Simulizi : Malaika Wa Kifo
Sehemu Ya Pili (2)
Dalili zikaanza kuonekana, mapenzi aliyokuwa akiyaonesha Edmund kipindi cha nyuma yakaanza kupotea. Hilo lilikuwa moja ya jambo lililomtesa sana Sheila, kila alipokuwa akimtafuta mpenzi wake huyo, hakuwa akimpata jambo lililomhakikishia kwamba kila kitu kilikuwa kikienda mwishoni.
Kwa mapenzi aliyokuwa nayo kwa Edmund, halikuwa jambo jepesi kukubaliana na ukweli uliokuwepo kwamba Edmund aliota mapembe baada ya kupata umaarufu, akaanza kutafuta mpenzi aliyeonekana kuwa bora zaidi yake
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/.
Moyo wake ukawa kwenye maumivu makali, hakuamini kuona kwamba kwamba mwisho wa kila kitu ulikwenda kuwa namna ile. Akawa mtu wa kulia tu huku simu yake ikiwa pembeni yake. Japokuwa hakuwa ameonana na Edmund kwa kipindi kirefu lakini tayari alijua kwamba hakuwa na chake na hivyo alitakiwa kuachana na mvulana huyo aliyeanza kujinyakulia umaarufu Tanzania.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo maumivu yalivyozidi kuongezeka moyoni mwake mpaka kufikia kipindi ambacho akawa hali, hanywi wala halali kwa raha kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Maumivu yale yaliyotawaliwa na hisia kwamba Edmund alikuwa katika mahusiano na msichana mwingine yaliendelea kumpelekesha mpaka pale alipoamua kuchunguza ili kupata ukweli juu wa kile alichokuwa akikifikiria na kumuumiza moyo.
Uchunguzi wake wa kwanza kabisa kuufanya ulikuwa ni Manzese alipokuwa akiishi Edmund. Alipofika huko, alijitahidi kufanya uchunguzi wa chinichini lakini mwisho wa siku akaja kugundua kwamba Edmund hakuwa na msichana yeyote yule.
“Mmmh! Sasa kwa nini inakuwa hivi?” alijiuliza Sheila.
Hakuishia hapo, alichokifanya ni kuanza kuelekea katika Shule ya Sekondari ya Tambaza ili kupata uhakika juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea kama ni kweli Edmund alikuwa na msichana mwingine au yalikuwa mawazo yake tu.
Alipofika huko, wala hakuhitaji kufanya uchunguzi kwani kila kitu kilikuwa wazi kabisa. Katika mapozi yaliyoonekana kuwa ni ya wapendanao, Edmund alikuwa ametulia na msichana Jamala pembeni kabisa ya shule ambapo wanafunzi walikuwa wakiitumia sehemu hiyo kujisomea.
Picha aliyoiona ilimuumiza, hapo ndipo alipojipa uhakika kwamba kile alichokuwa akikihisi kilikuwa kweli kabisa, Edmund alikuwa katika mahusiano na msichana mwingine, huyu alikuwa Jamala.
Mapenzi aliyokuwa nayo, ghafla yakabadilika na kuwa chuki kubwa, akaanza kumchukia Edmund kwa kumsababishia kidonda ambacho alikuwa na uhakika kisingeweza kupona maisha yake yote.
Kuondoka alikuwa akitaka lakini hata kubaki napo alikuwa akitaka. Aliendelea kuwaangalia wawili hao walioonekana kutokuwa na wasiwasi kabisa. Sheila hakuweza kuvumilia zaidi, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuwafuata huku mwili ukimtetetmeka.
“Edmund..” Sheila aliita kwa hasira, wote wawili wakashtuka na kuanza kumwangalia.
“Unafanya nini na huyu malaya wako?” aliuliza Sheila, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hasira zilikamata mpaka mwili kuanza kutetemeka.
“Sikiliza Sheila,” alisema Edmund huku akionekana kuhofia.
Wanafunzi wengine waliokuwa pembeni waliposikia sauti ya Sheila aliyekuwa akiongea kwa sauti ya juu, wakageuka na kuanza kuangalia watu wale kule walipokuwa.
Wanafunzi wengine na wafanyakazi wa shule wakaacha kazi zao na kusogea kule walipokuwa watu wale. Kila mmoja alikuwa akimshangaa Sheila, hakuwa mwanafunzi wa shule hiyo na hawakujua aliwezaje kuingia ndani ya eneo la shule hiyo.
“Supastaa kafumaniwa,” alisema mwanafunzi mmoja miongoni mwa wanafunzi zaidi ya mia moja waliokuwa wamekusanyika mahali hapo kushuhudia tukio hilo.
Edmund hakutaka kuongea kitu chochote kile, alinyamaza na kuanza kumsikiliza Sheila aliyekuwa akiongea maneno mengi huku akiwatukana wote wawili. Kwa jinsi alivyokuwa akiongea na kutukana, Sheila alionekana kuumizwa na kile alichokuwa akikiona mbele yake.
Hazikupita dakika nyingi, walimu wakafika mahali hapo na kumchukua Sheila na kuondoka naye kuelekea ofisini. Huko, Sheila hakutaka kuwaficha walimu kile kilichokuwa kimeendelea, aliwaeleza wazi kwamba alikuwa mpenzi wa Edmund aliyepanga naye mambo mengi ya kufanya maishani mwao, cha ajabu siku hiyo alimkuta na msichana mwingine.
Maneno hayo hayakuwashtua walimu kwani waliamini kwamba kutokana na umaarufu aliokuwa nao Edmund lilikuwa suala la kawaida kwa wasichana wengi kusema mambo mengi kuhusu yeye, walichokifanya, wakamuita Edmund ili kujiridhisha.
“Simjui msichana huyu, nashangaa amekuja hapa shuleni, amenifuata na kuanza kunitukana mimi na Jamala tulipokuwa tukijisomea,” alisema Edmund, Sheila akapigwa na butwaa kuona kwamba Edmund yule aliyekuwa akimpenda ambaye alikaa naye kwenye mahusiano kwa kipindi kirefu, leo hii alisema kwamba hamfahamu.
“Edmund.....” Sheila aliita huku akiwa haamini.
“Simfahamu, nashangaa kaja kutuvamia. Dada, naomba ufahamu mimi ni mtu wa tofauti sana nisiyependa skendo,” alisema Edmund.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa kumwangalia usoni tu, Edmund alionekana kumaanisha kile alichokuwa akikizungumza, walimu wote wakamuona Sheila kuwa msichana muongo ambaye alitaka kutengeneza kiki kupitia staa huyo.
Hayo yalikuwa ni zaidi ya maumivu, kitendo cha Edmund kudai kwamba hakuwa akimfahamu kiliuumiza moyo wake. Kilio kikaanza tena, mara hii alilia zaidi ya mara ya kwanza kwani kila alipokuwa akiyakumbuka maneno ya Edmund ya kumkataa ofisini hapo, yalimfanya kuwaona wanaume wote wapo kama Edmund.
“Ed..mu..nd..sa...w..a” alisema Sheila, hakutaka kubaki mahali hapo, huku akilia na huku akijisikia aibu, akaondoka ofisini hapo, wanafunzi wote walikuwa wakimzomea.
****
Hicho kiliendelea kuwa kipindi kigumu kwa Sheila, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, mvulana aliyekuwa akimpenda kwa dhati, Edmund alikuwa ameamua kuwa na msichana mwingine, hakika hayo yalikuwa maumivu makubwa ambayo hakuwahi kuyapata kabla.
Sheila hakuwa na furaha tena, kila kilichokuwa kimetokea, wakati mwingine alijiambia kwamba ilikuwa ni moja ya ndoto yenye kusisimua ambayo baada ya muda angeamka na kujikuta akiwa kitandani.
Hiyo wala haikuwa ndoto, kilikuwa ni kitu kilichoendelea kutokea katika maisha yake. Moyo wake haukupoa, kila alipokuwa akimfikiria Edmund, moyo wake uliendelea kuumia zaidi.
Alichokifanya ni kuzichukua picha zote alizokuwa amepiga na Edmund na kuzichoma moto, hakutaka kubaki na kumbukumbu yoyote ile ambayo ingemfanya kumkumbuka mvulana huyo ambaye katika kipindi hicho alimuona hafai na hivyo kumchukua msichana mwingine.
Japokuwa kuna kipindi alikuwa akitaka kuwa na roho ya chuki kwa asilimia mia moja kwa mvulana huyo, alishindwa kufanikiwa katika hilo kwani ukweli wa moyo wake ni kwamba aliendelea kumpenda kwa kiasi kikubwa mno.
“Hivi Edmund anaweza kunikana kweli? Hivi nimemfanyia kitu gani kibaya mpaka anifanyie hivi?” alijiuliza Sheila bila kupata jibu lolote lile.
Hakutaka kusikia kitu chochote kile kutoka kwa mvulana huyo japokuwa mara nyingi alikuwa akikaa chini na kuanza kumfikiria huku akiwa na msukumo mkubwa moyoni mwake wa kutaka kuwasiliana na mwanaume huyo.
Alimtendea jambo moja kubwa na baya ambalo hakuwa amelitegemea katika aisha yake, katika kipindi ambacho alimuona Edmund akiwa na Jamala, alikasirika na kuuahidi moyo wake kwamba kamwe asingeweza kuwasiliana na mtu huyo.
Mpaka wiki kukatika, akaanza kujisikia kitu cha tofauti moyoni mwake. Alijua fika kwamba alifanyia jambo baya lakini hiyo akaiona kutokuwa sababu ambayo ingemfanya kutokuwasiliana na mwanaume huyo.
Kama binadamu, wakati mwingine ni lazima ufanye makosa hili msamaha uchukue nafasi, hivyo, kitu alichokuwa akikitarajia ni kumuona Edmund akimfuata na kumuomba msamaha na hatimae kuishi kama zamani.
Kile alichokuwa akitaka kitokee, hakikutokea, Edmund hakupiga simu kumjulia hali wala kumuomba msamaha. Sheila alizidi kuumia zaidi, aliendelea kuisubiria simu kutoka kwa Edmund lakini mwanaume huyo hakuweza kumpigia.
Kila alipokuwa akimuona kwenye Kituo cha Televisheni cha Global moyo wake ulijawa na furaha huku akijipa matumaini kwamba inawezekana mwanaume huyo angeweza kumpigia simu lakini kutokana na mambo mengi aliyokuwa nayo alishindwa kufanya hivyo.
“Nipigie simu mpenzi, nataka kuisikia sauti yako simuni,” alisema Sheila kila alipokuwa akimuona Edmund kwenye televisheni.
Bado maisha ya maumivu yaliendelea kama kawaida, kuna kipindi alikuwa akijuta kuchukua hatua ya kuwa na mvulana huyo ambaye mpaka katika kipindi hicho alimuona kuwa msaliti ambaye hakustahili kupata aina yoyote ile ya msamaha.
Alimpenda sana Edmund na kumpa nafasi kubwa ya kufanya mambo mengi lakini kila kitu kilibadilika huku akiamini kwamba usupastaa aliokuwa ameupata ghafla ndiyo uliobadilisha kila kitu.
“Nilijua tu, nilijua tu, ususpastaa umebadilisha kila kitu,” alisema Sheila huku akiwa na hasira.
“Ngoja, nitampigia simu,” alijisemea Sheila.
Hicho ndicho alichokuwa akikitaka wakati huo. Moyo wake ulijaza chuki kubwa lakini alitambua kwamba mapenzi aliyokuwa nayo juu ya Edmund yalikuwa makubwa mno. Japokuwa alikuwa akimsikilizia mwanaume huyo ampigie simu lakini wakati mwingine alikuwa na hamu ya kutaka kuichukua simu yake na kumpigia Edmund.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Namba hakuwa nayo kwa kuwa aliifuta kitambo mara baada ya kumfumania akiwa na msichana mwingine. Namba hiyo haikuwepo simuni mwake lakini akashindwa kuifuta moyoni mwake.
Alikuwa amekariri kila namba iliyokuwa imehusika na hata kama angeamshwa kitandani usiku, angeweza kuitaja namba hiyo pasipo tatizo lolote lile.
Hicho nacho kikawa kitu kingine kilichomtesa sana. Alijitahidi kuchoma moto picha za Edmund, baadhi ya zawadi alizokuwa amepewa na mwanaume huyo na kutupa kila kitu ambacho kwa namna moja au nyingine ingemfanya kumkumbuka mwanaume huyo, ila kuifuta namba hiyo moyoni mwake, alishindwa kabisa.
“Nitateseka mpaka lini?” alijiuliza Sheila.
“Nitampigia simu tu, hivi ataweza kuipokea kweli? Hivi simu namba yangu bado anayo? Kwanza sijui anayo! Na kama atakuwa ameifuta, hivi anaweza akawa anaikumbuka kama ninavyokumbuka yake? Jamani Edmund, kwa nini unanifanyia hivi?” aliuliza Sheila kana kwamba Edmund alikuwa mbele yake.
Aliendelea kubaki kimya bila kuwasiliana na Edmund. Siku ziliendelea kukatika lakini kikafika kipindi ambacho akashindwa kabisa kuvumilia, akatamani kuichukua simu yake na kupigia Edmund kwani kilipita kipindi cha wiki mbili hakuwa amemuona machoni mwake.
“Pokea simu mpenzi,” alisema Sheila wakati simu ilipokuwa ikiita.
Moyo wake ukapatwa na shauku kubwa, mtu ambaye alikuwa amempigia simu katika kipindi hicho alikuwa ni mwanaume pekee ambaye alimdharirisha lakini katika kipidi hicho alikuwa radhi kutoa msamaha.
Simu iliita kwa muda wa sekunde thelathini, ikakata na kupiga tena huku kila wakati akijisemea ‘Pokea simu Edmund’.
Simu iliita, mara ikapokelewa na sauti ya Edmund kuita. Kitendo cha kuisikia sauti ile, moyo wake ukahisi amani, tumaini na furaha ya ajabu. Maumivu aliyokuwa ameyapata kutokana na tukio lile lililokuwa limetokea, yakapotea kabisa.
“Hallow Edmund mpenzi,” aliita Sheila.
“Naongea na nani?”
“Unaongea na Sheila.”
“Sheila, ndiye nani?”
“Wewe si Edmund Zilikana?”
“Ndiyo, Sheila ndiye nani?” aliuliza Edmund, Sheila akajikuta akikata simu, akaanza kulia kwa kilio cha sauti ya juu, hakuamini kama kweli Edmund alikuwa amemsahau.
Yalikuwa ni zaidi ya maumivu, kidonda alichokuwa nacho moyoni mwake, maumivu yake yakaongezeka zaidi, kitendo cha kumpigia simu Edmund kwa lengo la kuongea naye na mwisho wa siku kumuuliza kwamba alikuwa nani, kilimuumiza mno.
Swali hilo lilimaanisha kwamba Edmund aliifuta namba hiyo, yaani hakutaka kuwa nayo na wala kichwani mwake haikuwepo. Mbali na hivyo, hiyo ilimaanisha kwamba hata sauti yake alikuwa ameisahau mpaka kumuuliza alikuwa nani.
Sheila akalia mno mpaka kichwa kumuuma. Upendo mkubwa aliokuwa nao kwa Edmund ukamletea matatizo moyoni, unyonge ukamkumba, mwisho wa siku akatokea kuyachukia mapenzi kuliko kitu chochote katika dunia hii.
“Edmund, kwa nini? Kwa nini unanifanyia hivi?” alijiuliza Sheila huku akiendelea kulia kama mtoto.
Kutokana na mabadiliko yake, mama yake, bi Halima akagundua kwamba binti yake hakuwa katika hali nzuri, alichokifanya ni kumuita na kuanza kuongea naye, alitaka kujua kilichokuwa kikiendelea.
“Kuna nini Sheila?” aliuliza bi Halima.
“Edmund, mama.”
“Amefanya nini tena?”
“Ameniacha kwa maneno ya shombo.”
“Hebu tulia kwanza. Niambie kimetokea nini.”
Hapo ndipo Sheila akaanza kuelezea kile kilichokuwa kimetokea. Katika kipindi chote cha simulizi yake, machozi yalikuwa yakimbubujika huku mashavu yake yakiloanishwa na machozi hayo.
Bi Halima alikuwa kimya akimsikiliza binti yake, kwa kila kitu alichokuwa akikisimulia, Sheila alitia huruma, alionyesha ni jinsi gani alikuwa ameumizwa moyoni juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
“Usupastaa,” alisema bi Halima.
“Kisa amekuwa supastaa, ameniacha, imeniuma sana mama,” alisema Sheila.
“Nyamaza Sheila, Allah anajua kuhusu maisha yako ya mbele, achana naye, Mungu atamleta yule aliye sahihi maishani mwako,” alisema bi Halima.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Japokuwa siku hiyo aliambiwa maneno mengi yenye kutia faraja lakini Sheila hakutaka kufarijika, bado moyo wake uliendelea kuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama kweli mwisho wa mapenzi yake na Edmund ungekuwa namna ile.
Kila alipokuwa akimwangalia Edmund katika televisheni, Sheila alikuwa akiumia, chuki za waziwazi zilikuwa usoni mwake, mwisho wa siku, akamchukulia Edmund kwamba ni adui yake namba moja duniani.
“Nitakuchukia milele, hata ukija kwa magoti, hakika sitokusamehe,” alisema Sheila huku akilichana gazeti lililokuwa na picha ya Edmund.
Maisha hayakuwa yakimsubiri, kila kilichokuwa kimepita, kwake kilionekana kama historia, akaamua kukipuuzia na kufanya mambo yake mengine. Hakutaka kumkumbuka Edmund, alitaka kuishi peke yake tu huku akiyatupilia mbali mapenzi.
Siku zikaendelea kukatika, mpaka anamaliza kidato cha sita, Sheila hakutaka kuwa katika mahusiano na mtu yeyote yule.
Wanaume waliokuwa wakimfuatilia, wakaongezeka, bado Sheila hakuonekana kuwa mwepesi kuwakubalia wanaume hao kwani kila alipokuwa akimkumbuka Edmund, hakumtofautisha na wanaume hao.
Wapo waliokuwa wakimfuata na gari, fedha na usupastaa lakini bado Sheila aliamua kuwa peke yake.
Edmund alikwishamfundisha kwamba hakutakiwa kuwa na mwanaume yeyote yule, kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yake kilikuwa fundisho kubwa, hakutaka kurudia makosa yake.
Baada ya matokeo yake kuwa mazuri, Sheila akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Uzuri wake ukawa chachu kubwa kwa wanaume wengi. Usumbufu ule aliokuwa akiupata kipindi cha nyuma shuleni na nyumbani, ukahamia chuoni hapo.
Mara kwa mara walikuwa wakimfuata lakini bado Sheila hakutaka kuwa nao, aliwakatalia kitu kilichomfanya kuonekana msichana aliyekuwa na msimamo.
“Siwezi kupenda tena Ignas,” alisema Sheila.
“Kwa nini?”
“Mapenzi yameniumiza sana, siwezi kupenda maishani mwangu,” alisema Sheila huku akikumbuka ubaya aliotendewa na Edmund.
“Unafikiri mimi ni kama hao waliokuumiza?” aliuliza Ignas.
“Wanaume wote mnafanana, hamna tofauti yoyote ie,” alijibu Sheila.
“Hapana bwana, nipo tofauti sana.”
“Siwezi kuwa nawe Ignas, naomba tu uniache,” alisema Sheila na kuondoka.
Huo ndiyo ulikuwa uamuzi aliokuwa aejiwekea, hakutaka kuwa na mwanaume yeyote yule. Wanaume hawakusikia, kila siku waliendelea kumfuatilia msichana huyo lakini hakuwa radhi kuwa na yeyote yule.
Kwa Ignas, hakuonekana kuchoka, kila siku ilikuwa ni lazima amwambie Sheila jinsi alivyokuwa akimpenda lakini msichana huyo alikuwa akimkatalia kwa maneno ya kistaarabu.
Ignas hakutaka kusikia, kukataliwa kwake kilikuwa ni kitu pekee kilichokuwa kikimpa hamasa kubwa ya kuendelea kumfuatilia msichana huyo. Ilikuwa ni lazima kila siku aongee naye simu na hata kutoka katika mitoko mbalimbali lakini kila alipokuwa akikumbushia kuhusu mahusiano ya kimapenzi, Sheila hakuwa radhi kukubali.
“Ignas, wewe ni rafiki yangu wa kawaida sana, naomba usitake kuubadilisha huu urafiki, hatuwezi kuwa wapenzi,” alisema Sheila.
“Kwa nini lakini?”
“Si nilikwishakwambia kabla, nimeumizwa sana katika mapenzi, siwezi kufanya kosa kama nililolifanya kipindi cha nyuma,” alisema Sheila.
Maneno hayo yaliingia katika sikio la kushoto na kutokea sikio la kulia. Ignas hakuataka kumuacha msichana huyo, bado aliendelea kumsisitizia kwamba alikuwa akitamani sana kuwa naye.
Mawazo juu ya Sheila yalikuwa makubwa, kila alipokuwa akimuona msichana huyo, mapenzi makubwa yalikuwepo moyoni mwake. Kila wakati alikuwa akikaa na kumtukana mwanaume aliyekuwa amesababisha maumivu kwa msichana aliyekuwa akimtaka ambaye alisababisha ugumu mkubwa wa yeye kukubaliwa.
Msichana mrembo kama Sheila hakutakiwa kuwa na maisha yenye maumivu, alitakiwa kupata mwanaume ambaye anaweza kujitoa kwa kila kitu kwa ajili yake. Kila alipokuwa akijiangalia jinsi alivyo na mapenzi yale aliyokuwnayo juu ya msichana yule, alijiona kustahili kuwa naye.
“Nitampata tu. Ila huyu aliyesababisha maumivu kwa Sheila ni nani? Hakika ni mwanaume mjinga sana ambaye hajitambui. Yaani japokuwa Edmund anatuoneshea kwenye muvi zake jinsi ya kuishi na msichana, bado kuna wanaume wajinga wanaendelea kuwasaiti wanawake! Aibu juu yao,” alijisemea Ignas bila kuja kwamba msanii aliyekuwa amemtaja ambaye alipenda kuziangalia filamu zake, ndiye huyo aliyesababisha maumivu kwa msichana huyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Umaarufu bado uliendelea kuwa upande wake, kila alipokuwa akipita, watu walikuwa wakimuita na kumpongeza kutokana na kazi kubwa aliyokuwa akiifanya. Wasichana, kama kawaida yao, mara kwa mara walikuwa wakimfuata Edmund na kutaka namba yake ya simu lakini hakuwa radhi kuwagawia.
Mchakato mzima wa kuigiza filamu ulipofikia, filamu ya kwanza kabisa kuigizwa huku yeye akiwa mhusika mkuu ilikuwa ni Ondoka na Laana Yangu. Hiyo ndiyo ilikuwa filamu ya kwanza kabisa kuigizwa nchini Tanzania ambayo iliwasisimua watu huku Edmund kama kawaida yake akiwa amesimama vilivyo.
Jina lake kubwa na uigizaji wake mkubwa, ukaufanya umaarufu wake kuongezeka. Kitu cha kwanza kabisa kukifanya, akaachana na shule, akahama Manzese na kuhamia Sinza. Maisha yake yakabadilika, mauzo ya filamu ile yalipofanyika, akapata kiasi kikubwa cha fedha kilichompelekea kununua gari yake ya kwanza kabisa, Carina ambayo ilikuwa imeanza kuingia miaka hiyo.
Japokuwa haikuwa gari ya gharama kubwa kulingana na umaarufu wake, lakini kwake, hilo likaonekana kuwa muujiza mkubwa ulioendelea kuishi maishani mwake.
Kumbukumbu za maisha yake ya nyuma zilimuumiza, kila alipokuwa aiwafikiria wazazi wake waliokuwa wamefariki katika mafuriko makubwa yaliyowahi kutokea Jijini Dar es Salaam, moyo wake ulikuwa kwenye majonzi makubwa.
Leo hii, alikuwa mtu mwenye fedha zake ambazo alizipata kupitia kipaji chake cha kuigiza, kutokana na maisha yake ya kimasikini aliyowahi kuishi kipindi cha nyuma, akatamani kama angekuwa na wazazi wake na kuyafaidi maisha pamoja nao.
“Nina kila kitu kwa sasa, ningetamani wazazi wangu wangekuwa pamoja nami,” alijisemea Edmund.
Mara kwa mara waandishi wa habari walikuwa wakimfuata na kumuuliza mengi kuhusiana na maisha yake kwa ujumla, Edmund hakuficha, kila aliulizwa kuhusiana na wazazi wake, aliwahadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea katika mafuriko yale.
Historia yake ilikuwa ni ya kuhuzunisha mno, kila aliyeisikia, alidiriki kusema kwamba mtu huyo alikuwa amepitia sehemu mbalimbali zenye matatizo, na wakati huo alikuwa akihitaji kuipumzisha akili yake kwa kuyafaidi mafanikio yake.
Kwa wakati huo, hata mapenzi yake kwa Jamala yalikuwa yamepungua. Japokuwa bado msichana huyo alikuwa mrembo lakini kwa Edmund alionekana kuwa si kitu kabisa kwani kulikuwa na wasichana wengi waliokuwa wakimfuata ambao walikuwa wazuri hata zaidi yake.
Kwa sababu alitaka kumuacha msichana huyo, hakutaka kuwa na pupa, alichokifanya ni kupunguza ukaribu naye tu. Japokuwa Jamala alilalamika sana lakini hiyo haikuweza kumshawishi Edmund kuwa naye, bado aliendelea kufanya hivyohivyo mpaka pale Jamala alipoona kwamba hakuwa na nafasi kwake.
“Mbona umekuwa hivi mpenzi?” aliuliza Jamala.
“Nimekuwaje? Mbona kawaida tu. Wewe ndiye umekuwa wa ajabu, wakati mwingine, hata kama kusoma hujui, jaribu kuielewa picha,” alisema Edmund kwa mbwembwe.
Maneno hayo yalieleweka vizuri sana kwa Jamala, yalimaanisha kwamba alitakiwa kuelewa kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Edmund akabadilika, akawa mtu wa wasichana tu kwani hakuona kama kulikuwa na sababu ya kuwaacha wampite na wakati walikuwa wakimpapatikia.
Alikuwa na fedha, umaarufu ulikuwa umeongezeka na kuwa muigizaji bora nchini Tanzania. Akaanza kusaini mikataba ya kushiriki kwenye matangazo mengi yakiwepo ya mitandao ya simu, magari na mengine mengi ambayo yakamfanya kuingiza kiasi cha shilingi milioni mia tano kwa mwaka.
Edmund akawa mtu mwenye mafanikio zaidi, akajenga nyumba ya kifahari na kusahau shida zote alizowahi kupitia katika maisha yake.
“Tunasikia una mahusiano ya siri na yule video queen, Shufaa, ni kweli?” aliuliza mwandishi mmoja wa Gazeti la Tifutifu.
“Ni tetesi, acha ziendelee kuwa tetesi tu kwani kamwe hatuwezi kuziepuka,” alijibu Edmund.
Hizo ndizo zilizokuwa tetesi zilizobamba kipindi hicho. Kutokana na umaarufu aliokuwa nao kipindi hicho, habari zake zilikuwa zikiongozwa kuandikwa zaidi ya mtu yeyote yule. Tetesi juu ya uhusiano wa kimapenzi aliokuwa nao na msichana Shufaa aliyekuwa akionekana kwenye video nyingi ziliendelea kuvuma zaidi lakini kila alipokuwa akiulizwa, Edmund alikuwa akikataa tofauti na mwenzake.
“Mbona mwenzako anakubali?”
“Sijajua kwa nini, siko katika mahusiano naye,” alisema Edmund.
Mpaka kufikia kipindi hicho, Edmund hakukumbuka kama alikuwa na mahusiano na msichana aliyeitwa Sheila. Wasichana waliokuwa wakimiminika na kulala nao kila siku ndiyo waliokuwa wakikumbukwa kichwani mwake.
Starehe zilikuwa mbele lakini hata kwenye kupiga kazi, Edmund alikuwa akifanya vizuri zaidi jambo lililomfanya kuwa juu kila siku. Alipoona kwamba alipiga kazi nyingi na wasanii wa hata Bongo, hapo ndipo akaamua kuhamia kwa wasanii wa nje.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mtu wa kwanza kupiga naye kazi alikuwa Nkhiloma Mbuyitho, huyu alikuwa muigizaji kutoka katika tasnia ya filamu nchini Afrika Kusini. Mara baada ya kuonana naye tu, wakapanga kufanya kazi huku lengo lake kubwa likiwa ni kujitangaza kimataifa, akafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Umaarufu wangu utabaki siku zote za maisha yangu, hakika ninataka kuacha jina litakalowafanya mnikumbuke siku zote za maisha yenu,” alisema Edmund alipokuwa akitazama filamu yake aliyoigiza na msanii huyo iitwayo GOLDEN ANGEL ambayo ilimpatia umaarfufu Afrika nzima.
****
Bado Edmund hakutaka kumpa pumzi Sheila, kila siku ilikuwa ni lazima amuite na kumwambia maneno mengi ya kimapenzi huku akihitaji kuwa naye. Hilo halikuwa jambo jepesi kutokea, kila siku aliendelea kula kwa macho tu.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo uzuri wake ulivyozidi kuongezeka zaidi. Wanaume hawakukoma, waliendelea kujitokeza huku kila mmoja akihitaji nafasi lakini hakukuwa aliyeipata nafasi hiyo.
Kikafika kipindi ambacho Ignas akaona kama angeweza kumpoteza Sheila kutokana na idadi ya wanaume waliokuwa wakimfuata. Alichokifanya ni kuongeza ukaribu na msichana huyo.
Kila alipokuwa Sheila, Ignas alikuwa pembeni yake, kitu alichokuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuwa karibu na msichana huyo tu ili kutowapa nafasi wanaume wengine kumfuata msichana huyo kwa kuogopa kumpoteza kwani siku zote aliamini kwamba uwezo wa kumlaghai msichana ulikuwa ukitofautiana.
Mwaka wa kwanza ukakatika na wa pili kuingia, bado Ignas alikuwa akipigwa danadana mpaka wakati mwingine akaonekana kukata tamaa. Uzuri wa Sheila ulizidi kuongezeka, hata Ignas mwenyewe alipokuwa akimwangalia, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio tu.
“Unaonekana kama malaika,” alisema Ignas huku akitoa tabasamu.
“Asante sana.”
“Ningependa uje nyumbani kwangu tuangalie muvi siku nzima,” alisema Ignas.
“Muvi gani?”
“Zipo nyingi tu, hasa tutaangalia hii inayotamba kwa sasa iitwayo Golden Angel, ni nzuri na Edmund ameigiza vizuri mno na wale Waafrika Kusini, ningependa tuiangalie wote,” alisema Ignas.
Hakuelewa ni kitu gani kilitokea, ghafla, macho ya Sheila yakaanza kuwa mekundu na baada ya sekunde kadhaa, machozi yakaanza kububujika mashavuni mwake, Ignas akashtuka, hakujua tatizo lilikuwa nini.
Edmund hakuwa na mpinzani, yeye ndiye alikuwa ‘top’ katika tasnia ya filamu Tanzania. Kila siku, maisha yake yalitawaliwa na fedha, alinunua kila kitu alichokitaka huku akienda kila sehemu ambayo angeona kufaa kutembelewa na mtu kama yeye.
Katika maisha yake yote, Edmund alikuwa mtu wa wasichana tu. Kutokana na kuwa na jina kubwa na fedha, wasichana wengi wakataka kuwa naye na bila hiyana akawa akifanya nao ngono kadri alivyotaka.
Magazeti na vyombo vya habari vingine havikuacha kumtaja, kila siku alikuwa akitokea katika kurasa za mbele kitu klichomuongezea jina kila siku. Kazi zake zikazidi kupendwa zaidi, wasichana wakazidi kumiminika huku akionekana kuwa msanii bora mwenye pesa kuliko wote.
“Kufanya tangazo na mimi ni milioni sabini, zipo?” aliuliza Edmund alipofuatwa na mkurugenzi wa kampuni inayotengeneza pafyumu ziitwazo The Prince.
“Hakuna tatizo, tunaweza kulipa kiasi hicho cha fedha,” alisema mkurugenzi huyo.
“Basi sawa. Nipo tayari, nafikiri kinachotakiwa kufanyika ni kusaini mkataba tu,” alisema Edmund.
Siku hiyo, Edmund akasaini mkataba na kampuni hiyo ya kutengeneza pafyumu ya nchini Uingereza huku kwa hapa Tanzania wakiwa na matawi yao kadhaa. Maisha ya kuingiza fedha ndiyo ilikuwa sehemu ya maisha yake, kila siku alikuwa akijivunia kipaji chake huku akiamini kwamba kila siku atakuwa juu katika maisha yake.
Kutokana na umaarufu mkubwa aliokuwa nao, vijana wengi wakaanza kumtafuta Edmund kwa kutaka kuwatoa katika uigizaji. Edmund hakuwa mwepesi kupatikana, leo alikuwa hapa na kesho alikuwa pale.
“Huwezi kutoka bila kupitia huyu mtu, cha msingi mtafute, utafanikiwa tu,” alisema kijana mmoja.
“Kweli nitaweza kumpata?”
“Utaweza tu, au shida iwe kulisikiliza tatizo lako.”
“Nitampatia wapi?”
“Nenda Leaders Club, pale, kila Jumamosi wasanii huwa wanajikusanya, ukienda, utampata tu,” alisema jamaa huyo.
Filbert alikuwa kijana aliyemaliza elimu yake ya Sekondari kwa kidato cha nne na katika kipindi hicho alikuwa akitaka kitu kimoja tu, kuwa muigizaji na kujiingizia fedha kama alivyokuwa akifanya Edmund.
Kila siku alikuwa akihangaika katika sehemu mbalimbali hasa zilizokuwa na vikundi vya kuigiza na kujaribu kuomba nafasi lakini hakuwa akiipata kwa madai kwamba hakuwa na mvuto machoni mwa watu.
Hilo lilimuumiza lakini hakutaka kukata tamaa, kila siku alijitahidi kutafuta bila kuchoka kwa kuamini kwamba mwisho wa siku angefanikiwa kupata kundi la kuigiza na hatimae naye kuanza kuonekana katika televisheni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila siku, naye ndoto yake kubwa ilikuwa ni kuigiza na kupata umaarufu kupitia filamu. Hakujali sana fedha kwa kuamini kwamba endapo angepata umarufu kupitia uigizaji basi naye angeweza kupata fedha.
Kila alipokuwa akimwangalia Edmund alivyokuwa akiigiza, moyoni mwake alishikwa na shauku ya kutaka kuwa muigizaji mkubwa na hatimae kufanikiwa kama alivyofanikiwa Edmund.
“Nitakuwa kama Edmund tu. Ila kwanza nipewe nafasi ya kuonesha uwezo wangu,” alisema Filbert huku akijiangalia kwenye kioo na kuanza kuigiza.
“Ninafaa sana, sasa kwa nini kila ninapokwenda natolewa nduki?” alijiuliza Filbert bila kupata majibu sahihi.
Maisha yalimpiga, alitoka katika familia masikini huku akiishi na mama yake aliyekuwa mlemavu wa mguu ambaye kila siku alikuwa akitembelea kibaiskeli kidogo kilichoonekana kuchoka mno.
Kila alipokuwa akimwangalia mama yake, moyoni aliumia, hakutaka kumuona akiwa ombaomba, alitaka kumuona akiwa nyumbani amekaa huku yeye akishughulika kwa kila kitu alichokuwa akikihitaji.
Maisha yake hayakubadilika, mama yake aliendelea kuomba mitaani kwani hiyo ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuwaingizia fedha. Moyoni aliumiza mno lakini hakuwa na jinsi. Kila siku asubuhi alikuwa akimsukuma mama yake mpaka Kariakoo ambapo huko alikaa na kuomba, inapofika jioni, anakwenda kumchukua.
“Ila na mimi maisha yangu yatabadilika tu, cha msingi kwanza ngoja nimtafute huyu Edmund, nadhani atanisaidia tu,” alisema Filbert.
Siku ya Jumamosi, hakutaka kuchelewa, asubuhi na mapema akajiandaa kwa ajili ya kwenda katika Viwanja vya Leaders kwa ajili ya kuonana na Edmund tu. Alipofika hapo, wasanii kadhaa walikuwepo huku watu wengine ambao hawakuwa waigizaji wakiwepo kwa ajili ya kuonana na wasanii mbalimbali.
Kila alipokuwa akiwaangalia wasanii hao, Filbert alionekana kufarijika huku akijiambia moyoni mwake kwamba kuna siku angekuwa kama hao, angeheshimika na kuthaminiwa.
Alifika viwanjani hapo kwa ajili ya kumuona Edmund na kuongea naye kuhusiana na suala lake la kutaka kuigiza lakini kila alipoangalia huku na kule, Edmund hakuwepo.
“Nitamuona tu, hata iwe vipi, kama atakuja, nitahakikisha naonana naye tu,” alijisemea Filbert huku akionekana kutokuwa na muda na wasanii wengine.
Aliendelea kukaa mahali hapo, baada ya saa moja, gari la kifahari, VX S768 likaanza kuingia, wasanii wote wakakaa kimya huku wakiliangalia gari lile.
Liliposimama, mlango ukafunguliwa, Edmund akateremka na kuanza kuelekea kule walipokuwa wasanii wenzake. Filbert akabaki akiwa ameduwaa tu, kila alipokuwa akimwangalia Edmund, aliona kama anaiangalia taswira yake.
“Daaah!” alisema Fibert, akainuka na kuanza kumfuata Edmund.
“Braza,” aliita Filbert huku akimsogelea Edmund aliyekuwa bize akiwasalimia wasanii wenzake, akageuka nyuma na kumwangalia Filbert.
“Shikamoo.”
“Marahaba. Mambo vipi!”
“Poa. Samahani, wewe ni role model wangu, nataka kuwa kama wewe braza,” alisema Filbert
“Kuwa kama mimi?”
“Ndiyo, najua kuigiza kaka, nipe nafasi nitakuoneshea uwezo wangu,” alisema Filbert, watu wote waliokuwa mahali hapo walikuwa wakimshangaa, lakini hakuonekana kusikia aibu yoyote ile.
“Hakuna nafasi rafiki yangu.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nakuomba unipe nafasi braza, mama yangu mgonjwa, sina hela, nataka kuigiza na kuwa kama wewe,” alisema Filbert, machozi yakaanza kumlenga.
“Haiwezekani, kajiunge na kundi lolote lile, nitauona uwezo wako huko,” alisema Edmund na kuendelea na mambo yake.
“Braza, nisikilize braza, mama yangu mgonjwa,” alisema Filbert, Edmund hakutaka kujali, kama kumsikiliza, alimsikiliza na kumshauri, hakutaka kuongea naye lolote lile.
Filbert akaumia moyoni mwake, hakuamini kama mtu ambaye kila siku alijimsifia huku akimwambia kwamba alikuwa role model wake leo hii hakutaka hata kukaa naye chini na kumsikiliza zaidi ya kumpa ushauri wa juu kwa juu tu.
Machozi yakaanza kumlenga na mwisho wa siku kuanza kumbubujika mashavuni mwake.
Filbert aliumia moyoni, hakuamini kama yule mtu aliyekuwa akimchukulia kama ‘role model’ wake alikuwa amekataa kumsaidia kile alichokuwa akikihitaji, kumtoa kwa kuigiza naye filamu ili apate umaarufu na hatimae naye atambe katika muvi za kibongo.
Siku hiyo ikawa ni siku yenye majonzi kuliko siku zote katika ndoto zake za kuutamani usupastaa ambao kila siku alikuwa akiuhangaikia. Kila alipokuwa nyumbani nyakati za usiku, alikuwa akikipa kichwa chake kazi ya kufikiria maisha ya usupastaa kwa jinsi yangekuwa endapo Edmund angemkubalia kuigiza pamoja naye.
Mama yake alizidi kuumwa, hakuwa na msaada wowote ule, kila alipokuwa akimwangalia, bado moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali. Hakupenda kumuona mama yake akipata mateso kitandani, alikuwa akitaka sana kumsaidia ili aondoke katika ugonjwa wa kansa ya koo ambao ulimfanya kuwa kwenye mateso makali.
Kila siku Filbert alikuwa mtu wa kuhangaika huku na kule, ni kweli kwamba alikuwa na kipaji kikubwa cha kuigiza lakini hakuwa amepata nafasi za kutosha. Kila alipokuwa akienda na kufanya majaribio, alitawaliwa na hofu na mwisho wa siku alionekana kutokuwa na uwezo wa kuigiza na hivyo kufukuzwa.
“Hivi nitaweza kuigiza kweli na kuwa supastaa?” alijiuliza Filbert na jibu lake kuwa ‘hapana’.
Hakukata tamaa, japokuwa alikuwa ameshauriwa na mtu aliyemhusudu, Edmund kwamba atafute sehemu ya kuingiza na kuigiza ambapo huko angeonekana, alifanya hivyo lakini hakufanikiwa.
“Ni lazima nimtafute tena Edmund, haiwezekani nishindwe kirahisi,” alijisema Filbert.
Siku iliyofuata, kazi yake kubwa ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa Edmund lengo la kuonana naye na kumwambia kwamba bado alikuwa akihitaji msaada mkubwa wa kutaka kuigiza na kuwa kama yeye.
Nyumbani hapo, hakuwa peke yake, watu wengi hasa vijana walioonekana kuwa na uhitaji wa kuigiza walijukusanya mahali hapo, kila mmoja alitaka kutolewa kiuigizaji na msanii huyo aliyepata usupastaa katika mazingira magumu.
“Na wewe unataka kumuona Edmund?” aliuliza jamaa mmoja aliyekuwa mahali hapo.
“Ndiyo,” alijibu Filbert.
“Duuh! Kweli leo balaa, hivi jamaa ataweza kutusikiliza wote kweli?”
“Bado hatujajua, kwani hawa wote wanamsubiri Ed? ,” aliuliza Filbert.
“Ndiyo, wote wanamsubiri.”
Idadi ya watu waliofika mahali hapo ilizidi kuongezea, kila mmoja alikuwa akitaka kumuona Edmund ambaye mpaka muda huo alikuwa amelala. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku, alikuwa bize sana huku wakati mwingine akichelewa kulala kutokana na kuzifanyia kazi muvi zake mbalimbali alizokuwa akiigiza.
Kila mgeni aliyekuwa mahali hapo alikuwa alitaka kuongea na Edmund. Kukosekana kwa ajira ndiyo kulimfanya kila kijana kutaka kuigiza kwani hiyo ndiyo ilionekana kuwa kazi iliyowafaa hata wale vijana ambao hawakwenda shule.
Muda wote alipokuwa mahali hapo, Filbert alikuwa akisali kimoyomoyo, alimuomba Mungu ili aweze kufanikiwa kuongea na supastaa huyo kwa mara ya pili na kuendelea kumsisitizia kile alichokuwa akikihitaji kwa kipindi kirefu, kuwa supastaa baada ya kuigiza filamu kadhaa na mtu huyo.
“Nitafanikiwa tu,” alijisemea Filbert.
Watu hao zaidi ya ishirini waliendelea kukaa nje ya nyumba hiyo kwa takribani masaa manne, na ndipo geti likafunguliwa na mlinzi kutoka. Mlinzi akatabasamu, kwake, watu waliofika mahali hapo siku hiyo, walikuwa wachache tofauti na siku nyingine.
“Afadhali, leo mpo wachache sana,” alisema mlinzi yule.
“Kaka, unaweza kutusaidia kuonana na braza?”
“Mna shida gani? Wale wanaotaka kuigiza, leo hana nafasi ya kuzungumza nao, mtatakiwa kuja kesho, ila kama mna shida nyingine, hakuna noma,” alisema mlinzi yule.
Japokuwa alimsikia mlinzi akisema kwamba waliokuwa wakitaka kupewa nafasi ya kuigiza hakuwa na muda wa kuzungumza nao, hilo halikumfanya Filbert kuondoka mahali hapo, shida yake ilikuwa ni kuonana na supastaa huyo, Edmund na kumwambia lilelile la kutaka kuigiza naye.
“Sirudi nyuma, hapa ni kumuona tu. Daah! Hivi nitaweza kupata nafasi kweli?” alijiuliza Filbert bila kupata jibu lolote lile.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wapo waliosimama na kuondoka mahali hapo ila kwa Filbert, hicho kilikuwa kitu kisichowezekana kabisa, shida yake ilikuwa ni kutaka kuonana na Edmund tu. Baada ya dakika ishirini, akaanza kuitwa mmoja baada ya mwingine huku Filbert. akiwa na presha ya kuonana na Edmund.
Zamu yake ilipofika, Filbert akazama ndani na moja kwa moja kuelekea katika ofisi aliyoelekezwa na mlinzi, alipofika mlangoni, akagonga hodi na mlango kufunguliwa, akaingia.
Sura yake haikuwa ngeni machoni mwa Edmund, alikwishawahi kuiona sehemu fulani japokuwa hakukumbuki ni mahali gani. Alimwangalia Filbert machoni huku akijitahidi kuvuta kumbukumbu juu ya mahali alipowahi kumuona mtu huyo, hakukumbuka kitu chochote kile.
“Sura yako si ngeni machoni mwangu,” alisema Edmund.
“Yeah! Braza, tulishawahi kuonana pale Leaders Club,” alisema Filbert.
“Kama nakumbuka hivi. Ok! Unataka nikusaidie nini?” aliuliza Edmund.
“Mama yangu ni mgonjwa, anasumbuliwa na kansa ya koo, nahitaji msaada wako,” alisema Filbert.
“Msaada wa nini? Fedha au?”
“Ninataka kuwa supastaa kama wewe.”
“Unataka kuwa supastaa?”
“Ndiyo.”
“Sasa ukiwa supastaa mama yako atapona?”
“Ndiyo.”
“Kivipi?”
“Nitapata fedha na mwisho wa siku nitamtibia mama yangu,” alisema Filbert.
“Usupastaa si tiba.”
“Naomba unisaidie braza, najua kuigiza ila sijapewa nafasi.”
“Nitaamini vipi kama unajua kuigiza?”
“Ngoja nikuoneshee, najua mpaka kulia kimaigizo braza,” alisema Filbert.
“Hapana, usinioneshee. Unachotakiwa kufanya ni kwenda pale Leaders wiki ijayo.”
“Kuna nini? Utanisaidia?”
“Hapana. Kutakuwa na shindano la watu wanaotaka kuigiza, ukifanikiwa, basi utapita.”
“Nitaigiza na wewe? Ninatamani kuigiza na wewe, wewe ni role model wangu braza, nataka kuigiza na wewe,” alisema Filbert.
“Hapana, hutoweza kuigiza na mimi, hilo shindano limeratibiwa na kampuni nyingine kabisa, jaribu bahati yako,” alisema Edmund
“Asante braza kwa kunipa taarifa. Nashukuru sana.”
“Usijali. Karibu tena,” alisema Edmund na Filbert kuondoka mahali hapo huku moyoni mwake akiendelea kuwa na ndoto ya kuwa muigizaji mkubwa barani Afrika kama alivyokuwa Edmund.
***
Siku nzima Filbert alikuwa na mawazo, kichwa chake kilikuwa kikiifikiria siku hiyo ambayo kwake ikaonekana kuwa siku pekee ambayo ingemfanya kujisafishia njia na hatimae kuwa muigizaji mkubwa.
Mara kwa mara akawa akienda katika Ufukwe wa Msasani na kuchukua mazoezi ya sauti hasa kuongea kwa nguvu kama mtu aliyekuwa akilalamika jambo fulani. Wiki nzima hiyo ndiyo kazi kubwa aliyokuwa nayo, hakutaka kutulia hata siku moja, kazi yake kubwa ilikuwa ni kwenda huko na kuchukua mazoezi zaidi.
Hakujua ni kampuni gani ambayo ingekuja na kutafuta waigizaji, ndoto ambayo kila siku ilikuwa moyoni mwake ni kuwa muigizaji mkubwa ili tu aje kuigiza na Edmund ambaye alikuwa juu sana katika kipindi hicho.
“Nitafanikiwa tu, nitafanikiwa tu,” alijisema Filbert kila alipokuwa akitoka kufanya mazoezi hayo.
Siku ambayo aliisubiria kwa hamu ikawa imewadia, idadi ya watu zaidi ya elfu mbili walikuwa wamejikusanya katika Viwanja vya Leaders Club, walikuwepo wanafunzi kutoka katika shule mbalimbali, wanavyuo kutoka vyuo mbalimbali, wote kwa pamoja walikuwa mahali hapo kujaribu nafasi yao ya kuwa muigizaji ambaye angepata nafasi yakuonesha uwezo wake.
“Wakina nani hawa? Mbona wazungu wengi?” aliuliza Filbert kuhusiana na watu waliokuwa wakihusika katika utafutaji wa wasanii hao.
“Hawa ni wazungu kutoka kampuni ya Panorama kutoka nchini Marekani, wapo hapa kwa kuwa wanataka kutengeneza tamthilia itakayooneshwa dunia nzima, hizo ni tetesi tu nilizozisikia, sijui kama ni kweli,” alijibu jamaa mmoja, Filbert akashtuka.
“Kwa hiyo washikaji wamekuja kutafuta waigizaji? Hii ndiyo nafasi aisee, kumbe ndiyo maana hata wasanii wakubwa nao nawaona mahali hapa. Kweli kazi ipo,” alisema Filbert kwa mshangao kwani hata wasanii wengine wakubwa ambao walikuwa wakivuma, walikuwa mahali hapo.
Mchakato ukaanza mara moja. Kila mtu aliyekuwa akitaka kuigiza, alijaza fomu na kupewa namba ambayo hiyo ndiyo ingetumika kumuita kule alipokuwa akihitajika. Watangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Global ndiyo waliokuwa majaji siku hiyo huku wale wazungu wenye kampuni hiyo ya Panorama wakihakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawa na hakuna kubebana katika kuchaguana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Japokuwa alikuwa akijiamini, lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele, akaanza kutetemeka, tayari hofu ikaanza kumuingia. Wasanii walikwenda kwa namba tena kwa zamu. Mpaka zamu yake ilipofika, tayari ilikuwa ni saa nane mchana huku akiwa ameingia mahali hapo saa mbili asubuhi.
Kila alichokuwa akiambiwa akiigizie, Filbert alifanya hivyo, uwezo wake ulikuwa mkubwa uliowafanya majaji kumuongezea vipengele vya kuigiza zaidi na zaidi kwani alionekana kuwa na kipaji kikubwa cha kuigiza, alipomaliza, akapewa taarifa kwamba kama atapita, atapigiwa simu lakini akiona kimya, ajue kwamba hakupita hivyo angeendelea na mambo yake mengine.
“Mungu wangu! Kweli nitapita masikini mimi? Mungu, naomba nipite nimuuguze mama yangu,” alisema Filbert huku akiyainua macho yake juu kama ushara ya kumwangalia Mungu.
***
Panorama ilikuwa ni moja ya kampuni kubwa za filamu nchini Marekani ambayo ilikuwa ikijihusisha zaidi na filamu za muvi na tamthilia ambazo zilikuwa zikitazamwa zaidi katika kipindi hicho.
Viongozi wa kampuni hiyo walikuwa wakijiingizia kiasi kikubwa cha fedha kwa kuziuza filamu zao sehemu mbalimbali duniani kote huku wakiendelea kujikusanyia mapato mengi kupitia majumba ya kuoneshea filamu duniani hasa katika nchi za Marekani na Ulaya.
Kila mwaka, kampuni hiyo ilikuwa ikitoa tahmthilia tatu ambazo zilikuwa zikitikisa sana kiasi kwamba wapenzi wengi wa tamthilia hizo walikuwa wakizifuatilia hatua kwa hatua kwani zilikuwa na mvuto na kiwango cha juu zaidi.
Wao, ndiyo waliomtoa Nemes Ononko, Mnigeria ambaye alikuwa akivuma sana kipindi hicho katika filamu hasa zile zilizokuwa zikiigizwa nchini Marekani, jina lake lilikuwa kubwa na hatimae kuwa muigizaji aliyeingia kiasi kikubwa cha fedha.
Mishemishe zao hazikuishi hapo, bado waliendelea kufanya mapinduzi makubwa ya filamu, wakaanza kutunga tamthilia mbalimbali ambazo zilikuwa zikihusisha sehemu mbalimbali kama Afrika, Asia na sehemu nyingine, kote huko ilikuwa ni kutafuta watazamaji zaidi.
Mara baada ya kufanya mizunguko yao sehemu nyingi duniani, moja kwa moja wakaamua kuja nchini Tanzania huku lengo lao likiwa ni kuiendeleza tamthilia iitwayo Wicked Journey ambayo iliigizwa zaidi ya nchi kumi duniani, Tanzania ilikuwa ni nchi ya kumi na moja.
Walipofika Tanzania tu, kitu cha kwanza wakawasiliana na Kampuni ya Global Publishers ambayo ikahusika katika kutoa taarifa ya mambo mbalimbali, hapo, lengo lao kubwa lilikuwa ni kutaka kuwasaidia katika kutangaza kwamba walikuwa wakihitaji waigizaji.
Hilo wala halikuwa tatizo, walichokifanya ni kuchapisha taarifa hizo magazetini, kutangaza katika televisheni yao, Global, kote huko, walitaka watu wajitokeze kwa wingi katika Viwanja vya Leaders Club kwa ajili ya kufanyiwa usaili.
“You are all the best and you deserve to be an international actors, but, we have to choose someone who deserves and who did acting more than others” (Nyie wote ni bora. Mnastahili kuwa waigizaji wa kimataifa, lakini yatupasa kuchagua mtu ambaye amefanya vizuri katika uigizaji kuliko wengine) alisema meneja mkuu wa kampuni hiyo, Antonin Martuzo.
Wiki nzima ilipita, walikuwa na kazi kubwa ya kuziangalia video za watu waliofanyiwa usaili ambao walikuwa na kazi moja tu ya kuigiza mbele ya majaji. Haikuwa kazi nyepesi, waliwachuja wale waliotakiwa kutoka, mwisho wa siku, watu walioonekana kuwa bora walikuwa watano, Filbert alikuwa mmojawapo.
“We need two actors, remember?” (Tunahitaji waigizaji wawili, mnakumbuka)
Hao waigizaji watano walitakiwa kupungua na kubakia waigizaji wawili tu ambao wangejiunga moja kwa moja na kampuni hiyo na uigizaji kuanza mara moja. Mchujo haukuwa mwepesi kwani kila mtu alionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuigiza.
Mwisho wa siku, waigizaji wawili wakapatikana, wanaume wawili, Thomas na Filbert, ambao wote walitakiwa kupewa taarifa ili wafike katika Hoteli ya Atrums kwa ajili ya maongezi machache.
“Call them” (Wapigie simu)
Hapohapo, bila kuchelewa simu zikaanza kupigwa kwa watu hao. Mtu wa kwanza kupigiwa simu alikuwa Filbert, simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu lakini haikuwa ikipatikana.
Huo haukuwa mwisho, waliendelea kuwapigia waigizaji hao wawili waliokuwa wamechaguliwa lakini majibu yalikuwa ni yaleyale tu, simu hazikuwa zikipatikana. Walichokifanya ni kumpigia Thomas, wala simu haikuita muda mrefu, ikapokelewa na sauti ya Thomas kusikika, wakampa taarifa kwamba alichaguliwa kuigiza Tamthilia ya Wicked Love iliyokuwa ikiendelea. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kubwa kwake.
“What should we do?” (Tufanye nini?) aliuliza muongozaji mara baada ya Filbert kupigiwa simu yake na kutokupatikana.
“Make a call to someone else” (Mpigie simu mtu mwingine) alisema meneja wa kampuni hiyo, Martuzo na muongozaji huyo kuanza kuwapigia simu washiriki wengine walioingia kwenye tano bora.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wasiwasi bado ulikuwa umemshika Filbert, alikuwa akijiona kushindwa na kuna wakati alitamani dakika zirudi nyuma ili aweze kuigiza vizuri zaidi katika usaili ili aweze kushinda lakini hicho kilikuwa kitu kisichowezekana kabisa.
Alikuwa akihitaji sana fedha kwa ajili ya kumtibia mama yake aliyekuwa akiumwa kansa ya koo. Hakuwa na fedha na ni kwa msaada wa ndugu wachache tu ndiyo waliokuwa wakijichangisha fedha na kumsaidia mwanamke huyo.
“Siku nikipata fedha tu, lazima nikupeleke India ukatibiwe mama,” alisema Filbert huku akiwa pembeni ya mama yake aliyeonekana kutia huruma.
“Utapata tu, vipi ulipokwenda kuigiza?”
“Mama, mambo magumu sana, yaani hapa sielewi chochote kile, leo hii ni siku ya tatu, wale waliotufanyia usaili hawajanipigia simu, sijui nimepita au la, sijui chochote kile, bila shaka nitakuwa nimechujwa tu,” alisema Filbert.
“Hapana Filbert, utapigiwa simu tu.”
“Lini sasa mama? Muda unazidi kwenda na bado sipigiwi simu,” alisema Filbert.
“Vumilia tu,” alisema bi Linda.
Filbert akawa mtu anaiyeishi kwa matumaini tu, kila siku masikio yake yalikuwa katika simu yake kwa kuhisi kwamba angeweza kupigiwa na watu hao kwa ajili ya kuitwa kuanza kazi ya kuigiza.
Kila siku alikuwa karibu na simu yake, hakutaka kuwa mbali nayo, kila ilipokuwa ikikaribia kuisha chaji, alikuwa akiichaji ili isije ikatokea kuisha chaji. Siku ziliendelea kukatika lakini hali ikawa kimya, mpaka kufikia kipindi hicho, tayari alikwishakata tamaa kwa kuona kwamba hakuwa amefanikiwa, hivyo alitakiwa kutulia.
“Ndiyo basi tena,” alijisemea Filbert.
Siku ambayo alipigiwa simu na kuita bila kupokelewa, siku hiyo alikuwa amelala chumbani kwake huku simu akiwa ameiweka kwenye ‘silent’ hata ilipokuwa ikiita zaidi, hakuwa akiisikia.
Alipoamka, kitu cha kwanza kuangalia kilikuwa ni simu yake. Alikutana na simu iliyopigwa zaidi ya tatu, alipoiangalia, namba ilikuwa ngeni, hakuonekana kuwa na wasiwasi kwani hakutarajia kupigiwa simu na watu hao kwani tayari alijiona kushindwa kuvuka katika kinyang’anyiro kile.
“Watu wasumbufu sana, tunataka kutiana presha bure na namba zao ngeni,” alijisemea Filbert na kuamua kutoka chumbani mule huku akiiacha simu ile kitandani.
Edmund hakutaka kuishika simu yake, alikwenda kutembea na hakutaka kabisa kuwa na simu hiyo kwani namba ngeni iliyokuwa imempigia ilimtia presha na wakati alikuwa kwenye majonzi ya kutokuchaguliwa kuigiza filamu kutoka katika Kampuni ya Panorama.
Filbert alitumia saa zima kuwa katika mizunguko yake, alipochoka kutembea, akarudi nyumbani. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuiangalia simu yake, alikutana na baadhi ya namba za marafiki zake zilizokuwa zimeingia katika kipindi cha nyuma, akazipuuzia kama kawaida yake.
Alichokifanya mara baada ya kuona hakukuwa na namba iliyokuwa na umuhimu kwake, akalala zake kwani akili yake kwa kipindi hicho ilikuwa imechoka sana.
****
Hapo ndipo simu zikaanza kupigwa kwa washiriki wengine mara baada ya kuona simu ya Filbert haikuwa ikipokelewa. Mtu wa kwanza kumpigia simu alikuwa kijana Hassani ambaye alishika nafasi ya tatu, walipompigia, simu yake haikuwa ikipatikana jambo lililowakasirisha kwa kuona kwamba watu waliofika mahali pale siku ile hawakuwa ‘serious’ kwa kile alichokuwa wamekwenda kukiomba kwani waliwaambia kabla kwamba walitakiwa kuwa karibu na simu zao na hawakutakiwa kuzizima.
Hawakutaka kupoteza muda, walichokifanya ni kumpigia mtu wa nne, huyu alikuwa msichana aliyeonekana kuwa na uwezo mkubwa pia, aliitwa Loveness, tatizo la simu ya msichana huyu, muda wote ilikuwa bize, kila alipopigiwa, simu ilikuwa ikitumika tu.
Hawakuchoka, walichokifanya ni kumpigia simu mtu mwingine, huyu alikuwa wa mwisho, alikuwa kijana ambaye naye uwezo wake ulikuwa mkubwa japokuwa hakuwa amevuka kwenye tatu bora, Vicent. Simu yake iliita na kupokelewa.
“Habari yako,” alisalimia jamaa aliyepiga simu ambaye alishughulika na wadau wote waliokuwa wakiongea Kiswahili.
“Poa, ni aje kaka!”
“Shwari tu. Napenda kukupongeza kwamba umechaguliwa kuigiza tamthilia ya Wicked Love iliyo chini ya Kampuni ya Panorama,” alisikika jamaa huyo. Sauti kubwa ya shangwe ikasikika kutoka kwa Vicent.
“Huleeeee, namshukuru Mungu sana. Kwa hiyo inakuwaje?” alisikika akiuliza Vicent.
“Tunataka uje hapa leo ili kesho asubuhi na mapema mchakato unaanza,” alisema jamaa huyo.
“Leo? Daah! Kaka hatuwezi kufanya hata keshokutwa?” aliuliza Vicent.
“Kwa nini?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nipo Mwanza kwa sasa,” alijibu Vicent.
“Upo Mwanza!! Haiwezekani, hawa washikaji wanakwenda kwa muda, hilo halitowezekana, si unajua Wazungu wanakwenda kizunguzungu” alisema jamaa huyo.
“Bro naomba unisaidie, nilikuwa naitaka nafasi hiyo kinyama.”
“Haiwezekani.”
Jamaa hakutaka kuendelea kuongea na Vicent, alichokifanya ni kukata simu na kuwaelezea Wazungu wale kile kilichokuwa kimetokea. Kila mmoja alisikitishwa na wazo lililotolewa tena mahali hapo, ni kumpigia simu mtu wao wa kwanza ambaye hakupokea simu, Filbert. Alipopigiwa tu, simu ikapokelewa.
“Niambie,” alisema Filbert mara baada ya kupokea simu.
“Tunakupongeza kuchaguliwa kuigiza tamthilia ya Wicked Love iliyo chini ya Kamp.....” jamaa alisema lakini hata kabla hajamalizia, akasikika kelele kutoka kwa Filbert.
“Mamaaa...mamaaa..mamaaaa....nimechaguliwa,” Filbert alisikika.
“Hallooooo....” jamaa aliita.
“Kaka, kaka, niambie, furaha yangu hapa haielezeki, hebu niambie inakuwaje,” alisema Filbert.
“Unatakiwa kuja hapa Atrium Hotel leo hii ili kesho asubuhi mchakato uanze,” alisema jamaa huyo.
“Naweza kuja sasa hivi?” aliuliza Filbert huku kwa kusikika tu, alionekana kuchanganyikiwa.
“Unaweza, tunakusubiri,” alijibu jamaa huyo.
“Sawa,” alisema Filbert na kukata simu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment