Search This Blog

NILITAFUNA MAITI YA MWANANGU NIWE TAJIRI - 3

 







    Simulizi : Nilitafuna Maiti Ya Mwanangu Niwe Tajiri

    Sehemu Ya Tatu (3)





    ILIPOISHIA...

    "Sawa Mkuu," wote wakaitikia wakiinamisha vichwa chini.

    "Galos..." Mkuu akaniita.

    Sikuitikia!

    Siyo kwamba nilionyesha kiburi, sikuweza kufanya hivyo!

    SASA ENDELEA...



    KAMA moyo ungekuwa unaweza kuonekana, naamini bila shaka yoyote moyo wangu ungeonekana ukiwa unatetemeka kwa hofu. Sikuwa na hili wala lile. Nilihisi kuchanganyikiwa.

    Niliinua uso wangu na kuwatazama wale watu waliokuwa wamenizunguka, nikawaona kama wananikodolea macho mimi wakinishangaa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikazidi kuchanganyikiwa. Kuna mambo matatu yalikuwa yakiuchanganya sana ubongo wangu. Kwanza kuhusu mkataba! Naweza kusaini mkataba wa kishetani?



    Naweza kuingia kwenye makubaliano nisiyoyaelewa? Inamaana mimi niwe mchawi? Niliwaza. Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu lazima jambo hilo lingemchanganya kama ilivyokuwa kwangu.



    Pili ni kuhusu kunywa damu! Mimi nilikunywa damu ya mwanangu? Inawezekana vipi? Ni kweli nilipewa kitu kama juisi ambayo ladha yake sikuijua mara moja, lakini kwa nini niambiwe ilikuwa ni damu ya mwanangu?



    Damu ya mwanangu kivipi? Lingine kubwa kabisa lililoniumiza ni kuhusu kula maiti ya mwanangu. Nitaweza kumtafuna mwanangu? Kwa muda mrefu kiasi gani mimi na mke wangu tumehangaika kupata mtoto na mimba zinatoka!



    Leo iweje nije kula maiti ya mwanangu? Ni mambo ambayo yalizidi kunikoroga! Kwa namna fulani niliona ni bora kufa kuliko kula maiti ya mwanangu. Potelea mbali hata kama Rita atabaki katika mateso lakini hatanyanyasika tena maana atapata mwanaume mwingine ambaye atamzalia watoto.



    Mimi nisingeweza kumpa watoto kwa sababu tayari nilikuwa kama kafara la majini! Moyo wangu ulijaa huzuni sana, nikapata nguvu mpya na jeuri ya hali ya juu kunijaa moyoni. Nilimwangalia Mukulungu kwa hasira, sura yangu ikatangaza dharau ya wazi.

    Nilionekana waziwazi nilikuwa tayari kwa lolote!



    Ni kama nilikuwa nimejipanga sawasawa. Nikazidi kumkazia macho bila kuyapepesa kabisa. Naye akaniangalia kwa ukali. Muda uleule, nikaona kitu kama machozi yakidondoka machoni mwa Mukulungu. Nilipotazama vizuri, niligundua jambo jingine la kushangaza sana.



    Macho ya Mukulungu yalikuwa yakidondosha damu! Tena ilikuwa damu mbichi kabisa!

    "Galos! Galos! Galos!" akaita kwa ukali.

    "Ukali wako haunitishi," nikajikuta nimetamka kwa haraka nikiwa najiamini kuliko kawaida.

    Pamoja na woga niliokuwa nao tangu mtiririko wa tukio lile ulivyoanza, nilijishangaa sana kupata nguvu ya ajabu na ya ghafla sana mbele ya Mukulungu ambaye aliogopwa na kila mtu!

    "Unasemaje?"

    "Nipo tayari kwa lolote!"

    "Umeuuzunisha moyo wangu. Kwa hakika moyo wangu sasa unavuja damu....damu inachuruzika. Sasa nitakuuliza kwa mara ya mwisho kabla sijachukua hatua inayokustahili. Uko tayari kusaini mkataba au haupo tayari?" akauliza Mukulungu akinikazia macho.

    "Sipo tayari!"

    "Unasema?"

    "Sipo tayari."

    "Galos, una hakika na kinachotoka kinywani mwako."

    "Nasema sipo tayari kusaini ujinga!"



    "Paaaaa! Paaaaa! Paaaa!" ilikuwa ni mlio wa mikanda ikishuka mwilini mwangu.

    Sikuelewa ni nani aliyenipiga na alikuwa wapi. Nilihisi maumivu makali sana, mwili wangu ukaishiwa nguvu ghafla na nikahisi kutapika. Nilijilazimisha kutoa matapishi lakini haikuwezekana. Nikajitahidi tena na tena lakini haikuwezekana.



    "Mpelekeni kwenye hatua ya pili haraka! Huyu nitamalizana naye mwenyewe, hana ujanja huyu. Mpumbavu kabisa. Wa kumlaumu ni baba yako aliyeingia mkataba na sisi!" akasema Mukulungu.

    Wale watu haraka wakanivaa. Kila mmoja alikuwa akinisukuma huku akinipiga sehemu anayoona inamfaa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndani ya dakika kumi tu, tayari kila kiungo katika mwili wangu kilikuwa kimeshapigwa. Nililainika na nilipatwa na maumivu makali kuliko kawaida.



    Waliniburuza hadi kwenye chumba ambacho sikukielewa kilivyokuwa, lakini muda mfupi sana baadaye, nilipoteza fahamu kabisa! Sikujua chochote kilichoendelea.

    ***



    Nilihisi maumivu makali sana miguuni, mwili wangu ulikuwa una joto kali kuliko kawaida, baadaye nikagundua kuwa siyo joto tu, ni moto mkali ulikuwa unatembea mwilini mwangu. Nilipofumbua macho, nilishangaa kujiona nimening'inizwa, kichwa chini, miguu juu.



    Miguu yangu ilikuwa imefungwa kwa mnyororo juu ya kamba, mikono yangu ilikuwa chini lakini nayo ilikuwa imefungwa kwa mnyororo, chini kukiwa na moto ambao ulikuwa ukinielekea pale juu nilipokuwa nimefungwa!



    Nilikuwa nachomwa kama nyama!

    Ni eneo ambalo sikulijua ilikuwa ni wapi, lakini ilikuwa pembeni ya kitu kama ziwa au bahari, maana niliona nipo ufukweni. Nilipoangalia kando nikamuona Mukulungu akiwa na wenzake wawili wananitazama.



    Wote walikuwa wamekenua meno yao wakinicheka. Mukulungu ndiye aliyekuwa amebeba kitu kama faili lenye makaratasi. Akaacha kucheka na kusogea karibu yangu. Akanitazama kwa macho ya hasira sana.



    Alionekana kuwa na neno alilotaka kuzungumza...

    "Utakufa hapo mtini taratibu kama ng'ombe anavyobanikwa baada ya kuchomwa. Hili ni zoezi la mwisho kwako. Ni adhabu ya mwisho. Narudia tena hakuna adhabu nyingine, maana adhabu hii itakufikisha moja kwa moja kwenye kifo.



    "Sasa ni hiyari yako kusema, upo tayari kusaini mkataba uendelee na maisha yako na tukupe utajiri au ufe hapo mtini ukibanikwa kama nyama ya ng'ombe?" akasema Mukulungu akiniangalia kwa macho yanayosubiri majibu.



    "SITASAINI UCHAFU WENU, KAMA KUFA NIPO TAYARI KUFA!" nikamjibu kwa kujiamini.

    Nilihisi maumivu makali sana lakini sikuwa tayari kabisa kujiunga na mambo nisiyoyajua wala sikuwahi kuyaota. Nilikuwa tayari kwa lolote! Mukulungu na wenzake wakaonekana kunishangaa sana!

    "Unasemaje wewe?" Mukulungu akauliza.

    "Nilivyosema ndiyo hivyohivyo!"

    "Ongeza moto tafadhali," akasema Mukulungu.

    Muda huohuo, moto ukaongezeka ghafla. Nikahisi mwili mzima ukiungua.



    NIkweli kabisa, tena ukweli usio na shaka kwamba mara nyingi nimewahi kupata maumivu. Hata hivyo, nakiri sijawahi kupata maumivu makali kama ya moto ule uliokuwa ukiwaka chini yangu, nikiwa nimening’inizwa juu.



    Moto ulikuwa mkali sana, nilihisi mwili wangu ukiniteleza. Nikamkumbuka Rita wangu. Mwanamke wa maisha yangu ambaye nilimpenda kwa kila hali. Nakubali vipi kufa nimwache mwenyewe?

    Nilimwonea huruma sana. Sikujali mimi kufa, nilikuwa tayari kufa kuliko kuingia kwenye uchawi. Hata

    siku moja sikupenda uchawi. Sikuwahi kufikiria kuwa naweza kujiingiza kwenye mambo ya uchawi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mamaaaaaa...” nilipiga kelele.

    Nilipojaribu kuangalia eneo ambalo Mukulungu alikuwa amekaa na wale wazee, hakuwepo. Hapakuwa na mtu. Kwa mbali sasa nilianza kufikiri kubadilisha mawazo. Hata kama sitakuwa mchawi, nilikuwa tayari kukubaliana nao ili tu niokoke katika ule moto.

    “Rahisi sana...nasema nipo tayari, halafu wakinitoa hapa natoroka,” nikawaza.

    “Mkuuuuuu...” nikapiga kelele.

    Muungurumo mkali ukasikika.

    “Mkuuuuu,” nikaita tena.

    Muungurumo ukazidi.



    “Unataka nini? Kufa hapohapo mtini,” nikasikia sauti ambayo sikuwa na shaka kuwa alikuwa ni Mukulungu.

    “Hapana Mkuu, hapana.”

    “Hapana nini?” Sasa nikasikia sauti hiyo mbele yangu.

    Nikafumbua macho haraka, nikamuona Mukulungu akiwa mbele yangu. Amesimama ananitazama kwa macho makali. Machozi yalikuwa yakinitoka kwa kasi sana machoni mwangu. Machozi ukichanganya na damu, ilikuwa ni balaa juu ya balaa.

    “Nisaidie,” nikamwambia.

    “Umeshakuwa tayari kuwa nasi?” akauliza.

    “Ndiyo.”

    “Unasema?”

    “Ndiyo Mkuu.”

    “Ondoa moto!” akasema Mukulungu.



    “Myvuuuuuu!” mlio mkali kama upepo ukasikika, ghafla ule moto ukaondoka.

    Nikatetemeka. Mwili ulikuwa umeanza kutoka malengelenge, nikavuta pumzi ndefu sana kisha nikazishusha taratibu kabisa.

    “Niokoe Mkuu.”



    “Huwezi kuokolewa hapo kabla ya kukubali ninachokuambia,” akasema huku akiketi chini.

    “Ndiyo Mkuu.”

    “Kwanza lazima ujue kuwa sisi hatuna lengo baya na wewe. Kubwa zaidi ni kukusaidia. Tunahitaji kukusaidia maisha yako, acha ujinga.”



    “Sawa, lakini kwa nini mmenichagua mimi?”

    “Ngoja ushuke hapo juu kwanza tuzungumze,” akasema.

    Nilihisi kizunguzungu cha ghafla, kisha nikahisi kama nimepoteza fahamu hivi. Naam! Ni kweli nilipoteza fahamu. Sikujua kilichoendelea tena baada ya pale.

    ***



    Ni muda mfupi baada ya kutolewa kule kwenye ufukwe nilipokuwa nimening’inizwa. Sasa tupo kwenye chumba kilekile cha awali. Tofauti ni kwamba, wale watu waliokuwepo mwanzoni, safari hii hawakuwepo tena.



    Pale kulikuwa na Mango na Ngoma tu. Mukulungu alikuwa amekaa mbele yangu, tukawa tunatizamana. Kitu cha kushangaza ni kwamba, ule uvimbe na malengelenge niliyokuwa nayo kule ufukweni, hayakuwepo tena.



    Mwili haukuwa na maumivu tena. Ni kama hapakuwa na jambo lolote lililotokea kabla. Mukulungu alinikazia macho...

    “Sasa nisikilize...” akasema.

    “Ndiyo!” nikaitikia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ngoma na Mango, waliposikia kauli ya Mukulungu ikisema, sasa nisikilize, walisimama kwa wakati mmoja. Wakashikana mikono, halafu wakainamisha vichwa vyao chini, kisha wakaanza kutembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea mlangoni.



    Walipomalizikia mlangoni tu, Mukulungu akaendelea: “Galos kijana wangu.”

    Sauti ya Mukulungu sasa ilikuwa ya taratibu iliyojaa uungwana. Nilimshangaa kwa kweli. Sikutegemea kumsikia akizungumza nami kwa sauti iliyojaa unyenyekevu kama ile.

    “Unajua watu wanafikiria vibaya sana kuhusu uchawi na ushirikina. Nikuambie tu ukweli kuwa, siyo



    kitu kibaya. Hii ni aina ya sanaa ambayo huwa na makubaliano rahisi. Makubaliano hayo yakifanyika, utajiri unafuata.



    “Si kwamba unapewa utajiri kwa manyanyaso au unamdhuru mtu, hapana. Ni waongo wanaosema hivyo. Kwa mfano wewe ni kijana mzuri, una nyota nzuri, ni rahisi kuogelea kwenye utajiri kwa muda mfupi sana.



    “Mazungumzo haya yakifikia mwisho na tukakubaliana vizuri, wewe utakuwa tajiri mkubwa sana. Acha woga, achana na mawazo potofu. Tumia uwezo wako kinyota kubadili maisha yako. Hebu nikuulize, unafaidika nini kuishi maisha ya kijinga pale Tandale?



    “Kipi unachonufaika nacho kwa kiburi chako huku mkeo akiwa mgonjwa kila siku? Tumia akili. Sisi hatuna lengo baya na wewe. Jambo la msingi kujua ni kwamba, mwisho wa mazungumzo haya, ukiendelea na ule msimamo wako wa kukataa, UTAKUFA.



    “Lakini ukiwa mwerevu, ukaingia mkataba na sisi ambao kimsingi ni wa lazima kwa sababu ya marehemu baba yako, basi utaanza maisha mapya. Acha ujinga mwanangu. Acha upuuzi, wewe ni mtu mkubwa sana mwenye utajiri mkubwa kwenye maisha yako. Unanielewa?” akasema.

    Maneno yake yaliniingia sana, kiukweli nilijawa hofu sana. Sikuweza kumjibu haraka. Nilibaki namwangalia tu nisijue cha kufanya.



    “Galos...” akaniita.

    “Mkuu.”

    “Umenielewa?”

    “Ndiyo, lakini nataka kujua kuhusu baba yangu.”

    “Vizuri sana. Hebu sasa nikueleze kwa undani kuhusu baba yako,” akasema.



    “Angalia pale...” akasema akisonza kidole kwenye ukuta ambao kulikuwa na ngozi ya mnyama.

    Sikujua ni mnyama gani!

    Nikaangalia!

    Nilishuhudia mambo ya ajabu ya kushangaza. Hofu kuu ikanijaa, nikazidi kukodoa macho yangu. Mwili mzima ulitetemeka.



    Ngozi ile ya mnyama ukutani ambayo kwa kuiangalia ilifanana na ya Fisi ingawa sikuwahi kumwona zaidi ya picha zake na wakati mwingine kwenye runinga, ilikuwa ni kama runinga, kila kitu kilionekana kama naangalia filamu fulani ya kutisha.



    Ulikuwa ni wakati wa usiku, chini ya mti mkubwa wa Mbuyu, watu wote wakiwa kama walivyozaliwa, wameshikilia vibuyu mikononi mwao. Usoni wakiwa wamepaka dawa nyeusi iliyofanana kabisa na masizi, hakika niliyokuwa nikiitazama kwenye runinga ya ngozi ya Fisi, ilikuwa ni tafrija ya wachawi usiku wa manane.



    Maiti za walioonekana ni kama watoto wachanga zilikuwa zikiletwa na kuwekwa juu ya jiko kubwa lililokuwa likiwaka moto kama makaa ya mawe kwa jinsi ulivyokuwa mkali, muda mfupi tu baadaye maiti hizo zilikuwa zikidondosha mafuta mengi zilikauka kisha kushushwa zikiwa bado za moto, bibi vizee wakakamata miguu na kuichana katikati, kisha kuanza kula kwa furaha kama vile walikuwa wakila nyama nyingine yoyote, hawakujali kabisa kwamba ilikuwa ni maiti.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Awali sikuelewa ni kwa nini Mukulungu aliamua kunionyesha tafrija ile, lakini baadaye watu hao walipoanza kunawa nyuso zao ndipo nilielewa, baba yangu mzazi mzee Matima Matimandole alikuwa ni miongoni mwao! Nikashika mikono yangu yote mdomoni kwa mshangao, sikuwahi hata mara moja kuwaza kwamba baba yangu alikuwa mchawi, kwani alikuwa mcha Mungu kupita kiasi.



    "Babaaa? Mchawi?" nilijikuta natamka maneno hayo.

    "Ndiyo! Baba yako alikuwa mwenzetu, kwenye chama chetu, alishaua watu wengi mno, kama sharti ili mimi nikiachia ngazi yeye aendelee, lakini ghafla alipotakiwa kukutoa wewe kafara, ili achukue cheo akakataa na kuanza kusali kanisani, jambo ambalo sisi halikutufarahisha, tukaamua kumuua!



    Tunachotaka kufanya ni kusaini mkataba wetu wa uchawi, usipofanya hivyo hata wewe tutakuua!"

    "Je, mnaona kufanya hivyo ni sawa?"

    "Ndiyo, lazima uwe mchawi, ili siku moja ukikalie kiti hiki ninachokikalia mimi maana baba yako alikistahili, mrithi ni wewe."

    "Siwezi!" nilisema na hapo hapo runinga ya ngozi ukutani ikazima, Mukulungu akatoka kwenye kiti chake na kunisogelea akionekana kabisa kuvimba kwa hasira.

    "Umesemaje?"

    "Siko tayari kufanya mambo ya aina hii kama ni kufa acha nife, lakini nisiwe mchawi."

    "Yaani pamoja na kuongea muda wote huo bado hujaelewa?"

    "Sitaelewa."



    "Sasa sikiliza, nakuachia uende nyumbani ukafikirie, huwezi kutukimbia sisi, himaya yetu ni kubwa mno tutakufikia wakati wowote tukikuhitaji."



    Baada ya kusema maneno hayo Mukulungu aliondoka na kupotelea gizani, hapohapo nikafumbua macho na kujikuta nimelala kando ya mke wangu Rita, akiendelea kugugumia kwa maumivu makali, damu nyingi zikimtoka sehemu za siri na kulowanisha mashuka.

    "Darling yaani kweli mimi nateseka na maumivu wewe umelala usingizi?" Rita aliongea.



    Hakuwa kabisa na picha ya mahali nilipokuwa, kwenye ulimwengu usioonekana kwa macho ya kawaida, nikipambana na Mukulungu akinishawishi nitie saini mkataba wa kuwa mchawi jambo ambalo sikuwa tayari kulifanya.



    Hakika nilikuwa nimejifunza mambo mengi ambayo sikuwahi kuyafahamu, taswira ya baba yangu mzazi akiwa utupu huku akila maiti za watoto bado ilinitisha kila nilipoikumbuka. Ukweli kwamba mimba za mke wangu mpenzi zilizokuwa zikitoka ilikuwa ni adhabu sababu baba alisaliti wachawi wenzake uliniumiza sana lakini sikuwa na uwezo wa kumsimulia Rita, nikaahidi ingebaki kuwa siri yangu.



    "Nipeleke hospitali, ona ninavyovuja damu nyingi!"

    Nikajikusanya haraka na kuanza kuvaa nguo, nilipomaliza nilitoka nje hadi nyumba ya jirani ambako aliishi mwanaume mmoja mwenye moyo safi, nikagonga kwenye lango kubwa, mlinzi akafungua na nikamweleza shida niliyokuwa nayo, akanyanyua simu na kumpigia bosi wake aliyekuwa amelala, saa iliyokuwa imetundikwa ukutani ndani ya kibanda cha mlinzi ilisomeka saa tisa na nusu.



    Muda mfupi baadaye mwanaume huyo mwenye umri kati ya miaka hamsini na sitini alitoka ndani ya nyumba yake akiwa amevalia bukta na shati tu, akanisabahi nami nikampa heshima yake kisha kumsimulia mateso ambayo mke wangu alikuwa akiyapata.

    "Yuko wapi?"

    "Nyumbani kwangu."

    "Mnaishi nyumba ipi kweli?"

    "Pale kwa mzee Mwinyimkuu, tuko banda la uani."

    "Subiri."



    Akarudi ndani ya nyumba yake akikimbia, nikagundua alikuwa amefuata ufunguo wa gari, mawazo yangu yakawa sawa kwani aliporejea muda mfupi baadaye alinitaka niingie garini na kurudi kinyumenyume kisha kuendesha kwa kwenda mbele hadi mbele ya nyumba tuliyoishi, tukashuka naye hadi kwenye banda letu la nyuma ambako tulimsaidia Rita kuvaa kisha kumbeba hadi kwenye gari, nguo zote zikiwa zimelowa damu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Safari kwenda hospitali ikaanza, kichwa changu kikiwa kimejawa na mawazo mengi ya vitisho vya mzee Mukulungu na serikali yake ya Kichawi, sikujua jinsi ya kujinasua kutoka kwenye mtego huo lakini jambo nililoelewa ni kwamba sikuwa tayari kusaini mkataba wa kichawi na kuanza kuua watu.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog