Search This Blog

MALAIKA WA KIFO - 4

 





    Simulizi : Malaika Wa Kifo

    Sehemu Ya Nne (4)





    Kwa mbali moyo wake ulikuwa na hofu tele, yule kiumbe wa ajabu ambaye alikuwa akimwangalia mbele yake alitisha mno. Si huyo tu bali hata viumbe wengine waliokuwa pembeni yake, walionekana kuwa kama yule.

    Japokuwa alitakiwa kuhofia sana lakini alijishangaa, hofu haikuwa kama ile iliyotakiwa iwe, moyo wake ulikuwa na hofu kwa kiasi kidogo mno. Watu waliokuwa ndani ya jengo lile waliendelea kumsujudia yule mungu wao ambaye ndiye shetani, waliimba nyimbo ambazo hazikuwa zikieleweka masikioni mwake.

    Mavazi ambayo waliyavaa watu wale hayakuwa ya kawaida hata kidogo, yalikuwa mavazi yenye kutisha ambayo kwa mtu wa kawaida angeweza kuyaona ni lazima angeogopa sana.

    Mbali na watu waliokuwa ndani ya jumba hilo, pia kulikuwa na mapipa makubwa yaliyokuwa yamejazwa damu huku pembezoni kukiwa na mafuvu ya watu ambayo yalikuwa maalumu kwa ajili ya kuchotea damu kutoka katika mapipa hayo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tunataka tulete mapinduzi, tunataka tuwabadilishe watu waendelee kuvipenda vitu vyetu,” alisikika akisema kiumbe yule.

    “Tutawaangamiza watu kupitia wanamuziki, waigizaji filamu, watu maarufu na hata kupitia serikali. Ajali zimepungua kwa kiasi kikubwa, tunataka tuongeze wingi wa ajali ili damu iwe nyingi mahali hapa,” alisikika mtu yule.

    Siku hiyo, baadhi ya viumbe vya ajabu vikagaiwa majukumu, kuna wale ambao waliwekwa katika kundi ambalo kazi yake kubwa ilikuwa ni kusababisha ajali sehemu mbalimbali duniani.

    Ukiachana na hao, kulikuwa na kundi jingine ambalo kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwapa watu uvivu wa kwenda katika nyumba za ibada, kusoma vitabu vya dini, kupenda kusinzia katika nyumba za ibada na kupuuzia kila kitu ambacho kingekuwa kikizungumziwa katika nyumba za ibada.

    Ukiachana na makundi hayo, pia kulikuwa na kundi jingine ambalo kazi yake kubwa lilikuwa ni kuwaangamiza watu kupitia tamaa za miili. Hizi zilikuwa roho ambazo kama zingemuingia mtu yeyote yule ilikuwa ni lazima kumtamani mwanamke au mwanaume.

    Zilikuwa roho zenye nguvu na ambazo ziliwachukua watu wengi mno. Katika roho hizo, pia kulikuwa na roho zilizokuwa na nguvu ya kumshawishi msichana yeyote kuvaa nguo fupi kwa ajili ya kuwatega wanaume na mwisho wa siku watende dhambi kupitia mawazo machafu.

    Edmund alikuwa akiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea kule kuzimu. Kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hofu ikapungua na mwisho wa siku kupotea kabisa.

    Baada ya dakika kadhaa, akafuatwa na viumbe ambavyo hakuvielewa, vilikuwa na sura ya mbuzi, viumbe vile vikamwambia wamfuate kwa sababu mkuu asingeweza kuzungumza naye muda ule kutokana na ubize aliokuwa nao.

    Bila hofu yoyote ile, yeye na Yusnath wakaanza kuwafuata viumbe wale ambao wakaingia ndani ya chumba kimoja kilichokuwa na mwanga hafifu.

    Yusnath, msichana mrembo, mara baada ya kuingia ndani ya chumba kile, akaanza kubadilika na kuwa kama viumbe wale, akaota mkia, matiti yake yakapotea, mdomo wake ukawa mkubwa na wa kutisha kama wa bata, macho yakawa makubwa na huku kichwa chake kikianza kuota mapembe.

    Japokuwa hali iliyokuwa mahali hapo ilikuwa ni ya kutisha lakini bado Edmund hakuonekana kuwa na hofu hta kidogo, moyo wake uliwekwa na ujasiri ambao hata yeye mwenyewe hakujua ulitokea wapi.

    “Tumekwishajua shida yako, nenda duniani na huyu atakusaidia,” alisema kiumbe mmoja huku akimaanisha mtu wa kutoa msaada alikuwa Yusnath.

    “Hawezi kunisaidia ndiyo maana amenileta huku ili mnisaidie wakuu,” alisema Edmund.

    “Amini kila tunachokwambia, fanya chochote atakachokwambia na hakika utafanikiwa katika kila ulifanyalo,” alisema kiumbe yule.

    Edmund akayageuza macho yake na kumwangalia Yusnath kwa mara nyingine tena, bado alikuwa katika umbo lake la kutisha, Edmund hakuonekana kuhofia kitu chochote kile, kwa sababu aliambiwa kwamba msichana huyo angemsaidia, hakutaka kumtilia mashaka.

    Siku hiyo alitembezwa sehemu kubwa huko kuzimu, aliweza kupelekwa mpaka sehemu iliyokuwa na mitungi mikubwa iliyokuwa na mirija mikubwa, ilikuwa ikitumika kwa ajili ya kupitisha damu kutoka katika sehemu iliyokuwa imetokea ajali na hivyo damu kuingia kwenye mitungi ile kupitia katika mirija na mwisho wa siku kuiamisha na kuipeleka damu yote kwenye mapipa.

    Hawakuishia hapo, akapelekwa katika sehemu zilizokuwa na shule za kufundishia watoto mbalimbai. Huko akakutana na watoto wengi ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kufundishwa mambo mengi kuhusu uchawi.

    Hawakuwa watoto wa kawaida, walikuwa wenye kutisha ambao walikuwa wakitolewa hospitalini kila walipokuwa wakifa, hasa mama zao walipokuwa wakijifungua. Hawakuwa watoto halisi, wale waliokuwa wakifa walichukuliwa na Mungu, wao walichokifanya ni kutengeneza mtoto wao kwa kutumia sura za watoto wale ambao walikuwa wakiwalea mpaka kuwa wakubwa na mwisho wa siku, kuwageuza na kuwa majini.

    Baada ya kuzungushwa sehemu kubwa huko kuzimu, wakafika katika sehemu ambayo kulikuwa na duka kubwa ambalo lilitumika kuuzia manukato mbalimbali na mafuta ya kujipaka yakiwepo lotion. Alipoviangalia vitu vilivyokuwa vikuzwa ndani ya duka hilo, alikumbuka kwamba alikwishawahi kuviona katika maduka duniani vikiuzwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Navijua hivi, inakuwaje kuwepo huku tena?” aliuliza Edmund.

    “Hivi ni vitu ambavyo vinatengenezwa humu, haya manukato unayoyaona ni yale ambayo binadamu wanapenda sana kujipulizia kila siku, ni manukato yenye nguvu ambayo yanasababisha watu wengi kupata ajali, kufariki, vingi husababishwa na manukato haya,” alisema kiumbe yule wa ajabu.

    “Kivipi? Inasababishaje?”

    “Ushawahi kuona mtu akiingia ndani ya gari, mwanamke anamwambia kaka unanukia vizuri na mwisho wa siku kufanya ngono?”

    “Nimekwishaona sana.”

    “Ndiyo kazi kubwa ya manukato haya, yana harufu nzuri ambayo yanaifanya mishpa ya mtu kusisimka kwa kiasi kikubwa.”

    “Na kuhusu gari kupata ajali?”

    “Unapokuwa umejipulizia manukato haya, unapokuwa garini, harufu yake husambaa kila sehemu, na hiyo ndiyo husababisha ajali zisizokuwa na sababu, ndiyo maana unaweza kukuta gari limepata ajali na kuua watu katika barabara tambarare, unaweza kujiuliza gari limepata vipi ajali lakini ukweli ni kwamba dereva alichanganywa na harufu ile,” alisema kiumbe yule.

    Ilikuwa ni siku ya kutembezwa huku na kule, kila kitu alichokuwa akionyeshwa alikiweka akilini mwake. Mambo mengi aliyokutana nayo huko yalimchanganya sana. Baada ya ziara yao kukamilika, wakarudi katika jumba lile la mara ya kwanza, akapewa kikombe chenye damu ya binadamu na kutakiwa kunywa.

    “Ninywe damu?” aliuliza Edmund huku akionekana kushtuka.

    “Ndiyo.”

    Hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kunywa damu ile huku akikunja uso wake. Japokuwa alikuwa akijua kwamba damu haikuwa tamu, lakini alipoanza kuinywa tu, ilikuwa na ladha ya tofauti kabisa, ilikuwa tamu kama asali, akajikuta akinywa zaidi na kutaka kuongezewa.

    Damu hiyo ndiyo ikawa agano lake na ulimwengu huo, akawa ameingia katika agano la damu na ulimwengu huo wa shetani ambao alitakiwa kuutumikia kwa kipindi hicho.

    Kila kitu kilipomalizika, Edmund na Yusnath wakarudi duniani. Msichana huyo akawa katika umbo la kawaida kabisa. Walipotoka baharini na kuelekea nchi kavu, Edmund akashangaa kujiona kwamba hakuwa amelowa japokuwa alitoka baharini.

    Kwa kuwa ilikuwa usiku na hakukuwa na mtu aliyekuwa akiwaona, Yusnath akamsogelea Edmund na kumpiga busu zito shavuni, kitendo cha Edmund kufumba macho kwa hisia, alipofungua, akajikuta akiwa chumbani kwake. Akabaki akishangaa tu.



    Filbert alikuwa ndani ya ndege, kila wakati macho yake yalikuwa yakiangalia nje kupitia katika kidirisha kidogo cha ndege ile. Mawazo yake yalianza kurudi nyuma kabisa, toka siku zile ambazo mama yake alikuwa akiumwa lakini hakuwa na uwezo wowote wa kumpeleka hospitalini kutibiwa.

    Mbali na hiyo, alikumkumbuka pia siku zile ambazo alikuwa amehangaika sana kumtafuta Edmund kwa ajili ya kuomba nafasi ya kuonekana katika televisheni kupitia filamu zake.

    Kila kitu kilichokuwa kimetokea katika maisha yake kilimhuzunisha, hakuamini kwamba mara baada ya mihangaiko yote aliyokuwa ameipitia, mwisho wa siku alikuwa mmoja wa waigizaji wakubwa duniani.

    Kila kitu kilichokuwa kimetokea kwake kilionekana kuwa kama ndoto na baada ya muda mfupi angeshtuka kutoka katika usingizi mzito. Kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele ndivyo alivyozidi kumuomba Mungu kwamba aache kila kitu kama kilivyokuwa, isije baadae ikagundulika kwamba alikuwa kwenye ndoto moja ya kusisimua.

    Abiria walikuwa kimya, wengi walipomwangalia na kumtambua, walimfuata na kupiga naye picha. Ndani ya ndege, mara kwa mara watu walikuwa wakimwangalia Filbert, alikuwa kijana makini ambaye hakuonekana kuwa na maringo hata kidogo, kwa kila mtu aliyetaka kupiga naye picha, hakukataa, aliwakaribisha na kupiga nao.

    "I am going back to Tanzania, where many people didn’t care about me!” (Narudi tena Tanzania, sehemu ambayo watu hawakunijali kabisa) alijisemea Filbert.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndege iliendelea kukata mawingu, baada ya kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Filbert akajiandaa kwa ajili ya kuteremka katika kituo cha uwanja ujao nchini Tanzania.

    Ndege ilichukua masaa kadhaa, ikachomoa matairi tayari kwa kutua katika uwanja huo. Alichokifanya Filbert ni kuchungulia nje kupitia dirishani. Moyo wake ukashtuka, aliwaona watu wakiwa wamekusanyika kwa wingi uwanjani hapo huku kwa mbali, wengi wao wakionekana wakiwa na mabango.

    Hakuwa akijua kama watu hao walikuwa wakimsubiri yeye au kulikuwa na mtu mwingine. Hakutaka kuwa na wasiwasi japokuwa kichwa chake kilijaza maswali mengi juu ya uwepo wa watu hao mahali hapo.

    Ndege iliposimama, akaanza kutazama mule ndani kama alikuwa amepanda na kiongozi yeyote wa nchi, kila alipoangalia, hakukuwa na kiongozi yeyote yule, watu weusi, walikuwa wanne tu akiwepo na yeye mwenyewe.

    “Mmmh! Sasa hawa wamekuja kumpokea nani?” alijiuliza lakini akakosa jibu.

    Hakuonekana kujali, alichokifanya ni kuchukua begi lake na kuufuata mlango wa kutokea. Alipoufikia na kusimama katikati ya mlango, akaanza kusikia kelele kutoka kwa watu hao waliokusanyika uwanjani hapo, aliposoma vizuri mabango, aliyaona yakiwa yameandikwa jina lake.

    Moyo wake ukapigwa na mshtuko, hakuamini kama umati mkubwa wa watu uliokuwa mahali hapo ulikuwa kwa ajili yake tu. Akashindwa kuvumilia, pasipo kutarajia, akajikuta akianza kububujikwa na machozi ya furaha, akaanza kupiga hatua kushuka ngazini.

    “Is all this for me? (Hii yote ni kwa ajili yangu?) aliuliza Filbert mara baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kumsogelea.

    “Yeah! It’s all this for you (Ndiyo! Hii ni kwa ajili yako!) alisema waziri Pawasa.

    Filbert hakuamini, machozi ya furaha yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake, alikuwa kijana masikini hasiyekuwa na kitu, leo hii alirudi nyumbani nchini Tanzania huku akiwa na heshima kubwa mpaka kumpelekea kupokelewa na waziri.

    Aliwapungia watu mikono, kelele zikazidi kuongezeka, hata pale alipotaka kupanda kwenye gari maalumu alilokuwa ameandaliwa, watu wakakataa, wakataka atembee kwa miguu ili waweze kumuona vizuri kwani alikuwa mtu pekee aliyeitangaza Tanzania mpaka Marekani.

    “Hakuna tatizo, mimi mtoto wa Manzese, kutembea siyo ishu, kama niliwahi kutembea kutoka Manzese mpaka Kawe, nitashindwa vipi kutembea hapa!” alisema Filbert katika kipaza sauti na safari ya kutembea kwa miguu kuanza.

    “Jamaa yupo simpo sana, daah! Mcheki, yaani mpaka naona wivu. Hapa nina wasiwasi na yule malaya wetu wa kike, Susan, lazima ajisogeze tu,” alisema jamaa mmoja katika umati huo.

    “Umeonaeee...yule demu hapitwi, hapo atatafuta kiki tu,” alisema jamaa mwingine.

    Barabarani ilionekana kuwa kama fujo, magari hayakupita hali iliyopelekea barabara kufungwa kwa muda. Waandishi wa habari hawakutulia, kila wakati walikuwa wakihangaika huku na kule kutaka kupiga picha nzuri na hatimae zitumike katika magazeti yao siku inayofuatia.

    Wale waliokuwa kwenye daladala walipoona zimesimama, nao wakateremka na kuungana na umati huo na kuanza kutembea kwa miguu. Kila mtu alitaka kumgusa Filbert, walizoea kumuona katika filamu mbalimbali nchini Marekani akiigiza na wasanii wakubwa, leo hii kuwa mbele yao ulionekana kama muujiza.

    “Safi sana Filbert, hongera sana kaka,” alisikika msichana mmoja, alikuwa mmoja wa waigizaji wakongwe nchini Tanzania, alimfahamu vilivyo, alikuwa akiitwa Bupe.

    “Asante sana Bupe, nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa filamu zako, nashukuru sana kwa kuwa kupitia nyie, leo hii nipo hapa,” alisema Filbert huku watu wakiendelea kupiga hatua, walikwishaingia Buguruni, ngoma ilikuwa mdogomdogo mpaka Manzese alipokuwa akiishi.

    “Ila kuna ujumbe wako hapa,” alisema Bupe.

    “Ujumbe wangu! Kutoka wapi?”

    “Kutoka kwa Susan.”

    “Susan!”

    “Ndiyo!”

    “Huyu muigizaji?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yaap.”

    “Huyuhuyu demu wa msanii Yusuph The Ruler?”

    “Yaaap! Ila washaachana kitambo!”

    “Mmh! Uko wapi huo ujumbe?”

    Filbert hakuongea kitu, kichwa chake kikaanza kujiuliza kuhusu msichana huyo. Alimfahamu vilivyo, alikuwa muigizaji mkubwa aliyekuwa akiandikwa sana kuhusiana na skendo chafu zilizokuwa zikimkumba.

    Japokuwa hakutaka hata kumsikia lakini ukweli ulikuwa ni kwamba Susan alikuwa msichana wa tofauti sana, umbo lake lilikuwa la kuvutia amblo ilikuwa ngumu sana kwa mwanaume lijari kama alivyokuwa kumkataa.

    Mbali na umbo lake, Susan aliringia uzuri wake, alikuwa msichana wa tofauti mno japokuwa pepo la ngono ndilo lililokuwa likimsumbua maishani mwake. Aliyapenda mapenzi japokuwa hayakuwa yakimpenda.

    Alibadilisha wanaume kama nguo, leo alikuwa akilala na mwanamuziki, kesho mcheza mpira na keshokutwa tajiri kutoka Arusha.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha aliyoyachagua, alipenda sana kuwa katika mahusiano na ndiyo kitu kilichomfanya kulala na wanaume wengi ambao walikuwa masupastaa na matajiri wakubwa.

    Alihangaika sana lakini akili yake ilikuwa kwenye kuyatengeneza maisha yake tu. Hakufikiria kitu kingine zaidi ya pesa, alifungua biashara na kuyaendesha maisha yake kupitia migongo ya wanaume mbalimbali.

    Baada ya kuhangaika sana, leo hii alikuwa akitaka kulala na muigizaji wa kimataifa, Filbert. Alimpenda mwanaume huyo toka moyoni, alijua fika kwamba alikuwa na mwanamke kutoka nchini Marekani lakini hilo halikuwa kipingamizi hata mara moja.

    Alichokifanya ni kuandika ujumbe mfupi na kumpa Bupe huku akimtaka kumfikishia Filbert ujumbe huo, kweli akafanya hivyo, alichokuwa akisikilizia ni kupigiwa simu tu, kwani kwenye ujumbe ule aliokuwa ameuandika, kulikuwa na namba ya simu yake pia.

    ‘Siku nikikutana na wewe, naamini ndiyo nitakuwa nimekamilisha ndoto niliyokuwa nayo kila siku. Filbert, naomba ukamilishe ndoto yangu. 0780786543’ ilisomeka sehemu ya ujumbe huo.

    Leo, kijana aliyekuwa masikini ambaye kila siku alikuwa akimtamani Susan kila alipokuwa akimwangalia kweny filamu mbalimbali, kijana ambaye hakuwa na mbele wala nyuma, msichana ambaye alimsifia na kumtamani kutokana na uzuri wake, alikuwa amejileta mwenyewe kwa kutaka kuonana naye.

    Bado Filbert alihisi kama ndoto lakini kila kitu kilichokuwa kikitokea, kilikuwa katika maisha halisi na haikuwa ndoto kama alivyokuwa akihisi.

    “Daaah! Nilikuwa namtamani sana huyu mtu, leo kajileta, hakuna kuremba hapa, kwani Stacie atajua? Kwanza yupo Marekani, haina noma, ngoja niruke naye kiaina,” alijisemea Filbert

    Kila kitu kwake kilionekana kuwa furaha tele, Filbert hakujua kamba kupitia mafanikio yake alikuwa amemtengeneza adui mkubwa ambaye kila siku alitaka kumuona akifa ili jina lake liendelee kuwa juu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

    Edmund alikuwa akihangaika, mara baada ya kuambiwa kwamba damu ya Filbert ilikuwa na gharama kubwa sana na ingesababisha kuuawa kwa watu wengi, hakutaka kujali, kitu pekee alichokuwa akikitaka ni kumuona mtu huyo akifa na hata kama kungehitajika damu za watu wengine, yeye alikuwa tayari kuzichangia kwa kuwatoa watu kafara.

    Kitendo cha kumuona Filbert akiwa amepokewa na watu wengi, heshima kubwa aliyokuwa amepewa, ilionekana kuwa kama msumari wa moto moyoni mwake, hakutaka kuyaona mafanikio mengi zaidi kwa Filbert na ndiyo maana leo hii alitaka kumuua kwa kutumia uchawi huku akiamini zile nguvu za giza zingeweza kumsaidia kupitia kwa demu wake aliyekuwa akimpenda, Yusnath huku akiwa hajui kama msichana huyo alikuwa Jini Maimuna.

    “Nitamuua tu, tena kabla hajarudi nchini Marekani,” alisema Edmund, moyo wake uliwaka kwa hasira.



    Bado kichwa chake kilimuuma kutokana mafanikio aliyokuwa akizidi kuyapata Filbert, moyo wake uliwaka moto kwa wivu mkali kiasi kwamba kuna wakati alijiona kama anachelewa kufanya mauaji kwa muigizaji huyo.

    Kila siku alikuwa mtu wa kupanga mipango ni kwa namna gani angeweza kufanikisha mauaji kwa Filbert hali iliyompelekea wakati mwingine kushinda usiku kucha akikiacha kichwa chake kifikirie zaidi kile kilichotakiwa kufanyika.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakumuamini mtu, hakutaka kumtumia majambazi kumuua kwa kuwa Filbert hakuwa nchini Tanzania, silaha pekee ambayo aliiaminia ilikuwa ni uchawi pekee. Alikumbuka vilivyo kwamba alipokwenda katika ulimwengu wa kuzimu aliambiwa kwamba aongee na mpenzi wake, Yusnath na angemwambia kile alichotakiwa kukifanya.

    Ni kweli moyo wake ulimuamini msichana huyo lakini kuna wakati aliona ni vema kufanya vitu kivyakevyake kwani wanawake hawakuwa watu wa kuwaamini kwa sana.

    “Hivi kweli nimshirikishe Yusnath! Lakini yeye ni nani? Mbona siku ile naye alibadilika sana na kuwa kiumbe wa kutisha!” alisema Edmund huku akiendelea kujiuliza pasipo kupata jibu lolote lile.

    Baada ya kuhangaika kwa kipindi kirefu, hapo ndipo alipoamua kwamba ilikuwa ni lazima kumshirikisha zaidi Yusnath kwani hata kipidi kile alichokwenda kuzimu, alikuwa na msichana huyo.

    “Au na yeye ni jini? Hapana, mbona msichana mrembo tu,” alijiuliza Edmund na kujijibu mwenyewe.

    Alichokifanya ni kumuita Yusnath na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea, japokuwa alijua fika kwamba msichana huyo alikuwa akifahamu kila kitu lakini akaamua kumuhadithia kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

    “Nakumbuka niliambiwa nikushirikishe, sawa, nimekwishakushirikisha, niambie nitaweza kumuua vipi,” alisema Edmund.

    “Kwa sasa kumuua Filbert ni kazi kubwa mno, na kama ukimuua, kuna damu nyingi utatakiwa kulipia,” alisema Yusnath maneno yaliyomfanya Edmund kushtuka.

    “Kivipi?”

    “Filbert ni staa.”

    “Sasa vinahusiana na nini hapo?”

    “Kule alipo nchini Marekani, kuna mtu amewekwa mahususi kwa ajili ya kuhakikisha anajiunga na dini hii, baada ya hapo, tunataka kupata damu nyingi kupitia yeye kwa kuwa ni staa,” alisema Yusnath.

    “Lakini ninataka kumuua.”

    “Haujakatazwa ila utakapomuua jua kwamba zile damu ambazo tulitakiwa kuzipata kupitia yeye hatutoweza kuzipata, kwa hiyo kama utataka kumuua, haina budi kutuletea damu hizo,” alisema Yusnath.

    “Mimi nipo tayari, yaani ninachotaka ni kumuona akifa tu, hizo damu nitazilipa,” alisema Edmund kwa hasira, alionekana dhahiri kutokumpenda Filbert.

    “Basi sawa, hakuna tatizo, ila itakupasa kusubiri.”

    “Cha kusubiria nini tena?”

    “Mpaka atakapokuja Tanzania, kulekule itakuwa ngumu kidogo.”

    “Kivipi tena? Yaani mpaka uchawi wa kule chini hauvuki bahari?”

    “Hapana, ule unavuka, unaweza kwenda sehemu yoyote ile, ila unatakiwa kusubiri, tunapenda kusababisha kifo ambacho hakitokuwa kikihusishwa na hii dini yetu,” alisema Yusnath.

    “Sawa. Ngoja nisubiri.”

    Japokuwa alikuwa na presha sana lakini hakuwa na budi kusubiri, bado moyo wake uliendelea kuwa kwenye maumivu makali mno kiasi kwamba kila alipokuwa akikaa, alikuwa akikunja ngumi na kuupiga mkono wake mmoja.

    Hasira zake hazikuelezeka, jina la Filbert lilimchefua kupita kawaida. Kila alipokuwa akilikumbuka, alijikuta akishikwa na hasira zaidi. Alipokuwa akipita barabarani kwa gari lake na kuona magazeti yakiwa yamemwandika, alisikia maumivu zaidi moyoni mwake.

    “Simpendi huyu mtu, nitampoteza tu,” alijisemea Edmund, alikuwa akiuma meno yake kwa hasira, japokuwa hakuwa amefanywa kitu chochote kile na Filbert, lakini moyo wake haukumpenda hata kidogo kwa kisingizo cha kusema kwamba alikuwa ameiba nyota yake.

    *****

    Taarifa zikaanza kutangazwa katika vyombo vya habari kwamba yule muigizaji mashuhuri duniani, Filbert alikuwa akitarajiwa kuingia nchini Tanzania wiki ijayo. Kwa wafanyabiashara, wakachapisha fulana harakaharaka kwa ajili ya kuziuza siku hiyo. Katika kila fulana iliyokuwa ikichapishwa, ilikuwa na picha zake mbalimbali zilizozifanya kupendeza mno.

    Kwa wale waliokuwa wanahusika sana na uchoraji wa mabango, wakayaweka vizuri mabango yao kwa ajili ya kuyaonyesha katika siku ambayo Filbert angeingia nchini Tanzania.

    Kadiri siku zilivyokuwa zikienda mbele na ndivyo ambavyo watu walizidi kuwa na presha ya kutaka kumuona Filbert ambaye aliitangaza vilivyo nchi ya Tanzania na kuifanya kujulikana dunia nzima.

    “Mimi nitataka anioe, nampenda sana Filbert,” alisema muigizaji mmoja mwenye jina kubwa zaidi ya Wema Sepetu, aliitwa Susan Chichi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/*

    “Hahaha! Wewe tena shosti ulivyokuwa mzuri, mbona ataingia kingi tu,” alisema muigizaji mwingine.

    “Kwanza akija tu, nitataka nimpe mabusu mfululizo, halafu nitamuomba kula naye chakula cha usiku, akikubali, nitamuomba nilale naye, akikubali tu, amekwisha, nitatumia ufundi wote kama mtoto halisi wa Kitanga,” alisema Susan.

    “Mmmh! NA hiyo shepu yako, mbona atamsahau demu wake. Hivi kwanza atakuja na yule demu wake wa Kizungu?”

    “Nimesikia haji naye, kama ni kweli, hiyo ndiyo nafasi yangu sasa,” alisema Susan.

    Susan Chichi alikuwa miongoni mwa waigizaji waliokuwa na majina makubwa nchini Tanzania. Uwezo wake wa kuigiza ndiyo uliompa jina kiasi kwamba akaonekana kuwa lulu kwa kila mtu aliyekuwa akimwangalia.

    Susan hakuwa mrembo wa sura tu bali hata umbo lake lilikuwa likimvutia kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia. Alikuwa na hipsi kubwa, alikwenda hewani, kifua kilichosimama huku kila alipotembea, mwendo wake ulikuwa wa madaha.

    Japokuwa alikuwa muigizaji aliyetawaliwa na skendo za kutembea na wanaume wengi nchini Tanzania, lakini kitu kilichokuwa kikishangaza, Susan hakushuka, bado aliendelea kuwa mrembo kila siku.

    Susan hakuwa masikini, alikuwa mmoja wa waigizaji waliokuwa na fedha. Fedha zake hazikutokana na uigizaji tu bali hata mabwana waliokuwa wakitembea naye walimpa fedha za kutosha zilizomfanya kulitikisa Jiji la Dar es Salaam.

    Wafanyabiashara waliokuwa wakitoka Mwanza na Arusha, walipokuwa wakifika Jijini Dar es Salaam tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumuulizia Susan ambaye kumpata wala haikuwa gharama, fedha zako tu, zilikuwa ndoano kubwa ya kumpata mrembo huyu.

    Alitembea na mastaa wengi, kila alipomuona mwanamuziki anachipukia ilikuwa ni lazima kutembea naye, hakuwaacha hata wanasiasa, wote hao, alikuwa akitembea nao na kupata kiasi kikubwa cha fedha.

    Maisha ya Susan yalitawaliwa na fedha, alikuwa mwingi wa skendo lakini alikuwa na uwezi mkubwa wa akili. Alijua kujipanga na kuyaendesha maisha yake. Japokuwa alikuwa akitumia kiasi kikubwa cha fedha lakini alifanikiwa kujenga nyumba tatu za kifahari na kufungua biashara zake nyingi zikiwepo saluni za kike.

    “Nitampata tu, kama niliweza kumpata yule mwanamuziki wa Marekani, sembuse yeye Mtanzania mwenzangu! Nitampata tu, ngoja atue Bongo,” alisema Susan huku akionekana kuwa na uhakika na kile alichokuwa akikizungumza.

    “Nakuaminia shosti wangu, wewe tena, mbona atakoma na roho yake.”

    Siku ziliendelea kukatika huku maandalizi yakiandaliwa kwa kasikubwa. Mpaka inafika siku moja kabla ya tukio lenyewe, kila kitu kilipangiliwa kama kilivyotakiwa kuwa.

    Siku ambayo Filbert alikuwa akifika nchini Tanzania, zaidi ya watu elfu thelathini walikusanyika katika endo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kumpokea shujaa wao.

    Kila mtu aliyekuwepo mahali hapo alikuwa amevalia fulana zilizokuwa na picha zake huku wengine wakiwa wameshika mabango yaliyokuwa na maneno ya kumpongeza kwa kuliletea sifa Taifa la Tanzania.

    Watu hao hawakuwa peke yao, waliongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, bwana Andrea Pawasa alikuwepo uwanjani hapo kwa ajili ya kumpokea Filbert ambaye alitarajiwa kuingia muda mchache ujao.

    Nyimbo za shangwe hazikuisha, waandishi wa habari hawakutulia, kila wakati walikuwa wakirandaranda huku na kule kwa ajili ya kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

    Ilipofika saa 6:16 mchana, ndege ya Shirika la American Airlines ikaanza kuonekana angani, watu wakajiandaa, wale waliokuwa pembeni wakajisogeza kwani walijua fika kwamba ni lazima Filbert alikuwa ndani ya ndege hiyo.

    “Pipa lishaanza kutua, hebu ngoja nisogeesogee,” alisema jamaa mmoja, ndege ilikuwa ikitembea ardhini, kila mmoja akajua kwamba Filbert alikuwa ameingia nchini Tanzania na alikuwa ndani ya ndege hiyo.



    Kila kilichokuwa kikiendelea kilimkasirisha, umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa ndege ulionekana kuwa mwiba mkali moyoni mwake, hakumpenda Filbert na kubwa zaidi ambalo lilimtawala moyoni mwake kwa kipindi hicho ni kwamba alikuwa akitaka kumuua ili moyo wake ufurahi.

    Alichokifanya ni kumuita Yusnath na kuanza kuzungumza naye, japokuwa alikuwa ameongea naye mara nyingi kwamba alitaka kumuua muigizaji huyo lakini hakutaka kukaa kimya, bado aliendelea kumwambia kwamba huo ndiyo ulikuwa muda muafaka wa kufanya hivyo.

    “Kumwaga damu ya mtu si kazi ndogo, kuna sehemu tunatakiwa kwenda,” alisema Yusnath.

    “Kwenda wapi? Kurudi kulekule?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana, kuna sehemu nyingine kabisa, huko, utafanya kila kitu unachotaka kufanya,” alisema Yusnath.

    Hakutaka waendelee kubaki mahali hapo, kwa sababu alionekana kama mtu mwenye haraka nyingi, akashindikiza waondoke muda huohuo kuelekea huko alipotaka waelekee.

    Safari ikaanza mara moja, walikuwa ndani ya gari na safari ya kuelea Sinza ikaanza mara moja. Kichwani, bado Edmund alikuwa na mawazo tele, utawala wa Filbert ulikisumbua kichwa chake kiasi kwamba hakuwa na amani hata kidogo.

    Walipofika Sinza Makaburini, kitu kilichoonekana kumshangaza zaidi, hakukuwa na makaburi eneo hilo, basli sehemu iliyokuwa na makaburi kulikuwa na nyumba moja kubwa iliyoonekana kuwa ya kifahari sana.

    “MmmH!” alijikuta akiguna.

    “Nini tena?”

    “Hapa kulikuwa na makaburi, si ndiyo?”

    “Mmmh! Sidhani.”

    “Hapana Yusnath, hapa ni Sinza Makaburini, na njia ile kule ni ile inayokwenda kuungana na Barabara ya Sam Nujoma ile inayokwenda Mlimani City, sasa mbona hakuna makaburi?” alisema Edmund na kumalizia na swali.

    “Kwani hapa kulikuwa na makaburi?”

    “Ndiyo!”

    “Sidhani, labda umechanganya sehemu.”

    “Jamani! Mimi nisiijue Sinza Makaburini mpaka kuichanganya!”

    “Inawezekana.”

    “Sidhani!”

    Wakateremka kutoka garini na kuanza kuelekea katika nyumba ile. Sao zao za mikononi zilionyesha kwamba tayari ilikwishafika saa mbili usiku. Edmund alitembea kwa tahadhali kubwa kani kila alipokuwa akiiangalia nyumba ile, hakuonekana kuamini kama kweli pale hakukuwa na makaburi.

    Geti likafunguliwa na kuingia ndani. Nyumba ile ilonekana kuwa na mvuto wa hali ya juu, sehemu nzima ilikuwa na marumaru zenye kung’aa, kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea huku kukiwa na magari ya kifahari zaidi ya matano tena yote yakiwa yale ya bei kubwa.

    “Mmmh! Lamboghin hizo, milioni mia nane dukani, aiseeee, hii nyumba anaishi nani? Mpaka Ferrari zipo!” alisema Edmund huku akionekana kushangaa.

    Japokuwa alikuwa na fedha lakini kila kitu alichokuwa akikiona mahali hapo alikuwa akikishangaa, nyumba ilionyesha wazi kwamba ilikuwa ikimilikiwa na mtu mwenye fedha nyingi nchini Tanzania, aliitamani, kila alipokuwa akiiangalia, alitamani kuona ikiwa yake.

    Walipoufikia mlango, wakaingia ndani. Japokuwa nje kulikuwa na vitu vingi lakini kilichoshangaza, ndani hakukuwa na kitu chochote kile. Sebule ilikuwa wazi kana kwamba watu waliokuwa wakiishi humo walikuwa wamehama.

    Huku macho yake yakiwa na mshangao, Yusnath akamwambia waelekee katika chumba kingine, walipofika huko, wakaingia katika chumba kimoja miongoni mwa vyumba saba vilivyokuwa ndani ya nyumba hiyo.

    Kitu kilichomuacha mdomo wazi, chumba kile hakikuwa cha kawaida,hakikuwa kidogo kama inavyotakiwa kuwa chumba cha kawaida katika nyumba, kilikuwa ni chumba kikubwa mithiri ya uwanja wa mpira wa miguu.

    Watu zaidi ya thelathini walikuwa wamepiga magoti huku wakiwa wamevalia nguo kubwa kama shuka huku wakiwa wamejifunika mpaka vichwani mwao.

    Mbele ya watu wale kulikuwa na kioo kikubwa, mbele ya kioo hicho kulikuwa na meza ndogo ambayo juu yake kulikuwa na kisu na pembeni kuwa na birika moja kubwa.

    “Chukua nguo moja pale,” alisema Yusnath, alimwambia Edmund ambaye akaifuata nguo moja nyeusi kama walizokuwa wamezivaa watu wale na yeye kuvaa huku akiambiwa apige magoti na kuangalia mbele, akafanya hivyo.

    “Hapa ndipo utakapomuua Filbert,” alisema Yusnath, Edmund akashusha pumzi ndefu, moyo wake ukajaa furaha.

    ****

    Baada ya dakika kadhaa, mwanaume mmoja akatokea mahali hapo, naye alikuwa kama wale wengine lakini vazi lake kubwa alilokuwa amelivaa halikuwa jeusi, lilikuwa jekundu.

    Mara baada ya kuwaona watu hao wakiwa mahali hapo huku wakiwa wanatoa sauti kama za kuabudu, akawasalimia katika lugha ambayo Edmund hakuwa ameielewa na kisha kusimama mbele ya kioo kile.

    Alichokifanya mtu yule ni kumuita Edmund mbele kabisa na kumtaka azungumze kile alichokuwa akikitaka mahali pale huku kila mmoja akimsikiliza. Alipokwenda mbele na kusimama, alipowaangalia watu wale waliokuwa wamepiga magoti, wengi wao hawakuwa wageni machoni mwake.

    Aliwafahamu kwani yale mavazi yaliyokuwa yameziba mpaka nyuso zao yalikuwa yametolewa na kubaki wazi. Miongoni mwa wale watu walikuwepo wanasiasa, waigizaji na watu waliokuwa na fedha nyingi nchini Tanzania.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hapo ndipo akagundua kwamba dini ile ilikuwa ni mkusanyiko wa watu wengi maarufu na wenye fedha. Hapo, akajisikia amani, akatokea kuwaamini kwa kuona kwamba hata na yeye angeweza kufanikiwa na kuwa kama wale watu waliokuwa mahali pale.

    “Upo tayari?” aliuliza mwanaume yule aliyeonekana kuwa kiongozi.

    “Kufanya nini?”

    “Kwani wewe umekuja kufanya nini?”

    “Kumuua Filbert.”

    “Ndiyo! Upo tayari kufanya hivyo?”

    “Hata sasa hivi, nipo tayari,” alisema Edmund.

    Alichokifanya mwanaume yule ni kumpa kisu na kumwambia aangalie katika kioo kile, ghafla, taswira ya Filbert ikaanza kuonekana, alikuwa bafuni akioga huku sebuleni kukiwa na msichana aliyekuwa akivuma sana kwa wakati huo hasa katika uigizaji, Susan.

    Alichoambiwa ni kumchoma kisu Filbert katika kioo kile, hilo halikuwa tatizo, huku akiwa amekishika kisu kile, akamchoma Filbert katika kioo kile, ghafla, Filbert akaonekana akianguka bafuni, akalishika tumbo lake huku akiwa kwenye maumivu makali, mapovu yakaanza kumtoka mdomoni, akajitahidi kujikongoja mpaka mlangoni, akashindwa kuendelea mbele zaidi, akajikuta akitulia mlangoni, akakata roho.

    Damu zikaanza kumiminika na kuingia katika kibuyu kile. Sauti za vicheko vya furaha vikaanza kusikika kutoka kwa watu wale, kila mmoja akaonekana kufurahishwa na kile kilichokuwa kimefanywa kwa mkono wa Edmund.

    “Kazi nzuri, unahitaji tukufanyie nini?” aliuliza mwanaume yule.

    “Niwe na fedha nyingi.”

    “Umepata, kingine?”

    “Niwe na umaarufu mkubwa, kama aliokuwa nao Edmund, niigine filamu mpaka nje ya nchi, hasa Hollywood,” alisema Edmund.

    “Umepata, ila tunataka kukupa sharti moja.”

    “Hakuna tatizo.”

    “Tutahitaji utuletee damu za watu watano kila wiki, zoezi hili litakwenda kwa miezi sita, baada ya hapo, utakuwa ukimtoa mmoja kila mwaka,” alisema mwanaume yule.

    “Hakuna tatizo, ni watu gani nitatakiwa kuwatoa kafara?”

    “Tutakwambia.”

    “Sawa.”

    Huo ndiyo ulikuwa uamuzi mgumu ambao aliwahi kuuchukua katika maisha yake. Japokuwa kama moyo wa binadamu ulivyo kuna kipindi alijisikia vibaya mno lakini hakuwa na jinsi, kadiri alivyokuwa akifikiria kwamba kile kilichokuwa kimetokea kingempa mafanikio zaidi, aliridhika moyoni mwake.

    Siku hiyo, akapewa pete maalumu ambayo haikutakiwa kutoka kidoleni mwake, ilikuwa pete pekee ambayo ilitakiwa kukaa kidoleni kwa muda wa miezi sita na kama angetaka kuivua basi ni pale ambapo angekamilisha kafara ambazo alitakiwa kuzifanya.

    “Watu watano kwa wiki kwa muda wa miezi sita,” alisema Edmund.

    “Ndiyo, ila si kazi kubwa.”

    “Najua. Kwa hiyo kama wiki mwezi mmoja una wiki nne, ina maana kwa miezi sita ni wiki ishirini na sita, sasa kwa watu watano kila wiki ina maana ni watu mia na thelathini?”

    “Yeah! Upo sahihi.”

    “Mmmh!” nitaweza kweli?”

    “Utaweza tu, hautotumia bunduki, silaha yako kubwa itakuwa katika kioo hiki, utafanikiwa tu, nipo kwa ajili yako,” alisema Yusnath.

    “Basi nitafanya, ninachotakiwa ni kuona nikifanikiwa zaidi,” alisema Edmund na kuondoka katika jumba hilo la kifahari.



    Kila alipokuwa akimfikiria Susan, mwili wake uliwaka moto, japokuwa alikuwa msichana malaya lakini hakutaka kumuona akipita mbele yake pasipo kufanya kitu chochote kile.

    Kama kutembea na wanawake wazuri alitembea nao sana kuanzia nchini Marekani, hivyo kwa Susan hakuona kama angeweza kumsumbua hata mara moja.

    Kwa kipindi kirefu mno alikuwa akimtamani msichana huyo, figa yake matata ilimtoa udenda kila alipokuwa akimwangalia. Alikuwa msichana mrembo ambaye alichukuliwa na masupastaa tu au watu wenye fedha, kwa kijana kama alivyokuwa yeye, masikini wa kutupwa, asingeweza kumpata hata siku moja.

    Mara baada ya kupata umaarufu na kuona msichana huyo akianza kujivutavuta kwake, Filbert hakutaka kujivunga hata mara moja, kitu alichokifanya ni kukubaliana kuonana naye na hivyo kumpigia simu.

    Hakutaka kuonana naye sehemu yoyote ile zaidi ya hotelini, alitaka kuonana naye huko, alale naye na kisha kuachana naye kwa kudhani kwamba asingeweza kumfuatilia tena. Alipompigia simu msichana huyo na kumwambia kwamba amfuate hotelini, Susan alikuwa na furaha tele.

    “Karibu mrembo,” alisema Filbert mara baada ya kumuona Susan mara baada ya kufika hotelini hapo.

    “Asante,” alisema Susan na kuingia ndani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Susan alikuwa Susan haswa, kila wakati Filbert alipokuwa akimwangalia msichana huyo, uchu wa kufanya naye mapenzi ulikuwa ukimkamata, sketi yake fupi iliyobana aliyokuwa ameivaa na kuyaruhusu mapaja yake yawe wazi yalimpagawisha mno, akabaki akiyaangalia kwa matamanio makubwa.

    “Umependeza,” alisema Filbert huku akiyaangalia mapaja ya Susan.

    “Nashukuru.”

    Walikaa na kuanza kuzungumza mengi, kila Filbert alipokuwa akiongea maneno kumi, alikuwa akimwaga sifa kwa msichana huyo kwamba alikuwa mzuri kupindukia na alikuwa miongoni mwa wasichana ambao kila siku alikuwa akiomba Mungu akutane nao.

    “Ninakupenda sana, naomba leo uwe usiku wa bahati kwangu wa kulala nawe,” alisema Filbert.

    “Hakuna tatizo. Wewe tu,” alisema Susan.

    Filbert akasimama na kuanza kumfuata Susan kitandani pale, alipomfikia, akambusu shavuni na kisha kwenda mdomoni ambapo wakaanza kubadilishana mate. Alipoona ameridhika, akavua nguo zake na kuchukua taulo.

    “Acha nikaoge kwanza, narudi kwa ajili ya mechi,” alisema Filbert na kisha kuelekea bafuni.

    Susan akabaki chumbani hapo, kwanza kitu cha kwanza alichokifanya ni kumtumia Bupe ujumbe kwamba alikuwa amefanikiwa kukutana na Filbert na wakati huo alikwenda bafuni kuoga na kisha kile kitu alichokitaka kuanza rasmi kitandani.

    Hakutaka kukaa kipweke, alichokifanya ni kuvua sketi yake na kubaki na nguo ya ndani tu na kujilaza kitandani. Aliendelea kukaa kitandani pale, muda ulizidi kwenda mbele lakini Filbert hakutokea chumbani hapo.

    “MmmH! Kuoga gani dakika arobaini,” alisema Susan, alichokifanya ni kuinuka na kuanza kuelekea bafuni.

    Alichokiona, hakuamini, Filbert alikuwa mlangoni amelala, mapovu yalikuwa yakimtoka na mwili ulikuwa umekakamaa, alipoyasikiliza mapigo yake ya moyo, hayakuwa yakidunda hali iliyomaanisha kwamba mwanaume huyo alikuwa amekufa.

    “Mungu wangu!” alisema Susan kwa mshtuko.

    ***

    Susan akaanza kupiga kelele, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, mwanaume aliyepanga kufanya naye mapenzi, mwanaume aliyekuwa maarufu duniani alikuwa sakafuni, mapovu yalikuwa yamemtoka na mwili kumkakamaa.

    Kelele zake zikasikiwa na wahudumu wa hoteli hiyo ambao moja kwa moja wakaja chumbani hapo na kumkuta Susan akilia kama mtoto huku akisema kwamba hakujua kile kilichokuwa kimetokea. Mwili wa Filbert ulikuwa chini, kila aliyekuwa akiuangalia, alionekana kushtuka.

    Walichokifanya wahudumu wale ni kumpigia simu meneja wao na polisi ambao baada ya muda mfupi wakafika mahali hapo. Kitu cha kwanza kabisa kufanyika ni kumuweka Susan chini ya ulinzi kabla ya mambo mengine kuendelea.

    “Jamani sijafanya kitu chochote kile, nimemkuta akiwa ameanguka,” alisema Susan huku akilia kama mtoto.

    Polisi hawakujali, walichokifanya ni kumfunga pingu, hata kama hakuwa amemfanya kitu chochote kile, yeye ndiye alitakiwa kuwa shahidi namba moja juu ya kifo cha Filbert.

    Mwili wa ule ukachukuliwa na kupelekwa hospitalini. Taarifa zikaanza kusambazwa kwamba Filbert, mwakilishi mzuri wa Tanzania dunia kupitia filamu alikuwa amekufa katika chumba cha hoteli huku Susan akiwa ndani ya chumba hicho.

    Kila aliyezipata taarifa zile alipigwa na mshtuko, hakukuwa na mtu aliyeamini, usiku huohuo baadhi ya watu wakaenda katika Hospitali ya St. Peter Medical Center kwa ajili ya kupata uhakika juu ya kile walichokuwa wamekisikia.

    Ukweli haukubadilika, kile walichokuwa wamekisikia ndicho walichokutana nacho kule, Filbert, muigizaji aliyekuwa akipendwa sana leo hii alikuwa marehemu kitu kilichoonekana kumchanganya kila mmoja.

    “Amekufa saa ngapi?” aliuliza Monnie, muigizaji wa kike, mbele yake alikuwa amesimama daktari, alikuwa akitaka uhakika.

    “Kwani nani amesema kwamba amekufa?” aliuliza daktari yule.

    “Jamani, mbona mnataka kutuficha tena, kwani mkituambia ukweli mtakufa?” aliuliza Monnie, alionekana kukasirika.

    “Subiri, mtaambiwa kila kitu, mimi si msemaji,” alisema daktari yule na kuondoka.

    Ilikuwa ni usiku lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo watu wakazidi kuongezeka mahali hapo. Mpaka inafika saa tano usiku, zaidi ya watu sabini walikuwa katika eneo la hospitali hiyo, kila mmoja alikuwa akitaka kuufahamu ukweli.

    Waandishi wa habari hawakukosa, kama kawaida yao walikuwa wamejikusanya sehemu hiyo huku nao wakitaka kuufahamu ukweli. Hawakutaka kuacha kufanya kazi zao, walikuwa wakipiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

    “Kumbe ameuawa!” alisikika jamaa mmoja.

    “Nani alimuua?”

    “Susan!”

    “Mmmh! Una uhakika?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo! Nimesikia kauawa, yaani ni balaa, yule demu kashakuwa tishio.”

    “Ngoja tuendelee kusikilizia, bado hali inachanganya. Sisi tunasema amekufa, madaktari wanasema kwamba hajafa, subiri tuwasikilizie,” alisema jamaa mwingine.

    Kila mmoja alikuwa kimya, mawasiliano kwa njia ya simu bado yalikuwa yakiendelea kufanyika kama kawaida. Taarifa kutoka kwa madaktari ndiyo ilikuwa ikisubiriwa mahali hapo, hakukuwa na mtu aliyetaka kuondoka bila kujua kama Filbert alikuwa amekufa au la.

    Ilipofika saa sita usiku, madaktari wakamuita Mwenyekiti wa Bongo Muvi, Mrisho Abdallah na kumwambia ukweli kwamba Filbert alikuwa amefariki na hivyo alitakiwa kuwaambia waigizaji wengine.

    Ilikuwa ni taarifa mbaya iliyopenya masikioni mwa kila mtu, hawakuamini kama kile kilichokuwa kimeongelewa kilikuwa kweli au la! Filbert, muigizaji kutoka nchini Marekani alikuwa amekufa ndani ya chumba cha hoteli katika mlango wa chooni.

    Hospitalini hapo kukageuka na kuwa sehemu ya msiba mzito, watu wakaanza kulia kwa sauti kiasi kwamba ikaonekana kuwa kama fujo mahali hapo. Mpaka inafika saa nane usiku, sehemu kubwa nchini Tanzania taarifa ilikuwa imesambazwa ikisema kwamba Filbert alikuwa amefariki huku Susan akihusishwa na kifo cha muigizaji huyo.

    Katika mitandao ya kijamii, kila mtu alikuwa akimshtumu Susan kwamba ndiye alikuwa muuaji wa Filbert na hivyo alitakiwa kukutana na hukumu nzito ya kufungwa jela maisha au kunyongwa.

    Chuki kubwa za Watanzania zikawa juu ya Susan, akapoteza mvuto kwa asilimia kubwa, hakupendwa na mtu yeyote kutokana na kile kilichokuwa kimetokea. Kila mmoja alikuwa akimlalamikia, hakukuwa na mtu aliyejua kwamba nyuma ya kifo cha Filbert kulikuwa na mkono wa Edmund ambaye siku zote alitamani kuona mtu huyo akifa na yeye kuchukua heshima yake kama aliyokuwa nayo kipindi cha nyuma...hiyo ilikuwa siri kubwa.

    ****

    “Sijaua, sijamuua Filbert, sijaua afande...” alisema Susan huku akilia kama mtoto mdogo.

    “Utasema tu, unajidai kuigiza kumbe ni muuaji mkubwa, kifo kinakuhusu sana,” alisema polisi mmoja.

    “Afande, sijamuua Filbert, nilikuta akiwa ameanguka katika mlango wa choo, haki ya Mungu sijauaaaaaa....”

    “Wewe unafikiri ukiapia ndo tutakuacha, subiri, yaani kifo kinakusubiri,” alisema polisi yule.

    “Kweli afande, sijaua mimi!”

    “Wewe subiri tu, utajitetea mahakamani muuaji mkubwa wewe, unatufanya sisi wajinga!”

    Susan alikuwa katika chumba kimoja cha polisi, alikuwa ameshikiliwa na kuwekwa chini ya ulinzi, japokuwa alikuwa akijitetea sana kwamba hakuwa amemuua Filbert lakini hakukuwa na mtu aliyemuelewa hata kidogo.

    Kila mmoja alimuona kwamba ni muuaji ambaye alistahili kuhukumiwa kifo kwa kile kilichokuwa kimetokea. Alilia mno lakini hakukuwa na mtu aliyeonekana kumjali, kila mmoja alimuona kwamba ni muuaji aliyestahili kifo.

    Ndugu zake wakafika katika kituo hicho cha polisi usiku huohuo lakini hakukuwa na aliyeruhusiwa kumuona, alikuwa chini ya ulinzi na hakukuwa na mtu aliyetakiwa hata kumuona.

    Usiku huo, Susan alishinda huku akilia tu, hakunyamaza, kuna wakati alikuwa akijuta sababu iliyompelekea kumfuata Filbert hotelini, kila kitu kilichokuwa kimetokea, kilimfanya kujutia uamuzi wake wa kuwa hotelini.

    Hakukuwa na kitu cha kupoteza, ilipofika asubuhi, jalada la kesi likafunguliwa hasa baada ya kusikilizwa na maelezo yake kuandikwa, baada ya hapo akapewa taarifa kwamba ilikuwa ni lazima kufikishwa mahakamani kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    “Afande, sijaua, sijawahi kuua, mimi mwenyewe nilimkuta amekufa,” alisema Susan.

    “Utayazungumza hayo mahakamani, sisi tunachokifanya ni kukupeleka huko tu, ukishindwa kueleza ukweli, kifo au kifungo cha maisha kitakuhusu,” alisema polisi mmoja, kila polisi aliyekuwa akiongea naye, alikuwa akimtisha tu.

    “Sijaua, Mungu nisaidie, hakuna anayeniamini! Mimi sijamuua Filbert,” alisema Susan kwa sauti kubwa huku machozi yakimbubujika kwa wingi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog