Search This Blog

URITHI WA BABU - 2

 





    Simulizi : Urithi Wa Babu

    Sehemu Ya Pili (2)



    Yule dereva wa Muhoza alipoondoka pale hoteli sikumuona tena. Nikalala pale hoteli hadi siku iliyofuata ambapo nililazimika kujilipia mwenyewe chumba.

    Nikafanya mipango ya usafiri wa kwenda Afrika Kusini. Nikagundua kuwa ulikuwepo usafiri wa treni wa kutoka Zimbabwe hadi hadi Afrika Kusini.

    Nikasafiri kwa treni hadi Cape Town. Nilipofika kwenye kituo cha treni cha Cape town, nikampigia simu Domesan Dube kumjulisha kuwa nilikuwa nimewasili kwa treni kutokea Zimbabwe.

    Dube akaniambia kuwa anamtuma dereva wake anifuate. Baada ya kupita kama saa moja hivi, dereva huyo akawasili na gari. Alinipakia akanipeleka nyumbani kwa Dube.

    Wakati anasimamisha gari mbele ya jumba lake la kifahari nilimuona yule msichana muuaji akitoka katika jumba hilo. Alipungia mkono teksi iliyokuwa inapita barabarani. Teksi iliposimama akajipakia na kuondoka.

    Yule dereva hakushituka kumuona msichana huyo lakini mimi nilishituka sana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mimi nilishituka kwa sababu nilikuwa namfahamu na nilikuwa nafahamu visa alivyovitenda kule Botswana na Zimbabwe.

    Lakini pia nilishituka vile nilivyomkuta Afrika Kusini wakati jana yake tu aliuaa mtu Zimbabwe.

    Kitu kingine kilichonifanya nishituke ni kuona msichana huyo alikuwa akinifuatia kwa wale wadaiwa wangu ambapo kile nchi niliyokuwa ninakwenda nilikuwa namkuta akiwa na mtu niliyekuwa namfuata.

    Baada ya gari kusimama, dereva alishuka na mimi nikafungua mlango haraka na kushuka. Tayari uso wangu ulikuwa umeshatahariki baada ya kumuona yule msichana.

    Dereva alitangulia kuingia ndani ya jumba hilo akaniambia.

    “Karibu ndani”

    Nikaingia ndani. Tulitokea kwenye sebule pana iliyokuwa imepambwa vizuri.

    Mimi na yule dereva tulishituka tulipomuona mtu aliyekuwa amelala chini akiwa ametoa macho karibu na mlango.

    “Oh Bwana Dube!” Dereva alitoa sauti ya kimako kisha akachutama na kumtazama yule mtu.

    “Bwana Dube…Bwana Dube…!” akamuita huku akijaribu kumtikisa.

    Mtu huyo alikuwa kimya huku macho yake yakitazama dari bila kupepesa. Sikuwa daktari na sikuwa na uzoevu wa kutazama miili ya watu waliokufa lakini nilipotazama yale macho, niligundua mara moja kuwa mtu huyo alikuwa ameshakufa.

    “Huyo ndiye Bwana Dumesan Dube?” nikamuuliza yule dereva.

    “Ndiye yeye. Sijui amepatwa na nini!”

    “Kuna msichana alitoka humu ndani wakati tunafika, ni nani?”

    Dreva akatikisa kichwa.

    “Sikumfahamu. Ngoja nimuite daktari wake, labda ni presha”

    Dereva huyo aliyekuwa ametaharuki aliinuka akatoa simu yake na kutafuta namba ya daktari wa Dube kasha akampigia.

    “Bwana Dube ameaguka chini, sijui amepatwa na nini?” alisema baada ya simu kupokelewa.

    Niliisikia sauti ya upande wa pili ikiuliza.

    “Ameanguka wapi?”

    “Nyumbani kwake. Nilikuwa nimetoka kidogo niliporudi nilimkuta yuko chini lakini hasemi na inaonekana hana fahamu”

    “Subiri, ninakuja”

    Dereva akakata simu na kunitazama.

    “Daktari wake anakuja. Tumsubiri”

    “Kwani Bwana Dube ana tatizo la presha?” nikamuuliza.

    “Presha ni tatizo linaloweza kutokea ghafla tu, si lazima uwe nalo siku za nyuma”

    Huyo daktari alliyeitwa aliharakisha kufika. Baada ya dakika thelathini tu aliusukuma mlango na kuingia ndani.

    Alipomuona Dube akiwa chini hakuuliza chochote, alichutama na kuanza kumpima. Alianza kumpima presha kwa kutumia kipimo cha kufunga kwenye mkono.

    Alipomaliza aliinuka na kutuambia.

    “Nasikitika kuwambia kuwa Bwana Dube ameshakufa. Apelekwe hospitali kwa uthibitisho zaidi”

    “Ameshakufa!” Dereva wa Dube alimaka uso wake ukionesha kutoamini.

    “Apelekwe hospitali” Daktari akasisitiza.

    “Lakini ni jambo la kushangaza sana kwa sababu niliachana naye muda mchache tu uliopita”

    “Umeniambia kwamba alianguka?” Daktari akamuuliza.

    “Itakuwa alianguka kwani tulipokuja tulimkuta hapo chini”

    “Ana dalili kama ya kukabwa kwenye shingo yake”

    Dereva alizidi kupata taharuki.

    “Amekabwa? Amekabwa na nani? Humu ndani hakuna mtu. Au aliingia mtu na kumkaba?’

    “labda ni yule msichana tuliyemuona akitoka?” nikamwambia.

    “Msichana anaweza kumkaba?”

    “Anaweza”

    “Mimi naondoka. Nimewambia mumpeleke hospitali. Huko atafanyiwa uchunguzi na sababu ya kifo chake itajulikana” Daktari akatuambia na kutoka.

    Nikajiambia kwamba kwa vile suala hilo linahusu mauaji, ingebidi lifike polisi na likifika huko, mimi na dereva wa Dube tutakuwa ndio watuhumiwa wa kwanza.

    Kwa sababu ya kuogopa ushahidi, sikueleza chochote kuhusu yule msichana, nikamuacha yule dereva akishughulikia suala hilo. Mimi nikatafuta hoteli nikapanga chumba.

    Kwa kweli suala la yule msichana muuaji lilisumbua akili yangu. Nilishindwa kujua msichana huyo alitokea wapi na kwanini alikuwa akiwaua wale watu. Pia nilikuwa nikijiuliza alikuwa akiwaua kwa namna gani?

    Kile kitendo cha kumuona akitoka katika jumba la Dube kilitosha kunithibitishia kuwa ndiye aliyemuua Dube.

    Nilikuwa nina pesa chache ilizobaki ambazo zilitosha kukata tikiti ya kurudi Dar. Asubuhi kulipokucha nikaenda kukata tikiti na kuondoka. Safari yangu haikuwa na mafanikio yoyote. Zaidi ilikuwa ni kupata hasara tu na kupotea muda.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndege ilipaa hewani kwa takribani saa sita kabla ya kutua katika kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam.

    Ndege ilipotua, abiria walianza kushuka. Nilikuwa miongoni mwa abiria wa mwisho mwisho. Nilikuwa nimechoka na nilionesha wazi kukata tamaa.

    Wakati namalizia kushuka ngazi ya ndege, macho yangu yalimuona mtu aliyenishitua akiwa mbele yangu.

    Alikuwa ni yule msichana muuaji! Alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa wamepanda ile ndege wakitokea Afrika Kusini. Alikuwa amefuatana na mwanamme mmoja aliyekuwa amevaa suti nyeusi wakizungumza.

    Kusema kweli sikutambua kama yule msichana alikuwemo ndani ya ndege ile. Nilimgundua wakati ule wa kushuka. Yule mtu aliyekuwa amefuatana naye sikuweza kumtambua.

    Tulipotoka nje ya jengo la kiwanja cha ndege, msichana huyo pamoja na yule mtu aliyekuwa amefuatana naye walikodi teksi na kuondoka. Na mimi nikakodi teksi na kumwambia dereva awafuate.



    “Una maana niifuate hii teksi ya mbele yangu?” Dereva wa teksi akaniuliza.

    “Ndiyo ifuate hiyo hiyo”

    “Inaelekea wapi?”

    “Popote itakapoelekea”

    “Ina maana wewe hujui inaeleka wapi?”

    “Kwani tatizo lako ni nini, hapo tutakapofika utanitoza kiasi utakachotaka”

    “Sawa. Nilitaka tupatane tu”

    “Hatuwezi kupatana kwa sababu sijui wanakwenda wapi”

    “ Nimekuelewa”

    Dereva wa teksi akaanza kuiandama teksi iliyokuwa mbele yetu. Wakati mwingine gari lilitinga katikati yetu lakini dereva alijitahidi kuhakikisha teksi hiyo haitupotei.

    Wakati tunaendelea kuiandama teksi hiyo, mawazo yangu yalikuwa kwa yule msichana. Bado nilikuwa nikijiuliza msichana yule ni nani na kwanini nakutana naye katika kila nchi ninayokwenda. Pia nilijiuliza yule mtu aliyenaye ni nani na anatoka wapi.

    Nilihisi kwamba kwa vile msichana huyo alikuwa katika jiji ambalo nilikuwa nikilijua vyema, ningeweza kufanya uchunguzi na kumgundua.

    Hata hivyo jambo moja nilikuwa na uhakika nalo moyoni mwangu kwamba msichana huyo alikuwa wa hatari na muuaji aliyeonekana kuwa na uzoevu wa kuua.

    Mara moja niligundua kuwa teksi iliyowapakia ilikuwa ikielekea Mbezi. Tuliendelea kuifuata hadi iliposimama mbele ya jumba moja la kifahari. Dreva wa teksi niliyopanda alitaka kusimama nikamwambia apitilize moja kwa moja.

    “Sitaki wagundue kuwa ninawafuata” nikamwambia dereva huyo na kuongeza.

    “Utasimama kule mbele”

    “Nimekuelewa”

    Wakati teksi ikiendelea kwenda, mimi nilikuwa nikitazama nyuma kwenye kioo. Nilimuona yule msichana akishuka kwenye ile teksi pamoja na yule mwanaume aliyekuwa naye. Teksi iliondoka na wao wakafungua geti na kuingia ndani.

    Kwa vile nilikuwa nimeshaikariri ile nyumba, nilimwambia dereva wa teksi ageuze anipeleke nyumbani kwangu.

    “Umeshawaona?” akaniulia wakati akiigeuza teksi.

    “Nimewaona. Nilitaka kujua wanaishi wapi?”

    “Kwani ni kina nani wale?”

    “Nilisafiri nao kutoka Afrika Kusini. Nilitaka kujua wanaishi wapi hapa dar”

    Dereva alitaka kuendelea kuniuliza

    lakini alibadili mawazo akanyamaza kimya.

    Baada ya nusu saa tu alinifikisha katika mtaa ninaoishi. Aliisimamisha teksi mbele ya nyumba yangu nikamuuliza gharama yake ni kiasi gani.

    Alinitajia kiasi alichotaka nikatoa pochi yangu na kumpa kiasi hicho bila kusita.

    “Asante sana” nilimwambia huku nikifungua mlango wa teksi na kushuka.

    Huku nikiwa na begi langu nilikwenda kufungua mlango wa nyumba yangu nikaingia ndani. Niliondoka kwenda nje ya nchi kwa matumaini ya utajiri lakini nimerudi kama masikini. Safari yangu haikuwa na mafanikio yoyote, nilijiambia kwa huzuni.

    Mbali ya kutokuwa na mafanikio, ilikuwa safari ya balaa na iliyonitia hofu kutokana na wale watu niliowafuata kuuawa mmoja baada ya mwingine, tena wameuawa na msichana huyo huyo ambaye aliwafuata Botswana, Zimbabwe na Afrika Kusini.

    Msichana yule sasa amekuwa ni kitendawili ambacho nilihitaji kukitegeua kadiri itakavyowezekana. Kwa vile nilikuwa nimeikariri sura yake pamoja na nyumba aliyoingia, niliamini kwamba ningewea kumfuatilia na kumjua vizuri.

    Siku ile ikapita. Asubuhi ya siku iliyofuata wakati nimeketi sebuleni nikitazama televisheni, niliona kitu kilichonishitua.

    Kilikuwa ni kipinidi cha taarifa ya habari. Habari ya kwanza kutangazwa na kuoneshwa ilikuwa ya mauaji ya mkazi mmoja wa Mbezi aliyetajwa kwa jina la Abdul Baraka.

    Hilo jina lilinishitua kwa sababu lilikuwa katika orodha ya wale wadaiwa wa marehemu babu yangu. Jina hilo lilikuwa la kwanza na mtu huyo ndiye niliyeanza kumpigia simu lakini simu yake haikupatikana nikaamua nimuache kiporo.

    Yeye hasa ndiye aliyekuwa tegemeo langu baada ya wale watu niliowafuata nje ya nchi kuuawa na kusababisha nisipate kitu.

    Taarifa hiyo ya televisheni ilieleza kwamba mwili wa Abdul Baraka ulikutwa mchana wa jana yake nyumbani kwake ukiwa umelazwa sebuleni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Uchunuzi wa madaktari wa hospitali ya Muhimbili ulionesha kuwa marehemu aliuawa kwa kukabwa koo na kukosehwa pumzi kwa zaidi ya dakika tano jambo lililosababisha moyo wake kusimama na hivyo kusababisha kifo chake.

    Sasa mshituko mkubwa niliupata wakati picha ya Abdul Baraka ilipooneshwa. Alikuwa ni yule mtu niliyemuona amefuatana na yule msichana muuaji jana yake.

    Hapo hapo nikajua kwamba aliuawa na yule msichana ambaye alitoweka baada ya kufanya mauaji hayo.

    Nikajiuliza ni kwanini hawa watu wanaodaiwa na marehemu babu yangu wanauawa na anayewaua ni mtu mmoja tena msichana, amezunguka nchi zote kuwafuata?

    Jambo jingine la ajabu nililoliona ni kuwa mauaji hayo yanafanyika wakati ule ninafuatilia madeni hayo. Kulikoni!

    Nilitamani kwenda polisi kueleza nilichokuwa ninakifahamu kuhusu yule msichana lakini niliogopa kwa sababu sikuwa nikijua yule msichana alikuwa nani. Angeweza kuwa gaidi au ni mtu aliyetumwa kufanya mauaji.

    Nikajiambia kama nitajitia kimbele mbele cha kumripoti polisi ningeweza kuuawa. Nikaamua kuwa kimya.

    Wiki moja ikapita. Siku hiyo nilikuwa nimekaa nyumbani kwangu nikiwaza, simu yangu ikaita.



    Namba iliyokuwa ikinipigia ilikuwa ngeni kwangu. Nikaipokea ile simu.

    “Hello!”

    “Hello, nazungumza na Kassim Fumbwe?’ Sauti ya mwanamke ikaniuliza.

    “Ndiyo. Kassim Fumbwe. Nani mwenzangu”

    “Naitwa Ummy. Nilikuwa na mazungumzo na wewe. Nilihitaji tukutane”

    Moyo wangu ulishituka kidogo.

    “Tukutane wapi?”

    Mimi niko Suzy Hotel hapa Masaki. Niko chumaba namba 35. Ukifika utanikuta”

    Nikasita kidogo kabla ya kumuuliza.

    “Unanifahamu vipi?”

    “Ninakufahamu. Kama unataka kujua zaidi nitakufahamisha utakapofika”

    “Hayo mazungumzo yanahusu nini?”

    “Yanahusu mali za marehemu babu yako”

    Aliponiambia hivyo sikutaka kuendelea kumhoji, nikamwambia.

    “Nisubiri ninakuja sasa hivi”

    Simu ya upande wa pili ikakatwa. Nilikuwa nimeketi sebuleni nikainuka na kutoka. Gari langu ambao nililirithi kwa babu nilikuwa nimeliegesha nje. Nikajiapakia na kuliwasha.

    Gari lilipowaka nilitia gea na kuelekea Masaki huku nikijiuliza huyo mwanamke aliyenipigia simu alikuwa nani na alitaka kunieleza nini kuhusu mali za marehemu babu yangu.

    Kilichonifanya nikurupuke na kumfuata haraka haraka ni ule utata wa mali za marehemu babu. Babu alikuwa tajiri lakini baada ya kufa alionekana hakuwa na mali yoyote.

    Nilitarajia kuwa mwanamke huyo alikuwa akijua siri ya mali za marehemu babu na angenifichulia.

    Nilipofika Suzy Hotel iliyokuwa Masaki niliegesha gari katika eneo la kuegeshea kisha nikatoa simu na kumpgia yule mwanamke.

    “Nimeshafika?” nikamwambia.

    “Uko wapi?” Sauti ya mwanamke ikauliza kwenye simu.

    “Niko hapa mbele ya hoteli”

    “Njoo chumba namba 35 kipo ghorofa ya kwanza”

    “Sawa”

    Nikashuka kwenye gari na kuingia hotelini humo. Nilipanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza, nikakitafuta chumba namba 35. Nilipokiona nikakifuata na kubisha mlango.

    Baada ya sekunde chache tu mlango

    ulifunguliwa na msichana.

    “Karibu ndani” akaniambia huku akitabasamu.

    Nilipomtazama vizuri, sura yake ikanijia akilini mmwangu.

    Alikuwa ni yule msichana muuaji niliyekutana naye Botswana, Zimbabwe na kisha Afrika Kusini.

    Nilipogundua kuwa alikuwa ni yeye nilishituka nikarudi nyuma hatua moja

    kisha nikageuka na kutoka mbio.

    “Mbona unakimbia?” Niliisikia sauti yake ikiniuliza kwa nyuma.

    Sikujibu wala sikusimama. Nilishuka ngazi mbili mbili nikafika chini. Pale chini niliona nikikimbia nitawatia watu wasiwasi nikatembea taratibu na kutoka

    nje ya hoteli. Nikajipakia kwenye gari langu na kuliondoa kwa kasi.

    Bila shaka yule mwanamke alitaka kunimaliza na mimi, nilijiambia kimoyomoyo huku nikizidi kukanyaga mafuta.

    Nilishindwa kujua aliipataje namba yangu na alijuaje kuwa ninaitwa Kassim Fumbwe kwani aliponipigia simu aliniuliza kama mimi ni Kassim Fumbwe.

    Aliponipigia simu sikutarajia kama alikuwa ni yeye. Si kwa sababu ya kunitambua kuwa mimi ni Kassim Fumbwe bali vile alivyoniambia kuwa ana mazungumzo na mimi kuhusu mali ya babu yangu.

    Nikahisi kwamba likuwa akijua mengi kuhusu mimi hasa vile ambavyo alihusika katika safari yangu nzima kutoka Botswana, Zimbabwe, Afrika Kusini hadi kurudi tena Tanzania.

    Sasa nikapata wazo moja kwamba ni kweli alikuwa akiifahamu siri ya mali ya marehemu babu yangu kwa sababu yeye ndiye aliyeifanya safari yangu isiwe na mafanikio. Yeye ndiye aliyewaua watu wote waliokuwa wakidaiwa na babu yangu. Sababu za kuwaua alikuwa akizijua mwenyewe.

    Nikaendelea kujiambia, kwangu mimi msichana huyo atabaki kuwa adui. Ingawa sikuweza kujua ni kwanini aliwaua wale watu lakini nilijenga hofu kwamba alitaka kuniua na mimi.

    Hii ndio sababu nilimkimbia pale hoteli.

    Nilipofika nyumbani nilikaa sebuleni na kuendelea kujiwazia kuhusu yule mwanamke. Ghafla simu yangu ikaita. Nilipotazama namba nikaona ni ile ya yule msichana. Nikaipokea.



    “Mbona umekimbia?” Sauti ya msichana ikaniuliza.

    “Hebu niambie ukweli wewe ni nani?” nikamuuliza.

    “Kama ulikuwa hunijui kwanini umenikimbia?”

    “Nimekukimbia kwa sababu”

    “Sababu gani?”

    “Wewe si nilikukuta Botswana siku chache ziliopita halafu nikakuona tena Zimbabwe na jana ulikuwa Afrika Kusini?”

    “Kumbe umenikariri vizuri”

    “Nimekukariri kwa sababu nimeona kila nchi niliyokwenda nilikuwa nakuona”

    “Ndiyo sababu nilitaka kukutana na wewe”

    “Kwani wewe ni nani? Unamjuaje marehemu babu yangu na umenijuaje mimi?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa hayo ndiyo mambo ambayo tutazungumza tutakapokutana ”

    Nikatikisa kichwa changu ingawa niliyekuwa nikizungumza naye hakuwa karibu yangu.

    “Hilo la kukutana na wewe litakuwa gumu kidogo”

    “Hutaki kujua zilipo mali za marehemu babu yako”

    “Ninataka sana lakini kuna mambo

    ambayo yamenishitua”

    “Niambie ni mambo gani?”

    “Kuna watu ambao ulikuwa karibu nao.

    Hao watu waliuawa katika mazingira ya kutatanisha” nikamwambia.

    “Wapi huko?”

    “Botswana, Zimbambwe na Afrika Kusini”

    “Umetaja lakini bado mmoja”

    “Abdul Baraka wa Mbezi hapa Dar aliuawa pia”

    “Waliuawa na nani?”

    “Nilikuona wewe na Abdul Baraka mkishuka kwenye ndege kutoka Afrika

    Kusini”

    “Swali nililokuuliza, wameuawa na nani?”

    Hapo niligwaya kujibu. Niliona kama

    nitamwambia aliwaua yeye anaweza kukasirika na akajua kuwa nina ushahidi kuwa yeye nndiye muuaji. Akipata uhakika huo nilihofia kuwa anaweza kunisaka kwa udi na uvumba ili aniue.

    Nikamuuliza. “Uliponiambia bado mmoja ulikuwa na maana gani?”

    “Nilikuwa nina maana unayoijua wewe”

    “Mimi sijui kitu”

    “Haiwezekani kuwa hujui kitu. Usingeniambia kuwa kuna watu walikuwa karibu na mimi na wameuawa. Ulikuwa na maana gani?”

    “Usinielewe vibaya. Nilimaanisha hao watu walikuwa na wewe kabla ya kuuawa”

    “Hao watu wanakuhusu?”

    “Walikuwa wakidaiwa na marehemu babu yangu”

    “Tunarudi pale pale katika mali ya marehemu babu yako. Bado hutaki kujua kile kilicho nyuma ya pazia”

    “Ninataka”

    “Sasa naomba kukutana na wewe kwa mara nyingine”

    Nikafikiri kidogo kisha nikamwambia.

    “Kwanini tusizungumze kwenye simu?”

    “Hatuwezi kuzungumza kwenye simu kila

    kitu. Kuna maongezi mengine ni lazima tukutane mimi na wewe”

    “Ungejitambulisha kwanza ili niweze kukujua vizuri, wewe ni nani na

    unamjuaje babu yangu?”

    “Sasa ili unijue vizuri mimi, nitakuelekeza mahali ambapo utapata habari zangu kikamilifu na tutaweza kuonana mimi na wewe”

    “Nielekeze ni mahli gani??”

    Msichana akanielekeza mtaa mmoja ulioko eneo la Mwananyamala. Pia akanitajia namba ya nyumba.

    “Ukifika uliza Sharif Nasri” akaniambia.

    “Huyo Sharif Nasri ni nani?”

    “Ni baba yangu”

    “Umeniambia wewe unaitwa nani?”

    “Naitwa Ummy Sharif Nasri”

    “Wewe ni sharifu?”

    “Hilo ni jina tu”

    “Kwa hiyo kama nitampata huyo mzee nimuulize kuhusu wewe?”

    “Ndiyo muulize na mimi utanipata hapo hapo”

    “Sawa. Nitafanya hivyo”

    “Basi nakutakia mchana mwema”

    Msichana akakata simu.

    Aliniacha na mawazo yaliyochanganyika na fadhaa. Nilijiuliza maswali mengi sana yaliyokosa majibu.

    Imani niliyokuwa nayo ni kuwa huyu

    msichana ndiye aliyewaua wale watu niliowafuata kule Botswana, Zimbbabwe na Afrika Kusini. Na ndiye pia aliyemuua Baraka Abdul aliyeuawa nyumbani kwake Mbezi.

    Kama kweli ndiye aliyewaua, ilikuwa ni lazima niwe na hofu naye na ni lazima nishuku kuwa pengine alitaka kuniua na

    mimi ingawa sababu za kufanya mauaji hayo nilikuwa sizijui.

    Sasa kwa kunielekeza kwa mtu mwingine ambaye aliniambia ni baba yake, alizidi kunichanganya. Nilijiuliza huyo mtu atanieleza nini kuhusu msichana huyu aliyeonesha kila dalili ya kupata mafunzo ya uuaji.

    Nikaendelea kujiuliza, huyo mzee anajua nini kuhusu watu hao waliouawa na mwanawe na anajua sababu za mauaji hayo?

    Au mzee huyo anamjua babu yangu au ananijua mimi?



    Vile vile nilitaka kujua jinsi yule msichana anavyohusika na mali za babu yangu. Amejuaje kama mali za babu yangu zimepotea?

    Au ana maelezo gani ambayo anataka kunipa kuhusu mali hizo na ameyapata wapi?

    Suala la mali lilinipa shauku lakini suala la mauaji lilinitia hofu. Ilibidi nigwaye na nifikiri vya kutosha kabla ya kuamua kwenda huko Mwananyamala.

    Baada ya kuwaza kwa muda mrefu nilitoka pale nyumbani, nikaenda

    kwenye mkahawa uliokuwa jirani. Niliagiza chakula nikala huku nikiwaza.

    Nilipomaliza kula niliitoka. Siku ile kulikuwa na mechi kati ya Simba na Yanga. Nikaenda uwanja wa taifa. Nilikuwa mpenzi wa mpira wa miguu na shabiki wa moja ya timu hizo.

    Niliangalia mpira hadi saa kumi na mbili jioni. Sikupata furaha kwa vile timu zilitoka sare bila kufungana. Nikarudi nyumbani.

    Mpaka muda huo nilikuwa nimepuuza kwenda Mwananyamala kumuulizia

    Sharif Nasri.

    Asubuhi ya siku ya pili yake yule msichana akanipigia simu.

    “Mbona hukwenda kule nilikokuelekeza?” akaniuliza.

    “Nitakwenda leo”

    “Ni muhimu. Tafadhali usipuuze”



    Baada ya kunywa chai niliona niende huko Mwananyamala alikonielekeza huyo msichana ili nikapate taarifa zake. Nilitarajia si tu ningeweza kugundua

    msichana huyo alikuwa nani pia ningeweza kujua sababu ya kuwaua wale watu.

    Hata hivyo wakati nikienda huko Mwananyamala nilikuwa nikijua fika kwamba yule msichana alikuwa mtu wa hatari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini kubwa zaidi lililonisukuma niende, ni vile alivyoniambia kuwa alikuwa na

    tarifa ya malli za babu yangu ambazo mpaka muda ule zilikuwa ni kitendawili nilichoshindwa kukitegua.

    Kadhalika mauaji yale ya watu wanne ambao walikuwa wakidaiwa na babu yangu yalizidi kunipa shauku ya kutaka kumjua vyema msichana huyo ambaye mpaka muda ule nilikuwa nikiamini kwamba ndiye aliyewaua.

    Nilipofika Mwananyamala niliutafuta mtaa niioelekezwa hadi nikaupata.

    Nikaitafuta nyumba yenye namba aliyonitajia yule msichana. Nilipoiona nilijisikia kuanza kupata hofu nikajiambia kuwa nami leo naenda kufa.

    Sikujua ni kwanini nilipata hofu. Lakini nilihisi nilipata hofu kwa sababu nilipagundua mahali ambapo ningepata taarifa za yule msichana ambazo zilikuwa zikiumiza kichwa changu.

    Mbele ya ile nyumba nilikuta mzee aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha uvivu akivuta mtemba.

    Alikuwa mzee mrefu na mwembamba aliyekuwa na ndevu nyingi nyeupe. Alikuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeupe. Kichwani alikuwa amevaa kofia ya darize.

    Jinsi nilivyomsoma kutokana na mavazi yake na sura yake, alikuwa mswahili wa pwani aliyekuwa amechanganya na ushirazi. Umri wa mzee huyo haukuwa chini ya miaka sabini na mitano ingawa bado alionekana kuwa na nguvu za kutosha.

    Nilisimamisha gari karibu na baraza ya nyumba hiyo nikaizima moto na kutoa gea zote na kuvuta hand break na kushuka.

    Vile nilivyomuuona mswahili nikamtolea salaam.

    “Asalaam alaykum”

    “Waalayka salaam” aliniitikia. Ingawa alikuwa mwembamba, sauti yake ilikuwa nzito inayokwaruza.

    “Habari za hapa?” niliendelea kumsalimia nikiwa nimesimama mbele yake.

    “Nzuri. Karibu” akanikaribisha huku akinitazama kwa macho ya udadisi.

    Macho yake yalikuwa madogo yaliyokuwa na kope nyeupe.

    “Samahani mzee wangu, kulikuwa na mtu ninamuulizia. Aliniambia ninaweza kumpata hapa”

    “Ni nani?”

    “Anaitwa Ummy Sharif Nasri”

    Mzee nilipomtajia jina hilo alishituka akautoa mtemba wake midomoni kisha akaniuliza tena huku akiwa amenikazia macho.

    “Unasema nani?”

    “Ummy Sharif Nasri”

    Mzee aliendelea kunikazia macho.

    “Wewe unatokea wapi?”

    “Natokea hapa hapa Dar”

    “Unamfahamuje Ummy?”

    “Sikuwa nikimfahamu tangu zamani ila

    jana nilipigiwa simu na msichana aliyejitambulisha kwa jina hilo akaniambia nikutane naye kwa sababu ana taarifa za mali za marehemu babu yangu”

    “Alikwambia anaitwa Ummy Sharifu Nasri?”

    “Ndiyo”

    “Alikuelekeza uje kwenye nnyumba hii?”

    “Ndiyo”

    “Uliwahi kumuona yeye mwenyewe?”

    “Nilimuona jana”

    “Una hakika kwamba ulimuona Ummy?”

    “Ndiyo nnilimuonna”

    “Nikikuonesha picha yake unaweza kumtambua”

    “Ndiyo nitamtambua”

    “Hebu subiri”

    Mzee alionesha wazi nilimchanganya akili. Aliinuka kwennye kiti akaingia

    ndani.

    Sikujua ni kwanini alitaharuki. Baada ya muda kidogo alitoka akiwa ameshika kitabu cha picha.

    “Hebu sogea hapa karibu” akanniambia huku akifungua karasa za kile kitabu.

    “Hebu angalia hii picha. Msichana uliyemuona ndiye huyo?”

    Mzee alinionesha picha moja ya ukubwa wa bahasha ya barua. Ilikuwa ikumuonesha yule msichana akitabasamu.

    “Ndiye huyu?” Mzee akaniuliza.

    “Ndiye yeye”

    “Mtazame vizuri”

    “Nimemtazama vizuri, ndiye yeye Ummy Sharif Nasri”

    “Unaponiambia hivyo unanichanganya…!”





    Kama vile magoti yalimnyong’onyea, mzee alirudi ghafla kwenye kiti chake.

    “Kwanini ninakuchanganya mzee wangu?” nikamuuliza kwa sauti tulivu nikiwa sijui nililokuwa ndani ya moyo wa mzee huyo..

    “Mimi ndiye Sharif Nasri. Huyu ni binti

    yangu na alishakufa miaka mitano iliyopita!”

    Kauli ya yule mzee ikanishitua na mimi.

    “Umesema alishakufa miaka mitano iliyopita?” nikamuuliza.

    “Ndiyo alishakufa. Hivi sasa ni marehemu. Uliponiambia ni huyu umenichanganya sana”

    “Kama alishakufa miaka mitano iliyopita, mbona nimemuona na ameniambia nije kumuulizia hapa?”

    Nikaona mama mmoja na binti mmoja aliyekuwa amefanana na Ummy, wakitoka pale barazani. Pengine ni baada ya kusikia yale maneno.

    “Kuna nini?” Yule mama akauliza.



    “Huyu kijana amekuja na habari za kushangaza kidogo” Yule mzee alianza kumueleza.

    “Kwani yeye ni nani?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sikiliza nikueleze. Yeye amekuja kumuulizia Ummy”

    Yule mama akanitazama kisha akaurudisha uso wake kwa yule mzee.

    “Yeye hajui kama Ummy hivi sasa ni marehemu? Amekuja kutukumbushia msiba tuliokwishausahau”

    “Anasema alikutana naye na alimuagiza aje hapa nyumbani!”

    “Alikutana naye lini?” Yule mama aliuliza kwa mshituko.

    “Eti mlikutana llini??” Yule mzee akaniuliza.

    “Nilikkutana naye jana na leo niliongea naye asubuhi kwa simu” nikamjibu.

    Mama akatikisa kichwa.

    “Huyo siye Ummy. Ummy alikwishakufa mmika mitano iliyopita” Mama alisema.

    “Nimemuonesha hii picha ya marehemu. Ameniambia Ummy aliyekutana naye ndiye huyo”

    “Haiwezekani. Huyo aliyekutana naye si Ummy”

    Yule msichana aliyetokana yule mama akanitazama.

    “Umesema uliongea naye kwenye simu leo?” akaniuliza.

    “Ndiyo niliongea naye”

    “Ulimpigia au alikupigia?”

    “Alinipigia yeye”

    “Hebu tuoneshe namba yake”

    Nikatoa simu yangu na kuitafuta namba aliyonipigia yule msichana, nikamuonesha.

    Msichana aliisoma ile namba kisha akagutuka.

    “Mama hii ndiyo iliyokuwa namba ya marehemu dada!” akasema kwa sauti ya

    kutaharuki.

    “Kwani unaikumbuka vizuri?”Yule mama akamuuliza.

    “Naikumbuka” Msichana alisema na kurudia kuitaja ile namba kwa kuikariri

    kisha akaongeza.

    “Ni namba ya marehemu kweli”

    Nyuso za watu wote watatu zikawa zimebadilika. Nilijuta kufika pale nyumbani na kukuta niliyoyakuta.

    “Hebu tueleze vizuri unajuana naye vipi huyu Ummy?” Yule mama akaniuliza.

    Ikanibidi nieleze ukweli wote tangu babu yangu alipofariki mpaka nikaenda

    katiika nchi nilizokwenda kufuatilia madeni ya babu. Nikaeleza jinsi msichana huyo alivyowaua watu niliowafuata katika kila nchi niliyokwenda. Na mtu wa mwisho aalimuua Dar es Salaam mara tu niliporudi kutoka Afrika Kusini.

    Niliwaeleza kwamba niliporudi nilimuona

    huyo msichana akishuka kwenye ndege akiwa amefuatana na mtu mmoja.

    “Niliwafuatilia hadi Mbezi ambako niliona wakiingia katika nyumba moja. Siku ya piili yake nikaona kwenye vyomba vya

    habari yule mtu ameuawa na alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa wanadaiwa na

    babu yangu”

    Mama alitoa mguno mzito akamtazama yule binti kisha akamtazama yule mzee ambaye nilikwisahisi kuwa alikuwa mume wake.

    “Huyu kijana amekuja na habari kubwa” akawambia kisha akanitazama na kuniuliza.

    “Sasa mlikutana wapi na huyu msichana mkiwa hapa Dar”

    “Tulikutana jana. Sijui alipataje namba yangu akanipigia simu…”

    “Wewe ulijuaje kuwa ni yeye aliyekupigia simu?”

    “Sikujua kama alikuwa yeye. Aliniambia nimfuate katika hoteli moja pale Masaki, akaniambia alikuwa na taarifa kuhusu mali za babu yangu. Nikafika

    hapo hoteli. Nikaingia katiika chumba alichoniambia ananisubiri.

    “Nilipoingia humo chumbani nikamuona yeye. Kwa vile nilivyojua kuwa ndiye aliyeua wale watu, nilidhani alitaka

    kuniua na mimi nikatoka mbio bila kumsikiliza. Niliporudi nyumbani alinipigia simu akaniuliza kwanini nilimkimbia”

    Niliendelea kuwaeleza jinsi nilivyojibizanana na msichana huyo hadi akanitajia jina lake na ubinti wake na akanitaka nifike nyumbani kwao Mwananyamala ili nionane naye.

    “Namba ya nyumba hii alikutajia

    yeye?”

    “Ndiyo alinitajia yeye. Jana sikufika. Leo asubuhi akanipigia simu na kunisisitiza kuwa nifike kumuulizia. Ndio nikafika

    na kukutana na huyu mzee hapa”

    Palipita kimya cha karibu robo dakika. Wenyeji wangu hao walikuwa wameduwaa wakinitazama. Sikuweza kujua walikuwa wananiwazia nini.

    Nikahisi kijasho chembamba kikinitiririka kwenye mfereji wa uti wa mgongo wangu.

    Nilikuwa nikijiuliza kama ule ulioua watu Botswana, Zimbabwe na Afrika Kusini uulikuwa ni mzuka wa Ummy na kwamba nilikutana na kuzungumza na mzuka?

    Maswali hayo yalikuwa yakipita akilini mwangu kimya kimya huku nikikabiliwa na kazi ya kukwepa macho ya wale wazee waliokuwa wakinitazama.

    Ni vyema niseme ukweli kwamba wakati ule tunazungumza, miguu yangu ilikuwa inatetemeka kwa hofu.



    “Sasa mwanangu, huyu msichana uliyekuja kutueleza kwamba ulikutana naye na kuzungumza naye alishakufa na mdogo wake amethibitisha kwamba namba ya simu uliyopigiwa ni ya marehemu kweli, je mpaka sasa una wazo gani?” Yule mama akaniuliza lakini swali lake lilikuwa ni gumu kulijibu.

    “Sijui nikujibu nini mama yangu. Hiyo taarifa kwamba huyu msichna alikufa

    miaka mitano iliyopita imenichanganya akili yangu” nikamjibu.

    “Kwani alipokupigia simu alikueleza alikuwa na uhusiano gani na babu yako?” Yule mzee naye akaniuliza.

    “Hakuniambia kama alikuwa na

    uuhusiano wowote na babu yangu isipokuwa aliniambia alitaka anipe taarifa za mali ya babu yangu”

    “Na mimi nina wazo langu” Yule msichana naye akasema na kuongeza.

    “Hebu mpigie simu hapa hapa tumsikie”

    “Hilo ni wazo zuri” nikasema na kuitazama simu yangu ambayo nilikuwa nayo mkononi.

    Nikampigia Ummy Sharif Nasri.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Simu ilikuwa inaita lakini ilikuwa haipokelewi.

    “Simu inaita lakini haipokelewi” nikawambia.

    Niliiondoa simu sikioni mwangu na kuielekeza kwa yule msichana.

    “Sikiliza simu inaita” nikamwambia.

    Msichana aliishika ile simu akaiweka kwenye sikio lake na kusikiliza.

    “Ndiyo simu inaita kweli” akasema.

    Aliendelea kuiweka sikioni kwake hadi simu ikakata yenyewe. Akaiondoa sikioni

    na kunipa.

    “Simu inaita lakini hapokei” akasema tena.

    “Una maana kwamba Ummy yuko hai?” Mama yake akamuuuliza.

    Msichana akabetua mabega.

    “Tunachojua sisi ni kuwa amekufa, sasa hii habari kuwa dada yuko hai hatuijui. Kama angekuwa hai si angekuja

    nyumbani”

    “Ni miujiza hii!” Mzee akasema huku uso wake ukiwa umefadhaika.

    “Hebu piga tena” Yule mama akaniambia.

    Nikapiga tena ile namba.

    Safari hii simu haikupatikana.

    “Inaita” Mama akaniuliza.

    “Simu haipatikani tena” nikawambia.

    “Mara moja hii!” Mama akashangaa.

    “Inawezekana ameizima” nikawambia.

    “Huyo Ummy ndiyo ameizima?”

    “Ndiyo yeye. Mnaponiambia kuwa amekufa niinashangaa kwa sababu nimemuona na nimezungumza naye”

    “Huyu huyu ambaye umemuona kwenye picha?”

    “Ndiye huyo huyo”

    “Sasa ili uamini kuwa amekufa twende nikakuoneshe kaburi lake. Makaburi hayako mbali” Mzee akaniambia.

    Mzee huyo alinichukua hadi katika eneo la makaburi ambalo halikuwa mbali sana. Akanionesha kaburi la Ummy Nasri. Lilikuwa na kibao kilichoandikwa jina lake, tarehe aliyokufa na aliyozikwa.

    “Kaburi lake ni hili hapa”

    Sikuwa hata na la kusema. Nilibaki kushangaa tu.

    Mzee aliendelea kuniambia.

    “Marehemu amelala ndani”

    “Sasa mzee huyu atakuwa nani?” nikamuuliza.

    “Sisi hatumjui. Sisi tunachojua ni kuwa binti yetu alishakufa na aliyekufa hafufuki”

    “Lakini mzee fikiria kwamba alinielekeza yeye mwenyewe kuwa nije pale nyumbani nimuulizie”

    “Mtu yeyote hawezi kukubaliana na maelezo yako” Mzee akaniambia huku akiondoka.

    “Nimekuja kukuonesha hili kaburi ili uthibitishe kuwa Ummy alikwishakufa” akaongeza.

    “Na mimi nathibitisha kuwa nilimuona”

    “Basi itakuwa ni miujiza mikubwa”

    Tukarudi pale nyumbani.

    “Ni vizuri kama utakutana naye tena uje naye hapa mguu kwa mguu” Mzee akaniambia wakati akiketi kwenye kiti chake cha uvivu.

    Wakati narudi na gari langu nilianza kuzikumbuka zile safari za kimiujiza za yule msichana amabaye kwanza nilimkuta Botswana. Halafu nikaenda kumuona Zimbabwe. Nilipokwenda Afrika Kusini nikakutana naye tena. Bado wakati narudi Tanzania nikashuka naye kwenye ndege moja ingawa wakati wa kupanda ndege sikumuona.

    Na huko kote alikuwa akiwaua watu niliokuwa nimewafuata. Mtu wa mwisho alikuwa mkazi wa hapa hapa Dar ambaye alishuka naye kwenye ndege.

    Watu wote aliowaua walikuwa wakidaiwa na marehemu babu yangu na mauaji yalifanyika wakati ule nafanya ziara yakufuatilia madeni.

    Mwisho wa siku msichana huyo alinipigia simu na kuniambia kuwa ana mazungumzo na mimi kuhusu mali za babu yangu.

    Aliniona Botswana. Aliniona Zimbabwe. Aliniona Afrika Kusini lakini hakuniambia kuwa ana mazungumzo na mimi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika nyumba aliyonielekeza niende nimeambiwa kwamba msichana huyo wanamfahamu lakini alikwisha kufa miaka mitano iliyopita.

    Sasa napata picha kwamba msichana huyu hakuwa wa kawaida. Zile safari alizozifanya kule Botswana, Zimbabwe na Afrika Kusini pia hazikuwa za kawaida. Niliona kama alikuwa akiibuka tu katika zile nchi nilizomkuta. Hakuwa akisafiri. Hakukuwa na hadi leo hakuna usafiri wa haraka kiasi kile.

    Pia yale mauaji aliyokuwa akiyafanya hayakuwa ya kawaida. Kwa mwanamke kuwaua wanaume kirahisi rahisi namna ile haikuwa kawaida.

    Baada ya kuwaza hayo nikajiuliza, yule msichana alikuwa shetani au mzuka wa Ummy niliyeelezwa kuwa alikwishakufa?



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog