Search This Blog

JINI WA KUZIMU - 1

 





    IMEANDIKWA NA : BABLON JESUS CR



    *********************************************************************************



    Simulizi : Jini Wa Kuzimu

    Simulizi : Safari Ya Kuzimu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Mtoto Yasini alikuwa ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya mzee Shabani iliyokuwa ikiishi katika kijiji cha Mkanyageni mkoani Tanga. Wazazi wao walikuwa wakiwapenda sana vijana wao hao wawili yaani Yasini na kaka yake Jumbe.

    Jumanne moja Yasini alipokuwa darasani alihisi maumuvu ya kichwa. Alijitahidi kuvimilia lakini muda ulivyosonga ndivyo maumivu yalizidi kwenye kichwa chake. Hivyo ilimlazimu kuomba ruhusa ili aende nyumbani kupumzika. Kwakuwa hali yake haikuwa nzuri mwalimu alimruhusu na kumpa vijana wawili wamsindikize kwenye kituo cha afya.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kutokana na maumivu makali yaliyokuwa yakimkabili mtoto Yasini, alitamani sana afike Hospitalini haraka ili apatiwe huduma ya kutuliza maumivu yale. Kwa hali hiyo aliwalazimisha wenzake wapite njia za mkato ambazo zingewafikisha haraka. Vijana wale walifanya kama ambavyo Yasini alikuwa anataka kwasababu walikuwa wakimuonea huruma mtoto mwenzao.

    Pamoja na kwamba Yasini alikuwa akisikilizwa na wale wenzie lakini waliposhauriwa na Yasini kukatiza katika njia moja iliyokuwa ikifahamika kwa jina la mauaji vijana wale walisita.

    Njia ya mauaji ambayo aliin'gan'gania Yasini ilikuwa inatisha kutokana na kuwa na msitu mnene pamoja na vichaka vikubwa, pia kulikuwa na viumbe vya kutisha kamavile nyoka, na fisi na wanyama wengine wakali. Pia ilisemekana kuwa kwenye msitu huo kulikuwa na majini. Kutokana na mbo hayo watu waliogopa kupita kwenye njia hiyo hasa wanawake na watoto. Hata hivyo Yasini kutokana na haliyake njia hiyo aliiona ndiyo ingemfaa zaidi kwa kumfikisha haraka kwenye matibabu.

    “We Yasini acha ubishi huko kunatisha” alisema mtoto mmoja aliyekuwa akifahamika kwa jina la Hassan.

    “Halafu we unaumwa unataka kupita Mauaji” mtoto Shafii alidakia.

    “Naenda kumwambia mwalimu, mimi naumwa halafu mnataka kunizunguusha” Yasini alizungumza kwa sauti ya kutaka kulia.

    “Sasa huko pekeetu tutapitaje?” Hassani alihoji huku akimkodolea macho Yasini.

    “Tupite Mauaji! tukikumbwa na majini je utasemaje?” alisema Shafii.

    “Kwanza leo Jumanne majini kibao Mauaji” Hassani aliongeza

    “Tena saa nane hii majini ndio mida yao kutembea” Shafii akajazia.

    “Kama mlikuwa hamtaki kunisindikiza mngemwambia mwalimu” Yasini alizungumza huku akivuta hatua kukamata ile njia ya Mauaji.

    “We Yasini usipite huko!” Hssani alipaza sauti huku mikono ameiweka kichwani kwa woga.

    Shafii alimkimbilia na kumshika mkono akaanza kumvuta asipite njia ile. Yasini naye akawa anajivuta ili aachiwe aendelee na safari yake.

    “Niachie Shafii!” Yasini alilalama huku akijivuta kuchomoka kwa Shafii.

    “Sikuachii, kwani lazima tupite mauaji?” alisema Shafii huku akiendelea kumvuta mtoto mwenzie.

    “Kama nyie hamtaki nitapita mwenyewe bwanaaa” Yasini alizungumza huku akilia.

    “We Hssani nisaidie tumrudishe!” Shafii aliomba msaada kutoka kwa mtoto Hassani. Yasinialipo ona anazidiwa nguvu na Shafii akatumia meno kama silaha yake. Shafii alipoona anang’atwa hakuwa na namna zaidi ya kumwachia. Yasini alichomoka pale alitimua mbio kuelekea kwenye ile njia ya Mauaji iliyokuwa ikiogopwa na watu wazima.

    “Tunaenda kukusemea kwa mwalimu umepita mauaji” Hassani alipaza sauti kujaribu kumtisha Yasini ambaye alikuwa akizidi kutokomea.

    “Namimi naenda kuwasemea mmekataa kunisindikiza” Yasini aliwajibu huku akiendelea kukimbia kuingia kwenye msitu wa njia ile ya Mauaji.....

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yasini alikatiza kwenye msitu ule wa Mauaji huku akiwa na wasiwasi. Alikuwa akitembea huku akiangaza kulia na kushoto, mbele na nyuma kila sekunde. Kwa hali ya msitu ule ilikuwa ni vigumu kwa mtu yeyote kupita pasipo kuwa na woga. Njia ile ilikuwa ikitisha kweli kweli.

    Alipofika katikati ya msitu alishituka kusikia sauti ya mtoto akilia msituni mle. Alitamani kutimua mbio lakini akasita na kujiona mjinga kwa kukimbia kitu asichokiona. Alipokuwa anaendelea na safari yake alisikia ile sauti ikizidi kuongezeka, hali ambayo ilimfanya kuongeza mwendo na kutembea kwa tahadhali kubwa huku akijipa moyo mwenyewe kuwa angefika salama.

    Ghafla alimuona mtoto wa kike akiwa amejiegemeza kwenye shina la mti kando kidogo kutoka barabarani huku akilia. Mtoto mwenyewe alikuwa ni mdogo mno yaani kwa kukisia anaweza kuwa na miaka kama mitano au sita hivi. Yasini alisimama kwa muda kidogo akitafakari cha kufanya juu ya yule mtoto. Alitamani kumuacha kwa kuhofia kuwa anaweza kuwa ni miongoni mwa mizimu iliyokuwa ikiishi humo msituni lakini akapata wazo kuwa inawezekana mtoto yule alikuwa anahiltaji msada. Alijipa moyo kisha akaanza kumsogelea kwa tahadhali. Alipobakiza hatua kama sita kutoka paple alipokuwa yule mtoto Yasini alisimama.

    “We nani?” alihoji Yasini kwa wasiwasi.

    Mtoto yule baada ya kusikia sauti ikimsemesha alinyamaza kulia na kuinua macho yake kumtazama Yasini usoni.

    "Unaitwa nani?" Yasini alimuuliza tena kwa sauti ya mkazo.

    "Husna" alijibu mtotoyule kwa sauti yenye kukatakata kutokana na kulia.

    "Unafanya nini hapa?”

    “Nalia” mtoto yule alijibu kwa mkato

    “Nini?” Yasini alihoji kwa mshangao.

    “Niko hapa nalia”

    “Huogopi humu Mauaji pekeyako?” yasini alihoji kwa mshangao.

    “Siogopi, Nalia nikimaliza naondoka” Mtoto yule alijibu kwa sauti iliyotoka kulia.

    “He! unalia nini sasa?”

    "Mama nataka kunipiga"

    "Umefanya nini?" Yasini aliendelea kuhoji lakini swali lile hakujibiwa hivyo ikambidi kubadilisha maswali.

    "Nyumbani kwenu ni wapi?

    "Kidutani"

    "Kidutani?" Yasini alishangaa kwasababu huko Kidutani kulikuwa ni mbali mno kutokea pale kwenye njia ya Mauaji.

    "Ndiyo Kidutani"

    “Huku umefikaje, na huogopi humu msituni pekeyako? twende kwetu nitamuomba kaka akusindikize kwenu kwa baiskeli" Yasini alijikuta akimuonea huruma mtoto yule na kuamua kumsaidia. Husna alinyanyuka na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwa kina Yasini.

    Walipofika wakamkuta dada wa kazi ameshaandaa chakula cha mchana, walikula na baada ya hapo walikwenda kucheza. Yasini alijikuta yupo mzima kabisa tofauti na alivyo ondoka shuleni na kusahau kama alikuwa anaumwa. Walicheza michezo mingi ya kitoto, walikimbizana hapa na pale, wakaimba nyimbo zao za kitoto. Kila mmoja alionekana kufurahi kukutana na kuwepo kwa mwenzie, lakini ilipofika mida ya Alasili Husna alibadilika na kuwa mnyonge.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Vipi Husna mbona hivo?" Yasini alihoji kwa upole baada ya kumuona mtoto mwenzie amepoteza amani.

    "Nataka kwenda nyumbani" Husna alijibu kwa upole na wasiwasi.

    "Basi ngoja nikamwambie kaka Jumbe akusindikize" alisema Yasini na kukimbilia ndani akimuacha Husna pale nje pekeyake. Kwa bahati nzuri alimkuta kaka yake Jumbe akijiandaa kwenda mazoezini kulekule Kidutani ambako alikuwa anakwenda Husna. Yasini akamuelezea kakayake kilakitu, Jumbe naye hakuwa na hiyana alikubali kumpeleka Husna nyumbani kwao.Yasini alifurahi sana hivyo alitoka nje mbio kwenda kumpa Husna habari ile njema. Lakini alipofika nje Husna alikuwa amekwishaondoka. Yasini alijaribu kumtafuta kila mahali lakini hakufanikiwa kumuona mtoto mwenzake.





    Baada ya miaka kadhaa Yasini alihitimu elimu ya msingi na kufauru vizuri kuweza kuendelea na masomo ya sekondari. Alichaguliwa kujiunga katika shule moja iliyokuwepo Kitisa kijiji chenye umbali wa kilomita kama kumi na mbili kutokea mkanyageni ambako alikuwa akiishi na wazazi wake. Kutokana na umbali ule ilimbidi kukaa kwenye hosteli za shule ile.

    Aliendelea kufanya vizuri darasani hadi alipofika kidato cha pili ambapo mambo yalianza kubadilika katika familia yao. Mzee shabani ambaye alikuwa ni baba yake alisimamishwa kazi kutokana na kukumbwa na kashfa ya ubadhilifu wa mali za uma. Nyumba mbili ambazo alizijenga mjini Tanga nazo pia zilipigwa mnada, na akaunti zake zote zikafungwa. Hali ya kimaisha nyumbani kwa mzee Shabani ilianza kubadilika na kuwa ngumu. Mama Juambe ndiye aliyekuwa akitegemewa kwa kilakitu. Ni yeye aliyekuwa akilipa karo za shule pamoja na fedha za chakula na matumizi mengine ya nyumbani.

    Fedha alizokuwa akizipata Mama Jumbe hazikutosha kumlipia Yasini ada ya hosteli pamoja na karo ya masomo. Kutokana na hali ile Yasini alifukuzwa hosteli jambo ambalo lilipelekea kwenda shule akitokea nyumbani. Alitembea kwa miguu kwenda na kurudi shule kila siku. Alijikuta akichoka sana wakati wote na mara kwa mara alikuwa akisinzia darasani wakati wa masomo, na aliporudi nyumbani alishindwa kujisomea kutokana na kuchoka kupita kiasi.

    Siku moja Yasini alikuwa njiani akitokea shule. Siku hiyo jua lilikuwa kali mno, Njaa na kiu vilikuwa vikimsakama sana ukizingatia kwamba hapakuwepo na nyumba karibu ambayo angeweza kuomba hata maji ya kunywa. Alijikaza na kuendelea na safari yake. Ghafla alishituka baada ya kusikia sauti ya mtu ikiliita jina lake kutokea kwenye mti mkubwa ulio kuwepo hatua chache kutokea barabarani. Sauti ile ilirudia kwa mara ya pili jambo ambalo lilimfanya ageuke upande ule. Alimuona msichana aliyekuwa ameshikilia kikapu chini ya ule mti mkubwa uliokuwepo karibu na vichaka. Msichana yule alinyanyua mkono na kumuita Yasini. Kwa taabu Yasini alimsogelea na alipofika karibu akamsalimia.

    “Mambo”

    "Safi Yasini habari za siku?" msichana yule alisalimia kwa kulitaja jina la Yasini.

    "Salama" Yasini alijibu kwa mkato.

    "Unaonekana umenisahau Yasini?"

    "Nikweli dada, naomba unikumbushe"

    Msichana yule alicheka kidogo kabla ya kuzungumza neno lolote.

    "Mimi ni Husna” msichana yule alijitambulisha.

    “Mnh! sikukumbuki kabisa dadaangu” alisema Yasini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni miaka mingi sana imepita si rahisi kunikumbuka” alisema msichana yule.

    “Yaani hata picha yako hainijii kichwani kabisaaa” alizungumza Yasini.

    “Yule mtoto uliye mkuta kule Mauaji analia miaka mitano iliyopita unamkumbuka?" msichana yule alijieleza.

    “Mnh! hapana sikumbuki” Yasini alijaribu kukumbuka lakini kumbukumbu hazikumjia kabisa kwenye kichwa chake.

    “Siku hiyo uliondoka shule mapema sana kwasababu ulikuwa unaumwa. Ulipofika mauaji ukasikia sauti ya mtoto akilia, ukamsaidia na kwenda naye nyumbani kwenu lakini aliondoka katika mazingira ya kutatanisha” msichana yule alijieleza kwa kirefu.

    “Ahaaa nimemkumbuka, dah ni zamani sana” Yasini alimkumbuka mtoto huyo.

    “Basi mtoto mwenyewe ndiye mimi” alisema yule msichana.

    “Unasemaje?” Yasini alihoji kwa mshangao wa kuto kuamini yale aliyokuwa anayasikia kutoka mdomoni mwa binti yule.

    “Mimi ndiye mtoto Husna uliyemsaidia”

    "Husna!! waoooo" Yasini alionekana kumkumbuka yule msichana. wote kwa pamoja wakakumbatiana kwa furaha.

    "Husna ni wewe?"

    "Ni mimi jamani"

    "Umekuwa mkubwa Husna"

    "Jamani hata wewe umekuwa mkubwa"

    Yasini alifurahi sana kukutana na Husna kwa mara nyingine wakiwa wakubwa hadi njaa pamoja na uchovu wote alijikuta vimempotea ghafla.

    "Hongera sana nimesikia umefauru”

    "Ahsante sana Husna"

    "Tena nikaambiwa kuwa unakaa hukohuko shuleni"

    "Nikweli nililkuwa nikiishi kwenye hosteli"

    "Umesema ulikuwa ukiishi hosteli, kwahiyo sasahivi unaishi wapi?"

    "kwasasa nipo nyumbani"

    "kwanini sasa umehama hosteli wakati shule ni mbali sana?"

    "Ah, usijali sana Husna ni mambo ya kifamilia" Yasini alikatiza yale maongezi na kubadilisha mada. Alitaka kujua sababu zilizomfanya Husna kuwa maeneo yale ya porini mida ile………





    Husna alisema kuwa alikwenda shambani kumpelekea chakula mjomba wake lakini hakumkuta. Kwahiyo alikuwa ameamua kurudi nyumbani. Alimuomba Yasini ale kile chakula. kwa upande wa Yasini suala lile aliliona kama ni bahati kwake kwasababu njaa ilikuwa ikimtesa sana.Hata hivyo aibu ilikuwa kikwazo kwake.

    "Naomba ule hiki chakula unipunguzie mzigo"

    "Hapana Husna mimi nimeshiba" Yasini alijifanya kujivunga huku akikitamani. Husna naye aliendelea kumbembeleza na hatimaye Yasini akakubali. Vilikuwa ni viazi vya mviringo vilivyokuwa vimepikwa kwa ustadi wa hali yajuu. Vilivutia kuliwa mara utakapoviona. Yasini alikula vyote pasipo kusaza hata kimoja. Husna alitoa maji ya kunywa kutoka kwenye jagi na kumpa Yasini ashushie msosi aliokula. Baada ya kumaliza alijikuta kuwa nae pia ni miongoni mwa viumbe walio na matumaini ya kuendelea kuishi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Alimshukuru sana dada yule kwa wema aliomtendea.

    "Ahsante sana Husna Mungu atakubariki"

    "Usijali Yasini"

    "Sasa sijui tutaonana lini tena?" alihoji Yasini huku akisimama na kujikung'uta vumbi lililokuwa limeganda kwenye suruali yake ya shule.

    "Usihofu tutaonana siku yoyote Mungu akipenda" alisema Husna na kutoa noti ya shilingi elfu kumi akamkabidhi Yasini. Yasini aliipokea ile pesa huku akisitasita kwa aibu. Baada ya hapo waliagana na kila mmoja alielekea upande wake.

    * * *

    Ilikuwa ni siku ya Jumanne siku ambayo kulikuwa na upepo mkali sana, vumbililitimka mara kwa mara. Ilikuwa ni miezi miwili tu imepita tangu Mama Jumbe asimamekwenda kazini kutokana na kampuni ya kimarekani aliyokuwa akiifanyia kazi mkatabawake wa kuwa hapa nchini kumalizika. Yasini alirudi mapema sana siku hiyo. Mwalimumkuu aliwarudisha wanafunzi wote waliokuwa hawakulipa karo ya muhula wa pili wa masomo.

    Yasini alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi waliorudishwa kwasababu hiyo ya kutolipa ada. Kwa wakati ule alikuwa anasoma kidato cha nne na alibakisha takribani miezi minne tu afanye mtihani wake wa taifa. Alikata tamaa kabisa ya kurudi tena shuleni kutokana na hali ngumu ya maisha iliyokuwepo nyumbani kwao. Aliuona mwisho wa masomo yake ukiwa umefika, na ndoto zake zote kutoweka. Mama Jumbe alishituka sana baada ya kumuona Yasini akirudi nyumbani mapema sikuhiyo.

    “Vipi mbona leo mapema sana?” Alihoji mama Jumbe.

    “Shikamoo mama”

    “Mbona leo mapema?”

    “Lakini nakuamkia mama”

    “Marahaba, mbona leo umewahi kurudi”

    “Mwalimu amenirudisha kwasababu sijalipa ada. Tena amesema hataki kuona pua yangu kama sikwenda na karo” Yasini alisema maneno yale na kumfanya Mama yake kuishiwa na pozi.

    Baada ya Yasini kubadilisha sare za shule alikwenda jikoni ambako alichukua vipande vya mihogo na kuanza kujifaidia akimezea kwa maji bila ya chai.

    Baada ya kumaliza kula alipumzika kwa dakika kadhaa kisha akachukua ndoo ndogo mbili na kuelekea kisimani. Visima vilikuwa mbali sana kutoka kwenye makazi waliyokuwa wakiishi watu. Visima hivyo vilikuwa katika bonde moja lililo julikana kwa jina la MZIZIMA. Bonde hilo halikuwahi kukaukiwa na maji hata wakati wa kiangazi. Wananchi wengi wa kijiji hicho cha mkanyageni walitegemea kuchota maji kutoka kwenye bonde hilo. Kulikuwa na mteremko mkali na mlima mrefu kutoka kwenye visima vile. Watu walikuwa wakipandisha milima hiyo na ndoo zilizojaa maji zikiwa Vichwani.

    Yasini alitembea kwa mwendo wa kukimbia huku akiwa ameshikilia ndoo zake mbili mkononi. Ghafla alijikwaa kisiki kilichokuwepo kando ya njia na kuanguka chini. Alipokuwa akijiinua aliona bahasha ikiwa pembeni yake. Akaiokota na kuitazama kwa makini. Haikuwa imeandikwa chochote kwa nje. Alifungua ndani ili kuona kilichomo. Maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwenye karatasi iliyokuwemo kwenye bahasha ile yalimuacha mdomo wazi. Ilikuwa imeandikwa kama ifuatavyo:

    “Kwako Yasini;CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Leo ni siku ya Jumanne, fahamu kuwa kuanzia leosiku hii itakuwa ni siku ya mapumziko kwako na hutatakiwa kufanya kazi yoyote ngumu siku kama ya leo. Tafadhali naomba urudi nyumbani ukapumzike.

    Wako,

    Husna.”

    Yasini alibaki ameduwaa asijue nini cha kufanya kwani hakujua Yasini aliyetajwa kwenye ile barua alikuwa ni nani. Aliwaza kuwa Husna aliyemfahamu yeye asingeweza kuandika maneno ya ajabu kama yale. Aliikunja ile barua na kuitia mfukoni kisha akachukua ndoo zake na kuendelea na safari ya kisimani…





    Alipofika kisimani aliwakuta wanawake watatu tu, jambo ambalo halikuwa la kawaida kwasababu sikuzote kisimani hapo watu walikuwa wanajaa sana. Yasini aliwasalimia wale wamama lakini hakuna hata mmoja aliyejibu salamu yake. Alipaza sauti na kuwasalimia kwa mara nyingine akidhani kuwa walikuwa hawakusikia salamu yake ya mwanzo. Hata hivyo wale kinamama hawakuitikia tena na badala yake waliguna na kuendelea kuchota maji.

    Yasini alichagua kisima kingine kilichokuwa na maji safi na kuwaacha wale wamama waliokataa salamu yake wakiendelea kuchota maji. Alijaza ndoo zake kisha akaiweka moja kichwani na nyingine aliining’iniza mkononi na kuanza safari ya kurudi nyumbani. Wakati akipandisha mlima kulitokea upepo mkali sana ambao ulimyumbisha huku na kule hatimaye maji yote yalimwagika.

    Upepo ulipokatika Yasini alirudi tena kisimani. Pale kisimani alikuwa amebaki mama mmoja tu wengine wawili hawakuwepo. Safari hii aliteka maji kwenye kisima kilekile alichokuwepo Yule mama mmoja. Baada ya kujaza alibeba ndoo zake na kuanza tena safari ya kurudi nyumbani , lakini alipotembea kama hatua tano kutoka pale alipokuwa Yule mama alisikia msonyo kutokea nyuma yake. Alipogeuka kumuangalia mtu aliyemsonya hakuona mtu. Hata yule mama pale kisimani pia hakuwepo. Aliangaza huku na kule lakini hakuona mtu, akaamua kuendelea na safari yake kwa haraka.

    Alipofika usawa wa mbuyu uliokuwepo kando kidogo ya njia, upepo ulianza tena kuvuma kutokea kule alikotoka. Alijaribu kukazana ili usimkute lakini haikusaidia kitu, ulivuma kwa kasi na kumkumba, ulimuangusha chini yeye pamoja na ndoo zake. Alilala pale chini hadi upepo ulipokatika ndipo alipojiinua na kujikung’uta vumbi. Alitaka kurudi kisimani kwa mara nyingine lakini ilishindikana kwasababu ndoo zote zilikuwa zimepasuka kutokana na kuangushwa na upepo.

    Hapakuwa na namna nyingine zaidi ya kuelekea nyumbani. Alipofika alimuelezea mama yake jinsi upepo ulivyomsumbua na hatimae kuangusha ndoo na kupasuka. Mama jumbe alimhurumia sana.

    “Pole sana mwanangu”

    “Ahsante mama”

    Yasini alitamani kumwambia mama yake juu ya ile barua aliyoiokota njiani lakini aliona ulikuwa ni upuuzi akaamua kumyamaza.

    Ilipotimia mida ya saa mbili usiku Mzee shabani akiongozana na mtotowake Jumbe walirejea kutoka kibaruani na fungu la magimbi, walikuwa wamechoka sana. Mama Jumbe alikuwa bado hajapika chakula cha usiku kutokana na kutokuwa na kitu cha kupika usiku ule. Aliyamenya yale magimbi na kupika machache akiacha mengine kwaajili ya kifungua kinywa cha kesho asubuhi. Walikula na kwenda kulala mapema kwasababu taa hazikuwa na mafuta ya kutosha hivyo zisingeweza kuwaka kwa muda mrefu.

    Yasini alipokuwa kitandani usingizi haukuja kabisa. Muda wote alikuwa akiwaza juu ya maisha yake na

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/kukosa elimu kwani alichokuwa akisikia kwa watu ni kwamba elimu ni ufunguo wa maisha. Alitamani kuche haraka ili asikie baba yake angesema nini kuhusu suala lake la kurudi shule. Aliamka mapema siku iliyofuata na kuanza kujishuhulisha na kazi za nyumbani.

    Siku hiyo ilikuwa ni jumatano tulivu, hapakuwa na upepo kama siku iliyopita. Mzee Shabani aliamka asubuhi na mapema kama kawaida yake kwa kujiandaa kwenda vibaruani. Alitoka nje na kumuita Yasini. Yasini alifika kwa baba yake na kumsalimia, na baada ya salamu mzee Shabani alimueleza dhumuni la wito ule.

    “Yasini mwanangu, mamayako amenieleza kilakitu juu ya matatizo yako ya shuleni na nimemuelewa vyema” Mzee Shabani aliongea kwa upole

    “ndiyo baba”

    “mwanangu wewe ni mtu mzima na hali yetu hapa nyumbani nadhani unaifahamu, si ndio?”

    “ndio baba” Yasini aliitikia kwa unyonge.

    “ningependa sana usome mwanangu ili uje kutukomboa kutokakwenye hii hali tiliyokuwanayo.

    Kaka yako Jumbe ndiyo hivyo tena amekataa shule na kuamua kujiingiza kwenye mambo ya kijinga. Sasa maisha yanampiga, anatamani hata sasa kurudi shule lakini ndiyo hivyo tena uwezo haupo”

    ”kwahiyo baba?”

    “Hakuna jinsi mwanangu. Kesho itabidi tutoke pamoja kwenda vibaruani” mzee Shabani aliongea kwa uchungu. Yasini hakujibu kitu bali alikaa kimya na hakuweza kuzuia machozi

    kufanya ziara katika mashavu yake. Mzee Shabani aliingia ndani na kumuacha Yasini bado ameinamisha kichwa kwa mawazo. Baada ya dakika kadhaa mzee Shabani alitoka akiongozana na Jumbe.

    “Yasini yote ni maisha na wewe ni mwanaume, fahamu kuwa mwanaume ameumbwa kuteseka. Hata vitabu vya dini vinasema mwanaume atakula kwa jasho lake. Sisi tunakwenda vibaruani, jiandae kesho tutakwenda sote” Mzee shabani alisema na kuondoka....





    Yasini alijifungia chumbani kwake na kuanza kulia. Alibaki humo kwa muda mrefu hadi aliposikia sauti ya mtu akibisha hodi. Alijifuta machozi na kutoka nje ambako alikumbana uso kwa uso na Husna. Alimkaribisha na kutoa mkeka ambao aliutandika barazani na wote wawili walikaa.

    “vipi Yasini leo hukwenda shule” Husna alihoji mara baada ya kuketi

    “hapana”

    “Kwanini, au unaumwa? Naona hata macho yamekuwa mekundu tena yamevimba”

    “siumwi Husna”

    “Sasa tatizo ni nini?”

    “ah, usijali ni mambo ya kawaida tu”

    “mambo ya kawaida wakati yanakutoa amani”

    “Hata kama nikikuambia hutaweza kunisaidia Husna”

    ”Yasini tambua kuwa mimi na wewe tupoje, pia ninaweza kukusaidia tatizo lolote

    linalokusumbua” . Yasini alitulia na kukumbuka jinsi urafiki wao ulivyoanza. Akaona zilikuwepo

    sababu za kutosha kueleza tatizo lake kwa Husna hata kama asingekuwa na uwezo wa kumsaidia.

    “Husna” , Yasini aliita na kumeza mate kisha akaendelea

    “ukweli ni kwamba, nimesimamishwa shule”

    “umesimamishwa shule! Kwasababu gani?”

    “sijalipa karo ya masomo”

    “kwahiyo unampango gani?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “baba hana pesa” Aliongea Yasini na kujikuta machozi yakimtoka.

    “Pole sana Yasini. Lakini usilie mimi nitakusaidia”

    “utanisaidiaje Husna?”

    “nitakusaidia kama utakuwa tayari kusaidiwa”

    “Nipo tayari Husna”

    “sawa, lakini unatakiwa kuwa jasili ili niweze kukusaidia”

    “Niwe jasili! Unamaana gani?”

    “Sikiliza Yasini, wewe ni mwanaume. Unatakiwa usiogope kufanya kitu ambacho kina manufaa

    kwako. Unatakiwa kujitoa ili ufanikiwe”

    “Husna, nitakuwa tayari kwa lolote ilimradi nirudi shule”

    “usihofu nitaongea na baba, na naamini atakusaidia” alisema Husna.

    Hata hivyo bado Yasini hakuwa na matumaini ya kusaidiwa na huyo baba yake Husna kwasababu alifahamu kuwa ni ngumu kwa binadamu kutoa msaada kwa mtu asiyemfahamu.

    Husna aliendelea kumpa moya kijana Yule huku akimhakikishia kuwa endapo angekubali tu kutimiza masharti ambayo angempa basi ingekuwa ni rahisi kupata msaada kutoka kwa baba yake. Alimueleza kuwa yeye ni mtoto wa pekee katika familia ya Mzee MASUDI na BIBI NYANDUNDU, Hivyo alikuwa akisiklizwa na kutekelezewa chochote ambacho angekihitaji hapa ulimwenguni. Kwa kiasi Fulani Yasini alianza kupata matumaini ya kurudi tena shule.

    Pamoja na matumaini ya kusaidiwa lakini bado alijiwa na wasiwasi juu ya suala la kutimiza masharti aliyoahidiwa na Husna. Alimuuliza sababu ya kuwepo kwa masharti hayo wakati amesema kuwa Baba yake yupo tayari kumfanyia chochote anachokitaka. Husna alimueleza Yasini kuwa masharti aliyotaka kumpa yalikuwa ni yakwake na sio ya baba yake. Alimwambia kuwa asiwe na wasiwasi kwasababu hayakuwa masharti magumu lakini pia hayakuwa mepesi…

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog