Search This Blog

NILIOA JINI NA KUZAA NAE - 3

 





    Simulizi : Nilioa Jini Na Kuzaa Nae

    Sehemu Ya Tatu (3)



    ILIPOISHIA..

    ”Kama wewe ni Mtemi Wembe, mimi ni Banuna mwana wa Ziraili…mimi wa ukoo wa kifalme. Wewe huwezi kuniita mimi….”

    “Nakwambia…..!” Mtemi wembe alitaka kusema lakini Banuna hakumpa nafasi.

    “Una shida gani na mimi?” akaendelea kumuuliza kwa sauti yake kali na ya kiburi.

    “Nataka kukutenganisha na Alfred, leo iwe mwisho wako kumfuata!” Mganga akamwambia kwa sauti kali.

    Bananuna kwa jeuri alikishika kiuno chake akamwambia mganga.

    “Nakwambia huniwezi! Alfred nitakuwa naye hadi kifo chake. Simuachi! Unasemaje?”

    Hapo hapo mganga naye akapandisha jini lake.

    “Shiit! Wewe nani Tanzania? Utakwenda tu!. Leo nitakuondoa kwa sababu umekosa adabu!” Jini wa mganga huyo akasema kwa ghadhabu.

    SASA ENDELEA

    Nikajiambia kimoyomoyo, leo patazuka balaa! Kabla sijamaliza kuwaza, Banuna alishavuta mkono, akamtandika Mtemi Wembe kibao cha shavu. Mtemi Wembe akaanguka chini. Hakuinuka tena. Povu likawa linamtoka mdomoni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kitendo hicho kilitufanya mimi, Juma na wasaidizi wa mganga huyo tukurupuke na kutimua mbio. Juma na mimi tulitimua mbio za ajabu. Kila mmoja alikimbilia upande wake. Tulikuja kukutana barabarani.

    Kwa sekunde kadhaa tulikuwa tumesimama tukihema, hatukuweza kuzungumza lolote. Punde tu ikatokea daladala ikielekea mjini, nikaipungia mkono. Daladala hiyo iliposimama tukajipakia.

    Humo ndani ya daladala pia hatukuzungumza kitu. Kila mtu aliyetuona alijua kuwa tumepatwa na jambo tena jambo kubwa.

    Tulipofika stendi ya Tanga tulishuka. Mwili wangu ulikuwa bado ukutetemeka. Juma akanitazama kisha akatikisa kichwa kusikitika.

    “Ni hatari!” akaniambia na kuongeza.

    “Sikutarajia kuwa yatatokea mambo kama yale!”

    “Mimi nilikuwa na mashaka tangu mapema”

    “Yule msichana aliyekuja pale na kumpiga yule mzee ni nani?”

    “Si ndiye huyo jini anayenifuata!”

    “Kumbe jini mwenyewe ndiye yule, mkali namna ile!”

    “Umemuona mwenyewe Juma!”

    “Kwa uzuri ni mzuri sana lakini anatisha. Sijui kama yule mganga atapona!”

    “Kama mganga mwenyewe amepigwa, je mimi mwenyewe itakuwaje!”

    “Na ni mganga niliyemtegemea sana. Inaonesha tatizo lako ni kubwa sana”

    “Sasa tufanyeje rafiki yangu?”

    “Twende nyumbani, tutashauriana”

    Tulipofika nyumbani kwa Juma, tulikaa na kuanza kujadiliana.

    Juma aliniambia kuwa yule mganga ameshashindwa na haitakuwa na maana yoyote kurudi kwake tena. Na kama ni suala la pesa zetu tulizompa ndio zimeshapotea. Tusingeweza kwenda kumdai. Na pia hatukujua hali yake itakuwaje.

    “Kwa jinsi hili tatizo lilivyo, mimi ningekushauri uende Pemba. Kule kuna waganga hodari sana wa majini”

    “Hata mimi nimewahi kusikia hivyo”

    “Nimesikia wanawafuga majini majumbani na kuwatuma”

    Sikumjibu kitu. Nilikuwa nikiwaza jinsi nitakavyofika huko Pemba wakati sikuwa na akiba yoyote ya pesa.

    “Mimi nadhai Alfred uende Pemba” Juma akaendelea kuniambia.

    “Ushauri wako ninaukubali, lakini sina pesa, nitakwendaje?”

    “Hilo nalo ni tatizo jingine. Itabidi tusubiri mwisho wa mwezi nikupe mshahara wangu”

    “Halafu wewe utatumia nini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Usijali Alfred, nitakopa kopa hivyo hivyo”

    Kwa kweli nilihuzunika sana lakini sikuwa na jinsi.

    “Usihuzunike rafiki yangu. Yote yatakwisha. Hakuna lisilo na mwisho”. Juma akaniambia kwa moyo wa huruma.

    Kutokana na hofu niliyokuwa nayo kuhusiana na Banuna, niliendelea kuishi kwa Juma nikisubiri mwisho wa mwezi ufike anipe mshahara wake niende Pemba kutafuta waganga. Lakini kutoka siku ile tuliyokwenda Amboni kwa yule mganga na kutokea lile tukio, sikumuona tena Banuna.

    Usiku mmoja wa kuamkia ile siku ambayo Juma angepata mshahara wake na kunipa kama alivyoniahidi, lilitokea tokeo ambalo sitalisahau.

    Usiku huo nilikuwa nimelala na Juma, nilishituka usingizini na kumuona Banuna amesimama kando ya kitanda upande ninaolala mimi. Alikuwa amevaa nguo nyeupe tupu. Ilikuwa ni hali ambayo ingenifanya nishituke na pengine kupiga kelele au kutoka mbio.

    Lakini sikushituka wala sikupiga kelele wala sikutoka mbio. Nilikuwa kama zezeta. Nilijiona kama nilikuwa katika ndoto kwani akili hazikuwa zangu.

    “Alfred!” Banuna akaniita alipoona nimeamka.

    “Ndiyo Banuna!” nikamuitikia kwa sauti tulivu.

    “Umeniona?” akaniuliza kama aliyekuwa ananisomesha.

    “Ndiyo nimekuona, si Banuna wewe?”

    “Nimekufuata twende kwetu”

    “Kwenu wapi?”

    “Kwetu baharini. Uko tayari twende?”

    “Niko tayari” nikamjibu”

    “Amka basi twende zetu”

    Nikainuka na kushuka kitandani. Juma alikuwa amelala fofofo.

    “Vaa nguo zako” akaniambia.

    Nikavaa suruali, shati na viatu.

    “Sasa twende”

    Akanishika mkono.

    Tukatoka mle chumbani. Akafungua mlango wa mbele na kuniambia nitangulie kutoka nje. Nilipotoka na yeye akafuatia.

    Aliinama chini akachora msitari mbele yangu kisha akaniambia.

    “Vuka huo msitari”

    Nikiwa kama zezeta ambaye sikuwa na uwezo wa kuwaza chochote, nilitii alichoniambia, nikapiga hatua na kuvuka ule msitari. Kufumba na kufumbua nikajiona niko katika eneo jingine ufukweni mwa bahari. Banuna alikuwa amesimama kando yangu, akanishika mkono na kuniambia.



    “Twende kule”

    Alinionesha kule baharini.

    Tukawa tunatembea kwenye ufukwe kuelekea baharini. Sikuju tulikwa tunakwenda wapi. Ulikuwa usiku mwingi na kulikwa kunatisha lakini sikupata hofu yoyote.

    Punde tu tukayafikia maji, sasa tukawa tunatembea kwenye maji huku nguo zetu zikitota. Tangu maji yalikuwa kwenye viwiko vya miguu hadi yakawa kwenye magoti. Tukaendelea kwenda hadi maji yakatufikia kifuani.

    Sasa nikawa ninayumbishwa na maji. Ilibidi Banuna anishikilie ili maji yasinichukue.

    “Tunakwenda hadi wapi?” nilimuuliza Banuna nilipoona maji yametufika shingoni.

    “Tunakwenda kwetu” Banuna akanijibu.

    “Kuna mji huku?”

    “Ndio upo”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Uko wapi?”

    “Utauona, twende tu”

    “Tutafika saa ngapi?”

    “Usiwe na wasiwasi. Tutafika sasa hivi”

    Banuna aliendelea kunipeleka hadi maji yakawa yananikosesha pumzi kwani mawimbi yalikuwa yanapiga kwenye uso wangu. Banuna akaniambia nipande kwenye mgongo wake.

    “Panda ukae kwenye mabega yangu”

    Banuna akanisaidia nikaweza kukaa kwenye mabega yake. Jambo la ajabu ni kuwa Banuna aliweza kunibeba na kutembea na mimi kwenye maji huku kichwa chake kikiwa kimeshazama baharini Sikuweza kujua alikuwa akipumua kwa namna gani.

    Muda si muda niliona ananizamisha cihini ya bahari. Nikapiga kelele.

    “Sasa tunakufa!”

    “Usiogope, hutakufa” niliisikia sauti yake ikitokea ndani ya maji.

    Licha ya kunitoa wasiwasi kuwa sitakufa, sikuamini. Nikizama chini ya bahari. nitapata wapi pumzi?

    “Banuna sitaweza kupumua ndani ya maji!” nikamwambia Banuna kwa sauti ya kutetemeka.

    “Utaweza. Mbona mimi ninaweza”

    Banuna akazidi kunizamisha. Sasa maji yalikuwa kwenye shingo yangu. Nilikuwa nimefunga mdomo lakini ndani ya moyo wangu nilikuwa ninapiga kelele. “Nakufa…nakufa…nakufa…!”

    Ghafla kichwa changu chote kikazama chini ya bahari. Nilikuwa nimetaharuki kwa hofu lakini niliona miujiza mikubwa. Vile ninazama tu chini ya bahari niliona tumetokea mahali kweupe kusiko na bahari.

    Banuna akiwa amenibeba kwenye mabega yake alikuwa amesimama kwenye mnara mrefu ulioteremka chini. Huko chini kulikuwa na mji mkubwa uliokuwa unawaka taa. Kulikuwa na minara kadhaa iliyoonekana kila upande

    Ulikuwa mji wa ajabu na mzuri usio na magari wala pikipiki isipokuwa watu wa ajabu walioonekana wakienda huku na huku kama vile ni mchana.

    Kwa upande mmoja niliona kulikuwa na gulio. Watu walikuwa wamejazana wakinunua mahitaji.

    Wengi wa watu niliowaona walikuwa wamevaa nguo zilizofanana na nguo zenyewe zilikuwa shuka, ama shuka nyeupe ama nyekundu. Wengine walikuwa wamechanganya shuka nyeupe na nyekundu. Baadhi ya watu hao walikuwa wamejifunga vilemba vikubwa kama waarabu.

    Mbali ya watu hao, pia niliona punda wengi na farasi wa rangi mbalimbali.

    Banuna akaniambia nishuke kutoka kwenye mabega yake. Huwezi kuamini kuwa msichana huyo aliweza kunibeba, labda kwa vile alikuwa ni jini kwani hata kwa uzito nilikuwa nimemzidi.

    “Umeuona mji wetu?” Banuna akaniuliza.

    “Nimeuona. Ndiyo mji wenu huu?”

    “Ndio huo. Wale wote unaowaona chini ni majini!”

    “Sasa huu mji ndio uko chini ya bahari?”

    “Ndiyo. Na hapa tulipotokea ndio nyumbani kwetu”

    “Huu mnara ndio nyumbani kwenu?”

    “Hii ni ghorofa, imekwenda chini. Humu ndani kuna wazazi wangu”

    Nikawa nimeshangaa.

    “Hii ni nyumba kabisa. Tutaingia na utaiona” Manuna akaniambia.

    Mnara huo wa mawe ulikuwa na matundu kama madirisha na kulikuwa na sehemu yenye uwazi mrefu kama mlango. Banuna akaniambia nimfuate.

    Akatangulia kuingia kwenye ule uwazi na mimi nikamfuata nyuma. Kulikuwa na kiza sana. Nilikuwa sioni.

    “Nishike bega twende” Banuna akaniambia.

    Nikanyoosha mkono wangu wa kulia na kumshika bega.

    Kulikuwa na ngazi. Tukashuka taratibu. Tulikuwa kama tunaoshuka kwenye shimo. Kila tulivyozidi kushuka ndio kiza kilivyozidi.

    “Huoni kabisa?” Banuna akaniuliza baada ya ukimya mrefu.

    “Sioni!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mimi naona. Tunapita katika kuta za mawe, karibuni tutafika”

    “Sasa mnaishije kwenye kiza namna hii?”

    “Tunapokuwa kwenye mwanga, mboni zetu za macho zinakuwa

    Ndogo lakini tukiwa kwenye kiza mboni zinakuwa kubwa na kutuwezesha kuona”

    “Kwa hiyo mimi sitaweza kuona”

    “Tutatokea kwenye mwanga muda si mrefu”

    “Kiza hiki kinatisha sana bora mngeweka taa”

    “Usijali, utazoea tu”

    Mara nikasikia Banuna akisemeshana na mwenzake mwenye sauti ya kiume ambaye sikuweza kumuona kutokana na kiza. Lugha waliyozungumza haikuwa ya Kiswahili.

    Hapo hapo nikaona mlango unafunguliwa. Nikaona mwanga mzuri mweupe umetokea.

    “Tuingie” Banuna akaniambia.



     Tukaingia mle ndani. Kwa vile sasa kulikuwa na mwanga niliondoa mkono wangu kwenye bega la Banuna. Licha ya kuuona ule mwanga sikuweza kujua ni kitu gani kilichokuwa kinatoa mwanaga huo.

    Tulikuwa tumetokea katika ukumbi mpana uliokuwa umetandikwa mazulia mazuri na wenye hewa safi lakini ulikuwa mtupu usio na kitu chochote.

    Ulikuwa na milango mitatu iliyoingia ndani ambayo ilikuwa imezibwa kwa mapazia mazito ya hariri. Banuna alinipeleka katika mlango uliokuwa katikati, tukaingia.

    Tulitokea katika ukumbi mwingine mdogo uliokuwa na ngazi za kupanda. Tukapanda ngazi hadi juu kidogo, tukaingia kwenye mlango mwingine ambao pia ulizibwa kwa pazia. Tulipoingia katika mlango huo tulitokea katika ukumbi mwingine uliokuwa kama sebule iliyokuwa ina meremeta.

    Ulikuwa na fanicha zilizotengezwa kwa madini. Fanicha hizo zilikuwa zikitoa rangi mbalimbali za kupendeza. Muundo wa fanicha hizo sikuwahi kuuona popote. Nikabaki ninakikodolea macho kila kitu ninachokiona kwani kilikuwa

    cha ajabu kwangu. Mbali na vitu hivyo, harufu iliyokuwa inasikika humo ndani ilikuwa ni ya marashi na udi wa Ajemi.

    “Kaa hapo chini” Banuna akaniambia.

    “Nikae chini wapi?” nikamuuliza.

    “Kaa popote tu, sisi huku tunakaa chini”

    Nikakaa chini huku nikiendelea kuikodolea macho ile sebule. Kila kitu nilichokiona kilikuwa kigeni kwangu.

    “Sasa nisubiri nikamuite mama yangu, aje muonane” Banuna akaniambia na kupotea kwenye pazia lililokuwa mbele yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya muda kidogo niliona pazia likipenuliwa akatokea tena Banuna na mwanamke mmoja mzee. Alikuwa mfupi aliyevaa shuka nyeupe. Alikuwa na nywele ndefu nyeupe zizilizomteremka kwenye mabega. Hata hivyo alikuwa amefunga kilemba cheupe kichwani. Licha ya kumtazama kwa makini bibi huyo, sikuweza kutambua alikuwa muarabu au muhindi.

    Bibi huyo wa kijini alikuja hadi pale nilipokuwa nimeketi. Nikayaona macho yake ya kijivu, yalikuwa na mboni zilizosimama kama mboni za paka. Hata Banuna anapokasirika mboni zake hubadilika na kuwa hivyo..

    Jambo la ajabu ni kuwa sikutishika kukaa na viumbe hao waliokuwa na maumbile tofauti na mimi.

    Yule bibi aliketi karibu yangu akakunja miguu yake kisha akaniambia.

    “Asalaam alaykum”

    “Alaykumu salaam” nikamjibu.

    Banuna naye akaketi palepale.

    “Alfred, huyu ni mama yangu. Anaitwa Ummi Mariam” Banuna akaniambia.

    “Nimefurahi kumuona” nikamwambia Banuna.

    Banuna akamtazama mama yake na kumwambia.

    “Maa, huyu ndiye yule kijana niliyekuwa ninakwambia. Leo nimekuja naye umuone”

    Yule bibi akanitazama na kuniuliza.

    “Mmekubaliana nini na Banuna?”

    Swali hilo lilinishitua kidogo. Hata hivyo nilibetua mabega yangu na kumjibu.

    “Hatukukubaliana chochote!”

    “Alipokwambia mje huku alikwambia manakuja kufanya nini?”

    “Hakuniambia kitu”

    “Amekuleta tu!”

    “Aliniambia twende kwetu”

    Yule mama akamtazama Banuna.

    “Mbona mwenyewe hajui amekuja kufanya nini huku?”

    “Anajua” Banuna akasema kisha akabadili lugha na kusema kwa kiarabu, lakini sikuelewa alisema nini.

    Mama yake akanitazama mimi tena.

    “Eti mmekubaliana kuwa mnakuja huku kuoana?” akaniuliza.

    “Hatukukubaliana kuwa tunakuja kuoana” nikamjibu.

    “Na wala hakuwahi kukueleza jambo hilo?”

    “Aliwahi kunieleza”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Je ulikubali kwa hiyari yako?”

    “Hapana, sikukubali”

    “Alikuwa anakutisha?”

    Hapo nikanyamaza. Sikutaka kusema ukweli kuwa alikuwa ananitishia maisha.

    Yule mama alitambua mawazo yangu, akaniambia.

    “Sema usifiche”

    “Ndiyo alikuwa ananitisha” nikamwambia.

    Banuna akanitazama kwa uso wa tadhaa.

    “Alfred sema ukweli, nimekutisha mimi? Si tumekubaliana tuoane, uliniambia kuwa umenipenda?” Banuna akaniambia lakini sauti yake haikuwa na nguvu kwa vile maneno aliyosema yalikuwa ya uongo.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog