Search This Blog

NCHI YA WACHAWI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS





    *********************************************************************************



    COMPLETE - IMEKAMILIKA YOTE



    Simulizi : Nchi Ya Wachawi

    Sehemu Ya Kwanza (1)







    “Kwa jina naitwa Israeli, lakini si yule mtoa roho za watu, hili ni jina ambalo linapatikana katika utaratibu wa maisha ya kila siku duniani.



    Nimezaliwa mwaka 1950, (kwa sasa 2010 ana miaka 60) wilayani Misungwi, mkoani Mwanza, ni mtoto wa kwanza katika familia yenye kujiweza kidogo kimaisha, ikiwa na watoto tisa, wote wanaume. Wazazi wangu (sasa marehemu) walikuwa wacha Mungu sana.



    Kama kweli kuna uhai baada ya kifo na wakayajua mambo yangu ya duniani, naamini nimewaumiza sana wazazi wangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa sasa naishi Mbagala, jijini Dar es Salaam na familia yangu yenye mke na watoto saba, wote wa kike. Mke wangu pia kwao ni mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto tisa, wote wanawake.



    Nimelazimika kusimulia mkasa huu wa kichawi baada ya watu wengi kusimulia mikasa yao wakidai waliwahi kuwa wachawi wakaacha kwa sababu mbalimbali ambazo wengine huzisema, wengine hufanya siri kubwa.

    Naweza kusema kwamba, karibu wote waliokuwa wakisimulia maisha yao ya kichawi na mikasa yake, hakuna hata mmoja aliyewahi kufikia hata robo ya maisha ya kichawi ya kwangu.



    Mimi niliishi maisha hayo kwa miaka kumi, na nilifika ‘levo’ ya mbali, mfano kuwa Mkuu wa Kikundi na kusafiri sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya mikutano mikubwa ya kimataifa ya wachawi na niliporudi, nilikuwa nakutana na wachawi wakubwa wa hapa nyumbani Tanzania na kuwapa maagizo ya utendaji katika makundi yao sehemu mbalimbali za nchi.



    Katika kipindi chote cha kuwa mchawi nilibaini mambo makubwa mawili, kwamba, maisha ya wachawi katika ulimwengu wao hayana tofauti yoyote na maisha ya watu wasio wachawi katika ulimwengu huu wa macho ya kawaida.



    Maandiko yanaposema kuwa, Mungu aliumba vitu vinavyoonekana na visivyoonekana ni kweli kabisa. Wachawi wanaamini kwamba, vitu visivyoonekana pia vilikuwa na siku sita katika uumbaji wa Mungu, siku ya saba akapumzika. Na hiyo ndiyo sera ya mchawi mara tu baada ya kujiunga katika kazi hiyo inayolaaniwa na wengi ulimwenguni kote.



    Kabla sijaenda mbele zaidi nataka kusema kuwa, kama kuna shughuli mbalimbali za binadamu zinazoonekana kwa macho ya kawaida duniani, pia kuna shughuli kama hizo hizo zisizoonekana kwa macho ya kawaida, lakini zinashirikisha wachawi na mambo yao.




     Wachawi wana kila kitu, wana mikutano ya nchi, mikutano ya kimataifa, ya kanda ya mabara na pia wana mabenki, japokuwa kwa macho tunazungumzia mabenki ya pesa, wao wana mabenki ya damu, nyama na dawa za kienyeji.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huwa wanakopeshana, wanalipana na wapo wasiotaka kulipa ambapo huchukuliwa adhabu mbalimbali kulingana na makosa. Zipo nchi ambazo wachawi wake wanafukuzwa katika uanachama, zipo zinazoingizwa, wapo wakuu wa wachawi wa nchi wanaopinduliwa wengine hata kuuawa na pia kunakuwa na uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano kuchagua viongozi wa kichawi wa nchi husika ambapo wapiga kura huandikisha majina yao na kuwa na vitambulisho vya kupigia kura.



    Pia kuna bendara ya umoja wa wachawi barani Afrika, Ulaya na duniani kote. Aidha, kila nchi ina bendera yake inayoonesha utambulisho wa kitaifa. Mfano, bendera ya kichawi ya Tanzania ni rangi nyekundu, nyeusi na kahawia, katikati ina picha ya mnyama Twiga.

    Nchi ya Nigeria, bendera yake ya kichawi ina rangi nyekundu bila mchanganyiko, katikati ina picha ya mkono mweusi umeshika kibuyu chenye shanga.



    Kuna wachawi wanaofanya biashara za kimataifa, mfano kutoa dawa za kienyeji Tanzania kupeleka India kwa njia za kichawi na kule mchawi anaweza kununua ngozi za wanyama akaja kuuza Tanzania, Kenya au Uganda kwa wachawi wengine ambao hawana mitaji mikubwa.



    Ilikuwa mwaka 1980 nikiwa na umri wa miaka thelathini tu, ndipo niliposhawishiwa na mzee mmoja, sasa marehemu kujiunga na wachawi. Huyu mzee namtaja kwa jina moja la Madume, tulikutana kwenye shughuli ya uvuvi samaki ziwani Victoria, alitokea kunipenda sana kutokana na tabia yangu njema na kuwa kama kijana wake.

    Usiku mmoja nikiwa nimelala alinijia katika ndoto, lakini baadaye niligundua ilikuwa ’laivu’.



    “Kijana wangu Israeli, unaoenekana unaweza kukifanya kile ambacho mimi ninacho, nitafurahi sana kama utakipenda ili nikupe,” aliniambia kwa sauti ya utu uzima.

    “Kwa wewe baba nitapenda, na ikibidi naomba unipe sasa,” nilimjibu.



    Mzee Madume akanishika mkono na kunivuta, nikasimama. Tulisimama sanjari, akanisogezea uso wake kwenye uso wangu, kwa hiyo pua yake ikagusa pua yangu, midomo yake ikawa kwenye midomo yangu, paji lake la uso halikadhalika, kuna wakati alitembeza uso wake mpaka kidevu chake kikagusana na changu.



    Kufumba na kufumbua, tukawa kwenye nyumba ya udongo, dhaifu kwa kila hali, katika chumba ambacho koroboi ndiyo ilikuwa ikitoa mwanga hafifu uliofanya tuonane kwa tabu. Tulikuwa watatu, mimi, mzee Madume na mtu tuliyemkuta ndani ya chumba kile.



    “Kaa chini kijana wangu,” mzee Madume aliniambia kwa sauti ileile niliyoizoea.

    Nilikaa chini kwenye ngozi nyeusi, kila nilipokuwa nikimkamata sura yule mtu tuliyemkuta mle ndani, kibatari kilipoteza nuru na kumfanya aonekane kwa tabu kidogo, hivyo kuna wakati nililazimika kufumbua macho mpaka mwisho ili nipate nafasi ya kuona sawasawa.

    “Fumba macho,” mzee Madume aliniambia, lakini si kwa amri.



    Nilifumba macho na kusubiri tamko jingine kutoka kwa mzee huyo au yule mwenyeji wetu. Nilihisi hali ya kama maji yakinigusa mwilini, kuanzia shingoni kuteremka na uti wa mgongo hadi kiunoni. Yalikuwa ya baridi mfano wake hakuna, nikasema siiiii.



    “Sii nini kijana wangu? Wewe sasa ni mtu kama mimi, utaishi kama mimi na wala hakuna binadamu yeyote atakayekuweza,” mzee Madume aliniambia lakini tukiwa palepale kwenye kitanda alichonikuta.



    “Ha!” Nilisema na kushtuka.




     “Ha nini kijana wangu?”

    “Si tulikuwa kwenye..!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwenye nini kijana wangu? Nimekukuta hapa na hata sasa tuko hapahapa,” alisema, lakini safari hii akiachia tabasamu pana kidogo tofauti na mara zote, nikajua ananitania tu, lakini ukweli tulikwenda mahali.

    “Nahisi kama naota, kwanza umeingiaje humu ndani kwangu?” Nilimuuliza.



    “Aa, hata wewe utaweza kijana wangu, ndiyo maana nimekwambia wewe sasa ni mtu kama mimi, utaishi kama mimi na wala hakuna binadamu yeyote atakayekuweza.”



    Nilitaka kumwambia kitu, lakini sikumwona mle ndani, nikashtuka zaidi na kujikuta nimekaa kitadani. Sasa jasho jembamba lilinichuruzika mwilini, hofu ilinipanda, niliamini niliingiliwa na kiumbe wa ajabu aliyejifanya binadamu ninayemfahamu. Niliangalia huku na kule lakini sikuona mtu.



    Nilitoka nje, nikasimama kwa muda mlangoni kuangaza kama ningeona kiumbe cha ajabu, pengine kama mtu, lakini mwenyewe akiwa na mguu mmoja, mkono mmoja, jicho moja na kalio moja, lakini hakukuwa na dalili yoyote. Hivyo nilirudi ndani nikifunga mlango kwa uhakika na kujiami, moyoni nikisema: “Simfungulii mtu yeyote akitaka kuingia.”



    ***

    Nilishtuka asubuhi ya saa kumi na mbili, nikatoka kitandani haraka sana, nilikwenda nje nikiwa na shuka tu. Nilipofika niliangaza huku na kule, nikaona mambo ni shwari, nikarudi ndani.



    Nilijiandaa kwa ajili ya kwenda ziwani ambapo nilipofika mtu wa kwanza kukutana naye ni mzee Madume ambaye alinilaki kwa furaha sana huku akinisifu kwa kuwahi kuliko siku nyingine.



    “Kijana wangu, umewahi, hongera sana. Good.”

    Nilimkubalia huku nikiuonesha uso wangu kuwa, hauna amani kama siku zote. Naamini hata yeye alinijua kwani alionekana kusinyaisha sura yake.



    Kikubwa ambacho alinishangaza ni kitendo cha kunisifia kuwahi wakati ilikuwa kawaida yangu. Labda mimi ndiyo ningeshangaa kwa yeye kuwahi kwani haikuwa kawaida yake, mara nyingi alikuwa akifika jua liko juu.

    Basi, nilibadili nguo, kwa kuvua nilizokwenda nazo na kuvaa za kazi, yeye alikuwa ameshabadili za kwake. Wakati navua nguo ili nivae, alinisogelea na kunishika begani na kuniambia:



    “Uko tayari ufanye majaabu kwa kazi hii ye leo?”

    Nilisitisha nilichokuwa nakifanya na kumkazia macho ya mshangao:

    “Wewe nijibu kwanza, unashangaa nini? Wewe kijana wangu bwana.”



    Nilimkubalia kwa kutingisha kichwa kisha nikatulia kumsikiliza alitaka kuniambia nini. Wakati huo huo akili ikanikumbusha lile tukio la usiku na mzee huyo huyo, nikataka kumuuliza, lakini nikasema moyoni, si ndoto tu.

    “Kabla hatujaanza shughuli nenda kasimame pale,” aliniambia akionesha kidole kwenye mashua moja chakavu saana.

    Nilikuwa nimemaliza kuvua na kuvaa nguo nyingine, nikaenda mpaka pale aliponielekeza palikuwa na umbali wa kama hatua kumi za miguu ya mtu mzima.



    Wakati nakwenda niligeuka kumwangalia nikiamini kuwa na yeye anakuja nyuma yangu, lakini kumbe ilikuwa ni mimi tu ndiyo nikasimame pale.



    Baada ya kusimama niligeuka kumwangalia, yeye naye akawa anageuka huku na kule kuangalia wenzetu wengine kama wanakuja, kasha akaniambia:

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa kijana wangu, mimi nakuja huko huku kama nakimbia kidogo, na wewe fanya hivyo hivyo, njoo kama unakimbia, tukikutana tunagonganisha vifua vyetu, halafu utaona matokeo yake tukiingia ziwani.”

    Nilimkubalia kwa kutingisha kichwa, akaanza kuja huku kama anakimbia, na mimi nilianza kufanya kama yeye, tulikutana katikati ya umbali, tukagongeshana vifua tii.



    “Rudi kinyumenyume hadi pale pale kisha tunaanza upya, mara tu ndiyo kipimo chake,” alisema akiwa anarudi bila kuangalia nyuma.



    Wakati tunakimbia kwa mara ya tatu, kabla hatujakutana, wavuvi wawili walitokea na kutushangaa.

    “Ha! Nyiye, huo ni uchawi au mazoezi?” Mmoja alisema, mwenzake akasisitiza kuwa, ni uchawi na kuanza kulalamika kuwa, kumbe ndiyo maana amekuwa akifanya vibaya kazini kumbe kuna watu wanaroga.



    Alisema maneno machafu sana licha ya yule mzee kumwomba samahani tena akimwomba asije kusema kwa wavuvi wengine wa eneo letu, lakini yule mzee hakutaka kuelewa, aliendelea kutoa maneno ya kejeli na shutuma.

    Nilimwona Mzee Madume ameanza kukasirika huku akiinama na kuchota mchanga mwingi kwenye kiganja cha mkono wa kushoto, akakifumba na mchanga wake kisha akaumwaga pale pale alipouchota.



    Sijui nini kilitokea, lakini ghafla wale watu, wote wawili walikimbilia majini na kujirusha huko kimyakimya.

    Licha ya kuingia wenyewe, walijitahidi kupiga mbizi ili wasinywe maji, lakini wapi! Wakazama na kutoonekana tena juu.



    Niliogopa sana, nilimwogopa sana mzee Madume na kitendo kile. Ilibaki kidogo na mimi nianze kutimua mbio kurudi kwangu. Wakati huo, mke wangu na watoto wawili walikuwa kijijini kwa wazazi wangu kutokana na ugumu wa maisha niliokuwa nao kwa wakati huo.



    “Kijana wangu usikimbie, mimi si mbaya kwako, ila hawa walitaka kutuhadhiri, we unadhani ingekuwaje leo baada ya wavuvi wengine kufika na kuambiwa?” Aliniambia mzee Madume akiwa amenitumbulia macho.






    “Hapana, wewe si mwema kwangu,” nilimwambia.

    “Simama kijana wangu.”

    “Sisimami mzee.”



    “Hapana, nakutakia mema tu.”

    “Mema si hayo mzee wangu.”

    “Ungesimama basi ili unisikie kwa umakini.”



    “Sina haja kwani nimeona kwa macho.”

    “Hujaona kijana, simama uone sasa.”

    Niliendelea kukimbia hadi kwenye kibanda kimoja jirani kabisa na akina mama wanauza chakula, nikasimama pale.



    Kwa hali yangu ilivyokuwa, wale akina mama waliniuliza nini kilinipata.

    “Hakuna kitu.”

    “Hakuna kitu wakati unaonekana haupo sawa?”



    “Nipo sawa mama zangu.”

    “Unafukuzwa na nani?”

    “Hata, nakimbia mwenyewe tu.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilipoangalia kwa mbali upande niliotokea, nilimwona yule mzee akija mbio.

    Kwa vile nilikuwa na watu wengine sikuona sababu ya kukimbia, nilisubiri afike ili nimsikie, lakini pia sikuwaambia wale watu habari za yule mzee.



    Mwanamke mmoja alipomwona yule mzee anakuja huku anakimbia, aligeuka kuniangalia na mimi.

    “Mpo pamoja na huyu mzee?”Aliniuliza.



    Nilifikiria kwa muda cha kujibu, lakini likaja lenyewe.

    “Hapana, simjui.”

    “Mbona anatokea ulikotokea wewe?”

    “Kwani haitakiwi?”



    Yule mama akabaki kimya kwa jibu langu hilo. Lakini aliendelea kuwa matumatu kwa kuangalia kwa yule mzee na kwangu.

    Inaonekana alikuwa akisoma mambo fulani usoni kwangu, kwani kuna wakati alianza kutabasamu.



    Yule mzee alipofika, akanishika mkono.

    “Jamani namchukua kijana wangu,” alisema.

    “Sawa, lakini mwenyewe mbona alikataa hamjuani?” Yule mama alihoji akipakulia chakula wateja wake.

    “Aa, unajua tena, ujana unamsumbua,” alisema yule mzee.



    “Ujana au kuna tatizo?” Yule mama akauliza tena. Alionekana yeye aliguswa sana na mazingira yale kuliko mtu mwingine pale.

    “Ujana tu.”

    “Sawa, lakini iwe amani siyo kesho na keshokutwa tunasikia mengine.”



    “Wala hakuna hatari,” alimalizia kusema yule mzee.

    Sijui kwanini kwani nilikubali kirahisi kukokotwa na yule mzee wakati si kawaida. Niliamini ana mambo yake ya kumfanya mtu alegee kiakili.



    Tulirudi mpaka kwenye kile kibanda, akaniambia nikae chini kwani hata yeye alitakiwa kukaa.

    Nilikaa nikimtazama kwa macho ya woga sana.



    “Niambie sasa,” nilisema.

    “Kijana, kazi tunayofanya kubwa sana na ya hatari, hivi unajua kama ziwani kuna vitu vingi sana? Kuna viumbe, samaki, maji na vingine vingi vinavyoonekana na visivyoonekana, unajua hilo?”

    “Najua.”



    “Enhee! Kama unajua hilo jua na hili. Ili tufanikiwe tunahitaji kufanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuisikiliza mizimu, hivi huoni mi mwenzenu ninavyoendelea kila kukicha?”

    Ki ukweli katika wavuvi wote, yule mzee ndiye aliyekuwa amepiga hatua sana kuliko wengine, kwa hiyo kwa kauli yake hiyo na mimi nilijikuta nikihamasika kutaka kuwa kama yeye.



    “Kwa hiyo mzee wangu tufanyaje?”

    “Hilo neno. Sasa nataka wewe uwe kama mimi, unakubali?” Alisema akiniangalia kwa macho ya kujiamini.

    “Niko tayari.”



    Mzee Madume alicheka sana, akataka hata kuanguka chini kiasi kwamba, niliamini alikuwa anatania kumbe, hakuna lolote.

    “Kwanini unacheka sana?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo nacheka kijana wangu, unajua wengi nimetaka kuwaingiza huku wamekataa, mpaka leo wanasumbuka na maisha.”

    “Kwa hiyo mimi sitasumbuka nikiingia huko uliko wewe mzee?”

    “Wala, ni raha tupu!”



    “Niko tayari mzee wangu, tunafanyaje kwani?”

    “Hakuna cha kufanya, hebu twende mara moja,” alisema akinyoosha miguu pale alipokaa.

    Nilibaki nimetumbulia macho nisijue la kufanya.



    “Na wewe nyoosha kama mimi,” alisema mzee Madume akiniangalia huku akicheka.

    Nikanyoosha miguu, mara tukafutika pale, kwangu nilihisi kizunguzungu mpaka tulipojikuta tupo sehemu ya wazi. Kuna mwanga lakini hakuna jua, kuna majani ya kijani kwa wingi huku miti ikiwa sehemu kwa sehemu.

    “Hapa tumefika,” alisema yule mzee.



    “Kwa hiyo kuna sehemu tunakwenda?”

    “Hapana, tumefika.”

    “Ni wapi?” Nilimuuliza.

    “We unahisi wapi?”



    Niliangalia kulia, kushoto, juu na chini.

    “Moshi?”

    “Hapana.”

    “Iringa.”



    “Hapana.”

    “Basi, Dar es Salaam.”

    “Umekosea.”



    “Sasa wapi?”

    “Hapa ni chini ya maji ziwa Victoria, kwa hiyo tumetoka juu tumekuja chini.”

    Nilishtuka sana.




    “Kwa hiyo kinachotakiwa hapa kijana wangu ni kuhakikisha kila kitu kinakubalika, usije ukapinga kitu cha huku, kinaweza kukuingiza matatizoni,” mzee Madume aliniambia kwa sauti ya kunibembeleza sana kama vile alijua tabia yangu.

    Kusema ukweli, karibu wavuvi wote walijua mimi ni mbishi na nisiyependa kushindwa na jambo lolote lile.

    “Sawa, sawa,” nilimjibu nikitikisa kichwa juu na chini.



    Tukiwa bado tunashangaa wote, mara sauti kwa nyuma ilisikika.

    “Mnataka kumwona nani?”

    “Mkuu,” alisema mzee Madume.

    “Nifuateni,” ilisema ile sauti ikiashiria kuondoka.



    Mzee Madume alinishika mkono na kunivuta huku akiniambia.

    “Twende inakosema hii sauti.”

    Nilitii, tuliifuata ile sauti kwa mtindo wa kuisikiliza.

    “Hivi mzee, huku wewe ni mara yako ya kwanza kuja?” Nilimuuliza mzee Madume.

    “Hapana, mara nyingi.”



    “Sasa watu wa huku hawaonekani kwanini?”

    Kabla mzee Madume hajajibu, ile sauti ilimuwahi.

    “Huku hakuna maswali, unataka kuona, unataka kumwona nani kwani?”

    Nilibaki kimya, tukiendelea na safari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ghafla, baada ya umbali wa kama mita mia moja, nikaona jumba kubwa, jeupe mbele yetu, weupe wake ni kama bati linalopigwa na jua.

    Nilipeleka mkono usoni ili kukinga ule mwanga kwani ulikuwa unanichoma sana usoni na kushindwa kuona sawasawa mbele licha ya kwamba, nilikuwa nimeshikwa mkono na yule mzee.

    “Karibuni,” ile sauti ilisema mbele yetu.



    Kwa jinsi ya uzoefu wangu, ile sauti ilikuwa ikitafsrika kuwa, ni ya mwanamke mtu mzima, mnene sana, halafu mfupi sana, na tena alikuwa amefanya kazi ya kukaribisha wageni siku ile kwa muda mrefu kwa hiyo amechoka sana.

    Wakati anasema karibuni sana, tulikuwa kwenye geti kubwa la chuma, jeusi na nondo ndefu sana. Kwa nje sikupata picha ya haraka kwamba, ndani kulikuwa na kitu gani.



    Mlango ulianza kufunguka wenyewe na kuacha nafasi ya kutazamika kwa ndani.

    Kulikuwa na nyumba kubwa sana ya ghorofa moja, nayo nyeupe ikiwa na madirisha ya vioo vizuri vyenye mapambo ya kuvutia, milango mbalimbali ya mti wa mninga.

    “Sasa mnakaribishwa rasmi,” ile sauti ilisema huku ghafla akionekana ni kiumbe kinachofanana na binadamu kwa asilimia sabini na tano.



    Kwa maana gani? Kichwa kama cha binadamu, macho, masikio, pua, lakini tofauti yeye, kwenye paji la uso alikuwa na pembe kama la ng’ombe, fupi nene.

    Halafu miguu yake, yaani makanyagio, yeye alikuwa na kwato za ng’ombe badala ya miguu hii ya kibinadamu.

    Alivaa nguo kama binadamu, alikuwa mwanamke kweli, kama nilivyohisi, mnene, mfupi, tena mweusi tii. Alivaa gauni lililofika chini kidogo ya magoti, ndiyo maana niliweza kuona miguu kirahisi.



    Sikujua haraka ni kwanini kote, tangu kutupokea hadi kufika pale alikuwa amejificha na kuachia sauti tu.

    “Sawa, tunashukuru sana kwa msaada wako, sisi tunaendelea,” alisema mzee Madume akimpa mkono yule mwanamke.

    Mimi naye nilinyoosha mkono wangu ili kumpa, lakini wake akaurudisha nyuma kwa haraka kama mtu asiyependa kupeana mkono na wakati huo huo, mzee Madume naye aliubetua mkono wangu kama vile nilikuwa nafanya kosa kubwa sana kumpa yule kiumbe mkono.

    “Huruhusiwi kwa sasa,” alisema mzee Madume huku akihema kwa nguvu kama vile alikuwa ameokoa kitu cha hatari sana kwangu.

    “Sawa, sawa,” nilisema kwa aibu.



    Yule kiumbe alianza kuondoka, akienda getini, mara alipovuka geti akapotea.

    Mzee Madume alinishika mkono na kunivuta hadi kwenye mlango mmoja wa kioo ambao kwa juu uliandikwa MAPOKEZI VI lakini maandishi yake yaligueka miguu juu, kichwa chini. Ili usome kirahisi, ilikuwa lazima uwe kama unainamisha kichwa huku ukiyaangalia, naamini unapata picha.



    Ilikuwa ni ofisi kubwa sana, yenye viti vingi vya sofa, vikiwa vimezunguka meza moja kubwa sana, ambayo ilikuwa na msichana aliyeonekana ndiye mwenyeji au kwa duniani ningesema ndiye Sekretari wa eneo lile.

    Ukubwa wa eneo lile unalingana kabisa na ukubwa wa uwanja, yaani ukubwa wa mle ndani Mapokezi.

    Huyu msichana naye alikuwa binadamu kwa asilimia zilezile kwani hata yeye alikuwa kama yule mwanamke, pengine tofauti kubwa ilikuwa kwenye umri tu na mavazi.



    Yeye alivaa sketi ya kimini, miguu, yaani makanyagio ni kwato za ng’ombe, juu alivaa kikoti kinachofanana na sketi, au niseme alivaa suti.

    Kukosa kuwa na pembe ya katikati ya paji la uso na weusi tii, angekuwa msichana mzuri mfano hakuna. Alipotabasamu, meno tu ndiyo yalionekana, kwani yalikuwa meupe sana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mzee wangu, sidhani kama nitaweza kuvumilia kuwepo eneo hili ambalo linatisha,” nilimwambia mzee Madume.

    “Hapana, hatua uliyofikia ni nzuri sana kijana wangu, kuwa mvumilivu tu,” alisema yule mzee.

    Mle ndani, mlikuwa na watu wengi sana wakionekana kama sisi, nao walikuwa na shida kama sisi.

    Ghafla, yule msichana alisimama na kusema:




    “Karibuni sana ndugu, jamaa na marafiki zetu. Kwa wale wageni kabisa, sasa mko katika taifa linalojitegemea kwa kila kitu, nina maana kwa raia wake, utawala wake na hata sayari yake. Wote mliofika humu, hakuna uhusiano wowote kati ya duniani na huku, hivyo kama una wasiwasi jisikie una amani na uko huru.”



    Alipomaliza kusema hivyo, alitoka kwenye lile eneo lake akiwa ameshika kitu kama faili, akatembea kwa kuliza mlio kama wa viatu ambapo baadaye nikaja gundua kuwa, naye alikuwa na kwato kama za ng’ombe badala ya miguu ya binadamu.

    “Ko ko ko ko!” Ndivyo mlio wake ulivyosikika, akazama sehemu. Pale kwenye meza yake pakabaki tupu.



    Ukimya uliotawala baada ya yule msichana kuondoka hakuna mfano wake. Ilikuwa kama tumemwagiwa maji ya baridi kwenye msimu wa baridi.

    Nilimsogelea yule mwenyeji wangu, mzee Madume na kumuuliza:

    “Sasa huku mwanga unatoka wapi, maana hakuna jua.”



    “Tusikilizane mara moja jamani,” yule msichana alirejea akiwa ameongozana na mwanaume mmoja, mnene sana. Mweusi sana. Meno yote nje, katikati ya paji la uso ana pembe la ng’ombe, si kwamba ameipachika, bali imeotea hapo. Kwa kweli alikuwa anatisha sana, sana!



    Yule msichana ambaye mimi naweza kusema ni katibu Muhtasi au Sekretari wa kule.

    “Huyu ni msaidizi wa Mkuu wa taifa hili, yeye ndiye mwenye ujumbe wa kutoka kwa Mkuu mwenyewe, anayo ya kusema. Namwachia yeye sasa.”

    Alipomaliza kusema, aliinama kidogo kama ishara ya utii kwa mkubwa wake, kisha akainua shingo kuwa kama kawaida.



    Kulisikika mkoromo kama wa spika ambayo ina matatizo. Lakini spika haikuwepo wala dalili za waya.

    “Santeni sana, santeni sana,” ndivyo alivyoanza kusema, badala ya ‘asanteni’ akasema ‘santeni’.



    Akaendelea: “Mimi ni mtoa maagizo tu, lakini mwenyewe atafuatia muda kidogo. Kuna wale waliokuja toka duniani kwa lengo la kuwa matajiri, waende kule,” alisema akinyoosha kidole mahali ambapo alitaka watu hao waende.

    Mimi nilianza kusimama, lakini mzee Madume akanishika shati na kunikalisha chini vilevile kama mwanzo.



    “We huhusiki,” alisema, akanishangaza sana, kwani maongezi yetu toka mwanzo ni mimi kuwa tajiri, yaani kupata pesa nyingi kupitia biashara ya uvuvi wa samaki.

    “Khaaa!” Nilimshangaa sana kwa kukoroma.

    “Unashangaa nini, si nimekwambia bado.”

    “Sawa mzee.”



    “Haya, wale waliokuja ili wawaue wabaya wao waende pale,” yule mtu aliendelea kusema.

    Watu wakatoka kwenda sehemu iliyoelekezwa, kundi hili lilinishangaza sana, lilikuwa na watu wengi sana.

    “Oke, santeni sana. Santeni sana. Wale waliokuja wakitaka kuutawala uchawi watoke huku, waje nyuma yangu.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mzee Madume alinishika mkono na kunivuta kwa nguvu, nikataka kukataa, lakini akanizidi nguvu.

    Wakati huo, bado watu walikuwa wanaingia kwa wingi toka duniani kiasi kwamba, niliamini kuwa, kuna wakati dunia inakosa watu, kwani wengi wanakuwa wamekwenda huko.



    Na hapa nataka kusema jambo, sitaki kuitaja jina siku, lakini katika siku saba za wiki, kuna siku mbili, watu wengi wanakwenda huko, iwe kwa kupelekwa au kujipeleka. Lakini wengi huenda huko. Ukitaka kuamini, fuatilia, utakuta katika kila wiki, hizo siku mbili watu huwa wachache sana mijini, hata foleni za magari si kubwa na kunakuwa hakuna shida sana ya usafiri.



    Siku moja ipo mwanzomwanzo mwa juma, nyingine mwishomwisho mwa juma. Kazi kwako kuzijua siku hizo mbili.

    Wakati tunapita mbele, yule Mkuu akasema:



    “Nyiye wengine mngejua kwamba, hakuna kundi zuri kama la wale wanaotaka kuutawala uchawi, naamini wote mngetaka kundi hili. Lakini si mbaya, santeni. Santeni sana.” Aligeuka, akaondoka akimwacha yule msichana pale. Naye akaendelea:

    “Haya, kundi la kwanza mkaingie chumba namba tatu, kundi la pili, chumba namba moja, na kundi la tatu, chumba namba mbili.”



    Alipomaliza kusema akawa anayaangalia makundi yote kama anataka kuhakikisha kwanza maagizo yake yanatekelezwa au la.

    Ilikuwa ni miingiliano, watu wa kundi hili wakienda kundi lile, wa kundi lile wakija huku, ili mradi tu.



    Kulipotulia, mimi na yule mzee tulikuwa ndani ya chumba tulichotakiwa kuwepo.

    Kilikuwa chumba kikubwa sana, umbali wa kutoka chini hadi juu darini ni kama umbali wa uwanja wa mpira toka goli moja hadi jingine.

    Mapana yake, kama viwanja vitano vya mpira na bado tulibanana kwa sana tu.

    Mwanga ulikuwa hafifu sana kiasi kwamba, haikuwa rahisi kumtambua wa mbele yako kwa umbali wa mita kumi.



    Kwa mbali ilikuwa kama kuna AC kwa ajili ya kuweka hewa ya baridi badala ya joto, mlio wa AC ulisikika kwa mbali sana, lakini kila nilipojaribu kuchunguza huku na kule, sikuona AC wala dalili zake.

    Mambo niliyoyaona katika chumba hicho yalinishangaza sana, nilitamani kumwuliza mwenyeji wangu kuhusu mahala pale nikasita.



    Nikiwa nipo katika hali hiyo, ghafla mwanga mkubwa sana ukamulika kote, lakini bila kuwepo kwa taa, wala mishumaa, wala mlio wa Jenereta, nikazidi kupigwa butwaa.




    Akatokea mtu mmoja, yeye weusi wake si kama wenzake, alikuwa zaidi. Alikuwa mweusi kama chungu kilichozeeka.

    Akiangalia hivi, macho yake yalikuwa kama yanatoa mwanga hafifu huku kichwa kikiwa kipara chote.

    Kilichonishangaza zaidi ni kitendo cha mtu huyo kuwa na rangi hiyo, lakini eti alivaa kanzu nyeupe sana.

    Sasa ile rangi nyeusi ya mwili na ile rangi nyeupe ya kanzu, akaonekana kutisha sana, hasa ikizingatiwa kuwa, naye kwenye paji la uso alikuwa na pembe refu lenye kama mita moja.



    Alisimama akatuangalia kama vile aliyetaka tunyamaze ili aanze kusema ingawa hakukuwa na watu wanaosema sema, pengine ni kutokana na wasiwasi na hofu iliyokuwepo eneo lile, hasa pale kila mtu mgeni alipojua eneo tulilokuwa si duniani.



    Lakini mimi kwa akili zangu nilijua ni duniani, bali ni chini ya dunia. Maana hata ndani ya dunia ni dunia. Nje ya dunia, ingekuwa sayari nyingine, kama vile Uranus, Venus, Mercury au Jupiter.

    Basi, ukimya ulitawala, yule mtu akiwa amesimama pembeni ya yule msichana PS, akasema:

    “Kazi yangu kubwa si kutoa elimu, bali uwezo. Kama ni elimu mtapewa huko huko duniani kila mmoja kwenye eneo lake.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipomaliza kusema, akamgeukia yule msichana huku akinyoosha mkono kupokea kitu. Yule msichana akainama, akanyanyua ndoo nyeupe kama kioo cha kujitazamia, akampa, naye akapokea na kuishika mkono mmoja.



    Huyu mtu alikuwa mrefu kidogo, kwa sisi wote tuliokuwa ndani, hakuna aliyekuwa mrefu kama yeye, hata yule msichana hakuwa mrefu kama yeye, ingawa na yeye kati yetu hakuna aliyemfikia kwa urefu.

    Akiwa ameshika ndoo ya maji, alichovya mkono, akachota maji akayarusha kwetu, yakaja kama maji yayorushwa na mpira wa kumwagilia.



    Yalitupata wote na tulilowa sana, lakini wapo waliolowa zaidi na wapo waliolowa kidogo, mimi nililowa zaidi.

    “Hongera sana kijana wangu, umekuwa mtu mwingine sasa, si kama ulivyokuwa wakati hatujaingia humu ndani,” mzee Madume aliniambia huku akiniangalia kwa macho yenye kunipa pongezi.



    “Kwa hiyo inakuwaje?” Nilimuuliza.

    “Kuanzia sasa, wewe ni jasiri, una nguvu za ajabu na una uwezo wa ajabu.”

    “Nitajuaje?” Nilimuuliza.



    “Tukifika duniani utajua tu.”

    Mara sauti ya yule mtu ikatukatisha:

    “Kuanzia sasa, kila neno kutoka kwenye vinywa vyenu litakuwa na maana, kila mtakachotenda kwa kutegemea nguvu hii pia kitafanyika.”



    Alipomaliza kusema hivyo aligeuka na kurudi. Kama nilivyosema, ukumbi ulikuwa mkubwa kama viwanja vya mpira, kwa hiyo mpaka anaondoka tulimkazia macho hadi anapotea zake.

    Pale alibaki yule msichana, lakini naye baada ya yule mzee kupotea, aligeuka na kutoka ndani ya ule ukumbi tukisubiri amri nyingine ya juu.



    Mara alitokea yule mwanamke ambaye naye ni wa ajabu aliyetupokea na kutuingiza mle. Akasimama mbele ya watu wote na kupaza sauti akisema:

    “Hiki ni kipindi cha wageni kupotezana, sasa kila aliyekuja na mwenzake amshike mkono, mnatoka nje kabisa, huko kila mmoja anakutana na maelekezo mengine.”



    Alipomaliza kusema, akageuka na kuondoka zake.

    Kwa haraka sana nilichojifunza mimi ni kwamba, utawala wa kule ulikuwa kama wa duniani, kwa maana kwamba, kulikuwa na protokali. Kila mtu alitambua jukumu lake ni lipi na linaanza kufanya kazi wakati gani.



    Basi, tulianza kutoka nje na kila aliyekuwa na mwenzake alimshika mkono, mimi mzee Madume alinishika mkono. Tukaongozana hadi nje kabisa ambako tulikuta watu, wanawake kama yule aliyetuamuru kutoka nje, lakini wakiwa wengi sana. Kila mmoja alikuwa na ubao mweupe, maandishi mekundu yakisomeka mahali mtu alipotokea.



    “Sisi wetu yule pale,” aliniambia mzee Madume baada ya kusoma ubao wa mtu yule ambao uliandikwa Wavuvi Mwanza.

    Tulimfuata yule mwanamke, naye alipotuona akasimama ghafla, kisha akageuka kutupa mgongo huku akisema:

    “Nifuateni.”

    Tulimfuata kwa nyuma hadi nje ya geti kubwa la jengo hilo, akatuonesha njia akisema:

    “Hii njia inafika mlikotoka, ifuateni moja kwa moja. Tahadhari, msikate kulia wala kushoto,” alisema akisimama pembeni ili kutupa nafasi sisi ya kuanza safari.



    Tulitembea umbali wa mita kama mia moja hivi, njia ilikuwa ya kupita kwa miguu tu na si gari, halafu udongo wake kama mchanga wa pwani mweupe.

    Tukiwa tunazidi kwenda, tulifika eneo fulani mbele yetu tuliona ukomo wa njia. Kwa maana kwamba, endapo tungeendelea kwenda tungetumbukia, mzee Madume akasimama na kusema:

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Tatizo la huku bwana ni hili. Kila ukija kunakuwa na ugeni wa jinsi ya kuingia na jinsi ya kutoka, sijawahi kuja nikatoka kwa mtindo huu wa kukutana na gema kama hili, sasa mbona njia hapa imefika mwisho na yule alituambia moja kwa moja, tumekosea wapi?”

    Mimi sikumjibu kitu zaidi ya kukaa kimya, maana kama ni kujua yeye mwenzangu ndiye alikuwa mwenyeji zaidi.

    “Nimesema nyoosheni, sasa mnasita nini, nyoosheni,” sauti ile iliyotupokea ilisema huku ilikotokea hakujulikani.



    Mzee Madume alinishika mkono, akanivuta, tukanyoosha hadi kwenye mwisho wa njia ambapo ni gema kubwa na kwa chini kulikuwa kunaonekana mawingu ya bluu. Yaani ilikuwa kama vile sisi tupo juu ya dunia.

    “Sasa rukeni hapo mrudi kwenu,” sauti ilisema.




    “Mzee Madume alinishika mkono, tukaruka, lakini mimi huku nikipiga kelele.

    “Haa!” Nilihamaki kwani kufumba na kufumbua tulikuwa pale pale tulipoondokea.

    Mzee Madume akawa anacheka.

    “Ha ha ha haaa! Ulijua tunakufa leo?” Aliniuliza kwa utani. Lakini sikumjibu.



    Maisha yalianza kubadilika hapo. Nilirudi kwenye makazi yangu, mzee Madume naye alirudi kwake. Lakini akiniambia kuwa, kila nitakapotaka kumfanyia ubaya mtu niwe nanuiza kwa maneno ya kumtaka mkuu wa nguvu za giza ambaye ni shetani aitwaye Lusifa.



    “Kama kuna mtu anakusumbua unataka tumbo lake livimbe, unasema “Lusifa nataka tumbo la mtu fulani livimbe”, basi kufumba na kufumbua litakuwa limevimba na litaendelea kuvimba kutokana na unavyotaka,” mzee Madume aliniambia huku tukiachana.



    Nikiwa nyumbani, upepo mkali sana ulivuma kiasi kwamba, niliamini unaweza kuezua paa. Nilivumilia kwanza, lakini hali ikaendelea mpaka nikaanguka chini na kujikuta niko kwenye ulimwengu mwingine.

    Huko nilikutana na watu kibao kama mimi, yaani vijana vijana sana.

    Kila mmoja alionekana anakaa kwenye sehemu kwa ajili maalum. Kama vile kuna mgeni alikuwa akisubiriwa.



    Na mimi nikatafuta sehemu yangu, nikakaa.

    Mara akatokea mtu mmoja, mrefu sana, mweupe kama mwarabu, amevaa kanzu nyeupe, inaburuza chini sakafuni. Alipotembea, mwili wake ulizungukwa na mwanga kama miale ya jua.

    Uso wake wakati mwingine ulionekana kama unawaka, wakati mwingine kama giza, nywele zake zilikuwa ndefu sana, lakini zikionekana zenye matunzo mazuri.



    Huyu mtu alikuwa peke yake na mwendo wake ulikuwa wa taratibu sana huku mikono ameshika kwa mbele jirani na kifuani kama vile ishara ya unyenyekevu.

    Aliposimama akatugeukia, ndipo nikamwona kwa uzuri zaidi na pia nikabaini tofauti kubwa kati yake na binadamu sisi.



    Macho yake yalikuwa ya pembe tatu, midomo mipana sana, kidevu kirefu kupita kawaida na masikio kama ya sungura.

    Alikohoa kidogo, moto ukatoka kinywani, akapiga chafya, pia moto ukatoka puani. Na wakati anakohoa na kupiga chafya, lile jengo tulimokuwemo lilitikisika kama kuna tetemeko la ardhi.



    Aliinua mikono juu, mikono ya kanzu ikashuka hadi mabegani, kitu cha ajabu sana kikajionesha, mikono ilikuwa myeusi tii tofauti na usoni. Kwa hiyo ni kama alikuwa na sura mbili ya mtu mweupe na mtu mweusi.



    “Kila mmoja ainue mikono kama mimi,” alisema.

    Mara, mikono ya watu wote ikawa juu.

    “Pokeeni nilichonacho,” alisema.



    “Sawa,” tulisema.

    Nikashtuka na kujikuta nipo nyumbani kwangu, chumbani kama nilivyokuwa kabla.

    “Khaa!” Nilishangaa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ***

    Ilikuwa ni asubuhi ya siku iliyofuata tukasikia habari ya maiti za wavuvi wawili zimepatikana ziwani zikielea. Mimi nilijua ni wale wavuvi waliosukumwa majini na mzee Madume.

    Nilikutana na mzee Madume ziwani, alionekana mchangamfu sana huku akisema ana mpango wa kubadili shughuli, badala ya uvuvi anataka kununua matrekta ili awe anakodisha kwa watu kulimia mashamba. Hapo tulikuwa tumekaa na wavuvi wengine kama sita.



    “Hivi jana mlikuwa wapi nyinyi?” Mvuvi mmoja aliuliza, wengine wakadakia.

    “Tena kweli.”

    Kusema ukweli hakuna aliyeweka wazi, si mimi wala si mzee Madume aliyekuwa tayari kuanika safari yetu.



    “Jamani, si tunawauliza nyinyi?”

    Mzee Madume akawa anacheka tu.

    Zamu ya kuanza kazi ilifika, nikaingia mtumbwini. Tuliingia watu watatu, lakini mzee Madume hakuwepo.

    Siku hiyo tulivua samaki wengi sana, sana tu. Kiasi kwamba hata mtumbwi ulielemewa na mzigo mkubwa wa samaki.



    Njiani wakati tunarudi, wenzangu wakawa wananitania.

    “Au mwenzetu mlikoenda jana na mzee Madume ndiyo majibu yake haya nini?”

    Nilicheka tu, lakini sikuwafungulia moja kwa moja kwamba, ni kweli yale ndiyo yalikuwa majibu ya safari tuliyokwenda jana yake au la!



    Tulipofika ufukweni, tulikuta wenzetu wengine nao wakiwa wamerudi. Mtumbwi wa mzee Madume nao ulijaa samaki wengi kiasi kwamba, maswali yakawa kibao kwa wavuvi wengine.

    “Mh!” Mvuvi mmoja aliyekuwa kwenye mtumbwi mmoja na mimi aliguna, mguno huo uliashiria kuwa, alishangazwa na wingi wa samaki kwenye mtumbwi wa mzee Madume. Kusema ukweli hata kama ningekuwa mimi ningeshangaa, kwanini mitumbwi ambayo sisi tuliokuwa hatupo jana yake ndiyo iwe na mapato ya samaki kwa wingi vile?!



    Kifupi biashara ilikwenda vizuri kwa upande wangu kiasi kwamba, maisha yangu pia yalibadilika. Ikafika mahali, nikafungua duka kubwa mjini Mwanza, akawa anauza mke wangu. Wakati huo mzee Madume alishahamia Kagera ambako alikuwa akimiliki matrekta na magari ya kubeba abiria toka mjini Bukoba kwenda Muleba.



    Baada ya muda nilifungua duka jingine la pili kubwa sana kuliko lile la kwanza. Nikawa nauza mwenyewe, hapo ndipo maisha yangu ya uchawi yaliponoga.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog