Simulizi : Malaika Wa Kifo
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Edmund akaingia vitani kwa ajili ya kukamilisha idadi kubwa ya watu ambao alikuwa amekabidhiwa. Kazi yake kubwa haikuwa kuingia msituni, kuchukua silaha na kisha kuanza kuua, kazi kubwa aliyokuwa nayo kwa wakati huo ni kukitumia kioo kilekile kuwaua watu aliokuwa akiwataka na kuwa kama sadaka.
Siku moja baada ya kumuua Filbert, Edmund akarudi katika jumba lile la kutolea sadaka kwa ajili ya kumtoa sadaka mtu mwingine. Alitaka kuhakikisha idadi ya watu mia moja na ishirini inakamilika hata kabla miezi sita haijatimia.
Mtu ambaye alikuwa akimfikiria kwa wakati huo alikuwa muigizaji mwingine ambaye alikuwa akichuana naye vikali, huyu aliitwa Mrisho Rajab ambaye alikuwa hoi kitandani akiugua Ugonjwa wa Dengu.
Mara baada ya kuingia ndani ya jumba hilo, moja kwa moja akapiga magoti chini na mwanaume mmoja akatokea mahali hapo huku akiwa amevaa nguo kubwa nyekundu iliyomziba mpaka kichwa chake.
Akaanza kumsogelea Edmund mahali pale alipokuwa na kisha kumchukua na kumpeleka mbele kabisa. Alipofika, akamkabidhi kisu na kutakiwa kulitaja jina la mtu aliyetaka kumtoa kafara mahali hapo hata kabla mambo mengine hayajaendelea.
“Ninataka kumtoa kafara Mrisho Rajabu, muigizaji mwenzangu ambaye ninadhani ana nyota kali zaidi yangu,” alisema Edmund kwa sauti kubwa, mara giza likatokea katika kioo kile, moshi ukaanza kufuka na Mrisho kuonekana katika kioo kile huku akiwa kitandani.
Alichokifanya Edmund ni kukishika kisu vizuri na kisha kukichoma katika kioo kile. Ghafla, katika hali iliyowashangaza hata madaktari waliokuwa ndani ya chumba kile, Mrisho akaanza kurusharusha miguu yake huku na kule na mapovu yakianza kumtoka.
“Kuna nini tena?” alisikika dokta mmoja akiuliza kwa mshtuko.
“Hata sisi hatujui dokta,” alijibu nesi aliyekuwa ndani ya chumba hicho.
Kila mmoja alikuwa amechanganyikiwa, mabadiliko ya hali ya Mrisho kitandani pale yalimshangaza kila mmoja. Walichokifanya ni kumuwekea mashine ya oksijeni lakini hali haikuonekana kubadilika, bado aliendelea kutoa povu mdomoni.
“Lete dripu, ichome sindano yenye dawa ya Micresiphine, fanya haraka,” alisema dokta akimtaka nesi kuchanganya dawa hiyo iliyowezesha kuyaweka mapigo ya moyo katika hali ya kawaida.
Kwa haraka dripu ikaletwa na kutundikwa huku ikichomwa sindano yenye dawa hiyo. Hali haikuonekana kubadilika, bado iliendelea kuwa vilevile, Mrisho alirusha miguu yake huku na kule na mapovu yakimtoka na mwisho wa siku, akatulia kimya.
Mapigo yake ya moyo yakasimama, daktari yule akajaribu kuyashtua ili yarudi tena lakini hilo likaonekana kuwa gumu kutokea, Mrisho akakata roho mbele ya macho yao.
“Mungu wangu! Ni nini tena hiki?” aliuliza nesi mmoja.
“Hata mimi nashangaa, Bongo Muvi imevamiwa kwa kweli, si jana tu ndiyo Filbert alikufa?”
“Ndiyo, tena sasa hivi watu wapo makaburini hapo Kinondoni wakiaga mwili wake.”
“Kwa hiyo na staa mwingine wa tasnia hiyo amekufa, aisee hii kweli sijawahi kuona,” alisema nesi mwingine.
Taarifa zikaanza kusambazwa kwamba Mrisho alikuwa amefariki dunia. Kilio kikawa mara mbili zaidi, ndani ya siku mbili, watu wawili tena wenye uwezo mkubwa wa kuigiza walikuwa wamekufa katika vifo vya kutatanisha.
Magazeti yakapata cha kuandika, watu wakaitumia mitandao ya kijamii katika kuzitawanya habari katika sehemu mbalimbali. Bongo Muvi ikapata pigo kubwa ambalo hawakuwa wamelitegemea hata siku moja, vifo vya watu wawili ndani ya siku mbili viliwashtua kupita kawaida.
“Mungu! Ni nini hiki? Tunaomba Edmund asife, manake amebaki peke yake, akifa huyo, bora Bongo Muvi nayo ife,” alisikika akisema jamaa mmoja.
Bado kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilikuwa siri kubwa, hakukuwa na mtu aliyefahamu kwamba nyuma ya pazia Edmund ndiye aliyekuwa akihusika na vifo vyote hivyo.
Mazishi yalifanyika harakaharaka, hakukuwa na Mmarekani yeyote aliyekuja nchini Tanzania na hata mpenzi wake, Stacie hakuweza kufika. Hali ya mazishi kufanyika kwa haraka ikaonekana kuwachanganya watu, kitendo cha kamati ya mazishi kukataa mwili kuagwa na watu waliofurika makaburini kiliwashtua wengi lakini hakukuwa na mtu aliyeonekana kujali.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kila kitu, Edmund aliendelea kuua kama kawaida yake. Kila siku watu waliokuwa wakifuatilia filamu nchini Tanzania walikuwa wakimuomba Mungu aweze kumlinda mtu huyo pasipo kujua kwamba yeye ndiye alikuwa mhusika mkubwa.
Bongo Muvi ikatawaliwa na damu, wasanii waliendelea kufa mfululizo mpaka wakati mwingine watu wengine kujitoa kabisa na kukataa kuigiza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Huyu ni malaika wa kifo, hakuna kingine!” alisema jamaa mmoja.
“Kwa hiyo unamaanisha Israel mtoa roho?”
“Ndiyo, atakuwa akifanya kazi yake, Mungu wangu! Hivi kwa nini inakuwa hivi jamani, au kwa sababu tasnia hii imetawaliwa na mambo ya kishetani?” aliuliza jamaa mmoja.
“Hilo sisi hatujui, cha msingi tumuombe Mungu tu na wale waliokufa, kwa pamoja tunasema ‘Inna lillah wainna ilaih rajiun’
*****
Kesi ilianza kuunguruma, watu zaidi ya mia tano walikuwa wamekusanyika katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo iliyokuwa ikimkabiri msichana mrembo aliyekuwa amejipatia jina kutokana na uigizaji mkubwa, Susan.
Watu hawakuonekana kutulia mahakamani hapo, kila mmoja alionekana kuwa na hasira mno, kitendo cha Susan kuhusishwa na kumuua Filbert kiliwafanya kumchukia msichana huyo.
Kila mmoja aliyekuwa amekusanyika mahali hapo alikuwa akitaka msichana huyo apewe hukumu ya kifo, hakukuwa na mtu aliyempenda, hata wale marafiki zake wa karibu, kwa wakati huo walikuwa maadui zake.
Ilipofika saa mbili asubuhi, karandinga likaanza kuingia katika eneo la mahakama hiyo, waandishi wa habari ambao walikuwa wamekaa mbali kidogo wakasogea na kisha kuanza kupiga picha.
Susan na maabusu wengine waliokuwa na kesi siku hiyo wakashuka kutoka katika karandinga lile na kuanza kuelekea mahakamani. Watu wakaanza kusikika wakizomea kwa sauti kubwa huku wengine wakipiga kelele ahukumiwe kifo kwa kitendo alichokifanya cha kumuua Filbert.
Hakukuwa na mtu aliyefahamu kile kilichokuwa kikiendelea. Susan akabaki akilia tu, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama mwisho wa kila kitu ungekuwa namna ile.
Japokuwa alikuwa akiufahamu ukweli halisi lakini hakukuwa na mtu aliyeonekana kuukubali ukweli huo, hata mahabusu wenzake alipokuwa akiwahadithia kilichokuwa kimetokea, hakukuwa na aliyemuamini hata kidogo.
“Sijaua, Mungu naomba unitetee, hakuna anayejua ukweli zaidi yangu na wewe, naomba unitetee Mungu wangu!” alisema Susan huku akibubujikwa na machozi.
Siku hiyo Susan hakutakiwa kuongea chochote kile, alikuwa akisomewa mashtaka kwa kile alichokifanya na baada ya hapo kesi kuahirishwa mpaka mwezi ujao.
“Boooooo....booooo....booooo....” watu walisikika wakimzomea kwa sauti za juu.
Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, kila wakati alikuwa mtu wa kulia tu, sauti za watu waliokuwa wakimzomea ziliuchoma mno moyo wake. Hakuwa na jinsi, kila kitu kilichokuwa kikitokea, alikiacha kikitokea kwa kuamini kwamba kuna siku watu wangekuja kujua kwamba hakuwa ameua kama ilivyokuwa ikijulikana bali Filbert alikufa kwa mipango ya Mungu.
****
Siku zikaendelea kukatika, waigizaji walikuwa wakipuputika kama kuku waliokumbwa na ugonjwa wa mdondo. Hofu kubwa ikatawala, kitendo cha wiki tatu kufariki kwa wasanii kumi hakikuonekana kuwa cha kawaida, kila mmoja akajua kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
‘MALAIKA WA KIFO AIMALIZA BONGO MUVI, MALAIKA WA KIFO AKATAA KUTOKA BONGO MUVI’ vilikuwa vichwa vya habari vya baadhi ya magazeti yaliyokuwa yakitolewa kila siku.
Magazeti yalinunulika, kila mtu alikuwa akitaka kujua ni kina nani walikuwa wakihusika na mauaji hayo au huyo Malaika wa Kifo alikuwa nani.
“Jamani, yatupasa tumuombe Allah sana, hii hali si kawaida kabisa,” alisikika mwanamke mmoja, alikuwa amevalia juba jeusi.
“Lakini sawasawa, nao wamezidi kufanya uasherati, acha waendelee kufa,” alisikika jamaa mmoja.
“Wewe Omari, hebu muogope Allah! Wewe msafi?”
“Afadhali yangu mimi, ila hawa waigizaji, bora wafe tu.”
Huo haukuwa mwisho, bado Edmund aliendelea kuwamaliza waigizaji kwa kisingizio cha kutaka kuwa juu zaidi ya watu wote. Kila kifo kilichokuwa kikitokea kilijaa utata mtupu.
Kuna wengine walikuwa wakifa huku wakiwa wamelala, wengine walikufa huku wakiwa wanatembea na hata wengine wakifa huku wakiwa wanafunga kamba za viatu. Hakukuwa na kifo kilichoonekana kuwa kifo halisi, kila kifo kiliacha utata mkubwa kwa watu.
Mpaka mwezi mmoja unakwisha, tayari waigizaji kumi na nane walikuwa wamefariki dunia katika vifo vya kutatanisha sana. Mwezi uliofuatia, ulikuwa mwezi wa vifo vya wanamuziki.
Alianza mwanamuziki King Junior. Alikuwa miongoni mwa wanamuziki waliokuwa wakivuma tena aliyekuwa akiitangaza sana Tanzania nje ya mipaka ya nchi hii, alikufa katika kifo cha kutatanisha kama wengine.
King Junior alifariki baada ndani ya gari lake alipokuwa akisoma gazeti. Kifo chake kilimshangaza kila mmoja, watu wakapigwa na bumbuwazi, hawakuamini kama kweli msanii huyo alikuwa amefariki dunia.
Nchi ya Tanzania ikawa kama imefunikwa kwa turubai kubwa, kila siku ulikuwa ukitokea msiba ambao uliwahusisha zaidi wanamuziki na waigizaji. Mara baada ya mwezi wa pili kukatika, wakaanza kufa wanasiasa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hali ilikuwa ni ya kutisha mno, walianza mawaziri kufa na baadae manaibu waziri, kwa kila kifo kilichokuwa kikitokea, kilikuwa chini ya Edmund, mtu huyo alikuwa akihusika kwa asilimia mia moja.
Watu wa maombi kutoka katika makanisa mbalimbali wakaanza kufunga na kuomba, walikuwa wakimuomba Mungu azuie kile kilichokuwa kikitokea. Maombi yalionekana kama kutokusaidia kwani watu wenyewe waliokuwa wakiombewa, walikuwa watenda dhambi wakubwa na walionekana kutokujali kitu chochote kile.
“Umemsikia mchungaji wa lile kanisa la walokole la pale Sinza?” aliuliza msanii mmoja wa muziki wa kufokafoka, Mc Nyami.
“Yupi? Yule anayejifanya kutenda miujiza?”
“Ndiye huyohuyo.”
“Kasemaje?”
“Eti wanamuziki waende kuombewa kwake kwa kuwa kuna roho ya umauti imeingia, si uchizi huo! Yaani anataka kushindana na Mungu aliyeumba kifo!” alisema Mc Nyami.
“Hahah! Sasa si anataka uende ili apige sadaka yako! Wachungaji waongo sana,” alisema msanii mwingine, huyu aliitwa Dingi.
Wala hazikupita siku nyingi, msanii mwingine akafariki dunia, huyu alikuwa Mc Nyami ambaye alimdhihaki mchungaji kwa kusema kwamba alitaka kupiga hela za sadaka lakini hakukuwa na kilichokuwa kikiendelea.
Huku watu wakijiuliza kwa nini vifo viliendelea kutokea, naye Dingi akafariki dunia, tena jukwaani alipokuwa akiimba na madaktari walipompima, wakasema kwamba presha ilikuwa kubwa.
Kila kifo kilichokuwa kikitokea, kiliwekewa kisingizio. Vipimo vya madaktari havikuona uchawi, walikuwa wakiona kama magonjwa ndiyo yaliyokuwa yakiwaua.
Siku ziliendelea zaidi mpaka kufikia mwezi wa nne, bado watu waliendelea kufa kama kawaida. Nchi nzima ikajaa hofu.
Siku ziliendelea kukatika, huku watu wakiendelea kufa bado kesi ya Susan ilikuwa ikisubiriwa kama kawaida. Watu wakagundua kwamba Susan hakuwa amemuua Filbert kutokana na matukio ya vifo yaliyokuwa yakiendelea kutokea nchini Tanzania.
Msichana huyo hakuonekana kuwa na hatia yoyote ile lakini hakuweza kuachiwa huru kwani bado kesi iliendelea kuendeshwa kisheria na hata hivyo serikali haikuamini uchawi.
Baada ya mwezi kukatika na siku ya kesi kufika, watu wakakusanyika mahakamani kwa mara nyingine. Leo hii walionekana kuwa tofauti, hawakuwa na furaha kama mwezi mmoja uliopita, kitendo cha kumuona Susan akishuka kutoka kwenye karandinga na kupelekwa mahakamani, wakinamama wanashindwa kujizuia, wakaanza kulia.
Chuki zikapotea, hakukuwa na mtu aliyetaka kuona Susan akihukumiwa kifo au kifungo cha maisha kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, kitendo cha wasanii na watu maarufu kufa katika mazingira ya kutatanisha ilionyesha wazi kwamba hata Filbert alikufa kama ilivyokuwa hao wengine.
“Sipendi ahukumiwe kifo, ninampenda Susan, nina uhakika hajaua,” alisema mwanamke mmoja, mashavu yake yalilowanishwa na machozi yaliyokuwa yakimbubujika.
“Hata mimi natamani iwe hivyo, hana hatia, mwangalie jinsi alivyokonda. Mungu msaidie Susan wetu,” alisikika mwanamke mwingine.
Mawazo yalimsonga, kila alipokuwa akikaa sero akisubiri kesi yake isomwe, hakuonekana kuwa na raha hata kidogo, kila wakati alikuwa mtu wa mawazo tu. Hakuonekana kuwa kawaida, suala la kuambiwa kwamba alikuwa amemuua Filbert lilimuumiza moyo wake.
Ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wamemtenga mara baada ya kuona kwamba wasanii wengi walikuwa wakifariki dunia wakaanza kujirudi na mwisho wa siku kuanza kumtembelea huko alipokuwa.
Kila walipokwenda, walimfariji na kumtia moyo kwa hali aliyokuwa akikutana nayo. Alipitia katika hatua ngumu maishani mwake, bila kumtia moyo, kila mmoja aliona kwamba msichana huyo angeweza kujiua.
“Utashinda kesi hii, utashinda tu,” alisema Bupe.
“Mmmh! Kila mmoja anajua kwamba nimeua, nitashindaje?” aliuliza Susan.
“Haujaua, mambo yamebadilika, wasanii wanakufa sana, tena katika vifo vya kutatanisha kama alivyokufa Filbert,” alisema Bupe.
“Na vipi vipimo vya madaktari kuhusu kifo cha Filbert?”
“Mwili ulichunguzwa na ripoti kuonyesha kwamba alikufa kwa shindikizo la damu, hakuguswa wala hakujeruhiwa kwa kitu chochote kile,” alisema Bupe.
“Kwa hiyo taarifa inaonyesha kwamba sijaua?”
“Ndiyo maana yake.”
“Asante Mungu!”
Kidogo moyo wake ukarudi katika faraja mpya, akaona kwamba kwa jinsi hali ilivyokuwa ikielekea, inawezekana kwamba angeshinda kesi ile. Moyo wake ulikuwa ukimshukuru Mungu kwa taarifa ya majibu ya Postimotum ambayo iliionyesha kwamba Filbert hakuwa ameshambuliwa na mtu yeyote yule.
****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Edmund alikuwa akikimbia kwa kasi, jasho lilikuwa likimtoka huku mwili ukimsisimka kupita kawaida. Alikuwa porini, japokuwa alipiga sana kelele lakini hakukuwa na mtu aliyetokea na kumsaidia.
Nyuma yake, kulikuwa na watu wengi ambao kwa kuwaangalia, hakuweza kuwafahamu zaidi ya mtu mmoja tu ambaye alikuwa na sanda nyeupe iliyokuwa imeloanishwa na damu kifuani, alikuwa Filbert.
Alijitahidi kuongeza kasi zaidi, aliruka matuta huku akipita katikati ya miti ya porini alipokuwa akikimbia lakini watu wale hawakuweza kusimama, waliendelea kumkimbiza zaidi.
“Mamaaaaa...nakufaaaa...” alijikuta akipiga kelele.
Aliendelea kukimbia zaidi mpaka alipofika sehemu iliyokuwa na mlima mrefu ambapo akaanza kuupanda huku watu wale wakiendelea kumkimbiza kwa kasi. Alipokaribia kileleni, ghafla akajikwaa na kuanguka chini, kila alipojaribu kuinuka ili akimbie, hakuweza kusimama, watu wale walikuwa wakizidi kumsogelea.
“Mama...mama...wananiuaaa...” alipiga kelele Edmund lakini kelele zake hazikuweza kusaidia kitu chochote kile.
Watu wale waliokuwa wakiongozwa na Filbert wakamfikia, mikononi walikuwa wameshika mapanga, walichokifanya ni kuyainua na kutaka kumkata nayo, hapohapo Edmund akashtuka kutoka usingizini.
*****
Ilikuwa ni moja ya ndoto mbaya alizokuwa akiota kipindi hicho, tangu alipoamua kufanya mauaji kwa ajili ya kutafuta utajiri na umaarufu zaidi, maisha yake yakawa yamebadilika kabisa, hakuwa mtu wa kusikia amani kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, kila wakati alipokuwa akikaa, mwili ulikuwa ukimsisimka tu.
Ndoto za ajabuajabu hazikumuisha, kila alipokuwa akilala usiku, moyo wake ulikuwa na hofu tele, alipokuwa akiyafumba macho yake, ni ndoto mbaya ndizo zilizokuwa zikimjia tu.
Maisha yake ya hofu hayakuishia hapo, kila alipokuwa akikaa chumbani na kuangalia filamu au kufanya kitu chochote kile, sauti za ajabuajabu ziliendelea kusikika masikioni mwake kutoka nje, mara asikie sauti za paka waliokuwa wakilia kama watoto huku kwa mbali wakitaja majina ya watu aliowaua, na wakati mwingine kusikia sauti za bundi ambazo zilimuogopesha kupita kawaida.
Japokuwa aliahidiwa kupata kile alichokuwa akikitaka mara baada ya kufanya mauaji, lakini mpaka katika kipindi hicho hakuwa amepata kitu chochote kile zaidi ya maisha yaliyojaa hofu.
“Yusnath...”
“Abeeee...”
“Hivi unawasikia hao paka?”
“Paka gani?”
“Hao wanaolia kama watoto!”
“Hapana.”
“Mmmh! Hata majina wanayoyataja huyasikii?”
“Hapana! Sisikii chochote kile.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo. Paka gani tena jamani baby, sisikii kitu chochote kile, kupo kimya!”
“Hapana, mimi mbona nasikia sauti za paka, tena za ajabuajabu!”
“Mmmh! Sijui. Sasa hayo majina unayoyasikia ndiyo ya kina nani?”
“Ya hawa niliowaua! Mungu wangu, nini tena hiki?” aliuliza Edmund.
Maisha yake yakabadilika kabisa, kila siku akawa mtu wa kusikia hofu moyoni mwake, hakuwa akiishi kwa raha tena, maisha yake yalikuwa ni mateso makubwa mpaka kufikia wakati ambao ulimfanya kujuta kila kitu kilichokuwa kimetokea maishani mwake.
Ukiachana na sauti hizo, kuna kipindi kila alipokuwa akikaa, mbele yake alikuwa akiziona sura za watu aliokuwa amewaua. Moyo wake uliogopa kupita kawaida, ukiachana na kuwaona watu hao njiani, mwisho wa siku alikuwa akianza kuwaona mpaka ndani ya gari lake na nyumba yake.
Kila alipokuwa akiingia garini, alimuona Filbert kupitia kioo cha mbele akiwa amekaa siti ya nyuma, aliposhtuka na kugeuka, hakuwa akiona mtu. Hayo ndiyo maisha aliyoanza kuyapitia, hofu ikaongezeka, alikuwa akiweweseka kila wakati mpaka kikafikia kipindi akatamani kufa ili kuepuka maisha aliyokuwa akipitia.
“Mungu wangu! Naomba unisaidie,” alisema Edmund, mbaya zaidi, hata hayo mafanikio hakuyapata, yaani ni kama kule kuzimu waliamua kumgeuka.
****
Fikiria, unakuwa na fedha, umaarufu, una uwezo wa kwenda sehemu yoyote Tanzania, kula chochote ukipendacho, kumchukua msichana yeyote umtakaye, kununua kitu chochote kile, lakini pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya hivyo, unakuwa hauna amani wala furaha maishani mwako.
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Edmund, alikuwa na uwezo wa kufanya mambo mengi maishani mwake lakini alikosa amani moyoni. Kila alipokuwa akikaa, mwili wake ulikuwa ukiweweseka tu, hakuwa na amani hata kidogo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu aliokuwa amewaua kwa kuwatoa kafara katika ulimwengu wa kuzimu, walikuwa wakimfuata na kuwa kama mizimu ambayo mara kwa mara ilikuwa ikimsumbua mno. Macho yake yalikuwa yalikuwa mazito, akili yake ilichoka sana kwa sababu hakuwa na muda wa kulala.
Kwake, usiku ulionekana kuwa kama jehanamu, kila ulipokuwa ukiingia, alijua kwamba muda wa kukosa amani na kuweweseka ulikuwa umeingia.
Idadi ya watu aliokuwa amewaua ilikuwa kubwa, alipokuwa akiingia chumbani, alisikia sauti za watu hao zikimuita na kumlaumu kwa kile alichokuwa amekifanya. Hali hiyo ilimuogopesha mno kwani kila alipokuwa akimwambia mpenzi wake ambaye hakuwa mtu wa kawaida, alimwambia kwamba hakuzisikia sauti hicho kitu kilichomchanganya sana.
Siku ziliendelea kukatika, wakati mwingine alionekana kama chizi, hakuamini kwamba kila kitu alichokuwa amekifanya kwa wakati huo kingekuwa kama kilivyokuwa. Alijaribu kumuomba Mungu japokuwa alikuwa mtenda dhambi mkubwa lakini hakuweza kupata msaada wowote ule.
“Yusnath...” alimuita mpenzi wake kwa sauti ya chini.
“Nipo mpenzi.”
“Nimefikiria kitu kimoja.”
“Kipi?”
“Nataka nikatubu kanisani, siwezi kuwa katika hali hii kwa miaka yote, sina raha, nataka nimpe Mungu maisha yangu kwani nahisi naweza kuwa na amani,” alisema Edmund.
“Uende kanisani?”
“Ndiyo!”
“Haiwezekani!”
“Kwa nini sasa?”
“Haiwezekani tu, bado haujamaliza kazi uliyopewa.”
“Sitaki tena, sitaki tena kuua, roho za watu niliowaua zinanitafuta usiku na mchana, sitaki tena kuua!” alisema Edmund huku akilengwalengwa na machozi.
“Hapana, hauwezi kuishia kati, ni lazima uimalizie kazi uliyoianza.”
“Siwezi, siwezi kuua tena.”
“Basi tutakuua wewe.”
“Sawa, nipo tayari kufa lakini si kuendelea kuua zaidi!” alisema Edmund.
Alionekana kuchoka, moyo wake ulijawa na hofu kubwa, hakutaka kuua tena kwani maisha aliyokuwa akiishi hayakuwa ya kawaida hata mara moja. Kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, hakutaka kusikia jambo lolote lile kuhusiana na mauaji mengine, kitu alichokuwa akikitaka ni kumkabidhi Mungu maisha yake tu.
Yusnath ndiye aliyeonekana kuwa kipingamizi kikubwa kwake, hakutaka kumuona Edmund akielekea kanisani kwani kama angekwenda huko, maisha yake yangebadilika zaidi na hata yeye nyumbani hapo asingeweza kukaa.
Hakutaka kuona hilo likifanyika, alijiahidi kujitahidi kwa gharama zote lakini mwisho wa siku Edmund asiende kanisani hata mara moja.
Siku zikaendelea kukatika, wakati mwingine Edmund alionekana kama chizi. Hakuwa na amani hata na mali zake. Kuna siku nyingine alikuwa akiendesha gari lake vizuri, alipofika sehemu fulani, alijikuta akipaki nje na kuanza kukimbia huku akipiga kelele.
“Vipi kaka?” aliuliza jamaa mmoja, Edmund alikuwa amelipaki gari lake aliloliacha umbali wa mita thelathini, alikuwa akikimbia hovyo huku akipiga kelele, bila kudakwa na mtu huyo, angekuwa kashafika mbali.
“Nimewaona ndani ya gari!”
“Umewaona ndani ya gari! Wakina nani?”
“Nimewaona ndani ya gari!”
“Sawa, wakina nani uliowaona ndani ya gari?”
Edmund hakujibu kitu, alikuwa akiogopa kusema juu ya wale aliokuwa amewaona, alionekana kuwa na hofu nyingi, moyo wake ulikuwa ukidunda kwa kasi huku mwili wake ukimtoka jasho jingi.
“Edmund!” aliita jamaa yule.
“Nimewaona, wapo ndani ya gari, wamejaa!” alisema Edmund huku akionekana kuwa na hofu usoni mwake.
Kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo watu walivyozidi kujaa mahali hapo, kila aliyekuja, alikuwa na kamera yake au simu na kuanza kumpiga picha.
Hakutaka kulirudia gari lake la kifahari, alikuwa ameliacha mbali kisa aliwaona wale watu aliokuwa amewaua wakiwa ndani ya gari lile. Kwa sababu alikuwa akiogopa kuendesha gari lake, kijana yule aliyekuwa amemdaka, akaanza kwenda naye katika gari lile.
Mwendo wa Edmund ulionyesha hali aliyokuwa nayo, alionekana kuwa muoga mno, alikuwa akiangalia huku na kule kana kwamba alijua kwamba kungekuwa na mtu ambaye alimfuata.
Mpaka wanalifikia gari lile, hakukuwa na mzimu wowote ule. Alichokifanya kijana yule ni kuchungulia ndani ambapo Edmund alisema kwamba kulikuwa na watu, alipoangalia, gari lilikuwa tupu.
“Mbona hakuna mtu?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Niliwaona.”
“Lakini wakina nani hao?”
Hilo ndilo swali lililokuwa gumu kujibika, kila alipokuwa akiulizwa hivyo, hakusema kitu, alinyamaza na kuanza kuangalia huku na kule.
Siku iliyofuata, kila gazeti liliandika lake. Mengine yaliandika kwamba Edmund alikuwa ameiona mizimu lakini taarifa iliyokubalika zaidi ni ile iliyoandikwa kwenye Gazeti la Ijumaa kwamba Malaika wa Kifo alitaka kumuua Edmund garini.
Taarifa hiyo na kile kilichokuwa kimetokea kilionekana kuwa kweli kabisa, kwa sababu wengi wa wasanii walikuwa wamekufa katika vifo vya kutatanisha, basi kila mmoja aliona kwamba hata Edmund alitaka kufa katika aina ya vifo vile.
Siku zikakatika tu, kuna kipindi kikafika, Yusnath akawa haonekani ndani ya nyumba hiyo kitu kilichomtia Edmund wasiwasi mkubwa. Alijaribu kumtafuta msichana huyo kila kona, kila alipoulizia, aliambiwa kwamba hakuonekana kabisa.
Hakujua mahali alipokuwa amekwenda. Moyo wake ulimuuma mno, alimpenda msichana huyo na hakutaka kumpoteza katika maisha yake yote, kila kitu alichokuwa amekifanya na msichana huyo, kikabaki kuwa historia.
“Naomba unisamehe Mungu, nipo tayari kutubu dhambi zangu, kusema wazi kile nilichowahi kukifanya maishani mwangu hasa hiki cha kuwaua wasanii wenzangu na wanasiasa,” alijisemea Edmund.
Muda ulikuwa ukienda sana, alikuwa amekaa kitandani chumbani kwake, shuka lake lililowanishwa na machozi, kila kilichokuwa kimetokea maishani mwake kilimuumiza mno.
Ilikuwa ni asubuhi sana, siku hiyo hakuwa amelala, usiku mzima alikuwa mtu wa kulia tu. Paka walilia sana juu ya bati la nyumba yake, bundi walisikika kila wakati, kutokana na hali hiyo, hakutaka hata kuyafumba macho yake.
Pembeni yake kulikuwa na Biblia, alijitahidi kuisoma huku wakati mwingine akiamini kwamba ni ulinzi wake, kwamba akiwa nayo karibu wachawi wasingeweza kumfuata. Mpaka inafika asubuhi ya siku hiyo, hakuwa amepata hata lepe la usingizi.
Ilipofika saa moja na nusu asubuhi, akatoka chumbani kwake na kuelekea nje. Alipofika, akasikia akiitwa na mtu nyuma yake, sauti aliyoisikia aliifahamu sana, ilikuwa ni sauti ya Filbert.
Mapigo ya moyo yakaanza kudunda kwa kasi, hata kabla hajageuka na kupata uhakika kama alikuwa Filbert mwenyewe au la! Alipogeuka tu, hisia zake zilikuwa sawa na kile alichokuwa amekiona, alimuona Filbert akimwangalia, alikuwa amevaa sanda huku kifuani akiwa na damu nyingi, kwa uoga, Edmund akatoka nje ya eneo la nyumba yake na kuanza kukimbia huku akipiga kelele.
Hakusimama, kila alipokuwa akigeuka nyuma, Filbert alikuwa akimfuata kwa kasi. Woga uliokuwa ukimshika, ukamfanya kuongeza kasi zaidi mpaka kufika Posta bila kusimama hata sehemu moja, bila kutegemea wala kujua aliwezaje kufika mahali hapo, akajikuta akiwa ndani ya mahakama, watu walikuwa wamejazana huku mbele yake akiwepo msichana aliyekuwa akimfahamu sana, alikuwa Susan, tena akiwa kizimbani.
Kila mmoja akabaki akimshangaa Edmund, japokuwa polisi mahakamani hapo walimnyoonyeshea bunduki na kumtaka kutoka mahakamani lakini hakutaka kutoka, alionekana kuwa na hofu kubwa, kila wakati alikuwa akiangalia mlangoni kuona kama Filbert alikuwa akimfuata au la.
Wala hazikupita sekunde nyingi, Filbert akatokea mlangoni, hakuwa peke yake, alikuwa na kundi la watu, watu wote ambao waliuawa na Edmund kichawi.
“Mamaaaa....hao hapo wanakuja kuniuaaaa...” alipiga kelele Edmund mahakamani hapo.
Kila mtu akabaki akiwa amepigwa na mshangao, hawakumuelewa Edmund, alikuwa akipiga kelele huku akiangalia mlangoni, na wao walipoangalia, hawakuwaona watu waliokuwa akiwasemea zaidi ya polisi waliokuwa wameshika bunduki, tena wakimtaka kutoka mahakamani hapo na kesi ya Susan isikilizwe.
****
Japokuwa Susan alikuwa sero lakini alipewa kila taarifa juu ya matukio yaliyokuwa yakiendelea uraiani. Kwa jinsi wasanii walivyoendelea kupukutika, akajikuta akimuomba Mungu ili aweze kumpigania na kushinda kesi iliyokuwa ikimkabili na pia asikumbwe na kifo cha aina yoyote ile.
Akataka kuyabadilisha maisha yake, hakutaka kuishi kama alivyokuwa akiishi, alitaka kumtumikia Mungu katika maisha yake yaliyobakia. Alikuwa mtu wa starehe sana, hivyo, kitu cha kwanza ambacho alimuomba Mungu sana ni kumpigania na kuachana na starehe.
Susan akabadilika, hakuwa Susan yule aliyekuwa akijulikana kwa mambo yake ya kijinga, Susan huyu alikuwa tofauti kabisa. Kila siku akawa mtu wa kusali japokuwa hakuwa amemuita mchungaji kwa ajili ya kumpa sala ya toba.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Susan, unamaanisha kweli unaposema kwamba unataka kuokoka?” aliuliza Bupe.
“Nipo siriazi, sitaki tena kuishi maisha haya, ninataka kumtumikia Mungu maisha yangu yote,” alisema Susan.
“Mmmh! Sawa. Kwa hiyo nikusaidie nini?”
“Nataka umuite mchungaji aje kuniongoza sala ya toba!”
“Sawa, hakuna tatizo. “
Baada ya siku mbili Bupe akarudi katika sero hiyo huku akiwa ameongozana na mchungaji wa Kanisa la Praise And Worship lililokuwa Sinza na kuanza kumuongoza sala ya toba.
Muda wote Susan alikuwa akilia kama mtoto, kila alipokuwa akikumbuka maisha ya starehe aliyokuwa ameishi katika kipindi cha nyuma, moyo wake ulijihisi kuwa na hukumu kubwa mbele za Mungu.
Baada ya kila kitu kumalizika, mchungaji huyo akamkabidhi Biblia na kumwambia kwamba kila siku aendelee kumuomba Mungu kwa ajili ya kumuongoza katika maisha yake yote.
Bado kesi yake ilikuwa ikisubiriwa, baada ya mwezi mmoja kumalizika, siku ya kesi ikaandaliwa na hivyo alitakiwa kwenda kusimama kizimbani na kuanza kusikilizwa utetezi wake, upande wa mashahidi na kisha kumsikiliza hakimu angesema nini.
Siku ya kesi, karandinga likafika mahali hapo na kuchukuliwa na kuanza kupelekwa mahakamani. Susan alikuwa kimya, uso wake alikuwa ameuinamisha chini huku sala ya kimoyomoyo ikiendelea kama kawaida yake.
Alitamani kuwa huru, hakutaka tena kuendelea kuteseka sero, alihitaji kwenda nyumbani na kuanza maisha yake ya mitaani huku akiwa na Mungu moyoni mwake.
Siku hiyo, magazeti yote yalikuwa yakizungumzia kuhusu kesi hiyo iliyokuwa ikienda kusomwa mahakamani mara baada ya Susan kusomewa mashtaka yanayomkabili mwezi mmoja uliopita.
Kama kawaida waandishi wa habari walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba wanapata picha juu ya kila tukio litakalokuwa likiendelea mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa katika vyombo vyao vya habari.
Kwa kuwa kesi yake ndiyo ilikuwa ikisubiri kwa hamu, ratiba ikapangwa na kuonyesha kwamba ndiyo kesi ambayo ingeanza asubuhi ya siku hiyo kisha zile kesi ndogondogo kufuata.
Baada ya kila kitu kukamilika, hakimu aliyetakiwa kuiendesha kesi hiyo, bi Hawa Saidi akatokea mahakamani hapo. Kwa heshima, watu wote wakasimama na kukaa baada ya kuona Hakimu Hawa amekaa, nao wakakaa.
Mawakili wa pande zote mbili wakajiandaa huku mashahidi ambao walikuwa ni wafanyakazi wa hoteli ile nao wakiwa mahakamani hapo. Wakili wa upande wa mshtaki ambaye ni serikali, akasimama na kuanza kumhoji.
“Bila shaka wewe ndiye Susan Chichi unayeishi Kijitonyama?”aliuliza wakili huyo, Bonito Masegule.
“Ndiyo mimi,” alijibu Susan.
“Unajua kwa nini upo hapa?” aliuliza Bonito.
“Nipo hapa kwa sababu ninashtakiwa kwa kosa la kumuua Filbert,” alijibu Susan.
“Kwa nini ulimuua Filbert?”
“Hapana, sikumuua Filbert wala sikumgusa!”
“Hukumuua Filbert! Una uhakika?”
“Ndiyo mheshimiwa.”
“Maiti ya Filbert ilikutwa ndani ya chumba ulichokuwemo, tena ikiwa sakafuni na wewe ukiwa karibu na mwili huo, kelele zako ndizo ziliwashtua watu, kwa nini ulipiga kelele?”
“Kwa sababu niliogopa baada ya kumuona Filbert sakafuni akiwa amekufa.”
“Ulijuaje kama amekufa na wakati unasema kwamba hata kumgusa haukumgusa?”
“Nilijua tu.”
“Unawezaje kujua mtu amekufa kwa kumwangalia tu?”
Susan akanyamaza!
“Taarifa zinasema kwamba ulimsukuma Filbert na hivyo kuanguka chini, unaweza ukaielezea mahakama kwa nini ulimsukuma Filbert?”
“Hapana mheshimiwa, sikumsukuma Filbert!”
“Hivyo ndivyo taarifa zinavyosema. Ukiachana na hilo, kwa nini ulikwenda hotelini kumuona Filbert?”
“Aliniambia niende.”
“Nani alijua kwamba ulikuwa ukienda kuonana na Filbert?”
“Hakuna.”
“Kwa nini uliamua kufanya siri? Au kwa sababu ulijua kwamba siku hiyo ungemuua Filbert kwa kumsukuma?” aliuliza Bonito.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana, sikumsukuma na sikutaka kumwambia mtu kwa kuwa sikutaka mtu yeyote afahamu.”
Japokuwa maswali aliyokuwa akiulizwa yalikuwa mepesi lakini kwa upande wake aliyaona yakiwa na mitego mingi. Alijitetea na kujitetea huku muda mwingi akilia kama mtoto mahakamani hapo.
Kwa maswali aliyokuwa akiuliza wakili wa serikali, ilionyesha kwamba Susan alikuwa amemsukuma Filbert na kuanguka kitu kilichompelekea kufariki dunia. Baada ya maswali ya wakili huyo kumalizika, akaja wakili wa upande wake.
Bado Susan hakuonekana kuwa na amani, kwa jinsi kesi ilivyokuwa ikienda na maswali aliyokuwa akiulizwa, alijua fika kwamba siku hiyo angeweza kuhukumiwa kifo au kifungo cha maisha gerezani.
Mara baada ya maswali yote kumalizika, kila mtu akaanza kumwangalia hakimu Hawa, walitaka kusikia kitu ambacho angekiongea mahali hapo. Huku kila mmoja akiwa kimya, ghafla wakasikia mtu akiingia mahakamani hapo kwa kasi, alikuwa akipiga kelele na kusema kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakimkimbiza.
Walipomwangalia vizuri mtu huyo, alikuwa Edmund. Kila mtu akashtuka, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka mtu huyo kuingia ndani ya mahakama hiyo huku akipiga kelele kama chizi.
Polisi wa mahakamani hapo wakashikilia bunduki zao tayari kwa kumpiga risasi lakini mara baada ya kugundua kwamba mtu huyo alikuwa Edmund, wakamtaka kumtoa mahakamni hapo ili kesi iendelee.
Edmund hakutoka, alionekana kuwa na hofu kubwa usoni, alionekana kuweweseka huku jasho likimtoka. Kila aliyekuwa akimsogelea, alikataa kuguswa na mtu yeyote yule.
“Mamaaaa....hao hapo wanakuja kuniuaaaa...” alipiga kelele Edmund mahakamani hapo.
Kila mmoja akabaki na mshangao!
“Filbert anakuja...Filbert anataka kuniua, huyo anakujaaa...Nyami anataka kuniuaaaaaa...” alisema Edmund kwa sauti kubwa ndani ya mahakama ile.
Kila mtu alipigwa na mshangao, muigizaji mkubwa aliyekuwa akipiga kelele mahali hapo walimfahamu, alikuwa na jina kubwa, kitendo chake cha kuwataja watu waliokuwa wamekufa kilimshangaza kila moja.
Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba mtu huyo alikuwa amehusika katika mauaji ya watu hao, machoni mwao alionekana kuwa mtu mwema ambaye naye alijumuishwa katika orodha ya wasanii waliotakiwa kuuawa katika kipindi hicho.
“Edmund vipi! Amechanganyikiwa au?” aliuliza mwanamke mmoja.
“Hata mimi nashangaa! Au ndiyo malaika wa kifo kaanza kumnyatia!” alisikika jamaa mmoja.
“Jamani, hebu tumsaidieni, anaweza kuwa na tatizo kubwa,” alisikika jamaa mmoja.
Hakukuwa na mtu aliyethubutu kumsogelea, hata kwa muonekano aliokuwa nao ulionyesha kwamba hakuwa mzima kiakili, hivyo kama alionekana kuwa kama chizi, basi alikuwa na uwezo wa kumdhuru mtu yeyote pasipo kuhukumiwa mahakamani.
Hakimu Hawa hakuongea kitu, yeye mwenyewe alionekana kumshangaa Edmund. Polisi waliokuwa mahakamani hapo, waliishia kushika bunduki zao lakini walionekana kupigwa na butwaa.
Kadiri dakika zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo Edmund aliendelea kupiga kelele kwamba alikuwa akifuatwa na watu waliotaka kumuua, watu ambao hawakuwa wakionekana na watu wengine isipokuwa yeye tu.
Baada ya dakika kadhaa, kwa kasi ya ajabu, Edmund akachomoka mahakamani na kutoka nje, huko, akaanza kukimbia na kuelekea pasipofahamika.
Baadhi ya waandishi wa habari hawakutaka kubaki ndani ya mahakama ile, walichokifanya ni kutoka na kuanza kumkimbiza, walitaka kujua ni mahali gani alipokuwa akikimbilia kwani hata kwa muonekano wake tu kwa kumwangalia, alionekana kuwa kama chizi.
Mahakamani hakuwa na utulivu tena, kesi iliyotakiwa kuendelea, ikaonekana kuwa vigumu kuendelea, minong’ono ilisikika kila kona, kila mtu alikuwa akiongea lake huku akionekana kuwa katika hali ya sintofahamu kutokana na kile kilichokuwa kimetokea.
Alichokifanya hakimu Hawa ni kuiahirisha kesi ile mpaka baada ya miezi miwili ndiyo ingesikilizwa tena, hakuishia hapo, hata Susan mwenyewe akampa dhamana ya kuwa nje mpaka pale kesi yake itakaposikilizwa tena kwani kwa kila kitu kilichoelezwa mahakamani, akaonekana kutokuwa na hatia.
“Afadhali, The Queen Lady is back, sasa hicho ndicho tulichokuwa tukikitaka,” alisema jamaa mmoja, kila mmoja mahakamani hapo alionekana kuwa na furaha kuona kwamba msichana huyo alikuwa huru kurudi uraiani.
****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yusnath alikuwa na hasira, maneno aliyoongea Edmund kwamba alitaka kurudi kanisani na kutubu dhambi zake yalimvuruga kupita kawaida. Uso wake ukawa mwekundu, hakutegemea kusikia maneno yenye kukera kama aliyoongea Edmund tena mbele ya macho yake.
Usiku wa siku aliokuwa ameambiwa maneno hayo hakulala vizuri, alihisi kichwa chake kilikuwa kimechanganyikiwa, alitamani kuzuia jambo hilo lisitokee lakini kwake likaonekana kuwa gumu, kitu pekee ambacho kingemfanya kulizuia jambo hilo lilikuwa ni kumuua mtu huyo, basi.
Hilo, kwake halikuwezekana hata mara moja, alimpenda sana Edmund, hakutaka kumpoteza, kwake, alikuwa radhi kumpoteza mtu yeyote lakini si Edmund.
Hakuwa binadamu wa kawaida, kitendo cha kuingia kwenye mahusiano na binadamu, kufanya naye mapenzi kilimpa msisimko wa ajabu ambao uliufanya uamuzi aliotaka kuuchukua kuwa mgumu kutekelezeka.
Usiku huohuo, huku Edmund akiwa amelala, Yusnath akasimama na kuanza kumwangalia mwanaume huyo. Macho yake yakaanza kuwa mekundu, akausikia moyo wake ukiunguzwa na moto, maumivu makali yalikuwa yakimtesa mno.
Bila kutarajia, machozi yakaanza kumtoka. Hayakuwa machozi ya kawaida, yalikuwa machozi ya damu yaliyokuwa yakibubujika mashavuni mwake. Alijihisi tofauti, pamoja na hasira kali alizokuwa nazo dhidi ya Edmund, lakini aliusikia moyo wake ukiwa kwenye mapenzi ya kweli.
Hakujua ni kitu gani kilitokea, ghafla akaanza kujibadilisha umbo lake na kuingia katika umbo la nyoka mkubwa aliyefanana na chatu mwenye rangi za mchanganyiko, alipokuwa kwenye umbo hilo, akaanza kupanda kitandani na kuanza kumtembea Edmund mwilini mwake huku wakati mwingine akijiviringisha mwilini mwa Edmund.
Edmund hakushtuka, alikuwa kwenye usingizi mzito uliochanganywa na uchawi, aliviringishwa, akabebwa juu kisha kurudishwa chini huku nyoka huyo akitoa ulimi wake lakini Edmund hakuweza kushtuka.
Yusnath alikuwa katika hatua za mwisho za kummaliza Edmund lakini bado jambo hilo liliendelea kuwa gumu kwake. Nguvu ya mapenzi iliuendesha moyo wake kupita kawaida, alichokifanya, ni kuondoka ndani ya chumba hicho huku akitambaa sakafuni.
Alipofika ukumbini, ghafla moshi mzito ukatokea mahali hapo, huku akiwa kwenye umbo la nyoka aina ya chatu, Yusnath akaanza kupiga kelele kubwa, sehemu hiyo ikaanza kutetemeka kana kwamba kulikuwa na tetemeko la ardhi, ghafla, akapotea.
Alikuja kuonekana akiwa kuzimu, mbele yake kulikuwa na viumbe vingi na vya ajabu, viumbe vyote hivyo vyenye kutisha vilikuwa vimejifunika mavazi meupe yaliyofanana na sanda za maiti, pembeni yao, kila mmoja alikuwa na kikombe chenye damu.
Mara, kiumbe mmoja wa ajabu mwenye kichwa cha paka, mapembe, tumbo la binadamu, manyoya mwili mzima lakini miguu ya ng’ombe akatokea mahali hapo huku akiwa ameshika fimbo kubwa yenye alama ya fuvu, alipoviona viumbe vile vya ajabu vimepiga magoti mbele yake, akanyoosha fimbo yake juu.
“Bwana wangu, kuna tatizo,” alisema Yusnath, muda mwingi alikuwa akibadilikabadilika katika maumbo ya ajabuajabu, hiyo yote ilitokana na hasira kali aliyokuwa nayo.
“Shida gani?” kiumbe yule aliuliza.
“Edmund anataka kwenda kanisani, sitaki iwe hivyo, ninataka auliwe,” alisema Yusnath, muda huyo alikuwa na umbo la muonekano wa ngozi ya chui, kichwa cha nyani mwenye mapembe, macho makubwa zaidi ya bundi, miguu yake ilikuwa imejaa manyoya mengi, kwa kifupi, Yusnath alikuwa anatisha.
“Ni lazima tumuue...”
“Bwana wangu.”
“Kuna tatizo?”
“Hapana. Ninataka afe, ila kwanza ni lazima awe kichaa, amekataa kufanya kile tulichomwambia, amebadilika na anataka kumrudia muumbaji,” alisema Yusnath.
“Ni lazima tumuue, ila kabla ya kumuua, ni lazima tumtese,” alisema kiumbe yule.
Hiyo ilikuwa ni amri iliyotolewa na Yusnath hakutakiwa kupingana nayo hata mara moja. Kitu kilichokuwa kikisubiriwa ni utekelezaji wake tu.
Yusnath akaondoka mahali hapo, pepo wachafu wakatumwa na ndiyo ambao walikuwa wakimsumbua kwa kumletea ndoto za ajabuajabu, wakamkosesha furaha, wakamchukulia amani na kumjaza maisha yaliyokuwa na hofu kila wakati.
Mpaka kinafika kipindi cha Edmund kukimbia na kuelekea mahakamani, kila kitu kilikuwa chini ya mipango yao, kwa kuwa alikuwa ameamua kutaka kwenda kanisani na hivyo kuachana na kazi waliyotaka aimalizie, nao wakaamua kumuamulia.
“Wanakujaaaaa...wanakujaaaa” alisikika Edmund akipiga kelele mahakani.
Hakukuwa na watu waliokuwa wakija, ilikuwa ni mizimu iliyovaa taswira za watu aliowaua Edmund na kuanza kumtia hofu moyoni mwake. Kwa sababu walikuwa ni roho chafu, waliruhusu Edmund peke yake ndiye awaone kwa kuwa alikuwa mhusika mkuu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Si kwamba polisi hawakuwa na uwezo wa kumzuia au kumtoa nje, uwezo huo walikuwa nao lakini hawakuwa na nguvu za kufanya hivyo kwa kuwa roho wale wachafu, majini waliamua kuwazuia polisi kufanya hivyo kwa kuwashika huku wenyewe wakiwa hawajijui.
Hakimu Hawa alikuwa kimya pale alipokaa, bila kujua, mdomo wake ulikuwa umefumbwa na jini mmoja na kumfanya kutokuweza kuufumbua kabisa japokuwa alitamani kufanya hivyo.
Kila kitu mahakamani hapo kiliongozwa na majini hayo yaliyoonekana kuwa na nguvu kuliko watu wa kawaida. Baada ya kuridhika, wakamruhusu Edmund kutoka na kuanza kukimbia.
Edmund alikuwa akikimbia kwa kasi, kila baada ya hatua hamsini alizokuwa akipiga alivua moja ya nguo zake, mpaka anapiga hatua ya mia na hamsini, alikuwa na boksa tu mwilini mwake.
Kila mtu alionekana kushangaa, hawakuamini kama Edmund yule waliyekuwa wakimfahamu ndiye alikuwa katika hali ile au huyu alikuwa Edmund mwingine. Aliendelea kukimbia huku watu wakimpiga picha, lakini ghafla, akafuatwa na watu watatu, wanaume wenye nguvu, wakambeba juujuu na kuanza kuondoka naye.
Kila kitu kilichokuwa kikionekana mahali hapo, kilikuwa kama filamu ya kibongo iliyosisimua. Wananchi waliokuwa wakifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea hawakuishia hapo, nao wakaanza kuwafuatilia watu wale walioonekana nadhifu kwa kuvaa mashati yao yaliyochomekewa vizuri.
“Wanampeleka wapi?”
“Mmmh! Wale si washikaji wa kanisa la hapo nyuma, hebu tuwafuatilie,” alisema jamaa mwingine.
Zaidi ya watu elfu mbili walikuwa wakiwafuatilia watu hao, na kadiri walivyokuwa wakipiga hatua na ndivyo ambavyo watu walizidi kuongezeka zaidi. Baada ya dakika nne, watu hao walikuwa wakiingia katika kanisa kubwa lililoandikwa Praise And Worship Church lililokuwa maeneo ya Upanga.
“Shetani hana nguvu zaidi ya Mungu! Haya ni mapepo, leo yamefika kikomo,” alisikika mchungaji wa kanisa hilo, mchungaji Joshua.
Kilichofuata mahali hapo, ni maombi mazito ya kanisa zima. Hakukuwa na mtu aliyenyamaza, kila mmoja alikuwa akikemea kwa nguvu zote huku watu wakiendelea kufuatilia kila kitu mlangoni na madirishani.
“Tunaunguaaaa....tunaunguaaaa...tunatokaaa...” alisikika roho chafu akiongea kwa kutumia mdomo wa Edmund.
“Wewe ni nani?’ aliuliza mchungaji Joshua.
“Ninaitwa makata...naomba usituunguze...”
“Mmetoka wapi?”
“Tumetoka kuzimu, tunaomba usituunguze....usituunguzeeeee....”
“Mpo wangapi na mmekuja kufanya nini?”
“Tupo elfu moja, tumekuja kumsaidia Edmund, alitutaka tumsaidie kuua kwa ajili ya kupata umaarufu na fedha zaidi, awe zaidi ya wasanii wote...naomba usituunguzeeeee...” alisikika jini huyo.
“Mmmekwishaua watu wangapi mpaka sasa?’ aliuliza mchungaji Joshua, jasho lilikuwa likimtoka.
“Tumeua watu wengi, tumeua wasanii wengi, wanasiasa, wote aliotaka tuwaue.”
Kila mtu kanisani hapo akapigwa na butwaa, hakukuwa na mtu aliyeamini kile kilichokuwa kimezungumzwa mahali pale.
Edmud kuwaua watu wote kwa ajili ya kupata umaarufu na fedha zaidi! Kilikuwa moja ya kitu kilichomshtua kila mmoja.
“Sasa ni lazima mrudi mlipotoka...Kwa jina la Yesu rudiniiiiiiiiiiii...”
“Tunatokaaaa....tunaunguaaaa....tunaunguaaaaa....” alisema pepo huyo mchafu.
Maombi yalikuwa yakiendelea, kanisani, kila mmoja alikuwa bize kukemea, baada ya dakika ishirini, hakukusikika sauti yoyote kutoka kwa Edmund, alionekana kuwa kama mtu aliyekufa.
Alichokifanya mchungaji Joshua ni kumfuata na kisha kumuinua, Edmund alionekana kuchoka, hakuwa na nguvu za kutosha. Wenye simu, kamera, waliendelea kupiga picha kila kitu.
Edmund akapewa dakika kumi za kujielezea, hakutaka kuficha, akaanza kuelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea, toka siku ya kwanza aliposhikwa na tamaa ya kutaka kuwa kama Filbert, kila kitu kilichotokea ambacho alikiweka na kuwa siri, akakiweka hadharanmi.
“Mikono yangu imejaa damu! Mikono yangu imejaa damu mchungaji!” alisema Edmund huku akilia.
“Mungu anasamehe! Kama umekiri dhambi zako, Mungu atakusamehe!” alisema mchungaji Joshua.
Kila mtu alipigwa na mshangao, wengine wakashindwa kuvumilia, wakaanza kulia kanisani humo, idadi ya watu aliokuwa amewaua ilikuwa kubwa, tena mbaya zaidi, walikuwa watu maarufu Tanzania.
“Yaani huyu jamaa kweli alikuwa katili...” alisikika jamaa mmoja dirishani.
“Huo haukuwa ukatili, alikuwa akiendeshwa na roho chafu!”
“kivipi?”
“Huwezi kuelewa kama na wewe si mtu wa kiroho, wewe sikilizia tu,” alisema jamaa mwingine huku uso wake ukiwa na tabasamu pana,
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
****
Hakukuwa na siri tena, kila kitu kilikuwa wazi, siku iliyofuata, magazeti yote yalikuwa yamechapisha habari kuhusiana na kutubu kwa Edmund kwamba alikuwa chanzo cha mauaji yote yaliyokuwa yametokea.
Watu walilia mno, walishindwa kuamini kwamba mtu waliyekuwa wakimpenda ndiye alikuwa chanzo cha kila kitu kilichotokea. Wapo waliokuwa wakimkashifu kwa kumuita muuaji asiyekuwa na huruma hata kidogo, muuaji aliyekuwa na roho mbaya hata zaidi ya Adolf Hitler.
Magazeti yote ambayo yaliandika kuhusu habari ya kutubu kwa Edmund, mpaka inafika saa sita mchana, hakukuwa na gazeti lolote lililokuwa likionekana mitaani, yote yalikuwa yamenunuliwa kwa wingi.
Kwa mwaka huo, hakukuwa na kitu kilichovuma sana kama tukio hilo. Watu wakaanza kuvuta kumbukumbu zao juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea, bado hawakuamini kama Edmund alikuwa nyuma ya kila kitu.
“Unajua nashangaa sana, inawezekana vipi Edmund kuwa nyuma ya kila kitu, nahisi hainiingii akilini kabisa,” alisema jamaa mmoja, mkononi alikuwa ameshika Gazeti la Risasi.
“Kaka, dunia imebadilika sana, mtu unayemdhania ndiye, kumbe siye na yule unayemdhanie siye, kumbe ndiye, yaani binadamu hatuelewekieleweki,” alisema jamaa mwingine.
Nchi nzima, jambo lililokuwa likizungumzwa siku hiyo lilikuwa ni kuhusu Edmund tu, kila kona, watu walikuwa wamekaa makundimakundi huku mikononi wakiwa na magazeti na kuanza kumjadili muigizaji huyo.
Hakukuwa na haja ya kuwa na mikanda wa cd zake, skendo ile kubwa ilikuwa imewachukiza watu na hivyo vitu vyote vilivyohusu Edmund kuvichoma moto. Makampuni yaliyokuwa yameweka mikataba naye, ikasitisha mikataba na hivyo kumuacha akiwa hajui la kufanya.
Huo ndiyo ulikuwa muda wa majuto kwake, kila alipokuwa akikaa, alikuwa akilia tu. Alijuta kwa nini alifanya kile alichokuwa amekifanya miezi kadhaa iliyopita.
Alikaa sebuleni kwake huku akiwa na mawazo tele, hakutaka kuwa na mtu yeyote ndani ya nyumba hiyo, wafanyakazi wote, akawafukuza, kwake ilikuwa ni aibu, hakutaka kuonana na mtu yeyote yule.
Alikuwa amechanganyikiwa, japokuwa alifanyiwa maombezi na roho yake kuwekwa huru lakini bado hakuwa sawa kabisa. Alikuwa na mawazo lukuki huku kila wakati wazo la kujiua likimjia kichwani mwake.
“Utaweza vipi kuishi ukiwa katika hali hii? Hebu tazama watu wanavyokuchukia, wanaweza kukua popote watakapokuona, kwa nini usijiue, kwa nini uendelee kuteseka na kusubiri kuuliwa na watu?” alisikia sauti ikizungumza moyoni mwake.
“Mungu! Naomba unisamehe, nimefanya dhambi kubwa kwa sababu ya tamaa za maisha yangu hapa duniani, ninatubu dhambi zangu, ninaomba unisamehe,” alisema Edmund huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake.
“Ninajuta, ninaujutia moyo wangu, ninajuta kwa kila kitu nilichokifanya, tamaa yangu ndiyo imenifikisha hapa nilipo. Mungu! Nimejipaka mavi usoni, hakuna binadamu yeyote anayetaka kuniona, naomba unisafishe Mungu!” alisema Edmund huku akilia kama mtoto.
Washirika wa Kanisa la Praise And Worship walikuwa wakifika nyumbani kwake kwa ajili ya kumuona, kumfanyia maombezi na vile kuwa karibu naye huku wakimtia moyo. Kwake, kwa wakati huo hakutaka kuonana na mtu yeyote yule, kitu pekee alichokuwa akikitaka ni kufa tu.
Japokuwa kila mtu alitamani sheria ichukue mkondo wake na kumkamata Edmund kisha kumshitaki kwa mauaji aliyoyafanya lakini hilo likaonekana kuwa gumu kufanyika na sababu kubwa ni kwamba serikali haikuamini uchawi.
Kumkamata ilikuwa kazi nyepesi lakini kupata ushahidi wa kuwaambia kwamba alikuwa amewaua watu hao ilikuwa ngumu, hivyo serikali ikaamua kukaa kimya.
Kwa sababu mioyo yao ilikuwa kwenye huzuni na hasira kali dhidi yake, zaidi ya watu themanini walikuwa wamejikusanya, siku hiyo walitaka kuona hasira zao zikiisha kwa kufanya kitu kimoja tu, kumuua Edmund.
Hakukuwa na mtu aliyetaka kumuona mtu huyo akiendelea kuishi, kama alivyokuwa amewaua wenzake, naye walitaka kumua pia ili iwe nafuu ndani ya mioyo yao.
Walipojikusanya, kuna wengine walikuwa na marungu, wengine fimbo, mapanga, mijeredi, visu, yaani kila mmoja alikuwa na silaha yake kali, hata waliokuwa na matofali nao walikuwa miongoni mwao.
“Jamani! Hivi hatufiki tu?” aliuliza jamaa mmoja.
“Siyo mbali sana, tunakaribia.”
Walionekana kuwa wengi barabarani kiasi kwamba baadhi ya watu walifikiri kwamba walikuwa Panya Road hivyo waliokuwa wamefungua maduka yao, wakayafunga na kujificha ndani.
Siku hiyo, watu walikuwa wamedhamiria kufanya kitu kimoja tu, kumuua Edmund kwani kwa kile alichokuwa amekifanya, hakukuwa na mtu aliyeonekana kuridhika nacho.
****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliendelea kujuta, alijuta na kujuta, japokuwa ndani alikuwa amekaa peke yake lakini bado alikuwa akijisikia aibu. Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kutoka ndani ya nyumba yake na kutembea mitaani kama kawaida yake.
Hakuwa na hamu ya kuendelea kuishi tena, alionekana kukata tamaa ya maisha kabisa. Pembeni yake alikuwa na Biblia kwa kuamini kwamba ingeweza kumsaidia katika kumfariji lakini kila alipokuwa akiishika na kufungua kurasa, kulikuwa na sauti kichwani ikimwambia amri moja kati ya amri zote alizopewa Musa jangwani, ‘usiue’
Alitetemeka na kuogopa sana, hakujua ni kwa jinsi gani angeendelea kuishi. Baada ya kujifikiria sana, wazo la kujiua akaliweka mbele. Alichokifanya ni kuinuka pale alipokuwa amekaa na kisha kuanza kuelekea chumbani kwake, aliporudi baada ya dakika moja, alikuwa na bunduki mkono wa kulia, kisu mkono wa kushoto na kamba shingoni mwake.
Kabla hajafanya chochote, akachukua karatasi na kalamu na kuanza kuandika ujumbe mrefu katika karatasi hiyo. Alitumia dakika tano, aliporidhika, akaichukua na kuiweka juu ya meza na kuvishika vifaa vyake vya kujiulia.
Alivifikiria vifo vitatu, alitaka kujiua kwa kujinyonga, akishindwa, ajiue kwa kujipiga risasi lakini kama aliona ngumu sana, basi ajiue kwa kujichoma kisu.
“Hapana, mbona vifo vigumu sana!” alijisemea moyoni lakini mwisho wa siku, aliamua kuifunga kamba staili ya kitanzi na kuifunga katika sehemu iliyokuwa na feni.
Roho ya uuaji ilikuwa imemwingia na hakuweza kuikemea tena, alipoona kwamba kamba imekaa vizuri, akachukua kistuli na kupanda juu.
“Mungu! Naomba unisamehe!” alisema Emund, machozi yalikuwa yakimtoka lakini mwisho wa siku, akakipiga kistuli kile na kuning’inia.
****
Watu waliizunguka nyumba ya Edmund, walikuwa na silaha mikononi mwao na walifika mahali hapo kwa ajili ya kumuua mtu huyo tu. Getini hakukuwa na mlinzi, walichokifanya ni kulivunja geti na kuingia ndani.
Ukimya ulikuwa umetawala, walijifanya ndiyo wenyeji, wakaufuata mlango wa kuingia sebuleni na kuuvunja ili waweze kuzama ndani.
“Huyu mjinga lazima tumuue! Yaani hadi Filbert alimuua yeye! Kumuacha ni dhambi kubwa!” alisema jamaa mmoja.
“Au tuichome nyumba moto?” aliuliza jamaa mmoja.
“Hapana! Tuingieni tukamcharange mapanga!” alisema jamaa mwingine.
Nje ya nyumba hiyo, watu wengi walionekana kuwa na mapanga, kila mmoja alikuwa akitaka kumuua Edmund aliyeiumiza mioyo yao. Kila mmoja alionekana kuwa na hasira mno na Edmund kiasi kwamba kila wakati walikuwa wakiyanoa mapanga yao.
Walipohakikisha kwamba mlango umevunjika wakaingia sebuleni. Kile walichokuwa wakikiona, hawakuweza kukiamini, Edmund alikuwa akining’inia huku mwili ukiwa umemkakamaa.
Katika hali ambayo hata wao walionekana kuishangaa, kwa haraka sana wakamsogelea na kisha kumshika na kuipandisha miguu yake juu ili kama kamba inamkaba asiweze kufa.
Hiyo haikusaidia, Edmund alikuwa amekufa muda mrefu uliopita. Waliokuwa na simu zao, wakachukua na kuupiga picha mwili ule na kuzisambaza kwa marafiki zao mpaka kwenye mitandao ya kijamii.
Hicho ndicho kilikuwa kifo chake, aliamua kujiua kwa kuwa alishindwa kuvumilia kuwa katika hali ile. Walipokuwa wakiangalia huku na kule, pale mezani kukaonekana kuwa na barua, kijana mmoja akichukua na kufungua.
“Hebu isome kwa sauti na sisi tusikie,” alisema jamaa mmoja huku akiwa ameliweka panga lake begani.
“Poa, ngoja niisome, daah! Ila jamaa alikuwa na mwandiko mzuri,” alisema jamaa huyo huku akitabasamu, akaanza kuisoma barua hiyo.
Watanzania,
‘Kuna mengi yaliyotokea kabla ya siku hii ya leo, ningependa kuyazungumza machache lakini kwanza ningependa mnisamehe. Nimefanya makosa makubwa maishani mwangu, sikuwahi kufikiria kama ingetokea siku ningemuua mtu yeyote yule.
Nilishikwa na tamaa ya umaarufu na utajiri zaidi, Filbert alikuja kwangu kipindi cha nyuma, alikuwa kijana mdogo, aliyechoka ambaye alihitaji kuwa na mafanikio kwa kuwa muigizaji mzuri.
Sikutambua kipaji chake hivyo kuachana naye na kumwambia aende akashiriki shindano moja la kutafuta waigizaji pale Leaders Club. Baada ya siku nyingi kupita, kijana yule akafanikiwa na kuwa muigizaji mkubwa na maarufu zaidi yangu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sikufurahia, sikupenda mtu awe juu zaidi yangu, hasa Filbert ambaye alikuja kwangu na kutaka kuwa maarufu, hivyo nikaanza kupanga mimikati ya kutaka kumuua.
Nikaja kumpata msichana aitwaye Yusnath, huyu ndiye aliyeyabadilisha maisha yangu, hakuwa binadamu, kwa lugha nyepesi naweza kusema kwamba alikuwa jini.
Kila alichokisema, nilimsikiliza na kumtekelezea isipokuwa suala la kutokwenda kanisani tu kutubu dhambi zangu. Nilipokuwa na msichana yule, nilibadilika, woga ukanitoka na mwisho wa siku akanipeleka kuzimu.
Nilikwenda huko kwa kuwa nilitaka kumuua Filbert, nilipofika, walinipa masharti makubwa sana kwa kusema kwamba Filbert alikuwa kwenye mipango yao ya kumuweka katika dini yao, ile ya kumuabudu shetani, hivyo kama nilitaka kumuua, ilinipasa niwaue watu mia moja na ishirini, nikianza na masupastaa, kweli nikafanya hivyo.
Watanzania, naomba mnisamehe, najua kwamba wengi mna hasira dhidi yangu, ila jueni kwamba shetani alinizidi nguvu, akili yangu ikashikwa na akajaa moyoni mwangu na kufanya kile nilichokifanya.
Nisingependa kuzungumza mengi, ila naomba nitangulie kifoni kwa kuamini kwamba wengi mtanifuata. Mungu awapiganie katika mchakato wa kutafuta waigizaji wengine watakaoiinua Bongo Muvi.
Wenu, Edmund.
****
Kesi ya Susan haikuwa na nguvu tena, mara baada ya kutolewa kwa dhamana, kesi ikaendaenda na mwisho wa siku kuachiwa huru kwa kuonekana kutokuwa na hatia kwani hata alama za mikono yake hazikuweza kuonekana katika mwili wa Filbert.
Hiyo ilikuwa furaha kwake, Watanzania wakafurahi lakini kwa upande mwingine, kumpoteza Filbert na Edmund vilikuwa vitu vilivyowauma mno.
Kila baada ya mwaka kupita, Watanzania walikuwa wakikusanyika katika makaburi ya watu hao na kuwaombea rehema kwa Mwenyezi Mungu. Kila kitu kilichopita, yakiwemo maisha ya Filbert na Edmund, yalionekana kuwa historia ndefu ambayo ingesimuliwa kizazi mpaka kizazi.
Watanzania wakaendelea kuwakumbuka, filamu zao walizokuwa wakiigiza zikabaki kuwa kumbukumbu japokuwa filamu nyingi za Edmund zilizuiliwa kutolewa kutokana na kile alichokuwa amekifanya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment