Search This Blog

URITHI WA BABU - 3

 





    Simulizi : Urithi Wa Babu

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Nikajiambia kama hatakuwa shetani atakuwa ni mzuka. Lakini sikuelewa ni kwanini mzuka huo uliwaua wale watu na kwanini uliniambia kuwa unajua siri za mali za babu yangu.

    Kwa vile suala la msichana huyo lilikuwa limenipa dukuduku, nilipofika nyumbani nikapata wazo moja. Wazo hilo lilikuwa ni kufanya utafiti ili kumjua huyo Ummy niliyemabiwa kuwa alikufa, alikuwa msichana wa aina gani. Alikuwa

    akifanya kazi gani na pia nijue kama alikuwa na uhusiano na marehemu babu yangu.

    Sikutaka tena kumpigia simu Ummy kwa sababu huenda angeipokea na kunieleza maneno ya kunitisha.

    Ili kuanza upelelezi wangu niliona niende katika mtaa ule ule aliokuwa anaishi Ummy nitafute mtu aliyekuwa anamfahamu nifanye naye urafiki na kisha nianze kumhoji kuhusu maisha ya Ummy mpaka kufa kwake.

    Ule mtaa nilikuwa mgeni nao, nilijua isingekuwa kitu rahisi kumpata rafiki wa kunipa habari za Ummy lakini

    nilijiambia ni lazima nijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu nimpate mtu ambaye ataweza kunifumbulia kitendawili cha Ummy Nasir.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ile yule msichana hakunipigia simu na mimi sikumpigia. Mimi sikumpigia kwa hofu niliyoipata baada ya kuelezwa kuwa msichana huyo alishakufa. Na kama alishakufa na nimekuja kukutana naye, basi atakuwa ni mzuka.

    Asubuhi ya siku ya pili yake nikaenda katika ule mtaa niliyokwenda jana yake kumuulizia Ummy. Safari hii sikwenda na gari langu. Nilipanda daladala.

    Sikutaka kufika tena pale nyumbani kwa mzee Nasir. Nilizuga zuga katika nyumba zilizokaribiana na nyumba yake nikitafuta mtu ambaye ningeweza kufanya naye urafiki na kumuuuliza kuhusu marehemu Ummy.

    Katika kutupatupa macho nikaona

    sehemu iliyokuwa na meza ya kahawa na kashata. Kulikuwa na mabenchi matatu ya kukalia. Muuza kahawa aliyekuwa amevaa kofia kubwa lililosukwa kwa minyaa kama la mvuvi wa samaki, alikuwa amekaa upande wa pili wa meza yake akiwa na ndoo mbili, jiko na birika la kahawa lililokuwa likifuka moshi jikoni.

    Muda ule kulikuwa na mtu mmoja tu aliyekuwa amekaa akinywa kahawa. Nikaona niende nikakae mahali hapo ili nifikirie la kufanya.

    Mara tu nilipoketi akaja mtu mwingine. Tukawa watu watatu.

    Muuza kahawa akatutilia kahawa bila hata kutuuliza. Ukishakaa kwenye benchi lake maana yake ni kuwa unataka kahawa.

    Nilichomsikia akiuliza ni. “Nikutilie tangawizi?”

    Alikuwa akimtazama yule mwenzangu aliyekuja baada ya mimi.

    “Ndiyo tia” Mtu huyo akamjibu.

    “Na wewe?” akaniiuliza mimi.

    Wakati ananitazama, sura yake ikanijia akilini mwangu. Zilinichukua kama nukta tatu hivi kumkumbuka Selemeni Mzaramu.

    Wakati namkumbuka, yeye alishanikumbuka zamani.

    “Ah! Kasim Fumbwe… kumbe ni wewe?” akaniuliza kwa mshangao.

    “Mzaramu! Bado upo Dar hii!” nikamuuliza.

    “Twende wapi ndugu yangu. Tunabangaiza humu humu. Makamba alituambia tutabanana hapa hapa”

    Tukacheka.

    “Nikuwekee tangawizi?’ akaniiuliza tena.

    “Ndiyo niwekee”

    Selemani Mzaramu alikuwa rafiki yangu wa miaka mingi. Nilisoma naye shule ya msingi hadi darasa la saba. Wakati mimi

    naendelea na masomo ya sekondari, mwenzangu hakuchaguliwa. Na baada ya hapo sikuwahi kukutana naye tena hadi siku ile nilipomuona amevaa kofia la minyaa akiuza kahawa.

    Mzaramu alinisogezea kikombe cha

    kahawa akaniuliza.

    “Uko wapi Kasim?”

    “Mimi niko hapa hapa Dar. Nilikuwa Morogoro , maisha yakanishinda, nikarudi hapa Dar”

    “Unafanya kazi wapi, nije unipe kibarua?”

    “Bado nipo nipo tu, sifanyi kazi popote. Nilikuwa na duka Morogoro, duka likafa, nikarudi Dar baada ya babu yangu kufariki. Na ndiyo nimeamua niendelee kuwa hapa”

    “Mimi baada ya masomo nilihangaika na malori mpaka yamenitia kilema. Sasa

    nipo hapa?”

    “Alah! Umepata ulemavu?”

    “Mguu wangu ulivunjika mara tatu. Mfupa ulisagika vibaya. Nimeokolewa na vyuma…”

    Mzaramu alinionesha mguu wake wa kushoto baada ya kuisega suruali yake. Mguu huo ulikuwa hautazamiki kwa mishono!

    “Nje unaouna ni mguu lakini ndani ni vyuma vitupu, yaani ulikuwa ukatwe lakini kaka yangu alijitahidi sana kunipeleka hospitali za pesa ambako niliwekewa vyuma. Nikasema sasa malori basi”

    “Loh! Pole sana rafiki yangu. Ulikuwa dereva?”

    “Nilikuwa taniboi. Basi nilikaa hospitali karibu mwaka mzima”

    Nikatikisa kichwa changu kumsikitikia.

    “Pole sana rafiki yangu lakini kama unapata riziki yako na maisha yanakwenda, shukuru Mungu”

    “Nashukuru. Nimeoa na nina watoto

    wawili lakini mke wangu alinikimbia aliposikia nitakatwa mguu. Kaniachia watoto lakini nimewalea mwenyewe na hivi sasa wanasoma”

    “Kumbe ulipata mkasa mkubwa rafiki yangu….”

    “Kula kashata” Mzaramu akaniambia.

    Nikaokota kashata moja na kuing’ata.

    “Unazitengeza mwenywe?” nikamuuliza.

    “Nazitengeza mwenyewe usiku. Asubuhi nakuja nazo”

    “Kwani unaishi wapi??’

    “Naishi hapa hapa Mwananyamala”

    “Mtaa huu?”

    “Ndiyo naishi mtaa huu huu lakini ni kule mwisho”

    “Umeishi mtaa huu kwa miaka mingapi?’

    “Nina miaka kumi na mitano sasa”

    Nikajiambia kimoyomoyo kuwa atakuwa anamjua Ummy ambaye alikufa miaka mitano tu iliyopita.

    “Katika mtaa huu alikuwa akiishi msichana mmoja aliyekuwa akiitwa Ummy Nasri…”

    “Nyumba yao ile paleee lakini huyo msichana alikwisha kufa zamani ila namfahamu sana”



    “Maana yake mtu amekufa halafu anakuja kuonekana tena”

    “Sasa yule si mtu yule yule”

    “Ni nani sasa?”

    “Kwanza mtu akifa hawezi kuonekana tena”

    “Mbona mimi nimemuona Ummy?”

    “Uliyemuona si Ummy”

    “Ni yeye. Licha ya kunielekeza kwao alinipa namba ya simu yake na nilimuonesha ndugu yake pale nyumbani kwao akasema ni namba ya Ummy kweli”

    “Kwani ulifika kwao kumuulizia?’

    “Ndiyo, nilifika jana”

    “Wakakuambia nini?”

    “Wakaniambia hivyo hivyo kwamba Ummy alikufa”

    “Si ndiyo nilivyokueleza mimi?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilihisi kwamba maelezo ya Mzaramu badala ya kunisaidia yalizidi kunichanganya. Mzaramu hakutaka

    kukubaliana na miimi kwamba niliyemuona alikuwa ni Ummy wakati nilikuwa na imani kuwa niliyekutana naye alikuwa ni Ummy Nasri.

    Kitu muhimu kilichonifanya niamini kuwa niliyemuona ni Ummy Nasri aliyedaiwa kufa ni ile picha ya Ummy niliyooneshwa na baba yake huku mdogo wake akikiri kwamba namba ya simu niliyopigiwa na Ummy ilikuwa namba ya Ummy kweli. Mdogo wake huyo alikuwa ameikariri.

    Sasa kulikuwa na vitu viwili vilivyonitia mawazo. Kwanza ni yale maelezo ya Mzaramu kwamba Ummy kabla ya kufa alikuwa na uhusiano na mzee mmoja

    ambaye Mzaramu alinithibitishia kuwa ndiye yule niliyemuonesha katika picha iliyokuwa kwenye simu yangu.

    Picha hiyo ilikuwa ni ya babu yangu marehemu mzee Limbunga. Hivyo maelezo ya Mzaramu yalionesha kwamba babu yangu alikuwa na uhusiano na Ummy.

    Kitu cha pili kilichoniitia mawazo ni maelezo ya Ummy kwamba anazijua siri za malli ya babu yangu. Inawezekana kweli anaijua siri ya mali ya babu yangu kwa vile alikuwa na uhusiano naye. Ila kinachotatanisha hapo ni kuwa Ummy mwenyewe anadaiwa kuwa alishakufa.

    Yakanijia mawazo yale yale kwamba niliouona ulikuwa mzuka wa Ummy, yaani iliwezekana kuwa Ummy alishakufa kweli lakini nilichokutana nacho kilikuwa kivuli chake. Nilishasikia hadithi nyingi za watu waliokufa kuonekana tena ikidaiwa kuwa ni mizuka ya watu hao.

    Lakini mara nyingi mizuka hiyo

    inapotokea inakuwa na sababu.

    Sasa nikajiambia labda nijaribu kutafuuta sababu ya kutokea kwa mzuka wa Ummy ambaye aliwaua watu wote waliokuwa wakidaiwa na babu yangu na kusababisha nisilipwe pesa ambazo ningelipwa na watu hao.

    Nikajiuliza kama Ummy alikuwa mzuka ni kwanini aliwaua watu hao halafu aniambie kuwa anaijua siri ya mali ya babu yangu na kutaka nikutane naye?

    Kwa kweli kila nilivyowaza niliona sivyo na kila nilivyojiuliza sikupata jibu. Hapo ndipo nilipozidi kuchanganyikiwa.

    “Mbona umeduwaa rafiki yangu?”

    Mzaramu akaniuliza akiwa hajui yaliyokuwa yanapita akilini mwangu.

    Nikazinduka kutoka katika mawazo yangu na kumwambia.

    “Nilikuwa nafikiria hadithi uliyonieleza”

    “Kahawa imekutosha?” akaniuliza.

    “Imetosha. Ni kiasi gani?”

    “Sijakuuzia, nimekupa kiurafiki kwa vile siku nyingi hatujaonana”

    “Asante, nakushukuru sana. Naona nikuage, tutaonana siku nyingine”

    Nilipoondoka kwa Mzaramu nilikusudia nipite pale nyumbani kwa kina Ummy na kama nitakutana na yule mzee nisalimiane naye.

    Wakati nipo barabarani nikitembea kwa miguu kuelekea upande ule ilikokuwa nyumba ya mzee Nasri, nikakutana na mdogo wake Ummy akitokea dukani.

    Msichana huyo aliponiona akasimama.

    “Kaka wewe ndiye uliyekuja nyumbani jana ukatuambia kuwa ulimuona dada?” akaniuliza.

    “Ndiye mimi”

    “Jana ulitutia wasiwasi sana. Ilibidi mama aende kwa mganga kumueleza kuhusu kuonekana kwa Ummy ambaye alishakufa. Mganga akamwambia kwamba huyo aliyeonekana alikuwa Ummy kweli, amechukuliwa msukule”

    “Amechukuliwa msukule na nani?” nikamuuliza.

    “Huyo mganga alimwambia amechukuliwa msukule na mwanamke mmoja ambaye aliwahi kugombana naye”

    “Waligombania nini?”

    “Huyo mwanamke alikuwa akidai kuwa marehemu alikuwa anatembea na mume wake”

    Nikayakumbuka yale maelezo ya Mzaramu. Nikafikiri kidogo kisha nikamuuliza.

    “Kama alichukuliwa msukule mbona yuko vizuri tu, anaongea kwenye simu na nilikutana naye Botswana, Zimbabwe na Afrika Kusini. Mtu aliyechukuliwa msukule anapanda ndege?”

    “Hayo ni maelezo ya huyo mganga lakini baba alipoelezwa amesema hataki mambo ya kishirikina, anachojua yeye ni kuwa mwanawe amekufa, huyo aliyeonekana siye mwanawe”

    “Mimi pia hayo madai ya kuchukuliwa msukule sikubaliani nayo. Waganga wengine wanakisia tu”

    “lakini wewe una hakika kuwa ulimuona dada?”

    “Nilimuona na ni yeye aliyenielekeza nije kwenu. Mimi nilikuwa sijui kwamba amekufa”

    “Na tangu jana hajakupigia simu?”

    “Hajanipigia bado”

    “Na wewe hujampigia?”

    “Sijampigia”

    “Ungempigia umuulize vizuri”

    “Kusema kweli nimetishika baada ya kusikia kuwa alishakufa”

    “Hebu jaribu kumpigia sasa hivi?”

    Nikatoa simu na kuitafuta namba ya Ummy, nilipoipata nikampigia.

    Simu ikaita. Nikajua itapokelewa ili nimpe mdogo wake azungumze naye lakini simu haikupokelewa. Ilipokata nikapiga tena.

    “Hapokei simu?” nikamwambia yule msichana.

    “Labda alikudanganya tu?”



    “Hakunidanganya. Baba yako alinionesha picha yake, ndiye yeye

    niliyemuona na hata namba ya simu anayotumia ulisema ni yake”

    “Namba ya simu ni yake kweli, niliikariri

    kichwani mwangu”

    “Basi ndiyo ujue niliyemuona alikuwa ni Ummy kweli”

    “Sasa mbona hapokei simu?”

    “Tena mwanzo alikuwa akinipigia yeye, ndiyo nikaipata hii namba yake”

    “Basi atakapokupigia tena utakuja kutuambia”

    Nikaagana na yule msichana. Sikwenda kwao tena. Nikaenda kupanda daladala na kurudi nyumbani.

    Vile nafika nyumbani tu, simu yangu ikapigwa. Nilipoangalia namba inayonipigia, nikaona namba ya Ummy.

    Nilishituka halafu mwili ulinisisimka.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikajiuliza niipokee au nisiipokee? Kama nitaipokea msichana huyo atanieleza nini? Nikajiambia chochote ambacho ataniambia kitazidi kuniweka njia panda kwa vile nimeshathibitisha kuwa msichana huyo alikuwa ameshakufa.

    Vile vile tayari nilikuwa na hofu ya kuzungumza na mtu ambaye kuna ushahidi kuwa alikuwa amekufa.

    Lakini kwa upande mwingine nilikuwa na shauku ya kumsikia yeye mwenyewe atakachojibu kuhusu madai kuwa alikuwa ameshakufa miaka mitano iliyopita.

    Nikajiambia nisipopokea simu yake, bado nitabaki kuwa njia panda kwani sitapata mtu mwingine wa kunipa ufafanuzi kuhusu madai ya kufa kwake.

    Mbali na hayo, bado nilitaka kujua ni siri gani ambayo alitaka kunieleza kuhusu mali za babu yangu. Nikaamua kupokea ile simu.

    “Hello!” Nikasema kwa sauti ya kujikaza ili nisioneshe hofu niliyokuwa nayo.

    “Hello! Kassim unajua nimekupenda sana, ninataka uwe mume wangu!”

    Maneno hayo yalinishitua. Niwe mume wa mtu aliyekwisha kufa!

    “Natumaini kuwa naongea na Ummy?” nikamuuliza.

    “Mimi ni Ummy Nasri”

    “Uliniambia nifike nyumbani kwenu Mwananyamala, nimefika jana na leo lakini sikukuona”

    “Ulimkuta nani?”

    “Nilimkuta baba yako mzee Nasri”

    “Vizuri sana. Alikuambia nini?”

    “Aliniambia maneno ya kunishitusha sana”

    “Kama yapi”

    “Aliniambia kwamba mwanawe anayeitwa Ummy alikwishakufa miaka mitano iliyopita”

    “Na mimi ni nani?”

    “Umeniambia kuwa wewe ni Ummy Nasri”

    “Na uliyembiwa amekufa ni nani?”

    “Ni Ummy Nasri”

    “Sasa una shaka gani?”

    “Kwanza nataka unieleze ni kwanini nimeambiwa kuwa umekufa?”

    “Kuna umuhimu wa mimi na wewe kukutana”

    “Kwanza nataka ujibu, kwanini nimeambiwa kuwa umekufa?”

    “Ndiyo maana nikakwambia kuna umhimu tukutane ili tuzugumzie hilo pamoja na kukueleza kuhusu mali za babu yako”

    Nikanyamaza kwa sekunde kadhaa nikifukiria la kumjibu.

    “Lakini ni kweli kuwa ulikufa?” nikamuuliza baada ya kimya kifupi.

    “Ni kweli?”

    “Sasa wewe ni nani?”

    “Ni Ummy”

    “Umekubali kuwa ulishakufa, sasa mbona uko hai?”

    “Mimi ni kivuli cha Ummy”

    “Sijakuelewa. Kivuli maana yake nini?”

    “Maana yake ni mzuka wa Ummy!”

    Moyo wangu ulipiga kwa nguvu kisha ukaanza kunienda mbio. Nikahisi mkono ulioshika simu ulikuwa ukitetemeka.

    “Kassim tutakapokutana kila kitu utakielewa vizuri”

    “Unadhani nitakutanaje na mzuka?”

    “Tutakutana tu na tutazungumza, usijali”

    “Mmmh…!”

    Pakapita kimya kingine.

    “Niambie nikiuone wapi na muda gani?” Sauti ya Ummy ikautanzua ukimya uliokuwepo.

    “Acha nifikirie kwanza”

    “Ufikirie nini Kassim?”

    “Umenitisha. Umeniambia kwamba wewe ni mzuka”

    “Sasa unataka ufikirie nini?”

    Sikujibu.

    “Kassim!” Sauti ya Ummy ikaita kwenye simu.

    Sikujibu. Nilibaki nimeduwaa kama gogo.

    “Nitakupa muda wa kufikiria lakini usizidi saa arobaini na nane”

    “Sawa” nikamuitikia.

    Ummy akakata simu.

    Yale maneno ya kwanza ya Ummy kuwa ananipenda na anataka niwe mume wake, yalipita katika akili yangu.

    Nikajiambia hata wale watu aliowaua kule Buswana. Zimbabwe , Afrika Kusini na hapa Dar, inaelekea walianzana kwenye mapenzi,

    Kitendo cha kuniambia anataka niwe mume wake si tu kimebadili mada yake ya kwanza ya kutaka tukutane ili anieleze ziliko mali za babu yangu bali pia nilifikiri kwamba ilikuwa ni hatua ya kutaka kuniua.





    Niliendelea kujiambia kama msichana huyo amekiri kuwa ni mzuka, atakuwa ni muuaji tu. Pengine alikuwa na kisasi na

    babu yangu ambaye niliambiwa alikuwa mwanamke wake.

    Nitakutanaje na kuzungumza na mzuka? Nilijiuliza huku nikifikiria niende Mwananyamala nikamjulishe mzee Nasri kuhusu yale maelezo ya Ummy.

    Hata hivyo upande mmoja wa akili yangu ulinikataza kwenda Mwananyamala kwa vile nilijua yule mzee atapuuza maelezo yangu kwa ile imani yake kuwa Ummy alishakufa na aliyekufa hawezi kurudi tena duniani.

    Sasa nifanye nini, huyu msichana ataendelea kuniandama?” nikajiuliza

    Sikuweza kupata jibu la haraka kwa vile akili yangu ilikuwa imetaharuki. Nilijiambia nitakapotulia na kurudi katika hali ya kawaida, huenda nitajua nitafanya nini.

    Wakati nazungumza na Ummy nilikuwa nimesimama kwa kutaharuki, nikakaa kwenye kochi na kuendelea kuwaza.

    Hisia zangu tangu nianze kumfahamu Ummy sasa zilikuwa zimebadilika. Mwanzo nilikuwa nikihisi kuwa Ummy alikuwa binaadamu anayetumia miujiza kuua watu. Nilijua hivyo tangu nilipoanza kumuona kule Botswana.

    Na hata pale nilipomkimbia katika chumba cha hoteli aliponiita, nilimkimbia kwa hofu kuwa alitaka kuniua kama alivyowaua wale wadeni wa marehemu babu.

    Lakini sasa mtazamo haukuwa huo. Hisia zangu zilikuwa upande mwingine kwamba Ummy hakuwa muuaji mwenye miujiza kama nilivyokuwa nikidhani bali alikuwa mzuka wa mtu aliyekwisha kufa

    miaka mitano iliyopita.

    Kama Ummy aliyekufa alikuwa binadamu, huyu Ummy wa sasa si binaadamu tena. Huu ni mzuka kama alivyoniambia wenyewe. Hauna akili ya kibinaadamu. Mara nyingi mzuka

    unapotokea unakuja kuua watu halafu unapotea.

    Niliwaza kwamba mimi pia nilikuwa katika orodha ya kuuawa na mzuka huo kwani wale waliouawa kwanza walikuwa wako pamoja na mzuka huo kiurafiki wakidhani alikuwa binaadamu mwenzao. Na wote waliuawa katika mazingira ya kimapenzi.

    Sasa kama mzuka huo wa Ummy umeanza kuniambia kuwa umenipenda, ndio unataka kunitia kamba ili uniue kirahisi.

    Lakini wakati nawaza hivyo suala la mali za babu lilikuwa likitikisa kichwa changu. Kwanini mzuka huo aliniambia unazijua siri za mali ya babu yangu?.

    Ilikuwa ni muhimu nikutane naye lakini niliogopa. Huenda hapo tutakapokutana ndio nikauawa hapo hapo.

    Nikajiuliza niende nikaripoti polisi ili Ummy akamatwe na kuhojiwa? Au, niliendelea kujiuliza, niende kwa mganga ili anieleze ukweli kuhusu kiumbe huyu na nia yake kwangu?

    Wazo la kwenda polisi sikuafikiana nalo. Nilijiambia polisi hawashughulikii masuala ya mizuka. Ningeweza kudai kuwa huyu msichana anadaiwa kuwa alikufa miaka mitano iliyopita lakini ninamuona na ananipigia simu kutaka nikutane naye.

    Madai hayo yanaweza kuwavutia polisi wamuandalie mtego na kumkamata. Lakini nikajiuliza kama Ummy ni mzuka kweli, anaweza kukamatika au ninajidanganya?

    Wazo zuri, niliendelea kujiambia, ni la kwenda kwa mganga. Mganga anaweza kunitegulia kitendawili hiki.

    Baadaya kuwaza hivyo nikaamua niende kwa mganga mmoja wakati ule alikuwa akikaa Chanika. Alikuwa mzigua wa Handeni. Alikuwa akifahamiana na babu na kuna siku niliwahi kwenda kwake nikiwa na babu. Babu yangu licha ya utajiri aliokuwa nae alikuwa mshirikina sana.

    Siku ambayo nilikwenda naye kwa mganga huyo alikwenda kumroga mfanyabiashara mwenzake ambaye naye alikuwa na vituo vya mafuta. Walikuwa wakishindana kibiashara na babu akaamua kuingiza na uchawi.

    Siku hiyo nakumbuka, mganga alizika mbuzi watatu wakiwa hai kwenye kaburi la mwanamke aliyekufa zamani. Juu ya kaburi pakamwagwa mchanga wa alama za viatu za mfanyabiashara aliyekuwa akishindana na babu yangu.

    Babu alikuwa ametuma watu kuzitafuta alama za viatu za mfanyabiashara huyo kwa dau la shilingi milioni tatu kwa mtu atakayefanikisha kuzipata. Watu hao wakawa wanamuandama mfanyabiashara huyo usiku na mchana mpaka wakafanikiwa kupata alama zake.

    Alama hizo walizipata aliposhuka kwenye gari na kukanyaga mchanga kabla ya kwenda kulikagua eneo ambalo alitaka kulinunua pale Ubungo.

    Baada ya mchanga huo kumwagwa juu ya kaburi hilo palikutwa kibao kilichokuwa na jina lake. Baada ya siku saba mfanyabiashara huyo aliaga dunia baada ya gari lake kugongwa na lori la mafuta! Babu akafurahi.

    Mganga huyo alikuwa mzigua aliyetoka Handeni. Wenyeji wa Chanika walimpa jina la “mashine ya kuua”

    Tangu kipindi hicho miaka mingi ilikuwa imepita na sikuwahi kwenda kwake tena kwa vile sikuwa na tabia za kwenda kwa waganga wa kienyeji. Hiyo tabia alikuwa nayo babu yangu.

    Nikaona niende nikamueleze matatizo yangu nikiamiini kuwa anaweza kunipatia ufumbuzi.

    Nikaenda kwa gari langu

    Nilipofika niliikuta ile nyumba yake ambayo wakati ule ilikuwa ikiendelea kujengwa, ilikuwa imeshakamilika. Lakini nilikuta msururu wa watu.

    Ikabidi na mimi nipange msitari. Hadi nafanikiwa kuingia katika chumba chake cha uganga ilikuwa karibu saa kumi na moja jioni. Nilikuwa na matumaini madogo sana kama angelishughulikia suala langu kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana.

    Mganga mwenyewe alikuwa amenisahau, nikamkumbusha. Mara moja akamkumbuka babu yangu lakini mimi hakunikumbuka.

    “Wewe ni mjukuu wa yule mzee?” akaniuliza.

    “Ni mimi lakini babu mwenyewe alishakufa”

    Mganga akashituka.

    “Kumbe mzee Limbunga alikufa?”

    “Alikufa”

    “Alikufa mwaka gani?”

    “Alikufa mwaka huu”

    “Kwa hiyo wewe ndiye umesimamia shughuli zake?”

    “Ni mimi lakini kuna matatizo yamejitokeza”

    “Matatizo gani?”

    “Wewe unajua kuwa mzee Limbunga alikuwa tajiri lakini alipokufa mali zake hazikuonekana”

    “Kwanini?”

    “Sijui”



    “Mmmh…! Mganga akaguna. Baada ya kuwaza kidogo aliniambia.

    “Nakumbuka kulikuwa na msichana alikuwa akimsumbua sana babu yako. Huyo anaweza kujua siri ya mali ya babu yako. Babu yako alikuwa akimpenda na alifikia kumshirikisha kwenye biashara zake”

    Mganga aliponimbia hivyo nilishituka, nikamuuliza.

    “Aliwahi kukutajia jina lake?’

    “Aliwahi kunitajia lakini muda ni mrefu nimelisahau”

    “Sio Ummy?”

    “Sawasawa. Ni Ummy Nasri…”

    “Lakini huyo msichana si alikufa?”

    “Mimi sijui kama alikufa”

    Hapo sasa nikaona nimueleze mkasa mzima wa Ummy Nasir.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati wote nilipokuwa nikimueleza mganga huyo, alikuwa amenikazia macho kama vile nilimueleza kitu kigeni ambacho hakuwahi kukisikia.

    Nilipomaliza maelezo yangu aliniambia

    “Subiri”

    Alichukua kipande cha ubao akauchorachora vistari kwa kutumia chaki. Alichora mara ya kwanza akafuta. Akachora mara ya pili akafuta. Alipofuta mara ya tatu alifungua kitabu akasoma kisha akatikisa kichwa.

    “Nikwambie ukweli. Mimi ni mganga na

    nimeshafanya kazi hii kwa zaidi ya miaka thelathini sasa, sijawahi kuona ramli yangu ikiwa na kiza kama leo” Mganga akaniambia.

    Nilishituka kidogo.

    “Sijakuelewa. Unaponiambia ramli yako ina kiza una maanisha nini?” nikamuuliza.

    “Ninamaanisha kwamba sina ninachoona. Ramli imefunga. Hapa ninaona kiza kitupu”

    “Inapokuwa hivyo inadhihirisha nini?”

    “Inadhihirisha kwamba tatizo lako halitambuliki au kwa maneno mengine nimeshindwa kulifumbua”

    “Ni kwa sababu gani?”

    “Sijui”

    “Kwa hiyo huyu msichana atakuwa ni mzuka kama alivyonieleza mwenyewe”

    “Inawezekana”

    “Sasa kama yeye ni mzuka ni kwanini ananitokea mimi?”

    “Hilo jambo liko nje ya elimu yangu. Siwezi kujua”

    “Kwa hiyo unanishauri nifanye nini?”

    “Kwa tatizo kama hili, mimi ninakushauri nenda polisi. Huyu mwanamke atakamatwa na atajieleza”

    “Sidhani kama polisi watashughulikia suala hili”

    “Mimi naamini watalishughulikia”

    “Basi nitakwenda kuripoti polisi”

    Mazungumzo yangu na mganga huyo yakaishia hapo hapo. Wakati niko kwenye gari nikirudi, niliamua nifuate ushauri wa yule mganga wa kwenda polisi kwa sababu sikuwa na mahali pengine pa kwenda kuomba msaada.

    Wakati ninakwenda kwa mganga huyo nilikuwa na furaha kutokana na imani kuwa tatizo langu lingepatiwa ufumbuzi. Lakini wakati ule narudi nilikuwa nimepatwa na wasiwasi hasa kutokana na maelezo ya mganga kwamaba anaona kiza kitupu.

    Kwanini aniambie anaona kiza kitupu? Tafsiri ya kiza ni kitu gani? Kifo au uzima? Nilikuwa nikijiuliza bila kupata jibu.

    Licha ya mganga huyo kutonifumbulia chochote juu ya kitendawili cha Ummy,

    jambo mmoja lilikuwa wazi kwamba lile suala lilikuwa gumu na si la mzaha.

    Niliamua niende kituo cha ppolisi cha Kinondoni. Nilipofika nilikutana na polisi waliokuwa kaunta ambao baada ya kuwaeleza tatizo langu walinipeleka ofisini kwa Inspekta Amour.

    “Una tatizo gani?” Inspekta huyo akaniuliza.

    Nikamueleza. Maelezo yangu yalianzia kupigiwa simu na Ummy. Sikutaka kueleza kuhusu ziara yangu ya nchi tatu nilizozitemnbelea ambapo Ummy aliua watu watatu.

    Nilimueleza inspekata huyo kwamba nimekuwa nikipigiwa simu na msichana ambaye sikuwa nikimfahamu akinitaka nikutane naye kwa ajili ya kunipa siri ya mali ya babu yangu aliyekuwa amefariki.

    Nikaendelea kumueleza kuwa mara ya kwanza aliniita katika hoteli mmoja iliyoko Masaki ambako nilikwenda kumuona na kuzungumza naye.

    Hapo pia sikutaka kueleza ukweli wa tukio hilo isipokuwa nilieleza kwamba nilizungumza na msichana huyo na akanitaka niende kwao Mwananyamala ili nikutane naye kwa mazungumzo zaidi.

    Nikaeleza kuwa nilipofika Mwananyamala katika nyumba aliyonielekeza, nilitaja jina lake lakini watu walioniambia kuwa ni wazazi wake waliniambia kuwa Ummy alikuwa ameshakufa miaka mitano iliyopita..

    Nilimwambia Inspekta huyo kwamba wazazi hao wa Ummy walinionesha picha zake na nikathibitisha kuwa Ummy niliyemuona alikuwa ni yeye lakini la kushangaza ni kuambiwa kuwa alishakufa miaka mitano iliyopita.

    Nikaendelea kueleza kuwa baba yake alinipeleka katika kaburi aliloniambia kuwa ni la Ummy na hakutaka kukubaliana na mimi kwamba Ummy yuko hai..

    “Lakini namba yake ya simu waliikubali. Mdogo wake Ummy aliniambia namba niliyowaonesha ilikuwa ya Ummy kweli” nikaeleza.

    “Huyo msichana alinipigia tena simu akakubali kuwa yeye alikufa na kwamba ni mzuka uliokuwa unataka kunipa taarifa ya mali za babu yangu na la kunishangaza zaidi ameniambia kuwa ananipenda na anataka niwe mume wake. Haya mambo yameitia wasiwasi sana” nikamaliza.



    “Sasa ulitaka tukusaidieje?” Inspekta huyo akaniuliza baada ya kumaliza maelezo yangu.

    “Ninaiomba polisi ichunguze kuhusu huyu msichana na ikiwezekana akamatwe ili ajieleze ni nani. Nimepatwa na wasiwasi sana hasa baada ya kuambiwa kuwa alishakufa”

    “Kazi ya jeshi la polisi nni kulinda

    usalama wa raia na mali zao. Vile vile tunashughulikia masuala ya jinai. Kwa vile suala hilo linahusu usalama wako na linaweza kuingia pia katika jinai, tutakusaidia kufanya uchunguzi”

    “Nitashukuru sana”

    “Nipatie namba ya huyo msichana”

    Nikampatia kachero huyo namba ambayo Ummy amekuwa akinipigia simu.

    Nilipompa namba ya Ummy aliipiga na kuitega simu sikioni. Baada ya kusubiri kwa sekunde kadhaa aliniambia.

    “Namba inaita lakini haipokelewi”

    Akaiondoa simu sikioni na kuniambia.

    “Twende huko nyumbani kwao”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dakika chache baadaye, kachero huyo aliyeonekana kuipenda na kuithamini kazi yake alikuwa amenipakia kwenye gari la polisi tukielekea Mwananyamala.

    Alilisimamisha gari mbele ya nyumba niliyomuonesha. Mzee Nasri alikuwa amekaa barazani kwenye kiti cha uvivu akisoma gazeti la lugha ya Kiingeza.

    Tulishuka kwenye gari hilo tukamsalimia mzee huyo.

    Baada ya salamu Inspeketab Amour alijitambulisha kwake kabla ya kumuuliza kama alikuwa anafahamu Ummy Nasri.

    “Namfahamu. Ni mwanagu lakini alishakufa” Mzee akamjibu.

    “Alikufa lini?”

    “Alikufa miaka mitano iliyopita”

    Inspekta Amour alinitazama kisha akayarudisha macho yake kwa yule mzee.

    “Unamfahamu huyu kijana?” akamuuliza.

    “Huyu kijana aliwahi kuja juzi akatuambia kuwa alionana na marehemu lakini hilo jambo tulilipinga sana kwa sababu marehemu alishakufa”

    “Ana uhakika kwamba alikutana na binti yako unayedai kuwa amekufa na amekuja kutoa ripoti kituo cha polisi hii leo. Amedai kuwa huyo msichana anamsumbua na kumsababishia hofu kwani kila mara anampigia simu. Hiyo ndiyo sababu tumekuja kwako ili tupate ukweli”

    “Ukweli ndio huo niliokueleza kwamba huyo binti alishakufa. Sasa sijui huyo anayemsumbua yeye ni nani”

    “Huyo msichana amemwambia kuwa yeye ni mzuka wa Ummy”

    Mzee akatikisa kichwa.

    “Hakuna kitu kama hicho”

    “Namba ya simu anayotumia huyo msichana umewahi kuiona?” Inspekta alimuuliza mzee huyo.

    “Alituonesha juzi. Binti yangu alikubali kwamba ilikuwa namba ya marehemu lakini tangu alipokufa hadi leo ni miaka mitano. Mtu mwingine anaweza kupewa namba hiyo”

    “Una picha za huyo marehemu??”

    “Picha zipo”

    “Ningeomba nizione”

    Mzee akainuka na kuingia ndani.

    Baada ya muda kidogo alitoka akiwa na mke wake pamoja na mdogo wake Ummy.

    Mke wake na mdogo wa Ummy walitusalimia wakati yule mzee akituonesha picha za Ummy.

    “Ummy mwenyewe ndiye huyu?” Inspekta akauliza.

    “Ndiye yeye. Picha zote hizi ni yeye”

    “Na mna uhakika kwamba alikufa??”

    “Alikufa, naweza hata kwenda kukuonesha kaburi lake”

    “Kwanza ningeomba unipatie picha mojawapo kwa ajili ya uchunguzi”

    “Unahitaji ipi?”

    Inspekata alichagua picha aliyoitaka. Mzee akaichomoa kwenye albamu na kumpa.

    “Sasa nipeleke nikalione hilo kaburi lake”

    Mzee akatupeleka. Baada ya Inspekata Amour kuliuona kaburi la Ummy alimwambia mzee Nasri.

    “Kaburi nimeshaliona, sasa turudi nyumbani”

    Tukarudi. Mke wa Mzee Nasri pamoja na binti yao walikuwa wakitusubiri barazani.

    “Baba kuna mazingara yanafanyika siku hizi. Unaweza kuambiwa mtu fulani amekufa kumbe yuko hai. Sisi tulikwenda kwa mganga tukaambiwa Ummy yuko hai amechukuliwa msukule lakini baba yake amekataa jambo hilo” Mke wa mzee Nasri akatuambia.

    “Tukiingiza imani kama hizo tutaharibu uchunguzi. Lakini vyovyote vitakavyokuwa ukweli utabainika muda si mrefu kwamba Ummy amekufa au amechukuliwa msukule. Tutajua tu….” Ispekta alimwambia.

    “Huo uchunguzi utakuwa ni muhimu sana kwa sababu hilo jambo limeshaanza kututia wasiwasi” Mke wa mzee Nasri alisisitiza.

    “Sawa. Hivi sasa tunakwenda katika kampuni ya simu ili tujue ni nani anayetumia hii namba ya Ummy”

    “Naamini utampata mtu aliyezusha huu utata” Mzee Nasri akatuambia kabla ya kuagana naye.

    Tuliondoka na Inspekta Amour hadi katika ofisi ya kampuni ya simu inayomiliki namba ambayo Ummy amekuwa akinipigia.

    Baada ya Amour kujitambulisha aliomba aoneshwe usajili wa namba hiyo.

    Sekunde chache tu kompyuta ya kampuni hiyo iliutoa usajili wa namba ya Ummy pamoja na picha yake. Kitu ambacho kiliniacha hoi na pengine kilimuacha hoi Inspekta Amour ni kuona kuwa usajili huo ulikuwa na jina la Ummy Nasri na picha ya kitambulisho pia ilikuwa ya Ummy.

    Ndipo maswali yalipoanza.

    “Hii namba ilisajiliwa lini?” Inspekta Amour akauliza.

    “Kwa mara ya kwanza namba hii ilisajiliwa miaka sita iliyopita. Baada ya kutumika kwa mwaka mmoja iliacha kutumiwa kwa karibu miaka mitano, tukaifuta”

    “Baada ya kuifuta nani alikuja kuirudisha?”

    “Ni mhusika huyo huyo, alikuja mwezi uliopita akaitaka namba yake. Kwa vile hatukuwa tumeiuza kwa mtu mwingine tukampatia na hivyo alifanya usajili upya”

    “Huyo huyo Ummy Nasir ndiye aliyefanya usajili upya?”

    “Ndiye huyo huyo kama ambavyo picha yake inaonekana”



    Kitu ambacho kilitushangaza zaidi mimi na Inpekta Amour ni kuwa tarehe ile ile ya usajili wa mara ya pili ndiyo tarehe hiyo hiyo ambayo Ummy alianza kunipigia simu. Kumbukumbu za tarehe zilikuwa bado zipo kwenye simu yangu.

    “Sasa tunaomba utupatie namba nyingine ambazo zilimekuwa zikiwasiliana na namba hii” Inspekata Amour akatoa ombi jingine.

    Msichana baada ya kuangalia kwa makini alisema.

    “Hii namba tangu iliposajiliwa kwa mara ya pili rekodi yake inaonesha kuwa iliwasiliana na namba moja tu”

    Alipoitaja namba hiyo ilikuwa ni namba yangu mimi.

    Amour akanitazama kwa mshangao kabla ya kuuliza swali jingiine.

    “Ilifanya mawasiliano mara ngapi?”

    “Mara tano”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Inspekta Amour akanigeukia mimi.

    “Mlifanya mawasiliano mara tano?” akaniuliza.

    “Nafikiri inaweza kufika mara tano”

    “Inaonekana kama aliifufua namba yake ili kukupigia wewe tu”

    “Sasa swali, katika kipindi chote cha miaka mitano alichoacha kutumia hii namba alikuwa wapi?”

    “Ndicho hicho kipindi anachodaiwa kuwa alikufa lakini usajili wake unaonesha kuwa hakuwa amekufa miaka mitano iliyopita kwani alikuja mwenyewe kuifufua namba yake”

    Wakati tukiwa garini tukirudi kwa mzee Nasri, Amour aliniambia.

    “Nina mashaka na madai kuwa Ummy alikufa”

    “Kwa hiyo wazo la kuwa ni mzuka kama alivyoniambia yeye halina ukweli?”

    “Mimi kama polisi siwezi kukubaliana na wazo kama hilo”

    “Pale kwao wanasisitiza kuwa Ummy alishakufa na hata majirani niliowauliza wameniambia kuwa Ummy alikufa kweli”

    “Sasa kama Ummy alikufa kweli, yule aliyekwenda kuisajili ile namba ni nani?”

    “Ndiyo maana ninaliona wazo la huo mzuka linahitaji kufanyiwa kazi”

    “Hivi wewe unaamini kuwa mtu aliyekufa anaweza kuibuka tena na kuwa mzuka?”

    “lisemwalo lipo. Ni vizuri jambo hili lichunguzwe”

    Tulipofika kwa mzee Nasri tulishuka kwenye gari. Mzee Nasri hakuwepo barazani. Amour akabisha mlango wa nyumba yake.

    Mzee Nasri akatoka.

    “Karibuni” akatuambia.

    Safari hii alitukaribisha sebuleni.

    Baada ya kuketi Amour alimwambia.

    “Tumekwenda katika kampuni ya simu tumeambiwa kuwa usajili wa ile namba ni wa mwanao Ummy”

    “Inawezekana. Ile namba aliisajili yeye mwenyewe”

    “Tuliambiwa aliisajili kwa mara ya kwanza miaka sita iliyopita. Baadaye alacha kuitumia kwa miaka mitano. Hivi karibuni alikwenda kuifufua kwa sababu namba yenyewe ilikuwa imefutwa”

    “Alikwenda kuifufua nani?” Mzee akauliza akiwa amemkazia macho Inspekta Amour.

    “Alikwenda kuifufua Ummy mwenyewe. Tumeoneshwa kitambbulisho chake na siku hiyo hiyo alimppigia huyu kijana”

    “Hilo jambo haliwezekanai. Bado nasisitiza kuwa Ummy amekufa… Ummy amekufa…”

    “Mzee huwezi kufufua namba ya mtu mwingine. Ni lazima uoneshe kitambulisho chako ili utambulike kuwa wewe ndiye mwenyewe”

    Niliona jasho likimtoka yule mzee.

    “Sijui niseme nini..!” akajisemea peke yake.

    “Itabidi tulifukue kaburi la Ummy” Ispekata akamwambia.

    Mzee akamkazia macho tena Inspekta.

    “Kwanini?”

    “Kwa sababu kuna madai kuwa Ummy hakufa. Na kama itathibitika kuwa Ummy hakufa anaweza kukabiliwa na kosa la jinai”

    “Kama italazimika kuwa hivyo, mimi niko tayari kuruhusu kaburi lake lifukuliwe ili mtibitishe kuwa mwannangu alikufa”

    Mzee akanitazama kwa kunilaani. Alikuwa kama anayejiambia mimi ndiye niliyeyaleta yote yanayotokea.

    Siku ya pili yake kikosi maalum cha polisi kikiongozwa na Inspekta Amour kilipewa kibali na mkuu wa polisi wa wilaya, cha kulifukua kaburi la Ummy kwa madai kuwa Ummy hakuwa amekufa.

    Tulifika katika eneo hilo la makaburi saa nne asubuhi. Mzee Nasri na familia yake walikuwa wamesimama pembeni wakiangalia. Uso wa Mzee Nasri ulikuwa umefadhaika. Kitendo cha kufukuliwa

    kaburi la mwanawe kilikuwa kimemkera.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mkewe na mdogo wake Ummy wallikuwa

    na mawazo tofauti. Wao walitaka kaburi hilo lifukuliwe ili wathibitishe ukweli wa mambo.

    Kulikuwa na daktari kutoka hospitali ya

    Muhimbili ambaye aliletwa kwa ajili ya kuuchunguza mwili utakaopatikana ndani ya kaburi hilo.

    Kazi ya kulifukua kaburi hillo ilianza saa nee na dakika tano.

    Kwa vile wafukuaji walikuwa polisi wawili, baada ya nusu saa tu kaburi hilo likawa wazi.

    Makaburi ya kiislkamu yanakuwa na mfereji mwembamba unaolazwa mwili wa marehemu. Mfereji huo unaoitwa mwanandani hufinikwa na ubao wakati marehemu anapozikwa.

    Ule ubao ulikuwa umeshaanza kuoza. Lakini sanda ya marehemu ilikuwa bado ipo ingawa ilikuwa imefubaa.

    Polisi waliokuwa wamevaa mipira waliutoa mwili huo na kuuweka juu ya kaburi kisha wakaifungua ile sanda upane wa kichwani.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog