Search This Blog

JUMBA LA WACHAWI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : ZULFA HUSSEIN



    *********************************************************************************



    Simulizi : Jumba La Wachawi

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    28/3/1989

    Ulikuwa ni msafara wa watu watano, wawili kati yao, pamoja na mimi mwenyewe, tukiwa ni waandishi wa habari waajiriwa wa kampuni ya film Tanzania ambayo ilikuwa ni kampuni ya habari na matangazo iliyo jihusisha pia uchapaji wa magazeti ya Tabasamu na Sunday, wakati wale wengine wawili walikuwa ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao walikuwa wanafanya tafiti kwa ajili ya shahada yao ya pili pale mlimani.

    Tulikuwa ni watu wenye furaha kubwa kutokana na namna ambavyo kazi yetu ilivyo kwenda sawa bin sawia, ilituchukua zaidi ya wiki mbili tukiwa mkoani Geita tulikokwenda kikazi, ambapo kampuni ilituteuwa kwenda huko kuangazia matukio yaliyokuwa yakiendelea kutokea katika mkoa wa geita ambayo kwa kiasi kukubwa yalikuwa yakigusa hisia za watu wengi nchini na hata duniani kwa ujumla…migogoro ya wakulima na wafugaji.

    Siku hii ya Juma tano ya tarehe 28/3/1989 ni tarehe ambayo haiwezi kufutika katika akili yangu kwa miaka mingi mno.

    Safari ilikuwa ndefu mno kiasi fulani ilinichosha, lakini hata hivyo kila nilivyo fikiria matunda ya kazi iliyotupeleka huko kwakweli nilipata nguvu kubwa.

    Mwendo mkali wa Landcruser iliyokuwa ikiendeshwa na bwana Magembe Matiku tulitazamia kati ya saa mbili ama saa tatu tutakuwa tumekwisha wasili jijini Dar.

    Tulindoka mkoani Geita mapema alfajiri. Awali wakati tunaanza safari ndani ya ile Landcreuser kulirindima maongezi vicheko na utani mwingi miongoni mwetu, lakini kadiri muda ulivyozidi kuyoyoma ndivyo zile bashabasha zilivyo zidi kuyeyuka,hii ni kutokana na umbali mrefu wa safari yetu uliosababisha kukinaiwa na safari ile ndefu.

    Saa tisa juu ya alama tuliingia mkoa wa Dodoma, hapo bwana Magembe Matiku dereva wa ile landcruser alitutaka tupate chakula cha mchana kabla ya kuendelea na safari ile, tuliingia katika hotel iliyokuwa ndani ya kituo cha mafuta cha Gapico na kujipatia chochote.

    Jua lilikuwa ni kali mkoani Dodoma tofauti na mikoa tuliyopita huko nyuma, jacket nilililokuwa nimevaa halikuwa na nafasi tena katika maungo yangu.

    Nililivua.

    Wakati naliondoa lile jacket maungoni mwangu nililiweka katika mgongo wa kiti nilicho kuwa nimekalia kisha nikaendelea kushambulia chakula kilichokuwa mezani kwangu kwani njaa ilikuwa ikiniuma kisawasawa.

    Katika meza niliyo kuwa nimeketi, sikuwa peke yangu tuliketi wawili mimi na Lovenes huyu alikuwa ni mfanya kazi mwenzangu tuliyekuwa pamoja katika ule msafara wa geita.

    Hatua chache kidogo kulikuwa na meza iliyokaliwa na watu watatu yanii bwana Magembe Matiku ambaye ni dereva wa kampuni yetu,pamoja na john, na mwenzake Fidelix hawa ni wale wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salama waliokuwa katika utafiti wa masomo yao.

    Sambamba na hilo, katika viti vingine vilivyokuwa mule katika hotel ile kulikuwa na watu wengine wengi tu ambao walikuwa wakijipatia chakula mchana ule,upande wa mbele wa meza niliyokuwa nimekaa kulikuwa na meza nyingine iliyokaliwa na mkaka aliyekuwa akinitumbulia macho pindi tu nilivyo saula jacket katika maungo yangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Macho yetu yaligongana mara mbili, awali nihisi imetokea bahati mbaya na nikaendelea kushughulika na kula, macho yakiwa katika sahani.

    Angalau sasa tumbo langu lilishiba, nikanyanyua uso wangu kuangaza eneo la kunawia mikono,lakini wakati nafanya hilo, bahati mbaya tena nikagonganisha macho na yule mwanaume kwa mara nyingine tena, hapo nikagundua kuwa yule kaka alikuwa akinitizama muda wote, pia alikuwa akiniangalia katika namna ambayo ilinielewesha kitu gani kilikuwa kinapita katika akili ya yule mtu.

    Ajabu ni kuwa, pindi nilivyo pata kugonga nisha macho na yule mtu kwa mara hii ya tatu nilipatwa na kitu fulani cha ajabu katika mwili wangu hali iliyo nifanya nistajabu.

    Nilipapatwa na ganzi chini ya mapaja yangu lakini wakati huohuo nikajikuta naingia katika siku zangu japo nilikuwa na wiki moja tangu nitoke katika hedhi na siku zangu za hedhi huwa hazina kawaida ya kubadilika kiasi kile.

    Upesi akili yangu ikaanza kufikiri kuhusu mkoba wangu ulio kuwa ndani ya ile landcrueser ambao ndani yake kulikuwa na pedi ambazo huwa natembea nazo wakati wote.

    Nazipiga hatua kwenda kunawa mikono, kabla ya kuendea mkoba kwa ajili ya kujihifadhi na damu iliyokuwa inachafua nguo yangu ya ndani.

    Wakati niko nanawa mikono, niligeuza shingo kumwangalia yule mtu, nikaona bado ananitizama katika namna ile ile. Nafikiri macho yake yalikuwa yakivutiwa na uzuri wa sura nilio jaliwa na Muumba, na pengine labda macho yake yalivutiwa na umbo langu lililokuwa kama namba nane, ninge kuwa nimevaa blauzi ya kubana ningesema labda yale macho yalikuwa hayajiwezi kwa sababu ya maziwa yangu saizi ya embe dodo bichi, lakini kwa bahati mbaya au nzuri nilikuwa nimevaa shati lilionikaa vizuri ikiwa kwa ndani ya kifua changu nikiwa nimeyabana maziwa yangu kwa sidiria ndogo.

    Sasa vipi huyu mtu anitumbulie mimacho kaisi kile..!

    Anajua yeye mwenyewe.

    “Zahara vipi tena mbona hivyo?” Lovenes alinistua wakati nikitoka ndani ya hotel ile kuelekea mahala lilipokuwa gari.

    “Aagh!. we acha tu shost niko period mwenzio nafuata mkoba garini nichukue pedi nijistiri”

    Nilimjibu haraka haraka kwa sauti ya chini, kisha nikazipiga hatua upesi kwenda lilipokuwa gari. Lakini wakati huo huo bwana magembe matiku na Fedelix pamoja na John nao walikuwa wanatoka mule hotelini

    “Jamani hatuna muda wa kupoteza wapenzi inabidi tufike Dar kabla ya saa tatu usiku” alisema bwana Magembe akichezesha chezesha lundo la funguo mkononi mwake.

    Niliongeza mwendo hadi katika ile landcruser nikachukua mkoba wangu uliokuwa na pedi kisha kikaelekea maliwato na kujihifadhi.

    Wakati huo, yule mtu aliye patwa na ugonjwa wa kuniangalia angalia hovyo nilikuwa nimekwisha msahau katika akili yangu.

    Dakika kumi zilizo fuata tulikuwa ndani ya gari tukiuacha mji wa Dodoma na joto lake, gari lililokuwa likiendeshwa na bwana Magembe likiwa katika mwendo mkali hatari.

    Kulikuwa na maongezi ya hapa na pale ndani ya gari..lakini wasaa ule niliishia kuelekeza macho yangu huko nje nikiangalia vijumba vifupi na vidogo vya makuti vilivyo kandikwa kwa udongo, yakiwa ni makazi ya wanakijiji wafugaji jamii ya wagogo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dakika arobaini baadae watu wote walikuwa wanasinzia isipokuwa mimi na bwana Magembe. Kulirindima ukimya garini zaidi ikiwa ni mlio wa gari uliokuwa ukilalama kutokana na vile bwana magembe alivyokuwa akilivuta kisawasawa.

    Ni hapo nilipo kumbuka walkman yangu ya CD kifaa nilicho kitumia kusikiliza muziki mbalimbali niliyo ihifadhi katika CD…..na wakati nakumbuka kifaa kile ndipo hapo moyo wangu ulipopiga “paaaaaaa” kila kitu kilipita katika akili yangu kama tamthilia.

    Nikajikuta napiga ukulele wa fadhaa. “Jacket languuuuuuu!!..” Nikamstua kila mtu aliyekuwa amelala.

    Na sasa nikakumbana na maswali lukuki kutoka kwa wenzangu..vipi nibwate kwa sauti kubwa kiasi kile kwa ajili ya jacket..thamani yake ni kubwa kwa kiwango gani hata nibweke namna ile na kuondoa kabisa utulivu wa watu mule garini.

    Nilibaki nimeganda nimekodoa macho, mdomo wangu ukiwa wazi,lakini mkono wangu wa kushoto ukiwa umefunika domo lile, sura yangu ikiwa imejaa mshangao mkubwa.

    “Zahara kwani hilo Jacket la kazi gani tena ilihali Dar lingeenda kukaa katika begi, tena pengine lingeishia kuwa chakula cha mende na panya”.

    Alisema John akimaanisha hapakuwa na sababu ya kujutia kulisahau Jacketi ilihali mahala ninako kwenda ni sehemu ya joto kali ambapo uhitaji wa masweta na majacket haupo.



    “Naenda kufanya nini Dar bila lile jacket jamani? ndani ya hiyo nguo kulikuwa na kila kitu ambacho kilitupeleka Geita.kitabu chenye data zote kipo katika mfuko wa jacket, camera ndogo yenye picha za video na still ipo katika mfuko wa jacket, kinasa sauti kilichokuwa na sauti za mahojiano tulizo fanya na wale jamaa waliokuwa wanagombana kuhusu mipaka, kifaa kile kimo katika mfuko wa jacket,na hata zile karatasi za maswali na majibu ya mkuu wa mkoa zoote zimo katika mfuko wa jacket.. lakini pia, hata vitambulisho vyangu vyote vimo katika lile jacket”

    “Nooooo!!.” Nini tunafanya jamani!!. nini hiki aagh” bwana Magembe alipiga kelele baada ya kutoa malezo yale. Na mwisho alikanyaga breki ghafla na gari likasimama katikati ya barabara huku tairi za gari zikijiburuza katika lami na kutoa mlio mkali wa mburuzo.

    Kwakweli maelezo yangu yalimchanganya kila mtu hasa wale wafanyakazi wenzangu,vifaa vilivyokuwa katika jacket vilikuwa ni vitu muhimu kwa mustakabali mzuri wa ajira zetu.

    Kamwe mkurugenzi isingeweza kutuelewa kama tungerudi bila taarifa yoyote ya geita ilihali ofisi iligharamia gharama zote za utafiti wa makala ile na hata kutulipa pesa nzuri tu kwa kipindi chote ambacho tulikuwa mkoani Geita.

    “Sasa tunafanya nini jamani” aliuliza Lovenes.

    “Unajua kama huu ni uzembe wa kipuuzi ulio ufanya wee Zahara” badala ya kujibu bwana Magembe Matiku aliyekuwa amefura kwa hasira alinitupia lawama.

    Nilijisikia vibaya mno kwa maneno yale ya bwana Magembe lakini sikuwa na lakufanya kwani kweli kosa lilikuwa langu japo sikukusudia kulitenda.Sikujibu chochote zaidi ya kuwa kimya nikingoja maamuzi ya wenzangu juu ya ni kitu gani watafanya.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hatuna chaguo jingine zaidi ya kurudi Dodoma” Fidelix aliyekuwa kimya muda mwingi alishauri,ushauri ulioungwa mkono na John na hata Lovenes, Bwana Magembe alikuwa amevimba kwa hasira alitizama saa yake ya mkononi na kuona ilikuwa ni saa kumi na mbili na robo za jioni.

    Aliachia breki na kuingiza gia kisha akaliondoa gari kwa kasi na kukata kona kwa kasi na kulielekezea kule tulikotoka.

    Safari ya kurudi Dodoma ikaanza.

    Ilituchukua dakika arobaini na tano nyingine kufika Dodoma mjini na hapo tukanyooka na barabara kama tunaelekea singida na kilometa moja nyingine tukawa tumefika katika kile kituo cha mafuta ambacho kilikuwa na huduma ya mgahawa.

    Hapo ilikuwa yapata saa mbili kasorobo usiku.

    Nilikuwa wa kwanza kushuka katika gari na kukimbia ndani ya ule mgahawa,nilipo ingia ndani macho yangu moja kwa moja katika kiti nilichokuwa nimekalia ambapo ndipo nilipo weka lile jacket.

    Moyo wangu ulinidunda kwa nguvu kutokana na kile nilicho kiona, kiti kile kilikuwa kitupu.lile jacketi halikuwepo mahala pale.

    Sasa nilianza kuona dalili ya kupoteza kibarua chuangu kinacho niweka mjini mimi na familia yangu.

    Kwa muda wa nusu dakika niliweza kuona maisha ambayo nitakwenda kuishi muda mfupi ujao baada ya kufukuzwa kazi katika kampuni.

    Nilimwona mama mwenye nyumba wangu {mama Leila} namna atakavyo kuwa akinisumbua juu ya kodi yake ambayo ilikuwa ikielekea ukingoni, niliona namna wazazi wangu watakavyo kuwa wakinipigia simu mara kwa mara na kuhitaji msaada wa kifedha kutoka kwangu hali ya kuwa wakati huo mifuko yangu itakuwa imetoboka kwa kutokuwa na ajira yenye kuniingizia pesa.

    Lakini pia, niliona namna mdogo wangu Nasri namna anavyo sitisha masomo yake kwa kushindwa kuendelea kumsomesha kwa kukosa ajira yenye kuniingizia fedha.

    “Vipi dada yangu kulikoni?” nilistushwa na sauti ya muhudumu wa mgahawa ule aliyekuwa amesimama nyuma yangu na kunishangaa namna nilivyokuwa nimeganda mithili ya sanamu.

    Lakini kabla sijamjibu, muda huohuo akina Lovenes nao wakaingia.

    “Vipi umeliona” wote waliniuliza kwa pamoja kana kwamba waliambizana.

    “Hapana, kiti ni kitupu, jacket halipo”

    “Shuuuuph” mr Magembe alishusha pumzi huku mikono yake ikiwa kiunoni.

    “Kwani kuna nini jamani”Muhudumu wa ule mgahawa aliuliza.

    “Kuna jacket nililisahau katika kiti hiki wakati tulipo kuja kula chakula hapa kama lisaa limoja hivi limepita”

    “Jacket la rangi ya kaki..?”

    “Ndiooo” niliitikia upesi upesi nikihisi kuna uwezekano wa kulipata ile nguo kwa kuona muhudumu yule anaifaahamu.

    “Hiyo nguo niliichukua na kuipeleka ofisini lakini alikuja mkaka mmoja jina lake nimelisahau alisema lile jacketi ni la mwenzenu ambaye mpo nae katika safari moja mkitokea geita na ulikuwa umelisahau na mmemtuma yeye aje kulichukua hapa”

    “ Whaaat!.”

    Wote tuliuliza kwa mshangao, kwa pamoja.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwani ninyi huyo mtu hamjamtuma na hamjui?!” Muhudumu aliuliza tena kwa mshangao.

    “Hicho kitu unacho sema kigeni kabisa.hatumjui huyo mtu” John alisema.

    “Na kwani huyo mtu yukoje” niliongezea kwa kuuliza.

    “Mkaka mweusi mrefu ana kitambi kidogo, wakati ninyi mnakula chakula yeye alikuwa amekaa katika kiti hicho hapo” Hapo taswira ya yule mtu aliyekuwa akinikodolea mimacho yake mibaya hadi nikaingia katika siku zangu, sura yake ikanijia mbele yangu

    “Blood fool mijitu mingine sijui ikoje kudada’deki ni lile likaka lililokuwa limekaa hapo likiniangalia hovyo” nilisema kwa ukali huku nikihisi huzuni isiyo na kifani

    “Basi huyo mvulana atakuwa ni mwizi” lovenes alisema pia kinyonge.

    “Sasa tunafaanya nini?” mtu mwingine aliuliza, mie nguvu zilikwisha, niliona nilichokuwa nimebakiza ni kufukuzwa kazi na kuingia uraiani na kupambana na ukali wa maisha kwa namna nyingine.

    “Kuna kituo cha polisi hapo mbele kama hamto jali tuongozane tukafungue kesi” alisema yule mfanya kazi wa ule mgahawa.

    Tulikubaliana na ushauri wa yule muhudumu tulikwenda kituo cha polisi na kufungua kesi kisha tukapewa Rb.

    Baada ya hapo safari ya Dar ikaanza tena.

    ********

    Saa sita na nusu za usiku tuliingia jijini kila mtu alikuwa amechoka vibaya..baadhi ya watu walishukia Ubungo ila kwakuwa mr Magembe alikuwa akiishi Gongo la mboto na mimi nilikuwa nikiishi Buguruni malapa alinisogeza hadi buguruni sheli na kuniacha pale.



    Pale nilichukua bajaji usiku ule na kumtaka dereva anipeleke malapa.

    Njaa ilikuwa inauma lakini sikuwa na hamu ya kula chakula chochote, nilikuwa mnyonge mno.

    Usiku ule nilikuta geti la nyumbni kwangu limefungwa nilizunguka katika dirisha la mama mwenye nyumba na kumgongea anifungulie mlango.

    “Eeh Zahara huyoo!”

    “Ndiye mimi mama”

    “Karibu mwanangu za huko”

    “Salama tu mama za hapa”

    “Hapa kwema mwanangu sijui mnatunyima nini huko”

    “Mvua, matope na baridi”

    Nilisema kwa utani, na hapo mama akacheka huku mimi nikifungua komeo la mlangoni kwangu na kuingia ndani.

    “Halafu….we zahara ”

    “Abee mama”

    “Kuna baba mmoja amekuja hapa leo kukuulizia mara kumi kumi” alisema mama mwenye nyumba.

    “Baba yupi huyo?”

    “hajaniambia jina lake ila anasema mlikuwa wote huko usukumani huko uliko kuwa na mlikuwa katika safari moja leo”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unasema!!” moyo wangu ulipiga mkumbo kama mdundo wa nyimbo za Marijani Rajabu, taswira ya yule mtu kule katika mgahawa ikanirejea tena usoni mwangu.

    “Unasema kweli mama?”

    “Ndio..kwanini nikuongopee mama”

    “Hakuacha chochote hapa”

    “Ameacha”

    “Kaacha nini?”

    “Namba ya simu”

    Kidogo nilipata nguvu nikaona tumaini jipya la maisha yangu.,kwani niliamini nitavipata vifaa vyangu,na kwa mara ya kwanza nilijikuta naomba toba kwa Mungu wangu kwa kumuhisi vibaya yule mtu.,kwakweli hakuwa ni mtu mbaya angekuwa mwizi kama ambavyo tulimuona kamwe asinge fika pale nyumbani kunitafuta ilihali akiwa ameiba vitu vyangu

    “Mungu wangu nisamehe kwa kumuhisi vibaya huyu kaka” nilisema kimoyo moyo huku nafsi yangu ikiwa na furaha.

    Jambo moja ambalo sikuwahi kujiuliza muda ule ni vipi mtu yule alinifahamu mimi kuwa nilikuwa geita na pia kujisema kuwa alikuwa na mimi pamoja huko geita, lakini kubwa kuliko yote ni vipi alipajua nyumbani kwangu ninapo ishi.

    Nikiwa bado ni mwenye faraja moyoni, mama mwenye nyumba alinipa kipande cha karatasi kilicho kuwa kimeandikwa namba ya simu.

    Kwa mara nyingine nilishukuru mno,niliingia ndani mwangu na kuwasha taa kisha nikaketi kitandani, kabla ya kufanya lolote nilitoa kadi yangu ya posta na kutoka nje kutafuta vibanda vya simu.

    Sikupata tabu kupata kibanda cha simu,.niliandika zile namba kisha nikazipiga

    Simu ilita upande wa pili kwa muda kidogo kisha ikapokelewa na sauti nzito yenye mkwaruzo.

    “Hellow”

    “Habari yako kaka” nilisalimia

    “Sijambo..ooh Zahara, hujambo bibie” alijibu yule mtu, nilistuka kidogo, vipi huyu mtu anijue namna hii,amejua vipi jina langu.

    “Safi tu, nafikiri ni wewe uliyekuja kunitafuta nyumbani kwangu?”

    “Bila shaka”

    “Na bila shaka ni wewe uliye ondoka na jacket langu kule Dodoma?”

    “Haswaaa” alijibu tena yule mtu, nilishusha pumzi ndefu nikahisi furaha ikiongezeka moyoni kwa kulipata jacket langu lililokuwa na vitu muhimu.sikujali wala sikuwa na habari tena na namna yule mtu alivyotumia utaratibu wa kulichukua lile jacket kule katika mgahawa, kilicho kuwa katika akili yangu wakati huo ni kuhakikisha naipata ile nguo yangu hususani vitu vilivyokuwa ndani ya lile jacket

    “Sasa nalipata vipi hilo jacket?” niliuliza.

    “Njoo agrey kariakoo”

    “Sasa hivi?” niliuliza kwa mshangao huku nikitizama saa na kuona ilikuwa yapata saa saba na nusu usiku.

    “Ndio lazima iwe sasa hivi vinginevyo unaweza kulikosa, mie kesho asubuhi naondoka na basi la chakito kuelekea mlalo huko lushoto.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilisimama wima nikapatwa na taharuki ya kulikosa jacket, japo sikuwa tayari kabisa kulikosa tena lile jacket.

    Niliagana na yule mtu na kumuhakikishia kuwa nitakuwa mtaa ule wa Agrey muda mchache ujao.

    Nilikurupuka na kutoka mule ndani bila hata kumwaga mama mwenye nyumba usiku ule na kutokomea mtaani.

    Nilipanda basi la mjini kwa miaka hiyo yalikuwa ni yale mabasi ya kizamani kabisa yenye kuitwa chai maharagwe lililo nipeleka hadi mtaa wa agrey kariakoo.

    Hapo nilisimama mbele ya stendi ya mabasi ya tabata na buguruni kisha nikaingia katika kibanda cha kupiga simu na nikampigia simu tena yule mtu.

    “Shuka mbele kidogo huku, kama unakuja mnazi mmoja, tizama upande wa kushoto utaona ATM ya NMB kisha ingia katika ghorofa inayofuatia, panda juu hadi orofa ya nne, utanikuta katika korido ya milango ya lifti nakungoja..”

    Baada ya kupewa maelekezo hayo nilizipiga hatua kuelekea eneo lile nililoelekezwa, bahati ni kuwa hapakuwa mbali.

    Dakika chache nyingine nilikuwa katika lift ya jengo lile ambalo sikujua ni jengo linalo jishughulisha na nini, kilicho nistajabisha ni kuwa hapakuwa na mlinzi katika jengo lile.

    Lakini hata hivyo sikujali sana kwani kilicho nipeleka pale ni vitu vyangu vya ofisini na si vinginevyo.

    Sekunde kumi nyingine milango ya lifti ilifunguka,tayari nilikuwa orofa ya nne,

    Nilitoka ndani ya ile lift.

    Hapo nikakutana na yule mtu mwenye kupenda kunitizama. Alipo niona aliachia tabasamu ambalo nililiona kule Dodoma,lile tabasamu liliongea kitu, nafikiri lilisema “nimekutana na mwanamke mrembo”.

    “Karibu Zahara” alinikalimu huku akinipa mkono tabasamu lake likizidi kustawi usoni mwake.

    “Nakushukuru sana”. Nilijibu huku na mimi nikimpa zawadi ya tabasamu, akanionyesha ishara nimfuate, wakati naongozana nae, macho yangu yalikuwa yakisaili ile nyumba ilikuwa ni kama hotel ya kisasa kwani kila tulipo pita katika korido, niliona vyumba vilivyo andikwa namba mithili ya vyumba vya hoteli ya kisasa, sikuwa na uhakika sana na hisia zangu kuwa huenda ile nyumba ikawa hoteli kwani nilivyo ingia katika ile nyumba sikuona mapokezi wala sikukutana na mtu yeyote mbali na yule mbaba mwenyeji wangu.



    Safari yetu ilishia mbele ya mlango mmoja ulio andikwa Room No 104. alisukuma mlango wa chumba kile na kujitoma ndani, “karibu Zahara..pita ndani”

    “Asante”, niliingia ndani ya chumba kile, kilikuwa ni chumba nadhifu ndani kukiwa na kila kitu cha thamani kinacho takiwa kuwapo chumbani.

    Niliketi katika kochi huku macho yangu yakizidi kusaili mule ndani,.sikuwa na wasiwasi na lolote.

    Kitu kimoja ambacho sikuwahi kukijua wasaa ule ni kuwa uwepo wangu eneo lile ungeweza kunisababishia madhila makubwa mno ambayo nisingeweza kuyasahau kwa milongo mingi juu ya mgongo wa ardhi.

    Yule mtu alisogea katika kabati la nguo na kufungua, kisha alitoa jacket langu na kunikabidhi, nilifurahi, muda huo huo nilianza kulipekua ili kuona kama vifaa vyangu vipo salama.

    Naama vitu vyangu vyote vilikuwa salama, nilishusha pumzi ndefu na kuhisi furaha nyingi moyoni. “Asante sana kaka yangu, sina cha kukulipa kwakweli, ila nashukuru mno kwa wema wako vitu hivi ni muhimu mno”

    Yule mtu alitabasamu, lakini hakufumbua mdomo, alitizama pembeni bila kujibu shukrani zangu kwa sekunde sita au saba kisha akasema, “usijali Zahara ilikuwa ni lazima hili litokee ili upate kunifahamu”

    “Yeah.. ni kweli, hakika Mungu ndio mapangaji wa kila kitu ulimwenguni”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “No, no,no hili halihusiani na mipango ya Mungu Zahara, huu ni mpango wa sisi wanadamu”

    “What!!”

    Niliuliza kwa mshangao, maneno ya yule mtu yalinichanganya.

    Yule mtu alinisogelea pale sofani na kuketi mkabala na mimi.

    “Huu ni mpango wangu mahsusi” alisema tena kwa utulivu huku akinitumbulia macho yake makali pasina kupepesa kando.

    Nilifikiri kwa muda, nikaona kwa dakika nyingine tena nashindwa kabisa kumuelewa yule mtu yale maneno yake.

    “Any way, acha niseme tu nashukuru na sasa wacha mie niondoke maana usiku usha kuwa mkubwa” hatimae niliona ni kheri niage na kuondoka maana sikuwa na sababu nyingine ya kuumiza kichwa kwa maneno ya yule mtu ambayo nilihisi alitamka pasina kufikiri, aidha hisia zingine zikaniambia pengine alikuwa amekunywa pombe kidogo na kuvuruga kidogo ubongo wake.

    Nilisimama na kuzipiga hatua kuelekea mlangoni, “sawa kila kheri mrembo” yule mtu alisema, sikumjibu zaidi ya kuachia tabasamu lililosema “tuko pamoja”

    Nilipita katika ile korido na kukata kulia kuelekea katika lifti. Pale katika korido ya lifti nilikuta lifti zote tatu zikiwa zinatumika, hivyo nilisisima na kusubiri kwa muda kidogo.

    Dakika moja badae mlango wa lifti moja katika zile tatu ukafunguka, bila kuchelewa nikajitoma ndani.

    Nilibonyeza kitufe kilicho andikwa G1, lifti ilishuka chini na sekunde tano tayari taa ya kijani ikaonyesha nimekwisha fika G1, nilitoka ndani ya lifti ile nikiamini sasa naweza kutoka nje ya jengo lile na atimae kurejea nyumbani usiku ule.

    Ajabu ni kuwa, pale lifti ilipo simama na mimi kutoka nje, nilikutana na mzingira mageni machoni mwangu. Halikuwa eneo la nje ila nilipo chunguza vizuri niligundua nilikuwa orofa ya kwanza, hapo nikagundua nilifanya makosa wakati nilipo kuwa mule ndani ya lifti ile, sikutakiwa kubonyeza ‘G1’ badala yake nilitakiwa kubonyeza ‘G’ pekee, hiyo ingenipeleka hadi chini kabisa ya ghorofa lile.

    Lakini hata hivyo sikuona tabu kwani chini hapakuwa mbali ni kiasi cha kushuka ngazi kama nne na kuweza kuwa nje ya jengo lile.

    Nilizifuata ngazi na kuanza kushuka chini. Eneo lile lilikuwa kimya, kulikuwa na taa za bulb kubwa zilizo toa mwanga hafifu wa rangi ya njano, nilishuka ngazi ya kwanza na sasa nikashika ngazi ya pili. Chini ya ile ngazi ya pili, nilipata kuona kitu..

    Eneo lilikuwa kimya kama nilivyo pata kusema. Mwendo wangu wa kasi wa kushuka ngazi ukabadilika na sasa nilishuka taratibu nikitupia macho kitu nilicho weza kuona, na hapo nika jua alikuwa ni mtu.

    Alikuwa amejikunyata pembezoni mwa zile ngazi, alikuwa amejifunika shuka nzito la rangi nyekundu mwili wote kasoro kichwani.

    Jambo moja lilipita kichwani mwangu, kwa vyovyote vile yule mtu atakuwa ni mlinzi, wazo hilo lilizidi kustawi katika akili yangu baada ya kutizama saa na kuona ilikuwa yapata saa nane kasoro dakika kumi za usiku, “ hawezi kuwa mtu wa kawaida eneo hili,tena muda huu pasina kuwa ni mlinzi”

    Hatua zangu zikiwa za kawaida kabisa nilifika eneo lile ambapo mtu yule alikuwa amejikunyata, nilimpita pasina kumsemesha lolote na kukuta kushoto kwa ajili ya kuanza kushuka ngazi zinazo fuatia.

    Ila ghafla.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sauti ilitoka kwa yule mtu ilinifanya nitishike vibaya mno,yule mtu alisema, “Usiku mwema Zahara” niligeuza shingo na kutupa macho yangu na kumwangalia yule mtu, hapo nikakutana na kitu ambacho kilinifanya hali ya mshangao, niliduwaa, macho yamenitoka,midomo imefumbuka kama lango la daradara aina ya UDA la mbagara, nikaanza kutokwa na jasho, kitu kisicho cha kawaida nikaona kinanyemelea maisha yangu.alikuwa ni yule mtu aliyekuwa na jacketi langu lililokuwa na vitu muhimu vya ofisi.

    Nilijikuta nataka kutimua mbio ila miguu ilikuwa mizito nikabaki nimeganda namtizama yule baba.

    “Hivi Zahara pamoja na kusaidia kibarua chako hujataka kunifahamu hata jina langu bibie?”. Yule mtu aliuliza huku akisimama kwa tabu eneo lile.

    “We umefikaje fikaje hapa?” badala ya kujibu nilijikuta namtupia swali huku nikiendelea kumshangaa na sasa haukuwa mshangao tu bali ulikuwa ni hofu kubwa iliyochanganyikana na mshangao.

    Yule mtu alisimama wima akiwa bado amejifunika lile shuka jekundu, miguuni akiwa peku.

    “Katika maisha yangu ya Kichawi sijawahi kuona mwanamke msomi lakini wakati huo huo ni zumbukuku wa mwisho kama wewe!.” Yule mtu alisema, kauli ile ilinifanya mwili wote uingiwe na baridi na kuwa kama mithili ya mtu aliye mwagiwa maji ya baridi. Pumzi zilinitoka kwa kasi sasa nikaona kumbe nimekutana na kiumbe kisicho cha kawaida, sikutaka zaidi kuyatafakari maneno mengine ya yule mtu, neno ‘Mchawi’ lilitosha kabisa akili yangu kuiamrisha miguu yangu ikimbie kwa kasi eneo lile.

    Nilitoka mbio nikiwa nimekumbatia jacket langu kifuani nikitoa yowe dogo la msaada, nilizishuka ngazi upesi upesi upesi huku nikiyumba hovyo.

    Nikamaliza zile ngazi sasa nikashika ngazi za mwisho na kuwa chini ya jengo lile, wakati nashuka ngazi ya kwanza, ngazi ya pili ile nashuka ngazi ya tatu tu.. nilijikuta nikifunga breki ghafla na kubaki nimesimama huku nikiweweseka.

    Yule mtu alijitokeza kutokea kona ya mwisho ya ile ngazi, alitembea kikakamavu kunisogelea huku mwendo wake ukifanana kabisa na viumbe aina ya saibogi, alikuwa akinijia kwa mwendo wa kunyata lakini akijiamini, macho yake yakiwa makali, huku sura yake kwa ujumla akiifinya na kufanya awe na mwenekano wa kutisha, alichanua vidole vya mikono yake na kutanua mikono yake huku akitoa ngurumo ndogo mithili ya mtu aliye pandisha majini na akawa ananisogelea. Kwakweli niliogopa mno.

    Kwa muda wa sekunde zisizo zidi tatu, nilibaki nimebung’aa nikishangaa yale mambo yaliyo kuwa yanajiri mbele yangu katika jumba lile kabla ya kujikuta nikipiga kelele kwa nguvu.

    “Mamaaaa, mamamaaa nakufaaaa uwiiiiii nisaidieniii” nilipiga kelele nyingi huku nikitoka mbio kupandisha ngazi kurudi juu.

    Nilikuwa nahema kwa kasi, nikizidi kupiga kelele huku nikijitahidi kuzipanda ngazi za jengo lile kujitenga na yule mtu wa ajabu, mashaka makubwa yalikuwa kifuani kwangu.

    Sikumbuki vizuri nilipanda ngazi hadi orofa ya ngapi, ila ninacho kumbuka ni kuwa ilifikia hatua mapafu yangu yalichoka, nilichoka kupiga mayowe kwa nguvu huku nikizipanda ngazi tena nikiwa nakimbia.



    Niliangaza nyuma yangu na kuona niko peke yangu, hapakuwa na mtu yeyote aliye kuwa akinifuata lakini pia hakujitokeza mtu kunisaidia, pamoja na kwamba nilikuwa nikipiga makelele ya hali ya juu, lakini hata hivyo sikumwona tena yule mtu wa ajabu.

    Sasa nikiwa najisukuma kwa mbele kwa mwendo wa kutembea nikiendelea kuzipanda zile ngazi, nilikuwa nahema kwa kasi, machozi na kamasi vilikuwa vikinitoka kwa pamoja, woga wa kuingia katika mikono ya mchawi ulikuwa mkubwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mungu wangu wa mbinguni uko wapi sasa muda huu!.huoni ninavyo ingia katika madhila haya? Sasa unangoja nini kunisaidia Yarabii..” nilijikuta nikitamka yale maneno huku nikiwa nimepagawa katika kiwango cha mwisho.

    Nilizidi kuzipanda ngazi bila kuona dalili yoyote ya kufatwa ama uwepo wa mtu katika jengo lile, eneo lote lilikuwa kimya, ilikuwa ni sauti ya vishindo vya hatua zangu kupanda zile ngazi ndio zilizo sikika.yanii ilikuwa ni kama kwamba kile kilicho tokea muda mchache kilikuwa hakija tokea.

    Ni hapo nilipo ingiwa na fikra hizi, kuwa huenda ndani ya ghorofa hili kulikuwa na mtu mmoja tu yanii yule mtu mchawi.

    Wakati nalitafakari hilo akilini mwangu wazo jingine likanijia, “kwanini nazidi kuelekea juu ama ndani zaidi ya jengo hilo?” nilijiuliza mwenyewe swali hili lakani jibu lake lilikuwa ni jepesi tu, nikajipatia jibu mwenyewe kuwa “naelekea juu ama ndani zaidi ya jengo lile kwakuwa namkimbia yule mtu asiye wa kawaidi” lakini nikajiuliza tena, “kama namkimbia yule mtu asiye wa kawaida kwa kuingia ndani zaidi ya jengo lile eneo ambalo inavyo onyesha ndio himaya yake na anajua kona zote za jengo lile, je zile hazitakuwa ni sawa na mbio za siafu.? Na hiyo si ni sawa na kujiingiza ndani ya kichaka cha adui?.”

    Nilijiuliza..

    Lakini ubongo wangu haukupata jibu. Ni hapo nilipo hisi sauti fulani ikinitahadhalisha kuendelea kuzipanda ngazi za jengo lile.

    Nilisimama ghafla na kubaki nimeganda. “Sasa nifanye nini Mungu wangu” nilisema kwa sauti ya ya kunong’ona. Mwisho niliazimia Lazima nitoke nje ya jengo hili liwalo na liwe lakini lazima niwe nje.

    Kwa mara nyingine nikajikaza kama mwanamke nikageuka nyuma na kuanza kuzishuka ngazi tena, wakati nikiwa nashuka chini kwa bahati upande wangu wa kulia mwa ukuta niliona kuna mtungi wa gesi lakini pembeni ya mtungi huo kulikuwa na shoka ndogo ya chuma yenye rangi sawa na ile ya ule mtungi wa gesi.

    Bila kujiuliza mara mbili niliifyatua ile shoka iliyokuwa umepachikwa katika kishikizio chake pale ukutani, sasa nikawa tayari kupambana na yule baba machawi pale itakapo bidi.

    Nikaendelea kuteremka taratibu nikiwa na tahadhali kubwa, wakati huo ilikuwa yapata saa saba na dakika hamsini.

    Kitu kingine ambacho ningependa ndugu msomaji ufahamu, ni kuwa, tangu niingie katika jengo lile nilipata kutizama saa yangu ya mkononi mara mbili, ajabu ni kuwa muda ulikuwa ikienda taratibu zaidi ya kawaida.

    Kwa kipindi ambacho nimetumia kuwasili katika lile jengo hadi kutokea kwa sinto fahamu, kwa makadirio ilikuwa yapata kiasi cha dakika thelathini lakini saa yangu ilinionyesha ni kiasi cha tofauti ya dakika tatu tu toka niingie hadi sasa.

    Sikufikiria zaidi hilo kwani akili yangu ilifikiria zaidi ni kwa namna gani nitatoka Mule ndani.

    Nikiwa bado nashuka zile ngazi kwa mbali nikahisi kuna chakala chakala za mtu kutokea huko chini niliko kuwa naelekea, nilipunguza mwendo nikauvaa ujasiri na sikuwa tayari kurudi nyuma, sasa nikaelewa kuwa kutokea kule chini kulikuwa kuna mtu aliye kuwa akipanda ngazi kwa kasi, zaidi ni kuwa mtu huyo alikuwa akitweta huku akitoa sauti kama ya mtu aliyepagawa kutokana na taharuki Fulani.

    Sauti iliendelea kunikaribia na ilikuwa ni sauti ya mwanamke, nilisogea pembeni na kutupa macho kule chini, nilimwona mwanamke mnene kiasi, akizipanda ngazi kwa kasi lakini akiwa ni mtu aliye changanyikiwa vibaya mno.

    Nilipata hofu moyoni, nikalewa kwa vyovyote vile mwanamke yule lazima atakuwa amekutana na yule baba mwenye kujisema kuwa yeye ni mchawi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilisimama pale katika ngazi kumngoja yule mwanamke nikiamini kwa vyovyote vile masaibu yaliyomkuta yanafanana na yangu hivyo sina budi kuunguna nae na kuangalia njia ya kutatua sintofahamu ile.

    Yule mwanamke sasa alianza kupanda ngazi moja kabla ya kuanza ngazi ya pili niliyokuwa nimesimama mimi.

    Na wakati anamaliza zile ngazi ile anaanza tu kupanda, alisimama ghafla na kupiga ukulele mwingi wa hofu baada ya kuniona mimi.

    “Nyamaza,..nyamaza..tulia tafadhali, mie sio mtu mbaya”, nilisema kwa sauti ya juu, yule mwanamke alitulia kidogo akawa ananiangalia kwa mashaka makubwa.

    “Tulia tafadhalia mimi pia nina matatizo kama yako” niliendelea kumsihi yule mwanamke.alibaki akihema huku akiliangalia lile shoka nililokuwa nimelikamata, kwakweli ilimchukua sekunde kadhaa kabla ya kuniamini.

    “Wanakuja” yule mwanamke alisema huku akihema kwa kasi.

    “Akina nani!”

    “wanakuja kuniua tukimbie..wako wengi..wanakuja” alisema yule mwanamke wa makamo pasina kunipa taarifa vizuri.

    “Wako wapi akina nani?” nilimuuliza.

    Lakini hakujibu zaidi ya kusonta kwa kidole kuonyesha kuwa wako huko aliko toka na kabla sijasema kitu kingine yule mwanamke alitoka mbio na kuzidi kupanda juu.

    Moyo wangu ulipiga paaaa, nilihisi tumbo linapata joto huku mate mepesi yakijaaa mdomoni lakini pia jasho jembamba lilinitoka maungoni mwangu.

    Nikabaki nimesimama pale moyo wangu ukishindwa kabisa kwenda mbele lakini pia akili yangu haikuwa tayari kabisa kurudi nyuma nilibaki nimegenda kama sanamu la askari pale posta.

    Yule mama alizidi kuziparamia ngazi na kutokomea kabisa kule juu. Sasa nikaelewa kuwa kumbe kuna watu zaidi ya mmoja katika hili jengo, si kama nilivyokuwa nikifikiria hapo awali.

    Nikiwa bado pale, shoka langu likiwa mkononi, nilitupa macho yangu kule chini nilikokuwa naelekea, nilicho kiona kilinitisha sana.

    Watu wanne wanaume walikuwa uchi wa mnyama, walikuwa wamebeba mwili wa mtu aliyekuwa kama mtu aliye ungua na moto,mwili wa yule mtu aliye kuwa amebebwa katika machela ulikuwa na nyama nyekundu iliyoonyesha kama mtu yule amebabuliwa na mafuta ya moto, wale watu walikuwa wamejipaka masizi meusi usoni mwao na kufanya waonekane kama vinyago vya kimakonde. Walikuwa wakizipanda ngazi kuja juu nilikokuwa mimi huku wakiimba nyimbo Fulani kwa lugha ambayo sijawahi kuisikia hapa duniani.

    Kwakweli nilijikuta nikipiga kelele nyingi na kutoka mbio huku nikitupa kile kishoka na kupanda juu mradi nijiweke mbali na jambo lile la kutisha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog