IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : Malaika Wa Kifo
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kilikuwa ni kipindi cha mvua za vuli ndani ya Jiji la Dar es Salaam, mara kwa mara mvua kubwa zilikuwa zikinyesha na kukatika. Watu waliokuwa wakiishi mabondeni, kama kawaida walikuwa kwenye mateso makali kutokana na mafuriko ya mara kwa mara yaliyokuwa yakitokea.
Kwa kipindi kirefu sana walikuwa wamekwishaonywa na Serikali kwamba walitakiwa kuhama, wakati mvua zilipokuwa zikinyesha, walisema kwamba watahama lakini mvua zilipokuwa zikimaliza na kiangazi kufikia, wakasahau kwamba walitakiwa kuhama.
Kipindi hiki, mvua hizi zilikuwa zikiendelea kunyesha, tena zilionekana kuwa kubwa kuliko za vipindi vyote. Serikali haikutaka kuongea kitu chochote kile, kwa sababu walikuwa wamekwishawaonya watu hao kuhama mabondeni na kuhamia sehemu salama, wakaamua kuwaacha.
Mvua zile zilisababisha mafuriko, watu wakapoteza mali zao na wengine kupoteza uhai. Hakukuwa hali ya usalama ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kila siku watu walikuwa wakisumbuliwa na mvua hizo.
Shughuli hazikuendelea kama kawaida, wale waliokuwa wakitembeza magazeti, wakawa kwenye wakati mgumu na hata wale waliokuwa wakiuza vitu vinavyotumika hasa katika kipindi cha kiangazi wakaanza kuuza miamvuli.
“Lazima nihame bondeni, haiwezekani,” alisema jamaa mmoja huku akitoa maji chumbani kwake.
“Wewe kama mimi, bondeni si sehemu salama tena,” alijibu jamaa mwingine.
Kila mmoja alikuwa bize akitoa maji ndani kwake, mvua ilileta maafa makubwa huku waandishi wakiripoti kwamba kulikuwa na sehemu nyingine ambapo watu walifariki dunia. Wakati kila mmoja akiwa bize kutoa maji ndani kwake, mvua zikaanza tena.
Edmund, mwanafunzi wa darasa la pili nne aliyekuwa akisoma katika Shule ya Mwalimu Julius Nyerere alikuwa amekaa chini ya mti huku akiwa amekumbatia madaftari yake. Mwili wake ulikuwa umelowa na maji na katika kipindi chote alikuwa akitetemeka.
Japokuwa alikuwa chini ya mti, bado mvua iliendelea kumnyeshea pale alipokuwa amejificha. Hakujua afanye nini kwani kutoka hapo Muembechai shule ilipokuwa mpaka nyumbani kwao, Jangwani kulikuwa na umbali mrefu.
Mvua, kwake ilionekana kuwa sehemu ya mateso makubwa, kila wakati alikuwa mtu wa kulalamika kwa kuzaliwa katika familia ya kimasikini huku akiumia sana kuwaona watoto wenzake hasa kutoka katika familia zilizokuwa na fedha wakiwa katika magari yao na kurudi nyumbani hasa katika kipindi kama hicho cha mvua za vuli.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Japokuwa alikuwa akitaka kurudi nyumbani, lakini bado hali haikuonekana kuwa na usalama. Alikuwa akiishi na wazazi wake maeneo ya Jangwani ambapo kulikuwa maarufu kwa kupatwa na mafuriko kila wakati hasa mvua kubwa zilipokuwa zikinyesha.
Hakukuwa na unafuu, alikaa chini ya mti huku akitetemeka, lakini pia alijua fika kwamba endapo angekwenda nyumbani, asingeweza kulala na kupumzika kwani ilikuwa ni lazima angekuta maji yameingia ndani na baba yake kuwa bize kuyatoa maji hayo.
“Lakini bora niende nyumbani tu, hata kama maji yatakuwa yamejaa, poa tu, nyumbani ni nyumbani kuliko kukaa chini ya mti,” alijisemea Edmund.
Hakutaka kuendelea kukaa chini ya mti ule, japokuwa mvua kubwa ilikuwa ikinyesha, akayashika vizuri madaftari yake na kisha kuondoka mahali hapo. Kila alivyokuwa akizidi kulowanishwa na mvua na ndivyo alivyozidi kuuchukia umasikini ulioukumba familia yao.
Mpaka anafika katika Kituo cha Jangwani, Edmund alikuwa amelowa chapachapa.
Eneo zima la Jangwani lilikuwa limefurika maji, hakujua ni kitu gani alichotakiwa kufanya. Hakutaka kuendelea kukaa barabarani, alitaka kuondoka na kuelekea nyumbani.
Alichokifanya mara baada ya kugundua kwamba mvua hiyo isingeweza kukatika, akaamua kuyavamia maji hayo na kuanza kutembea, yalimfikia kifuani.
“Mungu nisaidie,” alisema Edmund huku akiendelea kupiga hatua ndani ya maji yale huku mvua ikiendelea kunyesha mfululizo.
Sehemu nzima ilionekana kuwa kama mto mmoja mkubwa, kadri mvua zilivyokuwa zikiendelea kunyesha na ndivyo maji yalivyozidi kwenda juu kuzifunika nyumba hizo. Mpaka anafika nyumbani kwao, tayari maji yalikuwa yamefika madirishani na yaliendelea kwenda juu zaidi.
“Mamaaaaa, mamaaaaa,” Edumund alianza kuita.
Nyumba yao ilikuwa imeanza kuzamishwa na maji hayo. Hakukuwa na mtu aliyeonekana zaidi ya mlango kuwa wazi huku maji yakiwa yameingia mpaka ndani. Edmund hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuingia ndani huku akiogelea, hata madaftari aliamua kuyaacha kwa kuona kwamba yalimuongezea uzito.
Masufuria yalikuwa yakielea tu, hakukuwa na mtu yeyote jambo lililomfanya kugundua kwamba wazazi wake waliokuwa wameondoka, naye akaanza kuondoka kurudi barabarani.
Akaendelea kuogelea huku akipiga mbizi, mvua iliongezeka zaidi, Edmund akawa akipiga mbizi kurudi barabarani kwani pale alipokuwa hakukuonekana kuwa salama tena.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa jinsi maji yalivyozidi kuongezeka na kuwa mazito, Edmund akashindwa kabisa kuvumilia, mikono yake ikaanza kuchoka kupiga mbizi, maji yaliyokuwa yakienda katika Mto wa Jangwani yakaanza kumpeleka yalivyotaka, akajikuta akianza kuzama.
“Nakufaaaaa, niokoeniiiii, nakufaaaaa,” alipiga kelele Edmund, wakati huo alikuwa akizamishwazamishwa huku akipelekwa katika mto huo.
Maji yakamzidi nguvu, yakampeleka mbali kabisa, akaishiwa nguvu, akajikuta akianza kuzama. Nguvu za kupiga kelele hakuwa nazo tena na alikunywa kiasi kikubwa cha maji. Hakuwa na cha kufanya, mikono ilimlegea, mwisho wa siku akaona kwamba hiyo ndiyo ilikuwa siku yake ya mwisho, ghafla, akaanza kuona giza, hakufahamu kilichoendelea baada ya hapo.
Mvua zilizidi kuongezeka kila siku, watu waliendelea kupoteza maisha huku wengi wakikosa sehemu za kuishi. Dar es Salaam ikageuka kisiwa, katika kila sehemu ambayo kulikuwa na bonde, maji yalikuwa yamejaa.
Vikosi vya waokoaji vikajiweka tayari na kusambazwa sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuwaokoa watu waliokuwa katika hali ngumu ya kupoteza maisha yao.
Kazi hiyo ya uokoaji ilifanyika mchana na usiku, serikali ilitenga sehemu maalumu zilizotumika kwa watu wasiokuwa na makazi. Dar es Salaam nzima, vilio vilikuwa vimetawala kwani takribani watu laki moja walikuwa wamepoteza makazi yao kutokana na mvua za vuli zilikuwa zikiendelea kunyesha.
“Yule siyo mtu?” aliuliza muokoaji mmoja aliyekuwa amev-alia viatu vikubwa huku akiwa katika mtumbwi mmoja mdogo uliokuwa na waokoaji zaidi ya watano.
“Yupi?” aliuliza muokoaji mwingine.
“Yule kule kwenye matope.”
“Mmh! Hebu twendeni.”
Hapo ndipo waokoaji wale walipoamua kumfuata mtu huyo waliyekuwa wamemuona mahali hapo. Walipobakiza hatua kama thelathini kumfikia, wakateremka kutoka ndani ya mtumbwi ule na kuanza kumfuata.
Kutokana na tope jingi lililokuwepo mahali hapo wasingeweza kumfuata na mtumbwi huo na hiyo ndiyo ilikuwa sababu iliyowafanya kuteremka. Walipiga hatua kwa umakini kwani tope lilikuwa jingi hivyo kama wasingekuwa makini, kazi iliyotakiwa kuwachukua dakika kumi wangetumia hata nusu saa.
“Mmh! Mtoto,” alisema muokoaji mmoja mara baada ya kumfikia Edmund.
“Mzima?”
“Hebu subiri,” alisema muokoaji mmoja na kusikilizia mapigo ya moyo ya Edmund.
“Anapumua kwa mbali sana, anatakiwa kuwahishwa hospitalini,” alisema muokoaji huyo.
Walichokifanya ni kumbeba Edmund na kuanza kumpeleka ndani ya mtumbwi waliokuja nao. Mwili wote wa Edmund ulijawa na matope na hakukuwa na muokoaji yeyote aliyegundua kwamba mtoto waliyekuwa wamembeba alikuwa mwanafunzi aliyevalia sare za shule.
Wakamuingiza ndani ya mtumbwi na safari ya kuelekea katika eneo lililotengwa maalumu kwa ajili kuwahifadhi watu wasiokuwa na makazi kutokana na mvua ambayo bado ilikuwa ikiendelea kunyesha ikaanza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hawakuchukua muda mrefu, wakafika sehemu husika, kwa haraka sana wakamshusha Edmund kutoka mtumbwini na kumpeleka katika sehemu iliyokuwa na turubai, ndani yake ilitumika kama zahanati.
Kwa sababu mapigo yake ya moyo yalikuwa chini sana, kitu cha kwanza kilichofanyika kilikuwa ni kuyashtua mapigo yake ya moyo kwa kutumia Cardiopulmonary Resuscitation Machine (CPR).
Madaktari walijitahidi kufanya kila waliwezalo kuhakikisha Edmund anarudi katika hali yake ya kawaida. Kwa kiasi kikubwa, mashine ile iliweza kufanikisha kile kilichokuwa kikihitajika, mapigo yake ya moyo yakaanza kurudi katika hali yake ya kawaida na kuwekewa dripu.
“Anaendeleaje?” lilikuwa swali alilouliza dokta mkuu wa mahali hapo.
“CPR imesaidia kwa kiwango kikubwa, mapigo yake ya moyo yameanza kurudi katika hali ya kawaida,” alijibu nesi mmoja.
Katika kipindi chote, manesi waliokuwa mahali hapo walikuwa bize wakiwashughulikia watu walioleta ambao walikumbwa na maafa ya mvua hizo za vuri.
Edmund alikaa katika sehemu hiyo kwa takribani masaa mawili na ndipo akarudiwa na fahamu, kitu cha kwanza kabisa, kilikuwa ni kuwaulizia wazazi wake.
“Wazazi wangu wapo wapi?” lilikuwa swali alilouliza Edmund.
“Pumzika kwanza,” alijibu nesi mmoja.
“Hapana. Wazazi wangu wapo wapi?” aliuliza Edmund huku akitaka kuinuka kutoka kitandani pale.
Bado nesi aliendelea kusisitiza kwamba alitakiwa kutulia kwa sababu sindano ya dripu ilikuwa imepita katika mshipa wake hivyo kutotulia kwake kungesababisha matatizo mengine.
Edmund hakutaka kutulia, kitu alichokuwa akikitaka mahali hapo ni kuambiwa mahali wazazi wake walipokuwa. Hakukuwa na mtu aliyekuwa akiwafahamu wazazi wake, aliletwa kambini hapo kama mtu aliyezidiwa kutokana na maafa ya mvua yaliyokuwa yametokea.
“Tulia kwanza, unaitwa nani?” aliuliza nesi huyo.
“Naitwa Edmund.”
“Unaishi wapi?”
“Naishi Jangwani. Dada, wazazi wangu wako wapi?” alijibu Edmund na kuuliza swali.
“Subiri kwanza. Unasema unaishi wapi?” aliuliza nesi yule.
Katika kipindi chote hicho cha maswali nesi alikuwa akijitahidi kumuweka Edmund bize mpaka pale dokta angefika na kuendelea na kazi yake. Edmund hakutaka kutulia, kitu alichokuwa akikitaka mahali hapo ni kujua mahali walipokuwa wazazi wake tu, na si kingine.
Alichokuwa akikitaka nesi ndicho kilichotokea, baada ya dakika kadhaa, dokta akafika mahali hapo, kitu cha kwanza akamjulia Edmund hali yake na mambo mengine kuendelea.
“Amesema anataka kufahamu wazazi wake walipo,” alisema nesi kwa sauti ya chini.
“Amesema anaishi wapi?”
“Jangwani.”
“Mmmh! Hivi kuna mtu kanusurika kweli kule?” aliuliza dokta.
“Cha msingi tukaangalie majina,” alishauri nesi.
“Sawa, ila alisema baba yake anaitwa nani?” aliuliza dokta.
“Subiri.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nesi akamrudia Edmund na kumuuliza jina la baba na mama yake, jinsi walivyokuwa kimuonekano.
“Baba anaitwa Zilikana, mama anaitwa Mary,” alisema Edmund na kuanza kuwaelezea muonekano wa wazazi wake.
Nesi akaondoka huku akimuacha dokta akiendelea na kazi ya kuwahudumia wagonjwa wengine walioletwa ndani ya hema hilo la zahanati.
Edmund alikuwa kimya kitandani pale, uso wake ulikuwa kwenye majonzi makubwa, mawazo yake yalikuwa juu ya wazazi wake ambao mpaka katika kipindi hicho hakujua walikuwa mahali gani.
Hakujua kama walikuwa wamekufa au wapo hai, nesi ambaye alimuuliza juu ya wazazi wake hawakumpa majibu yoyote yale zaidi ya kumvuta dokta na kumwambia maneno ambayo wala hakuyasikia kabisa.
Baada ya nusu saa nesi akarudi, uso wake ulikuwa tofauti na alivyoondoka, alionekana kuwa na majonzi mno, kwa muonekano wake tu, tayari kulikuwa na majibu ya swali alilokuwa akijiuliza Edmund kama wazazi wake walikuwa hai walikufa katika maafa hayo, nguvu zikamuisha, akabaki akitetemeka, muonekano wa nesi yule ulimueleza kabisa kama wazazi wake walikuwa wamekufa.
“Wamekufa?” aliuliza Edmund huku akianza kutoka na machozi, nesi akabaki akichezesha lipsi tu.
Machozi yalikuwa yakimbubujika Edmund, muonekano wa yule nesi ulimfanya kuwa na wasiwasi kwa kuona kwamba kulikuwa na uwezekano wazazi wake walikuwa wamefariki dunia.
Bado nesi yule hakuonekana kuwa katika hali ya kawaida, macho yake yalikuwa yakielezea kila kitu kwamba wazazi wa Edmund walikuwa wamefariki dunia.
Edmund aliendelea kumuuliza yule nesi kuhusiana na wazazi wake lakini bado nesi hakutaka kuongea kitu chochote kile zaidi ya kuzichezesha lipsi zake tu. Dk. Edmund alionekana kugundua kitu, alichokifanya ni kumvuta nesi pembeni, Edmund alikuwa akilia tu.
“Umefanikiwa kuwaona?” aliuliza Dk. Maliki.
“Nimefanikiwa, lakini wamefariki,” alijibu nesi yule.
“Una uhakika?”
“Ndiyo. Kwa jinsi alivyotuelezea, nina uhakika kwamba ni wao,” alijibu nesi yule.
“Hebu twende,” alisema Dk. Maliki na kuondoka na nesi yule kuelekea huko aliposema kwamba aliziona maiti hizo huku akiwa na uhakika kwamba hao walikuwa wazazi wa Edmund.
Baada ya dakika moja, wakafika na moja kwa moja kuangalia majina ya watu waliofariki katika maafa hayo, jina la mzee Zilikana na mkewe, bi Restuta yalikuwa miongoni mwa majina yaliyokuwepo katika karatasi hiyo.
Hawakuridhika, kwa sababu maiti bado zilikuwa mahali hapo, wakaelekea katika chumba kilichotengwa kwa ajili ya kuhifadhia maiti na kuanza kuzitafuta maiti hizo.
Maelezo ya Edmund kuhusiana na muonekano wa wazazi wake ulikuwa sawasawa na muonekano wa maiti mbili zilizoonekana mahali hapo, hakukuwa na tofauti yoyote ile.
“Nina uhakika ndiyo zenyewe,” alisema Dk. Maliki kwa sauti ya huzuni.
“Ila itatupasa tuwe na uhakika zaidi,” alisema nesi.
Walichokifanya ni kuwafuata waokoaji ambao walionekana kumaliza kazi zao na kuwauliza kuhusiana na maiti hizo, sehemu walipokuwa wamezipata.
“Zimetoka Jangwani hizo,” alijibu muokoaji mmoja.
“Una uhakika?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yeah! Tulizitoa kule karibu na ule mto, tena tulizipata zaidi ya nne,” alisema muokoaji huyo.
Mpaka kufikia hapo, tayari walikuwa na uhakika kwamba maiti zile walizokuwa wakihisi kwamba zilikuwa za wazazi wake Edmund, hisia zao zilikuwa kweli, jambo moja likawa limebakia, namna ya kumpa taarifa Edmund.
“Itakupasa ukaongee naye,” alisema dokta yule, alikuwa akimwambia nesi.
“Nahisi nitashindwa dokta, nitaanza kulia hata kabla sijatoa taarifa,” alijitetea nesi.
***
Bado Edmund alikuwa akilia, alikuwa katika kipindi kigumu mno kilichompelekea kuona giza mbele ya macho yake. Mawazo yake yalikuwa yakiwafikiria wazazi wake, uso wa nesi aliyetoka ndani ya chumba hicho ulimtia wasiwasi mkubwa kwa kuona kwamba tayari wazazi wake walikuwa wamefariki dunia.
Wagonjwa wengine waliokuwa katika hali mbaya ambao walikuwa ndani ya chumba kile walikuwa wakimuonea huruma Edmund ambaye muda wote alikuwa mtu wa kulia tu.
Umri wake ulikuwa mdogo mno, kitendo cha kuwapoteza wazi wake huku akiwa hana taswira juu ya maisha yake kilikuwa ni kitu chenye kuumiza mno.
Baada ya dakika kadhaa, Dk. Maliki akaingia ndani ya chumba hicho, kama alivyokuwa nesi yule naye uso wake ulionekana kuwa kwenye majonzi tele, alikuwa akijifikiria namna ya kumpa Edmund taarifa ile ambayo kwa namna moja au nyingine ingemliza sana.
Edmund alipomuona Dk. Maliki, akainuka kutoka kitandani na kuanza kumsogelea, kitu pekee ambacho alikuwa akihitaji kukifahamu wakati huo ni suala zima juu ya wazazi wake tu.
“Una miaka mingapi?” aliuliza Dk. Maliki
“Nina miaka 11,”
“Unasoma wapi?”
“Mwalimu Nyerere,” alijibu Edmund.
Katika kila swali alilokuwa akiuliza Dk. Maliki, alikuwa akimwangalia usoni Edmund. Bado mtoto huyo alionekana kutokuwa na uvumilivu wa kupokea taarifa za vifo vya wazazi wake, hivyo wakaona lingekuwa jambo jema kama wangeonea na ndugu zake.
“Una ndugu hapa Dar es Salaam,” aliuliza Dk Maliki.
“Ninao.”
“Unapafahamu kwao?”
“Napafahamu.”
“Wapi?”
“Kule Manzese.”
“Unaweza kunipeleka?”
“Nitakupeleka, nataka kuwaona wazazi wangu kwanza,” alisema Maliki.
Katika kila kitu alichokuwa akiambiwa kukifanya Edmund alikuwa akitaka kuwaona wazazi wake kwanza, huo ukaonekana kuwa mtihani mgumu kwa Dk. Maliki.
Alichokifanya Dk Maliki ni kumchukua Edmund na kutoka naye nje. Manyunyu bado yalikuwa yakiendelea kunyesha, mvua hazikuwa zikipumzika kabisa, kila wakati ilikuwa ikiendelea kunyesha hali iliyoongeza hofu kwa wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam, hasa wakaao mabondeni.
Safari yao ilikuwa ni chini ya mti mmoja mkubwa, hapo ndipo ambapo Dk Maliki alitaka kumwambia Edmund ukweli kuhusiana na wazazi wake ili hata kama angelia basi asiweze kuwasumbua wagonjwa wengine.
Japokuwa alikuwa na wasiwasi mwingi lakni hakuwa na jinsi, Edmund alitakiwa kupewa taaarifa ukizingatia kwamba hakukuwa na muda wa kupoteza.
“Wazazi wako hawapo,” alisema Dk. Maliki, alionekana kuwa na wasiwasi.
“Wamekwenda wapi?”
“Wamefariki,” alijibu Dk Maliki.
Lilikuwa ni jibu moja tu lililomfanya Edmund kulia, kusikia kwamba wazazi wake wamefariki dunia ilimuumiza. Alishindwa kuvumilia kabisa, akaanza kulia kwa maumivu makali.
Mvua za vuri zilizokuwa zikiendelea ndizo zilizowaua wazazi wake waliokuwa wakiishi Jangwani, moja ya eneo jijini Dar es Salaam, ambalo lilikuwa likiongoza kwa kupatwa na mafuriko hasa kipindi cha mvua.
Edmund aliendelea kulia zaidi, Dk. Maliki alijitahidi kwa uwezo wake weote wa kubembeleza lakini mtoto huyo hakuweza kunyamaza, aliendelea kulia mpaka kulala chini, hakujali matope, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila kitu kilionekana kupotea, ndoto ambazo alijiwekea maishani mwake za kuwa mtu mwenye heshima mkubwa hapo baadae zikapotea kutokana na kufariki kwa wazazi wake. Kila siku Edmund akawa mtu wa majonzi huku akiwa haamini kile kilichokuwa kimetokea.
Hakuwa na budi, hapo, alitakiwa kukubaliana na kila kitu kwamba wazazi wake walikuwa wamefariki dunia na sasa alitaka kuishi bila kuwategemea wazazi.
Alichokifanya mara baada ya kuona hana sehemu ya kuishi, akaelekea nyumbani kwa mama yake mdogo, Amina aliyekuwa akiishi Manzese na kuishi huko. Maisha bila ya wazazi wake hayakuwa ya kawaida, japokuwa mama yake mdogo alimpa kila kitu alichokitaka lakini aliukosa upendo wa mama.
Majonzi hayakupungua, kila siku alikuwa mtu wa mawazo tu akiwafikiria wazazi wake ambao hakuwa pamoja nao. Shuleni, bado alionekana kuwa mpweke, alikwishazoea kukaa na wazazi wake huku baba yake akimfundisha hesabu na masomo mengine, ila kipindi hicho, kila kitu kilionekana kubadilika.
“Rafiki yangu awe daftari na vitabu vya shuleni ili nifikie malengo,” alisema Edmund.
“Ila nitaweza kusoma kweli? Au ngoja nimwambie Sheila awe ananifundisha,” aliendelea kujisemea.
Sheila alikuwa msichana aliyekuwa akisoma naye. Msichana huyu, japokuwa alikuwa mdogo lakini alionekana kutisha kwa uzuri katika siku za usoni, ndiye aliyekuwa akiongoza darasani hapo, alikuwa na uwezo mkubwa darasani kitu kilichomfanya kuongoza katika kila somo walilokuwa wakisoma.
Kwa kuwa karibu na Sheila, Edmund aliona kwamba ingekuwa rahisi kwake kusoma na hatimaye kufaulu mitihani yake, hasa Mtihani wa Taifa wa darasa la nne waliokuwa wakitarajia kuufanya.
“Nataka unifundishe,” Edmund alimwambia Sheila.
“Siwezi kumfundisha mtu.”
“Naomba unifundishe Sheila, nataka na mimi nifaulu,” alisema Edmund.
Japokuwa alikuwa akikataa, lakini kutokana na kuomba sana kwa Edmund, Sheila akakubali kumfundisha mvulana huyo ambaye kwa mtazamo tu hakuonekana kama alikuwa sawa, mawazo yalikuwa yamemkabili.
Hapo ndipo ukaribu wao ulipoanza, mara kwa mara walikuwa pamoja huku Sheila akijitahidi sana kumfundisha masomo mbalimbali shuleni hapo.
Ukaribu wao ukaendelea, kila siku Sheila alikuwa akijitahidi kumfundisha Edmund mpaka pale mitihani ilipofanyika na wote kufaulu vizuri na kuingia darasa la tano.
Urafiki uliongezeka zaidi, walimu wakaonekana kuufurahia kwani kupitia ukaribu huo pia ulimfanya Edmund kufaulu masomo yake jambo lililoonekana kuwa kama msaada mkubwa katika maisha yake.
Mwaka huo ukakatika, wakaingia darasa la sita na mwaka uliofuata wakaingia darasa la saba. Hapo ndipo mabadiliko yalipoanza kutokea, kwanza ukaribu wao ukaongezeka zaidi huku muda wao wa kusoma wakiwa wanautumia kufanyia mambo mengine.
Kifua cha Sheila kikaanza kuchomoza na sauti yake kuwa nyororo iliyoutetemesha moyo wa Edmund kila siku. Kila walipokuwa wakikaa pamoja, mihemko ilikuwa ikiwapata lakini wote walionekana kuwa waoga.
Mioyo yao ikaanza kutengeneza mapenzi, hakukuwa na mtu aliyekuwa radhi kumwambia mwenzake, wote walikuwa wakihofia. Walibaki wakitamaniana kila siku, hata walipokuwa wakisogeleana, kuna vitu vya ajabu walikuwa wakivisikia miilini mwao.
“Mbona unaniangalia sana?” aliuliza Sheila.
“Nani? Mimi? Hapana, mbona sikuangalii,” alijitetea Edmund.
“Mmh! Umekuwa ukiniangalia sana, unanipenda?” aliuliza Sheila.
“Hapana, wala sikuwa nikikuangalia wewe,” alijibu Edmund.
Kila mmoja alijua fika kwamba mwenzake alikuwa akimpenda lakini hakukuwa na aliyekuwa tayari kumwambia mwenzake. Walisoma pamoja na hata wakati mwingine kula pamoja lakini suala la kuwafanya kuzungumzia mapenzi, lilikuwa siri ya kila mmoja.
Siku zikaendelea kukatika huku kila mmoja akiogopa kumwambia mwenzake ukweli. Dalili kubwa ambayo walikuwa nayo katika kipindi hicho ni kuangaliana tu. Pale ambapo hawakuwa pamoja, kila wakati waliyagonganisha macho yao jambo lililompa uhakika kila mmoja kwamba alikuwa akipendwa.
Siku ya kufanya Mtihani wa Taifa wa darasa la saba ilipofika, wote wakaonekana kuwa wapweke kwa sababu walijua kwamba wiki hiyo ndiyo ingekuwa wiki ya mwisho kuonana na hawakuwa na uhakika wa kuonana tena.
“Hivi tutaweza kuonana tena?” aliuliza Edmund huku akionekana kuwa mtu mwenye majonzi.
“Sijui, ila ningependa kuonana nawe,” alisema Sheila.
“Mungu akipenda tutaonana tu. Ila kuna kitu nataka kukwambia,” alisema Edmund, Sheila akajiweka tayari, kitu alichokuwa akikifikiria ni kwamba Edmund angezungumzia kuhusu mapenzi kwani hata macho yake yalikuwa yakionesha hivyo.
“Niambie, kitu gani?”
“Au basi, nitakwambia mitihani ikiisha,” alisema Edmund huku akionekana kuwa na hofu kupita kawaida.
“Jamaniii, niambie.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitakwambia tu.”
Sheila akanyong’onyea, kitu alichokuwa akikitarajia ni kuambiwa ukweli kwamba alikuwa akipendwa na mvulana huyo, kitendo cha kuambiwa kwamba angeambiwa baada ya mitihani kumalizika kilimyong’onyeza.
Siku ya mwisho kabisa ya kufanya mitihani, ilipomalizika, Edmund akaanza kumtafuta Sheila huku akionekana kuwa na shida naye sana. Siku hiyo, ilionekana kuwa tofauti na siku nyingine, Sheila hakuwa akionekana shuleni.
Edmund hakukata tamaa, aliendelea kumtafuta msichana huyo, alipoona kwamba asingefanikiwa, akaamua kumuulizia na kuambiwa kwamba alikuwa katika darasa jingine na wanafunzi wengine, walikuwa wakiagana.
“Ngoja nimfuate,” alijisemea Edmund na hapohapo bila kupoteza muda kuanza kuelekea katika darasa aliloambiwa kwamba msichana Sheila alikuwemo.
Mara baada ya kufika nje ya darasa lile, hakuingia, akabaki nje huku macho yake yakichungulia dirishani kisiri, tena huku akiwa amejificha.
Mkononi alikuwa na barua ndogo aliyokuwa ameiandika kwa mkono wake, kila kitu ambacho alitakiwa kumwambia Sheila alikuwa amekiandika katika barua hiyo. Alipomuona mwanafunzi mwingine akipita, akamuita na kumpa barua ile ili aipelekea kwa Sheila.
Sheila alipoipokea barua ile, mapigo yake ya moyo yakaanza kumdunda kwani picha ya kopa iliyoonekana nje ilionyesha kile kilichokuwa ndani ya barua ile. Alichokifanya, akatoka darasani na kuangalia kama Edmund alikuwepo, alikuwa amekwishakimbia kitambo.
Sheila akasogea pembeni, akawa na shauku ya kutaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kimeandikwa ndani ya barua ile. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimdunda kwa nguvu huku kijasho chembamba kikaanza kumtoka.
“Edmund, umeniandikia maneno gani matamu?” aliuliza Sheila kana kwamba Edmund alikuwa mahali hapo. Alipomaliza kuifungua, akaanza kuisoma huku kila mstari aliokuwa akiupitia, tabasamu pana lilimtawala, barua hiyo ilisomeka hivi....
KWAKO SHEILA
Najua ni kwa kipindi kirefu sana tumekuwa pamoja huku tukiwa karibu kama kaka na dada. Umekuwa msichana wa mfano bora sana kwangu kitu kilichonipa faraja kwa kujua kwamba endapo tungeendelea kuwa pamoja basi kila kitu kingekuwa vizuri.
Kuna mengi ya kukwambia kama rafiki yangu wa karibu, kabla ya kuyaweka wazi, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa msaada ulionipa kwa kipindi kirefu, natumaini nami nitakwenda kufaulu vizuri kama wewe utakavyofaulu.
Ukaribu wetu, ukatufanya kuwa marafiki wa dhati, urafiki ulipoendelea zaidi, kuna kitu nilikihisi moyoni mwangu juu yako, MAPENZI.
Nimekuwa na hisia kali za mapenzi moyoni mwangu, kila siku nimekuwa nikitamani sana kukwambia hili lakini nahisi kwa maandishi ningewakilisha vizuri sana.
Una macho mazuri, umbo zuri na hata sura yako inaonyesha ni kwa jinsi gani unaweza kumteka kimapenzi mwanaume kama mimi. Kila nilipokuwa nikikaa karibu yako, kiukweli mwili wangu ulikuwa ukinisisimka sana.
Ninakupenda na kukuhitaji, hicho ndicho kitu pekee ambacho ninaweza kukisema hata kama ningepata nafasi ya kusimama mbele yako. Najua kwamba unalifahamu hilo kwa sababu kuna mengi nilijaribu kuyafanya ambayo yote kwa pamoja yalikuoneshea ni kwa jinsi gani ninakupenda.
Naomba uwe wangu, nakuahidi kutokukuumiza.
Wako Akupendaye,
Edmund Zilikana.
Sheila akaachia tabasamu zaidi, maneno aliyoyasoma ndani ya barua ile yalimfanya kujisikia vizuri. Alikijua hicho, alijua kwamba alipendwa na Edmund japokuwa mvulana huyo alikuwa mgumu kuzungumza mbele yake.
Kama alivyokuwa akitamani kumwambia Edmund, maneno yote yalikuwa yamekwishaandikwa ndani ya barua ile. Wakati mwingine alijisikia kurukaruka kwa furaha kwani Edmund alikuwa amemrahisishia kila kitu alichotakiwa kukizungumza.
“Ninakupenda pia, upo wapi Edmund?” alisema Sheila huku akiibusu barua ile.
Kwa sababu mitihani ilikuwa imekwishaisha, alichokifanya Sheila ni kuondoka shuleni hapo huku mawazo yake yalimfikiria Edmund ambaye alikuwa ameondoka mapema sana kwani hakutaka kuonana naye kutokana na aibu kubwa aliyokuwa akijisikia moyoni.
Kuanzia njiani mpaka nyumbani, mawazo ya Sheila yalikuwa yakimfikiria Edmund tu. Kila wakati alikuwa akiisoma barua ile aliyoiona kutokumchosha kabisa. Kuanzia siku hiyo, mapenzi yake kwa Edmund yakaongezeka maradufu.
Tayari wanafunzi wa darasa la saba walikuwa wamekwishamaliza masomo yao na ni matokeo tu ndiyo waliyokua wakiyasubiria. Kwa Sheila, maisha yalionekana kuwa magumu mno, alijiona kuonjeshwa asali na mmiliki wa asali kutoweka mbele ya macho yake huku akiwa katika uhitaji wa kuendelea kuionja.
Aliandikiwa barua na Edmund lakini bado kiu yake ilikuwa ni kuonana na mvulana huyo macho kwa macho ili kila kitu alichokisoma katika barua ile basi aweze kukisikia kwa masiko yake kikitoka mdomoni mwa Edmund.
Kwa sababu hakuwa akifahamu alipokuwa akiishi Edmund, alichokifanya ni kuwafuata baadhi ya marafiki zake na kuwauliza juu ya mahali alipokuwa akiishimvulana huyo. Kwa sababu alikuwa akijulikana sana shuleni, hiyo haikuwa ngumu kwa wanafunzi wote kupafahamu kwao.
“Napajua anapoishi, au kama alihama,” alisema Mwajuma.
“Anaishi wapi?”aliuliza Sheila.
“Manzese.”
“Unaweza kunipeleka?”
“Hakuna tatizo.”
Siku iliyofuata wakaanza safari ya kuelekea Manzese, katika kipindi chote hicho Mwajuma alikuwa akimuuliza Sheila juu ya sababu iliyompelekea kumtafuta Edmund lakini alidanganya kwa kusema kwamba alimchukulia kitabu chake na hivyo alikuwa akikihitaji tena.
“Mmmh!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unaguna nini tena?”
“Nahisi kama unanidanganya.”
“Sikudanganyi, kweli tena.”
“Sasa wewe kitabu cha nini na wakati tumekwishamaliza darasa la saba?”
“Kwani sina ndugu wanaendelea kusoma?”
“Sawa, umeshinda.”
Japokuwa alimdanganya Mwajuma juu ya sababu iliyomfanya kumtafuta Edmund lakini kwa kimuemue alichokuwa nacho moyoni akajiona kubeba mzigo mzito na hivyo kuamua kumwambia ukweli kwamba alikuwa kwenye mapenzi ya dhati kwa Edmund.
Hilo ndilo alilokuwa akitarajia kulisikia Mwajuma, uso wake ukajawa na tabasamu, alionekana kufurahishwa na jambo aliloambiwa na Sheila.
“Sasa ulikuwa ukinificha nini?”
“Nilikuwa ikiogopa tu kukwambia.”
Hawakuchukua muda mrefu, daladala ikafika Manzese na kuteremka. Mwajuma ndiye aliyekuwa akizifahamu njia na hivyo kuwa kiongozi wa msafara. Kadri walivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo mapigo yake ya moyo yalivyozidi kumdunda zaidi.
Kuna kipindi alitaka kughairi kumfuata Edmund kwa kujipa matumaini kwamba mvulana huyo angemtafuta mwenyewe kwa kuwa alikwishaanza kumwandikia barua lakini wakati mwingine alijiona kwamba alitakiwa kumfuata kwani endapo angeamua kukaa kimya, alihisi kwamba hata Edmund naye angeweza kukaa kimya.
Baada ya kupita vichochoro vingi, hatimae wakatokea katika uwazi mmoja mkubwa ambapo kulikuwa na nyuma mbili. Wakaanza kuifuata nyumba moja ambayo ndipo Mwajuma alisema kwamba ilikuwa nyumba aliyokuwa akiishi Edmund.
“Tunamuulizia Edmund,” alisema Mwajuma mara baada ya mlango kugongwa na mama yake mdogo Edmund, bi Amina kuufungua.
“Nimwambie anaitwa na nani?”
“Sheila.”
Bi Amina akaondoka mahali hapo na kuelekea ndani, huko akamuita Edmund ambaye mara baada ya kusikia kwamba anaitwa na wasichana wawili akiwepo Sheila, akakurupuka na kuanza kuelekea nje huku mapigo yake ya moyo yakidunda kwa kasi kuashiria kwamba alijisikia woga kukutana na msichana huyo.
Alipofika nje na macho ya wawili hao kukutana, kila mmoja akingiwa na hofu zaidi, Edmund akatamani kurudi ndani huku Sheila akitamani kugeuka na kurudi alipotoka. Huku wakiendelea kuangaliana, Mwajuma alikuwa akicheka tu, wote walionekana kuogopana.
***
Kila mmoja alikuwa amekisubiria kipindi hicho kwa kipindi kirefu na leo hii walikuwa wamekutana. Hakukuwa na mtu aliyeongea kitu chochote kile, kila mmoja alibaki kimya huku akimwangalia mwenzake kwa hofu kubwa.
“Sheila aliniambia nimsindikize mahali hapa,” alisema Mwajuma.
“Sawa, karibuni ndani,” alisema Edmund.
Hakukuwa na mtu aliyetaka kuingia ndani kwa kisingizio cha kutaka kuondoka muda huohuo. Hilo halikuwa tatizo kwa Edmund, kwa sababu macho yake yalimuona msichana aliyekuwa akimpenda kuliko wote, alijisikia furaha moyoni mwake.
Wakaaga na Edmund kuwasindikiza, kila mmoja alijisikia furaha kubwa moyoni mwake, muda wote, Edmund ndiye alikuwa muongeaji mkubwa huku akitaka kuchukua nafasi kubwa ya kumzoea Sheila toka kipindi ambacho alimwambia kwamba alitamani kuwa mpenzi wake.
Mwajuma akaonekana kufahamu kila kitu, ukaribu wake na watu hao ukaonekana kuwabana, alichokifanya ni kuwaachia nafasi wawili hao waanze kuongea mambo ambayo yaliwafanya kukutana siku hiyo.
“Umependeza,” alianza Edmund, japokuwa Sheila alivalia kama alivyokuwa akivalia, siku hiyo alivalia mavazi ya kawaida kama alivyozoea kuvaa lakini kwa Edmund, hakuona sababu ya kukaa kimya zaidi ya kutoa sifa tu.
“Asante,” alisema Sheila.
Safari yao fupi ikaishia katika Daraja la Manzese, wakapanda juu na kwenda kutulia. Hiyo ndiyo ilikuwa sehemu pekee ambayo watu wengi walikuwa wakiitumia enzi hizo kwa ajili ya kuzungumza mambo mbalimbali.
Wote wakabaki kimya, kwa Edmund, huo ulikuwa ni wakati mgumu wa kumwambia Sheila juu ya kile alichokuwa amemwandikia katika barua ile. Alikaa kimya huku kichwa chake kikijifikiria ni kitu gani ambacho alitakiwa kuongea mahali hapo.
Kumwambia ukweli Sheila ana kwa ana lilionekana jambo gumu na kubwa kufanyika wakati huo. Moyoni mwake alikuwa na wasiwasi mwingi, hakuwa akiamini kama kweli agemkubalia kile alichokuwa amedhamiri kumwambia au la.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Uliipata barua yangu?” aliuliza Edmund. Si kwamba hakujua kama Sheila hakuipata barua ile, alijua fika kwamba aliipata kwani hata alipokuwa akikabidhiwa na mtu aliyemtuma, alikuwa akiona kwa macho yake hata kabla hajaondoka.
“Nimeipata, nimeipenda,” alijibu Sheila.
“Umeichukuliaje sasa?”
“Nimeichukulia kawaida.”
“Umekubali?”
“Kukubali nini?”
Edmund akabaki kimya, swali alilokuwa ameuliza lilikuwa jepesi kabisa, alikuwa na uhakika kwamba Sheila alikuwa akielewa kile alichokuwa amemaanisha. Akashusha pumzi ndefu na kuendelea.
“Kuwa msichana wangu.”
“Mmmh!”
“Kuna nini tena?”
“Mbona mapema hivyo?”
“Mapema? Hapana bwana,” alisema Edmund.
Kadri walivyokuwa wakizidi kuongea na ndivyo ambavyo Edmund alivyopata nafasi ya kuiona hali hiyo ya kawaida na mwisho wa siku, hofu yote ikatoka.
Siku hiyo waliongea mengi, kwa mara ya kwanza, Edmund na Sheila wakaanza mahusiano ya kimapenzi. Hicho ndicho kilikuwa kitu kilichosubiriwa na kila mmoja wao. Mbele ya Mwajuma, wawili hao wakaanza uhusiano wa kimapenzi.
Kila siku wakawa watu wa kuonana na kuongea mambo mengi kuhusiana na mapenzi. Japokuwa walikuwa wadogo kiumri lakini kila mmoja aliijua thamani ya mapenzi aliyokuwa nayo kwa ajili ya mwenzake.
Siku zikaendelea kukatika, wawili hao wakaendelea kuwa pamoja zaidi na hata matokeo ya darasa la saba yalipotoka, kila mmoja alifaulu kwa kiwango kikubwa.
“Hivi tutapendana kila siku mpaka kuoana?” aliuliza Sheila.
“Hilo ni jibu, nakuahidi kukuoa”
“Kweli?”
“Niamini. Nakuahidi kukuoa,” alisema Edmund huku akiwa na uhakika juu ya kile alichokisema.
“Ninashukuru mpenzi, nafurahi kusikia hivyo…mwaa,” alisema Sheila kisha kumbusu Edmund shavuni bila kujua ni mambo gani yangetokea katika maisha yao.
****
Wakati Edmund alipoingia kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa, hapo ndipo ambapo alipogundua kwamba alikuwa na kipaji kikubwa cha kuigiza hasa mara baada ya kuigiza igizo la jukwaani lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee katika tamasha maalumu lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili.
Siku hiyo, kila mtu aliyeliangalia igizo lile alilifurahia, wanafunzi waliohudhuria tamasha hilo hawakuamini kama kweli mwanafunzi waliyekuwa naye kila siku, Edmund alikuwa na uwezo mkubwa wa kuigiza.
Edmund akaanza kupata sifa kutoka kwa watu mbalimbali walioliangalia igizo hilo akiwepo Waziri Josephati Bilima aliyekuwa mgeni rasmi siku hiyo. Kwa sababu lililokuwa igizo lililobeba ujumbe uliojaa masikitiko, watu wengi wakaanza kuhuzunika kwani uhalisia aliokuwa akiuigiza Edmund ulimgusa kila mtu.
Wapo walilengwa na machozi lakini pia wapo wale walioshindwa kuendelea kuliangalia igizo hio na kuamua kutoka nje kwani liliwauiza mno. Kwa uigizaji alioufanya Edmund siku hiyo ulionekana kuwa kiboko ambapo wengi walitabiri kwamba angeweza kuwa muigizaji mzuri hapo baadaye.
“Kumbe unajua kuigiza namna ile!” alisema Sheila.
“Najua sana mpenzi, kwani haukuwa ukijua kama najua kuigiza?”
“Hapana, hukuniambia.”
“Basi natumaini utakuwa umejua, nitakuwa kuwa muigizaji mkubwa sana baadaye,” alisema Edmund.
“Kweli?”
“Niamini.” Alisema Edmund.
Kila siku kichwa chake kilifikiria uigizaji tu. Alipenda kuigiza na mara nyingi aliyaona mafanikio makubwa mbele yake. Japokuwa alikuwa akisoma lakini ndoto zake zilikuwa juu ya uigizaji tu.
Mara nyingi alikuwa akitoroka shuleni na kwenda katika kundi la Islamabad lililokuwa Manzese Tip Top kwa ajili ya kuigiza tu. Kila mmoja aliyemuona Edmund akiwa anaigiza akashtuka, hakuamini kama kungekuwa na mtu, tena mwenye umri kama wake ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kuigiza kama aliokuwa nao Edmund.
Kundini hapo, akapewa kipaumbele, hata kundi lilipotaka kufanya tamthilia itakayorushwa katika kituo cha Televisheni cha Global TV. Aliposikia kwamba kulikuwa na hadithi ya tamthilia ilikuwa ikitarajiwa kurushwa katika kituo hicho na yeye alikuwa miongoni mwa waigizaji watakaonekana, Edmund akashtuka, akaingiwa na furaha kubwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimechaguliwa kuigiza kwenye tamthilia, utaanza kuniona kideoni sasa,” alisema Edmund huku akionekana kuwa na furaha.
“Hongera yako,” alisema Sheila.
“Mbona umebadilika, haujisikii kuwa na furaha? Umechukizwa na taarifa hii?” aliuliza Edmund.
“Kawaida tu.”
“Haiwezi kuwa kawaida na wakati umebadilika ghafa, hebu niambie, kuna nini?”
“Hakuna kitu, ila nayahofia mahusiano yetu,” alisema Sheila.
“Usiogope, hakuna atakayeweza kuchukua nafasi yako moyoni mwangu, niamini,” alisema Edmund.
“Una uhakika? Utakuwa na uwezo wa kuwakataa wasichana watakaokufuata kwa sababu ya ustaa wako?” aliuliza Sheila.
“Usijali, sitoweza kuwakubalia.”
“Nihakikishe hilo.”
“Nakuahidi.”
Bado, hiyo haikuonekana kusaidia, hilo halikuonekana kumrudishia furaha Sheila, kila alipokuwa akimwangalia mpenzi wake, alihisi kabisa kwamba anegeweza kusalitiwa.
Alijua fika kwamba kulikuwa na wasichana wengi waliokuwa wakitaka kuwa na mastaa, kitendo cha Edmund kwenda kuonekana runingani, kilianza kumpa wasiwasi Sheila kwa kuona kwamba kipindi hicho kingeweza kuwa kipindi cha mwisho kuwa na mvulana huyo.
“Lakini si mwenyewe amenihakikishia kwamba hatoweza kushawishika kuwafuata wasichana wengine! Hakuna tatizo,” alijipa moyo Sheila lakini kila alipoangalia, hakuwa na uhakika kama Edmund angeweza kukaza mara tu pale wasichana watakapoanza kumfuata.
*****
“Mambo,” alisalimia Edmund, kwa jinsi alivyoonekana tu kipindi hicho, alikuwa kwenye mapenzi ya dhati kwa msichana huyo.
“Poa, u mzima?” alijibu Jamala na kuyainua macho yake kumwangalia usoni Edmund, mvulana huyo akaonekana kuchanganyikiwa.
“Mmmh!” Edmund alitoa mguno, kwa jinsi alivyoonekana Jamala siku hiyo, alionekana mrembo zaidi ya siku nyingine, hata Sheila akasahaulika.
Huo ulikuwa ukweli wenyewe, Edmund alikuwa kwenye mapenzi ya dhati na msichana aliyekuwa mbele yake, Jamala. Japokuwa alifika hapo kwa ajili ya kuongea naye machache lakini muonekano aliokuwa nao Jamala siku hiyo ulikuwa ni wa tofauti kabisa.
Ngozi yake nyeusi iliyokuwa iking’aa ilimpendeza na kumvutia kila mvulana aliyekuwa akimwangalia. Kwa Edmund, msichana huyo alionekana kuwa tofauti kabisa, Macho yake hayakutoka usoni mwa Jamala, alikuwa akimwangalia kwa makini huku akionekana kama mtu aliyekuwa akimfananisha na mtu fulani.
“Jamala...” Edmund alijikuta akiita.
“Unasemaje supastaa?” aliuliza Jamala swali lililomfanya Edmund kuanza kusikia aibu.
“Nani supastaa bwana?” aliuliza Edmund.
“Wewe hapo. Sasa hivi kila tukiwasha televisheni tunakutana na sura yako, na hata tukinunua magazeti, bado sura yako inaonekana kupamba kila ukurasa, tutakuweza wapi bwana,” alisema Jamala, maneno hayo yakamfanya Edmund kuzidi kujishtukia.
“Hapana. Mimi ni mtu wa kawaida, zali tu,” alisema Edmund.
“Sawa, kila mtu anapenda kuwa na zali hilo, hata mimi natamani.”
“Utakutana nalo tu siku moja. Upo bize sana?” alisema Edmund na kumuuliza Jamala.
“Hapana, kuna kitu?”
“Yaap, ningenda kutumia dakika zako ishirini tu,” alisema Edmund, macho yake yaliendelea kumwangalia Jamala kwa umakini, alionekana kama mtu aliyekuwa akimchunguza.
“Mmmh! Mbona nyingi hivyo?”
“Kwa sababu ni maongezi marefu kidogo, ila tutakavyozidi kuzungumza, dakika zitaonekana ndogo,” alisema Edmund.
Jamala hakuongea kitu, akaachia tabasamu lililoonekana kuwa ushindi mkubwa wa kuuteka moyo wa Edmund ambaye alibaki na tabasamu tu. Katika kipindi hicho, hakumkumbuka mpenzi wake aliyekuwa akimpenda kwa moyo wote, Sheila ambaye alimpa ahadi nyingi zikiwepo za kuoana na kuishi kama mume na mke.
“Sawa.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wanafunzi wote wakabaki wakiwaangalia wawili hao, Edmund, mvulana aliyekuwa muigizaji aliyeanza kusikika masikioni mwa wafuatiliaji wa tamthilia alisimama karibu na msichana mrembo mwenye sura ya kitusi aliyekuwa akipendwa na wavulana wengi shuleni hapo, Jamala.
Jamala akainuka na kuanza kuondoka mahali hapo, safari yao ikaishia darasani la kidato cha tano ambapo wakakaa chini huku wakiangaliana tu.
“Aya, niambie,” alisema Jamala kwa sauti ya chini aliyohakikisha haikuwa ikisikika na wanafunzi wachache waliokuwa darasani humo.
“Unapendeza sana siku hizi, nini siri ya mafanikio yako?” alianza Edmund.
“Jamaniii, mbona kawaida tu Edmund!”
“Hapana, upo tofauti sana, hebu jiangalie kwanza, unavutia sana, au haujawahi kusikia mtu akikwambia hivi?” alisema Edmund, muda wote, tabasamu alilokuwa akilitoa aliamini lingekuwa silaha kubwa kwa msichana huyo mrembo.
“Wapo wengi.”
“Sasa umeamini maneno yangu?”
“Hahaha! Acha zako bhana, unataka kuigiza hadi mbele yangu.”
“Jamala, hebu yatazame macho yangu kwanza, naonekana kama naigiza?” aliuliza Edmund, kidogo akalipoteza tabasamu usoni mwake na kujivika uso wa ‘usirisi’.
“Mbona kuna kuna wanawake wengi wapo kama mimi.”
“Najua, ila la msingi yakupasa kujiuliza, kwa nini nimeamua kukwambia wewe.”
“Labda umejisikia tu.”
“Hapana. Kuna kitu.”
“Kitu gani?”
Edmund akashusha pumzi ndefu, tayari alikuwa amefanikiwa kupiga hatua kubwa iliyoonesha mafanikio makubwa. Kila kitu alichokuwa amekizungumza kilionekana kuwa na uzito uliojaa mitego ambapo kila jibu alilokuwa akilitoa Jamala, lilianza kumpeleka kule alipotaka waende.
Edmund hakutaka kuzungumza kitu, alichokuwa akikitaka mahali hapo ni kumpa muda Jamala kuanza kujipa majibu ya swali alilokuwa ameuliza kwa kuamini kwamba majibu yote ambayo angeyaingiza kichwani mwake wakati huo yangekuwa na maana moja tu ya kuwa naye, basi.
“Ninakuhitaji Jamala, hicho ndicho kitu kilichonipelekea kutafuta muda mrefu wa kuwa nawe na kukwambia kuhusu kitu hiki. Ninakupenda na kukuhitaji maishani mwangu,” alisema Edmund kwa ujasiri.
“Hapana. Utakuwa umekosea Ed, unipende mimi?”
“Yaap. Una nini? Sistahili kumpenda mtoto mzuri kama wewe?”
“Hapana. Si mtoto mzuri, hivi wanawake wote wanaokufagilia, umeniona kinyago mimi tu?” aliuliza Jamala.
“Hapana. Wewe si kinyago, na kama ni kinyago, basi ni kile chenye mvuto. Nimetokea kukupenda sana, nimekutafuta kama Edmund na si kama supastaa. Nimekuchunguza kwa kipindi kirefu, nimeona kuwa unastahili kuwa mpenzi wangu. Upo tayari?” aliuliza Edmund mara baada ya kutoa maelezo marefu.
“Subiri kwanza nifikirie.”
“Unataka kufikiria nini tena Jamala? Unataka kwenda kumwambia mama akushauri?”
“Hapana Ed, natakiwa kujifikiria, mapenzi si kitu cha kukurupuka,” alisema Jamala kwa sauti ya chini.
“Kwa muda gani?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hata mwezi.”
“Imekuwa kusubiria majibu ya ajira tena?”
“Ed, naomba unielewe jamaniiiii,” alisema Jamala.
Edmund akabaki kimya, macho yake bado yalikuwa yakiendelea kumwangalia Jamala. Kadri alivyokuwa akizidi kumwangalia na ndivyo alivyozidi kuuona uzuri halisi wa msichana huyo mrembo.
“Kwa hiyo baada ya mwezi?”
“Yaap.”
“Ila naomba unipunguzie Jamala.”
“Wewe unataka lini?”
“Sasa hivi.”
“Hapana. Tufanye wiki moja basi.”
“Sawa.”
“Ila hauna msichana. Usije ukaniletea balaa.”
“Atoke wapi sasa?”
“Mmmh! Supastaa nyie, mnakosaga mademu kweli?”
“Hakuna. Niamini.”
“Sawa. Kuna jingine?”
“Hakuna, labda uniambie siri ya uzuri wako tu,” alisema Edmund na wote kuanza kucheka.
Mpaka kufika hapo, tayari Edmund alijiona kuwa na nafasi kubwa ya kufanikisha kile alichokuwa akikitaka. Bado aliuhisi moyo wake kuwa kwenye mapenzi ya dhati na msichana huyo. Kila siku alipokuwa akifika shuleni, ilikuwa ni lazima amfuate Jamala na kuanza kuongea naye.
Kwa jinsi mapozi waliyokuwa wakiyatumia kila walipokuwa wakiongea, mapenzi hayakuonekana kuwa siri, kila kitu kilijionesha kwamba walikuwa wakipendana. Sheila hakukumbukwa tena, Edmund alimsahau msichana huyo na kusahau kila kitu kilichokuwa kimetokea kati yake na msichana huyo.
“Duuh! Kumbe kuna Sheila pia! Nilikuwa nishamsahau,” alisema Edmund huku akijifanya kushtuka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment