Search This Blog

JINI WA KUZIMU - 2

 





    Simulizi : Jini Wa Kuzimu

    Simulizi : Safari Ya Kuzimu

    Sehemu Ya Pili (2)



    ILIPOISHIA JANA...

    Pamoja na matumaini ya kusaidiwa lakini bado alijiwa na wasiwasi juu ya suala la kutimiza masharti aliyoahidiwa na Husna. Alimuuliza sababu ya kuwepo kwa masharti hayo wakati amesema kuwa Baba yake yupo tayari kumfanyia chochote anachokitaka. Husna alimueleza Yasini kuwa masharti aliyotaka kumpa yalikuwa ni yakwake na sio ya baba yake. Alimwambia kuwa asiwe na wasiwasi kwasababu hayakuwa masharti magumu lakini pia hayakuwa mepesi.

    SASA SONGA NAYO YA LEO...CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Jana ulipata barua yangu?” Husna alimeza funda la mate kisha akaendelea.

    “naomba utambue kuwa siku ya jumanne itakuwa ni siku ya mapumziko kwako. Usithubutu kufanya kazi siku kama hiyo” Husna alimaliza na kumfanya Yasini kushtuka baada ya kusikia maneno yale.

    “Inamaana ile barua uliandika wewe?” Yasini aliuliza kwa wasiwasi baada ya kukumbuka maneno aliyoyaona kwenye ile barua aliyoiokota janayake jinsi yanavyowiana na maneno ya Husna. Alishindwa kuelewa kwanini Husna aliiweka ile barua kwenye njia ya kisimani, na alijuaje kama yeye kwa wakati ule angepita njia ile, na alikuwa na uhakika gani kama ile barua imemfikia. Wakati Yasini akiendelea kujiuliza maswali hayo, Husna alimgutusha kwa kumuongelesha.

    “usiogope bwana, wewe ni mwanaume. Hivi ni vijimambo tu” alisema Husna na kusimama tayari kwa kuondoka.

    “Sasa mimi ngoja nikuache, lakini nitarejea baadae ili tuweze kuongea vizuri” Alisema Husna na kumuacha Yasini akimtazama pasipo kummaliza. Yasini Aliendelea kumkodolea macho Husna hadi alipotoweka kabisa kwenye mboni ya macho yake. Moyoni alianza kuwa na mashaka juu ya Husna kutokana na maongezi yake.

    ****

    Hadi ilipotimia saa mbili usiku, Husna alikuwa bado hajatokea kama alivyoahidi mchana. Yasini alikata tamaa na kuamua kwenda kulala. Alijifungia mlango kwa ndani na kujitupa kitandani. Alijipindua huku na kule lakini hakupata usingizi. Wakati wote alikuwa akimuwaza Husna ambaye ndiye pekee aliyebakia kama tegemeo lake. Ingawa sharti alilopewa mchana lilimtia wasiwasi lakini aliona ni upuuzi na kuendelea kujipa moyo.

    Yasini alibaki macho hadi mida ya saa saba usiku. Nje hali ya hewa ilibadilika, upepo mkali ulikuwa unavuma na sauti za vitu vilisikika vikianguka. Baada ya dakika kadhaa alianza kusikia sauti za ajabu ajabu humo chumbani mwake. Alisimama na kuziba masikio lakini haikusaidia kitu kwani bado alizisikia. Harufu kali ya mafuta mazuri ilizikumba pua zake, hata hivyo alibaini kuwa harufu ile ilikuwa ni ya mafuta aliyokuwa akipaka Husna.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mambo yalizidi kuwa magumu kwa Yasini mara baada ya taa yake ya kandili kuwaka yenyewe. Alitupa macho mlangoni kuona kama kuna mtu ameingia lakini alichokibaini ni kuwa mlango ulikuwa umefungwa na hapakuwepo na mtu mwingine zaidi yake mle chumbani. Aliisogelea kandili ile na kuizima, lakini alipo rudi kitandani ile kandili iliwaka tena. Aliifuata tena kwa lengo la kuizima kwa mara nyingine kuizima lakini ilisogea mbele kumkimbia. Aliongeza mwendo ili kuweza kuidaka lakini alishindwa kwasababu kandili pia iliongeza mwendo kumkimbia. Mara akasikia sauti za watu wakicheka humo chumbani.

    Yasini alipoona mabo yanazidi kuwa magumu alishindwa kuvumilia akataka kupiga kelele ili kuomba msaada, lakini alisita baada ya kumuona Husna akiwa amesimama huku ameweka kidole mdomoni kumuashiria asithubutu kupiga kelele. Wakati huo zile sauti za ajabu ajabu na vicheko vilikuwa vimekoma. Hali ilikuwa shwari hapakuwepo tena na upepo nje wala chumbani. Kilichosalia kilikuwa ni harufu ya mafuta mazuri pamoja Husna. Aliamini kuwa Yule hakuwa Husna, kwani Husna aliyemfahamu yeye asingeweza kufanya vitu vya ajabu kama vile.

    Aalijikuta akitetemeka huku macho akimkodolea yule msichana aliyekuwa amefanana na Husna ambaye alikuwa akimsogelea taratibu pale kitandani alipokuwa amekaa.

    “Usiniogope Yasini, mimi siwezi kukudhuru” alisihi msichana yule kwa upole

    “Wewe ni nani?” Yasini akahoji kwa woga huku akitetemeka.

    “Wacha utani Yasini. Kwani we unaniona mimi ni nani?”

    “Sikujui”

    “ Usiletemasihara yako bwana. Mchana nilikwambia nitarudi, na sasa ndio nimekuja”

    “Wewe ni Husna?”

    “Haswaaa”

    “Umeingilia wapi?”

    “Mlangoni”

    “Mlango gani wakati nimefunga kwa ndani?”

    “Wacha maswali Yasini, ngoja nikuoneshe kitu” Husna alifungua pochi yake iliyokuwa kwenye mkono wake wa kushoto na kutoa pete ya shaba. Aliushika mkono wa Yasini na kumvisha kwenye kidole cha kati kisha akaichomoa na kuirudisha kwenye pochi…

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/





    Ghafla Yasini woga ulimwisha na kumuona Husna mtu wa kawaida.

    “Lakini Husna wewe ni mtundu sana” Yasini aliongea akiwa hana hata chembe ya woga.

    “Kwanini unasema hivyo?”

    “Sasa umeingilia wapi?” Alihoji Yasini huku akimvuta Husna akae kitandani.

    “Hapana Yasini mimi sitakaa hapo kitandani, ngoja nikae kwenye hii meza” Husna alikaa juu ya meza akimgeukia Yasini. Walitazamana kwa sekunde kadhaa kisha kila mmoja akatoa tabasamu.

    “Unajua Yasini mimi ninauwezo mkubwa sana. Naweza kufanya kitu chochote ambacho binadamu wa kawaida hawezi kujaribu”

    “Hongera sana Husna, kwa kweli umebarikiwa”

    “Ahsante, lakini hembu tuwachane na hayo kwanza na tuongee kilichonileta” Husna aliongea huku akijisogeza na kukaa vizuri pale juu ya meza.

    “Sawa mi nakusikiliza”

    “Baba amekubali kukusaidia”

    “What! Unasema kweli Husna?”

    “Hiyo ndiyo habari”

    “Ahsante sana Husna” Yasini alijikuta akimkumbatia Husna huku akimimina shukurani

    zake.

    “Usijali, lakini unakumbuka mchana nilikwambia kuwa unatakiwa kuwa Jasili?”

    “Usijali Husna hilo sio tatizo”

    “Baba anataka kukukabidhi mwenyewe hizo pesa za shule. Amekataa kunipa mimi nikuletee” Husna alisema.

    “Hakuna tabu ”

    “Unatakiwa kwenda kuonana nae leo”

    “Unamaana tunakwenda kwenu saa hizi?”

    “Hapana, hatwendi nyumbani. Amesema anakusubiri Mzizima”

    “Kwahiyo tutakwenda mimi na wewe pekeetu?”

    “Wewe na nani? Unakwenda pekeyako”

    “Thubutuuu! Mimi siendi Mzizima pekeyangu usiku huu, labda kesho”

    “Wacha ubishi Yasini, unatakiwa uende leo” Husna alisisitiza.

    “Husna, nimekwambia siendi kokote usiku huu” Yasini naye aliendelea kuwa na msimamo. Waliendelea kubishana hadi Husna alipotoa pete yake tena na kumvisha kwenye kidole kilekile cha katikati, safari hii aliiacha palepale kidoleni. Baada ya hapo Yasini alijikuta woga wote umemwisha. Akakubali kwenda Kwenye bonde la Mzizima kuchukua hizo pesa kwaajili ya shule. Alipewa maelezo na Husna jinsi ya kufika huko.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Husna alimuonya Yasini kutojishughulisha na chochote ambacho angekiona njiani. Alimwambia kuwa baada ya kuzipata hizo pesa arejee nazo hapo nyumbani ambapo angempa maelekezo zaidi. Kisha akaongeza kuwa ile pete aliyomvisha ingekuwa kinga kwake, adui yeyote asingeweza kumdhuru endapo akimnyooshea kidole chenye ile pete. Wakaagana na safari ya kuelekea kwenye Bonde la Mzizima ilianza rasmi.

    *****

    Yasini alifungua mlango na kutoka nje, akanganza kulia na kushoto lakini hakuona mtu yeyote zaidi ya giza nene lililokuwa limeipamba anga. Alikamata njia ya kuelekea kwenye Bonde la Mzizima, aliteremsha kwenye mlima wa Mdundiko na kupandisha kuelekea Mjimpya. Kwa mbali aliona moto ukiwaka maeneo ya makaburi ya Mjimpya. Alikumbuka maneno aliyoambiwa na Husna kuwa endapo angekutana na maadui au vitu visivyo eleweka ni pete pekee ambayo ingeweza kumlinda. Aliuinua mkono wake na kuitazama ile pete, akaibusu na kisha akaendelea na safari kuelekea kule kulikokuwa kunawaka moto.

    Alipofika kwenye yale maeneo ya makaburi, alikuta watu wengi wanacheza ngoma huku wakiwa kama walivyozaliwa. Watu hao walikuwa wakipiga ngoma na kucheza kuuzunguka moto, kuna wengine walikuwa wakila nyama mbichi ambazo Yasini hakuweza kufahamu kuwa ilikuwa ni nyama ya kiumbe gani. Akakumbuka onyo alilopewa kuwa asijishughulishe na jambo lolote ambalo halikumhusu, hivyo aliwapita wale watu kama vile hakuwaona.

    Alizidi kukazana ili awahi kufika na kurudi kwasababu Husna alibaki chumbani akimsubiri. Alitamani sana kupata pesa za kujiendeleza na masomo, hivyo alikuwa tayari kufanya chochote ili kufikia lengo lake. Akajisemea moyoni kuwa “Sio mbaya nzi kufia kwenye kidonda.” Alipofika reline alikuta jitu refu limesimama katikati ya njia na kutanua miguu akiacha njia katikati. Yasini akasimama ghafla. Aliinamisha kichwa kuitazama pete yake, na alipoinua macho lile jitu halikuwepo. Hivyo akasonga mbele.

    Alivuka reli na kuanza kuporomosha mteremko wa mzizima. Alipofika kwenye yale maeneo aliyoangusha ndoo siku iliyopita akaona mwanga mkali ambao haukufahamika ulitokana na nini umeenea kwenye shina la mti mkubwa wa mbuyu. Pale kwenye ule mbuyu kulikuwa na watu wakiuzunguuka.

    Wale watu walikuwa na maumbo ya ajabu. Walikuwa na mguu mmoja mmoja, macho matatu, na mapembe marefu vichwani mwao. Waliacha kuzunguuka mbuyu na kuangalia njiani kule alikokuwa Yasini. Meno yao yaliyokuwa marefu yalikuwa yakidondosha mate mazito.

    Yasini alijisahau na kuanza kuwa shangaa. Akashtukia kitu kizito kikimpiga kichwani na kumdondosha chini kama mzigo. Akafumbua macho kuangalia kitu mkilicho mgonga na kujikuta amezunguukwa na kundi la wale watu. Mmoja kati yao alikuwa amekamatia panga lililokuwa likimeremeta kwa makali, na wengine walikuwa wameshikilia mikuki. Hali ya hofu ikamtawala Yasini na kuhisi kuwa mwisho wa maisha yake ulikuwa umefika.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Wale watu walimchukua hadi pale kwenye shina la mbuyu, wakamlaza chini na shingo yake ikawekwa kwenye kigogo tayari kwa kuchinjwa. Walimkamata ipasavyo kiasi cha kushindwa hata kutingishika. Alikuja Yule mwenye upanga na kuunyanyua juu tayari kwa kufanya shughuli yake. Yasini akajitahidi kuuvuta mkono wake hadi mdomoni na kuibusu ile pete aliyopewa na Husna. Wale watu wakatoa makelele ya maumivu na kudondoka chini huku wakimuacha Yasini huru.

    Tukio lile kilimkatisha tamaa Yasini na kuchukua uamuzi wa kurudi nyumbani, lakini alipogeuza shingo kuangalia njia alijikuta nguvu zikimsaliti. Kulikuwa na mto mkubwa sana umekatiza kwenye njia ya kuelekea nyumbani. Hivyo hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuendelea mbele ambako ndiko kulikokuwa na njia.

    Alipofika kisimani akawakuta wale wanawake watatu aliowaona siku ya Jumanne mchana. Wanawake wale walikuwa wakipigana huku wakitamka maneno ambayo Yasini aliyasikia vizuri.

    “Leo ni zamu yangu” alisema mwanamke wa kwanza.

    “Haiwezekani kila binadamu utake kumla wewe” wa pili akadakia.

    “Wewe si tulikuachia juzi umemshindwa, leo ndio utamuweza?” wa kwanza akahoji.

    “Nyie msigombane. Binadamu huyu ni nyama yangu” mwanamke wa tatu akawajibu.

    “Alitaka kurudi, mimi ndiyo nikamvuta tena” wa kwanza akaongeza.

    “Hata kama usinge mrudisha sisi tungemrudisha pia” mwanamke wa pili jibu.

    “Hakuna sababu ya kugombana jamani. Tutamrarua vipande vitatu na kugawana sawa kwa sawa” mwanamke wa tatu alitoa wazo.

    “Haiwezekani. Huyu niachieni mimi siku nyingi sijakula binadamu mzima pekeyangu” Mwanamke wa pili alipinga.

    “Kwa taarifa yako unaweza usiambulie hata kiganja chake” wa tatu alisema.

    “Haswaa” wa kwanza akaunga mkono.

    “Thubutuuu!” alihamaki Yule wa pili.

    “Unabisha?”

    “Labda kama sikuzaliwa kwenye ukoo wa RUHANI”

    “Hata kama ungezaliwa kwenye ukoo wa MAITI, humtishi yoyote hapa”

    “Anhaa! Unajifanya kiburi sio? Ngoja nikuoneshe” alisema mwanamke wa pili na kutaka kumshika Yule wa tatu.

    “Ngojeni kwanza jamani…” mwanamke wa kwanza akawashitua.

    “Nini na wewe! niache nimuoneshe huyu BWENGO kuwa Maruhani tupoje” alisema Yule wa pili.

    “Nimesikia kama binadamu keshatupita”

    “Mnh! Tena kweli. Na mimi nimesikia harufu yake”

    “Hembu twendeni. Atakuwa amepita njia hii”. Baada ya maneno yale walianza kumfuatia Yasini kwa nyuma. Kumbe wakati wanabishana Yasini alitumia nafasi ile kuwapita. Kwa mwendo wa kukazana na kuelekea kule alikokuwa ameelekezwa na Husna ambako ndipo alipokuwepo Mzee Makwanda.

    Kwa mbali alianza kusikia sauti za wale wanawake wakija nyuma yake huku wakizungumza. Yasini alipanda kwenye mti na kujibanza. Wanawake wale walifika hadi pale chini ya mti na kusimama. Walionekana wakinusa nusa kwa pua zao zilizokuwa ndefu.

    “Jamani nasikia harufu ya kintu ntu hapa” mwanamke wa kwanza alisema.

    “Hata mimi”

    “Kweli kabisa. Huyu ntu yupo hapahapa”

    “Umesha anza uwongo wako wewe Bwengo”

    “Wewe huwezi kunusa kwasababu pua zako zina matege”

    “Unanitukana? Safari hii nakuteketeza kwa mizimu yetu ya Ruhani”.

    Wakati wale wawili wakiendelea kugombana, Yule wa tatu alitupa macho yake juu ya mti na kumuona Yasini amekamatia tawi huku akiwakodolea macho. Yule mwanamke akaanza kutokwa na mate ya uchu mdomoni. Hakuamini kuwa Yule binadamu waliyekuwa wanamgombania kumbe alikuwa palepale. Akawageukia wenzake ambao bado walikuwa katika mzozo.

    “Ntuuu!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Yukupi?” alihamaki Yule wa pili na kuacha kugombana.

    “Juu ya nti”. Wote wakaangalia juu ya ule mti. Yasini alikuwa akitetemeka kwa woga na kijasho chembamba kikimvuja. Wale wanawakewalishindwa kuzificha furaha zao. Kila mmoja alionekana kuwa na hamu kubwa ya kula nyama ya binadamu.

    Mti aliokuwa amekalia Yasini ulitoa sauti za kukatika. Alipotaka kuhama kwenye tawi linguine alikuwa amechelewa, tawi lilikatika na kudondoka chini. Wale wanawake walimshuhudia Yasini akifika chini pasipo hiyari yake. Wakamkamata na kumuweka katikati kisha wakaanza kumzunguka huku wakicheza na kuimba nyimbo ambazo Yasini hakuzifahamu.

    Maumbo ya wale wanawake yakaanza kubadilika. Macho yao yakawa mekundu kama damu, midomo yao iliyo shindwa kufunga ilikuwa na meno marefu yaliyochongoka na kuchungulia nje, makucha yao ya mikono nayo yakarefuka, Masikio yao marefu yalikuwa yakicheza cheza kila kama ya punda, na wote watatu walikuwa na mikia mirefu kama ya Nyani. Yasini alijikunyata pale chini huku akitetemeka kwa woga na wasiwasi….





    Mmoja kati yao aliinama na kutaka kumshika Yasini lakini mwenzake alimsukuma pembeni. Yule aliye sukumwa aliinuka kwa hasira na kumvaa Yule aliye msukuma. Purukushani zikaanza tena. Kukuru! Kakara! Kukuru! Kakara! Yule watatu alipoona mambo yanazidi kuwa magumu alitimua mbio kwenda kuomba msaada na kuwaacha wenzake wakiendelea kupigana. Ilikuwa ni piga nikupige, panda nikupande.

    Yasini alipoona ameachwa pembeni aliona hiyo ndiyo iliyokuwa nafasi pekee ya kuokoa maisha yake. Alijisogeza pembeni taratiiibu hadi alipofika umbali Fulani akatimua mbio. Baada ya kugundua kuwa alikuwa amewaacha umbali mkubwa alisimama chini ya mti mwingine huku akihema kwanguvu. Jasho liliendelea kumvuja kama maji yaliyokuwa yakitoka bombani. Hakuweza kuamini kama ameponyeka kutoka kwenye mikono ya viumbe wale wa ajabu.

    Kwa mbali aliona mwanga mkali ukiwa kwenye lile eneo alilokuwa anatakiwa kufika. Mwanga uliokuwepo eneo lile ulifanya kilakitu kuweza kuonekana kwa urahisi. Kwenye shina la mbuyu aliona kisanduku ambacho alihisi ndicho kilichokuwa na pesa. Alitazama kwa umakini labda angemuona baba yake Husna lakini hakumuona. Baada ya muda kidogo akaliona joka kubwa likikiviringa kile kisanduku. Moyo ulimpasuka Yasini akiamini kuwa baba yake Husna atakuwa amedhuriwa na Yule nyoka, kwasababu aliambiwa kuwa angemkuta pale chini ya ule mbuyu.

    Alipokumbuka pete aliyopewa na Husna kuwa ilikuwa ni kinga kwake, akapata nguvu za kuelekea kule kwenye mbuyu akiwa tayari kupambana na hali yoyote ambayo ingejitokeza mbele yake. Cha ajabu alipofika hakumkuta yule nyoka wala kisanduku. Alipokuwa akiendelea kushangaa shangaa pale chini ya mbuyu, lile joka lilitokea juu ya mti na kumfungafunga kwa mkia wake kisha akamuinua hadi kwenye usawa wa kichwa chake ambacho kilikuwa juu ya tawi la mbuyu. Wakawa wanatazamana uso kwa uso. Yasini akatamani kupiga kelele lakini alishindwa kutokana na kubanwa mbavu. Aliamini kuwa wakati ule mwisho wake ulikuwa umefika.

    Joka lilivimba maenea ya kichwa na kufunua mdomo wake tayari kwa kummeza. Yasini akajitahidi hadi akafanikiwa kusugua pete na kuibusu. Yule nyoka alitoa sauti kali za maumivu mithili ya mtu aliyechomwa na maji ya moto. Alimrudisha Yasini pale chini kisha akarudisha kichwa chake kilichoonekana kuwa na uchu wa nyama kwenye tawi la mbuyu. Yasini alitaka kukimbia lakini hakuwa na nguvu ya kunyoosha hata kidole.

    Alipokuwa pale chini akiendelea kuugulia maumivu ya kubanwa na lile joka, alisikia sauti ya mtu akikohoa kutokea kichakani. Aligeuka kutazama upande ule lakini hakuona mtu zaidi ya majani na miti mirefu na mifupi. Alirudisha macho yake juu kwa lile joka lakini hakuona kitu zaidi ya majani ya mbuyu na mabuyu yenyewe yakining’inia. Akahisi kuwa lazima joka lile litakuwa limeshuka na kumfuata pale chini. Hivyo alijaribu kujiinua ili aondoke maeneo yale lakini alidondoka chini baada ya kusimama. Nguvu zilikuwa bado hazijatengemaa vizuri. Akajaribu mara kadhaa lakini hakuweza kupiga hata hatua mbili.

    Wakati yuko pale chini alianza kusikia sauti za watu wakicheka na kupiga vigeregere. Akaziba masikio huku akiangaza kila upande kujaribu kuangalia hao watu waliokuwa wakimcheka lakini hakuona hata mtu mmoja. Sauti zile zilipokuwa zikiendelea wingu kubwa lilitanda angani na ngurumo za radi zikiambatana na mwanga wake zilisikika na kumulika. Kulitokea mwanga mkali uliokuwa na umbo la binadamu. Mwanga ule ulisogea hadi karibu na pale alipokuwa amelala.

    Yasini akawaza kuwa inawezekana Husna alikuwa amemtoa kafara kwa mizimu yao. Alijikuta akijutia sana nafsi yake kwa kukubali kujitoa kirahisi rahisi kiasi kile.Lakini angefanya nini wakati alikuwa na shida na hamu kubwa ya kuendelea na shule. Akakumbuka tena ule msemo wake kuwa “Nzi kufia kwenye kidonda si haramu”, hivyo hata yeye angekufa kwenye kupambana na maisha lisingekuwa tatizo.

    Mwanga wa binadamu ukiwa umemsimamia, zile sauti za vicheko na vigerere zilikuwa zimekoma. Sauti kali na nzito iliyokuwa ikitokea kwenye mwanga ule wa binadamu ikasikika ikiunguruma…



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “ Hongera sana kwa kuwa jasiri kijana, Mimi ndiye Mzee Makwanda mwenyewe, baba yake Husna” Baada ya yule mtu wa mwanga kusema yale, kile kisanduku alichokiona mwanzo Yasini kilitokea kwenye mikono ya ule mwanga. Ulinyoosha mikono kwa Yasini kuashiria kumkabidhi kile kisanduku. Pamoja na kupongezwa kwa ujasili lakini Yasini alisita kuusogelea ule mwanga uliokuwa ukizungumza naye.

    “Usiogope kijana, njoo uchukue mzigo wako” ule mwanga ulisihi.

    Yasini bado alijiona ni mzito kusogea pale. Alisikia sauti ya Husna ikimtaka akachukue kile kisanduku kutoka mikononi mwa yule mtu wa mwanga. Sauti ile ilimpa nguvu na kujiinua kuanza kupiga hatua ndogondogo kuelekea kwa yule mtu. Alipokea kile kisanduku huku akiwa ameziba macho yake kwa mikono kutokana na ule mwanga mkali kummulika machoni. Baada ya kukabidhiwa ule mwanga ulitoweka na kumuacha Yasini pekeyake pale chini ya mbuyu akiwa amesimama. Kisha ikasikika sauti.

    “Unaweza kwenda kijana. Humo ndani kuna pesa. Kilakitu utaelekezwa na Husna. Kwaheri” sauti ile ilitoweka kwa mwangwi. Vicheko vilianza tena na kudumu kwa sekunde kadhaa kisha vikakata. Yasini alijikuta amesimama akiwa pekeyake na hapakuwepo tena na vitisho wala kitu chochote kilichomletea mashaka.

    Akaanza safari ya kurudi nyumbani. Alitembea salama hadi alipofika maenea ya makaburi ya Mjimpya ndipo akawakuta wale wachawi wakiendelea kutimbwirika. Tena safari hii walikuwa ni wengi zaidi. Alipowakaribia waliacha kucheza ngoma kisha wakatanda njiani kumzuia asipite. Akatokea Mzee mmoja na kumsogelea. Alimlazimisha Yasini awape kile kisanduku. Yasini akaibusu pete yake na kumnyooshea kidole yule Mzee. Ilisikika sauti ya maumivu ikitoka kwa yule mzee kisha akaanguka chini na kuanza kutapatapa kwa muda kisha akatulia na kulala kama gogo la msufi lililokatwa miaka mitano iliyopita. Wale wachawi wengine walitawanyika na kutimua mbio wakimuacha yule mzee pale chini. Yasini alimpita na kuendelea na safari yake.

    Aliteremsha mlima wa Mdundiko hadi kwenye eneo lililokuwa na kisima miaka ya nyuma. Hapo alikuta shuka nyeupe sana zimeanikwa kwenye nyasi, alipozifikia zile shuka zilibadilika rangi na kuwa nyekutu. Juu ya shuka kulikuwa na watoto wachanga wengi waliokuwa na vichwa vya watu wazima wamelala. Aliposugua pete zile shuka zilianza kuungua na watoto walipiga kelele za maumivu. Baada ya sekunde kadhaa shuka pamoja na watoto wake zilitoweka. Yasini alipandisha kilima na kutokea kwenye kijiji chao cha Mkanyageni. Alitembea hadi nyumbani akiwa salama. Akafungua mlango na kuingia ndani.

    Alipoingia chumbani alimkuta Husna amekaa juu ya Meza akimsubiri. Alikwenda moja kwa moja na kumkumbatia. Walitazamana usoni na kufanya wote wawili kutoa tabasamu.

    “Pole sana Yasini kwa yaliyokukuta” alisema Husna.

    “Nashukuru Husna nimerudi salama”

    “Sasa kazi yako imekwisha. Imebaki ya kwangu”

    “Nisaidie Husna nirudi shule. Napenda sana kusoma”

    “Usijali. Nipe hicho kisanduku, mimi nitapeleka hizo pesa shuleni kwako. Sawa?” alisema Husna huku amenyoosha mkono kupokea kisanduku kile.

    “Kwanini nisingeenda nazo mimi mwenyewe?”

    “Hapana Yasini hizi pesa ni za masharti”

    “Kwahiyo?”

    “ Kama tukikosea basi tutazipoteza. Wewe niachie mimi nifanye mambo”

    “Sawa haina shida. Ilimradi nirudi shule”

    “Usijali, mimi ngoja nikuache. Nakutakia masomo mema” aliongea Husna na kuchukua kile kisanduku na kutoweka nacho mle chumbani. Yasini alipanda kitandani kwa uchovu na usingizi ukamuiba mara moja na kumpeleka kusikojulikana.

    * * *

    Haikuwa kawaida kwa Yasini kuchelewa kuamka, lakini siku hiyo alilala hadi alipoamshwa na mama yake, alikuwa amechoka sana siku hiyo. Mama yake alikuwa na wasiwasi na ndiyomana akamuamsha.

    “Vipi Yasini unaumwa?”

    “Hapana mama, leo nimepitiwa tu”

    “Jiandae, baba yako anakusubiri mwende kibaruani”

    “Sawa mama” Yasini alijibu na kuchukua mswaki akatoka nje kusafisha meno. Wakati akiendelea na usafi, alijiwa na mawazo ya mambo yaliyomtokea usiku. Alikumbuka tangu Husna alipoingia chumbani kwake, safari ya Mzizima, na mwisho kabisa akakumbuka jinsi Husna alivyotoweka na kile kisanduku cha pesa akidai anakwenda kumlipia karo ya shule. Mambo yote hayo aliyaona ni kama ndoto. Kwasababu aliamini kuwa yeye hakuwa na uwezo wa kufanya kama vile alivyofanya usiku. Alishituliwa na sauti ya mama Jumbe iliyokuwa ikimuhimiza kujiandaa haraka. Alipomaliza kupiga mswaki akapata kifungua kinywa na kutoka na baba yake pamoja Jumbe kuelekea kibaruani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa ni kazi ngumu sana kwa mtu ambaye hakuzoea, na ni nyepesi sana kwa wale wenye mazoea. Kilikuwa ni kibarua cha kukata mikonge na kuipaki kabisa tayari kwa kupelekwa kiwandani. Yasini alikuwa ni miongoni mwa wale wasiokuwa na mazoea ya kazi ile. Mara kwa mara alikuwa akichomwa na miba. Akiwa hapo kibaruani mara kadhaa alikumbuka mambo yaliyomtokea usiku na kujisahau kama yupo kazini. Hadi kufikia jioni hakuwa amefanya kazi kubwa kama wengine wote, hivyo alipata ujira mdogo.

    Walipofika nyumbani Mama Jumbe alitoa barua na kumkabidhi Mzee Shabani. Alisema kuwa ililetwa na watoto waliokuwa wakisoma na Yasini. Mzee Shabani aliisoma ile barua hadi mwisho akahitimisha kwa tabasamu la furaha, aliinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu ingawa hakuongea neno lolote. Alimkabidhi Yasini ile barua kisha yeye akaingia ndani na kuwaacha mkewe na watoto wake hapo nje wakiwa na hamu kubwa ya kutaka kujua kilichokuwa kimeandikwa kwenye ile barua. Yasini akaisoma kwa sauti barua ile ambayo ilikuwa imeandikwa hivi.

    Mzazi wa Yasini Shabani,

    Napenda kukufahamisha kuwa kijana wako amepata wadhamini wa kumsomesha. Wadhamini hao wamekwisha mlipia karo ya masomo pamoja na Hosteli. Hivyo anahitajika kufika shuleni haraka iwezekanavyo.

    Ahsante.

    Ni mimi mwalimu mkuu.

    Wote kwa pamoja walijikuta kwenye dimbwi la furaha. Yasini aliruka ruka kama mtoto mdogo.

    “Nenda ukajiandae sasa” Mama Jumbe alisema.

    Yasini aliingia chumbani kwake na kuanza kujifungasha. Mara kwa mara alijikuta akicheka pekeyake na kujirusha kitandani. Hakuamini hata kidogo juu ya yale yaliyokuwa yanaendelea katika familia yake wakati ule. Alihusisha jambo lile na yale yaliyomtokea usiku ambayo ilipofika asubuhi aliyaona yalikuwa kama ndoto. Baada ya kumaliza maandalizi alipata chakula cha usiku na kwenda kulala, siku hiyo usingizi haukuwa tatizo kwake. Ndani ya dakika tano tu alikuwa amekwisha lala fofofo.

    Ilipofika mida ya saa saba usiku aliamka na kwenda kuchungulia dirishani kuona kama kumekucha. Aliona giza bado limetanda hivyo akarudi kitandani na kujilaza. Alipokuwa anavuta shuka kujifunika, taa yake ya kandili iliwaka kama siku iliyopita. Aliwacha kujifunika na kuigeukia, ndipo akamuona Husna amesimama. Yasini alishtuka kidogo lakini alitulia pale kitandani...





    “Wacha woga Yasini, inamaana bado hujanizoea tu?” Husna alizungumza kwa sauti ya chini. Yasini alimtazama Husna usoni huku akiwa bado ana wasiwasi. Husna alisogea hadi karibu na kitanda. Alitoa tabasamu huku akimuangalia usoni Yasini ambaye alionekana bado kuwa na wasiwasi.

    “Yasini, kazi uliyonipa nimeimaliza. Nadhani umepata barua kutoka shuleni kwako” Husna aliongea maneno hayo na kutoa tabasamu. Baada ya Yasini kusikia vile wasiwasi ulianza kumuisha, akainuka na kumkumbatia Husna.

    “Ahsante sana Husna, Mungu akubariki”

    “Usijali Yasini. Siku zote mtenda mema hulipwa mema”

    “Unamaanisha nini Husna?”

    “Unakumbuka siku uliyoniokota kule kwenye njia ya Mauaji?”

    “Mnh! Lakini kiubinadamu nilipaswa kufanya vile”

    “Basi hii ni sehemu tu ya malipo yako”

    “ Nashukuru kwa hilo”

    “Nami pia nashukuru”

    Yasini alimtazama Husna usoni na kumuona ni mtu mwenye thamani sana maishani mwake. Hakujua ampe zawadi gani ili ilingane na yale aliyomfanyia. Husna alimeza funda la mate kisha akazungumza,

    “Lakini unakumbuka sharti nililokupa?”

    “Mnh!... sio vibaya kama utanikumbusha”

    “Ah! Wacha utani. Inamaana umesahau?”

    “Basi nikumbushe”

    “Sharti langu ni kwamba usifanye kazi siku ya Jumanne”

    “Kwanini?” Yasini alihoji.

    “Nimekwambia usifanye kazi siku hiyo, au hutaki? Husna alisisitiza

    “Ok. Nimekuelewa”

    “Utanifurahisha sana kama ukifanya hivyo. Lakini utaniangusha kama ukipuuzia”

    “Usijali Husna, naahidi sitokuangusha“

    “Ahsante“

    “ Vipi una jengine?” alihoji Yasini huku akiwa na amani ndani ya moyo wake.

    “Ndio ninalo”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Enhe, endelea”

    “Naomba jambo hili liwe siri. Usije ukamwambia mtu yeyote. Sawa?”

    “Nimekuelewa Husna”

    “Haya mimi naenda. Nakutakia masomo mema”

    Baada ya kumalizia maneno hayo walikumbatiana kisha Husna akatowekaa mle chumbani. Hali ile ilmshangaza sana Yasini kwani hakuwahi kufikiria kama Husna angekuwa ni mtu wa maajabu kiasi kile. Hata hivyo na yeye mwenyewe pia alijishangaa kwa jinsi alivyogeuka na kuwa jasili kiasi cha kuweza kukabiliana na vituko vya Husna. Wakati akiendelea kuwaza na kuwazua juu ya Husna usingizi ulimnyakuwa.

    * * * *

    Yasini aliendelea vizuri na masomo chini ya udhamini wa waingereza. Wazungu wale waliingia mkataba wa kumsomesha kwa miaka yote ambayo angekuwa masomoni. Mbali na karo za hosteli na ada ya masomo, pia walikuwa wakimpa shilingi elfu hamsini (50,000/=) kila wiki kama pesa za matumizi.

    Siku zilivyozidi kusonga mbele ndivyo uwezo wa Yasini darasani ulivyoongezeka. Alijikuta akipendwa na kila mtu, kuanzia wanafunzi wenzake hadi walimu. Nae alionekana kuwa na upendo kwa kila mtu, hakujali jinsia rangi wala umbo. Alikuwa ni kijana mcheshi, mpole ,muelewa, na mkweli. Kutokana na sifa hizo, alichaguliwa kuwa kiongozi wa taaluma na nidhamu hapo shuleni.

    Ilikuwa ni siku ya jumanne, siku ambayo iliteulia kwaajili ya kufanya kazi za shambani. Wanafunzi walifika kama kawaida asubuhi na mapema. Wanfunzi waligawanywa katika makundi mbalimbali kulingana na kazi za shamba zilivyo. Kuna waliopewa kazi ya kufyeka, wengine kulima, wengine Kukata miti, na wengine kuweka mbolea shambani.

    Kama kawaida kila kiongozi alipewa kundi la kulisimamia na kuwagawia wanafunzi kazi za kufanya. Yasini alipewa kusimamia kidato cha tatu ambao walihusika na kung’oa visiki. Wanafunzi hao walifurahi sana kusimamiwa na Yasini kwasababu walijua kuwa ni kijana mwenye huruma, hakupenda kuona mtu anateseka pasipo sababu ya msingi.

    Wakiwa shambani wanaendelea na kazi, Yasini alipita kila upande akipiga stori na kuwafariji vijana wenzie. Alipiga stori zilizo chekesha na kumfanya kila mtu kujisikia mwepesi katika kazi yake. Kazi zilisonga mbele pasipo na kikwazo wala mgogoro kati ya wanafunzi na kiongozi wao. Ila kwa upande wa madarasa mengine walilaani kitendo cha kutopangiwa kusimamiwa na Yasini. Hata hivyo hawakuwa na lakufanya kwasababu ndio ilikuwa imeshatokea.

    Wakati Yasini akiendelea na kuonesha ucheshi pale shambani, aligundua kuwa kulikuwa mwanafunzi mmoja aliyekuwa mdhaifu kiafya. Yasni alimuonea huruma sana yule mwanafunzi mwenzie. Kwakuwa idadi ya visiki na wanafunzi ilikwisha kamilika, hapakuwa na mtu mwengine ambaye angeweza kufanya ile kazi ya yule kijana dhaifu. Hivyo Yasini ilimbidi kushika yeye jembe kwaajili ya kukipoteza kile kisiki. Yule mwanafunzi alikwenda kupumzika chini ya mti wenye kivuli.

    Wakati Yasini akiendelea kuchakarika kiume kama wenzie, alijikuta macho yakimtoka mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango. Wenzake waliacha kazi na kumtazama yeye. Wengi wao walifikiri alikuwa akitoa burudani kama kawaida yake, kumbe haikuwa hivyo. Kisiki alichokikata kilikuwa kinatoka damu utadhani ni mnyama au binadamu aliyejeruhiwa kwa panga ama shoka. Damu ilikuwa ni nyingi mno.

    Alipokuwa akiendelea kushangaa ile damu, alishitukia anapigwa makofi na mtu ambaye hakumuona. Watu walikuja na kumzunguuka wakimshangaa akilia kwa uchungu ambao wao hawakujua umesababishwa na nini. Hapakuwepo na hata mmoja ambaye aliiona ile damu iliyokuwa ikitoka kwenye kile kisiki. Walishangaa kuona mikono ya Yasini ikikakamaa na kupinda. Sauti ilikata na kudondoka chini kama gunia la chumvi……

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog