Search This Blog

A BOOK OF SATAN ( KITABU CHA SHETANI ) - 4







    Simulizi : A Book Of Satan ( Kitabu Cha Shetani )

    Sehemu Ya Nne (4)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ILIPOISHIA…

    “Nakuomba uniambie au unielekeze huyo mwanaume ni nani na anaishi wapi, nipo tayari hata kutuma watu wakampige risasi afe, siwezi kukubali utajiri wangu niliouhangaikia kwa kipindi kirefu leo hii upotee kirahisi namna hii,” alisema baba Samantha huku akionesha kumaanisha kile alichokisema.

    Mama yeke Samantha akashusha pumzi ndefu na kumtazama mumewe.

    SASA ENDELEA...

    BAADA ya kumpoteza maboya baba yake, hatimaye Samantha alifika karibu na nyumba ambayo alimpangishia Edmund. Kwa kuhofia kujulikana kwa siri hiyo, aliamua kutofika kabisa nyumbani hapo akiwa na yule dereva wa bodaboda.

    “Nishushe hapahapa kaka,” alisema Samantha huku akimpigapiga begani dereva huyo wa bodaboda ikiwa ni ishara ya kumhimiza asimamishe bodaboda.

    “Shilingi ngapi itakuwa?” aliuliza Samantha na kufungua mkoba wake ambapo kabla hata hajajibiwa alichomoa noti zaidi ya nne na kumkabidhi dereva huyo wa bodaboda, bila hata kumuaga alianza kutembea kwa harakahara kuelekea kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Edmund.

    Kwa kuwa alikuwa na ufunguo wa ziada, hakubisha hodi zaidi ya kufungua na kumkuta Edmund akiwa amejilaza kwenye kochi sebuleni akitazama mpira kupitia runinga kubwa iliyokuwa ukutani sebuleni hapo.

    “Waoh! Karibu sana jamani, karibu kipenzi cha roho yangu,” alisema Edmund baada ya kumuona Samantha akiingia sebuleni hapo na kunyanyuka kwenda kumlaki kwa furaha ya ajabu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ahsante, vipi mzima hujambo Edmund wangu?” aliitikia Samantha na kumjulia hali Edmund huku akimbusu shavuni na kumkumbatia kwa nguvu zote.

    “Mbona unaonekana kutokuwa na furaha Samantha, kuna nini tena mama?”

    “Si baba, sina furaha tena na maisha yangu”

    “Kafanya nini tena?”

    “Yaleyale ya kuingilia uhuru wa maisha yangu, hataki kuelewa kabisa kuwa kwa sasa nahitaji kuishi maisha ya ajabu ya kitumwa,” alisema Samantha huku akimlalia kifuani Edmund na kuanza kutokwa na machozi yaliyolowanisha kifua cha Edmund.

    Bila kupoteza muda, Edmund alianza kumfuta machozi Samantha kwa kutumia kiganja na kisha kumshika mkono na kuingia naye chumbani ambapo alimkalisha kitandani na kuanza kumbembeleza.

    “Alipokuita alikwambia nini?” aliuliza Edmund huku akimshika Samantha kiunoni hali iliyoamsha hisia kali kwa msichana huyo na kuanza kujinyonganyonga badala ya kujibu swali alilokuwa ameulizwa na Edmund.

    “Unajua Edmund umemtia hasara kubwa sana baba?”

    “Mimi? Kivipi?” aliuliza Edmund kwa hamaki kubwa huku akimtazama Samantha kwa macho yenye maswali mengi.

    “Kitendo cha mimi kufanya mapenzi na wewe kimesababisha kuungua kwa maduka yote ya Kariakoo na Posta, ndiyo maana alinipigia simu kwa hasira,” alisema Samantha na kumtazama machoni Edmund huku akilegeza macho na kumuweka katika wakati mgumu Edmund.

    “Mmh, sasa ikawaje?”

    “Hivi ninavyokuambia nimemkimbia baba, hata hivyo alikuwa akinifuatilia lakini tumempoteza njiani nikiwa na bodaboda,” alisema Samantha na kumsimulia kwa kirefu kisa chote kilichotokea katika familia yake.

    Edmund alishusha pumzi ndefu na kuanza kutafakari mambo mbalimbali, haraka sana Samantha alimshika mikono na kumkumbatia huku akimtaka kutokuwa na hofu kwani alikuwa amejitolea mhanga kwa ajili ya penzi la kijana huyo.

    Wakibaki wamekumbatiana huku kila mmoja akisikiliza joto la mwenzake, hali iliyosababisha wote kujikuta wakishikwa na mhemko wa ajabu.

    Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Edmund alianza uchokozi kwa kumtekenya Samantha maeneo mbalimbali ya mwili, hali iliyomsisimua msichana huyo mrembo kwa kila idara, umbo hadi sura na kujikuta akimsukumia Edmund kitandani.

    Harakaharaka bila kupoteza muda, walijikuta wakiwa kama walivyotoka kwenye matumbo ya mama zao, wakipashana joto kwa staili mbalimbali na kuanza kulisakata kabumbu bila uwepo wa refa.

    ***

    “Hutaki kusema siyo?” alizidi kufoka Baba Samantha hali iliyozidisha hofu kwa mkewe, kwani alimjua vyema mumewe linapokuja suala la mali hakuwa na utani hata kidogo.

    “Jamani baba Samantha, binti yako hutumia muda mwingi kuwa na wewe, mimi nitajuaje mambo yake?” alijibu mama Samantha na kumwangalia mumewe kwa macho ya hofu.

    Wakati mazungumzo yakiendelea, mara simu ya baba Samantha iliita na kuitoa haraka mfukoni ambapo namba ya mpigaji ilikuwa ngeni na kuipeleka haraka sana sikioni baada ya kuipokea.

    “Unasema kweli?”

    “Eeh, Mungu wangu, aaah, ahsante kwa taarifa, ahsante sana,” alisema Baba Samantha huku machozi yakianza kumchuruzika.

    “Nini tena mume wangu?” aliuliza Mama Samantha baada ya kuhisi kitu kisicho cha kawaida.

    “Unaona sasa Mama Samantha, unaona?”

    “Nimeona nini tena jamani mume wangu, mbona sikuelewi jamani?”

    “Yote haya kasababisha mwanao, nasema safari hii namwaga ubongo wa mtu. Sikubali,” alizidi kulalama Baba Samantha.

    “Kuna nini?” Mama Samantha aliuliza tena huku safari hii akinyanyuka alipokuwa amekaa na kumsogelea zaidi mumewe.

    “Mabasi yangu mawili yamegongana uso kwa uso na kuua abiria zaidi ya 30, mbaya zaidi hapa nimepigiwa simu na afisa wa Sumatra akinijulisha kuwa baada ya trafiki kufanya uchunguzi wamebaini kuwa ajali hiyo inatokana na uzembe wa madereva, hivyo kampuni yangu ya usafirishaji imefungiwa kwa muda usiojulikana,” alisema Baba Samantha na kuendelea kulia kwa kwikwi nzito.



    “Basi mume wangu jikaze, hakuna haja ya kulia kwa sababu pesa zinatafutwa.”

    “Inauma mke wangu, nikikumbuka maisha niliyoishi kabla sijapata utajiri sitaki kabisa kuamini kwamba naelekea kuyarudia tena.”

    “Hatuwezi kurudi kwenye umaskini mume wangu, hata ikitokea hivyo ni suala la kumshukuru Mungu kwani yeye ndiye anayepanga kila kitu,” alisema mama Samantha lakini mumewe hakumuelewa kabisa, akawa anazunguka huku na kule ndani ya chumba hicho akiwa ni kama amechanganyikiwa.

    ***

    Kitendo cha Samantha na Edmund kukutana tena kimwili, hakikusabisha madhara kwenye utajiri wa baba yake Samantha pekee bali madhara yalikuwa makubwa zaidi.

    Kitendo cha wawili hao kufanya mapenzi, kilisababisha wanaume ambao walitolewa kafara baada ya kujaribu kufanya mapenzi na Samantha na baadaye kuhifadhiwa kwenye pango maalum ndani ya nyumba ya mganga Shiwinga aliyekuwa nyuma ya utajiri wa kishetani wa mzee huyo, watoroke katika mazingira ya kutatanisha na kuingia mitaani.

    Kibaya zaidi, kutokana na kafara nzito walizokuwa wakifanyiwa wanaume hao, hawakuwa binadamu wa kawaida tena na baada ya kutoroka kwa mganga Shiwinga, kila mmoja alikuwa akitorokea kwenye mazingira aliyokuwa anaishi kabla ya kutolewa kafara, jambo lililosababisha taharuki kubwa kwenye kila mtaa walipokuwa wakionekana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila mmoja aliyepatikana, alionesha kukonda sana, akiwa na nywele na kucha ndefu na chafu, huku karibu wote wakiwa hawana kabisa uwezo wa kuzungumza kama zamani, wakionesha pia kuwa na matatizo ya kiakili.

    “Maskini Mohamed, huwezi kuamini kama ndiyo yule kaka sharobaro, aliyekuwa anajipenda kiasi cha kufanya awe kipenzi cha mabinti hapa mtaani, ukimuona huwezi kuamini.”

    “Mimi nimemuona asubuhi, anatia huruma sana. Nasikia alitembea na mke wa mtu, mumewe akamuendea kwa mganga, wake za watu sumu jamani,” watu kadhaa walikuwa wakijadiliana, saa chache baada ya kijana maarufu, Mohamed au Muddy kama wengi walivyozoea kumuita, kupatikana jirani na nyumbani kwao akiwa na hali mbaya sana, ikiwa ni baada ya karibu mwaka mmoja na nusu tangu alipopotea katika mazingira ya kutatanisha.

    Taarifa za kuonekana kwa misukule kadhaa kwenye mitaa ya Jiji la Dar es Salaam zilimshtua kila aliyezisikia huku kila mtu akizungumza lake. Hata wale ambao kwa kipindi kirefu hawakuwa wakiamini kuhusu habari za misukule, nao walianza kuamini kwa kilichokuwa kinatokea.

    Wachungaji, viongozi mbalimbali wa dini na waganga wa kienyeji, waliitumia vyema fursa hiyo, wengi wakawa wanatangaza kwamba wanao uwezo wa kuwaponya na kuwarudisha misukule hao katika hali yao ya kawaida, jambo lililosababisha ndugu wa watu hao waliokuwa na tatizo hilo kuanza kuhangaika huku na kule kwenye nyumba za ibada, kila mmoja akitaka kumsaidia ndugu yake.

    Hata hivyo, hakuna aliyeonesha kupata ahueni wala kuwa na dalili za kupona, gumzo likazidi kuwa kubwa mitaani.

    ***

    “Unasema tukae tumshukuru Mungu, hivi una akili kweli mke wangu?”

    “Sasa mume wangu unafikiri tutafanya nini?”

    “Lazima tufanye kitu, au hujasikia habari za misukule inayoonekana huko mitaani?”

    “Sasa kwani wewe unahusika vipi na hiyo misukule?”

    “Usijifanye hujui mke wangu, hao ni wanaume wote waliojaribu kufanya mapenzi na Samantha na kujikuta wakiingia kwenye mtego wangu.”

    “Haa! Sasa si uliniambia kwamba wanakufa? Inawezekana vipi mtu aliyekufa akaonekana mitaani?”

    “Hawakuwa wakifa moja kwa moja bali wanachukuliwa misukule kwa ajili ya kutusaidia kwenye biashara, sasa inaonekana wanatoroka kule walikohifadhiwa, inabidi sasa hivi niende Bagamoyo kwa mganga Shiwinga kutaka kujua nini ninatokea, nahisi kuhujumiwa,” alisema baba yake Samantha kwa hasira, taarifa iliyomuacha mkewe akiwa mdomo wazi.

    “Sasa wakipona si wataeleza ukweli wa kilichotokea? Unafikiri tutaficha wapi sura zetu?”

    “Wewe si umeamua kushirikiana na mwanao kunihujumu? Mkae mkijua kwamba hili tatizo siyo langu peke yangu, ni letu sote kwa hiyo kama mtaendelea kufichiana siri na mwanao kitakachotokea tusilaumiane, nipo tayari kuua,” alisema baba yake Samantha huku akiichomeka bastola yake kiunoni, akatoka na kuingia ndani ya gari, safari ya kuelekea nyumbani kwa mganga Shiwinga, Bagamoyo ikaanza.

    “Mungu wangu, kumbe ndiyo mambo yenyewe yalivyo makubwa hivi,” alisema mama yake Samantha wakati akimsindikiza mumewe kwa macho wakati akitoka kwa kasi getini na kuianza safari ya kuelekea Bagamoyo, akionesha wazi kuwa na jazba kali kuliko kawaida.

    ***

    “Samantha.”

    “Abee mume wangu.”

    “Ni siku ya pili sasa hujarudi nyumbani, unafikiri wazazi wako watakuwa kwenye hali gani?”

    “Edmund, kumbe hunipendi eeh! Yaani yote niliyokuelezea kuhusu baba leo unataka nirudi tena? Unataka nikafe?”

    “Siyo hivyo mpenzi wangu, najua kama wazazi lazima watakuwa kwenye wakati mgumu sana, si ajabu wakaenda hata kutoa taarifa polisi.”

    “Achana nao. Mimi nina wazo Edmund, hatuwezi kuendelea kukaa kwa amani, unaonaje kama tukiondoka Dar kwa muda mpaka mambo yatulie?”

    “Twende wapi?”

    “Popote, Arusha, Mbeya au Mwanza, pesa siyo tatizo kwangu,” alisema Samantha, wazo ambalo Edmund alikubaliana nalo lakini wakakubaliana kwamba kabla hawajaondoka, ni lazima waende kwa mganga Shiwinga kumpa taarifa ya uamuzi wao na pia kupewa dawa nyingine za kuendelea kutumia huko watakakokimbilia.

    “Wazo zuri na inabidi twende sasa hivi Bagamoyo, moyo wangu hauna amani kabisa kwa sababu najua baba anatusaka kwa udi na uvumba na muda si mrefu atajua mahali tulipojificha,” alisema Samantha, bila kupoteza muda wakajiandaa kwa safari ya kuelekea Bagamoyo, bila kujua kwamba baba yake Samantha naye muda huo alikuwa njiani kuelekea Bagamoyo, kiunoni akiwa na bastola.

    Kwa kuwa safari hii Samantha hakuwa na gari, waliamua kukodi teksi ya kuwapeleka mpaka Bagamoyo, wakahakikisha wamefunga vizuri nyumba yao na kutoka mpaka mtaa wa pili kulipokuwa na maegesho ya teksi.

    Wakaingia ndani ya teksi moja na kuzungumza na dereva, baada ya kukubaliana, safari ya kuelekea Bagamoyo ilianza, wawili hao wakiwa wamekaa siti ya nyuma, Samantha akiwa amejilaza kwenye miguu ya Edmund kimahaba.

    Safari iliendelea mpaka walipowasili Bagamoyo, wakamuelekeza dereva kuiacha barabara ya lami na kuingia kwenye barabara ya vumbi iliyokuwa inaelekea nyumbani kwa mganga Shiwinga.

    Dakika kadhaa baadaye, waliwasili nyumbani kwa mganga huyo, wakamlipa dereva fedha zake na kumwambia aende kuwasubiri kwenye barabara ya lami, wakachukua namba zake za simu kisha wakaingia nyumbani kwa mganga huyo ambaye aliwakaribisha kwa uchangamfu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muda mfupi baada ya kuwasili nyumbani hapo, wakiwa wanapiga stori za hapa na pale, walisikia muungurumo wa gari nje ya nyumba hiyo, Samantha na Edmund wakahisi yule dereva teksi atakuwa amesahau kitu, ikabidi watoke kwa lengo la kwenda kumsikiliza.

    Katika hali ambayo hakuna aliyeiamini, walipotoka tu, walikutana uso kwa uso na baba yake Samantha ambaye tayari alikuwa ameshashuka kwenye gari lake na kuliacha likiendelea kunguruma.

    “Nilijua tu lazima nitawapata, kumbe wewe ndiye unayempa jeuri mwanangu si ndiyo?” alisema mzee huyo huku akipeleka mkono kiunoni, kufumba na kufumbua akachomoa bastola na kuikoki, akamnyooshea Edmund.

    “Tukimbie, Edmund tukimbie, atakuua, namjua baba yangu,” alisema Samantha kwa hofu na kumshika mkono Edmund aliyekuwa ameduwaa, asijue la kufanya, wakaanza kukimbia kuelekea nyuma ya nyumba yam ganga Shiwinga lakini kabla hawajafika mbali, mlio wa risasi ulisikika, paah!



    Mganga Shiwinga akiwa ndani ya nyumba yake, alishtuka kusikia mzozo mkubwa nje ya nyumba yake, akaacha kila alichokuwa anakifanya na kutoka nje lakini alipofika mlangoni, alishtuka kupita kiasi baada ya kusikia mlio mkubwa wa risasi, akajikaza kiume na kutoka nje.

    Akashindwa kuyaamini macho yake kwa alichokiona, baba yake Samantha alikuwa ameshika bastola, huku naye akionesha kupigwa na bumbuwazi, akiwa ni kama haamini kilichotokea.

    “Edmund! Kimbia mpenzi wangu, kimbia atakuua.”

    “Hapana Samantha, siwezi kuondoka bila wewe,” alisema Edmund huku naye akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona. Samantha alikuwa amedondoka chini, huku damu nyingi zikimtoka mithili ya bomba lililopasuka.

    Risasi iliyofyatuliwa na baba yake, badala ya kumpata Edmund kama mwenyewe alivyokuwa amepania, ilipenya na kuingia kwenye paja la mguu wa kushoto la mwanaye na kusababisha adondoke chini kama mzigo, damu nyingi zikiwa zinamtoka.

    Licha ya Samantha kuendelea kumsisitiza Edmund aondoke, kijana huyo hakuwa tayari, akaona ni bora apigwe risasi na kufa kuliko kukimbia na kumuacha Samantha akiwa kwenye hali hiyo.

    Kitendo cha kumpiga risasi mwanaye, kilimfanya baba yake Samantha abaki amepigwa na butwaa kwa sekunde kadhaa, huku akiwa bado ameishika bastola yake vilevile. Ni mpaka mganga Shiwinga alipotoka nje ndipo mzee huyo alipozinduka na kujikuta akijilaumu mno kwa kitendo alichokifanya.

    Baba yake Samantha na mganga Shiwinga wakakimbia mpaka pale Samantha alipokuwa ameanguka, huku Edmund akijaribu kuzuia damu zisiendelee kumtoka kwa wingi. Baada ya wawili hao kufika, kufumba na kufumbua baba yake Samantha alimpiga Edmund konde zito lililomfanya adondoke chini kama mzigo, akamfuata na kuanza kumpiga mateke ya tumboni huku akimtolea matusi ya nguoni, hali iliyosababisha zoezi la kumuokoa Samantha lisitishwe kwa muda.

    “Unakosea baba Samantha, tumsaidie kwanza huyu, atakufa huku tunamuona,” alisema mganga Shiwinga, baba yake Samantha akamalizia kupiga teke lingine kwa nguvu na kusababisha Edmund augulie maumivu makali.

    Wakaanza kumsaidia Samantha ambapo walimbeba juujuu na kumsogeza eneo lenye nafasi, mganga Shiwinga akakimbilia ndani na muda mfupi baadaye alitoka akiwa na dawa ya maji, akaanza kumpaka Samantha pale kwenye jeraha lake huku akimpa Edmund kazi ya kutwanga dawa nyingine ya majani.

    “Huyu mshenzi sitaki afanye kazi yoyote, kwanza ondoka hapa nisije nikakupiga risasi,” alifoka baba yake Samantha lakini mganga Shiwinga akaingilia kati na kumsihi mzee huyo atulize hasira zake kwanza kwa sababu kwa wakati huo, jambo la muhimu lilikuwa ni kuokoa maisha ya Samantha kwanza.

    Edmund ambaye alikuwa akitokwa na damu mdomoni kutokana na ngumi aliyopigwa na baba yake Edmund huku mikono yake pia ikiwa imetapakaa damu alizozishika wakati akimsaidia Samantha, alitii alichoambiwa na mganga Shiwinga, akaanza kutwanga dawa kwenye kinu kikubwa huku mara kwa mara baba yake Samantha akimkata jicho baya.

    Walipofanikiwa kuzuia damu zisiendelee kutoka, mganga Shiwinga na baba yake Samantha walisaidiana kumpakiza Samantha kwenye gari kwa ajili ya kumuwahisha hospitali.

    “Na wewe mshenzi ingia ndani ya gari,” alisema baba yake Samantha kwa ukali akimwambia Edmund ambaye alisitasita kwa sekunde kadhaa, alimpomtazama Samantha alivyokuwa akiendelea kuugulia maumivu, hakuwa na cha kufanya zaidi ya kutii alichoambiwa.

    Akakaa kwenye siti moja na Samantha ambaye japokuwa alikuwa kwenye maumivu makali, alishindwa kuficha furaha yake kumuona Edmund akiwa amekaa pembeni yake. Kwa kasi kubwa baba yake Samantha aliondoka gari na kumuacha mganga Shiwinga akiwa amesimama nyuma ya nyumba yake. Kila kitu kilikuwa kimetokea kwa kasi kubwa mno mithili ya filamu ya kusisimua ya Hollywood.

    Baba yake Samantha alikuwa na kazi moja tu nyuma ya usukani, kukanyaga mafuta! Gari likawa linakimbia utafikiri lipo kwenye mashindano. Takribani dakika thelathini baadaye, tayari walikuwa wamewasili jijini Dar es Salaam, mzee huyo akaenda moja kwa moja mpaka kwenye kituo cha polisi Oysterbay.

    Edmund akashikwa na mshangao kwani alitegemea breki ya kwanza ingekuwa hospitalini, mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda mbio kuliko kawaida. Kwa muda wote huo, Samantha alikuwa amepitiwa na usingizi mzito kutokana na kuugulia maumivu kwa muda mrefu.

    Kwa kupitia vioo vya gari la kifahari walilokuwa wamepanda, Edmund alimuona baba yake Samantha akizungumza jambo na askari kadhaa waliokuwa wamemzunguka, akawa anawaeleza jambo huku akiwaoneshea kwenye gari lake. Askari watatu wenye silaha wakatembea harakaharaka mpaka kwenye gari, Edmund akashtukia akishushwa chini na kukokotwa msobemsobe mpaka kaunta.

    “Afande kani nimefanya kosa gani?”

    “Umefanya jaribio la kuua kwa kutumia silaha,” alisema askari mmoja huku akimuamuru Edmund kuvua viatu na mkanda kisha kusalimisha kila kilicho chake kaunta. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baba yake Samantha aliyekuwa akiandikiwa fomu ya matibabu (PF3) na askari mmoja pembeni, alijifanya kutosikia chochote kilichokuwa kinaendelea, sekunde chache baadaye alitoka na fomu yake, akaenda kwenye gari lake, akapanda na kuondoka kwa kasi kubwa na kumuacha Edmund akiwa chini ya ulinzi mkali.

    “Mungu wangu! Kwani nimefanya kosa gani?” alihoji Edmund lakini kama ilivyokuwa mwanzo, hakuna aliyemjibu, baada ya kumaliza kukabidhi vifaa vyake kaunta, alibebwa msobemsobe na kuingizwa mahabusu.

    Akiwa nyuma ya nondo, Edmund alilia kwa uchungu sana, aliona kama baba yake Samantha anamuonea bila sababu yoyote ya msingi kwa sababu kama ni mapenzi, binti yake ndiye aliyekuwa akimpenda yeye.

    “Sasa mimi kosa langu nini? Nimemkosea nini Mungu kustahili mateso kama haya? Sijawahi kuingia selo hata siku moja, leo kwa sababu ya mapenzi nimeingia, kwa nini lakini?” Edmund alikuwa akijisemea mwenyewe kama mwendawazimu, akiwa amekaa kwenye kona moja ya mahabusu hiyo iliyokuwa imejaa wahalifu wengi huku kukiwa na hewa nzito.

    “Dogo vipi mbona unalialia?” mwanaume mmoja mwenye mwili mkubwa, aliyekuwa amevua shati na kubaki kifua wazi, alimuuliza Edmund huku akimgongagonga begani. Edmund alipomgeukia na macho yao kugongana, alijikuta akikosa cha kujibu kwani bila hata kuuliza, mwanaume huyo alionekana kuwa miongoni mwa wahalifu wazoefu kutokana na jinsi uso wake ulivyokuwa na makovu mengi makubwa.

    “Aah! Mambo ya kawaida tu braza.”

    “Ukishaingia humu inabidi uwe mgumu, mambo ya kulialia kama mtoto wa kike wenzako watakuoa, shauri yako,” alisema mwanaume huyo kwa sauti ya kukwaruza na kusababisha mahabusu wengine wacheke kwa nguvu. Ikabidi Edmund ajikaze kisabuni, akawa anaugulia maumivu ndani kwa ndani.

    ***

    “Hapa ni wapi? Nimefikaje hapa na Edmund yuko wapi?” Samantha aliongea kwa taabu baada ya kuzinduka na kujikuta akiwa sehemu tofauti kabisa ambayo hakukumbuka amefikaje.

    “Samantha, ooh! Ahsante Mungu. Nesi! Nesi! Ameamka,” mama yake Samantha aliyekuwa amekaa pembeni ya kitanda alicholazwa mwanaye alimuita nesi huku akiinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake.

    “Mama! Kwani hapa ni wapi?” aliendelea kuhoji Samantha huku akiishangaa chupa ya damu iliyokuwa ikitiririka kuingia kwenye mishipa yake.

    “Ni hospitali mwanangu. Uliletwa ukiwa hujitambui,” alisema mama yake Samantha huku akitokwa na machozi ambayo Samantha hakuelewa kama ni ya furaha au ya huzuni.

    Akataka kuinuka pale kitandani kwani bado hakuwa akikumbuka nini kimesababisha akawa kwenye hali kama hiyo lakini maumivu makali ya mguu yakamrudisha kitandani. Kwa mbali akaanza kukumbuka kilichotokea.

    “Nimefanya nini mguu mama?”

    “Edmund alitaka kukuua mwanangu, amekupiga risasi lakini usijali tayari ameshakamatwa hivi tunavyoongea yupo mikononi mwa polisi.”

    “Whaaat?” (Niniii?)



    “Ndiyo hivyo, baba yako amesema hatakubali, atahakikisha yule kijana anapotea.”

    “Baba muongo! Mama baba kakudanganya,” alisema Samantha huku akianza kulia kwa uchungu.

    Kumbukumbu za yote yaliyotokea zilijirudia ndani ya kichwa chake, akakumbuka jinsi alivyokuwa amepanga kutoroka na Edmund na kukimbilia mbali ili isiwe rahisi kwa baba yake kuendelea kuwafuatilia, alikumbuka jinsi walivyofunga safari mpaka kwa mganga Shiwinga, Bagamoyo.

    “Alikumbuka pia jinsi baba yake alivyowafuata mpaka kwa mganga huyo na jinsi alivyochomoa bastola kiunoni kwake kwa lengo la kumpiga risasi Edmund na jinsi msichana huyo alivyojitoa sadaka na kujikuta akipigwa risasi ya mguuni na baba yake.

    “Edmund! Kimbia mpenzi wangu, kimbia atakuua.”

    “Hapana Samantha, siwezi kuondoka bila wewe,” Samantha aliyakumbuka maneno ya mwisho aliyozungumza na mpenzi wake huyo, damu nyingi zikiwa zinamvuja mguuni.

    “Baba ndiye aliyenipiga risasi mama, alikuwa anataka kumuua Edmund,” alisema Samantha, kauli ambayo ilimshtua mno mama yake Samantha.

    “Unasema? Samantha utakuwa umechanganyikiwa mwanangu. Unajua umepoteza damu nyingi na isitoshe umechomwa sindano kali za kuzuia maumivu, hizo ndizo zilizokuchanganya.”

    “Hapana mama, nina akili zangu timamu, niamini ninachokizungumza. Hata mganga Shiwinga anaweza kuwa shahidi.”

    “Hapana mwanangu, inabidi upumzike, nesi muongeze dawa ya usingizi aendelee kupumzika,” alisema mama yake Samantha akiamini mwanaye atakuwa amechanganyikiwa kwani hakuamini kama mumewe anaweza kufanya kitendo hicho.

    Kwa kuwa nesi alikuwa jirani, alimchoma sindano Samantha ambaye bado aliendelea kusisitiza kwamba anachokizungumza ni kweli mpaka alipopitiwa na usingizi mzito. Maneno yaliyosemwa na mwanaye yaliendelea kujirudia ndani ya kichwa cha mama yake Samantha.

    Japokuwa upande mmoja alikuwa akibisha kwamba mumewe hawezi kufanya hivyo, upande mwingine alikubali kwamba anaweza kwa sababu tangu aanze kukumbwa na misukosuko ya utajiri wake kuanza kupukutika, alikuwa ni kama amechanganyikiwa mpaka kufikia hatua ya kumpiga mkewe, jambo ambalo hajawahi kulifanya hata siku moja.

    Muda mfupi baadaye, mumewe alifika hospitalini hapo huku akionesha kukosa kabisa utulivu, akaenda mpaka kwenye wodi maalum ya VIP aliyokuwa amelazwa Samantha.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Anaendeleaje huyu!” alisema baba yake Samantha huku akikaa pembeni ya mkewe.

    “Anaendelea vizuri, amerejewa na fahamu zake lakini inaonesha bado akili zake hazijatulia,” alisema mama yake Samantha huku akikaa vizuri pale kitandani kwa lengo la kumchunguza vizuri mumewe kwani alikuwa na uwezo mkubwa wa kumtambua kwamba anaongea ukweli au anadanganya.

    Akawa anaendelea kumhoji maswali ya hapa na pale ambapo kwa kumtazama tu aligundua kwamba kuna jambo alikuwa analificha. Hata hivyo, hakutaka kuonesha kwamba ameshtukia jambo lolote, wakaendelea kuzungumza mambo yao ya kawaida huku akimuunga mkono kila alichokuwa anakisema.

    “Umesema huyo kijana umempeleka kituo gani?”

    “Yuko Oysterbay, mshenzi sana yule kijana,” alisema baba yake Samantha huku akionesha kudhamiria kweli kumpoteza ili kulinda utajiri wake ambao tayari ulishaanza kusuasua. Baadaye aliondoka na kumuacha mama yake Samantha akiwa pembeni ya Samantha.

    Baada ya dawa za usingizi kuisha nguvu, Samantha alizinduka tena usingizi ambapo kama ilivyokuwa mara ya mwisho kabla hajachomwa sindano ya usingizi, aliendelea kumsisitiza mama yake kwamba Edmund hakuwa na kosa lolote.

    “Nakuomba umsaidie Edmund mama, anateseka bure kwa kosa ambalo hajalifanya,” alisema Samantha huku akilia, mama yake akamtaka atulie kwanza kwa sababu hata yeye ameanza kuwa na wasiwasi kwamba kijana huyo hana hatia. Akamtaka Samantha amuelezee kwa kirefu kilichotokea.

    Lengo la kumwambia amuelezee upya ilikuwa ni kutaka kufananisha maelezo aliyompa awali na ambacho angekisema muda huo kwa sababu kama alikuwa anadanganya, isingekuwa rahisi maelezo ya awali na ya muda huo kufanana.

    Hata hivyo, Samantha alieleza kama alivyoeleza awali bila kuongeza wala kupunguza jambo lolote, jambo lililomfanya mama yake Samantha aamini kwamba mwanaye alikuwa anazungumza ukweli.

    “Basi nisikilize mwanangu, mimi nitamsaidia Edmund na nakuhakikishia nitaenda kumtoa mahabusu lakini ni lazima nikusimamie wewe upone kwanza.”

    “Mama! Mpaka mimi nipone unafikiri itakuwa lini? Kamtoe kwanza Edmund, nataka kumuona, nakuomba mama.”

    “Usiwe na haraka mwanangu, kuwa mpole.”

    “Haiwezekani mwanangu, afya yako ni muhimu zaidi.”

    “Mama usipoenda kumtoa leo nachukua uamuzi mgumu wa kujiua,” alisema Samantha kwa sauti ya juu huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara. Kauli hiyo ikapenya kwenye ngoma za masikio ya baba yake Samantha ambaye alikuwa mlangoni akitaka kuingia, mkononi akiwa amebeba matunda na juisi alivyoenda kumnunulia mwanaye.

    “Anasemaje huyu? Eti Samantha unasemaje?” alihoji baba yake Samantha akiwa ameshafungua mlango na kuingia wodini humo, macho yake na ya mwanaye yakagongana.

    “Usipoenda kumtoa Edmund polisi najiua.”

    “Mtoto mshenzi sana wewe! Yaani matatizo yote yanayotutokea kumbe ni yule mshenzi ndiye anayesababisha na leo unadiriki kufumbua mdomo wako kuongea upuuzi kama huo? Jiue hata sasa hivi.”

    “Mh! Jamani mume wangu, mbona unashindwa kutumia busara,” ilibidi mama yake Samantha aingilie kati kutokana na mumewe kuonesha kutojali tishio kubwa lililotolewa na binti yao.

    “Kwanza Edmund siyo aliyenipiga risasi, wewe ndiyo ulikuwa na bunduki na ukataka kumuua kaka wa watu…”

    “Ishia hapohapo! Mimi ni baba yako na ndiye niliyekuzaa, kwa hiyo utachagua mwenyewe usimame upande gani, kama unataka kushirikiana na huyo mshenzi mwenzako niambie sasa hivi nitamke kwamba kuanzia leo wewe siyo mtoto wangu.”

    “Samantha hebu acha kubishana na baba yako, nisikilize mwanangu. Na wewe mume wangu, kwa nini tusitafute muda mwingine wa kuyazungumzia haya matatizo? Sidhani kama hapa ni sehemu sahihi,” alisema mama yake Samantha kwa upole, baba yake Samantha akashusha pumzi ndefu na kuweka matunda na juisi alivyomnunulia mgonjwa kisha akatoka bila kuzungumza chochote.

    “Mwanangu jikaze usibishane na baba yako kwa chochote, anaonekana amechanganyikiwa, msije mkasababisha matatizo mengine zaidi.”

    “Mama mimi nimeshasema, kama hamuendi kumtoa Edmund polisi tusilaumiane kwa kitakachotokea,” alisema Samantha huku akiangua kilio cha kwikwi.



    Mama yake akawa na kazi ya ziada ya kumtuliza lakini bado alishikilia msimamo wake uleule.

    ***



    Siku ya kwanza ilikuwa ngumu mno kwa Edmund kwani maisha yake yote hakuwahi kuingizwa mahabusu hata siku moja wala hakuwahi kufikiria kama inaweza kutokea siku akawekwa nyuma ya nondo. Kitendo hicho kikamvuruga kabisa kichwa chake, akajikunyata kama kifaranga cha kuku kilicholowanishwa na mvua.

    Aliona kama saa zinakwenda taratibu mno, muda ukawa unazidi kuyoyoma huku taratibu akianza kuzoea mazingira ya selo. Ile hewa nzito iliyompa sana shida kupumua wakati anaingizwa, akaanza kuiona kuwa ya kawaida.

    Siku hiyo ilipita lakini mpaka adhana ya alfajiri inasikika kuashiria mwanzo wa siku mpya, Edmund hakuwa amelala hata kidogo. Muda wote alikuwa akiendelea kusumbuliwa na mawazo machungu ndani ya moyo wake, muda mwingine akijikuta anashindwa kuyazuia machozi yasiulowanishe uso wake.

    Baadaye mahabusu wengine walianza kuamka mmoja baada ya mwingine na kumkuta Edmund akiwa kwenye mkao uleule waliomuacha nao kabla ya kulala. Wakawa wanamzodoa na kumchokoza kwa maneno ya hapa na pale lakini mwenyewe hakujali.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muda ulizidi kuyoyoma na baadaye, wafungwa wote walitulia baada ya kusikia mlango wa mahabusu ukifunguliwa. Kama ulivyokuwa utaratibu wa askari wanapoachiana zamu kuhakiki kama mahabusu wote wapo, ndicho kilichofuatia ambapo mmoja baada ya mwingine alianza kuitwa jina ili kuhakikisha kama yupo.

    Baada ya kukabidhiana, wale askari waliokuwepo usiku waliondoka kwenda kupumzika na wakaingia askari wengine ambapo taratibu za kazi ziliendelea kama kawaida, mahabusu walioletewa chai wakawa wanaitwa mmoja baada ya mwingine na kwenda kupokea mizigo yao.

    Edmund alijua hakuna mtu anayeweza kwenda kumuona kutokana na jinsi tukio lenyewe lilivyokuwa kwa sababu hata kazini alikuwa haendi kwa siku kadhaa, tangu siku aliponusurika kufa baada ya kukutana na Samantha kwa mara ya kwanza. Akajua itakuwa vigumu sana kwa taarifa za mahali alipo kuwafikia watu wake wa karibu, alichokuwa anasubiri ikabaki kuwa muujiza tu.

    Muda ulizidi kuyoyoma na majira ya kama saa sita mchana, Edmund alishtuka baada ya kusikia jina lake likiitwa na askari aliyekuwa mlangoni, harakaharaka akainuka na kumfuata yule askari.

    Akatolewa mpaka nyuma ya kaunta bila kusemeshwa chochote. Akashangaa anarudishiwa viatu na mkanda wake pamoja na vitu alivyovuliwa jana yake wakati akiingizwa.

    “Mheshimiwa, kijana mwenyewe ndiyo huyu?” askari yule aliyemfuata Edmund selo alihoji, Edmund akawa anageuka huku na kule kuangalia ni nani atayejibu swali hilo kwa sababu hakukuwa na mtu yeyote anayemjua.

    “Ndiyo yeye!” alisema mwanaume wa makamo aliyekuwa ndani ya gari lenye vioo vyeusi vilivyokuwa vimeshushwa kidogo.

    “Shikamoo!” Edmund alimsabahi mwanaume huyo kwa hofu huku akiwa makini kumchunguza kama alishawahi kumuona sehemu lakini kumbukumbu zake hazikumpa majibu.

    “Ingia ndani ya gari!” alisema mwanaume huyo bila hata kujibiwa salamu yake, Edmund akatafakari kama aingie au la kwa sababu hakuwa na imani na usalama wake tena, akawa anahisi jambo lolote linaweza kumtokea, hata kuuawa kinyama kutokana na jinsi baba yake Samantha alivyoonesha kuwa na hasira.

    Akiwa bado anasuasua, Edmund aliingizwa kwenye gari na yule askari aliyemtoa mahabusu, akashangaa naye akiingia kwenye gari na safari ya kuondoka eneo hilo ikaanza. Kitendo cha yule askari naye kuingia ndani ya gari, kidogo kilimpa amani Edmund ndani ya nafsi yake, akawa na uhakika kwamba hakuna jambo lolote baya linaloweza kumtokea.

    Safari iliendelea, dereva akawa anaendesha gari kwa kasi kama anayewahi tukio muhimu, muda mfupi baadaye waliwasili Kinondoni, gari likaiacha barabara kubwa ya lami na kuingia kwenye barabara za mitaani, likazidi kukata mitaa kabla ya baadaye kutokezea mbele ya jengo kubwa la ghorofa kadhaa ambalo ndani yake kulikuwa na Hospitali ya Planet Health au PH kama wengi walivyozoea kuiita.

    Sifa kubwa ya hospitali hiyo ilikuwa ni huduma za daraja la kwanza za afya ambapo licha ya gharama zake kuwa kubwa, watu wengi kutoka familia tajiri walikuwa wakipenda kwenda kutibiwa hapo kutokana na ubora wa huduma zake. Japokuwa Edmund hakuwahi kutibiwa hapo lakini alikuwa akizifahamu vyema sifa za hospitali hiyo.

    Hata hivyo, tofauti na siku nyingine zote, eneo lote la hospitali lilikuwa limezingirwa na umati mkubwa wa watu kuashiria kwamba kulikuwa na tukio kubwa lililogusa hisia za wengi, kiasi cha kuwalazimu kuacha kazi zao na kubaki wakishangaa.

    “Kuna nini tena hapa?” Edmund alijiuliza akiwa anaendelea kushangaa jinsi umati wa watu ulivyokuwa mkubwa. Miongoni mwao, aliwaona waandishi wengi wa habari waliokuwa bize kupiga picha huku na kule huku wengi macho yao yakiwa juu kabisa ya jengo hilo lililokuwa na ghorofa kumi.

    “Tumefika, kijana hebu shuka,” alisema yule dereva, askari aliyekuwa amekaa na Edmund akafungua mlango na kumshika mkono Edmund, yule dereva naye akateremka na ‘kulock’ gari, yule askari akawa anamuongoza Edmund kupenya kwenye umati mkubwa wa watu uliokuwa eneo hilo kuelekea mapokezi huku yule mwanaume mwingine akiwafuata kwa nyuma.

    “Mungu wangu, kwani kuna nini hapa? Mbona mapigo ya moyo yananienda kasi kiasi hiki?” Edmund alijiuliza wakati wakielekea mapokezi. Mpaka muda huo, bado hakuwa anaelewa kilichokuwa kinaendelea eneo hilo. Wingi wa watu na jinsi walivyokuwa na taharuki vikazidi kumchanganya kichwa chake.

    “Mhusika huyu hapa tumekuja naye, tunaomba msaada wa kumfikisha juu haraka iwezekanavyo kabla mambo hayajaharibika,” yule mwanaume alizungumza na askari wengi wenye silaha waliokuwa wametanda mapokezi, Edmund akazidi kupigwa na butwaa hasa baada ya kusikia akitajwa kwamba yeye ndiye mhusika.

    Akiwa bado anaendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu, Edmund aliingizwa kwenye lifti chini ya ulinzi na yule mwanaume akabonyeza kitufe ukutani. Lifti ikaanza kupanda juu mpaka ilipofika kwenye ghorofa ya mwisho.

    Harakaharaka wakateremka huku Edmund akiendelea kushaangaa huku na kule, akashangaa yule mwanaume akielekea kwenye ngazi ndogo zilizokuwa zinaelekea upande wa juu kabisa wa jengo hilo, mahali ambako hakukuwa kukitumika.

    “Nifuate harakaharaka,” alisema yule mwanaume, wakawapita askari wengine wawili waliokuwa wamesimama eneo hilo, kila mmoja akiwa na silaha mkononi, wakapanda ngazi hizo na kutokeza upande wa juu kabisa wa ghorofa hilo.

    “Mungu wangu,” alisema Edmund kwa mshtuko mkubwa baada ya kukutana uso kwa uso na baba yake Samantha aliyekuwa amemshikilia mama yake Samantha aliyekuwa analia kwa uchungu huku akilitaja jina la mwanaye kama anayemsihi jambo fulani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Edmund akiwa bado anatazamana na mzee huyo huku kijasho chembamba kikimtoka, aligundua kwamba macho yake yalikuwa yamevimba na kubadilika rangi na kuwa mekundu kuonesha kwamba naye alikuwa akilia.

    “Amekuja,” alisema baba yake Samantha kwa kifupi na kusababisha mkewe aliyekuwa akiendelea kulia apatwe na mshtuko mkubwa, akajitoa mikononi mwake na kusimama wima, akawa anamkodolea macho Edmund akiwa ni kama haamini.

    “Ahsante kwa kuja Edmund, tuko chini ya miguu yako tunaomba utusaidie,” alisema mwanamke huyo na kumvaa Edmund mwilini huku akiendelea kulia. Bado Edmund hakuwa anaelewa chochote kilichokuwa kinaendelea, ikabidi waanze kumfafanulia kwa kina.

    “Samantha anataka kujirusha ghorofani, ameweka mgomo kwamba kama asipokuona basi leo ndiyo mwisho wa maisha yake,” alisema mama yake Samantha huku akiendelea kulia.

    “Mungu wangu, yuko wapi?” alihoji Edmund huku na yeye akionesha kuchanganyikiwa kuliko kawaida. Alikuwa anatambua jinsi msichana huyo mrembo alivyokuwa anampenda lakini hakuwahi kudhani hata siku moja kwamba anaweza kuchukua uamuzi mgumu kiasi hicho.

    “Yupo nyuma ya haya matanki ya maji, hataki mtu yeyote amsogelee ndiyo maana tumekaa mbali, tunakuomba nenda kazungumze naye,” alisema mama yake Samantha huku akiendelea kulia. Yule mwanaume aliyeongozana na Edmund kutoka kituo cha polisi, akatingisha kichwa kuashiria kuunga mkono kilichokuwa kinazungumzwa na mwanamke huyo.

    Edmund akaelekezwa upande aliokuwepo Samantha na kutakiwa kuwa makini kwani kwa hali ilivyokuwa, Samantha alikuwa tayari kufa muda wowote. Huku akitetemeka, Edmund alianza kutembea kwa kunyata kuelekea upande ule alioelekezwa.

    Baada ya kuyavuka matanki yale makubwa ya maji yaliyokuwa yakisambaza maji kwenye jengo zima, alitokezea kwenye uwazi ambapo aliweza kumuona vizuri Samantha, akiwa amesimama kwa msaada wa magongo kutokana na mguu wake mmoja kujeruhiwa kwa risasi.

    Alikuwa amesimama kwenye kingo za ghorofa hilo, akiwa amevalia nguo wanazovaa wagonjwa wanaolazwa kwenye hospitali hiyo huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya hofu.

    “Samantha! Samantha!” Edmund aliita kwa sauti ya upole huku akiendelea kutembea taratibu kumfuata msichana huyo ambaye muda wote alikuwa akiwatazama mamia ya watu waliokuwa wamefurika chini ya ghorofa hilo, wakiwa na shauku kubwa ya kutaka kuona ni jambo gani litakalotokea.



    “Ni mimi Edmund, nimekuja mpenzi wangu,” alisema Edmund kwa sauti ya kubembeleza lakini msichana huyo hakutaka kugeuka, akaendelea kutulia vilevile kama hasikii chochote.

    “Samantha, niko chini ya miguu yako mpenzi wangu, naomba ugeuke unitazame, nimekuja kukuchukua. Nakupenda sana na sipo tayari kuona jambo lolote baya linakutokea,” Edmund aliendelea kumbembeleza msichana huyo, taratibu akaanza kugeuza shingo yake na muda mfupi baadaye alikuwa akitazamana uso kwa uso na Edmund.

    “Ooh! Mungu wangu, kumbe kweli ni wewe mpenzi wangu? Siamini! Siamini,” alisema msichana huyo na kuanza kuangua kilio kwa nguvu. Edmund akazidi kumsogelea huku akimuonesha ishara kwamba na yeye asogee ili wakutane katikati, jambo ambalo Samantha alilitii na kuanza kujikongoja na magongo yake huku akiendelea kulia kwa uchungu.

    Hatimaye wakakutana ambapo Samantha alitupa magongo yake, akamrukia Edmund na kumkumbatia kwa nguvu huku akiendelea kulia kwa sauti kubwa. Kufumba na kufumbua askari kadhaa waliokuwa na silaha waliwazunguka na kuhakikisha Samantha hasogei tena kule alikotaka kujirusha.

    Wazazi wa Samantha nao walisogea eneo hilo, kila mmoja akitokwa na machozi ya furaha kwani hawakuamini kwamba hatimaye Edmund alifanikiwa kumuokoa kutoka kwenye shimo la mauti. Waandishi wa habari nao hawakuwa nyuma, kila mmoja alikuwa akipiga picha kwa kasi kuhakikisha hakosi tukio hata moja.

    “Nini kimekusibu mpenzi wangu?”

    “Siwezi kuishi bila wewe Edmund na ndiyo maana nikafikia hatua ya kutaka kuyakatisha maisha yangu baada ya kujua kwamba wameenda kukufunga kwa makosa ambayo hujafanya,” alisema Samantha kwa uchungu kisha akambusu Edmund mdomoni huku akionesha kuwa kwenye hisia nzito.

    “Usijali mpenzi wangu, niko salama kabisa,” alisema Edmund huku naye akimbusu Samantha sehemu mbalimbali za mwili wake. Hakuna aliyejali kwamba walikuwa wamezungukwa na askari, wazazi wa Samantha na waandishi wa habari. Kila mmoja alimuonesha kwa vitendo mwenzake jinsi alivyokuwa anampenda.

    Muda mfupi baadaye, madaktari wawili na manesi walifika eneo hilo na kusimama pembeni kusubiri maelekezo yatakayotolewa.

    “Afande, naomba arudishwe wodini kwa sababu hali yake bado siyo nzuri.”

    “Hapana daktari, inabidi usubiri kwa sababu si unajua kujaribu kujiua ni kosa kisheria?” alisema askari mmoja aliyeonesha kuwa na mamlaka kuliko wenzake. Baba yake Samantha akamvuta pembeni askari huyo na kuanza kuzungumza naye.

    Muda mfupi baadaye, amri ikatolewa kwamba Samantha arudishwe wodini kisha Edmund arudishwe alikokuwa.”

    “Siendi sehemu yoyote bila Edmund, kama mnataka nirudi wodini lazima niende naye,” alisema Samantha huku akimng’ang’ania Edmund mwilini, askari wakatazamana kisha yule kiongozi wao akaomba kuzungumza tena na baba yake Samantha. Wakawa wanajadiliana nini cha kufanya.

    “Mzee unampenda binti yako?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nampenda sana lakini sipo tayari kumuona akiwa na huyu mshenzi, haiwezekani.”

    “Kwani kikubwa kinachokufanya umchukie huyu kijana ni nini?”

    “Anamtumia mwanangu kimapenzi na kama hiyo haitoshi, alijaribu kumuua kwa kumpiga risasi na tayari kesi yake imeshafunguliwa.”

    “Lakini mbona inavyoonesha ni kama wanapendana sana? Huyu kijana anaweza kweli kujaribu kumuua msichana anayempenda kiasi hiki?”

    “Kwa hiyo unafikiri mimi naongopa, si ndiyo?”

    “Hapana, siyo hivyo mzee, najaribu kuzungumza na wewe ili kuzuia lisitokee tukio jingine kama hili lililotokea. Unafikiri kama juhudi kubwa za kwenda kumtoa mahabusu huyu kijana zisingefanyika mwanao angekuwa hai mpaka hivi sasa? Angeshakuwa amejirusha ghorofani. Hulioni hili?”

    “Kwa hiyo unataka kusemaje afande?”

    “Najua una hasira lakini nakuomba uongozwe na busara katika hili, utasababisha madhara makubwa kwa binti yako mwenyewe. Kama kweli unampenda kwa muda huu mpe uhuru wa kufanya anachokitaka mpaka atakapopona, kwa sababu kwanza siyo mtoto mdogo kama unavyofikiri,” alisema askari huyo na kuendelea kumsisitiza baba yake Samantha kwamba kitendo cha kuendeleza ubabe wake dhidi ya Edmund kingesababisha madhara makubwa zaidi.

    Baada ya majadiliano ya muda mrefu, hatimaye mzee huyo aliamua kuruhusu kwa shingo upande Edmund akae wodini na Samantha lakini kwa maelezo kwamba ni lazima aendelee kuwekwa chini ya ulinzi. Baada ya askari kujadiliana, nao walikubaliana kwamba kwa sababu ya hali halisi ilivyo, Edmund aachiliwe kwa dhamana huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufanywa.

    “Ahsante Samantha! Ahsante sana.”

    “Ahsante kwa lipi Edmund? Mimi ndiyo natakuwa kukushukuru wewe.”

    “Msimamo wako thabiti umesababisha niachiwe kwa dhamana. Mahabusu kubaya mpenzi wangu, usiombe yakukute, bora usimuliwe tu,” alisema Edmund huku akitingisha kichwa chake kwa ishara ya kuhuzunika.

    “Usijali Edmund, nikisema nakupenda namaanisha kweli nakupenda, ni bora nife kuliko kuishi bila wewe,” alisema Samantha huku akionesha kumaanisha kile alichokuwa anakisema. Wakaendelea na mazungumzo ya hapa na pale huku Edmund akimsihi asirudie kufanya jaribio lingine la kuyakatisha maisha yake kwa sababu Mungu hajaribiwi.

    “Nimekuelewa mpenzi wangu lakini mimi nina wazo.”

    “Wazo gani mke wangu mtarajiwa.”

    “Kabla hatujatokewa na haya matatizo tulikuwa tumepanga tutoroke na kwenda kuishi mbali na jiji hili ili tuwe huru. Bado nataka mipango yetu iendelee.”

    “Mpaka upone Samantha, unafikiri tutaondokaje ukiwa na hali kama hiyo? Isitoshe mimi nimeachiwa kwa dhamana, huoni kama itakuwa ni tatizo jingine?”

    “Sasa tufanyeje mpenzi wangu?”

    “Kwa hapa tulipofikia, inabidi tuwe wapole haya mambo yatulie kwanza kisha baada ya hapo ndiyo tutajua nini cha kufanya,” alisema Edmund lakini Samantha akaonesha kutokubaliana na maelezo hayo. Wakaendelea kujadiliana kwa muda mrefu lakini bado hawakufikia makubaliano.

    “Halafu huu ni muda wa mimi kwenda kazini kuripoti, unajua tangu nilipopatwa na matatizo sijaenda hata siku moja.”

    “Wala huna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu kazi, hata ukiacha naamini kwa fedha nilizonazo tutaishi kwa raha mustarehe kwa kipindi kirefu wakati tukiangalia upya namna ya kuyajenga maisha yetu,” alisema Samantha, Edmund akamuitikia ili kumridhisha lakini moyoni alipanga kuwa ni lazima aende kazini kwao atakapopata nafasi. Baada ya wawili hao kukaa pamoja wodini kwa muda mrefu huku Samantha akionesha kuchangamka sana tofauti na kabla ya ujio wa Edmund, mama yake Samantha aliingia akiwa na mfanyakazi wake wa nyumbani, wakiwa na vyakula kwa ajili ya wawili hao.

    “Nakushukuru sana baba’angu kwa kutusaidia kumtuliza huyu mwenzio. Nakuomba usimsikilize baba yake, nisikilize mimi na Samantha, upo kwenye mikono salama,” alisema mama yake Samantha, Edmund akaitikia kwa adabu na kumshukuru kwa yote.

    Chakula kikaandaliwa ambapo tofauti na siku zote, Samantha alikula sana huku akiendelea kupiga stori za hapa na pale na Edmund, wakawa wanacheka kwa furaha.

    “Mwanangu, naomba kila muda wa chakula ukifika uwe unahakikisha unakula na Samantha. Unajua siku zote huwa anatusumbua lakini leo amekuona pembeni yake mpaka nimeshangaa jinsi alivyokula, akiendelea hivi atapona haraka,” alisema mama yake Samantha na kusababisha wote waangue kicheko.

    ***

    Baada ya kuona mpango wake wa kuwatenganisha Samantha na Edmund umeshindikana kwa njia za kawaida, baba yake Samantha aliondoka hospitalini hapo bila kuaga, huku akiwa na hasira kali ndani ya moyo wake.

    “Lazima kile kibabu Shiwinga kitakuwa kinajua kila kitu na kiliamua kunificha, sasa leo naenda kukifunza adabu,” alisema baba yake Samantha akiwa kwenye gari lake, akichanja mbuga kuelekea Bagamoyo, nyumbani kwa mganga Shiwinga huku kiunoni akiwa na bastola.

    Kwa kilichotokea, alihisi kama Shiwinga amemsaliti sana na adhabu pekee ambayo alikuwa akistahili ilikuwa ni kifo. Hakuna kitu ambacho hakuwa tayari kuona kinatokea kama utajiri wake kupukutika kwa sababu ya makosa ya mwanaye kuruhusu kuingiliwa kimwili na mwanaume.

    “Nitafanya kila kitu kulinda utajiri wangu, hata ikibidi kuua watu wote wanaonikwamisha,” alijisemea baba yake Samantha huku akikanyaga mafuta na kusababisha gari liwe linakimbia kwa kasi kubwa.

    Baada ya takribani dakika thelathini, tayari alikuwa amewasili Bagamoyo, akaiacha barabara ya lami na kuingia upande wa kulia na kuanza kuifuata barabara nyembamba ya vumbi iliyokuwa ikielekea nyumbani kwa mganga huyo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akawa anazidi kukanyaga mafuta kuelekea nyumbani kwa mganga Shiwinga huku mara kwa mara akiikagua bastola yake kama ipo sehemu husika. Kwa jinsi alivyokuwa amekasirika, alikuwa tayari kufanya chochote, roho ya akishetani ilishampanda na hakukuwa na kitu chochote cha kumzuia kutimiza azma yake.

    Mganga Shiwinga akiwa anaendelea na majukumu yake ya kawaida ya kuandaa dawa za mitishamba na tunguli za kufanyia shughuli zake za kiganga, alishtuka kuona nywele na vinyweleo vinamsisimka mwili mzima.

    “Hiki nini tena,” alisema huku akiacha kila alichokuwa anakifanya na kukimbilia kwenye chumba chake cha uganga. Kusisimkwa nywele na vinyweleo mwili mzima, kwake ilikuwa ni ishara tosha kwamba kuna jambo halikuwa sawa.

    Harakaharaka akakaa kwenye mkao maalum na kuseti mitambo yake ya kiganga kwa lengo la kutaka kuona kilichokuwa kinakaribia kutokea. Ndani ya muda mfupi tu baadaye, tayari rada zake zote zilikuwa zimewashwa na kumuonesha kilichokuwa kinataka kutokea.



    Kwa kutumia nguvu zake za giza, alifanikiwa kumuona baba yake Samantha akija kwa kasi kubwa, hali iliyoashiria kwamba lazima atakuwa anakuja kwa shari, akashusha pumzi ndefu na kuanza kutafakari nini cha kufanya.

    Japokuwa alikuwa amefanya kazi kwa kipindi kirefu na baba yake Samantha, alikuwa anazijua akili zake zinavyobadilika anapokuwa na hasira, hasa kwa mambo ambayo yalikuwa yakihusu utajiri wake. Akajua asipochukua tahadhari, anaweza kumdhuru kweli kama alivyofanya kwa Samantha wakati akijaribu kumdhuru Edmund.

    Harakaharaka aliinuka na kutungua furushi lililokuwa kwenye paa la nyumba yake, akalitoa na kuanza kupekuapekua, akatoa kimfuko kidogo cha ngozi ya mnyama wa porini ambacho ndani yake kulikuwa na unga mweusi.

    Akachukua shuka jekundu na kujifunika nalo huku katikati ya miguu yake akiweka kitezo kilichokuwa na mkaa, akaanza kunyunyiza ule unga mweusi kwenye mkaa huku akizungumza kwa lugha aliyokuwa anaielewa mwenyewe. Moshi mwingi mweusi ukaanza kufuka na kusambaa eneo lote la nyumba yake, akaendelea kunuiza kwa muda mrefu.

    Upande wa pili, baba yake Samantha alizidi kukanyaga mafuta lakini tofauti na siku zote, alishangaa akizidi kuchanja mbuga tu bila kufika nyumbani kwa mganga huyo.

    “Nimepotea nini? Mbona sijawahi kufika huku?” alijiuliza baada ya kuona anazidi kuchanja mbuga tu bila kufika. Ikabidi atafute nafasi na kugeuza gari lake, akakanyaga mafuta kwa kasi kurudi alikotoka huku akiwa makini kuangalia njia ya kuchepuka kuingia nyumbani kwa mganga huyo.

    Hata hivyo, mpaka anafika kwenye barabara ya lami ya kuelekea Bagamoyo mjini, hakufanikiwa kuiona njia hiyo, akabaki amepigwa na butwaa. Akatafuta sehemu ya kugeuza na kuanza tena safari ya kwenda kwa mganga huyo.

    Kama ilivyokuwa mara ya kwanza, alisafiri umbali mrefu bila kufika nyumbani kwa mganga huyo, akashangaa anazidi kuzamia porini bila dalili zozote za kufika kwa mganga huyo. Mara kwa mara alikuwa akiikagua bastola yake huku shauku ya kukutana ana kwa ana na mganga huyo ikizidi kumpanda.

    Hata hivyo, licha ya kupiga ‘mark time’ kwa muda mrefu, hakufanikiwa kufika nyumbani kwa mganga huyo, baadaye akakata tamaa na kuamua kurudi jijini Dar es Salaam huku akiwa na maswali mengi yaliyokosa majibu juu ya kilichotokea.

    “Au amenifanyia dawa ya kunipoteza nini? Maana hashindwi yule,” aliwaza baba yake Samantha wakati akiendelea na safari ya kurejea jijini Dar es Salaam. Kwa kuwa mkewe alikuwa akimuuguza Samantha, nyumbani hakukuwa na mtu zaidi ya walinzi na wafanyakazi wa ndani.

    Alipowasili, moja kwa moja alienda mpaka kwenye chumba chake alichokuwa anafanyia shughuli zake za kiganga ambacho hakuna mtu mwingine yeyote aliyekuwa anaruhusiwa kuingia zaidi yake yeye mwenyewe. Akakaa humo kwa muda mrefu akijaribu kufanya dawa za hapa na pale ili kunusuru mali zake zisiendelee kuteketea.

    Baada ya kujifungia kwa zaidi ya saa mbili, alitoka na kuendelea na shughuli nyingine za pale nyumbani. Kwa kitendo alichooneshwa na binti yake, alijiapiza kwamba hatarudi tena hospitalini hapo kumjulia hali.

    “Nahisi kuna ulazima wa kusafiri kwenda Kasumbalesa, Sumbawanga kuongeza nguvu za giza, maji yamenifika shingoni,” aliwaza baba yake Samantha wakati akitafakari kuhusu uharibifu mkubwa wa vitega uchumi vyake uliotokea katika mazingira ya kutatanisha.

    Alipofikiria wazo hilo, alishusha pumzi ndefu kwani aliamini, kama ilivyotokea kipindi alichokuwa anahangaika kutafuta utajiri kabla hajakutana na mganga Shiwinga, lazima mambo yake yatanyooka tu kama mwanzo.

    Masharti ya safari ya Kasumbalesa, mpakani kabisa kati ya Tanzania na Zambia upande wa Sumbawanga, nyumbani kwa mganga Kiswigo Kachele, ilikuwa ni lazima aondoke bila kuaga, jambo ambalo kwake halikuwa gumu kutokana na jinsi alivyokuwa akiishi kibabe na familia yake.

    Hakutaka kupoteza muda, harakaharaka akawasiliana na kampuni ya usafiri wa ndege ya Katavi Airlines aliyokuwa akiitumia sana kwa safari za Sumbawanga, akakamilisha taratibu zote kwa ajili ya safari ya kuelekea huko alfajiri ya siku ya pili.

    “Mtaalamu Kiswigo anaweza kunisaidia, sijui kwa nini sikupata wazo la kukimbilia kwake haraka nilipoona mambo yameanza kwenda ndivyo sivyo,” aliwaza baba yake Samantha. Siku hiyo ilipita, kesho yake alfajiri na mapema aliwahi kuamka na kutoka na dereva wake aliyemuwahisha uwanja wa ndege.

    “Usimwambie mtu yeyote kwamba umenileta uwanja wa ndege, tumeelewana?”

    “Ndiyo bosi, nimekuelewa,” alijibu dereva kwa unyenyekevu, wakaagana ambapo dereva huyo alirudisha gari nyumbani na kuendelea na shughuli zake za kawaida. Baba Samantha aliingia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na baada ya taratibu zote kukamilika, aliingia ndani ya ndege na abiria wengine.

    Baada ya abiria wote kukaa kwenye siti zao, sauti ya mhudumu wa ndege ilisikika ikiwataarifu abiria wote kufunga mikanda, muda mfupi baadaye, ndege iliondoka na kuanza kupasua mawingu kuelekea Sumbawanga.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Lazima yule mtoto afe, na mganga Shiwinga naye anatakiwa kufa vilevile, uchawi wa ‘Lyamba Lya Mfipa’ ndiyo dawa yao,” aliwaza baba yake Samantha wakati ndege ikiendelea kupasua mawingu.

    Baada ya kusafiri kwa saa kadhaa angani, hatimaye ndege iliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga, tangazo likasikika kutoka kwenye vipaza sauti vilivyokuwa ndani ya ndege hiyo, likiwataarifu abiria wote kufunga mikanda wakati ndege ikijiandaa kutua.

    Dakika kadhaa baadaye, ndege ilikuwa imeshasimama kabisa, abiria wote, akiwemo baba yake Samantha wakaanza kuteremka. Baada ya kushuka tu, baba yake Samantha alitembea harakaharaka na kuwapita abiria wengine, akatoka mpaka nje ya uwanja huo na kukodi teksi.

    “Nipeleke Kasumbalesa haraka,” alisema baba yake Samantha, dereva wa teksi akawa ni kama anatafakari kidogo kwa sababu safari hiyo ilikuwa ndefu na ugumu ulikuwa unaongezwa na ubovu wa barabara, hasa katika kipindi hicho ambacho mvua kubwa zilikuwa zinaendelea kunyesha.

    Hata hivyo, kwa kuwa pesa haikuwa tatizo kwa mzee huyo, alimuahidi kumpa kiwango chochote atakachokitaka, cha msingi wafike. Baada ya dereva kutangaziwa dau, alikubali na safari ya kuelekea kijijini huko ikaanza.

    Njia nzima, baba yake Samantha alikuwa akiendelea kufikiria kuhusu adhabu itakayomfaa Edmund, hakuna kitu alichokuwa tayari kukipigania kwa kadiri ya uwezo wake wote, kama utajiri wake.

    Safari haikuwa nyepesi, mara kwa mara gari lilikuwa likikwama kwenye matope yanayonata, hali iliyosababisha wawili hao wawe wanashuka na kusaidiana kulisukuma. Mpaka wanafika kwa mganga, baba yake Samantha alikuwa amechafuka mwili mzima kwa matope ya udongo mwekundu.

    “Itabidi unisubiri turudi wote mjini, kama nitachelewa sana basi nitakuongeza dau, usiondoke tafadhali,” baba yake Samantha alimwambia dereva huyo, baada ya kufika sehemu ambayo gari lisingeweza kuendelea na safari kutokana na kukosekana kwa barabara, ikabidi yeye aanze kutembea kwa miguu kuelekea kwa mganga huyo na kumuacha dereva teksi kwenye gari lake.

    “Utajiri mgumu, yaani mzee huyu na heshima zake zote kumbe anakuja kwa mganga wa kienyeji?” aliwaza dereva huyo wakati akimtazama baba yake Samantha alivyokuwa anahaha kutafuta njia ya kupenya kuelekea nyumbani kwa mganga maarufu, Kiswigo Kachele aliyekuwa anaishi katikati ya pori kubwa la Kasumbalesa, mpakani kabisa mwa Tanzania na Zambia.

    “Hahahaaa!” sauti nzito ya mtu aliyekuwa anacheka ilisikika baba yake Samantha alipoukaribia mti mkubwa wenye matawi mengi yaliyofungana kiasi cha kusababisha kigiza chini yake, ndani ya eneo la mganga huyo. Kutokana na uzito wa sauti hiyo, ndege wengi waliokuwa kwenye mti huo walianza kuruka huku na kule kukimbia.

    “Nilijua utakuja! Mimi ndiyo fundi Kiswigo Kachele, mfalme wa ‘Lyamba lya Mfipa’, vua viatu fuata njia ya upande wa kushoto,” ilisikika sauti hiyo na kumfanya baba yake Samantha atetemeke kwa hofu. Japokuwa haikuwa mara yake ya kwanza kufika kwa mganga huyo, mauzauza aliyokuwa anakutana nayo kila akija, yalimfanya awe muoga sana.

    Baada ya kuvua viatu kama alivyoelekezwa, baba yake Samantha aliifuata njia nyembamba iliyokuwa upande wake wa kushoto, akawa anapita katikati ya majani marefu yaliyokuwa na umande, akazidi kusonga mbele mpaka alipotokezea sehemu yenye uwazi.

    Kwa mbali, akaiona nyumba ya tembe ya mganga huyo iliyokuwa imejengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi. Akiwa bado anashangaashangaa, bundi wawili walianza kumzunguka baba yake Samantha huku wakitoa milio ya kutisha, akajikaza kiume na kutulia, akawa anawatazama bundi hao ambao baada ya kumzunguka mara kadhaa, wote waliruka na kuelekea kwenye mlango wa ile nyumba ya tembe, wakaenda kutua mlangoni, mmoja kushoto na mwingine kulia.

    Bila hata kuuliza, baba yake Samantha alijua kwamba wale ni wasaidizi wa mganga Kiswigo waliotumwa kwenda kumpokea, akatembea kufuata uelekeo wale bundi walikoelekea na hatimaye akausogelea mlango wa ile nyumba ya tembe.

    “Geuka nyuma na uingie kwa kutanguliza mgongo,” ile sauti iliyosikika kule kwenye mti mkubwa, ilisikika tena, baba yake Samantha akatii maelekezo na kuingia kinyumenyume mpaka ndani, ile sauti ikampa maelekezo mengine na hatimaye akakaa juu ya ngozi ya mnyama wa porini ambaye hakumtambua ni mnyama gani.

    Baada ya kukaa na kutulia, vishindo vizito vya mtu vilianza kusikika kutokea nyuma ya pale alipokuwa amekaa, akatulia kimya kwani alijua ndiyo mganga Kiswigo alikuwa anatoka kwa ajili ya kuja kuonana naye

    Mwanaume mzee mwenye umri wa kati ya miaka 80 na 85, mwenye nywele nyingi zilizobadilika rangi na kuwa nyeupe kutokana na mvi, akiwa amejifunga shuka jeusi na kutembelea mkongojo ambao kwa juu ulikuwa na fuvu la mnyama wa porini, macho yake yakiwa mekundu ya kutisha, alitokeza mbele ya baba yake Samantha na kukaa juu ya kiti cha miguu mitatu.

    “Najua kinachokusumbua, mwanao amevunja masharti na kusababisha mwili wake uchafuliwe na mwanaume, mkuu wa giza amekasirika sana na kama usingewahi kuja, huenda ndani ya siku chache baadaye, utajiri wako ungekuwa umepukutika wote na wewe ingebidi uchukuliwe msukule kwa ajili ya kwenda kuwasaidia wenzako kazi kama ambavyo wamekuwa wakikusaidia wewe kwa kipindi chote cha utajiri wako.

    “Kibaya zaidi, umeshindwa kuitunza misukule inayokusaidia kazi na imeanza kuingia mitaani, hujui kama wakipatikana wachungaji wenye upako wa ukweli wanaweza kuwafungua vijakazi wetu na kusababisha watoe siri ya tulivyokuwa tunawatumikisha? Ukirudia tena uzembe kama huu utaadhibiwa kulingana na makosa yako,” alisema mganga huyo huku akionesha kuwa na hasira kali.

    “Ulinielekeza kwenda kwa mganga Shiwinga wa Bagamoyo, siku za nyuma alinisaidia sana lakini sasa hivi amenigeuka na yeye ndiyo chanzo cha yote haya. Nataka yeye na kijana aliyenichafulia binti yangu wafe kwa namna yoyote, hata ikibidi kuwatumia radi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Shiwinga siyo mwenzetu tena, alishasaliti kambi yetu na tunaendelea na mikakati ya kumpoteza ingawa anatusumbua sana kwa sasa, nguvu zake zimeongezeka sana,” alisema mganga huyo na kukohoa mfululizo, akafungua upindo wa shuka alilokuwa amejifunga na kutoa ungaunga fulani ambao aliunusa na kupiga chafya mfululizo kisha ghafla akayeyuka pale alipokuwa amekaa.

    Sekunde chache baadaye, alirejea na kukaa vilevile lakini mkononi mwake alikuwa na kitabu kilichochakaa sana, akakifutafuta vumbi juu yake na kumgeukia baba yake Samantha.

    “Matatizo yako yamefikia hatua mbaya, ni lazima utumie hiki kitabu kuweka mambo sawa. Kinaitwa kitabu cha shetani, sijawahi kukitoa kumpa mtu yeyote tangu niliporithishwa na marehemu babu yangu lakini kwa sababu ya matatizo yako, nakupa ukakitumie kisha utakirudisha mambo yakiwa sawa, sogea nikuoneshe namna ya kukitumia,” alisema mganga huyo kwa sauti ya kutetemeka kisha akapiga tena chafya mfululizo.

    Baba yake Samantha alisogea jirani na yule mganga ambapo alianza kumfundisha namna ya kukitumia kitabu cha shetani, mganga akawa anamsisitiza kwamba ni lazima afuate masharti yote anayompa vinginevyo anaweza kupata madhara makubwa.

    “Kabla hujakigusa kitabu hiki lazima uwe na udhu.”

    “Udhu? Udhu ndiyo nini mtaalamu?”

    “Kwani wewe unaabudu dini gani?”

    “Mimi Mkristo.”

    “Ndiyo maana hujui maana ya udhu. Namaanisha kabla hujakigusa hiki kitabu lazima mwili wako uwe safi. Nitakufundisha namna ya kuchukua udhu. Pia hutakiwi kuwa umetoka kukutana kimwili na mkeo au mwanamke yeyote ndani ya kipindi cha saa ishirini na nne kabla ya kukitumia.

    “Hutakiwi kunywa pombe au kutumia aina yoyote ya kilevi katika kipindi chote utakachokuwa unakitumia kitabu hiki. Muda mzuri wa kukitumia kitabu, ni usiku kuanzia saa saba mpaka alfajiri kabla adhana haijalia.

    “Kabla ya kukitumia kwa mara ya kwanza, lazima ufunge kwa saa ishirini na nne, usile wala kunywa kitu chochote kisha baada ya hapo, utakuwa unakula asubuhi na mchana tu, usiku hutakiwi kula kitu chochote mpaka utakapomaliza kazi.

    “Inachukua siku ishirini na moja kukamilisha mzunguko mmoja wa kutumia kitabu hiki, kila siku inatakiwa uzifanyie kazi kurasa saba za kitabu hiki, kwa hiyo katika muda wa siku ishirini na moja utakuwa umezifanyia kazi kurasa 147 na kitabu chote jumla kina kurasa 441 ambayo ni mizunguko mitatu. Umenielewa?”

    “Nimekuelewa mtaalamu.”

    “Kingine cha muhimu, katika kila kurasa saba utakazokuwa unazisoma kwa siku moja, kuna maelekezo ya nini cha kufanya. Lazima kila kitu kifanyike usiku wa siku husika, hutakiwi kutumia mwanga wa taa za umeme kusomea, inatakiwa utumie mishumaa mitatu, ukikosea masharti tusilaumiane,” alisema mganga huyo kwa msisitizo, baba yake Samantha akawa anatingisha kichwa kuonesha kuelewa alichokuwa anaambiwa.

    “Haya njoo huku nikufundishe namna ya kuchukua udhu kisha nianze kukuelekeza kwa vitendo namna ya kutumia kitabu,” alisema mganga huku akiinuka, baba yake Samantha naye akainuka na kumfuata. Wakatoka nje kupitia mlango wa nyuma na kwenda kwenye kisima kilichokuwa ndani ya eneo la mganga huyo.

    Akachota maji kwa kutumia kata iliyotengenezwa kienyeji na kujaza maji kwenye chungu kilichokuwa pembeni kisha akamuelekeza baba yake Samantha kukibeba chungu hicho hadi bafuni.

    “Inabidi kwanza uonge kuondoa janaba.”

    “Janaba ndiyo nini?”

    “Yaani wewe kila kitu hujui, nimechoshwa na maswali yako, nenda kaoge na uhakikishe unajisafisha kila sehemu ya mwili wako,” alisema mganga huyo huku akimpa baba yake Samantha mswaki wa mti.

    Akabeba chungu kilichokuwa na maji na kuelekea kwenye bafu lililojengwa kwa miti, akaoga kama alivyoelekezwa na mganga huyo kisha baada ya hapo, alitoka na kurudi pale kwenye kisima ambapo yule mganga alikuwa akimsubiri.

    Akaanza kumuelekeza namna ya kuchukua udhu kisha baada ya hapo, walirudi tena ndani ambako maelekezo yaliendelea.

    “Nimesahau kitu cha muhimu, unapotumia kitabu hiki ni lazima mavazi uliyovaa nayo yawe safi. Hutakiwi kuvaa nguo yenye jasho au uchafu wa aina yoyote na ndiyo maana huwa tunashauriwa kuvaa shuka jeupe.

    “Inabidi ukifika kwako na wewe ukatafute shuka jeupe, kwa leo nitakuazima langu,” alisema mganga huyo, akainuka na kuingia chumbani kwake, muda mfupi baadaye akarejea akiwa na mashuka mawili, moja lake na jingine kwa ajili ya baba yake Samantha.

    “Kabadilishe hizo nguo zako, vua zote kisha ujifunge hili shuka,” alisema mganga Kiswigo, baba yake Samantha akainuka na kuelekea kwenye chumba alichoelekezwa, muda mfupi baadaye alirudi akiwa ameshabadilisha nguo na kujifunga shuka jeupe.

    Mganga Kiswigo akamuelekeza namna ya kukaa kisha akachukua kitabu na kumkabidhi baba yake Samantha. Akamwambia akifungue.

    “Mbona hakijaandikwa kitu?” alisema baba yake Samantha, mganga Kiswigo akawa ni kama amekumbuka kitu, akamuonesha ishara kwamba amsubiri kidogo, akainuka na kuelekea chumbani. Aliporudi, alikuwa na kichupa kilichokuwa na unga mweusi, akamsogelea baba yake Samantha na kufungua kile kichupa.

    “Itauma lakini inabidi ujikaze,” alisema na kuanza kumnyunyizia unga ule machoni. Japokuwa alikuwa na roho ngumu, baba yake Samantha alishindwa kujizuia kutokana na maumivu aliyokuwa anayahisi, akajikuta akipiga kelele kama mtoto mdogo wakati unga ule ukimuingia machoni.

    “Utazoea tu wala usijali, fumba macho na usifumbue mpaka nitakapokwambia,” alisema mganga huyo, baba yake Samantha akatii, akaanza kuzungumza maneno ambayo hakuyaelewa huku akimzunguka na kumpigapiga na usinga aliokuwa ameushika. Baada ya kufanya hivyo mara kadhaa, alimwambia baba yake Samantha afumbue macho.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hiki kitabu huwa kinasomwa kuanzia mwisho kuja mwanzo, anzia ukurasa wa mwisho,” alisema mganga Kiswigo, baba yake Samantha akajifuta kwanza machozi na kufuata alichoambiwa. Alipofungua ukurasa wa mwisho wa kitabu hicho, alishangazwa sana na alichokiona.



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog