo lingetokea hapo hoteli ningeahirisha mapema safari yangu!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuketi mhudumu alikuja kuniuliza kama nilikuwa nahitaji kitu, akanipa menyu.

    Kwenye menyu niliona ugali kwa samaki. Nikatamani kula ugali wa Kizimbabwe. Nikamuagiza mhudumu huyo aniletee ugali kwa samaki.

    Wakati nasubiri nilitewe ugali nilioagiza, nilimuona mtu mmoja aliyekuwa amevaa suti nyeusi akiingia hapo hoteli. Alipomuona yule msichana aliyekuwa amekaa karibu na mlango alisita kisha akavuta kiti na kuketi naye. Nikaona wanazunguma ingawa sikuweza kusikia walikuwa wanazungumza nini.

    Mhudumu alimfuata yule mtu, nikaona anaagiza kitu. Baadaye kidogo waliletewa chupa mbili za bia na kuanza kunywa. Mimi nilikuwa nimeshaletewa chakula nilichoagiza.

    Nilikuwa nikila ugali huku jicho langu likiwa kwa wale watu. Kama sijakosea walikunywa bia mbili mbili. Mimi nilikuwa nimeshamaliza ugali wangu wakati yule mtu alipoinuka na kwenda mapokezi. Alizungumza na mhudumu wa mapokeziki kabla ya kupewa funguo.

    Baada ya kupewa funguo alirudi kwa yule msichana akazunguma naye akiwa amesimama. Baada ya muda kidogo msichana aliinuka wakaenda kupanda ngazi.

    Nilihisi kama vile yule mtu alikuwa amechukua chumba na alikuwa akielekea chumbani na yule msichana. Huenda walikuwa wakijuana na kwamba yule msichana alikuwa akimsubiri yule jamaa pale.

    Niliendelea kuketi pale pale nikiangalia televisheni iliyokuwa imepachikwa katika ukuta. Nilipoona muda unazidi kwenda niliondoka nikarudi chumbani kwangu na kumpigia simu mwenyeji wangu.

    Nilitaka kumuuliza mbona hatokei kwani muda mrefu ulikuwa umepita tangu aliponiahidi kuwa anakuja. Simu ikaita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

    Simu ilipokata nikapiga tena lakini pia haikupokelewa. Nikaamua kusubiri kabla ya kupiga tena.

    Kwa vile sikuwa na kingine cha kufanya, niliona nijilaze pale kitandani. Bila kujitambua usingizi ukanipitia hapo hapo.

    Nilipozinduka ilikuwa usiku. Niliwasha taa kisha nikatazama saa. Ilikuwa saa mbili na robo usiku. Nikapiga tena simu lakini bado simu ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.

    Nikawa nimechukia. Nilihisi huyo mtu aliyefanya niende Zimbabwe hakuwa na ahadi za kweli. Nikaenda kuoga. Niliporudi nilipiga simu tena. Nilipiga mara tatu bila kupokelewa. Simu ilikuwa inaita tu.

    Nikashuka chini na kula chakula kisha nikarudi tena juu. Nikapiga tena simu lakini haikupokelewa. Ilikuwa kama vile simu ilikuwa peke yake au mwenye simu aliamua kunisusia.

    Kusema kweli nilichanganyikiwa. Nilikuwa sijui la kufanya. Nikalala. Asubuhi nilipoamka kitu cha kwanza kilikuwa kupiga simu. Simu ya Chusama bado ilikuwa ikiendelea kuita tu. Sasa nikaanza kupatwa na wasiwasi.

    Nikashuka chini na kupata kifungua kinywa. Wakati naendelea kunywa chai. Nilisikia nung’unung’u hapo hoteli kuwa kuna mtu aliyeuawa akiwa ndani ya chumba cha hoteli.

    Tukio hilo liligunduliwa na mhudumu wa usafi ambaye aliingia katika chumba hicho na kukuta maiti ya mwanaume iliyokuwa imelazwa chini.

    Baadaye polisi walifika hapo hoteli. Waliongozwa na baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo kuelekea katika chumba hicho kilichokuwa ghorofa ya kwanza. Na mimi kwa kutaka kupata ukweli niliinuka nilipokuwa nimeketi nikaelekea huko huko.

    Kilikuwa chumba kilichopakana na chumba nilicholala mimi. Mlango ulikuwa umeachwa wazi na polisi pamoja na baadhi ya wafanyakazi walikuwa wameingia ndani.

    Sikuweza kumuona vizuri mtu huyo mpaka mwili wake ulipokuwa unatolewa ukiwa kwenye machela. Nilipomuona tu nikamtambua. Alikuwa ni yule mtu ambaye alifika jana yake pale hoteli na kuzungumza na yule msichana na kisha wakaondoka pamoja kuelekea chumbani.

    Hata hivyo yule msichana aliyekuwa naye hakuwepo. Ilisemekana kwamba alitoroka kabla ya tukio hilo kugundulika.

    Mpaka mwili wa mtu huyo unatolewa, polisi hawakuwa wamegundua mtu huyo alikuwa ameuawa kwa kitu gani. Kwenye pua yake na kwenye pembe moja ya midomo yake kulikuwa na michirizi ya damu iliyoganda.

    Kulikuwa na baadhi ya wafanyakazi ambao walichukuliwa na polisi kwenda kutoa maelezo.

    Nikajiuliza kama yule mwanamke alikuwa muuaji kweli. Hakuonekana kuwa katili. Niseme ukweli kama ndiye aliyemuua yule mtu, tukio lile lingenikuta mimi kwani jana yake ilibaki kidogo niende nikakae naye.

    Nikashukuru kwamba Mungu alikuwa ameninusuru.

    Ingawa tukio hilo lilichnaganya akili yangu lakini kitendo cha mwenyeji wangu kutopokea simu kilinichanganya zaidi. Niliingia chumbani na kutafakari nifanye nini. Kwa kweli sikupata jibu.



    Ilipofika saa saba mchana wakati natazama taarifa ya habari kwenye televisheni, lile tukio la mauaji lililotokea pale hoteli lilitangazwa.

    Kitu ambacho kilinishitua ni kuwa mtangazaji alimtaja marehemu kuwa ni Isaac Chusama mtu ambaye alikuwa hafahamiki alikuwa akifanya kazi gani. Alitaja mtaa aliokuwa akiishi na kueleza kuwa hakuwa na mke wala watoto.

    Taarifa ilieleza kuwa Chusama alifika hapo hoteli majira ya mchana na kuzungumza na msichana mmoja aliyekuwa ameketi kwenye ukumbi wa hoteli hiyo kabla ya kukodi chumba na kuingia chumbani na msichana huyo.

    Taarifa ya televisheni iliendelea kueleza kuwa asubuhi ya siku ile mhudumu wa usafi wa hoteli hiyo aliigundua maiti ya Chusama iliyokuwa imelazwa chini na kutoa taarifa kwa uongozi wa hoteli.



    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchunguzi wa madaktari umeonesha kuwa marehemu alikabwa koo hadi mauti yakamkuta.

    Msemaji wa polisi akaeleza kuwa polisi wanamshuku msichana aliyekuwa naye kuhusika na mauaji hayo na wameanzisha msako wa kumtafuta.

    Baada ya taarifa hiyo kutolewa kwenye televisheni, nilibaini kuwa mtu aliyefika hapo hoteli na hatimaye kuuawa alikuwa ni mwenyeji wangu Isaac Chusama!

    Hapo niligundua sababu ni kwanini simu nilizokuwa nikipiga zilikuwa hazipokelewi. Zilikuwa haipokelewi kwa sababu Chusama mwenyewe alikuwa ameshauawa. Bila shaka alikuwa ameuawa siku iliyopita.

    Sasa nikabaki na maswali kuhusiana na tukio hilo. Nilijiuliza yule msichana alikuwa nani?

    Je alikuwa akijuana na Chusama?

    Na ni kwanini amemuua?

    Pia nilijiuliza baada ya Chusama kuuawa, kulikuwa na uwezekano kweli wa kulipwa pesa zangu? Na ni nani atanilipa?

    Baada ya kufikiri kwa kina niliona uwezekano wa kulipwa pesa zangu haukuwepo. Kwani licha ya kuwa ni pesa nyingi nilizokuwa nikimdai Chusama pia nilikuwa si mwenyeji wa hapo na pengine nisiaminike na huyo ambaye atapaswa kulipa deni hilo.

    Lakini baya zaidi, nilijiambia kama nitajitia kuwatafuta ndugu na jamaa wa Chusama ili wanilipe deni hilo wanaweza kuniripoti polisi na nikakamatwa na kuhusishwa na mauaji ya Chusama. Hapo nikaingiwa na hofu.

    Matumaini ya kupata pesa nilizozifuata huko Zimbabwe yakaanza kuota mbawa. Kule kukata tamaa na kuona safari niliyoifanya ilikuwa ya bure, nilijikuta nikimlaumu Chusama kwa uzembe. Licha ya kutojua kama yule msichana alikuwa na uhusiano naye au la, nilimlaumu Chusama kwa kuonesha kuwa na tamaa ya ngono iliyopitiliza.

    Niliamini kuwa Chusama alipokuwa anakuja pale hoteli alikuwa akinifuata mimi lakini ghafla akili yake ilikwenda kwa yule msichana akasahahu kwamba nilikuwa na ahadi naye na hata nilipompigia simu hakupokea. Matokeo yake yalikuwa ni kuuawa.

    Lakini ni kwanini auawe? Nikajiuliza na

    kuendelea kujiuliza, yule msichana alikuwa nani? Ana kisa naye gani na baada ya kumuua Chusama, alipotelea wapi?

    Sikuweza kupata jibu hata la kukisia. Nilikuwa nimeketi pale ukumbini nikainuka na kurudi chumbani.

    Wakati ninapanda ngazi nilijiambia ni vizuri niondoke haraka hapo Zimbabwe kwani licha ya kuwa nisingepata faida yoyote kwa kuendelea kukaa hapo bali pia nilitaka kuepuka uchunguzi wa polisi.

    Nilihisi kwamba katika uchunguzi wao polisi wanaweza kugundua kwamba Chusama alikuwa amenipangia chumba pale hoteli na ninaweza kukamatwa na kuulizwa nilikuwa na mpango naye gani.

    Baada ya kuingia chumbani nilichukua begi langu nikatoka kimya kimya. Nilikodi teksi na kurudi kiwanja cha ndege. Kwa bahati njema nilikuta kulikuwa na ndege inayokwenda Botswana ambayo bado ilikuwa na nafasi.

    Nikakata tikiti ya ndege ya kwenda Botswana. Ndege iliondoka maasaa matatu baada ya mimi kufika kiwanja cha ndege. Nilipofika Gaborone, nilimpigia simu Benjamin Muhoza na kumjulisha kuwa nilikuwa katika kiwanja cha ndege cha Gaborone.

    “Subiri ninatuma gari ikufuate” Sauti ya Muhoza ikasikika kwenye simu.

    “Dereva wako atanitambuaje” nikamuuliza.

    “Umevaa mavazi gani?”

    “Kwanza mimi ni mrefu wa wastani na mweupe. Nimevaa tisheti ya rangi ya samli, suruali aina ya jinzi ya rangi ya samawati. Nimevaa miwani ya jua”

    “Atakutambua. Nitakupa namba ya usajili ya gari atakalokuja nalo”

    “Sawa”

    Muhoza alinitajia namba ya usajili ya gari hilo, aina yake na rangi yake. Nikamwambia nitalitambua litakapofika.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Saa moja baadaye nikiwa hapo nje ya jengo la uwanja wa ndege nikaliona gari hilo likiwasili. Sikutaka kumpa dereva wa gari hilo taabu ya kunitafuta. Nikamfuata.

    Baada ya kujitambulisha kwake kuwa mimi ndiye mgeni wa Chusama aliniambia nijipakie kwenye gari.

    Nilijipakia katika siti ya mbele iliyokuwa kando ya dereva. Gari hilo lilinipeleka katika hoteli moja ambapo mwenyeji wangu tayari alikuwa amenichukulia chumba.

    “Sasa acha nimfuate mheshimiwa” Dereva akaniambia baada ya kunifikisha hapo hoteli. Akaongeza.

    “Aliniambia nikishakufikisha hapa hoteli nimfuate”

    “Sawa” nikamjibu. Wakati huo nilikuwa nimekaa katika bustani iliyokuwa mbele ya hoteli ambayo iliwekewa viti na meza.

    “Unaweza kuagiza kinywaji unachotaka au chakula”

    “Labda kinywaji tu, sitapenda kula kitu chochote kwa sasa” nikamwambia.

    Dereva huyo alipoondoka muhudumu alinifuata na kuniuliza kama nilikuwa ninahitaji huduma yoyote.

    “Nipatie soda tu” nikamwambia.

    “Soda gani?”

    “Fanta”

    Mhudumu akaondoka. Baada ya muda mfupi alirudi na kuniletea soda niliyomuagiza



    Wakati namaliza kunywa ile soda nikaona lile gari likisimama kando ya hoteli akashuka dereva wa gari hilo na mtu mwingine aliyekuwa amevaa suti nyeusi. Pia alishuka msichana.

    Watu hao watatu wakaingia katika eneo la hoteli. Kitu ambacho kilinishitua na kunipa mshangao ni kuwa yule msichana

    alikuwa ndiye yule muuaji wa Isaac Chusama aliyekuwa akitafutwa na polisi kule Zimbabwe.

    Kwa kweli nilipomuona kwa mara nyingine nilishituka sana. Yule msichana aliketi katika meza iliyokuwa mbali na meza yangu. Dereva wa lile gari pamoja na yule mtu mwingine wakaja katika meza niliyokuwa nimeketi.

    “Mgeni mwenyewe ni huyu hapa” Yule

    dereva akamwambia yule mtu ambaye alinipa mkono kunisalimia.

    Baada ya kusalimiana naye alikaa kwenye kiti akanitambulisha kuwa yeye ndiye Benjamin Muhoza niliyekuwa ninawasiliana naye.

    Na mimi nikamtambulisha jina langu na kumueleza kuwa nilikuwa mjukuu wa marehemu babu yangu mzee Fumbwe Limbunga.



    “Nimefurahi kukufahamu. Uliniambia kuwa ungekuja na hati zote za marehemu Limbunga zilizohusu biashara yetu na pia hati ya mahakama inayokuthibitisha kuwa wewe ndiye mrithi wa marehemu” Mtu huyo aliniambia kwa sauti tulivu.

    “Nimekuja na hati zote”

    “Nitolee”

    Nikafungua mkoba wangu ambao nilikuwa nimeuweka juu ya meza, nikatoa hati mbalimbali. Kwanza nilimuonesha cheti cha kifo cha mzee Fumbwe Limbunga akakitazama kwa makini.

    Kisha nilimtolea hati ya mahakama iliyonithibitisha mimi kuwa mrithi wa Fumbwe limbunga. Hati hiyo niliiwekea picha yangu kama mrithi na picha ya marehemu kama mrithiwa.

    Muhoza aliitazama hati hiyo kwa unagalifu.

    Nilimuachia sekunde thelathini ili amalize kuisoma hati hiyo iliyokuwa imeandikwa kwa kingreza kisha nikamtolea mkataba

    ambao aliwekeana saini yeye na babu.

    Alipouona ule mkataba alinitazama akatingisha kichwa chake kuonesha kunikubalia.

    “Nafikiri nimeweza kukuthibitishia” nikamwambia wakati akiupekua ule mkataba.

    “Hakuna tatizo. Nimeona hapa kuwa mzee Fumbwe amefariki na wewe ndiye mrihi wake ambaye unapaswa kulipwa madeni ya marehemu”

    Aliponiambia hivyo alinyamaza kimya kwa sekunde kadhaa kabla ya sauti yake kusikika tena.

    “Hivi unaiendeleza ile biashara ya marehemu babu yako?”

    Nikatikisa kichwa.

    “Hapana. Ile biashara ilikuwa ni yake mwenyewe. Mimi sikuhusika nayo”

    “Huwezi kuyapata yale madini ya Tanzanite?”

    “Sijui marehemu alikuwa akiyapata wapi”

    “Na hakuna mtu yeyote unayenfahamu anayefanya biashara ile huko Tanzania?”

    “Labda nikuulizie halafu nikufahamishe kwenye simu”

    Nilipomwammbia hivyo mtu huyo alinyamaza tena kama aliyekuwa akiwaza.

    Baada kimya cha sekunde kadhaa aliniambia.

    “Sasa sikiliza, nipe muda niweze kukutayarishia pesa zako”

    “Muda gani?” nikamuuliza.

    “Muda wa siku moja tu, yaani kesho asubuhi ninakupatia pesa zako uende zako”

    “Naweza kusubiri mpaka kesho. Hata hivyo nisingeweza kuondoka leo”

    “Sawa. Nimekuchukulia chumba hapa hoteli, utakula, utakunywa. Gharama ni juu yangu. Wewe hutalipa chochote hadi hapo kesho tutakapomalizana mimi na wewe”

    “Sawa”

    “Nitakufuata kesho saa tatu”

    Aliniambia na kuinuka kwenye kiti. Tukaagana kisha akaondoka pamoja na dereva wake. Walikwenda kwenye ile meza aliyoketi yule msichana. Yule mtu alikaa kwenye kiti lakini dereva wake aliondoka.

    Niliona wakiagiza vinywaji. Wakaendelea kunywa na kuzungumza kwa karibu masaa matatu kabla ya kuondoka.

    Kitu ambacho kilitia shaka katika moyo wangu ni kuhusu yule msichana muuaji ambaye alidaiwa kumuua mtu kule Zimbabwe na hatimaye kuibukia hapo Botswana.

    Nilijiuliza yule msichana ni nani na ni kwanini alipotoka kumuua Chusama, mtu ambaye nilikuwa na mipango naye, amekwenda huko Boswana kwa mtu mwingine ambaye pia nilikuwa na mipango naye.

    Nikaendelea kujiuliza iwapo Muhoza alikuwa na uhusiano na yule msichana na kama alikuwa anajua kama msichana huyo alikuwa anatafutwa na polisi wa Zimbabwe kwa mauaji.

    Kusema kweli sikupata jibu licha ya kujiuliza maswali kadhaa kichwani mwangu.

    Mwenyeji wangu alipoondoka na yule msichana na mimi niliondoka na kwenda chumbani kwangu. Nikajilaza kwenye kitanda huku mawazo yangu yakiwa kwenye utajiri.

    Nilijiambia ingawa nilizikosa pesa a Chusama baada ya kuuawa, nitaziata pesa za Muhoza ambazo nikichanganya na pesa nitakazopata kutoka kwa Dube wa Afrika Kusini nitakuwa tajiri.

    Nikajiwazia mipango ya maendeleo. Nilijiambia nitakaporudi Tanzania nitanunua gari la kifahari pamoja na kuanzisha miradi mikubwa ya biashara. Baada ya hapo nitatafuta mke nioe.

    Wakati nikiwaza hayo nilisikia mlango ukibishwa, nikainuka na kwenda kuufungua. Niliona wasichana wawili waliokuwa wamejipodoa huku nyuso zao ziking’ara kwa mkorogo.

    Walikuwa wamesimama kando ya mlango wakiwa wamevaa nguo fupi huku matiti yao yaliyokuwa yametuna kama mipira yakiwa nusu nje.

    “Naweza kuwasaidia? Nikawambia.

    Walinisalimia kwa heshima na kuanza kujitambulisha majina yao lakini sikujua mara moja kitu walichokuwa wanahitaji.

    Nikawambia kuwa nimefurahi kuwafahamu. Mmoja wapo akaniuliza jina langu. Nikamtajia.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walipoona uso wangu ulikuwa umeota alama ya kuuliza waliniambia.

    “Tulitaka kukuchangamsha tu mgeni wetu. Tunaona umekuwa kimya chumbani, huna mwenzako”

    Hapo ndipo nilipoelewa kuwa wale walikuwa changu doa waliokuwa wakijiuza kwenye mahoteli.

    Mawazo yangu yalikuwa tofauti na wao kwa upande mmoja na yalikuwa yanalingana na wao kwa upande mwingine.

    Yalikuwa tofauti na wao kwa upande mmoja kwa sababu kilichonipeleka Botswana hakikuwa kufuata machangudoa na yalilingana na wao kwa upande mwingine kwa sababu wao walikuwa wakitafuta pesa kwa njia zao na mimi vile vile nilikuwa natafuta pesa.

    Nilipowaza hivyo nilijikuta nikitabasamu.

    “Karibuni” nikawambia huku nikijiambia mwenyewe kuwa si vibaya kuzungumza nao mawili matatu kupitisha wakati.

    Wasichana hao wakaingia mle chumbani.



    Wote wawili walikimbilia kukaa kitandani wakaniwekea nafasi nikae katikati yao. Nikakaa.

    “Kwanini unataka kulala peke yako wakati sisi tupo?” Msichana mmoja aliyeonekana kuwa na macho ya juu aliniuliza.

    “Nimekuja peke yangu, nitalala peke yangu. Mlitaka nilale na nani?” nikamjibu.

    “Uchague mmojawapo kati yetu sisi” Msichana wa pili akaniambia.

    Kusema kweli hawakuwa malaya wa kuweza kunishawishi. Mkorogo ulikuwa umewaharibu. Lakini nilitaka kuzungumza nao tu nichangamshe akili yangu.

    “Je kama nitawachagua nyote itakuwaje?’ nikawauliza huku nikiwatazama kwa zamu.

    “Utatuweza?” Mmojawapo akaniuliza.

    “Nisiwaweze kwani nyie ni vyuma?”

    “Sawa. Utatupa dola ngapi?”

    “Tatizo litakuwa hapo kwenye dola”

    \

    “Utatupa dola ngapi?”

    “Sina hata dola moja”

    “Si kweli. Huoneshi kuwa huna pesa, usingekaa katika hoteli hii”

    “Kwani unatokea wapi?” Msichana mwingine akaniuliza.

    “Natokea Zimbabwe”

    “Wewe ni Mzimbabwe?”

    “Hapana. Mimi ni Mbongo”

    Wasichana hao wakaonesha kushituka.

    “Mbongo ni mtu wa nchi gani?”

    “Mtanzania”

    “Kumbe unatoka Tananzia?”

    “Unakufahamu?”

    “Sijafika lakini tumefundishwa shuleni kwamba Tanzani ilikuwa moja ya nchi zilizokuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa Afrika ikiwemo nchi yetu chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere”

    “Sasa kama mnajua hivyo kwanini mnanitoza dola?”

    “Ulitaka bure?”

    “Ikiwezekana”

    Wasichana hao walicheka kisha wakainuka na kusimama. Bila shaka waligundua kuwa nilikuwa nikiwapotezea wakati wao bure.

    “Mbona mnakwenda zenu?” nikawauliza.

    “Sisi tuko kazini bwana. Hamna bure hapa. Wewe hutaki kutoa pesa yako. Kwaheri” Msichana mmoja akanniambia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walitoka na kuniacha. Na mimi niliinuka nikafunga mlango wangu kisha nikarudi kitandani.

    Siku ile ikapita nikiwa hapo hoteli.

    Asubuhi ya siku iliyofuata nikiwa kwenye mkahawa wa hoteli hiyo nikipata kifungua kinywa, nilimuona dereva wa mwenyeji wangu Muhoza akinifuata. Uso wake ulikuwa umetaharuki.

    Akanisalimia kisha akaniambia.

    “Bwana Muhoza ameuawa!”

    Mshituko ulinifanya niinuke kwenye kiti na kusimama.

    “Bwana muhoza ameeuawa?” nikamuuliza kwa mshangao.

    “Jana alipoondoka hapa alikwenda katika hoteli nyingine ambako alilala na yule msichana aliyekuwa naye. Aliniambia nimfuate asubuhi. Asubuhi nilipomfuata nikakuta taarifa hiyo. Maiti yake ilikutwa chumbani hii asubuhi”

    Nikajiambia, ni yale yale yaliyotokea Botswana.

    “Kwani yule msichana aliyekuwa naye ni nani?” nikamuuliza yule dereva.

    Dereva huyo akabetua mabega yake.

    “Simfahamu na sijui walikutana wapi”

    “Yule ndiye aliyehusika na mauaji hayo!”

    “Inaaminika hivyo kwa sababu amekimbia”

    “Hebu kaa nikueleze kitu” nikamwambia Yule mtu huku na mimi nikikaa.

    “Unajua mimi natokea Botswana. Yule msichana nilimkuta katika hoteli niliyofikia pale Botswana. Baadaye nilimuona akiwa na mwenyeji wangu na wakachukua chumba pale pale hoteli. Asubuhi yake mwenyeji wangu akakutwa ameuawa katika chumba cha hoteli na yule msichana hakuonekana. Sasa nilipofika hapa Zimbabwe nilishangaa kumuona tena akiwa na Muhoza” nikamueleza yule mtu.

    “Kwanini hukutuambia tangu jana?”

    “Nilishindwa kuwambia, nilijua labda wanajuana”

    “Sasa yule msichana atakuwa ni nani na anatokea wapi?”

    Nikaguna na kushusha pumzi ndefu.

    “Hicho ni kitendawili na sidhani kama atapatikana”

    “Anaweza kupatikana”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nilikuwa namdai Muhoza pesa nyingi na tulikubaliana kwamba angenilipa hii asubuhi. Sasa sijui nitafanyaje?”

    “Huyu jamaa kama ulikuwa na mipango naye ya pesa ni bora usamehe. Kwanza mimi siwajui ndugu zake na isitoshe alishatengana na mke wake miaka mingi iliyopita”

    Nikatikisa kichwa change kusikitika.

    “Mkosi gani huu jamani…!” nilijisemea kimoyomoyo.



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog