Search This Blog

UCHAWI WA KURITHI - 3

 





    Simulizi : Uchawi Wa Kurithi

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Wakiwa wamelala usiku wa manane gafla wakashtushwa na hodi, wakajiuliza ni nani agongaye muda huo. Kila mmoja aliogopa kwenda kufungua.

    Mgongaji hakuchoka, bado aliendelea kugonga tu.

    Hakuna aliyeweza kutoka, na mlango nao ulizidi kugongwa, mwisho wa siku ikabidi Marium aende na mumewe wakafungue ila walipofika mlangoni kila mmoja aliogopa ikabidi waulize kuwa yule mgongaji ni nani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakauliza mara ya kwanza, kimya. Wakauliza mara ya pili mara sauti ya kike ikaitikia "mimi" wakamwambia ataje jina lake ila akakaa kimya, wakaogopa kumfungulia. Wakajaribu kuchungulia dirishani ili waone huyo mtu lakini hawakuona chochote.

    Maswali mengi wakajiuliza kwa ni nani awezaye kugonga mlango kwa kiasi kile.

    Ikabidi warudi tena kulala ila kila mmoja hakuelewa kuwa mgongaji yule alikuwa ni nani.

    Kesho yake wakawa wanajiuliza juu ya mtu aliyekuwa anagonga mlango usiku uliopita ila wote wakakosa jibu juu ya mgongaji huyo.

    MUSSA: Unadhani alikuwa ni nani?

    MARIUM: Kwakweli sielewi, na je alikuwa anataka nini?

    MUSSA: Hata na mimi sielewi.

    Watoto wao wakaamua kwenda kwa babu yao mzee Yusuphu ili wakakae huko japo kwa siku mbili au tatu.

    Kisu aliendelea kufanya atakacho na kuendelea kuwavuta mabinti warembo ili awe nao.

    Ilikuwa ngumu kwa wao kugundua mapema kuwa wanavutwa tu ila walijikuta wakiwa kwenye mahusiano na Kisu.

    Pia hakuacha kuangalia ili ajue cha kufanya tena kwenye familia ya kaka yake.

    Kuna mwanamke aliyempenda sana na akatamani awe nae, Kisu akajisemea kuwa atafanya chochote ili ampate mwanamke huyo na awe wa kwake.

    Huruma alimuhurumia kaka yake na familia yake, usiku ule mtu aliyekuwa anawagongea alikuwa Huruma ila wangeelewa vipi kama ni yeye wakati hakujitaja? Hata yeye mwenyewe Huruma akatambua ni kwanini walishindwa kumfungulia mlango.

    Alienda pale kiuchawi ila akataka kuingia ndani kwa njia ya kawaida.

    Aliporudi kwao aligombana sana na mama yake kwani hakufanya kile alichotumwa na Nyuta.

    NYUTA: Mbona umekuwa hivyo Huruma? Nimekutuma nini nawe umefanya nini?

    HURUMA: Mama, kaka ameshateseka vya kutosha. Sasa inatosha, muhurumie tafadhari.

    NYUTA: Kwani nikimuhurumia mimi na yeye atanihurumia?

    HURUMA: Mama kumbuka ni damu yako lakini?

    NYUTA: Kama na yeye analitambua hilo basi anapaswa afanye lile ninalomwambia, nilimwambia amuache Marium ila hataki.

    HURUMA: Mama usitake kumuachanisha kwa maslahi yako binafsi, angalia maisha yao kwanza.

    Huruma alielewa ni kwanini mama yao alikuwa akimchukia Marium ambaye hajawahi kumkosea hata mara moja, na mara nyingi chuki za Nyuta hufanya amuue mtu kwa kumtoa msukule, hili jambo hata Huruma lilimshangaza ingawa na yeye alikuwa na roho mbaya ila mama yake ilikuwa mbaya kupitiliza.

    Marium hakuchoka kutafuta msaada kwa familia yake, roho ilimuuma sana kuona ameshindwa kuwalipia wanae ada. Akaamua kwenda kwa Shangazi ambaye ni Nina ili kupata ushauri,

    NINA: Mara nyingine unaweza kukaa na adui na wala usijue kama ni adui.

    MARIUM: Unamaana gani shangazi?

    NINA: Na pia msaada wako unaweza kuwa karibu ila usijue huo msaada utakusaidia vipi.

    MARIUM: Nashindwa kukuelewa shangazi?

    NINA: Wengine tuna ukaribu sana na wakwe zetu na tuna uwezo wa kuwaeleza chochote wakatuelewa lakini wewe sikushauri ufanye hivyo.

    MARIUM: Bado sikuelewi.

    NINA: Hata mimi sikuelewa kaka alipoamua kuoa haraka haraka, sikuelewa ni kwa mapenzi yake au ya kusukumwa na sikuelewa kama wifi huyo ataleta maafa makubwa sana kwenye familia yetu.

    MARIUM: Unamuongelea nani shangazi?

    NINA: Maneno hayasaidii ila vitendo vyake vitakufanya umgundue mwenyewe.

    MARIUM: Jamani shangazi unaniacha njia panda!!

    NINA: Sina mengi ya kusema ila Funga safari, nenda kwa bibi yako ukazungumze nae.

    Ni kweli Marium hakumuelewa Nina kuwa alikuwa na maana gani ila hakutaka kupoteza muda akaamua kusafiri na kwenda kwa bibi yake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BIBI: Umekuja Marium, pole sana.

    MARIUM: Asante bibi, kwakweli matatizo yameniandama.

    BIBI: Usijari Marium, kila chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho ila nitakuwa nawe mjukuu wangu bega kwa bega kukusaidia.

    MARIUM: Asante bibi.

    BIBI: Tena nashukuru umekuja kabla wakati haujanichukua na tumeweza kuonana kwa kawaida.

    Marium alikuwa ni mtu wa kustaajabu mambo mengi yanayomtokea kwa kipindi hicho.

    Kipindi cha shida ndio utamjua rafiki wa kweli na mnafki, kwani ukiwa na raha wengi watakuwa upande wako ila ukitetereka kidogo tu wengi watakukumbia, ndivyo ilivyokuwa hata kwa Marium na familia yake kwani kipindi hiko cha dhiki wengi wakamkimbia hata wale marafiki zake wa karibu.

    Baada ya yote, Marium akaamua kurudi nyumbani kwake na kutafakari mambo mengi aliyoweza kuongea na bibi yake.

    Wakati akitafakari hayo, mara akahisi kuna kitu akili yake inamwambia kufanya. Akapata wazo la nini cha kufanya ili aweze kuikomboa familia yake ambayo ilikuwa inatetereka kwasasa.

    Akapata wazo la kwenda kuchukua mkopo na kuanzisha biashara ila biashara hiyo iwe mbali na wanapoishi kwani alitambua kuwa adui yupo karibu ila ubaya ni kwamba hakumjua adui huyo ni nani na dhumuni kubwa la adui huyo ni nini.

    Marium alikuwa ni mwanamke mwenye bahati sana katika maswala ya biashara hata yeye mwenyewe alishangaa kuona ameyumba kiasi kile kwenye mifugo yake aliyoitegemea sana. Tatizo hakumjua adui ila kama angemjua ingekuwa rahisi kwake kuelewa cha kufanya kwa haraka dhidi ya adui wake.

    Na hata kama akimgundua atamfanya nini wakati adui ni mama mkwe wake?

    Bado Marium alikuwa na wakati mgumu sana wa kutafakari.

    Kisu akaenda kuwatembelea huku amebeba ndizi za kuiva mkononi, baada ya salamu Kisu akamkabidhi Marium zile ndizi. Kutokana na njaa kumshambulia Marium akaona hana budi zaidi ya kufakamia zile ndizi, wakati huo watoto wake walikuwa nyumbani kwa babu yao.

    Alipomaliza kula zile ndizi mara akaona mwanga mkali ukimulika tumbo lake gafla akaanza kuumwa na tumbo.



    Marium alipomaliza kula zile ndizi mara kuna mwanga ukamulika tumbo lake na gafla tumbo likaanza kumuuma.

    Akajikuta akigalagala chini na mara kisu huyo akaondoka.

    Marium akaugulia sana matatizo ya lile tumbo na mara Mussa akafika na kumkuta Marium akiugulia, ikabidi amuwahishe hospitali baada ya vipimo Marium akaambiwa kuwa ana uvimbe tumboni.

    Marium akashindwa kuelewa kwakweli, imekuwaje hadi huo uvimbe ujitokeze au ucharuke baada ya kula ndizi za kuiva!! Akashindwa kuelewa mahusiano ya zile ndizi na ule uvimbe.

    Daktari akamwambia Marium kuwa anapaswa afanyiwe upasuaji ili kutoa uvimbe huo, Marium na Mussa wakahisi kuchanganyikiwa kwakweli kwani hawakuwa na uwezo wa kufanyiwa operesheni kwa kipindi hiko.

    Ikabidi wachukue tu dawa za kutuliza na kurudi nyumbani.

    MARIUM: Asante mume wangu, ila pesa ya kunihudumia hospital umeitoa wapi Mussa??

    MUSSA: Leo ndio nimeamini ule usemi unaosema kuwa ng'ombe wa maskini hazai na akizaa ni dume na dume lenyewe ni shoga.

    MARIUM: Kwanini umesema hivyo mume wangu??

    MUSSA: Leo katika shughuli zangu nilibahatika kupata pesa na nikafurahi sana ila cha kushangaza nafika tu hapa nyumbani nakukuta wewe ni mgonjwa, na ndio hivyo pesa yote imeishia hospitali.

    MARIUM: Dah mume wangu sijui hata ni ibilisi gani aliyetuingilia kwenye maisha yetu.

    MUSSA: Hata na mimi sijui kwakweli.

    Wakajikuta wakisononeka na kukosa raha kabisa.

    Baada ya siku chache, Marium alijikuta yale maumivu hayapo tena. Alijihisi kupona kabisa ila hakujua ni kitu gani kilichomponya.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Marium akafanya kama mawazo ya moyo wake yanavyomtuma, akaenda kukopa pesa na kuanza biashara nje kidogo ya familia yake, aliogopa kushirikisha watu mpango wake zaidi ya mumewe bwana Mussa na akamuomba swala hilo wafanye siri kwani walikuwa wanazungukwa na adui wasiyemjua.

    Marium alishaanza kumuwekea mashaka Kisu ila hakudhania kama mama mkwe wake ndio mbaya zaidi.

    Wakafanya siri kubwa, maisha nayo yakaendelea na Mussa nae akarudishwa kazini, wakaona sasa maisha ya dhiki yanakaribia kuwatupa mkono.

    Maisha yakaenda taratibu na mwisho wa siku wakawarudisha watoto wao shuleni na wao wakaendelea na kutengeneza maisha yao.

    Kisu akawa anaendelea na mchezo wake wa madawa ili avute chochote anachotaka kuwa nacho.

    Ila binti aliyemtaka kwa sasa alimpa tabu kidogo kwani dawa zake nyingi zilionekana kugonga mwamba, ikabidi atumie mbinu ya ziada kumpata.

    Ikabidi amshirikishe mama yake juu ya kumpata huyo binti.

    Na kwa kushirikiana na mama yake akafanikiwa kumpata huyo msichana.

    Huruma aliwaonea sana imani watu wote wanaoteswa na familia yake.

    HURUMA: Ila kaka, mapenzi ya dawa si mapenzi kabisa.

    KISU: Kwani wewe Huruma unatakaje?

    HURUMA: Kwanza ona hata mama kakimbiwa na baba sababu ya mapenzi yake ya dawa. Kila siku unagombanisha wapenzi ili umpate mwanamke umtakaye sasa mbona wanawake wenyewe ni wengi?

    KISU: Kila mmoja na starehe yake hapa duniani.

    HURUMA: Kwahiyo starehe yako ni uchawi na wanawake?

    KISU: (Huku akiwa amechukia), halafu sitaki tugombane kijinga Huruma.

    Kisu hakupenda kuambia ukweli, na alizidi kutenda ubaya na hali hiyo ilizidi kumuumiza Huruma na ndiomana Kisu alipoweka ugonjwa kwa Marium ni Huruma aliyekwenda kuutoa kwani alishajua nia ya kaka yake ni nini, alitaka kuwafilisi zaidi ya zaidi hadi waone dunia chungu. Kweli mchawi hana akili, yani mtu anaamua tu kumtesa ndugu yake bila sababu za msingi.

    Siku zote Nyuta alifanya vitu kwa kudhamiria na alijisikia amani sana anagofanya vitu vya ajabu na vya kusikitisha.

    Alishapanga kumjaribu mtoto Pendo ili kupima udadisi alionao juu yake.

    Nyuta hakuwa na huruma kwa mtu yeyote, yeye alichojua ni kufanya roho mbaya tu hakuona umuhimu wa kumuhurumia mtu yeyote.

    Tabia ya Huruma ilimkera sana Nyuta kiasi kwamba akafikiria hata kumuua kama asingekuwa amempa uchawi pia kwani Huruma alikuwa ni mchawi wa ajabu wakati siku zote wachawi wanakuwa na roho mbaya na ya kikatili kama roho ya Nyuta. Mchawi huwa hapendi mwenzie afanikiwe, alikuwa hapendi mtu aendelee kimaisha.

    Apendacho yeye ni kuona mtu akididimia siku zote.

    Kulikuwa na jirani wa Nyuta aliyeitwa mama Salome, mama huyu alikuwa na binti yake huyo Salome aliyekuwa akipenda sana shule na akaahidi kusoma sana ili kuleta maendeleo kijijini kwao, wanakijiji wengi walimpenda Salome kwa juhudi zake bila ya kujua kwamba kuna mtu mmoja wanae pale kijijini akiwa ni kungwi wa wachawi na kila mahali alipofika lazima apewe uwenyekiti wa uchawi.

    Nyuta akafanya taratibu kwanza kabisa kuizorotesha familia ya Salome.

    Siku hiyo Salome akiwa anaenda shule, akakutana na nyoka mkubwa jamii ya chatu njiani, Salome akaogopa na kukimbia kwao, alipowaambia nao wakaenda ili kushuhudia nyoka huyo ila hawakuona chochote.

    Gafla Salome akajikuta akipatwa na uoga wa kwenda tena shule, kila muda aliposhtuliwa alikuwa akisema "nyoka"

    Wote wakamshangaa Salome kwani mwisho wa siku akawa kama mtu aliyechanganyikiwa, hakuna neno lolote atamkalo zaidi ya nyoka kila mmoja aliogopa jambo hilo. Ila mama Salome akakumbuka kwamba kuna muombeaji mashuhuri pale kijijini ambaye ni Nyuta, ama kweli mchawi mpe mtoto akulelee.

    Mama Salome akamchukua Salome hadi kwa Nyuta na kumuomba amuombee mwanae.

    Nyuta atafanyaje na wakati anataka kuwadhihirishia watu kuwa yeye anatumiwa na Mungu.

    Ikambidi amchukue Salome na kwenda kumuombea kwenye chumba chake cha maombi, baada ya muda kidogo Salome alirudishwa akiwa mzima kabisa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mama Salome akafurahi sana na hakutaka kupoteza muda tena, akampeleka mwanae kijiji cha mbali ili akasome huko na yeye akawa anarudi kupambana na maisha ya pale kijijini.

    Nyuta alichukizwa sana kwa kitendo cha kumrudisha mtu aliyemroga ili awe katika hali ya kawaida kwa njia tofauti.

    Alichukizwa na mama Salome akaamua nae kumuweka katika mlolongo wake, tena yeye akaamua kumfanyia upesi kabla hajarudi tena na kusema aombewe.

    Mama Salome akiwa njiani anarudi, mara akatokea nyoka na kumgonga mguuni. Mama Salome hakuweza hata kusogea ikawa hapohapo akaanguka chini na kufa.

    Sasa hiyo ikawa ni furaha kubwa sana katika moyo mbaya wa Nyuta.

    Miaka ikapita na siku zikapita, ikawa ni afadhari kwao Marium na familia yake. Wakajua kidogo majanga yamepungua kumbe adui akiwa kimya ujue anajipanga kwa mashambulizi kwahiyo unapokuwa vitani lazima ujikamilishe muda wote ule ili adui asiweze kukushambulia.

    Marium aliendelea na maisha huku akijiwekea tahadhari kubwa sana baada ya kuambiwa kuwa adui wanaye karibu sana, hakutaka kutetereka kwa kipindi alichopata tena, hakutaka ile dhiki ya mwanzo impate tena.

    MARIUM: Kwakweli sasa hizi tuna amani.

    MUSSA: Kweli kabisa, sasa hivi ni amani.

    MARIUM: Hivi ule uvimbe nilioambiwa uko tumboni ulipoteaje?

    MUSSA: Labda mama yangu alikuombea ndiomana ukapotea.

    MARIUM: Mmh labda.

    Ingawa Mussa alimwambia hivyo Marium ila alijua wazi chuki aliyonayo mama yake dhidi ya Marium, kwani Nyuta hitaji lake kubwa ni kuwa Mussa aachane na Marium.

    Adui anapopumzika ujue mashambulizi yamehamia kwingine au anajipanga kwa mashambulizi ya zaidi. Ila Marium hakujua adui yake yupo kwenye mpango gani kwa sasa, na wala hakufikiria kama mama mkwe wake ndio adui yao mkubwa pale walipo yeye na mumewe.

    Pendo sasa akiwa sekondari, siku hiyo akiwa anatoka darasani kwenda bwenini, njiani akakumbuka na upepo mkali sana hadi akaanza kuogopa kwani alikuwa peke yake.

    Kesho yake akajikuta ametokwa na vipele vingi usoni na mapajani.

    Pendo hakujielewa kabisa, mara akaanza kuvimba mwili mzima na baadhi ya sehemu za mwili wake zikawa zinatoa povu.





    Pendo akaanza kutokwa vipele usoni na mapajani, mara akaanza kuvimba mwili mzima na baadhi ya sehemu za mwili wake zikawa zinatoa povu.

    Kila mmoja pale shuleni aliushangaa ugonjwa anaougua Pendo ilikuwa ni ajabu sana, sura ya Pendo ilitisha kwani ilibadilika na kuwa kama sura ya mnyama, walimpeleka Pendo hospital lakini haikuwasaidia chochote kwani kila siku hali yake ilizidi kuwa mbaya, walimu wakaona sasa watampoteza mtoto wa watu akiwa mikononi mwao, wakaamua kumsafirisha na kumrudisha kwao ili kama hata akifa afie mikononi mwa wazazi wake.

    Pendo alitisha sana hakuonekana kama ni binadamu wa kawaida.

    Nyuta nae akawa ameenda mjini kumtembelea mwanae Mussa na alijua tu kwa tatizo lile lazima Pendo atarudishwa nyumbani.

    Na kweli wakiwa pale nyumbani, wakawaona walimu wa Pendo wakija na mtoto wao pale nyumbani, hawakutaka kuamini kama yule ndio Pendo kwajinsi alivyoharibika.

    Marium alijikuta akilia sana kumuona mwanae akiwa kwenye hali ya namna ile. Walimu ndio walio waambia kama yule ni Pendo.

    MWALIMU: Tumeona hali yake inazidi kuwa mbaya ndiomana tumeamua kumrudisha nyumbani ili apatiwe uangalizi wa karibu zaidi.

    MUSSA: Asanteni walimu kwa kumrudisha mtoto wetu.

    Nyumba nzima ilitawaliwa na kilio kasoro Nyuta pekee kwani alikuwa anajua alichokifanya kwa mtoto Pendo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walimu walipomkabidhi Pendo pale nyumbani, wakaaga na kuondoka.

    Pendo alikuwa na hali mbaya sana hata ilikuwa ni ngumu kumtazama jinsi alivyokuwa.

    Nyuta alitulia tu kuona kama atapewa jukumu la kuombea ama vipi, mara akamsikia Marium akiwa na ujasiri na kuanza kumuombea mwenyewe mtoto wake.

    Nyuta akachukia na kuamua kufanya mambo ya haraka pale, akampigisha mweleka Marium na kuanguka chini, na kitendo cha gafla kikatokea mahali pale kwani Marium alipoinuka alijikuta amepatwa na kidonda kwenye mguu wake, mwanzoni ile sehemu ilikuwa na kipele cha kung'atwa na mbu ila sasa iligeuka na kuwa kidonda, Mussa aliweza kuyaona hayo ikabidi akamfate mama yake aliyekuwa amekaa nje na kumuomba.

    MUSSA: Mama najua wewe ni muombaji mzuri sana, tafadhari njoo uiombee familia yangu mama.

    Kwanza Nyuta alijisikia raha sana kwa kupewa hiyo heshima, lengo lake lilikuwa ni kumuombea Pendo hadi aonekane amepona kabisa.

    Basi akaingia ndani, akawaambia wamwache Pendo ili aende nae chumbani kumuombea, huko akakaa nae kama nusu saa.

    Baada ya kurudi kutoka huko akawaomba wampashie maji ili akamuogeshe mwenyewe, wakafanya hivyo na kumpa hayo maji. Akayafanyia dawa zake maji hayo na kuanza kumuogesha Pendo, uchafu wote ukatoka na kuondoka kabisa. Nyuta na Pendo walipotoka bafuni kila mmoja alistaajabu muonekano wa Pendo kwani alikuwa ni mzima kabisa kama sio yule aliyeletwa hoihoi na walimu wake.

    PENDO: Asante bibi kwa maombi yako na kuokoa maisha yangu.

    NYUTA: Mjukuu wangu wanadamu wabaya sana, hawakutaka usome jamani.

    PENDO: Bibi inamaana nilirogwa?

    NYUTA: Hapana mjukuu wangu, kwanza napenda kukwambia kuwa usipende sana kuamini habari za uchawi na ushirikina mjukuu wangu.

    PENDO: Hata serikali yetu haiamini hayo mambo bibi ila inasemekana yapo.

    NYUTA: Ushawahi kuona uchawi Pendo?

    PENDO: Sijawahi.

    NYUTA: Sasa unasemaje kuwa uchawi upo wakati hujawahi kuuona? (Nyuta alikuwa akiendelea kupeleleza uelewa mdogo wa Pendo).

    PENDO: Bibi sasa kama mimi ugonjwa niliokuwa nao ulikuwa ni ugonjwa gani?

    NYUTA: Ile ni aleji ndomana ukavimba mwili inaonyesha ulikula kitu kisichofaa.

    PENDO: Bibi kumbe wewe ni msomi eeh!! Hata hospitali walinambia ni aleji.

    NYUTA: Mimi ni msomi ndio wa kipindi kile cha mkoloni, na sifa kubwa ya wasomi huwa hatuamini uchawi kama upo.

    PENDO: Sawa bibi, na mimi kuanzia leo natoa kabisa imani kwamba kuna uchawi duniani.

    Nyuta akafurahi sana kwa kuweza kuiteka vilivyo akili ya Pendo kwani kati ya watoto wa Mussa, ni Pendo ndio alimsumbua akili yake kwa sana.

    Nyuta hakujishughulisha kabisa na kile kidonda alichompatia Marium kwani alikuwa hampendi kabisa Marium.

    Baada ya wiki Nyuta akaaga na kuondoka akarudi nyumbani kwani baada ya kukamilisha kazi yake iliyompeleka mjini.

    Kisu aliendelea na mambo yake ya uchawi na ushirikina, mtaa aliokaa alimjaribu kila mtu mgeni aliyefika na kuishi eneo lile, wengine wakaona mtaa ule mbaya wakahama, wenye makazi yao ya kudumu wakashindwa cha kufanya, kuna wengine wakawa kila leo kwa waganga kutafuta dawa ili wajinusuru kwani mbaya wao hawakumjua.

    Kisu yeye alikuwa akimuua mtu basi anamtoa kuwa nyama ya wachawi tofauti na mama yake ambaye kazi yake ilikuwa ni kutunza misukule ambapo alijisikia fahari sana kuwa na misukule mingi atakavyo.

    Kisu kama ambavyo alisaidiwa na mama yake aliyekuwa na nguvu ya ziada kumpata yule msichana aliyempenda wakati yule msichana hakumtaka yeye.

    Yule msichana alionekana kuwa na kitu kilichofanya asirogeke kirahisi, binti huyo aliitwa Gina. Huyu ndio binti aliyemsumbua sana kisu katika kumvuta kwenye himaya yake, na alipompata tu akaamua kumpa ujauzito ili asifurukute tena kwenye himaya yake.

    Kama ilivyo kwa Gina, kuna baadhi ya watu pia wamejikamilisha katika maisha yao na hawarogeki kirahisi kama afanyavyo Kisu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kukawa na mmama mmoja wa kitanga, akahamia mtaa anaokaa Kisu, mama huyu alijulikana kwa jina la mama Grace.

    Kama kawaida ya Kisu akaenda kumroga yule mama, badala yake ni yeye Kisu akarudi na ugonjwa nyumbani kwake. Akavimba tumbo likawa kubwa kama mama mwenye mimba ya miezi tisa, akababuka mwili la kila mtu akamshangaa Kisu jinsi alivyobadilika.

    GINA: Kwani unatatizo gani?

    KISU: Sijui hata nimepatwa na nini, nadhani ni upepo mchafu umenipitia.

    GINA: Pole sana Kisu, sasa itakuwaje maana kila siku hutaki kwenda hospitali.

    KISU: Usijari nitaenda kwa mama ataniombea kwani ni mwanamaombi.

    GINA: Pole sana, itabidi tufanye hima uende huko ukapate kupona jamani.

    Kisu alijilaumu sana kwa kitendo cha kwenda kumroga mama Grace kwani ndio kitu kinachomtesa kwa wakati huo.

    Kidonda cha Marium kilizidi kuwa kikubwa na pia kikawa kinavuja maji.

    Marium hakuelewa kuwa aende wapi ili akapate tiba ya kidonda chake.

    MUSSA: Pole sana mke wangu, hata sikufikiria kama kile kidonda ndio kingekuwa kikubwa kiasi hicho.

    MARIUM: Hata na mie kinanishangaza kila siku kinavyozidi kuwa kikubwa, kama sindano nimeshachoma hadi basi lakini bado hali mbaya.

    MUSSA: Labda tukajaribu na dawa za mitishamba mke wangu.

    MARIUM: Labda kwani kidonda hiki kinanipa maumivu makubwa na ya ajabu ambayo sijawahi kupata kwakweli.

    MUSSA: Pole sana.

    Kwakweli kidonda kile kilimtesa sana Marium na ubaya zaidi ni kuwa hakujua kama kile kilikuwa ni kidonda cha kutumiwa, kumbe siku aliporudi Pendo na kutaka kumuombea yeye, Nyuta alichukia na kuuchukua ugonjwa wote wa Pendo na kuuelekeza kwenye kidonda kile, kwani wachawi hupenda kutumia kitu kidogo kwenye mwili wako wanakikuza halafu kinakuwa ni mateso maishani mwako.

    Siku hiyo wakiwa wamelala, ile kushtuka Marium alishangaa kuona funza wakitoka kwenye kile kidonda chake.



    Wakiwa wamelala, ile kushtuka Marium akashangaa kuona funza wakitoka kwenye kile kidonda chake.

    Marium akamshtua mumewe, naye akamwangalia mkewe kwenye kile kidonda akastaajabishwa na wale funza waliokuwa wanene sana wakitoka kwenye kile kidonda. Marium akapata maumivu makubwa, mumewe akamshauri Marium kuwa waende hospital ila Marium aliona kuwa kwa hali hiyo hata huko hospitali pasingesaidia kitu.

    Marium alijisikia vibaya na alipatwa na maumivu sana pale kwenye kidonda.

    Kufika asubuhi kile kidonda kikawa kinatoa usaha na wale funza. Marium akachukua upande wa khanga na kujifunga kwenye kidonda chake, akamuaga mumewe kuwa anaenda kwa bibi yake na anatumaini huko atapata dawa za kienyeji za kumtibu.

    Marium akiwa njiani kuelekea kwa bibi yake, bus walilopanda likapata pancha ikabidi lianze kutengenezwa.

    Mguu wa Marium ulikuwa hautamaniki kwani nzi wengi waliufata na ulikuwa unatoa harufu kali sana kama samaki waliooza.

    Gari ilipotengemaa, wenye gari wakagoma kuendelea na safari, ni hapo Marium alipowaza kuwa kama angekuwa na usafiri wake basi yote hayo yasingewatokea.

    Ikabidi wasubirie usafiri mwingine.

    Hawakupata usafiri mwingine kwa siku hiyo ikabidi walale njiani, kesho yake likaja gari lingine na kuwabeba wale abiria na safari ikaendelea.

    Hadi Marium alipofika kwa bibi yake alifurahi sana ingawa alikuwa akiburuza ule mguu wake.

    Alipofika akamweleza yote yaliyomtukia bibi yake.

    BIBI: Pole sana Marium, safari yako ina vikwazo vingi.

    MARIUM: Kweli kabisa bibi, vikwazo ni vingi sana.

    BIBI: Adui amekuzingira, hataki uendelee kamwe.

    MARIUM: Ndio hivyo bibi, ona ninavyoteseka na huu mguu.

    Bibi yule akampondea dawa Marium na kumpaka kwenye kile kidonda chake.

    Akapatwa na maumivu makali sana ila baada ya siku mbili akiwa kule kwa bibi yake, kile kidonda kikaanza kukauka na yule bibi hakuacha kumpaka dawa Marium mwisho wa siku kikakauka kabisa.

    Bibi akafurahi na kuamua kumpa dawa ya kunywa Marium na kumwambia hakuna mtu atakayeutesa mwili wa Marium tena.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Marium akawa huru na mzima kabisa.

    MARIUM: Ila bibi si ungenitajia mbaya wangu tu.

    BIBI: Ipo siku utamjua mbaya wako ila sio sasa.

    Marium akashukuru kwavile alikuwa ameshapona kabisa.

    Marium alirudi nyumbani kwake akiwa mzima wa afya na akiwa na nguvu mpya na kasi mpya.

    Kila alichokifanya kipindi hiko kilifanikiwa, ndio hapo alipoamua kumpeleka mwanae Abra akasome nchi nyingine. Na watoto wake wengine wakaendelea na masomo vizuri.

    Maisha ya Marium na familia yake yalitengemaa sana na walikuwa na furaha ya kupitiliza.

    Marium alijua mambo yote yamekwisha bila kuelewa kwamba kimya cha adui siku zote ni kujipanga kwa mashambulizi zaidi.

    MUSSA: Mke wangu, angalau sasa tuna furaha na amani.

    MARIUM: Kweli mume wangu, sasa nadhani adui ameshindwa na hana uwezo tena wa kutudhuru.

    Ilikuwa ni furaha kwa upande wao, ila mara nyingi upande mmoja ukifurahi jua mwingine umeumia.

    Kilikuwa ni kipindi chema kwa Marium na familia yake.

    Kisu alizidi kuumwa na tumbo na pia lilizidi kuvimba.

    Ikabidi Kisu amwambie ukweli mkewe Gina kilichopelekea mpaka yeye akawa vile, kwanza Gina alishangaa kuwa kipindi chote hiko alikuwa anaishi na mwanaume mchawi sana.

    Ikabidi Gina aende kwa mama Grace akamuombe amuachie mumewe.

    GINA: Nakuomba mama, muhurumie mume wangu.

    MAMA GRACE: Nataka iwe fundisho kwake na wachawi wengine wote kuwa si kila mtu wamuonaye basi anafaa kurogwa.

    GINA: Jamani kuwa na huruma basi.

    MAMA GRACE: Wapo wa kuwahurumia ila siwezi kumuhurumia mchawi.

    Mama Grace alishikilia msimamo wake hadi mwisho kuwa hawezi kumuhurumia mtu mchawi.

    Hali ya Kisu ilizidi kuwa mbaya, ikabidi asafiri na kurudi kwa mama yake.

    Nyuta alimuhurumia sana mwanae ila pia hata yeye mwenyewe hakuweza kupata muelekeo unaofaa wa mwanae hakujua ampe nini ili apate kupona.

    Ila Kisu alizidi kuumwa kila siku hakupatwa na unafuu hata kidogo.

    Siku hiyo Kisu alihisi tumbo linataka kupasuka, akapiga kelele sana na mwisho wa siku akafa.

    Msiba ule ulipotokea Gina alikuwa bado yupo kwake.

    Akaenda kuangalia vitu vya mumewe ndani, ile kufungua kabati akakumbana na paka mweusi sana na mwenye macho makali hapohapo Gina nae akazimia.

    Majirani hawakuelewa kinachoendelea hadi pale waliposhindwa kumuona na kuamua kumfata ndani, wakashangaa kumkuta amezimia.

    Wakamchukua na kumtoa nje kwenye hewa.

    Wakiwa wanashangaa gafla wakamuona Nyuta akiwa mahali pale, nia yake ni kwenda kuchukua vitu vya kichawi alivyoacha mwanae ndani ya nyumba hiyo.

    Nyuta aliingia ndani na kuchukua vya kuchukua akatoka bila ya kuaga wala kumsemesha mtu yeyote akaondoka, kwakweli walishindwa kumuelewa kabisa mama huyo.

    Nyuta aliumia sana kumpoteza kijana wake, roho ilimuua ile kupitiliza. Nyuta akasema kuwa anajipanga kwa mashambulizi kwani hawezi kukubaliana na hali hiyo hata kidogo.

    Nyuta akamvizia yule mtoto atakayezaliwa na Gina ili amuweke rasmi kwenye kazi yake.

    Watu wakamuonya Gina nae akasikia maonyo yale akaamua kukimbia na kwenda kuishi mbali ili awe salama na mtoto wake.

    Nyuta alikuwa na hasira ya kupitiliza, sasa roho mbaya yake ilizidi kwa ile ya mwanzo. Hakumuhurumia mkubwa au mdogo, kila aliyechomoza mbele yake akawa adui yake.

    Alikuwa ni mchawi wa kuogofya kwa kipindi hiko, hakuwa na masihara na mtu yeyote.

    Ingawa Gina alimkimbia Nyuta lakini ilikuwa kazi bure, Nyuta akatumia uchawi wake kuiharibu mimba ya Gina na kukivuta kiumbe ambacho kilikuwa bado hakija timiza siku za kutoka kwenye uso wa dunia.

    Nyuta alikuwa zaidi ya mnyama hata mwanae Huruma aliamua kumuhama mama yake pale kwenye nyumba yao kwani hakupendezewa na unyama alionao mama yake kwa kipindi hiko.

    Baada ya miaka kama miwili kupita, Marium na mumewe wakiwa wamepumzika ndani kwao wakapatwa na taarifa ya kusikitisha sana, Marium hakuamini kabisa alichoambiwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Marium na mumewe wakiwa wamepumzika wakapatwa na taarifa ya kusikitisha sana.

    Wakapewa taarifa kuwa bibi yake na Marium amefariki, kwakweli Marium alisikitika sana kwani bibi huyo ndio alikuwa msaada mkubwa sana kwa Marium kipindi chake cha matatizo.

    Marium aliona nguzo yake imedondoka kwa sasa.

    MARIUM: (Huku machozi yakimtoka), kwanini amekufa jamani?

    MUSSA: Mke wangu, tusimkufuru Mungu. Twende tu huko msibani.

    MARIUM: Mussa jamani, nitakimbilia wapi mimi?

    MUSSA: Pole Marium mke wangu.

    Mussa na Marium ikabidi wasafiri waende kwenye msiba wa bibi yake Marium.

    Na huko ndipo wakapata taarifa rasmi za namna bibi huyo alivyokufa, kwani kwa mujibu wa daktari aliandika kuwa bibi huyo alikufa baada ya kuanguka kifafa.

    Nyuta alikuwa na hasira sana juu ya kifo cha mwanae, alitamani afanye mambo mbalimbali ili amrudishe duniani lakini ilishindikana.

    Nyuta akaenda kufanya mambo mbalimbali katika mtaa ambao mwanae alikuwa anakaa, kwanza kabisa alitengeneza mapaka ya kutosha na kuyatupia kwenye ule mtaa, na hiyo kitu ikafanya kuwa vigumu kumtambua paka wa kawaida na yule wa kutengenezwa.

    Mtu ukikatiza kwenye mtaa huo ilikuwa uthithubutu kuparuliwa na mmoja wapo wa mapaka yale kwani utazua ugonjwa wa ajabu mwilini mwako.

    Nyuta aliyaweka yale mapaka ili yajeruhi watu na mtu yeyote atakayekatisha basi akishambuliwa na paka mmoja ajue kifo kinamuita. Alifanya hivyo sababu alichukizwa sana na mambo ambayo yalimpata mwanae kipindi akiishi mtaa huo.

    Mapaka yale yalikuwa yamechanganyika na paka wa kawaida kwahiyo ilikuwa ni vigumu kuwajua paka wa kawaida ni wepi, kwani hakukuwa na tofauti ya haraka kati yao.

    Wale mapaka walikuwa na uwezo wa kuingia hata ndani, hasa kwenye zile nyumba zenye paka. Wanakuwa karibu na paka wa nyumba hiyo na mwisho wa siku wao wanajigeuza kuwa huyo paka, mtu akimsogelea ili acheze nae ndio hapo anapomparua wakati anapatwa na ugonjwa wa ajabu yule paka anaondoka na kurudi paka aliyezoeleka hapo.

    Ndio kitu kilichofanyika kwa bibi wa Marium, mmoja wa wajukuu zake alipokuwa mjini alikatisha mtaa huo alioishi Kisu, akakutana na kapaka kadogo akakapenda sana, akakabeba na kwenda kuishi nako kijijini bila ya kujua kama wale paka si wa kawaida, na kufika huko, bibi akapatwa na mashaka kuhusu yule paka ndipo hapo alipowaambia ili wafanye shauri la kumtupa ila kabla ya kufanya chochote kale kapaka kakamperuhi yule bibi, ndio hapo alipoanguka kifafa na kufa.

    Wakina Marium walipopata habari kwamba kifo cha bibi yao kimesababishwa na kuparuliwa na paka walishangaa sana na pia walistaajabu sana.

    Mama Grace alijikinga ila akasahau kuwakinga watoto wake, kitendo hiko kikafanya Grace aparuliwe na moja ya mapaka yale, aliporudi kwao alikuwa kama ni mtu mwenye kifafa, alikuwa anaanguka na kutoa povu jingi sana, na mwisho wa siku Grace akafa.

    Baada ya maziko yake, mama Grace hakutulia aliamua kufunga safari na kwenda kwao ili kufanya uchunguzi wa kifo cha mwanae.

    Huko akaambiwa kuwa kilichomuua mwanae si paka wa kawaida kama walivyoona ila ni mipaka ya kichawi.

    Mama Grace alisikitika sana, na huko akapewa dawa ya kuwakinga wanae wengine waliobakia.

    Ikabidi apeleke ile taarifa pale mtaani, watu wa mtaa ule walijikuta wakiwachukia paka kupitiliza kwani walishapoteza ndugu jamaa na marafiki waliojeruhiwa na mapaka hayo.

    Kila mmoja alijikuta akiwa na hasira na mapaka hayo, wengi waliamua kuwaua hata wale paka wa majumbani ili kuepukana na tatizo na wengine walibeba silaha na kufanya hiyo operesheni ya kuua paka kwenye mtaa huo.

    Paka ni mnyama ambaye ni mgumu sana kufa hadi watu wengine husema kuwa paka ana roho saba.

    Wachawi wengi hupenda kuwatumia paka katika kazi zao, kwasababu ni wagumu kufa na wanaendana na kazi yao kwani paka ni mnyama katili na mwenye kumbukumbu ya haraka sana tena kumbukumbu yake yaweza kupita hata ya binadamu ndiomana unapokwenda kumtupa hata iwe mbali vipi utashangaa amerudi kwa muda mfupi sana, paka ni mnyama mwenye ugunduzi wa hatari kwa haraka sana ndiomana ni mara chache sana kusikia paka amekula sumu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kutokana na sifa alizonazo paka ndiomana wachawi wengi hupenda kumtumia kwenye kazi yao ya kichawi.

    Baada ya kumaliza ule msiba wa bibi yao, Marium na Mussa wakawa na safari ya kurudi nyumbani kwao.

    Nyuta alikuwa anajua kuwa Marium anakaribia kurudi kwake, alichofanya Nyuta ni kutegesha dawa kwenye njia watakayopita kwa miguu ili Marium akanyage dawa hiyo kwani katika watu aliokuwa hawapendi Nyuta basi Marium alikuwa mmoja wao, alijikuta akimchukia Marium bila ya sababu yoyote ya msingi kwani Marium hakuwahi kutenda chochote kibaya kwa mama huyo ila Nyuta alikuwa akimchukia tu.

    Wakiwa wanatembea ili kufata mahali walipopaki gari yao, mara gafla Mussa akakanyaga kijiwe cha moto sana mguuni mwake, Mussa alijikuta akipiga ukelele kama mtoto mdogo, Marium akashaajabu sana kuona kuwa eti kuna kijiwe kiliingia kwenye kiatu cha wazi kwenye mguu mmoja wapo wa mumewe na walipojaribu kukiangalia hiko kijiwe hawakukiona tena.

    Baada ya maumivu kupoa kidogo, ndipo wakaondoka na kufata gari yao kurudi nyumbani.

    Walipofika nyumbani, Mussa bado aliendelea kulalamika kuhusu maumivu ya mguu kwenye unyayo wake.

    MARIUM: Hata sielewi mume wangu ni kijiwe cha aina gani ulichokanyaga.

    MUSSA: Hata na mimi nimeshangaa, kilikuwa cha moto sana kama vile kimewashwa moto.

    MARIUM: Pole ila pakiendelea na maumivu itabidi twende hospitali.

    MUSSA: Kweli kabisa maana mguu unapwita huo balaa.

    Hakuna aliyeelewa kati yao kama kile kitu kiliwekwa na Nyuta kwa lengo la kumdhuru Marium ila kwa bahati mbaya amekikanyaga mwanae mwenyewe.

    Baada ya maumivu ya ule mguu kuzidi, ikabidi waende hospitali ambapo Bwana Mussa akachomwa sindano moja na kuandikiwa baadhi ya madawa ya kumeza.

    Kumbe dozi hizo ndio zikaenda kuamsha kila kitu kwenye mwili wa Mussa bila ya kujua.



    Mussa akachomwa sindano na kuandikiwa vidonge ambavyo alitakiwa kutumi.

    Dozi hiyo ndo ikaenda kuibua kila kitu kwenye mwili wa Mussa.

    Alijisikia uchovu kwa muda wote kwenye mwili wake.

    MUSSA: Yani mwili wangu unachoka kweli.

    MARIUM: Pole sana ila ndo hivyo itabidi tutafute dawa ya hapo mapema sana.

    MUSSA: Kweli kabisa maana haya maumivu ni kama roho inatoka vile.

    MARIUM: Naelewa mume wangu ila yote haya ni mapito tu kuna muda yataisha yote.

    MUSSA: Ndio yataisha ila sisi tunaandamwa sana jamani.

    MARIUM: Tena sana ila ipo siku tutamjua mbaya wetu.

    Nyuta ambaye ni nguli wa uchawi aliendelea kufanya mambo ya ajabu mtaa kwa mtaa hakuona shida wala tatizo sana kuendelea kuua watu na kuwatokomeza kabisa. Nyuta alikuwa na roho mbaya iliyopitiliza.

    Hakuona shida kuweka wadudu wa ajabu ili kutisha watu, na pia aliwafanya watu wasijue moja kwa moja mambo yanayotendeka.

    Yusuphu aliyajua mambo mengi afanyayo mkewe, kitu hiko kilimfanya amchukie Nyuta siku zote ila tatizo ni kuwa hakujua ni jinsi gani apambane na huyo mdudu Nyuta.

    YUSUPHU: Ningekuwa na uwezo hata simu ningemuwekea.

    NINA: Ametufanya tuwe wapweke sana hapa duniani, kwakweli namchukia sana Nyuta.

    YUSUPHU: Ubaya ni kuwa mwanangu bado hajajua kama mama yake ni mtu mbaya.

    NINA: Ni vigumu kwake kujua mpaka yatakapo mtokea ndugu yangu.

    Mussa baada ya kurudi kwake mara nyingine alihisi kama mguu ukimpwita zaidi na mara nyingine alijihisi kupata unafuu.

    Binti zao Pendo na Amina wakaamua kurudi nyumbani.

    Amina akaamua awe anatokea nyumbani kuelekea kazini kwake nae Pendo aliamua awe anatokea nyumbani kuelekea chuoni.

    Kwahiyo kwa kipindi hiko walikuwa wakiishi na binti zao hapo nyumbani.

    Marium alipoona mumewe akizidi kulalamika maumivu ya mguu, akaamua kufunga safari na kuelekea kule alipokuwa akiishi bibi yake kama labda atapata dawa ambayo yeye alipakwa mwanzoni wakati amepatwa na kidonda mguuni.

    MARIUM: Nikiipata ile dawa nadhani itamsaidia na baba yenu pia.

    AMINA: Na aliyekupaka hiyo dawa ameshakufa, sasa utaipataje?

    MARIUM: Hata sijui ila naenda kujaribu tu labda nitaipata mwanangu. Ilinisaidia sana mimi ile dawa.

    AMINA: Sawa mama, tunakuombea ufanikiwe na uipate hiyo dawa mama yetu.

    MARIUM: Asanteni wanangu kwa dua zenu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku aliyoondoka Marium ndio siku hiyo ambapo ilikuwa mbaya na kuharibu historia ya familia hiyo. Mussa wakati yupo chooni, akaona kama kitu kikimsukuma na mara gafla akaanguka humo na kushindwa kuinuka tena, ndio hapo binti zake Amina na Penda walipomchukua na kumpeleka hospital na hata hivyo wakarudi nae nyumbani akiwa amepooza viungo vyote.

    Na hadi siku ambayo Marium amerudi alimkuta mume wake na hali mbaya sana.

    Hawakuwa na la kufanya na hata Marium hakuipata ile dawa aliyoenda kuifata kule kijijini. Na hali ya Mussa ilipozidi kuwa mbaya, wakamuwahisha tena hospital na Mussa nae akafariki.

    Wakalia sana na kuomboleza. Hawakujua kwanini imekuwa hivyo ilivyokuwa.

    Ukatokea mtafaruku wa mahali pa kumzika, mtafaruku huo ulitokea kati ya Marium na Nyuta ambapo Nyuta aling'ang'ania mumewe azikwe karibia na wanapoishi.

    Kwa wakati huo hakuna aliyeelewa kwanini Nyuta anang'ang'ania ile maiti. Kumbe Nyuta alikuwa na mambo yake ya kufanya kwa ile maiti.

    Kwavile Marium akafanya kiburi na kuzika anapotaka yeye ndio hapo akapanga kumkomesha Mariam.

    Walipokuwa kwenye matanga na tayari wameshazika ndipo usiku huo wakapatwa na maajabu mule ndani, hakuna aliyeelewa ila ilikuwa ni siku hiyo Nyuta alipoweka misukule kwenye nyumba ya Marium, lengo lake ni kumtesa na kumkomesha. Na kweli alimtesa sana na ile misukule yake.

    Hata ingia ya ile misukule mule ndani ilikuwa ni ya fujo sana, mara nyingine Nyuta anajilaumu kwa kumuua mwanae ila mara nyingine alijisemea kuwa alipaswa kufanya hivyo kwani alishaharibu mlolongo wa dawa toka mwanzo.

    Nyuta hakuishia hapo tu, akamvizia Abra aliporudi nae akamtokomeza na pia akang'ang'ania kudai ile maiti.

    Alipo kataliwa akawafanyia mambo mengi ya ajabu na ya kutisha walipokuwa makaburini na hakuishia hapo tu akaendelea kuwafanyia mambo ya ajabu hata walipokuwa nyumbani, akawa anafanya mambo ya ajabu na vitendo vya kuogopesha na kuzidi kuwaogopesha hata wale walikuwa wanataka kuwasaidia.

    Nyumba ya Marium ikageuka ni nyumba ya misukule. Hata hivyo wenye usaidizi wenyewe walishindwa kuwasaidia, basi Marium akawa ni mtu wa kuteseka tu kwani misukule ile ilikula kila kitu cha mule ndani ilitia hasara kubwa sana hakuna mfano hadi pale Marium alipopata mganga wa kwenda kuisafisha nyumba yake na ndio huko wakagundua kwamba mambo yote waliyoyaona na kuyasikia yalikuwa yakifanywa na Nyuta, mtu ambaye walikuwa kumsililiza sana.

    Pia Yusuphu aliweza kuwaeleza hali halisi kuhusu Nyuta, hapo wakapata kutambua mengi na kufahamu mengi kuhusu Nyuta.

    Wakajiuliza sana kuwa kwanini Nyuta aliwafanyia alivyowafanyia.

    Ni kipindi hiko ambacho Pendo akasema ya kwamba yeye ataenda kupambana nae.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog