Search This Blog

MZIMU WA WAUFI - 2

 







    Simulizi : Mzimu Wa Waufi

    Sehemu Ya Pili (2)



    Kwakua tayari Kikoko alikua ameshapewa maelekezo ya Wodi alikolazwa mwanae wala hakupata shida akaenda mpaka kwenye korido kuu ya kushoto na kisha akaanza kuianga WODI No 5, muda mfupi akawa ameiona akajielekeza huko, mkewe akiwa nyuma akimfuata, muda wote huo walikua hawaongi kitu chochote, Naam wakaingia WODINI

    *****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akiwa anamnywesha uji Masu ghafla moyo wa Judith ulifanya ‘PAAA’ Baada ya kukutanisha macho na Mzee Kikoko akiwa na mkewe pamoja na Sheikh Mwinyigoha, miguu ilianza kumtetemeka kwa hofu masikini dada wa watu, Kikoko alipomuangalia Judith alijisikia kama anataka kupasuka kwa hasira, akaenda mpaka pale kitandani alipofika wala hakuuliza akamnyanyua Juddy na kumsukumia pembeni mpaka uji ukamwagika

    “We mchawi nilikuambiaje? Nataka mwanangu apone haraka Nguruwe we”

    “Baba mbona hivyo lakini, mbaona mnaninyanyasa sana?” Juddy alilalama na hapo hapo mama Masu sasa akamdaka nae

    “Hivi umeona kumroga mwanangu haitoshi mpaka umletee hao wachungaji wako si ndio?” wakati hayo yanaendelea Masu alikua anajisikia vibaya sana kuona Judith anadhalilishwa kwa kosa ambalo si lake akashindwa kujizuia akataka kuinuka pale kitandani ili akamzuie Mama yake ambae tayari alikua amemkwida Juddy, ndani ya Wodi pakawa na kelele na zogo mpaka wagonjwa wengine wakawa wapatwa na mfadhaiko, lakini alipotaka kuinuka tu akazuiliwa na Sheikh Mwinyigoha ambae alikua ameshamsogelea pale kitandani na kuanza kutaka kumsomea dua

    “Tuli kijana, unataka kufanya nini sasa?”

    “Sheikh, wanamuonea bure tu huyo mwanamke”

    “Yote umeyataka wewe”

    “Kivipi Sheikh?”

    “Kama ungetunza siri za waufu unadhani yangefika huku? Na hata hivyo unabahati umemkuta Hunudu hiki kipindi ametulia vinginevyo saa hizi angeshakutia kilema wewe” Masu alishtuka sana akaanza kutetemeka, hakuamini kabisa maneno ya Sheikh Yule, inaonesha Sheikh huyu anajua kila kitu kuhusu Dini ya Waufi, Masu alitamani baba yasogee karibu ili amsikie huyu shekhe aliekuja nae lakini ilikua ngumu maana muda huo Kikoko na Mkewe walikua wakimshambulia Juddy

    “Sasa we na Shekhe au ni mfuasi wa Waufi? Masu alipouliza swali hilo Shekhe Mwinyigoha alicheka sana kisha akamjibu

    “Mimi ni mfuasi wa huyo hapo..” Mwinyigoha alisonta kwa kidole chake uswa wa mlango wa kuingia kwa Dokta, Ikabidi Masu ainuke ili amuangalie ni nani, ile kuinua macho yake hivi akamuona mtu akiwa amevaa mavazi ya kidaktari amesimama kule mlangoni, ikabidi Masu amuulize Shekhe Mwinyigoha

    “Kwani ni nani huyo?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Acha mzaha Masu inamaana we hujamjua huyo? Hebu muangalie vizuri” Masumbuko akajiinua tena na kuangali vizuri TOBAA! Macho ya Masu yakakutana na HUNUDU akiwa katika mavazi ya kitabibu

    “Nooooooooo..” Masu alipiga kelele huku akisimama pale kitandani, Hamad!! Mzee Kikoko akarudi mbio mpaka kitandani na kumshika mwanae

    “We una nini hasa?”

    “Baba, ni Hunudu huyo kaja mpaka huku, tuondokeni haraka” alijibu Masu huku akilia

    “Yuko wapi?” Masu akageuka ili amuoneshe baba yake lakini ghafla hakumuona tena hunudu

    “Baba hata huyu Shekhe wako nae ni Mfuasi wao” baada ya kusema hivyo tu Masu akatoka mbio na kumponyoka baba yake, akatoka mpaka nje ya Wodi na kutokomea kusikojulikana



    “Sheikh imekuaje tena na wewe?”

    “Mmh Mzee inaonekana mwanao ana matatizo makubwa, sasa kila mtu yeye anamtuhumu tu” Mzee Kikoko na mkewe wakachanganyikiwa wakamuacha Sheikh Mwinyigoha akiwa amesimama Wodini wao wakatoka kumtafuta Masu

    *****



    KUFUATIA taharuki ile pale hospital iliyoletwa na Mzee Kikoko na mkewe, hakuna aliebaki mule wodini baada ya Masu kutoka mbio. Judith alitoka na kukimbia, Mzee Kikoko na Mkewe mama Masu nao waliondoka bila hata ya kusemeshana na yule Shekhe waliokwenda nae pale Hospital, haikujulikana Masu amekwenda wapi walijaribu kumtafuta bila mafanikio mpaka usiku ikabidi tu sasa Mzee Kikoko na Mama suma warudi tu mwananyamala kwa Seikh Jabu ambako ndiko walikofikia na kulala ili kesho yake waendelee kumtafuta tena Masu, Sheikh Jabu hakuwapo pale nyumbani alikua safarini Tabora lakini siku hiyo alikua ndio yuko njiani anarejea Dar hivyo Mzee Kikoko hakua na mtu wa kuongea nae sana juu ya kadhia iliyomkumba mwanae Lakini kwakua familia nzima wanamfahamu na wanamchukulia kama mwanafamilia pia hivyo haikua tatizo kwake, ikawa ni yeye na mkewe tu chumbani

    “Baba Masu nakuambia hivi hata huyo shekh Mwinyigoha mimi simuamini kabisa”

    “Hapana, sidhani kama atakua ni mtu mbaya itakua tu ni kweli Masu amechanganyikiwa sasa”

    “Mie najiuliza muda wote ule alikua anaongea nae nini pale kitandani mpaka akapiga kelele?”

    “Masu Atakua tu amechanganyikiwa maana haiwezekani kila mtu kwake awe ni sijui Waufi ila kesho itabidi niende pale dukani nikamuulize yule kijana juu ya huyu shekh”

    “Mmh ananitia hofu sana, haya”



    Huku Buguruni nako Judith alikua peke yake Chumbani analia tu kama mwehu, alikua akiuumizwa sana na matatizo yanayoendelea kutokea ndani ya familia yake na Masu, alikua hata hajui Masu atakua wapi muda ule wa usiku, kama atakua mzima au Laa, na zaidi kila alipowafikiria wazazi wa Masu walivyomzushia kua kamroga mtoto wao ndio kabisa alihisi kuchizi lakini hakua na Jinsi zaidi ya kumuomba Mungu amuoneshe njia, nae alilala tu bila matumaini huku akitia nia kesho yake kwenda kumtafuta hovyo hovyo mumewe

    *****



    Saa kumi na moja alfajir Mzee Kikoko aliamka kwa ajili ya kusali kama ilivyo kawaida yake, akatoka nje kwa ajili ya kuoga na kujiandaa na swala, hakutaka kwenda msikitini aliamua tu kua ataswali pale pale nyumbani, Alipomaliza kuoga akatoka mpaka pale uani ndipo akamuonaSheikh Jabu akipigwa mswaki akamsogelea na kumsabahi

    “Assalamu alaykum”

    “Owhoo bwana Kikoko waalaykum salaam, habari za Shinyanga?”

    “Nzuri tu Sheikh, nawe za Tabora huko?”

    “Huko hawajambo, poleni tu na matatizo?”

    “Aaah bwana hivyo hivyo tupo nayo”

    “Nasikia umekuja na mama Masu..”

    “Ndio, yuko ndani humo bado amelala”

    “Vizuri nitamsalimia kukipambazuka, Enhee nasikia tena ikawa mambo ya aibu huko Amana hospital… kunani tena mzee mwenzangu?”

    “Unajua Yule mwanamke wake na huyo Masu ni mpuuzi sana, pamoja na Kishindo nae ndo wale wale, hapa hata mwanangu sijui yuko wapi” Kikoko alianza kufunguka sasa, Sheikh Jabu akaona yatakua makubwa ikabidi amkatishe

    “Sasa mi nadhani tukaswali kwanza halafu we ukapumzike tu kasha tutaonana kule Dukani ndo tutaongea vizuri”

    “Haya hakuna tabu” Kikoko akaingiachumbanikwake, huku nyuma Sheikh Jabu alikua amechia tabasamu la mamba huku akimuangali alwatan Kikoko akiingia chumbani kwake



    Baada ya swala tu Shekhe Jabu hakukaa tena akaondoka zake nakuelekea mjini alikua na miadi na mtu maeneo ya dukani kwake Kariakoo, lakini Kikoko yeye alirudi kulala akivuta muda kupambazuke vizuri ili baada ya kupata ‘Istiftahi’ yaani kifungua kinywa ndipo nae aende kwanza dukani akaongee na Sheikh Jabu halafu zoezi la kumsaka Masu lianze

    *****



    Majira ya saa nne asubuhi tu tayari duka la Sheikh Jabu lilikua limefurika, wengi walikua wameenda kuzungumza juu ya balaa liliotokea jana yake kule Amana hospital maana tayari taarifa zilkua zimeshafika pale, na kwakua Jabu hakuwepo Dar hivyo kila mmoja alifurahi kuonana na kuzungumza na Sheikh Jabu, muda si mrefu Mzee Kishindo nae aliwasili pale dukani akapokelewa vizuri na Sheikh Jabu na baada ya kuketi tu nae akaanza kuwapa mchapo kuhusu mikwara aliyopigwa na Mzee Kikoko juzi yake kupitia simu, Sheikh Jabu alikua akicheka mpaka machoziCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unajua Yule Bwana Kikoko hua simuelewi kabisa yaani anazeeka na upuuzi wake ha ha ha..” alichombeza sheikh jabu

    “Nakwambia jana ungemuona alivyoingia hapa na ule mustache wake kama AmrishPul ungepasuka mbavu” wakati wadau wakiendelea kupashana habari za udaku na ufyetere ghafla kwa mbaali akaonekana Alwatan Kikoko akivuka barabara na kuja usawa wa dukani

    “Jamani Kikoko huyo anakuja..”

    “Hebu badilisheni mada msije kutuletea songombingo hapa” wadau wakajifanya wanajadili suala la Katiba mpya anayoendelea kuandikwa huko Bungeni, Naam Kikoko akawasili



    “Karibu Alwatan Kikoko..” Sheikh Jabu alimpokea

    “Shukrani.. Assalamu alaykum”

    “Waaleykum salaam, karibu uketi hapo kwenye kiti chako cha uvivu” wakati anasogea kwenye kiti akakutanisha macho na Mzee Kishindo

    “Hapana nimeghairi, wala sikai tena kuna Mchawi humu ndani”

    “Acha mambo yako bwana Kikoko mchawi gani tena?”

    “Si huyu Kishindo, ninyi hamjamjua tu kua ndie anaemroga mwanangu huyu?”hapohapo Mzee Kishindo uzalendo ukamshinda akajibu

    “Tafadhali bwana Kikoko naomba heshma iendelee kujizungusha katika mhimili wake”

    “Kwahiyo we ni kidume sana? Haya inuke tupambane”

    “Naam mie ni Kidume tena Rijali haswaa, na ni baba wa Watoto watato”

    “Mpuuzi mkubwa wewe mwanaume mzima unajisifia kua na watoto watano, njoo kwangu uone timu ya mpira, na leo bora nimekukuta hapa unieleze sababu za kumroga mwanangu halafu wewe huyo huyo unajifanya eti utamsaidia”

    “Mie nimroge mwanao kwa lipi? Leo unajifanya humjui mchawiwako eeeh?Au nimwage mchele kwenye kuku wengi?”

    “Mwaga huo mchele, Kuku wakiula basi nawao usiku tutawala kwa wali, mzandiki mkubwa wewe”

    “Sikia bwana Kikoko, mie ni mtu mzima sasa hizo hila na shari unazonitafuta nimeshazijua kitambo kirefu tu ila kaa utambue kua Chiriku mzee hakamatwi kwa makapi..”

    “Unajifanya muungwana sasa baada ya kulikoroga, kwahiyo ulizikaanga Bisi halafu unataka kuwaachia wenye meno watafune si ndio? Sasa nakwambia hivi utanionesha alipokwenda mwanangu mwanga mkubwa wewe, Laa sivyo humu leo hatoki mtu kama Airtel money”

    “Tafadhali bwana mkubwa chunga ulimi wako, Kumbuka kua Cheche huchoma msitu na ulimi uliponzakichwa, jambo dogo sana unalolidharau lizaweza kukuletea madhara makubwa katikamaishayako..”

    “Utanifanya nini wewe? Mie ndio Alwatan Kikoko nitakuhamisha mji huu”

    “Debe tupu halichikutika, najua siku zote debe likiwa halina kitu ndani yake basi hata likidondokewa nakitu kidogo kamap punje ya haradani litapiga kelele tu ila debe lililojaa hata unga laini wa azam halitotoa kelele hata ulipige teke, sasa we Debe tupu endelea kupiga kelele tu”

    “Unaleta dharau sio? Ngoja nikuoneshe..” Kikoko akavua mfuko mdogo aliokua ameuning’iniza begani ili amvae sasa Mzee Kishindo, yaani Kikoko alikua amejawa shari mwili mzima, watu wote dukani walikua kimya ikabidi sasa Sheikh Jabu aingile kati

    Jamani wazee wenzangu hebu muogopeni mungu, angalieni sasa mnajenga picha gani kwa vijana wadogo hawa mbele yenu!!” Kwakua Kikoko hua anamuheshimu sana Sheikh Jabu akashusha pumzi kidogo kasha Seikh Jabu akaendelea

    “Wahenga wanasema Chungu kidogo huwahi kuchemka wakati chungukikubwa huchelewa kuchemka wakiwa na maana kua Kichwa kidogo kwa maana ya uchachewa hekma , busara, na maarifa huwahi kuchemka hata kwa mambo madogo tu, sasa wazee wenzangu mnashindwa kutumia hekma zenu kulimaliza jambo hili bila tafrani ukizingatia umri wenu umekwenda sana na wanasemakua ukimuona NyaniMzee ujue kakwepa mishale mingi sana”

    “Kwahiyo Sheikh Jabu unamaanisha haya mambo ni madogo wakati mie mwanangu amerogwa na tayari nimeshambamba mchawi wangu ukizingatia mpaka sasa sijui mwanangu amepotelea wapi” alidakia tena Kikoko

    “Hapana sina maana hiyo, nina maana ya kwamba kwa tatizo hili ilikua vema mkakaa kama watu wazima nakulimaliza, naamini katika maisha mmeshakutana na changamoto nyingi kuliko hii”

    “Mie siwezi Kukaa na huyu fatani na hasidiwa maisha yangu”

    “Usiseme hivyo bwana Kikoko kumbuka kua Dhoruba iliko ndiko shwari iliko bimaana kua wagombanao ndio wapatanao, lazima tuliongee na limalizike kwa salama jambo hili”

    wakati Sheikh Jabu akiendelea kuwanasihi wazee wenzie kwa mbali wakasikia wimbo wa Mwanameka ukitokea katika Mfukowa Koti wa Mzee Kikoko, ilikua ni simu yake ikiita alipoitoa akaona ni namba ya Masu, mojakwa moja akajua ni Mke wa Masu tu huyo

    “Enheee hongea upese na wewe mchawi namba mbili”

    “Baba shikamoo” Ilikua ni sauti ya Masu

    “Marahaba, we Masu uko wapi?”

    “Niko kwangu”

    “Ulikua wapi tangu jana sie tunakutafuta”

    “Nililala nyumbani kwa Boss wangu”

    “Nakuja huko sasa hivi” Mzee Kikoko akakata simu kasha akatoka bila hata ya kumuuaga mtu yeyote na kuanza kuelekea kwa Masu,CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huku nyuma aliacha gumzo kubwa na vicheko vya hali ya juu kwa wadau pale dukani japo Mzee Kishindo alionekana kutokuana furaha kutoka na majibizano yale

    ****



    BUGURUNI KWA MNYAMANI



    Masu alikua amejilaza kitandani akionekana ni mwenye mchoko wa hali ya juu huku kichwa chake akiwa amekilaza juu ya miguu Mkewe Judith, halafu kwa pembeni walikua wamekaa watoto wao wawili mapacha Zani na Fani ambao hawakuelewa chochote kinachoendelea kutokana na udogo wa umri wao,

    “Yaanimimi nahangaika hivi na wewe halafu wazazi wako wananitukana na kunidhalilisha mbele za watu kiasi kile..”

    “Nisamehe mimi mke wangu, wala usiwalaumu wale, uzee umeshawaingia”

    “Hapana ni bora nikakuacha uendelee kuishi na wazazi wako kwa amani kuliko haya mateso nayoanza kuyapata, yaani wananiita mimi mchawi”

    “Judith yaani uondoke kisa Baba yangu? Kama mimi na wewe tumependana hakuna wakututenganisha zaidi ya Mungu, kumbuka mwanzo wakati tunataka kufunga ndoa ya kiserekali alinikataza na kunitishia kunitolea radhi lakini niliongea nae na yakaisha sembuse hili”

    “Haya kwanini na jana ukakimbia hovyo a ukenda kulala kusikojulikana? Una jua mie nilibaki katika hali gani?..” wakati wanaendelea na mazunngumzo wakasikia sauti ya mlango ukigongwa



    “Ngo! Ngo! Ngo!..”

    “Ngo! Ngo! Ngo!..”



    Judith akainuka kitandani na kwenda kufungua mlango, alipofungua tu akakutana na Sura ya Alwatan Kikoko akiwa amenuna vibaya

    “Karibu baba” Kikoko hakujibu kitu akaingia mpaka ndani na kumkuta Masu akiwa amejilaza pale kitandani

    “Karibu mzee”

    “Ahsante” Kikoko akavuta kistuli karibu na kitanda alichojilaza Masu halafu akakaa nae, hapo hapo Zani na Fani wakamsogelea Babu yao na kumkalia miguuni. Mazungumzo yakaendelea

    “Enhee unajisikiaje?

    ‘Naendelea vizuri kiasi”

    “Mwanangu umeamini kinywa cha mzazi hakitoi harufu mbaya bali kinatoa maneno ya Baraka?”

    “kivipi Baba?”

    “Wakati unataka kumuoa huyu mwanamke mie na mama yako si tulikukataza wewe hukusikia sasa si unaona mabalaa hayo?”

    “Sasa baba lakini haya matatizo yanahusiana nini Judith?”

    “We umesharogwa huwezi kujitambua, tuulize sisi tulioko pembeni, sasa sikiliza mimi sitaki tena kukuona ukiwa na huyu mwanamke, hawa wanao nitaondoka nao nitaenda kuwalea Shinyanga..”

    “Lakini baba…”

    “Lakini nini? Nimeshamaliza, kwanza Hebu amka ukaoge tuondoke mara moja nikupeleke kwa sheikh Jabu”



    Masu akainuka akatoka mpaka nje akamuambia Mkewe ampelekee maji bafuni akaoge, Judith akachukua ndoo ya maji mpaka bafuni kisha Masu akafuata, Masu akaanza kuoga kama kawaida,

    Wakati huo huku chumbani Mzee Kikoko akiendelea kucheza cheza na wajukuu zake, lakini Judith akaamua tu kukaa zake nje maana aliona sasa tayari bwawa limeshaingia Ruba. Akiwa Bafuni Masu akijipaka sabuni, tayari alikiwa na mapovu mwili mzima ghafla alisikia mlango akigongwa, akajiuliza huyu nani tena?! Ikabidi ajimwagie haraka maji usoni ili atoe mapovu, alipomaliza akafumbua macho HAMAD!! Alipigwa na butwaa, alijiona yuko katika Bafu, zuri na la kisasa tofauti na kule alikokua akioga, akawa hajitambui kua yuko wapi, akaanza kutetemeka, alipojiangalia vizuri akajigunduakua alikua sio Masu tena, alikua amebadilika kabisa maumbile yake na sasa alionekana kama mwanamke mzuri na mrembo hasa, Masu alizidi kuchanganyikiwa, akajiangalia zaidi ya mara mbili, vile vile akiwa ni mwanamke kabisa tena alieumbika kike, akiwa bado hajaelewa ni nini kimemtokea akasikia tena mlango ukigongwa kwa mara ya pili, ikabidi ajikaze aulize

    “Nani?” heee! cha ajabu hata sauti yake ilikua imeshabadilika na kua sauti laini na nyororo kabisa

    “Hebu fungua haraka we Shamsa, kuoga gani masaa sita? Tayari wageni wameshafika huku?” Masu alizidi kupata hofu alijiuliza sauti ile ni ya nani? Na kwanini amebadilika vile? Na je huyo Shamsa ndio yeye au ni nani hasa? Na ni wageni gani waliokuja? Na pale yupo wapi? Lakini hakupata jibu, akaanza kupepesa macho huku na kule akijaribu kuangaza nguo zake lakini hakuona nguo zake zaidi ya Khanga moja ya laini pamoja na nguo ya ndani, ikabidi tu avae nguo ile ya ndani kisha ajifunge khanga ile nusu bega, nahivi alikua na maji maji mwilini ndio kanga ikayashika vema maungo yake na kumfanya azidi kuvutia, Akafungua mlango sasa ili atoke nje akukutana uso kwa suo na huyo Bi Mkubwa aliekua akimgongea mlango, Bi mkubwa huyu alionekana kupata jazba sana akaanza kumpokea huku akimtokomeza kwa maneno

    “Hivi we unaakili kweli wewe? Naomba usinisumbue mie nakuona siku hizi kama umekua jeuri sana, kama ulikua hautaki kuolewa si ungesema mapema kuliko kutusumbua hivi”

    “Mama mbona sikuelewi?” Masu alijibu kwa mshangao sana japo kwa wakati huo sio Masu tena ni Shamsa

    “Leo nimekua mama yako? Muone mpaka unayachanganya maneno, hebu pita huko ndani ukavae haraka, tayari mshenga ameshakuja yuko huko seating room” Masu alizidi kuduwaa ikabiditu sasa akubali kuingia ndani, ilikuani chumba kizuri na cha kisasa, inaonekana wanaoishi mule wako vizuri kiuchumi, Baadaya Masu kuingia akaanza kuvaa sasa baada ya kumaliza kupaka mafuta japo nguo za kike zilimchanganya zaidi, muda akaingia tena Yule Bi mkubwa akaanza kumtengeneza na kumremba vizuri Masu mpaka Masu akaonekana kua sasa amependeza na kuvutia mnoCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Inatakiwa hata huyo Shemeji yako alietumwa tu nae akutamani mtoto wakike” Masu akazidi kupata picha sasa kua pale anatambulika kama SHAMSA na anatakiwa kuolewa japo hakujua anaolewa na nani, pia alielewa kua kuna mtu ametumwa na baba harusi mtarajiwa kuja kuongea nae, Roho ilikua ikimuuma sana kwakua alishangaa ataolewaje wakati yeye ni mwanaume?, Masu akainua macho na kumuangali usoni huyuBi mkubwa ambae alikua Busy akimpodoa Masu a.k,a Shamsa

    “Unaniangalia nini hunijui? Shemeji anatakiwa mpaka mwenyewe ajilambe, na akikaa vibaya pita nae tu kwani kitu gani mwali wangu Hehee Haloo” Masu alizidi kupigwa na butwaakusikia maneno ya mama Yule ambae sasa alianza kumuelewa kua yuko pale kama Somo wake,

    “Naona umeshapendeza mtoto wa kike, haya naenda kumuita Shemejio ila sasa utulize kichwa uongee vizuri, sawa?”

    “Sawa..” Masu alikubali kishingo upande, kisha Somo akatoka nje



    Baada ya kama dakika mbili mlango ukagongwa, Masu akaa kimya tu mpaka ulipogongwa tena kwa mara ya pili ndipo akaitika

    “Karibu”

    “Ahsante” baada ya Masu kumkaribisha mgeni wake akaanza kuingia ndani mgeni Yule wakati huo Masu ameinamisha kichwa chini kwa hofu, mgeniyule ampaka alipokaa Masu na kumsalimia

    “Habari yako Shamsa” Masu akainua kichwa ili amjibu ndipo moyo wake ukafanya PAA!!! Hakuamini kilichokua mbele yake, Alikua Ni HUNUDU kutoka katika Dini ya Waufi

    “Hunudu???”

    “Ndio mimi Shem”

    “Hivi kwanini lakini umeamua kunitesa hivi?”

    “Hakuna anaekutesa, ila unajitesa mwenyewe, kama ungekubali kujiunga na Waufi na ukamtoa kafara mwanao mmoja wala tusingefika huku”

    “Kwahiyo mmeona suluhisho ni kunidhalilisha kiasi hiki?”

    “Hakuna anekudhalilisha, tumeamua kukugeuza jinsia na kukuleta huku katika ulimwengu mwingine ili uolewe kisha utuzalie mtoto ambae tutakuja kumtoa kafara, kisha kama Mumeo atakubali ukishajifungua akuache tukurejeshe katika maumbile yako ya awali sawa tutafanya hivyo japo sina uhakika kama atakubali maana jinsi mtoto ulivyoumbika ni balaa” Hunudu alikua akiongea maneno yake ya dhihaka huku akicheka kichinichini, Hakika Masu alikua amepatikana

    *****





    ILICHUKUA muda mrefu sana bila ya Masu kutoka bafuni, mzee Kikoko akapatwa na wasiwasi, ikabidi atoke mpaka nje, pale nje akamkuta Judith akiwa amekaa kwenye mkeka , kwakua Kikoko alikua hataki kuongea chochote na mkwe wake huyo akaenda moja kwa moja mpaka bafuni, alipofika bafuni akaanza kugonga mlango

    “Ngo! Ngo! Ngo!”

    Aligonga karibu mara tatu bila ya kusikia sauti ikimuitikia, akazidi kuingiwa na hofu, akawaza pengine Masu hakupendezewa na maamuzi yake ya kwamba aachane na mkewe na kwamba yeye(Kikoko) atawachukua wajukuu zake akina Zani na Fani kwa ajili ya kuwalea, Mzee Kikoko akaanza kuita kwa sauti

    “Masumbuko..”

    “We Masu!!”

    Hakuna sauti iliyomjibu, alipoangalia juu ya mlango wa bafuni kwa juu aliziona nguo alizokua amezivaa Masu zikiwa zimetundikwa hivyo inaonekana Masu yuko bafuni, sasa kwanini haitiki? Ni swali alilojiuliza mzee Kikoko bila ya majibu, ikabidi sasa amuite tu Mkwewe

    “We Mama Zani..”

    “Abee Baba..”

    “Hebu njoo” Judith akainuka pale alipokua amekaa na kuelekea kule lilipo bafu, hakujua anaitiwa nini ila tu alijua kua tayari kuna tatizo,

    “Huyu Masu ameshatoka bafuni?”

    “Hapana sijamuona kutoka”

    “Sasa mbona haitiki naona nguo zake tu?”

    “Mmmh labda amepatwa na tatizo” Hali ile pia ilimshtua sana Juddy, hofu ikamvaa, ikabidi amuite Mama Jay, ambae ndie mama mwenye nyumba ili wamueleze suala hilo, Baada ya mama Mwenye nyumba kutoka walimuelezea kila kitu, nae hofu ikamtinga, ikabidi sasa wakubaliane kuvunja mlango ili wamuangalie maana kila mtu sasa aliamini kua atakua ameanguka tu kutokana na kuzidiwa na hayo matatizo yanayomsibu maana watu wengi tu sasa mpaka majirani tayari walikua wameshaanza kujua kua Masu anasumbuliwa na vitu visivyoeleweka

    Mama mwenye nyumba akumuita kijana wake anaeitwa Jay ili ashirikiane na Mzee Kikoko kuuvunja mlango wa bafuni, muda wote huo mzee Kikoko alikua haoengei kitu, alionekana ni mwenye hofu kubwa, haikua kazi kubwa sana kuuvunja mlango ule kwakua ulikua umefungwa kwa ndani na kitasa kidogo tu hivyo Jay peke yake alitosha kuufungua mlango ule, Baada ya kuufungua tu wakaingia haraka Mzee Kikoko na Jay, Laa haula hapakua na mtu, Masu hakuwemo bafuni, Kikoko alichanganyikiwa maana nguo zote za Masu mpaka ile ya ndani kabisa zilikuwepo palepale kwa juu ya mlango lakini mwenye nguo haonekani, ingekua Choo na bafu viko kwa pamoja pengine wangeanza kuhisi kua huenda akawa ametumbukia kwenye shimo la choo, Mzee Kikoko akazichukua nguo za mwanae kasha akatoka nazo nje

    “Vipi Baba..?” Juddy aliuliza kwa hofu na woga huku mama Jay akiwa kasimama kwa pembeni

    “Kuhusu nini?” alijibu Kikoko kwa jeuri na hasira

    “Imekuaje?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “We usinifanyie mie mtoto wala mpuuzi mwenzio, umesikia?”

    “Jamani, sasa kukuuliza ni makosa?”

    “Unaniuliza nini?Wewe unajua vizuri Masu alipoenda utanieleza mpuuzi mkubwa wewe”

    “Lakini Baba mbona unaninyanyasa sana?”

    “Nakwambia hivi leo utanijua vizuri maana naona unataka kunizoea wewe, haiwezekani mtu ameingia bafuni halafu ghafla katoka bila wewe kujua wakati ulikua umekaa hapa hapa uani, inamaana kuna njia gani nyingine ya kutokea zaidi ya hii?” Mzee kikoko tayari alikua ameshachemka kwa jazba akatoa simu na kumpigia swahiba yake Sheikh Jabu akamueleza kila kilichojitokeza pale, Jabu akamuambia amsubiri huko hook Buguruni, baada ya Mzee Kikoko kukata simu tu akahamia kwa Judith akamfuta Juddy mpaka pale alipokua amesimama, akamkwida na kuanza kumpiga makofi huku akimtaka Juddy aseme Masu yuko wapi…

    “Baba mie unanionea bure, wala sijui Masu alikoenda”

    “Utanieleza tu nakwambia nitakuu mimi” Hali ile ilimtia sana uchungu mama Jay kuona mwanamke mwenzie ananyanyaswa kiasi kile bila ya sababu za msingi, akaingia ndani na kumpigia simu mume wake ambae ni askari polisi kituo cha polisi Buguruni na kumueleza juu ya tukio zima, kasha baada ya kumsikia Kikoko anaendelea kutoa kichapo kwa Juddy ikabidi atoke tena pale uani na kumvulia uvivu



    “Hivi we Mzee una matatizo ya akili?” Mama Masu aliongea kwa taharuki

    “Unanitusi mimi we mwanamke?”

    “Nakutusi ndio huna akili, mtu mzima hovyo kazi kuonea tu wanawake”

    “Naomba uwe na adabu nitakufata na wewe nikharibu sasa hivi huo mdomo wake”

    “Njoo uniharibu, nakwambia njoo, usinitishe nipo kwangu”

    “Huna hata haya wakiitwa wenye nyumba na wewe utatoka na hiki kibanda chako cha kuoshea maiti”

    “Wewe unayo? Ungekua nayo si ungempa mwanao akakaa kulioko kuja kupanga. Muone kwanza kwanzia zile sharubu zilivyomchachamaa” Kikoko akapata jazba akahamia kwa Mama Jay akamvaa ili aanze kumshushia kipigo lakini kabla hajafanya hivyo akazuiliwa na Jay ambae alikua akiangalia malumbano yale yakiendelea,

    Wakati hayo yakiendelea gari ya Polisi ikawa imepiga breki nje ya nyumba kisha wakashuka askari watatu, wawili wakiwa wamevaa kiraia na mmoja akiwa amevaa kikazi, wotw wakiwa na Bunduki wamezibeba mikononi, kisha wakaingia ndani na kukuta hali ile ya utata mule ndani kati ya mama Jay na Mzee Kikoko, huku Judith akiwa amesimama pembeni analia kwa uchungu

    “Habarini za saa hizi..” alisalimia mmoja kati ya wale maaskari polisi aliekua amevaa kiraia

    “Salama tu karibuni” alijibu Mzee Kikoko

    “Kuna nini tena mbona mmekwidana na huyu nae analia?”

    “Huyu mzee kampiga sana huyo mwanamke hapo halafu akawa anataka kunipiga na mimi?” alidakia mama Jay, ikabidi Yule askari amsogelee karibu Mzee Kikoko

    “Mzee imekuaje tena unapiga watu tena wanawake haogopi kupatwa na matatizo?”

    “We unaniuliza kama nani kwanza..”

    “Mimi ni ofisa wa Polisi kutoka kituo cha Buguruni”

    “Kwa ushahidi gani kwamba wewe ni askari?” alihoji mzee Kikoko bila ya kuonesha hata chembe ya Soni, Askari Yule nae akajaa hasira na kuanza kumbadilikia mzee Kikoko

    “Mzee naomba uwe na nidhamu, nitakunasa vibao sasa hivi, nikakuweke na ndani”

    “We unasemaje? Unipige vibao mimi? We unanijua mimi?

    “Nikujue ili inisaidie nini?”

    “Kama haikusaidii kitu umekuja kuingilia mambo yasiyokuhusu ili ikusaidie nini? Haya hebu thubutu kunipiga hata kibao kimoja uone nitakachokufanya, Hutopata hata kazi ya kupalilia hapa Dar” Kila mtu alibaki kashangaa jinsi Kikoko alivyokua akijibizana na maaskari bila ya hofu hata kidogo,

    “Nyie ni askari gani msiojua hata kujitambulisha kisheria? Taja jina lako, namba yako ya kazi, kitabulisho chako, nk” Yule afande akamuangalia sana mzee Kikoko kisha ikabidi Yule askari atoe Kitambulisho chake cha kazi akamuonesha Mzee Kikoko

    “Umeridhika eeh?”

    “Sio nimeridhika lazima utambue majukumu yako na ufuate taratibu za kazi yako, sasa usipojitambulisha nitakujuaje kama wewe ni askari? Kama ni hizo bunduki na sare hata majambazi wanazo, mie sio wa kijijini, mimi ni mtoto wa mjini”

    “Sawa mzee utaenda kutuonesha na hao majambazi wanaomiliki bunduki na sare zetu” Askari Yule alikua amekasirika sana,



    Wakati Mzee Kikoko anaendelea kujibizanana maafande hawa Sheikh Jabu nae akawa tayari ameshawasili na pikipiki yake akiwa amembeba Sheikh Mwinyigoha, Kikoko alipomuona Sheikh Jabu ndo akazidikupata kiburi lakini hakupata furaha kumuona Sheikh Mwinyigoha kutokana na malalamiko ya mwanae kua Mwinyigoha nae alikua ni mmoja wa wafuasi wa Dini ya Waufi

    “Habari zenu..” alisalimia Sheikh Jabu baada ya kuingia uani

    “Nzuri..” waliitikia kwa pamoja, wengine wakamuamkia

    “Poleni na matatizo jamani”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Matatizo ya kujitakia tu haya, huyu mwanamke anajua Masu alipo ila anataka kutuchezea tu vichwa” Mzee kikoko alijibu kwa hamaki ya hali yajuu

    “Hebu Bw Kikoko njoo faragha kidogo” Wakasogea pembeni Sheikh Jabu, Mwinyigoha, na Kikoko

    “Imekuaje tena mzee mwenzangu naona kuna polisi huku namuona mkweo analia, kuna nini hasa?”

    Kikoko akaanza kusimulia kila kitu kuanzia alipofikapale mpaka Masu alivyotoweka katika mazingira ya kutatanisha

    “Umefanya makosa makubwa Bw Kikoko” alijibu Sheikh Jabu baada ya kusikiliza maelezo ya Kikoko

    “Kivipi?”

    “Kwanza haukupaswa kuanza kuongea na Masu masuala ya kumuacha huyu mwanamke wake kwakua akili ya Masu bado haijatulia kabisa, Pili umefanya makosa kumpiga makofi huyo binti hiyo ni kesi kubwa ikifikishwa mahakamani inaweza kukuletea dhahama kubwa sana” Maneno yale yalimuingia sana Kikoko sasa akawa anaanza kujuta lakinitayari ameshatenda kosa na waswahili wanasema majuto ni mjukuu..

    “Mzee tunaomba tuelekee kituoni tafadhali..” Afande mmoja alimuita Kikoko ili waondoke nae

    *****



    Baada ya Masu(Shamsa) kuongea na Hunudu kwa muda mrefu Hunudu akatoka na kuaga kisha akaondoka zake, Shamsa alizidi kuumia sana kwa ndani. Alitamani wale kina mama wajue kua yeye ni mwanamke na wala haitwi Shamsa kama wanavyomuita, yeye ni Mwanaume na anaitwa Masu lakini hakuweza kufanya hivyo, alitamani hata ikiwezekana Baba yake na mkewe wangejua mahala alipo ili wamsaidie kumuokoa lakini haikuwezekana, alitamani angepata walau dakika moja tu kuonana na Mzee Kishindo ambae ndie alionekana kua mkombozi wake lakini haikua rahisi tena, Kikubwa zaidi kila akivuta picha kua sasa anatakiwa kuolewa wiki inayofuata ndio alitamani kupasuka lakini kila alipojaribu kujiangalia vizuri alikubali kua sio Mwanaume tena lakini aliendelea kupingana na ukweli huo!

    Alikaa mule ndani kwa takribani wiki mbili mpaka akayazoea Mazingira na kuwaelewa wenyeji wake, Yule Somo yake alikua ni Shangazi yake anaitwa Bi Habiba, pia alimjua Bi mkubwa mwingine kua ndie anaejulikana kama mama yake Mzazi anaitwa Bi Shammy. Maisha yaliendelea kusonga mbele kila siku alikua akifundishwa namna ya kwenda kuishi kwa mume, namna ya kumlea na kumtunza mumewe, nk.

    Siku moja zikiwa zimebaki siku mbili tu kufika siku ya harusi Masu(Shamsa) akiwa chumbani kwake waliingia watu watatu, Somo yake Bi Habiba na wadada wengine wawili ambao ukiwaangalia tu utajua kua ni magwiji wa unyago na ni watoto wa mjini haswa, mmoja anaitwa Nunuu alikua aemevaa kikuku mguu wa kushoto ile kiMombasa, na huyu mwingine anaitwa Shumbana, kama kawaida yao huja kumfunda mwali wao ambae ni Shamsa(Masu),

    Wakiwa wanaendelea na mafunzo yao yaliyojaa mambo ya ajabu ajabu kama muwajuavyo tena Makungwi walikua wakimpa somo Masu(Shamsa) huku wakifanya vitendo kabisa, Masu aliumia sana na mambo yale ghafla

    “Jamani lakini mnanifanyia hivi mjue kua mimi si mwanamke, mimi ni Mwanaume kabisa”

    “Unasemaje wewe?” aliuliza kwa ukali Bi Habiba huku wake madada wengine wakionesha mshangao mkubwa kutokana na maneno aliyoyatoa mwali wao

    “Ndi hivyo, mie Siwezi kuolewa, mimi ni mwanaume” Basi kwa hasira Bi Habiba akainuka kwa jazba mpaka pale alipokua amesimama Masu kasha akamvua kwa nguvu ile kanga aliyokua amejifunga, Masu akabaki kama alivyozaliwa kasha Bi Habiba akamuuliza

    “Haya jiangalie una uanamume gani?” baada ya Bi Habiba kusema hivyo wale wapambe wakacheka kwa sauti za kishangingi, kasha Nunuu akadakia

    “Dada Habiba kua makini, makungwi wenzio watakua wameshafanya yao hapo haiwezekani ghafla mtoto wakike aseme ahataki kuolewa eti ni mwanaume…”

    “Hakuna cha kuchezewa wala nini ni huyu huyu mpuuzi tu anataka kutuharibia shughuli, na hii si mara yake ya kwanza alishakataa kuolewa zaidi ya mara mbili huyu, ngoja tu nimuite Mama yake Bi shammy aje amalizane nae mie nimeshachoka na vioja hivi” Bi Habiba akatoka nje kumuendea Bi Shammy, hawa wadada nao wakatoka nje wakamuacha Masu(Shamsa) akiwa amesimama chumbani kama alivyozaliwa, walipotoka tu nae akainama akachukua kanga yake na kujifunga upya akijua sasa kua mambo yameshavurugika,

    Baada ya muda mfupi mlango ukafunguliwa, Masu akajua sasa balaa tayari limeshamfika, lakini aliponyanyua macho yake akakutanisha na macho yako na HUNUDU, Akataka kutaharuki Ila Hunudu akamsogelea na kumuuliza Masu

    “Ndo umefanya nini sasa?”

    “Kivipi?”

    “Kwanini umewaambia kua wewe ni mwanaume?”

    “Kwakua kweli mimi ni mwanaume, siwezi kuolewa”

    “Sasa hiyo ni hatari kwako, huyu Mama atakufanyia kitu kibaya sana”

    “Basi kama mmeamua kunimaliza nyie nimalizeni mmenitesa vya kutosha”

    “Khaa, yaani na wewe unajiona umeteswa? Tutakapoanza kukutesa si hautoamini”

    “Lakini Hunudu kwanini mnanifanyia hivi?”

    “Kwa sababu ya dharau na kiburi chako, na utateswa zaidi muda ukifika, taka usitake utaolewa tu na utazaa tu na kisha ndo mateso yataanza rasmi” Masu alijaribu kumuomba Hunudu amsaidie, Hunudu hakua na shida hata ya kumuangalia Masu usoni lakini baada ya Masu kulalamika sana Hunudu alimuahidi kumsaidia asipate tabu endapo tu kama atakubali kuolewa au Laa sivyo akubali kumtoa mwanae mmoja ndipo atarejeshewa maumbile yake ya kiume na kua huru huku akiwa ni mwanachama wa dini yao ya WAUFI, Kutokana na matatizo kumfika shingoni Masu akakubali kutekeleza matakwa ya Hunudu

    “Hii ni nafasi ya mwisho kwako, ukitoa siri na kuvuruga utaratibu sitakuvumilia tena, sawa Masu?”

    “Sawa mkuu”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ninakurejesha katika maumbile yako ya kiume na kisha nitakuchukua mpaka kwa Mkuu wetu ili ukaungame uovu wako.. halafu nitakurejesha duniani” Baada ya makubaliano hayo, Hunudu akatoa Pete katika mfuko wa suruali yake na kumvisha Masu katika kidole chake cha kati

    Baada tu ya kumvisha ile Pete Masu akajishanga ghafla anaanza kubadilika na kurudi katika maumbile yake ya awali, lakini ghafla akaanza kujisikia vibaya mwili mzima, mara kichefuchefu, mara kizunguzungu, yaani akawa taabani kama mtu anaekaribia kukata roho, Masu akajikua anaishiwa nguvu mwishowe akaanguka chini kama mzigo, wakati huo Hunudu alikua akiendelea kumtazama tu bila ya kumsaidia chochote bila shaka alikua akijua alichokifanya ndani ya Pete ile, Masu aljaribu kutaka kumuomba msaada Hunudu lakini mdomo ulikua mzito kutamka maneno huku akitokwa na udenda, ikabidi amuoneshe kwa Ishara kua anamuomba msaada Lakini Hunudu alionekana kutabasamu kwa dharau tu, Masu aliendelea kutapatapa bila msaada wowote mpaka akaanza kuhisi kupoteza fahamu, na kweli baada ya kama dakika mbili Masu akapoteza fahamu..

    Akawa kama alietoka usingizini bila ya kujua yuko wapi, Masu alijikuta akiwa Juu ya maji, katika kati ya bahari akiwa peke yake, Hofu ilimuingi sana mwilini, alijaribu kuangaza huku na kule lakini hakuona mtu yoyote, alikua amevaa nguo nyeupe tupu, nguo zake zilikua ni nyepesi mno kiasi cha kumfanya ahisi baridi kali lililotokana na upepo mkali wa baharini, Hakika Masu alikua kama chizi vile maana hakuna alichokielewa, ghafla kwa mbali aliwaona watu kama watano hivi nao wakiwa wamevaa nguo nyeupe, dalili zao zilionyesha wanakwenda usawa ule aliokuwepo yeye, Masu akachanganyikiwa akaamua kuondoka eneo lile huku akikimbia ghafla alipogeuka aliwaona vijana wale nao wakimkimbiza kwa kasi ya ajabu, alijitahidi kuongeza kasi ya kukimbia lakini vijanawale nao walizidi kumkaribia, alipoangalia mbelea aliona mnyama mkubwa mithili ya Kiboko lakini hakua kiboko, nae mnyama huyo alikua akikutana sasa uso kwa uso na Masu, Mnyama huyo alikua akiunguruma kwa sauti kali

    kama Radi vile, Masu alipomuona mnyama Yule akajikuta anapiga kelele hovyo kama mwendawazimu

    “Uwiiiiiiiiiiiiiiii, Nakufaaaaaaaaa”

    Ghafla akajikuta ametokea tena kule Bafuni kwake alikokua anaoga mara ya kwanza, Masu hakuamini kama amerudi huku tena, alikua anahema kwa nguvu sana,

    *****



    Mzee Kikoko na Sheikh Jabu walikua wakijadiliana nini cha kufanya ili ile kesi isifikishwe Polisi ndipo ghafla wakasikiahiyo Sauti kali ya Masukutoka Bafuni, wote wakashtuka, hawakutegemea kusikia sauti ile, haraka wakakimbilia kule bafuni wakiwa pamoja na wale maaskari, na kweli wakamkuta Masu akiwa amesimama, kila mtu aliogopa kumsogelea, maana ilikua ni kama mazingaombwe vile, hata maafande wale walioonekana kua ni majasiri nao walipigwa na butwaa, hakuelewa kabisa kinachoendelea,

    Safari hii Masu alikua amevaa nguo nyeupe alizotoka nazo kule baharini, kidoleni alikua na ile Pete aliyovishwa na Hunudu, Sheikh Jabu alijikaza na kumshika mkono kisha akamtoa nje ya bafu, Masu bado alikua hajielewielewi wala haelewi amefikaje tena huku ghafla kiasi kile

    “We Uliku wapi?” aliuliza Mzee Kikoko lakini swali lake lilikatizwa na Sheikh Jabu

    “Bwana Kikoko huu sio muda wa kuongea mambo hayo” Jabu akamshika mkono Msu mpaka ndani huku nyuma akifuatwa na Mzee Kikoko na sheikh Mwinyigoha, baada ya kufika ndani na kuketi ndipo Sheikh Jabu akamuuliza Masu

    “Vipi umeshakula?” Masu alijibu tu kwa kutikisa kichwa kua ameshakula

    “Ehnhee imekuaje tena?” Jabu alikua akimuuliza Masu maswali kwa mitego ya hali ya juu, lakinikabla Masu hajajibu kitu macho yake yakapiga kwenye kidole cha sheikh Mwinyigoha, Naam akaona Pete kubwa nyekundu, alipojiangalia kwenye kidole chake akagundua ni pete kama aliyoivaa yeye, ni PETE ya waufi

    “Noooooo” Masu alipiga kelele huko akmsonta sheikh Mwinyigoha, watu wote walitahayari, viti vikawa vichungu wakasimama juu, lakini Sheikh jabu alikua ni jasiri sana aliendelea kumshika tu masu huku akimuhoji

    “We una tatizo gani?”

    “Huyu mzee hafai, si shekh huyu, ni mfuasi wa Waufi”



    BAADA ya Masu kumtuhumu sheikh Mwinyigoha kua nae ni mmoja wa wafuasi wa Dini ya Waufi kila mmoja akapigwa na butwaa, lakini kabla hawajamjibu chochote Masu akendelea kusema

    “Hiyo Pete aliyoivaa ni kama hii yangu, zote ni za Waufi” Mzee Kikoko akashtuka, akamuangalia usoni Sheikh Jabu, kasha kwa pamoja wakamuangalia kidoleni Sheikh Mwinyigoha lakini cha ajabu hawakuiona hiyo Pete

    “Pete gani tena Masu? Mbona hana Pete yoyote” Sheikh Jabu aliongea kwa utulivu kiasi,

    “Jamani pete si hii hapo tena ni kubwa tu inaonekana vizuri” Masu alipomuangalia Mwinyigoha akaiona pete ile kidoleni, sasa ikawa ni kama muujiza yaani Masu anaiona ile pete lakini wazee wake hawaioni, Mzee Kikoko akawa anatikisa kichwa kwa unyonge kabisa akiamini kua sasa mwanae amaeanza kuchanganyikiwa, wakati wote wakiwa wamepatwa na mfadhaiko Masu akawaponyoka na kutoka nje

    “Sasa unaenda wapi wewe Masu” alihoji Mzee Kikoko lakini masu hakujibu kitu akaondoka kwa kasi.. Hali ya simanzi ikazidi kutamalaki pale nyumbani kila mtu sasa aliamini kua Masu amechanganyikiwa

    “Itakua Masu amechanganyikiwa tu” alisema Sheikh Mwinyigoha

    “Hapana, Masu ni mzima kabisa ila hapa kuna jambo tu, tena kubwa sana” alidakia Sheikh Jabu

    “Ni jambo gani sasa lisilojulikana?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Cha kujiuliza ilikuaje Masu akapotelea Bafuni, kisha akarudi ghafla akiwa amevaa nguo zingine?”

    Kabla Mwinyigoha hajajibu ghafla akadakia Yule Askari polisi huku akimuangalia usono Judith mke wa Masu “Tena akiwa na Pete kubwa, au hua anayo siku zote?”

    “No, sijawahi kumuona nayo hata sikumoja” alijibu Judith huku akitokwa na Machozi

    “No ndio nini sasa? Ongea Kiswahili ueleweke, unataka kuleta nyodo za kizungu hapa wakati mmeshamroga mwanangu, na wewe ndo chanzo” Kikoko alimkaripia Juddy mpaka kila mtu akashangaa maana hapakua na haja ya kuleta mada mpya

    *****



    ‘Ngo! Ngo! Ngo’



    Mlango wa mbele uligongwa kwa nguvu sana, ni maeneo ya Tabata Matumbi, nyumbani kwa mzee Kishindo, wakati huo Mzee Kishindo alikua chumbani akimalizia kuswali hivyo hakuweza kujibu hodi ile, akaendelea tu kuswali lakini kelele za kugongwa kwa mlango zilimshtua sana maana mlango ulikua ukigongwa kwa nguvu bila shaka palikua na mtu aliekua na shida ya haraka sana au mtu aliekuja kiushari vilivyo,



    “Mzee Kishindo! Mzee Kishindo!”



    Japo Mzee Kishindo hakumjibu kitu kwa kuhofia kuharibu swala yake kwani kwa mujibu wa dini yake hakupaswa kuacha kusali na kumjibu mtu lakini tayari alikua ameishaing’amua sauti inayomuita, Naam ilikua ni sauti ilyojaa mchoko na hofu, ni sauti ya MASUMBUKO. Baada ya kumaliza kuswali Mzee Kishindo akaenda mpaka kwenye mlango wake akaufungua taratibu ili achungulie nje ndipo ghafla Masu akaingia kwa kasi ndani huku akitweta, Mzee Kishindo alijikaza japo alikua nae ameshtuka kwa hali aliyokua nayo Masu ikabidi tu aurudishe mlango akihofia kujifungia nae ndani, alipomgeukia Masu alikua akilia sana kwa uchungu

    “Unalia nini Masu?” alianza Mzee Kishindo kwa kumtupia swali Masu

    “Mzee Kishindo, ninateseka sana, napitia kila aina ya taabu, Waufi wataniua” Baada ya Masu kujibu vile Mzee kishindo alikua amesimama wima, akamsogelea mpaka pale alipokua ameketi nae akaketi pamoja nae

    “Pole sana mwanangu”

    “Sijapoa hata kidogo”

    “Nadhani unakumbuka nilishakudokeza kua tatizo lako ni kubwa sana..”

    “Ndio nakumbuka, na ndio maana nimekimbilia kwako unisaidie”

    “Natamani sana kukusaidia ila baba yako mzee Kikoko anasumbua sana, ananitusi mbele za watu na kusema kua mimi ndie ninaekuroga na ananipa kila aina ya vitisho kwa ajili yako, unakumbuka nilikuuliza kua una kifua? Ukasema ndio, sasa ikawaje tena hata kabla sijakuelezea ukaanza kuvujisha habari mpaka zikamfikia baba yako na sasa unanileyea tabu mie?”

    “Mzee Kishindo huu sio muda wa kulaumiana kabisa, kwa sasa nahitaji tu msaada wako, pia mimi sijamueleza chochote baba ila nadhani ni mke wangu tu huyo kwakua walimbana sana baada ya mimi kuanguka” Baada ya maelezo hayo ya Masu Mzee Kishindo akainuka na kutoka uani kwake akamuacha Masu peke yake pale Sebuleni, Kisha baada ya muda mfupi Mzee Kishindo akarudi akiwa amebeba sahani mbili ya chakula, moja akampa Masu alionekana kua na njaa sana na nyigine akawa nayo yeye mwenyewe mkononi..

    “Kula kwanza upate nguvu mpya” aliongea Mzee kishindo

    “Ahsante lakini mie nimeshiba”

    “Hujashiba chochote zaidi ya kuvimbiwa na hofu tu, kula ukimaliza tufanye mazungumzo” Basi Masu japo alijisikia kushiba ikabidi tu aanze kula hivyo hivyo ili kumridhisha Mzee Kishindo aweze kumpa msaada maana Mzee hyu ndie anaeonekana kujua kila kitu kuhusiana na tatizo la Masu kulazimishwa kujiunga na Dini ya Waufi, Iliwachukua takribani dakika karibi ishirini wakawa wamemaliza kula na tayari mke wa Mzee Kishindo alikua ameshawasogezea maji ya kunywa na kunawa. Baada ya kumaliza kunywa maji na kunawa ndipo mazungumzo yakaanza tena



    “Hebu nihabarishe kwa mukhtasari mambo yako yakoje” alianza mzee Kishindo

    “Mkasa wangu ulianzia kwenye ndoto, kuna siku nilikua nimelala…”

    “Hapana huko unaanzia mbali ulishanihadithia tukiwa kule dukani, sasa anzia tangu baada ya pale” Kishindo alimkatisha Masu, maana Masu alikua ameshamsimulia jinsi tatizo lake lilivyomuanza, ikabidi sasa Masu aanzie pale alipokutana na Hunudu kwa mara ya kwanza ikiwa ni nje ya Ndito, ilikua ni stori ndefu nay a kuogofya sana, Masu alikua akiihadithia kwa uchungu mpaka anadondosha machozi, Mzee Kishindo alikua akimbembeleza huku akimfuta machozi mpaka akamalizia tukio la mwisho kule bafuni

    “We ni motto wa kiume hivyo achana na mambo ya kulia hovyo, jikaze hii sasa ni vita umeivaa”

    “Sawa Mzee”

    “Pili nakupongeza kwa ushujaa wako na ujasiri wa kua kila jambo unalisema wazi japo huyo Hunudu anakutishia kua usitoe siri maana ungemtii tu masharti yake ndio ingekua mwanzo wa kukutawala” Masu sasa akawa anamsikiliza kwa makini Mzee Kishindo akiamini kua huenda akapata ukombozi

    “Ulishajiuliza kwa nini uliitwa Masumbuko wakati kwenu hakuna hata mmoja katika babu zako aliewahi kuitwa jina hilo?”

    “Hapana”

    *****



    TABORA

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwaka 19970 ndipo bwana Rashid Kikoko alipohamia rasmi mkoani Tabora akitokea kwao Kigoma, na alipofika tabora alikua akijishughulisha na biashara ya kuuza samaki na dagaa aliokua akiwatoa Kigoma na kuwaleta Tabora, biashara yake ilikua nzuri mno, ilimpa faida nzuri na kubwa, ndani ya muda mfupi tu maisha yake yakawa mazuri nay a kuridhisha, akiwa Tabora alikutana na wazee na vijana wenzie kutoka kigoma ambao wanaishi hapo Tabora huku wakijishughulisha na masuala ya kiutafutaji… Kikoko nae alifanya Biashara zake kwa takribani miaka minne mpaka mwaka 1974 alipokwenda kwao Kigoma kufuatia wito alioitwa na Baba yake mzazi..



    Baada ya Kikoko kurudi Kigoma kuitika wito wa baba yake alikutana na baba yake huyo Mzee Hassan Kikoko, kikubwa alichoitiwa alitakiwa sasa Aoe maana umri wake ulikua ni mkubwa na pia uwezo wa kifedha alikua nao, japo alijaribu kutaka kuleta vipingamizi lakini alizidiwa na hoja za baba yake mzazi hivyo ikabidi tu akubali kuoa, Bw Kikoko alirudi mjini Tabora kujipanga kwa ajili ya kutafuta mchumba ndipo akakutana na Bi Kapemba Masanja kutokea Shinyanga nae alikua ni mfanyabiashara akiendea vitenge vya wax huko Bujumbura na kuja kuviuza Kigoma, Tabora, na Shinyanga kwao, Kikoko hakua na pingamizi kua amezama katika huba kwa dada huyo.



    Mwaka 1975 Bw Kikoko na Bi Kapemba wakafunga ndoa huko Shinyanga na kisha harusi ikaenda kumaliziwa Kigoma kwa baba yake na Kikoko, ilikua ni sherehe kubwa na ya kifahari, kila mtu aliburudika na kufurahikia harusi hiyo, baada ya sherehe za harusi Kikoko akarudi tabora alikokua ameweka makazi yake ili kuendelea sasa na utafutaji wa Riziki, Maisha ya ndoa yalikua mazuri kwao na miaka alikatika wakiwa na furaha. Tatizo Kubwa lilianza kuchomoza kama uyoga kwenye Kichuguu kutokana na Bi Kapemba kutopata ujauzito. Naam mpaka mwaka 1977 takribani mitatu baada ya ndoa bi mkubwa huyo hakupata ujauzito. Hivyo sasa ndugu zake na Mzee Kikoko wakaanza kuleta ghasia za chini kwa chini na hatimae ghasia zikaota mbawa na kutanda katika anga la huba kati ya Mzee Kikoko na Bi Kapemba. Wenyewe walijitahidi kuyapuuza malalamiko ya ndugu huku wakipambana kutafuta tiba kwa kila mganga mashuhuri waliesikia habari zake, lakini jitihada hazikuzaa matunda, ndipo sasa baba yake na Kikoko

    akamuamuru Kikoko aoe mke mwingine ili ampatie watoto kwa kua Bi Kapemba ni Mgumba



    Mwaka 1979 kwenye mwezi wa kumi na moja hivi, nakumbuka ilikua ni karibu na mfungo wa Mwezi wa Ramadhani hivi Bw Kikoko ilibidi tu sasa Aoe mke mwingine baada ya mikwara ya haja kutoka kwa familia yake, Alimuoa msichana fulani ambae huyu alikua ni mzawa na mwenyeji wa mkoani Tabora, aliitwa Bi Mwajabu Fundikira, ukoo wa Bi mdogo huyu ni ukoo wa kitemi hivyo ulikua ni ukoo ulioheshimika sana pale mkoani Tabora, akatekeleza suala hilo la kuoa lakini hakumuacha mkewe mkubwa Bi Kapemba Masanja, akawa sasa ana wake wawili, wote akiishi nao tabora. Maisha yakasonga mbele bila ajizi, Kikoko alijitahidi sana kuwaunganisha wakeze hao ili waishi kwa kupendana na kufurahiana, alijitahidi kwa kiasi Fulani kukawa na amani japo matatizo ya chichini hayaepukiki ila yalipojitokeza alijitahidi kuyatatua kwa ustadi wa hali ya juu



    Naam mwaka 1980 ndoa ikajibu, Bi Mwajabu alipata ujauzito ilikua ni kwenye mwezi wa kwanza hivi yaani miezi mitatu hivi baada ya kuolewa kwake, kila mmoja alifurahia suala hilo, habari zikafika mpaka Kigoma nyumbani kwao na Kikoko nao wakafurahi sana, Lakini hali ikawa tofauti kwa Bi Kapemba kwa kua yeye hakujaaliwa kupata ujauzito hivyo alijiona kama mzigo, lakini Mzee Kikoko aliendelea kumfariji mkewe huyo bila ya kumtenga, ilipofika kwenye mwezi wa tano na ujauzio wa Bi Mwajabu ukiwa nao na miezi mitano, ghafla Bi Kapemba akaomba ruhusa kwa mumewe ambae ni Mzee Kikoko ili akapumzishe akili kidogo nyumbani kwao Shinyanga ikiwa ni pamoja na kwenda kuwasalimu wazazi wake, Mzee Kikoko alimkubalia, akamuandalia safari na kasha wiki moja baadae akaondoka na kwenda Shinyanga..



    CHA AJABU, Ilipofika kwenye mwezi wa sita ghafla hali ya Bi Mwajabu ikaanza kubadilika, kila siku lile tumbolake la ujauzito likaanza kuyeyuka mithili ya pulizo lililotoboka na hatimae ujauzito ukatoweka kabisa, ilikua ni tukio la ajabu sana sit u kwa familia ya Bw Kikoko bali hata kwa baadhi ya majirani na wakazi wa mkoani pale, habari zilizagaa mji mzima, kila mtu alisema lake. Walipomuhoji Bi mkubwa huyo akasema aliondoka akiwa mjamzito ila tyeye alikua na tumbo dogo lisiloonekana kiurahisi, Ikabidi sasa Kikoko ampeleke mkewe Hospitali lakini nako vipimo vikaonesha kua hana ujauzito kabisa.. wiki mbili baada ya tukio hilo Bi mkubwa(Bi Kapemba) karejea tabora, kilichowashangaza wengi mpaka mzee Kikoko mwenyewe ni kwamba Bi Kapemba alirudi na Ujauzito mkubwa wa miezi kama sita hivi, hakuna alieaminikua tukio lile linatokea dhahiri lakini huo ndio ulikua ukweli wa mambo, yaani Ujauzito umetoweka kwa Kwa Bi mdogo na ghafla umehamia kwa Bi Mkubwa, Sulahilo

    lilizua zogo kubwa na hatimae wakaanza kushikana uchawi



    Ndugu zake na Bi Mwajabu walienda kwa waganga wakaambiwa kua Bi Kapemba aliinyakua kichwawi mimba ya mwenzie na kuihamishia kwake kwa kua hakua na uwezo wa kushika ujauzito na hapo ndipo ikafahamika kua Bi Kapemba amefanyiwa hivyo na mizimu ya kwao Shinyanga, unaitwa MZIMU WA WAUFI, Ni mzimu mkali sana na wenye nguvu hivyo sasa yakaanza mapambano ya kimizimu kati ya Mzimu wa Waufi wa kwao na Bi kapemba na Mzimu wa WASWEZI wakwao na Bi Mwajabu Fundikira, mpambano ulikua ni mkali sana kila siku ndani mauzauza, ushirikina, vurugu, nk lakini hatimae mwaka 1980 Bi Kapemba akajifungua motto wa kiume, na kutokana na tabu, shida, na mkasa ho ndipo wakampa jina la MASUMBUKO, Japo Bi Kapemba ndie aliejifungua lakini Bi Mwajabu alisema hakika Yule ni mwanae na ni damu yake hivyo hatokubali kamwe..

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Familia zilijaribu kukaa na kufanya suluhu ili kwakua mambo haya yanautata mkubwa waweze kuiyamaliza, ilikua ni suala gumu sana lakini hatimae waliridhiana kishingo upande huku kila mmoja akibaki na lake moyoni, inasemekana wakati Bi Kapemba alipokwenda Shinyanga Mizimu ya kwao iliinyakua kichwawi mimba ya Bi Mwajabu na kuihamishia kwake kisha wakampa sharti kua ni lazima atoe kafara ya damu haraka iwezekanavyo Laa sivyo watamchukua Masu wao na Pia walimtaka Bi kapemba kua Masu akifikisha miaka kumi ampeleke ili akaingizwe rasmi kwenye Ukoo wao chini ya Mizimu ya Waufi kwakua hakua damu yao lakini hakufanya hivyo….



    ***Mnh! Mambo hayo!



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog