Search This Blog

PENZI LA SHETANI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : ISACK FLORIAN



    *********************************************************************************

    Simulizi : Penzi La Shetani

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    Mark ni kijana ambaye alizaliwa na kukulia katika familia ya kimaskini sana.Tangu akiwa mdogo Mark, yeye pamoja na familia yake waliishi kwa kutegemea misaada kutoka kwa watu mbalimbali waliojitoa kuwasaidia.Licha ya familia yake kuwa na hali duni ya kimaisha Mark, alipofika umri wa kuanza shule, familia ilijitoa na kwenda kumuandikisha kwa ajili ya kuanza elimu ya msingi.Wazazi wake waliamini kupitia elimu atakayoipata kijana wao itaweza kumsaidi yeye asije kuishi maisha kama yao, kwa sababu wao waliishi vile kutokana hawakuwa na msingi wowote wa kielimu walioupata katika maisha yao.

    "Samahani mama naweza nikakuuliza swali?" Mark alimuomba mama yake ili amuulize swali.

    "Niulize tu mwanangu"

    "Tangu nizaliwe nimeshuhudia mambo mengi sana katika dunia hii, lakini jambo linalonishangaza ni kuwaona baadhi ya watu wakiwa na maisha mazuri na matajiri sana na baadhi ya watu wengine kama sisi tumekuwa na maisha ya dhiki na kuishi kwa kutegemea kuomba misaada tu.Swali langu mama, Je Mungu alichagua hapa duniani baadhi ya watu kuwa matajiri na na watu wengine kuwa maskini?", Mark alimuuliza mama yake na kumfanya mama atabasamu kidogo kabla ya kumjibu swali lake.

    " Mark mwanangu, Mungu hakuchagua mtu yoyote hapa duniani kuwa tajiri wala maskini ila kwake yeye wote sisi ni sawa.Maisha ya kifahari na utajiri yanapatikna hapahapa duniani tu, hata wewe Mark mwanangu unaweza ukawa tajiri."

    "Kweli mama!, kivipi naweza kuwa tajiri"

    "Ukiweka bidii katika masomo yako na kumuomba Mungu kila siku akusaidie kutimiza malengo yako."

    "Asante sana mama, basi naamini na mimi nitawafanya mje kuishi vizuri sana na naamini kupitia msaada wa Mungu anaonipatia, ipo siku moja naamini na mimi ndoto zangu zitakamilika."

    "Kwani wewe una ndoto zipi baba?"

    "Samahani mama sitokueleza sasa bali nitataka uzishuhudie wewe mwenyewe zitakapokuwa tayari nimezikamilisha." Mark alimjibu mama yake na kumfanya afurahi sana, mama alimpongeza kijana wake kutokana na kuwa madadisi sana na kumtia moyo wa kuwa na bidii katika masomo yake.

    Ndoto kubwa ya Mark ilikuwa ni siku moja kuifanya familia yake kuishi maisha mazuri na yeye kuja kuwa tajiri mkubwa sana, Mark aliamini ndoto zake hizi zote zinaweza kukamilika kama yeye atakuwa na bidii na kufanya vizuri katika masomo yake.



    Miaka ilizidi kusonga, na Mark alionekana akifanya vizuri sana katika masomo yake na watu wengi walimtabiria mambo makubwa Mark siku za usoni kutokana na bidii kubwa aliyoiweka katika masomo yake.Familia yake nayo ilifarijika sana na kujiona ijapokuwa wao ni maskini sana na watu wa kudharaulika kila siku lakini wanao utajiri mkubwa kutoka kwa kijana wao Mark.Licha ya elimu yake Mark kuipata katika mazingira magumu sana kutokana na hali ya kiuchumi iliyokuwepo nyumbani, lakini yeye hakujali wala kuyafikiri yale zaidi aliamini ipo siku moja yote yatabaki historia katika familia yake zaidi yeye ni kuongeza bidii katika masomo yake.Kutokana na muenendo ule wa Mark katika masomo yake, Mark alipofika darasa la saba alifanikiwa kufaulu kwa wastani wa juu sana na kufanikiwa kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya kidato cha kwanza.Mark alifurahi sana na aliona hii ni moja ya nafasi ya kwenda kufanya vizuri zaidi kwa ajili ya kukamilisha ndoto zake alizojiwekea awali.

    Japokuwa familia ilikuwa na furaha kubwa ya kijana wao kuweza kufaulu mtihani wake, lakini walikabiliwa na tatizo kubwa la kuweza kupata fedha za kumpeleka kujiunga na masomo ya sekondari.Baba yake Mark alijitahidi kutafuta misaada mbalimbali lakini bado ilikuwa ngumu kupata fedha za kutosha za kuweza kumsaidia Mark kujiunga na elimu ya kidato cha kwanza.Familia ilionekana kushindwa kabisa na kutokuwa na uwezo wa kupata fedha mahali popote kwa ajili ya kumsomesha Mark.Walikata tamaa kabisa na kutokuwa na uwezo kabisa wa kumundeleza Mark katika masomo yake.

    "Mark mwanangu?" mama alimuuita kijana wake Mark.

    "Ndio mama"

    "Mimi na baba yako tumejitahidi kadri ya uwezo wetu lakini mpaka sasa tumeshindwa na kupoteza tumaini kabisa la kukusomesha" Kwa uchungu mkubwa huku kilio kikiwa kimemtawala, mama alimueleza Mark.

    "Hapana mama, elimu yangu kuishia hapa si mwisho wa mimi kukamilisha ndoto zangu, nadhani Mungu atanionyesha mlango mwingine wa kupita." Kwa ukarimu mkubwa , Mark alimueleza mama yake huku akimfuta machozi machoni mwake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mark pamoja na familia yake wakionekana kukata tamaa kabisa ya yeye kuendelea na masomo, mara akatokea mtu na kuomba kumdhamini Mark katika masomo yake mpaka atakapomaliza elimu yake.Mdhamini yule alitokewa kuvutiwa na uwezo mkubwa wa Mark aliouonyesha katika masomo yake na akaona ni bora amdhamini kijana yule ili aweze kumsaidia kutimiza ndoto zake.



    Mtu yule ambaye alijitolea kumdhamini Mark, alikuwa ni raia wa Marekani na alikuwa akiishi Tanzania kwa ajili ya kusimamia miradi mbalimbali ambayo ilianzishwa na nchi yake hapa Tanzania.Hakika familia ilipata faraja na kumshukuru sana Mungu pamoja na mdhamini yule kwa kuwapa msaada ambao hawakutarajia kuupata kwa wakati ule.Furaha kubwa sana ilimjaa Mark na kuona sasa bado ana nafasi kubwa ya kukamilisha malengo yake aliyojiwekea katika maisha yake.Muda ulipofika, Mark akafanikiwa kujiunga na elimu ya Sekondari kwa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Dakawa huku akiendelea kupokea msaada mkubwa kutoka kwa yule mzungu aliyejitolea kumdhamini.Shule ya Sekondari Dakawa, hii ni shule ambayo ilikuwa inafaulisha wanafunzi wengi sana na ilikuwa inamilikiwa na mtu binafsi.Kutokana na uwezo mkubwa wa masomo aliokuwa nao Mark, Kuliko Mark akasoma katika shule za kiserikali mzungu yule akaona ni bora amsomeshe katika shule hii inayotoa elimu bora sana .



    Miaka ilizidi kusonga, ufaulu wake Mark ulizidi kuongezeka kutokana na jitihada kubwa ambazo alizielekeza katika masomo yake na akafanikiwa kufika kidato cha nne.Baadhi ya wanafunzi walimpenda sana Mark pale shuleni na kupenda kujifunza Mengi kutoka kwake lakini wanafunzi wengi walimchukia kwasababu hawakupenda kuongozwa katika masomo na mtu ambaye ni maskini.Kutokana wanafunzi wengi walitambua Mark anasomeshwa pale kwa kutegemea msaada, walidiriki kumbatiza jina na kumuita ombaomba.Changamoto zilikuwa nyingi sana kwa Mark pale shuleni, lakini yeye hakujali zaidi alishirikiana na wale ambao walipenda kushirikiana nae katika masomo.



    ********************************************

    Sala ni binti ambaye alizaliwa na kukulia katika familia yenye kujiweza kidogo kiuchumi.Pia sala alikuwa ni binti mpole sana na aliyekulia katika misingi ya kidini sana.Sala alikuwa ni binti mrembo sana na licha bado alikuwa ni mwanafunzi, wanaume wengi walitamani kuwa nae kimapenzi lakini yeye alisimama katika misimamo yake kwa sababu ni binti ambaye alikuwa mwenye kuheshimu sana usichana wake na kutambua nini anachopaswa kufanya kwa wakati sahihi.Sala nae alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari Dakawa.



    ****************************************



    Ikiwa ni mida ya asubuhi, Mark akiwa darasani huku akiendelea kujisomea mara anakuja moja ya marafiki zake pale shuleni na kumsemesha.

    "Mark, hivi unasoma kupitia njia gani rafiki yangu ambazo sisi hatuzitumii tukaweza kuongeza ufaulu wetu?' Aliuliza Nick ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Mark.

    " Nick, sina njia yoyote ninayoitumia zaidi ya kusoma sana na kumuomba Mungu tu."

    "Mbona sisi tunafanya hivo lakini bado hatufanikiwi."

    "Nick, tatizo lako hupendi kushirikiana na wenzako kwa kujiona unajua kila kitu, ukitaka kujifunza mengi na kufanya vizuri darasani ni lazima ujishushe na kupenda kushirikiana na wenzako kama ninavyofanya mimi."

    "Mark, mimi mwenyewe naweza nikasimama tu bila ya mtu mwingine, nikishirikiana na wewe rafiki yangu inatosha tu."

    "Sawa Nick, ila naomba tu ubadilike katika hilo, ushirikiano ni bora kuliko kusimama mwenyewe."

    "Mark embu tuachane na hayo, jana ulionana na Sala?, maana alikuja kukuulizia kwangu"

    "Sala!?, Sala ameniulizia mimi Nick!".Mark alishangaa sana baada ya kusikia Sala alimuulizia yeye.

    Sala alikuwa ni binti ambaye huwa anajitenga na kupenda kukaa peke yake kwasababu wanafunzi wengi pale shuleni walimsumbua kutokana na urembo wake.Wanafunzi wa kike walimuonea wivu sana Sala na baadhi ya wanafunzi wa kiume walimsumbua Sala kwa kutaka kuwa nae kimapenzi.Kuyaepuka yote hayo ndipo sala akaona ni heri akajitenga nao na kuamua kufanya mambo yake akiwa mwenyewe bila kuambatana na mwanafunzi yoyote wa pale shuleni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mark alishangaa na kujiuliza sana, kwanini Sala anamtafuta na kumuulizia yeye wakati si kawaida ya binti yule kuwa na ukaribu na mwanafunzi yeyote pale shuleni.

    "Nick una uhakika na unachokiongea?" Kwa msisitizo mkubwa, Mark alimuuliza rafiki yake Nick.

    "Mark, hata mimi mwenyewe nilishangaa kama wewe hivyo ila pengine bahati imekudondokea baba maana si unajua binti mwenyewe alivyokuwa mgumu yule." Alizungumza Nick na kumtania kidogo rafiki yake Mack.

    Wakiwa wanaendelea na mazungumzo mbalimbaki, Mark pamoja na rafiki yake Nick, mara Sala anaingia darasani na kwenda mpaka karibu yao akawasalimu na kukaa kwenye kiti ambacho kilikuwa karibu na sehemu aliyokaa Mark.

    "Nick, unaweza kutupisha kidogo nataka kuongea na rafiki yako kidogo." Sala alimuomba Nick awapishe, naye Nick akatii.

    "Sala, Nick alinieleza unanitafuta, vipi kuna tatizo lolote?" Mark akamuuliza Sala na kumfanya Sala atabasamu kabla ya kumjibu Swali lake

    "Naweza nikakuomba kitu Mark?"

    "Ndio Sala, nakusikiliza" Mark alijibu huku akiwa na hofu kiasi fulani.

    "Naomba tutoke nje ya darasa nikakueleza kitu" Sala alimuomba Mark, Akamshika mkono na kutoka nae nje ya darasa.Wanafunzi wengi waliokuwemo darasani walishangaa na kujiuliza sana, inawezekanaje Sala akawa na urafiki na maskini kama yule mpaka kufikia hata kushika mkono wake.





    Sala alimchukua Mark hadi nje, akatafuta sehemu iliyotulia, wakaketi na kuzungumza.

    "Sala, unajua umefanya kitu cha ajabu sana leo, hivi haugopi kabisa kupata aibu na kushuka kwa hadhi yako kwa kuongozana na mtu kama mimi?"

    "Mark kwanini unaongea maneno kama hayo?,

    Kwanini unapenda kujiona mtu usiyekuwa na thamani mbele ya watu?" Aliuliza Sala.

    " Hapana Sala, mimi najiona si mtu kati ya watu.Wengi wamekuwa wakinitenga na kunidharau kwasababu mimi ni maskini pamoja na familia yangu na..."

    "Shiiiiiiiii...!!?, inatosha Mark, acha kumkufuru Mungu kwa mambo yasiyokuwa ya msingi.Kama wewe unajiona hauna thamani ila kwangu mimi wewe una thamani kubwa sana."

    "Nini unachomaanisha Sala?"

    "Tangu nije katika shule hii sikufanikiwa kupata rafiki mwema kwangu, wengi wao walitengeneza urafiki na mimi kwa malengo yao binafsi.Lakini baada ya kukuangalia wewe uko tofauti kabisa na wanafunzi wengine hapa, kama hutojali Mark nina ombi moja kwako."

    "Una ombi kwangu!, sawa nakusikiliza Sala".Mark alishtuka kidogo.

    "Nahitaji uwe unanifundisha baadhi ya masomo ambayo yananisumbua mno darasani.Je uko tayari Mark?"

    "Katika suala la elimu, mimi huwa sibagui mtu wa kushirikiana nae kwahiyo usijali Sala tutakuwa wote pamoja katika hilo." Mark alimjibu Sala.Sala alifurahi sana na kumshukuru Mark kwa busara yake kubwa aliyoitumia katika kumkubalia ombi lake.



    Maisha ya shule yalizidi kuendelea,ushirikiano katika masomo baina ya Mark pamoja na sala ulizidi kukua huku wakipitia katika kipindi kigumu kutokana na changamoto mbalimbali wazipatazo kutoka kwa wanafunzi wengine lakini Mark na Sala hawakujali yale zaidi walijikita katika kusoma.Mark pamoja na Sala ushirikiano wao ulijikita zaidi katika masomo bila kuhusisha mambo mengine ya ujana.Kipindi cha kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne nacho tayari kilishakuwa karibu, hivyo Mark akiwa na baadhi ya marafiki zake pamoja na Sala, waliongeza zaidi bidii ya kusoma kwa ajili ya kujiandaa na mtihani huu muhimu katika maisha yao.



    Hali ya kimaisha nyumbani kwa kina Mark ilizidi kuwa mbaya, chakula kilikuwa tabu sana kupatikana na kukosekana baadhi ya mahitaji mengine ambayo ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu.Mama yake Mark nae alikuwa mgonjwa sana na hali yake ilizidi kuwa mbaya kila siku kutokana na kukosa dawa zozote ambazo zingeweza kumsaidia.Yote haya yalitokana na umaskini mkubwa uliotawala pale nyumbani.

    "Sijui nifanye nini mke wangu ili niweze kukusaidia maana nimeshahangaika sana kutafuta msaada bila mafanikio yoyote." Aliongea baba yake Mark na kumueleza mke wake.

    "Usiteseke na kuhangaika sana mme wangu, kama Mungu amepanga bado niwepo katika dunia hii basi nitaishi tu lakini kama atanichukua basi tumshukuru yeye tu." Huku akiongea kwa tabu sana, mama Mark alimwambia mume wake.

    "Hapana mke wangu usizungumze maneno hayo, yupo mtu mmoja wa mwisho ambaye nataka kwenda kumuona ofisini kwake ili aweze kunisaidia."

    "Nani huyo tena mume wangu!?"

    "Ni yule mzungu ambaye amejitolea kumsomesha kijana wetu."

    "Sawa mme wangu lakini naomba kama inawezekana umwa...!??" Alizungumza mama yake Mark, lakini kabla hajamalizia kuzungumza sentesi yake ghafla akaanza kukohoa na alikuwa akikohoa damu.Baada ya kukohoa sana damu, mara mama yake Mark akabaki akihangaika pale kitandani alipolala, huku macho yakiwa yamebadilika na kuanza kuwa na rangi nyeupe tu.Hali ile ilimshtua sana mume wake na kuona hali ya mkewe inazidi kuwa mbaya na anahitaji msaada wa haraka iwezekanavyo. Mzee Peter(baba yake Mark) huku akionekana kama amechanganyikiwa kiasi fulani kutokana na hali aliyokuwa nayo mkewe, bila kuchelewa alitoka haraka ndani na kukimbia kuelekea ofisini kwa yule mzungu ambaye ndiye alimdhamini kijana wao Mark katika masomo yake.Akiwa njiani mzee Peter, mawazo yalikuwa mengi sana na kuhisi pengine anaweza kumpoteza mke wake kama atakosa msaada wa haraka.Akiwa barabarani huku akiwa hana hili wala lile mzee Peter, ghafla inatokea gari nyuma yake ambayo ilikuwa katika mwendo mkali sana na kuja upande alipokuwa anatembea yeye ambapo ni pembezoni kidogo mwa barabara.Ukunga mzito ulisikika mahali pale na watu wote waliokuwa karibu na eneo lile walshtuka sana na kutoamini kwa kile kilichotokea pale.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mark akiwa pamoja na Sala, waliendelea kusoma kwa bidii sana huku muda mwingi wakiwa wanashirikiana kwa ajili ya maandalizi ya mtihani taifa wanaotarajia kuufanya siku za karibuni.

    Siku hii Mark hakuwa sawa kabisa, mawazo yalikuwa mengi sana kuhusiana na nyumbani hasa zaidi kuhusu hali ya mama yake.Kwakuwa Sala alishakaa na Mark muda mrefu sasa wakiwa pamoja akafanikiwa kuligundua lile.

    "Mark kwa jinsi nilivyokuzoea na ninavyokujua, leo naona haupo sawa kabisa.Vipi, kuna tatizo lolote linalokusumbua?" Aliuliza Sala.

    "Sala mimi nipo sawa tu, ila kuna baadhi ya mambo nyumbani hayajakaa sawa."

    "Unaweza ukanieleza Mark pengine naweza kukusaidia hata kwa kukupa mawazo kuweza kuyatatua hayo."

    "Sawa Sala, kwakuwa ni wewe pekee hapa shule umekuwa mwema sana kwangu, nitakueleza."

    "Ok, nakusikiliza Mark"

    "Kiukweli hali ya nyumbani kwetu sio nzuri kabisa Sala na ninavyoongea na wewe kwa sasa, Mama yangu ni......!!" Mark alimueleza Sala, lakini kabla hajamaliza maelezo yake kumuelezea Sala, mara anatokea mwalimu na kukatisha mzungumzo yao.Mwalimu yule alimtaarifu Mark kuwa anahitajika haraka sana ofisini kwa mkuu kwasababu yupo mtu amekuja kumuona.Wito ule wa ghafla ulimshtua sana Mark, huku akiwa na hofu kiasi fulani, akamuaga Sala na kuelekea ofisini kwa mwalimu mkuu.





    Mark alishangaa sana kumkuta baba yake pale ofisini tena akiwa katika hali ya huzuni sana, alimkimbilia baba yake pale alipokaa na kutaka kufahamu ni kitu gani kilichomkuta.

    "Mbona uko hivo baba, nini tatizo?,

    Au kuna kitu kibaya kimetokea juu ya mama yangu nyumbani?" Yalikuwa maswali ya Mark akimuuliza baba yake kwa mfululizo.Baba Mark alibaki kimya tu na kushindwa kumpa jibu lolote mtoto wake Mark.Mark alizidi kumuuliza baba yake maswali mengi na kutaka amueleze sababu iliyomfanya awe katika hali ile, lakini bado Mzee Peter alibaki kimya bila ya kumpa jibu lolote mtoto wake.

    "Mark usimsumbue sana baba kwasababu kuna matatizo kidogo yamemsibu na ambayo yamempelekea kuwa katika hali hiyo.Naomba umchukue baba na umpeleke nyumbani ili akapumzike." Mwalimu mkuu aliongea na kumtaka Mark amchukue na kumpeleka nyumbani baba yake.Huku akiwa na hofu na wasiwasi mkubwa Mark, akamchukua baba kwa ajili ya kumpeleka nyumbani.

    Wakiwa njiani Mark bado akawa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichomsibu baba.

    "Baba, kwanini unashindwa kunieleza chochote?, tafadhali baba naomba unieleze, nini tatizo." Mark aliongea na kumueleza baba yake.

    Baada ya kuona kiu kubwa ya kijana wake Mark ya kutaka kujua ukweli, Mzee Peter akaamua kufungua kinywa chake na kuzungumza.

    " Mark mwanangu, kwanza naomba ushukuru sana kuniona mimi baba yako nikiwa bado naendelea kuishi mpaka sasa."

    "Kwanini unasema hivo baba?"

    "Naomba tutafute sehemu tuweze kuketi ili niweze kukusimulia kila kitu Mark."

    "Sawa baba" Mark alimjibu baba yake na kutafuta sehemu kwa ajili ya kuketi ili aweze kuzungumza nae.



    ****************************************



    Hali ya Simanzi ilitawala kila kona, watu wengi hawakuamini kabisa kama ni kweli vifo vile vimetokea juu ya familia ile.Simanzi kubwa iliikuwa kwa binti yao kwa kuwapoteza wazazi wake wote wawili kwa mara moja.Alihisi dunia yote imemuelemea, aliona kama yale yote ni ndoto kwake na kujiuliza maswali mengi sana, kivipi anaweza kuishi peke yake bila ya uwepo wa mama wala baba katika dunia hii.Hakika binti huyu alibaki mpweke sana na hili lilikuwa pigo kubwa sana katika maisha yake.

    Baadhi ya ndugu na majirani walijitahidi kumbembeleza, kumpa pole na kuendelea kumsihi sana binti yule aweze kutulia na achukulie ile ni hali ya kawaida tu ambayo inaweza ikamtokea binadamu yeyote hapa duniani.



    *****************************************

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mark naomba unisikilize kwa makini mwanangu" Alizungumza mzee Peter

    "Sawa baba, nami nakusikiliza"

    "Siku ya leo katika mida ya mchana, hali ya mama yako ilibadilika na alikuwa na hali mbaya sana.Nilijaribu kuhangaika na kuzunguka sehemu nyingi kwa ajili ya kuweza kupata msaada wowote wa kuweza kumsaidia lakini kote huko sikufanikiwa kupata chochote kile.Baada ya kuona hali ya mama yako inazidi kuwa mbaya zaidi, ndipo nikapata wazo la kwenda kwa mdhamini wako ili nione kama naweza kupata msaada wowote kutoka kwake.Lakini wakati nipo njiani kuelekea huko, ndipo nilipokutana na balaa zito kijana wangu Mark."Aliongea mzee Peter lakini alishindwa kuendelea kumsimulia kijana wake kutokana na uchungu mkubwa kumjaa na kuanza kulia.

    "Balaa gani hilo baba!?,

    Tafadhali naomba unieleze baba." Mark alimuuliza baba yake na kumsisitiza amuelezee balaa hilo lililomsibu.

    " Mark, nikiwa natembea pembezoni mwa barabara, mara nikasikia kishindo kizito sana na nilipogeuka nyuma nikaona gari moja ndogo ambayo ilikuwa imegongwa vibaya sana na roli na sizani kama watu wale waliomo kwenye gari ile watakuwa wamesalimika.Mbaya zaidi, ilibaki kidogo tu gari ile ndogo iweze kunigonga kwasababu ilikuwa ipo katika mwendo mkali na ilikuwa ikija upande nilipokuwepo mimi kwa lengo la kulikwepa roli lile.Hayo ndiyo yaliyonisibu kijana wangu." Kwa uchungu mkubwa Mzee Peter alimsimulia kijana wake Mark.

    "Pole sana baba kwa hayo yote yaliyokusibu, hakika kweli Mungu ni mkubwa na muweza wa kila kitu hapa duniani.Naomba baba tusipoteze muda hapa, kwa sasa mama yupo peke yake nyumbani, naomba twende kwa yule Mdhamini wangu, tukaombe msaada ili tuweze kumuwaisha mama hospitali." Alizungumza Mark, na kutoka pamoja na baba yake kwa ajili ya kwenda kuonana na mdhamini wake.



    Mdhamini yule aliwaonea sana huruma Mark na baba yake na akachukua kiasi cha fedha akawakabidhi kwa ajili ya kwenda kumsaidia mama.Mzee Peter pamoja na Mark walishukuru sana kwa msaada ule na wakatoka haraka kwa ajili ya kuwahi nyumbani ili waweze kumchukua mama na kumpeleka hospitali kupata matibabu.

    Wakiwa karibu kabisa kufika nyumbani, Mark pamoja na baba yake walipigwa na butwaa na kuingiwa na wasiwasi baada ya kuona mkusanyiko mkubwa wa watu wengi pale nyumbani.



    "Baba mbona watu wengi wamekusanyika nyumbani kwetu!?, Pengine kuna kitu kipo tofauti pale nyumbani?" Mark alimuuliza baba yake, lakini baba alibaki kimya na kuongeza mwendo kwa ajili ya kuwahi ili akafahamu kinachoendelea pale nyumbani.Mark pamoja na baba yake walifika nyumbani na kukuta mwili wa mama ukiwa umefunikwa wote pale kitandani alipolala.Mzee Peter alipata hofu sana baada ya kuona hali ile iliyopo kwa mkewe.

    "Kwanini mmemfunika mke wangu namna hii!?,

    Nilitoka kidogo kwenda kuchukua fedha ya kuweza kumpeleka hospitali, naomba mfunueni niweze kumuwahisha hospitali." Huku akionekana kama amechanganyikiwa kidogo, mzee Peter alizungumza na kuuliza maswali ambayo yaikuwa magumu sana kupata majibu yake.

    Mzee mmoja ambaye alikuwa jirani na wanapoishi kina Mark, alimfuata mzee Peter ili aweze kuzungumza nae.

    " Mzee Dombo, naomba unisaidie kumuinua mke wangu pale kitandani niweze kumuwahisha hospital haraka." Alizungumza mzee Peter na kumueleza jirani yake yule.

    "Mzee Peter, kwa sasa umeshachelewa sana maana tayari mke wako hayupo tena katika ulimwengu huu.Pole sana jirani yangu lakini hiyo ndiyo hali halisi iliyokuwepo hapa." Mzee Dombo alimtaarifu mzee Peter kuwa tayari mke wake ameshafariki dunia.Nguvu zote zilimuisha mzee Peter, mapigo ya moyo wake yakawa yanaenda kasi mno, mara ghafla mzee Peter akadondoka chini baada ya kupata taarifa za kifo cha mke wake na kumshtua sana.

    Muda wote huo Mark alikuwa amebaki amesimama huku machozi yamkitoka machoni mwake, akashindwa kabisa kuamini na kukubaliana na lile kuwa mama yake Amefariki.Mark akakimbia hadi katika kitanda alipolala mama yake, akajitahidi kumuita mama kwa nguvu na kujaribu kumuamsha, lakini mama hakutikisika wala kutoa kauli yoyote ile.Watu wote walioudhuria pale waliionea huruma sana familia ile kutokana na mitihani migumu inayokutana nayo katika maisha yao.

    "Uliniahidi hutoniacha peke yangu mama, kwanini unanikimbia namna hii?,

    Ndoto zangu zote zitafutika kama sitokuwa na wewe mama, amka mama!, amka mama!

    Amka mamaaaaaaa.....!!!?", Ni baadhi ya maneno ambayo Mark aliendelea kuzungumza na kulalamika kwa kumtaka mama yake aamke pale kitandani alipolala.



    **************************************

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Binti aliendelea kulia sana na kuwalilia wazazi wake, kwanini wamemuacha peke yake katika dunia hii.

    "Uko wapi mama yangu mpendwa?,

    Kwanini mmeniacha peke yangu mimi?,

    nitaweza kuishi vipi bila ya ninyi wazazi wangu katika dunia hii?" Ni baadhi ya maswali ambayo aliendelea kujiuliza binti huyu na kwa uchungu mkubwa sana kutokana na msiba ule wa wazazi wake.

    Watu walio karibu nae, waliendelea kumtuliza binti na kumtaka awe mvumilivu katika wakati ule mgumu kwake.



    ***************************************



    Katika shule ya Sekondari Dakawa, kengele ya dharura ilipigwa na wanafunzi wote walihitajika kukusanyika haraka ili waweze kuelezwa kuhusiana na dharura ile.Baada ya muda mfupi, wanafunzi wote wakakusanyika mstarini ili waweze kuelezwa lengo la kengere ile ya dharura kupigwa.Wanafunzi wote baada ya kuwasili, mwalimu mkuu naye akawa tayari kuweza kuzungumza na wanafunzi wake.Aliwasalimu na kuwaeleza lengo la wito ule mahali pale.

    "Natumaini nyote niwazima na manaendelea vizuri na masomo yenu.Nimewaita hapa kwa ajili yakuweza kuwaeleza jambo moja kubwa sana ambalo limetokea siku ya leo hapa shuleni.

    Muda si mrefu, tumepokea taarifa kuwa wanafunzi wawili wa kidato cha nne na wanaosoma katika mchepuo wa sayansi, wamepata msiba na kufiwa na wazazi wao.Kiukweli taarifa hizi sisi kama shule zimetusikitisha sana na ukiangalia wanafunzi hawa wote wapo karibu kufanya mtihani wao wataifa kwa ajili ya kumaliza elimu ya ya Sekondari.Naomba wote tuguswe na jambo hili, kwasababu suala kama hili likilowakuta wenzenu, linaweza kumkuta mtu au mwanafunzi yeyote katika maisha ya hapa duniani.Kama nilivyosema awali, wanafunzi hawa wote hawa waliopatwa na misiba hii wanatoka darasa moja na majina yao ninayo hapa.

    " Mmoja ya mfiwa anaitwa Mark ambaye wengi wenu nadhani mnamfahamu kutokana uwezo wake mkubwa darasani.Na mwingine huyu ni binti ambaye ame....!?", Aliongea mwalimu mkuu, lakini alisita kuendelea kuzungumza baada ya kuwaona baadhi ya wanafunzi wakionekana kufurahia msiba ule uliomkuta Mark.Mwalimu mkuu alichukizwa sana na nidhamu ile mbovu waliyoiyonesha wanafunzi wale, akawaita wale wote walionesha tabia ile mbovu, ili aweze kuwaadhibu mbele ya wanafunzi wengine kwa ajili ya Kukomesha jamno lile na lisije likajirudia tena kwa Wengine.Wakati mwalimu mkuu akitaka kuwaadhibu wanafunzi wale, mara ikasikika sauti na kumsimamisha yeye kutoa adhabu ile.





    "Acha hiyo!?,

    Unataka kupoteza ajira yako!?

    Naongea na wewe mr.Maginja!", Ilikuwa ni sauti ya mmiliki wa shule ya sekondari Dakawa ambaye kwa muda huo naye alikuwa anawasili mahali pale.Mr maginja ambaye ndiye mkuu wa shule akajaribu kumuelezea kilichotokea bosi wake ili apate kumuelewa sababu ya kutaka kuwaadhibu wanafunzi wale lakini bosi alishindwa kuelewa kabisa.

    " Mr.Maginja, ni mara ngapi nimekueleza kuhusu shule yangu, haupaswi kuwapa adhabu wanafunzi wangu pasipo sababu ya msingi kwasababu wazazi wao hawa ndio wanaofanya wewe uwe hapa na upate mshahara wako." Huku akionekana kuwa na ghadhabu kiasi fulani alizungumza mmiliki yule wa shule ya Dakawa.

    "Nisamehe kwa hilo mkuu na pia nakuahidi hili halitajirudia tena." Mr.maginja ilibidi awe mpole tu na kutekeleza yale ayatakayo bosi wake.

    "Kama umenielewa nashukuru, unaweza ukaendelea na matangazo sasa"

    "Asante mkuu.Sasa wanafunzi pamoja na hilo la msiba wa Mark, pia tumepokea taarifa ya msiba wa mwanafunzi mwingine ambaye anaitwa Sala Mathias kutoka kidato cha nne pia.Binti huyu amefiwa na wazazi wake wote wawili ambao vifo vyao vimewakuta mchana wa leo baada ya gari lao kugongana na roli wakiwa matenbezini.Sisi kama shule tutapanga utaratibu kwa ajili ya kuweza kuhudhuria katika misiba hiyo lakini kwasasa naomba wote tukae kimya angalau kwa dakika mbili, ili tuweze kuziombea familia hizi zilizopatwa na maswahibu haya." Huku akionekana kuwa mnyonge sana, Mr.Maginja alizungumza na kuwaeleza wanafunzi wake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Binti Sala alikuwa katika wakati mgumu sana, na ilikuwa vigumu sana kwake kukubaliana na hali ile.Alijitafakari sana na kujiona yupo katika giza nene ambalo haelewi ni wapi ataweza kupata mwanga kwa ajili ya kuweza kumwangaza.Muda wote uso wake ulijawa na huzuni huku akikiona kilio ndio kama kinanda kinachoweza kumtuliza katika huzuni ile.

    "Wewe peke yako Mungu ndie uliyenipa mwangaza katika kila giza nilipitialo.Leo tena mimi mja wako nipo gizani na sielewi wapi nipite, naomba uniletee Mwanga baba nami niweze kutoka katoka giza hii nisiloliweza." Huku akiwa na uchungu sana na macho yake akiwa ameyaelekeza kuangalia katika mbingu, Sala alizungumza maneno haya.



    Vivyo hivyo hali hii iliyokuwepo kwa Sala, pia ilikuwa kwa kijana Mark.Mark aliona dunia yote kama imemuelemea yeye na kuona kila kitu kilikuwa kigumu kwake.Alikumbuka sana upendo mkubwa aliokuwa anauonyesha mama kwake, maneno ya mama ambayo yaliyokuwa yakimtia moyo na kumpa ujasiri wa kupambana na kila changamoto iliyopo mbele yake, yote haya Mark aliona kama yatabaki kuwa ndoto kwake.Hakika Mark aliumia sana na kujiona kama ni mtu aliyepoteza kila kitu katika dunia hii.Mwisho ya yote, Mark aliona ni heri akubaliane na hali ile iliyotokea kwake zaidi alizidi kumuomba Mungu ili ampe nguvu ya kuweza kusimama bila ya uwepo wa mama.

    "Japokuwa kwa sasa hautokuwa nami mama, lakini nakuahidi maneno yako yote uliyonihasa, uliyoniekekeza na kunitia nguvu ya kuweza kupambana na changamoto mbalimbali ninazokutana nazo hapa duniani, nakuahidi mama sitoyayaacha wala kuyasahau na nitayaweka akilini mwangu na kufanya yote yale uliyokuwa unataka mimi kijana wako nifanye.Pumzika kwa amani mama yangu mpendwa." Haya ni baadhi ya maneno ambayo Mark aliendelea kuyazungumza kwa lengo la kujipa matumaini na kujifariji kwa lile lililomkuta.



    Ikiwa ni siku ya pili imewadia, kila kitu kilikuwa kimekaa sawa kwa ajili ya kuwapumzisha wazazi wake, lakini Sala alikuwa akijiuliza maswali mengi sana kichwani mwake hasa zaidi kwanini Mark hakuudhuria kushiriki nae katika msiba ule mzito wa kufiwa na wazazi wake.

    "Kwanini Mark umenifanyia hivi!?,

    Uko wapi urafiki wako mwema uliokuwa unauonyesha kwangu kila siku!?,

    Siamini kabisa kwa jinsi ninavyokufahamu, umebadilika na kuja kuwa mkatili namna hii.Nilikuona mwema sana kwangu lakini kumbe nilikuwa kinyume kabisa na mawazo yangu.Naahidi sitoshorikiana nawe tena Mark na nashukuru sana kwa kukufahamu vizuri mapema." Ni maneno ya Sala ambayo alikuwa akiyaongea moyoni mwake na kumshtumu sana Mark kwa kutoonyesha ushirikiano wake katika tatizo lile lililomkuta.

    Ikiwa ni mida ya mchana, watu wote wakiwa tayari wameshafika katika kanisa la St.Anton kwa ajili ya kufanya misa ya kuweza kuwaaga na kuwasindikiza marehemu wote katika siku hii, Sala pamoja na ndugu zake nao wakawasili kanisani kwa ajili ya kushiriki katika misa ile.Baada ya kuingia kanisani Sala mbele yake akaona majeneza matatu, mawili akawa anayafahamu kuwa ndimo walimolazwa wazazi wake lakini jeneza moja hakuweza kulitambua.Akiwa kanisani huku kilio kikiwa kimemtawala muda wote hasa baada ya kuona majeneza ya wazazi wake, katika kupepesa macho na kuangalia huku na kule pale kanisani, mara macho yake yakakutana na uso wa Mark.Mark alishangaa sana kumuona Sala pale kanisani maana mpaka muda huu Mark, hakuwa na taarifa zozote kama nae Sala amepata msiba.Akili ya haraka Mark ikamtuma kuwa pengine Sala amekuja pale kanisani kwa ajili ya kuhudhuria misa ile ya msiba wa mama yake, moyoni mwake Mark alilifurahia lile.Lakini Mark alishangaa sana baada ya kuona uso wa Sala ukiwa umekunjamana kwa hasira tena akimuangalia yeye kwa macho makali sana.



    Mark akashindwa kuelewa kwanini Sala yupo katika hali ile, zaidi Mark aliona ni vyema atamfuata baadae ili aweze kuzungumza nae.Uchungu mkubwa ulimjaa Sala na kilio kikiwa ndani yake muda wote.Sala akashindwa kabisa kuendelea na Misa ile hasa baada ya kuona jeneza la mama pamoja na baba yake yamelazwa pale mbele, akatolewa nje kwa ajili ya kupumzika.Hali ile aliyokuwa nayo Sala ilimshtua na kumshangaza sana Mark, akajiuliza sana, Mbona Sala yupo katika huzuni kubwa sana, Je huzuni ile ni kuhusu msiba wa mama yake au kuna jambo lingeni lililomsibu.

    Akiwa katika hali hiyo nayo misa ilikuwa tayari inakwenda kuanza na ndipo Mark alipofanikiwa kujua ukweli juu ya matatizo yaliyomsibu Sala.

    "Katika misa hii ya msiba, tunapenda kuwaombea marehemu wote hawa waliotangulia katika ufalme wa Mbinguni.Mungu apate kumrehemu marehemu Angel Peter na marehemu Mathias Leonard pamoja na mkewe ambao nao wametangulia mbele ya haki." Alizungumza padri aliyekuwa anaongoza misa ile ya msiba.Ijapokuwa Mark alikuwa katika msiba mzito wa mama yake, lakini baada kusikia moja ya majina ya marehemu waliotajwa katika misa ile ni watu ambao anawafahamu sana.Yalikuwa ni majina ya wazazi wake na Sala ambayo yalimduwaza na kumshutua sana Mark baada ya kusomwa pale Kanisani.

    Mark alipata mshtuko sana moyoni mwake kutokana na lile, naye akatoka nje ya kanisa kwa ajili ya kwenda kuongea na Sala.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kumuona Mark mbele ya macho yake, Sala aliinuka alipokaa na kwenda kumkumbatia.

    "Mark naomba unisamehe kwasababu sikulitambua hili hapo awali!" Aliongea Sala na Kumueleza Mark baada ya kujua Mark naye alifiwa na mama yake, Sala alilitambua lile kupitia sauti ya padri wakati akiyasoma majina ya marehemu.

    "Naomba utulie Sala, hii ni mitihani ambayo Mungu aliiweka kwa ajili yetu sisi wanadamu, tukimtumainia yeye naamini kila kitu kitakuwa sawa juu yetu." Alizungumza Mark na kuendelea kumtuliza Sala.Baada ya misa kuisha, miili yote ikachukuliwa kwa ajili ya kwenda kuzikwa.



    Baada ya wiki moja kupita, kila kitu kilikuwa kimemalizika na marehemu wote walikuwa tayari wameshapumzishwa katika makao yao ya milele.

    "Mark, ni wiki sasa imepita tangu niwapoteze baba yangu na mama yangu.Katika mkono wangu nahisi nimepoteza kila kitu, naenda kuishi maisha ambayo sikuwa kuishi tangu kuzaliwa kwangu, wewe ni mtu wa pekee Mark ambaye unaweza ukanipa furaha na kunifariji katika mapito yote ninayopitia, naomba uniahidi Mark hutokuja kukaa nami mbali hata baada ya sisi kumaliza shule." Kwa unyenyekevu mkubwa na upole wa hali ya juu, Sala alizungumza na kumueleza Mark.

    "Ondoa hofu juu ya ilo sala, japokuwa kwasasa mama yangu hayupo katika maisha yangu tena, lakini nafarijika sana kwasababu ameniachia hazina kubwa ya kuweza kupambana na changamoto nizipitiazo hapa duniani kupitia maneno yake ya busara na ya kunitia moyo aliyokuwa akinieleza kila siku.Moyoni mwako najua una kidonda kikubwa sana Sala, lakini nakuahidi nitakuwa nawe siku zote na naomba kwasasa tuzidi kuongeza bidii zaidi katika masomo yetu kwasababu naamini elimu ndio kitu pekee ambacho kinaweza kutupa faraja na kutufanya tukawa na maisha bora siku za mbeleni." Alizungumza Mark na kumshika bega Sala kwa lengo la kumfariji na kumtia nguvu kwa yale yote yaliyopita.

    "Nashukuru sana Mark kwa kuendelea kuwa mwema kwangu, baba naye anaendeleaje?" Alishukuru Sala na kumuuliza Mark hali ya baba yake(mzee Peter) ambaye kwa sasa alikuwa amelazwa hospitali kutokana na kuanguka ghafla siku ya msiba wa mkewe.

    "Hali ya baba bado sio nzuri sana Sala na natajia baada ya kuagana na wewe hapa nitaenda hospitali kuchukua majibu maana tayari ameshafanyiwa vipimo vyote hapo jana." Alizungumza Mark.

    "Oooh!, pole sana Mark, naomba tuongozane pamoja kwenda hospitali ili nami nikamuone baba." Alizungumza Sala, na kutoka wote kwa pamoja na kuelekea hospitali.

    Baada ya kufika hospital, Mark pamoja na Sala wakaongoza moja kwa moja kwa dokta ili waende kuchukua majibu kuhusu ugonjwa wa mzee Peter.
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog