Search This Blog

NYUMBA YA MISUKULE - 5

 





    Simulizi : Nyumba Ya Misukule

    Sehemu Ya Tano (5)



    Lile lijitu likaanza kuwasogelea taratibu, wote wakawa wanatetemeka, bi.Marium na Pendo wakatamani wakimbie ila yule mganga akawazuia, na lile jitu likazidi kuwasogelea, basi yule mganga akatoa usinga wake na kumuelekezea yule msukule huku akiongea maneno anayoyajua yeye, basi ule msukule ukatulia tena,

    MGANGA: Tumeshawapa mlichotaka basi muondoke.

    MSUKULE: Bado hatujashiba vizuri.

    MGANGA: Kwahiyo mnataka nini?

    MSUKULE: Tunakaka nyama ya ng'ombe watano.

    MGANGA: Sawa tutawapatia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Basi ule msukule ukapotea, hapo yule mganga akaanza kuongea na bi Marium,

    MGANGA: Mama, hapa kazi ipo. Itakuwaje sasa?

    BI.MARIUM: Mie siyajui hayo mambo, wewe ndio unayajua. Nisaidie.

    MGANGA: Kuna watu nawafahamu pale machinjioni, sasa nikiwaagiza itakuwaje kwenye kuwalipa.

    BI.MARIUM: Waagize tu, pesa yao mimi nitawapa.

    Yule mganga akawasiliana na watu hao kwa njia ya simu.

    Baada ya muda, ikaja gari ikiwa imebeba nyama nyingi sana na hata waliyoileta walitamani kujua ni kitu gani lakini kwa wakati huo hakupaswa mtu kujua kwani kuna wengine huwa wanaharibu dawa za mganga. Kwani si kila anayefika nyumbani mwako basi anapaswa kuelezwa kinachoendelea, mara nyingine yafaa kujigelesha ili wengine wasijue hadi utakapolitatua tatizo.

    Wakaimwaga ile nyama kwenye kibaraza cha nyumba ile na lile gari likaondoka baada ya kukubaliana malipo na bi.Marium.

    Nyama ilikuwa ni nyingi sana lakini ililiwa kama upepo, maana baada ya dakika kama tano pale kibarazani pakawa hapana kitu kabisa.

    Baada ya muda kidogo yule msukule akatokea tena ila safari hii hakuwa na ghadhabu kama mwanzoni,

    MGANGA: Mmeshiba sasa?

    MSUKULE: Ndio tumeshiba.

    MGANGA: Kwahiyo mnaweza kuondoka sasa?

    MSUKULE: Ndio ila tutaenda wapi?

    MGANGA: Kwani nani amewaweka humu?

    MSUKULE: Bi.Nyuta.

    Pendo na mama yake walijikuta wakihamaki "bi.Nyuta!!" kwani ndio mama mkwe wa bi.Marium na ni bibi yao na wakina Pendo.

    MGANGA: Basi itabidi mrudi huko kwa huyo bi.Nyuta.

    MSUKULE: Kule tupo wengi sana ndio akatupunguzia huku.

    MGANGA: Basi mnatakiwa mrudi kule kule mlikotoka. Na wewe si ndio kiongozi wao?

    MSUKULE: Ndio mimi,

    MGANGA: Basi waongoze wenzio ili mrudi kule mlipotoka.

    Yule msukule akayeyuka, mganga akamgeukia tena bi.Marium,

    MGANGA: Kati ya misukule waliopo, kuna misukule ya kusikitisha kati yao. Nitawazuia kutoka hao misukule wa kusikitisha. Hawa wengine nitawaamuru waondoke sasa.

    BI.MARIUM: (Huku akishikwa na uoga), kivipi bwana mganga?

    MGANGA: Utajua tu na utaelewa kwanini nimesema wa kusikitisha.

    BI.MARIUM: Ila sijaelewa ujue bwana mganga!!

    MGANGA: Hujaelewa nini?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BI.MARIUM: Inamaana bi.Nyuta ni mchawi?

    MGANGA: Hayo mengine utayajua mbele ya safari, kwasasa tufanye hili kwanza.

    Mganga akafanya dawa zake, halafu akawasogeza wote eneo ambalo wataona vizuri yatakayotokea, kwakuwa alishagundua kuwa bi.Marium na mwanae wana imani ndogo sana.

    Yule mganga akanyoosha usinga wake kwenye pembe moja ya ile nyumba, baada ya muda wakaanza kusikia vitu vikilizwa hovyohovyo kwenye ile nyumba. Mara wakaanza kutoka watu wa ajabu ajabu, wengine wanatokea kwenye dari, wengine wanatokea kwenye ukuta wa nyumba ilimradi purukushani tu.

    Mganga akawaambia Pendo na mama yake kuwa wale ndio misukule na wameweza kuwaona sababu ya dawa aliyowapaka.

    Misukule wale wakawa wanatoka na kuelekea kwenye fensi ya ukuta iliyozungushiwa nyumba hiyo, ilikuwa wakifika kwenye pembe wanapotea.

    Bi.Marium alishangazwa sana kuona watu wengi waliosadikika wamekufa na kuwazika kule kijijini wakionekana wanatoka kwenye nyumba yake kama misukule.

    Alibaki akitetemeka na kumuonyesha mwanae, kwa kumtajia majina kabisa, kuwa yule alikufa mwaka jana na yule mwaka juzi. Ila watu hao walikuwa uchi na manywele mengi wakitembea kwa kuruka ruka si kama binadamu wa kawaida watembeavyo.

    Kweli misukule imetolewa ufahamu, yaani hakuna kujitambua kabisa ukishakuwa msukule, akili yako inakuwa si ya kibinadamu tena.

    Basi ndio kwa wale misukule, waliharibu vitu na kuvurugavuruga wakati wakiondoka kwenye nyumba hiyo.

    Pendo hakuamini macho yake alishangaa kuona mambo kama hayo yapo duniani tena yakiwa yamemtokea mwenyewe, siku zote alijua ni mambo ya kwenye filamu tu.

    Kwakweli wale misukule waliharibu kabisa mandhari nzuri ya nyumba ile.

    Mganga akamwambia bi.Marium na mwanae Pendo kuwa misukule iliyobaki humo ambayo alisema inasikitisha ni miwili, msukule mmoja ni mumewe na msukule mwingine ni mwanae ila haiwezekani tena kuwarudisha katika hali ya binadamu wa kawaida.

    Akawaambia kuwa wachague moja, je misukule hiyo ibaki ndani ya hiyo nyumba?? Lakini swala ni kuwa ikibaki itakaribisha misukule mingine. Na je aiache iende kule kwa wenzao wakaendelee kuteseka?? Au je awatoe halafu afanye dawa ili wafe kiukweli wasiwepo tena??

    Kwakweli bi.Marium na mwanae wakapata wakati mgumu wa kutoa maamuzi juu ya hilo swala.

    Na Pia mganga akawauliza kuwa je awatolee hiyo misukule miwili waione ilivyokuwa kwa sasa??

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakawa wanatetemeka na bila kuamini walichoambiwa kuwa mzee Mussa na mwanae Abra ni misukule.

    Wakabaki wanajadiliana tu na hawakuelewa wachague lipi kwanza.

    Wakajifikiria mengi sana na kukosa majibu ya maswali yao.

    BI.MARIUM: Kwahiyo mganga haiwezekani kabisa kuwarudisha katika hali ya kawaida?

    MGANGA: Haiwezekani, ila mngewahi mapema kabla ya kuzika ingewezekana.

    BI.MARIUM: Jamani jamani, bi.Nyuta kwanini aliamua kutufanyia hivi jamani? Yaani kumuua mtoto wake mwenyewe?

    MGANGA: Wachawi hawana ubinadamu kabisa na huona kawaida tu kufanya hivyo.

    Yule mganga akawaambia tena ili wachague, wakaomba waonyeshwe kwanza halafu mganga awaue kabisa.

    Pendo akaamua kumuuliza yule mganga,

    PENDO: Hivi hao misukule waliorudi walipotoka wataishi maisha ya kisukule kwa maisha yao yote?

    MGANGA: Mtu anapokuwa msukule, basi anaishi akiwa vile msukule hadi muda wake wa kufa kweli utakapofika.

    PENDO: Kwamaana hiyo kuna watu huwa tunadhani wamekufa kumbe bado wako hai wanatumikishwa?

    MGANGA: Na mfano mzuri ni kwa baba yako na kaka yako, utakaowaona hivi punde.

    Kusikia hivyo Pendo baridi lilimpata la gafla tena mwili mzima alikuwa akitetemeka.

    Mganga akafanya dawa zake pale walipokuwa na baada ya muda misukule ile miwili ikatoka ndani.

    Kwakweli Pendo na mama yake hawakuamini walichokiona mbele yao, kwani walimuona mzee Mussa na Abra wakiwa uchi kabisa tena wakiwa ni watu wasiojielewa hata kidogo.

    Pendo na mama yake walijikuta wakilia sana huku wamekumbatiana, walijikuta wakikumbuka jinsi mzee Mussa alivyodondoka chooni hadi akapalalaizi hadi alipokufa pia wakakumbuka jinsi Abra alivyoondoka nyumbani kwa hasira halafu akaenda kugonga mpapai na kufa, kwakweli walilia sana kuwaona kuwa wamekuwa ni misukule si watu wa kujielewa tena.

    Pendo hakuamini kabisa alihisi kupagawa, yeye na mama yake walijikuta wakilia hadi kupoteza fahamu.

    Basi yule mganga akamuacha yule msaidizi wake akiwashughulikia Pendo na bi.Marium halafu yeye akaenda kwenye shughuli ya kuwaua kabisa wale misukule wawili.

    Baada ya muda hali ilikuwa shwari kwani mganga alikuwa amerudi na bi.Marium na Pendo nao wakawa wameshazinduka.

    Ila bado walikuwa wakiyatafakari yale mazingira.

    Yule mganga akawafanyia dawa bi.Marium na Pendo na akafanya dawa kwenye nyumba yao.

    Ikabidi wampigie simu mama Sarah awaletee chakula, nae akawaletea wakala na kuoga na kubadili nguo ila bado uoga walikuwa nao kwani hata kuoga hawakuweza kuoga bafuni.

    Nyumba ile iliharibiwa sana na ile misukule mule ndani, sehemu zingine walichana dari pia wakaangusha makabati na baadhi ya vyombo kuvunjika.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pendo na mama yake hawakuweza kulala hapo badala yake wakaenda kulala kwa mama Sarah.

    Baada ya siku chache bi.Marium akaenda kupanga chumba na akaishi humo na mwanae.

    Akatafuta mafundi wakaikarabati ile nyumba yake, akaita wanamaombezi wakaiombea ile nyumba yake halafu akaiuza. Hakutaka tena kuishi kwenye ile nyumba, akaamua kwenda kununua nyumba nyingine kabisa na kuendeleza maisha yao.

    Amina nae akaenda kuwatembelea na kuwapa pole kwa yote yaliyotukia, huku akihuzunika na kusononeka alipopewa habari za kuhusu baba na kaka yao.

    AMINA: Dah nyie yamewapata makubwa sana poleni, mie yale mauzauza ya mwanzo yaliniogopesha sana na ndio yaliyofanya nipakimbie kwetu.

    PENDO: Unajua siku zote nilijua kwenye filamu tu ndio kuna mambo ya ajabu, kumbe ni kweli kabisa mambo haya yapo katika maisha halisi ya binadamu dah!

    BI.MARIUM: Ndio hivyo wanangu, binadamu roho mbaya tumeumbiwa. Ila hadi sasa nashindwa kuelewa kwanini bi.Nyuta alifanya haya.

    Bi.Marium alipanga kwenda kumtembelea mama mkwe kwani bado alikuwa na maumivu makali sana, ila kabla hajaamua kufanya hivyo akaenda kuzungumza na baba mkwe wake kwanza.

    Ambapo akapata wasaa mzuri sana wa kuzungumza nae.

    Akamwelezea kisa kizima na yote yaliyojiri baada ya msiba na kuhusu mganga waliyempeleka.

    BABA MKWE: Marium mwanangu, tatizo ulikuwa hujui tu, ila mimi najua kama mke wangu ni mchawi tena wa muda mrefu sana.

    BI.MARIUM: Baba sasa tutafanyaje? Kwa mtindo huu si atamaliza ukoo mzima?

    BABA MKWE: Hiyo ni kweli mwanangu, ila inapaswa itumike mbinu ya ziada, mke wangu yule ni mchawi sana. Nimekimbia nyumba yangu si kwa kupenda ila uchawi wake umevuka mipaka.

    BI.MARIUM: Inamaana hakuna la kufanya kabisa?

    BABA MKWE: Ndio hakuna.

    Mara Pendo akatokea na kuwaambia,

    PENDO: Babu, mimi najitoa kupambana na uchawi wa bibi.

    BI.MARIUM: Pendo mwanangu utaweza?? Sitaki nikupoteze jamani.

    PENDO: Niamini mama, nitapambana na bibi hata kama itachukua miaka mia ila nitapambana nae tu.

    Pendo akawa ameamua kabisa kupambana na bibi yake. Lilimuuma sana swala la baba yake na kaka yake kuwekwa misukule, aliumia sana na akajiapia kupambana na bibi yake.

    Pendo alijisemea,

    "nashindwa kuamini kama muda wote tulikuwa tukiishi kwenye NYUMBA YA MISUKULE lazima nipambane na aliyewaweka"



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog