Search This Blog

MZIMU WA WAUFI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : MAUNDU MWINGIZI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mzimu Wa Waufi

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    “Naitwa Hunudu, ni shefa mkuu katika Dini hii tukufu ya WAUFI, Dini hii inaongozwa na Wafalme wa Bahari, Wafalme wa Pande kuu za dunia, Dini yetu kama zilivyo dini zingine tunaongozwa kwa kuzingatia misingi ya Nidhamu, Adabu na Utii iliyoweka katika kitabu chetu ambacho ndio muongozo wetu wa Kiibada na shughuli zinginezo, Kitabu chetu kinaitwa HADHALUFI“ Maneno haya yalikua yakitamkwa na Kijana mmoja Mweupe, ana mwili wa wastani, alionekana ana jicho bovu(Chongo) kitu kilichofanya wajihi wake uzidi kuonekana ni wa kikatili sana, wakati huo akiyaongea maneno hayo Masumbuko alikua amesimama katikati ya Chumba hicho, huku kwa mbele akiwa amesimama kijana huyo mwenye jicho bovu aliejitambulisha kwa jina la Hunudu, pembeni mwa chumba hicho walikuwepo wazee kama watano hivi, wazee hawa walikua kimya muda wote wakati hunudu akiendelea kuoa maelezo

    “Taratibu zetu ziko kama ifuatavyo, Hua tunakutana mara tatu kwa wiki. Siku ya Jumamosi ni siku yetu ya kufanya Ibada maalumu huku huku chini ya mapango ya Bahari, siku ya jumatatu ni siku maalum ya kutoa Kafara ya damu na Adhabu kwa yeyote atakaekiuka miongozo yetu ikiwemo kutunza siri, kutohudhuria ibada, kukataa kutoa kafara, nk, na siku ya alhamisi ni siku ya kutoa hukumu za makosa, na kusikiliza Shida, mashitaka mapya.” Maneno hayo yalizidi kumuogopesha Masumbuko na sasa alianza kuelewa kua yupo chini ya mapango ya baharini, hakujua ni kwa nini yuko pale, kwanini anapewa maelezo hayo ya siri, alikua akitetemeka mwili mzima. Kisha kijana huyu Hunudu mwenye jicho bovu akamshika mkono Almas na kumpeleka chumba kingine huko alikuta watu wakipewa adhabu kali za ajabu ajabu, alioneshwa watu wakikatwa Ulimi, wengine wakiokwa kama mikate, wengine wakipigiliwa misumari katikati ya vichwa vyao, Masumbuko akawa anatokwa na Machozi,

    “Acha kulia we mtoto wa kiume, kua makini usije ukakiuka mashart yetu” alimkanya Hunudu

    “Kwani nani kaniingiza kwenye hii Dini bila ya Idhini yangu?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Si umetaka mwenyewe hakuna aliekulazimisha” akafikishwa sehemu akashuhudia kijana mmoja akichinjwa kama kuku na damu yake watu wanainywa, akamuona Hunudu nae anachuku kibuyu maalum kisha anakinga damu ile nae anakunywa, kisha akakinga tena damu nyingine akampa Masumbuko nae anywe lakini Masu akakataa kunywa ikabidi hunudu amshike mikono yake na kuwaamuru vijana fulani wawili wamnyweshe damu ile ya binaadamu, Masu akajikuta anapiga kelele “NOOOOO..” Ghafla akashtuka, akageuka huku na kule, akajiona kumbe yuko chumbani kwake, alikiua naota, Ni Ndota ya ajabu sana ambayo hajawahi kuota hata siku moja, akiwa anahema kwa hofu kubwa mara mkewe nae akashtuka kutoka usingizi ikabidi amuulize mumewe kulikoni?

    “Kulikoni, mbona hivyo”

    “We acha tu mke wangu”

    “Nini tatizo?”

    “Nimeota Ndoto ya ajabu sana”

    “Mmmh Ndoto gani tena?” akaanza kumuhadithia mkewe jinsi alivyoota, ilikua ni Ndoto ya kutisha sana mpaka mkewe nae akaanza kuogopa, ikabidi wakubaliane kua walale tu wataongea kesho lakini kila walipojaribu kulala ilishindikana, Usingizi haukupita kabisa mpaka asubuhi

    “Pole mume wangu, ni Ndoto tu wala usiwaze sana”

    “Mmmh haya mke wangu..”

    “Na kama itakusumbua nitaenda kwa Mchungaji kumuambia aje kukufanyia maombi” walijaribu kufarijiana mtu na mkewe japo Masumbuko hakupenda kusikia masuala ya Kuombewa na Mchungaji kwakua yeye Imani yake ni ya Dini ya Kiislam ila mkewe huyu yeye ni Mkristo, na wamekua wakiishi pamoja kwa ndoa ya Bomani, basi wakaendelea kuutafuta usingizi mpaka asubuhi bila ya mafanikio na kulipopambazuka tu Masu aliamka na kwenda bafuni kuoga kwa ajili ya kujiandaa kwenda kazini, japo siku hiyo hakua na amani kabisa kila saa Ndoto ile ilijirudia kichwani mwake Lakini alijitahidi kujisahaulisha akaenda kazini na huko akaendelea na shughuli zake za kila siku pale ofisini kwao, Maisha yaliendelea vizuri bila ya kuota tena ndoto za ajabu kwa takribani wiki nzima na sasa alikua meshaanza kuisahau Ndoto ile ya kutisha

    *****



    WIKI MOJA BAADAE

    “Tulikuambia kua wewe sasa ni mfuasi wa dini ya Waufi, haupaswi kuvunja kanuni zetu Lakini umeamua kwa jeuri kabisa kuvunja taratibu za wakuu wa Bahari na sasa utaadhibiwa” Hunudu alikua akimuambia Masu, wakati huo Masu alikua kidali wazi amesimama mbele ya kiti kirefu cheusi alichokalia mzee mmoja hivi mweusi ananywele nyingi kichwa, Nywele zikiwa zina mvi za mbali mbali, baada ya Hunudu kusema maneno yale, ikawa sasa ni zamu ya Mzee huyu nae kuongea, kaanza kwa kumuuliza swali Masu

    “Una watoto?”

    “Ndio Mkuu”

    “Watoto wangapi na wa Jinsi gani?”

    “Mapacha wawili, wa kiume na wa kike”

    ”majina yao?”

    ”Wakiume anaitwa Fani na wa kike anaitwa Zani” “Safi, sasa kwakua umevunja taratibu zetu kwa kosa la kutoa siri zetu za WAUFI kwa mkeo sasa tunakupa adhabu” Baada ya Mzee huyu kuongea kwa sauti yake Nzito nay a kukwaruza, akachukua kitabu kikubwa akampa Hunudu kisha Hunudu akakisoma kimya kimya na baada ya kukisoma akaniangalia Usoni na Kisha akasema

    “Utatoa kafara ya damu ya mwanao wa kiume siku ya Jumamosi na kama utathubutu kufuata ushauri wa huyo mkeo wa kwenda kuombewa kwa huyo mchungaji tutakuongezea adhabu nyingine”

    ”Bora mniue mimi ila mwanangu simtoi, nasema simtoiiiii!!!” Kumbe Masu alikua tena usingizini, ndoto ile ilikua imejirudia tena, alipokua akiweweseka kwa kusema kua hamtoi mwanae ndipo Judith(Mkewe) akaamka

    “Jamani nini tena mume wangu?”

    “Waufi, waufiiiii”

    “Umekuaje lakini, Waufi ndo nini?” Kabla hajajibu chochote alishtuka kutoka usingizini ndipo sasa kama fahamu zikawa zimekaa vizuri

    “Ile Ndoto imejirudia tena, wanataka kafara ya damu kwakua nilitoa siri yao kwako”

    “Nini?? Kafara?wamejuaje kama uliniambia chochote?”

    “Ndio, yaani watu walewale niliowaota wiki iliyopita ndo wamenitokea tena, Haiwezekani, hebu nipe simu yangu nimpigie baba”

    “Lakini saa hizi ni usiku mkubwa, angalia ni saa Tisa kasoro hii utawashtua sana nyumbani”

    “Hapana siwezi kuendelea kuvumilia nipe tu niongee nao sasa hivi” Masu alikua amechanganyikiwa sana akainuka na kwenda chumbani kwa wanae kuwaangalia akawakuta wamelala, akarudi mpaka chumbani kwake na kuchukua simu yake, akaiwasha na kuanza kutafuta namba ya baba yake, akaiona kisha akabonyeza kitufe cha kupigia halafu akaweka simu sikioni

    *****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    WIMBO mashuhuri ulioimbwa miaka kadhaa iliyopita na Jabari la muziki marehemu Marijani Rajabu, wimbo uitwao ‘Mwanameka’ ulisikika ukivuma kwa sauti kubwa kutoka katika simu ya Mzee Kikoko ambao ameu Set kama wimbo wa kupokelea kwenye simu yake, muda huo ndo kwanza alikua akivuta shuka na kujigeuza upande wa pili, alikua katikati ya usingizi mzito, Laikini kutokana na usiku kua tulivu sana aliweza kuisikia simu yake na akaamka haraka kuangalia ni nani aliekua akipiga simu usiku ule, akaichukua simu yake na kuiangalia kwenye kioo haraka haraka alimtambua kua ni Mwanae Masumbuko “Hallow” ilikua ni sauti ya Mzee Kikoko, sauti iliyojaa mchoko wa usingizi na hofu

    ”Shikamoo Mzee”

    “Marahaba, mbona usiku sana kuna nini tena?”

    “Babanina matatizo”

    “Matatizo, matatizo gani?”

    “Yaani hata sijui nianzie wapi kukueleza,”

    “Anzia hapo hapo, huko mbele nitakuelewa”

    “Baba basi we lala tu mie kesho asubuhi nitapanda Buss nakuja huko nyumbani”

    “Sasa ulinipigia simu ya nini?, niambie hata kidogo ni matatizo gani..” “nahisi kuchanganyikiwa Baba, Ni habari ndefu sana, nikija kesho tutaongea” Baada ya maelezo hayo akakata simu, mzee Kikoko akabaki na butwaa, alama ya mshangao ikajiandika moyoni mwake, Hakua na la kufanya,

    Maana Angefanye nini hasa!!

    Basi akaamua tu kulala lakini chango la uzazi liliunguruma hata usingizi ukakata alitaka kujua mwanae amekumbwa na jambo gani mpaka ampigie simu usiku mkubwa vile

    *****



    SIKU ILIYOFUATA

    Katika stand ya Ibinzamata, Stand ya mabasi ya mkoa wa Shinyanga, majira ya saa kumi na mbili jioni alikua amesimama Mzee Kikoko na Mwanae mdogo wa kiume, akiwa ameenda kumpokea mwanae Masumbuko akitokea jijini Dar es Salaam. Mzee kikoko alionekana kutawaliwa na hofu kubwa na shauku ya kujua kinachomsibu mwanae huyo anaefanya kazi jijini Dar es Salaam katika kampuni ya Birimuye Holdings Ltd inayojishughulisha na huduma za kifedha katika mitandao ya simu, Kila akikumbuka jinsi alivyoongea nae kwenye simu alipokua akimtaarifu juu ya ujio wake huo wa ghafla alizidi kuamini kua kuna zaidi ya tatizo katika ujio huo wa Almas.. Baada ya kama saa moja hivi tayari Buss la Super Sonic Safar lilikua limeingia katika viunga vya stand hiyo maarufu mkoani hapo, Mzee kikoko akajisogeza taratibu mpaka karibu ya mlango wa Buss kwa ajili ya kumpokea Mwanae, haikuchukua muda mrefu akamuona Masumbuko akiteremka kutoka ndani ya Buss, akamsogelea na kumpokea Begi lake Jekundu

    na kisha wakasogea pembeni kidogo ili wasalimiane

    “Shikamoo mzee”

    “Marahaba, mzima?”

    “Mie mzima namshukuru Mungu”

    “Enhee mmetembea salama?”

    “Salama kabisa baba”

    “Haya tukaangalie Tax sasa tuondoke” baada ya kujuliana hali wakatoka mpaka nje ya eneo hilo la Stand kisha Mzee Kikoko akamuita Dereva Tax akaanza kupatana nae Bei na baada ya mapatano wakaingia ndani ya gari, Masumbuko na mdogo wake wakiwa wameketi seat za nyuma na Mzee Kikoko akiwa ameweka kishoka katika seat ya mbele, Kama mjuavyo tena wazee wa mjini kwa mbwembwe, safari ya kwenda Mwasele nyumbani kwa Mzee Kikoko ikaanza, Haikua mbali sana kutoka Stand mpaka Mwasele japo ni ka hatua kidogo, na baada ya mwendo wa kama dakika arobaini dereva alikua tayari kaishapiga break mbele ya Nyumba ya matofari ya kuchoma iliyopigwa ‘plasta’ upande wa mbele tu, hapo ndipo nyumbani kwa mke mkubwa wa Mzee Kikoko ambae pia ndie mama yake Mzazi na Masumbuko. Mzee Kikoko ana wake wawili Bi Mkubwa anaitwa Kapemba Masanja, na mke mdogo ambae yeye anaishi maeneo ya Shaikom anaitwa Bi Mwajabu Fundikira. Baada ya kuwasili nyumbani hapo walitoka nje familia nzima

    kuja kumpokea Masumbuko.dada zake na wadogo zake walionekana kufurahi zaidi kumuona tena kaka yao, hawakujua kama ujio huu ni wa matatizo. Ilikua ni furaha kubwa kwao kuonana na ndugu yao aishie jijini Dar es Salaam, nyumba ilikua imefurika ndugu mpaka watoto wa mke mdogo wa mzee Kikoko aishie Shaikom nao walikuja kumpokea kaka yao, ki ukweli Mzee Kikoko alijitahidi sana kuwaweka pamoja na kiupendo wanae wote na wake zake japo changamoto za wake wawili hazikosi ndani ya nyumba Haraka haraka Jogoo akakamatwa kwa ajili ya mgeni japo na family nayo ‘Itasafiria nyota” kama ilivyo kawaida ya uswahilini, na baada ya salamu mazungumzo yakaanza kwa swalila Kikoko ambae alionekana kua hana raha tangu jana yake “Enhee mwanangu, hebu tutoe jaka la moyo maana hatujalala tangu jana tunawaza tu umepatwa na nini”swali hilo la Mzee Kikoko lilimtoa machozi Masumbuko ikabidi atoe kitambaa chake laini aanze kufuta machozi, kitu kilichozidi kuacha maswali kwa

    wazazi wake

    “Sasa ukishaanza kulia badala ya kusema tatizo nini ndo tutakuelewaje?” alidakia mama yake

    “Baba ni matatizo ya ajabu sana, sielewi ni nini hasa”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Matatizo gani hasa?” Ndipo sasa Masumbuko akaanza kuwasimulia wazazi wake kuhusiana na kadhia inayoendelea kutalii na kutanabahi katika falme za ubongo wake kupia Ndoto, Ndoto ya ajabu!

    “Yaani Ndoto tu ndo ikufanye Ulie, Ushindwe kulala, ufunge safari kutoka huko kote mpaka Shinyanga kuja kushitaki, we ni mwanaume wa aina gani?” Baada ya maelezo marefu kutoka Masu sasa ikawa zamu ya Mzee Kikoko ambae hakuonesha dalili za kuguswa na jambo hilo, aliongea kwa ukali na katika hali ya kumshangaa mwanae, ikabidi sasa mama yake na Almas nae aingilie kumtetea mwanae

    “Hii sio hali ya kawaida mume wangu, hakuna haja ya kumlaumu Masu, hata mimi nimeshangaa sana tu”

    “Ulichoshangaa wewe ni kipi hasa”

    “Haiwezekani mtu aote Ndoto halafu iwe na muendelezo kama Tamthiliya tena huku akipewa tahadhari ya kile alichokifanya, Haiwezekani”



    “Nyote mmekutana, Mama na Mwana sawa na Pipa na mfuniko tu, Ndoto ni ndoto tu hata uiote mara kumi, kwa hiyo we ukiota umepata pesa halafu baada ya kuamka usizione hizo pesa utaanza kuzitafuta chini ya Mto?” aliuliza Mzee Kikoko huku akisamama na kuashiria kua anaondoka zake, ikabidi Masu ajaribu kujielezea vizuri lakini Mzee Kikoko hakumuelewa na hatimae akatoka zake nje na kuwaacha mtu na mama yake wakifarijiana.

    *****



    Nje ya nyumba ya Mzee Kagomba, majira ya saa mbili za usiku walikua wamekusanyika watu wengi wakiwa wameketi huku wameizunguka meza ndogo ya mbao, wengi wa watu hawa walikua ni wazee mashuhuri kutoka maeneo tofauti tofauti ya mkoani Shinyanga, kama ilivyo Ada kila siku hukusanyika mahala hapo kwa ajili ya kupata kahawa ambayo ni sehemu ya Biashara zinazo msaidia Mzee Kagomba kujipatia Rizki, mbali ya kahawa Kikubwa zaidi kinachowafanya watu wengi kukusanyika pale na kuacha vijiwe vingine vingi vya kahawa si tu Ubora, usafi, na umahiri wa Mzee Kagomba katika kuiandaa kahawa hii Laa hasha Bali pia ni Mvuto wa Story za kila aina zipatikanazo maeno hayo, Kijiwe hiki cha kahawa kinafahamika zaidi kwa jina la BBC Kutokana na ukweli kwamba habari yoyote itakayotokea mjini hapo au hata nje ya mji huo iwe ya Kimichezo, kisiasa, kidini, nk basi lazima itaanza kufika hapo kabla hijazagaa kwingineko na wasimuliaji wa hapo ni mahiri kwa porojo sijapata kuona. Kila

    mtu ni mjuaji kijiweni hapo na hakuna anaekubali kushindwa katika hoja yake, hata kama ukiwa hauna pesa ya kununu kahawa unaruhusiwa tu kwenda kupiga Soga na kama ukija na habari tamu na ya kusisimua basi utanunuliwa kahawa mpaka umalize kutoa habari hiyo.. Ilikua ni siku ya pili sasa Mzee Kikoko hajaonekana kijiweni hapo kitu ambacho si kawaida yake kupitisha japo siku moja bila ya kukanyaga ardhi ile ya Waswahili wa mjini, Wazee wenzie walikua wakiulizana kama mzee mwenzao amekutwa na jambo au imekuaje mpaka hajakanyaga pale!! Walikua wakimkubali sana kwa Story zake za Tambo na Porojo, Ikawa kama bahati wakati wanaendelea kumjadili nae huyo akawasili, kila mtu akafurahi, akapatiwa kiti na baada ya kuketi Mzee Kagomba akaanza kumtania

    “We bwana haufi mapema hakyamungu..”

    “Kwanini tena, au Izraeli kamchumbia mwanao?”

    “Tulikua tukiulizana hapa hivi Mzee Kikoko amekufa na kuzikwa kimya kimya?”

    “Utaanza kufa wewe, mimi utaniacha..”

    “Haya hebu tujaalie hali ya Maungo yako..”

    “Kwakweli mpaka tunaingia mitamboni hali yangu ni murua, naendelea tu kuvuta pumzi mwanana bila ya malipo” watu wote wakaangua kicheko kutokana na majibizano ya wazee hawa watundu wa maneno “Enhee mwenzetu ukapotelea wapi?”

    “Ya kuacha tu, matatizo ya kila aina duniani hapa”

    “Hebu tujuze, hii ndo BBC Lete maneno upate ushauri kutoka kwa mabingwa wa saikolojia waliosomea miembeni”

    “Juzi alikua mwanangu Masu, lakini ujio wake haukua wa Kheri”..” “Enhee..”

    “Kwanza kabla hajaja, alinipigia simu usiku mkubwa akiwa ametaharuki vibaya, nilijaribu kumtuliza anieleze tatizo lakini hakusema akaniambia kesho yake angepanda buss ili aje huku Shinyanga tuyaongee vizuri” Wazee wote pale kwenye Kahawa walikua kimya wakimsikiliza Mzee Kikoko

    “Kesho yake sasa ambayo ni juzi ndo akaja na Buss nikaenda kumpokea stand kisha tukarudi mpaka nyumbani tulipofika nyumbani baada ya salamu na mazungumzo kidogo, nikamuuliza sasa anijuze tatizo lilikua ni nini hasa, cha ajabu mwenzangu akaanza kulia” Story ilionesha kuwatuliza masikio wadau wote pale, kisha baada ya kupiga funda moja la kahawa Mzee Kikoko akaendelea kutiririka na nyuzi

    “Baada ya kumbembeleza aniambie tatizo, nikabaki mdomo wazi akaniambia kua Anasumbuliwa na Ndoto, anaota vitu vya ajabu vinamnyima usingizi na kumkosesha raha” Alipofikia hapo kijiwe kizima kilizizima kwa vicheko vya hali ya juu ikawa sasa ni kelele tu bila ya msikilizano…

    “Amaa kweli ukiyastaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni, yaani badala umrithishe mtoto mali we umemrithisha huo uoga wako na uzezeta..” maneno hayo yalikua ni ya Mzee Kagomba akimtani mzee mwenzie kisha wakacheka sanaa akadakia Mzee mwingine nae akasemaCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yaani mimi sijatulia ila Kikoko na mwane mmeshinda tuzo..“ Mzee Kagomba akadakia tena

    “Waswahili wanasema Bata hata ale kokoto haachi kuharisha, mie nilijua una tatizo kubwa kumbe hujaacha tu maigizo yako“ wakati wakiendelea kucheka na kushangaa tukio hilo Mzee Kikoko hakumjibu mtu zaidi ya kuendelea kunywa kahawa yake, wengi walidhani ni mashara tu ya mzee huyu, na hapo ndipo ilisikika sauti ya Mzee Kapela aliekua muda wote kimya akivuta sigara yake taratibu, yeye akaja na Mpya

    “Mie nadhani ni utoto unawasumbua tu, badala tumsikilize amalizie hiyo ndoto ninyi mnataka kutuharibia mjadala huu, Hebu Kikoko Endelea..” Bila ya ajizi Kikoko akaendelea kuwasimulia jinsi Ndoto ilivyomuanza mwanae ikiwa ni pamoja na vitisho alivyopewa, kilichowashtua wengi ni pale sasa Kikoko alipoanza kuwaelezea jinsi ile Ndoto ilivyoendelea pale ilipoishia siku ya kwanza ikiwa na wahusika wale wale, kila mmoja alistaajabu na sasa hali ya kijiwe ikatulia tena na kila mtu akaonekana sasa kuguswa na mkasa huu, na baada ya Kikoko kuhitimisha uwasilishaji wa hoja yake wadau wakaanza kutoa ushauri. Wengi waliendelea kusisitiza kua japo ni Ndoto ya Kushangaza lakini itakua ni Ndoto tu na haitakua na athari yoyote, Lakini Kagomba alikua tofauti na baadhi ya vijana pale, ye aliwaambia kua ile si Ndoto ya Kawaida na kawashauri waende wakamuone Mzee Maguno kwakua yeye ni mtaalamu wa kutafsiri Ndoto. Hali ile ya malumbano pale kijiweni iliendelea bila ya

    kupata muafaka wa pamoja

    *****



    Baada ya siku mbili za kuwa pale Shinyanga, Sasa Masu alikua tena ndani ya Buss la SABENA Akirejea jijini Dar, Kichwani alikua bado anazungukwa na hofu, hafu ya kutokewa tena na Hunudu wa Waufi, mbaya zaidi alitegea kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa baba yake lakini hali ikawa tofauti aliambulia maneno makali ya dhihaka tu akiambiwa kua ni majiamizi tu hayo yanamsumbua Hatimae jioni majira ya saa moja tayari Buss lilikua limeegesha ndani ya Stand ya mkoa Ubungo Buss Terminal, alipoteremka tu alienda moja kwa moja mpaa nje akavuka upande wa pili wa bara bara kule zinapopaki daladala za Ubungo to Gongo la Mboto akadandia hiyo ili ashuke Buguruni, alifanya hivyo na bahati nzuri hapakua na foleni ndefu hivyo hakuchelewa sana kwani ndani ya Dk kama 30 tu alikua ameshashuka katika kituo cha Buguruni Shelly na hapo akaanza kutembea tu kwa miguu kutokea hapo Shelly kwenda kwake maeneo ya kwa mnyamani anakoishi hivi sasa, haikua mbali kutokea hapo kituoni

    Alipofika kwake alipokelewa na Mkewe Judith kwa shangwe na Furaha

    “Karibu mume wangu..”

    “Ahsante, habari za hapa?”

    “Nzuri tu nyumbani hawajambo wote?”

    “Hawajambo tu, vipi hawa(wanawe) hawajambo?”

    “Nao wazima wako ndani wanaanda madaftari yao ya kesho shule” “Enhee nipe habari za huko, Baba uliongea nae? Na kasemaje?” Swali hili lilimuumiza sana Masu na alijisikia vibaya kumuambia mkewe kua baba yake hajampa ushirikiano wowote zaidi ya maneno ya karaha tu, lakini haina jinsi ilibidi amueleze ukweli tu!



    *****

    JIRANI na msikiti mkongwe wa Idrisa uliopo Kariakoo mtaa wa Tandamti Jijini Dar es Salaam kuna duka kubwa la vitabu vya dini linalomilikiwa na Sheikh Jabu ambae mbali ya kuishi Dar es Salaam pia ana mke mwingine Tabora hivyo kufanya makazi yake kua sehemu mbili, Lakini pia Sheikh Jabu mzawa wa mkoani Kigoma, watu mbalimbali kutoka mikoa ya Kigoma na Tabora hufanya duka hilo kama vile sehemu ya kukutania na jamaa zao wa huko mikoani kirahisi kwa kua wengi wanapafahamu dukani hapo, pia Dukani hapo ni sehemu iliyozoeleka hata kwa wenyeji wa hapa jijini Dar es Salaam kama ni sehemu maarufu ambayo kila siku watu hukusanyika mida ya jioni kwa ajili ya kubadilishana mawazo, hua kuna mijadala mizito na malumbano ya hoja katika Nyanja tofauti toauti hasa Siasa, dini, michezo na uchumi Masumbuko nae hupendelea sana kwenda dukani hapo kupiga stori, Alipazoea dukani hapo kwakua mara kwa mara Baba yake Mzee Kikoko akija Dar hupendelea kwenda pale kupiga story na

    wazee wenzie hasa wa Kigoma pia Mzee Kikoko ni rafiki kipenzi wa mmiliki wa duka hilo Sheikh Jabu, Hivyo basi kutokana na umaarufu na usemaji wa Mzee Kikoko ikamfanya Masu nae akajikuta anafahamika sana Dukani hapo, Siku moja baada ya kutoka kazini kwake aliamua kwenda pale dukani kusikiliza habari za mjini lakini pia alikua ameweka nia kua kama atapata fursa ajaribu kuwadokezea kuhusu ile Ndoto yake maana hakika pale dukani ilikua ni uwanja wa wajuvi wa mambo, Lakini siku hiyo pale dukani hapakua na watu wengi, alikuapo muuzaji wa vitabu na Mzee mmoja kutoka kigoma ila nae kwa sasa anaishi pale Dar, anaitwa Mzee Kishindo, mzee huyu nae hua ni mtu wa maneno sana na hua ni rafiki pia wa Mzee Kikoko mara nyingi kikoko akija Dar hua karibu sana na Mzee huyu, ndipo Masumbuko akaona sasa acha achokoze kuhusu lile tatizo lake na ile Ndoto ya Ajabu

    “Mzee Kishindo samahani”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Bila samahani mwanangu”

    “Mie nina swali,,”

    “Kaswalie msikitini, hapa hakuna udhu” wakajikuta wamecheka wote “Hapana sio swala, nina jambo nataka kukuuliza”

    “Anhaa kumbe una suala, haya uliza”

    “Suala hilo linahusu Ndoto” baada tu ya Masu kusema hayo maneno mzee Kishindo akatabasamu kisha akanena

    “Unanikumbusha taaluma yangu niliyosoma miaka karibu thelathini iliyopita, taaluma waliyopewa Mitume na manabii”

    “Kumbe tatizo langu litakua limepata ufumbuzi”

    “Ndoto sio tatizo mwanangu, ni ishara muhimu na dalili zilizojificha za jambo Fulani ambalo ujumbe wake unaupata kupitia Ndoto, na kama utazifanyia kazi hautopata tabu ila ukizipuuza utajuta, utajikuta unahangaika kila siku, utayalaumu Maji machungu kumbe mdomo wako ndo una homa” Masu alikua akicheka kwa vionjo vya maneno kutoka kwa Mzee huyu,

    “lakini ziwe Ndoto kweli isiwe njozi zenu umelala haujaoga wala haujala sasa jinamizi linakukaba mpaka ufizi halafu unataka tukutafsirie ndoto yako tutawezea wapi!!!” Mzee alikua na maneno sana huyu mpaka sasa Masu akajikuta anaishiwa cha kuongea ikabidi tu ajitahidi kumrudisha kwenye mada

    “Mie kuna ndoto hua inanijia, ndoto ya kutisha sana, cha ajabu hua inajirudia kwa kuendelea pale ilipoishia”

    “Mmh,Hiyo kweli Ndot, enhee uliotaje?” Masu akaanza kumuhadithia mzee Kishindo kuanzia siku ya kwanza alivyoota kuhusu Dini ya WAUFI na jinsi anavyosumbuliwa na Hunudu, akaendelea kumsimulia mpaka ilipojirudia tena ndoto ile, ilikua ni hadithi ya kusisimua na kutisha, wakati Masu anaendelea kuongea wakaingia tena watu wawili nao wakawa wanasikiliza habari ile iliyoonekana kuwaingia sana lakini cha ajabu Masu akiwa anaendelea kuongea Mzee Kishindo alikua anacheka mpaka machozi ikabadi sasa Masu aache kwanza kusimulia, na alipoacha tu ndipo Mzee Kishindo akadakia

    “Dini ya Waufi?”

    “Ndio inaitwa dini ya Waufi, mbona unacheka sasa?”

    “Hakuna dini ya Waufi mwanagu hapa duniani”

    “Mzee usibishe, Mimi ndie nilieota, na wameniambia mambo yahusuyo dini yao hiyo karibu mara nne usingizini”

    “Hata wangekuambia mara mia lakini ujue hakuna Dini inayoitwa waufi”

    “Kwahiyo ni nini sasa?”

    “Ulishamueleza baba yako juu ya kadhia hii?”

    “Ndio nilienda mpaka Shinyanga kwa suala hili lakini kama unavyomjua Mzee Mwenzio, hakuna alichonishauri cha maana zaidi ya kuniambia kua naweweseka na majinamizi tu, akaniambia niwe nasali kabla ya kulala tu basi”

    “Ha ha ha aha, baba yako anajaribuKuficha moto sasa moshi utamuumbua”

    “Kivipi tena Mzee Kishindo?”

    “Nina uhakika kua Kikoko anajua kila kitu juu ya tatizo lako, au pengine amesahau, na kama amesahau basi amesahau kitu muhimu sana, na asipokua makini tatizo hili litakutesa na hata kukuua kabisa”

    “Mbona unanitisha Mzee, Kitu gani tena?”

    “Unajua sababu ya wewe kuitwa Masumbuko baada ya kuzaliwa? Maana kwenu hakuna babu yako hata mmoja aliwahi kuitwa jina hilo”

    “Hapana siijui” Mzee Kishindo akacheka tena kisha akaendelea

    “Tatizo lako ni kubwa sana, na pia ni dogo sana kama litawahiwa, kama litawekwa wazi bila ya kuogopa athari zitakazotokea, najua baba yako anaogopa athari za kuliweka wazi tatizo hili, ila kama utakua na ‘kifua’ nitakueleza na kukusaidia nini cha kufanya japo itahitaji muda, pesa na subra”

    “Nisaidie mzee, niko tayari kwa lolote”



    “Una kifua??, sio hicho kidali kama bao la kuchezea kamari, Kifua cha kutunza kila aina ya maumivu?”

    “Ndio, ninacho”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Lakini sio leo, uje nyumbani kwangu siku ya ijumaa, kwanza nitakupa historia yaw ewe kuitwa Masumbuko kisha nitakupa maana ya Waufi, na kisha tutaanza safari ya kukupeleka Umamani kwenu milima ya Unyanyembe huko” Mzee Kishindo alikua anaongea huku akicheka sana, Masu alibaki njia panda, hakujua ni nini alichokielewa mzee huyu, ni nini ambacho mzee kikoko anakificha, Waufi ni nini kama sio Dini? nk lakini ikabidi tu sasa akubaliane na mzee Kishindo kua wataonana Siku ya ijumaa Baada ya mazungumzo yale, tayari Masu alikua ameshaingia hofu hivyo hata hakukaa sana na kwakua tayari duka lilikua limeshaanza kujaa wapiga porojo, ikabidi aage na kuondoka zake mpaka barabarani ili akapande daladala ya kumrudisha nyumbani kwake, akiwa amesimama kituoni anasubiri gari ghafla kuna gari ilikuja na kusimama kwa mbele, ilikua ni gari aina ya Verosa, kioo kikashushwa mpaka chini na kumfanya aonekane vema mrembo aliekua akiendesha gari hiyo, dada huyo alikua amevaa

    Tshirt nyeusi na kofia ya kufuma ikiwa na rangi kama za wale Marasta, baada ya Masu kukutanisha macho na dada huyu akatoa mkono na kumuita kwa Ishara, lakini masu kila alipomuangalia dada Yule hakumtambua ila sura kama ilikua ikimuijia, ikabidi asogee tu kumsikiliza

    “Mambo” alianza Dada Yule kwa kumsalimia Masu

    “Poa, mzima?”

    “Mzima tu hujanijua?”

    “Hebu nikumbushe kidogo” Masu akajifanya kutabasamu kama kamjua kidogo

    “We si ni Masu wa pale Mtaa wa Nyamwezi kwa wale ma Agrigator wa Mpesa”

    “Naam ndio mimi, ofisi yetu inaitwa Birimuye”

    “Sasa hunijui mimi kweli au unajifanyisha tu nawe!? “

    “Sura inaniijia lakini sina kumbukumbuku za uhakika”

    “Mie hua ni wakala wenu hua mnaniuzia Float”

    “Aaah, nimekujua si unajua tena hua tunawahudumia watu wengi mpaka tunasahau, samahani wangu” Masu alijifanya kumjua lakini ukweli ni kwamba hakua akimkumbuka kabisa

    “wala usijali, unasubiri gari za wapi?”

    “Za buguruni”

    “Haya ingia nikusogeze mpaka ilala, mie hua ndo nakaa pale”

    “Ok ahsante nashukuru” Masu akaingia ndani ya gari kisha gari ikaondoka, ndani ya gari kulikua na kijana mwingine aliekua amekaa seat ya nyuma, ikabidi Masu ageuke ili amsalimie, Alipogeuka tu moyo wake ukalia ‘Paa!’ alishtuka mno, mara mapigo ya moyo yakabadilika, hofu ikazidi kutanda, alitamani ardhi ipasuke aingie, hapo hapo akatamani amwambie Yule dada amshushe haraka lakini akashindikana akahisi kama vile Mdomo ujeaa maji, jasho likawa linamfumka mwili mzima. Kijana huyo alikua ni kijana mweupe alievaa Tshirt nyeupe na kofia nyekundu, Masu alijitahidi kuvuta picha kua amemuona wapi kijana huyu, naam Kumbukumbu zake hazikimdanganya, ni kweli alimjua haraka kijana Yule.. Alikua ni Hunudu wa dini ya Waufi, na alimjua zaidi kutokana na ‘Chongo’ jicho buvu, Masu alichanganyikiwa sana kuona sasa yule kijana ambae hua anamsumbua usingizini kwenye ndoto kwa kujisifia kua nikiongozi wa dini ya Waufi leo amemuona ana kwa ana, Sasa alianza kuamini

    kua ile si Ndoto ya kawaida, akaanza kukumbuka maneno ya Mzee Kishindo, akiwa bado anatafakari nini cha kufanya mara gari ikawa imefika maeneo ya Ilala bungoni ikakatiza upande wa kulia kwenye kile kibarabara kidogo kinachochepuka kule kilipo chuo cha habari kisha ikasimama pembeni halafu Hunudu akamshika mkono Masu na kumsalimia, Masu alikua akivuja jasho la woga na hofu

    “Hali yako kaka Masu”

    “HUNUDU!!!!?” Masu aliuliza swali kwa wahka wa hali ya juu sana

    “Ndio mimi, kumbe una kumbukumbu sana!!,”

    “Yaani umeamua kunifuata mpaka huku duniani?”

    “Kwani hua tunaonanie mbinguni?” baada Hunudu kujibu vile wakacheka wote Hunudu na yule dada aliekua akiendesha Gari , ikabidi Masu amuangalie vizuri dada Yule maana aligundua kua nae ni lazima atakua ni mfuasi wa Waufu tu, wakati Masu anamuangali dada Yule huku Hunudu akaendelea kuongea

    “Punguza hofu na woga”

    “Shida yako nini hasa kwangu?”

    “Mimi sina shida yoyote kutoka kwako zaidi ya kuja kukukumbusha mambo kadhaa”

    “Mambo gani?!!” “Kwanza tambua popote uendapo na sie tupo, hauwezi kutukimbia, pili tulikukanya usitoe siri zetu hukusikia ukaenda kumuambia mkeo ukapewa adhabu ya kutoa kafara, ukakataa kumtoa mwanao, tukakuacha lakini sasa umeenda kutoa siri mpaka kwa watu baki tena huna hata woga, hivi haujipendi kijana?” Masumbuko alikua akitetemeka, mwili wake kama umeganda jinsi alivyokua katulia,

    “Sasa sikiliza Masu leo usiku nitakuijia ukanywe Damu na pia uingizwe rasmi katika kitabu cha kumbukumbu ya wafuasi wa Waufi pia utamtoa Mwanao mmoja kama kafara yako, ukileta tena upuuzi sasa tutakua kinyama, naomba usiniangushe” Baada ya Hunudu kuongea maneno yake yaliyojaa vitisho vikali dhidi ya Masu, haraka Dereva ambae ni Yule dada akafungua mlango wa mbele na kumuambia Masu ateremke ili wao waondoke, Masu akateremka kwenye gari kama aliemwagiwa maji ya jinsi alivyoroana kwa jasho lake mwenyewe, aliposhuka tu mlango ukafungwa halafu Yule dada akamchombeza kwa kimombo

    “Tutaonana usiku” halafu gari akatembea Masu alikua amechanganiyikiwa akaenda mpaka mbele huku kwenye Bara bara ya Uhuru akaiita bodaboda ikamchukua mpaka kwake

    “Tsh ngapi unanidai”

    “Elfu tatu tu kaka mkubwa” Masu akaingiza mkono mfukoni hata hakuhoji kwanini iwe pesa yote ile kutokea ilala tu hadi buguruni kisha huyo akaanza kuingia zake kwake

    “Kaka mbona haujachukua chenchi?” Dereva wa boda boda alimkumbusha Masu lakini naona hata hakusikia yeye akawa anawahi tu kwake alipoingia ndani akamkuta mkewe yuko pale uwani akifuafua ngua za watoto, akapita bila hata ya salamu mpaka chumbani, ile hali ikamshangaza sana Judith nae ikabidi amfuate Chumbani

    “Kuna nini mume wangu?”

    “Ni bora nife tu sasa?”

    “Ufe kwanini tena jamani?Hebu niambie kuna nini?”

    “Ile ndoto kumbe sio ya kawaida kabisa”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Imekuaje sasa?” Judith alijaribu kumshawishi sana Masu ili amuambie kilichotokea lakini Masu akawa anaogopa kumuambia akijua kua Waufi wanamuona, baada ya Judith kumsumbua sana ikabidi sasa amuambie tu ukweli wa mambo kuanzia yale maelezo ya kutatanisha aliyoambiwa na Mzee Kishindo halafu akamsimulia jinsi alivyomuona Hunudu uso kwa macho. Judith alipigwa na Butwaa na sasa badala amfariji mumewe yeye ndo akawa amechanganyikiwa mara mbili ya Masu mpaka Masu akawa sasa almanusura awe chizi,

    “Mume wangu haiwezekani, hili jambo zito mie naenda kwa Mchungaji Jofrey kumueleza jambo hili”

    “Hapana, acha tu”

    “Siwezi kuacha, ni bora ukaombewa maana wamesema usiku wanakuja tena” Masu alikua akikataa kuombewa na Mchungaji kwakua yeye ni muislam japo Judith yeye ni mkristo na hata ndoa yao walifungia Bomani tu, Masu alijua kua endapo Baba yake atasikia kua ameombea na Mchungaji itakua kasheshe lakini kwa ushawishi aliopewa na Judith akajikuta amelainika, na Judith akaenda mpaka kwa mchungaji na kumueleza kila kitu, baada ya mchungaji kumsikiliza vya kutosha akakubali kua wafuatane mpaka nyumbani kwake na Judith ili mchungaji akamuhudumie Masu pale pale Nyumbani.. Walipowasili walimkuta Masu akiwa ameketi chini kabisa kwenye kapeti, Mchungaji akamshika mkono na kumuinua kisha akamkalisha kwenye Sofa lake dogo halafu akaanza kusema nae, lakini kabla hajaanza kuongea nae chochote Mchungaji akamuomba Judith awapishe wazungumze, Judith akatoka kasha Mchungaji akaanza..

    “Pole sana Bw Masu”

    “Ahsante Baba Mchungaji” Masu alikua akijibu kwa utiifu, kwakua maji yalikua yameshamfika shingoni ikabidi tu amtii Mchungaji japo sio dini yake hiyo “Kuna jambo nataka kukushauri kijana”

    “Ndio Mchungaji..”

    “Najua Hunudu anakusumbua sana mpaka unakosa raha” Maneno haya ya Mchungaji yalimshtua kidogo Masu akawa anajiuliza kua huyu mchungaji kamjuajea Hunudu? Lakini akajipa moyo kua huenda Judith kamsimulia kila kitu, akaendelea kumsikiliza bila ya kumjibu chochote “Lakini usimlaumu sana, hata yeye pia ametumwa na Viongozi wakuu wa Waufi hivyo inabidi atekeleze maalekezo aliyopewa, hata lile jicho lake Bovu alitobolewa na viongozi hao zamani kabisa alipokua akiambiwa atoe kafara ya damu akawa hataki, hata yeye nilimshauri kua akubaliane nao tu japo alinipinga sana hatimae akatobolewa jicho na kafara akatoa, sasa nawewe nakushauri mapema kabla hujaumia, Toa kafara hiyo wanayoitaka na utakua salama vinginevyo utaumia na kafara utatoa tu utake usitake” Masu alisimama ghafla kwa uoga baada ya kusikia maneno mazito kutoka kwa Mchungaji akawa hajitambui sasa, akaanza kusikia kizunguzungu akajikuta ameropoka

    “Mchungaji sikuelewi kabisa”

    “Utanielewa tu, hata mimi pia ni Mfuasi wa Waufi na ukiendelea kujidanganya kutukwepa utaangamia, Acha kabisa kutoa siri zetu kwa Mkeo na kwenye vijiwe vya kipuuzi, hakuna atakae kusaidia huko” Masu hakuamini maneno yale aliyokua akiyasikia kutoka katika kinywa cha Mchungaji, Mtumishi wa Mungu anaeaminiwa sana, akaona sasa hana ujanja, ni kweli anaangamia, akaanza kusikia anaishiwa nguvu, kizunguzungu kikamzidia na ghafla akaanguka chini kama kifurushi na kupoteza fahamu pale pale

    *****



    BAADA ya Masu kuanguka chini na kupoteza fahamu, mkewe alishtushwa na mlio wa kishindo kizito uliotokea pale seating room ikabidi haraka akimbilie ndani kuangalia kuna kitu gani, alipofika pale ukumbini alipigwa na butwaa, akabaki kama Msukule au mwintunge kwa lugha ya kwetu baada ya kukuta Mchungaji akiwa amesimama anaendelea na maombi wakati huo Masu yuko chini amepoteza fahamu, Judith hakumuuliza kitu mchungaji akaenda mpaka pale chini huku akitetemeka akaanza kumtingisha na kujaribu kumuamsha lakini haikuwezekana, Judith akaanza kulia huku akimuuliza Mchungaji

    “Imekuaje tena jamani Mchungaji”

    “Mumeo ana mapepo, nimeyakemea sana yakamzidi nguvu na kumuangusha chini akapoteza fahamu” Mchungaji alikua akijibu kwa utulivu huku akijiamni sana lakini Judith alikua amechanganyikiwa sana akawa anaendelea kulia mpaka wapangaji wenzake wakasikia nao wakaja chumbani na kumkuta Judith akiwa amemuinamia Masu huku akilia wakati huo Mchungaji alikua amefumba macho akionekana yuko katikati ya Maombi, Kilichowashangaza wapangaji wenzao ni kile kitendo cha mchungaji kumuombea Masu wakati wanajua kua Masu ni muislamu, Lakini kwa hali ilivyokua wakashindwa kuhoji sana zaidi ya kujadili tatizo na kutafuta ufumbuzi mapema..CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya Judith, Mchungaji, na wapangaji wenzao wakakubaliana kumpeleka Masu hospitali haraka, hivyo mmoja kati ya wapangaji wale akaenda kutafuta Tax kisha akarudi nayo mpaka pale nyumbani wakambeba Masu mpaka kwenye Tax na safari ya kuelekea Hospitali ikaanza, Ndani ya Gari seat ya nyuma alikua amekaa Judith na Mchungaji wakiwa wamembeba Masu, na Seat ya mbelea alikua amekaa mpangaji mwenzie na Masu walikwenda mpaka Amana Hospital iliyopo Ilala na walipofika haraka mchungaji akaenda ndani kuongea na Dokta na baada ya muda wakaja manesi wakiwa na Machela zao, wakasaidizana kumtoa Masu kwenye Tax akiwa hajitambua na kumuweka juu ya machela kisha akapelekwa mpaka ndani kwa Dokta..



    Baada ya kutoa maelezo Dokta akaanza kumpa huduma ya kwanza, na kisha akapelekwa Wodini kulazwa, wakiwa Wodini Judith akakumbuka suala muhimu kua alikua hajamuambia mtu yoyote juu ya tatizo lile, akafungua mkoba wake akatoa simu ya Masu kisha akaiangalia namba ya Mzee kikoko na kumpigia alipoweka simu sikioni alisikia ujumbe huu “Asante kwa kutumia mtandao wa Vodacom, simu yako haiwezi kukamilishwa kwa sasa tafadhali ongeza salio na upige tena” Simu haikua na salio, Akainuka na kutoka nje kwenda kutafuta vocha..

    Baada ya kununua vocha na kuijaza katika simu ya Masu akampigia Mzee Kikoko

    *****

    Akiwa nje ya nyumba yake kwa mke mdogo maeneo ya Shaikom akiendelea na shughuli zake za kupalilia majani huku akifagia fagia ndipo Mzee Kikoko akasikia kwambali kutokea chumbani kwake wimbo wa Jabari la Muziki Marijani Rajabu ukivuma na upepo akajua kua ni simu yake inaita, akatupa jembe na kwenda kuchukua simu, alipofika na kuiangalia aliona kua ni namba ya Masu akapokea kwa uchovu

    “Hallo”

    “Baba shikamoo” Kikoko akashtuka kusikia sauti ya mwanamke kutoka kwenye simu ya mwanae, haijawahi kuokea hata siku moja Masu akampa simu mkewe ampigie baba yake, japo tayari Kikoko alikua amekwisha ing’amua sauti ya Juddy lakini bado alishangaa tu maana hakua na mazoea ya kuiwasiliana na Mkwe wake huyo kwakua kwanza hampendi kuliko maelezo kutokana na suala la utofauti wa Dini kati ya Masu na mwanamke wake huyo, lakini akaitikia na kujiulizisha kama vile hajamjua..

    “Marahaba, we nani?”

    “Mie mama zani?”

    “Mhuu kuna nini?”

    “Baba, hali ya Masu ni mbaya sana, Masu anaumwa sana, amezidiwa na amepoteza fahamu hapa tumemleta Amana hospital”

    “Amepoteza fahamu? Ilikuaje kwani?” Maneno haya ya Mzee Kikoko yalipenya sawia katika ngoma za masikio ya Mkewe mdogo aliekua Uani nae akaenda mpaka chumbani kusikiliza kinachoendelea, Mzee Kikoko alikua akimsikiliza Judith kwa makini sana kupitia simu yake nyeusi aina ya Nokia

    “Leo Masu alikuja nyumbani akiwa anatetemeka sana huku akiwa kama amechanganyikiwa”

    “Nikamuuliza kulikoni?, akaanza kunisimulia yaliyomkuta akaniambia kua alienda kule dukani kwa shekhe jabu akakutana na mzee mmoja ni rafiki yako wewe…”

    “Anaitwa nani huyo mzee?”

    “Anaitwa Mzee Kishindo..”Mzee kikoko kusikia jina la mzee kishindo sasa hofu ikamvaa lakini akajikaza

    “Enhee ikawaje?”

    “Masu akamuelezea huyo mzee kuhusu hii ndoto yake inayomsumbua, ndipo huyo mzee akampa maelezo mengi kuhusu hiyo ndoto yake na akamuambia kua yeye anakijua kinachomsumbua na akamuahidi kua atamsaidia, baaada ya Masu kuondoka pale dukani akiwa njiani ghafla akatokewa na yule kijana ambae hua anaemuta kila siku na kuanza kupewa vitisho..”

    “Nini?Yaani huyo anaemtokeaga kwenye Ndoto akamuona njiani?”

    “Ndio baba”

    “Haya makubwa sasa..Ikawaje sasa?”

    “Baada ya kupewa vitisho vingi wakamuacha, ndipo Masu akaja nyumbani akiwa amechanganyikiwa ndo mie nikaenda hapo jirani kwa Mchungaji Jofrey akaja kumuombea lakini wakati anamuombea mapepo yakapanda akapoteza fahamu ndio mpaka sasa tupo hospitali” Maelezo hayo yalimtoa jasho mzee Kikoko, hakuamini kila anachoambiwa..CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hivi we mtoto ni Shetani?” Judith akapatwa na mshangao kusikia maneno hayo, ikabdi akae kimya kidogo

    “Naongea na wewe, we ni Shetani? Aliekuambia ulete wachungaji kwa mwanangu ni nani? ”

    “Lakini baba mie kosa langu ni nini wakati mtu alikua amepatwa na matatizo?”

    “Aliekuambia kua Masu anatibiwaga na Wachungaji ni nani?”

    “Lakini baba mie sikufanya kwa nia mbaya”

    “Amaa kweli nimeamini Mchawi ni binadamu, Paka anatumwa tu, Kumbe wewe na Mzee Kishindo ndio mnanirogea mwanangu halafu mnajifanya kuwaleta hao wachungaji, sasa nakwambia hivi nataka Masumbuko apone Laa sivyo utakiona kilichomfanya kuku aanze kuota manyoa mkiani, Mie ndio Alwatan Kikoko” Baada ya mkwara huo mzito Mzee Kikoko akakata simu halafu akageuka nyuma ili aondoke ghafla akakutanisha macho na mkewe mdogo ambae alikua nyuma yake muda wote aliokua akiongea na simu

    “Kwani kimetokea nini Baba Masu?”

    “Naenda kwa Mama Masu..”

    “Lakini hujaniambia kuna nini?”

    “Tutaongea nikirudi” Kikoko akatoka ndani mule akamuacha mkewe huyu akiwa amesimama, cha ajabu huyu mwanamke akacheka kisha akasema kwa sauti ya chini

    “Kama ni haki yangu Mungu atanilipia hapa hapa duniani”



    Haraka haraka Kikoko akadandia baiskeli yake almaarufu kama Mkulima na kuanza kupiga pedeli kuelekea Mwasele kwa mkewe mkubwa mama Masu, Njia nzima alikua akimfikiria Judith kwa nini anampelekea mwanae wachungaji wakati anajua fika kua Masu ni muislamu, pia alikua akimuwazia Mzee Kishindo basi kwa kweli kichwa chake kilikua kimevurugika haswaa.. Baada ya kutembea umbali wa haja tu hatimae alikua amefika nyumbani kwake akateremka juu ya baiskeli na kisha akapita wima pale uani bila hata ya kusalimia

    “Baba Masu kuna usalama kweli?” aliuliza mama Masu huku nae akisimama na kumfuata mumewe ndani

    “Hakuna Usalama..”

    “Kuna nini tena mbona hivyo?” wakati huo tayari baba Masu alikua ameshaingia chumbani na mama Masu nae alimfuata huko huko ndipo sasa Mzee Kikoko alipoanza kumsimulia Mama Masu kila kilichotokea mpaka mama Masu nae akabaki mdomo wazi

    “Si nilikuambia Baba Masu, ile sio ndoto ya kawaida we ukawa unanipuuza?”

    “Huu si wakati wa kulaumiana tena Mama Masu”

    “Mguu umeshaota Tende ndo unakua muungwana sio, kwahiyo na huyo Mzee Kishindo na kamwambia nini sasa Masu?”

    “Tena ngoja, umenikumbusha” Mzee kikoko akatoa simu yake na kumpigia Mzee Kishindo

    “Asalamu alaykum Bwana Kikoko”

    “Hakuna cha Salama leko hapa, hivi unanitaka nini na maisha yangu we Kishindo?”

    “Hebu punguza spidi kwanza kaka, kuna nini hasa”

    “Nipunguze spidi ya nini? Reli haina bamzi mie nakuja moja kwa moja nieleza ni kiherehere gani kilichokutuma kwenda kumueleza upuuzi wako Masu mpaka umesababisha amezidiwa na kulazwa?!”

    “Masu amelazwa?”

    “Usiniulize hilo swali mimi, nakwambia hivi kama umemroga mwanangu kesho nakuja kupambana na wewe nataka nikute amepona”

    “Hivi Kikoko uko timamu kichwani wewe? Mie nimroge mwanao wa nini? Au unajifanya humjui anaemsumbua mwanao, sasa kama we ni jemedari na una nguvu sana kwanini usimdhibiti huyo aliesababisha yote hayo? Yaani unahangaika kukinyoosha kivuli wakati uliopinda ni mti?”

    “Nitolee maneno yako ya kibaradhuli mie Afirit minal Jinni wewe, nakwambia nitaanza na wewe hayo majungu uliyoyapika utayapakua uyale mwenyewe kesho nikifika”

    “Bwana Kikoko utamaliza kuni kwa kuchemsha mawe, huna utakalonifanya mie” Kikoko alikata simu kwa hasira, mkewe alijaribu kumliwaza lakini Kikoko alikua tayari ameshajaa jazba

    “Jiandae Kesho asubuhi tunakwenda Dar”

    “Mmh, Sawa”

    ****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    AMANA HOSPITAL

    Katika WOD No 5 kitanda kama cha nne hivi kutokea mlango wa kuingia alikua amelazwa Masu, kitandani alikuwa amezungukwa na watu kadhaa akiwemo mkewe Judith, wanae wawili wadogo Zani na Fani, pia alikuapo Mr Johaiven Kitale ambae ndie Boss wake na Masu katika kampuni yao ya Birimuye, Matibabu yalikua yakiendelea vizuri tu, na sasa Masu alikua ameshapata fahamu lakini hakua na uwezo wa kuongea sana, pia alikua akilalamika kua anasikia kizunguzungu na mwili hauna nguvu kabisa, lakini pamoja na matatizo yake hayo yote alikua akifarijika kwa ukarimu na upendo unaoupata kutoka kwa Mkewe, japo Judith alikua akimuhudumia Masu kwa moyo mmoja na kwa upendo lakini alikua na hofu kubwa kufuatia vitisho alivyopokea kutoka kwa baba yake Masu, hasa kila akiufikiria ujio wa Baba mkwe wake huyo alizidi kuingiwa na baridi ya hofu mwili,

    *****



    Majira ya saa kumi na mbili na nusu asubuhi, tayari Mzee Kikoko na mkewe Mama Masu tayari walikua ndani ya Buss la Raha Leo ambalo tayari lilikua limeshaanza kuuacha mji wa Shinyanga kuelekea Dar es Salaam, Kikoko alikua ametinga Kaunda suti ya rangi ya udhurungi na mkewe nae alikua amevaa baibui la ukaya la rangi nyeusi na mtandio wa kahawia, kama ungebahatika kuiona sura ya Mzee Kikoko lazima ungeangua ucheko maana alikua anaonesha dalili za ushari na alikua akitamani hata gari lifike Dar muda ule ili akapambane na Juddy na Mzee Kishindo ambao ndio anaamini kua ni wabaya wake..



    Baada ya safari ya masaa takribani kumi, tayari gari lilikua limeshaegesha ndani ya STAND YA MABUSS YA Dar es Salaam, UBUNGO. Kikoko na mkewe walikua wakiteremka kutoka ndani ya gari, hawakua na mizigo mingi isipokua ni begi moja tu waliloweka nguo zao, kwakua kikoko hakua mgeni Dar mara kwa mara alikua akija Dar alikua akifikia nyumbani kwa Sheikh Jabu na kijiwe chake kikuu akiwa ni Dar ni pale Dukani mtaa wa Tandamti, wakatoka mpaka nje ya stand kisha wakapanda daladala mpaka Kariakoo, wakateremkia kituo cha Msimbazi karibu na Shelly kubwa ya mafuta ya Big Bon, haikua mbali sana kutoka Hapo kituoni mpaka Mtaa wa Tandamti ambako ndipo lilipo duka la sheikh Jabu, Lengo lake apite kwanza pale ili kama atamkuta Mzee Kishindo aanze nae kabla ya kwenda Hospital



    Bahati haikua yake baada ya kufika Dukani alimkuta kijana mmoja, ambae ndie hua muuzaji wa vitabu na Mtu mmoja aliekua amevaa kanzu nyeupe na kilemba chekundu

    “Mzee Kikoko karibu” Muuza duka alimpokea kwa furaha Kikoko kwa kua alikua akimfahamu

    “Ahsante haujambo?”

    “Sijambo, Shikamoo” kijana Yule akampokea begin a kuliingiza dukani

    “Marahaba, habari za hapa?”

    “Aaah nzuri, poleni na safari”

    “Aaah hatujapoa, hivi kabla ya yote huyumzee Mshindo leo hajafika leo hapa?”

    “Sasa hivi ametoka hapa ameenda Hospital kuona Masu”

    “Anhaa, Saafi, ngoja nimkute huko huko, hilo begi utaenda nalo nyumbani kwa Sheikh Jabu mie nikitoka Hospital niatenda moja kwa moja nyumbani”

    “Haina tabu, lakini Mzee Kikoko kuna jambo nataka kukushauri”

    “Jambo gani tena”

    “Huyu mzee hapa ni Sheikh wetu na hua anajua sana kuwasomea wenye matatizo kama ya Masu sasa kwanini usiende nae huenda Mungu akasaidia”

    “Sawa tu ni wazo zuri, maana tayari nasikia wameshampelekea Eti Mchungaji akamuombee, nakwambia leo huyo mwanamke atanitambua” Baada ya maelekezo hayo ikabidi Kikoko amsogelee Sheikh Mwinyigoha na kumsalimu, na baada ya mazungumzo mafupi walikubaliana kwenda wote hospitali, waondoka wote, Sheikh Mwinyigoha, Kikoko na mkewe wakaongozana barabarani kwenda kupanda daladala ya kuelekea Ilala(Amana Hospital)



    Haikua kazi kubwa kwa alwatan Kikoko kupata sehemu ya kupandia Daladala, alikua akiijua vema mitaa hii ya mjini utadhani yuko Shinyanga, wakaenda mpaka barabara ya Uhuru na kupanda Daladala zinazokwenda Tabata Segerea na kwaku hapakua na foleni kubwa siku hiyo basi ndani ya dakika kadhaa kikokoko alisikika akimuambia kondaCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Shusha Amana hapo” ni kweli ilikua tayari gari imefika kituo cha amana, Kikoko alionekana kuyajua vema maeneo ya mjini, konda akagonga Bodi na gari ikazua upande wa kushoto mwa barabara, Kikoko na mkewe pamoja na Sheikh Mwinyigoha wakateremka huku kwa mkwara Kikoko akawa amemshika mkono mkewe ili amvushe barabara upande wa pili ambako ndiko iliko hospital, Kweli Wazee wa mjini wana mambo. Kwakua tayari Kikoko alikua ameshapewa maelekezo ya Wodi alikolazwa mwanae wala hakupata shida akaenda mpaka kwenye korido kuu ya kushoto na kisha akaanza kuianga WODI No 5, muda mfupi akawa ameiona akajielekeza huko, mkewe akiwa nyuma akimfuata, muda wote huo walikua hawaongi kitu chochote, Naam wakaingia WODINI

    *****

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog