Search This Blog

NCHI YA WACHAWI - 2

 





    Simulizi : Nchi Ya Wachawi

    Sehemu Ya Pili (2)





    Siku moja nikiwa dukani, nikagundua kuwa, duka lililopakana na mimi linaingiza wateja wengi kuliko mimi, jambo hilo lilinikasirisha sana. Haraka sana, nilifunga duka nikarudi nyumbani nikipitia kwa mke wangu kumlalamikia.

    Nilimweleza haiwezekani watu wafanye biashara kubwa kupita mimi wakati mimi nina uwezo mkubwa kuliko wao.



    “Sasa utafanyaje baba Masu?” Mke wangu aliniuliza.

    “Najua mimi mama Masu,” nilijigamba huku nikipigapiga mkono kifuani.

    Nilipofika nyumbani, nilifungua kabati langu. Nikisema kabati langu nina maana kwamba, funguo la kabati hili nakaa nazo mimi na mke wangu nilishamwambia kuwa, humo naweka vikorokoro nyangu tu, sitaki tuchanganye.



    Nilitoa kitu fulani mfano wa kitambaa cheusi, nikakishika mkononi, nikafumba mkono kisha nikaondoka kurudi dukani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliiingia dukani, lakini kabla sijafungua, nilikitembeza kile kitambaa mwilini huku nikisema:

    “Mimi ndiye mwenye nguvu kuliko wote hapa, nataka niendelee kuwa na nguvu. Wateja wote walione duka langu kama nyuki wanavyoona maua.”



    Baada ya kusema hayo, niliinua mguu mmoja juu kisha nikaupiga chini puu.

    Nikawa si mimi katika mwili, hapo ina maana sikuwa naonekana kwa macho ya kibinadamu.

    Nilikwenda kusimama nje ya duka la yule jirani yangu, lakini alishtuka na kusema:

    “Ushindwe katika jina…”



    Kabla hajamaliza, nilirudi kwangu, ndani. Nikajibadili kuwa kawaida, lakini sikufungua duka. Nilijiuliza ina maana yule bwana ni mtu wa Mungu au vipi? Na kama ni mtu wa Mungu mimi nimchukulie hatua gani ili nimzidi nguvu:

    “Oke, nimejua la kufanya,” nilijiambia mwenyewe.

    Baada ya hapo nilifungua duka langu na kuendelea kuuza.



    Ukweli ni kwamba, wateja walianza kuja kwangu kwa wingi huku nikifurahia moyoni. Mara, yule jirani yangu ambaye ana madevu mengi na nywele ndefu zinazoonesha hazichanwi kwa ufasaha, alikuja dukani kwangu na kusimama mbele yangu.

    “Kijana, huu ni moto wa gesi, acha kabisa kucheza na mimi.”

    Kisha akaondoka zake kurudi dukani kwake.



    Mbaya zaidi wakati anasema maneno yale, walikuwepo wateja wawili walioingia kila mmoja kivyake.

    “Huyu mzee vipi kwani?” Mteja mmoja aliniuliza.

    “Khaa! Kama kichaa!” Mwingine alisema.

    “Aa! Mwanza hii bwana,” wa tatu alisema huku akitoka nje, pia iliashiria kuwa, alichotaka ndani ya duka langu hakikuwepo.



    “Hata mimi namshangaa,” nilijikaza na kusema.

    “Kwani humfahamu?” Aliniuliza mmoja.

    “Namfahamu, si mwenye duka la pili hapo,” nilisema lakini kwa sauti iliyokuwa ikitoka nje kwa wasiwasi mkubwa.



    Baada ya wateja hao kuondoka, nilisimama mlangoni, nikainua mkono juu kuashiria nasimamisha mara moja ujaji wa wateja ili nishughulikie suala la jirani yangu kwanza.

    Nilirudi ndani na kukaa kwenye kiti nikiwaza, lakini sikufunga duka. Katika maamuzi yangu niliamua kumuumiza yule jirani kwa kumpiga upofu asione tena na hivyo kumfanya amweke mtu mwingine wa kuuza pale dukani ambapo niliamini atakuwa mwepesi ‘kiroho’ kuliko yeye.



    Nilipopata uamuzi huo, nilirudi mlangoni, nikanyoosha tena mkono na kufanya alama ya kuita, yaani nikafungulia wateja waingie.

    Nilitoka nje kidogo, nikasimama kwenye kizingiti cha mlango.

    Nilitoa kichwa kuchungulia nje, nikamwona yule jirani yangu naye amesimama kwenye kizingiti kama mimi, nikarudisha uso nyuma kwa ghafla. Lakini sehemu kubwa ya mwili ilikuwa tayari nje.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kumbe na yeye alifanya kama mimi, alirudisha uso nyuma na sehemu kubwa ya mwili ikabaki mbele, kisha akawa anatoa uso kwa kuibia na mimi vivyo hivyo. Ilifika mahali nikajikuta nacheka.

    “Kumbe mwoga,” nilijisemea moyoni.



    Nilirudi ndani kwani kuna mteja aliingia akitaka katoni ya sabuni ya kufulia. Wakati nampa, aliingia mtoto mmoja akitaka nimuuzie sindano za kushonea ishirini.

    “Unasema?” Nilimuuliza kwa mshtuko. Hata yule mteja pia alishangaa.

    “Wewe, sindano zote hizo za nini?” Mteja alimuuliza.

    “Si za kushonea…”

    Mimi nikasikia sauti ya upole ikiniambia.



    “Shtuka kijana, usikubali kumuuzia.”

    Nilimalizana na yule mteja wa kutaka sabuni, alipoondoka nikamgeukia yule mtoto.

    “Enhe, amekutuma nani?”



    “Ah! Unamtakia nini?” Aliniuliza na yeye.

    Kimyakimya niliinua mguu mmoja juu, nikaupiga chini.

    “Nakuuliza ili nikuuzie, au hutaki tena?”



    Ilifika mahali kile kivuli kikasimama na yule mtoto aliponiona nimekazia macho nje, naye akageuka huku akiniuliza.

    “Unashangaa nini?”

    “Wewe unaona nini?”



    “Sioni kitu,” alinijibu kwa ujasiri japo ni mtoto.

    Kwa kukiangalia kivuli, nilibaini kuwa, licha ya kusimama, huyo mtu mwenye kivuli alikuwa akicheza kwa kunesanesa kulia na kushoto, wakati mwingine akiinua juu mguu mmoja baada ya mwingine.



    Mara alisimama na kuchezacheza kwa kukata kiuno.

    Nilichoamua, nilitoka ili kumshuhudia mtu huyo kwa mwili wake kabisa badala ya kivuli.



    “Naweza kusema ilikuwa kitu cha ajabu sana kwa macho yangu kwani badala ya kumwona mtu kama nilivyoona kivuli chake, sikuona kitu chochote kila na badala yake yule jirani yangu alikuwa amesimama nje ya duka lake.



    Niligeuza kurudi ndani, lakini ajabu nyingine yule mtoto sikumwona, nikamsaka ndani kote hakuwepo. Nilistaajabu sana.

    Ili kuweka mambo sawa, niliamua kujiweka sawasawa na mimi. Nikasimama katikati ya duka, nikatumbua macho pima, nayo yakatoka mbele sana kiasi cha nusu futi, nikayashika polepole kisha nikayarudisha ndani, nikanyanyua mkono kama askari anayepiga saluti.



    Pale pale nikawa si mimi tena, nilipata nguvu ya ajabu ya uchawi, nikatoka nje, nikatembea hadi nje ya duka la yule mtu, nikasimama kumwangalia kwa kumtumbulia macho tena. Nikayatoa mbele umbali wa futi moja nzima huku nikiyashikilia.



    Safari hii yeye hakuwa na ubavu wowote wa kuniona wala kutambua kuwa, kuna mchawi amesimama mbele yake. Nilipeleka mguu mmoja wa kushoto mbele, kisha nikapeleka wa kulia na kuingia ndani.

    Hapa nataka kusema kitu, mara zote mchawi anapotaka kutembea huanza na mguu wa kushoto ilimradi kwenda kinyume na utaratibu mwingine uliozoeleweka na pia kutimiza amri za Mkuu wa Wachawi Duniani ambaye ni Shetani Mkuu, Lusifa.



    Hata wewe binadamu wa kawaida, unapotaka kutembea ukaanza na mguu wa kushoto hukawii kujikwaa, hata ukifuatilia kuanzia sasa, wengi wanaojikwaa walipoanza kutembea walianza na mguu huo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Basi, niliingia ndani ya lile duka, nikapita nyuma yake na kusimama sambamba na bidhaa zake. Yeye akiwa hajui lolote, akatoka na kusimama mlangoni akikata shingo kulia kuangalia kwangu bila kujua kuwa, nilikuwa ndani ya duka lake.

    Nilichofanya sasa, nilichukua bidhaa moja moja na kunipitisha kwenye makalio yangu mfano wa kutawaza.



    Hapa pia naomba niweke wazi jambo moja, mara zote ukiona mtu anamiliki duka, lakini wateja hawatokei, au wateja wanatokea wanaulizia bidhaa, wanaomba kuziona kwa kuzishika tu kisha wanarudisha tambua kuwa, bidhaa hizo zimetawaziwa na mchawi. Kwa hiyo kila mnunuzi anaiona bidhaa hiyo kama kinyesi tu.



    Basi, nilifanya hivyo kwa muda mrefu, miongoni mwa bidhaa nilizozitawazia ni pamoja na maboksi ya biskuti, dawa za meno, vocha za simu nakadhalika.

    Kuna wakati baadhi ya wateja walikuja pale na kumuuliza:

    “Huyu bwana yuko wapi?”



    “Sijui,” alijibu yule mwenye duka jirani yangu wakati mimi naendelea kutawazia bidhaa zake.

    Nilipojiridhisha, nilitoka kwa mwendo ule ule wa kutupa hatua ndefu mbele. Wakati wote huo macho yangu yalikuwa mbele kama nilivyokwisha yatoa.



    Nilipofika dukani kwangu, nilijirejesha kama kawaida na kuendelea kuuza huku wateja wengi wakiwa wanakuja na kununua huku wakimkwepa mwenzangu.



    Baada ya miezi tisa tu, duka la jirani yangu likafungwa kwani bidhaa nyingi zilipoteza sifa ya kuuzwa (expire) na kuzitupa. Nilisikia baadaye kwamba, aliamua kwenda kufanya biashara ya samaki Ukerewe.

    ***

    Baada ya mwaka mmoja kupita, kwa kutumia uchawi wangu niliweza hata kuua watu mbalimbali, wakiwemo ndugu zangu ili biashara zangu zikuwe na pia nilikuwa nakutana na wachawi wenzangu kwa ajili ya kufanya maangamizi katika jamii.



    Siku moja, usiku wa saa saba, nikiwa nimelala na mke wangu kitandani, nilisikia mlio wa ndege, nikashtuka na kukaa kitandani. Mara ule mlio ukasikika chumbani, lakini hakuonekana ndege.

    Nilipeleka mkono kwa mke wangu ili nimwamshe, lakini kabla sijamgusa, nikajikuta mkono umenata.

    “Usithubutu kufanya hivyo,” ilisema sauti bila kutokea kokote.



    Niliacha kushangaa kwani nilijua nini kinaendelea sasa.

    “Kuanzia leo, utakuwa Kiongozi Mkuu wa Wachawi Kitaifa. Majukumu yako utaambiwa utakapokuwa umelala,” sauti ile ilisema, ikakatika kisha mlio wa ndege ukasikika na kupotea.



    Nilirudia kulala, nikiwa usingizini nikaota ndoto. Nilikuwa kwenye chumba kikubwa mfano wa shule, lakini sikuwa peke yangu. Mwalimu aliyesimama mbele yetu alikuwa yule dada Sekretari wa kule dunia nyingine tulipokwenda. Alikuwa akisema:

    “…pia kila mmoja ambaye ni kiongozi kwenye nchi yake atakuwa akihakikisha hakosi kwenye semina za kimataifa, kuhudhuria mikutano ya kuangamiza afya na mafunzo ya kuhujumu ndoa zilizoshibana.



    “Kila mwakilishi atapewa barua ya mwaliko kupitia njia yoyote ile, lakini muhimu kuhudhuria ili kuifanya nchi yako kuwa mbele kimaendeleo katika sekta hii ya uchawi.



    “Mikutano mikubwa ya kanda itakuwa ikifanyika katika nchi husika, kwa kanda na mabara ya ulimwengu na nchi itakayokuwa mwenyeji itawajibika katika kubeba mzigo wa maandalizi kwa maradhi, chakula na usafiri kwa wajumbe watakaohudhuria.”



    Barua kubwa ilidondoka chini katikati ya wachawi wote, mmoja akataka kuishika, nikamkataza asifanye hivyo. Niliifuata mimi na kuiokota huku nikisema maneno ambayo, kama barua ile ingekuwa na madhara nisingedhurika.



    Nilipoiweka mikononi niliifungua na kukutana na maneno yaliyoandikwa kwa biki nyekundu yakisomeka hivi:

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa Mkuu wa wachawi upande wa taifa kuu, unatakiwa kuhudhuria mkutano maalum wa dharura utakaofanyika nchini Indonesia Juni 5. Maandalizi yote kule tayari.



    Lengo la mkutano huo wa dharura ni kupanga mkakati wa kupandikiza roho ya chuki kati ya viongozi na wananchi ili kuweza kuleta machafuko zaidi duniani kote. Kufika kwako ni muhimu kuliko kutokufika.”



    “Kusema ule ukweli nilishtuka sana japo nilijua ni barua iliyonilenga mimi moja kwa moja kwa sababu nilishataarifiwa mapema.”



    Lakini wakati nikifikiria mambo yatakavyokuwa, mara nikasikia sauti ikisema:

    “Usafiri wako utakuwa unauamrisha, utataja nchi unayokwenda na mkutano unaohudhuria, utafikishwa hapo. Kwa sasa funga mkutano wako hapo waache wanakundi wakalale.”



    Nilitii, niliwaambia wenzangu wakalale, lakini nikiwa nimemwachia madaraka mzee mmoja ambaye kabla ya kutawanyika alisimama mbele yangu nikamwapisha.

    Nikiwa nyumbani usiku huo, nikawaza jinsi ya kuondoka kwani Juni 5 ilikuwa usiku huo huo kuelekea Juni 6 ya mwaka huo.



    Kama kawaida, nilitoka kitandani ikiwa ni dakika ishirini tu baada ya kurudi. Nikatumia mbinu ile ile ya kulaza kinu kitandani ili mke wangu anaposhtuka ajue nipo. Lakini hata hivyo, yeye nilimfanyia mazingaombwe ya kumlaza kwa muda mrefu.



    Nilisimama katikati ya chumba, nikafunga miguu kama askari wa usalama wa raia.

    Nikafumba macho nikisema:

    “Hii ni safari ya kwenda Indonesia kwenye mkutano wa dharura wa kimataifa wa wachawi, nataka nifike huko.”



    Kufumba na kufumbua nilijikuta nipo nyuma ya nyumba, nikashangaa.

    “Ina maana mpaka leo hujui kuwa, ungo ndiyo ‘elopleni’ (ndege) yako?” Niliulizwa swali hilo na sauti ya mtu nisiyemwona. Nikakumbuka ungo nilishautumia mara moja, hata na usukani wake upo na pia tanki la mafuta lipo tena niliyaacha ya kutosha tu.



    Nilisimama wima, nikanyoosha mkono wa kulia mbele na kufumbua kiganja. Niliita ungo, ukaja mkononi, nikauweka chini. Nikaita usukani ambao ni shanga za kike zinazovaliwa kiunoni.



    Naomba hapa kabla sijaendelea niweke wazi kitu kimoja. Shanga au wengi siku hizi huita chachandu, ni kitu kikubwa sana ambacho wengi hawakifahamu.

    Kumekuwa na tabia ya wanawake kuvaa chachandu kwa idadi yoyote bila kujua ni hatari au ni salama.



    Wachawi wanavyojua, asili ya wanawake kuvaa chachandu ilikuwa kuwakinga na utasa au wale ambao tayari ni tasa kuwatibu, sasa ilitegemea idadi ya shanga.



    Ilikuwa ukimwona mwanamke amevaa chachandu tatu, ina maanisha anakinga kupata utasa, akivaa hadi tisa jua anatibu utasa.



    Siku hizi wanawake wanavaa kwa sababu ni mtindo bila kujua zina madhara na wengi wamejikuta wakijifunga na uzazi kwa sababu wanavaa idadi kubwa ya shanga kama mtindo. Sasa badala ya kutibu wanajikuta wanajiharibu kwa sababu hawahitaji tiba.



    Na shangaa ilivyo, haivaliwi kwa pacha hata siku moja. Yaani, mbili, nne, sita, nane, kumi, hapana! Shanga huvaliwa moja, tatu, tano, saba, tisa, kumi na moja na kuendelea hivyo.

    Basi, naomba niendelee. Chachandu nazo zilikuja, kikaja kibuyu cheusi ambacho ni kwa ajili ya mafuta sasa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilipojiamini kuwa, kila kitu tayari kwa safari, nilipanda ndani ya ungo, nikajivua ubinadamu na kukanyaga kile kibuyu kisha nikazishika shanga na kuanza kupaa kwa kasi ya ajabu.

    Anga usiku ule lilikuwa la ajabu sana. Kwani uzito haukuwa wa kawaida, kila baada ya dakika moja, ungo wangu ulitetemeka kuashiria kuwa, nilikuwa napita sehemu mbaya.



    Ninaposema sehemu mbaya kwa wachawi ni pale ambapo chini kuna majumba makubwa ya kuabudia au kuna mkusanyiko wa watu wanaosali au kumwomba Mungu, hasa wale wenye kujifanya wanakemea mapepo wachafu, ogopa sana wale.



    Kuna eneo niliona ungo unalemewa kiasi cha kutaka kupinduka, lakini unga unga mweupe niliojipaka kabla sijaanza safari uliokoa ajali kama nne.



    Sikumbuki ni dakika ngapi nilichukua angani, lakini mara nikaona natua kwenye uwanja mkubwa ajabu. Nyungo nyingi zilikuwa pembeni mwa uwanja huo wenye mwanga wa taa lakini hakuna taa iliyokuwa inaonekana kwa macho.



    Nilipotua chini tu, mtu mmoja alisimama mbele yangu na kupunga mkono wa kulia juu kama vile wanavyofanya askari wa Usalama Barabarani. Nikawa namfuata polepole mpaka pembeni ya barabara, akanionesha sehemu ya kuegesha ungo wangu.



    Niliuweka pale na kushuka ambapo nilipokelewa na watu wawili lakini waupe, waliovaa kama mimi, yaani nguo nyeusi (kaniki) ya kukata lubega nao walikuwa wamejichafua mwili mzima kwa masinzi. Chini walikuwa pekupeku.



    “Kutoka?” Mmoja wao akiwa ameshika ‘vikadi’ vingi vilivyoandikwa mambo mbalimbali ambayo haikuwa rahisi kusoma kwa hatua za mbali ingizingatiwa kwamba, ilikuwa usiku.

    “Tanzania,” nilijibu nikiwaangalia kwa umakini wa hali ya juu.



    “Ooo, Taifa Kuu TZN,” alisema yule mwenye vikadi huku akinipa kikadi chenye kamba na kuniambia nivae shingoni na ile sehemu yenye maandishi iwe mbele wazi, nikafanya hivyo.

    Nilichukuliwa hadi nje ya uwanja ambako kulikuwa na giza nene na la ajabu.



    “Tembea kuelekea mbele hatua kumi na tano utakutana na ukumbi wa mikutano,” aliniambia yule mtu.

    Nilitii agizo lile kwa kutembea huku nikihesabu hatua moja baada ya nyingine, moja baada ya nyingine mpaka nilipofika hatua kumi na nne, ikiwa imebaki moja, ghafla nilijikuta nimetokea kwenye eneo lenye taa nyingi na majumba mbalimbali. Ni mji kabisa, kwani watu mbalimbali ambao hawafanani sana na binadamu walikuwa wakipitapita kila mmoja na hamsini zake.



    Nilipokanyaga hatua ya kumi na tano, nikajikuta nimezungukwa na watu wengi wenye kufanana na wale walionipokea na wale waliokuwa wakiendelea na hamsini zao.

    Basi, walinichangamkia sana huku wakiniuliza habari za nitokako.



    Niliwajibu ni nzuri sana, mmoja wao akanishika mkono wa kushoto huku akiniambia nakaribishwa kuingia kwenye jumba la mikutano la nchi ya Mpingaji huku akisema sijachelewa sana kwani nusu ya wajumbe kutoka pande zote za dunia wameshafika, nusu bado.



    “Lakini ratiba ya mkutano inasema wakishafika robo tatu ya wajumbe wote, kikao kinafunguliwa,” aliniambia yule mtu, au naweza kusema kiumbe kwani ni kama mtu lakini si kwa kufanana na sisi binadamu.



    Nje ya jumba la mikutano kulikuwa na watu wa ‘sampuli’ ile ile wakipiga ngoma na wengine kucheza kwa furaha.

    Nje ya jumba, mlangoni kwa juu palikuwa na tambara kubwa jeusi, maandishi meupe yanayosomeka; Mkutano Mkuu wa Dunia wa Kujadili Mambo Mbalimbali. Karibuni nchi ya Mpingaji.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pembeni ya tambala na maandishi kulikuwa na picha ya kichwa cha mtu, alionekana hadi usawa wa shingo tu. Masikio marefu mfano hakuna, naweza kusema yalipita kichwa kama ya Sungura. Macho ya pembe tatu, makubwa na mbaya au cha kutisha zaidi alikuwa na pembe moja kwenye paji la uso, midomo mirefu kama mdomo wa kibuyu. Tafsiri ya haraka ungeweza kusema ni mnyama na si binadamu.



    Nilikazia macho zaidi chini ya ile picha kwani kulikuwa na maandishi. Nikasoma yakiwa yameandikwa; Mkuu wa Nchi ya Wachawi.



    “Mheshimiwa karibu sana, tuingie ndani,” mtu mmoja miongoni mwa watu wale wa ajabu aliniambia akinielekeza kwa mkono mlango mkuu.



    Niliingia ndani ya ukumbi ambapo nyuma ya mlango tu nilikutana na watu watano walionipokea na kunisindikiza sehemu ya kukaa.



    Macho yangu yalistaajabu sana kuona ukumbi umepambwa kama inavyokuwa kwa kumbi za ninazozifahamu mimi. Kifupi ulipambwa kama kumbi za sherehe mbalimbali, ikiwemo harusi.



    Ndaki ya ukumbi kulikuwa na meza kubwa moja na pana na kuna watu mchanganyiko walikaa kasoro viti vitatu vya katikati.



    Ninaposema watu mchanganyiko walikaa maana yangu ni kuwa, kulikuwa na binadamu wa kawaida kama mimi. Pia kulikuwa na watu wa kule ambao kama nilivyosema, hawakuwa wamefanana na binadamu sisi.



    Wale walionipokea walinielekeza hadi kwenye kiti kimoja kule mbele, lakini si kati ya vile viti vitatu vya katikati. Nilikaa kwenye kiti ambacho mbele yake kulikuwa na kibao kilichoandikwa; MWAKILISHI TAIFA LA TZ.



    Nilipokaa tu, nikapewa maelekezo ya kutumia waya nyembamba ‘headphone’ kwenye masikio endapo nitataka, lakini naweza nisitumie pia.



    Mimi nilisema situmii, kwani sikupewa ufafanuzi zaidi wa madhara ya kutumia au faida zake.

    Wageni waliendelea kuingia, wakati fulani waliingia kwa mpigo kama saba, wakapewa viti vya kukaa.



    Lakini ikumbukwe pia kulikuwa na viti vilivyopangwa mbele ya meza kuu. Watu wengine walikuwa wanakwenda kukaa huko, wengine wakiwa na kamera, wengine na mabegi tu wengine mafaili na kalamu.

    Nusu saa baadaye ukumbi wote ulikuwa umejaa, sauti ikasikika ikisema:



    “Sasa tunaomba utulivu kwani wakati wowote Mkuu atatokea ili kuanza kikao chetu.”

    Hii ilikuwa sauti isiyotoka kokote, yaani ilisikika tu, lakini msemaji hakuonekana licha ya kwamba alikuwa mwanamke kulingana na sauti.



    Ukimya ulitawala, kilichokuwa kikisikika ni watu kukohoa au makaratasi kukaa vizuri, pengine na watu waliokuwa wakidondosha vitu mbalimbali.

    Mara, mlango mmoja kulia kwa meza niliyokaa ulifunguliwa.



    Ghafla ulitangulia mwanga mkali, halafu mlio wa viatu vya ngozi vilivyoashiria kuwa, visigino vyake vilikuwa, ama vya chuma au vya kitu kigumu sana kwani mlio ulisikika kwa sauti na pia kwa wingi kuonesha kuwa, hakuwa na mtu mmoja.

    Mara, watu watatu walitokea, wawili wakiwa pembeni kwa yule mmoja ambaye ni wazi alikuwa ndiye Mkuu wa nchi ile ya Wachawi.



    Mkono mmoja alishika kitu kama chupa au labda almasi kwani ilikuwa ikiwaka sana, mkono mwingine wa kushoto alishika chupa kubwa mfano wa zile za pombe kali kama za whisky.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila walipopita, mwanga ulitawala kuwazunguka mpaka wanafika kwenye viti vyao kukaa. Yule Mkuu alikaa kiti cha katikati kati ya vile vitatu, wale aliofuatana nao walikaa pembeni yake kulia na kushoto.

    Nilijiuliza maswali mengi sana kwamba, ni kwanini Mkutano ule upo kama wa kimataifa wa duniani. Pia nilijiuliza kule ni wapi.



    “Mkuu wa nchi ndiyo ameingia, nashukuru wageni wote, naomba tukae.” Ile sauti iliyotuambia tutulie ilisema kwani wakati Mkuu anaingia tulisimama wote.



    Tukasikia mlio wa viatu ukitembea kutokea kusikojulikana kuelekea katikati ya ukumbi ambapo kulikuwa na mimbari ya kuhutubia.



    Habari zenu mabibi na mabwana, leo tunafanya Mkutano wetu mkuu wa kimataifa hapa. Karibuni sana wageni waalikwa na wageni wa heshima,” ilianza kusema ile sauti.



    Pale pale nilibaini mambo mawili makubwa muhimu. Kwanza nilibaini kuwa, aliyekuwa akiongea ingawa hakuonekana sauti yake ilionesha ndiye alikuwa MC wa Mkutano ule. Pia nilibaini kwamba, kila mtu mle ndani alikuwa akimsikia MC kwa lugha yake mwenyewe. Yaani mimi nilimsikia kwa Kiswahili, Mwingereza naye alimsikia kwa Kiingereza, vivyo hivyo kwa Mfaransa, Mhindi na kadhalika.



    Hapa pia nataka kusema kuwa, nilibaini utaratibu wa kidunia wa wajumbe wa mikutano kutumbukiza viwaya sikioni ili kuweza kusikia kinachoongelewa kilitokana na mfumo wa nchi hiyo.



    Pia naomba niseme na nieleweke kuwa, ukumbi tuliokuwemo kulikuwa na watu wa rangi mbalimbali. Katika maisha yangu mpaka wakati huo nilikuwa sijawahi kumwona binadamu ana rangi ya njano, lakini siku hiyo niliwaona, tena wafupi sana. Baadaye niliambiwa kuwa, watu hao walitoka katika nchi iliyopo Kaskazini mwa dunia, inaitwa Visiwa vya Barafu (Iceland) mji wao mkuu unaitwa Reykjavik.



    Nasema hivi kwa sababu kila mtu alipokaa, kulikuwa na kibao cha jina la nchi yake na mji mkuu, sasa sijui kama ilikuwa lazima iwe mji mkuu hata kama mjumbe alitokea mji mdogo. Mfano, mzee mmoja kama Mhindi, alikaa kwenye kibao kilichoandikwa Ulan Bator halafu mbele kukaandikwa jina la nchi, Mongolia. Mwingine kibao kiliandikwa Bangkok halafu jina la nchi Thailand.



    Mimi mwenyewe jirani yangu alikaa mtu mweupe, yaani mzungu na kibao chake kiliandikwa Brussels mbele kukaandikwa Belgium (Ubelgiji).

    Basi, mara ile sauti ikasema:



    “Naamini waalikwa wote mmekaa kila mmoja katika sehemu yake na kupata huduma zote, namwita kwenu msaidizi Mkuu wa nchi hii aongee na nyinyi kabla na yeye hajamkaribisha Kiongozi Mkuu wa Nchi ya Wachawi.



    Lakini kitu cha kushtua kilijitokeza kwamba, wakati ile sauti inaendelea kuongea kutokea pale kwenye mimbari, ulianza kuonekana uso wake, baadaye shingo, yakafuata mabega na kumalizikia na tumbo huku sehemu za chini nazo zikianza kujitokeza.



    Tukio hilo lilitufanya baadhi ya watu kumtumbulia macho mpaka alipomalizika kuonekana mwili mzima na kusimama kwa miguu miwili.



    Alitembea taratibu akiacha kifaa cha kuongelea juu ya mimbari lakini wakati huo huo mtu mmoja kati ya wale waliokuwa na Mkuu wa Nchi alionekana kusimama na kuelekea mbele alikotoka yule MC.

    Kwa sauti, MC ungeweza kusema ni msichana mrembo, mwenye sura ya mvuto na umbile la kumfanya atazamwe, lakini sivyo.



    Alikuwa mzee wa kama miaka 75, ngozi ya uso wake imejikunja-jikunja, mbele alionekana ana meno mawili tu, masikio kama wenzake, marefu yaliyopita kichwa halafu alikuwa mweusi kama mkaa ambao haujaingia jikoni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yule mtu alipofika mbele aliweka sawa vipaza sauti na kuweka kando kinasa sauti kile cha kuongelea alichokuwa akitumia yule MC. Alisimama na kuangalia kulia kwake, kushoto, akageuka kuangalia nyuma walikokuwa wamekaa Mkuu na watu wengine.



    Alianza kwa kusalimia wote huku akipunga mikono hewani na tukio hilo liliambatana na hali ya umeme kama wa radi kuwaka kwenye mikono yake.



    Akaanza kwa kusema kuwa, hayupo tayari kupoteza muda kwa vile tulikuwa pale kwa ajili ya kuelimishana, kupeana uwezo na kutahadharishana.



    Akasema: “Kwa nyinyi mliopata nafasi ya kuwakilisha nchi zenu, tunapenda kuwahakikishia kwamba, kwanza mtabadilika, kutoka kwenye uwezo wa kuwa mchawi hadi kuwa pepo wachafu.”

    Kusita kwake kuongea kunaonekana kulitokana na ukweli kwamba, kila mtu alionekana kushtuka, akaendelea:



    “Ninaposema kuwa pepo wachafu nina maana kwamba, mtakuwa juu zaidi kupita wachawi. Nyinyi mtaweza kubadilika kutoka maumbile hayo na kuwa kitu chochote, upepo, moto, ndege, kisiwa, bahari, ziwa, yaani kitu chochote kile.”



    Akaendelea: “Kuna mikakati mingi na mikubwa sana kuhusu nyinyi, kifupi mnatakiwa kuwa na uwezo wa kuwa kama majini sasa ambayo nguvu za uchawi haziwezi kushinda na wao ndiyo wanaosimamia kazi za majini.”



    Alipomaliza kusema, akamkaribisha Mkuu wa Nchi ambapo sote tuliokuwemo mle ndani tulitakiwa kusimama wakati kiongozi huyo akienda mbele na yule aliyekuwa mbele akirudi nyuma.



    Tulisimama, akaenda mbele akitembea kama mtumishi wa Mungu anayekwenda kutoa Neno la Bwana kwa kondoo wake. Alipofika, alisimama wima na kwa heshima zote.



    dhamira ya kiroho haipo tena kila mmoja anataka kufaidika na ubinafsi, wenyewe mashahidi, uongo?” “Karibu kila mtu kwenye ule ukumbi alisema:

    “Ni kweli kabisaaa,” kisha yakapigwa makofi mfululizo na kumfanya yule Mkuu kutulia kwa muda akisubiria ukimya. Baada ya ukimya akaendelea:



    “Kwa hiyo, mikakati ya sasa inatakiwa kuwa mikubwa sana na ndiyo maana tumetaka nyinyi muwe na uwezo wa kuwa viumbe wa moto.

    Mtakuwa na uwezo wa kuwaingia watu katika nafsi zao na kubadili mawazo yao ili kuweka ya kwenu na kuwafanya watende dhambi mbalimbali.



    Nasema hivi kwa sababu mikakati ya aliyeumba nchi ni kuhakikisha anavuna kwa wingi watu wake, na sisi lazima tufanye mipango ya kuwatumbukiza watu wengi kwenye kutenda maovu ili tuvune wengi.

    Miongoni mwa mikakati hii ni ule wa simu za mkononi.



    Tumeamua tutoe elimu ya uundwaji wa simu hizi kwa wingi na za kisasa zaidi ili watu wengi wavutiwe kuzimiliki. Watu wengi wakimiliki ni rahisi sana kumwasi aliyeumba nchi, kwani wezi, wasengenyaji, wazinzi na wengi wengine watatumia njia hii.



    Nataka nitoe mfano, mwanamke akiwa ndani ya daladala akakutana na mwanaume, wote wakawa hawana simu uwezekano wa kukutana baadaye wakafanya uzinzi mdogo, mkubwa?

    Wote tukajibu:

    “Mdogoo.”



    Mkuu akaendelea:

    Mnaona sasa, lakini je, hamwoni kwamba simu ndiyo zinawasukuma wengi kufanya uzinzi maana mtu akishapewa simu mawasiliano yanaanza palepale mpaka zinaa, na baada ya zinaa wanaachana, mtu anatafuta mwingine, uongo kweli?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kweliii.”

    Mkuu akaendelea:

    Mnaona, halafu mkakati wetu mwingine ni ule wa kusisitiza ile roho ya uzinzi kuwatoka watu mara baada ya tendo la zinaa kufanyika, haitakiwi hii roho iendelee kuwakaa wazinzi.”



    Aliposema hivyo nikakumbuka kitu, na hapa nataka kuwaambia hivi, binadamu hugandwa au huandamwa na roho ya uzinzi kwa muda ule wa kutaka kufanya dhambi hii na mara baada ya kufanya zinaa roho hii humtoka na kubaki na dhamira ya Mungu tu ndiyo maana watu wengi wanapozini baada ya kumaliza hutokewa na hali ya majuto.



    Hapa nataka kutoa mfano mmoja nao ni huu, utakuta mwanaume na mwanamke wanaingia gesti kwa kuongozana, hata kama ni mchana kweupe, hapo ni kwa sababu ya ile roho ya uzinzi, lakini baada ya kufanya tendo, watu hawa wanasikia aibu kutoka wakiwa wameongozana pamoja, ni kwa sababu tu ile roho ya zinaa imewatoka.



    Basi, yule Mkuu wa Nchi ya Wachawi akaendelea kutuambia:

    Pia, kuna roho hii ya usawa katika jamii, siku hizi inasisitizwa wanawake wawe sawa na wanaume, inabidi sisi tuisimamie hadi ipoteze maana au kusudio.



    Tuhakikishe wanawake wanadai haki zao kwa nguvu, hasa wale walio kwenye ndoa. Hii itasaidia ndoa nyingi kuvunjika kwa sababu hakuna mwanamke atakayekubali kutawaliwa na mumewe kipindi hiki cha usawa na hakuna mwanaume atakayekubali kuachia utawala nusu kwa nusu.



    Nyinyi kama roho mtakuwa mkiingia kwenye nafsi za viongozi wanaohusika na kushawishi mawazo yao kufanya semina, makongamano, warsha na mikutano mbalimbali ambayo itazungumzia jinsi ya kumkomboa mwanamke.



    Tutalazimisha wanaume waitwe waoneaji, wakandamizaji na wanaendesha maisha katika mfumo wa kibabe, kwa hiyo wanawake wanajitenga na ukweli wa hakai sawa, nao watakuwa kitu kimoja, wakitaka kumiliki mali zao wenyewe, utajiri wao wenyewe, kazi kubwa, viwanda hata majukwaa ya dini, mwisho wa siku mpaka makanisani kutahubiriwa usawa na wanawake watapigana vita ya kujikomboa kwa hiyo hawatawaheshimu tena waume zao na ndoa nyingi zitavunjika.



    Ndoa hizi zikishavunjika kwa wingi zitaifanya dunia isiwe tena na mfumo wa mke na mume kuishi hadi kifo kiwatenganishe kwani wengi watatenganishwa na talaka, hapo yule aliyeumba nchi atakasirika.



    Tukikazia hapo, hasa kwenye ndoa mpaka zikafa nyingi, ndipo tutakapoweza kupata watoto wengi wa mitaani kwani baada ya wanandoa kuachana, wataoa au kuolewa tena na watoto wao watazagaa, na kule watakakokwenda hawatakuwa wakijua historia za wenza wao kwa hiyo magonjwa kama Ukimwi yatawaingia wengi na hivyo kupatikana kwa kundi lingine la watoto yatima.



    Mkakati mwingine ambao huu licha ya kuwa mkubwa pia ni mgumu kwani sasa tunapambana moja kwa moja na roho wa aliyeumba nchi. Lakini mkakati wetu sisi ni wa kuhakikisha wachungaji, hasa wa makanisa ya kilokole wenyewe wanajiita ya kiroho, wanatumia muda mwingi kuvuta waumini kwa Mikate na si kwa kutengeneza Roho zao za baadaye.



    Kwa hiyo, mkiwa katika mwili wa kiroho mtakuwa mnawaingia wachungaji, hasa wale ambao hawajasimama sawasawa katika neno na kuwafanya watangaze habari za mikate na si usafi wa roho.

    Kuhusu hili mpaka sasa tumefanikiwa sana kwani hii roho inafanya kazi vizuri. Ndiyo maana siku hizi utakuta Mchungaji anasimama madhabahuni na kusema:



    “Ukiwa unataka kazi, kufika Chuo Kikuu, unataka kumiliki gari zuri kama mimi, nyumba ya kisasa, au pengine huzai, njoo kwa Yesu. Mwangalieni Sarah, mke wa Abrahamu alipata mtoto katika umri wa miaka 80. je, kama Sarah alizaa na umri huo wewe mwenye miaka 28 unahangaika nini?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kauli hizi ni za kupandisha imani tu lakini hakuna yenye kumwandaa mtu kiroho akawa wa Mungu kwa ajili ya maisha ya mbinguni baadaye. Na leo hii akitokea Mchungaji akahubiri acheni dhambi mwende peponi, utakuta kanisa lake halijai, maana sisi tumewafanya watu watafute ufalme wa Duniani na si wa Mbinguni.



    Ndiyo maana siku hizi muumini anasimama mbele ya kanisa kushuhudia jinsi alivyopata gari la kisasa, alivyokubaliwa kupata mkopo wa mamilioni ya pesa peke yake wakati walikuwa waombaji hamsini, anaamini ni muujiza wa aliyeumba nchi wakati yeye mwenyewe haenendi katika roho, msengenyaji, mzinzi, mnafiki, hana heshima, hawajui kama ni sisi ndiyo tunaowatendea miujiza ile!



    Kwa tathimini ya hivi karibuni kabla ya kikao hiki, tumefanikiwa kwa sehemu kubwa kuyafanya makanisa yote ya kilokole kuwa kama yale mengine tu, kwani ndani ya makanisa haya siku hizi watu wote wapo, wapo wazinzi, wapo walevi, wapo wasengenyaji, wapo wezi. Kifupi si makanisa ya kiroho tena, ila tumewaziba akili wasijue wameshika kisichoshikika.”



    “Lakini pia mnatakiwa kujua kuwa, mkiwa wenye uwezo wa kuwa pepo wachafu mtahakikisha mnabadili ratiba za vipindi vya Televisheni, Redio na Makala za kwenye magazeti, nyingi wapewe nafasi wanawake kujieleza, kuwe na vipindi vya wanawake kujikomboa, wanawake wawe wanamtaka wazi kuwa, ni wakati wa usawa.



    Hii hali itadakiwa na wakuu wengine, sasa shughuli za kikazi, nyingi zinafanywa na wanawake, hata kama watakuwa hawawezi, lakini tutafanya mazingira ya kufumba macho na akili za watu ionekane kuna kuweza.



    Hilo jingine, lakini kuna hili la kuhakikisha uchumi wa dunia unashikwa na wanawake, hili lazima lipigiwe vita kwa nguvu zote, lengo letu ni kupingana na utabiri wa vitabu vya aliyeumba nchi, yeye alisema siku za mwisho wanawake wengi watakuwa wakiishi na mwanaume mmoja na kujitegemea kwa kila kitu, lakini sisi tuhakikishe siku hizi za mwisho, mwanamke mmoja ndiyo aishi na wanaume wengi.



    Kuhusu vifo, tunatakiwa kuelewa kwamba, kipindi hiki ndicho kwetu tunatakiwa kuvuna kwa wingi zaidi roho za watu, hivyo hakuna namna zaidi ya kuhakikisha watu wanaangamia kwa kila njia, kila namna.



    Mtakuwa mkipita kwenye kingo za mito, bahari na maziwa na kuzifungua ili nchi ikumbwe na mafuriko, mtakuwa mkipaa angani na kuangusha ndege zenye abiria wengi, mtakuwa mkisababisha matetemeko makubwa sehemu na sehemu ili kuyasawazisha maghorofa yawe kama nyumba za kawaida na hivyo kuleta madhara.



    Lakini kingine nilipitiwa kuwaambia, ndoa nyingi duniani zinalindwa na watoto. Huu ni utafiti tulioufanya kwa kutuma roho zetu mpaka kwenye jamii, kila kona na kila pande za nchi.



    Katika kila ndoa kumi za halali zilizovunjika, ndoa tano zilichangiwa na kukosekana kwa watoto, ndugu wengi walichukua madaraka kwa kumshinikiza mwanaume amwache mke na kuoa mwingine.”

    Yule Mkuu wa nchi alipofika hapo, kuna mjumbe alinyoosha mkono. Huyu hakuwa na kibao kilichoonesha alitoka nchi gani.



    Mkuu: Enhe, wewe, una swali?

    Mjumbe: Ndiyo Mkuu.

    Mkuu: Uliza utajibiwa.

    Mjumbe: Sasa, ndoa kuvunjika, kutukuwepo watoto na mume kuoa mke mwingine, sisi tunapata faida gani?



    Mkuu: Sawa, lengo letu ni kuvuruga utaratibu wa aliyeumba nchi na kuondoa amani duniani, watu wengi watakuwa hawaendi na maagizo ya aliyeumba nchi, hivyo tutafanikiwa kuwapotosha wengi na watakwenda motoni na sisi.



    “Pia, mume akimwacha mkewe na kuoa mwingine si atakuwa anavunja ile amri yao na mnajua aliyeumba nchi hakuna kitu kinamkera kama kuachana.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yule mjumbe alikaa, Mkuu akaangalia pande zote ili kuona kama kuna mtu mwingine ana swali.

    Ilionekana hakuna mwenye swali, wote tulibaki kimya na ndiyo Mkuu aliendelea:



    “Hakuna kati yenu ambaye atadhurika, kwani uwezo tunaowapa sisi ni mkubwa sana. Si wa kichawi ila ni wa kiroho, mtakuwa mnaweza kuingia sehemu yoyote ikiwa ni pamoja na kwenye mwili wa binadamu na kukaa moyoni mwake na kumgeuza mawazo, kutoka yale ya kumpendeza aliyeumba nchi na kumfanya awaze mabaya tu muda wote.



    Kuhusu wanawake kutokuzaa, nyinyi mtakuwa mkiingia kukaa kwenye matumbo ya uzazi ya wanawake na kuharibu mfumo wa uwezo wa kupata ujauzito.”



    Alipomaliza kusema, alitoka kwenye mimbari na kuelekea walikotokea, wale aliokuja nao wakamfuata kwa nyuma na kupotea moja kwa moja.

    Mara, akatokea yule mwanamke mwenye sauti nzuri lakini sura ya kutisha.



    “Hatujafikia mwisho wa Mkutano wetu, sasa anakuja kiongozi mwingine ambaye anawafundisha jinsi ya kupata uwezo wa kuwa roho wanaoweza kuingia ndani ya mwili au mishipa ya fahamu ya binadamu na kuharibu uwezo wake na kufanyia kazi matakwa yenu.



    Alipita mbele haraka mzee mmoja aliyekuwa amevaa suti ya kitambaa cha kaniki. Hii suti ilikuwa haina kola ya shingoni na alionekana amechoka kwa kufanya kazi kwa bidii au nzito.

    Akasimama, akatuangalia kisha akapiga makofi mara tatu alipomaliza akaanza kwa kusema:



    “Sina salamu ya mazoea, ingekuwa mlikotoka (duniani) ningewasalimia kwa kila mtu na jinsi anavyojua yeye.



    Lakini nataka kuwaambia kuwa, ni wakati wa mavuno huu na si wa kuchezacheza. Nyinyi mlioamua kuwa kwetu na iwe hivyo, mpaka mmekuja huku naamini mmepitia mengi makubwa na mmeshinda, hakuna aliyekuja kwa upendeleo kwa sababu huku hakuna upendeleo wala rushwa, huku kila mtu anakuja kwa jinsi alivyokwishakataliwa na yule aliyeumba nchi.”



    Hapo nilishtuka sana, nikanyoosha kidole haraka.

    Kiongozi: Una swali?

    Mimi: Ndiyo.

    Kiongozi: Uliza, utajibiwa.



    Mimi: Umesema tuliokuja huku ni wale waliokwishakataliwa?

    Kiongozi: Ndiyo. Swali lako liko wapi sasa?

    Mimi: Ina maana sisi tulishakataliwa na Mungu?

    Kiongozi: We! Acha.



    Baadhi ya wajumbe: Wee, kelele ala!

    Mara yule mwanamke ambaye yupo kama MC alisimama mbele, yule kiongozi akaondoka zake akitembea kama anachechemea.

    Yule mwanamke alionekana kukasirika sana, aliniangalia kwa kunitumbulia macho na kushindwa kuongea.



    Karibu kila aliyekuwemo ndani ya ukumbi aliniangalia mimi, lakini wapo walioonekana kuniangalia kwa macho ya kutojua kitu, wengine walionekana kujua.

    Kusema ule ukweli mimi mwenyewe sikujua kwanini palitokea hali ile. Sikujua nini nilikikosea mpaka kuonekana wengine wakinishutumu wengine wakiniangalia kwa macho makali.

    Kingine kilichonishangaza sana ni kitendo cha yule kiongozi kuondoka akitembea kwa mwendo wa kuchechemea.



    Yule mwanamke akaniamuru nisimame, nikatii kisha akaniuliza kama nilipokuwa napita niliingizwa kwenye chumba cha sharti kuu, nikajibu sikumbuki.

    Akaitwa mtu aliyenileta mpaka nje ya ukumbi huo, alipofika aliulizwa hivi:

    “Huyu Mwakilishi kutoka nchi ya Tz ulimleta wewe?”

    “Ndiyo.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ulimpeleka chumba cha sharti?”

    “Hapana, nilisahau.”

    Ghafla Mkuu kabisa wa Nchi ile alitokea akiwa anatembea kwa kasi mpaka pale mbele na yule mwanamke akampisha kwenye eneo la kuzungumzia.



    “Ni kwanini hukumpeleka kwenye chumba cha sharti wakati unajua kile ndiyo chumba muhimu sana kuliko vyote humu ndani, unataka tupate madhara siyo?”

    Yule mtu alitulia tu kwa muda huku akiwa ameinamisha kichwa.



    “”Nisamehe Mkuu,” hatimaye alisema akiwa bado ameinama, alikuwa haangalii popote pale.

    “Sasa mchukue mpeleke, kisha mrudishe hapa haraka sana, kosa ni lako na utaadhibiwa wewe kwa sheria za Nchi hii,” alisema Mkuu huku akiwa amemkazia macho.



    Yule mtu, au tuseme yule kiumbe aliniangalia mimi kwa macho ya kunitaka kumfuata.

    Njiani nilijiuliza maswali mengi sana, ni sharti gani hilo ambalo haikuwezekana mimi kuambiwa mle mle ukumbini mpaka nifike kwenye chumba hicho?

    Alitembea mimi nikimfuata kwa nyuma mpaka akasimama mbele ya jengo moja la wastani, kwa nje lilionekana kama ofisi nzuri na ya kisasa.



    Na mimi nikasimama nyuma yake, akafungua mlango na kuniambia:

    “Ingia humu ndani, utakutana na tangazo kubwa jeupe ukutani, ukishalisoma hutakiwi kutoka na kuuliza swali jingine kwa sababu maelekezo yake yako humo kwenye tangazo mwanzo hadi mwisho.”

    Nilikubali kwa kutingisha kichwa. Akaendelea:



    “Ufanye haraka kwa sababu kule hawawezi kuendelea na kikao mpaka wewe urudi.”

    Pia nilikubali kwa kutingisha kichwa huku nikiingia lakini nikiwa gizani na kitu ambacho nitakikuta huko ndani.



    Baada ya kuingia, nilikutana na mlango mwingine tena, huu ni wa kioo, kioo cha kujiangalia lakini nikiwa nashangaa shangaa, ghafla mlango huo ulifunguka wenyewe na kunipa nafasi ya mimi kupita.



    Nikaingia na kutokea kwenye chumba cha wastani, ukutani kulikuwa na tangazo lenye maandishi makubwa yanayosomeka hivi:

    “UKIWA KWENYE NCHI YA WACHAWI EPUKA KUTAJA NENO MUNGU, UNAWEZA KUUAWA USIRUDI ULIKOTOKA. KUANZIA SASA FUNGA KINYWA CHAKO KUHUSU JINA HILI.”



    Nilijikuta nikiguna bila kutarajia, kila kitu kwenye mwili wangu kililegea, mara nikasika mlio wa kengere kisha kwenye lile tangazo kukawaka taa nyekundu, lakini ilikuwa ikimulika kama ‘indiketa’ ya gari.



    Nilitoka mbio, nikamkuta yule mtu ananisubiri akiwa anaonekana kukasirika sana. Aliponiona tu aligeuza na kuanza kuondoka. Ina maana aliamini kuwa, kwa kitendo cha yeye kugeuka mimi nitajua natakiwa kumfuata nyuma kurudi kule ukumbini.



    Basi, tulikwenda kwa mtindo ule ule, lakini njiani alianza kulia jambo ambalo lilinishangaza sana mimi.

    “Unalia nini sasa?”

    Nimekwisha,” alinijibu.

    “Umekwisha! Umekwishaje?”



    “Unadhani ni adhabu gani nitapewa?”

    “Sijui, kwani ni adhabu gani?”

    “Kifo tu, ndiyo adhabu kubwa ya huku!”

    Nilishtuka sana, nikamuuliza:

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wewe umejuaje?”

    Akanigeukia na kusema:

    “Ndiyo adhabu kubwa ya huku.”

    “Kwanini kusiwe na adhabu nyingine?”

    “Hakuna, kama ipi?”



    “Kupigwa viboko, kunyimwa chakula.”

    “Viboko hatuumii, chakula huwa hatuli, hata ukinipiga na panga hapo huwezi kunikata mimi.”

    Kusema ule ukweli nilishangaa sana, lakini bado nikawa na dukuduku, kama alivyokuwa anaongea ni kweli, sasa wataamuaje?

    “Sasa kama ni hivyo utauawa vipi?” Nilimuuliza.



    “Nawekewa mkono kichwani kisha nasemewa maneno fulani.”

    Mpaka hapo tukawa tumefika kwenye geti la kuingilia ndani ya jengo la mkutano.

    Nje, tulikutana na kiumbe kimoja kina sura mbaya sijapata kuona hata kwenye michoro ya hadithi za kutisha.



    Alikuwa na sikio moja tu, upande wa kushoto, jicho moja katikati ya paji la uso likiwa limevimba kama linataka kutoka, mdomo mrefu lakini upo upande kidogo na kidevu kilichopindia kulia.

    Wakati najiandaa kumwangalia miguuni, alimshika yule mtu niliyeongozana naye mimi na kuondoka naye.



    Niliogopa sana, lakini wakati niko kwenye mshangao, nilishikwa bega la kushoto na mtu au kiumbe kisichoonekana:

    “Ingia ndani ya mkutano unasubiriwa wewe tu,” sauti nene lakini isiyo na utulivu iliniambia.



    Haraka sana nikazama ndani na kukutana na macho ya wote waliokuwemo ukumbini wakinikodolea mimi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog