Search This Blog

KISIWA CHA HARISHI - 4

 







    Simulizi : Kisiwa Cha Harishi

    Sehemu Ya Nne (4)



    Nilijikuta nikiwa na furaha na mwenye matumaini kutokana na maneno ya Yasmin. Upendo aliouonesha kwangu ulitosha kunipa hamasa ingawa tulikuwa katika hali ngumu.

    Nilipofika katika ile nyumba niliwakuta wenzangu tayari wameshaanza kupata wasiwasi.

    “Ilibaki kidogo tu tukufuate kwa maana tuliona unachelewa” Haji akaniambia.

    “Mlijua na mimi nimeshakwenda na maji?” nikawatania.

    “Si ajabu. Haa tunahesabiana siku na saa tu”

    “Tusikate tama kiasi hicho. sisi ni wanaume. Mmeshakula?”

    “Tulikuwa tunakusubiri wewe” Shazume akaniambia.

    “Mimi nimeshakuja. Toeni chakula tule”

    Chakula kikatolewa. Tukakaa chini na kuanza kula.

    Tulipomaliza kula tulikaa uani tukawasha moto na kuuzunguka. Kiza kilikuwa kimeshaingia na kulikuwa na baridi.

    Tuliota moto hadi majira ya saa mbili usiku. Tukaingia vyumbani kulala. Usiku ule haukuwa wa mawazo sana. Nilipitiwa na usingizi mara moja.

    Nilipoamka asubuhi nilishituka nilipoona mlango wa nje ulikuwa umeng’olewa mzima mzima. Palibaki uwazi mtupu. Mlango wa chumba alicholala Haji pia ulikuwa umeng’olewa. Mlango wa chumba cha Shazume ulikuwa mefungwa.

    Nikaenda katika ule mlango wa chumba cha Haji na kuchungulia. Nilimkuta Haji akiwa amelala chini amekufa. Kichwa chake kilikuwa kimetobolewa kwenye utosi. Damu iliyoganda ilionekana kwenye nywele zake.

    Hapo nilijua kuwa tulikuwa tumeingiliwa. Bila shaka Harishi alikuwa amekuja usiku akang’oa milango na kumuua Haji.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lilikuwa tukio ambalo sikulitegemea. Katika kundi letu Haji ndiye aliyekuwa mdogo kuliko sote. Kifo chake kilinisikitisha na kunikatisha tamaa kabisa.

    Nilijiambia kama Harishi ameweza kutufuata huku na kumuua Haji na sisi hatutabaki. Tilichokuwa tunasubiri ni siku na saa zetu ziwadie.

    Baada ya kushangaa kwenye mlango kwa sekunde kadhaa nilikwenda kumgongea Shazume. Shazume akaamka na kufungua mlango.

    “Una habari gani?” nikamuuliza nikiwa nimetaharuki.

    “Sina habari yoyote” Shazume akanijibu huku akionesha kupata hofu.

    “Haji ameuawa!” nikamwambia.

    Shazume akagutuka.

    “Haa! Haji naye ameuawa? Si tulilala naye humu ndani jana usiku?”

    “Tazama ule mlango wa nje”

    Nilimuonesha Haji ule mlango uliong’olewa kisha nikamwambia. “Harishi ameung’oa usiku”

    Shazume aliutazama huku akitikisa kichwa.

    “Ameng’oa na mlango wa chumba cha Haji” nikaendelea kumwambia.

    Shazume akasogea kwenye mlango wa kilichokuwa chumba cha Haji. Alipoiona maiti ya Haji alishituka sana.

    “Mimi naona hatutapona”

    “Kupona tusitegemee ndugu yangu. Harishi ameshajua tupo hapa, usishangae kesho tukiamka mmoja wetu akawa hayupo!”

    “Hapa nyumbani hapafai tena kukaa. Tutafute sehemu nyingine ya kujificha”

    “Tutajificha wapi Shazume?”

    “Popote tu, nyumba ziko nyingi”

    “Sawa. Tumngoje Yasmin aje tumueleze kuwa mwenzetu ameuawa”

    “Pia tumueleze kuwa tunaondoka hapa. Harishi akija tena asitukute”

    “Sawa, tutamueleza”

    Tukaenda kunawa uso na kusukutua maji bila kupiga mswaki. Tulikuwa tumeshachanganyikiwa. Tulipomaliza tulikaa kumsubiri Yasmin.

    Yasmin alikuja majira ya saa tatu hivi. Hakuwa amechukua kitu.

    Akatusalimia na kutuuliza kwanini tumeng’oa milango.

    “Hebu chungulia kwenye hicho chumba” nikamwambia.

    Yasmin akachungulia na kugutuka.

    “Haji amepatwa na nini?”

    “Haji ameuawa usiku na Harishi” nikamwambia.

    “Mama yangu!” Yasmin alimaka huku akijishika kichwa. “Kumbe Harishi alipotoka usiku alikuja huku?”

    “Sisi tumeona asubuhi Harishi ameuawa na milango imeng’olewa”

    “Sasa tumepanga tuondoke hapa” Shazume akamwambia Yasmin.

    “Muondoke muende wapi?”

    “Twende mahali pengine. Tukiendelea kukaa hapa Harishi atakuja tena usiku”

    “Sasa mmepanga muende wapi?’

    “Mimi naona kama tunajisumbua, kama ni kufa tutakufa tu” nikasema.

    “Hata kama tutakufa lakini hapa tuondoke” Shazume akasisitiza.

    “Ni sawa. Sasa tufikirie hapo pa kwenda. Tutakwenda wapi?”

    “Nyumba ziko nyingi”

    “Yasmin unatushauri nini?”

    Machozi yalikuwa yanamtoka Yasmin. Bila shaka yalimtoka kutokana na ukweli kwamba sote tutakufa. Hakunijibu.

    “Yasmin usilie. Tunaomba ushauri wako” nikamwambia.

    Yasmin alijifuta machozi kisha akatuambia. “Niwapeleke katika nyumba nyingine”

    “Huko utakakotupeleka Harish hatafika?” nikamuuliza.

    Yasmin akaguna kisha akajibu. Hatafika”

    Nilijua alitujibu hivyo kututia moyo tu lakini mawazo ya Shazume yalikuwa tofauti.

    “Ni mahali gani?” Shazume akamuuliza haraka.

    “Kwanza twendeni mkanywe uji”

    “Turudi kule tena?” Shazume akamaka.

    “Mnakunywa uji tu halafu tunaondoka”

    Shazume akanitazama.

    “Mimi sitakwenda”

    “Si tunakwenda kunywa uji tu” nikamwambia.

    “Kwanza Harishi hatakuja muda huu” Yasmin akasema.

    “Mimi sitaki uji”

    “Utashinda hivyo hivyo na njaa?” Yasmin akamuuliza.

    “Sioni njaa na ile hamu ya kula pia sina”

    “Kama tumeandikiwa kuuawa tutauawa tu Shazume hata kama hutakula, ni bora ule tu” nikamwambia Shazume.



    Shazume akatikisa kichwa bila kusema lolote.

    “Kakangu najua umepatwa na fadhaa lakini tumbo lako likipata riziki ndio akili itakuja” Yasmin akamwambia Shazume.

    “Tulikuwa watu saba sasa tumebaki wawili tu bado nile? Sitakula!”

    “Wewe ni mwanaume Shazume usiogope kula. Unatakiwa upambane mpaka dakika ya mwisho. Mnaweza kuokoka ndugu zangu. Msikate tama kiasi hicho. Twende ukanywe uji japo kidogo!” Yasmin alimwambia.

    Shazume akakubali kwenda. Tukaondoka sote kwenda kwa Yasmin. Ile maiti ya Haji tuliiacha pale pale. Tangu wenzetu walivyoanza kuuawa hatukuzika maiti yoyote. Zote tuliziacha ziliwe na kunguru.

    Kwa hisia zetu tulikuwa kama watu tuliokuwa vitani. Akifa mtu hakuna kuzika. Kuzika kuna utaratibu wake ambao kutokana na hali tuliyokuwa nayo tusingeuweza.

    Tulipofika kwa Yasmin alituandalia uji tukanywa. Mimi nilikunywa vikombe viwili, Shazume alikunywa kikombe kimoja.

    Wakati tumepumzika Shazume akawa anahimiza tuondoke.

    “Tumeshakunywa uji sasa tunaweza kwenda”

    “Tusubiri kidogo nifikirie pa kuwapeleka” Yasmin akamwambia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kusubiri kwa muda kidogo Yasmin akatuambia. “Haya twendeni tukatafute nyumba nyingine”

    Tukatoka na Yasmin. Niliona wazi kuwa Yasmin alikuwa na wasiwasi. Alikuwa akitupeleka katika nyumba nyingine lakini hakuwa mtu aliyeonesha matumaini.

    Tulizunguka sana kutafuta nyumba nyingine ambayo ingeweza kutufaa kumkwepa Harishi. Tulikuta nyumba moja iliyokuwa ufukweni mwa bahari iliyokuwa na hali nzuri kidogo.

    “Mnaionaje nyumba hii?” Yasmin akatuuliza huku akituonesha nyumba hiyo.

    “Hii inafaa” nikamwambia kisha nikamtazama Shazume ili nipate mawazo yake.

    “Unaionaje Shazume?”

    “Hapa pamejificha kidogo, panafaa” akaniambia ingawa sauti yake haikuwa na nguvu.

    Tukaingia katika ile nyumba. Humo ndani ilikuwa kama stoo iliyosahauliwa. Vitu vilikuwa vimerundikwa ovyo. Ubuibui na vumbi vilikuwa vimetanda pande zote.

    Binaadamu mwenye akili zake timamu asingeweza kukaa ndani ya nyumba ile labda waduu kama vile nyoka na matandu. Lakini sisi hatukuwa timamu. Tulikuwa tumetingwa. Tungeweza kukaa.

    Kama tungehitaji kufanya usafi ili nyumba hiyo iweze kukalika tungelazimika kutoa nje vitu vyote vilivyokuwa ndani na kuanza kufagia, kupiga deki na kusafisha kuta. Ingekuwa kazi kubwa. Ingetuchukua hata kwa siku mbili.

    Tuliingia katika chumba kimoja tukatenga vitu na kupata upenyu mdogo ambao tuliusafisha na kuamua kukaa hapo.

    Kusema kweli siku ile sisi sote hatukuwa na furaha. Tulikaa chini pamoja na Yasmin. Tukawa kimya. Kila mtu akiwaza lake.

    Mimi nilkuwa nikiomba usiku usifike kwani karibu wenzetu wote waliuawa usiku.

    Sikujua Yasmin na Shazume walikuwa wakiwaza nini. Lakini kila nilivyomuangalia Shazume niliona mawazo yake yalikuwa mbali sana. Nilikisia kwamba alikuwa akikumbuka kwao Pemba, akiwakumbuka wazazi wake na ndugu zake. Pengine hakuwa na matumaini ya kuwaona tena.

    Bila shaka Yasmin alikuwa akiwaza kama tutauawa atakosa wenzake wa kuzungumza nao na ataendelea kuwa mkiwa.

    Mimi licha ya kuwa na hofu nlishajitolea kufa kupona. Sikupenda kujipa tama moja kwa moja kuwa nitapona na sikutaka kujikatia tama.

    Ghafla Shazume akaanza kuimba kwa sauti ya huzuni. Ulikuwa wimbo maarufu uliokuwa unaimbwa na vikundi vya ngoma za kiasili.

    “We Yauledi we niletee mashua twende Unguja!. We Yauledi niletee mashua twende Unguja!”

    Na mimi nikamuitikia. “Ukipamba mke nawe ujipambe ndio suna. Usipojipamba watu hukwambia umtumwa! We Yauledi niletee mashua twende Unguja!”

    Shazume aliendelea kuimba ubeti wake kwa kughani huku na mimi nikimuitikia.

    Sauti ya wimbo huo ilikuwa ya huzuni lakini ilituchangamsha. Yasmin alikuwa akitutazama. Wakati ninamuitikia Shazume, Yasmin alikuwa akinifuatisha ninavyoimba.

    Pengine tulikuwa tunajifariji kwa siku yetu ya mwisho kwani tangu tufike katika kisiwa kile, kila siku mwenzetu mmoja aliuawa na Harishi. Hakukuwa na siku yoyote ambayo hakukutokea kifo.

    Kwa hiyo hatukujua usiku wa siku ile atakufa nani kati yangu na Shazume.

    Shazume aliendelea kuimba kwa huzuni. Mimi nilikuwa nimenyamaza. Yasmin akawa anamuitikia.

    Shazume alipoona mimi nimenyamaza na yeye akaacha kuimba tukawa kimya. Baada ya muda kidogo nilipata wazo.

    “Tuombeni dua” nikawambia wenzangu.

    “Tulikuwa tumejisahau kidogo” Shazume akasema

    Nikasoma dua ndefu. Shazume na Yasmin wakawa wanaitikia “Amin”

    Nilipomaliza nilimwambia Shazume aombe na yeye. Shazume akaomba dua ndefu, sisi tukamuitikia “Amin”

    Alipomaliza nikamwambia Yasmin. “Omba na wewe”



    Yasmin naye akaomba dua.

    Kwa muda wa nusu saa hivi mahali hapo pakawa kama madarasa kutokana na kurindima visomo vyetu vya dua.

    “Pia tungekuwa tunaswali” Shazume akatukumbusha.

    Sikuzote binaadamu humkumbuka sana mola wake pale anapofikwa na matatizo. Siku zote hizo tulikuwa hatukumbuki kuswali ila ni kwa siku ile ambayo tuliona tutamalizika.

    “Pia ilitakiwa leo tufunge” na mimi nikawakumbusha.

    “Ni kweli” Shazume akanikubalia na kuongeza “Lakini tumeshakunywa uji”

    “Kama tutanusurika leo tutafunga kesho. Umesikia Yasmin?”

    “Nimesikia” Yasmin akanijibu.

    “Sasa sisi hatuko tohara, tutaswali vipi?’ nikawauliza wenzangu.

    “Twendeni tukaoge baharini tujitoharishe” Shazume akasema.

    “Hizi nguo zetu pia hazina tohara”

    “Tuoge na nguo zetu ziweze kutoharika, zikikauka tutaswali”

    Tukakubaliana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tukaamua sasa twende baharini tukaoge. Tukaenda sote watatu, mimi, Shazume na Yasmin. Yasmin alipotuona sisi tunajitosa kwenye maji na yeye akajitosa. Tukawa tunaoga na kuogelea pamoja.

    Tuliendelea kukaa kwenye maji kwa muda kidogo ili kujisahaulisha matatizo yaliyokuwa yanatukabili.

    Asubuhi ile maji yalikuwa matamu kwa mtu ambaye alikusudia aogelee kwa starehe ila kwa sisi ilikuwa starehe ya kujilazimisha. Mawazo mabaya yalituepuka kwa muda yakitusubiri tumalize kuogelea.

    Tulitamani tusitoke ndani ya maji lakini nilipomuona Yasmin aliyekuwa akiogelea karibu yangu anarudi ufukweni na mimi nikaamua kurudi.

    Tukakaa ufukweni na kumsubiri Shazume. Naye alipotuona tumerudi ufukweni akatufuata.

    Tukakaa kuota jua. Nguo zetu zilikuwa zimetota. Kitendo cha kuogelea na nguo zetu hakikuwa cha maana sana kwani mzizimo ungeweza kutuletea madhara ya kiafya lakini hatukuwa na la kufanya.

    Yasmin ambaye alikuwa na nguo za kubadili alizokuwa akiletewa na Harishi alikuwa akifuata mkumbo tu, haikumpasaaloweshe nguo zake ila alipotuona sisi tunaoga na yeye akajitosa.

    Tulikaa kwa muda kwenye ufukwe tukiangalia bahri na ndege waliokuwa wakiruka ruka. Ili miiliyetu isisinyae tuliamua kufanya mazoezi ya kukimbizana.

    Tulikimbizana mpaka tulipochoka tukarudi kwenye ile nyumba. Tukapanga kwamba itakapofika sa saba tuanze kuswali swala ya adhuhuri. Yasmin alituaga akatuambia kuwa anakwenda kupika chakula cha mchana.

    Kwa mustakabali wetu tatizo la chakula halikuwepo. Chakula kilikuwepo kwa Yasmin. Tatizo lilikuwa ni la kuuliwa na Harishi. Kama si tatizo hilo mahali pale pangekuwa ni pazuri pa kuishi. Sikuvutika na kisiwa hicho pekee bali pia nilivutika na Yasmin. Nilifarijika sana kuona jinsi alivyokuwa akitupa moyo na matumaini japokuwa hali ilikuwa tete.

    Baada ya Yasmin kuondoka tuliendelea kukaa, hatimaye tukapitiwa na usingizi.

    Tulipokuja kuamka yalikuwa majira ya saa nane. Tukaenda kutawadha kwenye maji ya bahari na kuswali swala ya adhuhuri.

    Yasmin alikuja saa tisa akiwa amechukua kapu la chakula. Alikuwa amebadili nguo zake na kuvaa mavazi mengine.

    “Mmepauka kwa chumvi. Mnasikitisha sana kaka zangu” akatuambia.

    “Ndiyo hivyo, tutafanyaje sasa” nikamwambia huku nikimpokea lile kapu.

    “Mmeshaswali?” akatuuliza.

    “Tumeswali na wewe umeswali?” Na mimi nikamuuliza.

    “Mimi naswali kila siku kuomba nusura na kuwaombea na nyinyi. Sijui kama nyinyi mmekumbuka kuniombea”

    “Tumekuombea” nikamdanganya. Tulikuwa tumemsahau.

    “Mngesema mmesahau kuniombea ningejua hamnipendi”

    “Tunakupenda sana. Umetuletea chakula gani?”

    “Wali”

    “Roho zetu zimekinai, hatutamani hata kula” Shazume akasema.

    “Shazume unaanza maneno yako!” Yasmin akamwambia Shazume.

    “Unafikiri nakudanganya, mimi sina hamu ya kula kabisa”

    “Mbona juzi na jana ulikuwa unakula?”

    “Nilikuwa na matumaini”

    “Si vizuri hivyo. kuleni japokuwa kidogo mpate nguvu. Mkiacha kula mtakuwa mnajitesa wenyewe. Mimi pia sikula. Nimekuja huku nile na nyinyi”

    Yasmin alitoa kile chakula akakiweka chini. Akatoa tasa la maji tukaosha mikono kisha tukaanza kula.

    Mimi pia sikuwa na hamu ya kula lakini nilikula kumridhisha Yasmin.

    Tuliendelea kula kidogo kidogo hadi Shazume alipomuuliza Yasmin.

    “Yasmin ukibaki peke yako itakuwaje?”

    “Hatuombei hivyo, tuombee tubaki sote. Ukiomba dua uweke matumaini, isiwe unakata tama”

    “Ni kweli Yasmin huwezi kuomba kitu bila kukiwekea matumaini. Kama huna matumaini na kitu hicho kwanini unakiomba?” nikasema.

    Shazume akaguna.

    “Pamoja na kuomba kwetu bado naona wakati wetu umekaribia sana” Shazume akasema kwa hali ile ile ya kukata tama.

    “Shazume usiseme hivyo, mnaweza kunusurika. Harishi ni kiumbe kama nyinyi”

    “Lakini mwenzetu amepewa uwezo”

    yasmin naye akaguna. Pakawa kimya. Yasmin ndiye aliyeutanzua ukimya huo alipotuambia. “ Jamani tukinusurika nitawachukua Comoro. Nitamwambia baba yangu nyinyi ni ndugu zangu wa damu. Mtaenziwa kama watoto wa rais”



    “Sidhani kama hapa ni karibu na kwenu Comoro. Mimi nadhani kama tutapata msaada wa kuokolewa tutapelekwa kwanza Zanzibar” nikasema.

    “Si vibaya Zanzibar pia ni nyumbani lakini baba akipata habari atatuma ndege siku hiyo hiyo ituchukue pamoja na nyinyi”

    “Itakuwa raha sana tukienda Comoro na kupokewa na rais” nikasema.

    Shazume alikuwa kimya akitusikiliza. Bila shaka alikuwa anaona tunajidanganya kujifariji. Kwa mawazo yake sisi tulikuwa ni wa kufa tu.

    “Si unajua mzazi aliyekwishamkatia tamaa mwanawe halafu anaambiwa amepatikana, atafurahije?” Yasmin akaniuiza.

    “Atafurahi sana”

    Iliwezekana tulikuwa tulikuwa tunajidanganya kweli kama alivyowaza Shazume lakini tulifarijika. Saa zikapita.

    Tulipomaliza kula Yasmin alileta storitofauti tofauti kutuondoa katika mawazo mabaya. Tukawa tunazungumza.

    Aliondoka jioni sana. Tukamsindikizakwa pamoja hadi nusu ya njia, tukarudi. Tukakaa kwenye kile kisehemu chetu kusubiri usiku. Hatukujua nini kitatokea kati yetu usiku huo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usiku ule tulikesha macho kwa sababu ya hofu. Tulikuwa tumejilaza chini kila mmoja upande wake lakini hakukuwa na aliyelala usingizi. Mara kwa mara nilimuona Shazume akijigeuza kila upande.

    Ilikuwa kati kati ya usiku Shazume aliposhika mguu wangu. Sikujua kama alikuwa anataka kuniamsha au alitaka kujua nilikuwa macho lakini aliponishika nilishituka nikarusha mguu wangu.

    “Nini?” nikamuuliza nikiizuia sauti yangu isisikike sana.

    “Nimebanwa na haja ndogo” akaniambia.

    “Sasa?” nikamuuliza.

    “Tunaweza kutoka nikajisaidie”

    “Haya tutoke” nikamwambia.

    Shazume akainuka na mimi nikainuka. Akatangulia kutoka kwenye mlango. Kulikuwa giza sana. Hatukuweza kuona kwa mbali.

    “Twende nje au uani?” Shazume akaniuliza.

    “Naona tutoke uani” nikamjibu.

    Shazume akaelekea upande wa uani. Mimi nilikuwa nikimfuata nyuma. Alifungua mlango akachungulia uani. Mwezi ulikuwa unaangaza, ua ulikuwa mweupe. Baada ya kuchungulia kwa tahadhari Shazume alivuka kizingiti cha mlango akatoka uani na mimi nikatoka.

    Yeye alikwenda upande wake na miminilikwenda upande wangu tukachutama na kujisaidia. Mimi sikuwa na haja ndogo lakini baada ya mwenzangu kuniambiana mimi nikaisikia.

    Tulipomaliza haja zetu tulirudi ndani tukajilaza tena. Safari hii tulipojilaza tu usingizi ulitupitia tukalala.

    Wakati nipo usingizini niliota Harishi anatufukuza baada ya kutufuma tukiwa na Yasmin kwenye lile jumba lake. Tukaingia katika chumba kimoja kujificha chini ya mvungu wa kitanda. Muda si muda Harishi akafungua mlango na kuingia mle chumbani kututafuta.

    Akaona mguu wa Shazume umetokeza chini ya mvungu. Akaushika na kuuvuta. Shazume akawa anapiga kelele kuniita.

    Kelele hizo ndizo zilizoniamsha. Nikaamka na kuangaza macho. Nikasikia Shazume akiendelea kupiga kelele kuniita lakini sauti yake ilitokea kwa juu, sio pale chini tulipolala. Nikashituka sana kwa kujua kuwa haikuwa ndoto.

    Nikatazama juu. Kwanza niliona kanzu nyeupe halafu nikaona upanga uking’aa. Nilipoona hivyo nilijisogeza zaidi ndani ya makorokoro na kuendelea kuchungulia.

    Nilimuona Shazume ameinuliwa juu juu na Harishi. Nikajiambia kumbe ile ndoto ilikuwa ni kweli. Shazume alitolewa mle chumbani. Sikuweza kujua Harishi aliwasili muda gani na kumkamata Shazume.

    Bila shaka kilichokuwa kimeninusuru mimi, ni kuwa nililala nyuma ya mlango. Harishi alipoingia alimuona Shazume na kumkamata yeye.

    Ile ndoto niliyoota ilikuwa ya kweli. Harishi alikuwa ametuingilia!

    Jitihada zetu za kujaribu kumkwepa zilikuwa za bure kwani Harishi alikuwa akitugundua kila tulipokwenda kujificha na sababu ni kuwa alikuwa akifuata harufu zetu kama vile m’bwa.

    Harishi alipomtoa Shazume ukumbini, nilimsikia Shazume akipiga ukulele mmoja tu “Nakufa!”. Halafu sikusikia kitu tena.

    Moyo ulikuwa ukinienda mbio na nilikuwa nikihema kwa nguvu kama niliyekuwa nafukuzwa. Tukio hilo lilikuwa la ghafla sana kiasi kwamba nililazimika kujiuliza, kama bado nilikuwa kwenye ile ndoto au kilichokuwa kinatokea kilikuwa kweli.

    Hofu yangu sasa ilikuwa kwangu. Nilijiua Harishi akimaliza kumuua Shazume ataniingilia na mimi kwani alipoingia humo chumbani alituona tukiwa wawili.

    Wazo hilo likanifanya nizidi kujisogeza kwenye makorokoro ili Harishi akiingia tena asinione. Lakini muda ulipita. Sikumuona tena Harishi.

    Nikaendelea kukaa hapo hapo hadi nikaona kunakucha. Nikahisi kwa muda ule Harishi atakuwa ameshaondoka. Nikajiburuza kujitoa kwenye yale makorokoro nilikojiingiza.

    Nilinyata hadi kwenye mlango nikaufungua na kuchungulia ukumbini. Nilichungulia upande wa mbele na upande wa uani. Niliiona maiti ya Shazume imelala chini kando ya mlango wa chumba tulichokuwemo. Harishi mwenyewe hakuwepo.

    Nikatoka nje na kuangalia kila upande. Sikuona kitu. Kando ya ile nyumba palikuwa na mti. Nikapata wazo kuwa nipande juu ya ule mti kujificha. Nikaenda kwenye mti huo nikaupanda na kukaa kwenye tawi mahali ambapo nisingeweza kuonekana.

    Wakati nipo juu ya ule mti nilimuona Yasmin kwa mbali akija. Nikajiambia tuliobaki katika kisiwa kile tulikuwa watu wawili tu, mimi na Yasmin.

    Sikupenda kujisifu kuwa nilikuwa nina bahati kwa sababu nimenusurika. Nilijua kuwa wakati wangu ulikuwa haujafika. Pengine niliandikiwa niwe wa mwisho kufa.

    Historia ya kisiwa hicho tangu tulipofika kila siku alikufa mtu. Leo nimeishuhudia maiti ya Shazume, huenda kesho Yasmin ataishuhudia maiti yangu.

    Yasmin alipofika pale nilimuacha aingie mle ndani. Mara moja nikamuona ametoka akiwa amechanganyikiwa. Bila shaka alikuwa ameshitushwa na maiti ya Shazume.





    Kile kitendo cha kutoniona mimi inawezekana kilimpa hisia kuwa na mimi nilikuwa nimeuawa kama Shazume. Tatizo ni kuwa mwili wangu hakuuona. Bila shaka alitoka nje kuutafuta mwili wangu.

    Alisimama mbele ya ile nyumba akaangalia kila upande kisha akarudi tena mle ndani. Mimi nikashuka kwenye ule mti.

    Yasmin alipotoka tena akanikuta nimesimama mbele ya mlango. Akashituka na kuniuliza. “Ulikuwa wapi?”

    “Nilikuwa nimepanda juu ya huu mti” nikamjibu.

    Akaja kunikumbatia kifuani kwangu. Kumbe alikuwa analia. Nilipoona analia na mimi nikaanza kulia. Kama Yasmin alikuwa anaona uchungu jinsi tulivyokuwa tunauliwa na Harishi, mimi niliona uchungu nilipowaza nitakavyouliwa na Harishi hapo kesho.

    “Buriani Yasmin, ndio tunaagana. Kesho hatutakuwa pamoja tena. Shazume ametutangulia leo” nikamwambia Yasmin.

    Yasmin akajifuta machozi yake na kunitazama.

    “Wewe hutaniacha, kama ni kufa tutakufa sote. Mwili wangu utalala juu ya mwili wako” Yasmin akaniambia kwa sauti nzito lakini ya kijasiri.

    Akaongeza. “Ili uamini kuwa wewe utakufa na mimi turudi kule kule kwenye lile jumba,hatuna sababu yoyote ya kujificha. Akija Harishi nitamwambia atuue sote, Anitangulize mimi kisha wewe”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Twende!” nikamwambia Yasmin bila kusita.

    Yasmin akanishika mkono tukatembea kuelekea katikalile jumba. Hatukuzungumza kitu tena mpaka tulipofika katika jumba hilo Yasmin aliniuliza.

    “Utakunywa uji?”

    “Sitakunywa” nikamjibu kwa mkato

    “Kwanini?”

    “Roho yangu imefadhaika sana”

    “Hata roho yangu imefadhaika lakini kama wanipenda tunywe kidogo”

    Ilikumridhisha Yasmin nilimkubalia. Yasmin aliniacha ukumbini akaenda jikoni. Baaada ya muda kidogo alikuja na vikombe viwili vilivyojaa uji wa ngano uliotiwa asali.

    Alinipa kikombe kimoja kisha aliketi nami.

    “Yasmin kweli tumeshindwa kuondoka kwenye kisiwa hiki cha mauti” nikamuuliza Yasmin

    “Tutaondokaje wakati tumezungukwa na bahari na hatuna chombo!”

    “Nashangaa kwamba hakuna wavuvi wanaokuja katika kisiwa hiki!”

    “Hiki kisiwa kiko mbali na pia kinajulikana. Hakuna wavuvi wanaoweza kufika hapa”

    “Chombo chetu kilipotuharibikia tulipokiona kisiwa hiki tulidhani tumeokoka kumbe tumekuja kuangamia”

    “Hata kama msingekiona hiki kisiwa pia mngeangamia. Mngekula nini? Mngekufa kwa njaa”

    “Mimi naona bora kufa kwa njaa kwa sababu njaa itakuwa imekulevya, hutajijua. Kuliko kusubiri….” sikumalizia sentensi yangu.

    Niliona nilikuwa najikumbusha kifo kibaya cha kutobolewa utosi kwa ncha ya upanga na kufyonzwa damu na ubongo1.

    Siku zote tulizokaa hapa kisiwani niliweza kujikaza na kuondoa hofu licha ya wenzangu kuendelea kuuawa lakini kwa siku ile ambayo nilibakimimi na Yasmin peke yetu, sikuweza kuzuia hofu yangu.

    Mawazo ya kifo cha kutobolewa utosi kwa ncha ya upanga na kufyonzwa damu na ubongo yalikuwa yametawala akili yangu.

    “Harishi ni kiumbe na sisi ni viumbe. Huwezi kujua Mungu amepanga nini” Yasmin akaniambia.

    “Namuamini Mungu na simkatii tamaa”

    “Hapo umezungumza kitu cha maana sana. Haifai kukata tama. Nimeshakwambia kama ni kufa leo tutakufa sote. Na mimi ndio nitakufa kwanza”

    “Unataka tuendelee kukaa humu hadi usiku”

    “Ndiyo. Unafikiri utakwenda wapi?”

    “Sioni pa kwenda”

    “Basi tukae tu humu”

    “Harishi akija atukute pamoja?”

    “Ndiyo”

    “Aniue mbele yako!”

    “Hapana. Ataniua mimi kwanza”

    “Mimi sipendi nikusababishie kifo, niache nife mwenyewe”

    “Na mimi sitapenda nikusababishie kifo”

    “Wewe hutanisababishia kifo, ni Harishi”

    “Sikiliza kaka yangu. Sisi tukae hapa hadi usiku.Litakalotokea lolote na litokee lakini kama ni kufa nitatangulia mimi”

    Nilimuangalia tu Yasmin, sikumjibu kitu tena. Nikaendelea kunywa uji huku nikiwaza kama ni kweli alikuwa amejitolea nafsi yake kwa ajili yangu.

    Maneno yake yalionesha alichokuwa akisema kilikuwa na udhati.

    Hata hivyo niliwaza kuwa msimamo wa Yasmin haukuwa na msaada wowote kwangu zaidi ya kuonesha upendo. Ulikuwa msimamo wa kukata tamaa na haukuwana maana.

    Atangulie yeye kufa halafu nifuatie mimi? Maana yake ni kuwa sote tutafikwa na mauti. Jambo hilo kwangu lilikuwa tishio ingawa yeye aliona lilikuwa la kijasiri.

    Jambo la maana lilikuwa kupata wazo la kutunusuru sote na sio tufe sote.

    Tulibaki kimya tukinywa uji. Uji huo niliunywa kwa kujilazimisha ili kumridhisha Yasmin. Kama ningekuwa peke yangu ningebaki na njaa hadi mauti yatakaponikuta.

    Nilipomaliza kikombe changu cha uji Yasmin aliniuliza.

    “Nikutilie tena?”

    “Umetosha’ nikamjibu.

    Yeye pia alikuwa amemaliza uji wake akaniambia.

    “Basi nenda ukaoge, umeshatia nguvu kidogo”

    Pamoja na kukabiliwa na tishio hilo la kifo kusema kweli nilihitajika sana kuusafisha mwili wangu. Nilikuwa nimechafuka sana na nilikuwa sijaoga kwa siku tatu.

    Niliona aibu kumwambia Yasmin kuwa sitaoga. Nikainuka.

    Yasmin akanipeleka bafuni kisha akaondoka. Nilioga haraka haraka. Nilipomaliza niliondoka bafuni na kumbishia Yasmin mlango.

    Yasmin alinifungulia mlango na kuniambia.

    “Karibu”

    Niliingia mle chumbani alimokuwa. Hamkuwa na kiti. Akaniambia.

    Kaa kitandani”

    Nikakaa.

    “Unajisikia vizuri kidogo?” akaniuliza.

    Nilijaribu kutabasamu bila kufanikiwa. Niliishia kubenua midomo tu, uso haukukunjuka.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yasmin akaja kukaa kando yangu.

    “Unajua maisha?” akaniuliza. Sikujua alikuwa na maana gani.

    “Maisha ni nini?” nikamuuliza.

    “Maisha ya mwanaadamu ni mtihani. Lolote linalokufika liwe zuri au baya ni mtihani kwako. Kama wewe ni muumini unatakiwa ulijue hilo”

    “Ndio ninalijua”

    “Mungu hashindwi kutuokoa sisi waja zake tunaomtegemea yeye ila anatupa mitihani kuona ni kwa kiasi gani tunaweza kuweka matumaini kwake na kwa jinsi gani tunaweza kumuomba kwa unyenyekevu katika siku hii ambayo mimi na wewe tunahitaji sana msaada wake”

    Ndani ya moyo wangu nilikiri kuwa Yasmin alikuwa amenieleza maneno ya maana kuliko aliyowahi kunieleza wakati wowote. Nilifarijika kuona juhudi zake za kunitia moyo zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuamsha imani yangu.

    Nikajiambia laiti kama ningekuwa na mke kama Yasmin nisingeshindwa kimaisha hata itokee shida ya kiasi gani

    Hatimaye jua lilikuchwa. Giza lilianza kuingia. Yasmin aliwasha taa za nyumba nzima. Alikuwa ameniacha mle chumbani mwake, akanifuata na kuniuliza. “Utakula chakula?”

    Nikatikisa kichwa.

    “Sitakula”

    “Hutakula hata kidogo”

    Nikaendelea kutikisa kichwa.

    “Sitakula”

    Yasmin akakaa karibu yangu.

    “Usiku ndio huu” akaniambia.

    “Kwani Harishi atakuja muda huu?”

    “Anaweza kuja wakati wowote kutoka sasa hadi alfajiri”

    “Anakujaje?” nikamuuliza Yasmin huku nikiitazama ile chupa iliyokuwa juu ya kabati.

    “Anakuja kama moshi. Unajaa ndani ya ile chupa kisha unatoka. Unapotoka unabadilika na kuwa jini”

    “Na ni kwanini anakuja hivyo?”

    Yasmin akabetua mabega yake

    “Sijui lakini ondoa hofu. Mwisho wa mateso yetu utakuwa leo”

    Sikusema kitu tena nikanyamaza kimya. Tulikaa kimya kwa muda mrefu. Ile shauku ya kuzungumza ilikuwa imetuishia. Tukaamua kukaa tu kusubiri muda wetu.

    Tulikuwa tumekaa chini tumeelekezana migongo. Kila mmoja alielekea upande wake. Yasmin alipochoka au kuhisi kusinzia aliuegemeza mgongo wake kwenye mgongo wangu.

    Kitu gani kilimfanya Yasmin asipande kitandani na kulala?

    Alikuwa amejitolea kufa na mimi. Alikuwa ameamua akae na mimi pale chini hadi Harishi atakapokuja.

    Ilikuwa kama saa saba usiku nywele zangu zilipoanza kunisisimka. Nikayapeleka macho yangu kwenye ile chupa ya Harishi iliyokuwa juu ya kabati. Moyo wangu ulishituka nilipoiona chupa inaingia moshi kwa ndani. Nikamgutusha Yasmin aliyekuwa anasinzia.

    “Yasmin!”

    “Abee!” Yasmin akaniitikia.

    “Tazama ile chupa!”

    Yasmin akageuza uso wake na kuitazama chupa hiyo.

    “Usimuogope kiumbe aliyeghulukiwa kama wewe. Muogope aliyeghuluku” Ndilo neno aliloniambia Yasmin.

    Ule moshi uliendelea kujaa ndani ya ile chupa. Kifiniko cha chupa hiyo kilikuwa pembeni. Moyo haukunipa. Mara moja nikanyanyuka na kwenda kando ya lile kabati. Niisubiri ule moshi ujae kabisa kisha nikakichukua kile kifiniko na kukifunga kwenye mdomo wa ile chupa.

    Baada ya sekunde chache nilisikia sauti ya Harishi kutoka kwenye ile chupa.

    “Nani amefunga kizibo?”

    Sote tukanyamaza kimya.

    Ile sauti ikasikika tena.

    “We Yasmin si nilikwambia usifunge hiki kizibo?”

    Tukaendelea kunyamaza lakini moyo wangu ulikuwa ukienda mbio.

    “Fungua sasa!” ile sauti sasa ilifoka.

    “Usifungue!” Yasmin akaniambia huku akinifuata.

    “Ahaa! kumbe uko na hawara yako! Sasa mtanitambua”

    “Sifungui!” Yasmin akasema kwa jazba.

    “Nimekwambia fungua, nataka nitoke!” Sauti ikafoka.

    “Toka mwenyewe!” Yasmin akajibu.

    “Yasmin umechoka kuishi? Nakwambia nitakuua wewe na hawara yako!” Sauti ya Harishi iliendelea kuunguruma kwa hasira.

    “Ndio tunavyotaka utuue. Tuue sasa hivi!” Yasmin aliendelea kujibu.

    “Wewe kijana nani amekuruhusu ufunge hiki kizibo, hujui kuwa hii ni nyumba yangu?” Sauti ya Harishi ikaniuliza.

    “Nimemruhusu mimi akifunge. Nimeshachoka na wewe. Kama unaweza kutoka toka mwenyewe utuue. Sisi tunasubiri kufa tu”

    “Yasmin umeamua kunigeuka leo?” Sauti ya Harishi sasa ilukuwa imerudi chini. “Nifungulie mke wangu. Nimekuletea zawadi nzuri”

    “Sitaki zawadi yako. Njoo utuue!”

    “Nani amekwambia kama nataka kuwaua?”

    “Si ndio kazi yako kuua watu. Watu wote wa kisiwa hiki si umewamaliza wewe!”

    “He he he!” Harishi alitoa kicheko kilichoonesha wazi kuwa ni cha uongo. Kisha akauliza kwa ukali.

    “Sasa utakifungua kizibo au hufungui?”

    “Sifungui!” Yasmin akamjibu.

    “Wewe kijana fungua kizibo hicho?’ Sauti ya Harishi ikanigeukia mimi.

    “Usifungue. Mwache atoke mwenyewe. Sisi tumeshajitolea, liwalo na liwe!” Yasmin akaniambia.

    Wakati wote nilikuwa najiuliza kama Harishi alikuwa hawezi kutoka mwenyewe kwenye ile chupa mpaka atuombe sisi tufungue kizibo. Nikataka kupata uhakika kama kweli Harishi alikuwa amenasa na asingeweza kutoka bila msaada wetu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog