Search This Blog

KISIWA CHA HARISHI - 3

 







    Simulizi : Kisiwa Cha Harishi

    Sehemu Ya Tatu (3)



    “Unahakika kuwa nitakuwa salama?”

    “Harishi hatakuja leo. Ameshakuja asubuhi ni mpaka kesho”

    “Ngoja niwaage wenzangu”

    Tukatoka ukumbini. Wenzangu walikuwa wameketi wakizungumza. Nikawambia kwa namsindikiza Yasmin.

    “Ninakwenda kupika, nitampa chakula awaletee” Yasmin akawambia.

    “Yaani utasubiri chakula huko huko?” Mmoja akaniuliza lakini uso wake haukuonesha furaha.

    “Ndio atakisubiri” Yasmin akamjibu.

    Masudi akawatazama wenzake kabla ya kuniambia.

    “Sawa. Sisi tutasubiri”

    Jina lake lilikuwa Masudi. Katika sisi watu wanne tuliobaki, yeye alikuwa ndiye mkubwa kwetu kiumri.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati mimi na Yasmin tunatoka kwenye ile nyumba tukirudi nyumbani kwa Yasmin, Yasmin aliniambia. “Yule kaka uliyezungumza naye anaitwa nani?’

    “Anaitwa Masudi”

    “Naona kama hakufurahi ulivyomwambia tunatoka mimi na wewe”

    “Inawezekana, ni binaadamu. Labda ameona tumewabagua”

    “Mbona wengine hawakusema kitu?”

    “Kila mtu ana mawazo yake. Yule amezoea kutuamrisha kwa sababu kwenye kundi letu yeye ndiye mkubwa kiumri na amekuwa kama kiongozi wetu”

    “Kwa hiyo alitaka anisindikize yeye”

    Yasmin aliposema hivyo nilicheka, na yeye akacheka.

    “Unafikiri nakutania?” aliponiuliza hivyo alitaja jina langu.

    “Hunitanii, unaniambia ukweli. Najua Masudi hakufurahi” nikamwambia.

    Pakapita kimya kifupi kabla ya Yasmin kuniambia.

    “Kisiwa chote hilki kilikuwa kina watu”

    “Wewe uliwakuta hao watu?” nikamuuliza.

    “Wakati Harishi ananileta hapa alikuwa ameshamaliza watu wote. Wengine walihama wenyewe kukimbia kifo”

    “Na kama leo anakuja na kutukuta hivi itakuwaje?”

    “Atakukamata wewe. Atakufyonza damu na ndio ataniuliza wewe ni nani na ulifuata nini hapa”

    “Ina maana wewe hatakuadhibu?”

    “Ananitisha tu pale ninapomuudhi lakini kama atanikuta na mwanaume nadhani ataniadhibu”

    “Lakini hatakufyonza damu?”

    “Hapo siwezi kujua”

    “Inatisha. Ni kwa vile tu umenihakikishia kwamba hatarudi tena leo”

    Tulipofika katika jumba la Yasmin. Tulikaa katika ule ukumbi tukaanza kuzungumza.

    Yasmin akanieleza wazi kuwa alikuwa amenipenda.

    “Wewe ndio ungefaa uwe mume wangu” akaniambia kiudhati.

    “Tayari umeshakuwa mke wa jini, huwezi tena kuwa mke wangu”

    “Jini amenioa wapi? Si ananibaka tu!”

    “Lakini ndio mume wako na amekuleta huku kusudi aweze kukudhibiti”

    “Hakuna kisichokuwa na mwisho. Mwisho wake utafika tu”

    “Inshaallah!”

    “Mimi na wewe tutakwenda kuoana Comoro!”

    Nikatikisa kichwa changu. Niliona Yasmin alikuwa anaota ndoto ya mchana.

    “Yasmin huoni kuwa tuko jela! Unawazia kwenda kuoana Comoro, hapa tutatoka vipi?”

    “Tutatoka tu iko siku. Kila siku mimi naswali kuomba”

    “Angekuwa ni mwanaadamu aliyekuweka hapa tungepambana naye. Lakini jini aliyemaliza kisiwa kizima ni hatari”

    “Usikate tama, usinivunje moyo. Wewe mwanaume!” Yasmin aliposema hivyo alinyanyuka.

    “Ngoja nikapike sasa” akaniambia na kuelekea jikoni.

    Wakati anatembea nilimtazama kwa nyuma. Nguo alizokuwa amevaa zilimpendeza. Kama alivyotueleza mwenyewe nguo hizo alikuwa naletewa na Harishi ambaye huziiba kwnye maduka ya miji mikuwa.

    Yasmin alipofika kwenye mlango wa kuingilia ndani aligeuka na kunitazama. Alipoona nilikuwa namuangalia akatabasamu kabla ya kuingia ndani.

    Nilikaa peke yangu nikiwaza hili na lile. Nilijiambia Yasmin alikuwa msichana mzuri, kikwazo kilikuwa ni lile jini. Kama nafanikiwa kumuoa binti wa rais ni heshima kubwa.

    Baada ya muda kidogo niliondoka nikamfuata Yasmin jikoni.

    “Umenifuata huku?” Yasmin akaniambia.

    “Nataka tusaidiane kupika” nikamwambia kwa mzaha.

    “Si ungekaa tu nikakupikia mume wangu mtarajiwa”

    Nilijua Yasmin alikuwa anajifariji kuniita “mume wangu mtarajiwa” Na mimi sikutaka kumvunja moyo. Kwa upande mwingine mimi pia nilihitaji faraja kutoka kwa Yasmin.

    “Hapana nataka nikusaidie mtarajiwa wangu”

    “Haya nisaidie”

    Nikamsaidia Yasmin kupika huku mizaha na dhihaka zikipita. Kwa mara ya kwanza niligundua Yasmin alikuwa mchangamfu na aliyependa mzaha. Alikuwa akicheka hadi sauti yake ilisikika nje. Alikuwa amesahau kabisa mateso yaliyokuwa yanatukabili sisina yeye.

    “Yasmin unacheka sana, sauti yako inasikika nje” nikamwambia.

    “Kwani nani atatusikia, si tuko peke yetu?”

    “Najua tukompeke yetu lakini usicheke sana”



    “Acha nifurahishe moyo wangu nisife na kinyongo”

    “Sikuwa nikijua kuwa umchangamfu kiasi hicho”

    “Mimi ni mchangamfu sana, sema hili jinni ndilo limeniharibia maisha yangu. Ningeweza kuliua ningeliua”

    “Hata ukiliua utaondoka vipi hapa kisiwani?”

    “Hayo yatakuwa masuala mengine, bora nimeshaliua”

    “Kama boti yetu ingekuwa nzima tungekutorosha tukaenda Zanzibar”

    “Halafu ungenioa huko huko”

    “Upendavyo”

    “Mimi ningependa unioe Zanzibar. Gharama zote angetoa baba yangu”

    “Mimi nisingekuwa na amri zaidi ya kukusikiliza wewe”

    Nilipomwambia hivyo Yasmin alifurahi sana. Chakula kilipokuwa tayari alikipekua sehemu mbili. Sehemu moja ilikuwa yetu mimi nay eye. Sehemu ya pili ilikuwa ya wenzetu.

    “Sasa wapelekee halafu urudi tuje tule” Yasmin akaniambia.

    Alinitilia chakula kwenye kapu nikaondoka. Wakati nakaribia kufka kwenye mlango wa kutokea, nikawaona wenzangu wamenifuata.

    “Tumeona unachelewa, tukapata wasiwasi” Masudi akaniambia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nilikuwa nasubiri chakula na ndicho hiki ninawaletea” nikamwambia Masudi.

    “Sasa na sisi tumeshakuja. Kuna haja ya kwenda tena kule”

    “Tunaweza kula hapa hapa”

    Masudi akawatazama wenzake.

    “Jamani tuleni hapa hapa, au mnasemaje?’ akawauliza.

    “Popote tu tunaweza kula”

    Nikarudi ndani na kuliweka lile kapu la chakula.

    Yasmin alikuwa amesikia sauti zetu akatufuata.

    “Jamani mmekuja huku huku?” akawauliza.

    “Tuliona mwenzetu anachelewa tukapata wasiwasi. Tulidhani labda ameshikwa na Harishi” Masudi akamjibu.

    “Hapana. Alikuwa anasubiri chakula, lakini mnaweza kula hapa hapa”

    Yasmin akaandaa kile chakula kwenye mswala. Kwa vile wenzetu walikuwa wamekuja, tuliona tule pamoja. Yasmin akaleta na kile chakula kingine.

    Tulipomaliza kula tuliendelea kuzungumza pale pale tukiwa pamoja na Yasmin.

    Masudi alikuwa akimtania sana Yasmin huku akimsifia kwa uzuri. Yasmin alikuwa akichekacheka tu na kuficha uso wake uliokuwa umejaa aibu.

    Masudi akaeleza kisa ambacho nilihisi kilikuwa cha uongo kwamba zamani alipokuwa anakaa Mombasa alipendana na msichana mmoja wa Kilamu.

    “Msichana. Alikuwa mzuri huyo. Alinipenda na mimi nilimpenda lakini wanawake wa Mombasa hawaoleki bwana!”

    “Kwanini?” nikamuuliza.

    Wana gharama sana. Huyo msichana wangu alikuwa anaitwa Nargisi. Kila siku alikuwa amechorwa piku, utadhania mwari wa harusi”

    “Sasa huyo atapata kweli muda wa kupika ukimuoa?” nikamuuliza.

    “Ndio maana nilishindwa kumuoa. Nilikuwa nikijiambia huyu msichana sijamuoa yuko hivi, je nikimuoa atakuwaje, piku kila siku…safari haziishi”

    “Mapenzi ya kweli yana gharama” Yasmin akamwambia.

    “Ni kweli lakini gharama ya mwanamke wa Mombasa ni kubwa. Kwanza kunai le gharama ya miraa. Kila siku ni lazima umnunulie kilo moja ya miraa, tena ile miraa safi ya bei ghali”

    “Wacha we!” Yasmin alimwambia kumtia jazba.

    “Halafu wkati wa kula ile miraa ni lazima apate kokakola na chupa ya maji safi pamoja na mfuko mzima wa Big G. Zote ni pesa” Masudi aliendelea kueleza.

    “Na wewe ulikuwa unakula?” nikamuuliza.

    “Mimi nilikuwa nakula lakini si sana. Simalizi hata nusu lakini mwenzangu anaua kilo nzima. Akianza saa tisa hadi saa nne usiku hakuna kitu”

    “Sasa akishakula hiyo miraa itamsaidia nini?” Yasmin akauliza.

    “Anapata handasi” Masudi akamjibu.

    “Handasi ni kitu gani?”

    “Handasi ni kileo cha miraa. Wengine wanakiongezea na kungumanga. Wanasaga kungumanga, ule unga wake wanachanganya na kahawa. Ashiki yake ni hatari!”

    Sote tukacheka. Yasmin ndio alicheka sana.

    “Yaani mwanamke akitoka hapo ni lazima apate bwana!” Masudi aliendelea.

    “Asipopata bwana inakuwaje?” Yasmin akamuuliza.

    “Yaani anapokula miraa na kuchanganya na kahawa ya kungumanga tayari anakuwa na ahadi ya bwana”

    “Kwa hiyo huyo mpenzi wako akishakula ndio mnakutana?’ Yasmin aliendelea kumuuliza. Maneno yalikuwa yamemkolea.

    “Ndiyo maana yake”

    “Unaonaje mapenzi yake?”

    “Ni mapenzi adhimu. Sijapata kuona na sitamsahau yule msichana” Masudi kwa kutaka sifa aliongeza. “Na yeye pia hatanisahau kwani nilikuwa…mh!...hata havisemeki”

    “Sema tu ulikuwaje?” Yasmin akamsisitizia.

    “Mwenyewe alikuwa akiniambia penzi nililokuwa nikimpa hajalipata kwa mwanaume yeyote”

    Hapo tulicheka tena. Lakini mimi nilicheka kwa kujua kuwa Masudi alikuwa akisema uongo kumfurahisha Yasmin. Na kwa kweli nilihisi alitaka kujipependekeza naye ili apendwe yeye.

    “Sasa ilikuwaje mkaachana?’ nikamuuliza.

    “Tuliachana baada ya mimi kurudi Unguja. Mama yangu aliniambia nirudi kwa sababu alikuwa akiishi peke yake”

    “Baba yako alikuwa yuko wapi?” Yasmin akamuuliza.

    “Alikuwa ameshakufa”

    “Nani ambaye hajaoa katika nyinyi?”



    Wenzangu wote walikuwa na wake zao isipokuwa mimi lakini Masudi alisema alioa kisha aliachana na mke wake. Nilichokuwa nakijua mimi ni kuwa Masudi alikuwa na mke wake.

    Sikujua ni kwanini Yasmin alituuliza vile.

    “Kwa hiyo wewe na Masudi ndio hamna wake?” Yasmin akaniuliza.

    “Ninachojua mimi Masudi anaye mke” nilimwambia Yasmin.

    Kauli ile ilimkera Masudi.

    “Nina mke mimi?” Masudi akaniuliza kwa ukali kidogo.

    “Unaye!” nikamwambia kwa mkazo.

    “Mke si nilishamuacha?. Au wewe ulikuwa hujui?”

    “Mimi najua watania tu lakini mke bado unaye”

    “Basi na yaishe. Mimi niliuliza tu kutaka kujua. Kama unaye mke au huna hakuna tatizo” Yasmin akaingilia kati.

    “Huyu bwana mdogo anapenda sana kuniingilia!” Masudi akaunguruma.

    Nikaamua kunyamaza.

    “Nimesema yaishe jamani. Ngoja tulete karata tucheze”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yasmin alitumia hekima kuyageuza yale mazungumzo akaenda kuleta karata, tukawa tunacheza.

    “Hivi hizi karata ulikuwa unacheza na nani?” nikamuuliza Yasmin wakati tunacheza.

    “Ninacheza na huyo aliyezileta”

    “Harishi?”

    “Ndiye huyo huyo. Anapoona nimepooza ananiambia kalete karata”

    “Anajua kucheza karata?” akaulizwa na Masudi.

    “Anajua. Hawa majini ni kama watu tu. Tofauti yetu ni ndogo sana. Wanafanya mambo mengi wanayofanya binaadamu”

    Mazungumzo ya Harishi yalitufanya tukose amani. Yalitukumbusha wenzetu waliouawa. Mwenzetu mmoja lakini si Masudi akatuambia.

    “Tuondoke twende kule tulikohamia”

    “Chukueni hizo karata mwende nazo. Mtakwenda kucheza huko huko” Yasmin akatuambia.

    Ilibidi tuondoke twende katika ile nyumba lakini Yasmin tulimuacha.

    Tulipofika tuliendelea kucheza karata. Baadaye sote tulipitiwa na usingizi tukalala.

    Tuliamshana jioni tukaamua tutoke twende tukatembee tembee. Tulizunguka sana katika kile kisiwa. Tulienda pia kuliangalia jahazi letu. Tuliporudi jua lilikuwalimeshakuchwa.

    Tulimkuta Yasmin akitusubiri. Alikuwa ametuletea chakula cha jioni.

    “Mnatoka wapi?” akatuuliza.

    “Tulikwenda kutembea tembea kidogo” Masudi akamjibu na kuongeza “Kukaa tu kunachosha”

    “Umetuletea chakula?” nikamuuliza Yasmin.

    “Nimewaletea kabisa. Ikifika usiku sitaweza kuja huku. Harishi anaweza kuja wakati wowowte” Yasmin alituambia na kutuwekea chakula hicho juu ya meza.

    “Ngoja nikusindikize” Masudi akawahi kumwambia Yasmin. Nilijua alitaka kunipiku mimi kwani alijua mimi ndiye ningemsindikiza.

    Yasmin akakubali kuondoka na Masudi. Kwa upande wangi kitendo kile cha Masudi nilikiona kama ulimbukeni uliopitiliza na kutaka kujipendekeza kwa Yasmin.

    Walipoondoka sisi tulikaa barazani mwa ile nyumba hadi giza likaingia.

    “Mbona masudi harudi?” Tukawa tunaulizana.

    Kusema kweli kitendo chake cha kuchelewa kurudi kilinikera. Nikaamua nimfuate peke yangu nijua alikuwa anafanya nini muda wote huo.

    Nikaenda huku nikiwa na hasira. Nilipofika sikuingia ndani. Niliamua kufanya upelelezi kwa kuchungulia kwenye madirisha.

    Wakati nachungulia niliana kusikia sautiya Yasmin ikiwa katika dhihaka, mwenyewe sikumuon. Nilibadilisha dirisha na ndipo nilipowaona wote wawili. Masudi alikuwa akikimbizana na Yasmin mle ndani kam waliokuwa wakicheza. Wakati mwingine Masudi alimkamata Yasmin na kuanguka naye chini akiwa amemshika kiuno.

    “Kumbe wana mchezo huu, ndio maana amesahau kurudi” nikajisemea kimoyo moyo.

    Licha ya moyo wangu kuuma nilijiambia chaguo la Yasmin ni mimi, Masudi alikuwa akijipendekeza tu.

    Macho yangu yaliwashuhudia wakiwa wamelala chini. Masudi alikuwa kama akibembeleza kitu kwa Yasmin. Yasmin alikuwa ametulia akimsikiliza.

    Sikuweza kufikiria chochote zaidi ya kuhisi kuwa Masudi alikuwa akimtongoza Yasmin na alikuwa akinifitini mimi.

    Sikutaka tena kuuona upumbvu wake. Nikaamua kuondoka kwani usiku ulikuwa unazidi kushamiri.

    Yasmin haweza kumkubali Masudi, Yasmin amenipenda mimi, nilijiambia kujifariji wakati naondoka.

    Nilirudi kwa wenzangu huku nikiuzuia moyo wangu usitaharuki kutokana na kitendo kile nilichokiona kwa Masudi kumkumbatia Yasmin.

    “Umemkuta?” Wenzangu wakaniuliza.

    “Sikufika” nkawadanganya. “Nimeamua kurudi njiani, naona usiku mwingi huu”

    “Au twendeni sote?” Mmoja akaniuliza.

    “Tumsubirini tu hapa hapa”

    Sikutaka kuwambia ukweli kuwa nilimkuta akifanya vitendo vya kipuuzi. Nilihisi wangeweza kuja kumwambia mwenyewe halafu kwa akili za Masudi tunaweza kugombana bure.

    Tukakaa kumsubiri hadi saa tatu. Tulipoona hatokeai tuliamua kula chakula na kumbakishia chake.

    Nilikuwa nimebaki na wenzangu wawili Shazume na Haji. Kwa upande wangu nilishakijua kilichokuwa kinamchelewesha Masudi lakini wenzangu walikuwa na wasiwasi kwamba huenda Masudi amepata matatizo.

    Walikuwa wakisisitiza kuwa twende tukamuangalie.

    “Kutoka usiku huu si vizuri” nikawambia. “Acheni tungoje kesho asubuhi tutakwenda kumuangalia”





    “Kaka Masudi ana matatizo sana. Kwanza hatuelewi ni kitu kilichomfanya amsindikize yule msichana” Shazume akasema.

    “Tusiwe na wasiwasi naye sana. Huenda mwenyewe ameamua kubaki” nikawambia wenzangu.

    “Atabakije kule wakati anajua kuwa lazima Harishi atakuja?” Haji akauliza.

    “Kila mtu ana akili yake jamani tusimuhukumu” nikawambia Shazume na Haji.

    “Atajua mwenyewe, shauri yake” ilikuwa sauti ya kukata tamaa ya Haji.

    Baada ya kujadiliana kwa kirefu tuliamua kwenda kulala. Kila mtu aliingia kwenye chumba chake.

    Unapofika wakati wa kulala mawazo hubadilika. Fikira zote huondoka na kichwa kujaa mawazo ya Harishi.

    Nilikuwa na hakika kuwa sikuwa mimi peke yangu bali wenzangu wote walikuwa na mawazo kama yangu. Likini hatukuwa na lolote la kufanya zaidi ya kukubali matokeo yatakayotokea usiku huo kwa Masudi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usiku ule tulilala na kuamka salama ingawa tulilala kwa mashaka.

    Lakini Masudi hakuwa miongoni mwetu. Tukadhani kwamba atatokea wakati ule wa asubuhi baada ya kushindwa kurudi usiku. Lakini tulikaa hadi majira ya saa bila kumuona yeye wala Yasmin.

    “Wenzangu mnaonaje twende tukamuangalie Masudi au tuendelee kumsubiri?” nikawauliza wenzangu.

    “Kwenda kumuangalia ni jambo zuri lakini tunaweza kukutana na Harishi” Haji akasema.

    “Nina wasiwasi kwa sababu Yasmin pia amekaa kimya. Kwa kawaida muda huu angekuwa ameshakuja” nikawambia wenzangu.

    “Hatuwezi kujua lolote linaweza kuwa limetokea” Shazume naye akasema.

    “Basi tusiende, tuendelee kusubiri hapa hapa hadi atakapokuja Masudi au Yasmin” nikawambia.

    Wakati tunaendelea kujadiliana tulimuona Yasmin akiingia. Sote tukageuka na kumtazama. Kitu kilichotushitua si tu alikuwa peke yake bali macho yake yalikuwa mekundu yaliyoonesha alikuwa analia.

    Akatusalimia na kutuambia kuwa amepatwa na fadhaa.

    “Kwanini?” akatuuliza.

    “Kaka yenu Masudi hakutumia busara hata kidogo” Masudi alituambia huku akitikisa kichwa kusikitika.

    “Kwanini hakutumia busara?” nikamuuliza huku nikifikiria mengine. Nilifikiria ama Masudi alitaka kumbaka Yasmin au alimbaka kwani ile hali niliyowakuta nayo usiku uliopita haikuwa ya kawaida.

    “Kama yeye amenipenda mimi kama alivyoniambia mwenyewe ni sawa lakini kitendo alichokifanya si kizuri kwa sababu anajua mimi nimemilikiwa na Harishi”

    Hapo nilijua moja kwa moja kuwa Masudi amembaka Yasmin na ndio sababu alikuwa analia.

    “Kwani amefanya nini?” nikamuuliza.

    “Ungetueleza alichofanya” Haji naye akamwambia.

    “Jana usiku nilimwambia arudi huku, ulikuwa ni usiku. Lakini alikataa kurudi, akataka kulala na mimi. Nilimsihi sana arudi lakini aligoma kabisa, tena alitaka alale na mimi chumba kimoja. Aliniambia ananipenda” Yasmin akatueleza.

    “Masudi ni kaka yetu lakini ana matatizo sana” Shazume akadakia.

    “Sasa ikawaje?” na mimi nikauliza kwa pupa.

    “Nilimuachia alale. Yule ni mwanaume nisingeweza kumzuia”

    “Ulilala naye chumba kimoja?” nikamuuliza.

    “Nilimuomba sana akalale chumba kingine kwa usalama wake. Nilimwambia Harishi akija na kukukuta atakuua. Akakubali kwenda kulala chumba kingine”

    “Sasa nini kimetokea?” Shazume akauliza.

    “Harishi alikuja muda ule ule akamkuta ukumbini anazungukazunguka, akashikwa”

    Alipofikia hapo Yasmin alianza kulia.

    “Sasa ameuliwa?’ nikamuuliza.

    “Harishi aliacha mtu siku gani?” Yasmin akaniuliza.

    Mimi na Haji na Shazume tulitazamana tukiwa tumeacha midomo wazi.

    “Aliyataka mwenyewe!” Yasmin akasema.

    “Ni kweli aliyataka mwenyewe, kifo kilikuwa kinamuita” nikamuunga mkono.

    “Angekuja kulala na wenzake pengine angenusurika” Yasmin aliendelea kutuambia.

    “Mbona hukuja mapema kutuambia?” nikamuuliza.

    “Harishi ameondoka sasa hivi. Jana usiku alipokuja alikuwa amelewa na alipomuua Masudi hakuondoka tena hadi hii asubuhi”

    “Kumbe majini pia wanalewa?”

    “Wanalewa kama watu. Harishi analewa sana”

    “Hiyo pombe anaipata wapi?”

    “Sijui mwenyewe”

    “Na anapokuta mtu mle ndani anakuuliza ni nani?”

    “Anaua kwanza halafu ndio anauliza. Mimi humwambia kwamba ni wavuvi wameingia kwa bahati mbaya. Lakini kama angenikuta nimelala naye angejua ni mwanaume wangu”

    “Angekuua?”

    “Sijui ingekuwaje?”

    Pakapita kimya cha sekunde kadhaa. Sote tulikuwa tunamkumbuka kaka yetu Masidi.

    “Mtanisamehe sikuwaletea chai. Nilikuwa nimetaharuki sana” Yasmin akatuambia baadaye.

    “Misiba kama hii. Kila siku anakufa mtu. Hamu ya kula pia inapotea” nikamwambia.

    “Nyinyi mtabaki huku huku mjaribu bahati zenu. Mnaweza kusalimika”



    “Tutakufa kama wenzetu. Sidhani kama tutapona kwa maana tulikuwa watu saba, sasa tumebaki watatu” nikamwambia Yasmin.

    “Msikate tama ndugu zangu. Kama ni kufa tutakufa sote. Hamuwezi kufa mkaniacha mimi”

    Nilimuona Haji akijifuta machozi.

    “Usilie ndugu yangu. Ushinde moyo. Safari yenu bado ni ndefu” akaambiwa na Yasmin.

    Shazume akageuza uso na kunitazama.

    “Nina tama ndogo sana kama tutapona” akaniambia.

    Sikumjibu kitu. Yasmin akanyanyuka.

    Nitawatayarishia japokuwa uji mchangamke” akatuambia.

    “Sawa” nikamjibu.

    “Naenda kuwapikia halafu nitawaletea”

    “Kama tutakusumbua ninaweza kuja kuuchukua”

    “Harishi hatakuja tena leo. Mnaweza hata kuja nyote”

    Nikawatazama wenzangu.

    “Eti mnasemaje?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Akituletea huku itakuwa bora” Haji akasema.

    “Tutakuwa tunamsumbua. Tungekwenda tu kwa vile ametuhakikishia kuwa leo hakuna tatizo” nikawambia wenzangu.

    “Haya twendeni ila tusikae sana” Shazume akasema.

    Tukaondoka pamoja na Yasmin kuelekea katika lile jumba la Harishi.

    “Tangu mmekuja nyinyi nimejisikia kuchangamka sana” Yasmin alituambia tukiwa njiani.

    “Kikwazo chetu kikubwa ni huyu Harishi. Kama si yeye tungekuwa na furaha sana” nikasema.

    “Roho zetu sasa zina wasiwasi. Kila siku mmoja wetu anakufa. Tulikuwa watu saba, sasa tumebaki watatu” Haji akalalamika.

    “Ni kweli Haji lakini kama nyinyi mtakuwa makini mnaweza kusalimika” Yasmin akatuambia.

    “Yasmin unatuambia ukweli? Tutasalimikaje? Hata kama hatutauawa na Harishi tutakaa katika kisiwa hiki hadi lini?” nikamuuliza Yasmin.

    “Kwani mimi nitakaa hadi lini?” Yasmin akatuulisa. Sauti yake ilikuwa imebadilika.

    “Wewe mwenyewe umeshajitolea” nikamjibu.

    “Kwa sababu sijipendi?”

    “Hapana, si hivyo”

    “Basi mimi na nyinyi ni sawa tu. Kama mimi nimejitolea na nyinyi mjitolee kama mimi. Muwe tayari kwa lolote”

    “Sisi tumeshajitolea Yasmin. Hatuna la kufanya” nikamwambia Yasmin aliyekuwa amekasirika kidogo.

    “Tunaona juhudi zako Yasmin” nikaendelea kumwambia. “Kama si wewe kutupokea kwa nia moja tungekuwa tumeshakufa kwa kuhangaika na njaa.

    Tulipofiak kwenye lile jumba tulipumzika ukumbini. Yasmin alituletea karata kisha tukaenda kupika uji. Uji ulipokuwa tayari Yasmin alituletea tukanywa. Huji huo ulikuwa umechanganywa na asali.

    Tuliposhiba Yasmin aliondoka tena kwenda kupika chakula cha mchana. Sisi tuliendelea kucheza karata, tulipochoka tukalala hapo hapo. Yasmin ndiye aliyekuja kutuamsha.

    “Wenzangu kumbe mmelala?” akatuuliza.

    “Ah! tumepitiwa na usingizi bila kujijua” nikamwambia na kumuuliza “Umeshapika?”

    “Nimeshapika, kwani mna njaa niwapakulie?”

    “Bado kwanza. Tusubiri kidogo”

    “Naona mko wachovu sana. Twendeni bahari mchangamke kidogo”

    Kwa vile hatukuwa na la kufanya tukakubaliana na wazo La Yasmin la kwenda baharini. Kisiwa hicho kilikuwa na fukwe nzuri zenye mchanga mweupe.

    Tukiwa kwenye fukwe za kisiwa hicho tulibuni michezombalimbali ya kujichangamsha ikiwemo kukimbizana. Mwisho tuliamua kujitosa kwenye maji na kuogelea tukiwana nguo zetu.

    Yasmin alikuwa hodari wa kuogelea. Alituambia alipokuwa Comoro kila siku za jumapili alikuwa akienda kuogelea na ndugu zake.

    Tulipochoka kuogelea tulikaa kwenye fukwe hadi tukakauka maji. Tukaondoka kurudi katika jumba la Harishi

    Yasmin alikwenda kuoga maji baridi. Alipomaliza na sisi tulikwenda kuoga. Hatukuwa na nguo za kubadili.

    Yasmin alitupa mashuka tukajifunga. Zile nguo zetu tulizifua na kwenda kuzianika nje kwenye jua.

    Tulipomaliza kuanika nguo ndipo Yasmin alipotuandalia chakula, tukala. Wakati tunakula alituambia kuwa tunaweza kuendelea kushinda hapo kwake hadi jioni lakini Haji akapinga ushauri wake na kutaka tuondoke tukimaliza chakula.

    Baada ya chakula tulikubaliana kuwa turudi katika ile nyumba tuliyohamia. Tukamuaga Yasmin na kuondoka.

    “Sasa wenzangu mna ushauri gani, hali ya hapa ndiyo kama hii tunayoiona?” nikawauliza wenzangu mara tu baada ya kufika kwenye ile nyumba

    “Kwani wewe una ushauri gani?” Haji akaniuliza.

    “Nia yetu sote ni kuondoka katika kisiwa hiki. Sasa nataka tujadili njia itakayotuwezesha kuondoka. Ni vizuri kila mmoja akatoa wazo lake alilonalo” nikasema.

    “Ni kweli ulivyosema lakini tunajikuta tumekwama, tusingekuwa hapa hadi leo” Shazume akatuambia.

    “Kwa hiyo hatujui tutaendelea kukaa hapa na Yasmin hadi lini?” nikauliza.

    “Ukweli ndio huo” Haji akanikubalia.

    Nikatikisa kichwa changu kusikitika, baada ya hapo sote tukawa kimya.





    Yalipofika majira ya saa kumi na mbili jioni Yasmin akaja.Alikuwa ametuletea chakula cha jioni. Ulikuwa ni wali ule ule tuliokula mchana. Tukakiweka chakula hicho kusubiri usiku.

    Yasmin akataka nimsindikize arudi. Nikawambia wenzangu “Namsindikiza Yasmin”

    “Usije ukachelewa kurudi. Kumbuka usiku umekaribia” Shazume akaniambia.

    “Sitachelewa” nikamjibu.

    Tukaondoka na Yasmin. Tukiwa njiani Yasmin alinitazama machoni mwangu kisha akaniambia.”Nimefurahi sana leo kuwa peke yetu mimi na wewe”

    “Kwanini?” nikamuuliza.

    “Tangu juzi hatujapata nafasi ya kuwa pamoja peke yetu. Mara nyingi unakuwa na wenzako. Jana jioni nilitaka kukwambia nisindikize lakini marehemu Masudi akawahi yeye. Sikuweza kumkatalia. Najua roho ilikuuma na mimi pia iliniuma” Yasmin akaniambia.

    “Unajua jana niliwafuatilia nikawakuta mnafukuzana ndani. Kuna wakati marehemu alikushika kiuno mkaanguka chini pamoja”

    Nilipomwambia hivyo Yasmin alinywea.

    “Kumbe ulikuja kutuchungulia?” akaniuliza.

    “Nilikuja, nilipouona mchezo wenu nikaamua kurudi”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Si mchezo wetu. Masudi ndio alikuwa analazimisha. Alikuwa akinitaka kimapenzi nikamkatalia” Yasmin aliniambia.

    “Basi tusimseme sana kwa sababu ameshakufa lakini nilishituka”

    “Naomba unisamehe kwa hilo kama limekuudhi”

    Nikanyamaza kimya.

    “Umeshanisamehe?” Yasmin akaniuliza huku akinitazama machoni mwangu. Alinitazama kwa macho ya huruma sana.

    “Kwani wasiwasi wako ni wa nini?”

    “Nataka unisamehe!” Yasmin akasisitiza.

    “Nimekusamehe”

    “Sasa tusizungumze tena habari hiyo. Tuzungumze yanayotuhusu mimi na wewe. Kama tutafanikiwa kuondoka katika kisiwa hiki utanioa?”

    “Wewe ndio uniambie mimi kama utakubali kuolewa na mimi”

    “Mimi niko tayari hata sasa hivi”

    “Unadhani wazazi wako watakubali?”

    “Watakubali”

    “Ujue kuwa wewe ni binti wa rais na mimi ni mtoto wa kimasikini”

    “Kusema hivyo si sahihi. Sasa hapa tulipo mimi na wewe tuna tofauti gani?”

    “Kwa hapa tuko sawa ila ukirudi kwenu wewe utakuwa mwana wa rais”

    “Huo ni ufinyu wa mawazo ya binadamu. Binaadamu wote ni sawa. Mfano halisi ni wa hapa tulipo. Umesema tupo sawa, basi tutakuwa sawa popote. Hata kama wewe ni mtoto wa kimasikini lakini nimekupenda, utakataa?”

    “Labda wewe unikatae mimi”

    “Una majibu yasiyoniridhisha. Kwanini huniambii kuwa unanipenda na utanioa. Mimi nataka utamke hivyo”

    “Nimekupenda na nitakuoa”

    Yasmin nilipomwambia vile alitabasamu. Nilihisi alikuwa akijaribu kuufariji moyo wake uliokosa mapenzi kwa muda mrefu.

    “Yasmin unaweza kusema maneno hayo hapa kwa vile hatuna matumaini ya kupona. Lakini kama tutafanikiwa kuondoka hapa unaweza kubadilika na kuniona mimi kama takataka”

    “Nakuhakikishia kaka yangu mpenzi sitabadilika. Mimi si kinyonga”

    “Tuombe tuokoke katika balaa hili lililotukabili”

    “Ishaalah tutaokoka. Tena wewe ndio utaniokoa mimi”

    “Sio wewe uniokoe mimi?”

    “Mimi nataka wewe uniokoe mimi”

    “Basi ishaala itakuwa hivyo unavyotaka”

    “Nikuimbie nyimbo?”

    “Niimbie”

    Yasmin aliacha kutembea akasimama mbele yangu akiwa amenigeukia mimi. Kitendo hicho kilisababisha na mimi nisimame. Akapeleke mikono yake kwenye mabega yangu.

    “Mimi ni nani wako?” akaniulza. huku akinitazama machoni mwangu.

    “Wewe ni mpenzi wangu” nilijua kuwa alikuwa anataka jibu hilo.

    Nilipomjibu hivyo alitabasamu na kuishusha mikono yake mabegani mwangu na kugeuka.

    “Sasa ngoja nikuimbie” akaniambia huku tunaenda.

    Akaimba wimbo mzuri kwa lugha ya Kikomoro. Wakati akiimba alikuwa akitingisha tingisha kichwa chake kufuatia mawimbi ya sauti yake. Wakati akiimba alikuwa akitia mziki kwa mdomo. Alionekana kuwa hodari sana wa kuimba na kutia mziki. Wimbo huo ulikuwa unavutia ingawa sikujua tafsiri yake.

    Alipomaliza kuimba alinitafsiria kwa Kiswahili. Akaniambia “Ndege wawili dume na jike wamepotea juu ya bahari. Hawajui watokako wala waendako. Wanalia swi! swi! swi!”

    “Wamesafiri mchana kutwa bila kupata mahali pa kutua. Sasa jua limekucwa na giza linaingia. Hawataweza kusafiri usiku. Wanalia swi! swi! swi!”

    Japo niliufurahia wimbo huo tafsiri yake ilinisikitisha.Nikahisi kama ndege wawili hao walikuwa ni mimi na yeye.

    “Kumbe Yasmin unajua sana kuimba!” nikamwambia.

    “Hapana, najaribu tu”

    “Si kujaribu, unajua”

    “Kweli eh?”

    “Umeniburudisha sana”

    “Ukinioa nitakuwa nakuimbia kila siku”

    Tulikuwa tumeshafika kwenye lile jumba analokaa.

    Nikasimama kwenye mlango.

    “Mimi sitaingia ndani” nikamwambia.

    “Kwanini?” Yasmin akaniuliza.

    “Si nimekusindikiza tu”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ukinisindikiza ndio huingii ndani, mbona siku nyingine unaingia?”

    “Yasije yakanikuta yaliyomkuta Masudi”

    “Mimi naamini wewe huko kama Masudi lakini kama umeamua uwahi kurudi, unaweza kurudi na nakutakia usiku mwema. Tutaonana kesho.

    “Asante. Usiku mwema na kwako”

    Nikamuacha Yasmin amesimama akinitazama. Mimi nikarudi kule nyumbani tulikotoka. Nilirudi kwa mwendo wa haraka haraka ili kiza kisinikute njiani kwani jua lilikuwa limekuchwa sana.

    Nilijikuta nikiwa na furaha na mwenye matumaini kutokana na maneno ya Yasmin. Upendo aliouonesha kwangu ulitosha kunipa hamasa ingawa tulikuwa katika hali ngumu.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog