Search This Blog

NITAKUFA MARA YA PILI - 5

 















    Simulizi : Nitakufa Mara Ya Pili

    Sehemu Ya Tano (5)





    Maandalizi ya mazishi yangu yaliendelea huku wazazi wangu wakionekana kupagawa sana. Nilimsikia akizungumza na watu waliomuuliza kuhusu mipango ya mazishi yangu. “Mzee mwenzetu pamoja na msiba kutokea ghafla una mpango gani?”

    “Yaani mpaka sasa hivi sijajua nifanye nini, la muhimu ngoja akili itulie kwa vile ni haraka sana kusema tutazika lini.

    Kwa vile tuna ndugu la muhimu kuwajulisha habari za msiba na pia shuleni kwake .” “Ni kweli, na kuhusu mwili wa marehemu tuupeleke hospitali au tutauhifadhi ndani?” “Hakuna haja ya kujipa usumbufu usio wa lazima, tutauhifadhi ndani tukiendelea na mipango ya mazishi.”

    “Poleni sana, si alikuwa kidato cha nne?” “Ndiyo.” “Na wiki ijayo alikuwa anafanya mtihani?” “Mungu wangu! Kwa nini jamani hakumuacha mtoto afanye mtihani?” “Maamuzi ya Mungu hatuwezi kuyaingilia japo inauma,” baba alionesha ujasiri kuwajibu majirani.

    Mara nilisikia baba akiitwa na mtu, sauti ya baba niliisikia kwa mbali sana, lakini sikusikia alikuwa akizungumza nini. Baada ya muda waliingia wanawake ambao walitoa vitu vyote na chumba kilibakia na kitanda tu, kama ilivyo katika misiba mingi ambapo chumba cha maiti hubakia na kitanda tu.

    Walipomaliza kufanya usafi wa chumba, waliingia wanaume wanne na kitanda cha kamba ambacho hutumika kumlazia maiti.

    Kitanda cha chuma kilitolewa na kuwekwa cha kamba, kisha mwili ulilazwa juu yake na kufunikwa shuka jeupe. 


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Baada ya matayarisho walitoka na kuuacha mwili wa bandia ukiwa umelazwa kitandani. Pamoja na roho kuniuma, lakini nilishuhudia vitu vingi ambavyo vinafanyika baada ya mtu kufa japo hapakuwa na msiba wa kweli. Muda ulikatika na usiku ukaingia.

    Kina mama waliingia kulala na mwili wa marehemu wakiamini kabisa mwili uliolala kitandani ni wangu. Usiku wa manane, nje ya nyumba yetu kulikuwa na ngoma ya kichawi.

    Baada ya muda, ukuta ulipasuka tena na wakaingia tena wachawi wakiwemo mama Helena na Sabina.

    Mama Helena ndiye aliyekuwa kiongozi aliyeshikilia matunguli. Kitu kilichonitisha kilikuwa jinsi walivyowafanyia uchawi waliolala mle chumban. Baada ya kuwamwagia dawa kina mama wote walianza kuwapanda kama farasi na kuzunguka nao mle chumbani. Waliwafanya vile huku nje ngoma ikiendelea kuchezwa.

    Mama Helena alinifuata na kunizomea na kunifanyia mzaha, sikuwa na la kufanya kwani nilikuwa kama mtu aliyefungwa nati ili nisitikisike. Ngoma ile iliendelea mpaka mapambazuko yalipokaribia, wakawalaza wale kina mama na kuwanyunyizia dawa kisha wakaondoka .



    Alfajiri nilisikia sauti za kina baba wakizungumza nje kuonesha wamekwisha amka. Lakini kina mama bado waliendelea kuuchapa usingizi kama wamelala majumbani kwao na siyo msibani. Niliwasikia kina baba nje wakiulizana.

    “Jamani wanawake hawajaamka?” “Ajabu! Au wamejisahau kama wamelala msibani?” Mara mlango uligongwa ukifuatiwa na sauti ambayo niliifahamu ni ya baba Godi, jirani yetu. “Kina mama kumekucha, mnajisahau kama mpo kwenu?”

    Sauti ile iliwafanya kina mama washtuke na kuona kumepambazuka, mmoja alisema: “Ha! Jamani kulala gani huku?” Alisema huku akimtikisa mwenzake wa pembeni yake ambaye bado alikuwa akiendelea kuuchapa usingizi. Waliamshana na kushangaa kwa nini walijisahau kama wapo msibani. Kila aliyeamka alilalamika kuwa anahisi mwili umechoka sana.

    “Jamani mbona mwili unaniuma,” alisema mmoja aliyekuwa akijinyoosha. “Mmh! Hii siyo kawaida, hata mimi mwili nahisi kama nilikuwa na kazi ya kumbeba mtu usiku kucha,” mama alisema huku akijinyoosha. “Jamani hata mimi,” kila mmoja alilalamika kuchoka mwili.

    Walitoka nje ya chumba kufanya mipango ya kifungua kinywa na mambo mengine, chumbani nilibakia peke yangu na mwili bandia uliokuwa umelazwa kitandani. Majira ya mchana nilisikia watu wakilia nje, baada ya muda mke wa mjomba toka Mwanza aliingia chumbani. Mama alipomuona alimpokea kwa kilio, kukawa ni vilio mtindo mmoja.



    Niliamini mtu ambaye alikuwa mbali ni mjomba, kama ameshafika mipango ya mazishi ingefanyika mara moja. Baada ya muda, kina mama walitolewa nje na wakaingia wanaume walioufanyia usafi mwili kabla ya kuuvisha sanda.

    Kama nisingeshuhudia jinsi wachawi wanavyofanya viini macho, ningeamini kilicholazwa kitandani na kufanyiwa usafi kabla kuuvisha sanda ni mtu wa kweli. Kwa macho yangu niliona mambo mengi ya kichawi ambayo siyo rahisi mtu wa kawaida kuyaona.

    Niliapa kuwa kama nitapona na kurudi tena kwenye uhalisia wangu, nitayatoa yote ya moyoni mwangu toka siku ya kwanza nilipokutana na mzee Manoni mpaka siku nitakapokuwa nimefikia. Nilijua wengi hawaamini uchawi, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba wachawi wapo na ni watu wabaya ambao ni kiwazo kwa wengine.

    Baada ya wale wanaume ambao wote niliwafahamu kuuosha mwili wa bandia, waliuvisha sanda na kuuandaa kwa ajili ya mazishi. Walipomaliza kazi yao ya maandalizi ya kuuandaa mwili, walitoka nje na baadaye aliingia kiongozi wa dini, Katekista Mathayo kuuombea mwili kabla ya kuingizwa kwenye jeneza. Baada ya maombi waliruhusiwa watu kuuingiza kwenye jeneza. 


    Waliingia wazee wawili na vijana wanne, walishirikiana kuuingiza mwili wa bandia kwenye jeneza. Baada ya zoezi lile lilibebwa jeneza na kutolewa nje, sikujua nini kinaendelea huko nje zaidi ya kusikia nyimbo za maombolezo zilizokuwa zikiimbwa na kina mama.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilifanywa sala ya kuombea maiti kisha niliwasikia wakiondoka kuelekea makaburini. Baada ya muda pakawa kimya kuonesha watu wote wameelekea makaburini kuuzika mgomba. Zilipita dakika tano, mara mlango ulifunguliwa na kuingia wachawi wanne wa kiume, walinibeba juu juu na kuelekea makaburini.


    Tulikuwa wa kwanza kufika kabla wazikaji hawajafika , nilipandishwa kwenye mti uliokuwa karibu na kaburi lililochimbwa kwa ajili yangu. Eneo lote la makaburi kulikuwa na wachawi zaidi ya hamsini.

    Sikujua wingi ule ulikuwa kwa ajili ya gani. Kwa mbali niliwaona watu waliobeba jeneza lenye mgomba wakisogea makaburini, baada ya muda walikusanyika . Jeneza lilipofika liliwekwa pembeni ya kaburi, nilishuhudia wazazi wangu hasa mama aliyeletwa akiwa ameshikiliwa na wanawake wenzake wakipita mbele karibu kabisa na jeneza.

    Uso wa mama ulikuwa umemvimba na macho kuwa mekundu kwa kunililia bila kujua mwanaye sijafa nipo kwenye mti nikishuhudia yote. Baada ya kimya kifupi, Kiongozi Msaidizi wa Kanisa, Mathayo alianza kuliombea kaburi kabla ya kuingizwa mwili wa bandia kaburini.

    Baada kulibariki kaburi, mchungaji aliruhusu mwili uingizwe kaburini. Nilishuhudia mwili bandia ukiteremshwa kaburini huku familia yangu hasa mama akilia mpaka kupoteza fahamu. Baba yangu mishipa ya kichwa ilimsimama, hakuweza kuzungumza zaidi ya kutokwa na machozi mfululizo.



    Wadogo zangu kila mmoja alilia ajuavyo kutokana na jinsi walivyonipoteza kaka yao, majirani nao walipatwa na mshtuko. Hata rafiki yangu wa kike, Lusia alizirai. Kifo changu kilimchanganya kutokana na siku ya jana yake kuwa pamoja tukisoma mpaka usiku wa manane.


    Alichanganyikiwa zaidi kutokana na ukaribu wetu na jinsi alivyonitegemea katika masomo. Si yeye tu, hata wanafunzi wenzangu hawakuamini hasa kutokana na kushirikiana nao katika mambo mengi ambapo nilikuwa msaada mkubwa katika mtihani wa mwisho. Kila mmoja alijua lazima nipasue tena kwa alama za juu kutokana na uelewa wangu.

    Baada ya mwili kuingizwa kaburini, ndugu wachache ndiyo walioweza kwenda kuweka mchanga kwenye kaburi kabla ya mwili kuzikwa rasmi. Baba alikuwa ameiva macho na kuwa mekundu. Alijikaza kwa vile ni yeye ndiye alitakiwa kusimama kidete kuyaongoza mazishi yale.

    Kama siyo hivyo naye alikuwa kwenye wakati mgumu, kila mara alifuta machozi kwa kitambaa cha mkononi na kufuta kamasi nyembamba zilizokuwa zikitoka bila kizuizi. Majirani wenye mioyo migumu waliweza kwenda kutia udongo kwenye kaburi, wadogo zangu walisaidiwa kufika kwa kushikiliwa.

    Baada ya watu muhimu kumaliza kuweka udongo kwenye kaburi langu, waliruhusiwa wote wazike kwa kupokezana. Niliushuhudia mwili bandia ukifukiwa na huku kila mmoja akiwajibika kutupa mchanga ndani ya kaburi.



    Wengi hawakuamini, wapo waliosema ni amri ya Mungu na wapo waliosema siyo bure kuna mkono wa mtu. Baada ya kuzika, kila mmoja aliweka shada la maua. Mama yangu ilibidi wambebe mpaka kwenye kaburi kutokana kushindwa kutembea, baba yangu aliangua kilio upya baada ya kupata uhakika kweli mwanaye nimefariki. Watu walimshika baba ambaye uvumilivu wa kujikaza kiume ulimwisha dakika za mwisho baada ya kuzikwa mwili wangu. Kilikuwa kilio kilichowaumiza wengi, kitendo cha baba yangu kulia kilifanya hata wenye mioyo migumu hasa wanawake kuungana na baba yangu kunililia kwa sauti ya juu. Mchungaji alifanya kazi ya ziada kuwakumbusha watu wote waliokuwepo makaburini kuwa isifike hatua ya watu kumkufuru Mungu pale tu misiba inapotokea katika familia zao. Aliwaeleza wanatakiwa kutambua kila neno aliloahidi Mungu lazima litimie kama mauti kwa mwanadamu.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndugu zangu, najua kifo kinapotokea huwagusa watu hasa wahusika, lakini watu wengi tumesahau kuwa Muumba wetu aliahidi kila kiumbe kilichotokana na mavumbi kitarudi mavumbini. Kinapotokea kifo ni somo kwa sisi tuliobaki ili tujiandae kwa vile hatujui siku wala saa. “Ndugu zangu, kila mwanadamu anapaswa kutengeneza makazi yake ya kudumu yaliyo mazuri kwa kutenda mema.


    Leo kijana wetu ameondoka tuliobaki tumejiandaa vipi? “Tusimkufuru Mungu kwa kuamini kuna imani za kishirikina, shetani hana mamlaka mbele ya Mungu. Hivyo basi tunatakiwa kumuombea kijana wetu Shija apumzike kwa amani katika makazi mazuri ya kudumu.

    Bwana alitoa! Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. “Wafiwa mtegemeeni Bwana Yesu kwani ndiye mfariji mkuu, enendeni kwa amani ya Bwana. “ Baada ya mazishi yaliyowaliza wengi, niliwaona watu wakiondoka makaburini kurudi nyumbani kila mmoja akizungumza lake.

    Nina imani mpaka hapa kila anayesoma mkasa huu amejua tafsiri ya mimi kufa mara ya pili. Nina imani umeona jinsi nilivyoona toka nilipoanza kupata misukosuko ya wachawi , kifo changu cha kichawi mpaka mwili wangu wa bandia kuzikwa



    Baada ya watu wote kuondoka, walibakia wale wachawi makaburini, waliniteremsha na kunikalisha katikati ya kaburi lililozikwa mgomba na kuanza kucheza ngoma kunizunguka. Walicheza kwa furaha huku wakishangilia kuonesha wamefanikiwa walichokitaka .

    Walicheza kwa muda mrefu bila kuchoka, sehemu ya makaburi yote ikawa vumbi mtindo mmoja. Katika watu walioonesha furaha ni mama Helena, alijirusha huku na huku na kila tulipokutanisha macho, alinizomea.

    Kingine kilichonishangaza ni kumuona Helena naye yupo kwenye ngoma ile, alionekana akicheza kwa furaha kama hakuwa mtu aliyenisaidia nisipatwe na wachawi . Nilijiuliza furaha ile ameitoa wapi, kwa nini alisema atanisaidia mpaka hatua ya mwisho na siku ya mwisho amefurahia kukamatwa kwangu.

    Nilijikuta nikipata wasiwasi na Helena na kukumbuka maneno ya Sabina kuwa Helena si mtu mzuri. Ilionesha wazi hata kuonesha ukaribu bado alikuwa na lake jambo la kuniteka kimawazo na mwisho wa siku kunitupia kwenye mikono wa wachawi kama siku ile.



    Ngoma ya wachawi

    makaburini ilikoma majira ya usiku giza lilipochukua nafasi kubwa. Baada ya kutosheka na ngoma yao, nilibebwa juu juu na kurudi nyumbani. Tulipofika nyumbani nilishangaa kurudishwa nyuma ya mlango.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilijiuliza wananirudisha nyumbani ili iweje, wakati tayari nyumbani wanajua nimekufa. Baada ya kunirudisha nyuma ya mlango waliondoka na kuniacha pale. Mazungumzo yote kuhusiana na kifo changu niliyasikia watu waliofika kuwapa pole wazazi wangu.


    Wapo walioamini kazi ya Mungu lakini wapo ambao hawakukubali na kusema ule ulikuwa mkono wa mtu. Walisema kifo kile si bure hasa kutokana na kina mama waliolala na mwili wa bandia kuamka wakiwa wamechoka sana.

    Kuna mmoja alisema kwa sauti ya juu kuwa msiba ule si bure kama wataangalia upande wa pili watagundua vitu vingi. Alitoa ushuhuda ulioungwa mkono na wengi kuhusu matukio kama yale. “Nataka kuwaambia kitu kimoja kuhusiana na hali iliyojitokeza siku ya jana, aminini msiamini kifo cha Shija ni cha utata kutokana na hali ya jana tuliyokutana nayo.

    Nataka kuwaelezea ukweli, piteni chini juu mtaniambia kuna kitu, si bure.” “Mama Suzana, huenda kuna matukio yasiyo ya kawaida lakini kama kiongozi wa familia nitabakia na msimamo kuwa mwanangu amefariki kwa amri ya Mungu.”



    Kauli ya baba iliuumiza moyo wangu na kuona yeye ni nani asiyeamini mambo ya kishirikina? Mbona alipoumwa alitumia mambo ya jadi? Nilimuunga mkono mama Suzana alikuwa ameona mbali. Lakini sikuwa na sauti ningeweza kuipaza ili baba yangu ajue mwanaye sijafa nipo hai, nahitaji nguvu za ziada kunirudisha duniani.




    Mazungumzo yaliendelea huku baadhi ya watu wakimuunga mkono mama Suzana kwa wazazi wangu kuhangaika zaidi kupata ukweli wa kifo changu. Lakini msimamo wa baba ulibaki palepale. Baada ya mazungumzo, watu walitawanyika na kubakia majirani wa karibu.




    Usiku wa siku ile kama kawaida, wachawi walikuja kunichukua na kunipeleka kwenye kilinge chao, walicheza ngoma mpaka ilipokaribia kupambazuka walinirudisha nyuma ya mlango, nilijiuliza maisha yangu yote yatakuwa pale nyuma ya mlango? Chakula changu kikuu kilikuwa uji ambao ulionesha kama ulichemshwa bila kuiva wala kuwekewa sukari.










    *******************

    Kutokana na njaa niliyokuwa nayo, sikuweza kukataa, nilikunywa hivyo hivyo , ilikuwa ajabu pamoja na uji ule kutokuwa mzuri, niliweza kushiba na kuendelea kusimama nyuma ya mlango bila kuchoka. Siku ya pili nilimsikia mama akizungumza kwa sauti: “Baba Misoji, una habari?” “Ipi?”

    “Ya mama Suzana.” “Mama Suzana! Kafanya nini?”

    “Mama Suzana amefariki dunia.” “Wewe!”


    Baba alishtuka hata mimi ndani nilipatwa na mshtuko mkubwa, niliamini kabisa mdomo wake ndiyo uliomponza kutoboa siri za wachawi mbele za watu.


    “Tatizo nini? Si jana jioni baada ya mazishi tumezungumza naye, ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu?” “Haswaa.” “Kipi kilichomsibu?” “Mumewe anasema kichwa tu.” “Mmh, mbona inatisha.” “Mimi, nina wasiwasi .” “Wa nini?” “Kauli yake aliyoitoa jana.”

    ”Ipi hiyo?” “Kuhusiana na wachawi .” “Sasa kauli yake na kifo chake vinahusiana vipi?” ”Baba Shija acha ubishi.” “Mke wangu ubishi wa nini?” “Nina wasiwasi huenda mdomo umemponza.” “Kumponza vipi?” “Mume wangu acha kujitoa akili, wachawi wanaweza kumtenda.”


    “Kwa maana hiyo mama Suzana hakufa?” “Sijui, inawezekana, kifo gani hicho?” “Ina maana na Shija hajafariki?” “Inawezekana pia.” “Mke wangu umeanza kuingia katika imani za ajabu, ina maana baba au bibi yako walipokufa , nao hawakufa ?” “Walikufa.”

    “Sasa kwa nini huyu mwanao na mama Suzana useme hawakufa ?” “Shija alikuwa mzima, tulimkuta amekufa bila kuumwa, mama Suzana kaumwa kichwa tu, kafa, huoni kuna kitu kimejificha hapo?” “Mke wangu sipendi kusikia tena upuuzi kama huo,” baba alikuja juu.

    Nilibakia nikiumia moyoni kwa majibu ya baba kujifanya haamini ushirikina wakati anaamini mizimu. Kingine kilichoniumiza ni ubishi wa baba, jambo linaonekana lakini yeye alijifanya hajui kitu. Nilijikuta nikipata wazo huenda baba kanitoa kafara na yeye ni mshirika wa wachawi .  

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya siku saba nilitolewa nyuma ya mlango na kwenda kuwekwa katikati ya shamba kubwa ambalo sikuelewa pale ni wapi. Muda ule ilionesha kama majira ya alfajiri kutokana na giza cha kufifia na baridi kali.

    Baada ya kuniacha pale, wachawi waliondoka na kuniacha peke yangu. Nilijiuliza pale ni wapi na kwa nini waniache sehemu ile peke yangu, nia yao ilikuwa nini kwangu? Kutokana na kuwa kifua wazi na kaptura pekee, baridi iliniingia mpaka kwenye mifupa.

    Nilishindwa nifanye nini au niende wapi kwa vile shamba lile sikujua pale ni wapi. Haikupita muda, mvua kubwa ya mawe ikashuka. Sitasahau mateso mazito yaliyonipata kwa kunyeshewa na mvua ya mawe kwenye mwili uliokuwa mtupu.

    Mawe ya kwenye mvua nayo yalinipiga na kusababisha maumivu makali. Shamba lilionekana la mihogo na mahindi yaliyokuwa marefu kiasi cha kushindwa kuona nipo sehemu gani. Nilijikunyata na kuanza kulia japo niliamini kilio changu kilikuwa sawa na samaki, machozi yalikwenda na maji.

    Mvua ilikuwa kama ya kutumwa kwani iliendelea kwa muda mrefu bila kukatika, nilijikunja kwenye tuta moja ambalo kwa maajabu ya ulimwengu, liligeuka na kuwa tope tupu. Kwa mateso yale, niliamini kifo changu kilikuwa kimetimia.

    Nilijikuta nikizama kwenye tope lile lililogeuka kuwa dimbwi, nilikumbuka maneno ya Helena kuwa, huenda ile mvua haikuwa ya kawaida ila ya kichawi. Niliamini yale ni mateso yaliyofanywa makusudi ili kunikomesha baada ya kunitafuta kwa muda mrefu bila mafanikio.

    Nilimkumbuka Sabina, kama angekuwepo asingekubali niteseke kiasi kile, pia nilijilaumu kuwa karibu na Helena ambaye niliamini ndiye aliyefanikisha kukamatwa kwangu na wachawi . Moyoni bado nilikuwa na wasiwasi na kauli za baba yangu kukataa kwenda kwa wataalamu kuangalia sababu ya kifo changu cha utata.

    Nilijikuta nikipoteza imani kwake kwa kumuona naye ni mhusika mkuu wa kifo changu kwa kuukataa ukweli. Nilikumbuka kauli moja ya Sabina kuwa kila mchawi hutoa mtu mmoja sehemu ya familia yake kama kafara ya kula nyama za wenzake.

    Kingine kilichonifanya niwe na wasiwasi na baba yangu ni kutokana na ngoma ya wachawi iliyokuwa ikichezwa nje ya nyumba bila kutoka. Nilijikuta nikiamini huenda na yeye ni mhusika, sikuwa na imani naye hata kidogo. Lakini nilijiuliza mbona baba yangu sikuwahi kumuona kwenye ngoma zote za wachawi nilizowahi kuhudhuria? Au alikuwa akijificha.

    Sikuwa na njia nyingine zaidi ya kumuachia Mungu. Tope lile lilianza kunimeza taratibu, nilijiuliza shimo lile limetoka wapi, wakati mwanzo kabla ya mvua kuanza kunyesha kulikuwa na tuta. Kila nilivyojitahidi kujitoa, tope lilinizidi nguvu na kuamua kutulia. Mvua ya mawe nayo iliendelea kunisulubu, usichukulie kama simulizi ya kusisimua bali mateso ya shetani motoni japo sijawahi kufika.

    Nilijikuta nimezama mpaka tumboni na tope liliendelea kunimeza taratibu, jinsi mvua ilivyokuwa ikiendelea, ndivyo nilivyozidi kuzama chini. Sauti ya Helena ilinishtua. “Shija...Shija,” nilifumbua mdomo kuitika lakini sauti haikutoka.

    “Shijaaaaa...Shijaaa upo wapi?” Ilionesha Helena hajui nilipo. Tope nalo liliendelea kunimeza taratibu, bahati nzuri aliniona na kusogea mpaka kwenye shimo la tope. Kilichonishangaza Helena alikuwa mtupu kama alivyozaliwa , kiunoni alikuwa amejifunga kitambaa cheusi kilichosokotwa kama kamba.

    “Shijaaa, nipe mkono,” alisema kwa sauti ya juu. Nilimpa mkono ambao aliudaka na kunivuta juu, ajabu hakusumbuka sana, aliponishika tu, alinitoa kwenye tope. Nilijiuliza Helena ana nguvu gani za kuweza kunichomoa kwenye tope kwa urahisi namna ile. Baada ya kutoka kwenye tope likiwa limenienea mwili mzima, Helena alinikumbatia huku akilia.

    “Jamani Shija pole,” nilishangaa kumuona akitokwa na machozi ambayo nayo yalikwenda na maji ya mvua. Nilifumbua mdomo ili nimjibu sauti haikutoka, Helena alichanganyikiwa kwa kunipapasa kila kona ya mwili kama ndiyo siku ya kwanza kuniona. Ilikuwa ajabu, pamoja na kuwa mtupu mbele yangu hakushtuka zaidi ya kuniangalia huku akibubujikwa na machozi.

    “Pole Shija,” niliitikia asante lakini sauti haikutoka. Helena baada ya kuona sauti haitoki, alielekeza nipanue mdomo, baada ya kufanya vile aliingiza vidole mdomoni kwangu kisha alinieleza. “Shija zungumza sasa.” “Helena,” nilimwita na sauti ilitoka. “Abee Shija, pole sana.”

    “Asante” “Shija ngozi uliiweka wapi?” “Hata sijui.” “Shija kwa nini umekiuka masharti yangu?” “Helena hata sijui imepotea vipi” Nilimueleza jinsi ilivyopotea siku nilipokwenda kuoga mtoni. “Shija ulishindwa vipi kusubiri mpaka ufanye mtihani ndipo ufanye upuuzi wako?” “Samahani Helena.”

    “Shija mbona hujipendi?” Nilikosa la kumjibu na kubakia kimya nimeinama chini. “Shija unanifanya nionekane mjinga mbele ya wachawi .” “Helena bahati mbaya.” “Haya bahati mbaya upo hapa, bora ningejua mapema kabla ya kujulikana umekufa.”

    “Helena naweza kurudi tena duniani?” “Mmh! Sijui lakini nitajitahi japo uwezekano ni mdogo sana.” “Kwa hiyo nimeshakuwa msukule?” “Toka siku ulipojulikana umekufa lakini ndani ya siku saba kulikuwa na uwezekano wa kurudishwa duniani. Kwa sasa hakuna ujanja.” “Sasa utanisaidiaje?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Shija umechelewa nina kazi ya ziada japo sina uhakika kama nitaweza.” “Mungu wangu basi nimekwisha.” “Shija usikate tamaa, hebu nifuate.” Alinishika mkono na kuanza kukatiza kwenye mahindi na mihogo, hali ilikuwa tofauti na siku zote, mvua ile ilikuwa bado inaendelea kunyesha.

    “Helena mvua hii ni ya kweli au kichawi?” “Shija mvua ya leo ya kweli wala si ya kichawi.” “Mbona sehemu niliyokuwa iligeuka shimo la tope?” “Shija hukuzama kwenye tope kama ulivyodhani, bali ulikuwa umelala kwenye tope.”

    “Ha!” Nilishtuka. “Mambo ya kichawi yana mauzauza, wamepanga kukutesa mpaka ufe kisha wakule nyama yako. Nami nimeapa nitahakikisha hawali nyama yako.” “Mungu wangu nimekwisha,” kauli ya kuliwa nyama ilinikata maini.


    Nilikumbuka jinsi kaka yangu Luhemeja alivyoliwa nyama na wachawi, woga ulizidi kuniongezeka, Lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kuendelea kumuomba Mungu aniepushe na balaa zito kama lile, japo Helena alinieleza ukishageuzwa msukule ni kazi kurudishwa duniani mpaka ifanyike kazi nzito.

    Tuliendelea kukatiza kwenye mashamba kwa kukanyaga mazao ya watu. Baada ya mwendo wa nusu saa ambao sikuelewa tunakwenda wapi, kutokana na kutofika safari yetu, ghafla Helena alisema: “Shija hebu subiri,” nilishangaa kumuona Helena akiinama. “Vipi Helena?”

    “Shija, nimeumia” “Nini?” “Nimeumia, sijui kama tutafika mbali,” Helena alisema huku akikaa chini na kushikilia mguu wake wa kulia.


    Nilishtuka kuona damu, niliinama kuangalia. “Mbona damu zinatoka kwa wingi umekanyaga nini?” “Hata sijui, hebu kivute kilichonichoma.” Nilipiga magoti na kuvuta kwa meno kipande cha mti kilichomchoma, baada ya kukitoa, Helena alinyanyuka na kuendelea na safari yetu kwa shida kutokana na Helena kutembea kwa kuchechemea.

    Hata kasi yetu ilipungua, kila hatua Helena alilalamika mguu unazidi kumuuma na damu iliendelea kumtoka. Nilivua kaputula yangu na kubakia na nguo ya ndani. Niliichana kwa meno japo ilinipa shida kutokana na kuloa na tope lakini nilijitahidi mpaka nikafanikiwa kutengeneza kitambaa cha kumfunga Helena.

    Wakati namfunga jeraha ambalo lilikuwa bado linavuja damu, Helena alipiga kelele. “Shijaaaa...” Kilichofuata sikujua baada ya kuhisi nimepigwa na kitu kizito kichwani na kupoteza fahamu. Nilipozinduka nilijikuta nimelala sehemu iliyokuwa na baridi kali na harufu mbaya, nilipofumbua macho kulikuwa na kiza kinene, nilijiuliuza pale ni wapi?

    Nilipapasa mkono na kuugusa mwili wa mtu aliyekuwa amekaa pembeni yangu.


    Mara nilimuona mtu akija na kibatari na kuanza kuwaamsha watu. “Haya amkeni,” mkononi alikuwa na fimbo kama ya kupigia ng’ombe. Nilisikia watu wakiamka kama ng’ombe kwenye zizi. Nami ilinibidi niamke kwa vile tuliamriwa kuamka wote. “Shija rudi ulale.”

    “Nilijiuliza yule ni nani mbona sauti yake ni ngeni.” Wengine niliokuwa nimelala nao walipochelewa kuamka walitandikwa fimbo za mgongo na kutoa mlio mkubwa kuashiria zimewaingia barabara. Watu wote walinyanyuka ilionesha walikuwa wengi sana.

    Baada ya muda, wote walitoka nje na nikabakia peke yangu. Nikiwa nimejilaza huku nikikung’utwa na baridi, nilibaki najiuliza pale ni wapi, mbona wale watu wametoka wote nje huku wakipigwa kama ng’ombe? Usingizi ulipotea kichwani na kunifanya nibakie nimejikunyata kwa baridi.

    Nikiwa bado sijapata jibu, alikuja yule msichana aliyekuwa akiwaamsha misukule wenzangu.


    “Shija.” “Naam.” “Vipi nikuletee chakula?” “Wewe nani na hapa nipo wapi?” “Utajua tu, la muhimu kwanza nikupatie chakula.” “Sawa.”

    Nilimkubalia kutokana na njaa kali iliyokuwa ikinichonyota. Yule msichana aliondoka na kuniachia maswali mengi, nilijitahidi kumfahamu bila mafanikio, nilishindwa kumjua kutokana na mwanga hafifu wa taa aliyoshikilia.


    Baada ya muda alirejea na bakuli lililokuwa na viazi, mkono mwingine alishikilia maziwa yaliyokuwa kwenye kibuyu kidogo.

    “Shija kula.” “Asante, lakini wewe nani na hapa nipo wapi?” Niliendelea kumuuliza. “Shija, nimekueleza utanifahamu na hapa utapajua tu, hebu kula kwanza nina kazi nyingi huu si muda wa mazungumzo.”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikula viazi pamoja na maziwa na kushiba barabara kutokana na ubao mzito, yule binti aliniuliza: “Vipi umeshiba?” “Nimeshiba.” “Basi pumzika tutazungumza kesho.” “Mbona sina shuka?” Kauli yangu ilimfanya yule binti kucheka kitu kilichonishangaza, kumuomba shuka yeye anacheka.

     “Hebu subiri.” Aliondoka na kuniachia maswali mengi ya kujiuliza pale ni wapi na Helena yupo wapi? Wakati nikiwa katika maswali yasiyo na majibu, alirudi yule binti ambaye alikuwa akinijua lakini mimi simjui, alipofika alinipa kipande cha gunia.


    “Shija, samahani kwa leo utalalia hili.” Nilipokea, kilikuwa kipande cha gunia, nilishtuka kupewa kipande cha gunia kujifunika. Lakini yule msichana hakutaka maelezo zaidi. Baada ya kunikabidhi, aligeuka na kuondoka.

    Nilijikuta nikizidi kuwa njia panda kwa maswali yasiyo na majibu. Nilijifunika kile kipande cha gunia ili kupunguza ukali wa baridi iliyokuwa ikiniingia hadi kwenye mifupa. Usingizi ulikuwa mbali kila nililowaza lilipotelea hewani, nilitamani ninyanyuke na kupapasa kutafuta mlango nitoke.

    Bado niliona ni kufanya kichekesho kwa vile siwezi kutoka sehemu nisiyoijua. Wazo la haraka lilinijia labda ndiyo nimeshakuwa msukule kamili. Akili yangu ilipingana na kile nilichokuwa nakiona na kushindwa kuamini, msukule anawezaje kula viazi na maziwa?

    Bila kujielewa usingizi ulinipitia, nilishtushwa na kitu kilichoniminya kwenye mbavu, nilinyanyuka haraka, kidogo nipige kelele za woga baada ya mguu uliokuwa na magaga kunikanyaga karibu na tumbo. Nilipofumbua macho, nilishtushwa kuona watu wakirudi wakiwa wamechafuka kwa vumbi na matope.

    Akili ya haraka haraka nilifahamu wale ni misukule kwa vile nilishawahi kuwaona nilipopelekwa na Sabina nyumbani kwao Helena kwenda kumuona marehemu kaka yangu. Watu wale wenye nywele nyingi na kucha chafu za mikono waliingia ikionekana wanatoka kufanya kazi za usiku.



    Kila mmoja alikaa sehemu yake, hali ya mule ndani ambako palikuwa kama kwenye ‘godauni’ la kutunzia vitu ilibadilika. Harufu kali ya jasho lilizidi kuumiza pua zangu. Hakuna hata mmoja aliyeonekana kumfuatilia mwenzake, wote walikuwa kimya wamejiinamia.


    Kitu kilichonishangaza watu wengi walionekana na afya kama wanabeba vitu vizito, nilijiuliza wanakula nini na wana furaha gani ya kuishi maisha yale kufikia hatua ya kunenepa. Nilikuwa nimekaa na kujifunika kipande cha gunia kutokana na baridi ya alfajiri.

    Aliingia binti mmoja, nilipomwangalia, nilimfahamu kuwa ni mdogo wake Helena. Alinisogelea na kunisalimia. “Mambo Shija?” “Poa.” “Vipi, baridi?” “Mmh! Wee acha tu.” “Pole sana.” “Bado sijapoa, Helena yupo wapi?”

    “Mmh! Helena amevimba mguu hawezi hata kutembea baada ya kuumia jana wakati akitaka kukutorosha.”

    “Mungu wangu na hapa nipo wapi?” ”Hapa ni nyumbani kwetu.”


    “Nafanya nini?” “Shija umegeuzwa msukule lakini bado hujawa msukule kamili.”

    “Una maana gani?” “Kuna kitu alinieleza Helena, sijui nini..,” ilionesha amesahau. “Kuhusu nini?” “Shija nimesahau nitakwenda kumuuliza Helena.”


    “Kwani yeye yupo wapi?”

    “Yupo nje amejilaza kwenye mkeka.”

    “Mbona hajaja, bado hawezi kutembea?” ”Ameniambia amekatazwa asikusogelee, la sivyo akifanya kiburi basi watakugeuza kitoweo.” “Mmh!” Niliguna. “Pole Shija.”


    “Hata sijui niseme asante au?” “Kwa nini?”

    “Matatizo yangu bado, unataka kuniambia nitaishi maisha haya siku zangu zote zilizobaki za kuwa duniani?” “Mmh! Siwezi kujua.” “Sundi, ina maana wewe hujui taratibu za kichawi?” “Ndiyo.”


    “Wewe si mchawi?” “Ndiyo.” “Mbona jana ulikuja kuwaamsha na huku ukiwatandika bakora?” “Hutumwa mara moja moja hasa au Helena anapokuwa na udhuru, pia yupo mama mdogo ambaye amesafiri.” “Kwa hiyo wewe si mchawi?” “Ndiyo.”

     Kama si mchawi mambo ya kichawi umeyajuaje?” “Shija sikuja kujibu maswali, chakula watakacholetewa wenzako usikiguse, wewe subiri chako.” “Mpe pole Helena.” “Amesema mtaonana usiku atakuja kuzungumza na wewe.” “Sawa.”


    Baada ya kusema vile aligeuka na kuondoka lakini baada ya muda alirudi na blauzi ya Helena na kunipa niivae. Niliifahamu nguo ile kutokana na kuwahi kumuona Helena ameivaa. “Shija utavaa hii.” “Asante.” Sundi aliondoka na kuniacha nikivaa blauzi ya Helena, kisha nilijiegemeza kwenye ukuta nikiyawaza maisha ya kimsukule.

    Nilijiuliza baada ya muda nami nitakuwa kama mwenzangu kuishi bila kuoga, nywele zisizo nyolewa wala kusukwa na kucha ndefu zenye kutunza uchafu. Nikiwa bado nipo kwenye maswali magumu ambayo niliamini mpaka kuingizwa mle ndani kuanza kutumikia kifungo cha maisha cha kimsukule, hakukuwa na mtu wa kuweza kuyajibu maswali yangu japo nilijipa matumaini huenda Helena ana kitu kipya cha kuniambia.

    Lakini nilikumbuka jinsi tulivyotaka kumtorosha kaka yangu na tuliposhindwa, nilishuhudia akiliwa nyama mbele ya macho yangu. Wasiwasi ulikuwa mkubwa kama Helena atanishawishi kunitorosha na kuishia mikononi mwa wachawi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikiwa nimezama kwenye dimbwi la mawazo waliingia watu wanne wanawake wawili na wanaume wawili wakiwa na masinia makubwa mikononi mwao yaliyokuwa na kitu kama uji huku yakifuka moshi kuonesha muda mfupi yametolewa jikoni.


    Baada ya kuyaweka chini yale masinia, wenzangu waliyavamia na kuanza kunywa kwa mikono bila mikono yao kuungua. Walioleta yale masinia walinishangaa na kuniuliza: “Wewe mbona huli? utakufa na njaa,” sikuwajibu niliwatazama tu.

    “Mwache ajitie kiburi atanyooka tu,” mwingine aliongezea. Sikuwajibu niliwatazama tu, niliziona sura zao ambazo zilikuwa ngeni kwangu, baada ya wenzangu kumaliza kula kwa kugombania kama mbwa, wale watu walibeba masinia na kuondoka nayo huku wakiwaacha wakilamba mikono yao michafu iliyokuwa na uji.

    Nilishindwa kuelewa kwa ulaji ule walishiba kweli au laa, walioleta chakula kile waliondoka huku nikiwasindikiza kwa macho. Kuna maneno waliyazungumza kwa kunong’onezana kisha walicheka na kutoka nje, baada ya muda mdogo wake Helena aliingia na viazi na maziwa ya mtindi, nami nilishambulia kisha nilijilaza kwenye kipande cha mkeka na kujifunika kipande cha gunia.

    Muda ule kulikuwa kimya hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akizungumza. Wote tulijilaza huku nikiwa bado najiuliza yale ndiyo maisha yangu mpaka kufa? Niliamini kulia kusingenisaidia kitu chochote zaidi ya kukubali matokeo, baada ya kufanya uzembe mwenyewe.

    Lawama zangu kwa Helena hazikuwa za msingi kwa vile ilionesha nimejitaki mwenyewe. Siku ile nilikula chakula muda tofauti na wenzangu, nilikula mara tatu, wao walikula mara mbili. Walikunywa uji alfajiri na chakula kingine walikula saa kumi na mbili jioni.

    Na usiku ulipoingia tulilala wote kila mtu sehemu yake, ilipofika katikati ya usiku aliingia mtu tofauti na mdogo wake Helena na kuwaamsha misukule kwa mtindo ule ule wa kuwatandika bakora.

    Kwa vile alikuwa mtu mwingine aliyeonekana hana mzaha hata kidogo, nilijikuta na mimi nikinyanyuka na kurudi nyuma ili nisipigwe na bakora walizokuwa wakipigwa misukule wenzangu.


    Nilishangaa kusikia aliyekuwa akiwapiga akiniita jina langu: “Shija toka huko.” Nilitoka kwenye kundi la msukule na kusogea sehemu iliyokuwa tupu, aliendelea kuwatandika waliokuwa wanachelewa kuamka. Baada ya kutoka wote kama kawaida nilibakia ndani peke yangu.

    Dada aliyekuwa akiwafurumusha misukule alirudi na kunieleza: “Shija unaweza kuendelea kulala.” “Asante,” nilimjibu huku nikijilaza kwenye kipande changu cha mkeka na kujifunika gunia. Alitaka kuondoka lakini alinigeukia na kuliita jina langu tena: “Shija,” “Naam.”



    “Umempa nini Helena kiasi cha kutaka kujitoa kafara kwa ajili yako?” “Sijampa kitu.” “Ni mpenzi wako?’ ”Ni rafiki yangu wa kawaida tu.” “Mmh, Shija niambie ukweli.” “Kweli kabisa.” “Mmh haya!” Baada ya kusema vile aligeuka ili aondoke, alinigeukia tena na kunisemesha:


    “Nilisahau,

    Helena amesema anakuja, alikuwa anasubiri mama yake aondoke.” “Sawa.” Yule dada aliondoka na kuniacha nimejilaza kwenye kipande changu cha mkeka, baada ya kuondoka nilijiuliza maswali ya yule dada juu yangu kuhusiana na Helena kujitoa muhanga kwangu, alikuwa na maana gani?


    Wakati najigeuza ubavu wa pili nilishtushwa na mwanga wa kibatari. Nilijigeuza kuangalia kuna nini tena, nilimuona Helena akija huku akichechemea. ”Shija,” aliniita. “Helena,” nilisimama. “Pole Shija.” “Asante.” “Shija upo sawa?” “Nipo sawa.” “Hawajakupiga?”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hawajanipiga si umewakataza.” “Shija wangu jamani,” Helena alinikumbatia huku akibubujikwa na machozi. “Usilie Helena,” nilijikuta nikimuonea huruma. “Siwezi kuacha kulia, Shija upo sehemu mbaya.”

    “Ni kweli, lakini sina jinsi.” “Shija nimepata kazi sana kukutetea, mama yangu ana roho mbaya aliitamani damu na nyama yako,” Helena alisema huku akiketi kwenye mkeka wangu. “Kwani nimemkosea nini?” “Toka siku tulipogombana shuleni bado nipo na Sabina, ulipotuambia sisi wachawi alikasirika sana.

    Kingine kukingiwa kifua na marehemu mzee Manoni, kitendo kile kilimuuma sana hasa siku ile tulipokuwa tunakutorosha na kushtukiwa na mzee Manoni na kupewa adhabu ya kutoa nyama ya mtu katika familia. Aliapa kuwa mzee Manoni aishi milele lakini akitangulia basi cha moto ungekiona.”

    “Lakini mbona aliona mimi na wewe tumepatana?” “Hata sijui kwa nini alikuchukia kiasi hicho.” “Kwa hiyo ndiyo kasemaje?” “Shija, wana bahati siku ile nilijikwaa na kuumia, lakini nisingekubali wakukamate kirahisi vile. Baada ya kukufikisha hapa walipanga kukula siku ile ile usiku.

    Lakini nilimuapia mama kuwa wakikula nyama atafuata yeye au mimi. “Mama alinibembeleza sana nikubali wakutie adabu, ujinga wa mara ya kwanza nilivyo kusaliti, lakini niliapa sitarudia tena kutenda kosa la kinyama kama lile.



    Niliapa sitakusaliti mpaka nakufa. Pamoja na kunitisha nilikuwa tayari kwa lolote kuhakikisha wanatula nyama wote. “Ilibidi kifanyike kikao usiku ule ule wakubaliane wakufanye nini, wapo waliopendekeza uwe mchawi kwa vile siri nyingi unazijua.

    Lakini ulikosa sifa moja, ulishafanyiwa zindiko la kifo. Wengine walipendekeza uwe msukule, wengi waliunga mkono. Wakati wanajiandaa kukufanya ndondocha, niliendelea kumbembeleza mama wasikutie undondocha, wakuache msukule freshi.

    Mama alisema analifanyia kazi, ndiyo maana mpaka leo hii upo katika hali hii.” “Asante sana Helena.” “Shija muda wa kunishukuru bado, mpaka nikutoe humu ndani.” “Helena! Bado tu hujakata tamaa?” “Siwezi kukata tamaa, kwanza kukuleta hapa ni nafasi yangu nyingine ya kufanya vitu vyangu kwa uhakika.”

    “Helena, unaweza kukosea na kusababisha nikageuzwa asusa.” “Shija wee acha tu, nitakachokifanya hutanisahau mpaka unaingia kaburini.” “Helena unataka kufanya nini?” “Shija ni siri yangu naijua mimi na Mungu wangu.” “Hivi wale walioletea chakula misukule wenzangu, kina nani?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wale ni wafanyakazi walioajiriwa kwa ajili ya kupikia misukule.” “Nao ni wachawi?” “Si wachawi, ila hujipaka dawa ili kuwaona misukule wakati wa kuwapa chakula.”

    “Hawawezi kutoa siri nje?” “Wapo waliojaribu lakini walikufa na wengine kuwa vichaa siku siri ilipovuja.”

    “Eti mama Suzana alikufa au ndiyo wamemfanya kama mimi?” “Mama Suzana kweli amekufa baada ya kutupiwa uchawi, lakini kaburi lake ndugu zake walizindika. Mwili wake haukuchukulika.” “Kwa hiyo walitaka kumfanya nini?” “Shija kuna kitu kingine zaidi ya kumla nyama.”

    “Mh! Kweli wamepania.” Siku ile tulizungumza mpaka kulipokaribia kupambazuka ndipo Helena aliponiaga na kuniachia kipande cha shuka. “Shija utajifunika hiki.” “Asante Helena.”

    Helena aliondoka na kuniacha nizidi kumfikiria na msaada wake mkubwa kuokoa maisha yangu.

    Haukupita muda Misukule wenzangu walirudi toka kwenye mashamba ya mama Helena. Siku zilikatika nikiwa naishi maisha ya kimsukule, tofauti yangu na misukule wengine ilikuwa, wao hawaongei lakini mimi nilikuwa naongea pia nilikula chakula kizuri, nililala kwenye kipande cha mkeka na kujifunika shuka.

    Lakini wenzangu walilala chini vifua wazi. Hata ulaji wao ulikuwa tofauti nmimi, wakati wa kula

    waligombea chakula kama nguruwe, hata chakula chao kilikuwa bora chakula, siku nyingine walikula mapumba au ugali ambao haufai mwanadamu kula. Helena naye alipona na kuweza kuingia ndani mle wakati wa kuwatoa misukule kwenda shamba. Siku nyingine alinichukua kwenda kuangalia kazi ya misukule mashambani.

    Asikuambie mtu wanadamu tunateseka, walilima kama trekta na anayetegea hutandikwa kama ng’ombe. Kuna kipindi Helena aliwatandika mpaka nikawa nafumba macho, kingine kilichonishangaza ni ukubwa wa shamba la mama Helena. Nilijiuliza shamba lile lipo wapi.  




    Lakini sikutaka kuuliza kwa kuonekana najifanya najua, kitu ambacho nilikiogopa ni kumuudhi Helena, mtu aliyekuwa muhimu sana kwa kipindi kile. Baada ya kuwahimiza kulima kwa viboko, alirudi chini ya mti niliokuwa nimekaa.

    Alionekana akitweta na kukaa pembeni yangu huku akivuja jasho. “Pole Helena, kumbe kutusimamia ni kazi!” “Shija wee acha, kuyasimamia majitu yasiyo na akili kazi kubwa.” “Mbona huwa mnawapiga bila huruma?” “Shija japo hawana akili lakini wana kiburi sana.

    Ukiwachekea kazi haifanyiki , nikuambie kitu?” Helena aliniuliza “Niambie.” “Kazi hii nilikwishaikataa na kumuomba mama atafute mtu mwingine wa kisimamia misukule yake. Na mtu alikwishapatikana , mama mdogo aliyekuletea chakula.”

    “Sasa mbona unaendelea nayo?” “Sababu yako, imebidi niendelee nayo kuhakikisha unakuwa salama, nahofia nikimwachia mtu mwingine, utateseka.” “Asante, kwa hiyo maisha yangu yote ya huku utaendelea nayo?”

    “Ndiyo Shija, kwa vile siipendi kazi hii, hata mimi huwa sipendi kuwapiga misukule kwa kuamini ni viumbe wenzangu.

    Nitatumia kila uwezo wangu kuhakikisha nakutoa kisha naachana na kazi hii.” “Utaiachaje?” “Nimeshapata mchumba, wewe ndiye unanichelewesha, nikishakutoa naolewa na kuachana na kazi hii ya kishenzi.” “Mmh! Haya.”

    Baada ya kilimo tulirudi nyumbani kuendelea na kifungo changu cha kimsukule.



    **************





    Siku zilikatika huku nikiendelea na maisha yangu ya kifungo cha msukule, nilikuwa na tofauti kubwa na wenzangu. Helena alihakikisha naishi maisha mazuri japo sehemu yenyewe haikuwa salama.





    Tofauti yangu kubwa na misukule wengine ilikuwa ni nywele . Wenzangu walikuwa na nywele ndefu zilizojisokota kwa uchafu, hawakuyajua maji ya kuoga wala kufua nguo, miili yao ilikuwa na harufu kali ambayo mwanzo ilikuwa kero kwangu. Kwa upande wangu Helena alininyoa nywele japo hakuwa mjuzi sana wa kunyoa lakini kichwa kilikuwa kisafi.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alitumia muda wa kwenda kusimamia misukule shambani kunifanyia usafi wa kuoga na kunifulia nguo zangu.

    Siku moja nilishangaa kumuona Helena akiniletea nguo zangu nilizoziacha nyumbani kipindi kirefu toka nijulikane nimekufa.





    Kabla ya kupokea ilibidi nihoji: “Helena nguo zangu umezitoa wapi?” “Nyumbani kwenu.” “Kwetu?” Nilishtuka. “Ndiyo, kwenu.” “Helena umezipataje?” “Nimezipata tu.” “Sawa umezipata, kumbuka ni muda mrefu toka nitambulike nimekufa, ina maana nguo zangu bado hawajazichoma?” “Shija, la muhimu kupata nguo, si maswali nimepataje.”



    “Mmh, sawa,” nilijibu kwa unyonge... “Shija umekasirika?” Sauti yangu ya unyonge ilimtisha Helena. “Walaa.” “Ngoja nikwambie japo sikupenda kukueleza kitu hiki.” “Kama si cha muhimu kiache tu.”

    “Hapana Shija, lazima nikueleze kwa vile umetaka kujua.”



    “Hapana Helena, kama unaona halina umuhimu wa mimi kulijua, achana nalo,” nilimtoa hofu Helena. “Si kihivyo .” “Basi niambie.”



    “Shija, jana wakati napita kwenu nilimwona baba yako akizitoa ndani baadhi ya nguo zako ambazo alizifukia kwenye shimo alilokuwa amechimba.





    Nilipoona vile, niliamini kama nitafukua nitapata nguo za kuvaa, usiku nilirudi na kufukua sehemu zilipofukiwa nguo zako na kuzichukua baadhi ya ambazo ndizo nimekuletea.”



    “Helena, hivi maisha yangu ya huku yataendelea hadi lini? Na ni nini hatima yangu juu ya uamuzi wa mama yako?” “Kwa kweli kipindi chote alichonieleza anatafakari hajanieleza kitu chochote, ni wazi amekusamehe.”

    “Na vipi mpango wako wa kunitoa huku, nimechoka na maisha ya huku, kuishi na viumbe ambao kila siku wananitisha.”







    “Shija shukuru mimi nipo, bila hivyo nawe ungeishi maisha ya wenzako wala usingefikiria kurudi kwenu.



    Hawa wenzako wapo kama wanyama wasiojua raha ni nini?” “Kwa hiyo nini hatima ya maisha yao?” “Kuendelea kumtumikia mama mpaka watakapofariki .” “Na wakifa miili yao huliwa nyama?” “Hapana, huzikwa tu, miili yao huwa hailiwi nyama, huwa haifai.” “Mmh! Na mimi je?” “Shija bado najipanga.”

    “Mpaka lini?” “Kumbuka bado una kesi na mama hivyo ninatakiwa nisifanye kosa wakati wa kukutoa. Kosa lolote litauumiza moyo wangu.” “Kosa gani?” “Kumbuka nilipojaribu kukutorosha nilikamatwa, ulikuwa uliwe nyama lakini nilikuwa radhi kufa kuliko kukuona unaliwa nyama.

    Pamoja na vitisho vizito sikuwa tayari. Lakini nakuhakikishia lazima nitakutoa nakuomba uvumilie tu.” “Mmh, haya nitavumilia japo sina raha na maisha ya huku.”

    “Pamoja na hayo lakini ulitakiwa kushukuru kutokana kuwa tofauti na wenzako, unakula chakula sawa na wenzako?” “Hapana.” “Unalala sawa na wenzako?” “Hapana.”



    “Hebu jiangalie tofauti na wenzako kwa kila kitu, wao hawazungumzi, wewe unazungumza, wao hawaogi wewe unaoga, wao hawafui wewe unafua, wao wanafanya kazi nzito lakini wewe hufanyi kazi yoyote . Shija naweza sema wewe si msukule ila upo huku.”



    “Helena usinifikirie vibaya lakini lazima niseme ukweli toka moyoni mwangu umenifanyia mambo makubwa sana maishani mwangu.” “Shija bado sijafikia nilichokidhamiria kukifanya kwako , nitahakikisha nakutoa humu ndani ukiwa salama.” “Nitashukuru sana Helena.”




    Shija nikwambie kitu?” “Niambie” “Wiki moja kuanzia leo nitakutoa humu ndani.” “Mwongo,” nilijua ananitania. “Kweli, niamini.” “Utafanyaje?” “Nitakueleza siku ikifika.” Nilijikuta nikiwa na hamu kujua Helena atanitoa vipi kwenye kaburi linalotembea.





    Lakini hakuwa tayari zaidi ya kunieleza atakavyoweza kunitoa kwenye hali ile na kurudi dunia ya kawaida. “Lakini Shija nikikutoa, chonde usirudi tena nyumbani kwenu ikiwezekana hata wazazi wako wahame.” “Sasa tutakwenda wapi?” “Si mnaweza kuuza eneo lenu na kwenda kuishi sehemu nyingine.”





    “Helena, unataka kuniambia wachawi hawatafika sehemu tutakayokimbilia ?” “Ooh, lakini kweli, basi nakuomba ukitoka salama ukaishi kwa mjomba wako, kinyume na hivyo wakikupata tena sitakuwa na uwezo wa kukuokoa, pengine nitakuwa kwangu baada ya kuolewa na mambo ya uchawi nitakuwa nimeachana nayo.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mmh! Sijui wazazi wangu na jamii itanichukuliaje nikitokeza mbele yao?” “Ikuchukulie kivipi? Maisha yako wao yanawahusu nini?” “Nitawezaje kujibu maswali yao.” “Shija hayo si maswali ya kujiuliza bali kujifikiria jinsi ya kutoka, mengine najua hayawezi kukusumbua kichwa.”





    “Hawawezi kunitafuta na kunipata?” “Hawawezi , kuna dawa nitakupa hawatakusogelea milele, dawa hiyo hupewa tunapoolewa ili tusishiriki mambo ya kichawi waka kudhuriwa nao.” “Unataka kuniambia hata Sabina naye alifanyiwa hiyo dawa?” “Ndiyo.”

    “Mmh! Si nitakuwa kituko mbele ya jamii?” “Shija hayo si yakuwaza , kwa hiyo niache kukutoa?” “Hapana Helena.”





    “Sasa unataka nikufanyie nini?” ”Nitoe tu, huku haya si maisha.” “Unataka nikutoe lakini unawaogopa watu?” “Helena siwaogopi bali nilikuwa najiuliza jamii itanipokeaje?” ”Kama utakuwa Mwanza hakuna wa kukuuliza kwa vile hawakujui lakini ukirudi kijijini kila mmoja atataka kujua ilikuwa vipi ufufuke kama Masia.”





    “Na Mjomba atanielewa vipi?” “Mweleze ukweli?” “Nikutaje?” “Usinitaje, tafuta cha kusema lakini mimi usinitaje wala kuwaeleza ulikuwa wapi.” “Helena nina siri nyingi toka siku ya kwanza kukutana na mauzauza yaliyopelekea kufungwa mdomo na mzee Manoni mpaka leo. Si wewe wala Sabina anayeijua siri iliyo moyoni mwangu.” “Kweli Shija, unaweza kuitunza siri naamini hata hii utaitunza.” “Ondoa shaka kuhusu hilo.”



    ********



    Ajabu wiki ilikatika bila dalili zozote za kutolewa kwenye kifungo cha kuzimu huku kila siku nikipewa matumaini kuwa nisiwe na wasiwasi nivumilie kidogo, wiki ya pili nayo ilielekea ukingoni. Niliamini maneno ya Helena yalikuwa ya kunitia moyo lakini hakukuwa na uwezekano wa kurudishwa duniani.







    Siku moja Helena alinieleza kuwa nipumzike nisifuatane naye shambani, nilikubaliana naye na kuendelea kuuchapa usingizi. Katikati ya usiku nikiwa nimejilaza kwenye mkeka wangu baada ya misukule kwenda kulima, nilishtushwa na sauti ya Helena. “Shija.” “Naam.” “Nifuate.” “Wapi?” “Sitaki maswali, fuata sauti.”





    Nilinyanyuka kwenye mkeka wangu na kuifuata sauti iliyokuwa kwenye kiza kinene, ilikuwa tofauti na siku nyingine ambazo Helena huja na taa. Ndani ya jumba lile bila taa mnatisha kama ndani ya kaburi. “Upo wapi?” “Fuata sauti yangu,” Helena alisema kwa wasiwasi kidogo.





    Nilitii amri na kuifuata sauti ya Helena kwa kupapasa kutokana na kiza kizito cha mle ndani. Nilijawa na maswali mengi yasiyo na majibu kuhusu ujio wa Helena muda ule kwani ulikuwa tofauti na siku nyingine zote za nyuma.





    Nilipoikaribia sauti yake aliniita: “Shija.” “Naam, upo wapi?” “Nipo hapa, nipe mkono.” Nilipapasa mkono hewani na kufanikiwa kulishika bega, Helena aliushika mkono wangu na kuanza kuondoka. Kwa vile ilikuwa giza sikujua ananipeleka wapi.




    Niliendelea kutii amri na kumfuata kwa nyuma kila kona aliyopita kwa kuvuka milima na mabonde. Muda ulionyesha ni alfajiri kutokana na nuru hafifu kuitawala anga huku baridi kali ikiendelea kunipiga.



    Baada ya mwendo usiopungua saa mbili tulifika kwenye kijito, hapo Helena aliniamuru nioge kwa sabuni aliyokuwa nayo. Maji yalikuwa ya baridi sana, nilihisi kama damu inataka kuganda mwilini.



    Nilipomaliza kuoga, alinipa dawa ya unga kulamba. Baada ya kulamba nilijiona mwepesi kuliko kawaida na kujiona nipo dunia mpya na mimi mtu kwenye watu.





    “Shija unajikiaje?” Helena aliniuliza. “Yaani nauona mwili mwepesi kama nimevuliwa kitu kizito nilichokuwa natembea nacho mwilini. Pia nimeona vitu vingi ambayo toka niingie ndani sikuwa kuviona, inaonesha nipo dunia ile niliyoizoea miaka mingi iliyopita na vile vile napata hewa safi ambayo ni nyepesi puani kwangu tofauti na mwanzo,”

    ilikuwa ajabu ya mwaka baada ya kulamba dawa nilijiona nimeingia dunia mpya.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuona tofauti ya mwanzo na muda ule nilipolamba dawa, Helena alitoa dawa nyingine na kuanza kunisugua baadhi ya sehemu za mwili wangu. “Helena kufanya hivi unamaanisha nini?” “Hapa nafuta chale za kichawi ambazo huwa kama muhuri wa kutambulika popote kuwa wewe ni mtu wao.”





    “Baada ya hapa inakuwaje?” “Shija mpaka sasa upo katika dunia uliyoizoea na hapa tupo maeneo ya Kahangara.” “Kahangara ya Magu?” “Ndiyo.” “Usiniambie Helena!” Nilishtuka nisiamini.





    “Kweli?” “Ina maana tayari umenitoa kwenye dunia ya wafu?” “Ndiyo Shija.” “Siamini.” “Kweli.” “Hawawezi kutukamata?” “Hawawezi .” “Siamini! Nimetoka kwenye umsukule.” “Amini sasa hivi wewe si msukule tena.” “Helena kweli?”





    Bado sikuamini niliona kama ananifurahisha kwa kitu kisichowezekana . “Kweli kabisa Shija.” “Yaani dunia naiona mpya bila kunieleza hapa wapi wala nisingepajua.” “Kweli, inaonekana kukaa ndani muda mrefu umeanza kusahau vitu vingi.” “Siamini kama kweli mimi si msukule sasa?” “Amini, sasa hivi tuna kazi ya kujipanga kufika kwenu na mtu yeyote asikutambue.”





    “Si umesema nisirudi nyumbani?” “Ndiyo, hii safari kwa mjomba wako.” “Tutafikaje?” “Nitakutanda khanga uonekane mwanamke, nilitaka nikuache uende peke yako lakini wasiwasi wangu unaweza kupotea na kuwa kituko kwa watu.





    Nitakupeleka mpaka kwa mjomba wako ukiifahamu nyumba mimi nitarudi.” “Kwa nini usiingie ndani?” “Kumbuka hii ni siri yetu wawili , hatakiwi mtu yeyote kuijua.” “Helena mama yako yupo wapi?” “Mmh! Amesafiri na baadhi ya wachawi wenzake.”





    “Wamekwenda wapi?” “Wamekwenda kwenye mkutano mkuu wa wachawi Sumbawanga.” “Mmh! Mkutano huo unachukua siku ngapi?” “Siku mbili.” “Tokea lini?” “Jana usiku na leo.” “Asiponikuta itakuwaje?” “Hawezi kunifanya lolote.” “Si atanitafuta?” “Atakupata wapi?”

    “Chale nilizokufuta zitamfanya asikuone tena, labda mkutane kawaida lakini kichawi hawezi kukuona.”





    “Tutakwenda Mwanza kwa miguu?” “Hapana, tutapanda basi.”

    “Nauli unayo?” “Shija mpango huu nimeupanga muda mrefu kwa hiyo kwa hilo usiwe na wasiwasi .” “Siamini mpaka nikutane na mjomba.” “Shija naomba uniamini sitaki tena maswali ya kijunga,” Helena alichoshwa na maswali yangu ya kijinga. “Samahani Helena kama nimekuudhi.”



    “Maswali gani kila nikikueleza unielewi?” “Najua nitakuudhi lakini bado naona kama ndoto.” “Pole Shija, samahani kwa kukukaripia, lakini sasa hivi kama mfungwa upo huru labda ufungwe kwa kosa lingine.” “Barabara ya kuelekea Mwanza iko wapi?”

    “Ni mwendo kidogo, tufanye tuondoke eneo hili kabla wanakijiji hawajaanza kupita kwenda kwenye kilimo.” Helena alifungua mfuko wa plastiki na kutoa kaptura na fulana ambavyo alinipa nivae na kuzitupa za zamani.





    Baada ya kubadili nguo, alinipa khanga mbili, moja nilijifunga chini na nyingine nilijitanda juu na kuwa kama mwanamke. Helena alifanya vile vile kisha tuliondoka eneo lile la mto na kufuata njia aliyokuwa akiijua Helena kuelekea barabarani. 




    Tulitembea kwa mwendo wa dakika kama kumi na kutokea kwenye barabara kuu itokayo Musoma kwenda Mwanza. Baada ya kuiona barabara, akili yangu kidogo ilianza kupata mwanga japo bado sikuelewa ile ni sehemu gani pamoja na kuelezwa kuwa ni Kahangara





    Muda ulionesha kuwa kunazidi kupambazuka kutokana na mwanga kuongezeka. Pia watu waliongezeka, kila mmoja akiwa na lake. Wakulima walielekea mashambani na wanafunzi mashuleni, pia kituoni tulipokuwa tumesimama watu wachache waliongezeka.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ******************

    Kijua nacho kilianza kuchomoza kuonesha kumepambazuka. Tulisimama kituoni nikiamini kabisa watu walijua sisi sote ni wanawake . Baada ya muda, basi la kutoka Magu liliwasili. Tulipanda na kusimama kutokana na siti zote kuwa na watu.

    Helena aliniuma sikio kwa sauti ya chini. “Usizungumze kitu, mambo yote niachie mimi.” “Sawa,” nilimjibu kwa sauti ya chini. Basi lilielekea Mwanza huku nikiwa bado siamini kama kweli nimetolewa kwenye umsukule japo ilikuwa tofauti na siku za nyuma Helena alipojaribu kunitoa kwenye himaya ya wachawi na kukutana na matukio ya ajabu yaliyonikwamisha .

    Japo gari lilikuwa likienda, bado sikuamini kama tutavuka salama. Basi lilipofika maeneo ya Kisesa, wingu zito lilitanda mbele na upepo mkali ukaanza kuvuma na kusababisha tufunge madirisha. Wasiwasi uliniingia nikajua mambo yameiva , nilijiuliza kama nikikamatwa tena na wachawi watanifanya nini?

    Haukupita muda mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilishuka. Kutokana na upepo mkali, nusura gari tulilokuwa tumepanda lianguke baada ya kuyumba na kuteleza mpaka pembeni ya barabara. Wakati huo mbele kulikuwa hakuonekani vizuri kutokana na mvua kuwa kubwa.

    Moyo ulinienda mbio kwa hofu na kuamini kabisa wachawi tayari wameshatuzingira. Pamoja na kuwa na baridi kali kutokana na mvua ile ya asubuhi, mimi kijasho kilikuwa kikinitoka. Helena aliugundua wasiwasi wangu na kuniuliza:

    “Shija vipi?” “Naona mambo yameharibika.” “Mambo gani?” “We huoni mvua.”

    “Sasa mvua imeharibu nini?”

    “Naona kama tumefuatwa.” “Na nani?” “Si wachawi !” “Shija hebu acha hofu, kwani mvua yote ni ya wachawi ” “Lakini si unaona jinsi hali ilivyo , bado kidogo gari lianguke.”

    “Ni hali ya mvua tu, inaonekana upepo umemfanya dereva asione vizuri mbele. Wazo la kusubiri mvua ipungue ni zuri, la sivyo anaweza kutuangusha. Barabara inateleza sana kwa muda huu.” “Helena ni kweli usemayo si hila za wachawi ?” “Walaa, niamini mimi.

    Hakuna kitu chochote kibaya kitakachokutokea , kama kikitokea ni amri ya Mungu wala si wachawi .” “Basi niliogopa sana, nilijua ni yale yale ya siku zote.” “Shija usiwe na wasi, mpango huu hakuna anayeujua mpaka mama arudi kwenye mkutano, muda huo utakuwa umeshafika kwa mjomba.”

    “Ooh, afadhali maana kwa upande wangu hali ilikuwa mbaya.” Tulisubiri mpaka mvua ilipokatika ndipo tulipoendelea na safari.

    Nilimshukuru Mungu baada ya kuingia Mwanza salama. Tulipanda daladala hadi Pasiansi kwa mjomba. Tulipokaribia, kutokana na maelezo ya Helena kuwa hataki kufika pale, aliomba nimuoneshe nyumba kisha tuagane. “Helena, tumekaribia kwa mjomba.”

    “Ni wapi?” “Nyumba hiyo hapo yenye rangi ya maziwa, nje kuna nguzo ya umeme.” “Sasa Shija, nafikiri kazi yangu imekwisha. Nakuomba uende salama na Mungu akulinde kwa kila jambo.” “Asante Helena, nawe Mungu akulinde japo najua nimekuachia mtihani mzito na mama yako.”

    “Shija hilo lisikutie hofu, hakuna chochote kitakachotokea. Muhimu katika ahadi yangu ilikuwa ni kukulinda. Niliposhindwa niliapa kukutoa kwenye dunia ya wafu, namshukuru Mungu ahadi yangu kwako imetimia.” “Nashukuru sana Helena, sijui nikulipe nini?”

    “Hakuna cha kunilipa, Shija umenifundisha vitu vingi maishani mwangu ambavyo sikutegemea kuvipata kwa kijana mdogo kama wewe .” “Helena busara si umri bali uwezo wa kuchambua baya na zuri na kufikisha maneno yenye kumfanya mtu apate kitu kupitia wewe bila kujali umri wako.”

    “Shija nakuomba tena usikubali kurudi kijijini. Kwa muda huu baki kwa mjomba, pia siri hii ibakie moyoni mwako.” “Nitafanya hivyo Helena.” “Mwisho Shija nakutakia maisha marefu yenye furaha, kwa vile nimepajua nitakuja siku moja, kwa heri! Msalimie mjomba, mkewe na wadogo zako.”

    Helena alisema kwa sauti ya majonzi huku machozi yakimtoka , kitu kilichofanya nami nitokwe na machozi.

    ”Asante Helena, nawe nakutakia harusi njema na Mungu akuepushe na nguvu za kichawi.” “Asante Shija.” Tulikumbatiana kabla ya kuagana, tulishikana kwa muda huku kila mmoja akilia kilio cha kweli.

    Baada ya kuachiana, Helena alisema kwa sauti ya mafua kutokana na kutokwa na kamasi nyembamba.

    “Shija nakupenda sana, hata sijui moyo wangu umeuwekea kitu gani.

    Nimekubali kuolewa kwa vile nauchukia uchawi lakini bila hivyo nisingeolewa kamwe, ningekusubiri.”

    “Asante Helena kwa kunipenda, hata mimi nakupenda na nitaendelea kukupenda siku zote za maisha yangu. Nakuona ni zaidi ya pumzi ninazovuta. Helena olewa ukijua Shija anakupenda sana.”

    “Na Sabina?” Helena aliniuliza swali la uchokozi. “Wote nitaendelea kuwapenda kama tulivyokuwa tukipendana tukiwa shule ya msingi.” “Asante Shija, kwa heri,” Helena aligeuka na kuondoka huku akilia kilio cha kwikwi , kitu kilichoniacha njia panda. Nilitaka kumwita lakini mdomo ulikuwa mzito.

    Nilimsindikiza kwa macho mpaka alipopotea machoni mwangu. Nilisimama kwa muda nikijiuliza Helena kanifikisha mpaka jirani kwa mjomba, sawa lakini swali kubwa ni mjomba atakaponiona atanipokea vipi? Niliamua niende tu, mengine yangejulikana huko huko.


    Nilitembea taratibu kuelekea nyumbani kwa mjomba, muda ulionesha bado asubuhi kwani hata mlango ulikuwa haujafunguliwa.

    Kabla ya kugonga nilijifikiria nizivue zile khanga au niingie nazo vilevile . Niliamua kuingia na khanga zangu ili wasishtuke mapema.

    Niligonga mlango na kusubiri, mke wa mjomba ndiye aliyekuja kunifungulia, nilijua hakunifahamu baada ya kuniona. “Karibu, una shida gani?”

    Aliniuliza akiwa bado amesimama mlangoni. “Nataka nimuone mjomba.” “Mjomba wako nani?” “Mayunga.” “Mayunga! Wewe nani?” “Shi..,” nilisita kulitaja jina langu. “Umesema nani?” “Shija.” “Shija si jina la kiume hilo?” “Ndiyo.”

    Nilisema huku nikitoa khanga niliyojitanda kichwani, nilimuona macho yakimtoka pima kama kaona ngamia akipita kwenye tundu la sindano.

    Akitaka kujirudisha nyuma ili anikimbie, niliamini kabisa aliniona si mtu wa kawaida bali mzimu wangu kwa vile aliamini nimekwisha kufa na kuzikwa . Shangazi alipiga kelele: “Jamani nakufa..,” alianguka chini na kupoteza fahamu, mjomba ambaye alionekana amemaliza kujiandaa ili aende kazini.

    Alikuja mbio na kumuwahi mkewe bila kuniangalia mimi ni nani. Bila kunitazama usoni aliniuliza: “Amefanya nini huyu,” aliendelea kumtazama mkewe aliyekuwa amepoteza fahamu.

    “Ameshtuka baada ya kuniona.” “Kukuona?” Aliuliza huku akinitazama aliponiona ni mimi alishtuka kiasi cha kumbwaga mkewe chini. “Ha! Wee nani?” “Shija mjomba.”

    “Hapana, hiwezekani haya ni maajabu.”

    “Siyo maajabu, sikufa mjomba.” “Kama hukufa aliyekufa ni nani?” “Mjomba kile ni kiini macho cha wachawi .” “Muda wote huo ulikuwa wapi?” “Mjomba mshughulikie kwanza shangazi nina mengi ya kuzungumza juu ya kifo changu cha bandia.”

    Mjomba alimpatia huduma ya kwanza shangazi ambaye alirudiwa na fahamu lakini ilionesha bado ananishangaa. “Huyu si Shija?” Shangazi aliuliza kwa sauti ya juu. “Ndiye.” “Mungu wangu! Haya si maajabu Shija katoka kuzimu si alikufa huyu?”

    “Sijafa Shangazi kilikuwa kiini macho cha wachawi .” “Kama hukufa nani alikufa tukamzika?” “Shangazi mimi sikufa ila kilichotendeka siku ile ni kiini macho tu, hamkuzika mtu bali kipande cha mgomba.”

    “Na wewe ulikuwa wapi siku zote?” “Ni stori ndefu shangazi.” “Jamani haya ni maajabu ni kweli Shija hujafa?” Shangazi aliendelea kunishangaa. “Kama ningekuwa nimekufa nisingeonekana leo.” “Muda wote ulikuwa wapi?” Mjomba aliniuliza.

    “Nilikuwa naishi maisha ya kimsukule.”

    “Mungu wangu! Umewezaje kutoka katika maisha hayo? Hizi khanga umezitoa wapi?” “Ni mtoto wa mchawi aliyenichukua msukule.”

    “Ndiye aliyekutoa?”

    “Ndiyo.”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Na siku ya msiba wako ulikuwa wapi?” “Nilikuwa nyuma ya mlango, yote mliyokuwa mkifanya niliyaona, wakati mnakuja nilisikia hata mlipoingia ndani kumpa pole mama na kuangua kilio, yote nilikuwa nayaona.

    Hata makaburini nilihudhuria mazishi yangu.” “Hii kali kweli wachawi viumbe wa ajabu,” alisema mke wa mjomba huku akishika mikono kiunoni.

    “Sasa wamekuachia au imekuwaje?” “Nimetoroshwa.” “Mungu wangu ilikuwaje mpaka ukatoroshwa?” “Ni habari ndefu, naomba nioge niondoe nuksi ya maisha ya nusu kuzimu na nipate chakula maana hapa njaa inaniuma kama kidonda.”

    Nilipatiwa vitu vyote kwa haraka hata safari ya mjomba na mkewe kwenda kazini iliahirishwa ili kutaka kujua maajabu chini ya jua. Baada ya kuoga na kupata kifungua kinywa nilikaa kitako kuwaeleza yaliyonisibu huku nikiificha siri ya kumtaja Helena na mama yake kwa usalama wa kijijini.

    Siku hiyo nilichukuliwa na kupelekwa kwenye kanisani kufanyiwa maombezi kwa utukufu wa Mungu kuonesha jinsi nguvu zake zinavyoweza kuushinda uchawi.

    Mjomba alitaka kunipeleka nyumbani, nilimweleza masharti niliopewa na mtu aliyenitoa kule kuwa nisirudi tena kijijini.

    Mjomba alikubaliana na mimi nibakie kwake , wazazi wangu walifuatwa , hawakuamini lakini niliwaeleza ilivyokuwa na kukubaliana na mimi, ilikuwa furaha isiyo kifani.

    Baada ya muda niligundua kumbe niliishi maisha ya umsukule kwa mwaka mmoja na miezi sita.

    Mjomba alinitafutia shule ambayo nilisoma kwa miaka miwili na kufanya mtihani wa kidato cha nne.

    Majibu yalikuwa mazuri kwa kupata ‘division two’ iliyoniwezesha kuingia kidato cha tano mpaka chuo kikuu

     


    MWISHO.....................    

0 comments:

Post a Comment

Blog