Search This Blog

NILIOA JINI NA KUZAA NAE - 2

 





    Simulizi : Nilioa Jini Na Kuzaa Nae

    Sehemu Ya Pili (2)



    ILIPOISHIA..



    Mchungaji aliinuka na mimi nikanyanyuka. Tukatoka kwenda kwenye lango. Tulipofika hatukumkuta yule msichana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naona ameshaondoka alikuwa amesimama hapa”

    Nilimuonesha Mchungaji mahali alipokuwa amesimama yule msichana.

    “Pia nataka twende ukanioneshe hilo gofu ambamo uliwakuta” Mchungaji akaniambia na kuongeza “Tutakwenda kwa gari langu”

    “Sawa, twende nikakuoneshe”

    ENDELEA

    Mchungaji alikwenda kutoa gari lake akanipakia na tukaelekea Gofu. Tulifika katika lile ghala nililokuwa ninalinda nikamuonesha. Kisha tukaenda katika lile jumba la zamani lililokaa kama gofu.

    “Ndipo hapa?” akaniuliza huku akishangaa.

    “Ndipo hapa” nikamjibu.

    Tulishuka kwenye gari tukawa tunalitazama gofu hilo.

    “Wewe ulikuja saa nane usiku mahali hapa?”

    “Ndiyo, nilikuja kumfuata yule msichana”

    “Inaelekea una roho jasiri sana. Mahali hapa wakati wa usiku panatisha sana. Hebu tuingie ndani”

    Sikutaka kutangulia kuingia. Nilimuacha Mchungaji atangulie yeye. Kabla ya kuingia alisali kwanza na mimi nikasali kisha tukaingia.

    Tulikwenda hadi katika kile chumba nilichomkuta yule msichana akiwa na mwenzake wakiwa katika maumbo yasiyo ya kibinaadamu.

    Tulipoingia ndani ya chumba hicho tulikuta mafiga matatu ya jiko na rundo la majivu. Licha ya kulikagua jumba lote hatukukuta mtu zaidi ya makorokoro ambayo tulihisi yalirundikwa na wendawazimu.

    “Basi twende zetu” Mchungaji akaniambia.

    Tulitoka, tukapanda gari na kuondoka.

    “Una hakika hukuwa umeota?” Mchungaji akaniuliza.

    “Sikuota, nilifika kweli na kuwaona hao wasichana”

    Mchungaji akanyamaza kimya.

    Tulikwenda hadi katika lango la kanisa. Mchungaji akaniambia.

    “Kesho ni jumapili, uje katika ibada ya asubuhi. Tutakufanyia maombi”

    “Nitakuja kesho asubuhi lakini nataka kuuliza, kwa leo hatanifuata tena?”

    “Hatakufuata kwa maana ameona umejisalimisha mahali ambapo hapawezekani”

    “Namshukuru sana Yesu”

    “Ondoa wasiwasi, tatizo lako litakwisha. Sasa unaweza kushuka uende zako”

    “Asante baba Mchungaji”

    Nikashuka kwenye gari na kufunga mlango na kwenda zangu. Nilizungukazunguka mjini kasha nikarudi nyumbani.

    Ilipofika usiku, nilikwenda kula chakula kisha nikarudi. Sikuwa na matembezi ya usiku. Baada ya kukaa kidogo nilichukua Biblia yangu nikasali kisha nikalala.

    Ilipofika saa nane usiku nilishituka usingizini, nikaona taa ilikuwa inawaka. Kumbe nilisahau kuizima kabla ya kulala. Mara nilisikia mlango wa chumba changu unabishwa. Moyo wangu ukashituka na kuanza kunienda mbio.

    Nikasikia sauti ya msichana ikiita

    “Alfred! Alfred! Nifungulie…”

    Mara moja niliitambua sauti ya yule msichana, nikanyamaza kimya. Lakini ghafla niliona mlango wa chumba unafunguka.

    “Mama yangu wee…nimekwisha!” nikajisemea kimoyomoyo.

    Mlango ulifunguka na kuwa wazi kabisa. Mbele ya mlango nilimuona msichana amesimama akiangalia ndani. Sikujua ule mlango aliufungua yeye au ulifunguka wenyewe kwani mikono yake haikuwa imeshika mlango.

    Alikuwa amevaa dera jeupe lililoziba viatu vyake. Na sikujua kama alikuwa na viatu au kwato. Alijitanda upande wa kitambaa cheupe kichwani, akauziba uso wake kwa mtindo wa kiarabu. Masikio yake hayakuwa yakionekana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa ajabu, jinsi macho ya msichana yule yalivyokuwa yanabadilika. Nilivyoyaona usiku ule hayakuwa kama nilivyoyaona wakati wa mchana pale kwenye lango la kanisa. Muda ule wa mchana yalikuwa macho ya kawaida lakini sasa yalikuwa yamebadilika na kuwa na mboni za kijivu.

    Alikuwa ameyapaka wanja mkali na kwenye nyusi pia alipaka wanja mweusi uliokaa kama upindi wa mvua.

    Alikuwa akitabasamu peke yake na kuifanya sura yake ionekane ya kupendeza na ya kirafiki.

    Mlango ulipokuwa wazi aliinua hatua na kuingia ndani. Moyo ulinilipuka ukawa unanienda mbio na kijasho chembamba kikaanza kunivuja.

    Kitu ambacho kilinishangaza muda wote ni kuwa nilikuwa nimejifinika shuka gubigubi na kuziba uso wangu lakini bado nilikuwa namuona yule msichana.

    Alipoingia ndani alisimama katikati ya chumba na kukitupia macho chumba changu kisha nikamuona anatikisa kichwa kama vile chumba changu hakikumridhisha.

    Wakati amesimama hapo, kupuo la harufu ya manukato yake ilienea chumba kizima. Sijawahi kusikia manukato mazuri kama yale niliyoyasikia usiku ule.

    Baadaye nilimsikia akishusha pumzi kisha akaenda kuketi kwenye kiti kilichokuwa kando ya meza, akauweka mguu wake mmoja juu ya mwingine kisha akanitazama.

    “Alfred!” akaniita. “Inuka tuzungumze, nimekufuata wewe mpenzi wangu”

    Nikanyamaza kimya.

    “Usiniendee kwa Mchungaji. Mimi si adui yako. Mimi ni rafiki yako mwenye lengo la kukusaidia” akaniambia.

    Ingawa nilijifanya nimelala, aliendelea kunisemesha kama vile alijua kuwa nilikuwa macho.

    “Alfred nataka tuwe marafiki. Tangu siku nilipokuona nilikuchunuka. Sitaficha kukwambia kuwa nimekupenda na utakuwa mume wangu”

    Ndani ya moyo wangu nilikuwa najiuliza, huyu msichana alikuwa kiumbe wa aina gani?

    Hapo hapo nikamsikia akinijibu. “Mimi ninaitwa Banuna. Ninatoka katika kizazi cha familia ya kijini. Kwetu ni chini ya bahari, karibu na kisiwa cha Unguja.”

    Alivyoniambia kwamba yeye ni jini anayeishi chini ya bahari alinishitua sana, nikakurupuka pale kitandani na kutoka mbio huku nikiburuza shuka. Nilifungua mlango nikatoka ukumbini nikiwa na chupi tu, shuka nilikuwa nimeishikilia. Nilikimbilia mlango wa mbele nikaufungua na kutoka nje kisha nikaufunga tena.

    Nilijifunga ile shuka kwenye shingo nikatembea kwa mwendo wa haraka haraka kuelekea mtaa wa pili alikokuwa akiishi rafiki yangu fulani aliyeitwa Juma.

    Nilikuwa natembea huku nikiangalia nyuma. Nilikuwa na wasiwasi kwamba yule msichana anaweza kunifuata.

    Lakini hadi ninafika katika mtaa huo sikumuona yule msichana. Nikaenda katika ile nyumba anayoishi Juma. Nilibisha kwenye dirisha la chumba

    chake lililokuwa upande wa mbele.

    “Juma! Juma!” nilimuita. “Amka unifungulie mlango”

    Baada ya muda kidogo, sauti ya Juma ikasikika ikiuliza.

    “Nani wewe?”

    “Ni mimi rafiki yako Alfred, nimepata matatizo, nifungulie mlango”

    “Wewe ni Alfred?”

    “Ndiyo”

    “Subiri”



    Nikasubiri. Baada ya kupita kama dakika tatu hivi, Juma alifungua mlango akatoka. Alipoona nimejifunga shuka alishituka.

    “Vipi tena Alfred?” akaniuliza.

    “Tuingie ndani nikueleze” nikamwambia.

    “Karibu”

    Tukaingia ndani. Alinikaribisha chumbani kwake. Yeye aliketi kitandani, mimi nikakaa kwenye kiti.

    Nikamueleza mkasa wa yule msichana wa kijini, tangu nilivyoanza kukutana naye hadi alivyoniingilia chumbani usiku ule.

    Juma nilipomueleza alishituka.

    “Unasema kweli?” akaniuliza huku amenikazia macho.

    Nakueleza ukweli, huyo msichana nimemuacha chumbani mwangu na kukimbilia hapa kwako. Hata nguo sikuwahi kuvaa”

    “Amekwambia mwenyewe kwamba yeye ni jini?” Juma akaniuliza.

    “Ndiyo ameniambia. Mlango niliufunga kwa ndani lakini ulifunguka wenyewe, akaingia”

    “Dah! Sasa utafanyaje rafiki yangu?”

    “Jana nilikwenda kwa Mchungaji akaniambia atanifanyia maombi hii leo”

    “Unadhani atakapokufanyia maombi, huyo jini hatakufuata tena?”

    “Hatanifuata”

    “Basi ni vizuri ufanyiwe hayo maombi haraka kwani inaonekana huyo msichana atakusumbua. Anataka uwe mume wake. Utaishije naye wakati yeye ni jini?”

    “Hapo sasa!”

    “Pole sana Alfred. Ni matatizo makubwa yaliyokukuta! Sasa utalala wapi?”

    “Nakuomba unisindikize nyumbani nikavae nguo na nifunge milango. Mlango wa chumbani mwangu na wa nje ipo wazi”

    ‘Umesema yule msichana yuko chumbani mwako?”

    “Atakuwa ameshaondoka baada ya mimi kukimbia”

    “Ngoja nivae twende” Juma akaniambia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya dakika kumi hivi, mimi na Juma tukawa tunakwenda katika nyumba niliyokuwa ninaishi. Kwa vile nilikuwa na mwenzangu. Hofu ilinipungua.

    Tulipofika nyumbani nilisukuma malango tukaingia ndani. Tulikwenda kwenye mlango wa chumba changu nikamwambia Juma aufungue yeye.

    Juma akaufungua mlango na kuchungulia ndani.

    “Yumo?” nikamuuliza kwa sauti ya kunonong’ona.

    “Sioni mtu” Juma alinijibu huku akitumbukiza mguu wake ndani. Aliangalia pande zote za chumba kabla ya kuingia kabisa.

    “Ingia, hayumo”akaniambia. Nikaingia.

    Chumba changu bado kilikuwa kina harufu ya manukato yake. Juma aliyasikia.

    “Mbona kunanukia hivi? Unatumia manukato gani?”

    “Ni yule msichana aliyeingia….”

    “Ananukia manukato namna hii!....ni jini kweli!”

    “Tena hii harufu imepungua. Naona ameondoka muda mrefu”

    “Viumbe hawa wanapenda sana manukato!”

    Wakati tunazungumza na Juma nilikuwa nikivaa suruali yangu na shati. Juma aliketi kwenye kiti.

    “Sasa unavaa uende wapi?”

    “Navaa turudi kwako”

    “Kwanini tujisumbue? Huyo msichana si ameshaondoka?”

    “Hata kama!. Ile imani ya kubaki humu sina kabisa”

    “Tutabaki sote mpaka kutakapokucha. Kule nimeshawambia wafunge mlango. Siwezi kwenda kuwasumbua tena.”

    “Basi tutabaki hapa hapa sote. Tukiwa wawili si neno”

    Tukakaa mle chumbani na Juma mpaka asubuhi. Juma aliondoka saa kumi na mbili asubuhi akaniacha ninakwenda kuoga. Niliporudi nilivaa nikawa nasubiri muda wa kwenda kanisani. Siku ile sikukumbuka kunywa chai kabisa

    Muda wa kwenda kanisani ulipowadia nilitoka nikaenda kanisani. Baada ya ibada waumini wenye matatizo mbalimbali waliitwa ili waombewe. Na mimi nikawemo.

    Wenye mapepo yalitolewa na wenye magonjwa mengine walipata nafuu. Mimi niliombewa mpaka machozi yakanitoka. Niliamini kabisa yule jini ametokomezwa mbali au ameshateketezwa kwa moto.

    Baada ya kipindi hicho cha maombi kilichochukua karibu saa mbili, tulitoka kanisani nikiwa na furaha. Furaha yangu ilinifanya nisalimiane na kila ninayemuona ingawa haikuwa kawaida yangu.

    Nilipotoka kwenye lango la kanisa, nilimuona Juma amesimama kando ya lango hilo. Nikamfuata.

    “Mbona uko hapa?” nikamuuliza.

    “Nimekufuata wewe. Umeshafanyiwa maombi?”

    “Tayari. Nashukuru nimeombewa sana”

    “Sasa hivi hofu yako imekwisha kabisa?”

    “Imekwisha. Leo najiona kama nimezaliwa upya”

    “Kwanini Alfred?”

    “Nimeepushwa na yule shetani aliyekuwa ananisumbua na nimeambiwa na Mchungaji nisiache ibada. Kwa vile nimeshampokea Yesu sitaacha kabisa”

    “Ni vizuri kama matatizo yale yamekwisha. Kwa sasa utaweza kulala peke yako?”

    “Bila shaka yoyote. Yule jini hawezi kunifuata tena

    “Na mimi nimefurahi Alfred. Twenzetu”

    Tukaondoka na Juma.

    “Juma umeshakunywa chai?” nikamuuliza wakati tukienda. Sasa nilikuwa nasikia njaa.

    “Mimi nimeshakunywa, sijui wewe?”

    “Mimi bado. Asubuhi nilikuwa na kihoro, sikukumbuka kunywa chai”

    “Sasa utakwenda kunywa wapi?”

    “Mimi nakunywa chai kwa kina mama lishe”

    “Tena kibanda cha mama lishe kile pale”

    Juma alinionesha kibanda cha mama lishe kilichokuwa kwenye uchochoro. Tukaenda.

    Nilikunywa chai. Baada ya hapo Juma alinisindikiza hadi nyumbani. Tukaagana.



    Kutoka siku ile yule jini hakunifuata tena, nikawa nimefurahi. Lakini baada ya kupita juma moja nilianza kuota ndoto za ajabu ajabu, nyingine zikiwa za kutisha.

    Kusema kweli hazikuwa ndoto za kawaida kwani zilifululiza kama mkanda wa sinema, ikimalizika hii inakuja hii. Wakati mwingine ninaota nipo kwenye majabali marefu nikiwa na msichana

    ambaye ghafla huanza kunilaumu kuwa nimemgeuka. Lakini mara sura yake hubadilika na kuwa ya yule msichana wa kijini. Hapo huanza kumkimbia na kila ninavyokimbia yule msichana hutokea mbele yangu.

    Wakati mwingine huzinduka usingizini lakini usingizi unaponijia tena, ile ndoto huendelea. Inapoendelea hujikuta nimefika kingoni mwa jabali ambapo yule msichana hunisukuma, nikajiona naanguka kutoka juu ya jabali refu huku ninapiga kelele.

    Inapomalizika ndoto hii inakuja nyingine. Huota nipo kwenye maeneo ya makaburi. Ghafla miili ya watu waliokufa hutoka katika makaburi na kunifuata ikiwa mifupa mitupu. Ninatoka mbio lakini najiona ninavutwa kwa nyuma kama ninayevutwa kwa sumaku hadi ile mifupa inanikaribia na kunigombania na ndipo ninapozinduka.

    Ndoto za namna hiyo ziliniandama karibu kila siku. Mwisho nilirudi tena kwa yule Mchungaji kumueleza, akanifanyia maombi tena lakini ndoto hazikukoma. Nilipoona hali inazidi kuwa mbaya nikahamia kwa rafiki yangu Juma.

    Kwa Juma pia sikupata nafuu yoyote. Ndoto ziliendelea kuniandama huko huko. Siku moja niliota nachinjwa nikapiga ukulele uliomuamsha Juma. Alipoamka aliniuliza.

    “Una nini Alfred?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jasho lilikuwa linanitoka na moyo ulikuwa unanienda mbio kama ulitaka kutoka. Nikaketi kitandani na kumueleza nilivyoota Hata yeye aliogopa. Siku ile hatukulala tena hadi asubuhi.

    “Uende kwa mganga” Juma akaniambia asubuhi. Alinielekeza kwa mganga mmoja aliyekuwa akikaa kitongoji cha Amboni. Kitongoji hicho kipo umbali wa kilometa 10 hivi kutoka jiji la Tanga.

    Akaniambia kaka yake alikuwa na tatizo kama langu la kuota ndoto za kutisha lakini alipokwenda kwa mganga huyo tatizo hilo likamalizika.

    “Huyo mganga anaitwa nani?”

    “Anaitwa Mtemi Wembe”

    “Nitakwenda Amboni kumuulizia”

    “Ningekupeleka lakini ndiyo hivyo ninakwenda kazini na kurudi ni jioni”

    “Hakuna tatizo, kwa vile umeshanielekeza nitakwenda mwenyewe”

    Juma alipoondoka kwenda kazini kwake na mimi niliondoka kwenda huko Amboni. Nilikwenda stendi nikapanda daladala za kwenda Amboni. Nilipofika Amboni nilimkuta mtu mmoja akichoma mahindi ya kuuza palepale kwenye kituo cha daladala. Nikamuuliza kama anamfahamu mganga Mtemi Wembe.”

    “Ni maarufu” akanijibu na kuongeza..

    “Kamata barabara hii, nenda moja kwa moja. Mbele kule utakuta njia mbili, moja inaelekea kulia na nyingine kushoto. Fuata ile ya kushoto, ukienda mbele utakuta mbuyu. Ukiupita mbuyu utakata tena kushoto. Nyumba utakayoikuta mbele yako ndiyo hiyo ya Mtemi Wembe”

    Ilikuwa kama alivyonielekeza Juma. Nikamshukuru yule mtu kisha nikafuata ile barabara aliyonielekeza hadi nikauona ule mbuyu. Nilipokata kona kushoto nikaiona ile nyumba. Nikaenda

    Nilikuta watu kadhaa wakiwa nje wameketi kwenye gogo la mnazi wakisubiri zamu ya kuingia. Na mimi nikaenda kujiunga nao. Kulikuwa na watu wengine waliokuja nyuma yangu. Sote tukawa tunasonga taratibu kuelekea kwenye mlango wa nyumba ya mganga.

    Ghafla nilisikia harufu ya manukato makali puani mwangu, nikageuza uso wangu na kumtazama msichana aliyekuwa ameketi kushotoni kwangu. Nikashituka nilipoona ni yule msichana wa kijini. Alikuwa ameketi sambamba na mimi. Wakati namtazama na yeye alikuwa akinitazama.

    “Amekuja muda gani?” nikajiuliza kimoyomoyo huku nikiwa nimepatwa na mshangao.

    Ukweli ni kuwa nilipofika hapo, msichana huyo hakuwepo. Bila shaka alikuwa miongoni mwa watu wanne waliokuja baada ya mimi. Lakini kwa vyovyote vile kuja kwake kulikuwa kwa kimiujiza kwani sikumuona alivyofika, nilishitukia tu yupo hapo baada ya kusikia harufu ya manukato yake.

    Kwa jinsi nilivyoshituka, moyo wangu ulianza kunienda mbio. Sikuwa na raha tena. Nikanyanyuka ghafla na kuondoka kama mtu ambaye nilikuwa nimeghairi kuingia kwa mganga kwani nilihisi angenifuata humo ndani.

    Nilitenbea haraka haraka nikakata kona kwenye ule mbuyu kisha nikaanza kukimbia. Nilipokata kona nyingine kuelekea upande wa kulia. Ghafla nikamuona yule msichana mbele yangu.

    Nikasisimama ghafla. Kwa kweli niligwaya. Nikawa namtazama na yeye akanitazama. Macho yake yalikuwa makali kama kaa la moto na uso alikuwa ameukunja.

    “Unajisumbua bure!” akaniambia.

    Ingawa alionekana kukasirika lakini sauti yake ilikuwa tulivu.

    “Mimi sikimbiliki. Nimeshakuzunguka pande zote. Kama unaweza kuingia chini ya ardhi ingia, ndio sitaweza kukufuata. Lakini huku juu ya ardhi hata kama utakimbilia Ulaya nitakufuata tu!” akaniambia.

    Nilikuwa nimenyamaza kimya nikimtazama na kumsikiliza huku nikirudi nyuma taratibu. Pakapita ukimya mfupi.

    “Ulienda kwa mganga kufuata nini?” akaniuliza ghafla na kuongeza.

    “Unadhani mganga ataweza kunifukuza mimi? Mimi sifukuziki!”

    Akaendelea kuniambia “Mimi ni Banuna mwana wa Ziraili. Ukoo wetu ni wa wachawi. Babu yangu ni mkuu wa wachawi! Hakuna mganga atakayeniweza mimi”

    Akanyamza na kunitazama jinsi nilivyokuwa ninahema kisha akaendelea.

    “Ni kwa sababu tu nimekupenda ninakuruhusu urudi nyumbani. Lakini ninakupa muda mwingine mfupi ufanye maamuzi sahihi. Ukiendelea kuniletea kisoi utajuta!”

    Baada ya kuniambia hivyo alichora msitari chini kwa mguu wake, akaniambia.

    “Vuka huu msitari urudi nyumbani”

    Nilikuwa nimepatwa na hofu isiyo na kifani. Sikuelewa alikuwa ananiambia nini,mpaka aliporudia kwa mara ya pili.

    “Nimekuambia vuka huu msitari urudi nyumbani. Nisikuone tena kwenye nyumba za waganga!’

    Nikapiga hatua haraka haraka kuvuka ule msitari aliouchora chini kwani alikuwa amesogea kando. Nilipouvuka tu ule msitari nikajikuta nipo mbele ya nyumba ninayoishi. Sikuwapo tena mahali pale nilipokuwa na yule msichana wa kijini!.

    Huku nikiwa nimeshikwa na mshangao uliochanganyika na hofu, niliangalia upande wa kulia na wa kushoto. Sikumuona tena yule msichana

    Nikawa najiuliza nimefikaje pale nyumbani? Hatua moja tu niliyopiga kuvuka ule msitari imenifikisha katika nyumba ninayoishi? Ilikuwa miujiza mikubwa!.

    Badala ya kuingia ndani niligeuka nikaelekea nyumbani kwa Juma, Juma alikuwa yupo kazini kwake lakini kwa vile alikuwa ameniachia ufunguo mmoja, nilifungua mlango nikaingia ndani. Nikafikia kujilaza kitandani.

    Ingawa sikuwa na yule msichana, hofu ilikuwa imenitawala na kusababisha nijisikie kupata homa.

    Siku ile sikutoka tena mle chumbani mpaka Juma aliporudi jioni. Alikuta nilikuwa nikitetemeka kwa homa.

    “Alfred unaumwa?” akaniuliza.

    “Nasikia homa”

    “Tangu saa ngapi?”

    “Tangu asubuhi”

    “Dah! Umeshakula dawa?”

    “Bado. Kwanza hebu kaa nikueleze yaliyotokea kule kwa mganga”

    Huku akionekana kupata wasiwasi, Juma alikaa kwenye kiti. Nikamueleza yale yaliyonitokea kule Amboni na nilivyorudishwa nyumbani kimiujiza.

    Juma akashangaa.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa baada ya tukio hilo umefanya nini?” akaniuliza.

    “Nimekusubiri wewe unipe ushauri wako. Unajua kwa sasa hivi mimi sina akili kabisa”

    “Kwa sasa hivi huna akili kabisa?” Juma akaniuliza. Kama si ule mkasa wa kusikitisha ulionipata, bila shaka Juma angeangua kicheko kikali kutokana na jibu langu hilo.

    “Kwa kweli sina akili” Lilikuwa jibu la kipumbavu lakini ulikuwa ndio ukweli wenyewe.

    “Alfred umefanya kosa moja kubwa!” Juma akaniambia.

    “Kosa gani?”

    “Usingeondoka pale kwa mganga. Ungesubiri zamu yako ya kuingia ukamueleza yule mganga matatizo yako na kumuonesha yule msichana. Ingekuwa vizuri sana”

    “Nilipatwa na hofu nikajikuta ninaondoka tu”

    “Labda ni yeye aliyekuondoa kimiujiza ili usiingie kwa yule mganga”

    “Inawezekana”

    “Sasa inaonekana wewe peke yako hutaweza kujishughulikia. Acha mimi niende Amboni kwa yule mganga nimueleze matatizo yako”

    “Utaenda sasa hivi?”

    “Itabidi niende sasa hivi”

    “Sawa, basi wewe nenda”

    Maelezo yangu pamoja na hali niliyokuwa nayo vilimtia wasiwasi Juma. Akaondoka muda uleule kwenda Amboni. Mimi nikaendelea kulala. Nilipojihisi kupata nafuu kidogo nilitoka barazani nikaketi. Ulikuwa ni wakati wa magharibi. Jua lilikuwa limeshazama likionesha miale ya rangi nyekundu upande wa magharibi.

    Sikukaa sana pale nje nikarudi ndani kuwasha taa kisha nikabaki mle mle chumbani. Baada ya kupita karibu saa moja na nusu, Juma akarudi.

    “Pole kwa safari” nikamwambia.

    Juma akaketi kwenye kiti.

    “Asante. Nimekwenda na nimezungumza naye. Nimemueleza kila kitu”

    “Amesemaje?”

    “Ameshangaa halafu amecheka. Kilichomchekesha ni wewe kuondoka pale. Amesema ni bora ungekimbilia kwake, angemkomesha yule jini palepale”

    “Sijui nilifanya upumbavu gani!”

    “Sasa amesema kesho twende asubuhi. Kuna vifaa atavihitaji”

    “Kesho si unaenda kazini?”

    “Hapana, kesho nitakuwa na mapumziko”

    “Vifaa gani ametaka?”

    “Ameniambia nisikutajie hivyo vifaa. Utavikuta huko huko”

    “Vina thamani gani?”

    “Kama elfu hamsini hivi”

    “Nitakupa”

    “Sasa hivyo vifaa utavinunua wewe?” nikamuuliza Juma.

    “Mganga amesema tumpelekee pesa. Atajua yeye”

    “Sawa. Sasa twende nyumbani nikupe hizo pesa”

    “Bado kuna gharama ya kazi yake”

    “Ni kiasi gani?”

    “Hajasema”

    “Nina akiba ya elfu themanini, nitakupa zote”

    “Halafu wewe utabaki na nini?”

    “Si kitu, nataka hili tatizo liishe”

    “Hapana, nipe elfu sitini, bakisha ishirini. Kama kutahitajika pesa zaidi nitakuongezea mimi”

    “Nitakushukuru sana. Sasa twende nikakupe hizo elfu sitini”

    Tukatoka mimi na Juma kwenda nyumbani ninakoishi. Tuliingia ndani nikawasha taa na kutoa shilingi elfu sitini kutoka chini ya godoro, mahali ninakoweka pesa zangu.

    Nikampa Juma zile elfu sitini kisha nikazima taa, tukatoka.

    Asubuhi ya siku iliyofuata tulikwenda kupanda gari tukaenda Amboni. Tulipofika kwa yule mganga, sisi tulikuwa wa kwanza kwani tulikuwa tumewahi mapema.

    Juma alipomueleza mganga huyo kuwa mimi ndiye niliyekwenda kwake jana yake na kuondoka baada ya kumuona yule msichana wa kijini, mganga aliniambia.

    ”Hebu niambie ilikuwaje jana?”

    Nikamueleza.

    “Ulifanya kosa kukimbia, ungekuja humu ndani”

    “Nilipatwa na kiwewe mzee”

    “Huyo jini anayekufuata ni Ummi Subiani. Majini hao wana matatizo sana”

    “Sasa mzee nimekuja na zile pesa. Umesema vile vifaa vinagharimu kiasi gani?” Juma akamuuliza mganga huyo.

    “Ni elfu arubaini”

    Juma akamuhisabia shilingi elfu arubaini na kumpa.

    “Vifaa vyote vinavyohitajika ninavyo hapa. Kazi yenu itafanyika ufukweni mwa bahari. Itabidi twende huko pamoja na vifaa vyote”

    Baada ya kutuambia hivyo mganga aliwaita wasaidizi wake wawili. Mmoja akamwambia atangulie na sisi huko ufukweni mwa bahari na mwingine akampa kazi ya kwenda kuchukua vifaa vilivyohitajika.

    Sisi tukatoka na yule mtu, tukaenda kwa miguu huko ufukweni. Ulikuwa mwendo mrefu kidogo. Tulipofika hapo mahali, bahari tulikuwa tunaiona mbele yetu. Tukakaa kwenye mchanga mkavu wa ufukweni kumsubiri mganga.

    Mganga alifika baada ya saa moja hivi akiwa na msiidizi wake wa pili. Mganga mwenyewe alikuwa ameshika mkuki na kapu lililokuwa na vifaa. Na msaidizi wake alikuwa ameshika kapu jingine na mkono mwingine alikokota mbuzi mweusi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilipowaona mwili ulinisisimka. Sikujua ni kwanini. Pia nilijiona nikipata hofu. Nilihisi labda ni kwa sababu shughuli hizo zilikuwa za kishirikina wakati mimi nilikuwa ni muumini wa kanisa. Pamoja na ukweli huo niliona sikuwa na budi nikabiliane na ushirikina huo kwani matatizo yaliyonikuta hayakuwa madogo.

    Mganga na msaidizi wake wakapanga vifaa vyao pale chini. Palikuwa na vifaa vingi vya kiganga zikiwemo nazi saba, kijungu, mchanga mweusi ambao niliambiwa ni mchanga wa kaburi na vitu vingine.

    Vitu hivyo vilipangwa kuzunguka duara na mimi nikaambiwa nikae katikati ya duara hilo. Mganga akaniambia nisiwe na hofu.

    “Tatizo lako litakwisha leo. Nitamuita yule jini hapahapa na nitawafarakanisha. Hatakufuata tena” akaniambia.

    Maneno yake kwa upande mmoja yalinipa matumaini lakini kwa upande mwingine yaliniongezea hofu.

    Yaliniongezea hofu kwa sababu yule msichana wa kijini alikwishanionya kuwa nisiende tena kwa mganga na kwamba yeye amezaliwa katika ukoo wa wachawi na hakuna mganga atakayemuweza.

    Lakini mganga huyo nilipomueleza maneno hayo alionekana kuyapuuza na kutoyatilia maanani. Akaniambia kuwa

    yeye ni kiboko wa majini. Hakuna jini anayemshinda yeye.

    “Maneno yake ni vitisho tu. Alitaka kukutisha ili usije kwangu, anajua mimi ni mkali” Mganga huyo akaniambia kwa kujitumainisha

    Mara tu baada ya mimi kuketi katikati ya lile duara, mganga alielekea upande wa baharini akapaza sauti yake na kutamka maneno ya kiarabu ambayo sikuweza kujua maana yake. Baadaye akasema kwa Kiswahili.

    “Ewe Banuna mwana wa Ziraili wa ukoo wa Ummi Subiani, ninakuita hapa kwa Alfred, uje hapa haraka sana, nina shughuli na wewe”

    Aliyarudia maneno hayo mara tatu. Baada ya hapo alianza kusoma kwa kiarabu huku uso wake ukutazama baharini.

    Alisoma kwa kiaribu kwa karibu saa nzima. Kwanza kulikuwa kimya. Kilichokuwa kikisikika ni mvumo wa mawimbi ya bahari. Lakini ghafla nazi tatu zikapasuka zenyewe vipandevipande!.

    Hapo hapo tukaona wimbi kubwa la maji ya bahari linakuja huku likitoa ngurumo kali.

    Nilitaka kukimbia lakini mganga alinizuia.

    “Usiondoke, jini wako anakuja!” akaniambia.

    Niliendelea kukaa huku nikitetemeka.

    Lile wimbi lilikuja kwa kasi, likawa limesimama kama ukuta, halafu lilitoweka ghafla. Lilipotoweka liliacha msichana aliyekuwa akitembea juu ya bahari bila kuzama kama aliyekuwa anatembea kwenye ardhi.

    Nikashangaa na kumuangalia kwa makini. Alipozidi kutukaribia nilimuona vizuri na kuweza kumtambua. Alikuwa ni Banuna yule msichana wa kijini. Alikuwa amevaa gauni refu jeupe alilolishikilia ili lisiloe maji.

    Alikuwa akitembea kwa taratibu huku mganga huyo akiendelea kumuita.

    “Njoo haraka njoo haraka!”

    Alipofika mwisho wa bahari alianza kutembea kwenye tope lakini miguu yake ambayo haikuwa na viatu wala kwato haikuwa ikititia kwenye tope hizo

    Alikuja taratibu hadi pale tulipokuwa. Mara moja tukasikia kupuo la manukato yake.

    “Ni nani aliyeniita mimi binti wa ukoo wa kifalme?” Msichana huyo akauliza kwa sauti kali ya kiburi huku akimuangalia yule mganga kwa macho makali.

    Mganga akajitutumua na kumjibu.

    “Nimekuita mimi mganga nina…..”

    “Unataka nini?” Msichana huyo akamkatiza. Uso wake ulikuwa umeiva na kuwa mwekundu.

    “Zungumza na mimi kwa adabu. Kama…..”

    “Wewe nani?” Msichana alimkatiza tena sasa akionesha kiburi cha wazi.

    “Mimi Mtemi Wembe…..’

    Msichana huyo akamkatiza tena.

    ”Kama wewe ni Mtemi Wembe, mimi ni Banuna mwana wa Ziraili…mimi wa ukoo wa kifalme. Wewe huwezi kuniita mimi….”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nakwambia…..!” Mtemi wembe alitaka kusema lakini Banuna hakumpa nafasi.

    “Una shida gani na mimi?” akaendelea kumuuliza kwa sauti yake kali na ya kiburi.

    “Nataka kukutenganisha na Alfred, leo iwe mwisho wako kumfuata!” Mganga akamwambia kwa sauti kali.

    Bananuna kwa jeuri alikishika kiuno chake akamwambia mganga.

    “Nakwambia huniwezi! Alfred nitakuwa naye hadi kifo chake. Simuachi! Unasemaje?”

    Hapo hapo mganga naye akapandisha jini lake.

    “Shiit! Wewe nani Tanzania? Utakwenda tu!. Leo nitakuondoa kwa sababu umekosa adabu!” Jini wa mganga huyo akasema kwa ghadhabu.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog