Search This Blog

NILITAFUNA MAITI YA MWANANGU NIWE TAJIRI - 4

 







    Simulizi : Nilitafuna Maiti Ya Mwanangu Niwe Tajiri

    Sehemu Ya Nne (4)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ILIPOISHIA...

    Safari kwenda hospitali ikaanza, kichwa changu kikiwa kimejawa na mawazo mengi ya vitisho vya mzee Mukulungu na serikali yake ya kichawi, sikujua jinsi ya kujinasua kutoka kwenye mtego huo lakini jambo nililoelewa ni kwamba sikuwa tayari kusaini mkataba wa kichawi na kuanza kuua watu. SASA ENDELEA...



    Dakika ishirini baadaye gari likiendeshwa kwa kasi, lilikata kona kuingia hospitali tukanyoosha moja kwa moja hadi mapokezi ambako muuguzi alikuwepo, akatupeleka moja kwa moja chumba cha daktari mke wangu akiwa amekalishwa kwenye kiti cha magurudumu.

    “Vipi?” Daktari aliuliza, alikuwa kijana mdogo tu, kwa miaka ya nyuma usingeweza kukubali daktari wa umri ule akuhudumie, alilingana kabisa na watoto wa kidato cha sita.

    “Mke wangu anaumwa.”

    “Nini?”

    “Tumbo.”

    “Mjamzito?”

    “Alikuwa mjamzito.”

    “Unamaanisha nini kaka yangu?”

    “Damu nyingi zinamtoka.”

    “Ooh! Dada unaweza kupanda hapo kitandani?”



    “Ndiyo.” Rita aliitikia na kwa msaada wa mimi na jirani yangu, tulimbeba na kumpandisha juu ya kitanda, daktari akachukua pazia lililounganishwa na vyuma na kukizungushia kitanda, kisha akatutaka mimi na jirani yangu tusimame nje ya pazia ili ampime mgonjwa, ampime bila mimi kuwepo? Nilijiuliza kichwani mwangu lakini sikuwa na jinsi, ikabidi nitii.



    Dakika kumi baadaye daktari alitokeza akivua mipira mikononi mwake, jambo lililoashiria kuwa alikuwa amempima mke wangu sehemu za siri, sikukipenda kabisa kitendo hicho lakini sikuwa na namna. Akaniangalia usoni, nami nikagundua masikitiko aliyokuwa nayo.

    “Pole sana ndugu yangu.”

    “Kwa nini daktari?”

    “Mimba imeharibika.”

    “Sijui kama tutakuja kupata mtoto?” niliuliza swali hilo nikimsikia Rita akigugumia kwa maumivu nyuma ya pazia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikuwa na siri nzito ndani ya moyo wangu ambayo nisingeweza kumweleza mtu, wachawi walikuwa wamedhamiria kuhakikisha sipati mtoto maisha yangu yote, mwisho wangeniua mimi mwenyewe kama adhabu sababu tu baba yangu alikiuka masharti ya uanachama wake wa uchawi. Jambo hili liliniumiza moyo sana, nikajiuliza jinsi ya kujinasua lakini sikupata jibu, nikainamisha kichwa chini huku machozi yakinibubujika.

    “Kwani ni mimba ya ngapi kuharibika?”

    “Ya tatu.”

    “Mna mtoto?”

    “Hatuna.”

    “Hii inaitwa kwa kitaalam Habitual Abortion, inabidi ufanyike uchunguzi wa kina kufahamu ni kwanini mimba zinaharibika.”

    “Hata ukifanya uchunguzi daktari sijui kama…”

    “Hapana usiseme hivyo, inawezekana kabisa tukaligundua tatizo.”

    “Siyo rahisi.”

    “Kwanini unasema hivyo? Kuna jambo unalijua?”

    “Hapana daktari!”



    “Acha tumpeleke chumba cha upasuaji tukamfanyie Evacuation, kesho utafanyika uchunguzi wa kina kufahamu ni kwa nini mimba zinatoka mfululizo.”

    “Hilo neno la Kiingereza ulilolisema sielewi maana yake.”

    “Evacuation?”

    “Ndiyo.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni kitendo cha kusafisha mfuko wa uzazi baada ya mimba kuharibika.”

    “Ahsante daktari.”

    “Mna bima?”

    “Hapana.”

    “Kwa hiyo mtalipia taslimu?”

    “Sina fedha.”

    “Mh!”

    “Ni kiasi gani daktari?” jirani aliuliza.

    “Inaweza kufika shilingi elfu arobaini.”

    “Nitazilipa.”

    “Ahsante jirani.”



    Tukaelekea dirishani kufanya malipo, baada ya hapo Rita akachukuliwa kwenye chumba cha upasuaji ambako mfuko wake wa uzazi ulisafishwa na kutolewa saa nzima baadaye, akiwa katika hali ya usingizi na kulazwa kwenye wodi ya wazazi.



    Jirani yangu baada ya hatua hiyo aliondoka na kuniacha nje ya wodi, nikabaki hapo mpaka asubuhi ya siku iliyofuata kichwa changu kikiwa kimejawa na mawazo mengi juu ya mambo yote niliyoyaona usingizini na vitisho nilivyokuwa nimepewa na mzee Mukulungu, ambaye tayari alishaitoa mimba ya mke wangu, hii ilionyesha kwamba alikuwa hatanii, kama nisingeusaini mkataba wao mwisho wa siku nisingekuwa na mtoto na wangeniua.



    “Siwezi kusaini, siwezi kuwa mchawi, bora nife!” niliendelea kukataa akilini mwangu.

    Mchana wa siku hiyo yote vipimo vingi vilifanyika ili kufahamu ni kwa sababu gani mimba za mke wangu zilikuwa zikitoka ilichukuliwa damu kwenda kupima homoni za uzazi na kitu kingine kiitwacho Rhesus Factor, ambacho niliambiwa huhusika sana na mimba kuharibika pale ambapo mtoto



    anakuwa na Positive wakati mama yake ana Negative, mama mjamzito hutengeneza askari mwilini mwake waitwao Anti D ambao huenda kumshambulia mtoto kwenye mfuko wa uzazi, kusababisha kifo chake na hatimaye mimba kuharibika.



    Pia akapigwa picha iitwayo Ultra-Sound kwenye mfuko wake wa uzazi, kuona kama kulikuwa na kasoro yoyote lakini vipimo vyote vilionyesha hapakuwa na tatizo la namna yoyote ile, madaktari wakashangaa, mwisho wakafikia uamuzi wa kuturuhusu mimi na mke wangu turejee nyumbani.



    Nililia mno tukiwa nyumbani kiasi cha kumfanya Rita awe na wasiwasi, kilichokuwa kikinisumbua moyoni mwangu ni siri nzito niliyokuwa nimeibeba ambayo nisingeweza kabisa kumshirikisha mke wangu. Niliumia kuona watoto ambao wangeniletea furaha maishani wakifa kikatili kwa sababu tu sikuwa tayari kuwa mchawi.

    “Darling mbona unalia sana?”

    “Basi tu.”

    “Au kuna jambo unajua?”

    “Mh! Mh!Mh!” niliishia kuguna tu.

    “Tafadhali nieleze.”





    “Naomba unieleze kama kuna chochote unachokifahamu juu ya haya yote yanayotutokea.” Rita alimuuliza Galos ambaye bado aliendelea kulia pamoja na kutulizwa kwa muda mrefu.

    “Hakuna ninachokifahamu.”

    “Sasa ni kwa nini unalia kiasi chote hicho?”

    “Inaniuma tu, kila ninapotarajia kupata mtoto, anayeyuka!”

    “Usijali mume wangu, tutapata tu mtoto mwingine, cha muhimu tuendelee kupendana.”

    Saa mbili baadaye Rita alikuwa usingizini, lakini Galos alikuwa macho, akili yake yote ikimuwaza Mukulungu na mambo aliyokuwa akimfanyia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakuwa tayari kusaini mkataka wa kichawi lakini pia alihitaji sana watoto maishani mwake akiwa na mke wake, kwa hali ilivyokuwa hofu ilikuwa imeanza kuugubika moyo wake kwamba Rita angeweza kumwacha, kama mimba zingeendelea kuharibika.



    Hilo ndilo jambo kabisa hakutaka litokee, maisha yasingekuwa na maana bila mwanamke aliyempenda. Macho yakaendelea kubaki wazi, akimsubiri kwa hamu Mukulungu, atokee na waondoke wote kwenda kwenye ulimwengu mwingine ambako alitaka kukutana na kuongea na Mukulungu ili amwache aendelee na maisha yake.



    Kulipokucha asubuhi alikuwa bado yu kitandani na mke wake, muujiza wa kwenda kwenye ulimwengu usioonekana haukutokea. Siku hiyo alishinda nyumbani na mke wake lakini siku iliyofuata aliingia mitaani kutafuta riziki, safari hii akiwa ameamua kufanya biashara ya kuuza maji kwa mkokoteni.



    Alifanya kazi hiyo asubuhi mpaka jioni na kurejea nyumbani akiwa taaban, hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, ya umaskini wa hali ya juu, akiishi eneo la watu maskini, ambalo lilitoa harufu mbaya saa ishirini na nne sababu watu waliachilia maji machafu ya chooni kutiririka mitaroni.



    Maisha yaliendelea kwa miezi sita, bila Rita kuugua, wala Galos kuchukuliwa tena na Mukulungu kwenda kwenye ulimwengu wa kichawi, lakini mwanzoni mwa mwezi wa saba, katikati ya usiku alishtukia anapigwa pigwa begani, alipofumbua macho alikutana moja kwa moja na uso wa Mukulungu ukiwa umejawa na tabasamu.

    “Twende!”



    Hakuwa na swali la kuuliza, akatupa jicho kumwangalia mkewe kando yake, usingizi aliokuwa nao ulikuwa mzito mno. Taratibu Galos alinyanyuka na kuanza kumfuata Mukulungu, kufumba na kufumbua wakajikuta wako chini ya mti mkubwa, mamia ya wachawi wakiwa wamekusanyika hapo, wakila nyama za binadamu zilizochomwa kwenye majiko makubwa.

    “Nimekupa muda mrefu sana wa kufikiria, umefikia uamuzi gani?”

    “Katika lipi?”

    “La uchifu.”

    “Wa wachawi?”

    “Ndiyo.”

    “Hilo nimekwishaligomea.”

    “Bado hutaki pamoja na kukufanyia mambo yote tuliyoyafanya?”

    “Ndiyo.”

    “Wewe maskini jeuri, lakini sikiliza, mkeo ni mjamzito tena, ukifanya mchezo hata huyo mtoto hutamwona.”

    “Ni mjamzito?”

    “Wewe hujui lakini mimi najua.”

    “Siyo kweli, angeshaniambia.”

    “Subiri utaona.”



    “Mukulungu tukamtese?” mtu mwingine aliyekuwa jirani aliuliza na Mukulungu aliuza akatikisa kichwa kuonyesha ishara ya kukataa, mwisho akamruhusu Galos aondoke zake, akanyanyuka na kuanza kutembea kuelekea gizani.

    ***



    “Mbona ulikuwa unaongea peke yako?”

    “Mimi?”

    “Ndiyo.”

    “Wapi?”

    “Usingizini.”

    “Nilikuwa naongea nini?”

    “Mambo mengi yasiyoeleweka, mara ujauzito, mara hutaki kusaini mkataba, ni mkataba gani huo?”

    “Ndoto tu darling.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Asubuhi kulipopambazuka, Rita aliondoka kitandani anakimbia kwenda nje kutapika, aliporejea alimpa Galos taarifa kwamba alikuwa na miezi miwili tangu apate hedhi mara ya mwisho, hapakuwa na sababu tena ya kutilia mashaka ambacho Galos aliambiwa na Mukulungu, roho ikamuuma kufahamu ya kwamba hata mtoto ambaye mke wake alikuwa naye tumboni pia asingemwona.

    “Sijui nitafanyaje?” aliwaza.



    Maisha yaliendelea vizuri baada ya hapo, ujauzito ukaendelea kukua na Galos akiendelea kufanya kazi zake ngumu za kimaskini, kila alichokipata alikitumia kumtunza mke wake. Wala hakujiwekea akiba yoyote ya kulea mtoto, sababu alifahamu lazima angekufa, mimba ilipotimiza miezi sita, Rita alianza kumsisitizia Galos aanze kununua vitu mbalimbali vya mtoto lakini kijana huyo aliishia kububujikwa na machozi.



    Mwezi wa saba, Galos akijua labda Mukulungu alishaahirisha adhabu yake, usingizi ulimpitia akajikuta katika ulimwengu wa wachawi ambako alianza kulazimishwa tena kusaini mkataba, akakataa. Vitisho vya kuua mtoto vikaendelea lakini bado hakubadilika, mwisho Mukulungu akabadilisha maelezo na kuanza kuzungumzia utajiri, hapo ndipo akaugusa moyo wa Galos.



    “Utakufa maskini, mimi naweza kukufanya uwe tajiri kuliko unavyofikiria, unachotakiwa ni kutimiza masharti.”“Kuwa tajiri nataka, ambacho sitaki ni kuwa mchawi.”

    “Basi kubali uwe tajiri kwanza!”

    “Bila kuwa mchawi?”

    “Inawezekana, suala la uchawi tutalifikiria baadaye.”

    “Sharti ni lipi?”

    “Kesho utarudi tutakuambia.”

    ***



    Ghafla Galos akazinduka akiwa kando ya mke wake aliyekuwa akiteseka kwa maumivu makali ya tumbo na kudai damu zilikuwa zikimtoka, mara moja akaelewa adhabu ilikuwa imefika. Hakuna la kufanya zaidi ya kutoka ndani ya nyumba kwenda kutafuta usafiri, jirani yuleyule wa awali alimsaidia kumpeleka Rita mpaka hospitali ambako ilithibitika mtoto alikuwa amefia tumboni.

    “Itabidi achomwe sindano za uchungu ili amsukume atoke, baada ya hapo atasafishwa.”



    Hicho ndicho kilichofanyika, Rita akapewa dawa hizo na kusukuma, mtoto mkubwa kabisa akatoka, baada ya hapo akasafishwa.

    Hali yake ilipotengemaa walikabidhiwa kichanga chao na kwenda kukizika makaburini, jirani kabisa na hospitali, wakarejea nyumbani wakiwa na huzuni, wote wakilia kwa uchungu, lakini Galos alilia zaidi.

    Usiku huohuo alipitiwa na usingizi mzito na kujikuta tena kwenye ulimwengu wa wachawi, Mukulungu alikuwa na maiti ya mtoto mchanga mikononi mwake,



    akamwambia Galos kwamba maiti ile ndiyo iliyotoka tumboni mwa mke wake, ilifukuliwa makaburini mara tu baada ya kuzikwa.

    “Hili ndilo sharti unalotakiwa kulitimiza, ule maiti hii ya mtoto wako, ndipo utakuwa tajiri! Uko tayari?”



    Mwili wa Galos ulikuwa ukitetemeka kama mtu mwenye homa kali, yote hiyo ilikuwa ni kwa sababu ya hofu. Moyo ulimuuma mno, kumwona Mukulungu ameshikilia maiti ya mtoto wake mkononi, tena kichwa chini miguu juu, akining’iniza.



    Machozi yakambubujika. Hakuna kitu alichokipenda maishani kama watoto, yeye na mke wake kwa muda mrefu walikuwa wametamani kuwa na mtoto pamoja na umasikini wao, waliamini huyo ndiye angewapa faraja lakini Mukulungu bila huruma aliua kila mtoto waliyempata.

    “Kwa nini mnanitendea hivi?” aliuliza kwa uchungu.

    “Unataka kuwa tajiri hutaki?”

    “Nataka!”

    “Basi timiza masharti.”

    “Huu ni unyama.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Umasikini unatenda unyama zaidi kuliko mimi, umeteseka kwa miaka mingi, hivyo basi kama umechoka na aina hiyo ya maisha, kula maiti ya mwanao!”

    Galos akainamisha kichwa, fikra zake zote zikarejea kitandani alikomwacha mkewe Rita akiwa



    mwenye huzuni. Mwanamke huyo asiye na hatia hakujua kabisa kilichokuwa kikiendelea maishani mwake, mwenye siri moyoni alikuwa ni mumewe, Galos akamwonea huruma, lakini hakuwa na jinsi, umasikini ulikuwa umemchosha, akapiga hatua na kusimama mbele ya Mukulungu.



    “Niko tayari, ili mradi tu mke wangu asije kufahamu siri hii.”

    “Hawezi kufahamu, mambo ya huku huwa hayasemwi, isitoshe yeye pia kama hatasaini mkataba wa kurithi kazi ya baba yako, atakufa!”

    “Tafadhali msimuue mke wangu.”

    “Achana na hiyo, chukua haka kamaiti ka mwanao ukakachome pale kwenye moto unaowaka, kisha ule, baada ya hapo utarejea nyumbani na kila kitu kitakachotokea kitakushangaza, utatajirika bila juhudi yoyote.”



    Galos akanyoosha mkono wake wa kuume, huku mkono wa kushoto akiutumia kufuta machozi na makamasi, akaishika maiti ya mwanaye miguuni, hivyohivyo akiining’iniza alitembea mpaka kwenye moto na kuiweka juu ya wavu, wachawi wote wakashangilia, wakimwita Shujaa.



    Maiti ilichomwa kama mshkaki au kuku juu ya jiko la mkaa, ikaendelea kudondosha maji na mafuta hatimaye ikakuka kabisa, ndipo Mukulungu akamwamuru Galos aiondoe kwenye moto na kwenda nayo kando ambako majani ya mgomba yalikatwa na kuwekwa juu yake, wachawi wengi wakamzunguka.

    “Kula! Kula uwe tajiri.” Mukulungu alisema.



    Huku akilia Galos akakata mguu wa maiti ya mtoto wake, macho yake yakiwa yamefumbwa, akaanza kuila bila huruma, kichwani mwake akiwaza utajiri, magari atakayokuwa akiendesha, majumba ambayo angemiliki, heshima ambayo angepewa katika jamii.



    Alipomaliza tu kula ghafla alizinduka usingizini na kumkuta mke wake ameketi kitako akilia, akaanza kumbembeleza na kumtuliza. Rita alitaka kufahamu ni kwa nini Galos alilia sana akiwa usingizini, lakini hakuambiwa ukweli. Wote wawili hawakulala usingizi, saa kumi na mbili kasorobo za asubuhi, Galos aliamka na kutoka nje ya nyumba yao kwenda msalani kujisaidia haja ndogo.



    Alipofungua tu gunia lililotumika kama pazia kwenye choo, alishangaa kuona kitu kiking’ara ardhini, taratibu akainama na kukiokota, kilimshangaza, alishasikia sana juu ya Almasi, Ruby na Dhahabu, hisia zake zilimtuma kudhani hiyo ilikuwa ni Ruby.



    Haja kubwa na ndogo zote zikakata, akasahau hata chooni alikwenda kufanya nini, haraka akarudi hadi ndani akiwa amekishika kipande cha jiwe alichokiokota mkononi mwake.

    Ndani hakuongea kitu, akaifuata suruali yake ya khaki iliyokuwa imetundikwa kwenye msumari na kukiweka ndani yake, uso wake ulikuwa umekunjuka na kujawa na furaha iliyomshangaza Rita.



    “Vipi tena?”

    “Ahaa!Ahaaa!”

    “Mbona umechangamka?”

    “Basi tu.”

    Jua lilipochomoza hakutaka hata kusubiri kifungua kinywa, aliondoka moja kwa moja akitembea kwa miguu hadi katikati ya jiji eneo la Kariakoo ambako alianza kutafuta mahali ambako watu walinunua madini, baada ya kuuliza alijikuta yuko mtaa wa Mafia, kulikokuwa na mnada wa wauza madini, akaingia kwenye moja ya ofisi.

    “Mnanunua madini?”

    “Ndiyo.”

    “Mnaweza kununua la kwangu?”

    “Lipi?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Galos hakuwa na jibu, alichokifanya ni kuingiza mkono mfukoni mwa suruali na kutoa kipande cha jiwe alichokuwa nacho na kukiweka juu ya meza, watu wote ndani ya chumba hicho walisimama na kuonyesha mshangao, hapo ndipo akaelewa alikuwa na kitu cha thamani alichokipata kimazingara.



    “Umeipata wapi Almasi kubwa kiasi hiki?”

    “Niliachiwa na baba.”

    “Mungu wangu! Hebu subiri.” Aliongea mtu huyo na kuiweka juu ya chombo kilichoonekana kuwa mzani.

    “Gramu ngapi?” mtu mwingine aliyekuwa chumbani aliuliza.

    “Mia moja na hamsini.”



    “Mungu wangu! Haijawahi kutokea hapa ofisini, nimefanya kazi hapa kwa miaka karibu thelathini, kijana umetajirika, una akaunti?”

    “Sina.”

    “Utatuuzia?”

    “Ndiyo, kama tutaelewana bei.”

    “Unauzaje?”

    “Kwani ninyi mna bei gani?”



    “Subiri.” Alisema mtu huyo akivuta mashine ya kupigia hesabu na kuanza kubonyeza namba fulanifulani, kisha akamwonyesha Galos, kulikuwa na sifuri nyingi zilizotanguliwa na mbili, kisha tano!

    “Kiasi gani hicho?”

    “Utapata milioni mia mbili na hamsini.”

    “Sawa.”



    Biashara ikawa imefanyika, bila Galos kuelewa thamani hasa ya Almasi yake, wanunuzi wakamsaidia kufungua akaunti kwenye benki ya kizalendo ya Wezesha Mzawa, kiasi cha milioni ishirini na tano akazichukua na kwa msaada wa watu haohao, akanunua gari aina ya Mark II, kuajiri dereva,



    kufanya manunuzi ya nguo za thamani kwa ajili yake ya mkewe, kutafuta nyumba ya kifahari ya kupanga maeneo ya Mikocheni.



    Mfukoni akabaki na milioni tatu baada ya kununua samani za ndani ya nyumba yake, ndipo akamwamuru dereva amwendesha kuelekea nyumbani. Alipofika, kitu cha kwanza alichofanya ni kupiga honi mbele ya kibanda chao, Rita akatoka akiwa ameshika sufuria la ugali na kumwaga ukoko kando ya barabara, kichwani mwake akiwa hajui kabisa ndani ya gari hilo alikuwemo mumewe.

    “Mpenziiiii!” Galos aliita, Rita akageuka kuangalia.

    “Hee!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog