Search This Blog

NILIOA JINI NA KUZAA NAE - 1

 



    IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS



    *********************************************************************************



    Simulizi : Nilioa Jini Na Kuzaa Nae

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Nilikuwa bado kijana na umri wangu ulikuwa wastani wa miaka ishirini na mitano. Sikuwa nimepata elimu ya kutosha baada ya wazazi wangu wote wawili kufariki dunia wakati nikiwa mdogo.

    Nilianza maisha ya kuhangaika tangu nikiwa mdogo baada ya wazazi wangu hao kufariki dunia. Nilianza kuajiriwa kazi ndogondogo ili nipate pesa za kujikimu na nilipofikia umri wa miaka kumi na minane ndipo nilipopata ajira rasmi.

    Ajira yenyewe ni ya kazi ya ulinzi. Niliajiriwa katika kampuni moja ya ulinzi, kazi yangu ikiwa ni kulinda zamu usiku. Kwa vile sikuwahi hata kupitia mafunzo ya mgambo nilifundishwa hapo hapo jinsi ya kutumia bunduki na jinsi ya kukabiliana na wezi na majambazi.

    Lindo langu la kwanza lilikuwa katika eneo la Gofu. Unapoingia katika jiji la Tanga eneo hilo unakutana nalo mwanzo mwanzo. Halikuwa eneo la makazi ya watu isipokuwa viwanda vidogo vidogo na maghala ya makampuni mbalimbali.

    Wakati wa mchana eneo hilo linakuwa limechangamka kwa sababu kunakuwa na pilikapilika za wafanya kazi lakini ikifika usiku mahali hapo hupooza na kuwa kimya kabisa.

    Mimi nilikuwa ninalinda ghala la kampuni moja ambayo wamiliki wake walikuwa ni Waasia. Ghala hilo lilikuwa liko mbali kidogo na maghala mengine na unapoliacha ghala hilo unaelekea katika maghala ya zamani ambayo yalikwa hayatumiki tena.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikuwa ninaingia kazini saa 12 jioni na kutoka saa 12 asubuhi. Kama si dhiki ya kimaisha niliyokuwa nayo nisingekubali kwenda kukesha usiku katika eneo hilo kwani lilikuwa linatisha sana.

    Siku za mwanzo mwanzo nilipoanza kazi nilikuwa na hofu na wasiwasi lakini kadiri siku zilivyoendelea hofu ilinipungua.

    Nikawa najiambia pengine ni kwa sababu sijaizoea kazi yenyewe ndiyo maana ninapata hofu, lakini nikiizoea hofu itaondoka.

    Nilipata mshahara wangu wa kwanza  ukanisaidia kununua vitu vidogo vidogo vya chumbani mwangu.  Nilikuwa nimepangisha chumba katika eneo la Chumbageni ambalo halikuwa mbali sana na lilipokuwa lindo langu. Ofisi zetu ndizo zilikuwa katikati ya jiji.

    Siku moja nilipokuwa katika lindo langu nikirandaranda huku na  huku nilimuona msichana mmoja akipita katika barabara iliyokuwa karibu na lile ghala ninalolinda

    Nilishituka kwa sababu kwanza ilikuwa ikikaribia kuwa saa nane usiku. Nilijiuliza yule msichana alikuwa anatoka wapi usiku ule?. Pili nilishituka kwa sababu mahali alikokuwa anaelekea hakukuwa na makazi ya watu bali kulikuwa na maghala ya zamani yasiyotumika tena na viwanda vilivyokufa.

    Nikasimama na kumuangalia. Kwa vile barabara ilikuwa mbali kidogo, msichana huyo hakuniona au pia inawezekana aliniona lakini hakunijali.  Alikuwa akitembea kwa hatua za haraka lakini bila kuonesha kuwa alikuwa na wasiwasi.

    Alikuwa amevaa vazi jeupe la aina ya dera lililoficha kabisa miguu yake na alijitanda ushungi mrefu uliofanana na rangi ya dera alilovaa.

    Wakati akitembea kulikuwa na mlio wa ko! ko! ko! uliokuwa ukisikika kwenye miguu yake. Nikahisi alikuwa amevaa viatu vya mchuchumio ambavyo vilikuwa vikitoa mlio kila alipopiga hatua.

    Kwa vyovyote vile kitendo cha msichana huyo kuwa peke yake usiku huo na akitembea kwa kujiamini bila kuonesha wasiwasi kilionesha ujasiri.

    Punde tu akawa amelipita eneo hilo na kupotea kwenye kiza. Hata hivyo niliendelea kuusikia ule mlio wa viatu vyake ko! ko! ko! japokuwa mwenyewe sikuwa nikimuona tena.

    Nikawa najiuliza msichana yule alikuwa nani, anakwenda wapi na anatoka wapi. Lakini sikupata jibu.

    Usiku wa siku ya pili yake muda kama ule nikaanza kuisikia tena ile sauti ya viatu ko! ko! ko!. Nilipotupa macho barabarani nikamuona yule msichana akitokea kwa mbali. Alikuwa amevaa mavazi yaleyale na akitembea kwa mwendo wake uleule wa harakaharaka lakini bila kuonesha kuwa alikuwa na wasiwasi.

    Wakati huo nilikuwa nimeketi kwenye kiti baada ya kuchoka kurandaranda. Nikawa namtazama.  Alipita karibu na lile lindo kisha akaendelea na safari yake. Punde tu akapotea kwenye kiza.

    “Huyu msichana anakwenda wapi saa hizi?” nikajiuliza.. Hata hivyo kama ilivyokuwa usiku wa jana yake sikupata jibu.

    Ilipofika saa 12 asubuhi nilibadilishana lindo na mlinzi mwenzangu, nikarudi nyumbani.

    Kama kawaida yangu ya siku zote nilipofika nyumbani nilioga kisha nikalala. Sikuamka hadi saa sita mchana. Nilivaa nguo zangu za kiraia, nikaenda katika mkahawa uliokuwa jirani na nyumba niliyopanga chumba. Nikala ugali na maharage. Nilikuwa natamani nile nyama au samaki lakini uwezo nilikuwa sina..

    Kila inapofika saa kumi jioni hununua kabisa chakula ambacho nitakula usiku. Chakula hicho hukiweka kwenye chombo kinachotunza joto. Kwa hiyo ninapokwenda kazini jioni ninakuwa na mfuko wangu wenye chakula changu cha usiku pamoja na chupa ya maji.

    Lakini si chupa ya maji safi yanayouzwa madukani bali ni maji ya bomba ambayo huyatia kwenye chupa tena bila kuyachemsha.

    Chakula ninachokwenda nacho hukila inapofika saa tatu usiku halafu naendelea na kazi yangu. Sikuwa nikivuta sigara kama  ilivyo kwa walinzi wengine ambao huvuta sigara sana usiku kwa sababu ya baridi.

    Nilikuwa na koti langu la mvua ambalo hulivaa usiku ili kujikinga na baridi. Ninapovaa koti hilo huwa sisikii baridi.

    Tangu nilivyofika katika lindo hilo saa 12 jioni, niliona dalili za kunyesha mvua kwani wingu lilikuwa limejikusanya na kulikuwa na upepo mkali.

    Hata hivyo hakukunyesha mvua lakini hali ya hewa haikuwa nzuri.

    Ilipofika saa nane usiku nikausikia tena ule mlio wa viatu vya yule msichana, ko! ko! ko!. Nilipotupa macho barabarani nikamuona. Alikuwa amechanganya mwendo kwani matone ya mvua yalikuwa yameanza kuanguka

    Msichana huyo alipokuwa karibu na lindo langu, mvua ikaanguka kwa kishindo. Nikamuona anakuja mbio kuelekea kwenye lile ghala kujificha mvua.

    Alipofika alipitiliza moja kwa moja hadi karibu na lango la ghala hilo mahali ambapo nilikuwa nimesimama. Mvua ilikuwa hainipati kwa sababu palikuwa pamepauliwa bati.

    ‘Asalaam alaykum’ akanisalimia.

    Nilikuwa Mkristo lakini nilikwishaizoea salamu hiyo ya kiislamu.

    Nikamuitikia. ‘Alaykumu salaam’

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alinitupia jicho mara moja tu kisha akauelekeza uso wake chini. Alikuwa amejikunja kwa sababu ya baridi na nguo zake zilikuwa zimetota kwa mvua.

    Ingawa alinitazama mara moja tu lakini uso wake niliuona. Alikuwa na pozi la kisomali. Na kama hakuwa msomali alikuwa chotara wa kiarabu. Alikuwa mweupe mwenye nyusi zilizopakwa wanja. Macho yake yalikuwa makubwa yenye mboni za kijivu, pia aliyakoleza wanja mzito na kuwa na mvuto wa kipekee.

    Midomo yake alikuwa ameipaka rangi ya waridi. Ilikuwa na papi za ukubwa wa wastani. Alikuwa amevaa mkufu wa dhahabu kwenye shingo yake.

    Mara moja eneo hilo likaenea hewa ya manukato ya udi wa mawaridi na manukato ya Al-uud na marashi alivyokuwa amefukiza nguo zake.

    ‘Hujambo?’ Nilijaribu kumsemesha ili niweze kumuuliza, anatoka wapi na anakwenda wapi.

    ‘Sijambo’ akanijibu bila kunitazama. Alikuwa akitetemeka kwa baridi iliyompata.

    ‘Pole sana. Unatoka wapi saa hizi?’



    Msichana hakunijibu mpaka nilipomuuliza mara ya pili.



    “Natoka hukoo!” akaniambia.



    “Wapi?”



    “Kazini”



    “Ni wapi?”



    Akanitajia klabu moja ya usiku ilikokuwa karibu na Posta.



    “Na unakwenda wapi?”



    “Ninaenda nyumbani”



    “Unaishi wapi?”



    “Hukoo”



    Akanionesha kwa kidole kule alikokuwa anakwenda.



    “Kwani kule kunaishi watu?” nikamuuliza.



    Akanikubalia kwa kichwa.



    SASA ENDELEA



    Pakapita kimya kifupi huku mvua ikiendelea kunyesha. Nikamsikia akisema.



    “Hii mvua haiachi, nakwenda nayo hivyo hivyo”



    “Subiri kidogo, inaweza kuacha”



    Msichana akatikisa kichwa.



    “Hii haitaacha, sitaki alfajiri inikute hapa”



    “Jinsi unavyotetemeka ukiendelea kunyeshewa unaweza kupata homa”



    “Si kitu, acha niende”



    “Ngoja basi nikupe koti langu uendenalo, utanirudishia kesho”



    Nikavua koti langu na kumvalisha yeye.



    “Asante kaka, nitakurudishia kesho” akaniambia kisha akaingia kwenye mvua na kwenda zake.



    Nilimsindikiza kwa macho hadi alipopotea kwenye macho yangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikabaki kujiuliza kama kule alikokuwa anakwenda kulikuwa na nyumba za watu. Kwa jinsi nilivyokuwa nafahamu mimi upande ule haukuwa na nyumba isipokuwa maghala ya zamani yaliyokuwa hayatumiki tena na viwanda vidogo vidogo vilivyokufa.



    Msichana huyo alipoondoka ndipo nilianza kujilaumu kwa kutomuuliza jina lake. Hata hivyo niliona hata kama ningemuuliza asingenitajia jina lake kwa vile ilikuwa ndio kwanza tunakutana. Baadhi ya wanawake wa pwani huwa hawapendi kutaja majina yao kwa watu ambao hawawafahamu vyema.



    Siku iliyofuata ambayo haikuwa na mvua, yule msichana alipita tena saa nane usiku. Nilikuwa nimemsubiri kwa hamu ili nizungumze naye.



    Alikuja mpaka pale kwenye ghala nilipokuwa nimesimama akanisalimia.



    “Asalaam alaykum”



    “Waalayka salaam. Hujambo?” nikamjibu.



    “Sijambo. Habari ya tangu jana?”



    “Nzuri”



    “Samahani kaka, nilisahau kukuchukulia koti lako asubuhi lakini kesho nitakupitishia” akaniambia kwa sauti ya kubembeleza.



    Na kweli nilibembelezeka. Hata sikujali kuwa koti hilo lilikuwa muhimu kwangu.



    “Usijali, utaniletea kesho”



    “Asante kaka”



    “Mimi naitwa Alfredy, wewe unaitwa nani?” nikamuuliza ghafla.



    Msichna aliguna kisha akanitazama machoni mwangu.



    “Nitakutajia jina langu kesho, kwaheri”



    Msichana huyo alikuwa ameshageuka ili aende zake.



    “Unakwenda zako?” nikamuuliza.



    “Ndiyo. Usiku mwema”



    Msichana akawa anachanganya mwendo kuelekea kule alikodai anaishi.



    Udadisi ukanipata. Alipofika mbali nikaamua kumfuata ili niweze kujua anakwenda wapi.



    Nilimfuata kwa kumnyemelea huku nikijificha ficha kwenye miti ili asinione au kugundua kuwa namfuata.



    Nilisahau kuwa niliacha lindo langu likiwa halina mlinzi. Tulikwenda mbali kidogo. Nilijiambia kama ni kukosa uoga msichana huyo alikuwa namba moja. Huko mahali alikokuwa anakwenda kulikuwa kimya na kulikuwa kunatisha.



    Binafsi kama nisingekuwa na bunduki nisingethubutu kufika katika eneo hilo usiku huo lakini yule msichana alikuwa haogopi kabisa.



    Baada ya mwendo wa nusu saa hivi nilimuona akiingia katika jumba moja la zamani ambalo upande wake mmoja ulibomoka na kuwa kama gofu.



    Jumba hilo kama sikosei lilijengwa enzi za wajerumani na sikuweza kujua lilikuwa likitumika kwa shughuli gani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kulikuwa na msufi mrefu uliokuwa umeota mbele ya jumba hilo na kusababisha kivuli kipana.



    Msichana huyo alipoingia ndani ya jumba hilo nilishituka, nikajiuliza kama alikuwa akiishi mle ndani.



    Udadisi wa kutaka kumchunguza ukanipata. Nikatembea haraka haraka na kufika katika mlango wa jumba hilo ambao ulikuwa wazi, nikaingia ndani.



    Nilipoingia ndani nilisimama kando ya mlango kwani kiza kilinifanya nisiweze kuona chochote. Nilitaka macho yangu yazoee kiza ili niingie ndani zaidi. Sikujua yule msichana aliingiaje wakati kulikuwa na kiza kiasi kile.



    Macho yangu yalipozoea kiza nilijikuta nimeingia katika chumba kipana kilichokuwa na vichuguu vya mawe baada ya sakafu iliyokuwapo kuvunjika. Pia kulikuwa na mimea iliyoota mle ndani.



    Kitu cha kwanza kilichonishitua ni kwamba nilikuta lile koti langu nililomuazima yule msichana limetundikwa kwenye moja ya kuta za chumba hicho



    Nilikuwa sitaki kutoa tochi yangu ndogo lakini nililazimika kuitoa na kulimulika lile koti, nikahakikisha kuwa ni langu.



    Hapo nikajiuliza yule msichana anaishi katika gofu lile?. Halikuelekea kuwa ni makazi ya binaadamu kwani licha ya kuwa linatisha, mazingira ya gofu hilo yalikuwa ni ya kuishi wadudu kama nyoka.



    Dukuduku likanifanya niharakishe kuingia ndani zaidi. Nilizima ile tochi ili mwanga usionekane. Nikapita kwenye sehemu iliyokaa kama ukumbi ambayo pia ilikuwa na mawe na mimea iliyoota.



    Upande mmoja wa ukuta palikuwa na tundu ambalo nilihisi zamani lilikuwa ni dirisha lililong’oka. Tundu hilo lilikuwa likiingiza mwanga wa mwezi ulionifanya nione uwazi mwingine mbele yangu. Nikaenda mbele zaidi.



    Uwazi uliokuwa mbele yangu ulikuwa ni wa chumba kipana kilichokuwa kinatoka moshi kama vile kulikuwa kumewashwa moto ingawa moto huo sikuuona. Nikabaki nimesimama nikiangalia huku na huku.



    Ghafla nikasikia sauti kutoka chumba kingine. Zilikuwa sauti za wanawake waliokuwa wakisemeshana kwa lugha ambayo sikuielewa. Nilipata uhakika wa kutosha kuwa sauti mojawapo ni ya yule msichana niliyemfuata.



    Nikaenda upande ule nilikosikia sauti hizo. Palikuwa na uwazi uliotokana na kung’olewa kwa mlango. Nikasimama pembeni mwa ukuta na kuchungulia ndani ya uwazi huo. Nikawaona wanawake wawili waliokuwa warefu kama mnazi. Mmoja alikuwa amechutama akipulizia moto na mwenzake alikuwa amesimama.



    Aliyesimama nilimtambua, alikuwa ni yule msichana niliyemfuata pale..



    Hata hivyo hawakuwa na maumbo ya kibinaadamu. Licha ya kuwa warefu, walikuwa na nywele ndefu nyeupe. Pia waliota manyoya marefu mwilini. La kutisha zaidi walikuwa na miguu yenye kwato kama za punda!.



    Moyo wangu ulishituka sana. Hapohapo yule msichana ninayemfahamu aligeuza uso na kuniona. Macho yake yalikuwa yamebadilika na kuwa na mboni zilizosimama kama za paka na zilikuwa za rangi ya kibluu.



    “Wewe umefuata nini huku?” akaniuliza kwa fadhaa.



     Hapo hapo nilianguka na kupoteza fahamu. Sikujielewa tena.



    Nikiwa katika usingizi mzito nilisikia sauti ya yule msichana wa pili ikiuliza.



     “Ni nani?”



    “Si yule kijana niliyekwambia” Sauti ya yule msichana ninayemfahamu ikajibu.



    “Ulimuonesha hili geto letu?”



    “Sikumuonesha labda alinifuata”



    “Amefuata koti lake”



    “Atakoma! Si nilimwambia nitampelekea kesho”



    Hapo hapo nikajiona nazinduka. lakini badala ya kujikuta niko kwenye lile gofu, nilijiona ninazindukia kwenye lindo langu, bunduki yangu nikiwa nimeishika mkononi. La kushangaza zaidi ni kuwa lile koti langu nililomuazima yule msichana nilikuwa nimelivaa!.



    Nikashituka na kujiuliza nimefikaje hapa, wakati nilianguka na kupoteza fahamu nikiwa ndani ya lile gofu.



    Nani aliyenileta hapa? Nilijiuliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kumbu kumbu zangu za mwisho zilikuwa ni za mazungumzo kati ya wale wasichana wawili. Baada ya hapo sikukumbuka kitu kingine.



    Nilijikuta nimelala mbele ya lindo langu, nikainua uso wangu na kuangalia huku na huku, sikuona mtu yeyote. Nilikuwa peke yangu. Nikainuka na kuketi. Niliikagua ile bunduki na kugundua ilikwa na risasi zake sawasawa. Shaka yangu kuhusu bunduki ikaisha.



    Sasa nikawa najiuliza yule msichana na yule mwenzake niliyemkuta naye, walikuwa viumbe wa aina gani? Sikupata jibu.



    Ile hofu iliyonipata ndani ya lile gofu nilikuwa bado ninayo. Nilijuta kumfuatilia yule msichana lakini nilishukuru kujikuta nipo salama.



     Hata hivyo nilijiambia kama yule msichana atatokea tena mahali hapo muda ule, ningeliacha lindo na kumkimbia. Sikutaka kukutana naye tena katika maisha yangu..



    Sikujua ni kitu gani kilichonifanya nitupe macho kwenye lango la lile  ghala. Nikashituka nilipoona lango hilo lilikuwa wazi. Nikanyanyuka haraka na kwenda kuliangalia. Nilikuta makufuli yalikuwa yamevunjwa. Nilitoa tochi yangu ndogo na kumulika mle ndani. Ghala hilo lilikuwa karibu tupu kwani vitu vyote viilivyokuwamo vilikuwa vimesafishwa.



    Huo ulikwa ni mshituko mwingine nilioupata. Ghala limeibiwa! Huenda majambazi hao walikuja wakati nimemfuatilia yule msichana. Wakakuta hakuna mlinzi, wakavunja na kuiba kila kitu



    Kwa kweli nilichanganyikiwa. Nilipiga mluzi na kutikisa kichwa changu kwa fadhaa.



    Sasa nimekwisha!, nikajiambia.



    Kama ghala limevunjwa nani atakuwa mtuhumiwa namba moja?. Jibu lilikuwa rahisi. Mtuhumiwa namba moja nitakuwa mimi.



    Nitamueleza nini mwenye mali au nitawaeleza nini polisi?. Kwa vyovyote vile itaonekana nimekula njama na majambazi waje wavunje na kuiba.



    Jela nilikuwa ninaiona kwenye macho yangu. Hakukuwa na chochote cha kuninusurisha na kifungo.



    Nikatoa simu yangu. Sikukumbuka kupiga mahali popote zaidi ya polisi.



    Iliwachukua nusu saa tu polisi kufika katika eneo hilo. Nilijua kuwa walifika kwa haraka si kwa sababu niliwapa taarifa za kushitusha za kuvunjwa kwa ghala bali kituo  kikuu cha polisi hakikuwa mbali sana na eneo hilo.



    Walifika polisi sita wakiwa ndani ya Land Rover 110, kila mmoja akiwa na bunduki yake begani.



    Niliwaeleza juu ya tukio la kuvunjwa kwa ghala hilo na kuibiwa kwa mali zilizokuwamo.



    Swali la kwanza ambalo mmoja wa polisi hao aliniuliza lilikuwa.



    “Wewe ulikuwa wapi wakati majambazi hao wanavunja ghala?”



    Ilibidi niseme uongo wa kipumbavu kuwa nilikuwa nimepitiwa na usingizi. Na nilipozinduka nikakuta ghala limeshavunjwa.



    “Haiwezekani. Wewe na hao majambazi mmekula njama moja!” Polisi hao wakaniambia.



    Walilikagua lile ghala lililovunjwa kisha wakaniuliza kama nimeshamuarifu mkuu wangu wa kazi na mwenye mali



    Nikajibu “Bado sijawaarifu”



    “Tupe namba ya simu ya mkuu wako wa kazi”



    Nikawapa namba ya mkuu wangu wa kazi. Nilikuwa nikiifahamu kwa kichwa.



    Polisi hao wakampigia simu na kumuarifu juu ya kuvunjwa kwa ghala hilo pamoja na wizi uliotokea.



    “Tunakuomba ufike hapa haraka sana ukiwa na askari mwingine kwa sababu huyu tutaondoka naye”



    Polisi huyo akakata simu na kuniambia



    “Maelezo yako hayaridhishi. Utakuwa mtuhumiwa wetu namba moja”



    Sikuwa na la kumjibu kwani mazingira ya tukio zima yanaonesha na mimi ninahusika.



    Mkuu wangu wa kazi James Makete  alifika dakika chache baadaye akiwa na askari mwingine.

    Akajitanbulisha na kuelezwa na polisi hao kilichotokea. Makete hakuamini. Alikwenda kulikagua ghala hilo na kupigwa na bumbuazi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Imekuwaje Alfred?” akaniuliza.



    Nilimueleza kama nilivyowaeleza polisi.



    “Lakini Alfred hukuja hapa kulala, ulikuja kulinda hili ghala”



    ‘Nilipitiwa mzee”



    “Sasa sisi tunakwenda naye kwa hatua zaidi. Askari wako mwingine ataendelea kulinda hili ghala. Asubuhi uje kituo cha polisi cha Chumbageni pamoja na mwenye ghala hili” Polisi mmoja akamwambia mkuu wangu.



    Nilikabidhi bunduki kwa askari mwenzangu kisha nikapakiwa kwenye gari la polisi.



    Karibu njia nzima polisi hao walikuwa wakinisema mimi. Walinituhumu kwamba nimekula njama na hao majambazi waliovunja lile ghala na kwamba endapo hawatapatikana nitashitakiwa peke yangu.



    Tulipofika kituo cha polisi nilihojiwa na maelezo yangu yaliwekwa katika jalada kisha nikatupwa mahabusi.



    Humo mahabusi nilikuta watu kadhaa, wengine wakiwa wamelala kwa mtindo wa kukaa huku wengine wakiwa macho. Nilitafuta kipembe nikaketi kwa kujiegemeza kwenye ukuta.



    Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza katika maisha yangu sio tu kukamatwa na polisi, bali kutiwa mahabusi. Usiku ule ndio niliiona na kuijua mahabusi ilivyo. Chumba kidogo lakini kilijaa watu wengi. Kilikuwa na joto na hakikuwa na harufu ya kupendeza kwani choo hakikuwa mbali.



    Hata hivyo adha iliyokuwemo humo ndani haikunizuia kujiambia kuwa hukumu ya kosa langu ni kifungo kisichopungua miaka 30 jela. Ukilinganisha miaka hiyo na umri wangu, ilikuwa wazi kuwa ningefia jela au nitatoka jela nikiwa nimeshazeeka.



    Nililia bila kujali kuwa mahabusi wenzangu walikuwa wakiniangalia. Kwa upande mwingine nilikuwa nikimfikiria yule msichana aliyenisababishia nipate balaa hili.



    Sikujua alikuwa kiumbe wa aina gani. Alipokuja katika lindo langu na kuzungumza naye alikuwa binaadamu wa kawaida lakini nilipomuona tena akiwa ndani ya lile gofu hakuwa mwanaadamu. Alikuwa amebadilika. Alikuwa mrefu kupita kiasi, mwili wake ulikuwa umeota manyoya marefu na alikuwa na miguu yenye kwato kama ya punda



    Kila nilivyojaribu kuliwaza umbo lake, mwili wangu ulikuwa ukisisimka. Sikuweza kujua alikuwa kiumbe wa aina gani.



    Wakati ninalia, usingizi ulikuja kunichukua ghafla. Nikaota eti yule msichana amekuja kule mahabusi kuniangalia. Akaniambia.



    “Mimi sikukuambia unifuate, ulinifuata mwenyewe. Unaona sasa!”



    “Lakini wewe ndiye uliyesababisha. Kama ungeniletea koti langu, haya yasingetokea” na mimi nikamjibu.



    “Sasa sikiliza nikwambie, najua una uchungu na unanilaumu mimi. Nitakuonesha mali zilizoibiwa zilikopelekwa. Twende”



    Nikaona nimetoka mahabusi na yule msichana. Tukaenda katika eneo moja linaloitwa  Kisosora katika barabara inayoelekea Mombasa. Akanionesha nyumba moja na kuniambia.



    “Vitu vilivyoibiwa vimewekwa ndani ya nyumba hii. Na mwenye nyumba hii anawajua wote waliohusika kuvunja ghala na kuiba”



    “Sasa nikiulizwa nimejuaje kuwa vitu vilivyoibiwa vimeletwa humu, nitajibu nini? Si nitaonekana ninahusika?”  nikamuuliza msichana huyo.



    “Basi nitakuja mwenyewe kituo cha polisi asubuhi niwambie polisi nimeona vitu vikiingizwa usiku ndai ya nyumba hii”



    Aliponiambia hivyo nikazinduka. Nikaona kulikuwa kumeshakucha.. Waliingia polisi wawili wakatuhisabu kwa kutuita majina. Walipomaliza kutuhisabu waliondoka. Kila mahabusu akaenda kunawa uso na kurudi. Baada ya muda kidogo tuliletewa uji. Ulikuwa uji wa sembe uliotiwa chumvi. Baadhi ya mahabusu waliletewa chai kutoka majumbani kwao.



    Ilipofika saa mbili asubuhi alikuja polisi kuniita. Nikaenda naye katika ofisi ya afisa upelelezi wa wilaya. Afisa upelelezi mwenyewe alikuwa ameketi kwenye kiti. Pia kulikuwa na polisi wawili miongoni mwa wale polisi walionikamata usiku wakiwa wesimama huku wakiwa na bunduki walizokuwa wamezibeba tumboni.



    Mbali ya polisi hao kulikuwa na raia sita waliokuwa wamewekwa chini. Nilishuku kuwa walikuwa ni wahalifu.



    Mara tu nilipoingizwa katika ofisi hiyo afisa upelelezi aliwauliza wale watu kama walikuwa wananifahamu. Wote wakajibu kuwa hawakuwa wakinifahamu. Na mimi nikaulizwa kama nilikuwa nawafahamu watu hao. Baada ya kuwaangalia sikuona yeyote niliyekuwa namfahamu. Nikatikisa kichwa na kujibu kuwa siwafahamu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Una hakika kuwa  hakuna yeyote unayemfahamu miongoni mwa watu hawa?”Afisa upelelezi akaniuliza kwa mkazo.



    “Nina hakika, hakuna ninayemfahamu” nikamjibu.



    “Basi mrudishe” afisa upelelezi akamwambia yule polisi aliyenileta huku akiwa ameshikilia bunduki yake huku nikiwa na hofu kweli kweli.



    Nikarudishwa mhabusi. Sikujua watu wale walikuwa kina nani na kwanini nilipelekwa kuulizwa kama ninawafahamu ilhali siwafahamu.



    Baadaye tena kama saa nne hivi nilitolewa nikapelekwa tena katika ofisi ya afisa upelelezi wa wilaya. Nilimkuta afisa upelelezi, mkuu wangu wa kazi na mtu mmoja mwenye asili ya kiasia ambaye nilihisi alikuwa ndiye mmiliki wa ghala lililovunjwa.



    Afisa upelelezi akaniambia kwamba mnamo saa moja asubuhi alifika msichana mmoja pale kituoni ambaye alidai alikuwa mkazi wa eneo la Kisosora.  Akawaeleza kuwa aliona gari likishusha vitu usiku katika nyumba moja.



    “Akaendelea kutueleza kwamba alishuku kuwa vitu vile vilivyokuwa vinashushwa vilikuwa vya wizi hivyo akatuomba twende katika nyumba hiyo kuchunguza” Afisa upelelezi huyo akaniambia na kuendelea.



    “Tukaenda katika nyumba hiyo ambayo yule msichana alituelekeza. Tulifanya upekuzi na tuligundua kuwa vyumba viwili vya ndani na vyumba vitatu vya uani vilikuwa vimejaa mali ambayo tuliikamata.



    “Vilevile tulikamata watu wawili tuliowakuta wamelala katika chumba kimoja. Baada ya kuwahoji tuligundua kuwa walikuwa majambazi kwani mmoja wao tulikuwa tunamtafuta. Wakatueleza kwamba walikwenda kuvunja ghala moja usiku huko Gofu na waliwataja wenzao wanne ambao pia tulikwenda kuwakamata”  Afisa upelelezi aliendelea kuniambia.



    Akaniambia mwenye ghala lililovunjwa  alipooneshwa ile mali iliyoletwa pale kituo cha polisi alithibitisha kuwa ni mali yake iliyoibiwa na kuonesha hati zote za umiliki.



    “Tulipokuita mara ya kwanza, wale uliowakuta walikuwa ndio majambazi wenyewe tuliowakamata. Tulipowahoji wote walisema hawakujui na wewe tulipokuuliza ulisema huwajui. Sisi tulikuwa tunadhani mlishirikiana, kumbe haikuwa hivyo. Kwa hiyo kwa vile mali iliyoibiwa imepatikana na majambazi waliohusika wamekamatwa, tumeamua kukuachia. Mshukuru sana yule dada aliyewezesha kupatikana kwa ile mali na wale majambazi kukamatwa”



    Nikashusha pumzi ndefu za faraja. Hapohapo niliikumbuka ile ndoto niliyoota nikiwa mahabusi. Yule msichana aliniambia atakuja yeye pale kituoni kutoa taarifa kuhusu majambazi hao, na ndivyo ilivyokuwa.



    Ingawa niliachiwa na kutakiwa kufika tena hapo kituoni kesho yake asubuhi, nilikutana na zahama jingine. Nilipofika ofisini kwetu nilipewa barua ya kufukuzwa kazi kwa kosa la kufanya uzembe na kulala nikiwa katika lindo na kusababisha lindo kuvunjwa na mali kuibiwa.



    Baada ya kupewa barua hiyo nilishukuru na kurudi nyumbani. Niliketi kitandani na kujiambia, balaa hilo  la kukamatwa na hatimaye kufukuzwa kazi, ulikuwa mkosi uliotokana na yule msichana ambaye mpaka muda ule sikuweza kutambua alikuwa kiumbe wa aina gani.



    Baada ya kutafakari kwa kina, nilijiambia yaliyopita yameshapita, sasa ni kuganga yaliyopo na yajayo. Kama ni yule msichana sitaweza kumjua. Na kama ni kazi nimeshafukuzwa. Sasa liliopo ni kujaribu kuandika barua kuomba sehemu nyingine. Kulikuwa na makampuni mengi ya ulinzi yaliyokuwa yanahitaji walinzi hasa vijana kama mimi.



    Siku ileile niliandika barua kadhaa na kuzipeleka katika ofisi za makampuni mbalimbali ya ulinzi. Nilitegemea katika makampuni hayo sitakosa kampuni mojawapo itakayonipatia kazi.



    Usiku wa siku ile kabla sijalala, nilisoma biblia yangu, nikasali na kuomba. Nilitegemea kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu sitakaa muda mrefu kabla ya kupata kazi.



    Ingawa nilikuwa nimesongwa na mawazo mengi kwa kuachishwa kazi ghafla, sikuchelewa kupata usingizi nikalala. Nikazinduka usiku mwingi. Nikahisi kama kulikuwa na mtu ananiita. Nikatega masikio yangu kusikiliza.



    Kwanza palipita ukimya wa kama dakika moja hivi kisha  nikasikia tena sauti ikiita jina langu. Ilikuwa sauti ya mwanamke niliyoitambua. Lakini sikuweza kukumbuka mara moja ilikuwa sauti ya nani na alikuwa wapi.



    “Alfred! Alfred!” Sauti hiyo iliendelea kuita. Moyo wangu ulishituka. Nikaendelea kutega masikio.



    Niligundua kuwa ile sauti ilikuwa ikitokea mlango wa nje.



    Ni nani anayeniita usiku huu? Nilijiuliza bila kupata jibu. Sauti iliyokuwa ikiniita iliacha kwa muda kisha ilianza kusikika tena. Na sasa aliyekuwa akiita alianza kubisha mlango.



    Hapo hapo akili yangu ikazinduka. Nilitambua kuwa ile sauti ilikuwa ya yule msichana niliyemuazima koti langu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ameijuaje nyumba ninayoishi na kwa nini amenifuata nyumbani? Anataka nini? Nilijiuliza kwa mshituko.



    Ataita na kubisha mpaka watu wa nyumba nzima wataamka, mimi sitatoka, nikajiambia.



    Na kweli, aliita na kubisha mpaka ile sauti ikapotea, kukawa kimya. Hata hivyo mimi sikulala tena mpaka asubuhi.



    Ile ilikuwa ni mara ya kwanza. Usiku wa siku ya pili yake nilishituka tena usingizini nikaisikia ile sauti ikiniita. “Alfred! Alfred!”



    Safari hii aliita na kubisha mara chache tu kisha nikasikia mlango wa nje unafunguliwa. Moyo wangu ulishituka. Hakukuwa na mtu yeyote mle ndani aliyeuliza “wewe nani?” Nikahisi pengine sauti ya msichana huyo na sauti ya kufunguliwa kwa ule mlango nilizisikia peke yangu.



    Baada ya mlango huo kufunguliwa nilisikia mlio wa ko! ko! ko! hapo ukumbini. Nikahisi ulikuwa mlio wa viatu ama wa kwato za yule msichana. Punde tu nilisikia mlango wa chumba changu unabishwa huku ile sauti ya msichana ikiita jina langu. “Alfred! Alfred!”



    Moyo ulikuwa ukinienda mbio kama uliotaka kutoka. Nilinyamaza kimya. Nilikuwa nimejifinika shuka gubigubi. Msichana aliendelea kubisha na kuniita kwa karibu dakika mbili. Alipoona siitikii wala sifungui mlango, nilisia anaondoka. Alirudi mlango wa nje akatoka kisha akafunga mlango. Baada ya hapo sikusikia kitu tena.



    Kwa kweli sikulala tena. Niliendelea kukaa macho hadi saa 12 asubuhi. Nikawa mtu wa kwanza kutoka chumbani. Nilikwenda mlango wa mbele nikitegemea ningeukuta mlango huo ukiwa umefunguliwa lakini nilikuta umefungwa kwa ndani vile vile.



    Nikajiuliza yule msichana aliufunguaje na kuweza kuingia wakati mlango huo ulifungwa kwa ndani? Kwa kweli sikuweza kupata jibu.



    Nilirudi chumbani nikakaa kitandani na kufikiria kwamba msichana huyo anaweza kuharibu maisha yangu kama ambavyo alishaanza kuyaharibu. Sikuweza kujua ni kitu gani kilichomfanya anifuatefuate.



    Hofu yangu ilikuwa kwamba usiku wa juzi alibisha mlango wa mbele, usiku uliofuata akaingia ndani na kubisha mlango wa chumba changu. Usiku wa leo anaweza kuja kuingia chumbani mwangu!



    Baada ya kutafakari vizuri nilitoka nikaenda kupiga mswaki na kuoga. Niliporudi nilivaa kisha nikatoka. Nilikwenda katika kibanda cha mama lishe ambako hunywa chai kila asubuhi. Nikanywa chai kisha nikatoka.



    Nilikuwa nimeamua kwenda kwa Mchungaji wa kanisa letu ili nimueleze matatizo yangu nione jinsi ambavyo atanisaidia.



    Nilikuwa nimepata hofu kuwa endapo sitamueleza Mchungaji, yule msichana wa ajabu anaweza kuendelea kunifuatafuata wakati sikujua lengo lake lilikuwa nini. Na baya zaidi nilishuku kuwa  usiku ule angeweza kuniingilia chumbani mwangu.



    Wakati nataka kuingia katika wigo wa kanisa niliona msichana amesimama pembeni mwa lango la kanisa akiniangalia kwa macho makali huku amekunja uso. Nilipomuangalia vizuri niliona alikuwa ni yule msichana wa ajabu.



    Nikashituka na kugeuza uso wangu haraka nikijifanya sikumuona. Nikaingia ndani ya ua wa kanisa. Baada ya kupiga hatua tatu dukuduku lilinishika, nikageuza uso nyuma kumuangalia. Akanionesha ishara ya kuniita.



    “Njoo “ akaniambia bila kutoa sauti. Aliniambia kwa midomo tu kama anayezungumza na mtu asiyesikia.



    Nilipoona ananiita niligeuza tena uso wangu na kuendelea kwenda. Lakini sikufika mbali niligeuka tena nyuma  kumuangalia

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sasa nilimuona amesimama katikati ya lango akiniita kwa kunipungia mkono.



    “Nimekwambia njoo!” akaniambia bila kutoa sauti yake.



    Nikawa ninaenda huku namuangalia yeye. Alipoona nazidi kwenda aliacha kuniita. Akawa ananitazama kwa uso wa huruma kama kiumbe kisicho na hatia. Alikuwa na uso wenye sura ya mvuto. Macho yake makubwa yalilegea na kutoa nuru ya kunilaani kwa kutomjali.



    Wakati ninakwenda huku naangalia nyuma, nilimkumba mtu aliyekuwa anatoka. Nikageuka haraka  na kumuomba msamaha. Kumbe alikuwa Mchungaji.



    “Bahati mbaya, endelea tu” akaniambia alipoona nimegwaya.



    “Nilikuwa nakuja kwako”



    “Na mimi nilikuwa natoka lakini naweza kurudi kwa ajili yako”



    “Nitakushukuru baba, nina matatizo makubwa”



    Mchungaji huyo alinipeleka katika ofisi yake akanikaribisha kwenye kiti kisha na yeye akaketi.



    “Sasa unaweza kuzungumza shida yako” akaniambia.



    Nikamueleza matatizo yangu tangu mwanzo hadi yalipofikia.



    Mchungaji akashangaa. “Sijawahi kusikia kisa kama hicho ulichonieleza!”



    “Na huyo msichana nimekutana naye kwenye lango sasa hivi, alikuwa ananiita. Pale nilipokukumba nilikuwa namtazama yeye!” nikamwambia.



    “Kwanini usinioneshe pale pale?. Hebu twende”



    Mchungaji aliinuka na mimi nikanyanyuka. Tukatoka kwenda kwenye lango. Tulipofika hatukumkuta yule msichana.



    “Naona ameshaondoka alikuwa amesimama hapa”



    Nilimuonesha Mchungaji mahali alipokuwa amesimama yule msichana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Pia nataka twende ukanioneshe hilo gofu ambamo uliwakuta” Mchungaji akaniambia na kuongeza “Tutakwenda kwa gari langu”



    “Sawa, twende nikakuoneshe”



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog