Search This Blog

A BOOK OF SATAN ( KITABU CHA SHETANI ) - 5

 







    Simulizi : A Book Of Satan ( Kitabu Cha Shetani )

    Sehemu Ya Tano (5)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hiki kitabu huwa kinasomwa kuanzia mwisho kuja mwanzo, anzia ukurasa wa mwisho,” alisema mganga Kiswigo, baba yake Samantha akajifuta kwanza machozi na kufuata alichoambiwa. Alipofungua ukurasa wa mwisho wa kitabu hicho, alishangazwa sana na alichokiona.

    Zile kurasa ambazo muda mfupi uliopita alikuwa akiziona kama hazijaandikwa chochote, zilikuwa zimejaa maandishi mengi ambayo yalikuwa yakibadilikabadilika, kikiwa pia na picha nyingi za kutisha.

    “Mbona kipo hivi?”

    “Ndiyo hivyo, utazoea tu baadaye.”

    “Sasa mbona maandishi yanachezacheza na kubadilika.”

    “Kinachochezacheza na kubadilika siyo maandishi, ni akili zako.”

    “Akili zangu?”

    “Ndiyo! Una udhaifu mkubwa kwenye akili zako. Inaonesha una hofu kubwa, hujiamini, umejawa na visasi na chuki ndani ya moyo wako. Huwezi kukitumia hicho kitabu ukiwa katika hali hiyo.”

    “Sasa nitafanyaje mtaalamu?”

    “Kwani Shiwinga hakukufundisha kufanya tahajudi?”

    “Alinifundisha na najua lakini sijafanya kwa kipindi kirefu sana.”

    “Ndiyo maana mambo yako yanakuendea kombo, huwezi kukitumia kitabu cha shetani kama akili yako haijatulia na njia pekee ya kutuliza akili ni kwa kufanya tahajudi,” alisema mganga Kiswigo na kukichukua kile kitabu kutoka kwenye mikono ya baba yake Samantha.

    “Sasa itakuwaje?”

    “Inabidi ufanye kwanza tahajudi kwa dakika thelathini kisha ndiyo mambo mengine yatafuatia,” alisema huku akiinuka na kumuoneshea ishara kwamba aanze kufanya tahajudi kama alivyomuelekeza. Akatoka na kufunga mlango kwa nje, akamuacha baba yake Samantha mle ndani.

    Baba yake Samantha alikaa juu ya ngozi ya mnyama aliyoelekezwa kufanyia tahajudi (meditation), akaikunja miguu na kukaa katika mkao uliomfanya atulie pale chini, akainua shingo katika namna iliyotengeneza nyuzi tisini, mikono akaiweka juu ya mapaja na kubana kidole cha shahada na kidole gumba kwa mikono yote na kugeuzia upande wa juu.

    Baada ya hapo alifumba macho na kuinua kidevu chake kidogo kama anayetazama juu kidogo, akavuta pumzi ndefu kwa kutumia tumbo kisha akazishusha taratibu huku akijitahidi kuelekeza uzingativu wake katika kutuliza akili zake.

    Akawa anayatazama mawazo yanavyoingia na kutoka kwenye kichwa chake kwa kutumia jicho la tatu huku akiendelea kuvuta pumzi ndefu na kuzitoa, akaendelea kutulia na dakika kadhaa baadaye, alikuwa kwenye ulimwengu mwingine kabisa, ubongo wake ukiachia hisia zote mbaya zilizokuwa zimerundikana ndani ya mwili wake.

    Huku nje, mganga alikaa juu ya gogo la mjohoro lililokuwa nje ya nyumba yake huku ndege wengi wa kutisha, wakiwemo bundi na popo wakimzunguka na kupigana vikumbo. Akawa anapiga mbinja na kuongea maneno aliyokuwa anayajua mwenyewe, wale ndege wakaanza kutua mmoja baada ya mwingine pale alipokuwa amekaa.

    Wengine walitua juu ya kofia kubwa ya mkeka aliyokuwa ameivaa, wengine wakatua mabegani na wengine juu ya lile gogo alilokuwa amelikalia, kila mmoja akawa anatoa mlio wake huku akiwa makini kuwasikiliza, akafumba macho na kuendelea kutulia wakati wale ndege wakiendelea kutoa milio ya kutisha.

    Alipokuja kusimama, wale ndege wote walikurupuka na kupotelea kwenye msitu mkubwa uliokuwa umekizunguka kibanda chake, akajinyoosha na kuvua kofia yake ya mkeka, akatingisha kichwa chake na kunguruma kama mnyama wa porini kisha akaingia ndani ya kibanda chake na kugonga kengele kubwa ya kizamani iliyokuwa ukutani, kuashiria mwisho wa tahajudi ya baba yake Samantha.

    “Unajisikiaje?”

    “Najisikia mwepesi sana.”

    “Wakati unafanya tahajudi na mimi nilikuwa nafanya mambo yangu hapo nje, nimegundua kwamba umebadilika sana tangu mara ya mwisho ulivyokuja kwangu. Kwa nini unatumia ushirikina kupata utajiri?” alihoji mganga Kiswigo, kauli iliyoupasua moyo wa baba yake Samantha kama mkuki wenye ncha kali.

    Mara ya mwisho alipofika kwa mganga huyo, baba Samantha alielekezwa kwamba hakuna uchawi mkubwa kama akili zake ambazo kama akizitumia vizuri, zinaweza kumpatia chochote alichokuwa anakitaka maishani mwake lakini baada ya kuondoka, aliamua kutumia njia za mkato kwa kushirikiana na mganga Shiwinga bila mtu yeyote kujua.

    “Hebu niambie kikubwa kilichokuleta. Usinifiche kitu kwa sababu najua kila kitu, nimezisoma fikra zako kwa hiyo ukiwa muongo utakuwa unafanya kosa jingine kubwa sana,” alisema mganga Kiswigo kwa sauti ya kukwaruza. Ikabidi baba yake Samantha awe mkweli.

    “Nimekuwa nikimtumia binti yangu kama chambo cha kupata misukule ya kuniingizia utajiri. Tulimfanyia zindiko kwamba kila mwanaume atakayejaribu kufanya naye mapenzi afe katika mazingira ya kutatanisha kisha tunamgeuza kuwa msukule.

    “Kwa kipindi kirefu nimekuwa nikifanya hivyo, najua ni kinyume na makubaliano yetu, naomba unisamehe sana, Shiwinga ndiye aliyenishawishi kufanya hivyo,” alisema baba yake Samantha huku kijasho chembamba kikimtoka licha ya hali ya hewa ya baridi ya eneo hilo.

    Maelezo hayo ya baba yake Samantha yalisababisha mganga huyo apige chafya mfululizo, hali ya hewa nje ikaanza kubadilika ghafla, wingu zito likaanza kutanda na muda mfupi baadaye, radi kali zilianza kupiga mfululizo na kupasua miti mikubwa iliyokuwa kwenye pori lililozunguka nyumba ya mganga huyo.

    Miti mikubwa minne ilichanwachanwa vibaya na radi hizo na kufuatiwa na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali. Kwa muda wote huo, mganga Kiswigo alikuwa akizungukazunguka mle ndani huku akiendelea kupiga chafya mfululizo, machozi mengi yakimtoka utafikiri mtu aliyekula ugoro mkali.

    Alipokuja kukaa chini na kutulia, ile mvua kubwa ilikoma kunyesha, wingu likayeyuka na kwa mbali kijua kikaanza kuchomoza, baba yake Samantha akawa anaendelea kutetemeka kuliko kawaida.

    “Ninyi ni mashetani, wewe na huyo Shiwinga mnapaswa kuadhibiwa vikali kwa makosa makubwa mliyoyafanya. Una bahati umekuja kukiri kwangu, vinginevyo hizo radi zote zilizoangusha miti huko nje zilikuwa zinakuja kupiga nyumba yako wewe na familia yako mkiwa ndani.

    “Umepatwa na nini mpaka ukawa na tamaa kali kiasi cha kuamua kuhatarisha maisha ya wengine ilimradi wewe ufanikiwe? Katika umri wangu huu, sijawahi kufanya hivyo hata mara moja. Ningeamua kutumia nguvu zangu nilizonazo, huenda ningekuwa tajiri namba moja duniani lakini unafikiri kwa sababu gani sijafanya hivyo?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Na kibaya zaidi, nimegundua kwamba hata safari yako ya kuja huku ilikuwa ni kwa ajili ya kukatisha maisha ya watu wawili, uongo kweli?”

    “Kweli mtaalamu.”

    “Mimi huwa siendekezi watu wa aina yako, nataka watu ambao wanatumia nguvu za akili zao kwa msaada wa elimu mbalimbali kama hicho kitabu cha shetani kujipatia chochote wanachokitaka, siyo kupata utajiri kwa kutoa watu wengine kafara.

    “Sasa kwa adhabu yako, utajiri wako wote utapukutika na utaanza na moja! Utakaa na mimi kwa siku saba, ndani ya hizo, tatu utafukiwa kaburini, mbili utalala juu ya mbuyu na mbili utalala kwenye maji ili kuondoa nguvu zote mbaya zilizokuingia kwa sababu ya tamaa zako. Vinginevyo siku zako kuishi zinahesabika,” alisema mganga Kiswigo na kusababisha baba yake Samantha awe mdogo kama Piriton.

    Zile mbwembwe zote alizokuja nazo ziliyeyuka, ikafikia kipindi akawa anaijutia nafsi yake. Hata hivyo, kwa sababu lengo lake lilikuwa ni utajiri, alijiapiza kuwa liwalo na liwe, hawezi kuacha utajiri wake upotee.

    “Nimekuja na dereva teksi nimemuacha kule nje ya msitu, naomba nikamwambie aondoke tu.”

    “Unataka kunikimbia si ndiyo? Hebu toka nje uangalie jinsi msitu wangu ulivyoharibika kwa sababu ya upumbavu wako. Ukijaribu kutoroka yatakayokukuta utakuwa umejitakia,” alisema mganga huyo huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.

    Baba yake Samantha akatoka nje lakini alichokutana nacho, kilisababisha aingie ndani haraka. Akaingia ndani huku akitweta, hofu kubwa ikiwa imetanda kwenye moyo wake.



    “Nimekwambia usijaribu kunitoroka, mimi huwa sikimbiwi kirahisi kama unavyofikiri. Kama ni huyo dereva wako nimeshatuma vijakazi wangu wakampe taarifa, atakuwa ameshaondoka,” alisema Mganga Kiswigo huku akikaa vizuri.

    Aliendelea kumsema baba yake Samantha kwa ukatili mkubwa aliokuwa anaufanya kwa lengo la kutaka utajiri kwa njia zisizo sahihi, akamsisitiza kwamba atamfanyia dawa kali ambazo endapo akithubutu tena kujipatia utajiri kwa njia kama alizozitumia mwanzo, atakufa kifo kibaya.

    Hakukuwa na muda wa kupoteza, mganga Kiswigo alimuingiza baba yake Samantha kwenye chumba kilichokuwa na giza, akawasha mshumaa na kumuonesha sehemu ya kukaa. Chumba kizima kilikuwa kimejaa tunguli, mafuvu ya wanyama, ngozi, mikia, na mifupa, hali iliyomfanya baba yake Samantha akae kwa wasiwasi mkubwa.

    “Jambo la kwanza inabidi kwanza unyolewe hizonywele zako,” alisema mganga huyo huku akichukua kisu kikali na kuanza kukinoa kwenye jiwe lililokuwa ndani ya chumba hicho, akatoka nje na aliporejea, alikuwa na bakuli la bati lenye maji ndani yake.

    Akachanganya na dawa nyeusi ya ungaunga kisha akamwambia baba yake Samantha ajisafishe kichwa chake. Akamuelekeza namnaya kukaa na muda mfupi baadaye, kazi ya kumnyoa nywele ilianza. Kwa ustadi mkubwa, mganga Kiswigo alimnyoa nywele zote baba yake Samantha, kichwa kizima. Baada ya kumaliza kumnyoa alimpaka dawa nyingine ya maji na kumalizia kumpaka nyingine ya unga.

    Akatoka kwenda kwenye chumba kinginena kumuacha baba yake Samantha mle ndani, muda mfupi baadaye alirejea akiwa na kimkoba kidogo, akakiweka chini, mbele ya baba yake Samantha na kukifungua.

    ***

    “Kwani baba yako ameenda wapi? Mbona ananiweka roho juu jamani?”

    “Siyo kwamba mimi ndiyo nilitakiwa nikuulize wewe? Mimi niko hospitalini nitajuaje alikoenda? Kwani si mlilala pamoja mama?”

    “Ndiyo tulilala pamoja lakini asubuhi wakati naamka nilishtukia mwenzangu akiwa ameshaondoka.”

    “Umejaribu kumpigia simu?”

    “Hapatikani hewani, yaani nachanganyikiwa mwenzenu basi tu.”

    “Ukimuuliza mlinzi anasemaje?”

    “Anasema aliondoka alfajiri na dereva wake.”

    “Na huyo dereva ukimuuliza anasemaje?”

    “Anasema alimpeleka mjini na kumuacha huko,” mama yake Samantha alikuwa akijadiliana na mwanaye wakiwa kwenye wodi aliyolazwa Samantha. Tofauti na alivyotegemea, Samantha alizipokea taarifa hizo kwa hisia tofauti kabisa, akajua ule muda aliokuwa anausubiri umewadia.

    Mama yake alipotoka kwenda kumnunulia matunda baada ya kuwa ameshakula chakula cha mchana, harakaharaka alimgeukia Edmund ambaye muda wote alikuwa amekaa kimya, akiwaza yake.

    “Umesikia mama alichokuwa ananiambia?”

    “Nimesikia vizuri.”

    “Wewe unasemaje?”

    “Nasemaje kuhusu nini mpenzi wangu!”

    “Ninavyomjua baba, akiondoka bila kuaga kama hivi, anaweza kukaa hata siku mbili au tatu bila kurudi nyumbani. Kwa vyovyote atakuwa ameenda kwa waganga wake, unaonaje tutumie nafasi hii kutoroka?”

    “Mh! Si tulishazungumza mpenzi wangu? Huonikama ni hatari sana? Isitoshe wewe bado hujapona.”

    “Hakuna cha hatari, please usiniangushe Edmund, mbona unakuwa kama siyo mwanaume?” alisema Samantha, kauli iliyomfanya Edmund ajiinamie kwa sekunde kadhaa, akatafakari kwa kina na alipoinuka, alimtazama Samantha usoni.

    “Vipi umeamua nini?”

    “Japokuwa ni hatari, nipo tayari kufanya chochote utakachosema mpenzi wangu, sitaki kukuangusha,” alisema Edmund, kauli iliyomfurahisha sanaSamantha, akatanua mikono yake kama ishara ya kumtaka Edmund amkumbatie, naye akafanya hivyo. Wakakumbatiana kwa nguvu huku msichana huyo akimbusu Edmund sehemu mbalimbali.

    “Vipi kuhusu mama?”

    “Hatakiwi kujua chochote kwa sasa, anaweza kutuharibia mipango yetu.”

    “Na vipi kuhusu huo mguu wako.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Utapona mbele ya safari, hapa cha kufanya ni kuchonga dili na daktari wangu anayenitibu aturuhusu kuondoka, mengine tutajua mbele ya safari,” alisema Samantha huku akigeuka hukuna kule kuangalia kama hakuna mtu aliyekuwa anawasikiliza.

    Baada ya kukubaliana, bila kupoteza muda Samantha alichukua simu yake na kuanza kuzungumza na mhasibu wao.

    “Naomba uende benki ukahamishe shilingi milioni ishirini kutoka kwenye akaunti ya kampuni na kuniingizia kwenye akaunti yangu ya Barclays, nina shida nazo haraka.”

    “Lakini mzee alisema kwa fedha nyingi kiasi hicho ni lazima aidhinishe mwenyewe.”

    “Hebu nisikilize ninachokwambia. Nimeshaongea naye na yeye ndiyo ameniambia nifanye hivyo, kuna dharura,” alisema Samantha, mhasibu huyo akamuitikia na kuanza utekelezaji wa alichoambiwa mara moja.

    “Akituhamishia hizo fedha, nikichanganya na zilizopo kwenye akaunti zangu nyingine, zitafika karibu shilingi milioni hamsini. Si zinatutosha kabisa kuanza maisha?” alisema msichana huyo, Edmund akawa anatingisha kichwa kuonesha kukubaliana na alichokisema Samantha huku akilini mwake akishangaa jinsi msichana huyo alivyokuwa akizungumzia kiasi kikubwa namna hiyo cha pesa kirahisi utafikiri anazungumzia fedha za kawaida kabisa.

    “Milioni hamsini? Sijawahi kufikiria hata siku moja kwamba naweza kushika kiasi hicho cha fedha,” aliwaza Edmund. Kama walivyokubaliana, Samantha aliomba kuonana na daktariwake ambapo alipofika, alimueleza mpango wake na kumtaka awasaidie.

    Alipotangaziwa dau la fedha tu, daktari huyo alikubali na kuahidi kuifanya kazi hiyo siku hiyohiyo kwa usiri mkubwa. Akiwa hana hili wala lile, mama yake Samantha alirejea wodini akiwa na matunda, akamuandalia mwanaye huku akiendelea kulalamika kuhusu ishu ya mumewe kuondoka bila kumuaga.

    Ilipofika jioni, aliaga na kuondoka kwa makubaliano kwamba atakuja tena asubuhi, akamuacha Samantha mikononi mwa Edmund huku akisisitiza kwamba kama kutatokea tatizo lolote, ampigie simu haraka.

    Alipoondoka tu, harakaharaka mipango ilianza kufanywa, yule daktari akaingia wodini akiwa ameongozanana manesi wawiliwaliokuwa wakisukuma kiti cha magurudumu (wheel chair), wakasaidiana kumkalisha Samantha huku Edmund akikusanya vitu vyake.

    Alipomaliza, walitoka mpaka kwenye maegesho ya magari ya kubebea wagonjwa, wakaingia kwenye ambulance ambayo tayari ilishaandaliwa. Muda mfupi baadaye, ambulance hiyo ilitoka hospitalini hapo ikipiga ving’ora, kila mtu akiamini kwamba ndani yake kulikuwa na mgonjwa aliyezidiwa, aliyekuwa akihamishwa na kupelekwa kwenye hospitali kubwa.



    Breki ya kwanza ilikuwa ni Ubungo Maziwa, gari la kubebea wagonjwa likaiacha Barabara ya Morogoro na kuingia ndanindani mpaka kwenye hoteli moja ya kifahari iitwayo Highway View iliyokuwa eneo hilo.

    Gari likaingia mpaka ndani ambapo Edmund kwa kusaidiana na wahudumu wa hoteli hiyo walisaidiana kumteremsha Samantha na kumuingiza hadi mapokezi. Harakaharaka Edmund alitoa fedha za kumlipa dereva wa ambulance na muda mfupi baadaye, gari hilo likaondoka.

    “Tunataka chumba, kesho asubuhi tunasafiri kwenda mkoani kwa hiyo tumeamua kuja hapa kwa sababu ni jirani na stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani,” Edmund alijieleza pale mapokezi.

    Harakaharaka wakapewa chumba kilichokuwa ghorofa ya chini kabisa, jirani na mlango mkubwa wa kutokea ili isiwe tabu wakati wa kuingia na kutoka kwa sababu bado Samantha alikuwa akitumia kiti cha magurudumu. Baada ya kukamilisha kila kitu, wawili hao waliingia mpaka chumbani.

    “Siamini kama tumefanikiwa kuondoka kilaini kiasi hiki,” alisema Samantha huku akitanua mikono yake kama ishara ya kutaka kumkumbatia Edmund ambaye naye alisomgelea na kumkumbatia msichana huyomrembo, wakagandana kama ruba kwa dakika kadhaa.

    Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda, wawili hao waliagiza chakula ambacho kililetwa na wahudumu wa hoteli hiyo, wakala huku wakiendelea kupiga stori za hapa na pale, kila mmoja akionesha kuwana furaha kubwa ndani ya moyo wake.

    Baada ya kumaliza kula, Edmund alienda kumuogesha Samantha kwani bado hakuwa na uwezo wa kuoga mwenyewe kisha akamrudisha kitandani na kumlaza vizuri. Naye akaenda kuoga na muda mfupi baadaye, wote wawili walikuwa kitandani.

    “Edmund, utaendelea kunidekeza hivihivi hata ukinioa au ndiyo unaniektia?” Samantha alihoji akiwa amelala juu ya kifua cha Edmund aliyekuwa amemkumbatia kimahaba.

    “Nitakupenda na kukudekeza siku zote za maisha yangu, siyo leo na kesho tu, bali katika siku zote za uhai wangu, kifo ndiyo kitakachotutenganisha,” alisema Edmund na kumbusu msichana huyo mdomoni, kauli iliyomfurahisha sana.

    Waliendelea na mazungumzo yao, wakawa wanapanga mipango ya safari yao na jinsi watakavyoenda kuyaanza maisha mapya.

    “Nina marafiki zangu wengi Arusha, na tayari nimeshamwambia mmoja atutafutie nyumba ya kupanga maeneo ya Njiro, unajua kuishi hotelini ni gharama sana,” alisema Arianna, wazo ambalo Edmund alikubaliana nalo, moyoni akawa anajipongeza kwani Samantha alionesha kuwa na akili za kimaendeleo sana.

    Baadaye walipitiwa na usingizi wakiwa wamekumbatiana kimahaba mpaka alfajiri ya siku ya pili walipokuja kugongewa mlango na wahudumu wa hoteli hiyo kama walivyokuwa wamewaomba. Harakaharaka Edmund aliamka na kuanza kumuandaa Samantha, akaenda kumuogesha na kumvalisha nguo nzuri, na yeye akaoga na muda mfupi baadaye alitoka kwenda kutafuta teksi.

    Dakika kadhaa baadaye, alirudi na teksi, wakasaidiana na dereva wa teksi pamoja na wahudumu wa hoteli hiyo kumtoa Samantha na kwenda kumpakiza kwenye teksi hiyo, wakaaga na kuondoka kuelekea kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani cha Ubungo.

    Baada ya kulipa nauli na kupewa tiketi, Samantha alipandishwa na kwenda kukalishwa kwenye siti yake, Edmund akasimamia mizigo yao yote nayo ikapakizwa kisha akaenda kukaa pembeni ya Samantha, ndani ya basi jipya na la kisasa la Dar Express. Wakawa wanasubiri muda wa basi kuondoka.

    ***CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kupambazuka, mama yake Samantha aliwahi kuamka kama kawaida yake, akasaidiana na msichana wake wa kazi kuandaa kifungua kinywa kwa ajili ya mwanaye na Edmund. Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa ndani ya gari akiwa na dereva wao, wakawa wanaelekea hospitalini alikolazwa Samantha.

    Walipofika hospitalini, aliteremsha mizigo yake na kuelekea mapokezi moja kwa moja, akamsalimia nesi aliyemkuta kisha akawa anaongoza kwenye korido ya kuelekea kwenye wodi aliyolazwa mwanaye.

    “Mh! Mama samahani mara moja,” nesi aliyekuwa mapokezi alimuita mama yake Samantha baada ya kuona kuna jambo halikuwa sawa. Kwa jinsi alivyokuwa anafahamu, ni kwamba mgonjwa wake tayari alikuwa ameruhusiwa kutoka usiku uliopita, akashangaa kumuona akileta kifungua kinywa wakati hakukuwa na mtu wodini.

    “Ameruhusiwa? Ameruhusiwa na nani na ameenda wapi? Mbona mimi natokea nyumbani sasa hivi, isitoshe mwanangu bado hajapona, nani aliyemruhusu?” alihoji mama yake Samantha huku akionesha kuchanganyikiwa kabisa.

    Hakutaka kuamini maneno yanesi huyo, alitaka kuhakikisha mwenyewe, akaenda mpaka kwenye wodi aliyokuwa amelazwa mwanaye, alipofungua mlango na kutazama ndani, mapigo ya moyo wake yalimlipuka mno baada ya kuamini kwamba ni kweli alichoambiwa.

    “Msitake kunitania, nitawafunga nyote nyie, hivi mnanijua au mnanisikia? Namtaka mwanangu,” alisema mwanamke huyo na kusababisha vurumai kubwa hospitalini hapo, hali ya sintofahamu ikatanda.

    Kwa bahati nzuri, muda mfupi baadaye mganga mkuu wa hospitali hiyo aliwasili, akashangaa kukuta vurumai kubwa hospitalini kwake, ikabidi amuite mama yake Samantha ofisini kwake kwa lengo la kutaka kufahamu kilichotokea.

    Baada ya kumueleza kilichotokea, ufuatiliaji ulianza kufanyika haraka ambapo baadaye ilifahamika kwamba msichana huyo aliruhusiwa kimakosa baada ya kula njama na mmoja wa madaktari hospitalini hapo na dereva wa ambulance.

    Ilibidi taarifa zitolewe polisi haraka, dakika kadhaa baadaye, askari kadhaa wakiwa kwenye difenda walifika hospitalini hapo na kumuweka chini ya ulinzi daktari aliyehusika kumtorosha Samantha pamoja na dereva wa ambulance. Baada ya kubanwa, ilibidi waeleze ukweli wa mahali walikowapeleka Samantha na Edmund. Hakukuwana muda wa kupoteza, wale askari wakatoka na difenda yao, wakiwa na yule daktari, dereva wa ambulance, mganga mkuu na mama yake Samantha kuelekea Ubungo Maziwa kwenye hoteli wawili hao walikopelekwa.

    Njia nzima mama yake Samantha alikuwa akijaribu kupiga simu ya mwanaye ambayo ilionesha kwamba imezimwa, hata alipopiga ya Edmund majibu yalikuwa ni yaleyale. Alipompigia mumewe, naye hakuwa akipatikana hewani na hakuwa na taarifa zozote za mahali alikoenda kwani aliondoka nyumbani bila kuaga. Mwanamke huyoakazidi kuchanganyikiwa, machozi yakawa yanamtoka kama mtoto mdogo.

    Walipofika hotelini hapo, wahudumu pamoja na meneja wa hoteli waliwataarifu kwamba wawili hao wameondoka muda mfupi uliopita kuelekea stendi ya mabasi ya Ubungo lakini hawakuwa wakijua wanasafiri kuelekea wapi.

    “Mungu wangu, wameamua kutorokea wapi? Nitamjibu nini mume wangu?” alisema mama yake Samantha huku akiwahimiza wale askari kuwahi stendi ya mabasi ya Ubungo kama wanaweza kuwakuta wakiwa bado hawajaondoka. Difenda iligeuzwa na kwa kasi kubwa safari ya kuelekea stendi ikaanza. Kwa kuwa hapakuwa na umbali mrefu, dakika chache baadaye tayari walishawasili kituoni hapo.



    Licha ya askari kujitahidi kufika haraka kwenye Stendi ya Mabasi, Ubungo, hawakufanikiwa kuwapata Samantha na Edmund kwani tayari basi walilokuwa wamepanda, lilishaondoka muda mfupi kabla askari hao hawajafika.

    Kazi kubwa waliyoifanya yakuzuia mabasi yote yasiondoke na kuanza kukagua moja baada ya jingine, haikuzaa matunda zaidi ya kusababisha usumbufu kwa abiria wengine waliokuwa wakitaka kusafiri asubuhi hiyo.

    “Tumejitahidikadiri ya uwezo wetu lakini wewe mwenyewe ni shahidi, hatujawapata,” askari aliyeonesha kuwa na mamlaka kuliko wenzake, alimwambia mama yake Samantha ambaye muda wote alikuwa akilia kama mtoto mdogo.

    ***

    Basi liliendelea kuchanja mbuga kwa kasi kubwa kuelekea Arusha huku Edmund na Samantha wakipiga stori za hapa na pale na kucheka kwa furaha. Hakuna aliyeamini kwamba walifanikiwa kuondoka kirahisi namna ile.

    “Nataka nikipona mguu tu nikubebee mimba, hata wakija kugundua tupo wapi watakuwa wamechelewa sana maana tayari nitakuwa na kiumbe chako tumboni mwangu,” alisema Samantha huku akilishika tumbo lake, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

    Baada ya safari ndefu, hatimaye waliwasili Arusha, wakatafuta hoteli nzuri kwa ajili ya mapumziko wakati wakiendelea na taratibu za kutafuta chumba cha kupanga.

    “Nadhani huu ni muda muafaka wa kuzungumza na mama ili asiendelee kuwa na wasiwasi, washa simu yako basi umpigie,” alisema Edmund, wazo ambalo msichana huyo alilikubali. Ile anawasha tu simu yake, meseji nyingi zilianza kuingia mfululizo na kabla hata hajajua aanze kuisoma ipi, simu ilianza kuita. Alipotazama namba ya mpigaji, hakuwa mwingine bali mama yake.

    “Huyo anapiga,” alisema Samantha na kushusha pumzi ndefu, akaipokea. Kitu cha kwanza alichokutana nacho ilikuwa ni sauti ya kilio ya mama yake.

    “Samantha uko wapi mwanangu? Uko salama? Angalia mama yako ninavyolia kama mtoto mdogo, nielekeze mahali ulipo nakuja kukuchukua sasa hivi,” alisema mama yake Samantha bila kuweka nukta, ikabidi Samantha amueleze kwamba yupo salama ingawa hataweza kurudi nyumbani.

    Alimueleza kwa kirefu kwamba yupo na Edmund na wameamua kutoroka ili kumkwepa baba yake ambaye alikuwa akiwakosesha raha. Akamuomba msamaha mama yake kwa kuondoka bila kutoa taarifa na kumsababishia usumbufu mkubwa kiasi hicho.

    “Unataka baba yako aniue? Unafikiri nitamwambia nini?” alihoji mama yake Samantha, wakaendelea kuzungumza kwa muda mrefu huku akimsisitiza mwanaye huyo kurudi lakini haikusaidia kitu.

    Mpaka simu inakatwa, hawakuwa wamefikia muafaka zaidi ya Samantha kuendelea kushikilia msimamo wake kwamba hayupo tayari kurejea nyumbani kwa kipindi hicho.

    ***

    Baada ya kukosa mbinu za kutoroka, ilibidi baba yake Samantha awe mpole, akakubali kufuata maelekezo ya Mganga Kiswigo ambapo jambo la kwanza alinyolewa nywele zote kwa kutumia kitu kikali, akapakwa mafuta maalum yaliyosababisha kichwa chake kiwe kinang’aa sana.

    Baada ya hapo, akaondoka na mganga huyo nakuingia kwenye msitu mkubwa uliokuwa jirani na nyumba yamganga huyo, miti mingi ikiwa imechanwachanwa na radi, huku maeneo mengine maji yakiwa yanaendelea kumiminika kwani haukupita muda mrefu tangu mvua ikatike.

    Inatakiwa tuchimbe kaburi hapa kufuata usawa huu,” alisema mganga Kiswigo huku akimuonesha baba yake Samantha kwa vitendo. Bila kupoteza muda, mganga akazama kichakani na muda mfupi baadaye aliporejea, alikuwa na jembe, sululu na koleo, kazi ya kuchimba kaburi ikaanza mara moja huku baba yake Samantha akiendelea kujiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.

    “Kwani hili kaburi tunachimba la nini?”

    “Nimeshakwambia utalala kaburini kwa siku tatu, hili ni lako.”

    “Nilale kaburini? Kivipi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Utajua tu, tuendelee kwanza na kazi, maswali siyo muda wake huu,” alisema mganga Kiswigo na kazi ya kuchimba kaburi ikaendelea huku baba yake Samantha akionesha kukosa raha kabisa.

    Baada ya kumaliza kuchimba kaburi lililokuwa na urefu wa futikadhaa kwenda chini, wanaume wawili waliokuwa wamebeba jeneza lililofunikwa kwa shuka jeupe, walichomoza kutoka vichakani huku wakiimba nyimbo ambazo baba yake Samantha hakuzielewa. Kitendo cha kuwaona watu hao, kilimshtua mno baba yake Samantha kwani aliamini wapo wawili tu, yeye na mganga Kiswigo ndani ya msitu huo.

    Watu hao walisogea mpaka pale jirani yao na kulishusha lile jeneza, wakaliweka pembeni ya kaburi kisha wote wakainama kama ishara ya adabu kwa mganga Kiswigo ambaye naye alizungumza maneno ambayo baba Samantha hakuyaelewa, akashtukia wote wakimzunguka.

    “Inabidi ujikaze kwa sababu haya mambo umeyasababisha wewe mwenyewe,” alisema mganga Kiswigo huku akifungua kichupa kilichokuwa na dawa nyeusi, akamimina kidogo mkononi kisha akamsogelea baba yake Samantha ambaye bado hakuwa akielewa kinachotaka kutokea.

    Akampulizia usoni na muda mfupi baadaye, akadondoka chini kama mzigo, akiwa amepoteza fahamu. Alipokuja kuzinduka, alijikuta akiwa ndani ya jeneza, akaanza kugongagonga mbao za jeneza hilo na kupiga kelele za kuomba msaada lakini hakuna aliyemsikia.

    Joto kali na hewa nzito vilivyokuwepo eneo hilo, vilimfanya aamini kwamba mganga Kiswigo ametimiza alichokisema kwa kumzika akiwa hai. Alipokumbuka kwamba mganga huyo alimwambia atakaa humo kwa siku tatu, alizidi kuchanganyikiwa, akawa anakiona kifo mbele yake.

    Alilia sana kila alipokuwa akifikiria hatima ya maisha yake. Ni kweli alikuwa akiupenda utajiri lakini kilichokuwa kinamtokea, aliona kama kimemzidi uwezo. Akiwa anaendelea kulia, alisikia vishindo kwa mbali vikisogea mahali pale, akatulia na kuanza kuvisikilizia. Vishindo vikawa vinazidi kuongezeka mpaka jirani kabisa na pale alipokuwa.

    “Msaada! Jamani msaada nakufa, nisaidieni,” baba yake Samantha alianza tena kupiga kelele huku akipigapiga mbao za jeneza lile. Kwa mbali akaanza kusikia kama lile kaburi alilokuwa amezikwa ndani yake, linaanza kufukuliwa. Akawa anasikia vishindo vya hapa na pale, jambo lililompa matumaini makubwa kwamba hatimaye alikuwa anaenda kuokolewa.



    Tofauti na mategemeo yake, baada ya vishindo vya muda mrefu, hatimaye jeneza alilokuwa amelazwa ndani yake lilifunguliwa upande wa kichwani, hali iliyompa upenyo wa kutazama nje ingawabado hakuweza kutoka.

    Mganga Kiswigo, akiwa amejifunga nguo nyeupe mwili mzima, alimuinamia babayake Samantha pale ndani ya jeneza, akatoa kibuyu na kuanza kukitingisha kwa nguvu kisha akakifungua na kujimimia unga mweusi kiganjani.

    Akawa ni kama ananuiza maneno ambayo baba yake Samantha hakuyaelewa kisha baada ya hapo akampulizia ule unga usoni. Kama ilivyokuwamara ya kwanza, ndani ya sekunde chache tu, baba Samantha alijikuta akipitiwa na usingizi mzito, kwa mbali akasikia jeneza likifungwa tena na kufuatiwa na vishindo vya udongo, kuonesha kuwa alikuwa akifukiwa tena kwa mara nyingine.

    ***

    Mpaka simu inakatwa, Samantha na mama yake hawakuwa wamefikia muafaka zaidi ya msichana huyo kuendelea kushikilia msimamo wake kwamba hayupo tayari kurejea nyumbani kwao, jijini Dar es Salaam kwa kipindi hicho.

    “Vipi anasemaje?”

    “Anasema turudi nyumbani, eti baba hatamuelewa halafu anaonekana ananihofia sana mimi kwa sababu ya huu mguu.”

    “Mama yako anakupenda sana, hataki upate shida hata kidogo.”

    “Sasa kwani mimi hapa napata shida? Nikiwa nyumbani ndiyo napata shida.”

    “Lakini unajua kama mzazi atakuwa anajisikia vibaya sana, unaonaje ukinipa simu ili niongee naye na kumtoa wasiwasi?”

    “Mh! Unafikiri itasaidia chochote?”

    “Itasaidia, naamini itasaidia,” alisema Edmund kwakujiamini, hali iliyomfanya Samantha akose cha kujibu zaidi ya kumpa simu yake. Muda mfupi baadaye, Edmund alikuwa akizungumza na mama yake Samantha ambaye bado alikuwa akilia kwa uchungu.

    “Wewe ndiyo umemtorosha mwanangu Edmund, si ndiyo?”

    “Siyo hivyo mama, nakuomba unielewe, nipo chini ya miguu yako ndiyo maana nimeona nikupigie nizungumze na wewe moja kwa moja.”

    “Uzungumze ninina mimi Edmund? Nilikuamini nikakuacha na mwanangu kumbe mlikuwa mnapanga kutoroka?”

    “Lakini mama…”

    “Lakini nini Edmund?”

    “Samantha yupo kwenye mikono salama.”

    “Mikono salama ipi? Hujui huyo bado hajapona huo mguu? Unataka uoze?”

    “Hapana, nitahakikisha anapata huduma zote za kimatibabu kila siku mpaka apone. Nakuahidi nitamtunza na kumlea kama ulivyokuwa unafanya wewe wala usiwe na wasiwasi, kama kukitokea tatizo lolote nitakuwa wa kwanza kukutaarifu,” alisema Edmund kwa busara, kauli ambayo kidogo ilimtuliza mama yake Samantha.

    “Kama ni hivyo naomba msizime simu ili muda wowote nitakaohitaji kuzungumza nanyi muwe mnapatikana.”

    “Hakuna tatizo mama,” alijibu Edmund kisha akakata simu. Samantha ambaye muda wote alikuwa amejilaza pembeni akimsikiliza Edmund, aliachia tabasamu pana na kutanua mikono yake kama ishara ya kutaka kumkumbatia, naye akamuonesha ushirikiano.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unajua mwenzio mimi wazazi wangu hawataki kuamini kwamba nimeshakuwa mkubwa na nahitaji kuwana maisha yangu, mpaka leo wananiona kama mtoto mdogo,” alisema Samantha na kumbusu Edmund mdomoni.

    Akaendelea kumshukuru kwa jinsi alivyoweza kuzungumza na mama yake na kumtoa wasiwasi.

    “Usiwe na wasiwasi mpenzi wangu, niliahidi nitakulinda na lazima nikuoneshe kwa vitendo.”

    Siku hiyo ilipita, kesho yake mipango ya kutafuta chumba cha kupanga ikaanza kufanywa. Kwa kuwatumiamarafiki zake waliokuwa wakiishi jijini Arusha, kazi ilikuwa nyepesi kwani walifanikiwa kupata nyumba yenye vyumba vitatu, sebule, jiko na vyoo vya ndani (self container) iliyokuwakwenye mtaa tulivu wa Njiro.

    Japokuwa kodi ilikuwa kubwa, Edmund na Samantha walilipa bila tatizo kwa sababu fedha walizoondoka nazo jijini Dar es Salaam zilikuwa zikiwatosha. Kilichofuatia ilikuwani kununua samani za ndani, kazi ambayo ilibidi ifanywe na Edmund kwa sababu Samantha hakuwa na uwezo wa kuzunguka huku na kule kutokana na jeraha la risasi mguuni kwake.

    Siku mbili baadaye, nyumba ilikuwa imekamilika kwa kila kitu, kuanzia sebuleni, jikoni mpaka chumbani. Ungeweza kudhani waliokuwa wanaishi ndani ya nyumba hiyo ni vigogo fulani serikalini kwa jinsi nyumba ilivyokuwa na mandhari nzuri kuanzia nje mpaka ndani.

    Kama alivyokuwa ameahidi, Edmund alihakikisha anatafuta daktari maalum ambaye kila siku alikuwa akienda kumsafisha Samantha kidonda na kumpa dawa zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kumponesha kidonda chake.

    “Ukiendelea hivi itabidi wiki ijayo nianze kukufanyisha mazoezi ya kutembea, unapona kwa haraka sana,” alisema daktari baada ya kumaliza kumsafisha Samantha jeraha lake, kauli iliyowafurahisha mno wote wawili. Hakuna kitu ambacho Edmund alikuwa akitamani kuona kinatokea kama Samantha kupona na kuwa kama zamani.

    “Ahsante Edmund kwa kunihudumia vizuri, najua hata mama siku akiniona ninavyopona kwa spidi atapunguza munkari wake,” alisema Samantha wakati akisaidiana na Edmund kuandaa chakula cha jioni. Japokuwa Edmund alikuwa nimwanaume, alikuwa akiweza kufanya shughuli zote za jikoni, kuanzia kwenda sokoni, kupika, kuosha vyombo na kufanya usafi, jambo lililomfanya Samantha azidi kuchanganyikiwa na penzi lake.

    “Siku zote nilikuwa na ndoto za kuishi maisha kama haya, nakupenda sana Edmund, sijawahi kudhani kwamba naweza kuja kumpenda mwanaume kiasi hiki.

    “Yaani siku chache tu nilizokaa na wewe huku mbali, najihisi kama nipo peponi,” alisema Samantha kwa hisia, wakiwa wamejilaza kitandani kwao baada ya kumaliza kula chakula cha usiku, Edmund akaachia tabasamu pana na kumbusu Samantha.

    Wakiwa wanaendelea na mazungumzo ya hapa na pale, simu ya Samantha ilianza kuita, harakaharaka msichanahuyo akaipokea na kuiweka ‘loud speaker’. Alikuwa ni mama yake Samantha na alichokisema, kilisababisha wote wawili wabakiwamepigwa na butwaa, wakiwa ni kama hawaamini wanachokisikia.



    “Watu kutoka serikalini wamekuja hapa nyumbani wanamsaka baba yako kwa udina uvumba. Wanasema wana mashaka na namna alivyopata utajiri wake na kuanzia leo wamezifungia akaunti zake za benki pamoja na kushikilia mali zote anazomiliki na kuna uwezekano mkubwa wakazitaifisha.

    “Kibaya zaidi mwenyewe mpaka leo hajarudi na haifahamiki yuko wapi, nahisi kuchanganyikiwa,” alisema mama yake Samantha kwa sauti iliyoonesha dhahiri kwamba alikuwa akilia.

    Kwa kuwa simu ilikuwa imewekwa loudspeaker, Edmund naye alisikia kila kitu, akabaki amepigwa na butwaa akiwa ni kama haamini alichokisikia. Baada ya kumaliza kueleza, mama yake Samantha alikata simu na kuwaacha wawili hao wakitazamana kama sanamu.

    “Lakini mimi nilikuwa namwambia baba, haya mambo ya kujipatia utajiri kwa njia zisizo halali mwisho wake huwa siyo mzuri akawa mbishi, sasa hata sijui itakuwaje,” alisema Samantha huku akionesha kuchanganyikiwa.

    “Usijali kuhusu utajiri wa baba yako, hayo ni makosa ambayo aliyafanya mwenyewe, cha msingi sisi tuangalie namna ya kujenga maisha yetu na kupata pesa kwa njia za halali.”

    “Yaani hata hizi pesa tulizoondoka nazo naona kama zinatuletea tu mkosi, natamani tuzipeleke kanisani au msikitini tukatoe sadaka,” alisema Samantha, mjadala ukaendelea kwa muda mrefu na mwisho wakakubaliana kwamba waendelee kuzitumia kuendeshea maisha yao wakati wakitafuta njia nyingine za kupata pesa kwa njia ya halali kisha baada ya hapo ndiyo wataamua nini cha kufanya.

    ***

    Kama mganga Kiswigo alivyomwambia awali baba yake Samantha, kweli siku tatu ziliisha huku akiwa kaburini, jambo ambalo hakuwahi kulihisi hata mara moja kwamba linaweza kumtokea.

    Baada ya siku hizo tatu kuisha, mganga Kiswigo akiwa na wasaidizi wake walienda kufukua kaburi alilokuwa amefukiwa baba yake Samantha na kumtoa. Kutokana na dawa kali alizokuwa akipuliziwa kila alipokuwa akirejewa na fahamu, ukichanganya na njaa ya kutokula chochote kwa siku tatu mfululizo na kukosa hewa safi, babayake Samantha alikuwa hajitambui.

    Baada ya kufukua kaburi, walilitoa jeneza alilokuwa amelazwa ndani yake na kulifungua, wakamtoa na kumvua sanda aliyokuwa amefungwa kama maiti, akabebwa kwenye machela ya miti na kupelekwa mpaka nyumbani kwa mganga Kiswigo akiwa bado hajitambui.

    Akaanza kuogeshwa kwa maji yaliyochanganywa na dawa kisha nyingine akanyweshwa ambapo muda mfupi baadaye, alianza kupiga chafya mfululizo na kuzinduka, akawa anashangaa pale ni wapi na amefikaje.

    “Kunywa hii upate nguvu,” alisema mganga Kiswigo na kumsaidia kuinuka, akaegamia ukuta na kupewa bakuli lililokuwa na mchuzi uliochanganywa na dawa. Baada ya kunywa, angalau alipata nguvu za kuweza kuzungumza.

    “Leo ni lini?”

    “Jumatatu.”

    “Kwa hiyo nimekaa kaburini siku tatu?”

    “Ndiyo, si nilikwambia tangu mapema? Bado siku nyingine mbili za kulala juu ya mbuyu na nyingine mbili za kulala kwenye maji. Ulikuwa na nguvu mbaya sana ndani ya mwili wako kwa sababu ya uovu ulioufanya. Narudia tena kukuonya, ukirudia kufanya uliyoyafanya ujue kaburi linakuita,” alisema mganga Kiswigo huku akiendelea kumuandalia dawa nyingine.

    Siku tatu tu alizokaa kaburini, zilitosha kumbadilisha kabisa baba yake Samantha, alidhoofika na kuwa mtu tofauti kabisa. Baada ya kumaliza kunywa mchuzi ule, aliandaliwa chakula chepesi na wasaidizi wa mganga huyo, akawa anakula harakaharaka utafikiri anafukuzwa kutokana na jinsi alivyokuwa na njaa kali.

    Baada ya kumaliza kula, aliendelea kupewa dawa ambazo taratibu zilikuwa zikimrejeshea nguvu zake mpaka giza lilipoingia.

    “Inabidi ujiandae kama nilivyokwambia, kwa siku mbili hizi utalala juu ya ule mbuyu mkubwa kule porini, inabidi ujikaze ili tumalize kazi, hakuna njia nyingine,” alisema mganga Kiswigo na kumfanya baba yake Samantha akose cha kujibu.

    Kuna wakati mwingine alikuwa akijilaumu sana kwa makosa makubwa aliyoyafanya wakati wa harakahati zake za kusaka utajiri kwa njia ya ushirikina. Wakati mwingine aliona kama hata mateso aliyokuwa anapitia alistahili kutokana na dhambi zake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye muda wa kwenda kulala uliwadia ambapo kama ilivyokuwa kwa siku kadhaa nyuma, mganga huyo alimpulizia dawa maalum usoni na kusababisha alegee kisha kupoteza fahamu.

    Alikuja kuzinduka kukiwa tayari kumeanza kupambazuka na kujikuta akiwa amelala juu ya tawi kubwa la mbuyu. Alipotazama chini, almanusra aanguke kwa mshtuko kwani alikuwa kwenye umbali mrefu ambao hakujua amepandaje, akawa anajiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.

    Muda ulizidi kuyoyoma, jua likachomoza kabisa lakini hakukuwana dalili za mtu yeyote kuja kumshusha, hata alipotazama chini, hakuwa na uwezekano wowote wa kuteremka, muda ukawa unazidi kuyoyoma huku njaa na kiu vikimtesa baba yake Samantha.

    Hatimaye siku hiyo ilipita akiwa bado juu ya mti, usiku wa pili ukamkuta akiwa palepale. Kutokana na hofu kubwa ya kuanguka aliyokuwa nayo, usiku kucha hakulala mpaka majira ya kumi na moja alfajiri ya siku iliyofuata ambapo alijikuta akizidiwa na usingizi na kujilaza kidogo.

    Alipokuja kuzinduka kukiwa tayari kumeshapambazuka kabisa, alijikuta akiwa ndani ya nyumba ya tembe ya mganga Kiswigo, akabaki akijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.

    “Nadhani kila kitu kinaenda vizuri, bado zoezi la mwisho ambalo siyo gumu kama haya yaliyopita, mambo yakienda vizuri keshokutwa nitakuruhusu uondoke lakini narudia kukusisitiza kwamba utakachokutana nacho nyumbani kwako kisikushangaze, unatakiwa kwenda kuanza upya kabisa, utajiri wa kishirikina hauna nafasi tena na mali zote ulizozipata kwa njia ya kishirikina zitayeyuka na kukuacha ukiwa huna kitu,” alisema mganga Kiswigo, baba yake Samantha akawa anatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye.



    Siku zilizidi kuyoyoma na hatimaye baba yake Samantha akamaliza dozi ya nguvu aliyopewa na mganga Kiswigo. Ndani ya wiki moja tu, mwili wake ulikuwa umepukutika na kupungua uzito kwa kasi kikubwa. Ukichanganya na nywele alizonyolewa na mganga huyo, isingekuwa rahisi kwa mtu anayemfahamu kumtambua haraka.

    Ungeweza kudhani ni mtu mwingine kabisa. Baada ya kukamilisha dozi, alipewa dawa nyingine za kwenda kutumia ili kumaliza kabisa nguvu za utajiri wa kishirikina aliokuwa nao na badala yake, mganga Kiswigo akamkabidhi kitabu ambacho alimhakikishia kwamba endapo atafuata yale yote yaliyomo ndani yake, basi angeweza kupata chochote maishani mwake.

    “Kitabu hiki kinataka mtumwenye imani na msafi waroho, ukiwa mchafu wala maandishi yake huwezi kuyaona. Bila kujali unaabudu dini gani, ni lazima uendelee kumuabudu Mungu wako nakumtukuza na kufuata yale yote yaliyoamrishwa kwenye vitabu vyake.

    “Unajua watu wengi huwa wanaamini kwamba kitabu hiki ni cha shetani kwa sababu kinapatikana mikononi mwa sisi watu wenye nguvu za giza lakini ukweli ni kwamba hiki ni kitabu kitakatifu kama vilivyo vitabu vingine vya dini nyingine.

    “Ukianza kusoma utagundua kwamba licha ya kusisitiza kufanya tahajudi (meditation) za aina zote tatu, kuanzia tahajudi ya pumzi (breath meditation), ya maneno (mantra meditation) na ya mwanga na sauti (light and sound meditation), inasisitiza pia mtu kuishi kulingana na misingi ya kibinadamu.

    “Upendo ni jambo lililoagizwa na vitabu vya dini zote lakini hata kwenye hiki kitabu pia tunasisitizwa upendo. Itakuwa haina maana kama utajifanya unampenda Mungu ambaye humuoni wakati unawatendea mabaya binadamu wenzako. Hakikisha katika kila siku inayopita, angalau unamfurahisha mtu mmoja, hata kwa jambo ambalo ni dogo.

    “Pia ndani ya kitabu hiki, utajifunza namna ya kukabiliana na hisia zako zikiwemo hofu, hasira, tamaa, wivu na mambo mengine mengi ambayo kimsingi ndiyo yanayoichafua nafsi ya mtu na kumuweka mbali na Mungu wake.

    “Utafuata maelekezo yote hatua kwa hatua na nakuhakikishia ukishaweza kuutakasa mwili wako ukawa safi kabisa, pia ukatakasa nafsi na akili zako, unaweza kuomba jambo lolote na hakika litatimia.

    “Hata kama utataka tena utajiri, ukifuata kwa umakini mkubwa kilichoandikwa kwenye hiki kitabu, ambacho kimsingi ndiyo kilichoandikwa kwenye vitabu vingine vyote vya dini, kila unachokitaka kitatimia kwa haraka sana. Mimi sina mengi ya kusema, kama una swali lolote unaweza kuniuliza,” alisema mganga Kiswigo huku akimkabidhi baba yake Samantha kitabu hicho.

    Akakipokea na kushusha pumzi ndefu kisha akamuuliza mganga huyo swali.

    “Umesema nikishaweza kuutakasa mwili wangu, roho na akili, kila nitakachokiomba kitatimia! Sasa nataka kujua nawezaje kuutakasa mwili, roho na akili?”

    “Swali zuri na ni rahisi sana. Mwili wako unautakasa kwa kuhakikisha kwanza unaufanyia usafi wa kutosha kila siku. Hakikisha unaoga kwa maji mengi mara kwa mara, unafanya mazoezi, unavaa nguo safi, unalala mahali pasafi, unakunywa maji mengi na mambo mengine ya usafi wa kawaida lakini kubwa, inatakiwa uhakikishe unakula vyakula ambavyo kiasili binadamu ndivyo anavyopaswa kula.

    “Unajua watu wengi wanakosea sana wakiamini kula vyakula vya kukaanga vyenye mafuta mengi, sukari nyingi, vyakula vya kusindikwa kwenye makopo na nyama ndiyo ufahari lakini kimsingi binadamu hakuumbwa kula aina hiyo ya vyakula. Ndiyo maana utashangaa kuona magonjwa ya kutisha hayaishi, mara kisukari, kansa, presha, kupooza na maradhi mengine ya aina hiyo!

    “Binadamu ameumbwa kula mbogamboga, nafaka na matunda. Tena jitahidi kula vyakula ambavyo havijawekwa mafuta ya viwandani. Mfano mwepesi, mtu anayekula ugali wa dona na mboga za majani, pembeni akiwa na matunda, amekula chakula bora kuliko anayekula baga, pizza na nyama za kukaanga. Ukizingatia hilo, utaufanya mwili wako utakasike na kubwa zaidi, kunywa maji mengi ya kutosha. Huo ni upande wa mwili.

    “Upande wa akili, hakikisha kila kinachopita kichwani mwako kipo katika taswira chanya. Acha kufikiria mambo mabaya kama visasi, wivu, chuki au kuwa na hasira zinazovuka mipaka.

    “Wasamehe wanaokukosea hata kama wamekukosea jambo kubwa kiasi gani, wasaidie wenye uhitaji, tenda haki kila mara si kwa sababu sheria inasema hivyo bali kwa sababu tumeagizwa kuishi kwa haki. Usimuonee wala kumkandamiza mtu yeyote, si mkubwa wala mdogo, si tajiri wala maskini! Wapende watu wote bila kujali huyu ni nani au atanisaidia nini. Ukifanya hivyo utazitakasa akili zako na hakikisha unafanya hivyo kila siku.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mwisho ni upande wa roho. Hakikisha unajiweka jirani na ulimwengu wa kiroho muda wote. Amini kwamba kuna nguvu kubwa inayoyaongoza maisha yako na ya viumbe wengine wote duniani. Fanya tahajudi kila siku, sali, timiza yale yote yanayoamrishwa katika vitabu vyote vya dini na epukana na anasa za hii dunia kwa sababu mwili utakapokufa, roho itaendelea kuishi.

    “Ishi hapa duniani ukiwa unaelewa kwamba sote ni wapita njia tu na kunamaisha baada ya kifo, jiandae leo kwa kutenda mema na kuishi kulingana na asili ya binadamu ili kesho hata zamu yako ya kufa ikifika, usiwe na hofu tena.

    “Ukiyatimiza hayo, utakuwa umefikia hatua ya utakaso,” alisema mganga Kiswigo, baba yake Samantha akawa anatingisha kichwa tu huku akiwa ni kama haamini kwa sababu alitegemea labda mganga huyo atakuwa anazungumzia habari za mashetani, majini, misukule na viumbe wa kutisha lakini haikuwa hivyo.

    Kwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kukaa nyumbani kwa mganga huyo, baba yake Samantha alimshukuru sana mganga huyo na kumwambia kwamba mpaka muda huo, alikuwa anajihisi ni kama amezaliwa upya, akaahidi kwenda kufanyia kazi mambo yote aliyoelekezwa.

    Mganga Kiswigo na wasaidizi wake walimsindikiza baba yake Samantha mpaka nje ya msituhuo, wakampeleka mpaka sehemu aliyokodishiwa baiskeli kwa ajili ya kumsogeza mpaka sehemu anayoweza kupata usafiri wa magari madogo au ya mizigo yatakayomfikisha mjini ili aendelee na safari yake. Walimfungashia zawadi mbalimbali za kuwapelekea watu wa mjini. Hatimaye safari ye kurejea jijini Dar es Salaam ikapamba moto.

    ***

    Maisha ya Edmund na Samantha jijini Arusha yaliendelea vizuri huku mara kwa mara wakiwasiliana na mama yake Samantha ambaye naye nafsi yake ilitulia na taratibu akaanza kuamini kwamba mwanaye yupo kwenye mikono salama kwani kila alipokuwa akizungumza naye, alikuwa anaonesha kuwa na furaha kubwa.

    Edmund naye aliendelea kuhakikisha Samantha anapata huduma zote za kiafya kama alivyomuahidi mama yake na baada ya wiki mojakuisha, Samantha alikuwa na ahueni kubwa kwani tayari jerahalake la kupigwa risasi mguuni lilikuwa likikaribia kupona kabisa.

    Ili kuharakisha kuponakwake, Edmund akawa anamfanyisha mazoezi ya kutembea ambapo safari hii alianza kumudu kutembea mwenyewe ingawa bado alikuwa akichechemea. Jioni moja akiwa anamfanyisha Samantha mazoezi ya kutembea, nje ya nyumba waliyokuwa wanaishi, simu ya Edmund ilianza kuita mfululizo, alipotazama namba ya mpigaji, alishtuka na kumtazama Samantha usoni.

    “Vipi?”

    “Bosi wetu kazini ananipigia simu, sijui anataka kusema nini? Naogopa hata kupokea.”

    “Pokea tu umsikilize, kwani tatizo liko wapi?”

    “Si unajua tangu nilipopatwa nayale matatizo kipindikile sijarudi tena kazini na wala hawana taarifa kama niko wapi kwa siku zote hizo?”

    “Pokea, nakuomba upokee na uzungumze naye,” Samantha alisemakwa sauti ya upole na kumkumbatia Edmund, ikabidi atii alichowambiwa, akapokea.



    “Edmund!”

    “Naam mkuu.”

    “Uko wapi wewe mbona unatupa wasiwasi? Tumekuja nyumbani kwako ulikokuwa unaishi karibu mara kumi, haupo wala hakuna taarifa za mahali ulipo, una tatizo gani?”

    “Nina matatizo ya kifamilia.”

    “Lakini ulipewa ruhusa kwa sababu ulikuwa unaumwa, kama una matatizo ya kifamilia kwa nini usitoe taarifa? Karibu mwezi mzima unaisha hujaripoti kazini. Au kwa sababu unajua unategemewa na kampuni ndiyo maana unaleta dharau?

    “Sasa sikia, nilichokupigia simu ni kwamba inatakiwa Jumatatu uje kazini, vyovyote itakavyokuwa lazima uje, kuna kazi maalum umechaguliwa kuifanya, no excuse! (Hakuna visingizio!)” alisema meneja mkuu wa Kampuni ya Hashcom Mobile, Erick Salawi kisha akakata simu.

    “Edmund alishusha pumzi ndefu na kumgeukia Samantha ambaye muda wote alikuwa ametulia akimsikiliza Edmund alivyokuwa anazungumza na simu.

    “Vipi anasemaje?” alihoji Samantha huku akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia atakachoambiwa, ikabidi Edmund amueleze kila kitu.

    “Umeamuaje?”

    “Siwezi kuondoka na kukuacha Samantha, nipo tayari kupoteza kila kitu lakini siyo wewe,” alisema Edmund, Samantha akamvutia kifuani kwake na kumkumbatia, mazungumzo mazito yakaanza. Huku akizungumza kwa sauti ya upole, iliyojaa ujumbe mzito, Samantha alimtaka Edmund asafiri mpaka Dar es Salaam kwenda kusikiliza alichoitiwa na kwamba asiwe na wasiwasi kuhusu yeye.

    “Napenda kukuona ukifanya kazi mume wangu mtarajiwa, nataka tuishi kwa kujitegemea, naamini tunaweza. Wewe ukifanya kazi na mimi nikifanya kazi, tukiunganisha mshahara wetu tunaweza kufanya mambo makubwa sana, tafadhali nakuomba usiniangushe,” alisema Samantha, Edmund akawa anatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana na kilichokuwa kinasemwa na Samantha.

    Siku hiyo ilipita, kesho yake Edmund akaanza kujiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea Dar es Salaam. Alihakikisha anamuacha Samantha katika mazingira mazuri, akamuandalia kila kitu ili asihangaike atakapoondoka.

    Hatimaye muda wa kuondoka uliwadia, akakumbatiana na Samantha kwa muda mrefu huku wakimwagiana mvua ya mabusu, wakaagana huku msichana huyo mrembo akimtakia kila la heri.

    ***CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya safari ndefu na yakuchosha ya basi, kutoka Sumbawanga, hatimaye baba yake Samantha aliwasili jijini Dar es Salaam majira ya saa tano za usiku. Alimshukuru Mungu kuwasili usiku kwani kwa hali aliyokuwa nayo, kila mtu anayefahamiana naye ambaye angemuona, asingeacha kumshangaa.

    Aliposhuka Stendi ya Mabasi ya Ubungo, alikodi teksi iliyompeleka moja kwa moja mpaka nyumbani kwake. Kwa muda wote huo hakuwa amewasiliana na mkewe wala hakumpa taarifa zozote juu ya ujio wake.

    Mlinzi wa nyumba ya kifahari waliyokuwa wanaishi, alishtuka baada ya kusikia kengele ya geti ikigongwa, jambo ambalo halikuwa kawaida. Harakaharaka akasogea getini na kutazama kupitia kioo maalum kilichokuwepo eneo hilo, akashtuka kumuona bosi wake huku akionesha kubadilika sana.

    Harakaharaka alifungua mlango na kumkaribisha kwa heshima, akaingia na kupitiliza moja kwa moja mpaka ndani ambako aligonga mlango na kufunguliwa na mkewe muda mfupi baadaye.

    “Mume wangu, ni wewe? Ooh! Ahsante Mungu, siamini macho yangu,” alisema mama Samantha na kumkumbatia mumewe kwa nguvu huku machozi yakimtoka kwa wingi.

    “Mbona umekonda hivi? Unaumwa?” alimuuliza wakati akimkaribisha ndani, baba yake Samantha akawa anatingisha kichwa kuonesha kwamba hakuwa akiumwa, akamwambia mkewe atamuelezea kila kitu. Walipoingia ndani, jambo la kwanza lilikuwa ni kwenda kuoga kwani udongo mwekundu ulikuwa umemchafua na kumfanya abadilike kabisa.

    Baada ya kuoga kwa zaidi ya dakika ishirini, akitumia sabuni nyingi, alitoka bafuni na kuelekea chumbani. Muda mfupi baadaye akatoka na nguo alizotoka nazo safarini na kwenda kuzichoma moto, akarudi ndani ambako alikuta tayari mkewe ameshamuandalia chakula.

    Wakakaa mezani ambapo alianza kukifakamia chakula kwa fujo kutokana na njaa kali iliyokuwa inamsumbua. Alipomaliza kula walielekea chumbani ambapo mama yake Samantha alianza kumuelezea kila kitu kilichotokea katika kipindi chote ambacho hakuwepo.

    Alimueleza kuanzia jinsi Samantha alivyotoroka hospitalini akiwa na Edmund, jinsi mali zao nyingi zilivyoshikiliwa na serikali kwa madai ya kutolipiwa kodi stahiki kwa muda mrefu na jinsi nyumba hiyo waliyokuwa wanaishi ilivyokuja kupigwa ‘X’ kwa madai kwamba ilikuwa imejengwa katika eneo la hifadhi ya barabara.

    “Na nyumba nayo imewekwa ‘X’?”

    “Ndiyo na nasikia tayari watu wengine wameshaanza kubomolewa mtaa wa pili, inabidi tufanye mpango wa kuhamia kwenye nyumba yetu ya Bunju haraka iwezekanavyo.”

    “Lakini ile bado haijaisha!”

    “Sasa unafikiri tutafanya nini mume wangu? Au unasubiri nyumba ije ivunjwe tukiwa humuhumu ndani?” alisema mama yake Samantha kwa sauti ya upole, akaendelea kumuelewesha mumewe mambo mbalimbali.

    “Utakachokutana nacho nyumbani kwako kisikushangaze, unatakiwa kwenda kuanza upya kabisa, utajiri wa kishirikina hauna nafasi tena na mali zote ulizozipata kwa njia ya kishirikina zitayeyuka na kukuacha ukiwa huna kitu,” kauli ya mganga Kiswigo ilijirudia kichwani mwake mithili ya mkanda wa video.

    Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na kila kitu, wakalala mpaka asubuhi ya siku iliyofuata ambapo maandalizi ya kuhamia Bunju yalianza. Hata suala la kuhamisha vitu lilikuwa gumu kwa sababu akaunti zote za benki zilizokuwa na mamilioni ya fedha zilikuwa zinashikiliwa na serikali.

    Ilibidi abangaize kwenye miradi yake mingine ambayo nayo ilikuwa ikisuasua, fedha zikapatikana na kazi ya kuhamisha vitu ikaanza huku pia mafundi wakilipwa kwa ajili ya kukamilisha vitu vidogovidogo ambavyo bado havikuwa vimekamilika kwenye nyumba mpya, ikiwemo madirisha na milango.

    Mpaka jioni ya siku hiyo, vitu vyote muhimu vilikuwa vimeshahamishwa. Wazo alilolitoa mama Samantha lilisaidia sana kwa sababu usiku wa siku hiyo, tingatinga la serikali liliwasili kwenye mtaa huo na kuanza kubomoa nyumba zote zilizokuwa zimewekewa alama ya ‘X’.

    Mpaka kunapambazuka, eneo kulipokuwa na nyumba ya kisasa ya akina Samantha, lilikuwa jeupe kabisa. Hakukuwa na nyumba wala bustani nzuri za maua tena. Kila kitu kilikuwa kikibadilika kwa kasi kubwa kwenye maisha ya familia hiyo, wakayaanza maisha mapya ya hadhi ya chini, Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

    ***

    Basi la Dar Express lililokuwa likitokea Arusha, liliendelea kuchanja mbuga kwa kasi kubwa na baada ya kusafiri kwa saa nyingi, hatimaye liliwasili Ubungo ambapo abiria walianza kuteremka, Edmund akiwa miongoni mwao.

    Akashuka akiwa na kibegi chake kidogo mgongoni na kutoka mpaka nje ya stendi ambapo alikodi Bajaj iliyompeleka mpaka Sinza. Hakutaka kwenda kulala kwenye nyumba waliyokuwa wanaishi na Samantha kabla ya kutokewa na matatizo, akaenda kupanga chumba kwenye nyumba ya kulala wageni iliyokuwa karibu na kazini kwao ili asubuhi iwe rahisi kuwahi kazini.

    Moyoni alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua aliitiwa nini kazini kwani ilionekana kuna jambo la muhimu sana.



    Kesho yake asubuhi, Edmund aliwahi kuamka na kujiandaa, akatoka na kuelekea kazini ambapo siku hiyo alikuwa miongoni mwa watu wa kwanzakwanza kusaini na kuingia ofisini.

    Kila mfanyakazi mwenzake aliyekuwa akikutana naye alikuwa akimshangaa kwani kilipita kipindikirefu bila kuonekana kazini. Kingine kilichofanya watu wazidi kumshangaa, ni kwamba licha ya kuelewa kwamba ametoka kwenye matatizo, Edmund alikuwa amebadilika sana kimwonekano.

    Alikuwa amenawiri, rangi ya ngozi yake ambayo awali ilikuwa imefifia ikawa inapendeza kuonesha kwamba sasa alikuwa akiishi maisha mazuri. Hata mavazi yake nayo yalibadilika kwani alipendeza sana kiasi cha kuwafanya mpaka marafiki zake waanze kumuonea wivu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hatimaye meneja mkuu aliwasili ambapo alimkuta Edmund akiendelea kufurahi na wafanyakazi wenzake, akamchukua mpaka ofisini kwake ambapo alianza kuzungumza naye. Alimuonya kuhusu tabia yake ya kukaa nyumbani bila kutoa taarifa yoyote ofisini na kumtaka asirudie tena tabia hiyo.

    Edmund alikiri makosa yake na kuomba asamehewe, meneja huyo akamwambia akaendelee na kazi wakati wakimsubiri mkurugenzi mkuu ambaye kimsingi ndiye aliyeagiza aitwe haraka iwezekanavyo.

    Saa tatu asubuhi juu ya alama, Edmund aliitwa kwenye ofisi ya mkurugenzi wa kampuni hiyo, alipoingia akashtuka kugundua kuwa karibu viongozi wote wakubwa wa kampuni walikuwepo, kuanzia mkurugenzi, meneja mkuu, mhasibu mkuu na maafisa wengine kadhaa.

    Meneja ndiye aliyevunja ukimya na kumueleza Edmund kwamba mkurugenzi alikuwa akihitaji kuzungumza naye, akakaribishwa ambapo alianza kumpa pole kwa matatizo yaliyomtokea lakini akamsisitiza tena kuacha tabia ya kukaa tu nyumbani bila kutoa taarifa.

    “Kikubwa nilichokuitia, kwa kipindikirefu tangu ulipoajiriwa, nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu mwenendo wako wa kazi na kimsingi nimeridhishwa na juhudi na maarifa ambayo unayaonesha ili kuhakikisha kampuni inasonga mbele.

    “Tumefikiria kufungua tawi letu jingine jijini Arusha na mambo yote ya kimsingi yameshakamilika. Kampuni imekuteua wewe kwenda kuwa meneja mkuu wa tawi la Arusha ambapo utakuwa ukiripoti moja kwa moja kwangu.

    “Maslahi yako yameboreshwa sana ikiwemo kuongezwa mshahara, kutafutiwa nyumba ya kuishi na gari la kukuwezesha kufanya kazi zako vizuri. Meneja mkuu atakupa maelekezo zaidi ya namna ya kupata vitu vyote nilivyovitaja na jinsi utakavyoenda kuanza kazi.

    “Kabla sijahitimisha, unachochote cha kuzungumza?” alihoji mkurugenzi na kumfanya Edmund ashindwe kuzizuia hisia zake, machozi ya furaha yakawa yanamtoka ambapo aliushukuru uongozi kwa kumuamini na kuahidi kwamba atafanya kazi kwa bidii kuhakikisha tawi jipya la Arusha linachanua kwa kasi.

    Baada ya hapo, mkurugenzi alifunga kikao hicho na kumpa mkono wa pongezi Edmund, akifuatiwa na viongozi wengine ambapo walipotoka, walielekea kwenye ofisi ya meneja mkuu ambaye alianza kumpa maelezo ya nini anachotakiwa kufanya akifika Arusha.

    Akamkabidhi barua mpya ya kupandishwa cheo na kuongezwa mshahara, akaambiwa akajiandae mpaka asubuhi ya siku inayofuata ambapo angesafiri na meneja huyo mpaka jijini Arusha kwa ajili ya kwenda kumkabidhi ofisi rasmi. Hakuna siku ambayo Edmund alikuwa na furaha kama siku hiyo, akawa anamshukuru Mungu wake kwa miujiza aliyomtendea.

    Kesho yake asubuhi, Edmund na meneja mkuu walisafiri mpaka jijini Arusha ambapo Edmund alienda kukabidhiwa rasmi ofisi mpya za Hashcom Mobile, akatambulishwa kwa wafanyakazi kuwa ndiyo meneja mkuu wa ofisi hizo. Kiumri, Edmund alikuwa bado mdogo ukilinganisha na madaraka aliyokabidhiwa lakini mwenyewe hakuogopa chochote kwa sababu alikuwa akiuamini utendaji kazi wake. Ofisi zilikuwa mkabala na Stendi Kuu ya Mabasi ya Arusha wakati nyumba ya kuishi, ikiwa na kila kitu ndani ilikuwa maeneo ya Njiro, jirani na pale alipokuwa anaishi kwa siri na Samantha. Alikabidhiwa pia gari la kutembelea, Toyota Harrier pamoja na dereva ambaye angekuwa akilipwa na kampuni.

    Baada ya meneja mkuu kumkabidhi kila kitu, alipanda ndege kurejea jijiniDar es Salaam ambapo Edmund naye alielekea kwenye makazi yake ya awali, alikomuacha mpenzi wake, Samantha. Alipofika alipokelewa kwa shangwe kubwa na Samantha ambaye alimtaka amueleze kilichotokea katika safari yake hiyo.

    Samantha alipoelezwa, naye alishindwa kuficha hisia zake, akamwaga machozi mengi ya furaha na kumshukuru Mungu kwa kilichotokea.Siku tatu baadaye, tayari walishahamia kwenye nyumba ya kampuni na Edmund akaanza kazi rasmi huku Samantha akiwa ndiyo mshauri wake mkubwa.

    ***

    Maisha mapya ya wazazi wa Samantha, yalimbadilisha kabisa baba yake. Muda mwingi akawa ni mtu wa kukaa na kujutia mambo yote mabaya aliyowahi kuyafanya. Hakukuwa na chochote tena baada ya serikali kutaifisha mali zake karibu zote huku nyingine zikiteketea kwa moto au kuharibika katika mazingira ya kutatanisha.

    Hata hivyo, kama alivyokuwa ameshauriwa na mganga Kiswigo, aliendelea kufuata maelekezo yote aliyopewa. Taratibu akaanza kubadilika na kurudi kuwa mtu mwema, kama alivyokuwa mwanzokabla ya kukumbwa na tamaa ya utajiri haramu.

    “Mke wangu!”

    “Naam mume wangu.”

    “Nimekaa na kufikiria sana kuhusu suala la Samantha na Edmund, nafikiri hakuna sababu ya kuendelea kuwazuia kuishi pamoja lakini cha msingi lazima wafuate sheria zote muhimu ili wafunge ndoa na kuishi kihalali, au wewe unasemaje mke wangu?” alisema baba yake Samantha, kauli ambayo ilimfanya mkewe apigwe na butwaa, akiwa haamini alichokisikia, akawa anamshukuru Mungu kwa miujiza yake.

    Bila kupoteza muda, mama yake Samantha aliwasiliana na Samantha na Edmund na mipango ya kuchumbiana ikaanza kufanywa. Wiki mbili baadaye, wawili hao waliwasili jijini Dar es Salaam ambapo taratibu za kuvalishana pete ya uchumba zilifanyika. Baadaye wakaoana kwa ndoa ya kawaida, wakala kiapo cha kuwa mume na mke na huo ukawa mwanzo wa kufungua ukurasa mpya wa maisha yao.

    Kwa kuwa Edmund alikuwa akilipwa mshahara mkubwa, alimsaidia baba mkwe wake mtajiwa kuanzisha upya biashara, jambo ambalo mzee huyo hakuwahi kuhisi linaweza kutokea hata mara moja!

    Yaani Edmund yule aliyekuwa anamdharau na kumkosakosa kumuua mara kadhaa, leo ndiyo anampa mtaji wa kuanza upya biashara baada ya kufilisika! Ilikuwa ni zaidi ya maajabu kwa mzee huyo. Maisha yalizidi kusonga mbele, taratibu biashara za baba yake Samantha zikaanza kuchangamka, ukiongeza na uzoefu aliokuwa nao, kazi haikuwa ngumu.

    Akaikarabati vizuri nyumba yake mpya na kurudisha vitu vingi alivyovizoea kablahajafilisika. Safari hii alikuwa amebadilika mno, hakuwa kama mwanzo, alikuwa na heshima kwa kila mtu, aliwajali maskini na wenye shida na kila siku ilikuwa ni lazima amuombe Mungu wake na kutubu dhambi zake zote alizowahi kuzifanya.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Vijana wengi ambao waliwahi kuchukuliwa misukule enzi za utajiri wake, nao waliendelea kuombewa na kupatiwa tiba za uhakika na wakaanza kurudi kwenye hali zao za kawaida kama walivyokuwa mwanzo.

    Miezi michache baadaye, Samantha alipata ujauzito, akiwa mke halali wa Edmund ambapo miezi tisa baadaye, alijifungua watoto mapacha, wa kike na wa kiume aliowapa majina ya Emanuel na Emanuela, yakimaanisha Mungu yupo pamoja nasi. Maisha yakaendelea kwa raha mustarehe, huku ufanisi wa Edmund kazini nao ukizidi kuongezeka kila kukicha.



    MWISHO





0 comments:

Post a Comment

Blog